Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Sabreena Hamza Sungura (5 total)

MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Mheshmiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imekuwa na tabia tata ya kuchukua fedha kwenye Mashirika ya Umma kama NSSF, LAPF na Mashirika mengine na kutokuzirudisha kwa wakati, ama kuwekeza katika miradi mfu kama mradi wa Machinga Complex na miradi mingine ambayo imekuwa haina tija Serikalini.
Ni lini Serikali itakoma mchezo huu wa kuchukua fedha ambazo zinawaathiri wachangiaji?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali imekuwa ikichukua fedha na hii ikifuata taratibu zote na Mifuko hii kuingia katika Mikataba ili Mifuko hii iweze kuwekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itasitisha utaratibu huu, siamini sana kwamba ni sahihi sana Serikali kusitisha, kama Mifuko inaweza kuwekeza na wakaingia katika mikataba ambayo tunaita ni Win Win Situation kati ya Serikali na Mifuko naamini ni sehemu nzuri ya uwekezaji kwa mifuko yetu hii. Kwa hiyo, naomba tuendele kufanya hivyo.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Moja; eneo la Karukwete lina wachimbaji wadogo na lipo jirani kabisa na Kijiji cha Busiri kinachazungumziwa kwenye swali la msingi. Waziri yupo tayari kulijumuisha kwenye mkakati wa kuwawezesha kielimu na uwezeshaji?
Swali la pili; naomba kujua orodha ya mambo ya kiuwezeshaji yatakayofanyika kwa wananchi wa Karukwete na Busiri na lini tutawenda kuzungumza nao kuwafahamisha? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mukasa kwamba eneo la Karukwete nalo litaongezwa kwenye maeneo ya kufikiriwa kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu langu la pili kwenye orodha ya huduma zitakazotolewa kwa msaada huu ni pamoja na kuwapatia ruzuku wachimbaji wadogo. Mwaka huu kwenye bajeti yetu mtaona tumetenga takribani shilingi milioni tisa za Tanzania pamoja na dola bilioni nne kwa ajili ya kuwawezesha wachimbaji wadogo. Pia tutaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo ili waweze kuwa na uchimbaji wenye tija.
Pamoja na hayo bado Wizara yetu itatuma wataalam wa GST iyafanyie tathmini maeneo yote yatakayotengwa ili wachimbaji wawe na uhakika wa uchimbaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuongeza kwa manufaa ya wengine kwamba maeneo ambayo tutayatenga yapo mengi tunategemea kutenga eneo la Kasubwiya hekta 495, eneo la Nyaluyeye hekta 658, eneo la Matabe hekta 659 na maeneo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tutaendelea kuwawezesha.
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Spika, kwanza kwa masikitiko makubwa nasikitishwa sana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, hii Serikali inajiita ni Serikali ya hapa kazi tu na kila siku imekuwa ikija na majibu mepesi kwa maswali mazito. Wamiliki wa mabasi ambao ni wananchi wa kawaida wenye uwezo wa kawaida wana uwezo wa kuwa na mawakala katika Wilaya mbalimbali nchini, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inashindwaje kuwa na mawakala ili kusaidia wananchi waweze kuzipata tiketi hizi kwa urahisi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu mtu anatoka Kasulu, mtu anatoka Kibondo, mtu anatoka Ilagala anatumia sh. 10,000, sh. 8,000, sh. 7,000, anakwenda na kurudi, anakaa saa kumi usiku mpaka nne asubuhi, tiketi zinaanza kuuzwa na anakosa tiketi anarudi kijijini. Hizo gharama kwa mwananchi anaziona ni ndogo kuliko Serikali kuweka mawakala katika maeneo husika?
SPIKA: Sasa swali!
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Spika, swali ni kwamba anaona gharama ya Serikali kuweka mawakala katika Wilaya husika ili kuwapunguzia wananchi mzigo wa usafiri ni kubwa kuliko gharama wanazozipata wananchi kuamka saa kumi ya usiku na kukosa tiketi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, …
SPIKA: Hee! Bado!
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Spika, bado, hilo ni swali la kwanza. Swali la pili, amekiri kwamba kuna ulanguzi wa tiketi. Tiketi ya daraja la tatu ambayo inauzwa sh. 24,000 katika soko la ulanguzi inauzwa sh. 35,000 mpaka sh. 40,000. Daraja la pili kwa bei ya sh. 56,000 inauzwa sh. 75,000 mpaka sh. 85,000 na daraja la kwanza kwa bei ya sh. 76,000 inauzwa sh. 100,000 mpaka sh. 110,000. Je, Serikali, ni lini sasa mtaondoa kero hii na kutoa ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ulanguzi wa tiketi ulikuwa kwa kiwango kikubwa sana kabla ya utaratibu huu ambao Serikali tumesema tumeubadilisha haujafanyika, baada ya utaratibu huu kufanyika tatizo hili la ulanguzi wa tiketi sasa halipo kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu gharama ambazo wananchi wanazipata tutaangalia uwezekano mwingine, badala ya kuanzisha wakala, tutaanzisha huduma ya wateja katika stesheni ile ile, upate uhakika wa tiketi kabla hujakwenda stesheni kulipa fedha na tunakokwenda TRL itaanzisha huduma ya kutoa tiketi ukiwa nyumbani huko kwa kutumia simu. Hatutaleta mawakala kwa
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
22
sababu kuleta mawakala kunaongeza gharama zaidi kwa TRL na vilevile ni gharama kwa uchumi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu suala la…
SPIKA: Umesikia Mheshimiwa Sabreena, Serikali hii ya hapa kazi tu inaleta digital! Mheshimiwa Waziri endelea! (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, namhakikishia kwamba tukishaanzisha utaratibu huo, hilo tatizo la pili ambalo analiongelea halitakuwepo tena.
MHE. SABREENA H.SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado kuna mambo ya msingi ambayo yanapelekea ajali za barabarani kuendelea kutokea ambayo hayajakuwa mentioned katika majibu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hususani njia inayoelekea Kigoma, kuanzia Itigi kwenda Tabora mpaka Kigoma, tumekuwa na railway cross nyingi sana katika eneo hilo, lakini nyingi katika hizo hazijawekewa alama kiasi kwamba msafiri anapokuwa anaendesha ama madereva wanapokuwa wanaendesha wanashindwa kutambua. Ni kwa mita chache sana alama hizo zipo na maeneo mengine alama hizo hakuna kabisa, kitu ambacho kinaweza kikapelekea sasa magari yetu na treni zije zisababishe ajali kubwa hapo baadaye. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wana-fix vibao vinavyoonesha railway cross barabarani katika njia hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa kumekuwa na shida kubwa sana hasa ya wafugaji, hususani wafugaji wa ng’ombe, hufuga maeneo ambayo ni pembezoni mwa barabara na wakati mwingine ng’ombe wale hupelekea ajili zisizokuwa za msingi na kwa kuwa kumekuwa na tendence ya traffic hasa katibu miji mikubwa kama Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma na kadhalika, hususani Dar es Salaam ambapo taa za barabarani zinafanya kazi, hapo hapo na traffic wanafanya kazi, kitu ambacho kinapelekea ku-confuse madereva barabarani na kuweza kusababisha ajali.
Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya mambo haya mawili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumekuwa tukikabiliana na changamoto za kukosekana katika baadhi ya maeneo alama za barabarani zinazotakiwa kuelekeza madereva kuona maeneo ambayo ni hatarishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kulitambua hilo ndiyo maana katika jibu langu la msingi nilieleza kati ya mikakati 14 moja katika eneo tulilokuwa tulifanyia kazi ni eneo hilo na kwamba tumejaribu kwa kiasi kikubwa sana kuweza kuwasiliana na kufanya kazi kwa karibu na mamlaka husika ili kuweza kudhibiti na kuweka hizo alama ambazo anasema kuwa zimekosekama. Bahati nzuri Makamu Mwenyekiti wa Baraza letu la Usalama Barabani ni Mheshimiwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, kwa hiyo tumelifanya hili kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kubwa ambalo linasababisha alama hizi kupotea. Mara nyingi ni kutokana na tabia mbaya za baadhi ya wananchi ambao wamekuwa waking’oa kwa makusudi alama za barabarani na kuvitumia vyuma hivi kama vyumba chakavu. Naomba nitoe wito kwa wananchi kuacha tabia hiyo na kwamba mamlaka husika ziko macho kwa wale wote ambao watakiuka sheria za nchi, kwa kung’oa vibao vya alama hizi tutawachukulia hatua za kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili lilikuwa linahusiana na askari wa barabarani pamoja na taa za barabarani. Mara nyingi askari wa barabarani wanakaa wakati ambao kuna msongamano wa magari barabarani, hasa wakati wa asubuhi wakati watu wanakwenda kazini na wakati wa jioni wanapokuwa watoka kazini. Hii ni kwa sababu taa za barabarani zilipowekwa haziwezi kukidhi mahitaji ya nyakati husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo kuna wakati ambao kuna msafara mwingi unatokea katika upande mmoja, kwa hiyo kutegemea taa za barabarani peke yake kunaweza kusababisha msongamano mkubwa. Kwa maana hiyo hao traffic police wanakaa pale kwa lengo la kudhibiti na kuzuia msongamano huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kuhakikisha kwamba askari hao wanaendelea kutumika kusaidia kupunguza msongamano wa magari hasa katika nyakati hizo za watu ambao wanakwenda kazini na kurudi kazini asubuhi na jioni.
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na tatizo kubwa la vyumba vya uendeshaji wa shughuli za Mahakama hususan katika Mkoa wetu wa Dodoma na ukizingatia mkoa huu umeshakuwa Makao Makuu ya nchi.
Mheshimiwa Spika, nataka kujua Serikali ina mkakati gani sasa wa kupanua Mahakama ya Wilaya ya Dodoma kwa maana ya District Court ili sasa ule mlundikano wa Mahakimu watatu kukaa kwenye chumba kimoja na kusikiliza mashauri na kesi nyingi kuchelewa, hususan kwa kesi za watoto wanaobakwa na kulawitiwa na hivyo kuathiri masomo yao uweze kwisha? Ni lini sasa Serikali itafanya upanuzi wa Mahakama hii ili kero hii iweze kuondoka kwa wananchi? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA - K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimekuwa nikisema mara zote, ni kwamba katika utaratibu tulionao sasa hivi katika utendaji kazi wa kimahakama, tunafanya kazi ya ukarabati wa majengo yetu mengi na upanuzi wa baadhi ya Mahakama. Kwa sababu sasa hivi tumeingia ubia pamoja na Chuo Kikuu cha Ardhi ambapo tunakwenda kujenga katika mfumo mzuri wa Moladi ambao unapunguza gharama, Waheshimiwa Wabunge waendelee kuvuta subira tu, pindi bajeti itakaporuhusu tutaendelea kufanya ukarabati na kupanua Mahakama ili kupeleka huduma za kimahakama zaidi kwa wananchi.