Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Juma Selemani Nkamia (10 total)

MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-
Je, Serikali itakamilisha lini ukarabati wa Mradi wa Maji wa Ntomoko ili kuwaondolea wananchi adha ya ukosefu wa maji kwenye vijiji vya Sambwa, Kirikima, Churuku, Jangalo, Jinjo, Hamai, Songolo na Madaha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati wa Mradi wa Maji wa Ntomoko ulianza kutekelezwa mwezi Februari, 2014 na mkataba wa kazi hii ulikuwa ni wa miezi sita. Kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha, kazi zilizopangwa kutekelezwa hazikuweza kukamilika katika kipindi cha miezi sita. Gharama ya mradi huo ni shilingi bilioni 2.87.
Utekelezaji wa mradi unaendelea na hadi sasa Mkandarasi amekwishalipwa jumla ya shilingi milioni 841.5 mwezi Agosti, 2015. Wizara ilituma shilingi milioni 600, mwezi Januari kwa ajili ya kuendelea na kazi. Aidha, Wizara itatuma shilingi milioni 728.7 mwezi Februari, 2016 na itaendelea kutuma fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi huo. Wizara imejipanga kukamilisha mradi huo mwezi Aprili, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huo utakapokamilika wananchi wa vijiji vya Makirinya, Hamai, Songolo, Kirikima, Lusangi, Madaha, Churuku, Jinjo, Kilele cha Ng‟ombe na Jangalo watanufaika na huduma ya maji.
MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kununua mashine mpya za CT-Scan kwa ajili ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na taadhima, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia, Mbunge wa Jimbo la Chemba, napenda kuwakumbusha Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla kwamba leo ni Siku ya Saratani Duniani. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Tunaweza, ninaweza kwa pamoja tuwajibike kupunguza janga la Saratani duniani”. Ili kupambana na ugonjwa wa saratani inabidi kuepuka matumizi ya tumbaku, ulaji usiofaa na utumiaji wa pombe kupita kiasi. Nawaasa mfanye mazoezi ili kuzuia kwa kiasi kikubwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefuatilia mwenendo wa huduma ya vipimo vya radiolojia inayotolewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kubaini baadhi ya upungufu. Miongoni mwa upungufu huo ni kuharibika mara kwa mara kwa CT-Scan na kupelekea usumbufu kwa baadhi ya wagonjwa kutopata huduma ya kipimo hicho kwa wakati muafaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na sababu mbalimbali, Serikali katika mwezi wa Desemba, 2015, ilifanya maamuzi na kupeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili mashine mpya ya CT-Scan ambayo inatumia teknolojia ya kisasa yenye X-ray tube mbili na uwezo wa kupiga picha ya 128 Slice mara mbili.
Faida ya mashine hii ni pamoja na kuhudumia mgonjwa kwa haraka na kutoa nafasi kwa mgonjwa mwingine hali ambayo inatoa nafasi kwa wagojwa wengi zaidi kwa maana ya zaidi ya 40 kupata kipimo hicho ndani ya siku moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida nyingine ni kwamba mgonjwa anapata mionzi michache, karibu nusu ya ile anayoweza kupata kutokana na mashine yenye tube moja. Aidha, mashine hii ina uwezo wa kuchunguza magonjwa yanayohusu moyo, mishipa ya damu, mishipa ya fahamu na ubongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ununuzi na usimikaji wa mashine hii, imefanya sasa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuwa na mashine mbili za CT-Scan. Kwa hali hiyo, hatutegemei kusimama kwa utoaji wa huduma ya vipimo vya CT-Scan. Aidha, Serikali pia imefunga X-ray mpya ya digitali na Ultra-Sound mpya ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa kuboresha huduma za vipimo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-
Wakulima wengi wa Wilaya ya Chemba wamefukuzwa katika mashamba yao Wilayani Kiteto licha ya kufuata taratibu na kudaiwa kuwa eneo hilo ni hifadhi.
Je, Serikali ipo tayari kufuta uamuzi uliotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara wa kuwazuia wakulima hawa ili kuondoa mgogoro huu wa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tamko lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara liliwahusu wakulima waliokuwa wavamizi katika eneo la Hifadhi ya Wanyamapori Makame kutoka Wilaya ya Kiteto, Babati, Chemba, Kondoa na Mkoa wa Iringa, waliokuwepo wakiendesha shughuli za kilimo katika hifadhi kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Spika, uamuzi huo ulitolewa kufuatia Azimio la kikao cha pamoja cha Kamati ya Ulinzi na Usalama za Wilaya ya Kiteto na Chemba kilichokaa tarehe 12 Novemba, 2015. Kikao hicho kiliwashirikisha viongozi wa Vijiji vitano vinavyounda Mamlaka ya Hifadhi (WMA) ambavyo ni Ngobolo, Katikati, Ndedo, Ikshubo na Makame, pamoja na wawakilishi wa wakulima 10 kutoka kila Wilaya.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria hairuhusiwi shughuli yoyote ya kibinadamu, iwe kilimo, ufugaji au makazi kuendeshwa katika hifadhi. Naomba kutoa wito kwa wananchi kuzingatia sheria za nchi ili kuepuka migogoro katika jamii. Aidha, Serikali za vijiji zinakumbushwa kusimamia vizuri sheria ya ardhi namba tano ya mwaka 1999 ambayo imeweka utaratibu wa kufuata kwa mtu atakayehitaji kupata ardhi kwa matumizi mbalimbali. Lengo ni kuzuia migogoro ya ardhi isiyokuwa ya lazima ambayo kwa sehemu kubwa inatokana na kutozingatia Sheria ya Ardhi.
MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-
Bei ya dawa za binadamu imekuwa ikipanda kila wakati na Serikali imekaa kimya wakati wananchi wake wanaumia:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha chombo maalum cha kudhibiti bei ya dawa za binadamu hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Seleman Nkamia, Mbunge wa Jimbo la Chemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli dawa za binadamu huwa zinapanda mara kwa mara kutokana na ukweli kwamba asilimia 80 ya mahitaji ya dawa yananunuliwa kutoka nje ya nchi. Pale ambapo sarafu yetu inaposhuka thamani, au sarafu ya dola inapopanda, basi bidhaa mbalimbali toka nje ya nchi zikiwemo dawa hupanda bei. Ili kudhibiti upandaji wa bei za dawa, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara na Viwanda, tunaandaa mkakati wa kuongeza uzalishaji wa dawa ndani ya nchi ili angalau kukidhi asilimia 60 ya mahitaji katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, pia inaangalia uwezekano wa kuunda chombo cha kusimamia gharama na bei zinazotozwa na vituo vya kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na bei za dawa na vifaa tiba. Vile vile bohari ya dawa imeandaa mipango ya kuanza kununua dawa moja kwa moja, toka kwa wazalishaji ili kudhibiti bei za dawa na kuongeza upatikanaji wake, kwa bei nafuu. Naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira wakati mikakati hii ya kudhibiti bei za dawa inaendelea kutekelezwa.
MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni alipotembelea Wilaya ya Chemba aliahidi kuongeza fedha za ujenzi wa Jengo la Halmashauri mpya ya Wilaya:- Je, katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga kiasi gani kuendeleza ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Seleman Nkamia, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017, Halmashauri ilitengewa jumla shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Chemba. Hadi Machi, 2017 fedha zote zimepokelewa na kazi inaendelea vizuri. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imepanga kutumia shilingi milioni 600 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi.
MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya ya Chemba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Suleimani Nkamia, Mbunge wa Chemba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali ni kusogeza huduma karibu na wananchi. Juhudi kubwa zinaendelea kufanyika kuhakikisha kuwa kila Wilaya nchini inakuwa na mahakama. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imepanga kujenga jingo la Mahakama Wilaya ya Chemba.
MHE. MOSHI S. KAKOSO (K.n.y. MHE. JUMA S. NKAMIA) aliuliza:-
Wilaya ya Chemba haina hospitali jambo linalowalazimu wananchi wake zaidi ya laki tatu kwenda kupata huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Kondoa.
Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuhakikisha Wilaya hiyo inapata hospitali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba imetenga kwa kupima eneo la ekari 23.7 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali ya Wilaya. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri imeomba maombi maalum ya shilingi bilioni mbili ili kuanza ujenzi wa hospitali hiyo. Aidha, upo mpango wa kukopa kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili kufanikisha ujenzi wa hospitali hiyo kwa awamu. Ofisi ya Rais - TAMISEMI itashirikiana na Halmashauri ya Chemba ili kuhakikisha mipango ya ujenzi wa hospitali hiyo unafanikiwa. (Makofi)
MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-
Wilaya ya Chemba haina Kituo cha Polisi; je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Polisi na nyumba za askari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Nkamia, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Jeshi la Polisi lina uhaba wa vituo vya polisi pamoja na nyumba za kuishi Askari kote nchini ikiwemo Wilaya ya Chemba. Ili kutatua changamoto hii Jeshi la Polisi linashirikisha wadau wa eneo husika pamoja na wadau wengine wa maeneo kwa maendeleo ili kufanikisha azma ya Serikali ya kujenga vituo vya kisasa vya polisi pamoja na nyumba za kuishi askari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilayani Chemba Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, wananchi na wadau wengine wapo kwenye hatua za awali za kuanza ujenzi wa kituo cha polisi. Aidha, kwa sasa mchoro wa ramani ya kituo na gharama za ujenzi (BOQ) zimeshakamilika na ukusanyaji wa mahitaji ya ujenzi unaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini jitihada hizi zitaungwa mkono na Mheshimiwa Mbunge ili kuhakikishia wananchi wake usalama wao pamoja na mali zao.
MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-
Je, ni lini barabara ya lami kutoka Handeni – Chemba - Kwamtoro hadi Puma Singida itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia, Mbunge wa Chemba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Handeni – Kiberashi - Kwamtoro – Singida yenye urefu wa kilometa 461 inayopita katika Mikoa ya Tanga, Manyara, Dodoma na Singida inaunganisha Ukanda wa Mashariki, Ukanda wa Kati na Ukanda wa Kaskazini Magharibi. Barabara hii inaunganisha mikoa ambayo mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda hadi Tanga unakopita. Mradi huu ni muhimu sana kwani utaweza kuinua uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutumia fedha za ndani tayari imekamilisha upembuzi yakinifu wa kina wa barabara hii. Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii utaanza katika mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo shilingi bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kazi ya ujenzi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta fedha za kutosha kukamilisha ujenzi wa barabara hii muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.
MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-
Shule za Sekondari za Farkwa na Msakwalo zilizoko Wilayani Chemba zimepandishwa hadhi kuwa za A – level na idadi ya wanafunzi imeongezeka katika shule hizo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuzipatia maji ya uhakika shule hizo ili kuwaondolea wanafunzi adha ya kutafuta maji badala ya masomo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia, Mbunge wa Chemba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Shule ya Sekondari Msakwalo ilikuwa ikitumia maji ya bomba kutoka katika kisima cha kijiji na Shule ya Sekondari Farkwa ilikuwa inatumia miundombinu ya kuvuna maji ya mvua na pia ilikuwa ikitumia maji ya bomba kutoka katika kisima cha kijiji. Visima hivi pamoja na uchakavu wa miundombinu havikuwa na uwezo wa kuzalisha maji ya kutosha kwa matumizi ya vijiji pamoja na shule. Hivyo, shule hizo kushindwa kupata maji ya kutosheleza kwa mwaka mzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua tatizo la maji katika Shule za Sekondari Msalikwa na Farkwa, Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018, ilitoa jumla ya shilingi milioni 104 kwa Shule ya Sekondari Msalikwa na shilingi milioni 87 kwa Shule ya Sekondari Farkwa kwa ajili ya kuchimba visima na kufanya ukarabati wa miundombinu ya mfumo wa bomba kwenye shule hizo. Kazi ya uchimbaji wa visima na ukarabati wa miundombinu ya mabomba katika shule hizo imekamilika na wanafunzi kwa sasa wanapata maji ya kutosha.