Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Susanne Peter Maselle (5 total)

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y. MHE. SUSANNE P. MASELLE) aliuliza:-
Mwaka 2007 Serikali ilipima viwanja vya Luchelele Wilayani Nyamagana, Mwanza na iliendelea na mpango huo ambapo mwaka 2012 ilifanya tathmini na uhakiki kwa ajili ya kulipa fidia lakini hadi leo wananchi hao hawajawahi kulipwa fidia zao.
Je, Serikali inatoa kauli gani kwa wananchi hao wa Luchelele kuhusu hatma yao hasa ikizingatiwa kuwa Waziri wa Ardhi alitoa ahadi mwaka 2015 kuwa atalitatua tatizo hili ndani ya mwezi mmoja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susanne Peter Maselle, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Luchelele lilipimwa mwaka 2008 likiwa na ukubwa wa hekta 873.38 ambapo viwanja vilivyopimwa ni 3,583. Katika zoezi hilo wapo wananchi waliokuwa ni wamiliki wa asili wa eneo hilo wapatao 683 ambao kwa makubaliano maalum yaliyofanyika tarehe 27/01/2013 chini ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, wamemilikishwa viwanja badala ya fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanaodai fidia katika eneo la Luchelele ni wale ambao walikutwa katika maeneo yao lakini baada ya upimaji, maeneo hayo ni kwa ajili ya Taasisi au barabara na idadi yao ni 671. Wananachi hao wanadai fidia ya shilingi bilioni sita. Kauli ya Serikali ni kwamba wananchi hao watalipwa fidia na tayari Halmashauri imeomba mkopo kutoka Benki ya CRDB ambao wamekubali kutoa mkopo huo ili wananchi hao waweze kulipwa fidia
MHE. SUSANNE P. MASELLE aliuliza:-
(a) Je, Serikali imechukua juhudi gani za makusudi kudhibiti vitendo vya kubambikizia watu kesi vinavyofanywa na baadhi ya askari wasiokuwa na maadili?
(b) Je, Serikali itakuwa tayari kuanzisha kitengo cha siri ndani ya Jeshi la Polisi kitakachoshughulikia adha hii?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susanne Maselle, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni, miongozo pamoja na taratibu na wale wanaobainika kukiuka maadili ya Jeshi, huchukuliwa hatua kwa kuwashitaki kijeshi kwa mujibu wa PGO 103 na 104 kwa kuwapa adhabu mbalimbali ikiwepo kuwafukuza kazi anaobainika kukiuka maadili ya Jeshi ikiwemo kubambikia watu kesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imefanya jitihada za kuanzisha Kitengo cha Malalamiko katika ngazi ya Makao Makuu, Mikoa na hata Wizara ili kutoa mwanya kwa mtu yeyote anayeona kuwa ameonewa, kuwasilisha malalamiko yake na malalamiko hayo kushughulikiwa. Hata hivyo, raia wanayo haki ya kulalamika katika vyombo vingine vya kisheria wanapoona hawatendewi haki kwa mujibu wa sheria za nchi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi limeweka wazi utaratibu wa namna ya kuwashughulikia askari wasio waaminifu, hivyo halitakuwa tayari kuanzisha kitengo cha siri kwa kazi hiyo kwani utaratibu uliopo unashuhudia na umekuwa na mafanikio.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, siku za usoni kama hivyo ilivyo kwa mikoa michache hapa nchini ambapo kazi ya polisi itabaki kuwa ni ya kupeleleza kesi na mwenye mamlaka ya kupeleka kesi mahakamani ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali. (Makofi)
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA (K.n.y. MHE. SUSANE P. MASELLE) aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali imewanyang’anya ajira vijana waliokuwa wamejiajiri kwenye Machimbo ya Ishokelahela na baadaye ikaamua kubadili umiliki wa leseni kwa siri?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susane Peter Maselle, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachimbaji wadogo waliokuwa wanachimba Ishokelahela hawakuwa na leseni ya uchimbaji bali walikuwa wanachimba katika eneo la utafiti la leseni ya Kampuni ya Carlton Kitongo Tanzania Limited.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, mwaka 2014, Serikali ilifanya mazungumzo na kampuni hiyo na kuwapatia wachimbaji wadogo hao leseni mbili za uchimbaji zenye jumla ya hekta 20. Wananchi hao waliweza kuunda kampuni yao inaitwa Isinka Federation Miners Co-operative Limited.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 kikundi kiliamua kubadilisha leseni zake mbili za uchimbaji mdogo na kuzifanya kuwa leseni moja ya mgodi wa uchimbaji wa kati lakini chini ya Kampuni yao ya Isinka Federation Miners Co-operative Limited. Umiliki wa leseni hizo haujabadilishwa hadi leo upo chini ya umiliki wa wachimbaji hao wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Machi, 2017, mgodi ulikuwa umeshakusanya tani 35,000 za mbale (ore) kwa njia ya ubia wa Kampuni ya Busolwa Mining pamoja na wachimbaji hao na waliweza kutoa fursa za ajira 164 za moja kwa moja.
MHE. SUSANNE P. MASELE aliuliza:-
Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, imekuja na mikakati yake mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakiki watumishi wa umma, zoezi ambalo halikuwekewa muda wa kuanza na kumaliza (time frame) hali hiyo imesababisha usumbufu mkubwa na hata kuharibu mfumo wa watumishi wa umma, ikiwemo namna ya kuajiri.
(a) Je, Serikali inatoa kauli gani kwa watumishi wa umma walioajiriwa na kusainishwa mikataba ya ajira ndani ya Serikali ambapo ghafla mwaka 2016 Rais alitoa kauli ya kusimamisha ajira kupisha ukaguzi wa watumishi hewa?
(b) Je, Serikali inatambua kuwa watu hao tayari walikuwa watumishi na mchakato wa kuwaingiza kwenye payroll ulishaanza, lakini ukasitishwa ghafla na sasa wako mtaani na hawajui hatma yao?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susanne Peter Masele, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba watumishi wote ambao walisitishwa kuingizwa katika orodha ya malipo ya mishahara (payroll) mwezi Mei, 2016 waliokuwa wakipisha zoezi la uhakiki wa watumishi wamesharudishwa katika orodha ya malipo na sasa wanaendelea na kazi na wamekuwa wakilipwa mishahara yao kama kawaida.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika sehemu (a) ya swali la Mheshimiwa Masele, watumishi hao wanatambuliwa kama watumishi wengine wa umma.
MHE. SUSANNE P. MASELE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza kauli ya Mheshimiwa Rais kuhusu kuwapatia wachimbaji wadogo wadogo kipaumbele cha leseni na vibali vya kuchimba madini kwa kuonesha mfano kwa wachimbaji wadogo wa machimbo ya Dhahabu ya Ishokelahela, Misungwi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Susanne Masele naomba nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mungu kwa kunipa kibali cha kusimama hapa, lakini vile vile nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa Imani kubwa aliyonipatia na akaona naweza kumsaidia kwenye Sekta hii ya Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Susanne Peter Masele Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachimbaji wa Madini wadogo wa Ishokelahela Wilayani Misungwi walivamia na kuanza shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la Leseni kubwa ya utafutaji wa madini inayomilikiwa na Kampuni ya Carlton KitongoTanzania Limited yenye ukubwa wa kilomita za mraba 12.4 tokea mwezi Julai, 2017. Kabla ya hapa wachimbaji hao walikuwepo lakini kwa kiasi kidogo. Mpaka kufikia sasa leseni hiyo imevamiwa na wachimbaji wadogo zaidi ya 1000 ambao wanachimba madini hayo ya dhahabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leseni ya Carlton KitongoTanzania Limited ilitolewa tarehe 5 Agosti, 2014 na itamaliza muda wake wa awali tarehe 4 Agosti 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi kwa kushirikiana na kampuni ya Carlton Kitongo Tanzania Limited ambaye ni mmiliki wa leseni hiyo waliamua kutenga eneo kwa ajili ya kuwaachia wachimbaji wadogo ambalo likuwa linamilikiwa na kampuni hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makubaliano hayo yalihitimishwa rasmi mwezi Desemba mwaka 2017 kati ya mmiliki wa leseni na vikundi ambayo viliungana kuunda kikundi kimoja kwa jina la Basimbi and Buhunda Mining Group. Nakala ya makubaliano hayo ipo Ofisi ya Madini Mwanza na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Misungwi. Vikundi hivyo vilipatikana baada ya Wizara kupitia Ofisi yetu ya Madini Mkoani Mwanza kutoa elimu ya umuhimu ya kujiunga katika vikundi na kuendesha shughuli za uchimbaji madini ili ziweze kuwa na tija zinazozingatia matakwa ya Sheria ya Madini na Kanuni zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza kauli ya Mheshimiwa Rais kuhusu kuwapatia wachimbaji wadogo kipaumbele cha leseni na vibali vya kuchimba madini, leseni za wachimbaji madini katika eneo hilo zitatolewa kwa vikundi hivyo mara tu baada ya taratibu za kisheria za kushughulikia maombi hayo kukamilika.