Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Riziki Shahari Mngwali (4 total)

MHE. RIZIKI S. MNGWALI aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo sugu nchini kwa baadhi ya vituo vya afya na zahanati kuwa na watumishi wasio na sifa za utabibu:-
Je, Serikali inatumia vigezo gani kuwapeleka watumishi wasio na sifa katika zahanati na vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Riziki Shahari Mngwali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu ambao unatumika kuajiri watumishi wa kada za afya ni kuwapanga moja kwa moja kwenye vituo vya kazi kadiri wanavyohitimu na ufaulu wa masomo yao. Aidha, ili kuhakikisha watumishi wasio na sifa hawaajiriwi, Serikali imekuwa ikafanya zoezi la uhakiki wa vyeti vyao kabla ya kusaini mikataba ya ajira. Hivyo, endapo Mheshimiwa Mbunge anazo taarifa za kuwepo kwa watumishi wa afya wasio na sifa atusaidie kupata taarifa hizo ili tuweze kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto kubwa ya upungufu wa watumishi wa afya, zipo baadhi ya zahanati na vituo vya afya ambavyo vina watumishi wenye sifa tofauti na muundo. Serikali kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) inaendelea kushughulikia changamoto hii ambapo tayari mikoa tisa yenye upungufu mkubwa zaidi wa watumishi imetambuliwa na kupatiwa kipaumbele cha kuwaajiri watumishi wa afya. Vilevile Serikali imepanga kuangalia maeneo yenye mlundikano wa watumishi ili kuweka uwiano wa watumishi baina ya zahanati na vituo vya afya vilivyopo mijini na vijijini.
MHE. RIZIKI SHAHARI MNGWALI aliuliza:-
Serikali ilijenga Gati kubwa la Kilindoni katika Wilaya ya Mafia kwa mabilioni ya fedha ili kuwezesha meli kubwa kutia nanga na hivyo kutatua tatizo sugu la usafiri wa majini Wilaya ya Mafia, licha ya Gati hilo kukamilika na kuzinduliwa na Rais aliyepita Mheshimiwa Jakaya Kikwete tangu mwaka 2013, bado Gati hilo halijaanza kutumika jambo ambalo limesababisha wananchi kuendelea kupata adha kubwa ya usafiri kwa kutumia bahari.
Je, Serikali itaelekeza meli kubwa na boti zenye viwango na bima kuanza kuwahudumia wananchi wa Mafia kwa kutumia Gati la Kilindoni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Riziki Shahari Mngwali, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, majukumu makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ni pamoja na kujenga miundombinu ya kibandari na kuendesha shughuli za Bandari. Katika utekelezaji wa majukumu yake, Mamlaka ilikamilisha Ujenzi wa Gati la Kilindoni-Mafia lililofunguliwa rasmi tarehe 2/10/2013 na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Ujenzi wa Gati hili uligharimu kiasi cha shilingi bilioni 27. Aidha, katika kuboresha matumizi ya Gati hili, mamlaka ilikamilisha kazi zifuatazo:-
(i) Landing barge kwa ajili ya kuegesha majahazi,
(ii) Shed kwa ajili ya mizigo, na
(iii) Uzio kwa ajili ya usalama wa waendao kwa miguu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza awali, Gati hili lilikamilika na liko tayari kwa ajili ya matumizi. Hata hivyo, pamoja na utayari huo kama tunavyofahamu, wadau wakubwa wanaoendesha shughuli za usafiri wa majini katika mwambao wa bahari ni sekta binafsi. Kwa kutambua hilo, Wizara yangu itaendelea kuwashawishi na kuwashauri wadau hao wawekeze katika usafiri wa kwenda Mafia kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Bunge ambazo zinasimamiwa na SUMATRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya usafiri wa majini ni kama ilivyo biashara nyingine yoyote. Hivyo, milango iko wazi kwa makampuni yanayotoa huduma hii, pia kuwekeza katika Mwambao wa Mafia. Hata hivyo, tunamuomba Mheshimiwa Mbunge aendelee vilevile kuwashawishi wananchi kwa ujumla kujitokeza na kuwekeza katika Mji wa Mafia ili ukue kibiashara zaidi ya ulivyo sasa ili kuwavutia watu na watoa huduma kushawishika na kuwekeza katika Mwambao wa Mafia.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI aliuliza:-
Kwa mila zetu za Kiafrika imezoeleka kuwa huduma ya ukunga kwa akinamama wajawazito wakati wa kujifungua hutolewa na wataalam wanawake:-
Je, Serikali haioni kuwa kwa kuweka Wakunga wanaume katika baadhi ya zahanati za Serikali nchini ni kuwadhalilisha akinamama wajawazito wanaojifungua katika zahanati hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Riziki Shahari Mngwali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wakunga wote nchini wanafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya mwaka 2010. Kwa mujibu wa sheria hiyo, Mkunga ana wajibu wa kutoa huduma ya kumsimamia mama mjamzito wakati wa uchungu, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua. Kwa mujibu wa sheria hiyo, Wakunga wote wa kike na wa kiume wanaruhusiwa kutoa huduma ya ukunga baada ya kufuzu mafunzo yao na kupata leseni ya kutoa huduma hizo kutoka katika Baraza la Uuguzi na Ukunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, japo Sheria ya Uuguzi na Ukunga inampa mtaalam aliyefuzu masomo hayo kutoa huduma lakini kumekuwepo na changamoto kwa baadhi ya wanajamii kutokana na mila na desturi zinazotawala jamii husika. Kutokana na hali hiyo, Serikali itaendelea kuajiri wataalam wengi ili pale penye changamoto iweze kupatiwa ufumbuzi bila kuwakwaza wanajamii husika.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina utaratibu gani maalum wa kuwapangia na kuwahamisha sehemu za kazi watumishi wake?
(b) Je, ni vigezo gani huzingatiwa katika kuwapanga au kuwahamisha watumishi sehemu za kazi?
(c) Je, ni kwa namna gani Serikali inahakikisha watumishi wake wanafanya kazi kwa ufanisi katika maeneo waliyopangwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Riziki Shahari Mngwali, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha watumishi wa kada ya ualimu na wale wa kada za afya ambao utaratibu wao wa kuajiriwa ni wa kupangiwa vituo vya kazi mara tu wanapohitimu mafunzo yao, utaratibu wa ajira kwa kada nyingine hufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 8 ya mwaka 2002.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sheria hii, mchakato wa ajira hufanywa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ambayo hutangaza kazi kulingana na mahitaji ya waajiri, kufanya usaili na kuwapeleka katika vituo vya kazi waombaji waliofaulu usaili.
Mheshimiwa Naibu Spika, uhamisho ndani ya utumishi wa umma hufanywa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298 ikisomwa kwa pamoja na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, Toleo la mwaka 2009 ambapo Katibu Mkuu (Utumishi) amepewa mamlaka ya kufanya uhamisho wa watumishi wa umma kutoka kwa mwajiri mmoja na kwenda kwa mwingine kwa lengo la kuimarisha utendaji ndani ya Utumishi wa Umma.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vinavyotumika kuwapanga au kuwahamisha vituo vya kazi watumishi wa umma ni pamoja na:-
(i) Mahitaji ya kila taasisi kutokana na kuwepo ikama na bajeti ya mishahara ya watumishi kwa mwaka wa fedha husika.
(ii) Sifa za kitaaluma kama zilivyoainishwa kwenye Miundo ya Maendeleo ya Utumishi kama inavyotolewa mara kwa mara na Serikali.
(iii) Umuhimu wa kuimarisha utendaji wa kazi na kuongeza ufanisi katika utumishi wa umma.
(iv) Kupangiwa kazi au uhamisho kutokana na mtumishi kupata maarifa/taaluma mpya (re-categorization).
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha watumishi wanafanya kazi kwa ufanisi katika maeneo waliyopangwa, zipo Mamlaka za Ajira na Nidhamu ambazo zimewekwa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298. Kwa mujibu wa sheria hii, mamlaka hizi zinapaswa kuhakikisha kuwa kila mtumishi anapangiwa majukumu kulingana na mpango mkakati wa kila taasisi, ambapo kila mwisho wa mwaka upimaji wa wazi wa utendaji kazi hufanyika. Pale mtumishi anapoonekana hajatimiza malengo yake kwa sababu yoyote ile, anapaswa kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazoongoza usimamizi wa utumishi wa umma.