Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Susanne Peter Maselle (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SUZANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuwasemea Wanamwanza. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako hili Tukufu, naomba nami nitoe shukrani kwa chama changu ambacho kimeniteua kusimamia Mkoa wa Mwanza kwa sababu wamejua kwamba naweza na nitakitendea haki. Nawashukuru pia akinamama wa CHADEMA wa Mwanza kwa kuniteua mimi na wananchi wa Mkoa wa Mwanza kwa kuniamini na kunituma ili nishughulikie kero zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wanamwanza hasa wavuvi, wafugaji na wakulima wamenituma niwasemee yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawa wanathamini sana habari na taarifa ndiyo maana Wavuvi wakiwa katika uvuvi huwa wanasikiliza redio, wanakuwa na redio. Wafugaji wanapokwenda kuchunga wanakuwa na redio na wakulima vile vile na ndiyo maana kuna redio zinaitwa redio za wakulima. Wamenituma nije niseme kwamba kwa Serikali kukatiza kuonesha live Bunge ni kuwanyima haki yao ambayo inatokana na kukatwa kodi zao. Kwa hiyo, wameniambia kwamba nilisemee hilo na nimelisemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wenzetu wamekuwa wakiunga mkono kwa sababu wanajua ni nini wanakuja kukifanya. Wamefanya hili Bunge ni kama resting house. Wanalala, tunawaona kwenye magazeti wamesinzia na ndiyo maana wanaleta hoja ya kwamba Bunge lisioneshwe live kwa sababu wanajua adhabu itakayowapata na kuna wengine ambao adhabu hiyo imeshawapata, hawakurudi Bungeni hapa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kuwasemea wavuvi. Wavuvi wamekuwa wakinyang‟anywa nyavu zao na kuchomewa moto; lakini sitaki nionekane na-support ila swali langu ni kwamba je, hawa watu wanaouza hivi vitu na viwanda vinavyotengeneza si wanajulikana? Kwa nini Serikali inaendelea kuchukua kodi kwao na kuwanyamazia? Hii ni double standard! Ndiyo maana Mkoa wa Mwanza ulipotangazwa kwamba ni mkoa unaoongoza kwa watumishi hewa, matokeo yake Mkuu wa Mkoa alihamishwa na kupelekwa sehemu nyingine wakati yeye ndiye aliyekuwa anasimamia mkoa huu na anasimamia watumishi hao. Hilo lilikuwa ni jipu ambalo lilitakiwa kutumbuliwa mapema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na uvamizi wa wavuvi na kunyang‟anya vifaa vyao vya uvuvi ambavyo wamevinunua kwa shida na kwa kujinyima. Naomba Serikali idhibiti hao wanaowanyang‟anya kwa sababu ulinzi umekuwa ukiwekwa kipindi tu ambacho sikukuu zinakaribia, lakini wanyang‟anyi hao wamekuwepo kila wakati. Kwa hiyo, naomba Serikali iimarishe ulinzi katika Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia kuhusu vifaa vya uvuvi. Wavuvi wamekuwa wakiuziwa vifaa vya uvuvi kwa bei ghali sana. Kwa mfano, kama engine ya Boti imekuwa ikiuzwa shilingi milioni nne mpaka shilingi milioni nne na nusu. Kwa mwananchi wa kawaida wa kipato cha chini hawezi ku-afford kununua engine ya shilingi milioni nne, kwa maana hiyo basi, tunaomba Serikali iwe inakopesha vifaa hivyo kwa wananchi wetu ambao wana kipato cha chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu kilimo. Mawakala wamekuwa wakiwauzia wakulima mbegu ambazo zimeoza, ambazo hazisaidii kwa kilimo. Kwa mfano, tarehe 22 Februari, 2016, wakulima wa Pamba wa Magu walikuwa wakiilalamikia Serikali kuhusu mawakala kuwauzia mbegu ambazo zimeoza na hii ilisababisha kero kubwa sana, lakini sikuona Serikali kuchukua hatua yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inavunja nguvu wakulima wetu kwa sababu wanapotoa malalamiko kwa Serikali na Serikali kunyamaza kimya, inaonekana kama vile wamedharaulika. Tukizingatia kwamba tunaenda kuingia kwenye uchumi wa viwanda na hatuko serious na hiki kilimo, sijui hivyo viwanda tutaviendesha vipi. Naomba Serikali na Wizara iwe inasikiliza maoni ya wananchi ili tuweze kusonga mbele na tusiwavunje moyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie Kiwanda cha Mwatex. Kiwanda hiki kimekuwa kikifanya kazi kwa kusuasua; na hii ni kwa sababu ya tatizo la umeme. Umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara. Kwa maana hiyo basi, kama tunakwenda kuwa na uchumi wa viwanda, tunaomba kwanza tuanze na hivi viwanda vyetu ambavyo vilikuwepo vilivyokuwa vinatoa ajira kwa mama zetu, wakipeleka pamba; ilikuwa inawasaidia hata kuendesha maisha yao. Leo hii tunasema kwamba tunataka kwenda kwenye uchumi wa viwanda huku viwanda vilivyokuwepo hamjavishughulikia. Tutakuwa kama vile tutacheza makida makida. Naiomba Serikali sasa iamue kwanza kukarabati viwanda ambavyo vilikuwepo Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumizie kuhusu ufugaji. Tanzania tuna mifugo mingi sana, lakini wafugaji wetu hawana elimu. Naomba Wizara husika itoe elimu kwa wafugaji hawa. Tunashindwa kuuza ngozi zetu katika masoko ya Kimataifa kwa sababu ngozi zetu hazina kiwango. Ng‟ombe anawekewa alama mwili mzima, sasa unapopeleka ngozi ya aina hiyo, huwezi kupata soko zuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo basi, naiomba Wizara husika itoe elimu kwa wafugaji wetu jinsi ya kutunza hizi ngozi. Kuna sehemu ya mwili wa ng‟ombe ambapo unaweza ukaweka alama na isiathiri ngozi. Kwa hiyo, waende mpaka kijijini wakatoe elimu hiyo ili tuweze kupata masoko mazuri katika masoko ya Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kiwanda ambacho kipo Mwanza, Ilemela, sehemu ya Saba Saba. Kile kiwanda kimekuwa godown. Sasa unashangaa yule aliyeuziwa alitoa nini kwa Serikali mpaka anashindwa kufuatiliwa? Kiwanda kimekuwa godown ya vyuma chakavu na Serikali inaangalia tu, mpaka najifikiria kwamba kulikuwa kuna nini hapo? Labda aliyeuziwa alikuwa ametoa kitu ambacho kinafanya Serikali inyamaze kimya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba viwanda hivyo vifuatiliwe kwa sababu ni aibu na ni dharau kwa Serikali. Mwekezaji anapewa kiwanda na anashindwa kukiendeleza na Serikali inanyamaza tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema kwamba sisi Wasukuma sio wavuta bangi. Hapo nyuma kuna Mbunge alisema kwamba Wasukuma bangi huwa inatusaidia kupata nguvu za kwenda kulima. Mimi nimezaliwa Mwanza na ni Msukuma; ninachofahamu ni kwamba sisi huwa asubuhi tunakula ugali na maziwa, tunakwenda kulima na ndiyo maana hata miili yetu ukiiangalia unaiona imepanda; hakuna Msukuma ambaye ni legelege. Nina wasiwasi sana na huyu Mbunge inawezekana siyo Msukuma. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuongelea kuhusu athari za upungufu mkubwa wa dawa na chanjo kwa akinamama na watoto. Itakumbukwa kuwa mwishoni mwaka jana hadi mwanzoni mwa mwaka huu na sina uhakika kama tatizo hilo limekwisha hadi tunapozungumza hapa ndani sasa kwenye Mkutano wa Bajeti, nchi yetu ilikumbwa na ukosefu au upungufu mkubwa wa dawa pamoja na chanjo za magonjwa mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ilikuwa mbaya kiasi cha Serikali kujichanganya katika kauli zake za kujitetea na kutaka kuonesha kuwa lilikuwa suala dogo lakini ukweli ni kwamba halikuwa suala dogo ndiyo maana Makamu wa Rais alisema kauli nyingine Wizara wakasema kauli nyingine. Wakati Waziri mhusika, Mheshimiwa Ummy Mwalimu akisema kuwa hakuna tatizo la ukosefu wa dawa na kwamba hizo ni habari za kwenye mitandao tu, kesho yake bosi wake, Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu akiwa pale Mwananyamala Hospitali akakiri kuwa nchi ina tatizo la upungufu mkubwa wa dawa na chanjo lakini eti halitakuwa la muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukiri kule, kauli ile ya Serikali ilikuwa ni ya ajabu na ilikuwa na ukakasi mkubwa sana masikioni mwa Watanzania ni kama vile walikuwa wanaambiwa wavumilie hali hiyo kwa sababu haitakuwa ya muda mrefu. Hivi kuna mahali mnaweza kucheza na maisha ya Watanzania kama kwenye afya na matibabu (uhai)? Hivi mnawezaje kusema ukosefu wa dawa halitakuwa tatizo la muda mrefu bali mfupi tu huku mnajua kuwa wakati huo kuna wagonjwa hospitalini wanahitaji dawa na wanakufa kwa kukosa dawa? Mnawezaje kusema kuwa tatizo hilo halitakuwa la muda mrefu wakati kuna akinamama wajawazito hospitalini wanasubiri matibabu na wengine wamejifungua wanahitaji matibabu na watoto wao wanahitaji chanjo? Huku ni kucheza na maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupata taarifa ya Serikali na wananchi wangu wa Mwanza wanataka kusikia Serikali ikisema hapa Bungeni, je, akina mama wangapi hususan wajawazito na wale waliojifungua na watoto waliozaliwa wameathirika na ukosefu huo wa dawa na chanjo hospitalini? Tumefikia hatua nchi inakosa dawa na vifaa tiba na chanjo za kifua kikuu, polio, surua, lubele, kichaa cha mbwa, manjano na magonjwa mengine hatari kwa afya ya mama na mtoto. Kwa hiyo, Watanzania na kipekee wananchi wa Mwanza wangependa kusikia Serikali ikiliambia Bunge hili athari ambazo Taifa hili limepata na litazipata miaka mingi ijayo kwa kitendo cha akinamama wajawazito kukosa dawa na chanjo, akinamama waliojifungua na watoto wao kukosa dawa na chanjo, nini athari zake kwa jamii yetu ambayo bado inapambana na utapiamlo, udumavu na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ujenzi wa vituo vitatu kila Halmashauri kuboresha huduma na uchunguzi na matibabu ya mapema ya saratani ya matiti na mlango wa kizazi kwa kina mama. Hivi karibuni wakati akizindua kampeni ya bure ya uchunguzi wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi kwa akinamama iliyofanyika mjini Mwanza, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu alisema kuwa Serikali ina mpango wa kujenga vituo vitatu kwa kila Halmashauri nchini kwa ajili ya kuboresha huduma na uchunguzi na matibabu ya mapema ya magonjwa hayo ili kuwanusuru akinamama. Ilisemwa kuwa zimetengwa shilingi bilioni saba na Serikali hii na Benki ya Dunia itasaidia shilingi bilioni tano katika kufanikisha suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimepitia taarifa ya bajeti ya Wizara hii kuangalia utekelezaji wa kauli hiyo ya Serikali sijaona mahali ambapo fedha hizo zimetengwa. Wananchi wa Halmashauri za Mwanza wanasubiri kwa hamu kuona utekelezaji huo ambao utaweza kuokoa karibu wanawake asilimia 60 walioko katika hatari ya vifo vinavyosababishwa na magonjwa hayo huku wakiacha nyuma watoto wanaohitaji malezi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia Serikali ituambie hapa imefikia wapi katika kusogeza huduma za magonjwa hayo katika hospitali za Bugando na KCMC kama alivyosema Makamu wa Rais ili kupunguza mahitaji ambayo hospitali ya Ocean Road inakabiliana nayo kwa sasa. Pia naomba kujua maendeleo ya kampeni hiyo ya bure hususan kwa Mkoa wa Mwanza ambayo ingepaswa kwenda sambamba na utoaji wa elimu au kujikinga au kuzuia magonjwa hayo kwa akinamama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kampeni ya malaria na ugawaji wa taulo za usafi wa mwili kwa mabinti kwenye shule zetu. Hivi karibuni taarifa kutokana na tafiti zilizofanyika zilionesha kuwa wasichana walioko shule au walio na umri mdogo wanapata athari kubwa sana kutokana na ugumu wa kupata mahitaji ya taulo za usafi wanapokuwa katika mzunguko wao wa kila mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, athari hizo ni mimba za utotoni kwa sababu ya kudanganywa ili wapate fedha za kununua taulo; wanashindwa kuhudhuria shuleni na kukosa masomo kwa siku tano hadi saba kila mwezi; kupunguza uwezo wao wa kufaulu kwa kukosa masomo na kuwa katika uwezekano wa kupatwa na magonjwa mbalimbali kutokana na kutumia vifaa visivyo sahihi na visivyo salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kumekuwepo na kampeni kubwa dhidi ya malaria ambayo nasikia imefika hadi kwetu Buchosa kwa ajili ya kupulizia dawa ndani na kwenye kuta za nyumba, ni wakati muafaka sasa Serikali ikalivalia njuga na kulipatia uzito mkubwa suala la kuwasaidia hawa watoto na mabinti zetu walioko shuleni wapate taulo hizo ili wabakie shuleni wasome, waepuke mimba za utotoni na magonjwa hatarishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara walione hili na walichukue kwa uzito mkubwa sana. Inaweza hata kwa kuanzia kushirikiana na watu au mashirika ambayo tayari yameanza kampeni hii kama walivyokuwa wakifanya watu wa East Africa Television na East Africa Radio ambao walifanya kampeni kubwa kuhamasisha watu kusaidia mabinti hawa walioko shuleni wanaoteseka kwa sababu ya kukosa taulo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, matibabu ya bure kwa wazee, kambi ya wazee wa Bukumbi na kambi ya walemavu Misungwi. Wazee wangu wa Mwanza, maeneo ya Buchosa, Sengerema, Ilemela, Nyamagana, Magu, Sumve, Ukerewe, Kwimba na Misungwi bado wanasubiri lini Serikali itatekeleza kwa dhati huu mpango badala ya kuwa kwenye makaratasi na maneno ya hapa Bungeni na kwenye mikutano au semina au warsha na makongamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati lilifanyika zoezi la kutoa vitambulisho kwa wazee wanaotakiwa kutibiwa bure, naomba Serikali kupitia Bunge lako iwaambie Watanzania zoezi hili limefikia wapi na wazee wangapi wamepata hivyo vitambulisho hususan kwa Mkoa wetu wa Mwanza ambako wazee wetu waliotumikia Taifa letu wakiwa wakulima, wafugaji, wafanyakazi Serikalini sasa wamestaafu wanahangaika sana kupata matibabu. Tunaomba mtuambie kama mtaweza kuitekeleza kwa vitendo sera hiyo ambayo tunajua haikuwa ya kwenu. Kama imewashinda tuwaambie wazee wetu na watu wengine ambao tu wazee watarajiwa kuwa hilo litawezekana tu pale ambapo Serikali ya UKAWA itaingia madarakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Mwanza wanapata shaka sana iwapo Serikali itaweza kutekeleza kwa vitendo sera hiyo wanapoangalia kambi ya wazee wasiojiweza ya Kigongo, pale Misungwi namna ambavyo wazee wale wametelekezwa na Serikali, hawana dawa, wanasumbuliwa na magonjwa na hawawezi kutibiwa, wanapangiwa bajeti isiyotosheleza kwa chakula wala matibabu. Hali hiyo mbaya ya kituo cha wazee cha Misungwi ambayo hata Mama Janeth Magufuli aliishuhudia mwenyewe haijaishia hapo pekee, kuna kilio kikubwa pale shule maalum ya walemavu wa ngozi ya Mitindo iliyoko Misungwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara hii ambayo inashirikiana na Wizara zingine kuhakikisha watoto wale wanapata stahili za kulinda afya zao. Vinginevyo iko siku tutaona machozi mengine humu Bungeni kuwalilia watoto wale kama ambavyo Waziri Mkuu aliyepita alitoa machozi kwa ajili ya albino.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. SUSANNE P. MASELLE: nakushukuru Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabla sijaanza kuchangia napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuilinda familia yangu, hasa baba yangu ambaye alikuwa anaumwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nipongeze hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani ambayo imesheheni vitu vingi sana na vya muhimu ambapo Serikali kama itavichukua na kuvifanyia kazi, basi sekta hii itafanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia kuhusu uvuvi. Kanda ya Ziwa katika sekta hii ina umuhimu sana hususan Mkoa wa Mwanza, maeneo ya Buchosa, Magu, Kwimba na Ilemela wanategemea sana uvuvi, lakini Serikali naona kama haitilii umuhimu sana hii sekta. Kwa sababu gani nasema hivi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wamekuwa wakinyanyaswa sana kwa kunyang’anywa nyavu zao. Siyo kwamba nabariki watumie nyavu ambazo hazifai, la hasha! Mwaka 2016 nilizungumza nilivyokuwa nachangia kwamba Serikali inatakiwa itoe elimu jinsi ya kutumia hizi nyavu, ni nyavu gani wavuvi wanatakiwa watumie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza na Waheshimiwa Wabunge wengi sana walizungumza kwamba ni kwa nini maduka bado yapo ambayo yanauza; na viwanda vinatengeneza nyavu hizo? Wavuvi hawa wamekuwa wakinunua kwa kutumia pesa, matokeo yake, wananyang’anywa, zinachomwa na wanajikuta wanaingia katika umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Februari kulikuwa na mgomo wa wavuvi na Serikali ikasema kabisa kwamba inaunga mkono mgomo huo. Sasa mimi nikashangaa ni kwa nini Serikali iunge mkono badala ya kutatua tatizo? Maana yake ni kwamba inaunga mkono tuwe na watu ambao hawana kipato na mtu asipokuwa na kipato matokeo yake anakuwa anafikiria mawazo mabaya ambayo yanapelekea hata kujiingiza katika vitendo vibaya ambavyo siyo vizuri kwa jamii. Kwa mfano, tunaweza tukatengeneza watu ambao ni vibaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetaka tu Serikali na Mheshimiwa Waziri anapokuja atuambie ni mkakati gani walionao wa kuweza kutatua hili tatizo ili wananchi wetu waweze kufanya hii shughuli wakiwa na amani na kusiwe na ile tabia ya Serikali na wavuvi kuviziana. N kama vile wanaviziana kwamba wakitumia hizo nyavu na wenyewe wanakuja kuwanyang’anya ni kama kuviziana. Sasa tukitoa elimu, tutakuwa tumewasaidia sana watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu kilimo, Mkoa wa Mwanza una eneo kubwa, takribani asilimia 53 ambalo limzungukwa na Ziwa Victoria. Hii inatoa nafasi kubwa kwa kilimo cha umwagiliaji, lakini mpaka sasa sijaona hatua yoyote ambayo imechukuliwa ili tuwe na kilimo cha umwagiliaji katika Mkoa Mwanza. Wakulima wengi wamekuwa wakitegemea kilimo ambacho ni cha majira, lakini majira yakibadilika, wanashindwa kulima. Kama kwa sasa, kumekuwa na ukame, tungekuwa na kilimo cha umwagiliaji wananchi wetu wangeweza kulima bila kutegemea majira ambayo yanakuwa yanawaangusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona chakula kimekosekana na wananchi wanapolalamika, kwa mfano Mheshimiwa Rais alikuja, nafikiri ilikuwa ni Shinyanga, watu wakamwabia kwamba wana njaa na akawaambia hawezi kuwapikia. Wanaposema kwamba wana njaa, siyo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Wizara hii. Kabla sijaanza kuchangia napenda kutoa pole kwa wananchi wa Mwanza kwa tetemeko ambalo limetokea jana na pia nitoe pole nyingi kwa askari wetu Joyce ambaye alifariki kwa kupata mshituko na majeruhi wengine ambao wamepelekwa hospitali, natoa pole sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ulikuja Mwanza najua ulifanya mambo mazuri sana kama alivyoongea Mbunge wa Nyamagana, lakini kuna migogoro ambayo hukuipitia, kuna migogoro ambayo iko Ilemela. mwaka 2009 Jeshi la Wananchi lilifanya utambuzi wa maeneo yake na iligundulika eneo la Mlima wa Nyagungulu Kata ya Ilemela ilikuwa inafaa kwa makazi ya Jeshi. Sasa utambuzi huu baada ya kufanyika ilionekana kuna kaya 448 ambazo zilikuwa na makazi ya kudumu na tarehe 04 Novemba, 2014 ilifanyika tathmini ambapo Serikali ya Mkoa pamoja na Jeshi la Wananchi waliona kwamba wananchi hao wanapaswa kulipwa, na waliamua kwamba baada ya tathmini hiyo walisema kwamba ndani ya miezi sita wananchi hao wangekuwa wameshalipwa, lakini mpaka sasa bado hawajalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna nyumba zingine ambazo ni za udogo mpaka zimeanza kuanguka hawawezi kufanya marekebisho yoyote au kuzikarabati kwa sababu wanaogopa eneo hilo linachukuliwa na Jeshi. Sasa Mheshimiwa Waziri ninaomba umalize huu mgogoro kwa sababu hawa wananchi wanateseka na wananchi wengi wamekuwa wakilalamika, wameandika barua nyingi sana. Wameandika barua kwa Mkuu wa Mkoa, barua hizi hapa nitakuletea, wameandika kwa Mbunge…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)