Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Eng. Joel Makanyaga Mwaka (6 total)

MHE. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:-
Barabara ya kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Chamwino kuelekea Kaskazini ni vumbi na ina madaraja mawili makorofi yaliyoko kati ya Chilonwa na Uzali na lingine kati ya Dabalo A na Dabalo B. Daraja lililopo kati ya Chilonwa na Nzali limewahi kuua watu mwaka 2014 na mifugo mingi pia imekufa kwenye daraja hilo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuyajenga madaraja hayo mawili ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa Wilaya ya Chilonwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Chilonwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, madaraja aliyotaja Mheshimiwa Mbunge yote yapo katika barabara ya Chamwino Ikulu Junction, kuelekea Chamwino Ikulu - Dabalo hadi Itiso yenye urefu wa kilometa 80.43 ambayo ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Dodoma.
Mheshimiwa Spika, kati ya Chilonwa na Nzali kuna daraja la mfuto (vented drift) lililojengwa mwaka wa fedha 2013/2014 ambalo linatumika ingawa linakabiliwa na changamoto ya kuziba yaani siltation. Aidha, kati ya Dabalo A na Dabalo B pia kuna daraja la mfuto ni solid drift lililojengwa mwaka wa fedha 2014/2015 ili sehemu hiyo iweze kupitika.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) itaendelea kuyafanyia matengenezo madaraja hayo mawili yaliyopo ili yaweze kupitisha maji na barabara hiyo iweze kupitika majira yote ya mwaka. Aidha, Wakala wa Barabara utaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii ili kuhakikisha inatumika kwa usalama wa watumiaji na kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii wananchi wa Chilonwa.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:-
Barabara inayounganisha vijiji vya Msanga na Kawawa ni muhimu sana kiuchumi kwa kata ya Msanga na Wilaya ya Chamwino na pia kuna mazao mengi ya uhakika kutoka Kawawa na vitongoji vyake, lakini barabara hiyo ni korofi sana kwa sababu ya mbuga iliyoko kati ya vijiji hivyo viwili na zaidi, daraja kubwa lililopo limevunjika kabisa kiasi kwamba halipitiki kabisa wakati wa mvua na wakati wa kiangazi hupitika kwa taabu sana.
Je, Serikali ina mpango gani wa kurekebisha barabara hiyo na kulijenga daraja husika ili kuboresha mawasiliano ya vijiji hivi viwili na masuala ya usafirishaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Jimbo la Chilonwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa barabara hii, Serikali katika mwaka wa fedha 2015/2016 imetenga shilingi milioni 46.3 kwa ajili ya kujenga kivuko (box culvert), kuichonga barabara kwa urefu wa kilometa tano na kuiwekea changarawe sehemu korofi yenye urefu wa kilometa nne. Aidha, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, barabara hii imeombewa shilingi milioni 130 kwa ajili ya ukarabati ili kuifanya ipitike wakati wote.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:-
Serikali ilikuja na mpango mzuri wa umeme Vijijini na kupitia mradi wa REA kukawa na REA I, REA II na sasa REA III na Serikali iliahidi kwamba miradi yote ya REA II ambayo haijakamilika hadi kuanzishwa kwa REA III itatekelezwa sambamba na REA III:-
(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza miradi yote ya REA II Jimbo la Chilonwa katika Vijiji vinne vya Kata ya Msamalo(Myunga, Msamelo, Mnase na Mlebe) Vijiji viwili vya Kata ya Zajilwa (Zajilwa na Mayungu) na Kijiji cha Kata ya Manchali?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuviingiza vijiji ambavyo havikuwepo kwenye mpango wa REA II katika mpango wa REA III?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Chilonwa, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi za kupeleka umeme katika Vijiji vya Kata za Manchali, Msamalo na Zajilwa kupitia mradi wa REA Awamu ya II zitakamilika mwezi Novemba mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vyote vya Jimbo la Chilonwa ambavyo havikupata umeme kupitia REA awamu ya II vitapatiwa sasa umeme kupitia REA Awamu ya III. Kazi ya kupeleka umeme kwenye vijiji hivyo itahusisha ujenzi wa umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 68, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 301, pia ufungaji wa transformer 45. Mradi huu pia utapeleka umeme kwa wateja wa awali 11,276. Kazi zitaanza mwezi Desemba mwaka huu na kukamilika mwaka wa fedha 2019. Gharama ya mradi huu ni shilingi bilioni 12.09
MHE. JOEL M. MAKANYAGA Aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia maji wananchi wa vijiji vya Jimbo la Chilonwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Chilonwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji nchini, kuanzia mwaka 2012/2013 hadi mwaka 2014/2015 imetekeleza miradi ya maji kwa vijiji vya Itiso na Membe kwa jumla ya shilingi milioni 758.7 vikiwa na jumla ya vituo vya kuchotea maji 23 ambavyo vinahudumia wakazi wapatao 7,475.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri inakamilisha mradi wa maji katika kijiji cha Wilunze ambao utahudumia jumla ya watu 2,867 kwa maeneo ya Makaravati, Mbelezungu, Majengo na Chalinze Nyama kwa jumla ya shilingi milioni 347.9 katika Jimbo la Chilonwa.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri imepanga kutumia shilingi bilioni 1.053 kwa ajili ya kujenga miradi ya maji ikiwa ni pamoja na vijiji vya Magungu na Segala katika Jimbo la Chilonwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuboresha huduma ya maji katika Jimbo la Chilonwa na maeneo mengine nchini kwa kadri rasilimali fedha itakavyopatikana.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:-
Wananchi wa Chilonwa wanaishukuru Serikali kwa kuendelea kukarabati daraja lililoko kati ya kijiji cha Mahampha na Nzali kwa kiwango cha mkeka, korongo hili hupitisha maji mengi sana wakati wa masika toka Bwawa la Hombolo kiasi cha kukosa mawasiliano kabisa kati ya Kaskazini na Kusini mwa Jimbo la Wilaya ya Chamwino kwa ujumla wake.
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kulijenga daraja hili kwa kiwango cha daraja la kupitika juu na sio ya mkeka ili kuondoa kero hii ya kukatika kwa mawasiliano kabisa wakati wa masika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Chilonwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikilifanyia ukarabati daraja la Mfuto yaani drift liitwalo Chilonwa lililopo kati ya kijiji cha Mahampha na Nzali ili kuhakikisha kuwa daraja hilo pamoja na barabara ya Chamwino Ikulu - Dabalo junction hadi Itiso yenye urefu wa kilometa 75 inapitika majira yote ya mwaka. Kwa kawaida daraja la mfuto (drift) hujengwa katika eneo lenye kina kifupi ambalo maji hukatisha barabara yaani shallow water crossing. Hali hii ndio iliyosababisha daraja la mfuto kujengwa kati ya kijiji cha Mahampha na Nzali. Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kufanya uangalizi wa karibu wa eneo hili ikiwa ni pamoja na kuangalia mapungufu yaliyopo na kupendekeza aina ya daraja ambalo litakuwa suluhisho la kudumu katika eneo hilo.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA aliuliza:-
Barabara inayounganisha Vijiji vya Msanga na Kawawa ni muhimu sana kiuchumi kwa Kata ya Msanga na Wilaya ya Chamwino na pia mazao mengi ya uhakika kutoka Kawawa na Vitongoji vyake lakini barabara hiyo ni korofi sana kwa sababu ya mbuga iliyopo kati ya vijiji hivyo viwili na daraja kubwa lililopo limevunjika kabisa kiasi kwamba halipitiki kabisa wakati wa mvua na wakati wa kiangazi hupitika kwa taabu sana.
Je, Serikali ina mpango gani wa kurekebisha barabara hiyo na kulijenga daraja husika ili kuboresha mawasiliano ya vijiji hivyo viwili na masuala ya usafirishaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, Mbunge wa Chilonwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa barabara hii, Serikali katika mwaka wa fedha 2015/2016 ilitoa shilingi milioni 40 ambazo zimejenga kivuko (box culver) na kufungua mifereji ya kuitisha maji ya mvua (river draining). Aidha, mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetumia shilingi milioni 100 kuifungua barabara hiyo urefu wa kilomita 8, kujenga madaraja mbonyeo (solid drifts) matano likiwemo la mita 50 katika mto unaopitisha maji kutoka Hombolo na kuweka changarawe sehemu korofi kwa urefu wa kilomita 1. Serikali itaendelea kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ili kuhakikisha daraja hilo linatengewa fedha na kujengwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 kupitia TARURA.