Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Rhoda Edward Kunchela (6 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kabla sijaanza kuchangia, naomba nitoe shukranI zangu mbele ya Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kufika hapa. Pia napenda kushukuru chama changu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kunifikisha hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia Mpango huu kuna mambo mawili au matatu ambayo nahitaji kuchangia. Jambo la kwanza ni kuhusiana na uvuvi haramu pamoja na uwindaji haramu ambao unaendelea katika nchi yetu. Sasa katika Mpango huu ambao nimeupitia sijaona kama kuna mkakati wa kuweza kuzuia hao majangili ambao wanaendelea kuua watu wetu na kuiba wanyama. Pia kuna wawindaji ambao wanapewa vibali halali, ningeomba Serikali sasa kupitia huu Mpango iweke mkakati wa kuhakikisha kwamba pamoja na kupewa vibali lakini ijulikane ndani ya hizo National Park wanafanya shughuli gani. Nikitoa mfano kwenye Mkoa wangu wa Katavi kuna Wapakistan zaidi ya 40 ndani ya lile pori, lakini ukiulizia ni shughuli gani wanafanya siyo za kiuwekezaji. Nimewahi kutembelea pale, unakuta wengi wao ni madereva lakini wengine wanapika, ndiyo wanaohudumia kwenye hoteli pale ndani. Kama Serikali tuangalie hawa wawindaji ambao wana vibali kabisa vya kuwinda katika mbuga zetu wanafanya shughuli gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya mbuga pia kuna viwanja vya ndege, sasa hatuwezi kuelewa hawa wawindaji wanasafirisha vitu gani. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge tusiendelee kulalamika kwamba ndovu wanaibiwa inabidi kuchukua hatua. Nitoe masikitiko yangu kwa rubani ambaye alitunguliwa na hawa majangili katika mbuga ya Meatu. Kama Serikali au TANAPA wameshindwa kuweka usalama kwa hawa mapolisi ambao wanalinda wanyama wetu pamoja na mbuga zetu basi ni bora tukajua ni jinsi gani tunawalinda hawa wanyama wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mchango wangu wa pili unajikita katika viwanda. Mapinduzi ya viwanda yanatakiwa yaendane na uzalishaji wa umeme yaani huwezi ukazungumzia viwanda bila kueleza unaongezaje nguvu ya umeme katika viwanda vyetu. Mpaka sasa Tanzania tunazalisha umeme megawatts 1,247 lakini Mpango Mkakati wa Miaka Mitano uliopita Serikali iliweka mpango wa kuongeza uzalishaji wa umeme wa megawatts zaidi ya 2,780 lakini hatukufikia malengo. Tunapozungumzia mapinduzi ya viwanda basi tuhakikishe kwamba nguvu kubwa tutaongeza kwenye uzalishaji wa umeme kwa sababu hatuwezi tukazungumzia viwanda bila umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme hatuzungumzii kwenye viwanda tu pia tunauzungumzia kwenye matumizi ya kawaida ya wananchi wetu nikitoa mfano wa Mkoa wangu wa Katavi. Mkoa wa Katavi mpaka sasa tunatumia umeme wa generator hata kama tuna viwanda vidogo vidogo kwenye mkoa wetu basi hatuwezi kuzalisha product ya aina yoyote kwa sababu umeme siyo wa uhakika. Kuna kipindi inafikia wiki nzima wananchi wa Mpanda au Mkoa wa Katavi wanakosa umeme. Kwa hiyo, mapendekezo yangu katika suala la umeme Serikali iangalie sasa ni jinsi gani tunakwenda kuweka mikakati mizuri katika kuweka nguvu ya kuzalisha umeme hasa kwenye kipimo cha megawatts. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa tatu unajikita zaidi kwenye afya. Kama Serikali tunahitaji kufikia malengo, maana nimesoma Mpango huu una mipango mizuri kabisa ambayo inatakiwa tuifikie kwa ajili ya ku-achieve hizo goals ambazo mmeziweka. Kitu ambacho nakiona kinafeli zaidi katika Mipango yote ni kwamba tuna mipango mizuri lakini lazima kuwe na implementation na monitoring lakini Serikali inawekeza fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali tatizo hakuna ufuatiliaji. Kwa hiyo, naomba Serikali hata kama mnajikita kwenye sekta binafsi, sekta za afya, pamoja na elimu, inapopangiwa bajeti fulani basi implementation iongezwe kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala hilohilo la afya, Mkoa wangu wa Katavi ni almost kama miaka saba iliyopita mpaka leo tumepata Manispaa Serikali ilitoa pesa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa na kuna eneo kubwa karibuni heka mia tatu lilishanunuliwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo lakini mpaka sasa hakuna dalili yoyote ambayo inaonesha hospitali itajengwa lini. Pia wale wananchi ambao walikuwa wanakaa kwenye eneo ambalo Serikali ililinunua mpaka sasa wengi wao hawajalipwa. Naomba Serikali katika mpango wenu mhakikishe ujenzi wa hospitali katika mikoa au manispaa mbalimbali unafanyika lakini pia bajeti yake ipangwe na kuonyeshwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nilitaka kuzungumzia kuhusiana na ukusanyaji wa mapato. Tunapozungumzia ukusanyaji wa mapato kama Serikali ya CCM miaka yote tunalalamika lakini mchawi ni nani? Kuna watu ambao hawalipi kodi lakini Serikali imekaa kimya, miradi inashindwa kutekelezwa, tuna mipango mizuri lakini kodi tunapata wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge katika Bunge lililopita 2010, kulikuwa kuna kashfa ya sukari, kuna watu ambao walihusika na kutoa vibali vya Serikali na wengine wakaenda kununua sukari nchini Brazil kuleta Tanzania. Hasara tuliyopata kwenye kashfa ile ya sukari ni zaidi ya shilingi bilioni 300. Wengi wao wengine tunawafahamu kwa majina akiwepo Mheshimiwa Mohamed Dewji. Kwa hiyo, naomba kabisa ile ripoti ya Kamati ya Bunge iletwe hawa watu washughulikiwe na walipe kodi hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa kama hizi zinapotea kumbe tungeweza kufanya maendeleo kutokana na kodi hiyo. Kuna watu tunawaachia wanarandaranda na wanatumia pesa za wananchi. Kwa hiyo, naomba Serikali tuwe strict kuangalia ni mianya gani inayosababisha tunapoteza pato la Serilkali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaposema tunahitaji kuwekeza katika elimu basi tuwakumbuke Walimu wetu kwa kuwalipa mishahara yao lakini pia tutengeneze mazingira mazuri katika shule zetu. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, nahitaji kuchangia katika maeneo machache kutokana na udhaifu na nini kifanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusu matatizo ya elimu duni nchini na kufeli kwa wananfunzi hasa katika Mikoa inayofanya vibaya kama Mikoa ya Tanga, Tabora na Mikoa ya Kusini. Hii inasababishwa na Walimu kukosa makazi mazuri kwa ujumla na hivyo Walimu kukosa moyo wa kufundisha katika shule walizopangiwa hasa vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukosefu wa miundombinu hiyo na umbali mrefu kufika mjini. Mfano, Mkoa wa Katavi inamchukua Mwalimu muda mrefu kufika mjini kufuatilia madai yake kutoka kijijini mpaka mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madai ya Walimu, hili limekuwa ni tatizo kwa nchi nzima. Walimu wanachukua muda mrefu kulipwa madai yao, madeni ya nyuma na kadhalika. Hii imesababisha Walimu kupoteza muda mwingi wakiwa mijini kufuatilia madai yao na hivyo kushindwa kufundisha na muda wa kufundisha wanafunzi unapotea bila sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike? Naomba sasa Wizara iweke mipango kwa namna ya kusaidia Walimu hawa wasipoteze muda mrefu mijini kufuatilia madai yao na hivyo wajikite zaidi kufundisha wanafunzi hawa ambao wanasoma katika mazingira magumu. Uchache wa Walimu na Walimu kuishi katika mazingira magumu, hivyo Serikali sasa ihakikishe utekelezaji wa ujenzi wa nyumba za Walimu kwa wakati ili kuondoa usumbufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo la baadhi ya shule hasa vijijini kuendelea kuwanyanyapaa wanafunzi ambao wanakuwa wamepata mimba kwa bahati mbaya (mimba za utotoni) kutokana na mazingira ambayo wanafunzi hao wanatoka. Nini kifanyike? Serikali itoe agizo sasa ili wanafunzi hawa waliojifungua mashuleni, warudishwe waendelee na masomo na wasinyanyapaliwe. Pia Serikali iweke mpango mkakati wa kuhakikisha wanafunzi hao wanaonyonyesha wawe na darasa lao maalum ili wawe huru na wale wasionyonyesha wasije kuharibika kisaikolojia kutokana na kuchangamana nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa mabweni ya wanafunzi umekuwa ukisuasua na kusababisha wanafunzi kukosa huduma nzuri za malazi na hivyo wanafunzi kutokana na umbali kushindwa kuingia darasani (utoro) na kusababisha wanafunzi kufeli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Serikali iwape nguvu wananchi katika baadhi ya maeneo ambao tayari wananchi wamechangishana pesa kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na hivyo wameshindwa kumaliza. Sasa Serikali ione umuhimu sasa wa kuwasaidia wananchi maana wamebeba majukumu ya Serikali, isiwapuuze wananchi, imalizie majengo hayo (Mabweni) ili kunusuru wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya shule za binafsi zimekuwa zikitoza ada kubwa na kuwaumiza wananchi. Hivyo Serikali iangalie upya ada hizi katika shule binafsi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabla ya kuanza kuchangia napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai ambao amenipatia. Napenda niunge mkono hotuba ya Kambi ya Upinzani kwa asilimia mia moja. Kwa nini naunga mkono asilimia mia moja, kwa sababu hotuba ya Upinzani imeeleza uhalisia wa maisha ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma katika document zilizopita kila siku Wizara hii inapunguziwa bajeti. Abuja Declaration ambayo mlisaini mwaka 2001 lengo lake hasa ili kuwa ni ku-improve afya ya Watanzania. Ukisoma kwenye vitabu vyenu kuanzia TAMISEMI mpaka hii hotuba yenu ambayo mmei-present leo inaonyesha dhahiri kabisa kwamba hamjajipanga kwa sababu pesa mlizotenga ni ndogo.
Pia ukiangalia kwenye hii bajeti ya TAMISEMI inasema kwamba mlitenga shilingi bilioni 277 lakini kuna shilingi bilioni 518, jumla inakuwa ni shilingi bilioni 796. Sasa ukipiga kwa asilimia 100 ya shilingi trilioni 22 ambazo zimetengwa unapata ni asilimia 4.5. Shirika la Afya Duniani linasema kwamba mnatakiwa mfikishe asilimia 15. Sasa hii inaonyesha ni kiasi gani mme-fail kutekeleza hii Abuja Declaration, ingekuwa haina maana msingesaini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nataka nichangie kidogo kuhusiana na Wilaya ya Mpanda, Mkoa wa Katavi. Siwezi kuunga mkono hoja kwa sababu ni aibu kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuendelea kupunguza bajeti, lakini wananchi wetu wanaendelea kufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hospitali hii Mheshimiwa Waziri hakuna vitendea kazi lakini aibu nyingine inayoikumba Serikali ya Chama cha Mpinduzi ni kwamba hospitali nzima hakuna BP machine wala thermometer na oxygen machine ipo moja na inatumika kwa wodi sita, sasa hii ni aibu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie kuhusiana na masuala ya wazee. Wazee ni watu ambao wanateseka kwenye nchi hii lakini ukisoma kwenye hii hotuba ya Waziri haijaonyesha specifically mmetenga kiasi gani kwa ajili ya kutunza hawa wazee, mme-generalize tu yaani inaonekana kama hampo serious na hawa wazee. Naendelea kuwashangaa wazee kwa nini wanaendelea kukipa kura Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kwa sababu Halmashauri zetu zimeshindwa kukusanya mapato haya basi sasa zingeachiwa Manispaa kukusanya mapato. Inaonekana kabisa kwamba Wizara ya Afya mmeshindwa kuchukua jukumu lenu la kuwahudumia wazee ingawa mnasema kwamba Sera ya Wazee ni kuwahudumia bure kitu ambacho mnawadanganya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye Sera ya Afya. Ukisoma hotuba ya Waziri katika kata 3,990 kwa Tanzania nzima kata 484 ndizo ambazo zina vituo vya afya. Huu ni utani mnaoufanya kwa Watanzania wetu kwa sababu haiwezekani kuna difference ya kata 3,506 hazina vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye sera hii ya afya inasema vijiji kuwa na zahanati katika vijiji. Tuna vijiji zaidi ya 12,245, ukisoma kitabu cha Waziri wanasema tuna zahanati kwenye vijiji 4,502 tuna difference ya vijiji 8,043 hatuna zahanati na moja ikiwa ni Wilaya ya Mpanda pamoja na vijiji na kata zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia suala la afya ni kwamba tukidumisha afya za wananchi wataweza kufanya kazi, watajenga uchumi wao lakini siyo kuendelea kutupa porojo hizi ambazo mnatupa kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie suala la ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi imekuwa ni wimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisoma kitabu cha bajeti hapa mmesema kwamba mmetenga shilingi bilioni 1.8 lakini ni second time, mara ya kwanza Serikali ilitenga pesa wajanja wakapiga ile pesa wakaila.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni Serikali gani ambayo haipo serious zinatengwa pesa kwa ajili ya wananchi kujengewa hospitali yao lakini watu wachache wanachukua pesa wanakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sijui kama hizi pesa zipo theoretically au mnaingia sasa kwenye utekelezaji kwa ajili ya kuwajengea Hospitali ya Mkoa wananchi wa Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe masikitiko yangu na hii inawezekana tukaendelea kupiga kelele kumbe Serikali ya Chama cha Mapinduzi sasa imelemewa na mzigo. Ni Serikali gani ambayo kila kitu ninyi mna-set kwamba ni priorities kwenu? Afya, elimu, katiba, viwanda yaani kila kitu, lakini hatuoni utekelezaji. Mna documents nyingi sana mmeandika, ni theoretically! Sasa ingewezekana basi ingekuwa vizuri mka-set kitu kimoja baada ya kingine, kwamba tunaweka afya na mipango yetu ni moja, mbili, tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ajitahidi basi akatembelee hata Zimbabwe; kuna hospitali inaitwa Palalanyatu, ni hospitali iko Harare pale, ni kama Muhimbili. Huwezi kukuta hata takataka, huwezi kukuta inzi, lakini leo wanapoka magazeti, media, wanasema Muhimbili ina vitanda, huduma zimeboreshwa. Ni uongo na unafiki mtupu! Wakatembelee waangalie Zimbabwe wanafanya nini? Wakaangalie wenzao wanafanya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijamaliza, labda niseme, kutokana na upungufu wa vitendea kazi kwenye hospitali zetu hasa Mkoa wa Katavi, maana imefikia kipindi sasa hata wauguzi wetu ni wachache katika zahanati zetu katika hospitali. Nitoe masikitiko yangu kwamba wiki moja iliyopita nilipigiwa simu na ma-nurse kwamba vifaa baadhi ya hospitali vipo lakini wauguzi wetu hawana ule ujuzi wa kuweza kutumia vile vifaa. Sasa unashangaa vifaa vipo lakini mama mjamzito anapelekwa wodini ma-nurse wanashindwa kutumia vifaa vile. Wanakwambia tumtangulize mama wodini wakati tunamsubiri Daktari ili kuja kumtibu huyo mgonjwa. Sasa ni vitu ambavyo vinatia hasira. Kama mko serious... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, soko la nyimbo na muziki wa Tanzania linazidi kukua kwa kasi kwa sababu Watanzania wanapenda burudani, sanaa na kujifunza kupitia nyimbo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tatizo la wasanii wa Tanzania kutofanikiwa kiuchumi; wasanii wananyonywa sana, wasanii wanapata faida kidogo huku hawa wasambazaji wakineemeka kupitia wasanii wetu. Lakini pia gharama za kurekodi kazi za wasanii wetu, muziki wa audio na video kurekodi gharama ziko juu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali kusimamia hasa kwa wasanii wetu wapunguziwe gharama za kurekodi na kuzalisha kazi zao. Kuna wasanii wengi wanashindwa kuzalisha kazi zao kwa sababu kipato chao ni cha chini sana. Nini kifanyike? Kuanzisha studio ya Serikali ili kuendelea kuwainua wasanii wachanga wenye uwezo mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wizi wa kazi za wasanii, Mheshimiwa Waziri Serikali ina uwezo kabisa kuzuia wizi wa kazi za wasanii hasa kuweka password katika nyimbo zao, CD, DVD ili hawa wasambazaji wakose mwanya wa kuiba kazi za wasanii ambao wanazalisha kazi zao katika mazingira magumu sana. Mheshimiwa Waziri, leo kuna baadhi ya studio ziko hapa nchini kurekodi video moja mpaka shilingi milioni saba, Je, Serikali haioni haja ya kudhibiti gharama hizi na wasanii wetu wakaweza kustahimili hizi gharama na nini kifanyike? Serikali idhibiti, soko la muziki hasa kwa hawa wamiliki wa studio mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la usajili wa haki miliki ya msanii, mzunguko wa kupata haki miliki ya msanii umekuwa ni mrefu sana, pia mzunguko wa kupata sticker ili kazi itambulike na usajili wa TRA. Hivyo basi, ninaomba Serikali kupunguza mlolongo wa usajili na pia kuweka ofisi za usajili kila Mkoa ili kupunguza mzunguko wa kupata hizo sticker za TRA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwako Mheshimiwa Waziri ni kuwashauri pia wasanii hawa wafanye kazi kwa ushirikiano. Nyimbo zifuate utamaduni wa Kitanzania, wasanii wasijiingize kufanya kazi za kisanii na siasa hii inashusha muziki wetu awe CCM, CHADEMA au ACT, wasanii wetu kujiingiza katika siasa kunashusha soko la Tanzania hususani muziki. Mfano wa nchi ambazo wasanii walishuka hasa kwa kuchanganya siasa na kazi za sanaa ni Zimbabwe na Congo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu rushwa katika mchezo wa mpira wa miguu na netball, Mheshimiwa Waziri chunguza kwa makini suala hili ili timu zetu zifanikiwe bila dalili za rushwa. Ngoma za jadi na ngoma za asili zisisahaulike kwa mustakabali kwa kutunza, kuendelea na kukuza utamaduni wetu na siyo kuendelea kukuza muziki wa kizazi kipya pekee.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hotuba ya Wizara ya Utalii ambayo imesheheni mipango mizuri ya utalii nchini ili kuongeza Pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi halali na wawindaji nchini, kuhusiana na wavuvi ambao wapo katika maeneo yenye mito, maziwa, mabwawa na bahari, naomba hawa wavuvi leseni zao zichunguzwe upya maana kumekuwa na malalamiko mengi kwa wageni kuingia nchini kwa lengo la utalii na kumbe baadhi yao wanavuka mipaka ya kilichowapeleka katika maeneo ya utalii, hawana vibali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na matatizo mengi sana ya ujangili katika mbuga zetu. Serikali imejipangaje kuhusiana na kudhibiti hawa wawindaji halali wanaoingia kama watalii katika mbuga zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike, Serikali ichunguze ni namna gani ya kudhibiti hawa watalii na siyo kuwaacha peke yao mbugani. Wanafanya nini hasa maana tumeona ujangili mwingi umekuwa ukifanyika na wanaokamatwa wengi ni wageni. Hivyo, Serikali iongeze vitendea kazi kama magari kwa ajili ya kufanya patrol ndani ya mbuga zetu, kuwapa silaha zenye uwezo askari wa wanyamapori. Pia Serikali iboreshe maslahi ya askari wa wanyamapori ili wafanye kazi kwa moyo na kuwazuia kufanya biashara haramu (pembe za ndovu).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwekezaji ndani na mbuga, kumekuwa na malalamiko mengi kwa baadhi ya mbuga kwamba wawekezaji hawa wanaajiri watu wengi ambao ni wageni kutoka nchi jirani na maeneo kama Pakstani, Wahindi na Wazungu. Je, Serikali haioni kwamba kwa kuendelea kuwapa uhuru hawa wawekezaji kuajiri wageni zaidi kuliko wazawa ambao wapo wenye uwezo na elimu kuweza kuhudumia mfano hoteli zilizopo mbungani, customer services na madereva. Shughuli hizo wangeweza kufanya wazawa kwa wingi kuliko wageni wanaoletwa kuchukua fursa hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbuga ya Katavi ichungwe zaidi. Je, ni jinsi gani wawekezaji hawa wanasaidia wakazi wa vijiji vya jirani kwa huduma kama maji, zahanati, barabara na madawati? Wawekezaji hawa wanaingiza vipato vikubwa hivyo wanapaswa pia kusaidia jamii inayowazunguka katika mbuga hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanja vya ndege, kutokana na uhaba, ukosefu wa vifaa vya kisasa kama kamera katika viwanja vya ndege inachangia kutoroshwa kwa rasilimali zetu mfano ndovu, vyura na kadhalika. Hivyo, Serikali ihakikishe inawezesha upatikanaji wa vitendea kazi bora kama kamera, mashine za ukaguzi, x-ray na screening machine. Nini kifanyike? Ulinzi uongezwe zaidi hasa katika viwanja vya ndege ambavyo viko ndani ya hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia kwa waathirika wa Operesheni Tokomeza Serikali iangalie namna gani ya kufidia watu walioumizwa, kuibiwa na kupigwa. Mfano katika Mkoa wa Katavi, Wilaya ya Mpanda Vijijini, Kata za Isengule na Kapalamsenga, askari polisi walijeruhi watu ambao hata hawahusiki. Je, Serikali ina mpango gani wa kushughulikia suala hili?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Diplomasia ya Uchumi. Mheshimiwa Waziri pamoja na kusoma hotuba ya Wizara kuna mipango mingi mizuri hasa ya namna gani tunaweza kukuza uchumi wetu kupitia balozi zetu za nje ya nchi. Najielekeza katika balozi zetu hasa uendeshaji wa balozi zetu, Majengo (Pango), wafanyakazi katika Balozi, biashara zinazoweza kuingiza kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uendeshaji wa Balozi; kumekuwa na gharama kubwa za uendeshaji katika balozi zetu kutokana na Balozi nyingi kupanga majengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pango la ofisi; kutokana na kukosa majengo ya ofisi, Balozi zimekuwa zikipanga, kitu ambacho ni gharama kubwa ukizingatia Balozi nyingi hawapati bajeti ya kutosha ya uendeshaji na hivyo pesa nyingi zinaishia kulipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike? Ni muda sasa wa Serikali kujikita katika kuhakikisha Balozi zinapewa bajeti ya kutosha ili wamiliki majengo kama ofisi na hivyo kuondoa aibu wanayoipata sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kushindwa kulipa kodi Zimbabwe. Licha ya Balozi kwa sasa kumiliki nyumba kama ofisi lakini pia inamiliki baadhi ya biashara kama Tanzania Club. Watanzania hupangishwa au mtu mwenye vigezo kuweza kuendesha lakini sasa Serikali ihakikishe inasimamia miradi hiyo kwa sababu kumekuwa na ubadhirifu mkubwa wa mali za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa za ajira nje ya nchi; pamoja na Tanzania kuwa na fursa za kiuchumi tumeona tatizo la wageni kupewa fursa kirahisi rahisi tu, kitu ambacho ukienda nje ya Tanzania si rahisi kupata fursa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Work Permit; Serikali sasa ihakikishe inaweka sheria ambazo zitawabana wageni kutimiza vigezo vya uwekezaji na si kupata fursa za ajira kirahisi rahisi kama ilivyo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wamekuwa wakipoteza fursa za ajira huku wageni wakipewa kazi hizo. Zimbabwe si rahisi kupata work permit. Imefikia hatua Watanzania wamekaa kule zaidi ya miaka 10 lakini kupata work permit si kazi rahisi na hivyo Zimbabwe ni moja ya nchi ambayo inajipatia pesa kupitia wageni, hivyo Serikali ya Tanzania iwe mfano mzuri ili tukuze uchumi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haya mahusiano ya Kimataifa sasa yawe na msaada kwa ajira mbalimbali za maana, si zao wageni wakija Tanzania wanapewa fursa nzuri na kazi za ngazi ya juu huku Watanzania wakiajiriwa nje ya nchi wanapata kazi zisizo na msingi kama viwandani, kusafisha viwanja vya mipira, kulea wazee na kuwasafisha wazee. Ifike sehemu sasa Watanzania waheshimiwe kwa sababu wageni wakija Tanzania wanaheshimika na kupewa fursa zenye maslahi mazuri kwao na si kunyanyasika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, balozi zitafute fursa mbalimbali za kiuchumi kwa kufungua miradi mbalimbali kama vile maduka ya vitu vya asili ya Tanzania vitakavyouzwa katika balozi zetu na zisibweteke na kukosa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usalama wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi. Tanzania imekuwa kimya sana, Watanzania wanateswa na wananyanyaswa na kuuliwa lakini Serikali imekuwa ya upole bila kutoa matamko makali kama nchi. Mbona wageni wakija Tanzania wanaishi kwa usalama na Serikali inalinda diplomasia ya nje ya Tanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadhi ya balozi zetu ni mbaya katika maeneo yafuatayo:-
Mishahara ya wafanyakazi katika balozi zetu, ukarabati wa ofisi zetu, majengo mengi hayana hadhi ya Balozi za Tanzania na ukizingatia majengo ya balozi baadhi unakuta yako nje ya miji mbali na mjini.