Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Sabreena Hamza Sungura (5 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa dakika chache nilizopata, lakini namwomba Mwenyezi Mungu niweze kuzitendea vyema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu napenda kujielekeza kwenye suala zima la usafirishaji wa binadamu ambao ni Watanzania kwenda nchi za nje kufanya kazi na wengi wao wamekuwa wakiuawa na clips zinatumwa hapa nchini, zinazagaa kwenye mitandao ya kijamii, sisi kama Wabunge tunaona, Serikali imekaa kimya haisemi jambo lolote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii ni hatari kwa sababu hawa wanaofanya biashara hii ya kusafirisha binadamu kwa maana ya human trafficking na kuwapeleka huko wanakwenda kuuawa kinyama, kwa nini Serikali haifanyi msako maalum wa kuhakikisha inawakamata? Vijana wetu tena vijana wa kike wanakwenda huko wanafanyiwa unyama lakini Serikali imekaa kimya. Tunataka tamko leo litoke, ni hatua gani zimechukuliwa kubainisha watu wanaosafirisha wasichana wa Kitanzania bila ridhaa ama kwa ridhaa lakini kwa udanganyifu. Wanakwenda kwa wazazi wanawahonga dola 200, 300 wanawaambia kijana wako anakwenda huko atafanya kazi nzuri supermarket, wapi, akifika kule anadhalilika anauawa, Serikali inasemaji juu ya hili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni conflict of laws. Nchi yetu ina tabaka za watu mbalimbali, kuna mila na desturi mbalimbali. Sheria zetu zimeingia kwenye mgongano, tuna Sheria ya Mirathi lakini pia tuna Sheria ya Ndoa, tunayo Islamic Restatement Act lakini pia tunayo Sheria ya Kimila ambayo ni Customary Declaration Order ya mwaka 1963.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi sheria zinakinzana, kuna sheria ambayo inamtambua mtoto ni kuanzia umri wa miaka 21 lakini kuna sheria inayosema mtoto mwisho wake itakuwa ni miaka 18, lakini kuna sheria za Kiislamu zinazosema mtoto mwisho wake ni pale anapobalehe. Sasa linapokuja suala la mtoto aolewe ama aozeshwe kwenye umri gani ama aoe kwenye umri gani kuna mwingiliano wa mila, desturi, dini na sheria. Je, mambo haya tunakwenda nayo vipi? Ni lazima mijadala ya kina ifanyike ili kuhakikisha kwamba pande zote zinabaki bila dukuduku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siungi mkono ndoa za utotoni, naunga mkono wanaopendekeza watoto waolewe kuanzia umri wa miaka 18. Hata hivyo, kuna watoto ambao na wenyewe wanaingia kwenye mapenzi kabla ya umri suala ambalo linapelekea ubebaji wa mimba. Sasa mtoto yule alivyopata mimba kwenye umri wa miaka 13, 14 ni mzazi gani atakayekubali kuona mtoto wake mwenye umri huo mdogo anakaa nyumbani na anazalishwa, hapohapo sheria zetu haziwaruhusu watoto hao kuendelea na shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukubaliane, kama tutaamua mtoto aanzie umri wa miaka 18 aweze kuoa na kuolewa, je, mtoto anayepata ujauzito kabla ya miaka hiyo status yake itakuwaje? Kama tutakubaliana miaka 18 basi kuwe kuna exception, kama atapewa ujauzito kabla ya hapo aruhusiwe kuozeshwa kwa sababu kuna watu ambao mila zao kukaa na binti nyumbani mama yake mzazi anapata ujauzito na mtoto anapata ujauzito ni matusi. Naomba hili lifanyiwe kazi kwa namna ya kipekee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuzungumzia suala moja, tunayo Sheria ya Probate and Administration of Estate Act ya Tanzania ambayo inaunda Waqf Commission. Wenzetu wa Zanzibar tayari wana Waqf Commission na watu ambao wanataka mali zao zigawanywe kwa mtindo huo wanakwenda kwenye Waqf Commission wanapeleka mapendekezo yao na yanafanyiwa kazi. Kwa upande wetu wa Tanzania Bara tume hii ipo kwenye sheria lakini haijawahi kuundwa toka uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, ni lini Serikali itaunda Waqf Commission kwa upande wa Tanzania Bara ili wale ambao wanajisikia kupeleka mali zao pale ambazo zitakuja kusaidia vizazi vinavyokuja basi waweze kuzingatiwa na waweze kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa hili ni nini? BAKWATA imekuwa na malalamiko mengi sana, watu wengi hapa nchini hawana imani na BAKWATA hususan Waislam wengi hawana imani na BAKWATA. BAKWATA wanauza mali za Waislam, BAKWATA wanaingia kwenye migogoro wamewauzia akina Yussuf Manji mali za Waislam, kesi, vita, ngumi kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini sasa msitengeneze hii Waqf Commission ambayo itatoa sasa mali hizi ambazo zinawekwa kwenye mikono ya watu ambao kwa kiasi fulani hawaaminiki ziweze kuwa kwenye mfumo wa Serikali ili…
T A A R I F A....
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namsikitikia sana Mbunge mwenzangu aliyesimama, kama ni Mtanzania ambaye anafuatilia vyombo vya habari na anafuatilia habari za kila siku katika nchi hii hawezi kuhoji BAKWATA kwamba haikubaliki na kundi kubwa la Waislam Tanzania. Kwa hiyo, hilo ni jibu ambalo linamtosha kama halijatosha aje nitampa research na mifano ya kesi ambazo BAKWATA wameuza mali za Waislam, kitu ambacho kinapelekea vita nchi hii.
Kwa hiyo, napendekeza kabisa kwamba Waqf Commission iundwe kama ilivyo Zanzibar ili hawa waporaji ambao wamejificha kwa mgongo wa BAKWATA suala hilo liweze kwisha na lipatiwe muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kugusia suala zima la migogoro ya kazi katika chombo chetu cha Commission of Mediation and Arbitration. Chombo kile tumekianzisha ili kiweze kupunguza mrundikano wa kesi za labour hususan katika mahakama zetu kuu. Hata hivyo, nasikitika kusema kwamba, majengo yake hayatoshi ku- accommodate wateja wanaokwenda pale. Ukienda pale unakuta makundi ya watu yamekaa kwenye vyumba vidogovidogo, kelele, hata wale wanaosikiliza mashauri hawawezi kuelewana, joto, giza, mrundikano wa watu, mpaka watu wengine wanafanya kupangiwa …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia muswada huu ambao toka nchi imepata uhuru ulikuwa haujaletwa na kusababisha usumbufu mkubwa kwa Watanzania na wapenda mabadiliko kwa ujumla. Ukiangalia muswada huu una lengo zuri, lakini una matatizo makubwa kwenye uteuzi wa Mthamini Mkuu wa kufanya uthamini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia hapa tumesema miaka yote kwamba, Mheshimiwa Rais amekuwa akilundikiwa vyeo kila mara, lakini katika Muswada huu bado tunasema kwamba, mthamnini huyu uteuzi wake utafanyika na mamlaka ile ile, hapa kuna tatizo. Mthamini Mkuu ni lazima angepatikana kwa sifa, watu mbalimbali waliopo Serikalini na walioko nje ya Serikali wapeleke sifa zao ili ziweze kuangaliwa, wachujwe, wafanyiwe interview na hivyo apatikane Mthamini Mkuu ambaye atakuwa na tija na hatakuwa na upendeleo kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi! Mthamini Mkuu anapochaguliwa na mamlaka ambayo iko Serikalini, kesho anaambiwa akafanye uthamini katika mali za Serikali, lazima huyu mtu atakuwa biased, lakini kama atateuliwa na mamlaka nyingine tofauti na Serikali ileile ambayo anaenda kuifanyia kazi, ataweza kufanya kazi yake kwa uhuru zaidi na hivyo hatakuwa na conflict of interest.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia suala zima la Muswada huu, ukija kwenye majukumu ya Mthamini Mkuu wa Serikali, tumeona hapa kifungu cha 6(1)(a), atakuwa na kazi ya kuishauri Serikali kwenye masuala yanayohusu shughuli za uthamini ikiwemo uuzwaji wa mali za Serikali na ununuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kupendekeza kwa kuwa, kumekuwa na tabia ya wanasiasa akiwemo Mheshimiwa Rais, Mawaziri na viongozi wengine Serikalini kwenda katika Halmashauri mbalimbali nchini na kuwahamisha wananchi wa maeneo hayo kwa sababu za kisiasa bila kupata ripoti ya tathmini ya awali kwamba nani atalipa gharama za fidia ya wananchi hao, ningependa muswada huu uwaonye na uwakanye wanasiasa wenye tabia hizo kwa sababu mmekuwa mnasababisha sintofahamu kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano namba moja; alikuja Mheshimiwa Rais wa Awamu iliyopita katika Manispaa ya Kigoma Ujiji akawazuwia wananchi wanaoishi katika maeneo ya mlima unao-face railway station kwamba wanatakiwa wahame kutokana na sababu za kijiografia. Ni zaidi ya miaka kumi mpaka leo hii anatafutwa mtu wa kulipa fidia hapatikani. Halmashauri wanaulizwa, wanasema fidia ile imekuwa ni kiwango kikubwa zaidi ya bilioni moja, hawana uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hamuoni kwamba tabia hizi za wanasiasa kwenda kutamka matamshi ambayo wanajua Serikali haiwezi kutekeleza ni kuwapa usumbufu wananchi wetu? Kwa hiyo, sheria hii i-declare kwamba wanasiasa na viongozi wengine wa Serikalini msiwe na mamlaka ya kwenda kuhamisha ama kusitisha shughuli za wananchi, shughuli za maendeleo pale ambapo Wathamini ambao mnawatungua sheria leo hii hawajafanya thamani halisi ya eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba vijana wetu ambao wana uwezo mzuri watashindwa kupata ajira kwa sababu tu watashindwa ku-meet hii condition ya umri. Hivyo basi, ili liendane sambamba na lile suala zima la miaka mitatu, tunasema kwamba tutakuwa na wasajili wa mpito na wasajili wa muda pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wasajili hawa tunawaambia wawe na experience ya miaka mitatu, lakini tujaribu kuangalia taasisi nyingine, kwa sababu siyo kwamba Wathamini hawa ndio wawekewe miaka mitatu lakini tunao Wahandisi ambao wanawekewa experience ya one year, wakitoka hapo wanapewa certificate waananza ku-practice. Tunao wanasheria ambao wanapewa elimu ya mafunzo kwa kipindi cha miezi nane mpaka mwaka mmoja; wakimaliza hapo wanapewa muhuri wanakwenda kufanya kazi. Kwa nini kwa Wathamini mweke kikomo cha miaka mitatu? Hii siyo fair, tupunguze kikomo hiki tuweze kupata muda ambao ni wa mwaka mmoja wafanye mafunzo ya vitendo na hivyo wataweza kujiajiri na kupunguza tatizo la ajira nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napendekeza makampuni na biashara ziwe zinafanya uthamini kila mwaka kama zinavyofanya Halmashauri zetu na Manispaa zetu mbalimbali. Tumeona mwaka 2015 Manispaa ambazo hazikufanya uthamini wa mali zake walipatiwa hati chafu, basi ni vyema makampuni na mashirika na taasisi zilizo za Umma ziweze kuwa zinafanyiwa tathmini kila mwaka ili tuweze kupanua wigo wa mapato katika nchi yetu na kuhakikisha kwamba miradi inayopangwa na Serikali inafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika muswada huu sijaona mkazo ukitiliwa kwa wazawa. Tumeona kuna hawa Wathamini wa mpito na wa muda mfupi wakiwemo na wageni. Kwa nini tunakumbatia wageni kwa condition ambazo ni rahisi sana? Tunapoingiza watu wengi waweze kusajiliwa hapa nchini kupitia Bodi yetu ya Wathamini inamaanisha kwamba kuna ajira nyingine Wathamini wetu wa Serikali ama binafsi ambao ni wazawa watazikosa na nafasi hizi zitakwenda kwa wageni. Lazima tuweke utaratibu ambao utawabana wageni waweze kuachia nafasi hizi kwa wazawa na kazi hii iweze kufanyika kwa viwango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutengeneza soko la ajira, ni vyema basi mabenki yetu na taasisi za fedha ziwe na wathamini wenye sifa kwa ajili ya kuangalia thamani ya wakopaji na isiwe ni suala la short time pale ambapo mkopaji anaenda benki ndiyo mthamini anatafutwa kufanya thamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema katika sheria hii basi tuweke kifungu ambacho kitasababisha taasisi zote za fedha, mabenki na mashirika mengine ya Kiserikali yawe na utaratibu wa kuwa na wathamini wao binafsi pale ambapo wateja mbalimbali watahitaji kwenda kukopa. Pia kuna Mashirika kama ya Bima, wenyewe wana loss assessors. Napendekeza kwamba hawa loss assessors wa Mashirika ya Bima basi nao wangekuwa wathamini ili pale inapotokea loss thamani halisi ya fidia ijulikane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kuchangia kwenye muswada huu ni kuhakikisha kwamba ili kufanya uthamini uliokuwa na tija hususan Serikalini, tumeona hapa awamu iliyopita ya Mheshimiwa Mzee Mkapa, nyumba za Serikali ziliuzwa kwa bei ya chini sana na Taifa likapata hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti kuna nyumba ambazo ziliuzwa mpaka shilingi milioni mbili, mpaka shilingi milioni 10; lakini ukiangalia hali halisi, nyumba hizi zilitakiwa ziuzwe kwa gharama ya juu zaidi. Je, ni vipi sasa sheria yetu hii tunayoitunga leo itawadhibiti watu ambao wataliingizia Taifa hili hasara kama iliyotokea miaka michache huko nyuma na kufanya wafanyakazi wetu wa mashirika mbalimbali na wafanyakazi wetu wa Serikalini kukaa mbali na miji kwa sababu tu nyumba za Serikali ziliuzwa tena kwa bei ya kutupa ama bei ya bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema basi sheria hii iweke msisitizo na iweke mkazo wa kuhakikisha ni jinsi gani basi Wathamini wa Serikali watatenda kazi kutokana na hali halisi ya soko na siyo kulitilia Taifa hasara kama ilivyokuwa ikifanyika siku za nyuma.
Pia napenda niseme kwamba lazima tuwe na appellate jurisdiction. Mthamini Mkuu wa Serikali amefanya uthamini, labda mtu aliyefanyiwa uthamini, aidha, wananchi ama shirika ama taasisi yoyote haikuridhika na uthamini uliofanywa na Mthamini Mkuu wa Serikali, taasisi hiyo au mtu huyo ama wananchi hao wanakwenda ku-appeal wapi juu ya maamuzi yaliyofanyika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kumwambia Mheshimiwa Waziri hapa mwaka 2015 katika uchangiaji wangu, nilimwambia kwamba kuna maeneo ambayo watu walifanyiwa uthamini. Mtu alihitaji kulipwa shilingi milioni 20, 30 mpaka 40 lakini alilipwa shilingi milioni mbili, tatu, nne, mpaka tano na kuna watu ambao walitumia fursa hiyo kuwahonga Wathamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ambaye alitakiwa alipwe fidia ya shilingi milioni 10 aliweza kulipwa mpaka shilingi milioni 60. Je, ni hatua gani za makusudi mnazoziweka kuhakikisha kwamba udanganyifu katika uthamini mnaudhibiti hivyo fidia ya haki stahiki iweze kulipwa kwa wananchi wetu na isiwe longolongo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mtu ambaye atakayesababisha mtu kupata fidia chini ya kiwango hatua kali ziweze kuchukuliwa chini ya sheria hii, aidha, iwe kufungwa miaka 10 mpaka miaka 20 kwa sababu watu hawa wanaliletea Taifa hasara na wanawatia umaskini Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Wizara ya Viwanda na Biashara. Kwa kuwa ni mchango wangu wa kwanza napenda kutoa shukurani za dhati kwa chama changu kwa kunirudisha Bungeni kwa awamu nyingine ya pili, ahsanteni sana ninawaahidi ukombozi mpaka pale nchi yetu kitakapoeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili; napenda kuchukua fursa hii kulaani vitendo vya kikatili na udhalilishaji vinavyofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi vya kupiga, kudhalilisha na kuburuza Wabunge ndani ya jengo takatifu, jengo linalotunga sheria, jengo linalofanya maamuzi katika nchi hii. Ni kitendo cha udhalili na ni laana kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye suala zima la viwanda na biashara. Kinachoendelea humu ndani ni maigizo. Ni ndoto za alinacha kusema mtafanya mapinduzi ya viwanda na biashara ilhali zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania hawana umeme, hawana maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi ni Mkoa wangu wa Kigoma, Mkoa ambao tunapata umeme kwa kutumia jenereta ambazo haziwezi ku-run heavy industry. Kwa hiyo tukisema tutaanzisha viwanda, alipita Mheshimiwa Rais Magufuli kwenye kampeni akasema kwamba atahakikisha Dangote anakuja kufungua kiwanda cha cement Mkoa wa Kigoma, swali langu ni kwamba kiwanda hicho kitafunguliwa kwa umeme upi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma hauna barabara za maana kwa maana ya barabara za kupitika. Leo hii naongea kuna wananchi walikwama zaidi ya saa 48 njiani kwa ubovu wa barabara. Mkoa hauna reli yenye standard gauge, mvua zikinyesha inakuwa ni shida. Mkoa hauna ndege za uhakika, Mkoa hauna boti ama meli za kisasa ambazo zitatusaidia kupeleka bidhaa mbalimbali katika nchi nne ambazo zinaungana na Mkoa wetu wa Kigoma. Ni viwanda gani hivyo mtakavyoleta kujenga, nchi imejaa urasimu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisikia Mheshimiwa Rais anasema kwamba kuna mishahara hewa, lakini nafikiri hajapewa information za kutosha, siyo tu mishahara hewa kuna fidia hewa nchi hii. Nimeshuhudia baadhi ya wananchi maeneo mbalimbali wakilipwa fidia hewa, mtu anahonga shilingi milioni 10 anapewa milioni 60. Sasa kama kuna fidia hewa hakuna kiwanda kitakachojengwa katika mazingira hayo, mnajidanganya na Serikali inajua kama fidia hewa zipo lakini kwa kuwa ni miradi yenu hamchukui hatua zozote za kudhibiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni kuhusu mitaji. Ni wajibu wa Serikali kuwawezesha wananchi wake kupata mitaji ya kuendeleza viwanda vidogo, viwanda vya kati na viwanda vikubwa. Mheshimiwa aliyemaliza kuongea hapa, amezungumzia matusi ambayo amepata mwekezaji wa ndani, mzalendo ndugu yetu Mengi. Lakini juzi juzi tumesikia Bakhresa naye akiambiwa kwamba ni mkwepa kodi, unaweza kukuta uhuni ule umefanya na management ya watu wachache tu katika kiwanda kile. Sasa nasema ni wakati muafaka wa Serikali kuweza kuwapongeza na kuwashikilia wawekezaji wa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu kama Ndugu Mengi, mtu kama Ndugu Bakhresa na familia zao, rasilimali walizonazo wakisema waweke kwenye fixed deposit kwa mwaka fedha, watakayopata matatizo yao na familia zao wanamaliza, lakini wanawekeza kwa niaba ya Watanzania. Please Watanzania wanaojitokeza kwenye uwekezaji, Serikali iwaunge mkono. Kwanza kwa kutoa ardhi, pili kwa kutoa sheria zozote ambazo ni kandamizi kwao, lakini tatu kwa kumaliza migogoro ya fidia kwa wananchi mbalimbali na nne kuhakikisha kwamba mnawapa ruzuku. Serikali isiwe kikwazo kwa wawekezaji katika sekta ya viwanda, biashara na uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, napenda kuzungumzia zao la mchikichi. Mkoa wa Kigoma nilizungumzia hapa miaka 40 iliyopita tuliwapa mbegu nchi ya Malaysia, Malaysia sasa hivi inafanya vizuri kwenye zao hili kutokana na kuliendeleza. Ajabu na aibu ya Tanzania, zao hili halijafanyiwa utafiti, zao hili halina bodi wala Serikali hamna mpango madhubuti wa kuendeleza zao la mchikichi. Tunaiomba Serikali ituambie ni lini mtawekeza nguvu za kutosha kwenye zao hili kwa sababu zao hili linazalisha bidhaa zaidi ya 20 ndani ya zao moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache naweza nikataja mafuta ya mawese, naweza nikataja mafuta ya mise, zao hili linazalisha sabuni, zao hili linazalisha chelewa, zao hili linazalisha majani ambayo yanafunikia mapaa katika nyumba zetu, lakini zao hili linazalisha makafi ambayo tunatumia kama nishati ya kupikia. Serikali ya Chama cha Mapinduzi miaka 54 ya Uhuru haijaona umuhimu wa zao hili na kuweza kuliendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nilizungumzia kuhusu bandari. Kulikuwa kuna kelele za sukari, imefikia mpaka shilingi 3,000, shilingi 3,500, shilingi 4,000 mpaka shilingi 5,000 baadhi ya maeneo, lakini wakati Serikali imelala hapa Dodoma, sukari mbovu inapitishwa kwenye mwambao kuanzia Pangani mpaka maeneo ya Mbweni kule Dar es Salaam. Bandari bubu zimejaa, Serikali inajua, watu wanakusanya kodi, Jeshi la Polisi liko pale, Serikali haipati mapato. Hii ni Serikali inafanya kazi kwa utashi ama ni Serikali inafanya kazi kama panya road? Lazima muamke, lazima muwe makini, fedha za nchi zinapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Tanzania sasa hivi wengi ukienda hospitalini figo zinafeli kwa sababu ya kutumia sukari za KK.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wanaotengeneza juice na vijana na akina baba, kijiko kimoja cha sukari kinahudumia ndoo mbili za lita 20. Wananchi wanafeli figo na wakienda katika hospitali yetu ya Taifa Muhimbili hakuna matibabu wanayopata ya ziada. Napenda kusema kwa kusikitika niliwahi kukutana na mgonjwa mmoja ambaye figo zake zimefeli na sababu kubwa ikiwa ni hizi juice ambazo zinaungwa KK. Mgonjwa yule figo zimefeli kwa sababu ya sukari hizi lakini kilichotokea gharama za matibabu zimekuwa ni kubwa akawaomba wauguzi arudi nyumbani nikapumzike nisubiri kuonana na muumba wangu kwa sababu siwezi kukidhi gharama hizi za matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mnaweza mkaona kwamba sekta hii inaathiri vipi sekta nyingine. Mnaingiza sukari mbovu, Serikali mmelala, mnashindwa kuziba mipaka ya nchi, bidhaa mbovu zinaingizwa, Watanzania wanakufa, mnajiita Serikali ya hapa kazi tu. Mimi nawaita Serikali ya hapa kuchoka tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni suala la uvuvi. Mkoa wa Kigoma tuna Ziwa Tanganyika na takwimu tu toka mwaka 2003 mpaka 2014 zaidi ya nyavu na mashine za bilioni sita zimeibiwa katika Ziwa Tanganyika. Lakini kama Serikali ingekuwa makini kudhibiti wizi huu basi ni imani yangu tungeweza kuvua samaki wa kutosha na tungeweza kutengenezewa viwanda vya kusindika samaki hivyo tungeweza kuuza samaki ndani na nje ya nchi. Sioni mkakati wowote wa viwanda vya kusindika samaki katika Ziwa Tanganyika. Tunaomba Waziri ukija kuhitimisha utuambie ni kwa kiasi gani utawekeza kwenye viwanda hivi ili vijana wa Mkoa wa Kigoma waweze kuajiriwa katika sekta hii ambayo ni muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna viwanda kama viwanda vya chumvi. Hivi ni viwanda ambavyo havijapewa kipaumbele kabisa. Ukiangalia Bagamoyo kuna chumvi inatengenezwa, ukiangalia Uvinza kule Kigoma kuna chumvi ambayo ilikuwa inatengenezwa, lakini Mtwara na kwenyewe walikuwa wanatengeneza chumvi, Serikali hatujaona hata siku moja mkitoa hata ruzuku ya madini joto kusaidia suala zima la chumvi. Kila mtu anayekuja hapa ni sukari, sukari, sukari, How about chumvi? Kwa nini mmesahau? Ama hamuoni kama Watanzania watakosa madini yenye chumvi yanaweza na yenyewe yakaathiri afya zao. Ningependa mtuambie mkakati gani wa kusaidia watu wanaosindika chumvi ili mambo yaweze kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ningependa kuzungumzia kuhusiana na suala zima la uwekezaji. Ukiangalia katika sekta ya uwekezaji maeneo mengi matumizi ya Taasisi na Mashirika ya Serikali, matumizi yamekuwa ni makubwa kuliko bajeti ya maendeleo. Huu ni udhaifu wa Serikali. Ukiangalia Taasisi nyingi hazina bodi, bodi zimeisha muda wake, TR ameikumbusha Serikali kwamba kunatakiwa kuundwe bodi mpya lakini Serikali bado imelala. Je, mna dhamira ya dhati ya hapa kazi tu ama mnaendelea kufanya mazingaombwe kwa Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaomba Mawaziri mnapokaa kwenye mabaraza yenu mumkumbushe Mheshimiwa Rais aunde bodi mbalimbali ziweze kusaidia kilimo katika nchi hii. Ninashukuru.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. SABREEN H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo:-
Kumekuwa na kero kubwa kuhusu ushuru wa vifaa vinavyopita bandarini hapa Dar es Salaam na bandari ya Zanzibar hali inayopelekea uwepo wa bandari bubu hasa Ukanda wa Pwani. Je, ni lini Serikali itaondoa hizi kodi za kero kwa wasafiri wa kawaida kabisa ambao si wafanyabiashara wanaotumia bandari hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na kero ya mifereji mikubwa hasa maeneo ya mijini kujaa taka hususan wakati wa mvua hali ambayo inahatarisha maisha ya Watanzania. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzuia taka hizi ili zisilete magonjwa ya milipuko hasa maeneo ya mijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na kero kubwa ya ukosefu wa maji hasa maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika kwa mfano uwepo wa Kambi kama Bulombola na maeneo mengine Mkoani Kigoma. Ukosefu wa maji kwenye kambi hizo unapelekea uchafuzi wa maji kwa kuwa vijana wengi kwenye kambi hizo wanategemea Ziwa Tanganyika kwa shughuli za kuoga, kufua na kujisafisha. Je, ni lini Serikali itazuia uchafuzi huu wa mazingira.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fursa hii adhimu ya kuweza kuchangia Wizara hii muhimu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inachukua asilimia 80 ya Watanzania yaani ukiangalia wakulima, wafugaji na wavuvi ni almost asilimia 80, asilimia 20 ndiyo ya Watanzania wanaofanya shughuli nyingine. Sekta hii isipoangaliwa kwa umakini wa hali ya juu ni dhahiri kabisa kwamba tunaweza tukaliingiza Taifa kwenye mgongano wa wenyewe kwa wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana, nchi hii imejaliwa maeneo mazuri, ardhi nzuri, mito, bahari, mabonde, milima na kila kitu na asilimia kubwa ya ardhi bado iko vijijini na wakulima na wafugaji wengi bado wapo vijijini, ni tatizo gani linalotushinda kama nchi kuweka sera nzuri zitakazohakikisha kwamba Taifa haliingii kwenye migogoro? Tuna Land Use Planning, tumejipanga kila kitu, kwa nini watu wanagombana, shida iko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kuna sababu za kijiografia zinazopelekea watu wanahama na mifugo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Kuna maeneo ambayo kwa mvua jinsi ilivyonyesha mwaka huu mifugo haiwezi ku-survive mafuriko lazima watahama kutoka eneo moja kwenda eneo lingine. Tumeona nchi nzima mvua inanyesha lakini Dodoma hii kuna maeneo kabisa mvua haikufika automatically lazima wakazi wa maeneo hayo ama wafugaji wa maeneo hayo ku-shift kutoka hapa kwenda sehemu nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni wakati gani mfugaji huyu atakwenda kuomba kibali cha kuhakikisha kwamba anahama na mifugo yake na wakati mifugo wale wanatakiwa ile ili wasife na njaa? Kwa hiyo, tunapoweka sera, sheria na sheria ndogo lakini lazima tuhakikishe mabadiliko ya kijiografia ambayo yanaweza yakapelekea watu wetu waweze kuhama yanazingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie suala la uvuvi. Mkoa wa Kigoma tuna Ziwa Tanganyika na lina samaki wa aina nyingi sana lakini samaki wale kwa kweli hawavuliwi ipasavyo. Tuna dagaa wazuri ambao wanapelekwa Uingereza, Marekani, Malaysia na sehemu zingine lakini bado wanavunwa kwa kiasi kidogo sana. Tunaomba kujua Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana wetu na wavuvi wanaotoka Ziwa Tanganyika waweze kuvua uvuvi wenye tija na kulisha nchi lakini pia na kulisha nchi za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shida kwa wavuvi wetu katika Ziwa Tanganyika wanatekwa na maharamia kutoka Congo na wengine kutoka Burundi wakiingia kule wananyang’anywa nyavu zao, pesa, mashine na kadhalika. Hali hii inawarudisha vijana wengi nyuma na kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi kwa kuhofia usalama wao. Serikali inawa-guarantee vipi vijana hawa ambao wana-risk kwenda kutafuta maisha katika ziwa lenye kina kirefu kuhakikisha kwamba wanafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kuweza kuchangia uchumi wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia bado kodi kwa wavuvi ni kubwa. Nilikuwa na-discuss na Mheshimiwa hapa wa Ukerewe, wavuvi wanatozwa kodi kubwa sana za uvuvi, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza kodi hizi? Kwa sababu mvuvi anapokwenda kuvua kwanza kuna mawili, aidha, arudi salama ama asirudi salama. Kwa hiyo, pamoja na kuchukua risk yote hii kwa nini tunawatoza tozo kubwa na ni za kero? Mna mkakati gani wa kuhakikisha kwamba tunapunguza kodi za kero kwa wavuvi wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mkoa wa Kigoma tunalima, tuna zao la mchikichi. Kwa taarifa ya research zilizofanyika hivi karibuni, zao la mchikichi linatumika katika kuzalisha bidhaa mbalimbali katika nchi ya Europe kwa asilimia 80. Chocolate hizi zinazotengenezwa ili ziweze kuganda na ziweze ku-survive zinatumia zao la mchikichi, lakini hakuna utaratibu wowote unaowekwa kuhakikisha kwamba unafanyika utafiti wa kutosha na zao hili liweze kulimwa kwa umakini wa hali ya juu.