Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Susan Anselm Jerome Lyimo (14 total)

MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:-
Ugonjwa wa kipindupindu umeendelea kukatisha maisha ya watu wengi, japokuwa chanzo chake ni uchafu ambao ungeweza kuzuilika:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha ugonjwa huu unatokomezwa nchini?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ulianza nchini tarehe 15 Agosti, 2015 katika Mkoa wa Dar es Salaam na baadaye kusambaa katika mikoa mingine ya Tanzania Bara.
Hadi kufikia tarehe 31 Januari, 2016, jumla ya watu 15,067 walikwishaugua ugonjwa huu na kati yao jumla ya watu 233 walifariki dunia. Mikoa ambayo haijaathirika na ugonjwa huu ni Njombe, Ruvuma na Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kudhibiti ugonjwa huu imeweka mikakati ifuatayo:-
(i) Kuunda Kamati za Kudhibitii Ugonjwa wa Kipindupindu katika ngazi zote;
(ii) Kuelimisha jamii kupitia njia mbalimbali ambazo ni pamoja na mabango, vipeperushi, redio na televisheni; na
(iii) Kuimarisha usafi wa mazingira na usalama wa maji na chakula kwa kufanya yafuatayo:-
(a) Ukaguzi wa vyanzo vya maji katika mikoa iliyoathirika na kufunga vyanzo vya maji vilivyobainika kuwa na vimelea vya kipindupindu na pia kuweka njia mbadala ya kupata maji;
(b) Kutibu maji katika ngazi ya kaya na kufanya ufuatiliaji wa wagonjwa kwenye maeneo yaliyoathiriwa na ugonjwa huu;
(c) Kusambaza dawa ya kutakasa maji ya kunywa (water guard) katika maeneo mbalimbali nchini;
(d) Kushirikikiana na Mikoa na Halmashauri za Wilaya kufanya ukaguzi wa baba au mama lishe na waliokiuka walipewa faini; na
(e) Kunyunyizia dawa ya kuua vAimelea vya ugonjwa wa kipindupindu kwenye vyoo.
MHE. SUSAN A.J. LYIMO aliuliza:-
Mwaka 2015 Haki Elimu walitoa tathmini ya utafiti wa elimu kwa kipindi cha miaka 10 ya Awamu ya Nne na kugundua ongezeko kubwa la udahili kwa ngazi zote na kuporomoka kwa ubora wa elimu:-
(a) Je, ni kwa kiasi gani utafiti huo umeakisi uhalisia wa hali ya elimu hususan ile ya sekondari?
(b) Je, Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati gani ya kuinua ubora wa elimu hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba udahili umekuwa ukiongezeka katika ngazi zote za utoaji elimu kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu. Ongezeko hili linatokana na utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo ya Elimu katika ngazi mbalimbali ikiwemo Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES). Sanjari na ubora wa elimu, lengo kuu la mipango hiyo lilikuwa ni kuwezesha watoto wote wenye rika lengwa kuandikishwa darasa la kwanza na idadi ya wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (darasa la saba) kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mafanikio ya MMEM na MMES yalisababisha ongezeko kubwa la shule za msingi na sekondari, sanjari na ongezeko la wanafunzi na kuleta changamoto ya utoshelevu wa mahitaji muhimu ikiwemo Walimu, miundombinu pamoja na vifaa vya kufundishia na kujifunzia na hivyo kuathiri ubora wa elimu kwa namna moja au nyingine hasa katika kipindi cha awamu mbili za mwanzo za mipango hiyo (2002 – 2010). Hivyo, kwa kiasi fulani utafiti wa Haki Elimu umeakisi uhalisia wa hali ya elimu nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ubora wa elimu unahusisha mambo mengi ikiwemo mazingira ya utoaji wa elimu ambayo yalianza kuboreshwa katika kipindi hicho. Kwa mfano, idadi ya Walimu wa shule za msingi wenye sifa iliongezeka kutoka Walimu 132,409 mwaka 2005 hadi 180,565 mwaka 2014 na Walimu wa sekondari iliongezeka kutoka 20,754 mwaka 2005 hadi kufikia 80,529 mwaka 2014. Aidha, morali wa Walimu hao kupenda kwenda kufanya kazi katika maeneo mbalimbali ya vijijini imeongezeka kutokana na Serikali kuimarisha miundombinu wezeshi kama vile barabara, upatikanaji wa umeme, maji na mawasiliano ya simu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa nchini inakuwa na ubora wa hali ya juu, Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mbalimbali kama ifuatavyo:-
(i) Kuimarisha na kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa kujenga na kukarabati miundombinu ya shule, ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, maabara, maktaba, vyoo, nyumba za Walimu na ununuzi wa madawati.
(ii) Kuendeleza mafunzo ya Walimu tarajali hususan kwa masomo ya sayansi, hisabati, lugha na elimu ya awali.
(iii) Aidha, Serikali inaendesha mafunzo kazini kwa Walimu kuhusu matumizi ya stadi za TEHAMA, sayansi, hisabati na lugha ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji kwa Walimu wa shule za msingi na sekondari.
(iv) Katika kuimarisha stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) mafunzo yanatolewa kwa Walimu wa darasa la kwanza na la pili.
(v) Vile vile ili kuimarisha ufuatiliaji wa tathmini ya ubora wa elimu itolewayo, Ofisi za Udhibiti Ubora wa Shule, Kanda na Wilaya zinaendelea kuimarishwa kwa kuongeza idadi ya Wadhibiti Ubora wa Shule na vitendea kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Idadi ya Shule za Awali Nchi

Elimu bora ni uti wa mgongo wa maendeleo ya jamii yoyote ile na ni msingi bora wa elimu kwa watoto unaoanzia toka shule za awali na za msingi:-
(a) Je, kuna shule ngapi za awali kati ya mahitaji halisi?
(b) Je, ni nini mipango ya haraka kuhakikisha shule za awali zinakuwepo katika shule zote za msingi za Serikali nchini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselim Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji halisi ya madarasa ya awali ni 16,014 ambayo ni sawa na idadi ya shule za msingi zilizopo nchini kwa sasa. Shule zenye madarasa ya awali ni 14,946 ambazo ni sawa na asilimia 93.33 ya mahitaji. Hivyo, shule za msingi 1,068 hazina madarasa ya awali.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa vyumba vya madarasa ya awali unafanywa na Halmashauri kwa kushirikisha na nguvu za wananchi kupitia Mpango wa Fursa na Vikwazo yaani O and OD (Opportunity and Obstacle to Development). Azma ya Serikali ni kuhakikisha inajenga na kukamilisha vyumba vya madarasa vya awali kwa shule zote 1,068 zenye upungufu huo. Hivyo nitoe wito kwa Halmashauri zenye mapungufu haya kuangalia upya vipaumbele vyake na kutenga bajeti ya kuwezesha ujenzi wa miundombinu hiyo muhimu.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:-
Tanzania ina upungufu mkubwa wa huduma ya tiba shufaa (Palliative Care Services) ukilinganisha na majirani zetu wa Kenya, Uganda na Rwanda. Hali hii inapelekea wagonjwa wengi walio katika hatua za mwisho za maisha yao kuwa na maumivu na mateso makali sana:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha tiba shufaa inaboreshwa hapa nchini?
(b) Kwa kuwa, kuna upungufu mkubwa wa watoa huduma hii, Je, Serikali inatoa tamko gani au ina mkakati gani?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi kama Balozi wa wanawake nina masikitiko makubwa sana kwa ndugu Hillary Clinton kupoteza uchaguzi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha huduma za tiba shufaa zinapatikana hapa nchini, Hospitali takriban 35 zikiwemo Hospitali za Rufaa za Kanda za Bugando, KCMC na Mbeya, Hospitali za Mikoa na Wilaya za Mwanza, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Morogoro, Kagera, Kigoma, Mtwara, Pwani, Mara na Tanga zinatoa huduma hii. Aidha, Hospitali za dini zilizopo chini ya ELCT kama Hospitali ya Seliani na zingine pia zinatoa huduma hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, huduma za tiba shufaa kwa majumbani zimekuwa zikitolewa sambamba kwenye maeneo yenye hospitali zinazotoa huduma hizo, hii ikimaanisha kwamba, watoa huduma za majumbani husaidia kumfikia mgonjwa nyumbani na kumpatia huduma. Kama tatizo litaonekana ni kubwa, hushauri mgonjwa apelekwe hospitali.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu uhaba wa watumishi katika Sekta ya Afya, hivyo Serikali katika Sera ya Kitaifa ya Tiba Shufaa (National Polliative Care Policy Guideline) iliyotolewa mwezi Juni, 2016, imeagiza mafunzo yafanyike kuwajengea uwezo watumishi waliopo katika vituo vya afya na hospitali ili watoe huduma hii ya tiba shufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Chama cha Tiba Shufaa hapa nchini (The Tanzania Palliative Care Association) na wadau wengine wameanza kusimamia utekelezaji wa sera hii ya tiba shufaa ili kuhakikisha huduma hii inapatikana kwa wagonjwa wanaohitaji na inapatikana kwa wakati wote. Lengo kuu likiwa ni kuwepo na watumishi watano katika kila kituo cha afya wenye uwezo wa kutoa tiba shufaa wakimemo Madaktari, Wauguzi, Wafamasia na Maafisa Ustawi wa Jamii.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:-
Sera ya Elimu ya mwaka 2014 inaeleza wazi kuhusu mitaala na utaratibu wa masomo katika elimu ya msingi (kidato cha kwanza - nne) na inasema watoto wa kidato cha kwanza – pili watasoma masomo yote ya sayansi na wanapoingia kidato cha tatu watachagua masomo wayatakayo kutokana na uwezo wao.
(a) Je, Waziri alipata wapi mamlaka ya kutangaza kuwa vijana wote wa elimu ya msingi hada kidato cha nne kusoma masomo yote ya sayansi?
(b) Je, kuna utafiti gani uliofanyika na matokeo kuonesha haja ya vijana wote kusoma sayansi yaani kemia na fizikia?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya Pili kipengele cha 4(1) na 5(f) cha Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1995 inampa Mamlaka Waziri mwenye dhamana ya Elimu kutangaza jambo lolote lenye maslahi kwa Taifa kutokana na hali halisi iliyopo kwa wakati huo. Kwa sasa kuna haja kubwa ya kuhamasisha ongezeko la wanasayansi kulingana na hali halisi ya mahitaji. Kwa mfano, kuna upunfufu wa walimu wa sayansi na hisabati 24,716, upungufu wa walimu 355 wa masomo ya ufundi katika shule za sekondari za ufundi na mafundi sanifu wa maabara wa shule takribani 10,000. Moja ya jukumu kuu la Waziri ni kuhamasisha wanafunzi katika elimu ikiwa ni pamoja na kuchukua masomo ya sayansi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika sehemu (a) taarifa mbalimbali zikiwemo za kimazingira halisi (evidence based) zinathibitisha juu ya upungufu wa wataalam wa sayansi, mfano kwa upande wa afya, ili kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua inatakiwa kina mama hao wahudumiwe na matabibu wenye ujuzi lakini hawapo wa kutosha, Wizara imekuwa ikihamasisha wanafunzi kuchukua masomo ya Sayansi ili kupunguza tatizo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia haijatoa waraka wowote unaowataka wanafunzi wote kusoma masomo ya sayansi, badala yake imejikita katika kuimarisha miundombinu ya maabara, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kupeleka walimu wa sayansi shuleni.
MHE. SUZAN A. LYIMO aliuliza:-
Makazi ya Wazee yapo katika hali mbaya sana pamoja na kuhojiwa Bungeni muda mrefu sana:-
(a) Je, Serikali inawaeleza nini wazee hao walioshiriki katika ukombozi wa nchi hii?
(b) Je, ni lini makazi haya pamoja na miundombinu itaboreshwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa waliotoa Wazee katika ukombozi wa nchi hii. Aidha, Wazee ni rasilimali muhimu katika ustawi na maendeleo ya nchi. Serikali inawahakikishia wazee wote nchini wakiwemo wale walioko kwenye makazi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuboresha utoaji wa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msukumo huu wa Serikali umejidhihirisha kwa kuweka sehemu kwa maana ya subsection ya wazee katika Idara Kuu ya Ustawi wa Jamii na katika jina la Wizara, ambalo linasomeka, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii na Jinsia, Wazee na Watoto. Aidha, Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeweka mkakati kuboresha maisha ya wazee.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuboresha hali ya miundombinu ya Makazi ya Wazee kwa kufanya ukarabati kwa awamu. Aidha, Serikali imekamilisha ujenzi wa mabweni ya Wazee katika makazi ya Kolandoto – Shinyanga, imekarabati Makazi ya Wazee ya Kilima- Kagera na kujenga uzio katika makazi ya Njoro- Kilimanjaro kwa jumla ya Sh.285,120,383.25. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga fedha jumla ya Sh.568,000,000 ili kukarabati Makazi ya Wazee Ipuli – Tabora, Nunge – Dar es Salaam na Kibirizi – Kigoma.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:-
Vitabu ni nyenzo muhimu sana ya kujifunzia lakini kwa muda mrefu sasa wanafunzi hawana vitabu vya kiada:-
Je, Serikali inawaambia nini Walimu na Wanafunzi wa Shule za Msingi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa vitabu vya kiada kama nyenzo muhimu katika utoaji wa elimu. Kwa umuhimuhuu, Serikali inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanafunzi wa shule za msingi hawakosi vitabu hivyo. Katika kuhakikisha hilo, Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 imechapisha jumla ya nakala 10,232,812 za vitabu vya kiada vya darasa la I-III na kuvisambaza katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Jumla ya mahitaji ya vitabu vya darasa la nne nchini kote ni vitabu 6,700,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imechapa nakala zote za vitabu vya kiada kwa darasa la IV. Kati ya vitabu hivi jumla ya nakala 4 000,000 vimesambazwa. Vitabu hivi vinaenda kugawiwa kwa uwiano 1:1 yaani kitabu kimoja mwanafunzi mmoja. Serikali inakamilisha zoezi la usambazaji katika Mikoa ya Tanga, Morogoro, Mbeya, Iringa na Ruvuma ambayo ilibaki kupokea nakala za kitabu kimoja kukamilisha idadi ya vitabu sita vinavyohitajika. Zoezi hili litakamilika ifikapo tarehe 15 Septemba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imezingatia mahitaji ya Walimu kwa kuchapa na kusambaza vitabu vya kiongozi cha Mwalimu darasa la nne ambapo, jumla ya nakala 190,036 vimechapwa na kusambazwa shuleni. Kwa sasa Serikali inaendelea na uchapaji wa jumla ya nakala 9,000 za vitabu vyote darasa la I-IV kwa ajili ya wanafunzi wenye uono hafifu na nakala 14,000 ya vitabu vya nukta nundu kwa wanafunzi wasioona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa mikakati ya kuboresha elimu, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa vitabu vyote vinapatikana ili watoto wote wa Kitanzania wapate elimu iliyo bora.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:-
Sera ya elimu ya mwaka 2014 inatambua elimu ya msingi kuwa ya lazima bila malipo.
Je, Serikali inaweza kuliambia Bunge hili na Taifa kwa ujumla ni lini ulazima huu utatekelezwa kwa vitendo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza naomba vilevile nipokee pole za Mheshimiwa Mbunge na nitazifikisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, lakini Wizara vilevile imezipokea.
Mheshimiwa Mweyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Jerome Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka utaratibu wa elimu ya msingi kuwa ya lazima na kuweka kipaumbele cha kuhakikisha kuwa kuna fursa sawa ya kupata elimu kwa ngazi hii yaani elimu ya awali, msingi na sekondari hadi kidato cha nne. Kwa sababu hii ndiyo ngazi ya elimu ambayo humpatia mhusika stadi za msingi za kuweza kukabiliana na mazingira yake. Dhana ya elimu bila malipo inazingatia uendeshaji wa shule bila ada wala michango ya aina yoyote ya lazima kutoka kwa wazazi au walezi wa wanafunzi na hivyo kuondoa vikwazo vya uandikishaji na mahudhurio ya watoto shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa sasa utekelezaji wa elimu ya msingi ya lazima ni kwa muda wa miaka saba kama inavyoelekeza Sheria ya Elimu iliyopo yaani Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 Sura ya 353.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa elimu msingi kuwa ya lazima kwa vitendo tangu mwaka 2015/2016 kwa kufidia gharama za uendeshaji wa shule za umma ambapo hupeleka fedha moja kwa moja shuleni kama fidia ya ada, na fedha za rukuzu ya uendeshaji wa shule yaani capitations grands. Serikali pia hupeleka fedha kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wa bweni wa shule za sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mpango huo mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ongezeko la uandikishaji na kuimarika kwa mahudhurio ya wanafunzi darasani. Aidha Serikali inafanya jitihada za kukabiliana na changamoto zilizojitokeza kama vile mahitaji ya vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, maabara, madawati, walimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuhakikisha kuwa elimu inatolewa kwa ubora unaotakiwa.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:-
Mwaka 2017 lilitolewa tamko la kukataza watoto wa shule wanaopata ujauzito kwa sababu yoyote ile kutoendelea na masomo.
Je, kwa katazo hilo, Serikali imejipangaje kuhakikisha kuwa zile sababu zilizo nje ya uwezo wa wanafunzi kuhimili zinapatiwa ufumbuzi haraka?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri, Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Jerome Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua tatizo la wanafunzi wa shule kupata ujauzito wakiwa masomoni kwa sababu mbalimbali zikiwemo zile wasizoweza kuhimili, sababu hizo ni pamoja na kubakwa, kutembea umbali mrefu kufuata shule, na hivyo kupata vishawishi, mila na desturi potofu ambazo humlazimisha au kumuingiza mwanafunzi katika ndoa au mahusiano ya kimapenzi na kukosa mahitaji ya msingi kutoka kwa mzazi, mlezi hali ambayo humlazimisha mwanafunzi kujiingiza katika mahusiano ili aweze kupata mahitaji yake.
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha sababu hizo zinapatiwa ufumbuzi kwa lengo la kumlinda mwanafunzi wa kike Serikali imetekeleza yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, imefanya marekebisho katika Sheria ya Elimu Sura ya 353 Toleo la 2002 kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 ya mwaka 2016 ambayo imeongeza kifungu cha 60(a) ambacho kinatamka wazi kuwa mtu yeyote atakaye muweka ujauzito mtoto wa shule atafungwa miaka 30 au kwa kiingereza naomba ninukuu; “Any person who impregnates a primary school or secondary girl commits an offence and shall on conviction, be liable to imprisonment for a term 30 years.” Imeweka mkazo juu ya elimu ya afya ya uzazi na jinsia katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu yaani unasihi ambayo kwa sasa Wizara imeandaa kiunzi kinachoitwa (guidance and counseling with services a guide for counselors and schools and teacher colleges) kwa ajili kutekeleza huduma hiyo.
Mheshimiwa Spika, pia imezifanya shule zote za sekondari za kidato cha tano na sita kuwa na mabweni hosteli kwa ajili ya wanafunzi wa kike; imehimiza ujenzi wa shule za sekondari kila Kata hasa kwenye maeneo yenye wanafunzi ili kupunguza wanafunzi wa kike kutembea umbali mrefu.
Pia Serikali imejenga hosteli katika baadhi ya shule za sekondai za kata kwenye maeneo ambayo wanafunzi wa kike wanalazimika kutembea umbali mrefu ili kufikia shule na kwenye maeneo ambayo kuna mila na desturi potofu ambazo umlazimisha au kumuingiza mwanafunzi katika ndoa au mahusiano ya kimapenzi.
Mheshimiwa Spika, mwanafunzi wa kike anayekatisha masomo anaweza kujiunga na masomo kupita mipango ya elimu inayotolewa na Taasisi elimu ya watu wazima na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) huandaa na kuendesha programu za elimu mbadala kwa vijana na watu wazima kulingana na mahitaji yao kama vile mafunzo ya muda mfupi na marefu ya ujasiriamali stadi za maisha, ufundi wa awali na programu za kimasomo cha kujiendelea kwa watu wazima ili waweze kuendesha maisha.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:-

Je, ni fedha kiasi gani zilitumika kujenga mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yajulikanayo kama H.E Magufuli Hostel?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan A. Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, mradi wa ujenzi wa mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yajulikanayo kama Hostel za Dkt. J. P. J. Magufuli ulianza rasmi tarehe 1 Julai, 2016 na mabweni hayo yalikamilika na kukabidhiwa rasmi tarehe 15 Aprili, 2017. Ujenzi huo ulifanywa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kama Mkandarasi na kusimamiwa na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, mradi huu uligharimiwa na Serikali kwa kiasi cha shilingi bilioni kumi tu.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:-

Utaratibu wa marejesho ya Mikopo ya Elimu ya Juu umeendelea kukumbwa na changamoto kubwa hasa baada ya ongezeko la asilimia 6 kama retention fee na hivyo kusababisha wanufaika wa mikopo kushindwa kumaliza kurejesha mikopo hiyo?

Je, kwa nini Serikali isilete Muswada wa mabadiliko ya Sheria husika utakaokuwa na masharti rahisi kwa wanufaika ili waweze kumaliza kulipa mikopo kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu hutoza asilimia 6 kwenye salio la deni yaani outstanding loan balance la mnufaika kwa mkopo kama tozo ya kutunza thamani yaani value retention fee. Lengo la tozo hii ni kulinda thamani ya fedha wanazokopeshwa wanufaika wa mikopo ili kuwa na mfuko endelevu utakaoendelea kutoa mikopo kwa wahitaji wengine bila kulazimika kuongeza fedha zaidi kutokana na upotevu wa thamani ya fedha.

Mheshimiwa Spika, kumbukumbu zinaonyesha kuwa wanufaika wanaoanza kurejesha mkopo kwa wakati humaliza kati ya miaka 4 hadi 10 kulingana na kiwango cha mshahara. Hata hivyo, Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya urejeshaji wa mikopo kwa wanufaika ili kuwawezesha kurejesha na kumaliza madeni yao kwa wakati.
MHE. SUSAN A. LYIMO aliuliza:-

Serikali ina utaratibu wa kutoza gharama miili ya marehemu iliyohifadhiwa katika vyumba vya kuhifadhia maiti (Mochwari) Hospitalini na hivyo kusababisha vikwazo na simanzi kwa wanafamilia wasiokuwa na uwezo wa kulipa gharama hizo:-

Je, ni lini Serikali itaacha kutoza gharama miili ya marehemu wanaofia hospitali na kuhifadhiwa katika vyumba vya kuhifadhiwa maiti (Mochwari) ili kupunguza simanzi kwa wafiwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili miili ya marehemu wanaofia hospitali au nje ya hospitali iweze kuhifadhiwa na kustiriwa kwa heshima inahitaji kutunzwa kwenya majokofu yenye ubaridi mkali na wakati mwingine kuwekewa dawa za kusaidia isiharibike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2017, wananchi wanapaswa kuchangia gharama za afya ikiwa ni pamoja na matibabu na hata huduma za uhifadhi wa maiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, panapotokea changamoto ya mwananchi kushindwa gharama za uhifadhi wa maiti mwananchi huyo anapaswa kutoa taarifa kwa uongozi wa hospitali husika ili kupata maelekezo ya namna ya kutatua changamoto hiyo. Ili kuondokana na changamoto kama hizi wananchi wanahimizwa kujiunga na Bima ya Afya kwa lengo la kupunguza gharama za matibabu toka mfukoni.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:-

Je, nini Mkakati wa Serikali kuhakikisha Magereza zetu zinajitegemea kwa chakula?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Lyimo Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha Jeshi la Magereza linajitosheleza kwa chakula cha wafungwa na mahabusu, Serikali imeendelea kulipatia Jeshi zana na pembejeo mbalimbali za Kilimo kupitia fedha za matumizi ya kawaida na za miradi ya maendeleo. Kwenye Bajeti ya mwaka 2018/2019 Serikali imetenga fedha kwa miradi ya maendeleo ya jumla ya shilingi Bilioni tatu kwa ajili ya ununuzi wa zana mbalimbali za Kilimo na kukamilisha miundombinu ya umwagiliaji Gereza Idete.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Magereza linaendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano wa mwaka 2018/2019 mpaka 2022/2023 kwa kutumia raslimali zilizopo ambapo katika msimu wa mwaka 2018/2019 Jeshi limelima jumla ya ekari 5,110 za mazao ya chakula kwa mchanganuo ufuatao; mahindi ekari 3,505, mpunga ekari 1,050 na maharage ekari 555 kwa matarajio ya kuvuna jumla ya tani 9,509.25.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika Awamu ya II ya utekelezaji wa Mkakati huu, Jeshi linaendelea kukamilisha andiko la Mapinduzi ya Kilimo kwa mwaka 2019/2020 na mwaka 2023/2024 likiwa na lengo la kuondokana na utegemezi wa chakula kwa wafungwa na mahabusu kutoka Serikalini.
MHE. QAMBALO W. QULWI (K.n.y. MHE. SUSAN A. LYIMO) aliuliza:-

Je, Serikali inasema nini kuhusu ucheleweshaji wa kupata hati za kumiliki ardhi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa hapo awali kulikuwepo na malalamiko ya ucheleweshaji wa upatikanaji wa hatimiliki za ardhi. Sababu kubwa iliyosababisha changamoto hiyo ni kuwepo kwa Kamishna mmoja tu kwa nchi nzima aliyeruhusiwa kutia saini hati kwa nchi nzima, hali hiyo ililazimu rasimu zote za hati kuwasilishwa Makao Makuu ya Wizara. Hata hivyo, tangu mwaka 2018 mpaka sasa Wizara imefanikiwa kuanzisha jumla ya Kanda 8 za usimamizi wa ardhi kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali ikiwemo hiyo. Utoaji wa hatimiliki za ardhi, upelekaji wa huduma za ardhi katika Ofisi za Ardhi za Kanda pamoja na kutumia mfumo wa kielektroniki katika utoaji wa huduma zimeondoa kwa kasi kubwa changamoto ya kuchelewesha utoaji wa hatimiliki kwa wanachi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na kuanzishwa kwa Ofisi za Kanda, Wizara imejenga Mfumo Unganishi wa Kutunza Kumbukumbu za Ardhi (Integrated Land Management Information System). Mfumo huu unalenga kurahisisha, kuharakisha na kupunguza gharama za utoaji huduma za ardhi. Kwa sasa tayari mfumo huo umeanza kutoa hatimiliki za kielektroniki katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na Ubungo. Aidha, Serikali imekamilisha ufungaji wa mfumo huo katika Ofisi za Ardhi za Manispaa ya Ilala, Kigamboni na Temeka na utaanza kutumika kuanzia Julai 01, 2019. Serikali inaendelea na utaratibu wa kusimika mfumo huu katika halmashauri zote nchini kwa awamu.