Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mgeni Jadi Kadika (24 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mungu kwa kunipa afya njema na kumwezesha kuchangia hotuba hii. Elimu ni ufunguo wa maisha na Taifa. Ikiwa wananchi wake hawana elimu, basi Taifa hilo haliwezi kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mungu amesema, anayejua hawi sawa na yule asiyejua. Ni lazima anayejua ana upeo mkubwa wa kuona mbali. Kuhusu Walimu, wana kazi kubwa sana na wanafanya kazi katika mazingira magumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wanapata changamoto nyingi katika mazingira ya kazi, kwanza kufundisha wanafunzi wengi katika Idara moja, upungufu wa vifaa vya kufundishia, ukosefu wa matundu ya vyoo, maji hawana, nyumba za kuishi hawana, usafiri hawana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imetangazwa kwamba elimu ni bure, wakati bado miundombinu ni mibovu. Kwanza tuiboreshe. Naishauri Serikali kwamba bajeti ya Wizara hii iongezwe ili iweze kuboresha miundombinu, madarasa yaongezwe ili kupunguza msongamano wa wanafunzi, vyoo, madawati, nyumba za Walimu na mishahara ya Walimu pia iboreshwe ili waweze kutoa hiyo elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza, ikiwa mti huutunzi, hauna mbolea wala maji, utawezaje kutangaza tenda ya matunda?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wanapofika muda wao wa kustaafu, wanapata usumbufu mkubwa kupewa mafao yao. Wastaafu hao hudai mafao yao mpaka wanafariki hawapati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iwatizame wastaafu hawa kwa jicho la huruma, pale tu wanapostaafu wapewe haki zao mapema ili wapate kuwasaidia katika maisha ya uzeeni na pia wapatiwe bima ya afya angalau waweze kuhudumiwa, kupata matibabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonekana kuwa mila potofu ya watoto wa kike kuchezwa unyago ni moja ya kichocheo kikubwa kupata mimba za utotoni, kwa sababu mtoto akishachezwa unyago, hujiona yuko huru na tayari amekamilika na kuingia katika daraja la ukubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipige marufuku kwa mtoto wa kike kuchezwa ikiwa bado ni mwanafunzi ili kupunguza tatizo hili. Vilevile sisi viongozi, wazazi, walezi tukemee kwa kupiga vita jambo hilo ili kumpa nafasi mtoto wa kike aendelee na masomo yake. Baadaye akimaliza kusoma atachezwa kama ndiyo mila zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Zanzibar, elimu ya juu bado kuna usumbufu mkubwa kuhusu mikopo ya wanafunzi. Wanacheleweshwa sana na hivyo kuchelewa kuanza kusoma. Tunaomba Serikali ya Muungano iweze kusimamia ili usumbufu uweze kuondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuchangia, naomba kuwasilisha. Wako mjenzi wa Taifa.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuniwezesha kuchangia hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyombo vya habari ni muhimu katika kuwaelimisha wananchi kwa kupata habari kwenye tv na redio pamoja na magazeti, lakini pia wakati wengine vyombo hivi hivi vinapotosha. Kwa hiyo wawe na umakini kwa sababu utaona habari ni ile ile lakini huwa tofauti wakati wa matangazo au machapisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo kilichofanywa na Serikali sio haki kuzuia vyombo vya habari kuonesha Bunge wakati wa vikao vya Bunge hii ni uonevu kwa sababu wananchi Bunge ni lao, vyombo ni vyao na Wabunge wanachangia ni Wabunge wao wamewatumia kero zao kwa nini wananyimwa uhuru wao wa kuona Wabunge wao waliowatuma?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini wanamichezo wetu hasa wanawake wapokwenda nchi za wenzetu kucheza hawapati ushindi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la TBC ni chombo cha Serikali lakini chombo hiki hakiwatendei haki Watanzania kwa sababu hizo pesa wanazotumia ni za walipa kodi wa Tanzania, ukiangalia hiki chombo kina ubaguzi hasa wakati wa uchaguzi, tafadhali mtende haki. Serikali ni yetu sote hata ikiwa hatoki katika Chama cha Mapinduzi wakati uchaguzi umekwisha sasa kiongozi yeyote aliopo ni wetu sote acheni ubaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mungu kwa kunipa afya ya kuweza kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Nishati na Madini
Mheshimiwa Naibu Spika, nishati ya umeme ni nusu ya maisha ya binadamu hasa kwa wanawake kwa sababu mwanamke ni mdau mkubwa ndani ya nyumba; ikiwa umeme hamna au gesi basi kwake ni mtihani, itabidi afunge safari kutafuta kuni ili familia waweze kupata chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira ya ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa ili aweze kupikia au kufanya biashara. Miti inakwisha na nchi inakuwa na ukame kwa sababu ukataji wa miti unaharibu vyanzo vya maji na wafugaji wanahangaika kutafuta maji kwa ajili ya kuharibika kwa mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu madini, wachimbaji wadogo wadogo: Watanzania wengi ni wachimbaji wadogo wadogo ndiyo ambao wana mchango mkubwa katika kulipatia Taifa mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hutoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo ili waweze kujiimarisha katika kazi zao, lakini la kusikitisha ruzuku hizi haziwafikii walengwa na kuanza kutoa malalamiko, mfano maeneo ya Mwanza, Geita na kadhalika. Naishauri Serikali iunde Kamati ya kusimamia jambo hili, ikibainika wahusika washughulikiwe, hayo ndiyo majipu ya kushughulikiwa kutumbuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nishati ya mafuta ni muhimu sana katika maisha ya binadamu kama ilivyokuwa maji ni muhimu katika maisha ya binadamu na mafuta ni hali kadhalika, kwa sababu mafuta tunaendeshea magari, meli, ndege na pia kuendesha mitambo, kama hakuna umeme yanatumika kwenye jenereta. Hivyo, nishati ya mafuta inaleta uchumi katika Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kusikitisha nchi hii haina formula ya bei maalum. Ukienda Dar es Salaam bei nyingine, Unguja bei nyingine, Ukienda Mtwara bei ni nyingine na nchi nzima bei hazilingani.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba Serikali ipange mpango maalum kwa kupanga bei ambayo inalingana ili wafanyabiashara wasiwanyonye wananchi, wengine ni wanyonge katika nchi hii wanahitaji kuangaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutoa mchango huu, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, mwenye kunipa nguvu na afya njema nikaweza kuchangia hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiunga mkono hotuba ya Kambi ya Upinzani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza Maalim Seif Shariff Hamad kwa hekima yake na busara zake kuweza kuwatuliza Wazanzibari kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu. Kama si hekima zake basi sasa hivi tungekuwa tayari wengi wamekufa na wengi wamepata vilema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, sasa nakuja kwenye hoja. Mimi naanzia kuchangia hoja kwenye suala la UKIMWI. UKIMWI ni janga la Taifa na unapoteza nguvu kazi za vijana wetu katika Taifa hili. Pamoja na utafiti wa Serikali kusema kuwa UKIMWI umeshuka kuanzia asilimia 8.8 mpaka kufikia asilimia 5.1 lakini bado UKIMWI unaongoza. Utafiti unaonyesha mikoa mitano ya Tanzania ndiyo inaongoza kwa UKIMWI ambayo ni Mbeya, Iringa, Shinyanga, Dar es Salaam pamoja na Njombe. Mimi nataka kuzungumzia Mkoa wa Shinyanga kwa sababu ndiyo tulioutembelea na tukaona hali halisi ya wagojwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ninukuu wanasema, kuanzia Januari mpaka kufikia Disemba wagonjwa waliofika kwenye kituo cha afya na kupimwa wakaonekana ni waathirika katika Mkoa wa Shinyanga walikuwa ni wagonjwa 34,826, maambukizi mapya yalikuwa 953, hii ni asilimia kubwa. Nakuja kwa wajawazito, wajawazito waliofika kupimwa kati ya mwezi wa Januari mpaka Disemba walikuwa 81,509 na waliogundulika wameathirika ni wanawake 2,737, ni asilimia 3.4. Hii inaonyesha ni maambukizi makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri alizungumzia kuwa ataongeza vituo na dawa lakini hakuzungumzia chakula. Wagonjwa hawa wa UKIMWI wanapokula dawa za ARV basi ni lazima wapatiwe chakula kwa sababu dawa zina nguvu na wanazidi kuathirika. Kwa hiyo, naomba Serikali itenge fungu maalum la kuwasaidia hawa waathirika walio katika mikoa hii iliyoambukizwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuja kwa wakunga jadi. Wakunga wa jadi ni watu ambao wanatoa msaada mkubwa katika kuwasaidia akina mama wajawazito vijijini. Naiomba Serikali wawape mafunzo hawa waliokuwa hawajapata na waliopata mafunzo waajiriwe, Halmashauri ziwatazame, ziwape angalau posho za kupata sabuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya afya na zahanati ziboreshwe kwa sababu miundombinu yake ni mibovu. Hakuna maji, umeme na vitendea kazi na isitoshe vituo vya afya vinajengwa mbali na wananchi. Kwa hiyo, ni shida, mzazi akipakiwa kwenye baiskeli mpaka akifika kwenye kituo cha afya basi huyo hali yake ni taabani, hana nguvu za kusukuma mtoto inampelekea kufariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali ifanye juhudi za makusudi ili kuwapatia wanawake hawa gari angalau kila kata au kila kituo kipatiwe ambulance. Wenzangu wengi wamesema na mimi naomba hilo ili kupunguza vifo vya akina mama na watoto.
Mheshimiwa Spika, sasa nazungumzia watoto wa mitaani. Watoto wa mitaani ni wetu lakini inakuwa ni kero. Watoto hawa ni kweli maisha ni magumu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kuchangia hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyezi Mungu ameijalia nchi hii kuwa na neema na mali nyingi yapasa kumshukuru. Maliasili ya wanyamapori inaingiza faida kubwa ya Pato la Taifa kwa kuvutia watalii wa nchi mbalimbali na Serikali imepata pato la asilimia 25 siyo kidogo. Tunajua kuwa TANAPA inafanya kazi kubwa katika kuchangia pato kubwa katika sekta ya utalii katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya wakulima na wafugaji ni lazima Waziri wa Maliasili na Utalii akae na wenzake wa Wizara ya TAMISEMI, Kilimo, Mifugo na Halmashauri ili waende pamoja katika kutatua migogoro hii ili kuleta amani juu kwa wakulima na wafugaji na kuleta suluhisho la kudumu ndani ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya kihistoria yaliyomo katika nchi hii yaboreshwe ili tuzidi kuvutia watalii katika maeneo yetu kama vile Kilwa au kule Zanzibar sehemu ya Chwaka, Tumbe na maeneo mbalimbali ili tuzidi kuukuza utalii na kuzalisha kipato zaidi.
Kuhusu suala la mazingira hususani ukataji wa miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa au kukata miti kwa biashara ya mbao vibali vinatolewa kiholela. Kwa kufanya hivi hii misitu itakwisha na ukame utashamiri katika nchi hii. Kwa hiyo, ni lazima Serikali iwe makini na kile wanachokifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango wangu huu, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kuchangia hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu deni la matibabu ya ndugu yetu, Marehemu Nassor Moyo ambalo hadi leo Serikali ya Uingereza inadai Tanzania. Deni hili ni aibu kubwa kwa nchi yetu, ni vyema Mheshimiwa Waziri alipatie ufumbuzi suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabalozi wetu walioko nje ya nchi wanadharauliwa kwa sababu nyumba wanazoishi haziridhishi na hazina ubora, hii ni dharau. Mabalozi wanaoishi katika nchi yetu ya Tanzania wanaishi nyumba za hadhi na ubora wa hali ya juu. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri suala hili alisimamie kwa nguvu zake zote ili lirekebishwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Watanzania walioko nchi za nje wanapopatwa na matatizo au dharura, ni njia gani za mawasiliano watumie kupata msaada wa Kibalozi? Naomba Mheshimiwa Waziri atufafanulie suala hili.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza sina budi kumshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kuchangia hoja hii ya Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari ya Dar es Salaam. Ni bandari ambayo inaipatia pato Serikali yetu kwa kiasi kikubwa, lakini leo hii tunakosa mapato makubwa kutokana na kodi kubwa kuongezeka na wafanyabiashara kukimbia bandari yetu kwa kuogopa kula hasara. Wafanyabiashara wa Congo, Zambia, Malawi, wote hao wamekimbia na kuifanya Bandari kuwa kavu. Kuna upungufu wa makontena, magari ya mizigo hayaingii, wengi wamekosa ajira na uchumi kudorora.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge kazi yetu ni kuelekeza Serikali na kuishauri na kuikosoa pale inapofanya vibaya na kuisifu pale inapofanya vizuri. Sasa umefika wakati wa Mawaziri kusema ukweli, wasimdanganye Mheshimiwa Rais kwa kuogopa kutumbuliwa, hii ni nchi yetu sote, Watanzania wanatutegemea, tunakokwenda siko. Uchumi unaporomoka kutokana na mipango mibovu kuanzia matajiri mpaka mama ntilie. Mheshimiwa Waziri tunakwenda wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano, kipaumbele chake inajipanga kufufua viwanda na kujenga viwanda, lakini haiwezi kufanikiwa ikiwa miundombinu ya umeme na maji ni mibovu, ni lazima kwanza ijipange. Serikali kwa kusimamia kupatikana kwa umeme wa uhakika ili wanapokuja wawekezaji kuingia nao mkataba waweze kufanya kazi na kuipatia nchi uchumi na vijana wetu kupata ajira na kupatikana maendeleo. Porojo za kwenye makaratasi hazitoshi tufanye maamuzi ya kiutekelezaji ndiyo dira ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu ya umeme wa uhakika inaweza kuendesha viwanda na kukidhi matumizi mengine ya wananchi wa kujikwamua kimaisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo bado hakijapewa kipaumbele kwani benki hazitoi mikopo ili miradi ya kilimo iendelee; ni usumbufu mkubwa. Pembejeo hakuna, vitendea kazi kama vile matrekta, mbegu bora hakuna za kutosha, hivyo wakulima wapate mbolea mapema na bei zipunguzwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, vyanzo maji vya vingi vimekauka kutokana na uharibifu wa mazingira na ukataji wa miti hovyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Waziri atatuambia nini kuhusu upatikanaji wa mikopo ya fedha kutoka benki ili wakulima waweze kufaidika kwa kupata mahitaji yao ili kukuza uzalishaji na kupunguza umaskini?
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango wangu huu, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kuchangia hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni suala la kikatiba, Ofisi hii ina jukumu ya kuvisajili Vyama vya Siasa na kuvishauri. Kutokana na majukumu hayo Ofisi ya Msajili haina mamlaka ya kuingilia maamuzi yaliyofanywa na vyama vya siasa na katiba zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msajili wa Vyama vya Siasa kuwapa viongozi wa siasa ambao tayari wameshajiuzulu katika vyama vyao ni kinyume na Katiba ya Vyama na hata Serikali zote mbili. Kwa maana hiyo, tunamwomba Msajili wa Vyama kutekeleza majukumu yake na kuwaachia vyama kutekeleza majukumu katika vyama vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mambo ya kisiasa kama yalivyoelezwa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu naomba niseme kwamba, suala hili si shwari ndani ya nchi yetu. Kauli ya Mheshimiwa Rais kuzuia mikutano ya vyama vya siasa ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hali hii inaashiria kutokuwepo na uhuru wa kisiasa wa viongozi mbalimbali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama cha CCM kina mamlaka pekee ya kufanya siasa katika nchi hii. Kwa mujibu wa Msajili vyama vyote ni sawa, leo iweje Msajili wa Vyama kuviona vyama vingine vina haki na vyama vingine vikawa havina haki; je, hii ni sawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, madawa ya kulevya, kwanza naipongeza Serikali kwa kudhibiti madawa ya kulevya katika nchi hii. Madawa ya kulevya yanaathiri nguvu kazi ya vijana wetu ndani ya nchi yetu. Ndani ya nchi yetu vijana wengi wamejishughulisha na biashara ya madawa
ya kulevya kama vile cocaine, bangi, mirungi, viroba na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imeunda Tume ya Kupambana na Madawa ya Kulevya, lakini fedha zilizotengwa ni kidogo kutokana na tatizo hili kuwa kubwa. Hata hivyo, hizi zilizotengwa zitumike vizuri ili lengo lililokusudiwa lifanikiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usafiri wa anga, Kiwanja cha ndege kilichoko Pemba ni kidogo mno kinahitaji kupanuliwa kwa sababu ndege zitakazowasili ni nyingi kutokana na abiria wanaingia na kutoka ni wengi hasa watalii wanaokuja kujionea vivutio kama vile nyumba iliyojengwa ndani ya bahari iliyoko, Panga Watoro, katika Kijiji cha Makangale, pamoja na vivutio vilivyoko Meseli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango wangu huo, naomba nijibiwe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuniwezesha kuchangia hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiukwaji wa haki za binadamu, kwanza kuna jambo la kusikitisha kuhusu vijana wanaokwenda kufanya kazi za ndani katika nchi ya Uarabuni- Dubai. Vijana hawa wanateswa, wananajisiwa, wanauliwa lakini hawana watetezi. Je, ni kwa nini Balozi zetu wanakaa kimya na kwa nini hawafuatilii matokeo haya? Huu ni ukiukwaji wa haki za kibinadamu kwa hiyo Serikali yetu ya Tanzania ifuatilie tatizo hili ni kubwa, Watanzania wetu wanapotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Masheikh wetu wa upande wa Zanzibar walishikwa huku Bara sasa ni miaka minne wako mahabusu mpaka leo upelelezi haujapatikana, basi sasa waachiliwe huru wakaishi na familia zao kwa sababu jambo hili linaonekana ni la kisiasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mahakama ya Kadhi, Mahakama ya Kadhi ni chombo cha Kisheria kwa dini ya Kiislam. Chombo hiki ndicho kinachosimamia mirathi na ndoa. Ni kwa nini nchi hii ina Waislamu wengi na inazuia chombo hiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingi duniani zinazo Mahakama ya Kadhi kama vile Kenya, Uganda, Zanzibar na kadhalika. Je, ni lini chombo hiki kitafanya kazi hapa Tanzania bara kwa faida ya Waislam wa nchi hii? Naomba Waziri atakapofanya majumuisho nipate ufafanuzi tafadhali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huu, naomba kuwasilisha.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sina budi kumshukuru Mwenyenzi Mungu, kwa kunijalia afya njema na leo hii kuweza kusimama kwa ajili ya kuchangia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipatia nafasi hii. Nampongeza Katibu Mkuu wa Chama changu CUF Maalim Seif Sharif Hamad, pamoja na uongozi wa Taifa kwa kazi kubwa aliyonayo kupambana na wanafiki walioko ndani ya chama chetu, kututaka kutugawa na kusambaratisha chama chetu. Nasema chama chetu kiko imara Maalim Seif chapa kazi tuko pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu uzazi salama. Takwimu za hivi karibuni zinaonesha wanawake 30 wanafariki kila siku kwa kujifungua. Hii ni idadi tu ya wale wanawake wanaofika kwenye vituo vya afya na wanaofika hospitali kwani wengi wanajifungulia majumbani, idadi ni kubwa na hii hali inatisha. Wanawake wengi tunapoteza maisha kwa uzazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto nyingi zinazo msababisha mwanamke kufariki. Kwanza ni kukosa vifaa tiba na dawa; pili, lishe bora na umaskini unachangia pamoja vituo vya afya kujengwa mbali na wananchi, hivyo, inapelekea kupata matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naishauri Serikali bajeti ya Wizara ya Afya iongezwe na wale watu wanaofanyakazi kwenye sekta ya afya waboreshewe pia maslahi yao ili wapate kufanyakazi kwa weledi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Serikali kwa kudhibiti na kupambana na madawa ya kulevya katika nchi hii vijijini na mijini. Waathirika wengi wanaopoteza nguvukazi ni vijana walio chini ya umri wa miaka 18. Watoto hawa wanatoroka shule na baadaye wanajiingiza katika vitendo vya kutumia dawa za kulevya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa za kulevya zinachangia kiasi kikubwa maambukizi ya UKIMWI na magonjwa ya akili, naishauri Serikali kupitia sober house ni lazima akiingia mle walipie ada, wengi wao hawana uwezo, wazazi wao tayari wameshawatelekeza, kwa hiyo Serikali iwatibu bure kupitia Wizara ya Afya kwa sababu hawana uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu ukatili wa kijinsia. Wanawake wengi katika nchi hii wananyanyasika, wananyanyaswa na waume zao, kupigwa hata kuuawa, kwa sababu ya mapenzi tu. Wengine ni waume zao, wengine ni wapenzi tu, hilo jambo lipo, mashuleni, vyuo vikuu watoto wanajiingiza kwenye mapenzi na baadaye wanauawa. Hili jambo ni la kutiliwa nguvu sana kwa sababu linapoteza vijana wetu wengi kwa ukatili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kuchangia hotuba hii. Elimu ni ufunguo wa maisha, kila mtu atahitaji elimu ili aondoe ujinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uhaba wa walimu, kuna shule nyingi katika nchi hii na mikoa mbalimbali zina uhaba wa walimu hasa walimu wa sayansi. Tatizo hili ni kubwa na hasa shule za vijijini kwa sababu walimu wengi wanataka kufundisha mijini kutokana na matatizo yaliyoko vijijini, mfano, nyumba za kuishi, umbali wa shule na hawana vipando na kukosekana kwa miundombinu ya barabara au mwalimu mwanamke kuwa mbali na mume wake au mume kupangiwa kusomesha mbali na mke wake. Tunaomba maslahi yaboreshwe angalau waweze kujikimu na maisha. Walimu hawa wana kazi kubwa, sisi humu Bungeni tusingefika kama si kazi ya walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iwaangalie sana walimu wenye tabia mbaya wanaoharibu wanafunzi kwa kuwapa mimba au kumpasisha mwanafunzi kwa kufanya naye ngono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo walimu wanawapa wanafunzi adhabu kubwa kupita kiasi. Kama vile mtoto kupigwa mpaka kupoteza fahamu au kupata ulemavu na wengine mpaka kuwapoteza maisha na wengine kutoroka shule au kufungiwa chumbani. Walimu hao watakapobainika wachukuliwe hatua zinazostahiki ili iwe fundisho kwa wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto waliopata mimba mashuleni ni wengi na wengi wao ni wale waliokuwa hawana uwezo kwa kudanganywa na wanaume kwa kupewa chips au matumizi madogo madogo. Kwa hiyo, naiomba Serikali watoto wakibeba mimba warudishwe shuleni ili waendelee na masomo. Naomba waige mfumo wa Zanzibar. Pia naomba shule ziwe na mabweni ili kuwapunguzia watoto wa kike tatizo la kubakwa na kupata mimba zisizotarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za Serikali ambazo hazina matundu ya vyoo vijengwe vyoo na miundombinu ya maji kwa sababu watoto wa kike wanapokuwa katika siku zao wengi wanakosa masomo na hii ni changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huo, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuniwezesha kuchangia hotuba hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanajeshi wanaostaafu wanahangaika, hawapati stahili zao mapema, wanapata taabu sana. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali iwaangalie kwa jicho la huruma. Hawa ni watumishi wetu kama watumishi wengine mpaka wengine wanafariki bila kupata haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu huduma ya umeme katika Kambi ya Jeshi, Jeshi ni taasisi kubwa leo kukatiwa umeme itakuwa hawajatendewa haki. Wanajeshi ndio wanatulinda sisi ndani ya nchi yetu na mipaka ya nchi yetu ni lazima tuwape heshima. Tunalipongeza Jeshi letu kwa kazi kubwa. Kwa hiyo, wanastahili kulipwa maslahi makubwa na marupurupu wapewe pamoja na kupandishwa vyeo ili waweze kuitumikia nchi yetu kwa weledi mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vitongoji Ali Haji Camp waboreshewe nyumba zao, ni za zamani na nyingi ni mbovu na nyumba zilizoko Matangatuani Pemba nazo ziboreshwe. Kambi na Wanajeshi iliyoko Matangatuani ina wanajeshi walio imara na wanafanya kazi kwa weledi mkubwa.

Nashauri wanapopata uhamisho wapewe fedha za kutosha ili watoto wao wasipate shida na matatizo ya kuendesha maisha yao. Pia nataka kujua ni kwa nini wanajeshi wanapopata uhamisho wasichukue familia zao ili kuwapunguzia matatizo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kusimama na kuchangia hotuba ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Pia nakushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano, imejipanga katika uchumi wa viwanda; na ina nia nzuri tu ya kutoa ajira kwa Watanzania. Nchi yetu kama mtajenga viwanda vingi kama utitiri, lakini ikiwa havina usimamizi na wataalam waliobobea kiuweledi mkubwa, basi viwanda hivi vitakufa kama vilivyokufa vilivyokuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nichangie ujenzi wa Viwanda vya Minofu ya Samaki katika Ukanda wa Pwani. Nchi yetu inayo maeneo makubwa ya bahari, lakini hakuna kiwanda hata kimoja. Viwanda vyote vinaelekezwa kwenye Ukanda wa Ziwa. Kwa hiyo, naishauri Serikali ijenge viwanda kwenye eneo la bahari kama vile Dar es Salaam, Tanga, Lindi, Mtwara, Pemba na Unguja. Ujenzi huu utatoa ajira na utainua maisha ya wavuvi na kupunguza umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nakuja kwenye Viwanda vya Mabati. Viwanda hivi vinazalisha mabati chini ya kiwango katika baadhi ya viwanda, yakiwemo mabati ambayo yanaingia kutu haraka, mabati mengine yanachakaa haraka na pia yanavuja siku za mvua. Pia bei ya mabati hayo iko juu, kulingana na bei ya saruji ambayo kwa sasa imeshuka. Kwa hiyo, Serikali ina mkakati gani wa kusimamia ubora wa viwango vya mabati na pamoja na kudhibiti bei? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bidhaa feki zimezungumzwa na wenzangu wengi hapa, lakini nami nataka nizungumzie kuhusu bidhaa feki. Kuna bidhaa feki nyingi zinazoingizwa katika nchi yetu. Maziwa ya watoto yana madhara makubwa juu ya kutumia maziwa haya. Nyaya za umeme zinaunguza majumba yetu, zinapelekea maafa. Matairi kupasuka kwa muda mfupi tu na kusababisha ajali nyingi barabarani. Vipodozi vinaharibu ngozi za akinamama na wengi wanapata kansa. Je, Serikali inatuambiaje kuhusu suala hili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli wanawake wengi tuko ambao huwa tunatumia vipodozi na tunaharibika ngozi na wengi wanapata kansa, wengine wanakufa, uzuri wao umepotea. Kwa hiyo, hili suala linatakiwa lishughulikiwe kwa nguvu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nazungumzia kuhusu viwanda. Vimo viwanda vingi tu, SIDO, lakini hata vikiwekwa viwanda vikubwa kwa kuwaboreshea wakulima mazao yao, itakuwa ni bora zaidi. Nashauri kila kiwanda kiwekwe kila mkoa ili wazalishaji waweze kutumia viwanda hivi kwa kuyaokoa mazao yao; kama vile mananasi,maembe, machungwa, mazao kama nyanya na mazao mengine mengi tu yanaharibika.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, naona muda wangu umekwisha, naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuchangia hotuba ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Kilimo ni uti wa mgongo. Katika nchi yetu asilimia 75 tunategemea kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Kilimo ni muhimu ila inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinaathiri ukuaji wake. Kwanza, ni utoaji mdogo wa fedha za bajeti ya maendeleo, upungufu mkubwa wa Maafisa Ugani, wataalam wa utafiti na upungufu wa kuchakata bidhaa zake. Kubadilika kwa tabianchi inaathiri kilimo kama vile kupata ukame, mimea kupata ugonjwa, mvua zisizotabirika, mashamba kupoteza ubora wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iwaangalie wakulima wadogo wadogo kwa kuinua juu mazao yao. Wakulima wanapata hasara kutokana na mazao yao kukosa soko la uhakika. Leo utaona mazao mengi yanaharibika, mfano, mananasi, embe, machungwa, nyanya na pesheni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inawarudisha nyuma wakulima na kumrudisha kwenye umaskini kwa sababu itambidi lazima auze mazao yake kwa hasara. Je, Serikali ina mkakati gani wa kumwinua mkulima ili aweze kurudisha angalau hasara ya nguvu zake (mbolea).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uvuvi ambao unainua pato la nchi yetu kwa biashara na pia kuwainua wananchi kimapato katika maisha ya kila siku. Pia samaki ni chakula chetu na kila mtu anahitaji kula samaki ili kupata protein nyingi na kujenga afya yake. Sekta hii imemezwa na Sekta ya Viwanda. Tunahitaji tupate viwanda vingi vya kusindika samaki ili kupata tija zaidi. Viwanda vyetu vilivyokufa vinahitaji vifufuliwe na vifanye kazi. Samaki wapo wengi, tutakula na wengine tutainua biashara kwa ukubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji viwanda katika Ukanda wa Pwani kwa mfano Dar es Salaam, Tanga, Lindi, Mtwara Mafia, Zanzibar na Pemba. Samaki hawa wakivuliwa na kusindikwa, wengi watapata ajira na Serikali itapata kodi mbalimbali na itainua uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni nchi ya tatu Afrika kwa kuwa na mifugo mingi ukilinganisha na nchi kama Ethiopia na Botswana. Pia ng’ombe hutoa maziwa mengi lakini tunashindwa kusindika. Tunahitaji kujenga viwanda vingi tukamwinue mfugaji na pia tukainua uchumi wa nchi yetu kwa kusafirisha maziwa ya kopo tuachane na kuagiza kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina haja ya kuwapa elimu kubwa wafugaji kuhusu kuitunza ngozi na kuzikausha vizuri ili apate bei nzuri ili apate kujua tija ya kazi yake. Mfano, Ethiopia inafaidika kupata dola milioni 186 kwa mwaka 2016 kwa uzalishaji wa biashara ya ngozi pekee. Je, Serikali yetu inaingiza shilingi ngapi kwa mwaka kwa biashara ya ngozi pekee?

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango wangu, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kuchangia Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai wa binadamu, kila mtu anahitaji maji safi na salama ili awe na afya bora. Kila kiumbe kilicho ulimwenguni kinahitaji maji, maji ni uhai, maji ni kilimo, maji ni viwanda kila kitu kinahitaji maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niko Kamati ya LAAC na nimetembelea miradi katika mikoa ya nchi yetu na kujionea hali halisi ya miradi ya maji na umwagiliaji. Miradi mingi imejengwa chini ya viwango, utakuta mradi ni mkubwa na unagharimu fedha nyingi lakini wananchi hawapati maji. Aidha, pipe ni nyembamba haiwezi kusambaza maji kwa vijiji vyote, kwa mfano vijiji sita watapata vijiji viwili, hili ni tatizo. Ikumbukwe hii ni Wizara kubwa na yenye mahitaji makubwa. Naomba bajeti ya maji iongezewe fedha ni ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa umwagiliaji Inalia. Mradi huu uko katika Manispaa ya Tabora, ni mkubwa na umegharimu fedha nyingi, jumla ya Sh.246,536,679, hizi fedha ni nyingi. La kusikitisha, mradi huu umekamilika zaidi ya miaka saba sasa lakini haujafanya kazi kwa sababu wamiliki wa mashamba haya mpaka leo hawajalipwa fidia ya mashamba yao na kupelekea mgogoro mkubwa baina ya Halmashauri na wenye mashamba. Mradi una ukubwa wa ekari 110 na wale wananchi waliopewa wameukataa kutokana na mgogoro huo. Je, Serikali ni lini watawalipa wananchi hao fidia ili mashamba hayo yaweze kuendelezwa? Namwomba Waziri aende akatatue mgogoro kwa sababu waathirika wakubwa ni wanawake kuhusu matatizo ya maji, wanapoteza muda mrefu kutafuta maji na wengine ndoa zao kuvunjika.

Mheshimiwa Naibu Spika, vyoo mashuleni kukosa maji ni tatizo kubwa lakini ni tatizo kubwa zaidi kwa mtoto wa kike pale anapokuwa kwenye siku zake za hedhi inambidi akae nyumbani na kusababisha kukosa masomo. Je, Serikali ina makakati gani kuhakikisha tatizo la maji linaondoka?

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango wangu huu, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa kunipatia nafasi. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema kuweza kusimama hapa kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Elimu. Pia natoa pole kwa Watanzania wote waliopata mafuriko wakafiwa na wapendwa wao pamoja na kupoteza mali zao. Baada ya kuzungumza hayo sasa naanza kuchangia hotuba hii iliyopo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuulize ni jambo gani linalotupa kuteremka kiwango cha elimu katika nchi yetu? Tuna changamoto kubwa sana ndiyo inayoleta kuporomoka kwa elimu.

Changamoto ya kwanza ni upungufu wa walimu. Tuna upungufu mkubwa wa walimu, ukosefu wa vitabu vya kusomea na vitabu vya kujifunzia, maslahi ya walimu ni madogo na wanafundisha kwa muda mrefu bila ya kupandishwa daraja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba wapandishwe madaraja na waongezwe maslahi yao kwa sababu mama ikiwa hashibi hawezi kutoa maziwa ya kumlisha mtoto wake. Kwa hivyo ni lazima tuwaangalie kwa jicho kubwa ili waweze kufanya kazi zao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna ukosefu wa matundu ya vyoo pamoja maji. Hilo ni tatizo kwa sababu maji ndiyo uhai wa binadamu. Leo watoto wengi wa kike wanafeli kutokana na kwamba wakiwa katika siku zao za hedhi kuwa hawawezi kuhudhuria masomoni muda wa wiki moja mpaka wiki mbili. Hiyo inachangia watoto wa kike kufeli, kwa hivyo ni lazima Serikali liitatue kwa haraka tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa walimu na hasa walimu wa sayansi. Tuna upungufu wa walimu wanaofika 15,968; huo ni upungufu kubwa sana. Tunataka nchi ya viwanda tutakwendaje kwenye viwanda ikiwa hatuna wasomi wa sayansi na ukiangalia upungufu mkubwa nao uko katika shule za msingi; kwa hiyo, ni lazima Serikali iajiri walimu mara moja kuziba mapengo ya wale wa vyeti fake waliotolewa na tupate walimu wa kuendeleza elimu ili elimu yetu iweze kupanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za Serikali zinasomesha lugha ya kiswahili wenzangu wengi wamezungumza. Lugha ya kiswahili kuanzia chekechea mpaka darasa la tatu. Wakati ni tofauti shule za private zinasomesha lugha ya kiingereza kuanzia chekechea mpaka darasa la tatu. Ukiangalia mtihani wao uko sawa sawa, je, watakuwa sawa hao kwenye matokeo wakati wale wameshaiva, wale ndiyo kwanza wanaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo natoa ushauri kwamba Serikali ikae na wadau wa shule za private ili kushirikiana na kutoa elimu iliyo bora ili wote wafaidike kwa sababu wote ni watoto wa Tanzania na wote ni watoto wetu, tusibague wale wakawa bora kwetu sisi wakawa si bora. Leo inafika hadi shule za Serikali darasa la saba mtoto hajui kusoma wala kuandika, hili ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kuhusu mitaala. Kila baada ya kipindi mitaala inabadilika. Inapobadilika tunawapa mzigo wazazi kwa sababu itabidi wanunue vitabu vipya. Wanaponunua vitabu vipya wengine wahana uwezo utawakutia watoto watano wanasomea kitabu kimoja, hilo ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunawapa mzigo mkubwa walimu, kwa sababu mwalimu lazima kwanza ajifunze mtaala ule ndipo aweze kufundisha. Kwa hiyo, nashauri angalau miaka 10 ndipo baadae mtaala uangaliwe na kufanya tathimini kwamba je, mtaala huu utaendelea au mtaala huu bado haufai ili ubadilishwe ili kuwaondoshea mzigo walimu na wazee? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia kuhusu watoto wenye hali ngumu. Tukiangalia hapa Dodoma ukienda pale… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuniwezesha kuchangia Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai wa binadamu, wanyama na kilimo na kila kilichoumbwa. Bajeti ya Wizara hii ni ndogo mno kwa sababu maji katika nchi hii ni tatizo kubwa na ndoa zinakatika kwa ajili ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wakati wa kampeni yake na baada ya kushika madaraka alisema atahakikisha kuwa anamtua mama ndoo kichwani, lakini bado tatizo liko pale pale, bado ndoo iko kichwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatenga fedha za miradi, lakini inachelewesha kuzifikisha fedha katika Halmashauri na utakuta utekelezaji wa mradi unakwama na kuchukua muda mrefu.Vilevile wakandarasi ni lazima wasimamiwe kikamilifu kwa sababu wananunua mabomba yaliyokuwa hayana viwango. Utakuta muda mdogo yanapasuka na kusababisha maji kupotea.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wako wakandarasi ambao hawana utalaam wa kutosha, wanachimba visima virefu lakini maji hayapatikani na baadae kufeli na kusababisha kuitia hasara Serikali na mradi kusimama, hili ni tatizo. Tunaomba watendaji waache kukaa ofisini, wafike kwenye miradi kuisimamia ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile fedha zitengwe kwa ajili ya kujengwa mabwawa ya kuhifadhia maji ya mvua ili kupunguzia wananchi tatizo la mifugo yao hasa wakati wa kiangazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wasomaji wa mita wana matatizo, hawasomi mita vizuri na wanawabambikia madeni makubwa wananchi ambao wanashindwa kulipa baadae wanawakatia maji na kupata usumbufu mkubwa.

Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha shule zote nchini zimepata maji ili kuwaondoshea usumbufu watoto wetu hawa wasichana pale wanapokuwa kwenye siku zao waendelee na masomo yao waondokane na kubakia nyumbani?

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango wangu huu naomba kuwasilisha na kabla sijawasilisha, nauliza; ikiwa hatuna maji ya kutosha hivyo viwanda vitafanyakazi vipi?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasiliaha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Nitajikita kwenye Wizara ya Afya hususani Bima ya Afya (NHIF). Kwa kweli kila mtu anahitaji kuwa na afya nyema, Taifa lililokuwa halina afya basi halina maendeleo wala halizalishi uchumi wala hatutazaana kwa haraka, naam! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, taarifa ya Wizara ya Afya kuhusu bima wanasema mpaka sasa hivi wanaotumia bima ni 34% tu. Hicho ni kiasi kidogo, bado Serikali haijajipanga kutoa afya kwa wote. Watu wengi hawana bima ya afya na tuna maradhi mengi yanatusumbua kama vile kansa, kisukari na maradhi mengine. Kwa hiyo, Serikali ifanye kila jitihada kutumia bima ya afya na wale waliokuwa hawajajiunga wajiunge. Wizara itoe elimu na ihamasishe ili watu wote wajiunge kwenye bima ya afya ili wapate matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilipata fursa ya kwenda Rwanda ili kuona Bima ya Afya inavyofanya kazi ni tofauti wanavyofanya hapa kwetu. Kule tajiri, maskini wote wanapata fursa sawa za kutibiwa. Wao kule wanatibiwa kwa mfumo wa daraja, tajiri anatibiwa kwa daraja lake, mwenye kipato kikubwa anatibiwa kwa daraja lake na watu wa kati na wa chini wana madaraja yao na wale waliokuwa na hali zao ni duni kabisa basi wanatibiwa bure wakiwamo hao maskini, watoto chini ya miaka mitano, walemavu pamoja na wajawazito. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisemi kwamba kwa nchi yetu wajawazito watibiwe bure, watibiwe kwa daraja, wale masikini kabisa ambao hawana hata hela ya kupanda daladala basi watibiwe bure. Tulikaa na Wizara ya Afya na wakasema watafanya mazungumzo ili kuleta Muswada hapa Bungeni tuweze kutunga sheria ya watu wote wapate fursa sawa ya kupata matibabu. Naiomba Serikali iharakishe kuleta Muswada huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie sasa masuala ya UKIMWI. Katika Mkoa huu wa Dodoma kuna asilimia kubwa ya maambukizi, kwanza ilikuwa 2.3% mpaka sasa hivi waathirika wamepanda imekuwa 5%. Je, Serikali inasemaje kuhusu Mkoa wa Dodoma? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi kama viongozi hapa Bima ya Afya wanatibu Mbunge na mweza wake na watoto wanne. Hata hivyo, kuna Wabunge wengine humu hawana wenza, hana mke na mwingine hana mume, kwa nini asitumie fursa hii kutibu wazazi wake? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Spika, mazingira ya kufanyika mikutano ya hadhara kwa Vyama vya Upinzani inaonekana kukataliwa na kutoruhusiwa mara nyingi na Jeshi la Polisi. Hivyo, kitendo hiki kinanyima fursa ya kidemokrasia kwa kukandamiza uhuru wa Vyama vya Upinzani. Je, Polisi sasa wana mkakati gani wa kuondokana na dosari hii?

Mheshimiwa Spika, msongamano wa mahabusu na wafungwa kwenye Magereza bado ni mkubwa na hii inatokana na upelelezi kuchukua muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, kesi ya Mashehe wa Uamsho imechukua muda wa miaka sita sasa bila kujua hatma yao ni ipi, kwani hadi leo upelelezi haujakamilika. Ninaomba jambo hili vyombo vinavyohusika hasa wanaotafuta upelelezi lifanywe haraka ili haki itendeke.

Mheshimiwa Spika, mchakato wa kupatikana kwa vitambulisho vya Mtanzania bado haujaridhisha, kwani unaonekana ni ndoto kwamba hadi kufikia 2020 kupatikana kwa vitambulisho hivyo kwa Watanzania wote. Ninashauri Serikali iongeze mtambo wa kuzalisha Vitambulisho vya Taifa.

Mheshimiwa Spika, ubovu wa Kituo cha Konde, Pemba unatisha. Mvua zikinyesha maji yanahatarisha afya ya Askari. Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati kituo hicho na Kituo cha Matongatuoni, Pemba ambacho ni kibovu?

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kuchangia hotuba ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali mwaka jana bajeti ya Wizara ilikua bilioni 1.408 mwaka huu imeshuka mpaka kufikia bilioni 1.357. Upungufu wa bilioni tano, ni kwa nini Serikali inapunguza bajeti ukiangalia maisha yanapanda, shule zinaongezeka na wanafunzi wanaongezeka na mahitaji yanaongezeka zaidi

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi ya Elimu ya Juu pamoja na bajeti kuongezeka kufikia bilioni 424 ambapo bajeti halisi bilioni 4.3 sawa na asilimia 18 ya bajeti ya maendeleo na mikopo ya wanafunzi asilimia 52 ya bajeti. kuna changamoto ya mikopo ya wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vitambulisho vya Taifa; wanafunzi wanakosa mikopo; kwa hivyo Serikali ishirikiane na NIDA ili wanafunzi wanaostahiki wapate mikopo kwa haraka ili wapate kuendelea na masomo mapema. Vile vile viko vyuo baadhi vina madeni kwa hivyo wanafunzi wanachelewa kupata mikopo hiyo. Kwa hivyo nashauri bodi watumie wanafunzi moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyuo vya VETA, Serikali imepanga fedha kidogo sana. Vyuo vya VETA vina mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya vijana wetu kwa sababu vijana wengi wanaomaliza kidato cha nne na wale waliofeli darasa la saba wanataka wajiunge na vyuo hivyo ili kupata ujuzi wa ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Serikali ya uchumi wa viwanda leo tukiwa na vijana wengi waliopitia vyuo vya VETA watapata ajira. Vile vile tunaishauri Serikali ijenge vyuo vya VETA kila wilaya ili vijana wengi wapate kujiunga na vyuo hivyo.

Baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mungu kwa kunipa afya njema na kuniwezesha kuchangia hoja hii. Pia napenda kuwapongeza kwa dhati Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa anazozifanya kwa kweli, wanajituma kwa nguvu zao zote kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya matibabu ya afya kwa kutupatia dawa na kupatikana vifaatiba katika hospitali zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, NHIF; huduma ya matumizi ya kadi ya bima ya afya NHIF tunahitaji watu wote wapate huduma hii ili wapate matibabu kwa kutumia huduma hii kwa urahisi, lakini bado tuko nyuma, mpaka sasa wanaotumia huduma hii ni asilimia 34 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Watanzania wanataka elimu ya kutosha itolewe hasa vijijini, ili wapate uelewa juu ya matumizi ya bima ya afya na vievile waweze kutibiwa kwa daraja lake ili yule mwenye maisha duni aweze kutibiwa kwa uwezo wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu viongozi wanaotumia huduma hii mfano Wabunge, wanatibiwa yeye pamoja na mwenza wake na watoto wanne, lakini mzazi wake hapati huduma hii. Swali langu ni hili je, hatuoni Serikali haijawatendea haki wazee kuwakosesha huduma hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, sina budi kuipongeza Serikali kwa Taasisi ya Moyo kuweza kutupatia tiba na wataalam mbalimbali kuhusu tatizo hilo. Tunaomba tiba hii ipatikane katika hospitali nyingine za rufaa mbalimbali katika nchi yetu, ili kuipunguzia mzigo Hospitali ya Muhimbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Madaktari na Wauguzi pamoja na wafanyakazi mbalimbali wa sekta ya afya. Hawa wote wanafanya kazi katika mazingira magumu kutokana na kazi zao. Kwanza tunaomba waangaliwe, maslahi yao yaboreshwe ili waweze kupata ari na upendo wa kazi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Madaktari, Wauguzi na Nesi wana changamoto mbalimbali zikiwemo posho ya nyumba, motisha ya saa za ziada. Hili tatizo kubwa linaweza kuathiri utendaji kazi wao, kwa hiyo, naiomba Serikali iliangalie tatizo hili kwani hawa ndio wanaotuokoa katika maisha yetu ya kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vifo vya wajawazito bado ni changamoto katika nchi yetu, baada ya kupungua bado vinaongezeka katika Taifa letu. Kwanza naipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya, juzi nilishuhudia kwenye vyombo vya habari kuwa inatoa michango mbali ya fedha kutaka kuwasajili Wakunga wa Jadi ili kuweza kusaidia kupunguza vifo vya akinamama wajawazito na watoto. Ahsante sana Waziri Ummy, wanawake tunaweza.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango wangu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii. Pia nawatakia kheri Waislamu wote wanaofunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitakwenda kwenye viwanda, kweli Serikali ya Awamu ya Tano imejenga viwanda vingi lakini viwanda hivi kama havikuangaliwa vizuri basi vitakufa haraka sana. Ni lazima viwe na watu wenye ujuzi wa kuviendesha viwanda hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia wawe na viwanda vya malighafi kwa sababu malighafi nyingi inaagiziwa kutoka nje ya nchi na kuleta hasara kwa Taifa. Kwa hivyo, ni lazima viwanda vijengwe hapa ili kupunguza gharama na kuipatia mapato Serikali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Mwenyezi Mungu katika nchi yetu ametujalia utajiri mkubwa yakiwemo maziwa na bahari. Katika nchi yetu tunazungukwa na bahari katika ukanda wa Pwani wa Dar es Salaam, Tanga, Lindi, Zanzibar, Pemba na sehemu nyingine lakini hakuna viwanda vya kuchakata samaki, tunakosesha Tanzania kupata mapato. Kwa hivyo, Serikali ijipange kujenga viwanda vya minofu ya samaki. Tunawaachia Wachina wanakuja na meli zao, wanavua samaki wanaondoka nao sisi tupo tunaangalia. Kwa hivyo, Serikali ijipange kujenga viwanda hivyo hata Zanzibar na Pemba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaambiwa kuwa Zanzibar siyo nchi, Tanzania ni Taifa moja lakini kinachosikitisha bidhaa zinazotoka Zanzibar kuja Tanzania Bara hawapewi vibali. Tuna sukari, maji ya drip na maziwa lakini haviruhusiwi kuingia Tanzania Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kushangaza Tanzania Bara inaleta vitu Zanzibar mfano bia, sigara, soda na vitu vinginevyo, kwa nini na wakati ni nchi moja? Kwa nini na sisi hatufaidiki? Nchi moja itakuwa tukiwa Zanzibar lakini tukiwa Bara ni nchi mbili? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, mfano wa magari. Gari linapotoka Tanzania Bara tunalipa ushuru, lakini linapoingia Zanzibar unalipa tena ushuru mara mbili. Ni kwa nini ilipe ushuru mara mbili? Hili ni tatizo.

MBUNGE FULANI: Na ni nchi moja.

MHE. MGENI JADI KADIKA: …na ni nchi moja. Kwa nini tufanye hivyo? Kuna nini? Naomba basi, kama ni nchi moja, basi isiwe tunalipishana ushuru mara mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu wafanyabiashara. Kwa kweli, Wafanyabiashara tunawarudisha nyuma au Serikali inawarudisha nyuma kwa sababu kodi inayotozwa ni kubwa mno. Mfanyabiashara anapewa mahesabu anaambiwa miaka mitatu hujalipa; sijui hivi, kuna hili, kuna hili, inapigwa thamani ya kupewa mfanyabiashara wakati ile biashara yake aliyonayo kwenye duka haitoshi. Ile biashara yake yote ikipigiwa thamani haitoshi, tunampeleka wapi mfanyabiashara huyu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana wafanyabisahara wengi wamefunga maduka yao, wafanyabiashara wengi wanarudisha leseni. Je, tunakwenda wapi? Tunakwenda wapi? Serikali hii hatuko masikini, tuna utajiri wa kutosha, kwa nini tuwabane wafanyabiashara wao tu? (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kutoa mchango wangu katika hotuba hii. Pia nawatakia Waislamu duniani kote Ramadhan Kareem.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga uchumi wa viwanda na ni ukweli usiofichika viwanda vingi vimejengwa. Hata hivyo, kama viwanda havitakuwa na usimamizi mzuri na wataalam wenye ujuzi mkubwa vitakufa na kukosekana kwa matarajio ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima Serikali iweze kuhimiza kujenga viwanda vya kuzalisha malighafi ili kupunguza kupoteza fedha nyingi kuagiza malighafi kutoka nje na kuisababishia Serikali hasara. Mungu ametupa utajiri mkubwa katika nchi hii ikiwemo maziwa na bahari lakini nitazungumzia bahari, tunazo bahari zetu kama Dar es Salaam, Mafia, Tanga, Lindi, Zanzibar lakini bahati mbaya hatuna viwanda vya kuchakata samaki, hii inapelekea kuwakosesha vijana ajira na kupoteza pato kubwa la Taifa. Pia inapelekea leo kuwaachia Wachina kuuza samaki wetu na kuondoka nao. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga viwanda hivi katika Miji niliyoitaja ili tupate maendeleo?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema Tanzania ni nchi moja na Taifa moja lakini la kushangaza bidhaa zinatoka Zanzibar mfano sukari, maziwa ya Azam, maji ya Drop hayaruhusiwi na hawapewi kibali kuingia Tanzania Bara lakini Zanzibar zinaingia mfano condom, sigara, bia na kadhalika. Nitoe mfano mwingine magari yanayotoka Tanzania Bara ni lazima ulipe ushuru wa bandari TRA na magari yale yale yanapofika Zanzibar yanalipa tena ushuru na TRA. Je, hiyo ni haki? Tunaomba changamoto hii itatuliwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango wangu huo, naomba kuwasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na leo hii kusimama hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya jambo la busara sana kukutana na wafanyabiashara ili kuwasikiliza kero zao, alizikuta kero zao ni kodi ya TRA kuwapandishia kwa muda mrefu na wafanyabiashara hao wakashindwa kulipa kodi hizo na wakafunga biashara zao na wengine wakaondoka katika nchi, Waziri siku zote hizo alikuwa hajaliona. Sasa hivi kasema biashara isifungwe mpaka apewe kibali, haya mapato ya Serikali yameshapotea kwa wingi ndiyo leo tunaamka na siku zote Wapinzani walikuwa wakisema neno hilo lakini ilikuwa bado hamjatafakari, kupotea njia ndiyo kujua njia. Ahsante.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii kwa kweli bado haijampenda mnyonge, kwa sababu Rais wa Muungano anasema yeye ni Rais wa wanyonge lakini hii haijawapenda wanyonge. Nitazungumzia kuhusu nguo za mitumba. Nchi yetu asilimia 80 wavaa mitumba hawawezi kuvaa nguo mpya kwa unyonge wao, leo mnawapandishia kodi kutokea asilimia 25 mpaka 35 kwa nini? Waziri nakuomba chondechonde hizi asilimia 10 uziondoe ili wanyonge wapate kuvaa nguo za mitumba ili wasitirike, nakuomba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu Dodoma. Serikali yetu imeipandisha hadhi Dodoma inakuwa Jiji la Dodoma na ndiyo Makao Makuu lakini bado ilikuwa haijajipanga vizuri.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mgeni weka vizuri hiyo Microphone yako ili kumbukumbu zisikike vizuri, hapo nimezima nakuelekeza wewe uiweke vizuri isimame karibu na kinywa chako.

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Serikali haijajipanga kwa sababu haiwezekani Makao Makuu ya nchi mpaka leo hii ikawa bado hawajaweka mtambo wa kuchapishia magazeti. Magazeti mpaka yatoke Dar es Salaam ndiyo yafike hapa ni kwa nini? Kwa hivyo jipangeni mkianza kufanya mambo ili mambo yote yaendane kwa sababu hapa ndiyo kitovu cha nchi, panapotungwa sheria, kwa hiyo leo mpaka gazeti litoke Dar es salaam lije hapa?(Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nataka kuzungumzia ni kuhusu Zanzibar. Serikali ya Muungano ni pamoja na Serikali ya Zanzibar ndiyo ikaitwa Muungano. Sehemu ya Serikali ya Muungano ni pamoja na Zanzibar ndiyo ikaitwa Muungano ni sawa lakini bado Muungano haujaitendea haki Zanzibar. Kwa sababu haiwezekani Kitabu cha Bajeti kuanzia ukurasa wa 25 mpaka 35 zote zinajenga Tanzania Bara wakati Tanzania Visiwani nayo inayo haki katika Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi Waziri wa Fedha wa Zanzibar alipohitimisha bajeti yake ya fedha alisema kuwa kuna miradi mitatu imeshindwa kutekelezeka kwa sababu Serikali ya Muungano hawajaweka saini na miradi mitatu hiyo kwanza ni barabara inayotoka Mkoani kwenda Chakechake, kilometa 40, vilevile akazungumzia kuhusu gati ya Mpigaduri.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar uchumi wetu ni bandari, uchumi wetu ni biashara Airport leo bandari ile ni nyembamba sana ikiingia meli moja tu inaweza kupakua mizigo kwa muda wa wiki nne haiwezi kuingia meli nyingine. Meli nyingine zinakuja inabidi zipindishe zikateremshe mizigo katika nchi jirani ya Kenya bandari ya Mombasa. Kwa hivyo, tukasema tutengenezeeni bandari ya Mpigaduri ili tuweze kufanikiwa lakini wameshindwa kutia saini, ni kwa nini? Hapo kweli Muungano mnautendea haki?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumzia Airport ya Chakechake sasa ni mwaka mzima, mashine ya ukaguzi haifanyikazi. Haifanyi kazi ukipita pale mizigo inabopabopa kama mafenesi au wewe mwenyewe, mpaka madawa ya kulevya yanaweza yakapitishwa kwa sababu hapana usalama katika Airport hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, jingine nazungumzie kuhusu Bandari ya Wete. Juzi niliuliza swali nikaambiwa pesa zimetengwa, itatengenezwa na mwenzangu amezungumzia hapa lakini hakuna kinachoendelea, kwa hivyo tunaiomba Zanzibar siyo wana wa kambo, tupo nasi katika sehemu ya Muungano, yaliyo ya Muungano tuyaaingize kwenye Muungano, yasiyokuwa ya Muungano basi tutafanya wenyewe lakini isiwe kutuonea.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Bandari ya Wete…

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)