Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Lucy Simon Magereli (8 total)

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Hata hivyo, nieleze masikitiko yangu tu kwamba eti unapata majibu ya Serikali, yanakwambia Mpango wa Serikali kuliwezesha Bunge kufanya shughuli zake kwa ufanisi ni kutoa
fedha toka Mfuko Mkuu wa Serikali kupeleka kwenye Mfuko Mkuu wa Bunge, Fungu 42 eti huo ndiyo mpango.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli sijaridhika na
majibu ya Mheshimiwa Waziri kwa sababu najua sisi wote hapa katika Bunge hili ni mashahidi, majukumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muhimu na nyeti sana kuliko hiki ambacho Serikali inataka kutuambia kwamba
mpango wake ni kutoa fedha Mfuko Mkuu wa Serikali na kupeleka Mfuko wa Bunge. Ninyi wote ni mashahidi kwamba kwa mujibu wa kanuni, muda wa Kamati za kuelekea bajeti ni wiki tatu lakini this time wiki moja imeondoshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye swali langu la msingi nilichouliza ni kwamba, muda wa uendeshaji wa shughuli za Bunge umepunguzwa mno kiasi cha kufikia siku 10 hadi 12, lakini hata muda wanaopewa Mawaziri kujibu hoja za Wabunge na wananchi wa Tanzania nao
umepunguzwa kufikia kiasi cha dakika tano. Kwa hiyo, hatutekelezi wajibu wetu kama Bunge kwa sababu tunakimbizana na muda ingawa hili la muda naona halikuzingatiwa, lakini bado hoja ya bajeti mpaka mweziwa Pili mmetupa asilimia 68, tu kwa hiyo bado hata hilo ambalo mlifikiri ni kazi rahisi tu kutoa Mfuko wa Serikali kuweka
Mfuko wa Bunge bado hamjatoa kiasi kinachokidhi, bado mnatusafirisha kwenye Hiace, bado…
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa binafsi yangu, naomba nielezwe kabisa straight forward kama hili ndiyo jibu la Serikali basi swali hili halijajibiwa
naomba lijibiwe.
..
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa swali langu lilirejea Taarifa ya Kamati ya Mambo ya UKIMWI iliyotolewa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Februari mwaka huu, nilitarajia majibu ya Mheshimiwa Waziri yawe at least na takwimu ambazo sasa zitaunga mkono hoja ya Taarifa ya Kamati au zitatengua ile hoja ya Taarifa ya Kamati kwamba fedha za wafadhili katika eneo hili zimepungua sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu, Mheshimiwa Naibu Waziri anisaidie kwamba hao wadau aliowataja ni wadau gani ambao wameendelea kutoa support katika eneo hili? Kwa sababu tunafahamu fedha za mambo ya UKIMWI zimekuwa zikichangiwa kwa asilimia kubwa sana na PEFA na Global Fund ambao kwa sehemu kubwa wame-pull out.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sijajua hao aliowazungumzia hapa Mheshimiwa Naibu Waziri ambao anasema wanachangia kwa kiasi kikubwa kinyume na Taarifa ya Kamati ni akina nani? Napenda kufahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na maendeleo kadhaa ya kitabibu na kimaabara ambayo yanaonesha majaribio yaliyofanikiwa katika upatikanaji wa chanjo na hata tiba ya Virusi vya UKIMWI. Je, Serikali ina maelezo gani kuhusu maendeleo haya na taarifa hizi ambazo zinatokana na vyombo mbalimbali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwamba ni wadau gani? Kwa mujibu wa sheria ambayo inaanzisha Mfuko wa UKIMWI Tanzania, malengo makuu ya mfuko huu ni kukusanya pesa ambazo zitakwenda kuweka uendelevu wa pesa ambazo zitakuja kuwa zinatumika sustainably kwenye kununua dawa za UKIMWI kwa kiwango cha asilimia 60, lakini pia kutoa huduma za kinga kwa asilimia 25, pia kwa asilimia 15 kusaidia kwenye mwitikio wa UKIMWI kwa maana ya kujenga mazingira mbalimbali wezeshi hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mfuko huu una malengo ya kuwa endelevu na ulianzishwa kwa malengo kutokana na mabadiliko yaliyofanyika kwenye Sheria ya UKIMWI ambayo ilianzisha TACAIDS mwaka 2001 Sheria Namba 22 kwa ajili ya kutengeneza sustainability kwenye eneo la upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya HIV/Aids.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mfuko huu bado ni mchanga sana na umezinduliwa mwaka 2016 tu mwezi Disemba na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano za Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan na kwa mwaka wa fedha uliopita tulitenga kiwango cha shilingi bilioni 5.5 na mwaka huu tumetenga shilingi bilioni tatu. Kwa hiyo, ndiyo tumeanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wadau ni akina nani? Wadau wa kwanza ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia bajeti yake, lakini pia tunatarajia mfuko huu utakusanya vyanzo vingine vya fedha kutoka kwa wananchi kwa ujumla ambao watajitokeza kuchangia kutoka kwenye sekta binafsi, asasi za kiraia, asasi za hiari, lakini pia wadau wa maendeleo hawazuiliwi pia kuchangia kwenye mfuko huo. Malengo yetu ni kwamba tuweze kufikia angalau asilimia 30 ya kujitosheleza kwenye fedha za dawa za kupunguza makali katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, chanjo ya virusi vya UKIMWI bado inaendelea kufanyiwa utafiti duniani, jitihada bado zinaendelea. Nasi Tanzania ni washiriki katika tafiti mbalimbali ambazo zitapelekea kupatikana kwa chanjo kwa siku zijazo, lakini kwa sasa tuko katika hatua za awali sana za Kisayansi za kutafuta chanjo hiyo na bado hakujawa na mwangaza mkubwa sana kwamba labda katika kipindi cha miaka kadhaa tunaweza tukawa tumefikia hatima ya kuwa na chanjo ya virusi vya UKIMWI.
Kwa hiyo, tuendelee kuvumilia wakati wanasayansi wakifanya kazi yao kwenye maabara zetu. (Makofi)

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nimesimama kwa sababu Mheshimiwa Mbunge Lucy Magereli anazungumzia upatikanaji wa dawa za ARV.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie Bunge lako Tukufu kusema kwamba tunazo ARV ambazo kuanzia mwezi Oktoba, 2016 zinatolewa kwa kila Mtanzania atakayepima na kukutwa na maambukizi ya VVU.
Mheshimiwa Naibu pika, sasa kwa nini nimesimama? Kati ya watu wenye maambukizi ya VVU, wanawake wanaotumia ARV ni asilimia 73, wanaume ni asilimia 48 tu. Kwa hiyo, nitoe wito kwa wanaume wote Tanzania watumie dawa za ARV ili kwa pamoja tuweze kupunguza maambukizi ya VVU nchini. Acheni kujiona nyie mna misuli, ni wababe, dawa za ARV zipo, tumieni ili tuweze kupunguza maambukizi ya UKIMWI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kwa sababu kati ya maambukizi mapya ya vijana wetu wenye miaka 15 mpaka 24 kwa wavulana ni asilimia nane na wasichana ni zaidi ya asilimia 80. Maana yake hawa wanaume ndiyo wanarudi tena kwa watoto wadogo na hivyo kufanya kuwepo kwa maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona nitumie fursa hii Waheshimiwa Wabunge wakawahamasishe wanaume watumie ARV, zipo bure, zinapatikana na mtu yeyote akipima anapata bila shida. Ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ninampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Afya kwa majibu ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa ili kuweza kulithibitishai Bunge lako kwamba mfuko huu ambao ulianzishwa kwa Sheria Namba 6 ya mwaka 2015 na unasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, umeanza kufanya kazi nzuri sana pamoja na uchanga wake.
Mheshimwa Naibu Spika, maagizo ya Kamati kama alivyosema Mbunge aliyeuliza swali, yalikuwa na malengo ya kuhakikisha kwamba Serikali inasimamia mfuko huu na unaanza kufanya kazi.
Mheshimwa Naibu Spika, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Waheshimiwa Wabunge wa Kamati inayohusika na masuala ya UKIMWI waliiagiza Serikali, kwa rasilimali ndogo iliyopatikana ni lazima sasa mfuko uanze kuhakikisha unatoa fedha kupeleka Wizara ya Afya ili kushughulika na dawa na kuongeza maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Kifungu cha 6(1) cha Sheria hiyo, mfuko unakaribia kutoa, umeshapitisha kwenye Bodi jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni 1.45 kwa ajili ya kununua dawa za septrine na kwa ajili ya kujenga Kituo cha Upimaji Mererani na kujenga kituo kingine cha upimaji kwenye Visiwa ndani ya Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niwathibitishie Wabunge kwamba Kamati ilifanya kazi nzuri na Serikali imepokea maagizo hayo na tayari mfuko wetu umeanza kuonesha kwamba tunaanza kujitegemea ndani ya Serikali yetu ingawa wafadhili bado wanaendelea kutusaidia. (Makofi)
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri sana inayofanywa na Wizara ya Ardhi lakini bado uhitaji wa suala hili la uandaaji ramani ningeendelea kupendekeza kwamba lifanywe na Wizara ya Ardhi badala kurudishwa kwa Halmashauri kwa sababu bado Halmashauri zetu zina mbinyo mkubwa sana wa bajeti.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuandaa mipango maalum kupitia Wizara ya Ardhi kuhakikisha kwamba ramani za Mipango Miji ya jumla kwa maana ya master plan zinapatikana nchi nzima na kuacha zile detailed plan ndiyo zifanywe na Halmashauri?
Swali la pili, kwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri anasema kwamba ameacha Halmashauri zishirikiane na sekta binafsi kwa ajili ya kuandaa hizi ramani za Mipango Miji. Sitaki kukubaliana na ningependa nieleze tu bayana kwamba katika kuliachia Halmashauri zetu suala hili linafungulia mianya ya rushwa na wananchi wengine kushindwa kumudu gharama, kwa sababu sasa hivi ukipeleka mchoro wako binafsi au kuomba mchoro binafsi unaambiwa wewe mwenyewe ndiyo uugharamie mpaka na kikao cha Halmashauri kikae kwa gharama ya mwombaji kupimiwa eneo la ardhi. Je, Serikali haioni kwamba inafungua mianya rushwa na kuwafanya wananchi washindwe kabisa kupata huduma hii kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme tu kwamba nakubaliana naye katika swali lake jinsi alivyouliza, kwa sababu taratibu zinazoendelea mpaka sasa suala zima la upangaji miji ni jukumu la Halmashauri zenyewe. Napingana naye kwenye suala la kusema kwamba Wizara ifanye kazi hii. Wizara kazi yetu ni kusimamia sera na tunaposimamia sera maana yake tunafanya ufuatiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukumbuke mwaka 2016 Waziri alitoa ramani kama kuleta chachu kwenye Halmashauri zetu zote ili waweze kufanya jukumu hilo ambalo ni la kwao kama mamlaka za upangaji miji. Mara nyingi kama wananchi kule na hasa kwenye maeneo ya vijiji Wenyeviti wa Mitaa kama hawatambui maeneo yao migogoro inakuwa mingi. Kwa hiyo, nitoe rai tu kwa Halmashauri kuendelea kutekeleza jukumu lao la kuandaa zile ramani na baadaye kuzishusha mpaka kwenye maeneo ya vijiji na mitaa kule ili wale wenye dhamana kule waweze kuchukua jukumu lao la kuelimisha watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika zoezi linaloendelea la urasimishaji kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi Ibara ya 37 (d)(4) ambapo urasimishaji unaendelea, bado zoezi la kugawa linatakiwa liendelee katika utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge akubaliane kwamba Wizara haiwezi kupora mamlaka ya Halmashauri isipokuwa tutaendelea kuwakumbusha ili watimize wajibu wao. (Makofi)
MHE. LUCY S. MAGERELI: Nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika, kwa fursa niulize swali la nyongeza.
Changamoto ya umeme kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni bado ni kubwa sana pamoja na kwamba mwaka jana wakati wa bajeti, wakati Waziri akijibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ndungulile, alieleza bayana ya kwamba tatizo la msongo mdogo wa umeme eneo la Kigamboni litakuwa limekwisha mwaka jana mwezi Agosti, lakini hadi tunapozungumza leo bado changamoto ya umeme mdogo Kigamboni ni kubwa, lakini ukiachilia hilo umeme huo unakatika mara 15 kwa siku.
Je, Serikali ina maelezo gani kuhusu suala hili na kuchelewa kwa kutekelezwa kwa mradi huu wa kufunga transfoma kubwa yenye msongo wa kutosha kutupa huduma ya umeme eneo la Kigamboni?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Lucy kwa swali lake zuri na ni muhimu sana. Kupitia Bunge lako Tukufu, napenda nitoe taarifa ya Serikali kuhusiana na utekelezaji wa miradi ya umeme muhimu sana kwa wananchi wa maeneo ya Kigamboni.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa wananchi wa Kigamboni hivi sasa hawana umeme wa uhakika, lakini hatua madhubuti tunayofanya ni kujenga substation itakayowapelekea umeme sasa wananchi wa Kigamboni wote, mradi huu utakamilika mwezi tarehe 25 Mei tutakuwa tumeshawapelekea wananchi wa Kigamboni.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya haraka tunachofanya hivi sasa tunakamilisha utekelezaji wa mradi wa kabambe katika Jiji la Dar es Salaam kwa eneo la Mbagala. Mradi tunategemea kuuwasha kati ya tarehe 20 mwezi huu kuanzia tarehe 12 tutakuwa tumeshawasha na tarehe 20. Mradi huu utahudumia wananchi wa Mbagala, Kurasini, Kigamboni pamoja na maeneo mengine ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge, kazi hiyo inafanyika na wananchi wa Kigamboni watarajie kwamba umeme utapatikana kufikia mwisho wa mwezi huu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante kwa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni tuna mradi mkubwa sana wa maji wa visima 20 ambao ulianza mwaka 2013 na mradi huo ulitarajiwa kukamilika mwaka jana Desemba, lakini haukukamilika. Kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri wa Maji alitutembelea Oktoba mwaka jana na akatoa maelekezo kwa Kampuni ya Serengeti kwamba ikamilishe mradi huo kabla ya Desemba mwaka jana na ikiwa haitakamilisha basi watatakiwa kulipa gharama za ucheleweshaji.
Niombe sasa Serikali itusaidie kufahamu ni nini kinachoendelea katika mradi ule mpaka sasa haujakamilika wakati ingekuwa suluhu ya tatizo la maji katika sehemu kubwa sana ya Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani Wilaya kama Mkuranga? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hilo ni eneo la Kimbiji na Mpera tunachimba visima 20, visima 17 viliishakamilika, vitatu bado vinakamilika mwezi Julai. Ni kweli teknolojia ya kuchimba visima katika eneo hilo imetusumbua kidogo, ni visima virefu sana vinakwenda zaidi ya mita 300 mpaka 600 na kuna maji mengi sana. Kutokana na hilo ilibidi tuwape addendum kutokana na hiyo teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo uchimbaji wa visima utakamilika mwezi ujao mwishoni visima vitakuwa vimekamilika, kazi itakayofuatia sasa tunatafuta fedha kwa ajili ya kuweka miundombinu ya usambazaji. Kwa hiyo maeneo ya Kigamboni na Temeke yote yatapata maji. Visima hivyo vitatoa lita millioni 260 kwa siku, ndio maana tunasema Dar es Salaam haitakuwa na shida ya maji.
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Kigamboni, Kata ya Kimbiji, tuna Kiwada cha Saruji cha Nyati. Nimesikia majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kuna Environmental Impact Assessment ambayo hufanyika lakini tuna changamoto kubwa sana ya vumbi linalotimka kutoka kiwandani katika kata ile. Bahati mbaya kabisa kile kiwanda kiko katikati ya makazi ya watu. Sasa hivi minazi yetu Kimbiji haizai, miembe haizai, michungwa haizai, mazao ya mahindi tukilima kuvuna tunashindwa kwenda kulima kwa sababu panakuwa na vumbi kali sana ndani ya mazao ambayo tunayalima.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba utusaidie kwenye hili, ni kweli Environmental Impact Assessment ilifanyika, na je ilitoa majibu sahihi? Mbona tunapata adha hii kubwa namna hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Nyati, nilipokea malalamiko ya kiwanda hiki na baada ya kuletwa, yalikuwa malalamiko mengi sana dhidi ya uchafuzi wa mazingira ya kiwanda hiki. Kwanza, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Environmental Impact Assessment ilifanyika katika kiwanda hicho na kiwanda kikajengwa, japokuwa katika utekelezaji wake zilijitokeza changamoto.
Mheshimiwa Spika, nilipokwenda kwenye ziara hiyo kulikuwa na changamoto ya hilo suala la vumbi, lakini suala la vumbi NEMC walikwenda kushughulika pamoja na kiwanda na kuhakikisha kwamba changamoto hiyo imetatuliwa. Kulikuwa na changamoto ya kulipa fidia wananchi waliokuwa wanaishi karibu sana na kiwanda, wananchi hao wote wamekwisha kulipwa fidia mpaka sasa hivi tunavyozungumza.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na tatizo la yale makaa ya mawe kwamba yalikuwa yako nje na yalikuwa mvua zikinyesha yanatiririka mpaka kwenye vyanzo vya maji na kuchafua vyanzo hivyo. Tatizo hilo lilishughulikiwa na sasa makaa hayo hayaendi tena kwenye vyanzo vya maji. Kama bado kuna tatizo hilo analolizungumza sasa hivi Mheshimiwa Mbunge, tutakwenda kujiridhisha kuona kama kiwanda hicho bado kina tatizo hilo na kuchukua hatua stahiki.
MHE. LUCY S.MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na nimeshukuru kupata majibu ya Serikali, lakini...
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijauliza maswali yangu mawili ya nyongeza naomba nitoe maelezo mafupi ya utangulizi kwamba ni fedheha na ni mambo ya aibu kabisa kwa Jiji kongwe kama Dar es Salam kwa Mji Mkuu wa biashara wa muda mrefu tangu uhuru wa nchi hii kupatikana kuendelea kuteseka na adha ya maji mpaka leo hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu ya Serikali anazungumzia habari ya visima 20 ambavyo vinachimbwa Mpera na Kimbiji. Kwa bahati mbaya ni kwamba visima hivyo mpaka sasa havijakamilika kwenye zoezi la kuchimbwa.
Je, fedha wanazosema wanatafuta, zinatafutwa kutoka wapi na zitapatikana lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwenye majibu ya Waziri anasema katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepanga kukamilisha miradi ya viporo kama kipaumbele. Tunavyozungumza bajeti 2017/2018 inakwisha siku chache sana zijazo na bado….
Mheshimiwa Mwenyekiti, swala hili linaitwa kipaumbele. Je, Mheshimiwa Waziri anajibu tofauti kwenye swali (b)?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyezi Mungu anasema unapaswa kushukuru kwa kila jambo na usipowashukuru binadamu hata Mwenyezi Mungu unaweza hutamshukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kabisa Jiji la Dar es Salam lilikuwa na changamoto kubwa sana ya maji, lakini mpaka sasa asilimia 78 ya wananchi wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza. Watu wa Mamlaka ya DAWASCO wana mpango mkubwa mkubwa wa kuongeza mtambo ile wa Ruvu juu na Ruvu chini katika kuhakikisha wananchi wa Dar es Salaam wanaendelea kupata maji, safi salama na yenye kuwatosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa katika maeneo ya viunga vya Dar es Salam kwenye changamoto ya maji Serikali imeshachimba visima 20 na sasa tumejipanga katika kuhakikisha tunasambaza maji ili wananchi wa Ukonga na maeneo mengine waweze kupata maji safi, salama na yenye kutosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miradi ya viporo, kazi inaendelea kufanyika, nimuombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kutuamini na sisi katika yale maeneo ambapo tunahitajika kukamilisha viporo vile tutaendelea kuvikamilisha kwa wakati, ahsante sana.
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza na nieleze masikitiko yangu kwamba swali langu nilileta mwaka 2016 lakini kwa bahati mbaya limekuja 2019. Nishukuru kwa maendeleo ambayo yamefanywa ya kusambaza hizo mashine za kielektroniki nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kusambazwa mashine hizo sasa hivi Jeshi la Polisi limekuwa sehemu ya chanzo kikuu cha mapato ya Serikali na wanapangiwa viwango vya fedha za kukusanya. Kwa hiyo, uwepo wa mashine hizi pamoja na kwamba tulidhani ingekuwa ni suluhisho lakini imekuwa chanzo cha kuwabambika makosa watumia barabara ili kuzalisha mapatao. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwanusuru watumia barabara kwa makosa haya ya kubambikizwa na kulazimishwa kulipa faini ili tu kufikia viwango za fedha walizokubaliana vitendo vinavyofanywa na askari wa usalama barabarani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, hivi karibuni Mheshimiwa Kangi Lugola, Waziri mwenye dhamana ya Mambo ya Ndani alitoa maelekezo kwamba gari linapokamatwa hata kama litakuwa na makosa zaidi ya moja basi liandikiwe kosa moja lakini hadi tunavyozungumza, magari mengi yanaandikiwa faini zaidi ya kosa moja na kutozwa faini na penalties kinyume na maelekezo ya Mheshimiwa Waziri. Je, Serikali inaweza kurejea tena agizo lake kupitia Bunge letu Tukufu ili liwe maelekezo rasmi ya Serikali kwa watekeleza sharia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na hoja ya kubambikiwa kesi ambayo ametuhumu Askari wa Usalama wa Barabarani, nimwambie tu kwamba yanapotokea matukio kama haya kwa baadhi ya askari wetu tunachukua hatua na hata hili agizo la Mheshimiwa Waziri lilikuwa linalenga kuziba mianya ya aina kama hiyo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge kwamba Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nchi ndiye mwenye dhamana ya mwisho ya Wizara hii na maagizo yake ni lazima yatekelezwe. Maagizo haya yanatekelezwa ikiwa kuna upungufu katika utekelezaji wake, kama labda kuna watu ambao hawatekelezi, hiyo taarifa hatujaipata rasmi lakini kimsingi Mheshimiwa Waziri ametoa agizo na linapaswa kutekelezwa kwa maslahi ya wananchi wa nchi yetu ambao wanatumia barabara.