Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Salma Mohamed Mwassa (7 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. SALMA M. MWASA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuteuliwa kuwa Mbunge wa Mkoa wa Dar es Salaam. Aidha, napenda kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kupewa ridhaa hii na wananchi pamoja na wewe Mheshimiwa Naibu Spika kuweza kuteuliwa kuwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nichangie hotuba ya Mheshimiwa Rais katika maeneo yafuatayo. Kwanza, napenda kuchangia katika eneo la elimu. Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aliahidi kuboresha elimu katika maeneo mengi na kusema kwamba elimu ni bure. Labda kabla hatujafikia kwenye elimu bure, napenda kufafanua yafuatayo. Mheshimiwa Naibu Spika, kuna matatizo mengi juu ya mpango huu wa elimu bure.
Kwanza, miundombinu ni tatizo. Ni wazi idadi ya wanafunzi inaongezeka kwa kuwa elimu ni bure lakini haiendani na miundiombinu iliyopo katika shule zetu. Kwa mfano, katika Wilaya ya Kinondoni kuna jumla ya wanafunzi wa shule za msingi 152,000 na vyumba vya madarasa 1,500 hivyo tunapata wastani wa wanafunzi 98 kusoma darasa moja. Idadi hii ni kubwa sana na haiendani kabisa na udhahiri wa kauli hii kwamba elimu itaboreshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kwamba upungufu wa madarasa katika Halmashauri ya Kinondoni ni jambo ambalo litadhoofisha suala hili la elimu. Halmashauri ya Kinondoni inahitaji vyumba vya madarasa 3,018 vilivyopo ni 1,656, pungufu ni 1,362. Inahitaji nyumba za
walimu 452 zilizopo ni 280 pungufu ni 172. Ofisi za walimu ni 222 zilizopo ni 104 pungufu ni 118. Vyoo vya walimu vinahitajika 452 vilivyopo ni 280 pungufu ni 172. Vyoo vya wanafunzi vinahitajika 6,338 vilivyopo ni 1,382 pungufu ni 4,956. Maktaba nazo ni tatizo, zinazohitajika ni 1,446 zilizopo ni 32 tu pungufu ni 114. Kwa hali hii, sasa elimu itakuwa bure kama kutakuwa na
mipango thabiti wa kuongeza miundombinu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Rais pamoja na kwamba elimu ni bure lakini aangalie tatizo la miundombinu kwani wanafunzi wengi wanarundikana kwenye darasa moja ambapo haitaleta ufanisi wa kutosha. Tukiangalia kwa mfano jinsia ya kike
inapata shida sana kutokana na upungufu wa vyoo. Tunajua matatizo mengi ya watoto wa kike kwani wanahitaji kutumia vyoo safi. Hivyo basi, tatizo la miundombinu liangaliwe ikiwemo vyoo, madarasa na maktaba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite tena kwenye elimu ya sekondari hasa katika Wilaya ya Kinondoni. Kwa mujibu wa taarifa ya makabidhiano ya Serikali ya Awamu ya Tano Wilaya ina matatizo makubwa. Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ina shule za sekondari 137 tu kati ya
hizo sekondari 48 tu ndizo sekondari za Serikali na 16 ni za mijini na 32 ni za vijijini. Hivyo basi, kuna upungufu wa nyumba za walimu, walimu wengi wanakaa mijini na kufundisha vijijini hali inayosababisha adha kubwa kwa walimu hao kutoka mijini kwenda vijijini na kudhoofisha elimu katika eneo hili la sekondari. Walimu hawa wanaishi kwenye mazingira magumu mno naomba tatizo hili liangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inadhihirishwa katika taarifa hiyo, kati ya mwaka 2011-2014, wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 34,000 lakini waliofanya vizuri ni 11,000 na waliofeli ni 22,000 ambao ni sawa na asilimia 63. Hivyo eneo hili liangaliwe tena katika kuboresha elimu ya watoto wetu ili tuweze kukidhi mahitaji yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu na pia napenda kushukuru Chama changu kwa kunipa jukumu hili kubwa, ni makini chenye maamuzi makini. Vilevile nikushukuru wewe Spika kwa kuliongoza Bunge lako kwa umakini kabisa wa hali ya juu. Nimshukuru Waziri wa Wizara hii mwenye dhamana kubwa na majukumu mengi, hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kuchangia hoja kwa kuishauri Serikali. Kwanza kabisa, naomba nijikite kwenye vifo vya akinamama wajawazito, hili ni tatizo kubwa sana. Akina mama 42 kwa siku ni watu wengi mno, hiyo inatutisha hata sisi wanawake wenyewe katika kutimiza hilo jukumu zito. Maana tunaona sasa uzazi ni probability, kujifungua ni tatizo na linaweza kupelekea maisha yetu kuwa hatarini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri atambue kwamba dhamana aliyopewa, Mheshimiwa Rais hakukosea kumchagua yeye mwanamke makini kwa maana anajua kabisa uchungu huu mzito wa jambo hili. Kwa sababu aliona kabisa Mpango wa Maendeleo ulivyofeli kupunguza hivi vifo vya akinamama ndiyo maana akatafuta mwanamke makini kama Mheshimiwa Waziri. Vilevile hakukosea kumtafuta professional ambaye ni Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla awe Naibu wako. Kwa hiyo, naomba mpambane kweli kweli kwenye hili tatizo la wajawazito, vifo ni vingi sana ukilinganisha na takwimu zilizopo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza tujiulize vifo hivi vinatokana na nini, kuna mambo mengi. Kwanza siyo tu vifaa tiba, wataalam lakini vilevile kuna mambo ya mimba za utotoni. Mimba za utotoni pia ni tatizo kubwa kwa sababu ukienda kujifungua ukiwa chini ya umri wa miaka 18 pia ni tatizo. Kwa hiyo, tuangalie tena tatizo hili kubwa. Pamoja na mikataba mbalimbali mliyoingia lakini vilevile tuliangalie hili tatizo la mimba za utotoni.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile saa nyingine vifo hivi vinatokea kutokana na handling ya wale watumishi wa afya. Nashauri kwamba Waziri aendeshe semina za mara kwa mara kwa watumishi wa afya jinsi ya kuwa-handle hawa wajawazito, wawe na special care kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kupunguza hivi vifo sijaona ikiongelewa mambo ya walemavu. Mwanamke mlemavu pia katika kujifungua anatakiwa umakini wa hali ya juu. Je, tuna hizo labour kwa ajili ya walemavu? Nashauri tuwe na vitanda special kwa ajili ya walemavu na labour special kwa wanawake walemavu kwa ajili ya kujifungua maana hilo pia ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nijikite kwenye ukatili wa kijinsia. Wengi wameongelea juu ya ukatili wa kijinsia na tumeongelea zaidi wanawake na watoto, lakini Wizara hii ni jinsia kwa ujumla. Naomba pia niongelee wanaume kwani nao wanafanyiwa sana ukatili wa kijinsia japo kwa idadi ndogo, lakini wao huwa hawana taratibu zile za kusema. Kiukweli wanaume wengi wanapigwa ila hawawezi kusimama hadharani wakasema kwamba tunapigwa kutokana na hizi sheria zetu za kiafrika, lakini wanapigwa na kufanyiwa mambo mengine mengi. Kwa hiyo, nimesimama pia kuwatetea wanaume pia na wao waangaliwe.
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Spika, naomba pia nijikite kwenye vifaa tiba na dawa pia ni tatizo sana hasa tukiangalia katika zahanati na vituo vya afya. Vituo vya afya kwa kweli ni tatizo havina vifaa tiba kabisa na dawa pia ni tatizo huko kwenye hivyo vituo vya afya. Kwa mfano, kama Jiji la Dar es Salaam Serikali imejitahidi kujenga vituo vya afya na zahanati kwenye kata mbalimbali lakini ni majengo tu hayana vifaa tiba wala wataam. Namwomba Mheshimiwa Waziri katika ziara zake aangalie sana hivi vituo vya afya ili kupunguza msongamano uliopo Muhimbili, Mwananyamala, Temeke na hospitali zote za kikanda kama hizo za Bugando. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongelee huduma za madaktari bingwa. Huduma za madaktari bingwa mara nyingi unazipata kwenye referral hospital lakini huku kwenye vituo vya afya hakuna kabisa huduma za madaktari bingwa. Naona kingekuwepo kitu kama utaratibu maalum angalau daktari bingwa aweze kuzungukia hivi vituo vya afya hata kwa wiki mara moja. Kuwe na ratiba maalum ili mtu akitaka kumwona daktari bingwa basi asifikirie tu Muhimbili, Bugando au KCMC afikirie hata hivi vituo vya afya kwamba atakuja labda Alhamisi. Kwa hiyo, hizi huduma za madaktari bingwa ningeshauri zisambae zaidi kwenye vituo vya afya na zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile katika ukurasa wa 92 wa hotuba, Mheshimiwa Waziri ameongelea maendeleo ya watoto. Watoto katika Taifa letu kwa kweli wana matatizo mengi especially ya kiafya. Naomba katika sera uangalie jinsi ya kuweza kujenga Hospitali za Taifa za Watoto pekee (National Children Hospital) nazo ziwe za awali mpaka referral kwa ajili ya kutibu watoto peke yake. Sambamba na vifo vya wajawazito lakini vifo vya watoto pia bado ni tatizo na tunatakiwa tuangalie kwa umakini sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niongelee Benki ya Wanawake. Benki ya Wanawake nayo ni tatizo kwa sababu iko zaidi mijini lakini hakuna wakala kama ilivyo hizi benki zingine za biashara, mfano Fahari Huduma kwa CRDB. Inatakiwa nayo iwe na huduma zake za kupeleka kwenye kata, mitaa na vijiji ili wanawake wengi wapate huduma za benki hii.
Mheshimiwa Spika, vilevile napenda kuongelea masuala ya utawala bora na hasa Wizara hii. Wizara hii inahudumia afya, wazee, watoto, kwa kweli ni Wizara ambayo ina majukumu mengi mno. Kwanza niwapongeze kweli kweli hawa Mawaziri wenye dhamana na namwomba Mheshimiwa Rais aiangalie tena hii Wizara yaani afya aiweke peke yake na hii jinsia angeiweka peke yake. Naona ameweka majukumu mazito mno halafu tena ukiangalia bajeti yenyewe nayo imeshuka kabisa. Ni vizuri Wizara hii ikajitegemea kwa maana ya Wizara ya Afya na ile jinsia ikawa sehemu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo yote nijikite kwenye kuongelea magonjwa haya yasiyoambukiza kama moyo, kisukari, figo, haya yote yanasababishwa na utaratibu mbaya wa maisha tunayoishi. Kwa hiyo, napenda kuishauri Wizara kwamba, tuwe na siku maalum ya kufanya mazoezi kama ilivyo ya usafi yaani siku hiyo tunafanya mazoezi toka asubuhi hadi jioni ili watu wapate hamasa kwamba tusile na kukaa kwenye magari, tuwe ni watu wa kufanya mazoezi na kuangalia mwenendo mzima wa maisha utakuwaje. Sasa hivi tabia ya mazoezi haipo kabisa, watu wanakula, wanaingia kwenye gari au wanapanda pikipiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongelee vilevile maslahi ya watumishi wa Wizara ya Afya. Watumishi hawa kwa kweli ukiangalia Manesi na Madaktari saa nyingine wanaongea lugha chafu kwa sababu ya maslahi yao. Maana ukiangalia kwa mfano hospitali hizi za private hatuoni kule kama wanajibu hovyo kwa sababu wanalipwa mishahara mikubwa. Kwa hiyo, naomba Wizara pia iangalie maslahi ya hawa watu wa huduma ya afya, semina hizo waandae mara kwa mara na waangalie matatizo yao yanayowasibu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda pia kuongelea majukumu ya Maafisa Maendeleo ya Jamii. Maafisa hawa kwa kweli hawaangaliwi kama ilivyo kada nyingine. Mheshimiwa Waziri nakushauri uwatembelee hao Maafisa Maendeleo ya Jamii na uwaangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uhai na afya njema niweze kuchangia katika Wizara hii na pia napenda kukishukuru chama changu, Chama cha Wananchi CUF kwa kuniamini kunipa majukumu haya mazito. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile napenda kuishauri Serikali, kwanza na-declare interest kwamba mimi nilikuwa mfanyakazi wa ardhi na ni mtaalam wa ardhi pia. Napenda kuishauri Serikali juu ya kupima maeneo ya umma, maeneo ya umma kwa kiasi kikubwa yanavamiwa sana. Maeneo ya umma kama shule, zahanati, maeneo kama ya polisi, majeshi, hasa kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni tatizo kubwa sana, wananchi wanaingilia maeneo haya kwa kasi kubwa sana kwa sababu hayana dermacation, hayana alama yoyote ambayo ya kueleza kwamba, hii shule inaishia hapa, kituo cha polisi kinaishia hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Wizara ifanye mkakati mzito wa kuyatambua haya maeneo ya umma kwamba yawekewe alama mahsusi na yapate hatimiliki kabisa kuepuka migogoro hii ambayo ni mizito. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile niongelee upungufu wa wafanyakazi wa sekta ya ardhi. Kwa kweli wafanyakazi wa sekta ya ardhi ni wachache, yaani wachache mno na Waziri mwenyewe analitambua hilo. Kuna Wilaya nyingi sana hazina hawa wataalam wa ardhi kabisa. Yaani unakuta hizi kazi za ardhi zinafanywa na ma-layman ambao hawana utaalam wowote na hiyo inapelekea kutokuweka mikakati ya Serikali kwamba ukiangalia Chuo Kikuu ya Ardhi ni kimoja mpaka leo, toka mwaka 1961 chuo kikuu ni kimoja! Ma-graduates wanao graduate pale hawatoshi na hata vile vile ukiangalia uajiri, Serikali kuajiri hawa wafanyakazi wa sekta ya ardhi hawaajiri kwa kasi kubwa, bado hao hao wachache, wanaendelea kukaa mitaani miaka mitatu minne mpaka kuja kuajiriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri waweke kipaumbele kwamba hawa watu waajiriwe sana na hivyo vyuo pia viongezeke, ikiwezekana tuwe na vyuo viwili vya ardhi, mpaka vitatu ili kuangalia hili tatizo kubwa la upungufu wa wafanyakazi hawa wa ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kwenye migongano ya kisera, migogoro mingi inatokana pia na migongano ya kisera, kwa mfano unakuta kwamba ile kutoa hatimiliki kwenye eneo moja; labda Jiji linatoa hatimiliki, Halmashauri zinatoa hatimiliki lakini hiyo sasa hivi angalau imerekebishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunaangalia kuna migongano kama hii ya wakazi ya mabondeni. Wale wanawatuhumu kwamba wako mabondeni lakini wana hatimiliki wale, wana zile wanaita leseni za makazi ambao anayesaini ni Assistant Commissioner wa Halmashauri na unakuta zile leseni wamechukulia mikopo. Kwa hiyo, pale wameleta mgongano kati ya mwananchi na benki kwa kwenda kumvunjia lile eneo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna hiyo migongano ya kisera sana kwamba wanatoa zile hati lakini hawaangalii je, tunapotoa kuna uhalali wa kiasi gani? Ile ni hati halali na benki wanaitambua na Wizara wenyewe wanaitambua kwa maana ni Assistant Commissioner wa Halmashauri ndiye amesajili zile hati. Kwa hiyo, huo mgongano wa kisera unafanya kwamba kuleta mgogoro mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile niangalie tena Mabaraza ya Ardhi, Mabaraza haya ya Ardhi kweli yanaisaidia Wizara kwa kiasi cha kutosha lakini hayapo sehemu nyingi, yaani yapo tu kama hizi Halmashauri za mijini, wilaya za mijini lakini huko ukiangalia hizi za pembezoni kabisa haya Mabaraza ya Ardhi hayapo. Vile vile haya Mabaraza ya Ardhi, napenda kwamba waajiriwe wataalam hasa wa kuweza kuishauri Serikali na vile vile waangalie utaratibu mpya kwamba je, tunawezaje kuisimamia hiyo Serikali katika sekta ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nisemee fidia. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri, fidia ni tatizo kubwa hasa katika Jiji la Dar es Salaam, fidia ni tatizo kubwa mno hasa tukiangalia katika miradi ya EPZ. Miradi ya EPZ unakuta uthamini umefanyika miaka 10 iliyopita, lakini mpaka leo wale wananchi bado bado hawajalipwa na zile nyumba zao wamepigwa stop order kila kitu. Sasa mnavyosema kwamba maeneo ya viwanda lazima yawepo, watafanyaje hiyo kazi ya kuweka miradi ya EPZ bila kumlipa mtu fidia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri yaani afanye hiyo survey kubwa kwenye hawa watu ambao hawajalipwa fidia, kwa sababu sheria inasema kwamba fidia iwe full, fair and prompt lakini hiyo haifuatiliwi kabisa. Ndani ya miezi sita iwe imeshalipwa, lakini hamna mtu anayefuatilia na mgogoro mkubwa unakuwa kwenye hilo tatizo la fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisemee pia juu ya land rent intention, Mheshimiwa Waziri tukichukua kwa mfano Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam, Wizara wanapeleka tu ile 30 percent kama uwakala wa wale wanaokusanya lakini hawapeleki yaani 30 percent ya viwanja vyote kwa mfano wale walipa kodi wakubwa wanalipia Wizara ya Ardhi, hawaji kabisa kwenye Halmashauri. Sasa wanaporudisha ile 30 percent wanarudisha zile za uwakala tu ambazo Halmashauri wamekusanya, hawarudishi zile zote ambazo zinazostahili, kwa mfano, Halmashauri ya Kinondoni wairudishie majengo yote na viwanja vyote kwamba land rent yenu ni hii hapa mnayotakiwa kupata, sio tu waseme kwamba zile za uwakala tu ndiyo warudishe. Temeke wafanye hivyo hivyo na Ilala wafanye hivyo hivyo kwenye viwanja vyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu vile vile niombe Mheshimiwa Waziri akija kuhitimisha atupe zile takwimu kwamba je, maana yake kwenye ukurasa wa 11 kwenye hotuba yake alisema kwamba bilioni nne amezirudisha kama land rent intention kwenye Halmashauri. Naomba atupe takwimu kwa sababu, najua kabisa yaani hizo asilimia kubwa hazirudi kama inavyostahili. Inawezekana kuna upungufu fulani wa hizi taarifa. Kwa hiyo, naomba akija kuhitimisha atuletee hizo takwimu alizokuwa amepeleka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile niongelee land bank. Mheshimiwa Waziri hawezi kufanya kazi bila kutenga maeneo wezeshi, lazimaauwe na maeneo ya ardhi hifadhi ambayo hata kama akija mwekezaji wasiende kumgombanisha kwa kumwambia tu nenda kule kijijini utaikuta ardhi au Wizara yenyewe inatoa tu mamlaka kwamba shamba hili hapa. Vile vile wamewapa mamlaka wale wanakijiji halafu vile vile wanaenda wanampeleka mwekezaji, hiyo migongano inatokea kutokana na kutokuwa na hiyo land bank, lakini ukiwa na land bank kama Wizara wanasema kabisa nenda sehemu fulani kawekeze hivi na hivi na wanampa hatimiliki wakisimamiwa na hiyo TIC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile naomba niongelee mradi wa Kigamboni City. Kwa kweli ule mradi ni tatizo na unaweza ukawa ni jipu!
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai, lakini vilevile naomba nichangie Wizara hii muhimu ambayo inagusa maisha ya Watanzania kwa kiasi kikubwa hasa wanawake na watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nichangie kuhusu upungufu wa maji Jijini Dar es Salaam. Pamoja na jitihada za Serikali za kupanua Mtambo wa Ruvu chini na Ruvu juu lakini bado Jiji la Dar es Salaam lina uhaba mkubwa wa maji. Ninyi wenyewe Waheshimiwa Wabunge asilimia 90 ni Wakazi wa Dar es Salaam; nafikiri ninapoongea hilo, mnanielewa vizuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uhaba mkubwa wa maji na maji kuwa bidhaa adimu hasa katika maeneo ya pembezoni kama maeneo ya Makabe, Maramba Mawili, Msigani, Kiluvya, Kibamba, Msakuzi, Mabwepande, Bunju na mengineyo ya pembezoni. Yaani maji katika maeneo hayo ni bidhaa adimu mno! Lita 1,000 zinauzwa kati ya 20,000 mpaka 30,000 kwa ujazo wa tank la lita 1,000. Sasa mwananchi huyo ukipiga hesabu kwa mwezi anatumia kiasi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atuambie huu mradi ambao alisema kwenye hotuba yake katika ukurasa wa 69 kwamba utagharimu Dola za Marekani milioni 32; atuambie utaanza lini na utakamilika lini? Kwa sababu Wananchi wa Dar es Salaam jamani wanateseka kwa kiasi kikubwa. Hivi mkoa mkubwa kama ule, maana yake unapoongelea Tanzania unaongelea Dar es Salaam; mpaka leo miaka 54 ya Uhuru kuongelea uhaba wa maji, kwa kweli ni tatizo kubwa na siyo vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niongelee kuhusu upotevu wa maji. Upotevu wa maji katika Jiji la Dar es Salaam ni mkubwa mno kutokana na uchakavu wa miundombinu. Mabomba mengi yamechakaa, sasa Mheshimiwa Waziri anaposema upanuzi wa huu mtambo wa Ruvu Chini na Juu, obvious utaleta maji mengi sana Dar es Salaam lakini hujatuambia ukarabati mkubwa utakuwaje nao, kwa sababu siku ambayo ni ya maji Dar es Salaam, ni mafuriko. Barabara zote zinaharibika kutokana na uvujaji wa haya mabomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kabisa huu ukarabati wa miundombinu ufanyike kwa haraka. Vile vile ni wazi kwamba, ongezeko la maji safi kutokana na mradi huu mkubwa wa maji utaendana kabisa na wingi wa maji taka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri aangalie miundombinu ya majitaka, kwa sababu majitaka ni tatizo Dar es Salaam. Yaani kila unapopita ni mafuriko hasa katika maeneo ya Tandale, Hananasifu, Kinondoni, Tandika, huko ni hatari! Ndiyo inasababisha mlipuko wa magonjwa kama kipindupindu mara kwa mara. Mfumo wa Majitaka kwa kweli Dar es Salaam ni tatizo, naomba aliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nijikite kwenye suala la maji mashuleni. Uhaba wa maji mashuleni katika Mkoa wa Dar es Salaam pia ni tatizo. Wanafunzi wetu wanahangaika mno, hasa shule za msingi, hawana maji kabisa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aangalie kama kuna uwezekano wa kuwatengenezea mfumo wa maji ya mvua kabla ya hii miradi ya kusambaza maji haijafika mashuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, haya maeneo ya pembezoni niliyotaja hapo mwanzo, mashuleni watoto hata maji ya kunywa hawana. Kwa hiyo, naomba kabla ya kuangalia hiyo miradi mikubwa ya kusambaza maji, lakini Mheshimiwa Waziri angeangalia mradi mbadala wa kuvuna yale maji ya mvua waweze kujengewa ma-tank, watoto waweze kunywa maji, wawe kwenye mazingira yaliyo sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nikiangalia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, kuna Taasisi za Serikali kuwa wadaiwa sugu. Wanadaiwa karibu shilingi bilioni 29, hili ni tatizo. Ukiangalia, siyo wananchi tu ambao hawalipi; hizi Taasisi za Serikali ndiyo zilitakiwa zioneshe mfano mzuri. Sasa Mheshimiwa Waziri wanamwangusha, kwa sababu kama anawapelekea maji halafu hawapili, yeye atafanyaje kazi? Naomba hii iwe mfano kabisa kwamba sisi kwanza tulipe, hizi Taasisi za Serikali ziwe mfano wa kulipa maji ili tunapokwenda kwa mwananchi, tunapomwambia kwamba lazima ulipe maji, sasa na yeye asiwe na mfano kwamba mbona Taasisi za Serikali hazilipi maji? Itakuwaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kabisa Mheshimiwa Waziri afuatilie, waweze kumlipa, la sivyo watamwangusha na ataitwa mzigo, kumbe wao wenyewe ndio wanaomwangusha. Ahakikishe madeni yao yote yamelipwa vizuri. Wasipolipa, aweke zile mita zake kama za Luku; lipa maji kadri utumiavyo. Kwa nini wamwangushe, anawapa tu maji mpaka wanamaliza, bado yeye hajalipwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile niongelee tena kuhusu upungufu wa hawa wataalam wa maji. Kwa kweli wataalam wa maji ni wachache na ndiyo maana hata elimu ya maji mbadala inakuwa ngumu. Kwa hiyo, naomba kabisa, Wizara hii iajiri wataalam wa maji kwa kiasi kikubwa. Wataalam wa maji wangeweza kwenda kule maeneo ya pembezoni wakawafundisha hata jinsi ya kuchimba visima, wakaelimisha watu njia mbadala za kupata maji kabla pale ambapo yale maji ya Serikali bado hayajafika. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aangalie kabisa ni kiasi gani atapata hii…
MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii lakini vilevile nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na mimi niweze kuchangia ripoti hii ya Kamati hii ya Bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nijielekeze kwenye ukusanyaji hafifu wa mapato. Kwa kiasi kikubwa kabisa ukiangalia kwenye taarifa hii ya Kamati imeonesha kwamba ukusanyaji hafifu wa mapato umeathiri bajeti kwa kiasi kikubwa. Tuangalie kwa mfano kodi ya majengo kwenda TRA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukusanyaji hafifu wa mapato kwanza unasababishwa kwa kiasi kikubwa na Serikali Kuu kuingilia hizi Halmashauri zetu au Serikali ya Mitaa hata kwenye vyanzo vyao wanavyovibuni na kuviona kwamba sasa vinakua badala ya kuwapa moyo zaidi na kuwasimamia katika sera wanavipora vile vyanzo kama kodi ya majengo na kuvipeleka Serikali Kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam, Kinondoni, Temeke, Ubungo zilikuwa zinafanya vizuri sana katika kodi hii ya majengo na ndiyo uti wa mgongo wa Halmashauri zetu lakini leo imepelekwa TRA hakuna hata mia iliyokusanywa. Wakati mwaka jana ukiangalia takwimu kwa mfano Manispaa ya Kinondoni imekusanya zaidi ya shilingi bilioni tisa kwa mwaka na ilikuwa ina uwezo wa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 800 mpaka shilingi bilioni moja kwa mwezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuna miezi nane toka kodi hii ihame kutoka kwenye Halmashauri kwenda TRA, TRA haijaleta hata senti tano kwenye Halmashauri. Unategemea huo utekelezaji wa bajeti utafanyika kwa kiasi gani wakati Serikali Kuu ndiyo chanzo cha kuvuruga hizi kodi badala ya kuzisimamia. Miaka miwili tu iliyopita kodi hii ilikuwa kwenye Halmashauri na ilikuwa ina perform vizuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi, kodi hii ni kodi ya local, inatakiwa ikusanywe kule kwenye local level na sio kodi ya central level hii. Ukiipeleka kodi ya majengo kwenye central level unaharibu mpango mzima kwa sababu kodi hii inatakiwa ikusanywe kwenye mitaa. Kwa hiyo, napenda kuishauri Serikali ingeandaa mfumo mzuri kuzisimamia Halmashauri ili kwamba wale Wahasibu wa Halmashauri waende kwenye mitaa na zile mashine za EFD wakusanye ile kodi ya majengo kutoka kule kwenye local level sio kwenye central level huku kwenye TRA ambayo kwanza akienda tu pale mwananchi wa kawaida anaulizwa, una TIN, majina yako matatu, sijui mfumo wa nini, yaani TRA kwa kifupi haina uwezo mzuri wa kukusanya kodi ya majengo kama ilivyokuwa kwa Halmashauri, tume-prove failure kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano sasa hivi ni miezi nane, miezi nane unajipanga vipi? Unajipanga mwezi wa kwanza, mwezi wa pili, wa tatu, mpaka miezi nane hujakusanya hata senti tano? Wakati Halmashauri yenyewe ilikuwa ina uwezo wa kukusanya kati ya shilingi milioni 800 mpaka shilingi bilioni moja kwa mwezi, wewe unajipanga nini? Wamechukua ma-valuer wa Halmashauri kuwapeleka TRA, wamechukua mifumo kutoka kwenye Halmashauri, majengo mengi kwa asilimia kubwa yamethaminiwa, kwa nini mpaka sasa hivi hawakusanyi, ina maana wameshindwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Bunge lako Tukufu lisimamie hii kodi irudi tena kwenye Halmashauri. Halmashauri zinakufa! Hii kodi ndiyo uti wa mgongo wa Halmashauri, Halmashauri zime-paralyze kwa sasa, hazina chochote kutokana na kuwanyang‟anya hii kodi yao na hiki ndiyo chanzo kikubwa cha mapato. OC zao kwa asilimia kubwa zilikuwa zinatoka kwenye kodi ya majengo. Kwa hiyo, naomba kabisa kwa miezi hii minane itoshe kutathmini kwamba TRA ni kama imefeli kukusanya kodi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nijielekeze kwenye kukopa zaidi ndani. Naishauri Serikali kwamba, ni vizuri tukatoka sasa kwenye wigo huu wa kutegemea mikopo ya ndani na tukaangalia kujenga mahusiano zaidi nje. Kukopa zaidi ndani, tuwaachie hawa sekta binafsi, lakini sisi kama Serikali tupunguze kukopa zaidi ndani, tukope nje ili tupate wigo wa kupata fedha za kigeni na kuja kuzisambaza ndani na uchumi uendelee kukua. Sisi kama Serikali ambao tuna uwezo wa kukopa nje kirahisi, tukiendelea kukopa ndani: Je, mwananchi mdogo atakakopa wapi? Kwa hiyo, tutaendelea kuudumaza uchumi wetu na hatutaweza kufikia lile lengo tulilojiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niende kwenye mada ya ukuaji wa uchumi kutokumfikia mwananchi wa kawaida. Kwenye ukurasa wa saba ripoti ya Kamati ime-quote kabisa, “pato la mwananchi wa kawaida bado ni dogo sana na asilimia kubwa ya wananchi wetu wanaishi kwa kipato cha chini ya dola moja za Kimarekani.” Nimemsikia Mbunge mmoja hapa anakana kabisa, hivi kweli sisi tunaotegemewa na watoto, sijui na akina nani, hivi kweli tungekuwa tunaishi kwa dola moja tungeweza? Kwa hiyo, ina maana unapingana na ripoti ya Kamati? Sijamwelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaishi chini ya dola moja kwa siku kwa sababu tu, sisi kwa ujamaa tuliojengewa toka huko nyuma na Hayati Mwalimu Nyerere kwamba huyu mwingine akiwa hiki, tunasambaziana; lakini ni ukweli kabisa tunaishi chini ya dola. Usibishe! Mheshimiwa Mbunge wewe tu kwa sababu tu maisha yako yako vizuri, uko hapa, lakini wananchi huko nje wanateseka. Sasa sisi tunaona tu uchumi unakua, unakuaje? Mbona hatuoni kwenye maisha halisi ya Mtanzania kwamba uchumi unakua! Sasa hizi taarifa tunazoambiwa kwamba uchumi unakua, unakua wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokukua kwa uchumi kwenye level ya chini inasababishwa na Halmashauri zetu zinaposhindwa kusambaza ule utajiri chini ya wananchi wake kutokana na kuingiliwa, mara hivi; wakiendelea kukusanya vitu vyao, wanaingiliwa, mara hivi. Kwa sababu huwezi ukawa Serikali Kuu kule juu ukapata maisha ya Mtanzania halisi. Maisha ya Mtanzania halisi yanapatikana huku chini kwenye Halmashauri. Kwa hiyo, Halmashauri zipewe uwezo, zitungiwe sera. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kikubwa cha kufanya, Serikali Kuu isimamie sera za kwenye Halmashauri. Siyo kuona kama, sasa hivi Halmashauri zime-perform kwa kiasi kikubwa kwenye chanzo hiki, inapora. Badala ya kubuni vyanzo vyao, wao wanatafuta tu kwamba chanzo hiki ipore iende kupeleka Serikali Kuu. Hii siyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye hoja ya wahisani kutokuleta pesa kwa wakati. Kwanza tujiulize, kwa nini wahisani washindwe kupeleka pesa kwa wakati kipindi hiki? Kama Serikali tufanye tathmini kwa nini mpaka leo wameleta tu asilimia 16 na wakati ilitakiwa walete 36? Kwa hiyo, tujiulize ni nini hasa? Kama wao walikuwa marafiki zetu wa karibu tu, lakini leo hawana hata sababu na ripoti ya Kamati inasema, hata wao hawakuambiwa sababu ni nini. Yaani hawana sababu zinazokwamisha. Sasa kwa nini hamna sababu? Inawezekana sababu zimejificha huko kwa ndani, lakini hamzisemi. Nadhani tujitathmini upya. Je, tuna mazingira rafiki na wenzetu? Kwa sababu sisi tumejifungia hapa kisiwa. Hatusafiri kwenda ku-interact huko nje, wafanyakazi wa Serikali wamekuwa blocked, hawaendi huko nje. Sasa hao wahisani, huo urafiki tunaujenga wapi?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli kwenda kuomba kwa mwenzako si lazima kwanza uende wakuone ndio uende kuomba! Unaomba ukiwa hapa, utaweza? Hawa wahisani tujenge mazingira mazuri kule, internationally. Sisi Wabunge tusafiri tuka-interact kule, ili tukienda kule kwa Wabunge wenzetu, tunawaambia jamani sisi bwana wenzenu twafa huku. Hivi na hivi tuambieni. Eeeh, sisi hatuna huku hivi na hivi! Mahusiano Kimataifa ni madogo. Serikali hii ya Awamu ya Tano ijitafakari upya, tutoke. Wabunge wenyewe hapa hatusafiri; sasa kama hatusafiri tutaendaje kuomba kwa wenzetu? Utaomba vipi wewe usaidiwe huku wakati huendi kule kwa mwenzako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo, tuangalie tena kwa nini hii misaada imekuwa midogo? Tutoke tuanzie na Mheshimiwa Rais, atoke; sisi wenyewe Waheshimiwa Wabunge tutoke, wafanyakazi wa Serikali watoke, wote; yaani isiwe ile kubana bana sijui kitu gani. Tutoke huko tukaombe! Sisi hatuwezi kujitegemea wenyewe hapa! Eeeh, tutoke, Mawaziri wenyewe watoke vilevile wakaangalie hata wenzao kule wanafanya nini kwenye Wizara zile. Tokeni hii misaada tuipate tena. Mbona mwanzoni huko ilikuwepo! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru kweli Mheshimiwa Rais Kikwete, alikuwa anatoka sana. Mbona mambo yalikuwa sawa! Eeh, tutoke. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye mambo ya ukame kuhusu chakula. Nakumbuka kabisa kwenye ndani ya Bunge lako hili, kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walilalamika kwamba mazao ya chakula yanaoza, hapa hapa ndani ya Bunge hili. Sikumbuki ni kikao kipi lakini akiwemo Mheshimiwa Keissy alikuwa analalamika kabisa; mazao yanaoza, hayanunuliwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii NFRA haipewi fedha za kutosha kununua chakula cha kuhifadhi na ndiyo maana leo Waziri wa Chakula anasema Halmashauri 55 zina upungufu wa chakula lakini hazina njaa; hivi hiyo si ni lugha tu! Yaani upungufu wa chakula na njaa, maana yake nini? Eti hazina njaa, lakini zina upungufu wa chakula. Sasa ndiyo nini? Mimi sijaelewa hapo, labda niombe kufafanuliwa zaidi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kabisa Serikali, sasa hivi tuendelee kuambiana ukweli kwamba hii mamlaka hii tumeiunda wenyewe, ipewe hela za kutosha inunue. Kama mahindi yapo Kibaigwa, basi yapelekwe Songea, yasambazwe kwenye magodauni yao ya mikoa ili hili janga la ukame na njaa lionekane kama linaweza kuepukwa, tujikidhi kwa mahitaji ya chakula kilichopo. Kwa mfano, kama hivi matetemeko, ingeku…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na uhai. Vilevile napenda kukishukuru chama changu kwa kunipa nafasi ya kuendelea kuwepo katika Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nielekeze mchango wangu kwenye Wizara hii ya TAMISEMI. Wizara hii kwa kweli ndiyo nchi, ndiyo inayoangalia Taifa zima la Tanzania hasa kwa upande huu wa Bara. Kwanza kabisa, nijielekeze kwenye mpango mzima wa elimu. Katika hotuba ya Waziri wa TAMISEMI, ukurasa wa 23 unaongelea miundombinu. Kwa kweli bado miundombinu katika elimu yetu siyo mizuri kwani upungufu wa miundombinu ni mkubwa sana. Kwanza nijielekeze kwenye upungufu wa vyoo.
Niliangalia kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri aliongelea kuhusu upungufu wa matundu ya vyoo kwa kweli bado ni tatizo kubwa. Sasa kama mpaka sasa hivi tunaongelea upungufu wa matundu 517,600 kwa ujumla wake lakini nikiangalia kabisa upungufu huu 50% upo katika Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na mlundikano mkubwa wa wanafunzi. Vilevile upungufu huu wa vyoo unafanya wanafunzi wetu kwanza wasome in uncomfortable way halafu vilevile unasababisha magonjwa makubwa hasa UTI.
Sasa hivi ratio kwa Mkoa wa Dar es Salaam kwenye tundu moja inaenda kati ya wanafunzi 80 - 100 wanatumia tundu moja la choo katika shule zetu za msimngi. Sasa nijiulize, haya magonjwa kama ya UTI hasa kwa upande wa wanafunzi wa kike yataisha? Hayawezi kwisha. Tunatumia gharama kubwa sana za matibabu ya UTI na kusababisha watoto kutokusoma kabisa.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile niende kwenye vyumba vya madarasa, nako kuna upungufu wa takribani 200,000 na kwenye nyumba za walimu 182,000. Takwimu hizi bado ni kubwa sana, vyumba vya madarasa kwa sasa yaani ni issue. Huu mpango wa elimu bure umesababisha darasa moja sasa liwe na wanafunzi kati ya 200 - 400 hasa kwenye Mkoa wa Dar es Salaam. Mimi naomba kabisa Serikali ije na mkakati wa kupunguza huu uhaba wa madarasa hasa kwenye Mkoa wa Dar es Salaam na Tanzania nzima kwa ujumla, yaani itueleze kabisa itafanyaje? Kama haiwezekani basi Halmashauri zipewe uwezo yaani kusimamiwa ili zikope zianze utaratibu huu wa kujenga vyumba vya madarasa kama ilivyokuwa kwenye madawati. Madawati tumeona kabisa sasa hivi yameenda vizuri mpaka Bunge lenyewe
limechangia madawati, basi sasa sera ya madarasa na matundu ya vyoo ianze upya, tuendelee kabisa kusema kwamba, sasa hivi katika kila wilaya na mkoa lazima huu upungufu wa vyoo na vyumba vya madarasa uishe.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile niongelee uhaba wa walimu. Uhaba wa walimu bado ni tatizo hasa walimu wa hesabu na sayansi kwa ujumla. Kulikuwa na ile programu ya walimu kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma, imeingiliwa, ikavurugwa vurugwa, hatuelewi walimu wale wanamaliza
lini au wataajiriwa lini au itakuwaje. Kwa hiyo, uhaba wa walimu pia ni tatizo hasa katika upande wa masomo haya ya sayansi na hisabati.
Mheshimiwa Spika, nije kwenye masuala ya afya niongelee suala la kujenga Hospitali za Wilaya hasa kwenye wilaya hizi mpya. Kwanza tukiangalia kwenye Mkoa wa Dar es Salaam kuna tatizo kubwa la mlundikano wa wagonjwa hasa kwenye Hospitali za Mwananyamala, Ilala na Amana.
Kuna hizi Wilaya mpya za Kigamboni na Ubungo ambazo mpaka sasa hazina hii huduma kabisa ya Hospitali ya Wilaya. Naomba Waziri wakati anapokuja kuhitimisha atueleze atajenga lini Hospitali za Wilaya kwenye hizi Wilaya mpya ikiwemo Ubungo na Kigamboni ziwe au zilizopo zipandishwe mfano Hospitali ya Mbezi. Vilevile Hospitali za Ilala, Temeke, Mwananyamala zimepandishwa kwenda kwenye hadhi ya mkoa sasa Hospitali za Wilaya ziko wapi? Kwa hiyo, namuomba Waziri katika vipaumbele vyake kuwe na Hospitali za Wilaya kila wilaya na ziwe na vifaa vyote muhimu vya afya ikiwemo magari ya wagonjwa, labor zinazoeleweka, vifaa vya kujifungulia ili huduma za afya ziwe sahihi kabisa.
Mheshimiwa Spika, nije katika ujenzi wa majengo ya ofisi katika wilaya. Bado ofisi za wilaya hazina ule mwonekano wa majengo ya Wilaya hasa kwa wilaya mpya. Hivi inakuwaje unaigawa Wilaya halafu unaenda kukodi jengo kwenye majengo ya mtu binafsi? Basi hayo majengo
ya watu binafsi yangekuwa angalau yana nafasi kubwa lakini sivyo. Sasa sasa hivi wilaya hizi zimekuwa kama kitu cha ajabu, hazina majengo yanayoeleweka hasa Wilaya mpya mfano Kigamboni au Ubungo. Unakuta chumba cha 10 kwa 10 kina idara zaidi ya tatu mpaka tano. Mkuu wa Idara yuko humo humo, wafanyakazi wa kawaida wako humo humo kwenye hicho chumba yaani ni vurumai hata mafaili huwezi
kujua yanakaa wapi. Kwa hiyo, mimi naomba kabisa hasa kwenye hizi Wilaya mpya, kwa mfano Wilaya ya Ubungo na Kigamboni, Waziri anapokuja kuhitimishia atueleze majengo haya yatajengwa lini na kama anaendelea kukodi atakodi kwa muda gani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa niongelee maslahi ya watumshi. Kwa kweli maslahi ya watumishi katika ngazi ya utumishi wa umma kwa kweli bado ni tatizo. Mishahara ni midogo, mmeendelea kupunguza posho, zingine mmeziondoa kabisa, stahiki kwa viongozi pia hazieleweki.
Mnasema kwamba mnakuja kuleta uwiano wa mishahara kwa kuangalia ile mikubwa na kima cha chini, lakini sasa mbona huu mshahara wa kima cha chini hauangaliwi kabisa? Kwa muda mrefu mshahara wa kima cha chini umekuwa mdogo sana. Wafanyakazi wa umma sasa
imekuwa taabu yaani wanafanya kazi kwa mshahara mdogo, hawapandishwi madaraja yaani totally wamekuwa confused, wamekata tamaa hata ya kuwa watumishi wa umma. Madaraja yao hawapandishwi mnasema sasa hivi kwanza tunahakiki, lakini kuhakiki kunazuia mtu kupanda daraja? Inakuwaje mtu miaka mitatu hupandi daraja?
Mheshimiwa Spika, mimi mwenyewe hapa ni-declare interest nilikuwa mtumishi wa umma, nimekaa miaka karibu mitatu sijapandishwa. Naomba suala hili liangaliwe upya. Mtu mpandishe cheo kutokana na elimu yake na anavyoweza kufanya kazi. Bila kumpandisha madaraja hii motive ya kufanya kazi mtu ataipata wapi?
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile pia tuangalie mishahara yao bado ni midogo mno. Halafu posho zao nyingi mmezikata yaani hazieleweki. Kama mnakata posho basi muangalie ule uwezekano na maisha halisi ya mtumishi wa umma inakuwaje.
Mheshimiwa Spika, vilevile kumekuwa na mlundikano wa kazi kwenye ofisi hizi za umma kutokana na kutoajiri watu. Vijana wamejaa huko mtaani hawaajiriwi na kazi zimerundikana huku. Hawa watu mmewaondolea hata posho za mazingira magumu lakini mlundikano wa kazi
umezidi kwenye ofisi za umma kwa idara zote hasa Halmashauri yaani unakuta kazi ya watu 10 anafanya mtu mmoja. Vilevile overtime, extra-duty allowance, zote zimeondolewa huyu mtu anafanyaje kazi? Kwa hiyo, naomba kabisa muangalie tena suala hili.
Mheshimiwa Spika,
nakushukuru.