Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Savelina Slivanus Mwijage (7 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kuweza kurudi ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nakishukuru Chama change, Chama cha Wananchi CUF kuweza
kuniamini na kunirudisha hapa Bungeni. (Makofi)
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, namtaka Waziri wa Mawasiliano, kesho atuletee majibu hapa ni kwa nini wamezuia TV kuonesha Bunge. (Makofi)
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuchangia hotuba ya Rais, watu wengi hapa wanabeza mchango wa Wabunge kuhusu Zanzibar. Tukumbuke kipindi cha nyuma Zanzibar ilivyokuwa na vurugu leo hii badala ya kuomba Mwenyezi Mungu kuepusha balaa la siku za nyuma tunaendelea kubeza na Wazanzibari wenyewe wanajua matatizo yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, tusiendelee kubeza mambo ya kisiasa, tusije humu kuwasafisha au kuwapongeza watu kwa mambo ya kutuletea matatizo kama yaliyotokea siku za nyuma. Watu walikufa na walipoteza mali zao nyingi. Kwa hiyo, nawaomba tushirikiane kupiga magoti kumrudia Mwenyezi Mungu tuweze kuiombea Zanzibar iweze kuwa na amani.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Marais wengi wanavyoingia kwenye kampeni wanawalaghai watu wa Kanda ya Ziwa, nitaanza na usafiri wa majini. Wakati wa uhuru mwaka 1961, wakazi wa Mkoa wa Kagera na Kanda ya Ziwa tulikuwa na chombo cha usafiri kinachoitwa MV Victoria,
MV Kabilondo, MV Usoga na MV Serengeti. Kila Rais kuanzia Rais Mkapa walisema wataleta meli mpya, meli za kusafirisha mizigo na ya kusafirisha Watanzania amekuja Jakaya hivyohivyo, amekuja Magufuli hivyohivyo. Tunaomba msiwe mnalaghai kwa kuahidi kitu ambacho
hamtaweza kukifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naelekea kwenye huduma ya afya. Mkoa wa Kagera una zaidi ya watu milioni 2.8. Hivi sasa Serikali ya Mkoa wa Kagera inamiliki hospitali tatu na vituo vya afya 25, zahanati 207, mashirika ya dini yanaongoza kwa kutoa huduma ya hospitali ili kuwasaidia wananchi. Serikali inajivunia hizo hospitali kwamba ni za Serikali. Hospitali ya Rubya, Isingilo - Nyakanga, Bugeni ni za dini. Tunaomba kuanzia sasa na wakati huu wa Magufuli, Hospitali ya Mkoa wa Kagera ipatiwe CT-Scan na Madaktari Bingwa kwa sababu haina Daktari
Bingwa wala vifaa. Leo hii anasema ataboresha hospitali, aboreshe kwanza vifaa ndiyo ajenge hiyo Hospitali ya Mkoa na Wilaya anayotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye kilimo. Mkoa wa Kagera tuna zao la kilimo cha migomba. Mgomba ndiyo zao kuu la biashara na zao la chakula. Ilitolewa taarifa kwamba zao hilo lina ugonjwa unaitwa mnyauko. Mpaka sasa hivi wananchi wa Mkoa wa Kagera wana njaa kubwa sana kutokana na ugonjwa huu wa migomba lakini Serikali haioni umuhimu wa kuwasaidia kuwapelekea wataalamu ili kutibu ugonjwa huo ili waendelee kulima migomba yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1952, Serikali ya Kikoloni iliweka sheria ya kuwazuia kulima migomba bila kuweka mbolea ya chengachenga. Mwaka 2006 katika Kata ya Izigo, Wilaya ya Muleba, Mkoani Kagera ndiyo waliotangulia kupata ugonjwa huo wa mnyauko
ukitokea nchi ya jirani Uganda sasa hivi umeenea Mkoa mzima wa Kagera na watu wanalia na njaa. Kipindi kilichopita mkungu mmoja ilikuwa Sh.3,000, Sh.5,000 sasa hivi umefika Sh.16,000 mpaka Sh.30,000. Naiomba Serikali inayosema Kilimo Kwanza ianze kwanza kuwaboreshea wakulima wa Mkoa wa Kagera kwa kuwaletea wataalamu kuboresha zao hilo ili waweze kupata kipato cha kuuza ndizi Uganda na nchi nyingine jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naharakisha ili muda wangu usiishe, naenda kwenye elimu, wanasema elimu ni bure. Ukiangalia elimu ni bure lakini Mwalimu anayekwenda kufundisha elimu bure analala wapi? Darasani watoto wamejazana hawana mahali pa kukaa atapaje akili
ya kuweza kushinda darasa la saba au form four. Kwanza, boresha shule zilizopo, Walimu wapate sehemu ya kulala, tupate maabara za shule, wanafunzi wapate mahali pa kukaa na kusoma vizuri na Walimu wafundishe vizuri. Mwalimu hawezi kuacha mtoto ndani ya familia
anakosa chakula akapata akili ya kumfundisha shuleni na anafika darasani mtoto anasinzia kwa ajili ya kukosa chakula. Kwanza, tuboreshe kitu kilichopo ndiyo baadaye tuje kusema watoto wanasoma bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona fomu ya watoto wanaoingia form one, ukiangalia michango wanayoitoa ni mingi sana. Kama Serikali imekuwa tayari kuwasaidia wanafunzi ili wasome bure waanze kwenye chakula. Mtoto akiingia darasani ana njaa atashindwa kuendelea kusoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, watumishi walioajiriwa wanakaa katika Halmashauri miaka zaidi ya thelathini wanafanya kazi kwa mazoea. Juzi hapa mimi na Mheshimiwa Lwakatare tumekwenda kutoa misaada katika zahanati ambazo wanawake wanajifungua, kwa moyo safi tu lakini akatokea DMO akasema hospitali zote hazina shida ya beseni na unaangalia kila mwanamke anabeba beseni wakati huo unaona Wabunge wengine wa CCM wanatoa misaada inapokelewa. Hii ni kutokana na kufanya kazi kwa mazoea kwa miaka 30 yuko kwenye Halmashauri moja habadilishwi. Tunaiomba Serikali mfanyakazi yeyote akikaa miaka mitano inatosha ahamishiwe kwenda sehemu nyingine, siyo kufanya kazi kwa mazoea inaonekana pale ni nyumbani na anachokifanya anaamua mwenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye ajira, vijana wamejiajiri kwenye pikipiki lakini wananyanyasika, wanapigwa, wananyang‟anywa pikipiki na Maaskari halafu wanaziuza na hili tumeshuhudia. Kama kijana huyo hana elimu ya kuendesha pikipiki anaendesha kwa ajili ya
njaa na kutafuta ajira ya kulazimisha. Naiomba Serikali itoe elimu kwa vijana ambao wanaendesha bodaboda ili waweze kupata kipato chao kwa sababu ajira Serikalini hamna, inasema ajira, ajira, lakini ajira haipatikani. Kama hatuna viwanda, kama hatuna masoko makubwa, hakuna ajira yoyote vijana wataendelea kupigwa na Maaskari.
Mheshimiwa Naibu Spika…
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kagera ni wakulima wa zao la ndizi, ni zao la chakula pamoja na biashara. Mkoa huu umeanza kulima zao hilo toka mwaka 1952 likitokea nchini Uganda, hii ni enzi ya ukoloni. Serikali ilitunga sheria ya kuwabana wananchi ili kutokomeza ugonjwa huo wa mnyauko ukawa umetoweka lakini ukajitokeza tena mwaka 2006 katika Wilaya ya Muleba na Kata ya Izigo sasa umeenea Mkoa mzima wa Kagera pamoja na Kigoma, Geita, Ukerewe na Kyerwa. Karagwe ni asilimia 70, Bukoba Vijijini ni asilimia 65, Misenyi ni asilimia 55, Ngara ni asilimia 35 na Biharamulo ni asilimia 25. Serikali ijue ugonjwa huo umeenea kwa asilimia 85. Je, ni lini Serikali itatuletea wataalam wa kuweza kutoa elimu juu ya ugonjwa huu ili wananchi waendeleze kilimo hiki hasa ikizingatiwa kuwa ni zao la biashara na chakula?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kagera kuna wafugaji wengi lakini hawana faida na ufugaji wao ukizingatia sasa hivi kuna ufugaji wa kisasa wa kunenepesha ng‟ombe. Je, ni lini Serikali itatuletea viwanda hasa kiwanda cha kuchakata maziwa, nyama na ngozi? Tunaomba Serikali itukumbuke Mkoa wa Kagera kuondoa umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe, vijana wanajiajiri kuvua samaki na zana wanazotumia kuvua samaki wananyang‟anywa na kuchomwa kwamba ni haramu. Je, kama ni haramu zinatoka duka au kiwanda gani? Kwa nini Serikali isifungie kiwanda ambacho kina zana haramu? Badala ya kuwakamata wale wanaoingiza na kuuza wanakamata wanaovua si kuwaonea?
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia kwenye hotuba ya Waziri anasema anatoa elimu kwa wavuvi, je, Mkoa wa Kagera wamepata wangapi hiyo elimu? Tunaomba elimu hiyo itolewe ili vijana wafaidike na Ziwa lao Viktoria. Mkoa wa Kagera tuna kiwanda kimoja cha samaki, je, ni lini Serikali itatujengea kiwanda kingine ili vijana wapate ajira na wafaidikie na rasilimali ya nchi yao?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia Wizara ya Elimu, kwa kuwa elimu ndio jambo la muhimu sana. Bila elimu hakuna Daktali, hakuna Pilot, hakuna Mwalimu hakuna Rais, hata viwanda ambavyo tunavisema ni bure, wala barabara, hakuna chochote! Sasa Serikali iwekeze kwenye elimu, tusifanye wimbo elimu bure, tuwekeze kwenye mashule. Bado wanafunzi wanakaa chini, hawana vyoo, hawana maji, hawana vitabu, hasa vitendea kazi vyote hawana. Watoto hawawezi kukaa chini; wataweza kuwa na akili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa tabia kwa Mwalimu, anakaa hadi anastaafu bila hata daraja la kwanza. Heshima ya Walimu iko wapi? Kazi kulalamikia malipo, kulipwa stahiki zao. Kuna wanaostahili toka mwaka 2014 na ni wengi zaidi, unategemea hao Walimu watakuwa na akili ya kufundisha. Serikali ilipe stahiki zao ili tujenge elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye shule za binafsi tunaomba Wizara hii iangalie hata kama sheria nyingine ambayo itaweza kusaidia, tunasema watoto wapate elimu bure na karo zinakuwa juu. Hii watasoma watoto wa matajiri tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madawati yaliyotajwa na Mheshimiwa Rais, nashauri, kwanini zisitolewe pesa kila Wilaya ya kutengenezewa huko huko kuliko kubebwa na kusambazwa? Je, hiyo gharama nyingine? Ni ushauri wangu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wanaopata ajira wanapangiwa sehemu ya mbali na Wilaya, wanapata shida kufuata malipo yao. Pamoja na hayo, wanapokwenda kufundisha mishahara wanakatwa hapo na nauli anakuwa amejikopa na pesa hakuna. Sasa ninachoomba, Walimu wanapewa ajira na kupelekwa kwenye Wilaya wapewe na mishaara ili iwasadidie huko wanakokwenda kuanza maisha, hawana nyumba; kama kuna nyumba, hakuna choo; hayo ndiyo elimu bure? Elimu bure iko wapi bila miundombinu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoto wa kike akibeba mimba kama wote ni wanafunzi anafukuzwa wa kike tu. Hiyo ni adhabu ya mtu mmoja. Nashauri wote wapate adhabu hata kama sio mwanafunzi mwenzake, wote wape adhabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za watoto wenye mahitaji maalum ziko vibaya sana. Mimi nilishatembelea baadhi ya shule hizo, kuna Mgeza Mseto; kuna Mgeza Viziwi Bukoba Mjini. Kuna shida kweli! Vitendea kazi hawana hasa mahitaji maalum yote, hawana kabisa. Naomba Wizara msiwe mnasikiliza Watendaji tu jamani, hata wewe Waziri una muda, uende na Kamati kuzunguka kuja kubaini matatizo yaliyomo kwenye elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho natoa rai yangu hiyo. Tukirudisha elimu, tutakuwa na utajiri, tumeshatatua matatizo yanayotukwamisha. Huo ndio mchango wangu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu na napenda kumpongeza Katibu wangu Mkuu Maalim Seif kwa kuwa na msimamo wa kukataa kuburuzwa kwenye uchaguzi wa marudio wa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi napenda nichangie kwenye bajeti hii. Mkoa wa Kagera naona una tatizo kwenye Serikali kwa sababu kila wakipanga bajeti unaangalia huo Mkoa unatupwa pembeni. Bajeti yake ni ndogo sana na matumizi yao ni makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitaanzia kwenye usafiri wa majini, Ziwa Victoria, kila Rais anayeingia kwenye madaraka anaahidi meli mpya, meli tatu mpya, meli mbili mpya mpaka anamaliza uongozi wake anaingia Rais mwingine. Tumekuwa watu wa kujaribiwa kila miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliahidiwa meli na meli tuliyonayo ya Victoria wamepanga bajeti ya kufanya ukarabati. Meli hiyo ni ya miaka, imeshazeeka, hata wakifanya ukarabati siku mbili, tatu lazima yatokee maafa. Kuliko kukarabati, hizo pesa kwa nini wasikusanye wakawaletea meli mpya ya kuweza kuwasaidia ili isiwe mitego ya kuwa watu wanadumbukia kwenye maji mara kwa mara?
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye kilimo. Mkoa wa Kagera kilimo chetu hasa ni ndizi na kahawa na ndizi ni zao la chakula na la uchumi, sasa hivi zao hili limekuwa na matatizo. Halmashauri nyingi ziliandika barua na kuomba Serikali kuwasaidia kuwaletea wataalam wa kutibu ugonjwa ambao umeleta madhara, kwa kweli miaka miwili inayokuja mbele watu watakufa na njaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kahawa ni zao kuu ambalo sisi toka tumezaliwa tumekuta ni zao kuu la kiuchumi. Ukiangalia Uganda hilo zao lina bei kubwa lakini Mkoa wa Kagera zao hili limerudi chini. Inafika mahali watu wanakata miti ya kahawa na kuifanya kuni kwa sababu hawana faida nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye barabara. Fedha ya barabara inayotengwa ni ndogo kweli lakini ukiangalia ni barabara ambazo zina fursa ya kuingiza uchumi katika Mkoa wetu, imepakana na Uganda, Rwanda na Burundi. Ukiangalia barabara ya kutoka Kayanga kwenda mpaka Kyerwa, Karagwe ni barabara ya vumbi miaka nenda miaka rudi, hawakumbuki hata kuwatengenezea barabara lakini tukija humu ndani tunauingiza ushabiki wa vyama bila kuwafikiria watu wetu wanapata shida. Ukiangalia barabara ya kutoka Kanazi kwenda mpaka Katoro, kuzunguka kwenda mpaka Kyaka, ni barabara nzuri ambayo ina fursa nzuri ya kuzalisha uchumi katika mkoa wetu lakini mpaka sasa hivi Serikali haijagusa hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo la Bukoba Vijijini wana tatizo la kivuko na nimepiga kelele hapa kuanzia mwaka 2006. Mara kwa mara kivuko kilichopo kinakwama katikati ya maji na watu wanapata shida. Niliiomba Serikali angalau wawaletee kivuko hata kama kimetumika lakini kiwe na uimara siyo mara kwa mara kuwa kinatengenezwa, watu wanapata shida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye maji. Mkoa wa Kagera umezungukwa na mito mingi lakini akina mama wanapata shida ya maji. Unashangaa ukienda sehemu za Katoro, Karagwe, wanakunywa maji ambayo rangi yake utafikiri wameweka maziwa, lakini tukija hapa tunashabikia kuzomeana hatukumbuki watu wetu tuliowaacha nyuma wana matatizo makubwa. Akina mama wanapata shida, wanatembea zaidi ya kilometa 20, zaidi ya kilometa 50 wanatafuta maji. Ukienda pale mgeni wakikuletea maji utafikiri wamekuwekea maziwa kumbe ni maji ya kunywa lakini tukija hapa kazi ni kelele ya upinzani-upinzani, tunasema kitu ambacho kinatusaidia na sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye usafiri. Sisi Mkoa wa Kagera usafiri ni wa matatizo, mabasi yakishaharibika huku ndiyo wanatuletea kule kama nilivyosema kwenye meli. Sasa ni lini Serikali itaona umuhimu angalau wa kututengenezea bandari mbili, Bandari ya Kemondo na Bukoba Mjini kwa sababu bandari iliyopo ya Bukoba Mjini ilikuwa inaingiza meli kutoka Bukoba inabeba mizigo inapeleka Uganda, inatoka Uganda inapeleka Mwanza inakwenda Musoma, leo hii hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii inafanya mpaka mkoa wetu ushuke kiuchumi, Serikali ituangalie. Mara kwa mara watu tunakuja hapa tunapiga kelele, mimi nawaeleza Wabunge wa Mkoa wa Kagera, tukae pamoja tuangalie fursa za kuweza kutusaidia katika Mkoa wetu, vyama tuweke pembeni tuangalie fursa za mkoa wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri kuna wizi ambao hata pesa hizi zilizopangwa shilingi milioni 50 hazitafanya chochote bila kuwa na mikakati. Mfanyakazi wa Halmashauri anaiba pesa wanambadilisha hapo hapo wanamweka Wizara nyingine lakini anapokwenda kule anaendelea kufanya mambo kama hayo, kwa nini asifukuzwe? Mtu anakaa Halmashauri mpaka miaka 10 bado yuko Halmashauri. Anafanya kazi kwa mazoea, anafanya kazi kwa kujua hakuna mtu wa kufanya kitu chochote kwa sababu analindwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Muleba kuna mkandarasi ambaye alisimamishwa kazi na Mheshimiwa Mwanri, aliyekuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI lakini mpaka sasa hivi huyo huyo ndiyo amepewa kazi kwa sababu ana ushirika na mtu wa Chama cha Mapinduzi, anamkingia kifua aendelee kupewa kazi. Hatutakwenda kwa sababu pesa zinatengwa hapa kwenda kufanya kazi lakini tunaendelea kuweka mtu ambaye ana makosa na alishasimamishwa asiendelee kufanya kazi. Tunaomba haya tunayoyaongea na kushauri sisi wapinzani muwe mnayaangalia, siyo yote yanakuwa mabaya. Tunaishauri Serikali ili ikafanye kazi vizuri siyo tusimame hapa tuanze kuimba ngonjera ya vyama, kitu kilichotuleta hapa ni kuwatetea wananchi ambao ni maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wetu hawana uwezo wa kununua dawa. Anakwenda hospitali anaandikiwa dawa anaambiwa akanunue, pesa atatoa wapi? Kuna wazee ambao hawana uwezo, wanasema wazee watatibiwa bure, mimi sijawahi kuona wazee wanaotibiwa bure, anapanga foleni kama mimi, mzee anafia pale pale barazani hata kidonge hajapata. Naiomba Serikali kama wazee wanatibiwa bure wapewe bima za afya na watengewe dirisha lao ili wawe wanapata matibabu stahiki kwa sababu hawana pesa ya kununua dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda kwa wagonjwa walioathirika na UKIMWI. Tunaomba Serikali, kwa sababu inaonesha inawapa hata chakula, ni masikitiko makubwa, nilikuwa nashauri hata kwenye Kamati yangu, mtu anakwenda pale ameathirika badala ya kumweleza mapema kabla hajapimwa, anapimwa akirudi wanaanza kumwambia ukijua umeathirika utafanya nini, ukijua unaumwa utafanya nini? Mtu anaweza akafia palepale hajafika hata kuchukua dawa wala hajajua kama ameathirika ama hakuathirika. Naomba wale ambao wanawa-treat wale watu wawaeleze mapema kabla hawajaanza kuwaeleza kama wameathirika au hawajaathirika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Kamati tuliomba kwamba pale wanapopewa dawa wawe wanapewa na watu wengine kwa sababu ukiwaweka pale kwenye dirisha peke yao mtu mwingine anaogopa kuchukua dawa abaona aibu! Kwa nini umewatenga na hiyo ni kuwanyanyapaa. Naomba watibiwe na sisi lakini dawa zao zinakuwa zimeandikwa zinajulikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye elimu. Watoto wa kike wanapata shida na elimu. Nashauri mtoto wa kike akipata mimba aliyempa mimba na yule aliyempa mimba apewe adhabu. Siyo msichana peke yake anapata mimba anarudi nyumbani anakaa chini kijana anaendelea na masomo, huo siyo unyanyapaa? Huyo kijana na yeye apewe adhabu ili kama wanapewa adhabu wapewe adhabu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishie hapo lakini haya niliyoyaongea hapa naomba ushauri wangu ufanyiwe kazi na Mheshimiwa Waziri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nami kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu niweze kuchangia hotuba hii. Kwanza nichangie suala moja linaloniudhi na kuniletea kichefuchefu, barabara ya kutoka Mlandizi kuja Chalinze; barabara ambayo ina matuta utafikiri wanapanda viazi, inanikera. Ni barabara ambayo tunaitegemea wote, Maraisi wanapita pale, Mawaziri wanapita pale, ile barabara ni mbaya sijui kama Mheshimiwa Waziri ameweza kuitengea fedha kwa sababu wote tunapita pale, tunaiona hiyo barabara ilivyo. Ukipita pale kwa speed lazima upate mweleka.
Mheshimiwa Spika, Wakandarasi wanaopewa shughuli zote za barabara, sijui wanakuwa wametoa rushwa mimi sielewi, kwa sababu barabara inatengenezwa siku mbili, tatu imeshaharibika, unakuta mashimo. Ni kwa nini wasitafutwe Wakandarasi ambao ni wasomi, wana uelewa wanajua kutengeneza? Kwa sababu ukiangalia barabara zote zinazotengenezwa Tanzania nzima, ni miezi miwili, mitatu tayari ina mashimo. Naona Wakandarasi hawa huwa wanatoa rushwa ndiyo maana wanapata hizo kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende kwenye usafiri wa Ziwa Victoria. Nina majonzi makubwa sana kwa Wanakagera. Tumeanza kupata meli ya kwanza mwaka 1961 kwenye uhuru; Victoria, tukapata meli ya Usoga, tukapata Butiama, tukapata MV. Bukoba, lakini meli zote hizo unazozisikia zimeshakuwa chakavu na Victoria kila mwaka mnatenga bajeti ya kukarabati. Ni lini mtatuletea meli mpya? Kwa sababu tunapata ahadi kutoka kwa Marais na Rais kila anapoingia kwenye mchakato wa kampeni, anaahidi meli moja au meli mbili mpya; mpaka leo hii sasa naona mnaweka fedha za kukarabati. Hatutaki tena kukarabatiwa meli zikaja kuwaua watu, hatukubali tena kwa sababu kile kitendo cha MV - Bukoba kuendelea kuiweka ndani ya Ziwa Victoria imeua watu; mpaka mmekuja kusema kwamba irudi hiyo meli ya MV Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naiomba sana Serikali, watu wa Mkoa wa Kagera pamoja na wa Kanda ya Ziwa siyo watu wa kuwategeshea ili wakarabati siku mbili, tatu unakuta imezama, inakwenda Kemondo imezama, inakwenda kwenye Bandari ya Bukoba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza, Bandari ya Kemondo na Bandari ya Bukoba Mjini hazijawahi kufanyiwa ukarabati toka kwa mkoloni mpaka sasa hivi. Ukiangalia hizo bandari, zilikuwa zinatumika kupeleka mizigo Uganda, inatumia meli ya Umoja, inatoa mizigo pale Bukoba Mjini inapeleka Uganda, inatoa Uganda inapeleka Kemondo, inatoka Kemondo inapeleka Musoma. Mpaka leo hii wananchi wa Bukoba pamoja na wa Kanda ya Ziwa wamekuwa maskini kwa sababu hawana sehemu ya kusafirishia, kupata uchumi katika mkoa wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende kwenye barabara. Sisi tuna barabara ambazo zinaunganisha nchi zetu jirani. Tuna barabara ya kutoka Mushaka kwenda mpaka Kyerwa mpaka Uganda. Hiyo barabara nafikiri miaka nenda rudi haijawahi kutengewa fedha au kuisema katika orodha kwamba inatengenezwa au imewekewa fedha, sijawahi kusikia. Ni mashimo, kutoka Mushaka kwenda mpaka Kyerwa mpaka Mlongo. Ni barabara ambayo tunaweza kufanya biashara na watu wa Uganda kwa sababu ni njia ya karibu ya kuunganisha na Karagwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Mushaka kwenda mpaka Benako - Ngara ni barabara ambayo inatuunganisha kwenda Rwanda na Burundi, lakini ni mbaya na majambazi wanatuteka mle mara kwa mara, kwa sababu barabara ni mbaya. Sijawahi kusikia Serikali inaiongelea au kusema kwamba kuna kipindi ambacho itatengenezwa au wameitengea fedha kadhaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende kwenye barabara tena. Kuna barabara ya kutoka Kanazi inakwenda Kafunjo, kuna daraja Kafunjo pale linaitwa Kalebe kabla hujafika Ibwela. Hilo daraja ni bovu sana. Kinachonishangaza ni kimoja na kila Mbunge wa Mkoa wa Kagera akisimama hapa anaeleza hiyo barabara, ni mbaya sana na tunaitegemea, mtu akitoka Kanazi anakwenda Ibwela akitoka Ibwela anaenda Kafunjo, akitoka anaunganisha, yuko Kyaka, tayari ameshaingia Uganda.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninachoomba, Mkoa wa Kagera ukiangalia hata kwenye bajeti za Mawaziri wote sijaona bajeti ambayo inatugusa Wanakagera, naomba sana kwa Mheshimiwa Waziri, wawe wanatukumbuka, nasi ni wananchi wao. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakwenda kwenye viwanja vya ndege. Kiwanja cha Ndege cha Bukoba Mjini kimefanyiwa ukarabati, lakini tuna ahadi ya miaka nenda rudi Kajunguti. Kajunguti ina ahadi ya miaka mingi. Sisi tuna zao la ndizi Bukoba tuna mazao ya matunda; tungekuwa na uwanja ambao ni mkubwa na sisi tungekuwa tunasafirisha hata matunda yetu kupeleka nje, kwa sababu unakuta ndizi zinasafirishwa kupelekwa Uganda, Uganda wanasafirisha kupeleka nje, lakini sisi wenyewe hatuna. Ni kitu cha kukuza uchumi katika Mkoa wetu wa Kagera. Naomba sana na sisi wawe wanatukumba ni Watanzania wenzao. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, narudi tena hapo hapo kwenye uwanja wa Bukoba. Uwanja wa Bukoba ni mfinyu sana. Kila wanapopanga fedha, wanapanga fedha ambazo ni kidogo kwa sababu unakuta huku kuna wananchi na huku kuna wananchi. Wanapanga fedha kidogo! Kwa nini isitengwe fedha ambayo ni kubwa angalau watu wote wa upande mmoja wakaondolewa, wakabaki wa upande mmoja, ukapanuliwa, tukawa tunasubiri hizo fedha za Kajunguti zitengwe. Hata juzi ndege imeleta matatizo ni kwa sababu ya hali ya hewa ya pale Bukoba.
Mheshimiwa Spika, naomba sana hali hiyo hiyo, michango hiyo inayochangia kuhusu barabara kuhusu na uwanja wa ndege tuna masikitiko makubwa, ni kwa sababu na sisi tuna uchumi ambao tunaweza kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukipata uwanja wa ndege mkubwa, tukipata barabara za kuunganisha na sisi tungekuwa tunajivunia Mkoa wetu wa Kagera, urudi kama Kagera ilivyokuwa zamani.
Mheshimiwa Spika, tunazalisha kahawa; utapeleka wapi kahawa? Naomba sana Mheshimiwa Waziri akija hapa aweze kutueleza sisi Wanakagera wanatuweka upande gani? Upande wa kukosa kabisa bajeti ya Serikali au upande wa kuwekewa kiporo au upande wa kutokukumbukwa kabisa? Tuelewe, hata sisi tujue kwenye bajeti ya Serikali, hatukumbukwi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema, barabara za Bukoba Mjini. Nasikitika, barabara za Bukoba Mjini ukiangalia na kipato cha Halmashauri yetu ni kidogo sana kwa sababu hatuna kipato chochote pale Bukoba na ni kwa sababu ya maunganisho ya hizo barabara nilizozisema. Ni mbovu ni mbaya, hatuna Stendi, hatuna Soko, hatuna nini; ni watu ambao tunakaa kwa kukaa kufikiria tufanye nini.
Mheshimiwa Spika, naomba kwa mchango wangu huo, nina majonzi makubwa, naomba Serikali itoe macho iangalie Mkoa wa Kagera na sisi tuweze kupata kipato, tupate hata kale kasungura tulikonako kadogo, kaende Mkoa wa Kagera. Naomba kuishia hapo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie Wizara hii nikizingatia vitu muhimu sana ambavyo ni rasilimali zilizomo katika nchi hii ya Tanzania. Pamoja na kuingiza uchumi ili kuondokana na umaskini, jambo ambalo Wizara ya Maliasili na Utalii inafanya, nchi yetu ni tajiri sana kwa kuwa na vitega uchumi vya utalii. Tuna vivutio vingi sana na nchi yetu ni ya pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Serengeti, Ngorongoro, Tarangire, Momela, Mikumi, Katavi na Rubondo; tuna jiwe liko Ukerewe ambalo Serikali haijaona umuhimu wake kuipa kipaumbele ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi wanajua maajabu makubwa sana ya hilo jiwe pamoja na Wabunge wa huko Ukerewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Biharamulo tuna msitu ambao kwa sasa umeingiliwa na wafugaji wengi wamevamiwa, wanashambuliwa pamoja na wachoma mkaa, hata hao wa ng‟ombe wanajifanya wafugaji, tunawaogopa sana. Wanaweza kuwa sio salama; huwezi kujua kama ni Watanzania au ni wakimbizi. Matokeo yake kuanza kuteka na kurudi kwenye pori hilo. Je, msitu mkubwa kama huo wanakula nini? Tunaomba msaada wa Serikali, hata wanyama wameanza kurudi sasa, watakaa wapi kwa style hii? Je, tuna faida gani? Kwa nini wafugaji wasitengewe wakawa na mipaka? Vijiji ambavyo viko karibu na pori hilo, shida wanavamiwa na wake zao wanabakwa, wakikuta vyakula wanakula, wanaume wanapigwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango ya Wizara iliyomo kwenye vitabu iwe ya kutekelezeka. Msitu huo uko kwenye Ziwa la Buligi ambalo lina maajabu makubwa sana. Limepakana Bukoba Vijijini, Biharamulo, Karagwe na Ngara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana, tena sana, Serikali iweze kuweka mpango mkakati tuongeze kipato/ajira kwa vijana wetu. Vipo vitu vingi tu, ni mipango tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matangazo ya utalii wetu wa vivutio vyetu ni mdogo sana. Matangazo ya vipeperushi inafika mahali unakuta Kenya wanaongoza mbuga zetu kwa upande wao hata Mlima Kilimanjaro ni punde watasogea upande wa Kenya. Kweli tunakokwenda hili jambo mmekaa kimya, taratibu wanakuja. Hata Idd Amini alikuja hivyo hivyo kusogeza mipaka yetu ila angeingia kwenye nchi yetu, Mwalimu wetu Baba wa Taifa alipambana na Wajerumani, zimetolewa zinasogezwa matokeo yake nchi ikaingiakwenye vita. Sasa chonde chonde, Wizara iwahi mapema kusimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wizi wa pembe za tembo, hili suala limekuwa wimbo katika nchi hii. Ni maharamia wangapi wamefungwa? Ni kesi ngapi ambazo ziko mahakamani au zilizokwisha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato ya vivutio ni madogo sana ukilinganisha na vivutio tulivyonavyo vingi na kupata tofauti. Sisi tuna asili ya mali nyingi, hatupaswi kuwa hivyo, ni usimamizi siyo mzuri sana. Tuwe na usimamizi na mipango mikakati, tutaondokana na kutokuwa na plan za kudumaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu kama viwanja vya ndege vinatakiwa kuboreshwa hasa vya Musoma na Kilimanjaro (KIA). Kweli viwanja vya kuingiza wageni nchini viko hivyo na kama unavyojua wenzetu wanajali maisha yao na usalama. Miundombinu inashusha utalii. Viwanja vya mbugani vyote vya changarawe viboreshwe kwa kuwekewa lami. Sasa mvua ikinyesha wasije au?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoteli zetu tukiona wazungu tunapandisha bei, siyo vizuri. Naiomba hasa Serikali iingilie, ibadilike. Wizara inatengeneza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni ufugaji wa nyuki. Ufugaji nyuki ni ajira kubwa sana kwa vijana. Wapewe elimu wajiajiri wenyewe. Tuhamasishe vikundi vya kufuga nyuki wafuge kiutalaam zaidi. Misitu mingi ya nchi yetu inaruhusiwa kufuga nyuki, masoko ni mengi, lakini wanaofuga hawafugi kitaalam, wala hawapati elimu. Jambo hili liangaliwe au lipewe kipaumbele. Kadri tunavyochelewa kutenga bajeti ya kutosha, wakija wawekezaji watajipangia utaratibu wao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuweza kusimama hapa kuchangia Wizara hii ya Maji. Pia naomba niunge mkono hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Mheshimiwa Bobali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wenzangu walivyotangulia kusema maji ni uhai, bila maji hatuwezi kuishi. Nianze na mradi wa Ziwa Victoria wa Shinyanga - Kahama, sisi Ziwa Victoria limetuzunguka lakini sikuona kama huo mradi unaweza kujumuisha hata Mkoa wetu wa Kagera au kugusagusa Bukoba Mjini ambayo ndiyo iko karibu kabisa na Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba Waziri atueleze kama mradi huo unagusa katika Wilaya hiyo ya Bukoba Mjini. Mkoa wetu wa Kagera una matatizo ya maji, wanawake wanapata shida ya maji na sisi tumezungukwa na vyanzo vingi vya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka Mheshimiwa Rais alikuja kuzindua barabara ya Kyaka Bugeni, alitoa ahadi akawaeleza wananchi kwa sababu walimlilia wakapiga magoti, wakamwambia Mheshimiwa Rais tuna shida sana ya maji. Akawaahidi kwamba kuna mradi wa Omlukajunju, akawaeleza Omlukajunju huo mradi uishe haraka sana na Mheshimiwa Maghembe alikuwepo, lakini mpaka sasa hivi huo mradi haujaguswa wala haujasemwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende Bukoba Vijijini, ni matatizo makubwa sana, vijiji ambavyo unaweza ukaenda na hata ukawaonea huruma, wanawake wanaondoka saa kumi usiku wanarudi saa tano hawajapata maji, na maji wanayoyapata ni shida. Wakikuta tayari ng‟ombe ameshapita basi hawapati maji. Kuna Vijiji vya Kikomelo, Lubale, Kibirizi, Nyakibimbiri, Chaitoke, Izimbya, Luhunga na vijiji vingine vilivyopakana pale, vina shida ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanamke akienda kufuata maji anasahau kama nyumbani ameacha mtoto au anasahau kama kuna kula. Hawa watu ninaowasema ni wa kijiji ambacho kimezungukwa na vyanzo vingi vya mito. Kuna Ziwa ambalo linaitwa Ikimba, ni ziwa kubwa ambalo wanaweza waka-supply maji hata katika Vijiji vya Lubale kwenda mpaka Nyakibimbiri lakini tunashindwa kuelewa Serikali inashindwa nini kutenga fedha ambazo zitafanya vyanzo vidogo, kuliko kupanga miradi mikubwa ikashindwa kutekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi inakuwa mikubwa naona li-book lilivyo kubwa, li-book ni kubwa lakini sasa utekelezaji unakuwa mdogo, afadhali kupunguza sehemu nyingine, maji, maji maji ni shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Misenye tumezungukwa na Mto Kagera, Mto Kagera unaweza uka-supply maji katika Mkoa mzima wa Kagera. Ukienda huko sehemu za Misenyi unakuta wanatumia maji ya kwenye mabwawa, wakichelewa watoto wakaenda kuchota watu wengine hawapati maji, yanavurugika yote yanakuwa matope. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni shida, hebu Mheshimiwa Waziri aangalie Mkoa wa Kagera, hivi ulikosa nini huo Mkoa, jamani kila tukisimama hapa watu wa Kagera tunalilia Kagera, afadhali mtusaidie maji na afadhali acha barabara tunazolilia kila siku, lakini maji, maji, maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda sehemu za Izimbya mtoto kuoga ni shida, watoto hawaogi, anaoga mara moja kwa wiki kwa sababu unamwambia mbona hujaenda kufua anasema mimi nafuaga Jumamosi peke yake ni kwa sababu ya maji, siyo kusema anapenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana wageuze macho watuangalie, waangalie Karagwe wana shida ya maji, tuna mito, tuna mabwawa, tuna Ziwa Victoria hatuna hatuna maji, ni aibu. Wawaangalie hao akinamama, wawaangalie watoto, sisi ni watu wetu tunakwenda kuomba kura pale tunatoa ahadi za maji, tunatoa ahadi za barabara, na ahadi hazitekelezeki, itamalizika miaka mitano hata ahadi hizo tunazozisema hazijakwisha, tunazidi kuendelea kutoa ahadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba ni kwamba, sasa wakati umefika wa kutenga bajeti ambayo ni ndogo, ili kila mkoa angalau upate kitu ambacho ni muhimu. Kwa mfano, kama pale Bukoba unaweza ukatenga bajeti ya kusema kwamba halmashauri kwa sababu sisi, Idara ya Maji, sasa hivi wana mradi ambao tunaweza kusema hapa wanatumia vijiji vitano, vijiji vingine ni mwaka ujao, hivyo hivyo kila mwaka unatenga bajeti kidogo kidogo ili watu wote waweze kufikiwa na hayo maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyosema ni mkoa mzima hata ukienda Muleba, mama Tibaijuka yuko pale atakueleza ni matatizo yale yale ya maji hakuna sehemu ambako unasema kuna unafuu, labda wilaya fulani vijiji vitano vinapata maji, viwili havipati maji. Ukienda sehemu za Izimbya ninazozisema wanadanganywa wakati wa uchaguzi, kuna mwaka mmoja mwaka 2003 tulikuwa tuna uchaguzi mdogo, Mheshimiwa Karamagi alikuwa anagombea, Mheshimiwa Karamagi akawaahidi maji, akawaambia chimbeni mitaro, watu wakachimba mitaro wiki nzima, kumbe alikuwa anataka kura, alivyopata kura kwa heri, hawakupata maji mpaka leo hii. Wanasema angalau mtusaidie zile pump za kupiga za maji angalau tupate maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu za Kikomelo, twende Lubale, wanawake wakikuona tu, wanakwambia jamani sisi kura tunawapa lakini jamani maji, hakuna anayekwambia tupe pesa, ni maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana watu wa Kagera muangalie mikoa yao ina matatizo ya maji, hakuna kwenye unafuu na mito tunayo mingi, tuna Mto wa Kagera, tuna vyanzo vingi, Kalebe kuna vyanzo vingi, lakini hakuna maji. Kilimo cha umwagiliaji mmeshatunyima, kilimo ambacho kingesaidia vijana wapate ajira kwa kulima mbogamboga, huko pia hatuko, sasa si unaona kwamba tunasahaulika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende Dar es Salaam watendaji wako hapa, kuna vishoka wa maji, wanaitwa vishoka, ndiyo wanaosababaisha tupate na kipindupindu. Wale usiku kucha wanakata mabomba wanaiba maji usiku, mvua ikinyesha yale mabomba yanarudi tena kwenye matundu yale ya mabomba tayari kipindupindu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, waweke hapa, kuna mtu mmoja ameongea neno nimelipenda, nimependa neno la mawakala, tukiwa na mawakala, haya mengine tusingelalamika ingekuwa ni nafuu, mawakala wanazunguka kwa sababu nashangaa Dar es Salaam usiku kucha ukienda kwenye Mitaa ya Sinza, mimi huwa nafikia Sinza pale, usiku unaweza ukapita pakavu lakini ukirudi barabara imejaa maji, na wakishayakata hawajui tena kuyafunga yasiendelee kumwagika, tayari na yenyewe ni hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliangalie hili kama watendaji wa Dar es Salaam wako hapa wajue, kama wanatengeneza makundi au wanatengeneza timu za kuwa zina-supply kuangalia mitaa maji yanamwagika bure yanaingiliana na maji machafu, yanaingia na kwenye mabomba ya maji machafu tayari kipindupindu na hatutapona kama ni hivyo, tuwe tunaweka watu wa kwenda kuangalia na kuzunguka kuangalia watu wanaokata mabomba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, twende baharini, Ziwani, kuna uharibifu wa mazingira, tungekuwa tunasema watu watachota maji ziwani au baharini lakini huwezi kuyachota yale, ni machafu. Uchafuzi wa mazingira umekuwa mkubwa sana na ndiyo unasababisha wakati mwingine vyanzo vya maji vikauke. Unakuta watu wanalima kwenye vyanzo vya maji, wengine wanayatumia vibaya, kama mito hii kule Kalebe na wapi wanalima mle mle, wakishalima yale maji hata watu kusema labda wakinge ya kuweka kwenye visima hawawezi kwa sababu ni machafu na yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri akija kutujibu hapa, anijibu mradi huo nilimwambia wa kwanza wa Ziwa Victoria kama na sisi tumo Mkoa wa Kagera, atueleze ni lini watakuwa na mikakati ya kuweza kutuvutia maji kutoa Mto Kagera, angalau na Kalebe kupate vyanzo vya Kalebe vyanzo vya Kenyabasa ili watu waweze kupata maji yaliyoko salama kuliko kupata maji ya shida, kwa sababu nimefanya ziara kwa Mheshimiwa Mkuchika, wana matenki ya wakoloni mpaka sasa hivi yako pale, nikauliza hivi maji yanatoka mle wanasema humu hamna maji unaona mbwa wanakokanyaga na paka ndimo tunakochota maji, hiyo ni Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa kwenye kampeni nimeona Tandahimba, nimeona Newala watu wana shida ya maji, ni Tanzania nzima siyo kusema ni Kagera peke yake ni Tanzania nzima, watu wana shida. Nimeshindwa kunywa chai Tandahimba kwa Mheshimiwa Katani; nimekwenda kunywa chai, nilivyofika pale wanasema tumekwenda kuchota maji tumekuta mbwa wamekunywa mle tukashindwa kuyachota, sasa hiyo ni Tanzania ya wapi?. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama ni Tanzania ya viwanda ianzie kwenye Tanzania ya maji, tuje twende kwenye viwanda kwa sababu bila maji hata viwanda hakuna. Sasa tunasema hapa kazi, hapa kazi tunataka kupata maji salama, tunataka kupata elimu, tunataka kupata barabara safi, ndiyo tutajua kwamba hii ni Tanzania ya hapa kazi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie maji mashuleni wamesema wengi…
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.