Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mary Deo Muro (13 total)

MHE. MARY D. MURO aliuliza:-
Je, ni kwa nini Mkoa wa Pwani usiwe na Mamlaka yake ya Maji kuliko ilivyo sasa kuwa chini ya DAWASCO ambapo hakuna huduma ya uondoaji maji machafu na bei ya maji iko juu kuliko ile ya Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Pwani huduma ya maji safi na usafi wa mazingira inatolewa na Halmashauri za Wilaya na Mamlaka za Miji Midogo isipokuwa kwa Miji ya Kibaha na Bagamoyo ambayo inahudumiwa na DAWASA kwa kupitia Shirika la Usambazaji Maji la DAWASCO. Muundo huu ni kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, Miji ya Kibaha na Bagamoyo imewekwa chini ya DAWASA kwa sababu za kijiografia na kiuendeshaji. Vyanzo vikuu vya maji yanayotumika kwa Kibaha, Bagamoyo na Dar es Salaam viko Wilaya za Kibaha (Ruvu Juu) na Bagamoyo (Ruvu Chini). Aidha, wakati mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini inajengwa, Miji ya Kibaha na Bagamoyo haikuwa na watu wengi wanaokidhi kuanzishwa kwa Mamlaka inayojitegemea.
Mheshimiwa Spika, bei ya maji kwa wananchi wa Kibaha na Bagamoyo ni sawa na ile inayotumika Dar es Salaam. Hakuna huduma ya uondoaji majitaka katika miji ya Kibaha na Bagamoyo hivyo wananchi hawalipii huduma hiyo. Kwa sasa DAWASA imepangiwa na EWURA kutoza bei ya majisafi kwa Jiji la Dar es Salaam na Miji ya Kibaha na Bagamoyo, Mkoa wa Pwani kiasi cha Sh. 1,663 kwa lita 1,000 na bei ya majitaka kwa Jiji la Dar es Salaam ni Sh.386 kwa lita 1,000. Hivyo kwa mteja aliyeunganishiwa mtandao wa majitaka na majisafi Jiji la Dar es Salaam analipa jumla ya Sh.2,049 kwa lita 1,000 za majisafi na majitaka.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa uondoaji majitaka kwa Miji ya Kibaha na Bagamoyo. Utaratibu wa kumpata Mhandisi Mshauri atakayesanifu mradi huo umekamilika na usanifu unatarajiwa kuanza Mei, 2016 na kukamilika Oktoba, 2016. Mshauri atatayarisha mpango kazi pamoja na nyaraka za zabuni zitakazotumika kutangaza zabuni ya ujenzi.
MHE. MARY D. MURO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa uendelezaji wa kilimo cha umwagiliaji katika Mto Rufiji ili kuongeza ajira na chakula?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mto Rufiji umepita katika maeneo mengi ambayo yanafaa sana kwa kilimo cha umwagiliaji ingawa maeneo mengi huwa yanakumbwa na changamoto ya mafuriko wakati wa kipindi cha mvua.
Mheshimiwa Spika, mpango kabambe wa umwagiliaji (National Irrigation Master Plan) wa mwaka 2002 uliahinisha maeneo yanayofaa kujenga skimu za umwagiliaji katika maeneo ya Mto Rufiji yakiwemo maeneo ya Segeni, Nyamweke, Ngorongo na Ruwe.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilishaanza kuendeleza scheme ya umwagiliaji ya Segeni, Wilayani Rufiji ambapo hekta 60 zilishaendelezwa na kuna mpango wa kuongeza hekta 60 zaidi. Aidha, Serikali imetuma shilingi milioni 358 kwa ajili ya scheme ya Nyamweke ambayo ina hekta 300 iliyopo Wilayani Rufiji kupitia mradi wa kuendeleza scheme ndogo za umwagiliaji kupitia ufadhili wa Serikali ya Japan.
Mheshimiwa Spika, Serikali iliainisha pia mashamba ya makubwa ya uwekezaji kwa kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya miwa na mpunga. Baadhi ya mashamba yaliyoainishwa ni pamoja na Lukulilo hekta 8,000 kwa ajili ya kilomo cha mpunga, Mkongo hekta 10,551 kwa ajili ya kilimo cha miwa, Muhoro hekta 10,000 kwa ajili ya kilimo cha miwa, na Tawi/Utunge hekta 15,924 kwa ajili ya kilimo cha miwa. Aidha, taratibu za kuwapa wawekezaji katika maeneo hayo zinaendelea kupitia Tanzania Investment Centre.
MHE. MARY D. MURO Aliuliza:-
Maji ni mahitaji muhimu kwa wanadamu na viumbe vyote lakini gharama za maji ni kubwa sana.
Je, ni lini Serikali itawasambazia maji wananchi waishio pembezoni mwa bomba kuu la Ruvu Juu Mlandizi - DSM katika maeneo ya Pangani, Lumumba, Kidimu na Zogowale ikizingatiwa kuwa maeneo hayo yapo karibu na bomba hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa mradi maeneo mengi ndani ya kilometa 12 ya pembezoni mwa bomba kuu la Ruvu Juu yameanza kupata huduma ya maji.
Hata hivyo, maeneo ambayo bado hayajaanza kupata huduma ya maji yatapata huduma hiyo baada ya utekelezaji wa miradi mipya ya kujenga mtandao wa mabomba ya kusambaza maji katika maeneo yote ambayo hayana huduma hiyo. Miradi hii itatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa kuanzia, tayari tunaye mkandarasi anayejulikana kwa jina la M/S Jain Irrigation System Limited ameanza kazi ya ujenzi wa mabomba ya usambazaji katika maeneo ya Malamba Mawili, Msigani, Mbezi Luis, Msakuzi, Kibamba, Kiluvya, Mloganzila na Mailimoja na atakamilisha kazi hiyo mwaka huu 2017. Maeneo ambayo yanapata maji kutoka Bomba la Ruvu Juu ni pamoja na Mlandizi na vitongoji vyake, Visiga, Misugusugu, Soga, Korogwe, Picha ya Ndege, Kwa Mathias, Tumbi, Mailimoja, Pangani, Kiluvya, Kibamba, Mloganzila, Mbezi kwa Yusufu, Mbezi Mwisho, Kimara, Kilungule, Mavurunza, Baruti, Kibo, Kibangu, Tabata, Segerea, Kinyerezi na Karakata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha za usambazaji maji katika bajeti 2017/2018 ili maeneo yote ya pembezoni mwa bomba kuu la Ruvu Juu, toka Mlandizi hadi Dar es Salaam umbali wa kilomita 12 yakiwemo maeneo ya Pangani, Lumumbana, Kidumu na Zugowale yapate huduma ya maji.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI (K.n.y. MHE. MARY D. MURO) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha Mbuga ya Saadani iliyoko Mkoa wa Pwani ili kuongeza pato kwa wananchi walio kando ya mbuga hiyo?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Utalii ya 1999 inaelekeza vema jamii zinazoishi ndani au jirani ya maeneo ya hifadhi kushirikishwa katika uhifadhi, uendelezaji na usimamizi wa vivutio vya utalii ikiwa ni pamoja na kunufaika kutokana na mapato yatokanayo na shughuli za utalii katika maeneo husika.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba miundombinu bora na ya kutosha na huduma bora kwa watalii ni miongoni mwa sababu za msingi za kukua kwa shughuli za utalii katika Hifadhi za Taifa na kuongezeka ka idadi na shughuli za watalii na hivyo kuongezeka kwa pato la Taifa litokanalo na utalii ikijumuisha ajira za kudumu na za muda pale zinapojitokeza; kukua kwa soko la bidhaa zitokanazo na shughuli za kiuchumi za wananchi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii na uwekezaji kwenye vijiji inayohusisha sekta za afya, elimu, maji na mazingira.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuboresha miundombinu katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani ikiwa ni pamoja na kujenga daraja la muda kuunganisha hifadhi na Mji wa Bagamoyo na Jiji la Dar es Salaam. Aidha, katika mipango ya muda mfupi na muda mrefu, Serikali itakamilisha ujenzi wa daraja la kudumu katika eneo la daraja la muda; kuboresha miundombinu ya malazi kwa wageni ambapo Kampuni ya mwekezaji ijulikanayo kama “Camden Hospitality Group” inakamilisha taratibu za kujenga kambi ya kudumu ya vitanda 30 na kuboresha miundombinu ya barabara na huduma nyingine za utalii ndani ya hifadhi.
Mheshimiwa Spika, Wizara pia inakamilisha utafiti wa wanyamapori waliokuwepo siku za nyuma na wakatoweka ili kuona uwezekano wa kuwarejesha kutoka katika maeneo mengine walikokuwa wameelekea. Wizara itaendelea kuboresha zaidi utangazaji wa vivutio vyenye upekee vya Hifadhi ya Taifa ya Saadani. Jitihada zote hizi zinatarajiwa kuongeza pato kwa wananchi waishio jirani na Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
MHE. MARY D. MURO aliuliza:-
Tangu mwaka 2014 TANESCO iliweka alama ya X kwenye maeneo ya Kiluvya, Kibaha hadi Chalinze kupisha ujenzi wa kupitisha umeme wa Gridi ya Taifa lakini hadi sasa hakuna fidia iliyolipwa kwa wananchi hao na pia wanashindwa kufanya uendelezaji wa maeneo hayo. Je, ni lini wananchi hao watalipwa fidia stahiki?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANESCO inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Kinyerezi Dar es Salaam kupitia Chalinze, Segera hadi Arusha yenye urefu wa kilometa 600. Pia mradi huo utahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wenye msongo wa kilovoti 220 kutoka Kibaha hadi Bagamoyo yenye urefu wa kilometa 40 na kutoka Segera hadi Tanga yenye urefu wa kilometa 60. Mradi huu pia unahusisha ujenzi wa vituo vya kupoozea umeme vya Chalinze, Segera, Kange na Zinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo ya mradi huu ni kuongeza upatikanaji wa umeme katika Ukanda wa Mashariki na Kaskazini mwa nchi kutoka kwenye mitambo ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi. Gharama za mradi huo ni dola za Marekani milioni 693 ambazo zitagharamiwa kwa mkopo kutoka benki ya Exim-China kwa asilimia 85 na Serikali ya Tanzania asilimia 15.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kutathmini mali za wananchi watakaopisha mradi huo kutoka Kibaha hadi Chalinze imekamilika na kuidhinishwa na Mtathmini Mkuu wa Serikali. Jumla ya shilingi bilioni 21.6 zitahitajika kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wapatao 855 wa Halmashauri za Kisarawe, Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini, Bagamoyo ikiwemo eneo la Kiluvya. Fidia hiyo italipwa na Serikali na fedha hizo zimetengwa katika bajeti ya Wizara kwa mwaka 2017/2018. Taratibu zote za uandaaji taarifa na majedwali ya malipo ya fidia zimekamilika na malipo yamepangwa kulipwa katika mwaka huu wa fedha 2017/2018.
MHE. MARY D. MURO aliuliza:-
Shamba la Vikuge lilikuwa mkombozi kwa wananchi wa Kibaha na Dar es Salaam kujipatia majani ya kulisha mifugo yao, lakini kwa sasa shamba hilo limegeuka pori. Je, Serikali ina kauli gani kuhusu shamba hilo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI nlijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba la kuzalisha mbegu bora za malisho la Vikuge - Kibaha, ni moja wapo kati ya mashamba saba ya Wizara yanayozalisha mbegu bora za malisho. Mbegu hizo huuzwa kwa wafugaji na wadau wengine ili kuwekeza katika uzalishaji wa malisho kwa ajili ya kuwa na ufugaji wenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba hili pia huzalisha hei na kuwauzia wafugaji wa Kibaha, Dar es Salaam na kwingineko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba lina ukubwa wa jumla ya hekta 515 ambapo eneo la hekta 30 ni makazi, hekta 20 ni hifadhi ya vyanzo vya maji na eneo linaloendelezwa ni hekta 250. Eneo lililobaki si pori bali ni eneo la akiba lenye malisho ya asilia ambalo huwa linafyekwa vichaka na kuvunwa malisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa 2017/2018 shamba la Vikuge limezalisha jumla ya marobota ya hei 26,000 na mbegu bora za malisho kilo 1,500 ambazo zinauzwa kwa wadau wa malisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shamba la Vikuge katika mwaka wa 2018/2019 Serikali imejipanga kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za malisho na hei kwa kuendeleza eneo jipya la hekta 20.
MHE. LUCIA M. MLOWE (K.n.y. MARY D. MURO) aliuliza:-
Kumekuwepo na mkanganyiko wa watumishi wa zimamoto kwenye viwanja vya ndege na viwanja hivyo kutokuwa huru katika kuwatumia kutokana na kuwa si sehemu ya waajiri wao:-
Je, nini kauli ya Serikali kuhakikisha viwanja vinajitegemea?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linasimamiwa na Sheria Namba 14, Sura ya 427 ya Mwaka 2007 iliyounganishwa Vikosi vya Zimamoto vilivyokuwa chini ya TAMISEMI na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kuwa chini ya Kamandi moja ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ni Taasisi za Serikali ambazo hufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kutoa huduma ya kulinda mipaka ya nchi, hivyo hakuna mkanganyiko wowote wa kiutendaji. Hata hivyo, naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa upo ushirikiano mzuri kati ya vyombo hivi vya ulinzi na usalama na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege katika kutekeleza majukumu yao.
MHE. MARY D. MURO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya TAMCO Kibaha kupitia Vikawe kuunganisha na barabara ya Bagamoyo ili kupunguza msongamano wa magari yanayoenda Mbezi Boko na Bagamoyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya TAMCO kupitia Vikawe hadi Mapinga yenye urefu wa kilometa 23 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ambapo kilometa 22 zimejengwa kwa kiwango cha changarawe na kilometa moja imejengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na tathmini ya fidia katika barabara hii ilikamilika katika mwaka wa fedha 2012/2013. Utekelezaji wa ujenzi wa kiwango cha lami umeanza kwa awamu ambapo kilometa moja imekamilika kujengwa. Vilevile taratibu za ununuzi kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa kipande cha kilometa 2.5 zimekamilika ambapo Mkandarasi Skol Building Contractors amepatikana na anategemewa kusaini mkataba mwishoni mwa mwezi huu wa Septemba, 2018.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kimetengwa kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Aidha, taratibu za ununuzi wa mkandarasi wa ujenzi kwa kiwango cha lami kwa kipande kingine cha kilometa 1.5 zimeanza. Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Pwani anaendelea kufanya matengenezo mbalimbali barabara hii ili iweze kupitika majira yote ya mwaka ambapo shilingi bilioni 1.789 zimetengwa katika mwaka huu wa fedha kutoka Mfuko wa Barabara.
MHE. MARY D. MURO aliuliza:-
Uanzishaji wa Vyuo vya Ufundi ulilenga kuwapatia elimu ya vitendo hasa vijana wetu, lakini Chuo cha Ufundi Kibaha kilicho chini ya Shirika la Elimu Kibaha hakina vifaa wala miundombinu ya kujifunzia:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka vifaa pamoja na kufufua miundombinu katika chuo hicho?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inasimamia Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha kilichokuwa chini ya Shirika la Elimu Kibaha. Chuo hiki ni mojawapo ya vyuo 55 vilivyohamishiwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuanzia Mwaka wa Fedha 2016/2017. Vyuo hivi vina changamoto nyingi za uendeshaji ikiwemo; upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na uchakavu wa majengo ya madarasa, karakana, mabweni, nyumba za watumishi na miundombinu.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali ya vyuo hivyo, Serikali imetoa Kandarasi kwa vyuo vitatu ambavyo ni Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia, Mbeya ili vifanye uchambuzi wa kina wa hali halisi ya miundombinu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika vyuo hivyo. Baada ya kukamilika kwa zoezi hili taratibu za kuvifanyia ukarabati zitaanza.
Mheshimiwa Spika, aidha, Wizara pia inafanya zoezi la kubaini mahitaji ya watumishi katika vyuo vyote vya FDC. Zoezi hili linatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2018. Baada ya zoezi hili kukamilika, ujenzi, ukarabati na ufungaji wa mitambo na vifaa vya kufundishia na kujifunzia utafanyika kulingana na mahitaji. Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha ni mojawapo ya vyuo vilivyo katika mpango huu.
MHE. MARY D. MURO aliuliza:-

Je, ni lini Kituo cha Misugusugu “Check Point” kitahamishwa, kwani kimekuwa kero kutokana na vumbi linalosababishwa na miundombinu mibovu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mradi wa kituo cha pamoja cha ukaguzi wa mizigo (One Stop Inspection Station) ili kuziwezesha mamlaka za ukaguzi wa mizigo kufanya kazi ya ukaguzi katika eneo moja. Mradi huu unatekelezwa sambamba na mradi wa mizani ya ukaguzi wa mizigo iliyopo Vigwaza Mkoa wa Pwani. Taasisi zinazohusika katika mradi huu ni pamoja na TANROADS, Polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka ya Mapato Tanzania ipo katika hatua za awali za kujenga na kusimika mifumo ya ukaguzi katika eneo la mradi lililopo Vigwaza, hivyo basi kituo cha ukaguzi wa mizigo kitahamishiwa kutoka Misugusugu kwenda vigwaza mara baada ya kazi ya kujenga na kusimika mifumo itakapokamilika.
MHE. MARY D. MURO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalipa fidia Wananchi wa Kiluvya, Madukani, Mwanalugali na Mikongeni ambao wamepisha ujenzi wa njia ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalumu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANESCO inatekeleza mradi wa kujenga njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovot 400 kutoka Kinyerezi (Dar es Salaam) na Rufiji (Pwani) kupitia Chalinze hadi Dodoma kupitia maeneo ya Kiluvya, Madukani na Mwanalugali. Mradi huu unalenga kuongeza upatikanaji wa umeme katika ukanda wa Mashariki, Kati na Kaskazini mwa nchi kutoka katika mitambo ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi na mradi wa Rufiji.

Mheshimiwa Spika, upimaji wa njia na uthamini wa mali za wananchi watakaopisha mradi ulikamilika mwaka 2018. Jumla ya shilingi bilioni 21 na milioni 600 zinatakiwa kulipwa kama fidia kwa wananchi katika maeneo ya Halmashauri za Kisarawe, Kibaha Mjini na Kibaha Vijijini ikiwemo wananchi wa Vijiji vya Chalinze, Kiluvya madukani na Mwanalugali. Katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali imetenga fedha shilingi bilioni 50 kwa ajili ya malipo ya fidia kwa wananchi wa maeneo hayo baada ya kukamilisha uhakiki wa madai hayo.


Mheshimiwa Spika, Serikali inawaomba wananchi wavute subira wakati Serikali inaendelea kukamilisha taratibu za malipo haya, ahsante sana.
MHE. MARY D. MURO aliuliza:-

Viwanja vya Mwanalugali Mjini Kibaha vimeshindwa kupimwa kutokana na mgogoro uliopo kwa wenye ardhi hiyo kutolipwa fidia wakati wa upimaji mwaka 2000:-

Je, Serikali inatoa msaada gani kwa wananchi hao ambao wameshindwa kuendeleza maeneo yao na kuwasababishia umaskini mkubwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha uthamini na kubaini watu 62 wanadai fidia kiasi cha Sh.575,017,858. Serikali imepanga kulipa fidia hiyo kwa kutumia fedha zitatokana na mauzo ya viwanja vilitolewa kwa wananchi na taasisi tangu mwaka 2004 lakini mpaka leo bado havijalipiwa na havilipiwi kodi ya Serikali.

Aidha, Serikali inakusudia kubadili matumizi ya eneo moja la ibada ambalo wananchi wanadai fidia ili wananchi wamilikishwe maeneo yao. Vilevile, Halmashauri inakusudia kuomba kibali kwa Kamishna wa Ardhi ili kufuta baadhi ya viwanja ili viweze kuuzwa kutunisha Mfuko wa Fidia na vingine kukabidhiwa kwa wananchi wanaodai fidia ili kumaliza mgogoro uliokuwepo kwa muda mrefu.
MHE. MARY D. MURO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha Chuo cha FDC kilichoko Shirika la Elimu Kibaha ambacho hakina vifaa vya kujifunzia, karakana zimechoka pamoja na miundombinu mibovu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (Kibaha Folk Development College -KFDC) kilianzishwa mwaka 1964 kikijulikana kama Farmers Training Centre kwa ufadhili wa Serikali ya Norway chini ya Mradi wa Tanganyika Nordic Project. Baada ya mradi huu kukabidhiwa kwa Serikali ya Tanzania mwaka 1970, jina la mradi lilibadilika na kuitwa Shirika la Elimu Kibaha na hivyo chuo kikawa chini ya Shirika hili. Mwaka 1975 wakati huo Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilipoanzishwa nchi nzima, chuo hiki kilianza kuitwa Kibaha FDC chini ya Wizara ya Elimu kikiwa miongoni mwa vyuo 55 nchini. Kwa kipindi kirefu chuo hiki hakijafanyiwa ukarabati mkubwa, hata hivyo, kupitia mapato yake ya ndani chuo kimekuwa kikifanya ukarabati mdogo mdogo.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kupitia Chuo Kikuu cha Ufundi cha Dar es Salaam (DIT) imekifanyia chuo tathmini na kuandaa mpango mkubwa wa ukarabati. Vilevile chuo kiliandaa andiko la mradi na kuomba fedha kutoka Serikali ya Uholanzi ili kuboresha chuo ambapo vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 70 vilipatikana na kusaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa vifaa chuoni.

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kukarabati chuo hicho utakaotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.