Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Salma Mohamed Mwassa (9 total)

MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini nina swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na mazoea ya kuchelewa kurekebishwa kwa sheria hizi ndogo ndogo na Serikali Kuu na badala yake kwa zile Halmashauri ambazo zinajitahidi zenyewe hasa zikiwemo za mijini, zinakuwa zinanyang’anywa mamlaka yake na Serikali Kuu. Kwa mfano, Kodi ya Majengo (Property Tax) kupelekwa TRA na tume-prove kwa miaka miwili ya nyuma TRA ilishindwa kabisa kukusanywa kodi hii; na sasa tunaambiwa kodi hii inaenda tena TRA. Je, ni lini hasa Serikali Kuu itaacha kuingilia mamlaka au kunyang’anya mamlaka ya Serikali za Mitaa ili ziweze kujitegema?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wakati mwingine Marekebisho ya Sheria yanachelewa lakini mara nyingi sana yanafanyika mara baada ya mahitaji mahususi yanapotokea. Kwa sababu tuelewe kwanza katika suala zima la Serikali za Mitaa kuna maeneo matatu; kuna Sura Namba 287, 288 na 290. Sura ya 290 ndiyo inalenga hasa katika ukusanywaji wa kodi na ushuru mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ajenda ya kusema kwamba ni lini sasa Serikali itaanza kuzuia suala zima la kunyang’anya mamlaka ya Serikali za Mitaa, kutoa kodi kwa mfano katika kodi ya majengo; Serikali sasa hivi tuko katika Serikali ya Awamu ya Tano, naamini Bunge hili ndiyo Bunge ambalo mara ya kwanza tunajadili bajeti yetu katika kipindi hiki cha Awamu ya Tano na ninaamini kwamba mjadala huu wa bajeti utakapofika katika suala zima la Wizara ya Fedha, mwisho katika Wizara ya Fedha kuna ile Sheria ya Fedha ya mwisho pale ndio tutapata way forward tunapokwenda ni wapi. Lengo kubwa la Serikali ni kuhakikisha mapato yanakusanywa katika Serikali yake ili mradi mambo yaweze kuendelea vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwahiyo, nina imani tutakapofika katika suala zima la Sheria ya Kodi ambayo mwisho wa siku Waziri wa Fedha ata-table hapa mezani, tutakuwa tumefika mahali muafaka na kupewa maelekezo ya kutosha nini tunataka tufanye. Lengo kubwa ni kwamba Serikali iweze kukusanya kodi ya kutosha na miradi ya maendeleo iweze kufanikiwa.
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Pia nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kuna migogoro ambayo hasa inatokana na tatizo la usimamizi mbovu wa sera. Kwa mfano, kuna matatizo yanayotokana na hawa Viongozi wa Serikali za Mitaa kuuza maeneo ya umma kama shule, zahanati, majeshi na hiyo inatokana na kwamba Serikali haijaweka zile demarcation au kutoa hati miliki katika maeneo hayo, kwa hiyo, hicho ni chanzo cha migogoro. Je, ni lini Serikali itapima haya maeneo ya umma ili kuondoa migogoro hii hasa kwa Jiji la Dar es Salaam?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, fidia ni tatizo pia, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba wanaanzisha Mfuko wa Fidia. Kuanzisha Mfuko wa Fidia tu sio suluhu ya mgogoro. Mgogoro wa fidia unatokana hasa na yule mlipaji kutokuwa na hela stahiki wakati anafanya uthamini. Je, ni lini sasa Serikali itasimamia kabla ya schedule ya kwenda kuthaminiwa na Mthamini Mkuu wa Serikali yule mlipaji wa fidia awe tayari ameshaweka hizo hela kwenye Mfuko wa Fidia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ameulizia suala la tatizo la watu kuvamia maeneo ya Taasisi. Hata kabla ya upimaji ambao unatakiwa kufanyika kwa nchi nzima, Wizara ilishaelekeza kwa halmashauri zote kuhakikisha kwamba, maeneo yote ya umma yaweze kupimwa na hii inafanyika katika Halmashauri zenyewe husika kwa sababu ni maeneo ambayo wako nayo na wanayatambua katika maeneo yao. Kwa hiyo, haya hayasubiri ule upimaji wa Kitaifa ambao unaendelea kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotakiwa ni Halmashauri zenyewe ziweze kulinda maeneo yake na kama hiyo haitoshi, tumekwishaanza zoezi kwa Dar es Salaam ambapo Wenyeviti wa maeneo husika wamepewa ramani za maeneo yao kuweza kutambua maeneo yapi ya wazi, yapi ya umma na yapi ambayo yanatakiwa kuangaliwa ili yasiweze kuvamiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwakumbushie tu kupitia katika swali la Mheshimiwa Mwassa, halmashauri zote zihakikishe kazi ya upimaji maeneo yanayomilikiwa na Taasisi mbalimbali ifanyike ili kuepusha migogoro ambayo inaendelea kutokea siku hadi siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ameongelea suala la fidia, nadhani tulishalijibu katika hotuba wakati tunazungumzia na bado nitaendelea kulijibu tu. Ni kwamba, Mfuko wa Fidia umewekwa pale ili kuweza kukaa tayari katika kupitia yale masuala ambayo yatakuwa yana migogoro ambayo haijatatuliwa katika ukamilifu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata h ivyo, Wizara kazi yake siyo kulipa fidia katika maeneo ambayo yanatwaliwa na Wawekezaji au na watu binafsi katika maeneo hayo. Ni jukumu lao kuona kwamba analipa fidia, Wizara imetoa maelekezo, haitaweza kupitisha uthamini wowote utakaoletwa, yale majedwali yatakayoletwa, kabla ya kujiridhisha kwamba kuna pesa ambayo imeshatengwa na ndiyo maana Mfuko huu utakuwa na bodi yake ambayo itafanya kazi zake katika kuhakikisha pia wanajiridhisha na kile ambacho Wizara imeelekeza kabla ya fidia kulipwa au kabla ya watu kuondolewa katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishawaelekeza kama Wizara, hakuna mtu kuondolewa katika eneo lake kabla hajalipwa fidia. Kwa hiyo, hilo ni lazima lizingatiwe kwa wale wanaokuwa na mawazo ya kutwaa ardhi za watu.
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Spika ahsante. Pamoja na majibu ya kuleta matumaini ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika Sheria hii ya Mabaraza ya Ardhi inasema kwamba; Baraza la Ardhi la Wilaya lisiongelee kesi inayozidi au kiwanja kinachozidi thamani ya shilingi milioni 50, na Baraza la Nyumba la Kata lisiongelee kiwanja au nyumba inayozidi shilingi milioni tatu.
Meshimiwa Spika, kwa mikoa kama Dar es Salaam, Mwanza, maeneo yoye ya mijini Nyumba nyingi zimezidi thamani ya shilingi milioni 50. Sasa kutokana na sheria hii kutokukidhi matakwa halisi ya mwenendo wa thamani ya ardhi iliyopo mijini kwa sasa, ni lini sheria hii itarekebishwa au iletwe hapa Bungeni irekebishwe au ifanyiwe amendment ili iendane na hali halisi ya sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, migogoro mingi ya ardhi ya ardhi nchini inasababishwa na ardhi kutopimwa na kumilikishwa kwa ufasaha, na hii inasababishwa na gharama kubwa na mlundikano wa kodi ya umilikaji wa ardhi kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano kodi ya premium katika umilikaji wa ardhi ambayo ni asilimia 7.5 ni kubwa mno kwa sasa, ni lini kodi hii itashushwa au itafutwa ili kuwaletea tija wananchi au kuwapunguzia mzigo wananchi katika kupata haki yao hii ya kumiliki ardhi kwa sasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza anazungumzia sheria kutokidhi kwa mana ya kwamba viwango vilivyopo kwa sasa na hasa mijini ukiangalia kwa Mabaraza ya ardhi kiwango chake ni shilingi milioni 50 lakini nyumba nyingi zimezidi.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu haya masuala yanakwenda kisheria, na kama hitaji linaonekana kwamba sheria imepitwa na wakati nadhani ni wakati muafaka pengine wa kuweza kupitia upya na kuweza kuangalia kwasababu kadri siku zinavyokwenda ndivyo jinsi na majengo yana-appreciate value zake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili ni wazi kweli anavyolisema limepitwa na wakati, lakini bado pale inapoonekana kwamba viwango, au kiwango cha kesi husika kinazidi Mamlaka ya Baraza husika kesi hiyo huwa inapelekwa kwenye mahakama ya juu. Kwa hiyo bado linaweza kufanyika wakati bado tunasubiri kubadilisha sheria hii.
Mheshimiwa Spika, suala la pili ni suala la viwango. Tukumbuke katika bajeti nadhani ya mwaka 2015/2016 kiwango cha premium kilishuka kutoka asilimia 15 kwenda kwenye asilimia 7.5. Sasa tuna miaka kama miwili tu toka hii imeanza kutumika na bado inaonekana ni kubwa. Lakini tukumbuke pia kwamba viwango vingi vya ardhi ambavyo vilikuwepo vilishushwa ikiwepo hata ile ya upimaji wa ardhi kwa kiwanja kutoka shilingi 800,000 kwenda shilingi 300,000. Kwa hiyo, haya yote ni mapitio yanayofanyika kulingana na muda jinsi ulivyo.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu hili nalo bado linaonekana ni tatizo siwezi kuahidi hapa ni lini tutaleta sheria hiyo kwa sababu ndiyo kwanza imeanza. Lakini tutazidi kufanya utafiti wa kina na kuweza kujua kama kweli ni kikwazo kikubwa tuweze kuona namna gani tutapitia tena viwango vyetu ili wananchi ambao tunategemea wanufaika wa ardhi hii ambayo sehemu kubwa haijapimwa waweze kunufaika na kupata ardhi zao na kuweza kupata hati ili waweze kufanya shughuli zingine za maendeleo.
MHE. SALMA M. MWASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kumekuwa na utaratibu wa vituo vya polisi vidogo (police post) hasa kwa Mkoa wa Dar es Salaam kufungwa saa kumi na mbili hii inasababisha matukio mengi ya uhalifu hasa yanatokea usiku. Je, Serikali haioni inahatarisha usalama wa wananchi hasa Mkoa wa Dar es Salaam wenye wakazi zaidi ya milioni tano?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa PGO kuna vituo vya polisi vya aina tatu; kuna Class A, Class B na Class C. Kwa hiyo, vituo vya Class C kwa kawaida havifunguliwi zaidi ya saa 12. Sasa sina hakika Mheshimiwa Mbunge kituo ambacho anakizungumzia ni kituo kiko katika class gani labda pengine baada ya hapo tuone kama kitakuwa kipo katika nje ya class ambayo inapaswa kifungwe zaidi ya hapo na kinafungwa basi tutachukua hatua tuone nini kinafanyika tufanye uchunguzi tujue tatizo ni nini. Lakini nadhani kulijibu moja kwa moja swali lako kwasababu hajaainisha kituo chenyewe ni kituo gani kwa wakati huu itakuwa ni vigumu.
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante
kwa kuniona. Sheria ya Fidia inasema kwamba watu walipwe ndani ya miezi sita, lakini katika Jiji la Dar es Salaam kwa sasa kuna uwekaji wa alama za X kwenye nyumba za wananchi usioeleweka na alama hizo zinawekwa hazina muda maalum hasa kwenye nyumba ambazo zipo pembezoni mwa barabara na maeneo mengine katika Jiji la Dar es Salaam. Unakuta alama ya X imewekwa miaka mitano, mitatu au sita; yule mwananchi haelewi hii alama ya X inakuwaje? Naomba niiulize Serikali, ni kwa nini alama ya X inapowekwa yule mtu asilipwe fidia ndani ya miezi sita awe ameshalipwa na kuondoka katika eneo lile? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ni wazi Sheria ya Ardhi kifungu namba 13(2) na (3) kinaelezea mtu unapotaka kuchukua eneo fidia ilipwe ndani ya miezi sita na kama hukulipwa ndani ya miezi sita basi kuna hali halisi ya kuweza tena kuchaji gharama hiyo kulingana na rate iliyopo katika financial institution kwa kipindi hicho. Hata hivyo, hii imekuwa haifanyiki kutokana pengine na wachukua ardhi wenyewe kutokuwa tayari kufanya ile kazi kwa wakati. Hii tumeisemea na tumeipigia kelele na ndiyo maana kukaja na ile Sheria ya Uthamini ambayo tumeifanya hapa; ambayo inazungumzia suala la baada ya miaka miwili kama mtu hajaweza kulipa fidia ule uthamini uliofanyika mwanzoni wote unakuwa umefutika. Hii ilikuwa imefanyika hivyo mwanzoni kwa sababu ile sheria ilikuwa inaachia mtu anaweza akaenda miaka 10 mpaka 20 hajalipa.
Mheshimiwa Spika, sasa tunasema baada ya kupitisha ile sheria hivi sasa ndani ya kipindi kilichotajwa lazima fidia ile ilipwe na hakuna kuchukua ardhi ya mtu kama hujalipa fidia, hili kila siku tunalirudia. Tunasema kuanzia sasa, kwa sababu wananchi wengi wameteseka katika masuala ya ulipaji fidia. Hakuna kuchukua ardhi ya mtu kama mwekezaji au yeyote anayechukua ardhi ile hajaweza kulipa fidia kwa gharama iliyopo katika soko baada ya kuwa imefanyiwa uthamini kwa kipindi hicho. Vinginevyo wananchi tunasema wasitoe maeneo yao kama hawajathibitishiwa katika kutoa eneo lile.
Mheshimiwa Spika, suala lingine katika hilo hilo, kuna shughuli zingine ambazo zinafanyika za kiserikali ambazo ukiing’ang’ania ile ardhi unakuwa umekwamisha mambo mengine. Sisi ndani ya Serikali tunajipanga vizuri kuona kwamba yale maeneo ambayo yanatumika kwa ajili ya manufaa ya umma tutayafanyia utaratibu wa haraka na mapema ili wananchi wale wasiweze kulalamika.
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kutokupandisha madaraja kwa wakati, kutolipa na stahili za wafanyakazi kwa wakati na kufuta posho mbalimbali kumefanya ufanisi wa wafanyakazi kushuka. Je, Serikali ina mpango gani katika hilo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 13 Juni, 2016, tulitoa Waraka wa Utumishi kupitia kwa Katibu Mkuu tukitoa maelekezo mbalimbali. Lengo kubwa la Waraka huo tulikuwa na mazoezi mawili; zoezi la kwanza ni kupitia upya muundo wetu wa Serikali pamoja taasisi zetu kuhakikisha kwamba tuna muundo wenye ufanisi lakini zaidi kuhakikisha kwamba tuna muundo ambao unahimilika. Kama mnavyofahamu tumepunguza idadi ya Wizara kutoka 26 mpaka sasa tunazo 18 au 19.
Kwa hiyo, ni lazima pia na ni dhahiri kwamba baadhi ya taasisi ambazo zitakuwa na muingiliano wa majukumu nyingine itabidi ziweze kuunganishwa, lakini vilevile baadhi ya Idara na baadhi ya Vitengo vingine pia itabidi viweze kuunganishwa kuhakikisha kuwa tunaenda na wakati na tunaendana na mabadiliko.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kutokana na Waraka huo huo tuliahirisha zoezi la kupandisha madaraja pamoja na kupandisha watu vyeo. Napenda kumtoa hofu Mheshimiwa Mbunge kuanzia mwaka ujao wa fedha tutapandisha madaraja zaidi ya watumishi 193,166 na hakuna atakayepoteza haki yake.
MHE. SALMA M. MWASA: Ahsante Mheshimiwa Naibu Spika, naomba urekebisa kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza swali langu lilikuwa ni Hospitali za Wilaya za Ubungo na Kigamboni, lakini hapa naona limekuja la Kigamboni peke yake. Sasa maswali yangu ya nyongeza ni mawili. La kwanza, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya kwenye Wilaya mpya ya Ubungo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, ni lini Serikali tena itapandisha hadhi kituo cha afya cha Mbezi? Kama huu mchakato wa kujenga Hospitali ya Wilaya utachukua muda basi ipandishe Hospitali ya Mbezi iwe Hospitali ya Wilaya.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli na tunafahamu hizi Kigamboni pamoja na Ubungo ni Wilaya mpya, zimezaliwa kutoka katika Wilaya mama ya Temeke na Wilaya Kinondoni, tukifahamu kwamba Wilaya ya Ubungo ina changamoto hiyo. Kwa hiyo, jambo la msingi ni kwamba, kwa sababu tumegawanyika si muda mrefu sasa niombe Baraza la Madiwani la Ubungo pamoja na timu yote ya Management wafanye utaratibu wa kuandaa hii mipango ya ujenzi wa hospitali mpya ya Ubungo na sisi Serikali katika nafasi yetu tutafanya kila liwezekanalo ili kuhakikisha kwamba eneo la Ubungo linakuwa na hospitali yake kwa sababu tunajua kwamba population ya watu wa Ubungo ni kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kupandisha hadhi kituo cha Mbezi kwa hivi sasa kiweze kutumika, kikubwa zaidi nimuagize Mkurugenzi pamoja na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ubungo kwamba kama wakiona kinatosha waanze kuhakikisha tunaanza harakati za kwanza kukiwezesha kituo hiki kama tulivyofanya kituo cha Vijibweni pale Kigamboni. Tukifanya hivi tutaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwasihi hasa Mkurugenzi na DMO wetu, waweze kufanya harakati za haraka na kufanya analysis ya kutosha nini kinaweza kufanyika pale ili kuweza kuongeza tija katika Sekta ya Afya katika wilaya ambayo Mheshimiwa Mbunge anaipigania sana.
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza naishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa urasimishaji, lakini naomba itekeleze kwa vitendo.
Mheshimiwa Spika, ili kupunguza migogoro ya ardhi suluhisho muhimu ni kupima, kupanga na kurasimisha na si
vinginevyo. Kumekuwa na miradi ya urasimishaji, kwa mfano mradi unaondelea sasa hivi katika Jiji la Dar es Salaam Kimara, mradi ule ni kama umetelekezwa. Wafanyakazi wale hawana hela za kwenda site, hawana mafuta na wala hawana vitendea kazi vyovyote katika.
Mheshimiwa Spika, kama hivi ndivyo sasa tuone kwamba kurasimisha inakuwa ni sehemu ya kufanya thamani
za ardhi zile kupanda hasa katika Jiji la Dar es Salaam ambako squatter sasa hivi katika Jiji la hilo ni tatizo kubwa.
Watu wanajenga hovyo, mji unachafuka, haupangwi inavyostahili.
Mheshimiwa Spika, sasa huu mradi uliokuwa pilot area kwa ajili ya Dar es Salaam ambao sasa ungeweza
kufanya huko kwenye mikoa mingine. Sasa ni kwa nini Serikali haipeleki fedha kwenye mradi ule na kutoutelekeza kama ilivyo sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali namba la pili, katika miradi ile ya MKURABITA kwenye urasimishaji huo huo, wananchi
walilipa fedha zao huko huko Kimara, wamelipa kati ya shilingi 400,000 mpaka 800,000. Wananchi wale bado wana zile risiti, sasa je, napenda Wizara inahakikishie ni lini hizo hela zitarudishwa kwa wananchi au kuwarasimishia ili waweze kuondokana na hiyo sintofahamu?
Mheshimiwa Spika, je, ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuongozana na mimi kwenda katika hiyo ofisi ya mradi hapo Kimara tuangalie hayo matatizo na mimi kama mtaalamu nimshauri?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mwassa kwa kufuatilia, lakini vilevile Mheshimiwa Mwassa ni mmoja wa Wajumbe wa Kamati yetu ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Amekuwa ni mstari wa mbele katika shughuli hizi na pia ni mwanataaluma hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba kwa maswali yake mawili aliyoyauliza habari ya kutopeleka fedha
katika mradi wa Kimara si kweli. Naomba nisema zoezi la urasimishaji linaloendelea Kimara halijakwama kwa ajili ya pesa, limekwama kwa ajili ya wananchi wengine kutotoa ushirikiano; na hii inatakiwa pia Halmashauri zote kule ambako zoezi hili linafanyika tuwasihi wananchi wetu watoe ushirikiano.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu suala la urasimishaji si la mtaalamu kwenda pale na kuamua nini kifanyike.
Anapokwenda katika eneo la mradi ni lazima ashirikishe viongozi waliopo lakini pia wale ambao wanapaka katika
yale maeneo yanayofanyiwa urasimishaji. Ikitokea mmojawapo akagoma au akakataa kukubaliana na kile
ambacho kinafanyika zoezi haliwezi kuendelea. Kwa hiyo, mimi niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge tuwasihi
wananchi wetu kwa sababu zoezi hili lina manufaa kwao na kwa nchi pia.
Mheshimiwa Spika, swali la pili amezungumzia habari ya MKURABITA, kuhusu habari ya kurudishiwa pesa.
Mheshimiwa Spika, miradi yote iliyoanzishwa na MKURABITA bado inaendelea kufanyika na hii ni kwa sababu
tu, kumekuwa na miradi mingi ambayo inaendelea katika maeneo ambapo baadaye MKURABITA walisimama
wenyewe, ikiwepo na ile Kusini, walisimama hawakuendelea na hilo zoezi kutokana na tatizo kama hilo hilo la mwanzo ambalo nimelizungumzia.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa wale waliolipa pesa zao hakuna atakayedhulumiwa na wote tutawatambua. Kwa
hiyo mimi naomba kama unayo orodha, kwa sababu pale ofisini kwetu hatujawa na orodha, hatujaletewa malalamiko hayo kwa maandishi na kujua kwamba kuna watu wamechangia lakini hawajapewa huduma hiyo. Kwa hiyo mimi nitamwomba Mheshimiwa Mbunge alete orodha hiyo, na Waheshimiwa Wabunge wengine kama kwao kuna watu wenye madai hayo wayalete na ofisi itakuwa tayari kuyashughulikia.
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam bado ni mkubwa sana, hasa kwenye maeneo ambayo hayana miundombinu ya maji. Miradi ile mikubwa ya maji imeainishwa kwamba itatekelezwa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa Serikali itatekeleza miradi hiyo ya maji ipasavyo ili wananchi hao wa Mkoa wa Dar es Salaam waweze kupata maji kwa uhakika na umakini, hasa kwenye maeneo ya Makabe, Goba, Msigani na maeneo yote ya Gongo la Mboto? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kama tulivyotoa taarifa katika Bunge hili, tumekamilisha miradi miwili mikubwa, Ruvu Juu na Ruvu Chini. Ruvu Chini inatoa lita milioni 270 kwa siku, Ruvu Juu inatoa lita milioni 196 kwa siku, pia mwezi huu tunakamilisha vile visima 20 Mpera na Kimbiji ambavyo vitatoa lita milioni 260 kwa siku. Kwa hiyo huduma ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam na sehemu ya Pwani itakuwa ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko changamoto ya kupeleka miundombinu, kwa sasa hivi tumesaini mkataba mmoja wa bilioni 32 ya kuweka mtandao wa maji pamoja na kuongeza matenki ya kuhifadhi maji kupeleka kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tumeshafanya mipango tayari, tunahitaji dola milioni 100 ili tuweze kuhakikisha kwamba tunakamilisha usambazaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam. Tunaendelea baada ya muda ambao siyo mrefu sana tutaona kwamba vijiji vyote, maeneo yote, mitaa yote ya Dar es Salaam inapata maji safi na salama, kwa sababu maji yapo kilichobaki ni kusambaza.