Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Juma Selemani Nkamia (29 total)

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niishukuru sana Serikali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuleta hizi fedha haraka na kujua umuhimu wa wananchi wa Chemba na Kondoa kutokana na tatizo hili la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ningeomba hizi shilingi milioni 600 anazosema Mheshimiwa Waziri, ziliingia akaunti ya DAWASCO Dodoma toka Januari mwaka jana, mpaka leo hiyo fedha haijaingia katika Halmashauri ya Kondoa. Je, yuko tayari sasa, kusukuma ili fedha hii iingie kati ya leo na kesho?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ucheleweshwaji wa miradi mingi ya maji umechangiwa sana na flow ya fedha kutoka Hazina kwenda kwenye Halmashauri. Je, Wizara sasa iko tayari kupeleka fedha hizi haraka ili miradi mingi nchini iweze kukamilika hasa hii ya maji ambayo wakandarasi wengi wameanza kutishia sasa kwenda Mahakamani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata taarifa kwamba hizo fedha zimekwama Mamlaka ya Maji Dodoma (DUWASA). Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafuatilia kuhakikisha fedha hizo zinapelekwa Kondoa, lakini ndiyo umekuwa utaratibu kwamba fedha zikitolewa kwanza zinaanzia DUWASA, baadaye ndiyo zinakwenda huko kwenye kazi.
Hoja ya pili ya Mheshimiwa Mbunge, sasa hivi tunaingia katika awamu ya pili ya programu ya maji. Miradi mingi haikukamilika kwa sababu ya matatizo ya kifedha, lakini sasa tunaanza programu ya pili na hii programu ya pili tayari tunaanza kupata pesa na Serikali itatenga fedha ili kuhakikisha miradi yote iliyokuwa inaendelea inakamilika na miradi ambayo ilikuwa haijaanza inaanza. Pia tunatarajia kuwa na miradi mipya kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuhakikisha tunapunguza hili tatizo la maji.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza kwa rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla, Naibu Waziri wa Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri wakati anajibu swali anasema, Serikali ilifanya maamuzi lakini swali langu lilikuwa Serikali ina mpango gani wa kununua mashine kwa ajili ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili? Mashine anayoizungumzia Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla ni mashine ambayo imechukuliwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Dodoma, katika Chuo Kikuu cha Dodoma, ikahamishiwa Muhimbili. Swali la kwanza, je, anaweza kukiri kwamba ni kweli hiyo mashine anayoizungumzia ni ile iliyochukuliwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa katika Chuo Kikuu cha Dodoma kupelekwa Muhimbili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Dodoma pia kuna wagonjwa. Unapohamisha mashine ya CT-Scan kutoka Dodoma kupeleka Muhimbili na unakuja hapa unasema ziko mbili sasa, unataka watu wa Dodoma wafe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSI, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, nitumie nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuonyesha mapenzi ya dhati na kuwajali watu wa Dodoma na Kanda ya Kati kwa ujumla wake kwa kujenga hospitali kubwa ya kisasa inayoitwa Benjamin Mkapa Ultra-Modern Hospital hapa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo pia nitumie nafasi hii kwa namna ya kipekee kumpongeza Rais wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa ziara ya kushtukiza aliyoifanya kwenye Hospitali yetu ya Taifa Muhimbili ambayo ilibaini upungufu mwingi wa vipimo na namna ya kuchunguza magonjwa kwenye hospitali hii kubwa ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najibu swali ya Mheshimiwa Nkamia kama ifuatavyo. Kwanza, nakiri kwamba mashine ambayo imefungwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni mashine ambayo ilikuwa ifungwe kwenye Hospitali ya Benjemin Mkapa. Kwa sababu mbalimbali za kitaalamu ndani ya Serikali, majengo ambapo ilikuwa ifungwe mashine hii kwenye Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Dodoma yalikuwa bado hayajakamilika wakati huo hospitali kubwa kabisa ya Taifa pale Muhimbili kulikuwa kuna mahitaji ya mashine kwani mashine iliyokuwepo ilikuwa imeharibika. Mheshimiwa Rais alifika pale Muhimbili akajitolea fedha na matengenezo yakaanza lakini huduma ikawa haiwezekeni kutolewa kwa kuwa mashine haikupona kwa wakati. Kwa hivyo, ndani ya Serikali tuliona ingekuwa ni vyema kwa kuwa tuna uwezo wa kununua mashine nyingine mpya na tulikuwa tayari kununua mashine mpya kwa ajili ya kufunga Muhimbili tu-switch ile ambayo imeshafika nchini ambayo ilikuwa ifungwe hapa Dodoma ifungwe sasa Muhimbili. Sasa hivi tupo kwenye mchakato wa kununua mashine mpya kwa ajili ya kuja kufunga Benjamin Mkapa na majengo ya kufunga mashine hiyo kwa sasa yanaelekea kukamilika. (Makofi)
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Nina swali moja dogo tu. Wilaya nyingi mpya za Tanzania hazina Hospitali za Wilaya ikiwemo Wilaya ya Chemba ninakotoka mimi. Je, Serikali itatuhakikishia ndani ya Bunge hili kwamba katika bajeti inayokuja wametenga fedha kujenga hospitali mpya katika Wilaya zote mpya Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, ni kweli na naifahamu Chemba, kaka yangu Mheshimiwa Nkamia tumeshaongea sana kufika Chemba pale kuangalia siyo suala zima la afya, lakini na mambo mengine. Ninavyojua ni kwamba katika bajeti ya mwaka huu ambayo tutakuja kuisoma wiki ijayo ina mikakati mbalimbali katika halmashauri mbalmbali. Halmashauri zingine wamejielekeza katika kuboresha vituo vya afya, wengine wamejielekeza katika Hospitali zetu za Wilaya, lakini wengine wamejielekeza katika Hospitali za Mkoa.
Mheshimiwa Spika, katika hili ninavyojua wazi kwamba michakato yote aidha ya ujenzi wa zahanati, Hospitali ya Wilaya au ya Mkoa, vikao husika kwanza vinaanza na mchakato huo. Imani yangu kwamba na wenzetu katika Jimbo la Chemba jambo hilo watakuwa wameliangalia kwa jicho la upana zaidi. Katika haya maana yake Serikali sasa itafanya juhudi kubwa kupeleka resources kutokana na mipango iliyopangwa kutoka katika Halmashauri ili mradi wananchi wetu waweze kupata huduma katika maeneo hayo.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali moja dogo la nyongeza. Katika usambazaji wa umeme kwenye hii REA Phase II, Makao Makuu ya Wilaya ya Chemba, umeme ule umepelekwa kwenye nyumba ya Mkuu wa Wilaya tu. Pia katika vijiji vya Gwandi, Farko na Kwamtoro ambavyo vilikuwepo kwenye programu hii havijapelekewa hata nguzo. Mheshimiwa Waziri naomba anihakikishie hapa kwamba je, mpaka kufika Juni miradi hii itakuwa imekamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa baadhi ya maeneo ambayo yamepelekewa umeme tumepeleka kwenye vituo vikubwa hatujaanza kusambaza kwenye vijiji, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Nkamia kwamba ni kweli vijiji ambavyo vimesalia kwenye ile awamu ya pili sasa hivi kazi inayofanyika ni kuvihakiki ili tubaini ni vituo gani na vijiji gani havijapata umeme kwenye REA Awamu ya Pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, azma yetu ya kwanza ni kuhakikisha kwamba vijiji vyote vilivyokuwa kwenye scope ya REA Awamu ya Pili kwanza vinakamilika ifikapo Juni mwaka huu, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kama itaoneka kwa dosari za kibinadamu vijiji vitasalia, vyote vitakavyokuwa vimebaki vitaingia kwenye REA Awamu ya Tatu pamoja na vijiji vya Mheshimiwa Nkamia.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kutuona hasa sisi watu wa huku nyuma. Mimi nina swali moja tu. Kipande cha barabara cha kilometa nane kutoka Chuo cha Mipango hadi Msalato, huu ni mwaka wa tatu hakijakamilika na wakandarasi walishaondoka eneo hilo, tunavyozungumza hivi barabara ya kutoka njiapanda ya Usandawe pale Zamahero hadi Bonga karibu inakamilika, lakini kilometa nane hizi hakuna chochote kinachoendelea.
Mheshimiwa Waziri atuhakikishie hapa wananchi wa Dodoma na Wabunge wote hapa, lini kipande hicho kitakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kipande hiki nimeshakijibu mara kama mbili na naomba niendelee kusisitiza na Waheshimiwa Wabunge mtuamini kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano inaposema kitu inamaanisha na inapoahidi itatekeleza.
Mheshimiwa Spika, nilisema kipande hiki cha kilometa nane nukta, Mkandarasi alikuwa ameondoka site kwa sababu Serikali hatukumlipa baadhi ya certificates ambazo alikuwa amezitoa na kwa sasa kutokana na makusanyo ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI aliendelea kufafanua, kwamba sasa hivi makusanyo ni mazuri na tunaelekeza katika miradi ambayo imekwama, tuondoe madeni ili wakandarasi warudi katika maeneo ambayo Wakandarasi waliondoka, moja kati ya maeneo hayo ni hilo eneo la Msalato, ili kuunganisha ile barabara ikamilike, maana yake hicho kipande cha kilometa nane nukta kidogo ndiyo kilichobakia.
Mheshimiwa Spika, naombeni sana Waheshimiwa Wabunge mtuamini na tutahakikisha huyu mkandarasi tunamfuatilia ili arudi kwa sababu yeye alikuwa na certificates nyingi ambazo hakulipwa na tumeshamlipa mpaka sasa lakini hatujamaliza zote, ni karibuni tu tunategemea kumaliza zote. Kwa kweli pamoja na kwamba hatujamaliza certificates zote, tunamtaka mkandarasi huyo arudi site, kabla hatujamalizia certificates za mwisho, akakamilishe hicho kipande kidogo kilichobakia ili tuhakikishe barabara hii inakamilika kama ilivyokusudiwa na wananchi waanze kutumia huduma kwa ustawi ule ambao ulikuwa unategemewa.

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kulikuwa na deni la mkandarasi huyo, lakini kwa ufupi mkandarasi tumeshamlipa na wakati wowote kuanzia sasa hivi mkandarasi huyo atarudi site aifanye kazi hiyo na tunaamini kazi hiyo itafanywa kwa viwango kama tulivyokubaliana.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja tu la nyongeza. Mji wa Dodoma ni Mji unaokua kwa haraka sana na leo tunategemea asilimia mia moja ya maji kutoka katika visima vilivyoko pale Mzakwe. Moja kati ya juhudi zilizokuwa zimebuniwa na Serikali ni pamoja na kutengeneza bwawa la Farkwa, ambalo litaleta maji hapa Dodoma kupeleka Bahi, Chemba na maeneo ya jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri awahakikishie Watanzania na wananchi wote wa Dodoma, kwamba ni lini mradi huu wa bwawa la Farkwa utaanza kujengwa kwa sababu sasa hivi tayari wananchi wameshaambiwa wasiendeleze nyumba zao na miradi yao mingine wakisubiri ujenzi uanze. Naomba Mheshimiwa Waziri atuhakikishie ni lini bwawa hili litaanza kujengwa na lini wananchi wataanza kulipwa fidia?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nkamia, kwanza umeuliza swali mara mbili lakini naona kama kuna maswali matatu.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, basi unisamehe tu kwa leo.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba ujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Nkamia.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba sasa hivi maji tunayoyapata tunayapata kutoka visima vya Mzakwe, lakini Serikali tayari imeishafanya upembuzi yakinifu, na usanifu wa kina kuhusiana na ujenzi wa bwawa la Farkwa. Sasa hivi Serikali inachofanya ni kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hili ili kuhakikisha kwamba Mji wa Dodoma sasa hautakuwa na matatizo ya maji. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, suala hili tunalitekeleza katika Program ya pili ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba unisamehe tu, maswali yangu yatakuwa marefu kidogo kwa mara ya kwanza katika historia yangu ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, nafahamu kabisa Mheshimiwa Naibu Waziri anachosema humu ndani ni majibu aliyoandikiwa kutoka huko huko kwenye matatizo, waliomwandikia ndiyo chanzo cha mgogoro huu. Sasa swali la kwanza; je, yuko tayari kwenda mwenyewe badala ya kusubiri majibu anayoandikiwa kutoka huko Kiteto?
Swali la pili, hivi sasa wapo wakulima kutoka Chemba, Kongwa, Kondoa na maeneo mengine ambayo wafugaji wameamua kwenda kuchunga mashamba yao wakati yakiwa na mazao shambani na hakuna chochote kinachofanywa na mamlaka ya utawala wa Kiteto. Je, kama ninyi Waheshimiwa Mawaziri mmeshindwa kutatua tatizo hili, mko tayari sasa kuturuhusu tumwombe Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli akamalize tatizo hili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini kwamba majibu haya tumeandikiwa na hao hao ambao wamesababisha mgogoro huo ni tuhuma nzito na nataka nikubaliane na ombi la Mheshimiwa Mbunge la kwenda kuuona ukweli ukoje sisi wenyewe. Kwa hiyo, tutajitahidi, tutajipanga ili tuweze kwenda. (Makofi)
Pili, ni kwamba migogoro ya ardhi nchini ya mwingiliano kati ya shughuli za kilimo na shughuli za ufugaji inachochewa sana na maendeleo, kwamba wananchi sasa kila mmoja anatafuta namna ya kupata maendeleo. Hivyo sidhani kama kuna namna ya muujiza unaoweza kufanyika kuimaliza kama tu wadau wote, Serikali, wakulima, wafugaji, hawatatumia busara na hekima zilizokuwa zinatumika na wazee wetu wa zamani wakati hakuna hata sheria nyingi kama ilivyo sasa.
Mheshimiwa Spika, kuthamini mali ya mtu mwingine ni jambo jema sana. Kinachotokea sasa hapa ni watu kuacha maadili na utaratibu wa kimila na desturi zetu. Zamani huko ilikuwa migogoro kama hii wanaimaliza kule, lakini unapokwenda kule unakuta kuna makundi na wanaochangia wengine ni sehemu ya watu wanaotakiwa kutatua migogoro hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sitaki nibishane na Mheshimiwa Mbunge hapa, ninachosema kesi zinatofautiana kati ya kesi moja na kesi nyingine, tutajaribu kwenda na tutakapokwenda tutajaribu kutatua tatizo hili kwa mazingira yake na kwa namna lilivyo.
Mheshimiwa Spika, lakini kusema ukweli, nikiri na nikubali kwamba liko tatizo kubwa na ni lazima sisi Serikali tulishughulikie na tuko tayari kufanya hivyo na nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nitakapokwenda huko nitajaribu kushughulikia tatizo hili kwa namna lilivyo, bahati nzuri nalifahamu sana.
niulize maswali mawili madogo ya nyongeza, lakini kabla ya hayo kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Afya, Dada yangu na Shemeji yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na Naibu wake, pamoja na Wizara nzima kwa hatua za haraka walizochukua baada ya ugonjwa wa hatari kuibuka kule Wilayani Chemba, kwa kweli nawashukuru sana na wanafanya kazi yao vizuri sana.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, bei ya dawa za binadamu hasa kwenye maduka ya watu binafsi imekuwa ni kubwa mno, kiasi kwamba watu wenye kipato cha chini wanashindwa kumudu gharama. Je, chombo hicho cha kudhibiti dawa kitaundwa lini?
Swali la pili, katika maduka mengi ya dawa, hasa vijijini dawa nyingi hazina ubora, lakini nyingi zinauzwa zikiwa tayari muda wake wa matumizi umekwisha na inawezekana wananchi wetu wengi wanatumia dawa hizi zikiwa tayari zime-expire. Je, Serikali hili inaliona? Kama inaliona inachukua hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru. Kwanza nimpe pole kwa kupatwa na madhila ya ungonjwa wa hatari ambao ume-claim maisha ya watu kwenye Jimbo lake, lakini Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo kama ambavyo yeye mwenyewe amesema.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni lini chombo hicho kitaanzishwa, bado tuko kwenye mchakato wa kutazama aina ya chombo ambacho tunakihitaji na namna ambavyo kitafanya kazi na pindi tutakapokamilisha utaratibu huo wa muundo wa chombo chenyewe na majukumu ya chombo hicho, kwamba yatakuwa ni yapi, ndipo tutaweza kusema ni lini chombo hicho kitaanza kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi zilizoendelea zina vyombo vya namna hiyo, kutokana na mifumo ya ku-finance mfumo wa afya kwa ujumla, zinaitwa health technology assessment na zinakuwa chini ya Wizara ya Afya, na sisi tumeona tuanzishe chombo kama hicho. Hivyo lini ni pale ambapo tutakamilisha utaratibu wa ndani wa utafiti kwamba tunahitaji chombo cha namna gani, chenye muundo upi na majukumu yapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, kwamba dawa saa nyingine zinakuwa zime-expire muda wake. Hili sidhani kama linaweza likajitokeza kwa kiasi kikubwa kwenye nchi yetu; kwa sababu Mamlaka ya Chakula na Dawa wakishirikiana na Kitengo cha Ukaguzi, kilichopo chini ya Wizara ya Afya, pia wakifanya kazi kwa ukaribu na Baraza la Madawa (Pharmacy Council) kwa ujumla wake, huwa tunafanya ukaguzi wa kushtukiza na pia tunafanya ukaguzi maalum wa Taasisi zote ambazo zinauza dawa ama zinatoa huduma za afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukaguzi ule tunaweza kubaini ni dawa kiasi gani zime-expire na nani anayeuza dawa ambazo zime-expire na huwa zinawekwa chini na zinawekwa sehemu maalum na zinakuwa labelled kwamba zime-expire. Kwa maana hiyo haziwezi kuuzwa kwa wananchi. Kwa maana nyingine ni kwamba dawa ambayo shelf life yake ime-expire haiwezi kuwepo kwenye shelf.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Shule ya Sekondari ya Kuryo, iliyoko Wilayani Chemba ina historia ndefu sana. Shule hii inamilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Chama cha Mapinduzi kupitia Jumuiya ya Wazazi kimeshindwa kuiendesha shule hii na sasa hivi imefungwa na ina miundombinu yote, je, Serikali iko tayari sasa kuichukua shule hii kutoka mikononi mwa Chama cha Mapinduzi na kuikabidhi Halmashauri ya Chemba ili iweze kufanya kazi yake vizuri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Nkamia amezungumzia Shule ya Sekondari ya Kuryo ambayo inamilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi. Kwa sababu hii ni mali ya Chama sitaki kuleta ugomvi kati ya Mheshimiwa Mbunge na Mheshimiwa Bulembo ambaye ni Mwenyekiti wa Wazazi Taifa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najua lengo kubwa la Mheshimiwa Mbunge ni vijana wale waende shule wakapate elimu kwa sababu majengo yapo na yana miundombinu mizuri. Mimi nimshauri Mheshimiwa Nkamia kwa sababu katika ahadi yetu tulipanga twende Chemba, siku tukienda Chemba, hata wiki ijayo, tufike angalau tukaione shule hiyo, tufanye ushawishi na Jumuiya ya Wazazi ili shule hii iweze kutumika na hivyo iwasaidie vijana wa Chemba kupata elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wazo la Mheshimiwa Mbunge ni zuri nadhani linataka consultation meeting kati ya watu wa Chemba na Jumuiya ya Wazazi. Kwa sababu Ilani ya Chama cha Mapinduzi ina lengo la kuhakikisha vijana wanapata elimu nadhani jambo hili litafikia mahali pazuri katika kuhakikisha vijana wa Chemba wanapata elimu.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Serikali imetoa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kukamilisha Mradi wa Maji wa Ntomoko ambao chanzo chake kipo Wilaya ya Kondoa kwa ajili ya vijiji vya Wilaya ya chemba, na Wilaya ya Kondoa. Mradi huu haujakamilika hadi sasa na tumeambiwa kwamba vijiji viwili, kijiji cha Jangalo na Madaha hawatapata maji, licha ya kwamba fedha hizi zilitolewa ili na wao wapate maji kwenye mradi huu.
Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuongozana kwenda kukutana na Mkurugenzi wa Kondoa na Chemba ili tufanye makubaliano sasa pesa zile zilizokuwa zikamilishe mradi huu zisogezwe ili tuchimbe visima walau viwili kwa ajili ya Jangalo na Madaha
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba ni kweli tumekuwa na huu mradi wa Ntomoko ambao ulilenga kwenda mbali. Lakini baada ya kufanya utafiti zaidi, tumegundua kwamba chanzo cha maji katika hili eneo hakiwezi kutosheleza vijiji ambavyo tulikuwa tumevilenga. Kwa hiyo kwa sasa pesa tuliyotoa itakamilisha huo mradi ili kuhakikisha vijiji viwili vimepata maji. Vijiji vingine vilivyobaki itabidi tufanye utaratibu wa kuchimba visima, kuhakikisha kwamba wananchi hao wamepata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi la kuongozana naye, ni sawa ngoja tumalize Bunge, lakini kikubwa ni kwamba tuhakikishe maji yanapatikana na kwamba Wizara ina taarifa na hata katika maandiko yetu tumeandika hivyo, kwamba maji yaliyopo Ntomoko yatatosheleza vijiji viwili tu, hivyo vijiji vingine vilivyobaki vinafanyiwa utaratibu mwingine.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naitwa Nkamia, ahsante. Najua umenikosea kwa sababu leo niko tofauti kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri nina swali moja tu la nyongeza. Wala sina tatizo lolote na Wakuu wa Wilaya, lakini kama Serikali Kuu inashindwa kumhudumia Mkuu wa Wilaya, anakwenda kuomba Halmashauri ambayo inaongozwa na Mkurugenzi, hiyo checks and balances inatoka wapi? Haoni kwamba Wakuu wengi wa Wilaya watakuwa ni ombaomba sasa kwa sababu OC wanazopata ni kidogo na matokeo yake wanaishi kwa kutegemea fadhila za Wakurugenzi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kumekuwa kuna maelezo kwa baadhi ya maeneo kwamba Wakuu wa Wilaya wanawaomba mafuta Wakurugenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi formally yaani kupata taarifa rasmi kwa maana ya kwamba hilo linatokea na kwamba limekubalika, kweli jambo hilo halipo. Kwa hiyo, kama linatokea pengine ni kwa kesi fulani fulani tu, lakini kusema ukweli kwanza hatulikubali na haliruhusiwi kwa mujibu wa sheria. Pia kama linafanyika, linakiuka sheria. Kwa hiyo, niseme tu, siwezi kuridhia udhaifu huu mpaka tufanye utafiti tujue kweli hili jambo linatokea? Kama linatokea, nini tufanye kwa kuzingatia hili linalosemwa na Mheshimiwa Mbunge?
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani jambo hili siyo maeneo yote tuka-generalise kwamba sehemu zote inatokea, siyo kweli. Pia kama linatokea, linakiuka taratibu, kanuni na sheria za mgawanyo wa madaraka na majukumu na the principle of checks and balances.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa suala la usalama ni jambo la msingi sana kwa raia wa Tanzania, kumekuwa na matukio mengi sana ya watu kupigwa na wengine kuuawa katika mpaka wa Kiteto na Chemba. Polisi wa eneo hili hasa wale wa Wilaya ya Chemba walioko Mrijo wanashindwa kufuatilia matukio haya kutokana na ukosefu wa vifaa ikiwemo magari, wengi wanaazima pikipiki na wakati mwingine baiskeli. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba vifaa vinapatikana katika maeneo ambayo kuna matatizo kama haya ili kunusuru wananchi na mali zao?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Nkamia kwa kulisema jambo hili na niwahakikishie tu wananchi wa Chemba kwamba Mheshimiwa Nkamia amekuwa akifuatilia sana suala hili. Ameshakuja mara kadhaa ofisini na mimi nimemuahidi kwamba tutakapopata magari kwa ajili ya Wilaya mpya na Wilaya Chemba tutaipa kipaumbele zikiwepo na Wilaya nyingine kama Mkalama ambapo Mheshimiwa Allan Kiula naye amekuwa akisumbua mara kwa mara. (Makofi)
Kwa hiyo, napenda kumwambia Mheshimiwa Nkamia suala la magari pamoja na nyumba za askari katika Wilaya yake mpya tutalipa kipaumbele kwa kutambua mazingira tete ya eneo hilo ambapo pana changamoto za kugombania matumizi ya ardhi ambayo yanahitaji sana askari kuwepo katika maeneo hayo. Nitoe rai kwa wananchi wa maeneo husika watoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi punde mtu mmoja anapokuwa amekiuka sheria katika maeneo husika ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Maswali mengi kuhusu hizi milioni 50 tunaulizwa sisi Wabunge kwenye majimbo yetu. Wakati mwingine tunashindwa kutoa majawabu sahihi kwa sababu Serikali haijatoa taarifa rasmi kuhusu utoaji wa hizi shilingi milioni 50. Je, Mheshimiwa Waziri Serikali iko tayari sasa kwenda front na kutangaza kwamba wananchi wasubiri mpaka Baraza la Mawaziri likae ili liweze kutoa utaratibu wa kutoa hizi fedha ili sisi Wabunge tusipate wakati mgumu tunapokuwa Majimboni mwetu kuulizwa suala la shilingi milioni 50?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ambayo ndio iliwaahidi Watanzania kwamba itatoa shilingi milioni 50 katika kila kijiji, inatakiwa itekelezeke, ninaomba niwahakikishie Watanzania Serikali hii kwanza imeshatenga hiyo bajeti, pili Serikali hii imeshaona umuhimu wa kuanza haraka utekelezaji wa jambo hili, tatu Serikali hii ili kuhakikisha fedha hizo zinawafikia wanyonge sasa imeanza kuweka mfumo mzuri wa kuratibu zoezi hili na mara tu utakapokamilika Serikali hii itawaambia Watanzania ni mfumo gani utakaotumika. Na kwa sababu fedha zimetengwa katika bajeti ya mwaka huu, fedha hizo tutaanza kuzitoa katika mfumo rasmi utakaowafikia wanyonge ili kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja tu dogo la nyongeza. Katika mwaka huu wa fedha kuna baadhi ya vijiji katika Wilaya ya Chemba vimeorodheshwa kwamba vitapata umeme. Nataka Mheshimiwa Waziri na Serikali nzima hii inihakikishie mradi huu utaanza kutekelezwa lini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yote niliyotaja ya REA awamu ya tatu inaanza kutekelezwa tarehe 15 Desemba, mwaka huu na itakamilika 2019. Kwa hiyo, eneo la Chemba Mheshimiwa Nkamia nimhakikishie vijiji vyake vyote, shule zake zote, pamoja na vituo vya maji vitapatiwa umeme kuanzia mwezi niliotaja na kuishia 2019.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya viongozi katika ngazi za Wilaya, hasa ma-DC na ma-DAS, wengi wao wamekuwa wababe na wamekuwa wakitumia madaraka yao kuwanyanyasa wananchi kwa kisingizio eti wao ni Marais wa Wilaya. Wakati nafahamu katika uchaguzi uliopita tumemchagua Rais mmoja tu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi)
Je, Serikali haioni hili linaweza kuwa ni tatizo kubwa sana? Na inawezekana kama tutaendelea bila kufanya utafiti wa kutosha na kuwachunguza watu hawa wanaweza kuharibu hata imani ya wananchi kwa Chama cha Mapinduzi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kama nilivyosema muda mfupi uliopita kwamba hawa ni binadamu na ni Watanzania wenzetu. Na kutokana na kazi na nature ya kazi wanazozifanya inawezekana mahali fulani kukatokea mikwaruzano, lakini tatizo la mtu mmoja haliwezi kuwa la watu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wanafanya kazi nzuri sana. Wanatusaidia maana wao ndio wasimamizi kwa niaba ya Serikali katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa jana lilitokea swali ambalo lilikuwa linataka kufahamu kofia au nafasi ya Mkuu wa Mkoa. Mkuu wa Mkoa ana kofia mbili, ana kofia ambazo zinashuka kwa Rais zile mbele, Head of Executive and Head of State. The President is Head of State and at the same time Head of Executive. Wakuu wa Mikoa wanashukiwa na zile kofia mbili na ndio maana wanalindwa na bunduki kati ya saba mpaka kumi na moja na askari saba hadi kumi na moja. Na ni haki yao wao kulindwa kwa sababu wanafanya maamuzi mazito, wanaweza wakaingilia jambo ambalo haliendi sawa kwa sababu ndio wawakilishi wa Serikali katika maeneo yao. Na kwa hiyo lazima vyombo vya ulinzi na usalama viwalinde kwa sababu ya nature ya kazi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuwaomba sana Waheshimiwa Wabunge ni suala la mawasiliano, sio na ninyi tena kutunishiana ubabe kule. Kinachowezekana kutokea kule sasa ikiwa hivyo itaonekana nani ni nani. Lakini kama tukiletewa, inapotokea upungufu tunaweza tukashughulikia administratively tu na jambo likaenda vizuri, kama nilivyosema hawa nao ni binadamu. Kwa hiyo, pale ambapo tunapata fursa tumekuwa tukitoa maelekezo kwao na tumekuwa tukitoa hata kwa maelekezo ya maandishi na wala semina sio jambo la msingi sana. Lakini kubwa hapa ni maelekezo na mtu kujua wajibu wake.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika,
nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuuliza swali moja tu la nyongeza. Tatizo la Hifadhi ya Ngorongoro linafanana sana na lile tatizo la Hifadhi ya Swagaswaga ambalo linaunganisha Wilaya za Kondoa na Chemba. Kumekuwa
na matatizo watu wengi wamezuiwa kulima na
nilishakwenda mimi na Mheshimiwa Naibu Waziri katika eneo hilo na akatoa maagizo kwamba, ufanyike utaratibu wa kuweka mipaka upya, lakini jambo hili halijafanyika hadi sasa. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuweka mipaka ili
wananchi wa Lahoda, Kisande, Iyoli pamoja na Handa waweze kuondokana na tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Ni kweli nilifanya ziara katika eneo hili ambalo linahusika na hifadhi yetu ya Swagaswaga na niliambata na Mheshimiwa Mbunge na ni kweli niliacha maagizo kama anavyosema. Pia siyo tu agizo, tuliendelea na utaratibu ule wa kuunda kikosi kazi ambacho kilihusisha Wizara nne na ambacho kimekuwa kikiendelea na kazi yake
kwa muda wa miezi michache iliyopita. Sasa hivi kamati ile imeshaandaa mapendekezo ya awali ambayo yamekabidhiwa tayari kwa Kamati ya Makatibu Wakuu, baada ya pale yanaenda kukabidhiwa kwa Baraza la Mawaziri, baadaye kwenye ngazi za juu, ili tuweze kupata
mwelekeo zaidi wa kwamba nini kifanyike ili kuweza kukamilisha utaratibu wa kuweka mipaka.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa maana ya maeneo yale ambayo hayana migogoro kabisa, suala la uwekaji wa mipaka limekuwa likiendelea na hifadhi kadhaa tayari zimeshakamilisha utaratibu huo. Mheshimiwa Mbunge akiniona baada ya hapa tutaweza kuangalia kwenye orodha kama eneo lake limepangiwa lini kukamilisha utaratibu wa
kuweza kuweka mipaka.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imekuwa ikipeleka fedha kidogo kidogo kwenye Halmashauri hizi ambazo ni mpya. Je, haioni kwamba sasa hakuna sababu ya kuanzisha maeneo mapya ya utawala kabla ya kumaliza maeneo ambayo tayari yameshaanzishwa na uendeshaji wake unasuasua?
Swali la pili, kuendesha Halmashauri ni gharama
kubwa; kunahitaji huduma za afya, miundombinu na
vinginevyo. Je, Serikali iko tayari sasa kuongeza bajeti kwenye
Halmashauri mpya zote nchini ili kuziondoa kabisa katika hali
ambayo sio nzuri sana kwa sasa na kuacha kabisa zoezi la
kuanzisha maeneo mapya ya utawala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, concern ya Mheshimiwa Juma Suleiman Nkamia tumeipata lakini nikujua uanzishwaji wa Halmashauri hizi mara nyingi sana unaanzia humu Bungeni. Hapa nimekuwa nikijibu maswali kadhaa kwa baadhi ya Wabunge na hasa Malocha anaeniangalia kwa jicho la karibu sana hapa; kila Mbunge kutokana na jiografia jinsi ilivyo anapenda Halmashauri yake iweze kugawanywa au kwa mfano Halmashauri ya Sikonge kule
nilikofika ina square kilometa karibuni 27,000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ukiangalia kweli kuna maeneo mengine ni kweli kulikuwa kuna haja ya kugawanya lakini vilevile na suala la kuhudumia hizi Halmashauri imekuwa ni changamoto kubwa. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tutaangalia kwa kina jinsi gani tutafanya; lengo
kubwa ni wananchi waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili jinsi gani hizi Halmashauri ziweze kuongezewa mgao wa fedha. Naomba niseme jambo hili kwamba, kama Serikali tunalichukua ndio maana hata ukiangalia suala la bajeti kidogo linaongezeka.
Changamoto kubwa ni kutokana na mapato yetu
tunayoyapata kama Serikali kwa ujumla. Kikubwa zaidi naomba kuzihamasisha Halmashauri sasa ziweze kuweka mipango mizuri ya jinsi gani itakusanya mapato yake ya ndani kwa sababu mpaka leo hii ukija kuangalia Halmashauri
mbalimbali hata ile bajeti tuliyoitengea mwaka huu zimesua sua katika ukusanyaji wa mapato. Kwa hiyo, naomba nizihamasishe Halmashauri zihakikishe japokuwa tunazigawanya, lakini lazima commitment ya kukusanya mapato iwe ni kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini concern yake
Mheshimiwa Nkamia naomba tuipokee kama Serikali, kama ni ushauri mpana ili Serikali yetu iweze kwenda vizuri.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja dogo la nyongeza. Gereza la Kondoa linahudumia Wilaya ya Chemba na Wilaya ya Kondoa. Gereza hili limejengwa mwaka 1919, lina hali mbaya sana.
Je, Serikali haioni ipo haja sasa pengine hata Waziri aende tu aone pale kama kweli hawa wafungwa bado ni binadamu, lakini wanaishi kwenye mazingira mabaya sana. Askari wana hali mbaya sana, hata Mkuu wa Gereza anatembea na boda boda. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari hata kwenda tu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na mwaliko wa Mheshimiwa Juma Nkamia na mara kwa mara amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada na mahitaji yanayotakiwa katika Wizara ya Mambo ya Ndani ikiwepo nyumba za Polisi, nyumba za Askari Magereza, Zimamoto pamoja na Uhamiaji. Kwa hiyo, sina tatizo na kwenda Wilayani kwake pamoja na Wilaya jirani ya kondoa ili kuweza kujiridhisha na mazingira hayo ili kuweza kuweka utekelezaji mzuri zaidi wa ujenzi wa gereza ili wafungwa pamoja na askari waweze kufanya kazi katika mazingira ya usalama zaidi. Nitafanya hivyo baada ya bajeti yetu kuwa imepita.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Mradi wa Ntomoko ambao ulipangwa kuhudumia Wilaya za Kondoa na Chemba unaonekana dhahiri ni kama umechezewa. Je, Serikali iko tayari sasa kupokea ushauri wangu kwanza kusimamisha malipo ya mkandarasi aliyekuwepo na ifanye ukaguzi wa kutosha kwa sababu mradi huu ni kama hauna manufaa yoyote kwa wananchi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kwamba tayari nimesimamisha malipo, hakuna malipo mengine yatakayolipwa katika mradi wa Ntomoko na mkandarasi alikuwa anadai shilingi milioni 700, nimesimamisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili tumefanya kikao cha pamoja kati ya TAMISEMI, Wizara ya Maji na Mamlaka ya Maji ya Dodoma wanapitia usanifu kwa muda wa mwezi mmoja na nimekabidhi huo mradi baada ya hapo utatekelezwa na Mamlaka ya Maji ya Dodoma yaani DUWASA. Kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge ni kwamba ule mradi umechezewa, hatua nyingine zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria kwa wale wote ambao wamechezea huo mradi.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri na ya uhakika ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Nilikuwa na swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya Chemba ni moja kati ya Wilaya kubwa sana katika Mkoa huu wa Dodoma na pengine kwa Tanzania kwa ujumla. Je, Serikali wakati inasubiri kujenga jengo la Mahakama katika Makao Makuuya Wilaya iko tayari sasa kuimarisha mahakama za Mrijo na kwa Mtoro ili kupunguza adha inayowafanya wananchi kutembea zaidi ya kilometa 170 kufuata huduma za mahakama Wilayani Kondoa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli anachokisema Mheshimiwa Mbunge kwamba Wilaya ya Chemba ni kubwa sana, na kwa sababu mahakama hii ya wilaya itaanza kujengwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019 niseme tu kwamba nimepokea ombi na mawazo ya Mheshimiwa Mbunge na sisi kama Serikali tutaona namna bora ya kuweza kuimarisha huduma katika maeneo ya Mrijo ili wananchi wasipate shida kutembea umbali mrefu kwa sababu alipokusema huko Mheshimiwa Nkamia ni mbali sana mpaka kufika katika makao makuu ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kama Serikali katika mpango wetu wa kuhakikisha kwamba tunasogeza huduma hizi kwa wananchi tutahakikisha pia tunalifanyia kazi jambo hilo la kuboresha huduma za mahakama katika maeneo hayo ili wakati tunaendelea kujipanga katika ujenzi wa Mahakama ya Wilaya wananchi waendelee kupata huduma katika maeneo ya Mrijo na maeneo mengineyo. (Makofi)
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nipate kuuliza swali dogo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliahidi ndani ya Bunge kwamba ingeweza kumaliza migogoro ya wananchi na mapori ya hifadhi mwezi Desemba mwaka jana. Moja kati ya maeneo ambayo yanakabiliwa na mgogoro mkubwa sana ni pamoja na eneo la Swagaswaga katika Wilaya ya Chemba ambako wananchi wamekuwa wakifukuzana na askari wanyamapori kila siku.
Ningeomba kauli ya Serikali, pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri anajiandaa kwenda Urambo, hapa Chemba ni karibu sana, yuko tayari kwenda Chemba pale kabla ya kwenda Urambo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu katika Pori letu la Swagaswaga na ninaomba nimjibu tu kwamba hivi sasa ninavyoongea, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii leo hii ameenda kutembelea hilo pori pamoja na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango kwa ajili ya kuangalia huo mgogoro ili waweze kulitatua hili tatizo ambalo limedumu kwa muda mrefu.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nipate kuuliza swali moja dogo tu la nyongeza.
Nheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaipongeza Serikali kwa kutoa shilingi bilioni mbili kwa ajili ya mradi wa maji wa Ntomoko kule Kondoa na Chemba.
Swali langu ni kwamba pamoja na Serikali kutoa fedha hizi mradi ule umehujumiwa Serikali inajua na wananchi wa Kondoa na Chemba wanajua na waliohujumu mradi huu wamehamishwa kutoka Halmashauri ya Kondoa kwenda Halmashauri nyingine. Nilitaka kujua ni nini kauli ya Serikali kuhusu hali hii? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli zipo dalili za ule mradi kuhujumiwa kutokana na utekelezaji kuchukua muda mrefu, lakini tumeamua kuchukua hatua mbili kwa sababu wananchi wa Kondoa/wananchi wa lile eneo wanahitaji maji tumechukua hatua mbili. Sasa hivi utekelezaji wa ule mradi tumeukabidhi kwa Mamlaka ya Maji Dodoma (DUWASA) wakati wowote tunatangaza tender.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuhakikisha kwamba sasa hawa wananchi wanapata huduma ya maji, ndiyo tunarudi nyuma kuangalia ni watu gani waliotufikisha hapa, kwa hiyo, stahiki zao zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria na Mheshimiwa Nkamia hata kama wamehamishwa hawajapelekwa nje ya nchi wako Tanzania hapa, kama mtu atabainika kwamba alihujumu atafuatwa, atakwenda kuchomolewa aliko ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa. (Makofi)
MHE. JUMA S NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri anasema Jeshi la Polisi likishirikiana na wadau Wilayani Chemba wamekaribia kuanza ujenzi ningeomba anihakikishie ni wadau gani hawa ambayo yeye ana taarifa kwamba tayari wanaanza kushirikiana kujenga kituo cha polisi?
• Binafsi nimechangia kwa kiwango kikubwa sana katika ujenzi wa kituo kipya cha Polisi kule Kwa Mtoro na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani Komredi Mwigulu alinihaidi hapa ndani ya Bunge kwamba kutokana na mazingira ya Kwa Mtoro hadi Makao Makuu ya Wilaya ya Chemba ambao ni karibu kilometa zaidi ya 120 Serikali ingeweza kuwapatia askari wale gari la kuweza kuwasaidia kwa sababu wanapita kwenye Hifadhi ya Swagaswaga na kuna wanyama wakali. Je, hilo gali litapatikana lini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi nilieleza kwamba Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ikishirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo wananchi wameanza mchakato wa ujenzi wa kituo hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na swali lake la pili kwanza nimpongeze kwa juhudi zake za kuchangia maendeleo ya Jeshi la Polisi katika Wilaya yake, lakini kuhusiana na hali ya Mheshimiwa Waziri nataka nimhakikishie kwamba ahadi ya Mheshimiwa Waziri kama alitoa iko palepale tatizo linalokwamisha ni kwamba bado magari hayo hayajapatikana, naamini kabisa wakati ambapo tumepata magari ya kutosha basi ahadi hiyo itatekelezwa.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa maeneo ambayo barabara hii inapita sasa hivi ni miaka mitatu walishawekewa alama za X na hawajaambiwa nini kinaendelea kwa sababu wameshindwa kuendeleza hata maeneo yao. Naomba kauli ya Serikali, Mheshimiwa Waziri anaposema hapa mbele ya Bunge kwamba imetengwa shilingi bilioni moja sina uhakika kama amesoma vizuri hapo au amekosea? Nini kauli ya Serikali kuhusu wananchi hawa wa maeneo haya ambao wamewekewa alama za X?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu alama hizi za barabarani ni muhimu sana zinavyowekwa kwa sababu alama hizi zinaleta mawasiliano, zinawajulisha wananchi kwa ujumla kwamba eneo hili litakuwa na mradi wa barabara. Kwa hiyo, tahadhari hii inasaidia kwenye mipango yetu ya wananchi na upande wa Serikali kwa ujumla ili wananchi hawa wasije wakaweka vitu vya thamani kama sheria inavyotaka. Kwa hiyo, niseme tu kwamba alama ni muhimu zinavyokuwepo zinatuweka kwenye alert ili tuweze kujua kwamba kuna mradi mkubwa wa maendeleo unakuja.
Mheshimiwa Spika, nini kauli ya Serikali, niseme kwamba ujenzi wa barabara hii umeshaanza. Nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Chemba na Watanzania kwa ujumla, barabara hii tumeiainisha kati ya barabara ambazo zipo kwenye integration ya East Africa (mtandao wa barabara za Afrika Mashariki). Kwa hiyo, kuiweka katika mtandao wa barabara za Afrika Mashariki kunaonesha namna gani barabara hii tumeipa kipaumbele cha hali ya juu katika kuitafutia fedha.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaambie tu wananchi kwamba alama hizi zimewekwa kwa ajili ya kuwatahadharisha wasiweke vitu vya thamani kubwa wakati tunafanya maandalizi ya kulipa compensation (fidia). Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, ni mpango wa Serikali. Mimi niseme tu ukweli kwamba ujenzi wa barabara hii umeshaanza kwa sababu ujenzi tunaanza katika hatua tofauti; unaanza kwanza usanifu, michoro halafu sasa tunatafuta fedha na tumeuza mradi huu kwa wafadhili wanaofadhili Afrika Mashariki. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge uvute subira, mambo mazuri yanakuja. (Makofi)
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali moja tu la nyongeza; Makao Makuu ya Shirika la Reli Tanzania pale Dar es Salaam hasa Ofisi ambako wanachapisha tiketi za Nchi nzima jengo lile lipo kwenye hali mabaya mno.
Je, Serikali haioni kwamba upo umuhimu sasa wa kulikarabati jengo lile ili wafanyakazi wanaofanyakazi mle ndani na wao wajione ni sehemu ya matunda ya Taifa hili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba jengo la Makao Makuu wa Shirika la Reli Tanzania pale Dar es Salaam linahitaji ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge siyo jengo lile tu peke yake, ni majengo mengi sana ya vituo vya Mikoa ambayo kwa kweli hali zake ziyo nzuri na kupitia Shirika la Reli Tanzania tumekwishatoa maelekezo kama Serikali wapitie maeneo yote yale na sasa hivi kuna timu ya wataalam ambao wanapitia kila eneo la majengo ya reli na kuhakikisha kwamba wanaleta gharama nzima pamoja na vile vituo ambavyo vinaitwa gangs na vyenyewe viweze kurekebishwa ili viendane na wakati na wafanyakazi wafanye kazi katika mazingira mazuri.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Chemba kwenye Kata za Kidoka, Jangalo na Msaada pamoja na maeneo ya vijiji vyake, kumekuwa na nyaya za umeme kwa muda mrefu lakini tatizo lililopo sasa ni kuwasha tu. Je, Serikali inanipa majibu gani ya uhakika kwamba ni lini maeneo haya yatapelekewa transfoma ili kuwasha umeme katika maeneo hayo?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Nkamia anavyofuatilia masuala ya umeme katika Jimbo lake la Chemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpe taarifa Mheshimiwa Nkamia, nivyoongea hivi sasa transfoma tatu zinakwenda katika Kijiji cha Kidoka kwa ajili ya kuwasha umeme, lakini kesho pia wataendelea kupeleka nguzo pamoja na transfoma na nyaya katika Kijiji cha Msaada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Jangalo, namwomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane baada ya vijiji hivi kuwashwa tutaendelea na Kijiji hicho. Wakati kazi hizo zinavyoendelea kule Kwa Mtoro nimhakikishie Mheshimwa Mbunge yapo magenge sita yanafanya kazi hivi sasa ili na yenyewe kabla ya mwisho wa mwezi wa kumi iweze kuwashiwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Nkamia anavyoshirikiana na Serikali. Ahsante.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona, naomba niulize swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Balozi wa Namibia alifanya ziara katika Tarafa ya Kwamtoro na kukutana na Wazee wa Kabila la Kisandawe. Moja kati ya maelezo yake ni kwamba lugha wanayoongea Wasandawe inafanana na lugha wanayoongea watu wa Kusini mwa Namibia halikadhalika na watu wa kabila la Xhosa kule Afrika ya Kusini. Alisema yuko tayari kuwachukua Wazee wa Kisandawe kwenda kule Namibia kwa ajili ya kutambuana na ndugu zao. Je, Serikali haioni kwamba upo umuhimu sasa wa kuangalia baadhi ya makabila ya Tanzania na makabila mengine Afrika ili kujenga mahusiano?
NAIBU WAZIRI HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Nkamia, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mkamia Serikali inaona kwamba kuna umuhimu mkubwa kwa sababu tunatambua kwamba lugha zote ambazo zipo hususani lugha za Kiafrika ni lugha za Kibantu ambazo zina mwingiliano mkubwa sana. kwa hiyo, sisi kama Serikali tunatambua kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa kuangalia hizi lugha ambazo zipo katika nchi yetu ya Tanzania namna ambavyo zinahusiana na lugha zingine ambazo zipo kwenye nchi zingine. Kwa hiyo, niseme kwamba wazo lake ni zuri na sisi kama Wizara tumelipokea na tunaahidi kwamba tutalifanyia kazi. Ahsante.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali, nina swali moja tu la nyongeza. Kwanza nitumie fursa hii kumpongeza sana Waziri wa Elimu, Profesa Ndalichako, Naibu wake na watendaji wote wa Wizara kwa juhudi walizochukua za kuhakikisha kwamba shule hizi za Msakwalo na Farkwa zinapata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni moja tu kwamba katika Shule za Sekondari za Mondo na Soya ambazo nazo ni shule za A-Level zilizopo katika Wilaya ya Chemba, wanafunzi wanatembea umbali mrefu kutafuta maji. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba wanafunzi na walimu wa shule hizi wanapata maji ya uhakika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, kaka yangu Mheshimiwa Kakunda kwa majibu mazuri, lakini sisi Wizara ya Maji tunatambua umuhimu wa elimu. Kupitia elimu mtoto wa mama ntilie anaweza kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sisi kama Wizara ya Maji katika bajeti hii tumewatengea Chemba Sh.1,468,000,000. Labda nimuagize Mhandisi wa Maji wa Chemba aone umuhimu sasa kwa shule ambazo ameziorodhesha Mheshimiwa Mbunge wa kuhakikisha wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Pori la Hifadhi ya Swagaswaga ambalo lipo karibu na Dodoma lina wanyama wengi na kwa kuwa Dodoma sasa ni Makao Makuu ya nchi. Je, Wizara haioni sasa ipo haja ya kuliimarisha pori hili ili liwe sehemu ya kivutio kikubwa cha utalii kwa wageni wanaokuja katika Mkoa wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juma Nkamia...(Kicheko) Kama ifuatavyo; samahani nimekosea jina lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba pori hili la Swagaswaga ni pori muhimu sana katika Mkoa huu wa Dodoma na hasa kwa kuzingatia kwamba sasa hizi hapa imekuwa ni Makao Makuu ya nchi. Kwa hiyo, tutachukua hatua mbalimbali za kuimarisha ili iwe ni kivutio cha utalii katika hili eneo na kuliwekea mikakati ya kutosha kusudi wananchi wengi ambao wanaishi katika Jiji hili la Dodoma waweze kutembelea katika hili eneo. Nikuhakikishie, kesho nitaenda kutembelea lile Pori la Mkungunero. Nikipata muda Jumapili nitapitia kwenye hilo eneo lingine ili tuone ni mikakati gani inaweza kufanyika tuweze kuimarisha utalii katika hili eneo.