Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Halima Ali Mohammed (12 total)

MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa ya Naibu Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tafiti zinaonyesha kwamba wanawake wanaathirika zaidi na maradhi ya moyo kuliko wanaume.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wanawake hawa ambao ndiyo walezi wa familia hasa wale waliopo kule vijijini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti uingizwaji wa vyakula vibovu ambavyo havina kiwango katika nchi yetu? Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Swali la kwanza Serikali ina mkakati gani wa kupunguza kiasi cha magonjwa haya kwa wanawake ambao wanaathirika zaidi kuliko wanaume.
Mheshimiwa Naibu Spika, tofauti ya upatikanaji wa magonjwa haya, kwa jinsia kwa maana ya baina ya wanawake na wanaume ni ndogo sana na kwa maana hiyo, mkakati wa kupambana na kuenea kwa magonjwa haya hauwezi kutofautishwa kwa jinsia. Hivyo mkakati wetu utakuwa ni wa pamoja na tayari Wizara ya Afya imeanza kutekeleza mkakati huo, kwanza kwa kutia umuhimu wa kipekee kwenye kuimarisha Kitengo cha NCD yaani Kitengo cha Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza pale Wizarani chini ya Kurugenzi ya Tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitengo hiki tayari kimeishaaza mkakati wa kuandika mkakati wa kupambana na magonjwa haya na mkakati huu utawafikia hao akinamama wa vijijini na watu wote kwa ujumla wake kuanzia ngazi ya huduma za afya kule vijijini, kwa maana ya ngazi ya zahanati, ngazi ya vituo vya afya na ngazi ya hospitali za Wilaya, Mikoa na hata ngazi ya Kanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kweli kumekuwa na hisia kwamba kuna vyakula visivyo na viwango vinaingia nchini mwetu kutoka nchi za mbali. Serikali kwa kushirikiana kwa maana ya Wizara yetu Wizara ya Afya, ambayo ina kitengo cha TFDA (Tanzania Food and Drugs Authority) ambacho kipo chini ya Wizara yetu ya Afya, pamoja na Kitengo cha Viwango (TBS), wanaendelea kushirikiana kwa pamoja, kukagua mizigo yote ambayo inaingia nchini kwa njia za halali.
Lakini pia vyombo vingine vya kusimamia Sheria kama Majeshi ya Polisi na Uhamiaji, wataendelea kuwa makini kwenye mipaka yetu yote, katika njia zilizo halali na hata zile ambazo siyo halali kudhibiti uingizwaji wa vifaa hivi ikiwemo vyakula na dawa ambavyo havijapitishwa kwa viwango vinavyostahili, kwa mujibu wa Sheria za nchi yetu. (Makofi)
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza:
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa yupo Mkandarasi ambaye amejenga makao Makuu ya Polisi Kusini Pemba pamoja na nyumba ya RPC kwa asilimia 100, vile vile amejenga Kituo cha Polisi cha Mkokotoni kwa asilimia 70, je, ni lini Serikali itamlipa Mkandarasi huyo?
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wakandarasi wako kibiashara zaidi na kwa kuwa muda aliojenga Mkandarasi huyu ni mrefu, je, sasa Serikali iko tayari kumlipa kwa thamani ya shilingi iliyoko sokoni sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyozungumza katika jibu langu la msingi ni kwamba, kila mwaka tunatenga bajeti kwa ajili ya maendeleo na katika fedha hizo, ndipo tunatumia sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya kuwalipa Wakandarasi na Mkandarasi ambaye amejenga kituo cha Tumbatu na kituo hicho ambacho umekizungumza kilichopo Kusini Pemba ni miongoni mwa Wakandarasi mbalimbali ambao wanatudai, tutakuwa tukiwalipa. Mwaka huu katika Wakandarasi ambao tumepanga kuwalipa kiasi kitakachoweza kulipwa ni huyo ambaye amemzungumza Mheshimiwa Mbunge.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Ni lini Serikali italeta marekebisho yaliyoahidiwa na Mheshimiwa Mwakyembe wakati wa bajeti yake ili kuzuia ndoa za watoto wa shule?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nayaunganisha yote mawili kwenye jibu langu hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza mchakato wa white paper toka mwaka 2008 na lengo likiwa ni kutafuta namna ya kuwashirikisha wananchi kwa ujumla wao kwenye kufanya maamuzi juu ya suala hili ambalo limegubikwa na misingi ya dini, lakini pia limegubikwa na misingi ya mila zetu kwenye makabila mbalimbali hapa nchini. Kwa maana hiyo, suala hili Serikali imeonelea isilichukue kwa haraka haraka na ndiyo maana ikaanzisha mchakato wa white paper.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa bahati mbaya mwaka 2010 Mheshimiwa Rais, niseme kwa bahati nzuri pia, aliamua kuanzisha mchakato wa Mabadiliko ya Katiba na ndani yake akidhani kwamba, ile Tume itakapokuwa inakusanya maoni ingewezekana kupata maoni ambayo yangehusisha nia ya wananchi ya kutaka kufanya mabadiliko kwenye sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Ndoa na Sheria ya Mirathi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya baada ya mchakato ule kukamilika, maoni yanayohusiana na suala hili hayakuonekana kama ni miongoni mwa mambo ambayo yalipendekezwa na wananchi. Hivyo, sasa hivi Serikali kupitia Wizara ya Sheria na Katiba imeamua kuanza upya jitihada za kuipeleka mbele white paper ili kupata maoni ya wananchi na hatimaye tuweze kuchukua maamuzi kama Serikali.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwa kuwa kuna malalamiko makubwa yanayohusiana na kubainika kwamba kuna rushwa ya ngono katika vyuo vyetu, jambo ambalo linapelekea wasichana wengi kupata ufaulu mdogo, lakini vilevile wasichana wengine kutoroka shule, lakini kama haitoshi kuna wasichana ambao wamefanya maamuzi ya kujiua na ushahidi upo. Sasa je, Serikali ina mkakati gani wa kufanya utafiti ni kiasi gani wasichana wameathirika na rushwa ya ngono?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wasichana wetu wanapatiwa elimu kuhusiana na rushwa ya ngono?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli taarifa hizo za rushwa za ngono zimekuwa zikisikika na hata hivi karibuni ilijitokeza taarifa ya aina hiyo kwa mwalimu mmoja ambaye ameendelea kuchukuliwa hatua na niseme tu kwamba suala la kufanya utafiti ni suala jema, mimi nichukulie kwamba ntalichukua ili kujifunza tatizo hilo kwa undani zaidi. Lakini niwaombe pia wanafunzi wa kike kutoa ushirikiano, lakini pia hata wanafunzi wa kiume wanaweza kusaidia kutoa ushirikiano kwa mambo ambayo yanajitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili katika suala la elimu, sisi wenyewe tumekuwa tukiongea na wanafunzi kupitia wakati tofauti tofauti tunapowatembelea, lakini pia nafahamu kuna taasisi mbalimbali zinazoshughulika na masuala ya kijinsia zimekuwa zikiendelea kuelimisha. Niwaombe pia hata Waheshimiwa Wabunge mnapopata nafasi muweze pia kuongea na wasichana hao ili kuweza kusaidiana kwa pamoja kuona kwamba wote tunakuwa pamoja katika kupigana na kupambana kwamba rushwa za ngono zisipatikane katika shule na hata katika maeneo ya kazi.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana.
Kwa kuwa, kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya mwaka ulioshia Juni 2015,
inaonesha kwamba kuna bohari ambazo hazina viwango. Sasa, je, Serikali
inasema nini kuhusiana na hatari ya afya za wananchi wetu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA
WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwanza naomba nikanushe vikali
sana kwamba kuna bohari za dawa zisizo na viwango. Kwa sababu, hiyo ni ripoti
ya CAG, sasa hii ni taarifa ya Serikali. Kwa hivyo naongea kama Serikali kwa
mamlaka kamili niliyopewa. Kwamba bohari tulizonazo pale MSD ni bohari zenye
viwango vya hali ya juu. Viwango hivi vimethibitishwa kwa ISO standards na
standards hizi zinakaguliwa kila baada ya miaka mitano ili kuthibitisha viability
yake na kwa msingi huo hatuwezi kutunza dawa kwenye bohari zisizo na viwango
kwa sababu zitaharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ifahamike kwamba dawa ni high value items,
hatuwezi kuzitunza hovyo hovyo kwa sababu tunazinunua kwa gharama kubwa
na ndio maana kuanzia utunzaji kwenda kwenye usambazaji mpaka kwenye
storage kwenye kituo cha afya kijijini kuna mnyororo uliokamilika unaozingatia
viwango vya ubora.


WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO:
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake lakini
pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, niseme tumepokea swali na
tutalifanyia kazi na tutaleta majibu Bungeni.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, Serikali ina mkakati gani mahsusi wa kuhakikisha kwamba Sera ya Tanzania ya viwanda inamkomboa kweli mwanamke wa Kitanzania?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia uwekezaji katika viwanda unazungumzia akina mama; na nguvu kubwa ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, viwanda ambavyo ni sustainable, viwanda ambavyo ni darasa, ni viwanda vidogo sana, viwanda vidogo na vya kati. Katika shughuli za kuhamasisha viwanda hivi mimi ninaokutana nao watupu ni akina mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shirika la akina mama la Food Processing liko Dar es Salaam, Binti Nasibu ndiye Mwenyekiti wake. Tunawatafuta akina mama tunawahamasisha kusudi muanze viwanda vidogo na vya kati ili kusudi mkue mfundishe na wazazi wenu. Mama akipata kiwanda na wajukuu wanapata kiwanda, na mama zao wanapata viwanda nchi yote inakuwa ya viwanda.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu ambayo hayaridhishi aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri naomba sasa ni muulize maswali mawili ya nyongeza:
Kwa kuwa, wanawake wanaposafiri na kupitia bandarini kwenda Zanzibar au kutoka Zanzibar kuja Dar es Salaam wanavuliwa nikabu kuanzia katika geti la bandari, na kwa kuwa wanawake hawa wanapata manyanyaso na lugha za kejeli.
Je, ni muulize Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa kupokea ushahidi?
Swali la pili, wapo wanaume wanaovaa mavazi na wakajipamba kujifananisha na wanawake, je, Serikali ina mpango gani wa kuwachukulia hatua wanaume hawa?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimezungumza katika jibu langu la msingi kwamba kama kuna matukio yoyote ambayo yameonekana kukiuka sheria za nchi ikiwemo hilo ambalo amelizungumza, kama ushahidi upo aulete tutaufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa nikiri kwamba kuna baadhi ya maeneo kwa mfano, tulifanya ziara katika bandari ya Zanzibar tuliona utaratibu ambao unatumika katika kuwakagua abiria siyo mzuri na bahati nzuri tulikuwa na Naibu Waziri wa Miundombinu wa Zanzibar, hilo tumelizungumza na Serikali italifanyia kazi karibuni utaratibu ule utabadilika.Hata hivyo binafsi sikushuhudia wala kutokea malalamiko yoyote juu ya yale ambayo ameyazungumza Mheshimiwa Mbunge, lakini kama yapo na ushahidi upo basi tutafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili kwamba kuna wanaume wanavaa mavazi ya kike na wanawake wanavaa mavazi ya kiume. Tafsiri ya mavazi ya kiume na ya kike nayo ni tafsiri pana maana suruali ni vazi la kiume sijui tuliite la kike, mwanamke anavaa na mwanaume anavaa. Kwa hiyo, sidhani kama kuna tafsiri sahihi ya kusema hili ni vazi la kiume na ipi ni ya kike ili Serikali iingilie katika uhuru wa wananchi kuamua jinsi gani wanataka kuvaa ni uhuru wao Kikatiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona swali lake hili linahitaji kwenda ndani kidogo, limekosa ufafanuzi kwa hiyo linakosa majibu ya wazi ya moja kwa moja. (Kicheko)
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Ahsante, Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja.
Mheshimiwa Waziri kwa kuwa suala la Mtwara linafanana sana na suala la Halmashauri ya Kisarawe kata ya Kibongwa, wananchi wamechukuliwa ardhi yao, ikakatwa viwanja, lakini wao hawakupatiwa viwanja wala hawakupatiwa fidia yoyote ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Waziri ni lini wanmanchi wa jimbo lako hili watapatiwa haki yao ya fidia?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli viwanja vilipimwa toka mwaka 2005 na ni kweli baadhi ya wananchi walichukuliwa eneo, lakini suala zima la mchakato wa fidia lilikuwa halijalipwa na ndio maana katika kulinda haki za wananchi tulisema hata vile viwanja vya mwanzo watu walitakiwa wapewe na wengine miongoni mwenu ni Wabunge humu ndani, tulivizuia kwamba watu wasipate vile viwanja mpaka wananchi wa pale wapate haki zao.
Kwa hiyo, jambo hili chini ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri linashughulikiwa vizuri na kila mtu atapata haki yake stahiki kwa sababu jambo hili viongozi tumelisimamaia kulinda haki za wananchi wetu.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize suala moja Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali inatilia mkazo suala la kukusanya mapato kwa njia ya kielektroniki. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri ana mpango gani wa kuhakikisha katika kituo cha Ubungo wanakusanya mapato kwa njia ya kielektroniki wakati abiria wakiingia na wakati magari yakitoka? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tumetoa maelekezo kwamba siyo maeneo ya vituo vya mabasi pekee isipokuwa maeneo yote, utaratibu wa Serikali ni kwamba tunaenda kukusanya mapato yote kwa njia ya kielektroniki.
Naomba nisisitize sana na nimuelekeze Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam ambapo eneo lile lipo, kama kuna upungufu kwamba sehemu zingine wamekusanya kwa njia ya kielektroniki na nyingine hawajakusanya washughulikie changamoto hiyo. Naomba niagize na mimi najua kwamba hilo zoezi limeshaanza katika Jiji la Dar es Salaam, kwamba ili kuziba mianya yote ile ya upotevu wa fedha, mifumo yote ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali katika vituo ya mabasi, hospitali na maeneo mengine ni kwa kutumia mifumo ya kielektroniki na si vinginevyo.
MHE. HALIMA A. MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba kwa kila Hospitali ya Halmashauri kunakuwepo huduma nzuri za watoto njiti kuliko ilivyo hivi sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mkakati tulionao kama Serikali tumetoa mwongozo sisi kama Wizara ya Afya, ambao unazitaka Halmashauri zote ambazo zinamiliki Hospitali za Wilaya kuhakikisha wana chumba maalum kwa ajili ya watoto njiti lakini pia wana chumba maalum kwa ajili ya Kangaroo Mother Care ambayo ni njia ya kisasa ya kuwalea watoto wachanga ambao wamezaliwa chini ya umri.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, mkakati ndio huo sasa Halmashauri kutekeleza hilo ni jambo lingine, lakini agizo letu kama Serikali ni kuzitaka Halmashauri zote kuhakikisha zinafuata mwongozo wa kuanzisha huduma za njiti katika hospitali zao.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, je, atakubali kwamba moja ya sababu zinazopelekea vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga wanapokwenda hospitali ni barabara na miundombinu mibovu.
Je, Naibu Waziri anasema nini katika suala hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa miundombinu ya barabara na mingineyo ili kuhakikisha kwamba watu wetu wanakuwa na ustawi unaotakiwa ikiwa ni pamoja na hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge Halima ameyaeleza na ndiyo maana miaka yote tumekuwa tukitenga bajeti kubwa zaidi katika eneo la miundombinu na hasa miundombinu ya barabara pamoja na miundombinu ya barabara vijijini na tukaunda kabisa TANROADS ishughulikie miundombinu ya barabara ili kuhakikisha kwamba changamoto ambazo wananchi wetu wanazipata za kiafya na changamoto zingine za kusafirisha mazao zinatatulika.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana, pamoja na majibu marefu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetangaza Tanzania ya viwanda na bila ya malighafi kutokana na mazao ya kilimo na uvuvi basi hatuna viwanda Tanzania.
Je, ni kwa nini Serikali haijajielekeza katika kilimo cha umwagiliaji maji ambapo Tanzania tuna mito mingi na mabonde mengi ili kuhakikisha basi tunakuwa na malighafi za kutosha kwa kipindi cha mwaka mzima? (Makofi)
La pili, kwa nini sasa Serikali haiwekezi katika mazao ya maua ambayo pia yanategemewa kuingiza income katika nchi yetu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema kuna uhitaji wa kuwekeza zaidi katika kilimo cha umwagiliaji na nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge katika Programu ya Kuendeleza Sekta Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kilimo cha umwagiliaji ni moja kati ya masuala ambayo yamewekewa mkakati mkubwa. Kwa hiyo, tunaamini huko mbele tunakokwenda kilimo chetu kitabadilika kwa sababu tutawekeza zaidi kwenye umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili; sekta ya maua ni moja kati ya sekta za kilimo ambazo Serikali inatilia mkazo. Ukienda Kaskazini mwa Tanzania, Kilimanjaro na Arusha kuna mashamba makubwa sana ya maua, lakini kwa ujumla wake horticulture ni moja kati ya maeneo ambayo vilevile tumeyawekea mkakati. Kwa asilimia kubwa kilimo cha maua kinaiingizia Serikali fedha za kigeni. Lakini ni kweli otential kubwa namna ya kuhamasisha kilimo cha maua.