Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Susan Anselm Jerome Lyimo (5 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipatia nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika hoja hii muhimu sana ya sekta ya afya, kwa kweli bila afya hatuwezi kuwa hapa ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nipongeze sana hotuba ya Kambi ya Upinzani na ile ya Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii na Maendeleo kwa sababu ndiyo ukweli wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda kuzungumzia statistics za Wizara na uhalisia wa mambo yanavyokwenda kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati hii.
Kabla ya kuanza kwa sababu Wizara hii pia inahusika na masuala ya maendeleo ya jinsia, nitoe masikitiko yangu kwa jinsi ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri ambaye anasema kwamba yeye ni balozi wa wanawake ameweza kukemea mambo yaliyotokea nje, lakini yaliyotokea humu ndani ameshindwa kukemea. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri kama kweli wewe ni balozi ungekuwa muwazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala zima la upungufu wa wataalam. Ni jambo la kusikitisha na nichukue fursa hii kuipongeza sana Taasisi ya Benjamin Mkapa kwa jinsi ambavyo inafanya kazi kubwa ya kuboresha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kusikitisha na nashangaa Serikali inakuwa wapi. Tumeambiwa na Benjamin Mkapa Foundation wametengeneza theatres tisa, wameshazikabidhi kwa Halmashauri, tena zile za mipakani Rukwa, Kishapu na nashangaa Mbunge wa Kishapu anayesema shapu lakini kwake upungufu wa wauguzi ni 86%. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, theatre hizi tisa zimekabidhiwa kwa Serikali ni tatu tu zinafanya kazi, sita zipo tu na kuna watumishi lakini hazifanyi kazi, sasa tunajiuliza hii Serikali ya namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ni vibali, tuna wataalam wa afya 4,491 wame-graduate toka mwaka 2014 mpaka leo hawajapata ajira. Madaktari Wauguzi na wataalam wa maabara wako mitaani, lakini hapo hapo tunasema tuna ukosefu mkubwa wa watumishi, sasa tunajiuliza kuna tatizo gani? Vibali hivi vinaenda kumaliza muda wake tarehe 30 Juni, watu wako nje. Kwa hiyo, naomba tutembee kwenye maneno yetu, tufanye kwa vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuje kwenye suala la dawa, hapa tunapoongea dawa muhimu yaani essential medicine tuna upungufu wa asilimia zaidi ya 87. MSD ambao wanaohitaji shilingi bilioni 21 kwa mwezi kununua dawa wanapewa shilingi bilioni mbili tu za dawa muhimu. Ina maana kwamba kwa mwaka wanatumia fedha za mwezi mmoja tu. Hii ina maana gani? Ina maana Watanzania zaidi ya asilimia 80 hawapati dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi kwenye suala la ukosefu wa watumishi na hapa nizungumzie lab technician. Tumetoka kwenye suala zima za symptom yaani mtu haangalii tu dalili zako kwa macho, inatakiwa upimwe majibu yatoke laboratory lakini tuna upungufu wa asilimia 100 kwenye maeneo mengi nchini hapa. Tunaambiwa mikoa ya pembezoni zahanati hazina wataalam hata mmoja. Kwa hiyo, muuguzi au daktari anaenda kwa kukuangalia tu unaeleza historia yako anakupa dawa, ina maana Watanzania wengi wanapata dawa ambazo labda siyo za magonjwa yanayowasumbua. Kwa hiyo, hili ni tatizo kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ambacho kinasikitisha zaidi ni data tulizopewa za wanawake wanaokufa kila siku. Haiwezekani whether ni za Serikali kwamba ni wanawake 24 au hizo ambazo zinatoka kwenye National Bureau of Statistics kwamba leo wanawake 42 wanakufa kwa siku maana yake ni wanawake 1,300 kwa mwezi, kwa mwaka ni wanawake 15,000 sawa na wapiga kura wa Jimbo moja kule Pemba au Zanzibar. Hatuwezi kama akina mama kukubali hali hii iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu nchi hii ina uwezo, kama tuliweza kununua magari ya washawasha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia, kama tuliweza kununua magari ya washawasha 777 na ni 50 tu yalitumika kwenye uchaguzi na gari moja nime-google kwa Alibaba ambao ndiyo wanaleta magari lina gharama ya shilingi milioni 150 mpaka 400 lakini tuchukue wastani wa dola 300,000 kwa moja ina maana kwa magari 700 ni dola 210 milioni. Ukizipeleka kwenye hela za Kitanzania ni bilioni 420…
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Shilingi bilioni 420 kwa kata 3,990 tulizonazo Tanzania nzima zingeweza kupata ambulance. Nime-google ambulance moja ambayo tena ni advance inaenda kwa shilingi milioni 105, ukigawanya ina maana kila kata hapa Tanzania ingepata ambulance. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunajiuliza priorities za nchi hii ni zipi, ni afya ya Mtanzania au ni kitu gani? Kwa sababu nimesema magari 77 ya washawasha yangeweza kubaki, tunazungumzia yale 700 yaliyobaki yaani yangetosha kununua ambulance kila kata hapa nchini. Kibaya zaidi hayo magari ya washawasha yametumika 50 according to data. Sasa tunajiuliza hivi huu utaratibu ukoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na mbwembwe sana, tukaambiwa kwamba CT-Scan imenunuliwa, hela zilizokuwa zifanye sherehe ya Wabunge zimenunua vitanda. Tumeenda Muhimbili ile CT-Scan ilitoka UDOM. Sasa watueleze hivi Wagogo na watu wengine wanaoishi Dodoma hawahitaji kutibiwa? Vilevile tunaambiwa hata vitanda vilitoka sehemu nyingine havikununuliwa. Sasa tunataka kujua zile hela za sherehe ya Wabunge zilienda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la Benki ya Wanawake. Kumekuwa na mazungumzo mengi hapa Bungeni kwa nini hatufungui matawi mikoani. Serikali hii hii ambayo iliahidi kutoa shilingi bilioni mbili kila mwaka kwa ajili ya hii benki hawajatoa. Mwaka huu ukiangalia kwenye kitabu cha maendeleo wametoa shilingi milioni 900. Tuliwashauri Wizara, Wizara hii ina taasisi kubwa nyingi, ni kwa nini taasisi kama ya Bima ya Afya, MSD, NIMR na nyingine wasipitishe fedha zao kwenye benki hiyo ili benki hiyo iweze kukua na kwenda mikoani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisikitika sana Mheshimiwa Waziri alivyomgombeza sana Mkurugenzi wa Benki hii lakini kwa kweli ukiangalia haiwezi kutoa riba nafuu kwa sababu haina fedha. Kwa hiyo, naomba kutoa pendekezo kwa Mheshimiwa Waziri kwamba ni lazima ifike mahali kama Serikali haina fedha iweze sasa kuchukua hayo mashirika niliyoyazungumza waweze kuwekeza fedha zao kwenye benki hii. Vilevile na Wabunge wanawake tunaweza kufungua akaunti kwenye benki hiyo ili iweze kwenda mikoani kusaidia akina mama ambao wanateseka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie sasa na suala la wazee. Naomba ni-declare interest mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Wazee wa CHADEMA Taifa. Wazee nchi hii wanajulikana kwa idadi lakini kibaya zaidi Sera ya Wazee imetungwa toka mwaka 2003 mpaka leo tunavyoongea miaka 14 baadaye hakuna sheria, hakuna kanuni, hakuna mwongozo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wazee wameteseka sana katika nchi hii, wameuwawa kwa sababu ya macho mekundu lakini hakuna sheria. Leo Waziri anasema mwezi wa tisa wataleta Muswada, tunakushukuru lakini tuseme tu kwamba umechelewa. Tunashukuru kwa hatua hiyo lakini ni kweli umechelewa. Tunaamini sasa huo Muswada na Sheria ikipitishwa, kanuni nazo zitatungwa mara moja ili wazee hawa waweze kuona kwamba wanaishi katika nchi yao kwa amani lakini wajue mchango wao katika nchi hii unathaminika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii. Kwanza kwa niaba ya wanawake wote Tanzania, Afrika na dunia nichukue fursa hii kumpongeza sana Fatma Samba Diouf kwa kuwa Katibu Mkuu wa FIFA kwa hiyo, nampongeza sana. Hii ni hatua kubwa sana kwa Waheshimiwa wanawake duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka tu naomba niseme mambo machache; la kwanza kuhusiana na ferry ya Dar es Salaam. Mwaka jana Mheshimiwa Waziri alituambia kwamba ile ferry ilinunuliwa kwa shilingi bilioni 7.9. Nilikuwa naomba kujua leo hii ferry hiyo iko wapi? Kwa sababu, taarifa nilizonazo hiyo ferry sasa hivi haipo kazini! Nilikuwa naomba kujua iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni suala la bajeti. Nilikuwa naomba Waziri anapokuja kutoa maelezo hapo anapo-windup atuambie inawezekanaje, tulipitisha bajeti ya Wizara hii nyeti sana kwa nchi yetu kwa shilingi bilioni 191 fedha za ndani kutoka Mfuko Mkuu, lakini mpaka Aprili 30, wametumia shilingi bilioni 607 zaidi ya asilimia 68 Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba maelezo ya kina inawezekanaje Wizara hii ipate fedha hizo na imezipataje wakati tuna matatizo makubwa kwenye Wizara nyingi ambazo hata asilimia 50 hawajafika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nililokuwa naomba kulichangia ni suala zima za nyumba za Serikali, limeongelewa sana. Nilikuwa naomba kujua, lile Azimio la mwaka 2008 kutoka kwenye maelezo binafsi ya Mheshimiwa Kimario mpaka leo limefikia wapi? Na je, mna mpango gani wa kuendeleza nyumba hizo au kuzirejesha, ili tujue wahusika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba nizungumzie barabara ya Kinondoni, kutoka Mwenge mpaka Morocco. Nimefuatilia vitabu vya bajeti kuanzia mwaka 2013 mpaka leo, fedha ambazo zimeshatolewa ni shilingi bilioni 126, lakini barabara ile bado. Sasa nilikuwa naomba ilikuwa ni kuanzia Morocco mpaka Tegeta, lakini kwa awamu mbili; nilitaka kujua hizi fedha zimefika wapi kwa sababu mpaka majuzi hapa tulisikia Mheshimiwa Rais akisema kwamba anatoa zile fedha zilizokuwa za sherehe za Uhuru kwenda kujenga hii barabara.
Sasa nilikuwa nataka tu kupata maelezo, hizi fedha ambazo zimeshatolewa kuanzia mwaka 2013 mpaka leo ziko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho…
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii ili na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana. Awali ya yote, nimpongeze sana Mheshimiwa Msigwa kwa hotuba yake nzuri sana pamoja na kwamba wengine imewakwaza lakini kwetu ni nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na jambo ambalo limezungumzwa sana na niseme kwamba last time nilikuwa kwenye Kamati ya Mambo ya Nje, suala la Chuo cha Diplomasia ni la msingi sana, wamezungumza wengi lakini naomba niende kwa maswali tu. Chuo hiki kilikuwa kipanuliwe na eneo walikuwa wanafuatilia kule Bagamoyo. Nataka Waziri anapokuja kujumuisha atuambie suala hilo limeishia wapi maana silioni mahali popote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni suala la diaspora, ni jambo la kusikitisha sana. Bahati nzuri nimeangalia hotuba ya mwaka juzi, ya mwaka jana, hotuba ya mwaka 2014 inaonesha kwamba walikuwa wanafanya utafiti kujua Watanzania wangapi wanaishi nchi za nje, two years ago. Leo Mheshimiwa Waziri anatuletea taarifa kwamba Watanzania waishio nchi za nje wanakadiriwa kuwa zaidi ya milioni moja. Tulitaka kujua idadi kamili ni wangapi ili tujue ni kiasi gani wanaweza kuleta nchini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi kama Nigeria leo inaingiza dola za kimarekani bilioni 21. Sawa Nigeria ina watu wengi lakini Kenya jirani zetu, bilioni 1.4 mwaka 2015, Tanzania wanaingiza kiasi gani, hatuna kiasi. Kwa hiyo, kama walivyosema wenzangu nadhani hii Wizara diplomasia iko kisiasa zaidi lakini haiko kiuchumi Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine na tulilizungumza sana ni suala la kuhakikisha kwamba Mabalozi wetu wote walioko nje ya nchi wanakuwa angalau na mkutano mmoja ili wajue huko kwingine kuna fursa kiasi gani wakae pamoja wapeane taarifa. Nina taarifa kwamba nchi nyingine wanafanya hivyo, nimekuwa Finland nimeona kila tarehe fulani Mabalozi wa nchi zote wa Finland wanarudi nyumbani ili kutoa feedback ya mambo gani au changamoto gani wanakutana nazo na fursa gani wanakutana nazo. Hapa Tanzania tuna utaratibu gani, ni mwaka gani Mabalozi wetu wote wamewahi kuitwa wakakutana ili angalau wazungumzie fursa na changamoto wanazozikabili ili tuone nchi yetu inaendelea kiuchumi zaidi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kusikitisha, nimepitia kitabu cha maendeleo, Wizara kubwa namna hii ina shilingi bilioni nane (8) tu fedha za maendeleo, unless kuna fedha nyingine. Ukiangalia hotuba ya Waziri anazungumzia suala la kupanua Balozi, kwa fedha zipi? Hizi ambazo tunazo tumeshindwa, ukienda kwenye Ubalozi wa Zambia ni matatizo, ukienda kwenye Balozi nyingine nyingi ni matatizo, bahati nzuri tumekwenda, ni matatizo makubwa, mpaka hata Ubalozi wetu Marekani ni shida. Kama mwenzetu Idd Amin aliweza kujenga jengo kubwa sana pale New York Tanzania tumeshindwa na alijenga miaka ile, ni jambo la kusikitisha, tunaendelea kupanga. Tulisema ni kwa nini makampuni kama NSSF, NHC wasiingie ubia na Serikali kupitia Wizara hii ili waweze kujenga nyumba huko nje lakini naona jambo hili nalo limekufa kifo cha kishujaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za nyuma akiwa Waziri Membe mwaka 2014 na huko nyuma tuliongelea sana suala la dual citizenship (uraia pacha) lakini leo halionekani mahali popote na ni kama vile limekufa. Mheshimiwa Waziri anajua watu kwenye Diaspora walilalamikia sana suala hili la uraia pacha na tukawa tumeambiwa na Mheshimiwa Membe kwamba jambo hili linafanyiwa utafiti, litaendelea kushughulikiwa na litaingizwa kwenye Katiba iliyokuwa inapendekezwa lakini leo hakuna kitu, sasa tuwaeleweje jamani? Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba tujue status ya uraia pacha ikoje sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuzungumza ni kwenye masuala ya ndoa. Tunajua kwamba ukiwa mwanaume Mtanzania, ukioa raia wa nje automatically yule mama anakuwa raia wa Tanzania lakini mwanamke wa Kitanzania akiolewa na mzungu au mtu mwingine ni tatizo kubwa. Sasa tunaomba kujua hii double standard inakuwaje kwa sababu hawa akinamama wananyimwa haki yao ya msingi. Kwa hiyo, naomba hilo lizingatiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulizungumzia ni suala la mjusi (dinosaur). Wizara hii pamoja na mambo mengine inashughulikia pia masuala ya kiutalii, huduma za jamii, elimu na kila kitu. Tuliambiwa kwamba yule dinosaur akiletwa hapa kwenye hili jengo hataenea, hiyo siyo issue yetu wala siyo hoja. Hoja ya msingi tunataka kujua, toka huyu mjusi amepelekwa huko Ujerumani ameingiza kiasi gani na Wizara hii ikishirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii wana utaratibu gani kuhakikisha kwamba tunapata fedha? Suala kwamba hakuna jengo la kuweza kumweka halituhusu, ilitakiwa Serikali ihakikishe kwamba inatafuta sehemu ambapo huyo mjusi akija atawekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani tupoteze fedha nyingi hivyo za kutoka nje, watu wanaenda pale maelfu kwa maelfu kumwangalia yule mjusi lakini Watanzania hatupati chochote. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri akishirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii wa-make sure kwamba wanatuletea utaratibu kidiplomasia ni jinsi gani huyo mjusi ama analetwa au Tanzania tunapata kiasi gani na hicho kiasi hakianzii leo, kinaanzia miaka hiyo waliyompeleka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili lilizungumzwa sana hapa Bungeni na Mheshimiwa Fatuma Mikidadi mpaka maskini na Ubunge hajapata. Kwa hiyo, ili kumuenzi mwenzetu hebu tuhakikishe hili jambo linafikia mwisho wake. Bahati nzuri ni Mbunge wa CCM kwa hiyo naamini suala hili litashughulikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niongelee suala la itifaki. Siku za nyuma Bunge jipya linapozinduliwa tunakuwa na semina ya masuala ya itifaki ili Waheshimiwa Wabunge waelewe ni mambo gani yanatakiwa na yanakatazwa na tulikuwa tunaletea Chief of Protocol anatupa semina. Sasa hivi utaona mtu amevaa suti bado ina label anaingia Bungeni anaenda popote, utaona mtu ana begi lake bado lina nylon yuko nalo tu. Kwa hiyo, haya ni mambo ambayo kwa kweli kama Wabunge tunapaswa kuyajua siyo tu hapa na Wabunge wengi wanasafiri nje, wanaenda hivyo hivyo. Kwa hiyo, nadhani ni wakati muafaka watuhakikishie kwamba hilo jambo linafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa ni suala la mtangamano wa Afrika Mashariki. Nilikuwa naangalia hivi ni lini tutafikia huo mtangamano wa Shirikisho la Afrika Mashariki kama kila leo tunaongeza nchi. Mimi najua kuna wengine wakiulizwa ni nchi ngapi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki watasema ni tatu, nne, tano na wengine watasema sita. Naomba kujua Sudan tayari imeshakuwa member au haijawa, maana yake mimi hata sijui. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaangalia vigezo gani, maana nilikuwa nafikiri, pamoja na geographical location lakini vilevile masuala mazima ya tabia yaangaliwe. Kwa hiyo, nadhani imefika wakati sasa tuangalie mambo haya. Pia napenda kujua ni nani wanaotoa kibali cha nchi kuwa ndani ya shirikisho?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kwanza ili niweze kuchangia hoja hizi tatu muhimu sana ambazo kimsingi zinahusiana na maisha ya Mtanzania. Kipekee nitajikita zaidi kwenye masuala ya elimu, lakini sitaacha kuzungumzia masuala ya UKIMWI, madawa ya kulevya pamoja na masuala ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianzia na masuala ya madawa ya kulevya; hapa kwenye Bunge lako Tukufu mwaka 2005 tulipitisha Sheria ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya na sheria ile ilianzisha Mamlaka ambayo pamoja na mambo mengine ni pamoja pia na kukamata (ku-arrest) pamoja na kushikilia mali zao. Hivi karibuni tunaona ni jinsi gani mamlaka hii inaingiliwa; Mkuu wa Mkoa anaamua tu kutaja majina ya watu bila kufuata utaratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuliambiwa Mheshimiwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alikuwa na majina hayo na vile vile tukaambiwa Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Kitwanga amepewa majina hayo. Ni kwa nini tume hiyo au mamlaka hiyo isishughulikie majina hayo ili tupate uhakika wa nani anatumia madawa ya kulevya. Ni kweli kwamba janga hilo ni kubwa sana, lakini lazima utafiti wa kina ufanyike, kwa sababu mtu na brand yake na kujijengea jina ni kazi kubwa lakini kulifuta ni jambo la haraka sana. Kwa hiyo, naomba utaratibu wa kisheria ufuatwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu. Mambo mengi yameongelewa, lakini niseme tu, ni wazi kwamba elimu ndio msingi wa Taifa lolote; hakuna Taifa duniani hapa lililoendelea bila kuwekeza kwenye elimu. Hata hivyo, kwa muda mrefu nchi hii imekuwa ikichezea elimu sijui kama ndio sera ya Chama cha Mapinduzi lakini kwa kweli inasikitisha sana. Amezungumza Mwenyekiti wa Kamati kwamba, Tanzania mfumo wetu wa elimu ni matatizo makubwa sana; hakuna nchi duniani yenye mifumo zaidi ya miwili katika elimu; Tanzania ndio nchi pekee yenye mifumo miwili ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani kuwe na shule za msingi ambazo medium of instruction (lugha ya kujifundishia na kujifunzia) ni Kiswahili wakati shule nyingine za level hiyo hiyo medium of instruction ni kiingereza. Pia tukiangalia tuna elimu za aina mbili; tuna elimu bure na elimu inayouzwa na matokeo tumeyaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii shule iliyokuwa ya kwanza Tanzania Feza ambayo wanalipa takribani milioni tano wanafunzi wametoka na division one na division two; division one 56 na division two wanafunzi watano au sita tu, lakini shule ya mwisho haina division one, two wala three, ina divison four wachache na zero zaidi ya 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia unaona wazi kwamba tuna matatizo makubwa sana ya mfumo wetu wa elimu na ndio sababu nitakuja pia na mapendekezo ya kuona ni jinsi gani tutaboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ni kutokana na fedha kutopelekwa kwa wakati na hata zinapopelekwa zinakuwa zimechelewa; na haya yanajitokeza zaidi kwenye miradi mikubwa; na matokeo yake ni nini! Tuna miradi mikubwa ya hospitali; Hospitali ya Bugando tulitegemea kwamba wataweza kusimika mashine kwa ajili ya uchunguzi wa saratani; tunatambua kuwa kanda ya ziwa ina population kubwa sana; lakini jambo hilo halijafanyika; leo watu kutoka kanda ya ziwa wanakuja ocean road ya Dar es salaam; wakati huo huo tumekuwa na utayari wa kujenga airport Chato ambayo iko kwenye kanda hiyo hiyo ya ziwa. Kwa hiyo ni lazima tuangalie priority zetu ziko wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua juhudi kubwa ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali kwenye maeneo mbalimbali, lakini juhudi hizo ni za watu binafsi, wamekuwa wabunifu. Kipekee nimsifie sana Profesa Mohamed Janabi, amejitahidi sana kwenye Hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na juhudi hizi binafsi bado Serikali haioni kuwa kuna haja ya kupeleka fedha nyingi. Leo Hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete imepewa Shilingi milioni 500 tu kati ya Shilingi bilioni nne ambazo wanazihitaji; wakati tunajua kwamba huduma zikiboreshwa kwenye ile hospitali ni rahisi sana watu wetu kutibiwa ndani na kwa maana hiyo Serikali itaweza kupata fedha nyingi sana za ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu, nadhani labda ile hospitali ibadilishwe jina iitwe JPM, Rais aliye madarakani sasa badala ya Kikwete labda sasa fedha zitakuwa zinatoka kwa sababu atakuwa madarakani. Naamini labda alivyokuwa Kikwete iliwezekana, kwa hiyo nashauri kwamba labda tukibadili jina likawa la Rais itasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuzngumzia ni madeni ya Walimu, hili suala ni kubwa sana. Na-declare interest mimi ni Mwalimu. Katika kuboresha elimu jambo la kwanza la kuliangalia ni Walimu na si madarasa wala vitabu. Walimu wa Taifa hili wamedharauliwa kiasi cha kutosha, wamenyanyaswa kiasi cha kutosha. Haiwezekani leo Walimu wadai hata kama ni trilioni 1.06 au milioni 800; ni kwa nini hawalipwi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuulizane, kada gani nyingine hapa Tanzania ambayo ina madeni makubwa kiasi hiki? Yaani leo Mwalimu anaweza kwenda kituoni asilipwe mshahara kwa zaidi ya mwezi mmoja; nani anayeweza kukubali jambo hilo? Kwa hiyo, upole wa Walimu usiendelee kuifanya Serikali iache kulipa madeni yao na kuwafanya kama watu wa mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa zaidi ni hili suala la uhakiki. Mimi sielewi definition yake kwa sababu haiwezekani Walimu waitwe kwenda kusimamia mitihani, wamalize kusimamia mitihani, leo ni takribani miaka miwili wanaambiwa wanafanyiwa uhakiki. Hivi una mhakiki mtu kabla ya kufanya kazi au baada ya kufanya kazi? Kwa hiyo, haya ni mambo ambayo tunaona yanaleta mushkeli katika elimu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze, na bahati mbaya sana Mheshimiwa Mwenyekiti wangu wa kamati, kwenye mapendekezo mwishoni kuna mengi hakuyasema lakini niseme; kuna suala la wanafunzi walioondolewa Chuo Kikuu cha Dodoma. Naamini kabisa kwamba kuondolewa kwa wanafunzi wale haikuwa bahati mbaya ilikuwa ni makusudi kwamba majengo yale sasa yawe wizara za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanini nasema hivyo? Nasema hivyo kwasababu ukiangalia mwaka 2014 uliletwa Muswada wa Mrekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo hapa ili tuweze kuwaingiza wanafunzi ambao wataenda kusoma special education kwa ajili ya masomo ya sayansi. Leo hakuna Mbunge humu ndani ataniambia kwamba kwenye Jimbo lake hakuna shida ya walimu wa sayansi; na Mheshimiwa Jenista wakati huo Naibu Waziri wa Elimu alilihangaikia sana hili jambo, lakini leo wanafunzi wale wameondolewa, tunapewa sababu za ajabu ajabu, tunaambiwa walikuwa vilaza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoambiwa jambo, wewe mwalimu unapoambiwa kuwa wewe ni kilaza; kilaza kwa wale wasiojua hii ni terminology, na watoto wa University of Dar es Salaam huko nyuma, ni watu ambao hawaelewi chochote yaani wajinga. Kwahiyo, unapowaambia walimu wajinga…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Umemaliza, ni ya pili hiyo. Ahsante sana.