Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Risala Said Kabongo (8 total)

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini vilevile nilikuwa na maswali ya nyongeza.
Kwa kuwa Serikali kupitia mradi wa UNDP na USAID umepata Dola za Kimarekani 100,000 kwa ajili ya kufanya ukarabati mbalimbali kwa maeneo ya utalii; inaonekana kwamba Serikali imejipanga kukarabati uwanja wa Songwe, Katavi, Kigoma na Mpanda:-
Je, kwa kuwa mwaka 2009 Iringa iliteuliwa kuwa kitovu cha utalii, Serikali imejipangaje kuwekeza uwanja wa Nduli - Iringa ambao umekuwa na gharama kubwa sana za usafiri kuanzia Dola 180 mpaka Dola 200 kwa safari sawa na shilingi 400,000/= kutoka Iringa mpaka Dar es Salaam, Serikali imejipangaje kuwekeza katika uwanja huu? (Makofi)
Swali la pili; kwa kuwa Serikali imejipanga kuwekeza kwenye mahoteli, Serikali imejipangaje kutathmini viwango vya mahoteli ambavyo viko katika nchi hii, ukizingatia kwamba zoezi hili limefanyika baada ya uhuru; Mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Mikoa ya Manyara kwa kuweka madaraja ya nyota katika mahoteli? Ni eneo ambalo tunapoteza mapato sana na mahoteli mengi yanalipa kodi kutokulingana na nyota. Kwa mfano, hoteli ya nyota moja, nyota mbili, nyota tatu.
MHE. RISALA S. KABONGO: Je, Serikali imewekezaje katika upande huo?
Sambamba na hilo, Serikali imejipangaje kuboresha barabara ya kuelekea hifadhi ya Ruaha yenye kilomita 130 ambayo ina hali mbaya sana na kusababisha gharama za utalii kuwa kubwa katika Mikoa hii ya Nyanda za Juu Kusini hususan Hifadhi ya Ruaha ambayo ndiyo hifadhi kubwa kuliko zote Tanzania? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kuhusu namna ambavyo Serikali imejipanga kuweza kuboresha uwanja wa ndege wa Iringa kwa sababu ambazo nilizisoma na ambazo na yeye amezirudia.
Kwanza, ni nia ya Serikali kuendelea kufanya utalii kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa Taifa hili. Kwa sababu hiyo, ili tuweze kufikia lengo hilo, lolote linaloweza kufanya Serikali ikafanya vizuri zaidi kwenye Sekta ya Utalii ni kipaumbele katika Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, basi nilipotaja viwanja vya ndege na barabara na miundombinu mingine inayoboreshwa chini ya mradi huu ambao una ufadhili wa Dola milioni 100, huu ni mradi mmoja tu peke yake na jibu lililotolewa lilikusudia kujibu swali lililotolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema tu kwa ujumla, Serikali inajipanga zaidi kutafuta miradi mingine zaidi na kutafuta fedha zaidi ili kuweza kuboresha maeneo yote ambayo yatachangia katika kuboresha Sekta ya Utalii kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kutathmini viwango vya mahoteli, ameuliza swali ambalo sasa hivi liko mezani tayari na ninamshukuru Mbunge kwa mawazo haya mazuri ambayo yanaendana na jitihada za Serikali ambazo tayari zimekwishaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatutafanya tu zoezi la kupanga hoteli kwenye madaraja, bali pia ni nia ya Serikali kuhakikisha kwamba tunatoa elimu na kusimamia wawekezaji wa Kitanzania waweze kufikia viwango hivyo. Hoteli nyingi za sasa hivi zilizopo, hata kabla hujaenda kuzipa madaraja, nyingi zinahitaji kufanyiwa kazi ili ziweze ziboreshe huduma ili kuweza kuwafanya watalii waweze kujisikia kwamba wamekaa kwenye hoteli.
Kwa hiyo, kwanza tutaanza kutoa elimu na hapa nitoe wito, wote wanaokusudia kuwekeza kwenye eneo hili, waweze kuwasiliana na Idara ya Utalii kwenye Wizara hii, pale ambapo watahitaji; au wanaweza kupata utaalam kutoka mahali pengine, lakini wote tuwe na nia ya kuweza kuboresha huduma za hoteli ili wageni wanapokuja waweze kujisikia kwamba wako mahali penye sifa zinazotakiwa na viwango.
Kwa hiyo, tunakusudia kuanza hivi karibu kupanga hoteli zote katika madaraja katika Mikoa yote, siyo tu kwa ajili ya kuboresha mapato ya Serikali lakini pia katika kuwafanya watalii waweze kupata huduma zinazostahili.
MHE RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa, Naibu Spika nakushukuru. Nakushukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yako.
Kwa kuwa, mradi huu ni Mkubwa na ni wa miaka mitano; je, Serikali inavipa vipaumbele gani vijiji hivi vya Oldadai na Sokoni II na Ngilesi, kwa kuwa wamekuwa na kero kubwa na ya muda mrefu ya kupata maji?
Eneo la pili, nitaomba Mheshimiwa Waziri, atakapopata nafasi baada ya Bunge hili, aweze kutembelea maeneo haya na kujionea hali halisi katika vyanzo hivi ambavyo vinatunza maji yanayosaidia katika Mkoa wa Arusha. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ni kweli tumepata ufadhili wa mradi mkubwa ambao utekelezaji wake utachukua miaka mitatu. Jana tulikuwa na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, amekuja ofisini kwangu pamoja na Meya, pamoja na Mbunge na tumekubaliana kwamba, tutatengeneza mpango wa muda mfupi ili hivyo vijiji unavyovisema tuweze kuvitafutia angalau wapate maji wakati tunatekeleza huu mradi mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa kulikuwa na Mradi wa Vijiji Kumi, tumekubaliana kwamba Jiji la Arusha litakabidhi kwenye mamlaka yetu ya Arusha ili kusudi waweze kuunganisha kwenye mtandao baadhi ya maeneo ambayo Arusha hayapati maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana pia kwamba na mimi nitakuja kuangalia utekelezaji wa mpago huu. (Makofi)
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza, naitwa Risala Said Kabongo siyo Kabogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuendelea kukauka kwa Mto Ruaha Mkuu mwaka hadi mwaka kunasababisha athari za kimazingira na athari za kukua kwa utalii katika hifadhi hiyo, pamoja na athari kwa wananchi wanaoishi kando kando ya hifadhi hiyo.
Swali la kwanza, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Mto Ruaha Mkuu ambao ndiyo kiini cha hifadhi ya Ruaha unatiririsha maji yake mwaka mzima?
Swali langu la pili, je, Serikali itawasaidiaje wananchi wanaoishi kandokando ya bwawa la Mtera ambao uchumi wao unategemea uvuvi na kilimo kupitia mto huu wa Ruaha. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimwombe radhi kwa kutamka jina lake ndivyo sivyo, nimepokea masahihisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la mkakati, Serikali inao mkakati siyo kuhusu tu eneo la Bonde la Usangu na Mto Ruaha Mkuu, Serikali inao mradi mkubwa kabisa ambao unakusudia kuboresha shughuli za utalii kwenye eneo la Kusini, mradi ambao unatamkwa kwa kifupi re-grow yaani the Resilient Natural Resources Management for Growth.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi huo eneo la Bonde la Usangu ambalo linajumuisha Mto wa Ruaha ni sehemu ya mradi huu. Tunakwenda kuboresha mambo yote yanayohusiana na uhifadhi katika eneo hilo ili kuhakikisha kwamba eneo hilo lote sasa linakuwa na sifa endelevu ya kuwa na kila kitu kilichomo ndani yake katika hali ya uhifadhi unaotambulika Kimataifa na unaokubalika katika kuwezesha shughuli za utalii ziendelee kubaki kuwa bora zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, mradi huu ambao unatekelezwa chini ya Benki ya Dunia sasa hivi upo katika hatua za awali katika siku zijazo za usoni tutautolewa taarifa kuhusiana na jinsi ambavyo tutakuwa tunaendelea kuboresha eneo ambalo nimelitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wananchi wa Mtera inafanana na jibu nililojibu kwa ujumla kwamba mradi huo ninaoutaja ambao upo chini ya Benki ya Dunia unajumuisha mambo yote, yakiwemo kuhifadhi mito iliyomo ndani yake, kuhifadhi misitu iliyopo ndani yake, pia kuangalia maisha ya binadamu na shughuli zao katika eneo linalohusika kama wafugaji, wakulima na wengine wanaofanya shughuli nyingine zote watajumuishwa katika malengo makuu ya mradi huu na kwa hiyo maslahi yao yatazingatiwa Kitaifa katika mradi huo.
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa kuanza kunipatia maji
katika vijiji vyangu vya Udadai, Ngiresi na Sokontuu. Swali langu ni kwamba, kumekuwa na tatizo kubwa la wizi wa maji maeneo mbalimbali nchini. Mfano, katika Jiji la Arusha asilimia 40 ya maji yanaibiwa; je, Serikali imejipangaje kukabiliana na tatizo hili kubwa la wizi wa maji. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali tayari imefanikiwa kupata fedha zaidi ya dola milioni 210 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ajili kutekeleza mradi mkubwa wa maji katika Jiji la Arusha. Mradi huo unaanza kutekelezwa katika mwaka fedha wa 2016/2017, utakuwa ni mradi wa miaka mitatu baada ya mradi huo kukamilika, Jiji la Arusha litapata maji asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Jiji la Arusha lina upungufu mkubwa wa maji lakini juhudi mbalimbali zinafanyika katika hiki kipindi kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amezungumzia kuhusu upotevu wa maji, ni kweli upotevu wa maji upo kwa sababu miundombinu ambayo ipo ni ya zamani, kwa hiyo maji yanavuja na pili, hiyo element ya wizi nayo ipo. Mamlaka ya Maji ya Arusha inaendelea kufanya juhudi kupunguza upotevu wa maji na katika mradi unaokuja iko item ya kutekeleza hiyo kuhakikisha kwamba tunapunguza upotevu wa maji na tunatarajia kwamba upotevu utapungua mpaka kufika asilimia 30.
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Swali la kwanza, kwa kuwa vyanzo vya maji ya Mto Ruaha Mkuu vinatoka nje ya Bonde la Usangu katika Milima ya Chunya, Mbeya, Mufindi, Mpanga na Kitulo, je, Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kushirikisha wananchi katika kutunza vyanzo vya maji visiendelee kuharibika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Bwawa la Lugola ili kunusuru uhai wa Hifadhi ya Ruaha na Bwawa la Mtera na Kidatu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Risala amesema Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inashirikisha wananchi kwenye utunzaji wa vyanzo vya maji. Katika muundo wa Wizara ya Maji tunayo Idara maalum ambayo inashughulikia utunzaji wa rasilimali za maji.
Mheshimiwa Spika, katika hali hiyo tunashirikisha maeneo ya vijiji, tunaunda kamati ndogo ndogo kwenye maeneo husika ili ziweze kulinda vyanzo vile ambavyo vina manufaa na wao wenyewe. Kwa hiyo, tunafanya ushiriki kupitia kwenye Wilaya, Halmashauri, Mikoa pamoja na vijiji ili kushirikisha hao wananchi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu sasa ni lini tutajenga hili Bwawa la Lugoda, sasa hivi tumeshakamilisha usanifu. Sasa hivi Serikali inafanya juhudi ya kuwasiliana na wadau mbalimbali kwa ajili ya kupata fedha ili tuweze kujenga hili Bwawa la Ndembera ambalo litatunza maji na kipindi cha kiangazi maji yatafunguliwa kuhakikisha kwamba Ruaha Mkuu inatiririsha maji wakati wote.
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Barabara ya kutoka Mlowo - Mbozi kwenda Kamsamba - Momba haipitiki wakati wa mvua, je, ni lini Serikali itatengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami ili kuweza kusaidia uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, yale ambayo tumeshayasema kabla ni ya kweli na tutayatekeleza. Tulichokiahidi, kitu cha kwanza ni kukamilisha daraja, tukishamaliza kukamilisha daraja tutashughulikia hii barabara katika kiwango cha lami. Tupeni fursa, hizo pesa ambazo tumezitenga kwa ajili ya daraja kwanza tukamilishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika, maadam tunatenga fedha za utengenezaji wa hii barabara kuhakikisha inapitika karibu muda wote, naomba tupeni fursa tutekeleze kwa namna tulivyopanga.
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nimesikia majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika Hospitali ya Vwawa ni kubwa, out patient tu wanaotibiwa pale ni 150 mpaka 200 kwa siku. Je, Serikali kwa nini isijenge jengo kubwa la OPD ili kuweza kukidhi mahitaji ya wagonjwa wanaopata huduma kwa sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, idadi ya wanawake wanaojifungua katika Hospitali ya Vwawa ni kuanzia 15 mpaka 20 kwa siku, huku vifo vya watoto kuanzia sifuri mpaka miezi 28 ni 180 kwa takwimu za2015. Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuongeza Madaktari, Wauguzi na vifaa tiba ili kupunguza vifo vya akina mama na watoto katika Hospitali ya Vwawa na pia kupunguza vifo vya wananchi katika Mkoa wetu wa Songwe? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la msingi la Mheshimiwa Risala aliongelea suala zima la kuwa na Hospitali ya Rufaa na katika majibu ambayo tumetoa tunamhakikishia na taratibu za ujenzi zimeshaanza na pesa imeshapelekwa. Sasa katika swali lake la nyongeza anarudi tena katika ile hospitali ambayo tumesema kwamba itaendelea kuwa Hospitali ya Wilaya na kwa sasa hivi inatumika temporarily kama Hospitali ya Rufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge, ni vizuri tuchague njia moja ya kupita, hatuwezi kuwa na mawili kwa wakati mmoja. Jitihada ambazo zinafanyika na Serikali za kuhakikisha kwamba inajengwa Hospitali ya Rufaa ikizingatia ramani ya Hospitali ya Rufaa ni vizuri tukaiheshimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili anaongelea juu ya suala zima la vifo vya watoto na akina mama kutokana na upungufu wa madaktari. Naomba nimhakikishie na yeye alikuwepo wakati Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Utumishi akiwa anatoa takwimu juu ya tarajio la Serikali la kupata vibali kwa ajili ya kuajiri watumishi wa sekta ya afya na elimu, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba tunaajiri watumishi wa kutosha ili kupunguza vifo vya mama na mtoto. (Makofi)
MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa wamiliki wengi wa hoteli za kitalii wanatumia wanafunzi waliopo kwenye mafunzo ya vitendo kufanya kazi za kuhudumia watalii na baada ya muda huo hawaajiriwi. Mchezo huu unasababisha ukosefu wa ajira kwa wahitimu kwa muda mrefu na kuikosesha Serikali mapato. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua taizo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza yeye mwenyewe ni mhifadhi mzuri sana, kwa hiyo nampongeza sana kwa kuwa mhifadhi mzuri na naamini atatumia taaluma yake vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kwamba, hoteli nyingi zimekuwa kweli zinawapokea vijana wanaotoka katika vyuo mbalimbali kwa ajili ya kupata field yaani kupata uzoefu ili waweze kwenda kuajirika katika maeneo mbalimbali. Hii ni hatua nzuri. Kwa hiyo, nafikiri hii ni ya kui- encourage zaidi ili kusudi hoteli nyingi zipokee hao vijana wetu, wafundishwe namna ya kufanya kazi kwa vitendo ili wanapoajiriwa pale waweze kutumia taaluma zao vizuri na waweze kufanya kazi ya kutoa huduma ile ambayo inastahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, kuhusu ajira, ni kwamba tutaendelea kuhamasisha wawekezaji na hoteli mbalimbali ili ziweze kuwapokea vijana wetu ambao wamehitimu katika vyuo mbalimbali ili waweze kuajiriwa na waweze kutoa ile huduma nzuri. Pamoja na yale majibu ambayo Mheshimiwa Waziri ameshayatoa, basi jitihada hizi tunaamini kabisa kwamba zitasaidia sana katika kuboresha suala la ajira hapa nchini. (Makofi)