Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Riziki Shahari Mngwali (9 total)

MHE. RIZIKI SHAHARI MNGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nina maswali mawili ya nyongeza na ukiniruhusu nina ombi pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuondoa huduma za usafiri wa majini kwa wananchi wa Mafia kwa upande wa Serikali, lakini bado Serikali hiyo ikatoa huduma kwa Mashirika yake ya Umma kwenye sehemu nyingine za Maziwa Makuu. Serikali haioni kama inawabagua watu hawa wa Mafia?
Swali la pili; Waziri atakubaliana nami kwamba, kwa sababu katika swali langu la msingi niliulizia pia viwango vya boti. Huo utaratibu ambao wameruhusu SUMATRA wauendeshe ndiyo huo wa kutuwekea boti ambazo hazina viwango na pia hazina bima. Je, Serikali haioni kuna ulazima sasa wa kuwa na mipango ya muda mfupi, kuwa na usafiri wa kuaminika wa majini kwa Watu wa Mafia wakati wakiendelea kushawishi hao wawekezaji binafsi kuja kutoa huduma hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nina ombi na hili ni kwa jumla siyo kwa Waziri wa Wizara hii tu, bali kwa Mawaziri wote kwamba tafadhalini sana, peaneni dose ya know your country, kwa sababu majibu mnayotoa ni standard namuomba Waziri husika aje Mafia aone kama hilo Gati analozungumzia lina viwango hivyo anavyovieleza hapa. Ahsante
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana kwa karibu sana na Mbunge wa Jimbo la Mafia, Mheshimiwa Mbaraka Dau. Wameondoa tofauti ya Vyama, wameungana, wanawatumikia watu wa Mafia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbaraka Dau muda wote amekuwa akisisitiza kuhusu gati la Nyamisati ili kuweza kuunganisha kati ya Kilindoni na Nyamisati ili uwezekano wa kuongeza uvutiaji wa wawekezaji wa kutoa huduma katika eneo hilo. Nawashukuru sana kwa kuungana na mimi nawahakikishia Muungano huo tutahakikisha unazaa matunda haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ubaguzi kwa kutoa huduma kwenye Maziwa Makuu, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba uamuzi huu wa kuondoa shirika ambalo lilikuwa linatoa huduma za meli baharini upande wa Bahari ya Hindi ulifanyika ndani ya Bunge hili na kama mnaona kuna ulazima wa kurudia tena ili tulianzishe Shirika la Kutoa Huduma kwenye Bahari ya Hindi tutafanya uamuzi humu ndani, baada ya Serikali kulitafakari suala hilo kwa kina na kuangalia faida na hasara zake. Suala la ubaguzi halipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu SUMATRA kutoa vibali kwa boti ambazo hazina standard, nimemsikia na naomba kumhakikishia nitalishughulikia hilo kuona ukweli wake, undani wake na sababu zake ili tuweze kurekebisha huduma zinazostahili na boti zinazostahili kutoa huduma pale Mafia ziweze kufanya kazi.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shahari nadhani ombi lako atakujibu Mheshimiwa Waziri baadaye baada ya kujiridhisha kama anaweza kuja huko.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza hasa kwa kuwa majibu hayakutosheleza haja.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunarudi pale pale kwenye kutoa huduma stahiki na kuajiri wahudumu stahiki, siyo suala la kuajiri wengi bali waajiriwe Wakunga ambao wanaendana na mila na desturi zetu na wale ambao wanakidhi haja. Je, Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba Serikali hii ya CCM imekuwa inafanya mambo yake kanyaga twende tu na siyo kwa kufuata taratibu maalum?
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali hii ya CCM itakubaliana na mimi nikisema kwamba haiendani na matamko yake? Leo hii gazeti linaandika kuboresha huduma za uzazi lakini wanatuambia wataendelea kutuwekea Wakunga wanaume kwa kuwahudumia wanawake. Naomba majibu.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali ya Chama cha Mapinduzi haifanyi mambo yake ya kanyaga twende. Hapa nilizungumzia sheria inasemaje kwa sababu kama Majaji Naibu Spika mna taratibu na sheria zenu. Nimeshangaa sana, kuna sehemu nyingine sasa hivi hata ukiangalia kuna ma-gyno wengi sana akinamama lakini siku nyingine wanaenda kwa ma-gyno wa pande zote mbili. Niseme kwamba siku zote Serikali inalenga kuona ni jinsi gani itawasaidia wanajamii kupata huduma bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na dhana nzima ya kusema kwamba tuwe tunaajiri watumishi wa kike na wa kiume, nimesema kwamba tutaendelea kuajiri na ndiyo maana nimesema jamii zetu zinatofautiana. Kuna maeneo mengine ambayo inaonekana kwa mila na desturi zao itabidi tuweke watu wa aina fulani na sisi tutafanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge katika Mkutano uliopita aliuliza swali hili hili na nilitoa maelekezo. Bahati nzuri hapa tumepata takwimu wataalam wangu wa afya na RMO wetu wa Mkoa baada ya agizo lile waliweza kufanya mchakato katika kila zahanati takribani nane wameweza kubadilisha wale wataalam kutokana na swali lako mama la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimepata taarifa hizo lakini nitaenda kufanya verification mwenyewe kuona hali ikoje, lakini taarifa nilizozipata toka wiki iliyopita ni kwamba walifanya mchakato huo na zile zahanati ambazo mwanzo zilikuwa na wataalam wa kiume peke yake sasa hivi wamepeleka na wataalam wa kike lengo likiwa ni kuwasaidia akinamama.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa Wilaya ya Mafia, napenda kuwashukuru sana kwa mchakato mlioufanya wa kupata mashine mbalimbali. Tulikuwa na tatizo la X-ray na Utra-sound machine, Mbunge wao Mheshimiwa Dau amefanya harakati watapata Ultra-sound na X-ray machine mpya, zimeshafika Dar es Salaam sasa hivi wanaendelea na taratibu za kuzisafirisha kwenda Mafia. Kwa hiyo, tutaendelea kuenzi juhudi kubwa zinazofanyika lakini Serikali itajitahidi kwa kadiri iwezekanavyo wananchi wapate huduma bora.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na kwa niaba ya wananchi wa Mafia niulize maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa majibu ambayo hayatoshelezi sana, namuuliza Mheshimiwa Waziri kama ataichukulia kesi ya Mafia kuwa ni special case ambayo inahitaji kushughulikiwa kwa haraka? Hili liko katika zahanati ya Chemchem ambapo zahanati imepewa jukumu la kuwa kituo cha afya kwa maana ya kushughulikia vijiji zaidi ya kimoja lakini ina mhudumu wa afya badala ya tabibu ambaye anahudumia wananchi. Je, analichukulia jambo hili kuwa ni suala la dharura na kwa hiyo atupatie tabibu haraka iwezekanavyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ataichukulia pia kama ni special case Zahanati ya Chunguruma ambapo pamoja na kumuweka Mkunga mwenye sifa lakini ni mwanaume. Je, atatupelekea haraka Mkunga mwanamke katika Zahati ya Chunguruma ili wanawake wa Mafia wapewe huduma stahiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeisikia changamoto hii na umezungumzia Zahanati ya Chechem na Chunguruma. Kama nilivyosema pale awali, ni kweli, ukiangalia Mafia ina Hospitali ya Wilaya na tuna zahanati takriban 16. Changamoto yake ni kwamba zinazo-function vizuri ni zahanati tano. Kwa hiyo, tuna upungufu mkubwa zaidi katika zahanati zipatazo 11.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili nini cha kufanya sasa, ndiyo maana Wilaya ya Mafia sasa hivi imepewa kibali cha kuajiri watumishi wapatao 18 lakini katika hilo kipaumbele cha awali ni kuajiri Clinical Officers ili ku-cover maeneo yale ambayo tunaona kuna watu ambao hawastahili kufanya hizo kazi lakini kutokana na changamoto iliyopo wanafanya kazi ambazo ziko nje ya kada yao. Kwa hiyo, tunalifanyia kazi hilo suala hilo na tunaishukuru Ofisi ya Utumishi imeshatupatia kibali. Si muda mrefu sana baada ya ajira hiyo watumishi hao wataweza kufika katika zahanati hizo ili waweze kutoa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika hili tumejielekeza, asubuhi tulikuwa tunawasiliana na RAS wetu wa Mkoa wa Pwani. Changamoto ya jiografia ya Mafia utakuta watumishi wengi sana wakipangwa wengine wanasuasua kufika. Tumeelekezana na RAS wa Mkoa wa Pwani kuhakikisha watumishi wote wanaotakiwa kufika Mafia hasa katika sekta ya afya waweze kufika ili wananchi wote wanaotakiwa kupata huduma waweze kupata huduma. Lengo letu kama Serikali ni kuhakikisha afya hasa ya mama na mtoto inalindwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya kwamba mhudumu mwanaume ndiye anayetoa hiyo service, tumelichukua hili. Nadhani ni angalizo kwa sisi watu wa Serikali japokuwa watu wa afya hasa Madaktari kazi zao wanafanya sehemu zote lakini tunatoa kipaumbele kwa akinamama. Inawezekana magonjwa mengine anapohudumiwa na baba inakuwa ni changamoto kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tulichukue hili na nimwelekeze RAS wetu wa Mkoa wa Pwani kuhakikisha kwa haraka anafanya juhudi iwezekanavyo kupeleka Madaktari au wahudumu wanawake katika zahanati hii ambayo inaonekana ina changamoto kubwa ili hata mtu akienda katika zahanati ile akiwa mwanamama aone kwamba sitara yake imesitirika. Nashukuru sana.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, actually swali langu lilikuwa ni nyongeza kwa hapo kwamba katika hiyo historia kinachogombewa zaidi katika kumbukumbu ni ile orodha sahihi ya majina ya mashujaa wetu wale ili waenziwe kwa namna inavyostahiki. Kwa hiyo, nyongeza yangu ilikuwa, je, Serikali katika huo utafiti wake itatuletea pia orodha sahihi ya mashujaa hawa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tumeshakiri kwamba tuko tayari sasa kufanya utafiti wa historia, kwa hivyo, orodha kamili itakayopatikana italetwa kama Mheshimiwa Mbunge anavyotaka.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Spika,
nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, hii barabara ambayo Mheshimiwa Dau ameisema, wenzenu ndiyo ilikuwa lami ya kwanza
tumeiona katika miaka 50 ya uhuru, kwa hiyo, ilipoharibika baada ya siku chache kwa kweli tumeumia. Sasa hii barabara ukitoka pale round about ya Kilindoni kwenda Utende ni kwamba zaidi ya theluthi mbili ya barabara ni mbovu. Sasa
nashangaa Mheshimiwa Naibu Waziri anavyotwambia
kwamba ni sehemu chache.
Sasa swali langu, je, Mheshimiwa Waziri
atatuhakikishia ushirikishwaji uliokamili wa wadau wote wa
Mafia na watumiaji wa barabara ile kabla ya hiyo kazi ya
kuanza ukarabati ili na sisi tujue hilo andiko mlilosema ninyi
mapungufu machache na kazi itafanyika kwa kiasi gani?
Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, nakubali, tutashirikisha wadau na kwa taarifa hii TANROADS Mkoa wa Pwani wawashirikishe wadau wa Mafia kabla CHICO hajaanza kurekebisha yale maeneo ambayo yamegundulika yana matatizo.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nishukuru kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri ameweka vizuri swali ambalo nilitaka kuuliza, ni hiyo hiyo kwamba kuja na misamiati ambayo mwisho wake tunaona kama tunakwama na pale mwanzo akazungumzia mpaka suala la bajeti. Lakini ni vipi Serikali sasa itarudisha katika shule za msingi na sekondari yale mafunzo au taratibu za elimu ya kujitegemea ambapo watoto walikuwa wanajifundisha kupika maandazi, kufuga kuku, kutengeneza mifuko na kazi kama hizo, hizo hazihitaji bajeti wala hazihitaji misamiati lakini watoto wakitoka pale wana ujuzi. Ni lini Serikali itafanya hivyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba kupitia stadi za kazi wanafunzi wamekuwa wakipata muda wa kujifunza masomo kama hayo. Lakini kuna wakati sera zetu huwa zinakuwa kama zina mgongano kidogo. Kwa mfano kuna wakati tulisema kwamba wanafunzi wasipewe kazi, watoto wasipewe kazi, watu wakachukulia hiyo ni kufuta mpaka hizo stadi za kazi. Lakini kwa kuacha kufanya hivyo, tumejikuta tumerudi nyuma. Kwa mfano, katika shule tunazosema kwamba wazazi wachangie chakula, kwa kweli kupitia mashamba hasa kwa shule zile ambazo zina maeneo huko vijijini wangeweza kulima mashamba yao na wakapata chakula, watoto huku wakiwa wanajifunza na wakati huo wanapata chakula.
Kwa hiyo, mimi nitoe rai yangu kwa shule zote kuona kwamba stadi za kazi hasa kulingana na mazingira yetu ni ya muhimu sana nawapongeza sana shule kama sekondari ya Rugambwa, wao wanafanya vizuri sana.(Makofi)
MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Niseme tu majibu ya Serikali yamekuwa ni yale ya ought to be, rather than what is the real situation. Sasa nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, je, Serikali inasema nini pale ambapo watendaji maalum kama DED, DAS, RAS na walimu wanapohamishwa kila baada ya muda mfupi katika Wilaya husika? Na mfano ni Wilaya Mafia ambapo katika miezi michache ma-DED walihamishwa na tukapata wapya kama watatu na hii ilitokana zaidi na jinsi walivyoendesha uchaguzi na kuusimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ufanisi sio tu kutunga sheria za kusimamia, hivi Serikali haioni kwamba masuala kama ya kuhakikisha watumishi wanapata makazi bora, wanalipwa stahiki zao ipasavyo na vilevile wana uhakika wa kuwa na periodic training za ku-upgrade zile nafasi zao ni namna za kujenga ufanisi katika utendaji kazi?Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kuzungumzia alipokuwa anasema kwamba tumejibu tu namna inavyotakiwa kuwa na siyo uhalisia. Sisi tunasimamia Menejimenti nzima ya Utumishi wa Umma na ndiyo maana tunatoa miongozo na taratibu mbalimbali na kuifuatilia. Ndiyo maana nimemueleza utaratibu kwa sababu yeye ameuliza utaratibu na vigezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza kwamba ni kwa nini unakuta watumishi wengine wanahamishwa bila kufuata taratibu. Tumekuwa tukitoa nyaraka mbalimbali za kiutumishi, tumetoa Waraka kwa TAMISEMI mwaka 2006, tumetoa pia Waraka mwaka 2007 kwa Makatibu Tawala wa Mikoa kueleza ni namna gani na masuala gani yanayotakiwa kuzingatiwa wakati wanapohamisha watumishi. Pia katika jibu langu la msingi nimemueleza muuliza swali, lengo kubwa ni kuangalia manufaa ya umma, kuangalia uwiano katika Halmashauri zetu na katika sehemu zetu za kazi na si kwa kumkomesha mtu wala kwa lengo lolote, lakini kubwa zaidi ni kuhakiksha kwamba ikama na bajeti ya fedha imetengwa ili kuhakikisha kwamba mtumishi wa umma hapati usumbufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumuongezea Mheshimiwa Mngwali, hata Mheshimiwa Rais ameweza kutoa msisitizo zaidi tarehe 1 Mei, 2017 wakati wa siku ya wafanyakazi. Maelekezo yamekuwa yakitoka lakini ameweka mkazo kwamba kuanzia sasa hakuna kumhamisha mtumishi yeyote wa umma kama gharama zake za uhamisho hazijatengwa na pia kama hakuna manufaa katika uhamisho huo na hakuna ufanisi wowote ambao unaenda kuongezeka katika kuboresha ikama hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la makazi pamoja na umuhimu wa mafunzo, niseme tu katika Sera ya Menejimenti ya Ajira katika Utumishi wa Umma pamoja na Sera ya Mafunzo, tunatambua umuhimu wa kuwa na mafunzo na watumishi wetu wa umma kuwa na makazi bora. Ndiyo maana kama Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania, Watumishi Housing, Shirika la Nyumba la Taifa, TBA na mashirika mengine tumekuwa tukiweka msisitizo na kuhakikisha kwamba nyumba zinajengwa kwa ajili ya watumishi wetu wa umma.
Vilevile katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wamekuwa mwaka hadi mwaka wakitenga fedha kwa ajili ya kujenga nyumba za watumishi wetu. Lengo kubwa likiwa ni kuwaboreshea watumishi wetu wa umma makazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zaidi ya yote nitoe rai kwa waajiri wetu kuona ni namna gani wanaweza kuweka vivutio mbalimbali ili kuhakikisha kwamba wanavutia watumishi waweze kufanya kazi katika maeneo yao ya kazi. Zaidi katika mafunzo pia ni vema waajiri wakahakikisha kwamba kila mwaka wanatenga bajeti kwa ajili ya kuwapatia mafunzo watumishi wao na kuwaendeleza.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza na ninalo dogo sana. Naomba niseme kwamba Serikali isituambie hapa kama vile inaanza upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu zote hizi za kupandisha vyeo na mengineyo yalikuwepo kabla; lakini sasa hivi kilichotokea kibaya, kuna watu walipandishwa cheo wakalipwa mshahara mpaka miezi mitatu, wakasitishiwa mshahara, wakarejeshwa pale pale. Hivi Mheshimiwa Waziri anatoa kauli gani kuhusu hili? Naomba nijibiwe kwa ufasaha zaidi ili watu waweze kufuatilia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru sana maana ningekosa kupata hili swali, roho ya mama yangu Mheshimiwa Riziki ingepata shida sana kwa sababu nilikuwa namwona hapa, hasa nikijua mama yangu ni Mwalimu, kwa hiyo, alikuwa anataka kujua katika kero hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwambie kwamba; bahati nzuri juzi nilipata viongozi wa Chama cha Walimu kutoka Mkoa wa Rukwa, nilikuwa nao pale ofisini na hiyo ni miongoni mwa concern ambayo waliileta pale ofisini kwetu. Ni kweli kuna watu ambao walipata mishahara ile miezi miwili, lakini baadaye mshahara ukakasitishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa changamoto kubwa ni kwamba kuna wengine wanaenda kustaafu. Sasa wakistaafu jambo hili linafanyika vipi? Leo hii mtu akistaafu atahesabiwa katika mshahara wa mwanzo wakati alipanda. Ndiyo maana nimesema jambo hili, kama Serikali, tumelichukua kwa uzito wa hali ya juu, tunafanya analysis. Kuna watu wengine ambao watastaafu hivi karibuni. Ina maana tusipo-address vizuri tutakuwa na changamoto kubwa katika hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna watu wengine walipanda, lakini kwa sababu ya utaratibu mzuri uliowekwa naomba niwaondoe hofu Waheshimiwa Wabunge, jambo hili tumelichukua sisi kama viongozi na tumelijua ni tatizo kubwa, lazima tuliweke vizuri. Yalifanyika kwa nia njema kwa sababu huko nyuma hali yetu ilikuwa siyo shwari. Suala zima la watumishi hewa lilikuwa ni jambo kubwa, watumishi takriban 19,000 plus, lilikuwa ni tatizo kubwa sana!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mpango huu ulikuwa ni mpango mkakati wa Serikali kusaidia kulinda mapato, lakini kupeleka fedha kwa watu wanaostahili . Kwa hiyo, naomba niwatoe hofu wafanyakazi kwamba kila mtu atapata stahili yake na Serikali inafanya kazi kufanya analysis kwa undani zaidi kuondoa hilo tatizo.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza na ninalo dogo sana. Naomba niseme kwamba Serikali isituambie hapa kama vile inaanza upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu zote hizi za kupandisha vyeo na mengineyo yalikuwepo kabla; lakini sasa hivi kilichotokea kibaya, kuna watu walipandishwa cheo wakalipwa mshahara mpaka miezi mitatu, wakasitishiwa mshahara, wakarejeshwa pale pale. Hivi Mheshimiwa Waziri anatoa kauli gani kuhusu hili? Naomba nijibiwe kwa ufasaha zaidi ili watu waweze kufuatilia. Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru sana maana ningekosa kupata hili swali, roho ya mama yangu Mheshimiwa Riziki ingepata shida sana kwa sababu nilikuwa namwona hapa, hasa nikijua mama yangu ni Mwalimu, kwa hiyo, alikuwa anataka kujua katika kero hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwambie kwamba; bahati nzuri juzi nilipata viongozi wa Chama cha Walimu kutoka Mkoa wa Rukwa, nilikuwa nao pale ofisini na hiyo ni miongoni mwa concern ambayo waliileta pale ofisini kwetu. Ni kweli kuna watu ambao walipata mishahara ile miezi miwili, lakini baadaye mshahara ukakasitishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa changamoto kubwa ni kwamba kuna wengine wanaenda kustaafu. Sasa wakistaafu jambo hili linafanyika vipi? Leo hii mtu akistaafu atahesabiwa katika mshahara wa mwanzo wakati alipanda. Ndiyo maana nimesema jambo hili, kama Serikali, tumelichukua kwa uzito wa hali ya juu, tunafanya analysis. Kuna watu wengine ambao watastaafu hivi karibuni. Ina maana tusipo-address vizuri tutakuwa na changamoto kubwa katika hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna watu wengine walipanda, lakini kwa sababu ya utaratibu mzuri uliowekwa naomba niwaondoe hofu Waheshimiwa Wabunge, jambo hili tumelichukua sisi kama viongozi na tumelijua ni tatizo kubwa, lazima tuliweke vizuri. Yalifanyika kwa nia njema kwa sababu huko nyuma hali yetu ilikuwa siyo shwari. Suala zima la watumishi hewa lilikuwa ni jambo kubwa, watumishi takriban 19,000 plus, lilikuwa ni tatizo kubwa sana!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mpango huu ulikuwa ni mpango mkakati wa Serikali kusaidia kulinda mapato, lakini kupeleka fedha kwa watu wanaostahili . Kwa hiyo, naomba niwatoe hofu wafanyakazi kwamba kila mtu atapata stahili yake na Serikali inafanya kazi kufanya analysis kwa undani zaidi kuondoa hilo tatizo.