Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Yosepher Ferdinand Komba (14 total)

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha hoja yake, atolee maelezo mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, gari la wagonjwa ambalo Wizara iliahidi kuwa imetenga shilingi milioni 20 katika mwaka wa fedha 2016/2017 katika Wilaya ya Muheza: Je, ni lini gari hilo la wagonjwa litafika Muheza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Mheshimiwa Waziri aliahidi kupeleka gari la wagonjwa katika Zahanati ya Mgambo, Amani itakapofika mwezi Januari, 2017 lakini sasa ni mwezi wa Tano hakuna utekelezaji. Wananchi wanapata usumbufu mkubwa katika upatikanaji wa dawa hasa wanaotumia bima kwa kuwa kuna upungufu mkubwa wa dawa katika hospitali zetu. Wizara imeandaa utaratibu gani kupitia MSD ili angalau kila penye Hospitali ya Wilaya kuwe na duka la dawa ambalo kadi ya bima inaweza kutumiwa na mgojwa kupata dawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamii ya mabohora Tanga wametoa mashine ya CT-Scan kwa Hospitali yetu ya Bombo, lakini inasemekana hakuna jengo special. Kama ni kweli, Serikali ina mpango gani kuharakisha ujenzi wa hilo jengo ili mashine zifungwe na kutumika?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabisa, naomba niwape pole wafiwa wote wa ajali ya watoto kule Arusha, lakini pia niwape pole wananchi wa Mkoa wa Tanga, hasa maeneo ya Muheza, Korogwe, Tanga Mjini, Pangani ambao wamepata madhara makubwa kutokana na mvua zinazoendelea. Vile vile, niwape pole familia ya mtoto wa miaka 12 pale Kata ya Genge-Muheza ambaye alifariki juzi kwa kudondokewa na ukuta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie machache kwenye Wizara hii ya Maji. Ukiangalia kwenye Kitabu cha Waziri, ukiangalia yaliyoandikwa humu, bado hawajawa serious kuhakikisha kwamba wanamtua mama ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa najaribu kufikiria msemo wenu wa kumtua mama ndoo kichwani, sidhani kama mnamaanisha. Kwa sababu, kwa Kiswahili cha kawaida, huwezi kutua kitu ambacho hakipo. Kwa hiyo, mnataka kusema mwanamke aendelee kubeba ndoo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kuwaambia na kuwaomba, nchi ilipofikia tangu tupate uhuru hatutaki kusikia ndoo kichwani, tunataka kusikia mama anabeba maji si zaidi ya mita 400, tunataka kusikia mtoto wa kike anaenda shule bila kufikiria maji, tunataka kusikia watoto wa chini ya miaka mitano hawafi kwa magonjwa yanayotokana na shida za maji, tunataka kusikia akinamama wajawazito wanapoenda kujifungua hawaendi na ndoo za maji hospitalini, tunataka kusikia na kuona mnafanya mambo ambayo yanaendana na umri wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi zilizoendelea sasa hivi wame-advance kutengeneza ATM za maji, Tanzania bado tunafikiria ndoo za maji vichwani, ni aibu! Nimepitia bajeti ya maendeleo mmezidi kuipunguza kutoka shilingi bilioni 900 mpaka shilingi bilioni 600, sijui lengo lenu ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba nichangie kidogo kuhusu Mfuko wa Maji. Tunajua faida zinazotokana na mfuko huu ambao mliutengeneza kwa sheria hapa Bungeni mkiamini kwamba tozo ya shilingi 50 kwenye mafuta itasaidia kwenye miradi ya maji. Cha kushangaza tozo imeenda vizuri lakini matumizi mmeanza ku-diverge. Matumizi mengi ya mfuko huu yameonekana yameenda kwenye administration kuliko kwenye miradi halisi. Niwaombe muongeze shilingi 50 kwenye mfuko huu iwe shilingi 100 ili miradi ya maji iweze kutekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia naunga mkono huu Mfuko wa Maji uendelee kuongezwa hela kwa sababu, kwenye Wilaya ya Muheza tuna Mradi wa Zigi - Pongwe ambao ni almost shilingi bilioni 2.7 na mfuko huu ndiyo chanzo kikubwa cha fedha kwenye huu mradi na fedha zimeanza kutolewa. Kuna miradi mingi inaanzishwa lakini inashia katikati, niendelee kuwaomba Serikali muutendee haki mradi huu kwa sababu hali ya maji Muheza ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba mtutendee haki katika mradi huu kwa sababu mpaka ninavyoongea Muheza Mjini ambapo tumeshaanza kuanzisha Mamlaka ya Mji Mdogo tuna asilimia isiyozidi 25 ya wananchi wanaopata maji safi na salama. Niwaombe sana muutendee haki mradi huu kupitia mfuko huu kwa kuongeza Sh.50/= ili iwe Sh.100/= ili angalau 70% iende vijijini, 30% ibakie mjini. Pia kwa kutengeneza mfuko haitoshi, tunaomba kuwe na utaratibu mzuri wa kusambaza hela hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kitu kingine naomba niongelee ukosefu waemergency plan. Tumeona kuna mafuriko yanaendelea maeneo mbalimbali ya nchi lakini hakuna plan yoyote ya Wizara ya Maji kwa ajili ya ku-control hali hii. Mafuriko yanatokea mabomba yanaziba, hivi sasa
ninavyoongea maji ya Mkoa wa Tanga katika maeneo mengi, Tanga Mjini, Muheza, Korogwe na maeneo mengine ni kama chai ya rangi, lakini kama mngekuwa na emergency plan, treatment plan na strainer za kuchuja maji ingesaidia sana inapotokea mvua na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia miundombinu ya maji kwenye nchi hii imechakaa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda ku-declare interest angalau haiko kwenye hela lakini mimi nimetokea Tanga na mnajua historia ya Mkoa wa Tanga katika suala la viwanda. Mnajua Tanga miaka ya 1980 ni kati ya Mkoa ambao ulikuwa maarufu sana kwa viwanda kwa Tanzania hii. Tunavyoongea sasa hivi, viwanda vingi vimefungwa, vilivyobinafsishwa, vimekufa, watu wameiba vifaa, viwanda Tanga hakuna tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanga tumejaliwa kuwa na bandari, viwanja vya ndege na reli ambayo mpaka sasa hivi hatujajua Serikali lini itaamua kutujengea kwa kiwango cha standard gauge.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi pia natokea Muheza, Wilaya ambayo ni maarufu sana kwa kilimo cha matunda hasa machungwa. Wilaya ambayo ina hali zote za hewa tunazozijua; kuna hali ya baridi na joto, kiasi kwamba tunaweza kulima mazao yanayotokana na baridi na mazao yanayotokana na joto.

Mheshimia Naibu Spika, nakumbuka Mheshimiwa Waziri wa Viwanda niliwahi kumgusia suala la Muheza nikaomba kwamba atafute mwekezaji kwa ajili ya machungwa yetu yanayozalishwa Muheza. Wakulima wamekuwa wakipata hasara sana ya machungwa yanayozalishwa pale, yamekuwa yakioza. Wamekuwa kama wana uwezo zaidi kutegemea soko la Kenya lakini Tanzania hakuna kiwanda karibu; Tanzania, Muheza hakuna kiwanda wakulima wanapata shida sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri tunajua lengo la Tanzania ya viwanda ni jema, lakini kama tusipokuwa makini hatuwezi kufikia huko. Kama hamkujiandaa, tafuteni namna nyingine ya kuliweka sawa. Kwa nini nasema hivyo? Waziri wa Viwanda yeye kama yeye hawezi kufikia lengo la viwanda kama Wizara nyingine hazijaonesha ushirikiano kwako. Yeye kama yeye hawezi kufikia kwenye viwanda, kama Wizara ya Fedha haijaamua kuona kama suala la viwanda ni muhimu. Pia hawezi kufikia lengo kama Wizara ya Ardhi na Wizara ya Usalama na mambo mengine hazijamsaidia. Kwa hiyo, inatakiwa suala la viwanda liwe ni la nchi, siyo Wizara. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa na miundombinu mizuri kwa ajili ya uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee viwanda na wanawake. Sensa ya viwanda inaonesha asilimia 99.15 ni viwanda vidogo sana na viwanda vidogo. Kwa haraka haraka ukiangalia katika sensa hii, utaona viwanda vidogo sana ni kati ya mtu mmoja mpaka wanne; viwanda vidogo ni kati ya mtu mmoja mpaka 50. Ukiangalia kwa undani zaidi utakuta hivi viwanda vidogo vingi vinamilikiwa na wanawake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, sijaona popote kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri ambapo ameonesha namna ambavyo atamsaidia mwanamke aingie kwenye uchumi wa viwanda akiwa anajiaamini. Tunajua hali ya kipato cha wanawake wengi wa nchi hii ni cha chini. Wizara haijaandaa utaratibu wowote kumwezesha mwanamke ambaye kwa asilimia kubwa ndio amewekeza kwenye hivi viwanda vidogo aweze kujikwamua. Kwa hiyo, tuna viwanda vingi vya mtu mmoja mpaka watano, tutafika lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kitu kingine tunapoongelea Tanzania ya viwanda, lazima tukubali na tuamue tunataka viwanda vya aina gani? Hatuwezi kuwa na viwanda nchi nzima kwa mara moja. Lazima tutenge maeneo, lazima tuwe na point ya kuanzia. Tanzania tunataka viwanda ndiyo, tunataka viwanda vya aina gani? Tunataka viwanda vya kutumia malighafi gani? Tutakapokuwa tumefanya hayo maamuzi, itakuwa ni rahisi. Hatuwezi kujenga viwanda nchi nzima, lazima tuamue baada ya miaka 10 miaka 15 tunataka katika viwanda Tanzania ijulikane katika kitu gani? Ziko nchi ambazo zinajulikana kwa ajili ya kuzalisha products za maziwa peke yake. Tanzania tunataka tujulikane kwenye nini katika viwanda? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niongee suala la VETA. Tunajua inatakiwa kuwe na elimu na ujuzi wa kutosha ili tuingie kwenye viwanda tukiwa tunajiamini. Kumekuwa na tatizo kubwa sana katika Vyuo vyetu vya VETA, siyo tu udahili lakini pia vifaa na mashine zinazotengenezwa VETA zina bei ghali kuliko sehemu nyingine yoyote. Sasa kwa namna hii hamwezi ku-encourage viwanda wakati watengenezaji wetu wa ndani wanapitia mazingira magumu katika kuanda hizo zana za kufikia kwenye viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali isaidie wale wataalam wa VETA ambao wanatengeneza mashine ambazo zinaweza zikatumika kwenye nchi yetu, wapunguzieni kodi ambazo ni mzigo kwa wafanyabiashara wengi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu na msimamo wa Wizara katika yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Wizara itasaidia upatikanaji wa Kiwanda cha Matunda Wilaya ya Muheza; kwa kuwa wafanyabiashara na wakulima wa Wilaya Muheza hawanufaiki na zao la matunda hasa machungwa? Katika Wilaya ya Tanga Mjini Kata ya Kiomoni, kuna Kampuni inaitwa NEEL KHANT Lime Limited Tanga, kinachomilikiwa na Bwana Rashidi Liemba.

Kiwanda hiki kimekuwa na madhara makubwa kwa wakazi wanaozunguka eneo hilo hasa wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari Kiomoni. Wizara inafahamu changamoto hiyo? Iko tayari kushirikiana na NEMC kufuatilia usalama wa raia wa eneo hilo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini Tanga Special Economic Zone (SEZ) imetengewa fedha kidogo; shilingi bilioni
2.7 katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa mwaka 2016/2017 - 2020/2021 wakati Tanga ni Mkoa wa Viwanda? Katika historia ya nchi, Tanga ndiyo mkoa wa kwanza ndani ya nchi hii kuwa na viwanda vingi miaka ya 1980.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanamke na viwanda. Sensa ya Viwanda inaonesha asilimia 99.5 ni viwanda vidogo sana na viwanda vidogo. Kwa takwimu hizi, ni wazi viwanda vingi vidogo vinamilikiwa na wanawake. Je, Wizara imejipangaje kuhamasisha wanawake kujiunga katika Sekta hii ya Viwanda?

Je, Serikali kupitia Wizara ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa viwanda vinakuwa gender sensitive katika product na ajira?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Samahani, jina langu ni Yosepher Komba sio Yosephu. Nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kitabu cha Waziri ukiangalia na uhalisia, hakuna kitu. Kwa sababu gani nasema hivyo? Inaonekana Tanzania ya viwanda ipo hewani, haina mizizi. Huu msemo ni msemo wa kisiasa ambao hauna mizizi. Kwa sababu gani nasema hivyo? Wameongea Wabunge waliopita kwamba hakuna uhusiano wa viwanda na mahitaji ya viwanda; hakuna uhalisia wa viwanda na mahitaji ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa nature ya nchi yetu, tukubali tukatae, kama tunataka viwanda, ni lazima viwe ni agro-industries, viwanda vinavyotegemea kilimo, vinavyotegemea mazao yanayotokana na kilimo, lakini hakuna uhusiano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wakulima wanahangaika, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo aliwahi kusema kwamba jembe tutalikuta makumbusho. Hizo ni lugha za kisiasa. Tumefikia Tanzania kutokutumia jembe! Tumefikia Tanzania ambayo hatutegemei mvua kwa ajili ya kilimo! Viwanda vinahitaji malighafi muda wote, lakini kilimo chetu cha kutumia mvua; isiponyesha hakuna kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, pamoja na kukaa na kupanga, kuna utaratibu mzuri na uhusiano mkubwa na sekta nyingine. Tusiongee kama sisi, tuongee kama nchi, tuongee kama Wizara ambazo zinafanya kazi pamoja. Kila mtu asiwe na personal interest kwenye Wizara yake; kila mtu anaongea anavyojisikia. Waziri wa Viwanda wewe huwezi kukamilisha lengo lako kama huna uhusiano mzuri na Waziri wa Kilimo, huna uhusiano mzuri na Waziri wa Ardhi, huna uhusiano mzuri na Waziri wa Miundombinu na sekta nyingine. Hakuna kitu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua mahitaji ya viwanda kama malighafi na teknolojia. Tuangalie suala la teknolojia. Ni kwa kiasi gani hivyo viwanda vitakavyojengwa vitaweza kukidhi teknolojia ambayo wananchi wetu wanayo? Tumelenga viwanda vidogo na viwanda vya kati ambavyo kwa asilimia kubwa ni wananchi wa kawaida, wenye elimu ya kawaida. Tumeongea kuhusu VETA, tumeongea kuhusu maeneo mbalimbali ambayo yangeweza kutoa ujuzi kwa wananchi wetu; hilo halijafanyika. Mheshimiwa Waziri anatuambia Tanzania ya Viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea miaka mitano hii ungetumia nguvu nyingi sana kutengeneza miundombinu ya viwanda, lakini siyo viwanda kwa maana ya majengo, tunadanganyana. Tungetengeneza miundombinu ambayo inge-facilitate viwanda. Tunasema uwekezaji, tunasema Serikali haijengi viwanda, tunawaita wawekezaji. Tujiulize, miaka yote wawekezaji walikuwa wapi kiasi kwamba Mheshimiwa Waziri amefanya lipi kubwa la kumvutia mwekezaji katika kipindi ambacho yeye amekuwa Waziri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ni yale yale ambayo miaka 20 au 30 iliyopita wawekezaji walishindwa kuja kuwekeza. Hata yale maeneo ambayo viwanda tulivibinafsisha, vingi vimekufa. Mimi natokea Mkoa wa Tanga, kuna viwanda vingi. Tulikuwa na viwanda vya chuma, viwanda vya blanketi, viwanda vya matunda, viwanda vya mafuta, viwanda vya kila aina, vimekufa. Tanga ilikuwa ni Mkoa wa Viwanda miaka ya 1980, lakini sasa hivi Tanga imekuwa ni magofu. Viwanda vingi vilivyokuwepo wameiba mashine, wameiba kila kitu, wengine wamehamisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunategemea zao la mkonge, tulikuwa tuna mashamba kwa ajili ya kuzalisha mbegu za mkonge, yamekufa. Tulikuwa na estate nyingi sana, zimekufa. Wawekezaji wameshindwa, wamerudi kwenye nchi zao, yale maeneo wananchi hawayatumii kwa kilimo, yamebakia kuwa mapori.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema tunataka viwanda, viwanda vipi ambavyo haviangalii malighafi? Tunajua bei ya katani katika Soko la Dunia; tunajua bei ya mkonge, tunajua thamani yake kwenye Soko la Dunia; lakini tunataka viwanda ambavyo tutawadanganya wananchi kwa maneno, kwenye uhalisia hakuna kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tujiulize, Mheshimiwa Waziri anapotuambia nchi ya viwanda, anataka ku-compete na nani? Amejiandaa ku-compete na nani? Anaposema Tanzania ya viwanda, ajue kwenye dunia hii kuna nchi kibao ambazo zipo katika hiyo level ya viwanda. Amejiandaaje ku-compete nao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 91, kuna hili Shirika la Viwango (TBS), naomba ninukuu baadhi ya maneno aliyoyaandika hapa. TBS imekuwa ikishirikiana na Jeshi la Polisi na Taasisi nyingine za Serikali kama TFDA, TRA FCC, GSLA na EWURA katika kufanya ukaguzi wa kushtukiza sokoni ili kuhakikisha kuwa bidhaa dhaifu zilizo chini ya kiwango na ambazo siyo salama kwa afya au matumizi ya mlaji zinaondolewa sokoni.
Kwa hiyo, sasa TBS wanaenda kuvizia sokoni. Wanaenda na Polisi, TRA na FDA kuvizia sokoni. Wakati zinaingia, hakuna utaratibu wa kuhakikisha kwamba haziingii. Hii kauli inajidhihirisha, hata Mheshimiwa Rais juzi amesema.
Wafanyabiashara wanavizia sukari ambazo zinaelekea kuharibika, wanazinunua, wanaziingiza Tanzania. Viongozi mnalijua hilo, mnangoja ziingie, zikifika sokoni, mnaenda kuzitafuta. Wangapi watakuwa wameathirika na hizo bidhaa? Tunajua bidhaa zinazotoka nje ni za hali ya chini; zinakuwa na bei ya chini kutokana na ubora pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wanazalisha bidhaa ambazo ni bora, lakini inakuja kwenye bei kutokana na hali halisi ya Mtanzania hawezi kununua kitu cha sh. 10,000/= wakati kuna kitu hicho hicho kwa sh. 5,000/=. Kwa hiyo, Watanzania wengi kutokana na hali ya uchumi, hatuangalii ubora, tunaangalia uwingi. Kwa hiyo, hakuna namna kama hamjaweka mkakakati mzuri, kuhakikisha kwamba wazalishaji wa ndani wanalindwa kuanzia kwenye utaratibu wao wa uzalishaji. Wanatumia gharama nyingi sana, mwisho wa siku sokoni lazima bidhaa yake iwe na bei ghali. Mtanzania anashindwa kuinunua, anangoja inayotoka nchi za nje. Tunalalamika, tunataka viwanda, tuna nchi ya viwanda, naona hiki ni kitu ambacho hakiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi nasoma shule ya msingi, kulikuwa kuna kitu tunaita mazingaombwe. Anakuja mtu, tunachangia shilingi hamsini hamsini, tunaingia, tunaonyeshwa namna ya kutengeneza shilingi elfu kumi. Sasa naona mazingaombwe yale ambayo nilikuwa naamini ni utoto kudanganywa, yanaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Waziri, tunajua ipo kwenye ilani, ipo kwenye maneno ya viongozi wako; Mheshimiwa Rais na viongozi wengine kwamba Tanzania ya Viwanda. Mkoa wa Tanga tuliahidiwa Tanga ya Viwanda mwaka 2010 na aliyekuwa Rais wa Awamu ile ya Nne, sasa leo hii ukisema Tanzania ya Viwanda, watu wa Tanga hawatakuelewa, kwa sababu walishasikia Tanga ya Viwanda, haikuwezekana. Tanzania ya Viwanda ni ndoto! Kwa miaka hii, kwa utawala huu ambao hauna uhusiano katika Taasisi zake, ambao kila mtu anataka kujinufaisha yeye kutengeneza jina lake! Ukiwa Waziri, cheo cha kisiasa kiweke pembeni. Ukiwa Waziri, jaribu kusikiliza wataalam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni kwamba Waziri anakuwa mkuu kwenye Wizara yake kushinda mtaalam, kushinda mtu yeyote hata kama hana utaalam wowote, kwa sababu tu ya cheo. Hiyo imekuwa ikiathiri sana mapendekezo na nia ambayo tunayo Watanzania. Naomba Mawaziri, Mwanasiasa yeyote anayejiamini na mwenye nia njema na nchi yake, lengo lake hata kama hana ujuzi wowote ni kuhakikisha wenye ujuzi wanafikia matamanio yao. Mwanasiasa lazima ahakikishe kwamba binadamu hafi; lazima ahakikishe mkulima anapata mazao mazuri kwa sababu ndiyo lengo la mkulima; ahakikishe kwamba engineer anatengeneza barabara nzuri; siyo kuwa na amri kwenye kila kitu ambacho hatuna utaalam nacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie suala la masoko. Tunajua wakulima wetu wanavyolima kwa shida na hilo jembe la mkono ambalo tumeambiwa litakuwa historia, sijui ni mwaka gani. Tangu mwaka 1961 tunapata uhuru lilikuwepo, hatujui limepungua kiasi gani, lakini tunaambiwa na Waziri wa Kilimo litakuwa historia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania kwa kilimo cha jembe la mkono wamejitahidi sana hapo walipofikia. Masoko yamekuwa ni shida! Masoko yamekuwa ni tatizo! Sijui ni kwa namna gani na kwa kiasi gani mnawaandalia masoko wakulima hawa ili hayo mazingira ya viwanda yawe rahisi kwao? Kwa sababu gani nasema hivyo? Masoko yanaendana na miundombinu, masoko yanaendana na bei, yanaendana na gharama za uzalishaji,…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Yosepher muda wako umemalizika.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja ya hotuba ya Upinzani.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kuunga mkono hoja ya hotuba ya Kambi ya Upinzani. Ninaamini yapo mazuri mengi ambayo Serikali ikiamua kuyafuatilia na kuyatekeleza tunaweza tukafikia lengo la Tanzania yenye Watanzania wenye afya bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuzungumzia vifaa tiba. Kumekuwa na tatizo kubwa sana, Dada yangu Waziri, Mheshimiwa Ummy Mwalimu unafahamu, wewe ni wa Mkoa wa Tanga, unafahamu hali ya Hospitali ya Bombo, unafahamu kwamba kuna changamoto kubwa sana ya vifaa, kuna changamoto kubwa sana ya mashine za x-ray, kuna changamoto kubwa sana ya vifaa. Lakini pia mmeweka duka la MSD pale, lakini mara nyingi na lenyewe pia linakosa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pana duka la MSD ambalo mmeliweka pale lakini inafikia hatua mgonjwa anatibiwa Bombo anaambiwa atoke akanunue dawa nje ya Bombo, kwa hiyo niwaombe sana na pia tumesikia tunaomba Waziri utakapokuja kuhitimisha utuambie, tumesikia jamii ya Mabohora wametoa msaada wa CT Scan, we are not sure utakuja kutuaminisha, lakini inasemekana kwamba hakuna eneo la kufunga zile mashine. Kwa hiyo, mashine zimetolewa zimewekwa pending, wananchi wanahitaji huduma hakuna pa kuweka mashine. Tunakuomba Waziri utakapokuja hapa utuambie kama kweli hakuna eneo, ni lini na mkakati gani mmepanga kwa ajili ya kujenga jengo kwa ajili ya kufunga hizo mashine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni bima ya afya. Kumekuwa na changamoto kubwa sana kwa watumiaji wa bima ya afya, pamoja na kuwa bado idadi ya watumiaji ni ndogo, ni asilimia nane tu ya Watanzania. Bima ya afya ukichukulia Wilaya ya Muheza wananchi wanachangia shilingi 10,000 ambapo wanatumia kwenye zahanati na kwenye Hospitali ya Wilaya, lakini katika ile bima ya afya tunaomba Serikali kupitia Wizara iandae utaratibu wa kuwa na maduka katika kila Hospitali ya Wilaya ambayo yatasaidia wale ambao wanakosa dawa kwenye hospitali kwenda kupata dawa kwenye maduka ambayo yanaweza kupokea bima. Kwa sababu ukikosa dawa kwenye hospitali kwa kutumia bima hakuna namna unaweza kupata dawa nje ya pale na wananchi wanapotumia bima wanaamini hakuna namna wanaweza kutumia hela zaidi ya kupata ile huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna magonjwa ambayo siyo ambukizi yanazidi kuongezeka kwenye nchi yetu kama kisukari, pressure, magonjwa ya wanawake yanayoambatana na uzazi, shingo ya kizazi na mambo mengine. Ninaiomba Wizara ije ituambie ina mkakati gani wa dhati kwa ajili ya kushughulikia suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee hapa kuhusu watoto wa kike, masuala yanayoambatana na uzazi. Kumekuwa na hilo tatizo kubwa tunaita fibroid kama sikosei, imekuwa ni tatizo kubwa sana kwa wanawake, kwa watoto wa kike kuanzia miaka 18 mpaka 25 wengi wanapata hilo tatizo, inavyosemekana kwenye jamii yetu kwa sababu hakuna elimu ya kujua hasa chanzo cha hilo tatizo, wengine wanasema ukiwa na hilo tatizo wewe ulikuwa unajihusisha na ngono na watu wengi, wengine wanasema wewe ulitoa mimba sana kwenye usichana wako. Kwa hiyo, hata wale wanaougua huu ugonjwa wanajificha kwa kuogopa jamii inavyochukulia huo ugonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kupitia Wizara mtoe elimu kwa Watanzania wajue kwamba ugonjwa huu sababu zake ni hizi ili yule anayeugua ule ugonjwa awe huru kutoa na kusema kwamba mimi naugua hiki. Wengine tunaogopa, wale wasichana ambao hawajaolewa wanaogopa kusema hilo kwa sababu inaweza ikapelekea kukosa watoto kwenye ndoa, kwa hiyo anakaa kimya, anaolewa, anaendelea na matatizo yake. Ninaomba Wizara itoe elimu katika haya masuala, pia watoe elimu ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua wananchi, wafanyakazi wa Serikali, mashirika binafsi wanakuwa na mazingira magumu ya kufanya mazoezi, pia wanakuwa na mazingira magumu ya kuwa na diet nzuri. Niombe kupitia Wizara yako, tengenezeni vipeperushi, tengenezeni utaratibu wowote ambao utasaidia kutoa elimu kwa wafanyakazi hasa wa Serikali, katika masuala ya mazoezi na chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu afya ukila vizuri, ukifanya mazoezi magonjwa mengi yatakuwa mbali na wewe. Kwa hiyo, ninaiomba Wizara itumie fursa hiyo, itoe elimu kwa wananchi, itoe elimu kwa viongozi, tuwe na tabia ya kufanya mazoezi, tuwe na tabia ya kujali afya katika chakula. Itasaidia kupunguza gharama nyingi ambazo tunazitumia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nianze kwa kumkumbusha dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Mbunge mwenzangu wa Mkoa wa Tanga, mwaka 2016/2017 kwenye bajeti aliahidi katika Wilaya ya Muheza, Hospitali Teule ametenga milioni 20 kwa ajili ya gari la wagonjwa, lakini mpaka hivi ninavyoongea halijafika. Sasa ningeomba atakapokuwa anahitimisha atuambie hilo gari limekwamia wapi kwa sababu Wilaya ya Muheza Teule tuna shida kubwa sana ya gari la wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hilo tu kwenye Wilaya ya Muheza, kuna upungufu wa watumishi wasiopungua 117 katika Wilaya ya Muheza, lakini pia kuna upungufu mkubwa wa dawa na vifaa tiba. Tuna tatizo kubwa la dawa kuwa ghali, hasa dawa ya nyoka na dawa ya mbwa. Wananchi wanaopata matatizo haya wamekuwa wakitibiwa kwa sindano moja Sh.250,000 ya nyoka na inatakiwa sindano tatu na kama hauna kunakuwa hakuna msamaha katika hilo. Wameshapoteza maisha wananchi wasiopungua watano katika Hospitali Teule kwa sababu ya tatizo hili la kuumwa na nyoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri alione hili kama ni ajali kama ajali nyingine. Wananchi ambao wanapata tatizo la kuumwa na nyoka au na mbwa wawe wanatibiwa bure kwa sababu wanakuwa hawajajiandaa na hili tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine napenda kuongelea haki na maendeleo ya watoto. Tunajua watoto wana haki zao, tunajua watoto wanatakiwa watunzwe mpaka kufikia umri fulani ambao wanaweza kujitambua. Haki ya kwanza ni haki ya kiliniki. Tumeshuhudia na kama Waziri na Wizara yake wafanye utafiti waone, watoto wengi wanapoachishwa kunyonyeshwa kati ya miaka miwili mpaka miwili na nusu wanakosa haki ya kuendelea na kiliniki. Watoto wengi wanabaki nyumbani wakati Sheria ya Afya inataka waende kiliniki mpaka miaka mitano. Kwa hiyo nimwombe Waziri kupitia Wizara yake waandae mkakati wa kufumbua hili suala. Watoto wengi wanabakia nyumbani kati ya miaka miwili na mitano wanapata magonjwa ambayo mwisho wa siku yanawasumbua kutibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haki nyingine ya watoto hawa ni makao na vituo kwa wale ambao wamekosa malezi ya wazazi wao. Nimeangalia takwimu za kwenye taarifa yako ya leo, kuna vituo 157, kituo kimoja tu ndicho kinamilikiwa na Serikali. Kwa hiyo wanataka kusema Serikali hawako serious na hili suala? Kama wanawaachia watu binafsi ndio wawe wanahangaika na watoto ambao wanatelekezwa, watoto wenye matatizo kwenye jamii, Serikali wana kituo kimoja tu kiko Kurasini, vituo 156 vinamilikiwa na watu binafsi. Hata hivyo, hawa watu binafsi hawawapi nafasi ya kutosha na kuwa-support ili waweze kuanzisha hivi vituo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kusajili vituo vya watoto yatima na watoto wenye mahitaji ni mgumu kwa watu binafsi, ni mgumu sana. Una mahitaji mengi sana kiasi kwamba mwenye nia anaishia njiani. Kwa hiyo niombe haki hizo za watoto zizingatiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine nataka kuongelea hapa. Sisi katika Wilaya ya Muheza tuna ujenzi wa hospitali ya wilaya katika Kata ya Lusanga, wananchi mpaka dakika hii wamejitoa kwa nguvu zao na mali zao kwa kiasi kikubwa, tuna michango ya kila kata kwa ajili ya hii hospitali. Tumeona imetengwa 1.5 billion, its ok, tunaomba kutenga huku kusiishie kwenye kitabu. Tunaomba hizi hela zifike Muheza tukajenge hospitali ya wilaya kwa sababu hospitali tuliyokuwa nayo tunachangia na kanisa lakini pia bado haikidhi mahitaji. Kwa hiyo niombe 1.5 ifike kwa wakati isije ikapotelea njiani kama vile ambavyo tunatafuta 1.5 trillion kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalotaka kuzungumzia, tunao ujenzi wa Chuo cha Utafiti kule Amani, ilizungumzwa sana na viongozi wameahidi sana kipindi cha kampeni lakini mpaka sasa hivi na nimepitia humu sijaona chochote ambacho kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa hiki Chuo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu. Tunayo NIMR iko kule lakini bado inashindwa kufanya kazi inavyotakiwa kwa sababu ya ufinyu wa maeneo. Waliahidi watajenga chuo kingine, tunaomba hilo suala Mheshimiwa Waziri atakuja kuniambia ni lini wtaanzisha ujenzi wa hiki chuo kwa sababu tunakihitaji sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala lingine; kuna kituo cha wakoma narudi tena, Kituo cha Wakoma kule Tononoka Ngomeni. Ugonjwa ambao unaanza kuonekana kama vile haupo lakini unazidi kukithiri, ugonjwa ambao dalili zake zinaonekana kuanzia miaka mitatu mpaka thelathini, ugonjwa ambao ukikupata unapata ulemavu wa viungo unapata na upofu, ugonjwa ambao unaongoza kwa kutengwa na jamii. Tunacho kituo kule kina hali mbaya kina wazee, kina wanawake, kina watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Waziri na Wizara yake, kwanza, wale wanawake wanahitaji kuinuliwa kiuchumi, lakini pili, wale watoto wanahitaji kupata mahitaji yao ya muhimu ya afya, tatu, wale wagonjwa wanahitaji kupata tiba na huduma zingine za afya, kwa wakati na kwa usahihi, lakini lishe ni tatizo na matatizo mengine naomba ni…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tanga tumeanzisha utaratibu wa kuhamasisha wakulima kila Wilaya kulima kilimo cha mihogo ambacho kitasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Tunaiomba Serikali itusaidie kuboresha Chuo cha Utafiti Mlingano ili kiweze kupata fedha, wataalam na vifaa kwa ajili ya kusaidia wakulima kulima kilimo chenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Muheza na Lushoto ni maarufu kwa kilimo cha matunda, mbogamboga na viungo, mfano, machungwa, ma-apple, maembe, mdalasini, hiliki, pilipili manga na pilipili mtama. Pamoja na wakulima kujitahidi lakini kumekuwa na tatizo kubwa la magonjwa ya mimea na dawa zimekuwa bei ghali kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni ni wakati muafaka wa kuwasaidia wakulima kwa kupunguza gharama za upatikanaji wa dawa za kuulia wadudu ili wakulima walime kilimo chenye tija? Je, Serikali iko tayari kuwasaidia wakulima hawa kupata masoko ya uhakika kwa kuwa hadi sasa wakulima wa matunda hasa machungwa wanategemea walanguzi kutoka Kenya, kitu ambacho kinasababisha wakulima kutokuwa na maamuzi juu ya bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha mkonge. Moja ya mikoa ambayo inalima mkonge kwa wingi ni Mkoa wa Tanga na karibu kila wilaya ina shamba au mashamba ya mkonge lakini cha kushangaza mashamba mengi yamegeuka mapori na mengine yamekufa. Serikali haioni kuacha hili zao kupotea ni kuwakosesha wananchi ajira na kipato? Je, Serikali iko tayari kuwanyang’anya wawekezaji na kuwapatia wananchi ambao wako tayari kufufua mashamba hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya samaki. Mkoa wa Tanga umejaliwa kuwa na bandari ambapo wavuvi na wananchi wanaozunguka au waliokaribu wanapata ajira lakini pia wanapata chakula. Wavuvi wamekuwa wakipata usumbufu wa kodi, ukosefu wa masoko ya uhakika na kupelekea kuuza samaki kwa bei ya hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili la bei linatokana pia na ukosefu wa viwanda vya samaki, hili limekuwa tatizo la muda mrefu. Je, Serikali kupitia Wizara hii ina mpango gani wa kujenga kiwanda cha kuchakata minofu ya samaki ili wavuvi wawe na uhakika wa kipato?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, fedha itengwe kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi hasa majumbani (house hold water treatment). Hii itasaidia kupunguza maradhi yanayotokana na maji kuchafuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, uchakavu wa miundombinu. Wilaya ya Muheza ni moja kati ya Wilaya ambazo zina miundombinu chakavu sana. Je, Wizara imeandaa utaratibu gani ili kuboresha miundombinu hii kwa kuwa kuna miradi mingi inaanzishwa lakini kwa uchakavu huu haiwezi fanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, treatment plant. Mji wa Korogwe unahitaji chujio na treatment plant yenye gharama ya shilingi bilioni sits. Wafadhili toka Australia wameonesha utayari wa kutoa mkopo wa riba nafuu kwa Mji wa Korogwe.

Je, Serikali iko tayari kusaidia Mji wa Korogwe kupata mkopo huo?

Mheshimiwa Naibu Spika, uvunaji wa maji. Wizara imeandaa utaratibu gani wa kusimamia Halmashauri ambazo hazijatengeneza Sheria Ndogo katika Halmashauri zao ili kila anayejenga nyumba yenye bati (shule na hospitali) aweke mifumo ya uvunaji maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mapango ya Amboni ni moja ya vivutio vikuu vya utalii katika Jiji la Tanga. Ni mapango ambayo ni muhimu sana kwa mapato na mvuto kwa Jiji la Tanga , lakini kuna changamoto zifuatazo:-

(i) Miundo mbinu ya barabara kwenda mapangoni;

(ii) Mto unaopita pembezoni unamega kingo za mapango; na

(iii) Uchimbaji wa kokoto unaharibu mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba Mpango mkakati na wa haraka na dharura ili kuboresha miundombinu yote muhimu ili kuongeza mapato; Eneo la mapango liainishwe ili liweze kutunzwa na kulindwa; Vivutio vingine kama Chemichemi ya Maji moto ya Sulphur Amboni, Mapango ya Tongoni na vivutio vingine ili kuvitangaza na kuviboresha zaidi; na Serikali ifuatilie na kuvitangaza vivutio ambavyo ni vya kipekee kama vile Msitu wa Asili wa Amani na Vipepeo adimu duniani ambavyo vinapatikana huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipaka katika hifadhi; kumekuwa na migogoro mingi na ya muda mrefu kati ya wananchi wanaoishi karibu na hifadhi na Serikali au wahifadhi wa maeneo yaliyotengwa kwa hifadhi. Kumekuwa na mgogoro mkubwa kwa wananchi wanaoishi Kata ya Lunguza kwenye mbuga ya Mkomazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba Serikali ikapime mipaka upya ili kuondoa migogoro; Katika kupima waweke free zone ili kupunguza migogoro na ukaribu wa makazi ya wananchi na hifadhi; Hifadhi zijitahidi na zisimamiwe ili zirejeshe kiasi cha mapato katika miradi ya kijamii ili kusaidia kuwajengea wananchi imani na nia njema ya kuwa na hifadhi ni kwa maendeleo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga viwanda vingi vimekufa kifo kitakatifu, Viwanda vya Chuma, Viwanda vya Mbolea, Viwanda vya Mafuta ya Kujipaka na kadhalika. Katika hotuba yako hakuna mkakati wowote wa kufufua viwanda mkoani Tanga. Naomba utakapohitimisha nipate maelezo kuhusu masuala yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Matunda Tanga ambacho kilipangwa kujengwa Segera ili kiweze kukusanya matunda ya Muheza, Lushoto na Handeni, je, ni lini na wapi Kiwanda cha Matunda kitajengwa Tanga?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Muheza Kata Magorofo kuna shamba kubwa la michikichi ambalo linakufa kwa kukosa kiwanda cha kukamua. Je, ni lini Serikali itafufua kiwanda cha kukamua mawese kwa ajili ya upatikanaji wa ajira kwa wananchi na bidhaa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mkakati gani wa kushughulikia matatizo ya wafanyakazi, viwandani ambayo nayo kwa asilimia fulani yanachangia kufa, mfano wafanyakazi wa viwanda vya chai, Tarafa ya Amani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inachangia zaidi ya asilimia 30 ya pato la Taifa na inaajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania na inachangia asilimia 65 ya malighafi viwandani. Cha kushangaza ni asilimia 0.52 ya bajeti kuu ya Serikali na imekuwa ikishuka kila mwaka wa bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge wa Mkoa wa Tanga na Mkoa wa Tanga tunalima mazao mbalimbali lakini mazao makuu ni mahindi, mihogo, machungwa, viungo na michikichi. Naomba Waziri atakapokuja atoe maelezo katika mambo yafuatayo:-

(i) Zao la machungwa limeingiliwa na wadudu. Wakulima wanalima kwa gharama kubwa, mfano mzuri wakulima wa Wilaya ya Muheza wanauza machungwa kwa bei ya hasara ya shilingi 40. Je, Waziri ana mkakati gani wa kusimamia soko la machungwa na dawa kwa ajili ya magonjwa yanayokumba zao hili?

(ii) Zao la minazi (Pangani) linasumbuliwa na wadudu, hivyo kufanya wakulima kupata hasara sokoni na mazao kukosa ubora unaotakiwa sokoni.

(iii) Katika Mkoa wa Tanga, Serikali ya Mkoa na Wilaya zake tulikubaliana kuwezesha wakulima wa zao la mihogo. Je, Serikali ina mkakati gani kuandaa soko kwa wakulima hawa pindi inapofika kipindi cha mavuno? Je, ni mpango gani wameuandaa kuhusu dawa ili kunusuru zao hili?

(iv) Zao la michikichi Tanga (Muheza), Kata ya Magoroto kuna estate kubwa ya shamba la michikichi lakini shamba hili halina faida kwa wakulima na viwanda vya kukamulia vimekufa. Je, Serikali ina mkakati gani wa kufufua zao la michikichi ili kukabiliana na upungufu wa mafuta ya kupikia nchini, hasa kuhamasisha wakulima wadogo wadogo kuendelea kulima michikichi na kufufua kiwanda?

(v) Chuo cha Kilimo cha Utafiti Mlingano kilikuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima wa Mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla. Chuo hiki kimesahaulika, wakulima wanapambana na magonjwa kwenye mazao mbalimbali hasa michungwa, viungo, mihogo na michikichi. Naomba

Waziri aje atuambie mpango mkakati wa Wizara katika chuo hiki hasa wataalam na vitendea kazi.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mungu kwa siku hii na nafasi ya kuchangia Wizara hii kwa maslahi ya Watanzania na wananchi wa Tanga. Katika Wilaya ya Muheza, Tarafa ya Amani kuna vivutio vizuri na vya asili vya utalii kama misitu mikubwa, maporomoko ya maji, vipepeo adimu duniani, kima na sokwe wa kipekee lakini pia katika Kata ya Magoroto kuna kivutio kikubwa cha mito na michikichi. Pamoja na vivutio vyote hivyo bado hakuna jitihada za makusudi kuvitangaza vivutio hivyo ili kuongeza watalii na pato la Taifa. Je, Wizara ina mkakati gani katika kufufua na kuvitangaza vivutio hivyo?

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Tanga na mikoa mingine ya Pwani imekuwa maarufu kwa mchezo wa bao ambao ni mchezo wa kipekee kwa jinsi unavyochezwa, na ni mchezo unaounganisha pamoja tamaduni za pwani kwa maana ya mavazi, ustaarabu wa dini hasa Waislamu. Naishauri Wizara iandae mkakati wa kuufanya mchezo huu unaoenzi tamaduni za watu wa Pwani ili uwe kivutio cha watalii wanapotembelea maeneo haya ya Pwani hasa fukwe na mapango kama ya Amboni.

Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Mamba, Jimbo la Bumbuli vipo vijiji vilivyo karibu na Mbuga ya Mkomazi ambao wamekuwa wakisumbuliwa na wahifadhi wa Mkomazi Park na wamekataliwa kufanya shughuli za maendeleo katika makazi yao ambayo wameishi kwa miaka mingi tangu mababu zao. Je, Wizara ina mkakati gani wa kumaliza tatizo hili la mipaka ili wananchi waweze kuishi kwa amani katika maeneo yao na hifadhi ziendelee kuwa na faida kwa wananchi wanaozunguka hifadhi hizo.

Mheshimiwa Spika, naomba kupatiwa ufafanuzi.
Ahsante na nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ufafanuzi na msimamo wa Serikali katika mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tanga, Wilaya ya Muheza ina upungufu wa Walimu wa shule ya msingi 487, kwani waliopo ni 846 na mahitaji ni 1,333. Je, Wizara ina mkakati gani kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Walimu hao 487 ili kujenga msingi imara wa kielimu kwa watoto wetu wa shule za msingi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa nyumba za Walimu ni mkubwa sana Wilayani Muheza, Serikali imejipangaje kuanzisha mpango mkakati wa haraka kusaidia kutatua changamoto ya makazi ya watumishi. Makazi ya askari polisi ni duni, chakavu na hayatoshi. Je, Serikali imejipangaje kutatua changamoto hiyo kubwa inayopunguza morali ya askari wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya; upungufu wa watumishi katika hospitali teule Wilayani Muheza, Serikali tunaomba mtufikirie. Katika hospitali ya Muheza (Teule) dawa ya nyoka ni 250,000 x3 na dawa ya mtu aliyeng’atwa na mbwa ni 50,000x3. Mheshimiwa Waziri, kung’atwa na mbwa na kung’atwa na nyoka ni ajali ambazo asilimia kubwa ni wananchi waishio vijijini (mashambani). Je, Serikali haioni ni wakati muafaka dawa hizi kuziingiza kwenye kundi la dawa muhimu ili wananchi wazipate bure. Serikali iliahidi katika mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga milioni 20 kwa ajili ya ambulance na mpaka sasa gari huko la wagonjwa halijafika Muheza katika Hospitali Teule. Je, ni lini tutapata gari la wagonjwa Hospitali ya Wilaya ya Muheza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utumishi; katika Wilaya ya Muheza wapo watumishi waliosimamishwa kazi na Serikali kwa sababu mbalimbali. Wapo wengi wa darasa la saba walinzi, madereva na watendaji wengine. Je, Serikali imejipangaje kuwalipa stahiki zao kwa wakati na kuwarudisha kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, posho kwa Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji kwani wanafanya kazi kubwa ya kuwahudumia wananchi lakini hawapati chochote. Je, Serikali imejipangaje kuwapa posho ili nao wapate utulivu wa kufanya kazi zao.