Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Salma Mohamed Mwassa (5 total)

MHE. SALMA M. MWASSA aliuliza:-
Miongoni mwa changamoto zinazokwamisha kuleta tija katika ukusanyaji wa kodi kwenye Halmashauri zetu ni pamoja na ubutu wa Sheria Ndogo Ndogo (By laws):-
Je, ni lini sheria hizo zitarekebishwa ili zilete tija katika ukusanyaji kodi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Mohamed Mwassa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria Ndogo katika Halmashauri zinatungwa chini ya Sura Namba 290 ya Sheria za Fedha za Serikali za Mitaa ambayo imewekwa sharti la faini isiyozidi shilingi 50,000/= na kifungo kisichozidi miezi mitatu au miezi sita au vyote kwa pamoja kutegemea na aina ya kosa ambalo mtu amefanya. Hivyo, kukosa umadhubuti kwa sheria ndogo hizi ni kutokana na masharti yaliyomo katika Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa inayotumika kwa sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) imeandaa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura Namba 290 ambayo yatawasilishwa hapa Bungeni ili Bunge lako liweze kuijadili na kuridhia. Lengo letu siyo kuwaumiza wananchi, bali kuongeza umadhubuti wa Sheria za Serikali za Mitaa na hatimaye kuzipa makali Sheria Ndogo za Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kukuza mapato ya Halmashauri.
MHE. SALMA M. MWASSA aliuliza:-
Kumekuwa na Migogoro mingi ya ardhi mjini na vijijini inayotokana na kutopima na kupanga matumizi bora ya ardhi:-
(a) Je, Serikali imejipangaje kupunguza au kumaliza migogoro ya ardhi?
(b) Je, lini Serikali itaandaa mipango Kabambe (Master plans) mijini na vijijini lili kuainisha matumizi bora ya ardhi na kuondoa migogoro ya ardhi nchini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Mohamed Mwassa, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Salma Mohamed Mwassa, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b), napenda kutoa maelezo mafupi ya vyanzo vya migogoro kama ifuatavyo:-
Utwaaji wa ardhi bila fidia stahiki; taasisi za umma na binafsi kuwa na maeneo au mashamba makubwa bila kuyaendeleza na kuyalinda; utata wa mipaka kati ya vijiji na wilaya pamoja na hifadhi; uvamizi wa viwanja na mashamba; kutokuwepo kwa mipango ya matumizi ya ardhi;ongezeko kubwa la idadi ya watu na shughuli mijini na vijijini katika ardhi ile ile na kutoheshimu sheria na mipango ya matumizi ya ardhi na shughuli za makundi ya watu wengine kama vile wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kupunguza na kutatua migogoro ya ardhi, Wizara imekuwa ikitekeleza mambo yafuatayo:-
(i) Kuandaa kitabu cha orodha ya migogoro ya Nchi nzima kinachoainisha vyanzo vyake ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa;
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI:
(ii) Kuwasiliana na Wizara zinazohusika na kilimo, mifugo na uvuvi; maliasili na utalii pamoja na TAMISEMI ili kutatua migogoro mtambuka;
(iii) Kuandaa matumizi ya ardhi katika vijiji na miji ambako migogoro ya ardhi imekuwa ikijitokeza na kusambaza miongozo inayohusu sera na sheria za ardhi;
(iv) Halmashauri zote nchini zimeelekezwa kuainisha viwanja na mashamba yasiyoendelezwa ipasavyo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa;
(v) Kuimarisha mfumo wa ki-electronic katika kutunza kumbukumbu;
(vi) Kuimarisha ofisi za kanda ili kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi;
(vii) Kuanzisha Mfuko wa Fidia ya Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utayarishaji wa mipango kabambe ya miji, Wizara imekuwa ikitekeleza mambo yafuatayo:-
(i) Kuunda na kukamilisha program ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi Tanzania itakayotekelezwa katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2015 mpaka 2025;
(ii) Wizara inasaidiana na Halmashauri za Wilaya na miji 18 kwenye program ya Urban Local Government Supporting Program katika utayarishaji wa mipango kabambe; na
(iii) Kujadiliana na Benki ya Dunia ili kuharakisha zoezi la utayarishaji wa mipango kabambe katika miji mingine 30 ya Tanzania bara.
MHE. SALMA M. MWASSA aliuliza:-
Je, ni nini umuhimu wa kuwa na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya katika nchi hii?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 78 la Mheshimiwa Salma Mohamed Mwassa, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya hapa nchini yanaundwa na kusimamiwa na kifungu cha 22 cha Sheria ya Mahakama ya Ardhi Namba 2 ya mwaka 2002.
Mheshimiwa Spika, umuhimu wa kipekee wa Mabaraza haya ni suala zima la utatuzi wa migogoro yote itokanayo na matumizi ya ardhi nchini kwa karibu zaidi ukilinganisha na vyombo vingine vya kutatua migogoro. Hivyo, Mabaraza haya yana umuhimu mkubwa sana katika kuleta amani na muafaka katika maeneo mengi yenye migogoro ya watumiaji wa ardhi nchini.
Mheshimiwa Spika, umuhimu mwingine ni kutatua migogoro yote ya ardhi kwa haraka na kwa njia rafiki na shirikishi kwa kuwa Mabaraza haya yako karibu na wananchi wa eneo husika.
Mheshimiwa Spika, umuhimu huu umejidhihirisha katika utendaji wake. Kati ya Oktoba, 2004 mpaka kufikia Oktoba, 2016 jumla ya mashauri 131,470 yalipokelewa na kati yake mashauri 100,744 yameamuliwa na mashauri 32,176 bado yanaendelea.
MHE. SALMA M. MWASSA aliuliza:-
Je, ni nini umuhimu wa kurasimisha ardhi kwenye maeneo ambayo hayajapimwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Mohamed Mwassa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, urasimishaji wa ardhi maana yake ni kutambua miliki za wananchi kwenye maeneo yaliyoendelezwa bila kupimwa kisheria. Matokeo ya urasimishaji ni kutoa hatimiliki na kuweka miundombinu ya msingi kama vile barabara, maji, mifereji ya maji ya mvua na
ikiwezekana kuweka majina ya mitaa. Kwa kawaida, urasimishaji ni zoezi shirikishi limalowezesha wananchi kukubaliana mipaka ya viwanja, kufungua njia na kutoa maeneo ya huduma za jamii kama vile shule, vituo vidogo vya polisi, makaburi, zahanati na maeneo ya wazi.
Mheshimiwa Spika, umuhimu wa kurasimisha maeneo haya ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, la kwanza, urasimishaji unatoa fursa kwa wananchi kutumia ardhi kupitia nyaraka za umiliki wa ardhi kama vile hati, kuweka dhamana ya mikopo katika taasisi za fedha, mahakama.
Mheshimiwa Spika, la pili ni kuongeza thamani ya ardhi au nyumba husika (value addition) iwe kwa kuweka dhamana (collateral) rehani, upangishaji na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, tatu ni kuboresha makazi hususan kwa kuweka miundombinu ya msingi ili kurahisisha usafiri, kupunguza madhara yatokanayo na majanga mbalimbali kama vile mafuriko na moto. Kwa upana wake urasimishaji ni dhana inayochangia kupunguza umaskini.
Mheshimiwa Spika, nne ni kutoa uhakika wa milki ya ardhi na hivyo kuwa kivutio kwa mazingira ya uwekezaji. Kwa mfano, maeneo mengi ambayo yamerasimishwa, kumekuwa na uwekezaji wa shughuli za kiuchumi kama vile mahoteli, maduka, shule, hospital na maeneo ya burudani na kadhalika Mheshimiwa Spika, tano vilevile ni kupunguza migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kuwa, urasimishaji si jibu la kudumu la kuzuia ujenzi holela mijini bali ni utayarishaji wa mipango kabambe ya miji yetu ambayo ikienda sambamba na uimarishaji wa usimamizi na uthibiti wa uendelezaji miji itaweka ustawi mzuri wa mandhari ya nchi yetu na hivyo kufanya nchi yetu kuwa sehemu nzuri ya kuishi.
MHE. SALMA M. MWASSA aliuliza:-
Kumekuwa na mrundikano wa wagonjwa kwenye Hospitali za Mwananyamala, Temeke na Amana:-
Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya mpya katika Mkoa wa Dar es Salaam.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Mohamed Mwassa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni, Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 10 katika Kata ya Somangila kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali kubwa ya Wilaya ya Kigamboni. Ujenzi wa Hospitali hiyo unatarajiwa kufanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali ya Morocco. Kwa sasa Serikali inaendelea na mazungumzo na Serikali ya Morocco ili kuanza ujenzi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali inaendelea kuboresha Zahanati na vituo vya afya vilivyopo ambapo katika bajeti ya mwaka 2017/2018 zimetengwa shilingi milioni 557.3 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba pamoja na ujenzi wa vituo vya afya na zahanati.