Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Halima Ali Mohammed (5 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nakushukuru kwa kunipa nafasi hii kwa mara ya kwanza kabisa kusimama katika Bunge lako hili Tukufu. Namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na utukufu kwa kunijalia afya njema. Nakishukuru Chama changu, Chama cha Wananchi (CUF) kwa kuniamini, nami nitajitahidi kuwatendea haki wananchi wote kwa kuwawakilisha vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusu afya. Suala la afya ni suala ambalo halina mjadala. Ni suala ambalo ni muhimu kwa maisha ya binadamu! Bila ya Afya, hakuna maendeleo. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, amezungumzia kuhusu idadi ya vituo vya huduma ya afya na vilevile akaelezea azma ya Serikali ya kuweza kuendeleza vituo vya afya katika ngazi ya kata, ngazi ya kijiji na ngazi ya halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kuna manung’uniko makubwa sana katika huduma ya afya; kuna matatizo lukuki katika huduma za afya katika zahanati zetu. Sasa hivi zahanati zetu ni kama madarasa matupu pamoja na mizani ya kupimia watoto. Kuna changamoto chungu nzima! Zahanati zetu hazina nyumba za madaktari, hakuna vifaa tiba, hakuna dawa, hata wafanyakazi hawatoshelezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoboresha huduma za afya, basi umewasaidia wanawake na umewasaidia wananchi wote. Naishauri Serikali iboreshe miundombinu katika huduma za afya, lakini vilevile Serikali iongeze bajeti katika Wizara ya Afya na kuwe na ukaguzi wa zahanati zetu, vituo vya afya na hospitali zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba nizungumzie kuhusu suala zima la fungu la UKIMWI. UKIMWI bado upo katika nchi yetu lakini vilevile ni tatizo na ni janga kubwa sana katika nchi yetu. UKIMWI unamaliza nguvukazi ya nchi yetu na ukitilia maanani zaidi wanaoathirika ni akina mama kwa sababu ndio wanaopata maambukizi kwa sababu ya maumbile yao na kama katika familia kuna wagonjwa, basi wanawake ndio wanaohusika katika kuhudumia wagonjwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa ruhusa yako nitoe takwimu za maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI kwa baadhi ya Mikoa iliyopo Tanzania Bara. Kwa mfano, Mkoa wa Njombe una asilimia 18.8, Mkoa wa Iringa una asilimia 9.1, Mkoa wa Mbeya una 9%, Mkoa wa Rukwa una asilimia 7.2 na Mkoa wa Shinyanga una asilimia 7.4. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonyesha kwamba ni asilimia 40 ya wananchi wetu bado hawana taarifa kuhusu ugonjwa wa UKIMWI. Ni jambo la kusikitisha sana katika bajeti yetu hii yote hakuna fungu ambalo limetengwa kwa ajili ya wagonjwa wa UKIMWI. Tunategemea wafadhili ambao hawana uhakika! Tunategemea wafadhili ambao wana interests zao! Kwa hiyo, naishauri Serikali itenge fungu la mapato ya ndani kwa ajili ya ugonjwa huu wa UKIMWI, ugonjwa ambao ni hatari na ni tishio katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka nizungumzie kuhusiana na suala la 10% ya mapato ya Halmashauri zetu kutengewa makundi haya mawili ya wanawake na vijana. Hili ni agizo na wala siyo hiari Halmashauri kama wakipenda watenge na wasipopenda wasitenge. Hili ni agizo, lazima litekelezwe lakini kwa bahati mbaya agizo hili halitekelezwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali itengeneze sheria ambayo itatia nguvu ili Halmashauri ambazo hazikutekeleza, basi ziweze kuwajibishwa. Vilevile nataka nisisitize kwamba katika fungu hili la 10% za wanawake, hizi ni pesa za walipa kodi wa nchi hii, kwa hiyo basi, ni budi fedha hizi zigawiwe bila itikadi za vyama. Wananchi wote ni sawa, kwa hiyo, wana haki sawa mbele ya sheria katika nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu miradi ya TASAF III. Mradi huu Serikali ilikuwa ina nia safi tu ya kusaidia kaya ambazo ni masikini, angalau basi na wao waweze kupata fedha kidogo ya kuweza kununulia angalau sare za shule za watoto wao pamoja na kudiriki kuwapeleka watoto hawa wachanga clinic. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu unatumika kinyume na utaratibu. Kuna baadhi ya viongozi wanatumia fedha hizi kwa ajili ya kuboresha au kujijenga kisiasa. Hili ni kosa mbele ya sheria, lakini vilevile kuna tatizo kule kwetu upande wa Zanzibar. Upande wa Zanzibar Masheha wanatumika vibaya katika mifuko hii ya TASAF; wamepewa uwezo wa kuingiza majina wanayoyataka na yale wasiyoyataka wanayafuta. Wanakiuka, maana yake Masheha kule kwetu wana uwezo zaidi kuliko CMC ambao ndio wahusika wa huu mfuko. Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo, naomba hilo ulichukulie kwa uzito wake uweze kulifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nilikuwa napendekeza kwamba posho ile ya shilingi 10,000/= ambayo wanalipwa wale vijana ambao wanasimamia ugawaji wa hizi fedha ambao ni CMC, haitoshelezi. Kwa hiyo, waangaliwe kwa jicho la huruma ili waweze kuongezewa kidogo, kwa sababu dhamana waliyonayo ni kubwa ya kusimamia fedha zile kuanzia Benki mpaka kuzigawa na wanapokosea mahesabu, basi wanafunguliwa kesi. Kwahiyo, ni vyema basi na wao wakaangaliwa kwa jicho la huruma ili wasiweze kufanya yale mambo ya kufanya wizi katika mfuko huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni dhahiri kwamba kipimo cha mtu yeyote kinapimwa kutokana na makazi yake anayoishi na hatopimwa kwa mlo wake kwani hii inakuwa ni siri yake mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu usajili wa hati na nyaraka za kisheria; kumekuwepo na malalamiko makubwa ya kukatisha tamaa kuhusiana na urasimu katika Halmashauri zetu hususani katika Mji Mkuu kama vile Dar es Salaam. Tatizo la njoo kesho, njoo kesho kutwa linakatisha tamaa kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fikiria kwanza mtu atakwenda Halmashauri kufuatilia kiwanja chake anatumia zaidi ya saa sita linatafutwa faili halionekani, kwa siku ile anakosa kazi nyingine kutafuta riziki ya chakula. Siku nyingine akienda atapewa ahadi ya kuwa anatakiwa afike mwezi ujao, mwezi ukiisha ataambiwa kila kiwanja kimeongezeka ukubwa unatakiwa ulipe fedha ya ziada ili utengenezewe hati au sehemu ile iko katika shamba la mzungu! Mheshimiwa Waziri nina ushahidi naomba Serikali iwaangalie sana watendaji ambao wanataka kukwamisha juhudi za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upangaji wa makazi ya vijiji. Mheshimiwa Waziri hili ni jambo zuri la mradi huu wa MKURABITA lakini bado jamii/wananchi hawajaelimishwa kuhusiana na jambo hili. Hivyo MKURABITA watoe elimu ya kutosha hasa kwa akina mama ambao bado wanatawaliwa na mila na desturi potofu zinazowagandamiza wanawake. Kwa mfano, katika makabila mengine wanawake hawawezi kuongea mbele ya wanaume na wala hawawezi kujiamulia kitu chochote wala kumiliki mali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali itilie mkazo MKURABITA watoe elimu stahiki kuhusiana na malengo yao. Hatimiliki ziwe na hadhi ya kuwafanya waweze kukopa katika mabenki kama zilivyo hati nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wafikiriwe kupunguziwa bei ya ardhi kulingana na vipato vyao, kwani wanawake ndiyo maskini wa mwisho, wanawake wana watoto na wao ndiyo walezi wa watoto hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu udalali wa Maafisa Ardhi hili ni tatizo, ukitaka kiwanja maeneo ya mji ukifuata utaratibu wa kisheria huwezi kupata kiwanja, utaandika barua ya maombi lakini kupata kiwanja haiwezekani ila ununue barua kutoka kwa Maafisa wa Ardhi ndiyo uweze kuendelea na utaratibu. Serikali iangalie suala hili ili kuweza kuwafanya Watanzania wawe na imani na Serikali yao. Naomba kuwasilisha.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote nichukue nafasi hii nimshukuru Mwenyenzi Mungu mwingi wa rehema na utukufu kwa kutujalia afya njema. Ninakushukuru wewe kwa kunipatia nafasi hii ili na mimi niweze kutoa mchango wangu katika mada iliyoko mbele yetu. Namwomba Mwenyenzi Mungu amjalie maisha marefu Katibu Mkuu wa Chama cha CUF Maalim Seif Sharif Hamad ili aweze kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuzungumzia kuhusu hoja ya haki za watoto. Tanzania tumekuwa tukiridhia mikataba mbalimbali inayohusiana na haki za watoto, kama Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1989, vilevile kuna Mkataba wa Haki za Mtoto wa Afrika ambao umeridhiwa mwaka 1979, lakini Tanzania tuna sheria inayomlenga mtoto wa Tanzania sheria hii imepitishwa katika mwaka 2009.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekusudiaKuna watoto wengi wa Kitanzania watoto hawa aidha baba ama mama wamehukumiwa jela kifungo cha muda mrefu ama wazazi hawa wako rumande kwa muda mrefu. Sasa watoto hawa wanakosa haki zao za msingi kwa mujibu wa sheria ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuangalia sheria, sheria hii imekaa kimya kuhusiana na mtoto ambaye mzazi wake mmoja ma wote wawili wako gerezani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wetu wanasoma, watoto wetu tunawatibia vizuri, watoto wetu wanacheza wanafurahi lakini watoto wa Watanzania hawa wanakosa haki zao za msingi. Sasa nilikuwa naiuliza Serikali je, imefanya utafiti kwa kiasi gani kuhakikisha kwamba watoto hawa wa Kitanzania nao wanapatiwa haki zao za msingi kwa mujibu wa Katiba? (Makofi)

Je, kwa sasa Serikali watakubaliana na mimi ili watoto hawa waweze kupatiwa haki zao za msingi kwa mujibu wa sheria za nchi hii? Hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naomba nizungumzie suala la uzazi salama. Uzazi salama umeshazungumziwa hapa kwa Wabunge waliotangulia na mimi nazungumzia, nawaomba na Wabunge wengine walizungumzie suala la uzazi salama. Takwimu zinaonyesha wanawake wengi wanapoteza maisha wakati wakitimiza jukumu lao la kuleta watoto duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu za hivi karibu ni kwamba wazazi 30 wanapoteza maisha kila siku. Sasa idadi hii ni idadi kubwa na inawezekana kwamba idadi hii ni wale ambao wanajifungulia sehemu husika ambao ni zahanati, vituo vya afya na hospitali. Lakini kuna idadi kubwa ambayo wanajifungulia vijiji, huko ambako wanakosa huduma halisia. (Makofi)

Kwa hiyo, napendekeza kwa Serikali yenye kusikia kwamba bajeti basi ya Wizara ya Afya iweze kuongezwa kwa maksudi ili kuokoa vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 37, aya ya 65 inazungumzia kuhusu Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Ninaishauri Serikali kwanza, iongoze bajeti ya Wizara hii ya Elimu ili wanafunzi wengi waweze kunufaika na mikopo hiyo na pili, kwa kuwa takwimu zinaonesha ufaulu wa wasichana katika elimu ya juu ni mdogo ukilinganisha na wavulana, basi naishauri Serikali hawa wasichana waliojitahidi kufanikiwa wapewe mikopo kwa asilimia 100 ili iwe ni motisha kwa wengine wajitahidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madeni ya walimu, elimu ni walimu, chonga mzinga ule asali. Walimu wasikilizwe vilio vyao ikiwepo mishahara, kupandishwa madaraja pamoja na posho za wale wanaofanya kazi katika mazingira magumu. Jambo hili ni kero ya muda mrefu na linapunguza ari ya kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la shule za bweni, uzoefu unaonesha wanafunzi wa shule za bweni ni dhahiri wanakuwa na mazingira rafiki ya kuwawezesha watoto wetu kutumia muda mwingi kujisomea kuliko wale wa day ambao huondoka nyumbani alfajiri na kurejea usiku. Jambo hili si tu linawasababishia uchovu na kushindwa kujisomea, lakini pia kwa wasichana usalama wao ni mdogo wanapokuwa njiani. Naiomba Serikali iwaangalie wasichana wetu kwa jicho la karibu kwa kuwajengea shule za bweni za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miundombinu ya shule zetu; miundombinu ya shule zetu nyingi si rafiki kwa wasichana wetu kuhusiana na matundu ya vyoo ambavyo vitakuwa havina maji ya uhakika, haviwezi kuwa ni msaada kwa watoto wa kike wakati wa hedhi zao. Nusu ya watoto wa kike waliopo shuleni wanakabiliwa na changamoto ya kupata maambukizi ya UTI. Magonjwa haya ni hatari kwani yana tabia ya kujirejea lakini pia kupata magonjwa ya figo ambayo ni hatari zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali ifanye utafiti kuhusiana na magonjwa ya UTI. Halmashauri zijiwekee malengo mahsusi ya kujenga matundu ya vyoo na maji ya uhakika. Shule zisipewe vibali vya kufunguliwa kwanza bila ya kuwepo mfumo mzuri wa maji ya uhakika, viongozi husika wakishindwa kulisimamia hilo, basi wawajibishwe kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iangalie uwezekano wa uwepo wa nesi mwanamke katika shule za msingi angalau mara mbili kwa wiki ili wasichana wawe na fursa ya kupeleka malalamiko yao yanayohusu afya zao, lakini pia wapate ushauri unaohusu mabadiliko ya maumbile yao na nini wafanye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu malezi; wazazi tuna wajibu wa kwanza wa kulea watoto wetu kimaadili kabla ya muda wa kwenda shule. Kambale mkunje angali mbichi, ukichelea mwana kulia mwisho utalia mwenyewe, inawezekana, timiza wajibu wako kwa faida ya Taifa. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa 33 aya 46 Mheshimiwa Waziri ameelezea kuhusiana na SUMA JKT kupitia kampuni yake ya SUMA JKT Guard Ltd. kuendesha shughuli za ulinzi katika Ofisi za Serikali, Mashirika ya Umma na sekta binafsi zikiwemo Benki na Migodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walinzi hawa maisha yao ni magumu, posho ni ndogo sana, mishahara hawana na Serikali iliwaahidi itawapatia mishahara kamili kama askari wengine. Nitoe mfano, walinzi wanaoimarisha ulinzi Ofisi ya TRA Bandarini, kazi wanayofanya ni nzuri tena katika ofisi nyeti, lakini Serikali haijali kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iangalie upya maslahi ya walinzi hawa, iwaboreshee mishahara, iwapatie vitendea kazi pamoja na stahiki nyingine, kwani sehemu ya bandari ni muhimu katika kuingiza mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu malipo ya wastaafu wa JWTZ. Hawa ni watumishi ambao walifanya kazi kubwa ya kulinda nchi yetu, kuweka heshima, lakini pia kuimarisha ujirani mwema. Siyo vyema kuwa sasa hivi wao ni ombaomba. Nashauri wapewe stahiki zao kwa kuzingatia thamani ya shilingi ya Kitanzania kwa sasa au mnawasubiri wafe wote? Hilo siyo jambo zuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako wananchi eneo la Kengeja, Jimbo la Mtambile, Wilaya ya Kusini Pemba ambao ardhi yao imechukuliwa na JWTZ. Hadi hii leo ni kimya, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na ni maeneo ambayo wanayategemea kwa kilimo cha chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali uthamini ufanyike kwa haraka. Mheshimiwa Waziri atoe kauli ni lini wananchi hawa watapatiwa haki zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya majeshi ya JWTZ wakati wa uchaguzi kwa mfano, uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani - Zanzibar ni uthibitisho kuwa na matumizi mabaya ya Jeshi letu, matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi, lakini siyo hivyo tu, ni uminyaji wa demokrasia, kwani walikuwa wakipita njiani na silaha. Hii inawatisha wananchi na matokeo yake wapo wananchi wengi tu ambao waliogopa na hawakujitokeza kutimiza haki yao ya kupiga kura. Hii ni aibu kwa nchi inayojigamba kama ina demokrasia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri, Serikali isitumie madaraka vibaya, badala yake wanajeshi wa JWTZ waachiwe wafanye majukumu yao kwa mujibu wa sheria za nchi yetu kwa manufaa ya ustawi wa nchi yetu na wanasiasa wafanye siasa. Kutumia fedha za walipakodi kwa jambo ambalo halina msingi, ni kuwanyima wananchi kutumia haki yao ya maamuzi na kuwanyima nafasi ya kupata maendeleo. Ahsante sana.