Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Saumu Heri Sakala (16 total)

MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, sasa Waziri anaweza kukubaliana nami kwamba kuna uhaba mkubwa wa elimu juu ya suala la sheria hizi na kwamba muda umefika sasa Serikali iweze kutilia mkazo juu ya kutoa elimu hii kwa wafanyakazi pamoja na waajiri?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, mpaka sasa Serikali imekwishashughulikia waajiri wangapi ambao kwa namna moja au nyingine wamewabagua wafanyakazi ambao tayari wamejiunga katika Vyama vya Wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la kwanza la elimu juu ya Sheria za Kazi, Wizara yetu imeendelea kutoa elimu hiyo kupitia Vyama vya Wafanyakazi, pia kupitia makongamano na warsha na semina mbalimbali, kuweza kuwaelimisha wafanyakazi, waajiri na umma kwa ujumla namna ambavyo sheria zetu zinaelekeza mambo gani yatiliwe mkazo. Hata hivyo, tunaendelea kutilia mkazo eneo hili na tutakuwa na vipindi tofauti kupitia katika redio na televisheni ili Umma wa Watanzania uweze kufahamu namna gani sheria hizi zinafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue wito huu kuwaomba wenzetu wa Vyama vya Wafanyakazi kwa kushirikiana na Wizara, tufanye kazi hii kwa pamoja ili tuweze kuwaelimisha waajiri na wafanyakazi sheria za kazi zinavyoelekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika sehemu ya pili ya swali lake, amezungumzia kuhusu idadi ya waajiri wangapi tumekwishawashughulikia ambao wamewabagua wafanyakazi. Ofisi yetu kupitia Maafisa Kazi ambao wamekuwa wakifanya kaguzi mara kwa mara, wamekuwa wakipita maeneo tofauti kubaini matatizo haya na kuwachukulia hatua wale waajiri ambao wanashindwa kutii masharti ya sheria, hasa hii Sheria Na. 6 ya Mwaka 2004.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana ya idadi, nitamtafuta Mheshimiwa Mbunge nimpatie taarifa kamili ni kwa namna gani tumewashughulikia hao waajiri waliowabagua wafanyakazi wao specifically, lakini tumekuwa tukifanya kaguzi hizi na tunayo orodha ya waajiri wengi tu ambao wameshindwa ku-comply na orders zetu ambazo zimefanyika baada ya ukaguzi.
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Anaitwa Mussa Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kutambua umuhimu wa barabara hii ambayo ina kivutio cha pakee ambacho imeunganika na mbuga pamoja na bahari. Je, Serikali kwa kuendelea kuchelewa kuitengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami, haioni kuwa inapoteza mapato mengi ya kiutalii kutokana na kivutio hiki? (Makofi)
Swali la pili, Wakazi wa Wilaya ya Pangani ambao wako pembezoni mwa barabara ile wamewekewa alama ya “X” nyumba zao, lakini bado wanaendelea kuishi na hawajui ni lini watalipwa fidia zao ili waendelee na maisha yao sehemu nyingine.
Je, Serikali ipo tayari kutoa ahadi kwamba ni lini itawalipa wakazi hawa fidia zao? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano inapotoa ahadi inatekeleza; barabara hii imeanza kufanyiwa usanifu na itakapokamilika maadam tumeshaona mtu anayetoa fedha tayari amepatikana kwa vyovyote vile ujenzi utafanyika kwa haraka itakavyowezekana ili mapato haya ya kitalii yaanze kuingia katika Mfuko wa Hazina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali la pili, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, hizo alama za “X” anazoziona ndiyo sehemu ya utaratibu wa kufanya fidia. Ni hatua ya kwanza, baada ya hapo wanamalizia hatua inayofuata na mara utaratibu wa kufanya uthamini utakapokamilika suala la ulipaji wa fidia litashughulikiwa.
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Suala hili la wazee kulipwa pensheni kila siku limekuwa likitajwa, lakini nashangaa kidogo nikisikia bado hata hayo maandalizi hayajaanza. Je, Serikali inaweza kusema nini kinakwamisha maandalizi hayo ambayo mpaka sasa hayajaanza na kwa kutambua umuhimu huo wa wazee?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, maandalizi hayo yataanza lini na yatamalizika lini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Saumu Heri Sakala, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza limeuliza ni nini kinakwamisha. Kwanza kabisa nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ina dhamira njema kabisa ya kuhakikisha inatekeleza ahadi yake ya kuwalipa pensheni wazee kwa kutambua mchango mkubwa ambao wazee wameutoa katika Taifa hili katika sekta za huduma za jamii, kiuchumi na kisiasa. Kwa hiyo, Serikali inatambua kabisa umuhimu wa wazee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kinachokwamisha hapa si kwamba kuna jambo ambalo linakwama, lakini mipango ya Serikali ilikuwa kwanza kuhakikisha inatengeneza miundombinu ambayo ndiyo itakwenda kulifanya jambo hili liwe endelevu. Kwa hiyo, katika uratibu wa zoezi zima, awali ilikuwa ni kutayarisha mpango rasmi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mpango huu unaanza kufanyiwa kazi na tayari mpango huu umekamilika zimebaki hatua chache tu za kuona ni namna gani mpango huu utaanza sasa kutekelezwa pale ambapo mamlaka husika zitahusishwa na fedha zitakuwa zimepatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ameuliza ni lini itaanza. Nirudie tu katika jibu langu la msingi kwamba zoezi hili ni kubwa sana ambalo linahitaji umakini mkubwa sana na lengo la Serikali ni kulifanya kuwa endelevu. Hata katika baadhi ya nchi ambazo wamefanya zoezi hili kwanza kabisa walifanya namna ambavyo ilikuwa inawapa picha waanzaje ndiyo baadaye waje walikamilishe kwa uzito wake. Kwa hiyo, na sisi kwa kutambua kwamba jambo hili ni kubwa na linahitaji rasilimali fedha, Serikali imeanza kwanza na ujenzi wa miundombinu ya kuratibu zoezi zima ili baadaye kuweza kuwafikia wazee hawa kwa maana ya kuwalipa pensheni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufuatilia jambo hili tulikwenda kujifunza katika baadhi ya nchi ambazo zimefanikiwa sana. Ukienda kule Nepal ambao ni kati ya watu waliofanikiwa, wana kitu wanakiita Nepal’s Senior Citizens’ Allowance na wenyewe walianza katika utaratibu huu huu. Walianza kwanza kuwalipa wazee kuanzia umri wa miaka 60 lakini baadaye wakaona namna gani waweze kuingiza na makundi mengine. Kwa hiyo, na sisi tunatafakari mpango huu mzima lengo letu ni kuufanya mpango huu uwe endelevu.
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa tatizo la barabara lipo nchi nzima na katika Jimbo letu la Pangani pia tatizo hili la uharibifu wa barabara limekuwa ni sugu. Licha tu ya barabara inayounganisha Wilaya ya Pangani na mikoa mingine kuwa mbovu, lakini pia barabara zinazounganisha vijiji na vijiji zimekuwa mbovu kiasi ambacho kipindi cha mvua hazipitiki kabisa. Je, Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha barabara zile zinapitika kipindi chote cha mwaka?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu itahakikisha ubora wa hizi barabara unaongezwa na unaimarishwa na tutaweka mipango maalum kuhakikisha magari makubwa ambayo mara nyingi ndiyo yanayoharibu barabara hizi hayataruhusiwa kupita katika barabara ambazo haziruhusu kupita magari yenye kiwango fulani cha tonnage.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, barabara hii anayoiongelea iko katika Ilani yetu na tutaendelea kuiimarisha na nichukue fursa hii kuwaomba au kuwaelekeza TANROADS, Mkoa wa Tanga kuhakikisha kwamba, kama ambavyo tuliwapa maelekezo kufungua barabara zingine na hii wahakikishe inafunguliwa na maeneo hayo yote yaliyoharibika yatengenezwe.
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Matatizo ya ukosefu wa Zahanati na Vituo vya Afya yapo kila sehemu. Jimbo la Pangani ni moja kati ya Majimbo ambayo yana Kituo cha Afya kimoja tu, lakini kituo chenyewe pia hakina wahudumu wa kutosha, hakina vifaa vya kutosha. Je, Serikali ina mpango gani, kuhakikisha Kituo kile cha Afya kinaboreshwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama sikosei amesema Pangani na bahati nzuri nilifika Pangani pale na kuona mahitaji, japokuwa sikwenda katika zoezi la kufanya assessment ya Sekta ya Afya. Bahati nzuri Mbunge wa Pangani ndugu yangu pale alikuwa kila siku ananikorofisha katika hili; na nikijua kwamba watu wa Pangani wana changamoto hii, kwa hiyo, naomba nikiri wazi kwamba, lengo letu kubwa ni kwamba, kwa watu wa Pangani siyo afya peke yake, Jimbo la Pangani ukiangalia lina changamoto kubwa hata ya miundombinu yake ya barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa pamoja mimi nitakwenda na Waheshimiwa Wabunge huko, tutashirikiana kwa pamoja kubaini sasa nini tutafanya kwa pamoja? Kwa sababu jambo hili lazima tushirikiane kwa pamoja, lazima tubaini pamoja, halafu tuweke vipaumbele. Ndiyo maana jana nilimwita mtaalam wangu pale TAMISEMI aniandikie special proposal, lengo langu ni kwamba, mwakani inawezekana tukaja na sura nyingine hasa kutatua tatizo la afya. Nikawaambia waandike proposal maalum tutafanyaje kutatua tatizo la Zahanati na Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya, kama special project ya five years kuangalia tutafanya vipi, tuje na mtazamo mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukisema kwamba tunatenga Halmashauri peke yake, lakini centrally kama Ofisi ya Rais (TAMISEMI), tunafanyaje kuhakikisha ili tunakuwa na global program ya kupambana kwenye suala la afya katika Tanzania yetu hii. Kwa hiyo ,Mheshimiwa Mbunge nimelichukua hilo suala, tutapanga kwa pamoja kuona ni jinsi gani tutafanya ili mradi kuboresha maisha ya wananchi.
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali la kuuliza.
Katika Kijiji cha Ushongo kilichopo Wilaya ya Pangani, wakazi wake wamejitahidi kujenga jengo la zahanati kadri ya walivyoweza hadi kufikia kiwango cha lenta, lakini kulikuwa na ahadi kuwa Serikali itamalizia jengo hilo pamoja na kuleta huduma muhimu ikiwemo wahudumu pamoja na dawa, mpaka sasa Serikali bado haijatimiza ahadi hiyo ikiwa ni takriban miaka mitatu sasa. Sasa Serikali itatimiza lini ahadi yake hiyo, hasa ukizingatia kijiji hicho hakina huduma ya usafiri wa umma? Wanatumia boda boda na gari za kukodi. Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tumesikia suala hili, ndiyo maana hapa katikati tulizungumza kwamba tunafanya tathmini ya maeneo yote kwa majengo ambayo yamejengwa hayajakamilika na katika upande wa zahanati, tuna takribani zahanati 1,358 ambazo ukiangalia tuna bajeti siyo chini ya shilingi bilioni 78 kuweza kumaliza shughuli hizi zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie kwamba tulifanya assessment ile ili tuweze kujua nini tunatakiwa tukipange katika mpango wa bajeti tuweze kuondoa haya maboma na kujali juhudi kubwa zilizofanywa na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Saumu na Waheshimiwa Wabunge wote, katika suala zima la magofu ambayo hayajakamilika yale ya zahanati na vituo vya afya sambamba na hospitali zetu za wilaya, tunaweka mpango mkakati kabambe ambapo tutawaomba Waheshimiwa Wabunge katika mchakato wa bajeti mtuunge mkono ilimradi tuweze kuondoa hivi viporo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini tukifanikiwa hata kwa asilimia 60 kwa hivyo viporo ambavyo vipo site huko, tutakuwa tumewezesha kwa kiwango kikubwa kuwapatia wananchi wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania afya bora na miundombinu ya ujenzi wa zahanati. Ahsante.
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Barabara ya Tanga - Pangani - Bagamoyo ni barabara ambayo imekuwa ikitolewa ahadi kila chaguzi kuu zinapofika na Uchaguzi Mkuu uliopita pia ahadi hiyo ilitolewa ya kwamba itaanza kutengenezwa na tayari tunaambiwa upembuzi yakinifu umekwishafanyika, sasa je, ni lini utengenezaji wa barabara hiyo utaanza ikiwa tayari upembuzi yakinifu umekwishafanyika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara hii nimepita mara kadhaa na juzijuzi nilivyokuwa natembelea Mkoa wa Tanga, ni miongoni mwa barabara niliyoipita kutoka Bagamoyo mpaka pale Pangani na kikubwa zaidi katika kufika pale nilikuta reference ya Waziri wa Miundombinu aliyekuwa akipita pale na kutoa ahadi hiyo ya ujenzi wa barabara hiyo lakini ikiwa sambamba na ujenzi wa daraja lile la pale Pangani. Mheshimiwa Mawenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu ni commitment ya Serikali na kipindi cha sasa kwa sababu ujenzi wa barabara ya lami lazima kwanza upembuzi yakinifu ufanyike na jambo hilo limekamilika, ninaamini suala la barabara hii kwa sababu ni barabara ya kimkakati, kwamba hata kwenda Mombasa ni barabara ya shortcut naamini Serikali hii itafanya kila liwezekanalo ujenzi wa barabara hii uweze kukamilika.
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ambayo nimepata kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini ningependa kumweleza kuwa Hospitali ya Wilaya ya Pangani ina magari mawili tu kati ya hayo magari 11 ambayo umeyataja, lakini magari yale ni chakavu mno kiasi kwamba yanapoenda service basi yanalazimika kutengeneza kitu zaidi ya kimoja yaani sio service tu ya kawaida, lazima unakuta na vitu vingine vinakuwa vimeharibika pale.
Mheshimiwa Spika, Serikali pengine haioni umuhimu wa kununua magari mengine mapya badala ya kuacha magari yale chakavu yaendelee kutumikia Hospitali ya Wilaya ya Pangani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli, na mimi nilivyofika Pangani, Mheshimiwa Mbunge anakumbuka nimefika pale nimeona changamoto hii ya magari. Magari yale ni kweli ni miongoni mwa magari chakavu kama ilivyo katika Halmashauri nyingine. Nikijua wazi kwamba kipaumbele cha kununua magari ya Halmashauri huwa yanafanywa hasa na Halmashauri yenyewe ikianzia katika mchakato wa awali. Hata hivyo, Serikali katika kuimarisha huduma ya afya, tulinunua karibu magari 50 tukapeleka katika maeneo ambayo vipo vifo vingi zaidi. Hata hivyo tuna mkakati mwingine, tukipata gari la ziada tutafanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, suala la ununuzi wa magari naomba watu wa Halmashauri ya Pangani tuweke kipaumbele, lakini Serikali haitasita kusaidia wananchi wa Pangani tukijua wazi Jimbo lile na eneo lile jiografia yake iko tata sasa; ukitoka pale Hospitali watu wa Mwela huku na watu wa upande mwingine wana changamoto kubwa sana mpaka kwenda eneo lile.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali tunaliangalia hilo, lakini tutashirikiana vyema na wenzetu wa Pangani kuhakikisha mambo yao yanaenda vizuri. (Makofi)
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu haya ambayo amejibu Naibu Waziri tatizo la maji ambalo lipo Makambako ni sawa kabisa na tatizo la maji ambalo kwa sasa limejitokeza katika Jiji la Tanga na linaendelea kujitokeza ambapo licha tu ya maji kukatika mara kwa mara bila ratiba na bila taarifa lakini pia maji yale takribani mwezi mmoja sasa yamekuwa yakitoka machafu yenye tope.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili nilimfikishia Mheshimiwa Waziri wa Maji, nilimwandikia barua lakini pia nilikwenda kumwona mimi mwenyewe lakini bado linaendelea na majibu ya uhakika bado hatujapata. Maji yamekuwa yakiendelea kutoka machafu, yakiwa na tope na bado pia yanaendelea kukatika mara kwa mara. Serikali itoe tamko sasa ni lini watu wa Tanga watapata maji safi kama walivyozoea na maji ambayo hayakatikikatiki?Ahhsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mbunge alikuja kwangu akilalamikia hali ya maji kuwa na tope katika Jiji la Tanga. Jiji la Tanga ni mojawapo la mamlaka katika nchi ambayo imekuwa siku zote inatoa maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichojitokeza ni kwamba kumetokea hitilafu katika mtambo wa uchujaji maji na hii imetokana na uchafuzi mkubwa wa maji kule kwenye vyanzo kwa sababu wamevamia wachimbaji wa madini kwa hiyo maji yanakuja na tope na rangi. Kwa hiyo, imebidi sasa tutengeneze design nyingine ya kuchuja maji yale na tatizo lile tumeshalimaliza sasa hivi Tanga wanapata maji safi kama walivyokuwa wanapata zamani.
MH. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Pangani kama zilivyo wilaya nyingine zilizoko pembezoni mwa bahari ina bandari bubu nyingi. Bandari hizi zinatumika kuingiza mizigo ambayo ni halali na ambayo pia siyo halali kama vile madawa ya kulevya, wahamiaji haramu hata na bangi kitu ambacho kinasababisha bandari hizi zinakuwa ni chanzo kikubwa cha rushwa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuzitambua bandari hizi ili zile zenye vigezo ziweze kurasimishwa na kutambulika rasmi ikiwa ni pamoja na kuzikarabati na zile ambazo hazifai zifungwe kwa maslahi ya Taifa na watu Pangani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, anayoyasema ni sahihi na nadhani anafahamu kwamba ndicho tunachotekeleza ndani ya Serikali kwa sababu tuna timu ya Wakuu wa Mikoa yote iliyoko kwenye mwambao na upande wa Zanzibar wanakutana kila wakati kuhakikisha wanapitia zile bandari bubu kuona zipi zinaweza zikaendelezwa na kurasimishwa na zipi ambazo zinatakiwa kufungwa inasimamiwa kufungwa. Nadhani ni kitu ambacho anafahamu tunakitekeleza na nimushukuru sana kwa sababu kwa kuuuliza hivyo maana yake anaunga mkono hatua tunayoichukua.
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nina swali moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo cha afya ambacho
kiko katika kijiji cha Mwera, Kata ya Mwera ni kituo ambacho kwa muda mrefu sana kimepandishwa hadhi ya kuwa kituo cha afya; lakini kituo kile hakina huduma zinazokidhi kuwa
kaama kituo cha afya. Hakina gari la wagonjwa, lakini pia vipimo vya damu salama bado havipo katika hospitali ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua ni lini
Serikali itakipa hadhi sahihi kituo kile ya kuwa kituo cha afya katika Wilaya ya Pangani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema lini kwanza naomba tuweke rekodi sawa za Mheshimiwa Mbunge kwamba kipindi kile mlinialika na Mheshimiwa Aweso tumefika pale Mwera na nikatoa maagizo kwamba
kituo kile kutokana na yule mwekezaji pale japo anawekeza aweze kujenga theatre.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru kwa sababu wodi ya wazazi imeedelea kujengwa, lakini hata hivyo Serikali kuufanya kuwe kituo cha afya lazima miundombinu ikamilike vizuri, ndiyo maana tukaona sasa hivi tujenge jengo la theatre pale kubwa lakini pia kujenga na wodi zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndiyo maana
nikamuelekeza Mheshimiwa Aweso kwamba awaambie watu waiandae mapema ile BOQ. Tuta deploy pesa pale, kwa sababu watu wa pale wakikosa huduma, suala la kuvuka Mto Pangani ni changamoto kubwa sana na usiku vivbuko hakuna. Kwa ajili ya kuwaokoa Watanzania
tumeamua kuweka nguvu kubwa za kutosha, fedha za kutosha kujenga jengo lile litakamilika huenda kabla ya mwezi wa saba mwaka huu ujenzi utakuwa umeshaanza.
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu marefu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati ambayo Naibu Waziri ameielezea inaonyesha kabisa nia ya muda mrefu na bado iko ndani, lakini tatizo hili huku nje bado linaendelea kuwa kubwa yaani watu bado wanaendelea kuathirika sana na bandari hizi bubu.
Swali la kwanza, je, Serikali haioni kwamba kwa kuendelea kuweka mikakati hiyo mirefu ndani wananchi wanaathirika na pengine sasa ingefika wakati ikachukua mkakati wa kudhibiti angalau wakati ile mikakati ya muda mrefu ikiwa inaendelea?
Swali la pili, bandari bubu hizi ziko katika vijiji vinavyozunguka mwambao wote wa pwani. Kwa kufanya mikutano na Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Bandari na watu wengine haoni kama anawatenga wale wanakijiji au wale ambao wanazitumia zile bandari na ambao wanaishi karibu na zile bandari na sasa pengine ingekuwa ni vizuri Serikali ikaenda kwa wahusika moja kwa moja kuzungumza nao ikaangalia? Kuna athari pia za mazingira uchafuzi wa mazingira ni mkubwa sana katika bandari hizi bubu. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, hii mikakati siyo mirefu sana nimejaribu tu kuisoma kwa kirefu lakini siyo mirefu sana. Ni mikakati mitatu tu maalum isipokuwa nimeileza kwa undani ndiyo maana inaonekana kama ni mikakati mirefu au ya muda mrefu.
Hata hivyo nadhani kitu cha kufahamu hapa ni kwamba bandari bubu inaanzishwa katika maeneo ambayo maeneo ya karibu tu kuna bandari ambayo ni rasmi. Kwa hiyo ni tabia ya watu kukimbia bandari rasmi na kujianzishia bandari bubu pembeni.
Kwa hiyo suala la kuahusisha walioanzisha bandari bubu tutalifanya katika maana ya kudhibiti, lakini siyo kwa maana ya kumshirika wakati yeye aliyeanzisha hiyo bandari bubu huku akijua kwamba anafanya makosa na anatafuta fedha kwa njia ambayo siyo sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, ni kweli wanaohudumia hizo bandari bubu kama nilivyosema ni watu ambao wamejianzishia uratatibu wao nje ya utaratibu wa Serikali na tutafanya kila njia kuhakikisha kwamba tunawashirikisha katika kudhibiti lakini wakati wa kurasimisha hata vile vijiji tunavyowapa mamlaka wanawatumia wale ambao wana uzoefu wa kuendesha hizi bandari na hivyo tukifanya hivyo masuala ya usafi na mazingira wa bandari hizo yatashughulikiwa kikamilifu.
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Pangani na Pwani ya Mkoa wa Tanga tunalima sana mwani. Sasa hivi wakazi wa Pangani wameacha kidogo kulima zao la mwani kutokana na kukosa soko. Sasa Mheshimiwa Waziri unatusaidiaje wakazi wa Pangani na Mkoa wa Tanga kwa ujumla katika zao hili la mwani katika kutuletea wawekezaji na soko pia? Mwani unalimwa baharini, ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia fursa nijibu swali la Hajat Saumu. Ilibidi aweke kiangalizo kunieleza mwani inalimwa wapi, mimi kwetu ni Pemba mama yangu anaitwa Mariam huyu unamfahamu, kwetu ni pemba kwa hiyo na mimi mambo ya mwani nayajua.
Mheshimiwa Mbunge ni kwamba nilikuwa Tanga juzi kwenye maonesho ya Kimataifa. Tija ya mwani ni kutengeneza kiwanda cha kuongeza thamani, na kiwanda cha kuongeza thamani ni kiwanda kidogo ambacho Mheshimiwa Mbunge unakimudu. Ninapoendelea na juhudi za kuhamasisha viwanda vidogo na vile vya kati, tunakwenda Tanga kuhamasisha namna ya kuongeza thamani kwenye mwani, hiliki na mdalasini ili tuweze kupata soko. Soko la bidhaa za wakulima ni kuziongezea thamani.
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali moja la nyongeza. Katika jibu la msingi la Mheshimiwa Waziri ametaja Wilaya ambazo zitapata fursa wavuvi hao Wilaya ya Pangani hakuitaja. Sasa ningependa kufahamu wana mpango gani na wavuvi wa Pangani hasa ukizingatia nao pia kuna uvuvi wa prawns, lakini pia wamesahaulika sana katika elimu, kitu ambacho wangeweza kupata elimu wangeweza kupata hiyo mikopo ambayo ingewasaidia katika suala zima la uvuvi. Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, orodha ya Halmashauri au Wilaya ambazo nimetaja ni zile ambazo tayari zimeshanufaika na mpango huo wa wavuvi kupatiwa asilimia 40 ya fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya uvuvi hasa injini za boti. Kwa hiyo, ninachosema mpango huu upo na unapatikana kwa Halmashauri zote ili mradi wenyewe wajipange na wakidhi vigezo halafu tutaoa asilimia 40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Pangani, mimi nimefika Pangani na watu wa Pangani nawapenda sana, Mheshimiwa Aweso nilikutana naye kule. Kimsingi niliwaahidi kwamba wakijipanga kwenye vikundi, nipo tayari kuwasaidia waweze kupata asilimia hiyo 40. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwambia vilevile mheshimiwa Mbunge wapangeni wavuvi wenu katika vikundi, watafute fedha asilimia 60 halafu baada ya hapo tutawasaidia kupata hiyo asilimia 40 waweze kununua injini na waweze kufanya uvuvi kwa njia ambayo ni rahisi zaidi. (Makofi)
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Wilaya ya Pangani miundombinu ya maji imechakaa mno na hii ni kutokana na maji ya chumvi ambayo yamekuwa yakitoka. Swali langu ni kwamba, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ambayo imekuwa ikiahidi kila mara ya kutumia maji ya Mto Pangani ili kuweza kuwapatia wakazi wa Pangani maji ambayo hayana chumvi? Lakini pia kukarabati ile miundombinu ambayo imeharibika kwa kiasi kikubwa kutokana na maji haya ya chumvi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu miaka ya sabini Serikali tayari ilishaanza kutumia maji ya Mto Pangani na pale Korogwe tayari tunayatumia maji ya Mto Pangani. Tunao mradi mkubwa ambao umefadhiliwa na BADEA, sasa hivi Kampuni ya Karathi inatoa maji kupeleka maeneo ya Mwanga, yatafika mpaka Korogwe pia. Lakini pia tumepata ufadhili wa aina mbili; tuna fedha kutoka Serikali ya India lakini pia tuna fedha kutoka Serikali ya Netherlands, usanifu unaendelea ili tuhakikishe kwamba tunapeleka maji maeneo mbalimbali, tutafika mpaka Pangani Mheshimiwa Mbunge, wala usiwe na wasiwasi.
MHE. SAUMU H. SAKALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, suala la ukaguzi katika vyombo vya majini kwa kweli bado halifanywi kwa asilimia 100, hasa nikizungumzia katika bandari ambazo ziko katika Wilaya zetuSUMATRA hawana ofisi katika kila Wilya ambazo ziko Pwani.
Nikizungumzia Pangani hakuna ofisi ya SUMATRA na badala yake SUMATRA wamekabidhi madaraka yale kwa watua wa TRA ili waweze kuwakagulia vyombo ambavyo vinasafiri. Pamoja na hayo TRA hawana wafanyakazi wa kutosha jambo ambalo wakati mwingine wakati chombo kinasafiri, iwe ni usiku au ni mchana, unakuta TRA hayuko pale kwa ajili ya kukagua kile chombo. Kwa hiyo chombo unakuta kinajaza kuliko uwezo wake na ndivyo hivyo vyombo ambavyo vinapoteza muelekeo Baharini vinapata ajali watu wanakufa na hatujui idadi ya watu waliokufa wala mizigo inayopotea.
Mheshimiwa Spika, nizungumzia Bandari ya Pangani mizigo mingi sana inapotea kutokana na hiyo hali na watu wengi wanakufa kutokana na hiyo hali na hawatangazwi. Sio hilo tu kuna zile bandari ambazo ni bubu, bado hazina kabisa usimamizi na watu wamekuwa wakipoteza maisha pamoja na mizigo. Sasa ni lini Serikali itachukulia kwa umuhimu wake suala hili la usafiri wa majini ambao umekuwa ukipoteza maisha ya watu bila kugundulika ili ajali hizi ziweze kupungua? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu la swali la msingi kwamba SUMATRA wamepewa mamlaka ya kusimamia bandari zetu zote na bandari zote ambazo zimesajiliwa. Nakiri kwamba kuna bandari zingine ni bandari bubu na huwa zinazuka kila wakati, ni bandari ambazo zinatumika na wahalifu, kwa sababu kila ukiwadhibiti hapa wanaenda kutafuta sehemu nyingine. Ni wahalifu kwa sababu wanakiuka sheria za shughuli za bandari zinazosimamiwa na SUMATRA na kila tukijaribu kuwaelimisha, kwamba jamani acheni kutumia bandari bubu mtumie bandari ambazo zimesajiliwa rasmi, bado tunakuwa na matatizo.
Mheshimiwa Spika, mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge, wakati mwingine kama tutataka SUMATRA iwe katika kila aina ya bandari inayozuka kila wakati uwezo huo tutakuwa hatuna. Niwaombe sana Waheshimwa Wabunge tusaidiane, tuhakikishe mizigo yetu ipite katika zile bandari ambazo ni rasmi, tuache kupitisha katika bandari bubu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu kukabidhi kazi za SUMATRA kwa upande wa TRA au hata taasisi nyingine, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pale ambapo TRA inaona kwamba zile kazi zimewazidi huwa wanarudi kwetu, kwa maana na SUMATRA na kuwaambia kwamba hapa tunahitajika tuwe na permanent station ya watu wa SUMATRA na hatimaye huwa tunafanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, katika maeneo yale ambayo traffic si kubwa sana tunawatumia wenzetu wa TRA na sehemu zingine TPA wanatumika kutegemeana na jinsi ya kutumia resources za Serikali tulizonazo. Sidhani kama tutaweza kwa SUMATRA peke yake kusimamia kila bandari tulizonazo, kuweka idadi ya staff inayotakiwa. Tunatumia taasisi zingine kufanya kazi hizo kwa kushirikiana na tasisi hizo zinawasiliana muda wote kuhakikisha kwamba pale ambapo panapolamika kuweka permanent station ya SUMATRA hatimaye tunafanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, lakini naomba nirudie tena. niwaombe sana ndugu zangu, na hasa ninyi wenzetu mnaotoka katika maeneo ya ukanda wa Pwani mtusaidie ili watu wetu wafuate sheria na Sheria za SUMATRA na Sheria za TPA ni sheria mama kama zilivyo Sheria zingine, si kwamba zile Sheria ziko kiwango cha chini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kila mmoja ana uwezo wa kuzivunja kwa kadri anavyoona inafaa. Niwaombeni sana tusaidiane ili tuhakikishe kwamba maisha ya wananchi wetu na mizigo yao haiathiriwi katika safari za baharini na kwenye maziwa.