Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Zainabu Mussa Bakar (1 total)

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa mtu husajili namba kwa mujibu wa mahitaji yake na mahali alipo akiwa ni Tanzania Bara au Tanzania Zanzibar. Je, haiwezekani usajili huo kwa kuzingatia sayansi na teknolojia kuratibiwa pamoja?
Swali la pili, je, ni kitu gani kinachozuia mtu anayesajili namba zake Zanzibar kuweza kutumia namba hizo hizo akiwa Tanzania Bara kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi sheria hii siyo sheria ya Muungano na ndicho kitu kinachozuia namba za Tanzania Bara kutumika Tanzania Zanzibar na Tanzania Zanzibar kutumika Tanzania Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili tumeliona kama Serikali na Kamati kikao cha pamoja kinachoshughulikia kero za Muungano kimeliona na kikao cha mwisho kimefanyika tarehe 13 Januari, 2017 chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais na kimetoa maelekezo kushughulikia kero zote za Muungano ikiwa ni pamoja na hii ya usajili wa magari. Hivyo, kwa Serikali yetu tumeliona na tunaona kwa sababu tumepewa maelekezo Mawaziri wa pande zote mbili, Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Waziri wa Fedha wa Tanzania pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, tutakaa pamoja kuhakikisha kero hii inaondoka, lakini kwa mujibu wa sheria itakapokuwa tayari sheria hii italetwa ndani ya Bunge lako Tukufu ili kama Bunge lako litaridhia, tuweze kubadilisha utaratibu huo.