Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Savelina Slivanus Mwijage (5 total)

MHE. SAVELINA S. MWIJAGE aliuliza:-
Viwanda vingi nchini vimekuwa vya kizamani, vingine vimetekelezwa na wawekezaji na baadhi hufanya kazi kwa kusuasua hasa katika Mkoa wa Kagera.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuviboresha viwanda hivyo ili viweze kufanya kazi vizuri kwa faida ya nchi yetu?
WAZIRI WAVIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vingi vinavyotumia teknolojia ya zamani ambavyo havifanyi kazi au kuzalisha kwa kusuasua vingi ni vile vilivyobinafsishwa. Tathmini iliyofanywa na Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina inaonesha kuwa kati ya viwanda vilivyobinafsishwa, viwanda 24 vinafanya kazi kwa kusuasua na viwanda 37 vimefungwa kote nchini.
Aidha, katika Mkoa wa Kagera kiwanda cha NMC Old Rice Milling kimefungwa wakati kiwanda cha Kagera Tea Co. Ltd (MARUKU) kinafanya kazi kwa kusuasua. Kusuasua kwa kiwanda hiki na vingine vyote nchini kutokana na uchakavu wa mitambo katika baadhi ya viwanda, ushindani katika soko, kupungua kwa mtaji na kutopatikana kwa malighafi nikizungumzia kiwanda changu cha MARUKU.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inashauriana na wawekezaji wa viwanda vinavyofanya kazi kwa kusuasua na vile vilivyofungwa ili kuviwezesha viwanda hivi kufanyakazi. Aidha, majadiliano yanayoendelea pia tunawahimiza kutumia teknolojia ya kisasa katika uzalishaji ili kuongeza tija na kupunguza athari za mazingira zinazohusiana na uzalishaji viwandani. Vilevile tunawashauri wawekezaji walioshindwa kuendesha ipasavyo viwanda vyao kuingia ubia na wawekezaji wengine wenye uwezo wa kuviendesha kwa tija ili tuongeze ajira, tuzalishe bidhaa kwa ajili ya soko la ndani lakini na zaidi walipe kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kwa kushirikiana na mamlaka nyingine itaendelea kulinda viwanda vya ndani kwa kuhakikisha bidhaa zote ziingiazo zinakidhi viwango na zinatozwa tozo stahiki. Aidha, tutahakikisha tunaboresha wepesi wa kufanya biashara kwa kuondoa tozo kero na kuhakikisha kuna umeme wa uhakika kama alivyosema Naibu Waziri wa Nishati.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA (K.n.y MHE. SAVELINA S. MWIJAGE) aliuliza:-
Pamoja na Serikali kuwa na mipango mizuri kwa wananchi wake lakini mipango hiyo baadhi yake haitekelezwi; wakulima wengi nchini wanalima bila ya kuwa na elimu ya kilimo na hivyo kushindwa kulima baadhi ya mazao ya biashara na chakula kama vile ndizi, kahawa, mahindi, maharage, karanga na kadhalika:-
(a) Je, Serikali itawasaidiaje wakulima hao ili wanufaike na kilimo pamoja na mazao yao kwa chakula na biashara?
(b) Je, Serikali ina mipango gani juu ya utoaji wa elimu kwa wakulima ili wafaidike na kilimo chao?
WAZIRI WA KILIMO MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Savelina Silvanus Mwijage, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kutoa elimu kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na tija kwa mazao wanayoyalima. Hatua mbalimbali zinachukuliwa kuhakikisha wakulima wanapata elimu ya kutosha. Mathalani mwaka 2006, Wizara yangu ilianzisha mpango wa kuimarisha huduma za ugani baada ya kubaini kuwa walikuwemo Maafisa Ugani 3,379 tu ukilinganisha na mahitaji ya Maafisa Ugani 15,022.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilichukua hatua kwa kuwasomesha vijana wengi zaidi kwenye vyuo vya kilimo na kuajiri Maafisa Ugani 5,377 na hivyo kufanya jumla ya wataalam kuwa 8,756 kwa sasa ambao wanaendelea kutoa elimu ya kanuni za kilimo bora kwa wakulima. Hata hivyo, bado kuna upungufu wa Maafisa Ugani 6,266 ambao Serikali itaendelea kuajiri kadri fedha itakapokuwa inapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya inaendelea kueneza matumizi ya Vyuo vya Rasilimali za Kilimo vya Kata (Ward Agricultural Resource Centers) ambapo jumla ya vituo 322 vimejengwa katika halmashauri 106 kwenye mikoa 20. Kati ya hivyo, vituo 224 vimekamilika na vinafanya kazi ya kutoa mafunzo kwa wakulima na wafugaji, mashamba ya majaribio, kutoa huduma kwa wafugaji na matumizi ya zana za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Wizara inaandaa na kurusha vipindi vya redio kuhusu kanuni za kilimo bora kupitia Redio ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC). Mwaka wa 2015/2016 jumla ya vipindi 122 vilirushwa ambapo vipindi 52 vilirushwa kupitia TBC Taifa na vipindi 70 vilirushwa kupitia redio binafsi za jamii. Maonesho ya kilimo yanayofanyika kila mwaka kitaifa na katika kanda mbalimbali za kilimo hutumika kama njia mojawapo ya kuwapatia wakulima elimu ya kanuni za kilimo bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu, naomba kuchukua nafasi hii kuziomba Halmashauri zote nchini kukamilisha, kuviwezesha na kuvisimamia Vituo vya Rasilimali za Kilimo vya Kata ili viweze kutoa huduma za kanuni za kilimo bora kwa wakulima kwa mazao mbalimbali wanayoyazalisha.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE aliuliza:-
Mkoa wa Kagera una mabonde mengi ambayo yanaweza kuzalisha vyakula pamoja na mboga mboga hususan mabonde ya Kalebe, Kagera na Kyabakoba:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuyaendeleza mabonde hayo ili vijana waweze kupata ajira?
(b) Je, ni lini Serikali itawapa mikopo wanawake na vijana ili waweze kujiongezea kipato?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Savelina Silvanus Mwijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa yenye fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya kilimo. Aidha, Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa yenye vyanzo vingi vya maji ikiwa ni pamoja na Ziwa Burigi na Ziwa Rwelu na Mito ya Kagera na Rusumo inayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Kwa sasa, Serikali inafanya upembuzi yakinifu, usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni ya mradi wa mabonde yaliyopo Kagera yanayofaa kwa umwagiliaji chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia ambapo mabonde aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge yapo ndani ya mradi huo. Aidha, zoezi la upembuzi yakinifu, usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni unatarajiwa kukamilika Aprili 2017 na baada ya hapo Serikali itaendelea kuwasiliana na wafadhili juu ya utekelezaji wa mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kwa kushirikiana na halmashauri husika inaendelea kuainisha maeneo yanayofaa kwa kilimo hasa kilimo kinachohusisha vijana na utekelezaji wa mpango na mikakati ya kuhakikisha vijana wengi wanajiajiri kupitia sekta ya kilimo. Suala la upatikanaji wa ajira kwa vijana na wanawake linachukuliwa kwa uzito wa hali ya juu hasa ukizingatia vijana kuwa ni takribani asilimia 67 ya nguvukazi ya Taifa kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) pamoja na wadau wengine wa maendeleo tayari inafanya upembuzi yakinifu kwa kutembelea maeneo mbalimbali nchini ili kuainisha shughuli za vijana pamoja na kuhamasisha kujiunga katika vikundi, kuongea na Serikali za Mitaa ili kubaini changamoto ambazo vijana wanakabiliana nazo wakati wa shughuli zao za kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara zingine za kisekta pamoja na sekta binafsi tayari imetayarisha mkakati wa kuhusisha vijana katika sekta ya kilimo uitwao National Strategy for Youth Involvement in Agriculture wa miaka mitano ambao utasaidia kuweka mzingira bora ya utekelezaji wa mipango kutoka kwa wadau ili kuwanufaisha vijana. Mkakati huu ulizinduliwa mwezi Oktoba, 2016.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE Aliuliza:-
Nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ni za muda mrefu na zimekuwa chakavu sana na nyingine zimeanza kubomoka.
(a) Je, ni lini Serikali itafanya operesheni kubaini uharibifu ulioko kwenye nyumba hizo?
(b) Je, ni lini Serikali itatenga bajeti kwa ajili ya kukarabati au kujenga upya nyumba hizo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Savelina Silvanus Mwijage, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambazo ni za muda mrefu na kati ya hizo zipo zilizo katika hali chakavu ambazo idadi yake si kubwa sana ukilinganisha na nyumba zilizo katika hali nzuri kimatengenezo. Ili kuhakikisha nyumba zote zinakuwa katika hali nzuri na bora kimatengenezo, Shirika limeweka mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba nyumba zote zilizo katika hali ya uchakavu zinafanyiwa ukarabati mkubwa na kwa nyumba ambazo kiwango cha ukachakavu ni kikubwa sana (beyond repair) shirika limeweka utaratibu wa kuzivunja na kuendeleza upya viwanja hivyo kwa kujenga majengo ya kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Nyumba la Taifa limefanya uhakiki wa nyumba zake zote na kubaini hali halisi ya kila nyumba na kuweka mpango wa kuzifanyia ukarabati nyumba hizo kwa awamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 shirika lilitenga takriban shilingi bilioni 11, kwa ajili ya kuzifanyia ukarabati nyumba zake ambapo hadi Machi, 2017 jumla ya nyumba 2,451 zilikuwa zimekwishafanyiwa ukarabati mkubwa kupitia bajeti hiyo. Aidha, idadi ya nyumba zilizofanyiwa ukarabati mkubwa inatarajiwa kuongezeka ifikapo mwisho wa mwezi Juni, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, shirika linatarajia kumaliza kuzifanyia ukarabati nyumba zote katika Mwaka wa Fedha 2017/2018. Hata hivyo, ni vema ikafahamika kuwa matengenezo ya nyumba ni kazi endelevu kwa shirika, hivyo bajeti ya matengenezo itaendelea kutengwa kila mwaka ili wapangaji wa nyumba za shirika waendelee kuishi katika nyumba na mazingira bora.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM (K.n.y. MHE. SAVELINA S. MWIJAGE) aliuliza:-
Serikali ilitoa tamko kuwa watoto chini ya miaka mitano, wazee pamoja na wagonjwa wa UKIMWI na TB watibiwe bure.
(a) Je, Serikali imetekelezaje mpango huo?
(b) Je, makundi hayo yameshaanza kupata matibabu bure kama ilivyopangwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri makini, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Savelina Silvanus Mwijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutekeleza Sera ya Afya ya mwaka 2007 ya kutoa huduma bila malipo kwa watoto chini ya miaka mitano, akina mama wajawazito na wazee wasio na uwezo ambapo sera na mwongozo wa uchangiaji unaelekeza wazi kuwa makundi haya hayapaswi kugharamia huduma za afya pale wanapohitaji. Pia wagonjwa wa UKIMWI na TB wamekuwa wakipata matibabu bure pale wanapohudhuria kliniki kupata dawa na ushauri nasaha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi cha mwezi Julai, 2015 hadi Juni, 2016 jumla ya watu 839,574 waliopatikana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI wamepatiwa huduma za dawa za kupunguza makali ya VVU. Kuanzia mwezi Oktoba, 2016 Wizara imeanza kutoa dawa za ARV kwa watu wote wenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI bila kujali kiwango cha CD4 badala ya kuanzia CD4-500 kama ilivyokuwa hapo awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile huduma hii hailipiwi. Huduma zote ni kwa gharama za Serikali. Takribani watu 1,200,000 wanatarajiwa kuhudumiwa katika mpango huo. Tutahakikisha kila mtu anayepima virusi vya UKIMWI na kugundulika na maambukizi, anapatiwa dawa ikiwemo wazee na watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano wameendelea kupata huduma za matibabu bila malipo katika vituo vyote vya Umma vya kutolea huduma. Huduma hizo ni pamoja na chanjo zote zinazotolewa kwa watoto pamoja na huduma nyingine zote bila malipo yoyote. Kutokana na juhudi hizo, tumeweza kufikia wastani wa asilimia 97 ya kiwango cha chanjo nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tiba kwa wazee, Serikali imekuwa pia ikitekeleza mpango wa huduma ya matibabu bila malipo kwa wazee wasio na uwezo nchini kote. Aidha, wazee katika maeneo mengi wametengewa maeneo ama madirisha maalum ya kuwapatia huduma kwa haraka bila bughudha. Ninaendelea kuwataka watumishi katika sekta ya afya nchini kuhakikisha wanatekeleza sera hiyo ya kutoa huduma kwa wazee wasio na uwezo bila malipo kwa umakini mkubwa zaidi.