Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Upendo Furaha Peneza (4 total)

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenisaidia na nimeweza kupata nafasi ya kuwa mwakilishi ndani ya Mkoa wa Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vile vile naomba nichukue muda huu pia kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini kwa sababu katika kikao kilichopita niliuliza maswali kutokana na madhara mbalimbali yanayowapata wananchi wa Geita Mjini kutokana shughuli za mgodi na aliwajibika kama alivyoahidi ndani ya Bunge lako Tukufu kufika na kuongea na wananchi, kutembelea sehemu za waathirika.
Mheshimiwa Spika, nina imani hatua tuliyofikia hatimaye hawa wananchi yawezekana wakaondolewa katika eneo husika, lakini pia ataweza kuwasaidia vijana wengi waliojiunga na ushirika na wataweza kupewa maeneo ya kuchimba dhahabu katika maeneo ya Mkoa wa Geita.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika huu Mpango, tunazungumzia sana maeneo ya viwanda na katika kuangalia eneo kubwa la viwanda, katika Mpango wanaonesha ni jinsi gani ambavyo Serikali imejipanga na kuwekeza katika maeneo ya viwanda. Wameongelea maeneo ya EPZ na SEZ, wameongelea pia maeneo ya industrial park. Vile vile ukisoma ule Mpango wa mwaka mmoja ulikuwa unazungumzia ni namna gani hizi EPZ na SEZ hazijaweza kuchangia vya kutosha katika pato letu la Taifa.
Mheshimiwa Spika, tukiongelea masuala ya viwanda, tunaongelea mambo ya EPZ, lakini tunawapa watu maeneo makubwa ya kuwekeza, hawa watu pia tunawapatia misamaha ya kodi. Kwa hiyo, tunawapa maeneo ya kuwekeza lakini bado kama Serikali tunapoteza kodi. Kwa hiyo, ni vizuri pia Serikali ikaliangalia hili suala kwamba tunasema kuweka viwanda lakini kitu cha kwanza tuboreshe vitu vya msingi ambavyo ndivyo vinavyohitajika ili kuweza kupunguza kutoa misamaha ya kodi.
Katika hotuba ya Kambi ya Upinzani, imeweza kuonesha ni jinsi gani katika upande wa nishati ongezeko lilijitokeza katika Mpango uliopita ni kidogo, lakini pia katika miundombinu kwa maana ya barabara na vile vile hata katika kilimo ukuaji bado ni mdogo. Hata hizi EPZ zenyewe, bado wanaagiza hata raw materials wanazozitumia katika viwanda vyao. Kwa hiyo, ni lazima tuangalie kama Serikali kuweza kuwezesha kwanza nishati, tuwezeshe miundombinu na ndipo tukimbilie kwenye viwanda ili tuweze kuondokana na misamaha ya kodi katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, naomba pia nizungumzie upande wa mapato ndani ya Serikali. Serikali imeonesha kwamba kuna upungufu na tunashindwa kutekeleza mambo mengi kutokana na kutokuwepo na mapato ndani ya Serikali yetu. Katika Sheria ya Local Government ya mwaka 1982 inaonesha kwamba Halmashauri zetu (local government), zitaweza kukusanya fedha ya asilimia 0.3 ya Service Levy katika maeneo hayo kutokana na shughuli za mgodi ama shughuli za uwekezaji wowote ule unaokuwa katika maeneo ya Halmashauri husika.
Mheshimiwa Spika, sheria hiyo pia imetoa kipengele ambacho Waziri ana uwezo wa kufuta kile kipengele cha 0.3 ya Gross Revenue na badala yake wanatoa kiwango ambacho wawekezaji hao wanalipa ndani ya Halmashauri husika. Kwa hiyo, tunapoteza fedha, tunapoteza mapato makubwa kutokana na sisi wenyewe kuzichezea sheria zetu na kutosimamia yale mambo ambayo tumeyapanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Service Levy hata hizo kidogo ambazo zimelipwa, tunashindwa kuona ni namna gani, kama Serikali kuu inaweza kusimamia kule chini ili angalau hii Service Levy inayotolewa 60% ya hiyo Service Levy iweze kutumika katika shughuli za maendeleo. Vile vile bado kama Serikali haiwajibiki kuhakikisha ya kwamba kiwango ambacho kinastahili kulipwa ili 0.3 ya Gross Revenue kuweza kui-determine, Serikali haiwajibiki kuwasaidia Halmashauri katika ku-determine hilo ili kuhakikisha kama Serikali na kama nchi tunapata mapato husika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naomba nimpongeze kwa moyo wa dhati sana, kwa jitihada yake ya kusema ya kwamba watu walipe kodi. Binafsi kila nikienda sehemu, tunatafuta risiti tuweze kulipa kodi. Sasa kuna tofauti mbili kati ya Mwalimu Nyerere na Magufuli. Kuna tofauti moja tu, wote wanawapenda wananchi na tunawasikia na wanatamani kuona mabadiliko ndani ya wananchi, lakini Mwalimu Nyerere alianza kwake; kama ni kupunguza mshahara alianza kupunguza wa kwake akafuata wa wengine. (Makofi)
Kwa hiyo, namwomba pia Mheshimiwa Rais kwa kushirikiana na Serikali yake, mshahara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haukatwi kodi ya aina yoyote ile. Kwa hiyo, nachukua pia fursa kuiomba Serikali iweze kuliangalia hili suala kwamba inawezekana kabisa kwamba labda fedha ambazo Mheshimiwa Rais anastahili kupata ni kidogo au hizo alizozitaja Shilingi milioni 9.5 ni kidogo, lakini siyo kukwepa kodi au kumwekea msamaha wa kodi kwa maana inaonesha kama ni upendeleo wa aina fulani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuwajibike kama Serikali, tuweke kodi kwenye mshahara wa Mheshimiwa Rais kwanza na kama ni kuboresha, iwe hatua inayofuata ili tupate ile leading by example, wananchi waweze kuwajibika kwenye kulipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna masuala ambayo yameongelewa katika Mpango, suala la monitoring and evaluation. Katika shughuli zetu za Kamati, mimi binafsi nimeona shida ambayo imejitokeza kule.
Kuna maeneo ambapo Wizara na katika Mpango inaonesha kwamba Waziri wa Fedha anasema, watashirikiana na Wizara nyingine kuhakikisha kwamba usimamizi huu au monitoring and evaluation inafanyika katika maeneo yote na Wizara zote. Hata hivyo, kuna shida ya hii decentralization by devolution. Binafsi naiona kama vile ina tatizo kwa sababu Wizara inashindwa kwenda kuwajibisha watu moja kwa moja kule chini. Kwa hiyo, naomba…
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA, SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA (MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE): Taarifa!
SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Waziri TAMISEMI....
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, hoja yangu ilikuwa ni kwenye mshahara wa Rais utozwe kodi, lakini pia vile vile kama Mheshimiwa Rais alituambia mshahara wake ni Shilingi milioni 9.5 sijui kama aliupunguza ama ilikuwaje, hilo mtatufafanulia ukoje, mimi binafsi siwezi kulisemea hilo. Hoja yangu ni kwamba mshahara wa Rais utozwe kodi, leading by example, yaani kuongoza kwa mfano. Ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, naomba niendelee katika hoja zangu nyingine. Nilikuwa nimeishia kwenye upande wa decentralization by devolution, naomba pia hilo liweze kufanyiwa kazi. Huu mkanganyiko uliopo kati ya TAMISEMI na Wizara uweze kuondoka ili Wizara iweze kufuatilia mpaka kule chini tuweze kuona mambo yanaendaje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna upande huu wa maendeleo ya watu. Naomba nizungumzie kipengele cha makazi bora. Naomba niishauri pia Wizara kama inawezekana ipunguze kodi kwenye vifaa vya ujenzi ili wananchi wapate kujenga nyumba nzuri na badaye Serikali iende ikatoze kodi kwenye kodi za majengo. Tuwasaidie wananchi wetu waishi kwenye nyumba nzuri, wasipate magonjwa wasipate kuumwa na wadudu mbalimbali na waweze kufanya kazi vizuri kwa sababu watakuwa na afya njema.
Mheshimiwa Spika, kuna mahusiano makubwa sana kati ya makazi bora na afya za watu, pia katika upande wa elimu, upande wa wanawake, naomba pia Wizara iangalie kutenga fedha kwa ajili ya wanawake, tuweke suala la equity kwenye elimu.
Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Serikali, imeweka msamaha wa kodi kwenye sanitary towels kwa upande wa wasichana, lakini sasa Serikali iweke fedha ya kusambaza pad mashuleni ili watoto waweze kusoma na wasikose muda wa darasani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la mwisho ni kwenye upande wa good governance. Ili tuweze kuongoza vizuri kama Taifa, tunahitaji sana kuwa transparency, tunahitaji sana kuwa na accountability.
Mheshimiwa Spika, namwelewa Mheshimiwa wangu Rais John Pombe Magufuli ana nia njema sana, sana; lakini hiyo nia njema lazima iendane na transparency. Hatuwezi kuwa na Bunge ambalo linachuja taarifa! Yaani Bunge ambalo linafanya parental control ambayo inaenda kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuwa na Bunge ambalo hawataki wananchi waelewe Wawakilishi wao wanasema nini. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali mliopo hapa, mzingatie suala la transparency. Transparency ikiwepo, accountability itakuwepo na utumbuaji wa majipu hautahitaji Rais aende kila mahali, lakini wananchi wakiwa na taarifa husika, watawatumbua wao wenyewe katika maeneo yao, hata Wabunge wasiowajibika na wenyewe wataweza kushughulikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia hata Bunge lenyewe, tuchukue zamu zetu, tuwe wazi na tuweze kufanya kazi kwa uzuri na kwa maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba tu niseme kwamba, kama Taifa na kama Wabunge, tunahitaji, vita ambayo tunakuwa tumeipigana na ambao wengine wameipigana kabla wengine hatujaingia Bungeni, inapaswa iendelee; lile suala la misamaha ya kodi na watu wanaosamehewa kodi kuweza kulipa. Kwa sababu tumechambua hata katika Sekta ya Afya, pesa nyingi haijapelekwa katika Sekta ya Afya, kwa hiyo, tunahitaji kuangalia kila pesa iliko ili tuweze kuhudumia watu wetu wasiweze kufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sekta hii ya Afya tuna Madaktari ambao wanatibu katika maeneo yetu, ambao wengi wamepata elimu kwa ngazi ya Diploma na hawa Madaktari wamekuwa wakisambazwa katika Vituo vya Afya lakini pia vile vile hata katika Hospitali za Wilaya katika maeneo mengi na wamekuwa wakifanya kazi na watu wasio na elimu ya Udaktari kama mimi, siyo rahisi sana kutambua kama ana degree ya Udaktari au hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo moja kwamba hawa watu pamoja na kutuhudumia vizuri na elimu ambayo wameipata kwa miaka mitatu, wakihitajika kwenda kusoma na kupata degree, inawalazimu tena kwenda kusoma kwa miaka mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iliangalie hili. Mimi sio mtaalamu wa Udaktari, lakini waweze kuangalia ni namna gani wanaweza wakafupisha hii miaka ili angalau, kwa sababu kuna masomo wameshasoma katika kipindi cha Diploma basi wanavyosoma degree miaka iweze kupungua. Mfano ni katika elimu ya engineering hapa hapa Tanzania, wanafunzi waliomaliza Diploma katika vyuo vya Technical Schools kama Arusha Technical, wanapokwenda kusoma degree za engineering wanaanzia mwaka wa pili. Kwa hiyo, naiomba Wizara iweze kuliangalia hilo kama angalau tunaweza kuwasaidia hao Madakatari wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile hawa wanaosoma Diploma kwa jinsia ya kike, inawalazimu wanapomaliza elimu ya Diploma kwenda kufanya kazi kwa miaka mitatu ndipo waruhusiwe kwenda kusoma Degree kwa miaka mitano. Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya alisema ndani ya Bunge hili Tukufu kwamba menopause inaanzia miaka 35.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukipiga mahesabu, kama binti atamaliza Diploma kwa miaka mitatu, akafanya kazi kwa muda wa miaka mitatu ndipo akasome hiyo degree ya miaka mitano, kwanza ndani ya hiyo miaka mitatu ya kufanya kazi kuna changamoto. Anaweza akaolewa na mambo mengine hapo katikati yakabadilika. Vile vile anaweza kufikia menopause hata hiyo elimu yenyewe ya Udaktari kwa maana ya MD hajaweza kuifikia. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iliangalie hilo na iweze kurekebisha ili watoto wetu wa kike angalau wapunguziwe muda wa kufanya kazi hapo katikati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile natambua juhudi za kuhakikisha kwamba tunaweka usawa wa kijinsia ndani ya Taifa letu. Kumekuwa na juhudi mbalimbali na harakati za wanawake mbalimbali na leo katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri Ummy aliweza kusema na kumshukuru mume wake kipenzi kwa maneno yake, kwa kumsaidia katika utekelezaji wa kazi. Pia nimemsikia Mheshimiwa Mama Mary Nagu, naye anamshukuru anasema mimi Nagu kanisaidia sana! Pia wanawake hapa ndani ya CHADEMA Mheshimiwa Mama Grace Tendega na mama zangu akina Mheshimiwa Susan Lyimo na wenyewe wanawashukuru waume zao kwa kuwasaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sasa Wizara iangalie umuhimu wa kuwashirikisha wanaume kuweza kuelewa uwezo wa wanawake katika kuwasaidia kuleta usawa wa kijinsia. Hatuwezi tukaifanya hii vita peke yetu, lakini tunahitaji kuwashirikisha wanaume. Kwa hiyo, naiomba Wizara iweze kutoa kama trainings kutoka kwa mashirika mbalimbali ili wanaume pia wapatiwe hii elimu wapate kuona nafasi ya mtoto wa kike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo, naomba pia nimshukuru baba yangu mzazi ambaye kwa kupitia kwake, kwa kuona umuhimu wangu kwake, ana watoto watano, wa kiume mmoja na wa kike wanne na aliapa kwamba lazima atengeneze wanawake wanaoweza kujitegemea katika maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto kubwa zinazowakabili watoto wetu wa kike. Mheshimiwa Ummy katika Hotuba yake ameweza kutaja kwamba kuna vifo vya wanawake, bado vipo na hii hali inatisha, lakini tunaweza tukatambua kwamba baadhi ya watoto au watu wanaokufa kutokana na hivi vifo ni watu wanaobeba mimba kabla ya kufikia umri halisi wa kuweza kupata mimba. Kuna changamoto za kielimu pia ambazo zinawakabili watoto wetu, ndiyo maana wanashindwa kwenda shule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, binti anaingia katika kipindi cha hedhi ambapo kama hana vifaa vya kujisitiri (Sanitary towels) anashindwa kwenda darasani sawasawa na mtoto wa kiume. Katika adult level msichana anaweza kwenda katika kipindi cha hedhi kwa siku nne, at maximum siku saba. Sasa binti akikosa darasani siku nne, somo kama ndiyo limeanza leo, baada ya siku nne maana yake hilo somo limekwisha. Kama ni siku saba, hivyo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tutambue kwamba Serikali imeweka msamaha wa kodi kwenye sanitary towels, lakini bado sanitary towels zinapatikana kwa bei ya juu. Sanitary towels kwa bei ya chini kabisa Dar es Salaam ni sh. 1,500/=, lakini nyingine ni sh. 2,500/= mpaka bei ya juu zaidi. Sasa hapa suala linalokuja ni kwamba, Serikali itengeneze chombo maalum ambacho. Humu ndani tunapitisha misamaha ya kodi ili iwanufaishe wananchi, lakini mwisho wa siku inakuwa ni manufaa kwa wafanyabiashara na siyo wananchi tuliowalenga hapo mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali itengeneze chombo maalum cha kuangalia kila bidhaa tuliyoiwekea msamaha wa kodi kinasimamia na kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana kwa bei iliyolengwa kwenye soko. Suala hilo pia linagusa mpaka maeneo ya dawa, kwamba dawa zimewekewa misamaha ya kodi, lakini ukienda madukani kwenye private pharmacies bei ni kubwa. Kwa hiyo, Serikali iliangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala hilo hilo, tunasema kwamba Wizara hii ya jinsia iweke kipaumbele na kuhakikisha kwamba, sekta nyingine zote zinaangalia jinsia katika utekelezaji wa mambo yake. Katika kilimo, watu wote wanaofanya kilimo 80% ni wanawake. Usipowaangalia wanawake katika kilimo, maana yake ni kwamba kilimo lazima kife. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika elimu, ni vizuri sasa Wizara ya Afya kushirikiana na Wizara ya Elimu, ikatenga pesa, kama ni sh. 10,000/= kwa ajili ya Shule za Msingi kila mwanafunzi, basi kwa mtoto wa kike iwe ni sh. 12,000/= ama sh. 13,000/= ili ile sh. 3,000/= iweze kugharimia kwenda kulipia sanitary towels. Vile vile katika Vyuo Vikuu mkopo wa Chuo Kikuu uweze pia kugusa kuhakikisha kwamba wa msichana uwe juu zaidi ili kumsaidia asikose darasani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi sasa katika masuala yangu ya Mkoa wa Geita. Mkoa wa Geita tuna changamoto nyingi na tuna vijiji vingi ambavyo havina umeme. Naiomba Wizara ya Afya ishirikiane na Wizara ya TAMISEMI kuhakikisha kwamba, zahanati na vituo vya afya vinapatiwa umeme wa solar ama umeme kabisa kutoka gridi ya Taifa. Kwa sababu, mtu anaweza akajifungua usiku! Sasa mtu anazaaje gizani kwa kweli? Ni kitu kidogo ambacho kinakuwa kigumu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi tuna tatizo hilo hilo la CHF ambapo wananchi hawapati dawa. Vile vile CHF mtu akitoka Geita akienda Chato hapatiwi huduma; akitoka Geita akaenda sehemu nyingine, hapatiwi huduma. Hili nalo muweze kuliangalia ili tuweze kuona ni namna gani tunaweza tukawasaidia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kuiomba Serikali kwamba, ikumbuke Hospitali ya Mkoa wa Geita ambayo mmeifanya sasa imekuwa ni Hospitali ya Rufaa, lakini haifanani hasa na kuwa na sifa hiyo ili iweze kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Geita. Pamoja na hilo, liangaliwe suala la kutafuta fast ferry kwa sababu, kutoka Geita kwenda Mwanza tuna maji pale katikati. Ukitegemea hizi ferry za kawaida, mgonjwa anaweza kufia ndani ya ferry. Kwa hiyo, ferry badala ya kwenda na mgonjwa inarudi na maiti. Kwa hiyo, tunaomba sasa tuweze kupatiwa pia fast ferry kwenye hilo ziwa kuhakikisha kwamba wagonjwa wanafikishwa on time katika hospitali zinazohusika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii, na naomba pia niweze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia tena fursa nyingine na kuweza kuzungumza ndani ya Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kusoma ripoti ya committee maalum iliyoundwa na Rais nimepata kutambua ya kwamba yawezekana kama nchi na katika vipindi vilivyopita na leo hii katika juhudi zinazofanywa na Rais wa sasa za kutafuta mapato mbalimbali lakini Serikali kwa vipindi vilivyopita ilishiriki kikamilifu kusababisha ukwepaji wa mapato ndani ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema kauli hiyo ukiangalia katika mikataba ambayo iliingiwa na nchi hii, katika mkataba wa Bulyanhulu ambao uliingiwa mwaka 1994 kutokana na ripoti maalum ya committee ya Rais inaonesha ya kwamba suala la fuel levy ama mapato au misamaha ya kodi inayotokana na mafuta yanayotumiwa mgodini ilipitishwa kama government notice mwaka 1999. Lakini mgodi huu ulipata mkataba mwaka 1994 ambapo Bulyanhulu ni sehemu ya migodi ambayo inapokea misamaha ya kodi kwenye mafuta. Mwaka 2014 Bunge hili hili tukufu lilitunga sheria na kuilinda mikataba ile ambayo imepita kwamba watu hawa hawafai kuguswa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri kwa Serikali kwamba tusifike hatua tukasema tufunike kikombe tuendelee na mambo mengine, lakini kuna haja ya kupitia pale tulipotoka tuweze kuona kwamba kama kuna mapato mengine tunaweza tukayapata na tusifunike tu kwamba mikataba tulishaifanya basi, sehemu maalum ziangaliwe kuangaliwa ili kuweza kuongeza mapato ndani ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna suala la service levy, mapato yanayolipwa na migodi ambayo ni asilimia 0.3 ya turn over ya migodi hiyo. Kwa miaka iliyopita Serikali iliweka fixed cost kitu ambacho ni tofauti kabisa na Sheria ya Serikali ya Mitaa ya mwaka 1982. Wakaweka fixed cost ya dola za Kimarekani 2,000 ambazo ndizo zinazofaa zilipwe katika Halmashauri zetu. Lakini mwaka 2014 yalifanyika mabadiliko na sasa service levy inalipwa kwa 0.3, ile ile ya turn over. Sasa naitaka Serikali iweze kusimamia na kuhakikisha kwamba inazisaidia Halmashauri hizi ili kuweza kutambua ni kiasi gani ambacho ni turn over wanayostahili kama Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua Halmashuri zetu hazina uwezo mkubwa kwa hiyo Serikali iweze kulifanya hilo na kuweza kusaidia. Lakini vilevile tuna TMA na wao wahusike kuangalia, isiishie tu udhibiti kwa maana ya madini lakini waangalie katika eneo kubwa la kuangalia kiasi gani ambacho Halmashauri zetu zinastahili ili kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa Wizara zingine hasa ile inayohusiana na Mambo ya Serikali za Mitaa ni muhimu pia wakatambua ya kwamba dhahabu au madini yoyote yale hayatarudi tena kuwepo kwenye ardhi. Kwa hiyo, ni vyema basi tukaweza kuzishauri Halmashauri zetu, tukashiriki kikamilifu ili walau kiasi kinachotolewa kwa ajili ya service levy kitumike kwa ajili ya kuendeleza Halmashauri, kuweka mikakati au uwekezaji mkubwa ndani ya Halmashauri zetu lakini pia kuendeleza huduma za kimaendeleo badala ya hizo hela kutumika kwenye OC ili Serikali nayo ipange mambo mengine lakini pesa zitumike kwa shuguli za maendeleo zilizokusudiwa kwa ajili ya wananchi wa eneo husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka Geita na katika maeneo ambayo yanapata shida kubwa sana kutokana na uwekezaji wa kampuni ya Geita Gold Mine, ni wananchi wa Geita. Wananchi hawa katika maeneo ya Katoma, Nyamalembo na Compound. Wananchi hawa wamekuwa wakiathirika na mitetemo, vumbi inayotoka migodini. Vilevile nyumba zao zimekuwa zikiathirika kwa nyufa. Mheshimiwa Naibu Waziri aliweza kuwatembelea wananchi hao na akagundua kasoro ambazo zipo na akaona matatizo ya kuchafuka kwa maji kwa maeneo ambayo wananchi wanaishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha kusikitisha, Mheshimiwa Naibu Waziri alitoa agizo kuwa mgodi kwanza kuziba mtaro ili maji yasiende kwenye visima vya maji, lakini pia kuhakikisha ya kwamba wananchi hawaendelei kunyanyasika katika eneo lao. Lakini nikutaarifu kwamba ni kitu cha kushangaza, mgodi huu una kiburi cha ajabu yaani hata agizo la Serikali hawakuweza kulitimiza na mpaka leo hii hicho hakijafanywa na badala yake Serikali inaangalia namna mbadala ya kuongea nao, badala ya kusaidia maisha ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna kesi mbalimbali ambazo zimejitokeza Geita, Mheshimiwa Waziri unafahamu kuna wananchi wa Maili Mpya katika eneo lile. Wananchi ambao walifukuzwa kwa kudhalilishwa, maeneo yao yakafukiwa, mgodi umechukua hilo eneo, lakini bado kuna wananchi wa Katoma ambao wengine hawakulipwa fidia hata kidogo, wamefukuzwa katika maeneo yao. Sasa haiwezekani kwamba tuna Serikali; kuna kipindi niliendelea kuitembelea nchi ya Norway katika mafunzo wakatuambia kwamba wafanyakazi walivyokuwa wananyanyaswa walifananisha manyanyaso yao na wafanyakazi wa Kiafrika wanaonyanyaswa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini leo tunanyanyaswa sisi ndani ya nchi yetu na wawekezaji hawa hawa bila kuzingatia haki za binadamu na uhuru wetu na afya zetu ndani ya Taifa letu. Kwa hiyo, ninaiomba sasa Serikali iweze kuangalia ni namna gani mtawasaidia wananchi wa Geita. Kutakuwa hakuna maana kwa wao kumpigia Rais Magufuli kura nyingi na kwa imani kubwa waliyonayo tena Rais kutoka nyumbani, halafu wakabaki na manyanyaso makubwa yanayofanywa na mgodi wa Geita Gold Mine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mtaa wa Nyakabale ni eneo ambalo liko ndani ya beacon ya mgodi. Eneo hilo wananchi wa Nyakabale kama unavyofahamu limefungiwa hata nyia yake. Wananchi hawawezi kutumia njia maalum waliokuwa wanatumia zamani kuelekea mjini, badala yake mgodi umeweka mabasi asubuhi na jioni, mgodi ume-limit movement ya wananchi katika eneo husika. Pia limechimbwa shimo la takataka ndani ya eneo lao ambapo sumu za mgodi zinamwagwa ndani ya Nyakabale katika Kata ya Mgusu. Hii inaathiri afya za wananchi wa Geita, zinaathiri afya za wananchi wa Nyakabale. Ninaomba Serikali mfuatilie hilo ili hali iweze kukomeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ni suala la wachimbaji wadogowadogo. Katika kipindi kilichopita Serikali iliwahamisha wananchi wa Samina na kusema kwamba inawapatia eneo lingine la uchimbaji. Kwa masikitiko makubwa sana Serikali ilitoa eneo ambalo halijapimwa na ilitoa pia sehemu ambayo utafutaji wa madini kwenda chini uko mbali sana. Sasa Serikali yetu hii naiomba inavyotoa maeneo ya madini yaliyo karibu kwa wawekezaji wawafikirie wazawa Watanzania ili waweze kufanya shughuli za uzalishaji.
ushirikishwaji katika maeneo ya uchimbaji wadogo wadogo. Kwa sababu wanawake wanapiga mawe, wanawake wanafanya shughuli za kwenye makarasha, wanawake wanafanya shughuli mbalimbali katika maeneo ya migodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia Wizara iweze kuliangalia hilo katika hizo ruzuku wanawake wa Geita pia ziweze kuwafikia na ziweze kuwasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia wananchi wa Nyarubuso, ni wananchi wanao athirika kutokana na shughuli za ellusion ama uchenjuaji wa dhahabu. Serikali naomba itoe elimu nzuri kwa wananchi wa Geita, kwamba pamoja na uchenjuaji huo lakini waweze kufanya shughuli ya makusudi ya kwamba uchenjuaji usiathiri vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ninaiomba Serikali itoe kauli humu ndani, Ilitoa ahadi kwa wananchi wa Geita kuwapatia magwangala ama mabaki ya dhahabu, lakini tunafahamu Serikali haijafanya uchunguzi kujua ni kiasi gani watapata dhahabu katika magwangala hayo. Ninaomba Serikali itoe kauli ili mchanga huo basi wananchi kwa sababu wamekosa maeneo ya kuchimbia, sasa wanatafuta mabaki ya mchanga wa dhahabu kutoka katika kampuni ya Geita Gold Mine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itoe kauli ili kauli iliyotangazwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu tuweze kuelewa ina faida ama haina faida na lini itatekelezwa kwa wananchi wa Geita ili walao kama hamjawapatia maeneo walau wapatieni huo mchanga ili waweze kujifanyia shughuli zao za maendeleo, ahsanteni sana.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami pia napenda nichukue fursa hii nichangie katika Muswada huu wa Upatikanaji wa Taarifa. Napenda nianzie katika section 6(1)(f) ambacho kinazungumzia infringe commercial interest.
Napenda kuishauri Serikali kwamba hapa hatujapata maelezo kamili ya kujua hizi commercial interest ni zipi kwa maana ya kwamba kuna taarifa ambazo zinaweza zikawa zinahitajika hasa katika maeneo ya mikataba ambayo nchi inakuwa imeingia na wawekezaji. Sasa kama tukisema na hizi pia ziko katika kile kipengele cha taarifa ambazo haziwezi zikapatikana, maana yake ni kwamba haya ni mambo pia yanayowagusa wananchi moja kwa moja na ni sehemu pia ya public interest.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia pia sehemu hiyo ya sub section 6(6) ambayo inazungumzia any person who discloses exempt information withheld by the public authority in controversion of this Act commit an offence and shall, on conviction, be liable to imprisonment for a term not less than 15 years.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kipengele hiki nilikuwa napendekeza ya kwamba maeneo haya mengine ya juu ambapo ukianzia kwenye sub-section (2) ambayo inazungumzia maeneo ya National Security, nilikuwa napendekeza kwamba hii adhabu au hiki kipengele kizungumzie yale mambo ambayo yako chini tu ya mambo ya National Security, lakini mambo ambayo yako juu, ambayo siyo mambo ya National Security, hayo basi tuyaache kwa sababu taarifa nyingine inaweza ikatoka chini ya hicho kipengele cha public interest.
Mheshimiwa mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia katika kipengele kingine cha (a), (b), (c), (d) na mengineyo, unaona kwamba kuna taarifa ambazo zinaweza zikatoka ambazo zinaweza zisiguse moja kwa moja usalama wa Taifa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba hiyo adhabu ibaki kwa yale maeneo tu ambayo yanazungumzia mambo ya National Security.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna kipengele cha 16 ambacho kinazungumzia; “The information holder may be defer the provision of access to information until the happening of a particular event including the taking of some action required by law or some administrative action or until the expiration of a specified time, what is reasonable to do so in the public interest or having regard to normal and proper administration practices.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuangalia hiki kifungu katika hii section ya 16, kitu ambacho kinaonekana hapa ni kwamba kwa hiki kifungu maana yake ni kwamba taarifa zozote zile hazitaweza kupatikana kwa sababu taasisi husika inaweza ikaamua kunyima zile taarifa kwa kisingizio cha public interest, lakini hii public interest tunai-define kwa muktadha upi ili angalau tuhakikishe wananchi hawawezi wakanyimwa taarifa?
Mhesimiwa Mwenyekiti, tukiiacha kama hivi na tukaipitisha, sheria hii na hii section ya 16 tukaiacha kama ilivyo, maana yake ni kwamba tunasema kwamba sheria tumeandika kama sheria ambayo inaruhusu mambo ya transparency, lakini kimsingi ni kwamba tunavunja. Tunatambua ya kwamba mambo ya uwazi na uwajibikaji ni sehemu ya msingi katika demokrasia na ni mambo muhimu pia katika Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika hiki kipengele cha 16, kama hatutaweza kukifanyia kazi, maana yake ni kwamba tutakuwa tumetimiza matakwa ya Kimataifa ya kututaka Tanzania pia tupitishe sheria hii ambayo inahusiana na mambo ya utoaji wa taarifa, lakini kama nchi hatutaweza kutekeleza haki ya Kikatiba ya wananchi katika kuhakikisha kwamba wanapata sheria. Kwa hiyo, naomba tu nitoe ushauri kwa Serikali ili kuweza kuona namna gani hiki kitu kinaweza kikaangaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni vyema tukafahamu ndani ya hili Bunge kwamba vyama vya siasa au upinzani kwa ujumla wake tusiuchukulie tu kwamba ni chama mbadala ambacho kiko tayari kusubiria nafasi ya kuweza kutawala, lakini tuchukulie kwamba ni sehemu pia ya kuwa wawajibishaji ndani ya nchi hii. Kwa hiyo, kama tunataka uwajibishwaji uweze kuwepo ndani ya nchi hii, lazima pia masuala ya uwazi yaweze kuwepo. Tunavyopitisha hii sheria tuangalie hicho kipengele, lakini pia tuangalie masuala mengine ambayo kama Serikali yamekuwa yakifungwa katika hilo suala zima la uwajibishwaji na upatikanaji wa taarifa, hasa kwa kuzingatia kwamba tulivyokuwa tunaanza hili Bunge, Serikali ilitangaza kuondoa Bunge la moja kwa moja la wananchi kutizama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba tumeifunga haki hiyo, leo tunapitisha hii sheria ambayo hatujui kiukweli kama hiki kipengele cha 16 kitabaki kama wananchi wataweza kupata hata hizi taarifa ambazo zimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapopata taarifa maana yake ni kwamba uweze kuwajibisha ofisi husika, maana yake ni kwamba uweze kupata majibu kutoka Serikalini. Nina imani kwamba vyama vya upinzani vina wajibu huo na hivyo Sheria ya Vyama vya Siasa naomba pia Serikali, viongozi walioko hapa, Mawaziri, waweze kumshauri Mheshimiwa Rais vyema kwamba ni bora kutii sheria za nchi zilizopo kwa sababu zimetungwa na Bunge hili. Kama tunaona ya kwamba sheria hazifai, basi ni vizuri pia Serikali ikaleta marekebisho ya hizo Sheria za Vyama vya Siasa ili tuweze kuziangalia na kuzibadilisha na kuweza kuondoa watu kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mlinga ametoa ushauri, tunamchukulia ni mtu wa masihara, lakini kuna vitu alivyoviongea vya msingi. Kwa hiyo, tuombe pia Serikali iweze kumshauri Mheshimiwa Rais kuweza kuitii Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo iliyomchagua, ndiyo iliyomweka madarakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mwalimu Nyerere mwenyewe aliweza kutamka katika hotuba yake akiwahutubia wananchi wa Tanzania kwamba Watanzania wasiruhusu kwa gharama yoyote ile mtu atakayeongoza kutoka kichwani mwake, lakini tuweze kuheshimu viongozi walioapa kwa Katiba na walio tayari kuilinda Katiba na wananchi wote tuweze kuwataka viongozi wetu kuweza kusimamia Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo siyo maneno yangu, ni maneno ya mtangulizi wetu Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ambaye anaheshimika na kila mmoja wetu. Ahsanteni sana.