Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng. Joel Makanyaga Mwaka (3 total)

MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Spika ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini naomba niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa madaraja haya jinsi yalivyojengwa, kipindi cha mvua huwa ni kero kubwa kiasi kwamba mawasiliano yanakatika kabisa pamoja na kwamba madaraja yapo watu wanashindwa kuja mjini, wanashindwa kwenda vijijini; na kwa kuwa tunafahamu kwamba uchumi unategemea sana barabara na barabara zinaunganishwa na madaraja; na kwa kuwa maeneo hayo ya Jimbo ndiyo maeneo yenye uchumi mzuri kwa maana yanapata mvua za kutosha na mazao yake ni ya kuaminika.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuyajenga madaraja haya katika kiwango cha kuyafanya yapitike hata wakati wa mvua ili Wilaya iweze kupata mapato na uchumi kipindi chote na watu kuondolewa kero za kusafiri wakati wa mvua?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Makanyaga kwa namna alivyoitikia wito wetu wa kuingia kwa umakini kuhusiana na matatizo haya ya madaraja mawili. Kwa taarifa tulizonazo kupitia TANROADS Mkoa, madaraja haya yanapitika isipokuwa kwa mwaka huu, mvua ilikuwa nyingi sana na siltation iliziba, maji yakawa yanapita juu ya daraja. Tunaamini hali ya mvua ya mwaka huu ambayo haikuwa ya kawaida pengine miaka ijayo hali haitakuwa hivyo.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tutahakikisha TANROADS Mkoa wanaendelea kuyaangalia haya madaraja na wakiona kuna umuhimu wa kuyapandisha, kuyaondoa, kuyapanua na kuyageuza ili tulete daraja tofauti na zaidi ya hii vented drift kupitia Road Board ya Mkoa, mapendekezo hayo yatapitiwa na hatimaye Serikali itaangalia namna ya kuyashughulikia. Kwa taarifa ya Road Board Mkoa pamoja na TANROADS Mkoa, mazingira ya madaraja hayo ambayo tumeyatengeneza mwaka jana tu na mwaka juzi yanatosheleza kwa mazingira ya kiuchumi yalivyo sasa katika hilo eneo.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri na naamini kwamba haya yaliyozungumzwa yote yataenda kutekelezwa. Naomba kuongeza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa, Vijiji vingi vya Jimbo langu ni vikubwa sana na kwa kuwa, umeme huu wa REA umekuwa ukifikishwa kwenye maeneo ya kati ya vijiji tu. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuusogeza umeme huu sasa kwenye vitongoji vilivyo mbali na maeneo ya kati ya vijiji ili wananchi hao katika vitongoji hivyo nao waweze kunufaika na umeme huu?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi, namshukuru sana Mheshimiwa Makanyaga kwanza kwa kuuliza swali hili.
Kwa kuwakumbusha tu, ni kweli kabisa kwa awamu ya II tumepeleka kwenye vituo, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Chilonwa kwamba awamu ya III inapeleka sasa kwenye vitongoji na kwenye vijiji vyote na kwenye mashine na kwenye taasisi za jamii ikiwemo shule. Nimhakikishie hata Kijiji chake Mheshimiwa Chilonwa cha Chalinze sasa kitapata umeme, Kijiji chake cha Kawawa kitapata umeme, Kijiji cha Malichela kitapata umeme, Kijiji cha Membe kitapata umeme, Kijiji cha Bwawani nacho kitapata umeme. Kwa hiyo, nimhakikishie kuwa vijiji vyote vitapata umeme.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini niweke wazi tu kwamba vijiji vilivyofaidika mpaka sasa ni vijiji vitatu ambavyo ukilinganisha na jumla ya vijiji 47 vya Jimbo langu ni sawa na asilimia 6.4. Kuna vijiji kama 12 hivi vilikuwa na huduma hii ya maji kabla, vinakuwa vijiji 15 vinavyofaidika ambavyo ni sawa sawa na asilimia 31.9.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Tanzania tunakimbilia kwenye Tanzania ya Viwanda. Tanzania inayotaka wananchi wafanye kazi kwa bidii, kwa nguvu bila maji, tukijua kwamba, maji ni muhimu katika maisha ya binadamu, tusipopata maji safi na salama uwezekano wa kuwa na magonjwa ya hapa na pale yatakayotufanya tushindwe kufanya kazi inayostahili na kwa hiyo, tushindwe kuipeleka Tanzania katika Tanzania ya Viwanda.
Je, Serikali ina mpango gani kuongeza kasi ya
upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Jimbo la Chilonwa?
Swali la pili, je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu sasa siyo lazima kila kijiji kichimbiwe kisima chake au kiwe na chanzo chake, wakati mwingine chanzo kimoja kiweze kuhudumia hata vijiji viwili/vitatu. Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kufanya hivyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu concern ya Mheshimiwa Mbunge ndiyo maana tukiangalia eneo la Wilaya ya Chamwino liko karibu katika Makao Makuu sasa ya nchi yetu. Mheshimiwa Mbunge ndiyo maana unafahamu takribani zipatato wiki Nne nilikuwa katika mradi wa maji wa Wihunze ambao nimeona kwamba Mkandarasi anafanya kazi kwa kusuasua na kutoa maagizo ikifika tarehe Tatu mwezi huu tulioanza nao mradi huo uweze kukamilika na ninasikia hali kidogo inaenda vizuri. Hiyo yote ni juhudi ya Serikali kuangalia jinsi gani tutafanya miradi hiyo ipatikane.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali hiyo, ndiyo
maana hapa nimezungumza katika majibu yangu ya awali kwamba, mwaka huu tumetenga shilingi bilioni 1.058 kwa ajili ya kupeleka juhudi hii ya maji, hata hivyo naomba nikuhakikishie kwa sababu, eneo la Wilaya ya Chamwino hasa Jimbo lako ni eneo la kimkakati na Ikulu yetu ya Mheshimiwa Rais ndiyo inapojengwa pale. Naomba nikuhakikishie kwamba Serikali itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wananchi wa maeneo yale wanapata huduma ya maji kwa sababu, ndiyo sehemu ambayo ni pumulio la katikati la Jiji la Dodoma, lazima tuweke juhudi za kutosha. Naomba ondoa hofu, Serikali itakuwa na wewe daima kuhakikisha kwamba mambo yanakuwa vizuri katika Jimbo lako.