Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Rhoda Edward Kunchela (4 total)

MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA (K.n.y. MHE. RHODA E. KUNCHELA) aliuliza:-
Kumekuwa na sintofahamu katika eneo la Kata ya Misunkumilo, Wilaya ya Mpanda Mjini, Wanajeshi wanadai eneo hilo ni la Jeshi, lakini makazi ya wananchi yalitangulia na wana hati ya maeneo yao:-
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutatua jambo hili ikiwa Jeshi limewakuta wananchi katika eneo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na sababu za kistratejia, JWTZ lilipewa eneo la Misunkumilo lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda mwaka 1985 lenye ukubwa wa hekta 3195. Serikali ililipa fidia kwa wananchi waliokuwepo katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1992 Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania lilihamisha kombania yake kutoka katika eneo hilo ila eneo alikabidhiwa Mkuu wa Wilaya kwa uangalizi. Kutokana na sababu za kiusalama hasa ukanda wa Ziwa Tanganyika, imebidi Jeshi lirejee kwenye sehemu hiyo tena. Hata hivyo, sehemu ya eneo hili sasa limevamiwa na kupangiwa matumizi mengine na uongozi wa Manispaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 16 Novemba, 2015 kilifanyika kikao cha pamoja kati ya JWTZ na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Katavi. Maamuzi yaliyofikiwa katika kikao hicho ni kulipima upya eneo hilo kwa kuzingatia maendeleo yaliyopo, lakini vile vile na mahitaji ya JWTZ.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi eneo hili litapungua kutoka ekari 3,195 za awali hadi 2,235. Zoezi la kupima upya litakuwa shirikishi na litatekelezwa mara fedha zitakapopatikana katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.
MHE. DEVOTHA M. MINJA (K.n.y MHE. RHODA E. KUNCHELA) aliuliza:-
Tatizo la umeme katika Mkoa wa Katavi hususan Wilaya ya Mpanda Mjini limekuwa kero kwa wananchi; tatizo hili linafanya maendeleo kuwa duni katika Manispaa ya Mpanda:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuachana na matumizi ya jenereta ambalo ni bovu linalosababisha ukosefu wa umeme kila mara?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua kero hii ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Gridi ya Taifa inayounganisha Mikoa ya Rukwa, Katavi pamoja na Kigoma. Ujenzi wa mradi huo utasaidia mikoa hiyo kuondokana na matumizi ya mitambo ya mafuta pia na gharama kubwa. Kwa maana hiyo ujenzi huo unahusisha njia ya umeme msongo wa kilovolti 400; ambao pia ambao pia wameanza kuunganisha katika mikoa Mbeya - Sumbawanga - Mpanda - Kigoma hadi Nyakanzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kuhuisha upembuzi yakinifu wa mradi kutoka kilovoti 220 za awali na kuwa kilovolti 400 zinazoendelea hivi sasa inaendelea. Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi (Mbeya - Sumbawanga) itakamilika mwaka, 2018 na awamu zote tatu za mradi zinatarajiwa kukamilika mwaka 2022; gharama za mradi huu zinakadiriwa kuwa dola za Marekani milioni 664.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu utakapokamilika utaupatia umeme wa uhakika Mji wa Mpanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ujenzi wa umeme wa Gridi ya Taifa unaendelea, Serikali kupitia TANESCO imeanza ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia jenereta mbili zenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 1.25; kila moja katika Mji wa Mpanda kupitia mradi wa ORIO. Mradi huu unafadhiliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Uholanzi kwa gharama ya shilingi bilioni 12.21. Kazi za ujenzi wa kituo hicho zimeanza mwezi Oktoba, 2016 na zitakamilika mwezi Julai, 2017.
MHE. RHODA E. KUNCHELA aliuliza:-
Ipo changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira kwa vijana wa Mkoa wa Katavi. Na hii ni kutokana na miundombinu mibovu inayosababisha wawekezaji kushindwa kuwekeza.
Je, Serikali ina mikakati gani ya kusaidia vijana hao wapate ajira na kuwa na mazingira ya kuwawezesha kujikwamua kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mikakati ya Serikali kusaidia vijana
wa Katavi pamoja na maeneo mengine kupata ajira na kuwa na mazingira wezeshi ya kujikwamua kiuchumi ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza ni kuzielekeza Mamlaka
za Serikali za Mitaa kuzingatia masuala ya ukuzaji ajira katika mipango ya maendeleo, hususan kutambua na kubaini mahitaji ya nguvu kazi katika maeneo husika. Kutenga na kuendeleza maeneo ya uzalishaji wa biashara kwa vijana, kuwezesha nguvu kazi kuwa na ujuzi wa kujiajiri, kuwezesha upatikanaji wa mitaji na vitendea kazi kwa makundi ya vijana, kukuza soko la bidhaa na huduma za wajasiriamali hasa vijana.
Mheshimiwa Spika, pili, kutekeleza programu ya miaka mitano ya kukuza ujuzi inayolenga kuwawezesha vijana takribani 4,419,074 kupata ujuzi wa kuajiriwa au kujiajiri katika sekta mbalimbali. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 vijana 1,469 wamepatiwa mafunzo ya ushonaji wa nguo kupitia viwanda vya Mazava Fabrics na Took Garment. Vijana 3,900 wametambuliwa na watapata mafunzo ya kurasimisha ujuzi wao kupitia VETA. Vijana 100 kati ya 1,001 wameanza mafunzo ya ujuzi kwa kutengeneza bidhaa za ngozi katika Chuo cha DIT, Mwanza.
Mheshimiwa Spika, tatu ni kuandaa na kuana kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Ajira kwa Vijana katika Sekta ya Kilimo (National Strategy for Youth Involvement in Agriculture) ambao unaweka mazingira wezeshi ya kuvutia vijana kujishughulisha na kilimo kwa kuwezesha upatikanaji wa ardhi, mitaji, pembejeo za kilimo, masoko, mafunzo ya ujuzi wa kilimo na ujasiriamali.
Mheshimiwa Spika, mikakati hiyo itasaidia pia kushirikisha vijana wote wa Tanzania, wakiwemo vijana wa Katavi kupata mazingira wezeshi ya kujikwamua kiuchumi. Aidha, Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya barabara inayounganisha mikoa yote nchini ikiwemo Mkoa wa Katavi kwa lengo la kuchochea uwekezaji na kukuza fursa za ajira nchini.
MHE. RHODA E. KUNCHELA aliuliza:-
Pamoja na lengo la Serikali kuhakikisha Manispaa zinakuwa safi na kuzuia magonjwa ya mlipuko, Manispaa ya Mpanda ina changamoto ya ukosefu wa vifaa kama magari ya taka.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Manispaa zinakuwa safi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Manispaa ya Mpanda ina maroli mawili kati ya manne yanayohitajika kwa ajili ya kuzolea taka ngumu. Kutokana na changamoto hiyo, uongozi wa Manispaa umejiwekea mikakati ifuatayo:-
(i) Manispaa ya Mpanda imebinafsisha (outsource) shughuli ya uzoaji na udhibiti wa taka kwa mzabuni anayelipwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri, mMzabuni huyu ana magari mawili na hivyo kufanya jumla ya magari kuwa manne.
(ii) Manispaa ya Mpanda imeanzisha mpango shirikishi jamii wenye jumla ya vikundi vya uzoaji na udhibiti wa taka ngumu katika mitaa 17, vimejengwa vizimba vitano kwa ajili ya kuhifadhia taka na vitakabidhiwa mikokoteni 17 tarehe 21/06/2017 siku ya uzinduzi.
(iii) Kila siku ya Jumamosi kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi wananchi wote hushiriki kufanya usafi katika maeneo ya makazi, biashara na maeneo mbalimbali ya kufanyia kazi.
(iv) Kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi usafi wa kina hufanyika ambapo wananchi pamoja na viongozi mbalimbali hushiriki kufanya usafi katika maeneo yao.
(v) Siku hiyo ya Ijumaa kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 3:30 asubuhi watumishi wa Manispaa hushiriki kufanya usafi katika maeneo ya Ofisi ya Manispaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuhamasisha usafi nchini ili kuepuka mlipuko wa magonjwa na kuongeza unadhifu wa miji yetu.