Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Eng. Joel Makanyaga Mwaka (9 total)

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Natambua umuhimu wa Mpango kwamba, ndiyo dira ya maendeleo ya nchi kwa maana ya kujua tunatoka wapi, tuko wapi na tunataka kwenda wapi, tunakwendaje na kwa sababu gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Waziri kwa Mpango huu. Naomba nichangie kwa kuzingatia kwamba mimi ni Mbunge wa Jimbo la Chilonwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, miundombinu; barabara zinazounganisha Wilaya, (maeneo mbalimbali na Makao Makuu ya Wilaya), ni mbaya sana na hazipitiki vizuri. Hii inafanya uchumi wa Wilaya inayotegemea sana ushuru wa mazao inakuwa mbaya sana. Kwa kuwa wanunuzi wengi wanafika kwa tabu na hivyo wananunua mazao kwa bei ya chini sana jambo linalodidimiza pia uchumi wa wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kuangalia kwa makini na kuzisaidia Halmashauri na hasa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kwa kujenga madaraja muhimu strategic kama haya yafuatayo:-
(a) Daraja linalounganisha Kijiji cha Msanga na Kijiji cha Kawawa.
(b) Daraja linalounganisha Kijiji cha Chilonwa na Kijiji cha Nzali.
(c) Daraja linalounganisha Kijiji cha Dabalo na Kijiji cha Igamba (Dabalo B)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, viwanda; Wilaya ya Chamwino na Jimbo la Chilonwa kwa jumla hakuna kiwanda chochote. Tunahitaji Agro-Based Industry/Factory na hasa cha ku-process zabibu. Jambo hili litainua uchumi wa mtu mmoja mmoja, lakini pia kukuza uchumi wa Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na kuunga mkono mpango mzima na kuomba hayo niliyoyaainisha hapo juu yafanyiwe kazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono mikakati mbalimbali inayochukuliwa na Wizara hii. Natambua changamoto nyingi zilizo mbele katika kutekeleza mikakati hii. Naunga mkono hoja kwa kusisitiza yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo ndiyo uti wa mgongo na unahitaji kupewa kipaumbele kwa kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo zote zinazohitajika kwa wakati; lakini vile vile tunapozungumzia viwanda hapa nchini ni lazima tujue kwamba viwanda vinategemea mazao yatokayo shambani (kilimo).
Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu kwa maana ya barabara ni muhimu sana kwani mazao hayo kutoka mashambani, ili yafike kiwandani kwa gharama nafuu, ni lazima yapite kwenye barabara zinazopitika kirahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia viwanda ni muhimu ili mazao yetu yapate soko la uhakika. Ndani ya Jimbo la Chilonwa tunalima sana zao la zabibu, lakini soko lake ni baya sana kwa kuwa, hakuna kiwanda cha uhakika cha kuweza ku-process zabibu. Naomba Wizara hii isaidie kuweka msukumo kwa Wizara za TAMISEMI na Viwanda kuweza kuharakisha ujenzi wa kiwanda cha uhakika cha ku-process zabibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya uhakika yatakayotupeleka kwenye nchi ya uchumi wa kati yatapatikana kwa kuwa na viwanda, tena viwanda vinavyotumia mazao yetu kama malighafi yake. Kufikia uchumi wa kati ni kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja ambao kwa ujumla wake ndio utakaopandisha uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza na kuunga mkono hoja ya Wizara kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijielekeza Mkoani kwangu Dodoma, Wilayani kwangu Chamwino na Jimboni kwangu Chilonwa, naomba kuomba yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweke mazingira rahisi kwa wananchi wa Jimbo la Chilonwa kuweza kukipa na kuanzisha viwanda vidogo vidogo vinavyochakata/process mazao yanayozalishwa jimboni kama vile mashine za kukamua alizeti, ufuta pia, mashine za ku-process mahindi na kuuza sembe mijini badala ya kuyauza mahindi (value addition).
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kipekee zao la zabibu ambalo kwa hakika ndio mkombozi wa uchumi wa wananchi wa Dodoma ambao bado unasinzia. Kwa zabibu naiomba Wizara ifanye kufuatilia Halmashauri ya Chamwino ili kuisaidia kufanikisha ujenzi wa kiwanda cha zabibu cha kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha kisasa ni kile kitakachowezesha uzalishaji wa juice, mvinyo na concentrate ya mvinyo. Hiki ni kiwanda tofauti na vile vidogo vidogo na vichache vilivyopo vinavyozalisha mvinyo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Wizara hii kama ifuatavyo:-
Nampongeza Mheshimiwa Waziri, Profesa Muhongo kwa hotuba yake nzuri iliyosheheni mambo muhimu kuhusiana na nishati na madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza kwa kupewa/kutengewa bajeti kubwa kwa lengo la kuboresha mambo ya nishati ambayo ni muhimu sana katika kuipeleka nchi yetu kwenye uchumi wa kati. Naomba nimwombe Mheshimiwa Waziri kwamba, wajitahidi kuhakikisha mipango inakwenda kama ilivyopangwa kwa faida ya wananchi wote wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri yafuatayo katika Jimbo langu la Chilonwa:-
Umeme wa REA Phase II ulikuwa ufike hadi Kata ya Zajilwa, Kijiji cha Zajilwa, lakini haujafika, naomba sasa ufike.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba umeme katika REA Phase III uende pia, maeneo yafuatayo:-
Vijiji vya Gwandi Bwawani na Magungu vilivyo Kata ya Zajilwa; Vijiji vya Izava, Umoja, Segala, vilivyo Kata ya Segala; Vijiji vya Ikombo, Solou na Itiso vilivyo Kata ya Itiso; Vijiji vya Manyemba, Chiwondo, Igamba, Nayu, vilivyo Kata ya Dabalo; Vijiji vya Chitabuli, Mlimwa, vilivyo Kata ya Membe; Vijiji vya Bwawani na Chalinze B vilivyo Kata ya Manchali; Vijiji vya Mlebe, Msamalo, vilivyo Kata ya Msamalo; Vijiji vya Makoja, Butiama, Ikowa, vilivyo Kata ya Ikowa; Kijiji cha Humekwa, kilicho Kata ya Haneti na Kijiji cha Kawawa kilicho Kata ya Msanga.
Mheshimiwa Spika, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, naomba nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitamke kwamba kwa vile leo ni mara yangu ya kwanza kusimama na kuchangia katika Bunge hili, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kwa kishindo mwaka 2015, lakini nimpongeze vilevile kwa kutufanyia kazi kubwa ya kutupatia Baraza la Mawaziri zuri sana. Tunaona kazi wanayoifanya na kila mtu anaiamini. Na mimi naomba nichukue fursa hii kuwaambia Mawaziri wachape kazi, tuko nyuma yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo nitamke vile vile kwamba kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama na kuchangia, niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Chilonwa, ambao waliona waniamini na mimi niwawakilishe katika mjengo huu katika kuleta matatizo yao na kushirikiana kutatua matatizo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mwigulu kwa hotuba yake nzuri ambayo ametupa asubuhi hii kupitia kitabu hiki ambapo amejikita vizuri katika masuala ya kilimo na nyanja zake zote. Amegusia kila eneo na namna gani Wizara yake inajipanga, kufanya kwa ajili ya Watanzania; lakini pia katika nyanja za mifugo, pamoja na sekta zote. Ameeleza kwa umakini kabisa, ni nini Serikali inataka kutufanyia sisi Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo amekwenda kwenye suala la uvuvi na sekta zake zote, masuala ya kupanga siku zote yana changamoto, na sisi tuko hapa leo kuijadili hii hotuba yake kwa lengo la kuonesha changamoto zilizopo tukitegemea kabisa kwamba watazichukua na kuzifanyia kazi na kuboresha yale ambayo wanakusudia kuyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii sasa nijielekeze kwenye Jimbo langu la Chilonwa. Jimbo la Chilonwa tunalima sana, lakini huwa tuna matatizo ya hapa na pale ya mvua. Jimbo la Chilonwa tunafuga kwa kiasi chake, tatizo hatuna uvuvi kwetu. Nikizungumzia suala la kilimo, naomba sana kwa upande wa pembejeo ambapo imeonesha dhahiri kwamba safari hii pembejeo zitapatikana kwa wakati na pembejeo zinazostahili. Isiwe kwamba tunaletewa mbegu ambazo unapanda hazioti tena, isiwe kwamba tunaletewa mbegu wakati wa kupanda umepita. Tunaamini haya yaliyozungumzwa hapa ndani ndiyo yatakavyotekelezwa na sisi tunaomba iwe hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kilimo ni biashara. Pale inapokuwa mwananchi analima halafu anakosa sehemu ya kupeleka mazao yake, au analima inakuwa ngumu sana kwake kusafirisha mazao yake kuyapekeka kunakostahili, linakuwa tatizo kubwa sana. Tatizo la miundombinu kuingia vijijini hebu lifanyiwe kazi. Najua Serikali inajipanga, lakini naomba nisisitize kabisa, lifanyiwe kazi na hasa katika Jimbo langu la Chilonwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanalima sana mahindi na kwa taarifa yako, najua Wabunge wengi tunajua humu, mahindi ya Dodoma yana soko kubwa sana duniani. Mahindi ya Dodoma hayatumii kemikali. Dodoma hatutumii mbolea za chumvi chumvi hata siku moja! Dodoma tunahitaji mvua tu! Tatizo letu ni mvua, ndiyo inayotusumbua. Kwa hayo, mazao kidogo tunayopata, yana soko kubwa sana. (Makofi)
Kwa hiyo, naiomba sana Serikali itusaidie kutuwezesha mazao yetu yafike sehemu yanapotakiwa kwenda kiurahisi. Inapokuwa ngumu kuyafikisha mazao sokoni, wanunuzi, walanguzi au wafanyabiashara, wanakuwa na sababu ya kununua mahindi kwa bei ya chini sana. Kama atasafiri kwenda vijijini kwa shida sana, njia haipitiki, anachukua siku tatu kufika sehemu ambayo angetumia masaa mawili, matatu, kwa vyovyote vile atataka kwamba atakapokuja kwenye soko, mahindi yake yawe competitive. Kwa hiyo, atataka anunue mahindi kwa bei ya chini na kwa kufanya hivi, mwananchi anaathirika sana kiuchumi. Kwa hiyo, naomba sana suala la miundombinu, barabara za kuelekea vijijini liangaliwe kwa macho mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mtu aweze kulima lazima kuwe na amani. Nasema wazi, katika Jimbo langu la Chilonwa, vilevile kuna tatizo la migogoro ya ardhi ambayo naweza kuisema vile ni migogoro ya mipaka. Ardhi kwa maana ya wakulima na wafugaji wanavutana. Mipaka inafika wakati fulani Wilaya moja na nyingine kama alivyozungumza ndugu yangu hapa Mheshimiwa Nkamia, tunavutana sana mipaka ya kulima na hasa unapofika wakati wa kulima na Wilaya tunazopakana nazo, ingawa tatizo kubwa kwa kweli ni wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba sana Serikali iangalie uwezekano wa kuwapatia wafugaji maeneo maalum kwa ajili ya malisho, lakini katika maeneo hayo njia rahisi ya kuwafanya waende kwenye maeneo hayo ya malisho ni kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanakuwa na majosho na maji ya kutosha kuwapatia mifugo yao ili waweze kwenda na kufuga huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye mazao ya biashara. Bahati mbaya Dodoma mazao ya biashara siyo mengi, lakini tuna alizeti na vilevile tuna zabibu. Namuombe sana ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu, zao la zabibu ambalo umetuheshimu, limeonekana katika kitabu chako, huku nyuma naona zao la zabibu, hili zao ni mkombozi mkubwa sana wa mwananchi wa Dodoma, lakini tunahangaika nalo kupita kiasi kwa sababu ya soko. Watu wanakuja wananunua kwa bei wanazotaka, wanakwenda kuuza bei kubwa. Mtu akija shambani atanunua kilo moja shilingi 500.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa yako, kilo moja inaweza kuwa na mikungu hata mitano ya zabibu. Ukija mjini hapa mkungu mmoja wewe unanunua shilingi 1,000, yeye ananunua shilingi 500 anakuja kuuza hapa mjini shilingi 5,000. Huyu mwananchi atainuka lini? Dawa peke yake ni kuhakikisha tunamwekea kiwanda cha uhakika cha zabibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ombi langu kwa Serikali, iangalie namna ya kuisukuma Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, ina mpango wa kuweka kiwanda, lakini inasuasua sana. Naombe kabisa, ndugu yangu Mheshimiwa Waziri chukua fursa hii, wasiliana na Halmashauri ile ujue shida yao ni nini? Tumefika mara nyingi, tunaambiwa kiwanda kinafuata muda siyo mrefu, lakini kila siku, sasa tuna zaidi ya miaka miwili, kiwanda hakionekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache, naomba nichukue nafasi hii kutamka kwamba naiunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwnyekiti, kwanza kabisa, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja kati ya wachangiaji wa hotuba ya Waziri wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hilo niendelee kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa kazi yake kubwa anayoifanya. Hapa tunapiga kelele ya vitu vingi lakini wenye kusikia wamesikia. Leo akiwa safarini kwenda Arusha amezungumza mambo mazito juu ya watu wanaoleta fujo na biashara yetu ya sukari. Ni jambo ambalo linawagusa wananchi na yeye mwenyewe linamgusa sana ndiyo maana analikemea kila anapokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza kwa dhati kabisa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa hotuba yake nzuri aliyoiwasilisha kwa umakini kabisa. Wakati akianza nilikuwa naangalia kitabu chake kilivyo kikubwa nikasema hii itakuwa kazi hapa lakini ikawa kazi kweli. Amei-summarize kwa uzuri kabisa, hakuna kitu alichoacha ambacho mtu hakuelewa. Utapitia na utapata details za yale aliyokuwa ameya-summarize, nampongeza sana. Amezungumzia kwa undani kuhusu viwanda kwamba Serikali yetu ya Awamu ya Tano inajipanga kufanya nini kwenye viwanda, akizungumzia viwanda vidogo sana, viwanda vidogo na viwanda vikubwa. Amezungumzia biashara na uwekezaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba namuunga mkono na naunga mkono hoja hiyo. Naiunga mkono kwa dhati kabisa nikitambua kwamba safari tuliyonayo ambayo tumejiwekea ya kuingia kwenye uchumi wa kati hatujakosea njia. Njia sahihi ni hii ya kupitia viwanda, kwa nini? Tunapozungumzia kuelekea kwenye uchumi wa kati maana yake tunazungumzia kipato cha mtu mmoja mmoja ambapo mwisho tunazungumzia kipato cha Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tuna shida ya ajira, kama mtu hufanyi kazi hakuna jinsi utajiongezea kipato lakini unapokwenda kuwainua wananchi kwa viwanda maana yake unakwenda kunyanyua vipato vyao. Unaponyanua vipato vyao maana yake unapandisha kipato cha Taifa na hii ndiyo njia sahihi ya kutupeleka kwenye uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia kilimo, ili kilimo kiweze kuboreshwa lazima soko la uhakika liwepo. Kilimo kipo lakini soko halina uhakika, kwa hiyo kilimo kiko katika levels za chini. Tutakapoweka viwanda vitakavyofanya processing ya mazao yetu ya viwandani maana yake nini? Maana yake watu wengi zaidi wataji-engage kwenye kilimo ambacho soko lake lipo. Tunapozungumzia ufugaji vilevile, tunataka watu wafuge wakiwa na uhakika wa masoko yao. Tunapozungumzia uvuvi tunataka watu wavue wakiwa na uhakika wa masoko ya mazao wanayoyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia viwanda maana yake tunazungumzia value addition ya products zetu tunazozipata. Hili ndilo tatizo kubwa ambalo tumekuwa nalo Watanzania, tatizo hili pia nchi za Afrika tumekuwa nalo sana, kazi yetu ni kuzalisha malighafi na kuwapelekea Wazungu na nchi za nje, wao wanaenda ku-add value, wanatengeneza faida kubwa na kuturudishia sisi tena.
Kwa hiyo, tunapokwenda kwenye hatua hii ya kuzalisha wenyewe, tunapata ajira. Tunapoweka viwanda maana yake kuna watu wanapata ajira viwandani kwa ajili ya ku-process yale mazao lakini mazao yanapotoka pale lazima yafanyiwe biashara, tayari watu wanapata biashara pale pale. Kwa hiyo, ukiangalia chain nzima, hii ndiyo njia sahihi ya kumuongezea kipato Mtanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda sasa nijikite kwangu kwenye Mkoa wa Dodoma, Wilaya ya Chamwino na hasa Jimboni kwangu Jimbo la Chilonwa. Jimboni kwangu ni wakulima na ni wafugaji. Tunalima kiasi cha kutosha pamoja na shida ya mvua iliyopo lakini Mungu anatujalia tunapata kiasi cha kutosha lakini tatizo kubwa ni soko. Nilizungumza juzi kwamba kama tukipata soko la uhakika watu watalima kwa wingi na viwanda vitapata malighafi za kutosha. Tunalima alizeti, ufuta na mahindi lakini soko lake ni duni. Kwa sababu hakuna soko la kuaminika wafanyabiashara wanakuja wananunua kwa bei wanazotaka. Kama tukiwa na uhakika wa viwanda kwamba nalima alizeti najua naipeleka kiwanda gani akinifuata mfanyabiashara nitamuuzia bei ambayo najua hii inanilipa mimi, inalipa muda wangu niliokuwa shambani, inalipa pembejeo zangu nilizotumia shambani na kupata faida kidogo lakini kwa sasa tunauza maadam tuuze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upande wa viwanda na mazao yetu, kuna mazao yanahitaji viwanda vidogo vidogo, vidogo sana lakini kuna mazao yanahitaji viwanda vikubwa na vya kati kwa upande wa alizeti, ufuta na mahindi. Ninachokiomba kwa Serikali na kupitia kwako wewe Waziri hebu tuangalie namna ya kuwawezesha wananchi wapate mikopo ya kuweza kuanzisha hivi viwanda vidogo vidogo vya ku-process mazao yao kama alizeti, ufuta na mahindi. Sisi kwetu Chilonwa tuna biashara ya uhakika ya zabibu yenye shida ya soko.
Naomba nikuombe wewe sasa Waziri kupitia kwako Mwenyekiti tunahitaji tupewe kiwanda cha uhakika cha kutengeneza mvinyo. Tukipata kiwanda cha uhakika cha kutengeneza mvinyo maana yake watu kwa wingi sana watajitokeza kulima zao la zabibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda hili niliweke sawa kidogo. Kuna mchangiaji mwenzangu mmoja alisema kuna viwanda vya aina mbalimbali, naomba nishauri katika hili tusikimbilie viwanda tu, tunapofikiria viwanda basi tuweke viwanda vyenye teknolojia ya kisasa. Kwa mfano, unapozungumzia Kiwanda cha Mvinyo ambavyo ndiyo vingi viko hapa Dodoma vidogo vidogo, kazi yao ni kukamua ile zabibu na kutengeneza mvinyo, basi! Hayo siyo mazao peke yake unayoweza kuyapata kutokana na zabibu. Viwanda vya wenzetu vina-process unapata juice lakini unaweza ukai-ferment ukapata mvinyo (wine) lakini vilevile unaweza ukai-concentrate ukapata kitu kinaitwa concentrates hizi ambazo tunapigia kelele hapa kwamba wafanyabiashara wengi wa viwanda vya mvinyo wengi wana-import concentrates wanakuja kutengenezea mvinyo hapa wakisema kwamba wametumia zabibu za hapa nchini, sio kweli! Basi na sisi tuanzishe kiwanda cha namna hiyo tuweze kutengeneza juice, mvinyo na concentrates. Tukifanya hivyo tutakuwa tumefanya value addition kubwa sana na kuipatia nchi hii hata fedha za kigeni hasa tukizungumzia concentrates ambazo zina soko la uhakika huko nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nitamke kwamba naunga mkono hoja na ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwanza kabisa nikushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamechangia wachangiaji wengi na mimi niko ndani yao yaliyozungumzwa kwa hakika ni yale ambayo na mimi ningependa niyazungumze kwa undani. Lakini nataka nijiweke kimsingi katika kukubaliana nao kwamba elimu ndiyo kila kitu, ndiyo msingi wa maendeleo bila kuwa na elimu bora Taifa halitapiga hatua yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuwa na elimu bora safari yetu ya kuelekea Tanzania ya uchumi wa kati itakuwa ni ndoto kwa sababu huko tunazungumzia kuwa na viwanda pamoja na kwamba tunapuzungumzia Tanzania ya viwanda maana yake tunazungumzia industrialization. Tukienda katika historia wenzetu wamepita huko miaka ya 1800 wakati sisi tuko kwenye primitive, lakini leo sisi tunazungumzia industrialization basi tuifanye iwe kweli kwa maana ya kwamba iwe elimu bora ndiyo maana wachangiaji wote wanapiga kelele elimu iwe bora tuweze kwenda jinsi tunavyotaka sisi Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme machache, kwanza nimevutiwa sana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri, hotuba imesheheni kila kitu ambacho kinahitajika kutufanya sisi tuweze kusonga mbele katika nyanja ya elimu na kwa hiyo kuweza kutubeba sisi kutupeleka katika Tanzania ya uchumi wa kati. Lakini tatizo liko wapi, tunapopiga kelele na elimu kuwa siyo bora, elimu duni tatizo liko wapi, mipango mizuri tunayo, mikakati mizuri tunaiweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tu ili tuweze kufika tunakotaka, tunahitaji kuwa na elimu bora inayozingatia usawa kwa wanafunzi wote. Tunapozungumzia elimu bora tunazungumzia elimu yenye mitaala iliyosimama na syllabus zilizosimama, zisizobadilika badilika, hii ni sera hatuwezi kuwa na sera ya kutufikisha popote inayobadilika badilika kila wakati. (Makofi)
Kwa hiyo, mimi naona sehemu moja ambayo inaleta shida kwetu ni hapo kwamba sera zetu mitaala yetu syllabus zetu zinabadilika na zinabadilika na watu. Leo yuko Mama Ndalichako anakuja kivyake, kesho anakuja Mwaka anakuja kivyake, keshokutwa anakuja Mheshimiwa Zungu anakuja kivyake hatuwezi kusonga mbele hata siku moja, tunatakiwa tuwe na sera iliyosimama, haijalishi leo yuko nani, kesho yuko nani ili tuweze kuwa na elimu bora.
Pili, tunahitaji kuwa na walimu bora, walimu bora utawapata wapi? Lazima uwapate vyuoni je wanadahiliwa vipi kuingia vyuoni. Tumesikia hapa tatizo la udahili wa vyuoni. Tumesikia hatua zilizochukuliwa na Mheshimiwa Waziri kwa wale waliotufikisha pabaya pamoja na kwamba tunalia hawa wanafunzi waliofutiwa masomo kwa kweli tunaomba Serikali iwafikirie mara mbili mbili, kuwapoteze muda mwingi na sasa waende wakaanze upya na hawajui waanzie wapi kwa kweli siyo sahihi. Tunaiomba Serikali iwafikirie kwa sababu halikuwa tatizo lao tunajua kuna namna yoyote inaweza ikafanyika ili nao waweze kujikwamua kimaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini udahili vyuo vya walimu viko vipi huko wanakosoma walimu kukoje vyuo viko sawasawa au wanakwenda kupitisha muda tu miaka miwili, mitatu wanatoka wanakuja kufundisha? Hayo ni mambo ya msingi katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na elimu bora. Mazingira ya kufundishia yako vipi? Madarasa yako vipi, madarasa yasiyokuwa na sakafu, madarasa ambayo darasa moja linaingia wanafunzi mia moja naa mpaka mwalimu anakosa pa kusimama, hilo ni darasa ambalo mwalimu anaweza akafundisha kweli? Tunajua mwalimu anapofundisha ana standard awe na wanafunzi wangapi darasani, aweze kuwapitia hata wale walio slow learners kuwavuta waende na wenzao. Sasa mwalimu anapokuwa na darasa limejaa hata pa kupita haoni atawasaidia vipi hao wengine slow learners na hata hao first learners hawawezi ku-learn chochote katika darasa ambalo limesheheni wanafunzi kiasi hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia vifaa vya kufundishia, viko mashuleni kweli? Maana yake sisi ndiyo tunaotoka huko vijijini, ndiyo tunaotoka huko kwenye majimbo yetu, shule zina vifaa vya kufundishia? Serikali ina mpango gani katika hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia maslahi bora ya walimu. Ukishakuwa na mwalimu bora lazima awe na maslahi bora maslahi bora ya mwalimu ni pamoja na mshahara wake uwe mzuri, tunazungumzia kwamba ukitaka kuwa Mbunge lazima utapita kwa mwalimu, ukitaka kuwa Rais lazima upite kwa mwalimu, ukitaka kuwa daktari lazima upite kwa mwalimu, lakini huyu mwalimu ukishapita umemuacha hapo nyuma, leo kuna mwalimu aliyenifundisha mimi pengine nikianza kumgeukia nyuma ninachokipata mimi kama mshahara wangu ukilinganisha na cha mwalimu hakuna heshima hata dakika moja. Wanavunjika moyo, wanaona kwamba kazi hiyo ni kazi ya kudharaulika sana, hebu tuifanye kazi ya walimu kuwa kazi ya heshima kwa kuwaangalia kwenye maslahi yao kwa upande wa mishahara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na mishahara hiyo waliyonayo stahili zao wanazostahili wanazipata inavyostahili? Mwalimu anahamishwa, hapati hela ya uhamisho. Mwalimu anatakiwa kwenda kwenye semina au walimu wanatusaidia kwenye kusahihisha mitihani pesa za kusahihisha mitihani hawazipati kwa wakati unaostahili. Hivi tunawaangalie kweli walimu kwa karibu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la nyumba za walimu. Walimu huko vijijini mkienda utawaonea huruma, wanakaa kwenye vibanda ambavyo huwezi kuamini, sasa tunaanza kuwaambia walimu wakipangiwa shule wakienda wakiripoti wanaondoka, hata mimi ningeondoka, anakwenda kuingia kwenye kibanda ambacho huwezi kuamini, kweli mwalimu ametoka chuoni anakuja kuwafundisha wanafunzi anaingia kwenye kibanda hamna taa okay mambo ya taa siyo tatizo watanunua siku hizi kuna mambo ya solar kuna nini, lakini kibanda kimejibana kidogo kidogo tu, kitanda hakuna nafasi ya kuweka kitanda cha sita kwa sita hakiingi kweli jamani? Hii siyo sawasawa hebu tuwaangalie kwa karibu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho na muhimu katika ubora wa elimu ni hili la kuzikagua shule. Shule hazikaguliwi kabisa, ukienda shuleni ulianza mara mwisho wamekaguliwa lini utacheka, hazikaguliwi na hiki ndicho chanzo kikubwa cha elimu kushuka pamoja na walimu kuwa wamekataa tamaa lakini kama wanajua kuna mtu anawafuatilia nyuma basi hata kawoga kidogo kanakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu naomba haya masuala Mheshimiwa Waziri ayachukue pamoja na mengine mengi waliyozungumza wenzangu ayachukue na Serikali iyafanyie kazi kama kweli inataka kufanya Tanzania tuwe na elimu bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili usawa kwa wanafunzi. Tuna wanafunzi wengine wenye mahitaji maalum, mahitaji maalum…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante,
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Ardhi. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai sisi sote tuliomo humu ndani, tumekutana leo tuweze kuifanya kazi hii muhimu kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kututunzia Rais wetu Mheshimiwa Rais. Dkt. John Pombe Magufuli tukitambua na kazi yake kubwa aliyonayo. Tunaomba aendelee kumtunza aifanye kazi kwa uaminifu kadri atakavyomjalia. Mwisho, nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Ardhi, kwa kuleta hotuba nzuri hapa, ambayo tumeisikia ina mantiki na changamoto nyingi ambazo tunazijadili sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nianze tu kwa kusema kwamba, nionavyo mimi ardhi ni eneo muhimu sana katika safari yetu hii tuliyoianza ya kuelekea kwenye Tanzania ya uchumi wa kati. Kama tulivyokwishaona katika mijadala yetu mbalimbali tuliyofanya ya Wizara ambazo tungezifanya kama viwanda, kilimo na mifugo, ujenzi na kadhalika. Wizara zote hizi tumezijadii zikizingatia mpango wa maendeleo wa miaka mitano ambayo ndani yake sasa tunajadili mpango wa maendeleo wa mwaka mmoja mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nianze sasa kwa kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri iliyoenea na kusheheni kila kile tunachokitegemea Watanzania nini kipo, nini tunakitegemea. Hata hivyo, niseme kwamba, nitoe mfano ambao tunaujua wote kwamba, nini kilianza kuku au yai, kila mtu ana majibu yake humu ndani, lakini nikikuuliza Wizara ipi muhimu katika Wizara zetu nyingi tulizonazo kila mtu atakuwa na majibu yake vilevile lakini nitakwambia Wizara ya Ardhi iko mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko mbele na wachangiaji wote waliopita wamekwisha yasema haya, Wizara ya Viwanda haitakuwepo kama hakuna ardhi utavijenga wapi hivyo viwanda, Wizara ya Kilimo na Mifugo utalima wapi, utafuga wapi kama ardhi haipo, ujenzi yawe wa barabara au nini utatengeneza wapi barabara kama hakuna ardhi, lakini kikubwa ni wapi unalima, wapi unajenga na wapi unafuga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndio kazi kubwa ambayo Wizara ya Ardhi inayo na ndiyo haya ambayo Mheshimiwa Waziri amejitahidi sana kuelezea mikakati na mipango aliyonayo angalau kwa mwaka huu wa 2016/2017, nini wanatarajia kama Wizara kukifanya. Niseme kama kuna tatizo kubwa katika Wizara hii ni migogoro ya ardhi, imekithiri na imedumu muda mrefu shida ni nini? Shida iko wapi? Kwa nini hatuitatui, kwa nini haifiki mwisho? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia kwako nichukue mfano wa kwangu Wilaya ya Chamwino na hasa Jimbo la kwangu la Chilonwa, Mheshimiwa Waziri Lukuvi, alishawahi kuwa Mkuu wa Mkoa hapa Dodoma, analifahamu sana Jimbo langu la Chilonwa, anafahamu sana matatizo ya ardhi yaliyopo Jimbo la Chilonwa, maeneo ya Kata ya Segala kule Izava, kule Walii ambako tumepakana na Wilaya ya Kongwa anafahamu sana tatizo la migogoro lililopo kule Dabalo katika Vijiji vya Chiwondo ambavyo pia vimepakana na Kongwa, kule hakuna usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa, wafugaji wanaleta fujo sana. Ninavyozungumza hapa nilipo wanaingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima, huku wakiwa wamejiandaa na mikuki na mishale, mkulima atokee wampige mishale, hakuna amani. Nimuulize tu Mheshimiwa Waziri, kuna mpango gani wa kutatua haya matatizo ambayo yameshakuwa ya muda mrefu, shida ni nini? Ukiangalia maeneo niliyoyataja maeneo ya Izava, Walii na Chiwondo yanapata huduma zote za kijamii toka Wilaya ya Chamwino, kuanzia maji, shule, ikija wakati wa sensa, kujiandikisha kupiga kura, hata mimi mwenyewe nimepigiwa kura na hawa, lakini ikifika wakati wa kilimo tayari utaona migogoro imeanza wanakuja wafugaji wanaotoka maeneo ya Kongwa wakidai kwamba yale maeneo ni ya Kongwa. Inaonekana labda kweli ni maeneo ya Kongwa, Serikali iko wapi wakati siyo wa kilimo kuingilia na kutatua yale matatizo once and for all. Shida ni nini? Kwa kweli niseme tu, sitaki kuingia kwenye historia lakini niseme kama hakutakuwa na maelezo mazuri wakati Mheshimiwa Waziri una-wind up…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza kabisa nichukue nafasi hii nikushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika bajeti yetu hii, ya mwaka 2016/2017 nikitambua wazi kwamba ni bajeti ya kwanza kabisa ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa, na ndugu yetu, kamanda wetu, Rais John Pombe Magufuli, Hapa Kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia nikupe pole kwa haya unayoyapita sasa, lakini ndiyo maisha yenyewe, tatizo huwa ni uelewa na ufahamu ilivyo kila sehemu kunapokuwa na jamii fulani lazima kuwe na sheria na kanuni zinazowaongoza. Bila kuwa na sheria na kanuni inakuwa vurugu mechi. Sisi kama Wabunge tunapaswa kwa hakika kuonesha dhahiri kwamba Wananchi hawakukosea kutuchagua kutuleta hapa tuoneshe kwamba tunatakiwa kwenda kwa sheria na kanuni mbalimbali za maeneo tunayokuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napata shida ninapoona humu ndani tunakuwa viongozi wa kutokufuata hizo sheria na kanuni. Lakini ni jambo nalo lisilokwepeka kunapokuwa na jamii tuko wa aina mbalimbali tuwasamehe tu, lakini naamini sisi humu ndani tunaifanya kazi ya watu waliotutuma hata kwa niaba yao kuhakikisha kwamba nchi hii inasimama na Serikali ya Awamu ya Tano inakwenda kutekeleza bajeti yake ambayo imelala sana katika kuwatetea wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia nimshukuru sana Waziri wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri na timu yake yote, kwa hotuba yao nzuri waliyotuletea hapa ambayo sasa tunaijadili inayohusiana na bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017. Nawapongeza kwa sababu ninatambua nchi yoyote itajiendesha kwa wananchi wake kulipa kodi, na hata misaada mbalimbali ambayo Serikali yetu inapata kutoka nchi za wenzetu ni kodi za wenzetu, kwa hiyo na sisi tunapaswa tulipe kodi tuendeshe nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahishwa zaidi na bajeti hii pale nilipoona imeweka asilimia 40, imelenga kumsaidia Mtanzania. Nasema kumsaidia Mtanzania kwa sababu imepelekwa kwenye maendeleo. Tatizo letu limekuwa kubwa, wananchi wetu wanapiga kelele sana na hata wenzetu upande wa pili wamekuwa wakilibeba sana. Hawaoni maendeleo ya haraka kwa sababu fungu hili lilikuwa linatengwa dogo sana. Kwa sasa kwa kuweka asilimia 40 nina amini tutakwenda na tutaona mabadiliko makubwa au maendeleo ya haraka kwa maendeleo ya wananchi kutokana na fungu hili kuongezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wengi wamechangia na wamechangia kwa umahiri wao, naomba nizungumze suala hili tu kidogo kwa mfano ulipaji wa kodi na maendeleo ya nchi kwa ujumla. Naamini tunapozungumzia kulipa kodi, kuna kodi mbalimbali, kuna kodi za mazao ya shamba, mazao ya viwanda, za biashara na kadhalika. Katika mzunguko huu wa hizi kodi ndipo tunapotengeneza maendeleo ya nchi na tunapoona ushiriki wa kila mmoja wetu katika kuleta maendeleo ya nchi yetu. Nichukue mfano wa mkulima wa pamba; analima pamba kama yeye anaipeleka kiwandani, kiwandani itatengenezwa nyuzi, itapelekwa kwenye kiwanda itatengenezwa nguo, itapelekwa dukani itauziwa watu mbalimbali na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichukue mfano huu nijikite kwenda kutetea hoja moja ya kwamba TRA sasa ikusanye mapato ya property tax badala ya Halmashauri. Majengo tunayoyaona mijini sehemu kubwa ni ya biashara, ni viwanda na ofisi. Wanahudumia akina nani? Wanahudumiwa wananchi wa Tanzania, wako wapi? Asilimia 70 ya Watanzania wako vijijini, ina maana gani? Ina maana kwamba hayo majengo, hizo biashara za mjini na ofisi za mjini zinaendeshwa pia na watu wa vijijini kwa kiasi kikubwa, kama ni vyakula vikitengenezwa vitakwenda mpaka kijijini kwenye asilimia 70, kama ni nguo zitakwenda mpaka vijiji kwenye asilimia 70 ya wananchi.
Tukiangalia Halmashauri za vijijini mapato yao ni kidogo, kwa sababu maendeleo makubwa yako mijini, Halmashauri za mijini zina mapato makubwa kwa sababu zinabebwa na Halmashauri za vijijini. Kwa hiyo, unapoacha wa mjini anafaidi wakijijini hafaidi, kwa kiasi fulani tunakuwa hatuwatendei haki, lakini naamini sasa kwa kusema TRA ikusanye itaweka ratios ambazo zitaisaidia kwamba hata Halmashauri za vijijini zipewe fungu na makusanyo hayo. Sawa mjini watapata fungu lao kubwa, lakini vijijini na wao hawataachwa watapewa fungu ili kwa pamoja tuweze kuangalia namna gani tunasukuma maendelo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache nichukue nafasi hii niseme tu kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia 100 asante sana.