Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Raisa Abdalla Mussa (6 total)

MHE. RAISA ABDALLAH MUSA: Mheshimiwa Spika, napenda nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kutokana na mfumo wa mabenki mengi, utitiri wa mabenki mengi hapa nchini, Serikali imejipanga vipi kuyasimamia mabenki yale na kuyawezesha ili iweze kuwakopesha wateja na kuleta tija kwa Taifa letu?
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwamba Serikali kupitia mabadiliko ya mfumo uliotokea mwaka 1991 ilijitoa katika kuendesha moja kwa moja sheria za kifedha hapa nchini, lakini hayajaachwa huru, Benki Kuu inayasimamia na ndiyo maana nimesema hata hizi taasisi ndogo ndogo tunaandaa Sera ya Taifa ya hizi taasisi ndogo ndogo za fedha ili zote tuweze kuzisimamia kiuhakika, lakini siyo kuingilia katika uendeshaji wa huduima hizi. Nina imani kubwa taasisi zetu hizi za kifedha zinafanya kazi kwa ajili ya Watanzania na kwa ujumla zinatenda vizuri ndiyo maana watu wengi wanaweza kuzifikia na kupata mikopo pale wanapohitaji.
MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA: Mheshimiwa Spika, asante kwa kuniona kwa sababu ni mgeni ndiyo maana jina langu hukunitaja naitwa Raisa Abdallah Mussa, Viti Maalum kutoka Zanzibar CUF. Napenda nimuulize Mheshimiwa Waziri swali moja la nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Waziri katika vituo vidogo vya polisi vilivyoko Zanzibar, kuna baadhi ya vituo vimehamwa na nikutajie kwamba kituo cha Kidongo Chekundu Mentally Hospital, pale ni kituo muhimu sana kwa maeneo yale ya Kidongo Chekundu na Sogea, sasa hivi kile kituo kimehamwa na pamekuwa hasa kama gofu mpaka pamefanywa vijana wamekaa maskani yao pale pembeni yake.
Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka uniambie una mpango gani na kukihuisha kituo kile cha Polisi cha Kidongo Chekundu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna baadhi ya vituo vya polisi ambavyo kidogo havifanyi kazi ikiwemo kituo hicho ambacho nilizungumza Mheshimiwa Mbunge, lakini pia kuna kituo cha Vuga na Shaurimoyo.
Mheshimiwa Spika, lakini kuna sababu mbalimbali ambazo zinasababisha vituo hivi kwa muda visiweze kufanyakazi. Vingine ni kwamba mahitaji ya vituo katika maeneo hayo yanakosekana umuhimu kulingana na changamoto za uhalifu na ukaribu wa vituo vingine vikubwa vya polisi vilivyopo maeneo hayo. Hata hivyo, kutokana vilevile na uhaba wa idadi ya askari waliopo tunashindwa kufungua vituo vyote katika maeneo yote ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, sasa niseme tu kwamba, kituo cha Kidongo Chekundu ni moja kati ya vituo hivyo, hata hivyo nimuhakikishie Mbunge pamoja na wananchi wanaosikiliza kwamba Serikali haijakitupa kituo hicho, pale ambapo mahitaji yatakapoonekana ya muhimu tutakifanyia ukarabati na kuweza kukitumia kwa haraka sana.
MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na mlolongo mrefu ambao majibu yake yamepatikana, Watanzania tunaona aibu majengo yetu yaliyopo nje pindi tukitembelea Ofisi za Mabalozi. Kwa muonekano wa wazi kabisa ni kwamba bajeti hasa inayopangwa ambayo ameisema Mheshimiwa Naibu Waziri hapa ni kwamba haikidhi haja na kutotolewa kwa wakati ile bajeti yenyewe iliyopangwa. Swali la kwanza, je, Wizara haioni umuhimu ya kuachia mapato ya viza au vyanzo vingine vya mapato vinavyopatikana katika Balozi zetu wakaachiwa wenyewe kule Ubalozini ili wakashughulikia suala la kuziimarisha Balozi zetu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, suala la uchakavu wa ofisi na majengo ni la muda mrefu. Mimi siyo Mbunge wa kwanza na wala hili si Bunge la kwanza kuulizwa masuala haya kuhusu Balozi zetu, lakini inaoneka kama tunababaishwa sasa hatupewi uhalisia ni upi.
Je, ni lini Serikali itaacha ubabaifu wa majukumu yake ya majengo haya ambayo sasa inaonesha uchakavu ni endelevu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, kuhusu Serikali kuachia ukusanyaji wa maduhuli kwa maana ya pesa zinazotokana na visa zitumike kule Ubalozini ili kufanya ukarabati katika Balozi zile zenye uchakavu wa majengo na kadhalika, nafikiri Mheshimiwa Mbunge pia ana uzoefu na Bunge hili linajua kwamba siku za nyuma maduhuli hayo yalikuwa yanaruhusiwa kutumika katika Balozi zetu. Hata hivyo, ilionekana kwamba zinapobakishwa pale baadhi ya Balozi zetu zilikuwa hazitumii vizuri maduhuli yale na utaratibu ule ukabadilishwa wakashauri urudishwe Serikalini.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi hatuwezi tukasema tunaweza tukaachia tu hivi hivi, suala hili sisi tulilipeleka tukalijadili na tumeona kwamba baadhi ya Balozi bado hazijawa na nidhamu ya matumizi mazuri ya maduhuli wanayokusanya katika Balozi husika. Lakini pale tutakapokuwa tumeona kwamba maduhuli au pesa wanazopelekewa wanatumia kwa utaratibu uliowekwa, basi sisi hatutasita kwa sababu tunachotaka ni kuhakikisha kwamba Balozi zetu zinakuwa katika hali nzuri na zinajenga taswira nzuri ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kwamba Serikali iache ubabaishaji, nafikiri Serikali haifanyi ubabaishaji. Ndiyo maana tumesema pamoja na kwamba tunaweka bajeti ya maendeleo ili iweze kutatua tatizo na changamoto ya ukarabati wa majengo yetu ambayo ni machakavu lakini tumesema pia kwamba kuna mpango kazi ambao tumeweka kwa utaratibu kwamba majengo tuliyonayo mangapi na yapi yamechakaa zaidi na yapi yaanze kutengenezwa. Serikali hata siku moja haitakuwa inatumia ubabaishaji katika kutekeleza kazi zake. Hilo tunamhakikishia Mheshimiwa kwamba tutalitekeleza ipasavyo.
MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kawaida wafungwa wanawake au kisheria wanatakiwa walindwe au wasimamiwe na askari magereza wanawake na tunaamini kwamba magereza wale ambao wamefungwa kule wako katika mikono salama. Inakuwaje akina mama wale wanapata ujauzito wakiwa katika magereza? (Makofi)
Swali la pili ni kwamba, je, Waziri haoni kwamba iko haja ya akina mama hawa kupewa vifungo vya nje ili kutoa haki kwa watoto wale wasiwemo ndani ya magereza kama walivyo mama zao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa mujibu wa utaratibu na ndivyo hali ilivyo kwamba wafungwa wanawake wanasimamiwa na askari magereza wa kike. Sasa hoja kwamba wafungwa wale wanapata mimba wakiwa gerezani hiyo inahitaji uthibitisho, kwa sababu katika hali ya kawaida huwezi kujua mimba ile ameipata vipi. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kimsingi mazingira hayaruhusu hali hiyo kutokea katika Magereza. Kwa hiyo, ni dhahiri kabisa kwamba inawezekana pengine waliingia pale hali ya kuwa walikuwa na mimba changa. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na vifungo vya nje kwa akina mama hawa. Tunao utaratibu ambao haubagui jinsia ya kuweza kuwapatia vifungo vya nje kwa mujibu wa taratibu. Tuna utaratibu wa huduma za jamii, tuna utaratibu vilevile wa msamaha na wanawake wanafaidika katika taratibu zote mbili. Kwa hiyo, utaratibu huo upo lakini inategemea na makosa. Kwa wanawake ambao makosa yao hayakidhi vigezo vya kuweza kupata fursa hiyo wataendelea kutumikia vifungo vyao kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona Waheshimiwa Wabunge wamesimama wengi sana.
Waheshimiwa Wabunge, nimezunguka takriban Magereza ya Mikoa yote na katika zunguka ile hakuna eneo hata moja ambako nimefika nikaelezewa kwamba mama ama mwanamke aliyekuwa amefungwa kifungo cha muda mrefu amegundulika amepata mtoto akiwa katika kifungo cha muda mrefu. Ni kweli unaweza ukakuta wale waliokuwa wana vifungo vya muda mfupi wakajifungua wakiwa gerezani, lakini kujifungua wakiwa gerezani haina maana kwamba mimba kaipatia gerezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge niwaambie tu vyombo vyetu hivi ni vyombo vinavyofanya kazi kwa sheria kali sana. Haingewezekana mwanamke apatie mimba ndani halafu ijifiche isijulikane kwamba kapatia mimba pale. Kwa hiyo, hatua zingeshachukuliwa na wale watu ni wachukuaji wa hatua kweli kweli. (Makofi)
MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kawaida wafungwa wanawake au kisheria wanatakiwa walindwe au wasimamiwe na askari magereza wanawake na tunaamini kwamba magereza wale ambao wamefungwa kule wako katika mikono salama. Inakuwaje akina mama wale wanapata ujauzito wakiwa katika magereza? (Makofi)
Swali la pili ni kwamba, je, Waziri haoni kwamba iko haja ya akina mama hawa kupewa vifungo vya nje ili kutoa haki kwa watoto wale wasiwemo ndani ya magereza kama walivyo mama zao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa mujibu wa utaratibu na ndivyo hali ilivyo kwamba wafungwa wanawake wanasimamiwa na askari magereza wa kike. Sasa hoja kwamba wafungwa wale wanapata mimba wakiwa gerezani hiyo inahitaji uthibitisho, kwa sababu katika hali ya kawaida huwezi kujua mimba ile ameipata vipi. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kimsingi mazingira hayaruhusu hali hiyo kutokea katika Magereza. Kwa hiyo, ni dhahiri kabisa kwamba inawezekana pengine waliingia pale hali ya kuwa walikuwa na mimba changa. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na vifungo vya nje kwa akina mama hawa. Tunao utaratibu ambao haubagui jinsia ya kuweza kuwapatia vifungo vya nje kwa mujibu wa taratibu. Tuna utaratibu wa huduma za jamii, tuna utaratibu vilevile wa msamaha na wanawake wanafaidika katika taratibu zote mbili. Kwa hiyo, utaratibu huo upo lakini inategemea na makosa. Kwa wanawake ambao makosa yao hayakidhi vigezo vya kuweza kupata fursa hiyo wataendelea kutumikia vifungo vyao kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona Waheshimiwa Wabunge wamesimama wengi sana.
Waheshimiwa Wabunge, nimezunguka takriban Magereza ya Mikoa yote na katika zunguka ile hakuna eneo hata moja ambako nimefika nikaelezewa kwamba mama ama mwanamke aliyekuwa amefungwa kifungo cha muda mrefu amegundulika amepata mtoto akiwa katika kifungo cha muda mrefu. Ni kweli unaweza ukakuta wale waliokuwa wana vifungo vya muda mfupi wakajifungua wakiwa gerezani, lakini kujifungua wakiwa gerezani haina maana kwamba mimba kaipatia gerezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge niwaambie tu vyombo vyetu hivi ni vyombo vinavyofanya kazi kwa sheria kali sana. Haingewezekana mwanamke apatie mimba ndani halafu ijifiche isijulikane kwamba kapatia mimba pale. Kwa hiyo, hatua zingeshachukuliwa na wale watu ni wachukuaji wa hatua kweli kweli. (Makofi)
MHE. RAISA ABDALLA MUSSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri wanayotoa Wizara ya Afya mara nyingi wanapoulizwa maswali hapa Bungeni nina swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la msingi ni kwamba kunahitajika vifaa tiba katika hospitali za Serikali. Sasa pamoja na vifaa tiba, kuna kitu muhimu ambacho kinatakiwa na Watanzania katika Hospitali hasa za Serikali nacho ni kauli nzuri ya wahudumu na wafanyakazi katika hospitali za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwambie Waziri na Naibu Waziri kwamba suala hili halipatikani katika katika Hospitali zetu za Serikali. Ama ukienda hospitali za binafsi jinsi wanavyofanya biashara zao wanawanyenyekea watu, lakini hospitali hizi za wanyonge hilo halipatikani. Je, Mheshimiwa Waziri anatuambia vipi kuhusu wafanyakazi ambao wanatoa kauli ambazo haziridhishi kwa Watanzania? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza natambua kazi nzuri na kubwa inayofanywa na wataalam wanaotoa huduma kwa watu wetu hapa nchini. Napenda sisi kama viongozi tutambue kazi kubwa wanayoifanya kwa kujitoa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia natambua kuwa kuna baadhi ya wafanyakazi ambao wana changamoto hizo anazozisema Mheshimiwa Raisa kwamba wana lugha mbaya, wanashindwa kuhudumia watu vizuri na customer care ni mbovu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwamba wataalam wote kwenye sekta ya afya wale wachache ambao bado hawajabadilika, huu ni wakati wa kubadilika. Kwa sababu kwa kweli tukipata taarifa za mtaalam ambaye amem-treat vibaya mteja wetu huwa tunachukua hatua bila kulaza damu. Kwa hiyo, nitoe rai wasiombe nikawakuta na tuhuma hizi kwa sababu nitawapeleka kwenye Baraza lao la Kitaalam waweze kuchukuliwa hatua za kitaaluma. Ahsante. (Makofi)