Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Upendo Furaha Peneza (14 total)

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, tarehe 26 mwezi wa kwanza hapa Bungeni, Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, alitoa Kauli kwamba wananchi wengine wanashindwa kupata haki ya malipo stahiki kutokana na kitendo alichoita utegeaji. Kwamba wananchi wengine wanapanda wakati ule wanasubiri kwamba waweze kulipwa kwa wakati unaofuata. Sasa kutokana na hicho lakini naamini kwamba Mheshimwa Waziri, anafahamu ya kwamba wananchi huwa wanalipwa kutokana na asilimia ya ukuaji wa mmea husika, kwa hiyo kama mtu amepanda mgomba stahiki ni 50 kama mmea huo umekuwa kwa asilimia 10 basi utalipwa kwa asilimia hiyo 10. Je, kutokana na kauli hiyo ya Mheshimiwa Waziri, haoni kwamba Wizara hiyo itakuwa inashirikiana na migodi hiyo katika maeneo hayo ambako madini yanapatikana ili kuweza kuwanyima wananchi malipo stahiki kutokana na kazi yao katika maeneo yao husika?
Vilevile swali la pili, Geita ni sehemu ambayo inazungukwa na dhahabu kwa kiasi kikubwa, lakini katika maeneo mengine ambayo yameshalipwa fidia wananchi wamelipwa milioni moja na nusu kwa eka nzima, kwa maana ya fidia ya ardhi katika lile eneo. Lakini ukiangalia kwa maana ya wale wananchi hao hao wa Halmashauri hiyo ya Mji wa Geita, walipewa tena na Serikali kwa kuuziwa ardhi na kiwanja cha ishirini…
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, najenga hoja. Kwa maana ya 25 kwa 30, wananchi hawa waliweza kununua eneo hilo hilo kwa milioni tatu. Maana yake ni kwamba ile milioni moja na nusu ambayo walilipwa haikuweza hata kutosha kununua heka nzima.
Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo ambayo yana madini waweze kulipwa malipo ya ardhi kulinganisha na bei ya soko iliyopo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kauli yangu, naomba uelewe Mgodi wa Geita Gold Mine, watu wameanza kulipwa enzi ya plasadom, miaka ya 1980. Kwa hiyo huo mtegesho ni kweli na bahati nzuri tumepanga tarehe 10 mpaka 14, nakukaribisha na wewe uwepo Nyamongo kwa sababu nitakuwa na Mbunge wako hapa. Halafu hili suala la tathmini siyo kufikiria kwamba mtu anahitaji fedha kiasi gani ili akanunue shamba au akawekeze, anayefanya thathmini ni Ofisi ya Serikali na kila Wilaya inafanywa chini ya DC. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sisi tunafuata taratibu za sheria ambazo zipo, tathmini siyo kukufanya wewe upate fedha kwa sababu umeshalenga mradi fulani. Ahsante.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ripoti ya PAC ya Januari 2015 iliyojadili ripoti maalum ya CAG ikionesha upotevu kutokana na watu kukiuka utaratibu. Je, Serikali imechukua hatua gani ili kuhakikisha watu waliokwepa kodi na kukiuka taratibu waweze kulipa pesa hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ripoti hazioneshi kiuhalisia faida ambazo Serikali inazipata kutokana na misamaha hii ya kodi na makampuni haya hayafanyi social responsibility kwa kiwango kinachoridhisha. Je, Serikali inafanya mkakati gani ili kuhakikisha kwamba makampuni haya yanaondolewa misamaha ya kodi, walipe kodi stahiki na wajibu wa huduma kwa jamii ubaki ni wajibu wa Serikali? Ahsante
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza misamaha ya kodi ambayo tumekuwa tunaitoa kwa makampuni ya madini imekuwa inapungua kutoka takriban asilimia 17.6 ya exemptions zote zinazotolewa za kodi, mpaka sasa imefika takribani asilimia tisa. Hatua ambazo tumekuwa tunachukua, moja ni kurekebisha Sheria za Kodi na Waheshimiwa Wabunge mlipitisha hapa marekebisho ya Sheria ya VAT ambayo iliondoa misamaha mingi ya kodi na VAT peke yake misamaha ya kodi ni takriban asilimia 56 ya mapato ya exemptions zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kurekebisha sheria hiyo, msamaha wa kodi umepungua kwa kiasi kikubwa. La pili, tunafanya jitihada kubwa kushughulikia mazingira ya biashara na uwekezaji, kwa kuwa uwekezaji hautegemei kodi peke yake, ndiyo maana Serikali imeelekeza nguvu kuongeza upatikanaji wa umeme ambayo ni malalamiko makubwa ya wawekezaji, lakini pia ulinzi kwa ajili ya wawekezaji na kuhakikisha kwamba tunaboresha mazingira ya kutoa leseni za biashara na vibali vya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeongeza kujenga uwezo wa kuchambua vipengele vya misamaha ya kodi, vile vitengo ambavyo ndani ya Wizara ya Fedha lakini pia ndani ya Mamlaka ya Mapato ili kuhakikisha kwamba misamaha inakuwa tu ile ambayo inafaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Waziri wa Fedha atakataa misamaha yote ambayo haina maslahi kwa Taifa. (Makofi)
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, suala la ulipaji wa fidia Ludewa pia linafanana na sehemu ya Wilaya ya Geita ambapo wananchi wa mtaa wa Mgusu wanaishi katika eneo ambalo liko ndani ya beacon ya Geita Gold Mine na wananchi hawa wamekuwa wakiathirika na taka zenye sumu zinazomwagwa katika eneo lao.
Je, Serikali inaweka msukumo gani kwa Geita Gold Mine kuhakikisha kwamba inawalipa wananchi wa mtaa wa Mgusu fidia ili waweze kupisha eneo hilo na wasiathirike na taka katika hilo eneo la Geita? Asante.(
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa wananchi wa Mgusu wanaishi sehemu ya leseni ya utafiti wa GGM, lakini taratibu ya Sheria za Ardhi na Sheria za Madini zote hulingana. Kimsingi, mahali ambapo mgodi haulitumii eneo hilo wananchi wanaweza waka-co-exist na shughuli za mgodi, lakini mahali ambapo shughuli za mgodi zinafanyika, basi wananchi wanaoishi katika maeneo hayo hufanyiwa fidia na kupisha shughuli za ujenzi.
Mheshimiwa Spika, eneo la Mgusu linalozungumzwa, Mgodi wa GGM haujaanza kulitumia. Kwa sasa hivi wananchi wanaishi Mgusu na kimsingi Mgusu imeshakuwa ni mjini na GGM sasa hivi haioni sababu ya kulichukua. Ila itakapofika wakati wa kulichukua eneo hilo, Mheshimiwa Mbunge atawasiliana na sisi na taratibu za fidia za wananchi wa Mgusi zitafanyika.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Kwa kuwa, ulipaji wa kodi ni suala la kizalendo na kwa kuwa, suala la ulipaji wa kodi ni wajibu wa kila mwananchi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile kwa kuwa Wabunge, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaji, ni wanufaika kutokana na mishahara na faida mbalimbali tunazozipata kutokana na kodi ambazo wananchi wanalipa.
Je, ni lini Serikali sasa italeta marekebisho ya Income Tax inayompa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Rais wa Zanzibar msamaha wa kodi kwenye mishahara yao? Pia ni lini Serikali italeta marekebisho kwenye sheria inayowapa Majaji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania misamaha ya kodi kwenye mishahara yao ili wote kwa pamoja tutimize wajibu wa kiraia wa kulipa kodi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyokiri yeye mwenyewe kulipa kodi ni haki ya kila mtu na ni wajibu wa kila mtu. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Upendo pamoja na Bunge lako Tukufu kwamba, muda sahihi utakapofika wa kuleta marekebisho ya Sheria hii tutaileta hapa Bungeni na marekebisho yatafanyika na watu wote watalipa kodi kwa msingi sahihi unaotakiwa. Pia naomba nimkumbushe kuwa, siyo kwamba Mheshimiwa Rais halipi kodi! Mheshimiwa Rais analipa kodi. Nashukuru.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Pamoja na Serikali kufanya jitihada za kuwapa maslahi watu wa Jeshi la Polisi, lakini askari hawa wamekuwa wakitumia nafasi zao vibaya kwa masuala binafsi, kwa kuwaonea wananchi. Serikali ina mkakati gani sasa wa kutoa elimu kwa wananchi ili kutambua ofisi hizo za malalamiko ili askari hawa waweze kuchukuliwa hatua kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Geita, vijana wa boda boda na watu wengine wamekuwa wakionewa na Polisi kwa masuala binafsi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, moja, Taasisi ya Jeshi la Polisi ina utaratibu wake mahususi wa kuchukua hatua kwa kila askari anapokuwa amefanya makosa na wanafanya hatua hizo hata licha ya kuwa pamekuwepo na mlalamikaji, kwa sababu suala la nidhamu kwenye Jeshi la Polisi ni jambo la kipaumbele hata bila kulalamikiwa, ndiyo maana utaona Askari wetu wana nidhamu kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, inapotokea matatizo ya aina hiyo, Jeshi la Polisi linachukua hatua. Hata hivyo, niseme tu kwa Waheshimiwa Wabunge na kwa Watanzania kwa ujumla, tunapodai haki ni vyema sana tukatambua kwamba tuna wajibu wa kutimiza na hivyo itaondoa taratibu za kuwepo malalamiko ya mara kwa mara. Kwa sababu katika maeneo mengine unaweza ukamnyooshea kidole askari, lakini ukifuatilia undani wake unakuja kutambua kwamba pana mtu ambaye hakutimiza wajibu wake vizuri ndiyo maana Askari akachukua hatua. (Makofi)
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, katika jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri suala zima la miundombinu; Mheshimiwa Rais alivyokuwa na ziara Mkoani Geita alitoa ahadi kwa wananchi wa Kasamwa kwa ajili ya kuwachangia pesa kujenga bwawa au lambo kama tunavyoweza kuliita. Lakini kazi iliyofanyika ni chini kabisa ya viwango na maji yale ni machafu, wananchi hawawezi kuyatumia. Na katika majibu yako pia katika hizi pesa ambazo zimetajwa hapa tumepata taarifa katika Kamati zetu kwamba Serikali haina pesa ya kutoa kwa ajili ya miradi ya maji katika sehemu nyingi hapa nchini.
Sasa naomba Serikali itoe tamko kwa wananchi ambao wana wasikiliza leo kwamba Serikali hii ina mkakati gani wa kuhakikishia wananchi kwamba wanapata maji safi na salama ambao wananchi wengi ambao ni wanyonge shida yao ni maji na sio bombardier? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali pili Mheshimiwa Rais Magufuli aliweza kutoa ahadi kwa wananchi wa Geita kuweza kuwapatia magwangala, lakini katika eneo la Nyarugusu ni kati ya maeneo ambayo yameathirika sana kutokana na uchenjuaji wa dhahabu na wananchi katika maeneo hayo hawana maji salama kutokana kwamba vyanzo vingi vimeathiriwa na mercury.
Serikali inatoa tamko gani kwamba pamoja na shughuli za magwangala ambazo Rais amezitoa kwamba wananchi wa Geita watapata maji salama ili waweze kuendelea na maisha yao? Ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema kwamba Mheshimiwa Rais ametoa ahadi pale, lakini kazi inaendelea chini ya kiwango. Naomba nikuhakikishie kwamba tarehe 27/08 nilikuwa katika Mkoa wa Geita na nilifanya harambee kubwa pale tulipata karibuni 1.4 billion kwa ajili ya madawati katika Mkoa wa Geita. Hata hivyo, katika sekta ya maji kwa sababu ni kipaumbele changu, nilitembelea maeneo mbalimbali ikiwepo Chato na mradi mwingine nikazindua lakini na mradi mwingine ambao ulikuwa watu wamefanya mambo ya ovyo na kuunda kamati. Na hivi sasa tutaenda kuchukua hatua stahiki kwa wale watu wote waliokiuka utaratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nikwambie ni commitment ya Serikali kama sehemu ambayo umefanya ubadhirifu na mambo ya hovyo tutaenda kuyasimamia. Nikwambie kama kamati sasa hivi timu niliyounda tayari taarifa ipo mezani kwangu tunaenda kuchukua hatua stahiki kwa ajili ya wananchi. Kuna mradi mmoja wa Changolongo ambao umefanyika mambo ya ovyo, watu hawakufanya mambo sawasawa hata hiyo tunaenda ku-cross check. Lengo letu ni kwa wananchi wa Mkoa wa Geita na Mikoa na mingine waweze kupata huduma ya maji na hatutokuwa na masihara hata kidogo kwa watu ambao wanachezea kwa makusudi nguvu yoyote ya Serikali inayopelekwa halafu watu wakafanye mambo ya ovyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwambie commitment yetu ipo hapo na Mkoa wa Geita tunaenda kuchukua hatua, lakini naomba niwaombe radhi sana kwa wale watu ambao hata wakiwa ndugu zenu tukiwachukulia hatua tunaacha sasa naomba tusileteane vi-memo tunaenda kuwachukulia hatua watu waliokiuka taratibu za manunuzi katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili; suala la kwamba kuna mercury wananchi wa Nyarugusu wanahakikishiwa vipi? Ni kwamba ni commitment ya Serikali na ndio maana hata nilipofika kule niliwaambia wataalam wetu wajiongeze. Haiwezekani Mkoa wa Geita ambao kuna Ziwa Victoria kila sehemu unakoenda unakuta maji wananchi wanakosa fursa ya maji. Tukawaambia kwamba waje na mpango jinsi gani tutafanya Mkoa mzima wa Geita kutumia fursa ya Ziwa Victoria badala ya kuchimba borehole, tupate vyanzo vya maji mbadala kutumia Ziwa Victoria na hili niliwaagiza watalaam wetu na hilo wanalifanyia kazi. Na nimewaambia nataka tulione katika mpango wa bajeti wa mwaka huu wa fedha unaokuja, lengo kubwa wananchi wapate fursa ya maji katika maeneo yao.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Wizara inatambua kwamba makazi duni huchangia katika kuleta afya mbovu kwa wananchi. Ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi yake ya kupunguza kodi kwenye vifaa vya ujenzi ili sasa wananchi waweze kujenga nyumba bora na kuepukana na nyumba za tembe na nyasi?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Sheria ya Madini
ya Mwaka 2010 inaongelea suala la resettlement; kwa wananchi wanaotokana na maeneo ambayo yana shughuli nyingi za wawekezaji, wakilipwa fidia hulipwa pesa na kuondoka, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 inazungumzia kwamba ahamishwe na ahakikishe kama alikuwa na mwembe, basi ataachana naye pale ambapo mwembe utakuwa umeota na kuanza kuzaa. Ni lini sasa Serikali italeta ndani ya Bunge hili mabadiliko ili Bunge liweze kufanya mabadiliko katika Sheria ya Ardhi ili sasa hilo suala la resettlement liweze pia kuzungumziwa katika Sheria ya Ardhi ili wananchi wapate fidia ambayo ni sahihi na waweze kunufaika na uwekezaji huu ndani ya nchi yetu? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza amezungumzia hali duni ya makazi ya watu na kufanya pengine wasiwe na makazi bora, pengine yanachangiwa labda na vifaa kuwa na bei ya juu.
Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la kupunguza kodi katika vifaa vya ujenzi ni suala ambalo linahitaji kupitiwa kwa upya katika utaratibu wake kwa sababu mwanzo Waheshimiwa Wabunge walileta suala la kutaka kupunga VAT katika vifaa vya ujenzi, lakini lilikuwa limelenga eneo moja. Katika kulitafakari ikaonekana kwamba ukishatoa loophole hiyo kwa sehemu moja; na ilikuwa imeongelewa upande wa National Housing, pengine lingeweza kuleta tatizo zaidi, watu wangetumia fursa hiyo vibaya.
Mheshimiwa Spika, tunachopendekeza pengine na kuona kwamba kina unafuu zaidi, ni pale ambapo tunaweza kutumia rasilimali tulizonazo katika maeneo yetu na hasa katika kutumia hivi vifaa vya ujenzi ambavyo vinaletwa kwa karibu zaidi. Sasa hivi ukiangalia hata cement imeshuka bei kulingana na uzalishaji umekuwa mkubwa. Kadri ambavyo uzalishaji unakuwa mkubwa, ndivyo jinsi na bei inashuka.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hapa tunachohimiza ni
ile sera ya viwanda; pale ambapo tutawezesha kuwa na viwanda vingi vitakavyoweza kutengeneza vifaa vya ujenzi bei zitashuka tu kwa sababu gharama zitakuwa zimepungua na viwanda vingi vitakuwa katika maeneo ambayo usafirishaji wa vifaa vyake utakuwa ni chini. Kwa hiyo, huwezi kusema tu kwamba utapunguza hili kwa sababu watu wengine watatumia fursa hii vibaya na tusingependa itumike hivyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunalipokea kama ni changamoto lakini pia tunahimiza kutumia rasilimali zilizopo katika maeneo yale ambapo pia ujenzi wa nyumba umeonekana kuwa ni nafuu zaidi.
Mheshimiwa Spika, hata ukiangalia katika ile Bodi ya Wakala wa Ujenzi wa Gharama Nafuu wa Nyumba ambayo iko kwenye Wizara yetu, wanatengeneza nyumba na vifaa vya ujenzi wanaandaa pale wanatengeneza, nyumba zake zinakuwa na gharama ya chini zaidi ukilinganisha na hali halisi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili ameongelea habari
ya Sheria ya Madini kwamba unapotaka kufanya resettlement kwa watu, anatakiwa afanyiwe malipo stahiki na pia kuandaliwa makazi kwa maana ya kuwezeshwa kupata makazi mengine. Suala hili kisheria lipo isipokuwa katika utekelezaji ndiyo unakuwa kidogo haupo vizuri. Hili tumesema kwamba Serikali tutalisimamia kwa sababu ni wengi wanaoonewa katika hali hiyo.
Mheshimiwa Spika, unakuta kwamba unamuondoa katika makazi yake, unamlipa pengine stahiki yake ya fidia, lakini hukamilishi lile linalotakiwa kwamba umlipe fidia yake na bado pia aweze kupata resettlement mahali pengine. Hili tunalisisitiza kwamba lazima unapomwondoa mtu apate kiwanja aweze kujenga katika maeneo mengine, kwa sababu unalitumia eneo lile kwa uzalishaji.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nilikuwa nimeanza kukata tamaa kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mji wa Geita tuna shida sana ya umeme na asilimia 70 ya vijiji vinavyozunguka Mji wa Geita viko katika giza. Ni lini Serikali itapeleka umeme katika kata za Nyanguku, Ihanamilo, Shiloleli, Bulela na Bugwagogo ili kuweza kusaidia katika huduma za jamii ambazo ziko katika maeneo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli vipo vijiji ambavyo havijapata umeme kwa Mji wa Geita na ametaja vitatu lakini viko zaidi ya ishirini. Nimhakikishie Mheshimiwa Peneza vijiji ambavyo ametaja vya Nyanguku na vingine baadhi yake viko katika mradi REA lakini viko katika mradi wa TANESCO. Bahati nzuri sana nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Mkoa wa Geita na mikoa ya jirani iliyokuwa inapata umeme wa low voltage sasa tunakamilisha ujenzi wa mradi wa kusafirisha umeme mkubwa unaotoka Mbeya kwenda Sumbawanga mpaka Nyakanazi na baadaye utatoka Nyakanazi mpaka Bulyankulu na baadaye Geita. Kwa hiyo, wananchi watapata umeme wa kilovoti 400 lakini tutaanza na kilovoti 220.
Kwa hiyo, napenda nimjulishe Mheshimiwa Upendo Pendeza kwamba vijiji hivyo vitapata umeme kupitia miradi ya REA na baadhi yake vitaendelea kupata umeme kupitia miradi ya TANESCO.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuangalia mpango wa kitaifa ambao ulikuwa umeweka vipaumbele 13 ambao ni National Adaptation Program of Action kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi Serikali iliweka vipaumbele 13 ambavyo vya kwanza vilihusu masuala ya maji pamoja na kilimo, lakini katika utekelezaji Serikali hela iliyopata imeweka katika ujengaji wa ukuta katika barabara ya Ocean Road na miundombinu mingine katika maeneo ya Dar-es-Salaam. Sasa Serikali haioni kwamba, inaruka vipaumbele vyake ambavyo iliviweka mwanzo na inakwamisha sasa kuhakikisha kwamba, nchi inakuwa na uwezo wa kuwa na uhakika wa suala zima la usalama wa chakula katika kuangalia hilo suala la vipaumbele?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni katika suala zima la NEMC ambalo lilichaguliwa na Makamu wa Rais, ili kuweza kupata hii ithibati. Imechukua sasa miaka mitano kupata hii accreditation na NEMC hawajaweza kupata. Tunavyopata pesa kupitia Multinational Implementation Entities Serikali inakatwa asilimia 10 na hizo taasisi kwa hiyo, NEMC ilivyopata hizo hela tulikatwa asilimia 10 kwa hiyo, inapunguza hela ambazo zingesaidia katika utekelezaji wa miradi ya kuweza kupunguza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Serikali ina mkakati gani na lini hasa kwa sababu, NEMC imeshachukua miaka mitano, Serikali sasa ni lini itakamilisha mchakato mzima na kukamilisha vigezo vyote, ili hatimaye Serikali iweze kuwa inapata hela zake moja kwa moja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, linahusu Serikali ilikuwa imeweka vipaumbele 13, lakini Serikali ikaamua kuchukua mradi ule wa Dar-es-Salaam kuhakikisha kwamba, wanaokoa fukwe zetu na kutekeleza shughuli zile ambazo zinahusu kutengeneza mifereji ya maji ya mvua na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, vipaumbele vyote ni muhimu, lakini pia tunaangalia katika vipaumbele vile, ukiacha pembeni kipaumbele ambacho tumeshaanza kukifanyia kazi, huwezi ukasema kwamba, hakina umuhimu kuliko hiyo ya kilimo. Hata hivyo, niseme tu kwamba, kama anavyojua katika ombi mradi huu una sehemu ya pili ambayo sasa hivi Serikali inaifanyia kazi. Suala la kusema kwamba labda NEMC imechukua muda mrefu, sasa miaka mitano kufanya process ya kupata usajili, ili iweze yenyewe moja kwa moja kuomba sehemu ya pili ya fedha hizi, kwa sababu najua kwamba ilikuwa inatakiwa iwe milioni kumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimwambie tu Mheshimiwa Peneza kwamba tayari NEMC imeshapita vile vigezo vyote ambavyo vilikuwa vimewekwa na hivi karibuni itaanza sasa yenyewe. Itapata usajili na kuanza kuomba ile sehemu ya pili ya fedha ambazo zinatakiwa kuokoa mazingira yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nimwambie tu kwamba, NEMC baada ya kupata huu usajili itaanza sasa kuangalia hivi vipaumbele ambavyo yeye amevizungumzia; kuhusu mambo ya kilimo. Vile vile labda nimwambie kwamba licha ya Serikali kutumia Mfuko huu wa Adaptation Fund tuna Mifuko mingine ambayo pia inaangalia masuala ya kilimo na umwagiliaji. Kwa hiyo, labda nimhakikishie tu kwamba, baada ya NEMC kupewa usajili ambao tayari imeshapita katika vigezo vile, sasa hivi tunasubiri wapewe hiyo barua ya accreditation ili waweze kuianza hii process ya kuchukua hizi hela milioni tano.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Katika suala la elimu bure, moja ya changamoto ni pamoja na utoro unaowakabili hasa watoto wa kike. Sasa ningependa kujua Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Serikali sasa ina mpango gani kuhakikisha ya kwamba watoto wa kike wanaoingia shuleni wanabaki shuleni kwa kumaliza, kwa Serikali kuweka pesa za ruzuku kwa ajili ya sanitary pads (vifaa vya hedhi) kuziongeza katika capitation fund ili kuweza kupunguza suala la utoro mashuleni. Sasa Serikali ina mkakati gani katika bajeti ijayo kuongeza pesa hizo ili watoto wetu waweze kupata pedi hizo bure mashuleni? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA
NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika makubaliano ya Jumuiya ya East Africa nadhani ni miongoni mwa jambo ambalo lilikuwa likijadiliwa sana hasa tatizo kubwa la watoto wasichana wanapokosa hivi vifaa kwa ajili ya kujikimu wakiwa shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tulichukue hili kwa sababu ni jambo la msingi basi tukifika kwenye mchakato wa bajeti sisi sote tushirikiane kwa pamoja tuangalie nini tufanye ili mradi kuhakikisha kwamba tuweze kusaidia vijana wetu watulie masomoni na wapate elimu vizuri. Kwa hiyo, tunalichukua kama mchango mzuri katika mchakato tutakuja tutaijadili. (Makofi)
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kutokana na swali la kwanza la msingi mazingira hayo pia yanafanana na kule kwetu Geita ambako wananchi wa Geita wamekuwa wakiathirika kwa kiasi kikubwa na shughuli za Mgodi wa Geita Gold. Serikali kipindi cha Waziri Muhongo na Naibu Waziri Kalemani waliunda tume kwenda kuchunguza matatizo hayo kule Geita na kubaini nyumba ambazo zimeathirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa suala hili litaisha? Kwa sababu, wananchi wanaishi katika maeneo yenye mitetemo, wanaathirika na vumbi, wanapata hata madhara ya kiafya. Ni lini sasa Serikali itasimamia huo Mgodi wa Geita Gold Mine kuhakikisha ya kwamba, inawaondoa wananchi katika maeneo ya Compound na maeneo ya Katoma ili kupisha shughuli za mgodi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kuna watu ambao wanaishi ndani ya maeneo ambayo ni square kilometer 290,000 ambazo zinamilikiwa na GGM. Kwa mujibu wa sheria ilivyo ni kwamba kuna watu ambao bado wanamiliki zile surface area, yaani kwa maana ya eneo la juu la ardhi, na maeneo ambayo ni ya chini yanamilikiwa na mgodi wa GGM, kwa hiyo, kuna wananchi ambao bado wanaishi maeneo ambayo yako ndani ya leseni ya GGM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kufika pale mwezi wa pili na nilitoa tamko kwamba kuna Kamati ziliundwa na Waheshimiwa Mawaziri waliotangulia na ilionesha kabisa kwamba kuna watu ambao wameathirika katika maeneo yale. Nikatoa tamko kwamba wale ambao wako ndani ya maeneo ya GGM, GGM kama kampuni ikae nao iwalipe fidia iwaondoe yale maeneo ambayo wale wananchi wanaathirika na mgodi huo.
Vilevile kuna watu ambao wako maeneo ya Katoma, wameathirika na matetemeko kutokana na milipuko inayofanywa na GGM. Kulikuwa kuna taarifa mbili ambazo zilikuwa zimetolewa moja ikiwa ya GST kuangalia ni namna gani yale matetemeko yalikuwa yanaathiri zile nyumba. Majibu yaliyokuwa yanatoka yalikuwa yanakizanzana kwamba kuna wengine walisema milipuko ilisababisha nyufa katika nyumba zile na kuna taarifa nyingine inasema kwamba ile mitetemeko haikusababisha zile nyufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumeamua kwa pamoja kwamba wakae waangalie tena upya na vile vile wafanye tathmini ya kutosha kwenye zile nyumba zilizoathirika wawalipe wale wananchi. Ikiwezekana wale wananchi walimo ndani ya hiyo leseni ya GGM waondolewe, wawalipe fidia, ikiwemo na watu wa Nyakabare, walipwe fidia waondoke yale maeneo ya uchimbaji. Kwa hiyo, hiyo tumeshawapa GGM na tunaendelea na maongezi na tunaendele na mikakati kuangalia namna gani ya kuweza kuwalipa fidia wananchi hawa. Ahsante sana.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mwaka 2016, Serikali ilitoa Kauli kupitia Naibu Waziri wa Madini kipindi hicho Mheshimiwa Dkt. Merdad Kalemani, kuwa Serikali inafanya mazungumzo na Geita Gold Mine ili uweze kupunguza baadhi ya maeneo ambayo yako katika leseni yake. Swali la kwanza, napenda kujua kwamba, hayo mazungumzo yamefikia wapi ili wananchi walau waweze kupata maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, wachimbaji wadogo wadogo Geita kati ya malalamiko ambayo wamekuwa nayo ni pamoja na maeneo yanayotengwa dhahabu kuwa mbali sana na kutokana na vifaa vyao duni wanashindwa kuweza kuzifikia. Serikali kupitia corporate social responsibility kwa maana ya huduma za jamii ambayo mgodi umekuwa ukitoa kama vitu vya afya na vinginevyo, haioni kwamba ni muhimu sasa ikatoa mwongozo kwa Geita Gold Mine na maeneo mengine ili katika upande wa corporate social responsibility kuwajibika kuwasaidia wachimbaji wadogo katika maeneo yao hata katika ule msimu wa kupasua miamba ili walau waweze kuzifikia dhahabu katika maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Upendo Peneza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza lile alilolizungumza la mazungumzo kati ya Serikali na Mgodi wa GGM kuwapatia maeneo ya kuchimba wachimbaji wadogo, ni kwamba Serikali inaendelea na mazungumzo hayo kwa maeneo mbalimbali ambayo migodi inaona kwamba inaweza kuyaachia kuwapatia wachimbaji wadogo. Hii siyo kwa GGM peke yake tu, wachimbaji na wenye leseni wengi kuna mahali tunazungumza nao ili waweze kuachia maeneo ya wachimbaji wadogo. Hii itawasaidia wale wanaochimba wenye leseni kuwa na mahusiano mazuri na jamii. Kwa sababu haina maana yoyote kama anachimba halafu kuna uvamizi unaendelea. Kwa hiyo, ili kudhibiti hilo, ni vizuri wakaangalia eneo fulani wawagawie wachimbaji wadogo ili kuwe na amani kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili juu ya matumizi ya CSR kwa ajili ya kuasaidia wachimbaji wadogo. Sheria na Kanuni mpya ya Madini CSR kwa sasa mpango unaandaliwa na mwenye leseni lakini mpango huo unapelekwa kwenye halmashauri, halmashauri yenyewe wajibu wake ni ku- approve kuona kwamba hicho wanachotaka kukifanya wanakihitaji. Kwa hiyo, naomba halmashauri pamoja na wenye migodi wakae chini wazungumze waone kama kipaumbele chao ni kutumia CSR kwa ajili ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wanaweza kufanya hivyo. Hata hivyo, Mgodi wa GGM umefanya kazi kubwa sana, tunajenga kituo cha mfano kule Rwamgasa cha uchenjuaji, Mgodi wa GGM umetoa fedha kwa ajili ya kusaidia kazi hiyo.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mbunge wa Jimbo husika Mheshimiwa Lijualikali anakubali kwamba ni kweli kazi inafanyika, lakini changamoto iliyopo ni kwamba umeme unawekwa kwa kurukaruka. Wakishafikisha kwenye centre vitongoji vingine havipati na kutoka kwenye centre kwenda kwenye vitongoji vingine kuna umbali mpaka wa kama kilomita sita mpaka kilomita nane, suala ambalo baadaye litakuwa gumu kwa wananchi kupeleka umeme katika hivyo vitongoji vingine.

Swali lake ni kwamba: Je, Serikali haioni umuhimu wa kuboresha usambazaji wa umeme kuhakikisha kwamba wanapopeleka kwenye kijiji basi wasambaze katika maeneo yote na vitongoji vyote vya kijiji hicho?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naomba pia niulize kwa niaba ya wananchi wa Halmashauri ya Geita Mjini ambako mimi natoka. Serikali ilituahidi ndani ya Bunge kwamba kuna maeneo ambayo yamekuwa mitaa sasa na zamani yalikuwa ni vijiji, lakini kiuhalisia bado yana mazingira kama ya vijiji hivi; Serikali iliahidi kwamba bado wale wananchi ingawa wanaishi kwenye mitaa ingewapa umeme kwa kupitia mradi wa REA. Maeneo hayo ni katika Kata za Ihanamilo; baadhi ya mitaa; Kata ya Kasamwa, Kata za Kanyara na Kata za Burela.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini sasa Serikali itatusaidia kupeleka umeme katika maeneo hayo na katika kata hizo kwa kupitia mradi huu wa REA kama ilivyoahidi ndani ya Bunge? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu maswali mawili ya nyongeza. Kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kushuruku kwamba Mheshimiwa Mbunge Lijualikali ametambua kazi mbalimbali ambazo zinaendelea katika Jimbo la Kilombero kuhusu mradi wa REA awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza. Ametoa ushauri kwamba ni namna gani Serikali inaweza ikaboresha zaidi katika usambazaji wa umeme inapofika kwenye eneo fulani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge, Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeliona hilo kwamba, kwa kuwa miradi hii ngazi yake kwanza ni ngazi ya kijiji, imetambua vijiji zaidi ya 3,559 kwa awamu hii ya kwanza, REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vina vitongoji. Kwa hiyo, Serikali ilibuni mradi ambao ilifanya majaribio ya ujazilizi kwa mikoa minane ambapo uligusa vitongoji 305 na iliwaunganisha wananchi kama 25,000 na mradi ule ulifanyika kwa mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa na mafanikio hayo, tutakuja na mradi mwingine densification awamu ya pili katika Bunge hili la Bajeti linaloendelea. Kwa hiyo tutaomba mtuidhinishie, lakini mradi huu unakwenda kutatua tatizo la vitongoji vinavyoachwa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine, hilo linatambulika.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuamini kwamba gharama za kupelekea umeme kwenye kijiji kimoja; kilimeta moja tu ni shilingi milioni 50. Kwa hiyo, Serikali ambayo inafanya mambo mengi ya kimaendeleo lazima kwenda hatua kwa hatua. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge waendelee kutuunga mkono na vitongoji vingine vitafikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge Upendo Peneza, ameelezea masuala ya Halmashauri ya Geita. Kwanza kata zote ambazo alizitaja, bahati nzuri na Mheshimiwa Mbunge mwenyewe wa Jimbo naye amelizungumzia, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maliasili, lakini naye nimpongeze pia amelielezea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba maeneo yote ambayo yako katika Halmashauri za Miji na tunatambua kwamba bado yapo katika pia katika maeneo ya vijijini, kuna mradi unakuja peri-urban ambako maeneo ya kata ambazo zimetajwa zitashughulikiwa na bei ni ile ile shilingi 27,000/=. Kwa hiyo, niwatoe hofu wakazi wa maeneo yote ya miji na mitaa, mradi wa ujazilizi na mradi wa wa peri-urban utakuja kutatua tatizo ambalo limebaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa bahati mbaya swali langu lilinukuliwa tofauti na nilivyowasilisha. Lakini kwa faida ya wananchi wa Nyakabale ninaomba kujua kwamba sehemu ya Nyakabale ni eneo limekuwa likipata shida kubwa kutokana na mgodi wa Geita Gold Mine kwa maana ya kimatatizo ya kimazingira lakini hata wananchi wenyewe kuzuia kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo ya kwamba itabidi wapishe shughuli za mgodi.

Mheshimiwa Spika, lakini ni miaka sasa hawawaondoi katika eneo hilo. Sasa ninaomba kujua tuliahidiwa na Mheshimiwa Waziri Kalemani kwamba wale wananchi wangeondolewa lakini mpaka leo hawajaondolewa. Je, Serikali inatupa leo kauli gani wananchi wa Geita hasa wananchi wa Nyakabale kuhusu kulipwa fidia ama kuruhusiwa kwamba waendelee na shughuli zao za kimaendeleo katika eneo hilo la Nyakabale?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili linahusu katika upande huo wa ulipwaji fidia, sheria yetu imeruhusu haya makampuni kuweza kutumia wathamini binafsi kwenda kuhesabu mali za wananchi na hatimaye kuweza kulipwa na hili limeleta malalamiko kwa maana ya wananchi wengine kuona kwamba wanapunjwa na kampuni hizo kutetea maslahi zaidi za makampuni hayo ya uwekezaji. Sasa Je, Serikali leo inatoa kauli gani kuhakikisha ya kwamba maslahi ya wananchi katika maeneo husika yanalindwa ahsante? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba maeneo ya Nyakabale yako ndani ya leseni ya uchimbaji yaani leseni ambayo ni special mining license ya mgodi huu wa GGM ndani ya zile kilomita 290 za mgodi huo.

Mheshimiwa Spika, ni kwamba sheria inasema kwamba ni lazima mtu ambaye anataka kuwekeza kuchimba maeneo yale watu wanaoishi maeneo yale ni lazima awalipe fidia waondoke ili aweze kufanya operation zake.

Mheshimiwa Spika, lakini eneo la Nyakabale liko nyuma ya mgodi huo na kweli kuna wakati fulani mimi mwenyewe niliweza kutembelea pale nikakuta kuna maeneo mengine ambayo wananchi walizuiliwa wasiendeleze yale maeneo yao au wasiendelee kujenga kwa sababu wako ndani ya leseni na mimi niliweza kuwapa nilitoa tamko kwa mgodi kwamba wawalipe wananchi hao na kuondoka kama wananchi hao wanaathirika na uchimbaji huo. Lakini vilevile ni kwamba mgodi walisema wako tayari wataweza kuwaondoa wale wote ambao wanaonekana wanaathirika na shughuli za mgodi.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile katika swali la pili kuhusu fidia ya yale maeneo ambayo yanazunguka mgodi ambayo yapo karibu na Mji wa Geita hapa tunavyozungumza ni kwamba uthaminishaji ulikuwa unaendelea na uthaminishaji ule ulikuwa unafanywa na kampuni binafsi lakini chini ya usimamizi wa Chef Valuer wa Serikali ambapo mpaka sasa hivi tumekwishakuona kwamba ni watu wangapi ambao wanatakiwa walipwe uthaminishaji umeshakubaliana waliothaminiwa na wathaminishaji wote wameshakubaliana na toka Jumatatu tayari fidia hizo zimeanza kulipwa na kampuni ahsante sana. (Makofi)