Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Savelina Slivanus Mwijage (16 total)

MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wilaya ya Bukoba Vijijini wanategemea Wilaya yao iliyoko Bukoba Mjini na ina umbali mkubwa sana, kata zake ziko mbali sana kuja kufika Bukoba Mjini, ni lini Serikali itaona umuhimu wa watu wa Bukoba Vijijini kupata Wilaya yao karibu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika hili tumelichukua, lakini mchakato wa Wilaya, mchakato wa Halmashauri upo na una taratibu zake. Mimi naomba niwahimize ndugu zangu wa Bukoba na Mheshimiwa Mbunge hapa nadhani katika hili atakuwa amejipnga vyema, tufuate ule mchakato wa kawaida, tupitishe katika Halmashauri zetu, tupitishe katika vikao vya DCC, RCC, mwisho wa siku ikifika katika Ofisi ya Rais -TAMISEMI jukumu letu kubwa ni kuweza kuangalia matakwa ya jamii na kuangalia mahitaji ya msingi yakiwa yamekamilika basi tutamalizia hilo zoezi. Ahsante sana.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa kituo cha Chalinze ni kituo ambacho kiko kwenye barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma na kituo hicho hakina computer hata photocopy hakuna.
Kwa hiyo, ukipata tatizo wanaenda kutoa photocopy nje kwenye stationery. Ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuwawekea photocopy machine ya kuwa wanatumia kuliko kusambaza nje siri za kituo hicho?
WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, juzi tu Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo hilo alinipigia simu, tuliongea naye na hayo anayosema Mheshimiwa Mbunge tuliyazungumza. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi ajue kwamba na Mbunge wa Jimbo hilo ameshanieleza tatizo hilo na tutalitatua.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana.
Kwa kuwa, viwanda vilivyopo Mkoa wa Kagera hasa ukiangalia Kiwanda cha TANICA kimejengwa mwaka 1967, kiwanda cha BUCOP 1967 na Kagera Sugar 1990. Viwanda vyote vimekuwa chakavu na viwanda vyote havifanyi kazi vizuri, tukitegemea Serikali au kutegemea wawekezaji ili waweze kuvitengeneza au kuviboresha tutakuwa tunaenda sehemu ambayo siyo nzuri.
Je, ni lini Serikali itaviboresha angalau vikawa viwanda vya kati?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Mkoa wa Kagera tuna wazalishaji wengi wa matunda na wazalishaji wengi wa maziwa, Mkoa wa Kagera hatuna hata SIDO angalau ya kuweza kujumuisha Mkoa mzima, je, ni lini Serikali itaweka viwanda vya kuzalisha matunda na kuweka viwanda vya SIDO ili vijana wapate ajira?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uboreshaji wa viwanda vilivyopo na mfano wake aliotolea ni Kagera Sugar, mmiliki wa Kagera Sugaranawekeza kisasa kutoka tani 60,000 za sukari anazozalisha akilenga tani 120,000. Nimefanikiwa kuongea na Waziri wa Uwekezaji wa Oman ambako kutoka tani 120,000 Kagera Sugar atazalisha tani 180,000 ili kusudi Kagera Sugar izalishe tani 300,000 tutosheleze soko la ndani na kupeleka Oman.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maziwa na matunda, Kagera ni eneo lenye fursa nzuri ya kuwekeza kwenye maziwa. Mkakati tulionao nawasiliana na wajasiriamali wenye Kampuni ya GESAPU Agro Farming ambao watawekeza pesa karibu bilioni 14, watatengeneza mtandao wa kukusanya maziwa kuanzia Chato kwenda Geita mpaka Kagera na wataweka kiwanda Misenyi na mimi niko tayari kupambana nao ili wafanikiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu SIDO Mheshimiwa Mwijage nitahakikisha SIDO inaanzia Kagera na inasambaa nchi nzima kwa nguvu zaidi.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa matatizo ya Itigi ni sawasawa na matatizo ya Wilaya ya Biharamulo hasa msitu tunaokatisha wa Kasindaga Muleba una matatizo ya mawasiliano na pale kuna barrier nyingi za maaskari ambao wanakaa pale saa zote. Ni lini Serikali itaweza kuwawekea mawasiliano pale hata mnara mmoja angalau wa Tigo au Vodacom?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASIALINO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu wa fedha wa 2016/2017 Serikali ina mpango wa kupeleka mawasiliano maeneo yote ambayo yana matatizo ya mawasiliano. Moja kati ya eneo hilo ni hilo alilosema Mheshimiwa Mbunge.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana. Kwa kuwa milipuko hii inaleta matatizo ya afya ya wananchi walioko karibu na sehemu ya mashimo hayo na kuacha mazingira yakiwa na mashimo. Je, ni lini Serikali itakuwa inahakikisha afya za watu hao zinakuwa sawa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikubaliane nae kwanza, kwamba, shughuli za madini hufanyika na kuacha madhara kiafya. Kuhusu ni lini, ni wakati wote shughuli za madini zinapofanyika tunatakiwa tuhakikishe kwamba afya za wananchi pamoja na wachimbaji zinabaki salama.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kabla sijauliza swali langu, naomba kuwashukuru wale wote ambao wanatoa misaada kwa Wilaya yangu ya Bukoba Mjini na naomba Watanzania wote na wasio Watanzania waangalie kwa jicho la huruma Bukoba Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kumuuuliza Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa Wizara yake inalinda raia na mali zao, hivi sasa Wilaya ya Bukoba Mjini watu wote wanalala nje na matatizo wanayoyapata ni kuibiwa mali zao na askari wanakwenda na kukamata wale watu ambao wanawasaidia wale wahanga. Je, Wizara yake imejipangaje kwenda kukabiliana na janga hili Bukuba Mjini kwa kuwalinda raia?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa jambo alilolileta ambalo liko muda huu. Niseme tu tangu tukio limetokea Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama Mkoa na Wilaya wameimarisha ulinzi katika maeneo husika. Kwa kuwa watu ni wengi inatokea katika kutafuta namna ya kujiridhisha kujua yupi anayeenda kwa ajili ya kutoa huduma na yupi anayeenda kwa ajili ya kukwapua ama kuchukua vile ambavyo vimezagaazagaa, kwa hiyo, ndiyo maana utaona kuna mwingiliano wa aina hiyo, lakini nia ya Wizara pamoja na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya ni kuhakikisha kwamba watu hawa ambao wamepata matatizo wao pamoja na mali zao wanakuwa katika hali ya usalama.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wakati wa Bunge la Tisa hili suala nililiuliza ikawa upembuzi yakinifu, sijui upembuzi yakinifu unachukua miaka mingapi kuweza kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama suala langu linavyosema na yeye mwenyewe Mheshimiwa Waziri amekiri, Mkoa wa Kagera sisi hatujawahi kuomba chakula; tunachoiomba Serikali ni kuwapa elimu wana-Kagera waweze kuwa na chakula cha kutosha. Kama hivi sasa tuna matatizo ya njaa, lakini ni mara ya kwanza, tungekuwa na utaalam wa kilimo cha umwagiliaji tusingekuwa na matatizo ya njaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ni lini Serikali itaupa kipaumbele Mkoa wa Kagera kwa kila kitu? Kwa kuwa kila kitu tunachokisemea kinakuwa ni kesho, kesho, hata na haya maafa itakuwa ni kesho. Ni lini Serikali itaona huruma kwa kuwapa elimu vijana na wanawake wakawa na chakula cha kutosha pamoja na chakula cha kuleta uchumi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema, kwamba upembuzi huwa unaelekea kuchukua muda mwingi kuliko ilivyopangwa, lakini kama nilivyosema tunatarajia sasa utakamilika mwaka unaokuja. Kwa hiyo baada ya hapo hatutakuwa tunazungumzia tena kuhusu kuchelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kuhusu Serikali kupeleka wataalam wa kilimo, nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba, tayari katika Serikali za Mitaa katika Halmashauri zetu tuna Maafisa Ugani wa Kilimo ambao wanafanya kazi za kutoa elimu kwa ajili ya kilimo na Wizara yangu imeweka mazingira wezeshi ya kisera ya kuhakikisha kwamba wataalam hao wanaotoa elimu wanatoa elimu sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mara nyingi vikwazo vimekuwepo kwamba hawana nyenzo, hata hivyo Serikali inaendelea kuboresha shughuli za ugani ili wananchi waweze kunufaika na elimu ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba, kuhusu vijana, Wizara yangu iko tayari muda wowote kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge ili kuangalia namna gani tunaweza kuwawezesha vijana kushiriki katika kilimo. Tayari katika Bunge hili kuna Mbunge mmoja, ambaye anashirikiana vizuri sana na Wizara yangu, Mheshimiwa Ester Mmasi, ambaye kupitia kwake na jitihada zake kwa vijana, tayari tumewafikia vijana 500 na tayari tumewapatia ardhi katika maeneo mengi; tayari tuko katika jitihada za kuwaunganisha na mabenki kwa ajili ya kupata mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimkaribishe sana Mheshimiwa Mbunge aje ofisini kwetu, tukae, tuongee tuangalie namna gani tunaweza tukawasaidia vijana wa Kagera ili waweze kuondokana na tatizo la ajira. Vilevile, niseme kwamba, tunawapongeza sana watu wa Mkoa wa Kagera kwa sababu ni kweli kama alivyosema kwa miaka mingi sana wamekuwa wakijitosheleza kwa chakula na hata sasa ambapo changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi yametokea, Serikali yao bado itaendelea kuwa nao ili kuhakikisha kwamba, wanaweza kukabiliana na hizo changamoto ili waendelee kujitegemea kwa chakula.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa nyumba nyingi zimefanyiwa ukarabati kama alivyosema Naibu Waziri, Bukoba Mjini kuna majumba ya NHC yaliyochakaa yanaonesha Mji kuchafuka kwa ajili ya nyumba hizo za NHC.
Je, ni lini Serikali itafanyia ukarabati au kujenga
majengo mapya ya NHC?
Swali la pili, kuna majengo ambayo yamechakaa yako kwenye mtaa wa Miembeni watu wameishi muda mrefu hayana miundombinu hayana sehemu za kuingilia watu wenyewe waliopanga mle ndio wanajiwekea miundombinu na Serikali inakusanya ushuru na inakusanya kodi za majengo.
Je, ni lini Serikali itajenga nyumba mpya au
kuwaruhusu wale waliomo ndani kuzinunua?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwijage amezungumzia suala la ukarabati wa nyumba za Bukoba zilizo chakavu. Kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi nimesema suala la ukarabati ni suala endelevu na pale ambapo nyumba zinaonekana zimechakaa haziwezi tena kufanyiwa ukarabati, shirika linabomoa nyumba zile na kujenga majengo mengine mapya.
Kwa hiyo, niseme kwamba kama nyumba za Bukoba anavyosema kwamba zimechakaa, zinahitaji ukarabati nadhani bado tutaangalia kwa sababu Meneja yupo pale anaziona na anajua na ndiyo maana nimesema ukarabati huu unaendelea nchi nzima, kwa hiyo na Bukoba pia ni moja ya eneo ambalo litaangaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili eneo la Miembeni nyumba zilizoko ni chakavu na hazina miundombinu. Kama nilivyosema jibu la msingi kama ni chakavu na haziwezi kufanyiwa ukarabati nadhani jukumu lililopo ni kubomoa na kujenga nyumba nyingine mpya na watu wakakaa katika mazingira yaliyo mazuri. Hatakubali kuendelea kuwa na nyumba ambazo ni chakavu na hazina
uwezekano wa kufanyiwa repear. Kwa hiyo, ni jukumu la Shirika la Nyumba tutawatuma waende waangalie hizo ambazo hazina miundombinu na haziwezi kukarabatika tena tuone utaratibu wa kuweza kuzijenga upya katika hali hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, umilikishaji kwa wananchi ni kwamba sasa hivi kuna ule utaratibu wa mpangaji mnunuzi, kwa hiyo, kuna maeneo ambayo kuna hizo nyumba ambazo zinajengwa bado mpangaji anaweza kuwa mnunuzi kwa hiyo mtu atamilikishwa nyumba pale atakapokuwa amelipia nyumba yake na amefikia mwisho wa gharama ya nyumba husika.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa ahadi za barabara ya Karagwe kwenda mpaka Benako kutoka Nyakaanga zimekuwa kero kwa muda mrefu; nimeingia Bungeni mwaka 2005 barabara ya kwenda mpaka Mlongwe nimeiongea barabara ya kutoka Nyakaanga kwenda Benako nimeiongea:-
Ni lini Serikali itachagua moja; kutengeneza upande
na mmoja kuumaliza na kuingia wa pili? Mnatafuta ma-engineer na Wakandarasi ambao hawana viwango. Barabara unatengeneza siku mbili, tatu, barabara inaharibika. Lini mtatafuta ma-engineer wa uhakika wa kutengeneza barabara zikawa za viwango?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia Mheshimiwa Mbunge kwa makini anachokiongelea. Huwa naamini kwamba tunachagua Wakandarasi makini, ila kwa kauli yake inaonekana tunatakiwa tuongeze nguvu zaidi na macho yaangalie zaidi ili kuhakikisha kweli tunapata Wakandarasi wanaoweza kusaidia kufanya kazi bila kurudia rudia mara nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa ushauri wake.
MHE. SEVERINA S. MWIJAGE. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa mradi wa Shinyanga – Kahama uko karibu sana na Bukoba, ni lini Serikali itafanya upembuzi yakinifu kuunganisha maji kuanzia Wilaya ya Muleba, Bukoba Mjini na Wilaya zingine zilizopakana kwa sababu tunapata matatizo ya maji na sisi tuko karibu na mradi huo, ni lini Serikali itaunganisha maji kuwapa watu wa Bukoba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza maji Bukoba tayari, mradi tumeshakamilisha na wananchi wanapata maji. Kazi iliyopo sasa hivi ni kuendelea kutanua mabomba ili yale maji yaweze kufika kwenye maeneo mengi. Kwa hiyo, kwa Mji wa Bukoba maji tayari tunayo.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwa kuwa Hospitali ya Wilaya ya Bukoba Vijijini, ni hospitali ya mission na leo hii walivyotoa ambulance imekwenda kwenye Zahanati ya Kishanje. Ni lini Serikali itapandisha hadhi Hospitali ya Mission ambayo tayari wameshakubali kuitoa Serikali, kuwa hospitali ya wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tumesikia lile suala la ambulance alilizungumza nadhani hii ni mara ya pili, kwamba maelekezo ilitakiwa iende katika kituo kingine na nimesema kwamba nitafika kule site kufanya verification, maagizo yalikuwaje na hii ambulance imeenda wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kuhusu mchakato wa kuipandisha hii hospitali tutapitia mikataba, tutawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Afya kuangalia nini kilichopo na jambo lipi ambalo ni rafiki zaidi tunaloweza kulifanya kwa mustakabali wa wananchi wa Bukoba. Kwa hiyo, tunachukua haya mawazo lakini lazima tufike field pale tuangalie uhalisia wa jambo lilivyo ili tupate majibu muafaka kusaidia wananchi wa Bukoba.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa matatizo ya Kibondo ya Madaktari wa meno ni sawasawa na matatizo ya Wilaya ya Bukoba Vijijini ya Izimbya - Katekana hawana Daktari wa meno hata mmoja wakipata tatizo la ugonjwa mpaka waende Bukoba Mjini na ni mbali sana kutoka pale kwenda Bukoba Mjini. Ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuwaletea Madaktari wa meno wa kuwasaidia hao watu wa Bukoba Vijijini?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso kuhusu upatikanaji wa dawa za kisukari na ongezeko la wagonjwa wa kisukari nchini. Ni kweli sasa hivi tunashuhudia ongezeko la wagonjwa wa kisukari lakini kwa sababu kwanza ya mfumo wa maisha ambao watu wanaishi, watu hawafanyi mazoezi, wanakula vyakula bila kuzingatia lishe lakini bila ku-check afya zao mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kubwa badala ya kujikita kwenye kutibu tumejikita kwenye kuzuia Watanzania wengi wasipate maradhi ya ugonjwa wa kisukari. Pale ambapo Mtanzania ana ugonjwa wa kisukari kwa mujibu wa Sera ya Afya dawa ya mgonjwa wa kisukari inatakiwa kupatikana kwa bei nafuu. Kwa hiyo, tunawaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanapoandaa maoteo ya dawa basi wahakikishe pia wana-order dawa za kutosha kwa ajili ya wagonjwa wa kisukari. Kama hawawezi ku-order za kutosha sisi hatuwezi kuwapelekea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili la uhaba wa Madaktari wa Meno, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri na hata wakati wa bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Utumishi alitoa maelezo kwamba Mheshimiwa Rais ameridhia kuajiri watumishi wa Serikali takriban 52,000 na kati ya hao tunategemea kupata watumishi wa sekta ya afya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Savelina Mwijage tutakapopata kibali tutawapanga pia kwa ajili ya hospitali za Mkoa za Kagera. Ahsante sana.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa Mkoa wa Kagera una ardhi kubwa ambayo inatumika hata kwa kuingiza wafugaji haramu na majambazi na kwa kuwa wewe Mheshimiwa Waziri ni mzaliwa wa Mkoa wa Kagera.
Ni lini utaiona Kagera kuweka viwanda angalau vya kuchakata kahawa, majani na vyakula mbalimbali ili tukajivunia kwamba tumekuwa na Waziri wa Viwanda na Masoko? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unitendee haki. Naulizwa mara ya pili swali hili. Mimi ni muumini wa Muammar Gaddafi, alianza kujenga mbali na kwao, akamalizia kwao.
Kuhusu Kagera, mapping ya viwanda Kagera, naomba nitoe jibu. Kagera ina fursa ya kujenga viwanda vya maziwa. Kinachofanyika sasa, tunatafuta mwekezaji wa kuweka Kiwanda cha Maziwa ili sasa soko lije livute uzalishaji. Tulikuwa na ufugaji wa ng’ombe, hatukufanya vizuri, sasa tunatafuta wawekezaji waweke viwanda vikubwa vya maziwa, ni rahisi kwa uoto wa Kagera kuweza kufuga ng’ombe wa maziwa, mkapata maziwa na by product.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikueleze, wapo vijana wajasiriamali na tumeshawaelekeza mahali pa kwenda kusudi waweze kujasiria. Shangazi usiwe na wasiwasi siwezi kuwa ngariba wa Kilwa. (Makofi)
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Gereza la Bukoba Mjini linakuwa na msongamano mkubwa sana wa wafungwa na tuna Magereza ambazo zimechakaa sana kwa mfano kama Kitengule, Rwamlumba ni lini Serikali itapanua hiyo Rwamlumba ili kuweza kuwapunguza wafungwa walioko Bukoba Mjini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukitenga pesa za bajeti kuongeza mabweni mwaka hadi mwaka na hii ni kwa sababu ya kutambua changamoto za msongamano wa Magereza yetu nchini. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hilo tumelipokea, tutajitahidi katika mwaka wa fedha ujao tuweze kuweka Gereza Bukoba Mjini miongoni mwa Magereza ya vipaumbele vya kuongeza mabweni ili kupunguza idadi ya msongamano katika Magereza yetu nchini.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa kuwa sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji ni sekta ambayo inapata shida sana kwa wananchi wetu. Ni lini Serikali itaona sasa wakati umefika kuwapa elimu ili wakanufaika na kilimo, mifugo na uvuvi wakaacha kuwa wanakamatwa mara kwa mara hasa wavuvi wanachomewa nyavu zao ni kwasababu hawapati elimu. Lini Serikali itajikita sana kuwasaidia hao wananchi maskini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu swali la Mheshimiwa Nassari, niseme tu kwamba Serikali hufikisha elimu kwa wakulima, wafugaji pamoja na wavuvi kupitia huduma za ugani na nieleze tu kwamba katika uvuvi kawaida tunatumia beach management unit kama njia sahihi ya kuwafikia wavuvi walio wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu mara nyingi hata wavuvi wanaofanya uvuvi haramu sio kwamba hawajui kwamba ni tatizo lakini wanafanya kwa kukusudia. Hata hivyo, Serikali itaendelea kutoa elimu na kusisitiza wananchi wetu wafanye uvuvi ambao unakubalika kisheria.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa ugonjwa wa TB unaenea kwa hewa na sanasana naona Wizara inahamasisha sana watu kujikinga na UKIMWI lakini sijaona wanaweka nguvu sana kwenye ugonjwa wa TB na umeenea kwa kasi sana. Ni lini Serikali itatoa hamasa na kuwajulisha watu ugonjwa wa TB kuwa ni mbaya sana kwa vile huenea kwa hewa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ugonjwa wa Kifua Kikuu ama Tuberculosis unaibuka tu kwenye mwili wa mwanadamu, pale ambapo kinga yake imeshuka. Ndiyo maana sasa unauona upacha wa maambukizi ya Virusi vya UKIMWI, UKIMWI pamoja na Kifua Kikuu, sio kwamba ugonjwa haupo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana hata sisi wazima na tuna afya tuna vimelea vya Mycobacterium tuberculosis kwenye miili yetu lakini havitajionyesha mpaka tutakufa navyo kama hatutoshusha kinga za mwili wetu. Kwa hiyo, kwanza tuepuke maambukizi ya Virusi vya UKIMWI, lakini pili tuwe na tabia ya kupima afya zetu kwa kweli ili tuweze kudhibiti magonjwa kama haya kabla hayajatokea.