Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Suzana Chogisasi Mgonukulima (4 total)

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, sijaridhika na majibu ya Mheshimiwa Waziri hasa kwa baadhi ya wastaafu hao kusitishiwa zoezi wakati walikuwa watumishi wa halali. Hii inaashiria kuwa Serikali haikuwa na orodha sahihi ya wastaafu hao. Pia stahiki walizolipwa ilikuwa ni kusafirishia mizigo na wala siyo kiinua mgongo. Je, Serikali itawalipa lini kiinua mgongo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imeomba fedha ya kulipa madeni kwenye bajeti ya mwaka 2016, je, madeni hayo ni pamoja na ya wastaafu hao?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme kwamba hawa watumishi wa iliyokuwa Afrika Mashariki walipokuwa wanastaafu kazi, mafao yao ya kustaafu yalikuwa yanakokotolewa na kuunganishwa na kipindi ambacho walikuwa wanafanyia kazi Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi chote walichofanyia kazi kwenye mashirika husika. Pamoja na kulipwa mafao yao kwa namna hiyo, walikwenda wakafungua kesi Na.93 ya 2003, wakidai walipwe mafao ya utumishi waliyotumikia kipindi wakiwa Jumuiya ya Mashariki. Serikali iliwaomba tufanye mazungumzo nje ya Mahakama wakakubali na tulifanya mazungumzo na 2005 Serikali ndipo ilikubali kuwalipa wafanyakazi 31,831. Mwezi wa Septemba, tulifikia makubaliano (Deed of Settlement) kwamba baada ya kuwalipa wastaafu hao hapatakuwa na madai mengine tena na ndiyo tuliwalipa kama nilivyoeleza katika jibu la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, swali la ni lini tutawalipa kiinua mgongo tulishamaliza na Serikali haidaiwi tena. Pia ni muhimu nieleze kabisa kwamba pamoja na kufikia Deed of Settlement bado tulitoa muda wa zaidi ya miaka saba ambapo wastaafu walikuwa wanakuja wanalipwa on a case by case basis. Kwa hiyo, Serikali hatudaiwi tena na wastaafu hao.
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na
majibu ya Waziri, Manispaa ya Iringa ina miradi mikubwa ya Machinjio ya Kisasa
ya Ngelewala, Soko la Ngome, Sekondari ya Mivinjeni, Nyumba za Waganga na
Wauguzi wa Zahanati ya Njiapanda na Nduli. Katika Baraza la Madiwani, kupitia
bajeti ya mwaka 2016/2017, Manispaa ya Iringa ilikadiria kukusanya mapato ya
ndani Sh. 4,532,000,000 ili kuweza kumalizia miradi midogo iliyokuwa inaikabili
Manispaa hiyo. Manispaa ya Iringa, vyanzo vikuu vya mapato vinatokana na
kodi ya majengo, Serikali ikaamua kodi hizi za majengo zikusanywe na TRA, je, ni
lini Serikali itaona umuhimu wa kupeleka hela za miradi hii kwa wakati ili kuweza
kumalizia miradi ambayo haijamalizika hadi sasa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika,
napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inaona umuhimu wa
miradi yote ya maendeleo kama ilivyopitishwa katika bajeti yetu mwezi Juni.
Hivyo, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, kinachopelekea kupeleka
fedha hizi ni upatikanaji wa fedha hizi. Kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge
ameongelea kuhusu kodi ya majengo, naomba nimwambie kwamba TRA
imekusanya kodi ya majengo mwezi wa Kumi, baada ya quarter ya kwanza
kupewa Halmashauri zenyewe kukusanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge,
anapuhudhuria Baraza la Madiwani aweze kusimamia mapato yaliyopatikana ili yaweze kutumika katika miradi aliyoitaja. Serikali yetu baada ya kukusanya
kuanzia mwezi wa Kumi, fedha zote tulizoahidi zitarejeshwa katika Halmashauri
husika kutokana na bajeti zilizopitishwa.
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitauliza maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Susane Maselle, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kutokana na majibu ya Naibu Waziri kuwa wachimbaji hawa wadogo walipata leseni, je, Serikali inatoa kauli gani juu ya Jeshi la Polisi lililotumia nguvu kupiga mabomu wachimbaji hao wadogo na kuwanyanyasa wenyewe na familia zao na kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia wanawake na watoto? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, je, Naibu Waziri yupo tayari kuongozana na Mheshimiwa Susane Maselle kwenda eneo hilo kuongea na wananchi hao kuhusu vitendo walivyofanyiwa na Jeshi la Polisi kuwa hawakufanyiwa kiusahihi kwa sababu walikuwa na leseni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na swali la pili, niko tayari kufuatana na Mheshimiwa Susane na kwa ridhaa yako kama itapendeza basi nitafuatana naye, nitembelee maeneo yale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na wachimbaji hao kupigwa mabomu pamoja na kufanyiwa harassment ni suala ambalo linatakiwa litazamwe kwa kina sana unaweza usiwe na jibu la moja kwa moja. Ninachoweza kusema ni kwamba pale inapotokea kunakuwa na vurugu katika maeneo ya uchimbaji kazi ya Jeshi la Polisi ni kutuliza ghasia ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na amani na utulivu katika maeneo yale. Inawezekana ilifanyika katika hatua hiyo, lakini Mheshimiwa Mbunge tutakaa pamoja tuone ni hatua gani zilichukuliwa ili tushirikiane na wenzetu wa Mambo ya Ndani tuone nini cha kufanya zaidi.
MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la barabara la Makambako - Songea yanafanana na matatizo ya barabara inayotoka Mwatasi -Kimara – Idete - Idegenda ambako uzalishaji wa mbao pamoja na matunda aina ya pears ni wa kiwango kikubwa sana lakini hali ya barabara hii siyo nzuri. Ni lini Serikali sasa itafanya mpango mkakati kuhakikisha hizi barabara zinatengenezwa kwa kiwango cha lami ili kupelekea usafirishaji wa mbao uwe salama na safi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Songea - Makambako ni trunk road wakati barabara anayoongelea ni ya district. Ni kweli zinafanana kwa sababu zote ni barabara lakini zina hadhi mbili tofauti na district road zinashughulikiwa na Halmashauri chini ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na hoja yake lakini naomba Watanzania wote tuungane kama watu wamoja, tuweke vipaumbele vya hizi barabara na vile ambavyo tunakubaliana tuanze navyo, tuanze navyo, kwa sababu hatimaye fedha zinahitajika na hatuwezi kujenga barabara zote kwa wakati mmoja, ni lazima tuanze hizi, baadaye tunafuata hizi, hatua kwa hatua. Kwa hiyo, nimuombe avute subira itafika wakati baada ya kukamilisha zile ambazo tumekubaliana ni vipaumbele chini ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2015 - 2020 tutakuja huku ambako Mheshimiwa Mgonokulima anakuongelea.