Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Halima Ali Mohammed (7 total)

MHE. HALIMA ALI MOHAMMED aliuliza:-
Takwimu zinaonyesha kuwa kuna kasi kubwa ya ongezeko la wagonjwa wa maradhi ya moyo, kisukari na vidonda vya tumbo (ulcers):-
Je, Serikali ina mkakati gani kukabiliana na tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima Ali Mohammed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania imeshuhudia kasi kubwa ya ongezeko la magonjwa ya moyo, magonjwa ya kisukari na magonjwa ya vidonga vya tumbo, ambayo ni magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Hii imechangiwa na mabadiliko ya mfumo wa maisha kama ulaji usiyo sahihi, kutokufanya mazoezi, kutokula matunda na mboga mboga kwa wingi, uvutaji wa sigara na tumbaku na unywaji wa pombe uliyokithiri. Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo ya utafiti wa STEPS uliyofanyika mwaka 2012 yalionesha kuongezeka kwa viashiria yaani indicators vinavyosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Aidha, utafiti pia ulionesha karibu asilimia 9 ya Watanzania, wanaugua ugonjwa wa kisukari na wengi wao kwa bahati mbaya hawajijui. Kwa kutambua ongezeko hili Wizara yetu imeanzisha sehemu ya kushughulikia huduma ya magonjwa haya yaani kitengo cha Non Communicable Diseases, Mental Health and Substance Abuse chini ya Kurugenzi ya Tiba pale Wizarani. Miongozo na mikakati mbalimbali imekwisha kutengezezwa ikiwa ni pamoja na mkakati wa Kitaifa wa kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yaani magonjwa ya kisukari, moyo na mengineyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu kwa jamii ni kubadili mtindo wa maisha yaani life style kwa kula vyakula vinavyofaa, kupunguza unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara na tumbaku na kuwa na tabia ya kufanya mazoezi ili kuepuka uwezekano wa kupata maradhi haya.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED aliuliza:-
Je, Serikali imefanikiwa kwa kiasi gani kuimarisha majengo na vituo vya Polisi sanjari na kulipa madeni ya Wakandarasi waliojenga majengo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Ali Mohammed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uchakavu na uhaba wa majengo ya ofisi za Polisi pamoja na nyumba za makazi kwa Askari. Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kukarabati ofisi na vituo vya Polisi na kujenga nyumba za kuishi Askari. Mathalani, mwaka 2012 Serikali ilijenga maghorofa 15, katika maeneo ya Buyekela Mkoa wa Kagera, matatu yenye uwezo wa kuchukua familia 12. Mkoa wa Mwanza Mabatini sita yenye uwezo wa uchukua familia 24 na Mkoa wa Mara Musoma sita yenye uwezo wa kuchukua familia 24.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiwalipa Wakandarasi wa miradi ya ujenzi wa ofisi na makazi ya Askari kwa awamu kadri ya upatikanaji wa fedha za maendeleo. Mathalani katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 Serikali imetenga kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni tano kwa ajili ya maendeleo.
MHE. ANNA R. LUPEMBE (K.n.y. MHE. HALIMA ALI MOHAMED) aliuliza:-
Serikali imedhamiria kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga wakati wa kujifungua:-
Je, Serikali ina mikakati gani kufanikisha dhamira hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima Ali Mohamed, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imedhamiria kupunguza vifo vya wanawake wajawazito, pamoja na watoto wachanga kwa kuweka mipango na mikakati mbalimbali ikiwemo; kwanza, kupandisha hadhi Vituo vya Afya na kuviwezesha kufanya huduma za upasuaji wa dharura wa kutoa mtoto karibu zaidi na wananchi. Hadi sasa vituo 189 vimeshakamilika na vinafanya kazi hiyo.
Pili, kuanzisha Benki ya Damu kwa kila Mkoa ili kuimarisha upatikanaji wa damu; tatu, kugawa kwa wajawazito vifaa muhimu vinavyotumika wakati wa kujifungua; nne, kutoa kutoa huduma majumbani kwa wajawazito hadi wiki sita baada ya kujifungua; na watoto chini ya miaka mitano kwa kuwatumia Wahudumu wa Afya katika Jamii; na tano, kuendelea kutekeleza Sera ya Afya ya kutoa huduma bila malipo kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, lengo likiwa kuhakikisha kwamba makundi haya maalumu yanapata huduma muda wote bila kuchelewa. Ili kuhakikisha kwamba haya yanatekelezwa, Serikali kwa kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto, imeandaa mpango mkakati wa mwaka 2016 hadi 2020, wenye mikakati ifuatayo:-
(1) Kuboresha huduma zinazotolewa kwa wanawake wajawazito na watoto wachanga, ikiwa ni pamoja na kuwapatia watoa huduma ya afya elimu kazini, kuongeza dawa, vifaa tiba na vitendea kazi;
(2) Kutoa elimu kwa jamii na hasa vijana kuhusu afya ya uzazi, pamoja na kutilia mkazo juu ya lishe bora;
(3) Kushirikisha jamii katika mambo yanayohusu afya ya uzazi, ikiwa ni pamoja na kuwahimiza wanawake wajawazito wajifungulie katika vituo vya kutolea huduma ya afya; na
(4) Kushirikisha wadau mbalimbali na kufanya kazi kwa pamoja, kwa kutekeleza afua zenye matokeo makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutekeleza haya, tunaamini kwamba vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga vitaendelea kushuka kwa kasi siku hata siku.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA (K.n.y. MHE. HALIMA ALI MOHAMMED) aliuliza:-
Serikali imejipanga kupiga vita suala la ajira kwa watoto na imekuwa ikiunga mkono matamko ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na ajira za watoto.
Je, kupitia Mradi wa TASAF III Serikali ina mikakati gani ya makusudi kuwasaidia watoto na tatizo la ajira za utotoni kwa upande wa Zanzibar?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Ali Mohamed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini au TASAF III ulianza utekelezaji wake mwezi Agosti mwaka 2012. Hadi kufikia mwezi Machi, 2016, mpango umeandikisha jumla ya kaya milioni 1.1 Tanzania Bara na Zanzibar. Kati ya hizo, kaya 33,532 zimeandikishwa na zinapata ruzuku ya malipo kwa upande wa Tanzania Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji, mpango unatilia mkazo uhawilishaji wa fedha kwa kaya maskini zilizoandikishwa. Uhawilishaji wa fedha umeziwezesha kaya hizi maskini kuwa na uhakika wa chakula, kupata huduma za afya na kuwawezesha watoto walio na umri wa kwenda shule kuanza shule na kwa walio katika shule za msingi na sekondari kupata mahitaji muhimu ya shule. Aidha, kaya hizi zinapata kipato cha ziada kupitia ajira za muda kwa wanakaya wenye uwezo wa kufanya kazi kwa kufanya kazi kwenye miradi midogo-midogo inayotekelezwa na TASAF.
Mheshimiwa Naibu Spika, uhawilishaji wa fedha kwa kaya maskini umewezesha watoto waliokuwa katika ajira za utotoni katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuongeza kipato cha kaya kutoka katika ajira hizo na kuweza kuhudhuria shule kwa kiwango cha 80% au zaidi. Kwa wale ambao hawajafikia umri wa kwenda shule waliweza kupata huduma za afya kwa kufuata taratibu za sekta husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu uliowekwa unashirikisha viongozi wa maeneo ya utekelezaji katika ngazi zote kufuatilia mahudhurio ya watoto shuleni ili waweze kufikia viwango vilivyowekwa. Kwa kaya ambazo watoto wao hawafikishi idadi ya siku zilizopangwa za kwenda shule hupunguziwa ruzuku kama njia ya kuwahimiza kutimiza masharti ya kuhakikisha kwamba watoto wao wanahudhuria shuleni ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni mategemeo ya Serikali kwamba Waheshimiwa Wabunge watashirikiana na viongozi wa Serikali katika ngazi zote ili kufanikisha mpango huu kwa kuhakikisha kwamba watoto walio na umri wa kwenda shule wanaotoka katika kaya maskini wanaandikishwa na kutimiza masharti ya Mpango kwa kuhudhuria shule kama inavyotakiwa.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED aliuliza:-
Wasichana wanaohitimu kidato cha sita wanakuwa na ufaulu mzuri lakini wanapojiunga na vyuo vya elimu ya juu ufaulu wao huanza kushuka hadi wengine hufikia kusimamishwa masomo kwa sababu ya ufaulu hafifu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wasichana katika elimu yao ya juu ili ufaulu wao uweze kuongezeka na kufikia malengo yao?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Ali Mohammed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufaulu wa wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu wa jinsi zote kwa kiasi kikubwa hutegemea juhudi binafsi katika kuzingatia masomo kwa kadri ya maelekezo ya uhadhiri wao. Hata hivyo, mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wa kike kwa baadhi ya vyuo vikuu yana changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa hostel na hivyo kusababisha wanafunzi hao kupanga nyumba za kuishi mitaani na hivyo kutumia muda mwingi katika kutafuta usafiri na mahitaji yao muhimu ya kujikimu. Hali kadhalika, katika mazingira kama hayo, kwa namna moja au nyingine baadhi ya wasichana hujiingiza katika vitendo vinavyoweza kuchangia kushuka kwa ufaulu wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo, Serikali imekuwa ikifanya jitihada za makusudi katika kuweka mazingira stahiki kwa wanachuo zikiwemo ujenzi wa hostel katika vyuo vikuu ambazo umuhimu wa pekee unatolewa kwa wanafunzi wa kike na watu wenye ulemavu.
Kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali imetoa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa hostel zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na utaratibu huo wa kuongeza mabweni utaendelea pia katika vyuo vingine.
Aidha, katika vyuo vikuu vya umma na binafsi kunatolewa huduma za ushauri na unasihi Dawati la Jinsia na Dawati la Malalamiko kwa nia ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kuathiri ufaulu wa wanafunzi wa kike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kuwashauri wanafunzi wa kike kuzingatia masomo kwa umakini wa hali ya juu na kujiepusha na vitendo ambavyo vinaweza kusababisha ufaulu duni na hivyo kushindwa kufikia malengo waliyojiwekea.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED aliuliza:-
Kwa mujibu wa Ibara ya 19(1) ya Katiba ya nchi, kila
mtu anayo haki na uhuru wa kuamini dini aitakayo, lakini pia chini ya Ibara ya 15(1) na (2) ya Katiba ni lazima sheria zifuatwe.
Je, ni kwa nini wanawake wa kiislamu wanapovaa hijabu nikabu wanavuliwa na Maafisa Usalama wanaume?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Ali Mohammed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kweli kuwa wanawake
wa kiislaamu wanapovaa hijabu na ama nikabu wanavuliwa na maafisa wanaume wa Jeshi la Polisi. Aidha, Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazoliongoza Jeshi hilo na kwa mujibu wa PGO 103(1) ambayo inasema malalamiko yote dhidi ya Polisi lazima taarifa itolewe mara moja kwa Mkuu wa eneo na hatua za uchunguzi upelelezi ifanyike kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaombe wananchi hususani wanawake, pindi wanapofanyiwa vitendo kama hivyo, kupeleka malalamiko yao polisi au kwenye mamlaka nyingine husika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED aliuliza:-
Tanzania ina dhamira ya kuwa nchi ya uchumi wa kati kwa kujikita katika uchumi wa viwanda; na viwanda vinategemea sana ukuaji wa sekta ya kilimo kwa ajili ya kupata malighafi.
Je, Serikali imewekeza kiasi gani cha fedha kwa ajili ya utafiti wa kilimo (agricultural research) ili kufanya tafiti za kilimo kubaini changamoto zinazodumaza kilimo nchini na kutoa ushauri kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji wa kilimo na hivyo kukuza sekta ya viwanda?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima Ali Mohammed, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa kilimo hapa nchini una lengo kuu la kugundua mahitaji halisi ya mkulima na walengwa wengine. Utafiti wa kilimo hufanywa kupitia vituo 16 vya utafiti vya umma vilivyopo katika kanda mbalimbali na taasisi za utafiti binafsi kama vile Taasisi ya Kahawa (TaCRI), Chai (TRIT) na Tumbaku (TORITA). Serikali imeanza kuboresha mfumo wa utafiti wa kilimo kufuatia kuanzishwa kwa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tanzania Agricultural Research Institute
– TARI) ili kuboresha zaidi uzalishaji wa mazao. Taasisi hii ndiyo itakayosimamia na kuratibu utafiti wa kilimo hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuwekeza katika utafiti kwa kuendeleza rasilimali watu na miundombinu ya utafiti. Idadi watafiti walioajiriwa ni takribani 360 na kati yao asilimia 16 wana kiwango cha elimu cha Shahada ya Uzamivu (Ph.D). Vilevile Serikali imeboresha maabara kuu nne za udongo katika Vyuo vya Utafiti vya Mlingano, Seliani, Uyole na Ukiriguru kwa kuzinunulia vifaa vya kisasa vya kutathmini virutubisho vya udongo/mradi wa kupima rutuba ya udongo na kuchora ramani yenye thamani ya takribani kuthamini ya takribani shilingi bilioni 1.8. Mradi huu utasaidia wakulima na wawekezaji katika sekta ya kilimo kufahamu viwango stahiki vya mbolea na mazao yanayostahili kulimwa katika eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hutenga takribani shilingi bilioni tatu kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo. Pia vituo hufanya shughuli za itafiti kwa kushirikiana na taasisi za kitaifa na kimataifa. Ni matarajio yetu kuwa mahusiano haya yataboreka zaidi baada ya TARI kuanzishwa rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, utafiti ni mojawapo ya vipaumbele katika Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II). Chini ya programu hiyo uzalishaji na usambazaji wa teknolojia za kilimo utaboreshwa zaidi kwa kuendeleza miundombinu ya utafiti na rasilimali watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka mitano ijayo utafiti utalenga zaidi katika utatuzi wa changamoto zilizokabili mazao yenye tija na yenye kipaumbele kitaifa ili kutekelezwa azma ya kufikia uchumi wa viwanda. Shughuli za utafiti zitakazowekewa mkazo ni pamoja na ugunduzi wa mbegu bora, uzalishaji na upatikanaji wake, magonjwa na wadudu waharibifu, matumizi sahihi ya mbolea, udongo na maji, lishe bora, uhifadhi wa mazao na uongezaji wa thamani ya mazao ili kufikia kilimo chenye tija na cha kibiashara. Jumla ya shilingi 164,532,000,000 zinatarajiwa kuwekezwa katika shughuli za kilimo wa mazao, mifugo na uvuvi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.