Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ruth Hiyob Mollel (9 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia mada iliyoko mezani hapo na nimshukuru Mungu kuweza kuwepo mjengoni mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiiti, nimepitia review ya mwaka 2014/2015, vilevile ya mwaka huu wa sasa ambao tunauzungumzia. Kimsingi, tumekuwa na malengo mengi ambayo hayapimiki na nina maana gani ninaposema hayapimiki? Unakuta kwa mfano, mapitio ya mwaka jana tumesema tuta-train walimu 460, lakini hatuambiwi katika ule mwaka ni wangapi wamekuwa trained. Kwa hiyo, tunashindwa kujua sasa, hawa waliokuwa trained ni wangapi na mmeshindwa wapi kwa wale ambao hatukufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hata ukipitia huu Mpango wa sasa hivi ambao Mheshimiwa Waziri ameuleta, bado tatizo liko pale pale, anazungumzia kusomesha vijana wengi kwa mkupuo katika fani mbalimbali, lakini hasemi anafundisha vijana wangapi, wa fani zipi na kwa mchanganuo upi. Kwa hiyo, napendekeza kwamba katika Mpango utakaoletwa yale malengo yawe bayana, yaweze kupimika kusudi tuweze kuisimamia Serikali kwa jinsi ambavyo inatenda kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mpango umezungumzia suala la viwanda, tunataka Tanzania iwe nchi ya uchumi wa viwanda, lakini suala la rasilimali watu halijajitokeza bayana. Kwa sababu kama ni viwanda tutahitaji fani mbalimbali za kuweza kusukuma hili gurudumu la viwanda, lakini Serikali haijaleta mchanganuo wa fani zipi ambazo tutazihitaji kwa ajili ya huu uchumi wa viwanda.
Kwa hiyo, ni ushauri wangu Serikali ikachambue, ikaangalie kwa miaka kumi ijayo tunahitaji human capital gani, katika maeneo gani kusudi kila mwaka mpango wa mwaka unapoletwa hapa muweze kuainisha kwamba, mwaka huu Serikali itafanya hiki, mwaka wa kesho Serikali itafanya hiki, kusudi Bunge liweze kufuatilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Mpango huu ambao Mheshimiwa Waziri ameuwasilisha, kwa maoni yangu mimi kama Mbunge wa Chadema, vipaumbele ni vingi, wala havitatekelezeka. Kwa mfano, katika ukurasa wa 25, Ardhi na Makazi. Tumesema upimaji na utoaji hati miliki, naomba muangalie hivyo vipaumbele vya Ardhi, Nyumba na Makazi; hivi kwa mwaka huu hatuwezi kuvifanya, haviwezi kufanyika wala havipimiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, tunataka Serikali ije na mchanganuo. Kwa mfano, anasema watapima majiji na vijiji na miji mikubwa. Sasa Serikali ituambie katika majiji, miji na vijiji ni vingapi? Ni mji mmoja, ni miji miwili, ni vijiji kumi kusudi itakapokuja taarifa ya utekelezaji tujue kama kazi hiyo imefanyika au haijafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumzia kuhusu rasilimali watu. Kama kweli tunataka kupata rasilimali watu ambayo itasaidia, Serikali katika kujenga uchumi huu, basi rasilimali watu hii iangaliwe tangu mwanzo. Waziri wa Elimu aangalie laboratories ngapi zinajengwa kwenye mashule, maana ndiko tunakochimbua wataalam ambao baadaye watakuja kusukuma huu uchumi wa kati ambao tunauzungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye suala la kilimo. Serikali imesema kilimo ni uti wa mgongo, ni kweli, lakini je, Serikali inafanya nini kweli kusimamia kilimo? Kwa sababu lazima tukubali, kilimo nchi hii bado ni subsistence farming. Kwa hiyo, wakulima wanatakiwa kuangaliwa kwa jicho la karibu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Serikali haijazungumzia kuhusu Extension Officers. Extension Officers wanahitajika wengi na ingependeza kama Serikali ingekuja kuangalia ratio ya Extension Officer na wakulima, kama tunavyofanya ratio ya madaktari na wagonjwa, nesi na wagonjwa, kwa hiyo na Extension Officers ifanywe hivyo hivyo, kusudi muweze kufanikiwa katika kuinua kilimo ambacho pia kinatoa ajira kwa watu wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa ushauri kwa Serikali; Wizara ya Kilimo, SUA na Vyuo vya Kilimo na mkulima wafanye kazi kwa pamoja (tripartite). Watu wa ugani wawezeshwe kwa vifaa, wawezeshwe kwa pikipiki, waweze kwenda kutembelea wakulima na wawe na mafaili kama ya wagonjwa hospitali. Nchi nyingine ndivyo wanavyofanya, unakuta Afisa Ugani anawajua wakulima wake kwa jina na ana file analokwenda kuangalia wakulima wake na kujua matatizo yao. Naishauri Serikali ichukue mapendekezo hayo ili iweze kwenda kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la viwanda tunavyo viwanda vingi na vingi vimekufaa. Serikali inahitajika kuangalia viwanda katika maeneo mbalimbali, kwa mfano, Tanga kuna matunda mengi sana, kiwepo kiwanda pale Tanga cha ku-process matunda. Mahali kama Shinyanga kuna nyama nyingi, ng‟ombe wengi sana, kuna pamba nyingi sana, viwepo viwanda vya ku-process vitu hivi ili itoe ajira na kukuza uchumi wa nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimshukuru Mungu kwanza kwa kuweza kusimama hapa na nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia kwenye hoja hii iliyopo hapa mezani.
Mheshimiwa Spika, naungana na Wabunge wote ambao wameshazungumza kuhusu afya, kwamba afya kwa kweli, ni msingi mkubwa sana wa uchumi. Taifa lenye afya ndiyo linaweza kujenga uchumi wa nchi hii. Kwa hiyo, nasema Mawaziri mna kazi kubwa sana ya kuona kwamba, Taifa hili linakuwa na afya njema.
Mheshimiwa Spika, ningependa kuzungumzia suala la mfumo wa afya. Mfumo wa afya umekaa vizuri kwa sababu tunaanza zahanati, tunakuja kituo cha afya, tunakuja mkoa na kadhalika. Mfumo umekaa vizuri sana kama tutautumia kwa ajili ya kuboresha afya ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, niseme kwamba, tukiangalia katika Hospitali ya Muhimbili kwa mfano, imejaa wagonjwa sana na huu mrundikano wa wagonjwa unatokana na kwamba hizi peripheral hospitals hazijawa na vifaa vya kutosha ambapo wagonjwa watatibiwa kule, kupunguza huu msongamano ulioko Muhimbili. Huu msongamano hautakwisha mpaka hizi peripheral hospitals Mwananyamala, Temeke, najua zimepanuliwa, lakini bado hazikidhi kuweza kupunguza msongamano ambao uko pale Muhimbili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri kwamba, Hospitali hizi za peripheral health centres, kuna hizi Hospitali za Rufaa ambazo zimeteuliwa za Mikoa zingepewa vifaa tiba vya kisasa kama CT Scan kusudi ianze kuchuja wagonjwa tangu pale mwanzo halafu Muhimbili waje wale ambao kwa kweli wanahitaji specialized treatment.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunapendekeza tuwe na CT Scan katika hizi referral hospitals, tuwe na CT Scans pia katika Hospitali za Mbeya najua pengine ipo, Bugando na KCMC kusudi hii influx kubwa inayokuja Muhimbili ipungue. Hata influx pia katika hizi Hospitali nyingine za Bugando, KCMC na Mbeya bado nao wanakuwa na wagonjwa wengi, lakini kama hizi referral hospitals za mkoa tulizoziteuwa zikifanya kazi, basi tutapunguza msongamano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nina mawazo kwamba hizi hospitali nyingine za Super Specialisation za Bugando, KCMC, Mbeya na Muhimbili na zenyewe zipewe vifaa tiba vya kisasa. Kwa mfano, tukiwa na vifaa tiba vya kisasa kabisa huu utaratibu wa kupeleka wagonjwa wengi nje utapungua.
Kwanza wagonjwa wengi watatibiwa hapa nchini na kwa yale maeneo ambayo hatuna uwezo nayo, kama kuna eneo ambalo hatuna specialization, tunaweza kuleta madaktari kutoka nje wakaja hapa kwa bei nafuu, wakatibu wagongwa wengi.
Mheshimiwa Spika, baada ya kutibu wagonjwa wengi vile vile tunajenga uwezo wa wataalam wetu ndani ya nchi, kama tunavyofanya katika Kitengo cha Moyo, hii system ingeendelea pia kwenye maeneo ya magonjwa mengine ambayo tunapeleka wagonjwa nje.
Kwa hiyo, ni maoni yangu na maoni ya Kambi ya Upinzani kwamba, tuzi-strengthern tupunguze wagonjwa kupelekwa nje na wagonjwa wengi zaidi waweze kutibiwa ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri na kuna eneo ambalo hajaligusia sana, amezungumzia kuhusu watoto na changamoto za watoto, lakini kuna hawa watoto ambao wako katika mazingira magumu, ukipita mitaani Dar es Salaam utakuta watoto wengi wanaombaomba, wanatumiwa kuomba.
Mheshimiwa Spika, sasa ningependa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja aweze ku-share na sisi kuona ni hatua gani Wizara itachukua? Najua itahusisha labda na Wizara ya Elimu kwa sababu watoto wale wana haki ya kupata elimu, ni kwa jinsi gani mkakati utakaoletwa ili kuona jinsi gani hawa watoto wanasaidiwa kuondoka katika haya mazingira ambayo yanasababisha kukosa haki yao ya elimu na haki ya kutokunyanyaswa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna eneo moja pia ambalo wengine wameligusia, eneo la magonjwa ya akili. Nimeshakuwa na mgonjwa pale Muhimbili kwa kweli hali ya pale ile Faculty ya Psychiatric ni mbaya sana. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana uweze kwenda pale mahali. Pale wagonjwa wanafungiwa kama wako jela! Wanafungiwa, hawatoki na hawapati hata nafasi ya kupatiwa counseling kwa sababu yale maeneo hayawezekani.
Mheshimiwa Spika, najua kwamba kuna kazi ambayo tayari kile kitengo kimeshafanya, wameshafanya sketch ya kujenga kituo cha kisasa lakini hawana architectural drawings kwa sababu hawana fedha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, naomba uende pale uone na tutafute namna, hata kama kutafuta joint venture, kama inawezekana au donors whatever, lakini waweze kujenga kituo cha kisasa kwa sababu sasa hivi magonjwa ya akili yamezidi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, magonjwa ya akili yamezidi sana kwa sababu ya ulevi wa kupindukia, msongo wa mawazo, umaskini na madawa ya kulenya. Kwa hiyo, hawa wagonjwa wanaongezeka kwa wingi sana na kile kitengo hakiwezi kuhimili. Kwa hiyo, ni rai yangu kwako uende ukatembelee pale hali ni mbaya sana. Naomba uende pale uweze kuona hali halisi na uonane na hawa wataalam wa pale ambao tayari wana sketch na wameshakisia ni kiasi gani cha fedha kitahitajika kujenga kituo cha kisasa cha magonjwa ya akili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wengi wamezungumzia kuhusu suala la tiba ya wazee. Tunasema kwamba tiba ya wazee ni bure, lakini ukweli ni kwamba sio bure kiasi hicho. Bure ni kumwona Daktari tu lakini ikija kwenye suala zima la matibabu ambapo ndiyo msingi uliompeleka yule mzee hospitali kwa kweli inakuwa ni matatizo makubwa sana. Kwa hiyo, napendekeza kwamba tutafute namna ambayo tunaweza tukachangia zaidi hata kwenye NHIF ili zipatikane pesa ambazo tutawawezesha hawa wazee kupata hizi kadi za NHIF waende wakatibiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi pia ni mzee lakini advantage niliyonayo ni kwamba nina kadi ya NHIF lakini wapo ambao hawana advantage ya NHIF anakwenda pale hawezi kutibiwa. Huyu mtu ujana wake wote kaumalizia katika kujenga nchi hii, lakini wakati sasa ana uhitaji mkubwa hawezi kusaidiwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, kwa kweli hili jambo la wazee naomba mliangalie kwa jicho la huruma kabisa, tuone ni jinsi gani wazee wetu wanaweza kupata tiba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu wamezungumzia kuhusu zahanati, vituo vya afya na hospitali za mikoa, kweli ziko chini ya TAMISEMI. Lazima tukubali kwamba pia anayesimamia na kutoa standards na kuona zahanati inatakiwa itibu nini, vituo vya afya vitibu nini, hospitali za mkoa ziwe na vifaa gani ni Wizara ya Afya. Kwa hiyo, napendekeza katika hospitali za mkoa, Wizara ya Afya iwe na wakaguzi ambao kazi yao itakuwa kwenda kutembelea hivi vituo vya afya na zahanati kuona kwamba zile tiba zinazotakiwa kutolewa pale zinatolewa.
Mheshimiwa Spika, udhibiti huu pia utasaidia kupunguza msongamano kwenye hospitali za wilaya na mkoa. Kwa hiyo, ni mawazo yangu kwamba tuwe na wakaguzi ambao watakuwa ni waajiriwa wa Wizara ya Afya ambao wataweza kwenda kusimamia afya kwa sababu usimamizi wa afya ni wa Wizara na hakuna mtu wa kumtupia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba ufanye hivyo kama fedha zitaruhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante! Napenda ku-declare interest kwamba, nilishafanya kazi katika ofisi inayohusika na mazingira na najaribu kuangalia uhusiano wa uchimbaji wa madini na mazingira. (Makofi)
Natambua kwamba uchimbaji wa madini au madini yenyewe unajenga uchumi wa nchi yetu na una faida kubwa katika nchi yetu, hilo halina ubishi. Hata hivyo, ni ukweli pia kwamba uchimbaji madini unaharibu mazingira kama usipodhibitiwa na kusimamiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo migodi mikubwa na najua kwamba kabla hawajapata leseni lazima huwa inafanywa tathmini ya athari kwa mazingira ambayo tunaita Environment Impact Assessment (EIA) - tathmini ya athali kwa mazingira na baada ya hapo leseni zinatolewa, baada ya kutoa ile EIA inakuwa kwamba tunasahau kabisa kwamba kuna jambo sasa la kufuatilia kwa karibu ile migodi mikubwa inavyofanya shughuli zake na kuweza kuona jinsi gani wanavyoharibu mazingira kwa namna ya maji yenye sumu, namna ya afya ya wale wafanyakazi na mara nyingi tunakuwa reactive jambo limeshatokea ndiyo tunakwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba leseni zinapotolewa pamoja na kwamba EIA inafanywa na Wizara nyingine, lakini kunakuwa hakuna uhusiano wa karibu sana na sector Ministry. Mapendekezo yangu ni kwamba EIA inavyotolewa na certificate inapotolewa, hizi Wizara ziweze kuzungumza ili kusudi hata wakati wa kwenda kufanya ukaguzi tupate wale wadau wakubwa wote ambao wanahusika na migodi na wale wanaohusika na mambo ya mazingira pamoja na Wilaya zile zenye madini yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesikia Wabunge wengi wakichangia wanasema kwamba, watu wanapata leseni wanakwenda kwenye maeneo yao wao wenyewe wenye Wilaya zao hawana habari. Ina maana kwamba, Serikali inafanya kazi mkono mmoja haujui mfuko mwingine unafanya kitu gani! Kwa hiyo, tunahitaji tuwe na timu ambayo anayetoa leseni, anayefanya EIA na yule mwenye eneo lake ambalo migodi ipo wote wafahamu ni kitu gani kinachoendelea katika lile eneo kwa ajili ya kudhibiti na kuhakikisha mazingira yanakuwa salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona katika speech ya Mheshimiwa Waziri kwamba kuna maeneo mwaka jana 2015/2016 walitenga heka 7,731 kwa ajili ya wachimbaji wadogo na mwaka 2016/2017 wametenga hekta 12, 000 ni jambo jema. Nashauri kwamba, wachimbaji wadogo nao pia wanaharibu mazingira sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepita Mererani, nilishapita wakati mwingine sehemu za kule kwenye diamond - Mwadui, wanachimba wanaacha mashimo, ile ardhi inakuwa tupu hakuna miti ni mashimo! Kwa hiyo, kuna umuhimu mkubwa sana kwa ajili ya kudhibiti na kuangalia kwamba mazingira yanarejeshwa katika hali yake ya asili. Najua wachimbaji wadogo wadogo wanakuwa na Environment Management Plans, lakini nani anawasimamia? Hakuna mtu anayewasimamia, wanachimba wanaacha!
Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza kwamba Wizara inayohusika ya Nishati na Madini, Wizara inayohusika na Mazingira na yale maeneo ambayo ile migodi inachimbwa, ile midogo midogo, watafute jinsi ya kuya-incentivised wale wachimbaji wadogo kusudi wahakikishe kwamba lile eneo lililochimbwa na kuharibiwa linarudishwa katika hali yake ya asili ya miti na majani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia pia katika taarifa ya Audit ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu alivyozungumzia kuhusu petroleum exploration na pia nimeona kwamba Ofisi ya Rais Mazingira wamefanya inspection tatu tu katika miradi karibu 71 na inaelekea kwamba hakuna uwezo mkubwa sana. Hili ni eneo pia ambalo ningependa Mheshimiwa Waziri alizungumzie ni jinsi gani inspections ya haya maeneo itaimarishwa ili kuhakikisha kwamba tunachunga mazingira yetu. Napendekeza pia hizi teams ziendelee kufanya kazi kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la umeme, najua kwamba mimi mwenyewe nilishavuta umeme nikaweka nguzo kama mbili, tatu na tunalipia gharama kubwa na naamini kuna wengi pia wanafanya hivyo na hizo nguzo baadaye ni za TANESCO pamoja na kwamba ni sisi ndiyo tumezilipia pamoja na LUKU tumezilipia.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda Mheshimiwa Waziri anapomalizia hoja yake atuambie ni kwa jinsi gani watu ambao wameweka hizo nguzo za umeme kwa gharama zao na hizo nguzo ni za TANESCO ni kwa namna gani wanaweza ku- compensate? Je, inawezekana ku- compensate kwa kupitia bill za umeme kwamba wewe umeweka nguzo tatu, bei ni kadhaa na kwamba labda bill ya umeme uwe unalipa kiasi fulani na ufidie kwa ile miti ya TANESCO ambayo umeweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitashukuru Mheshimiwa Waziri akitujibu hilo suala tuweze kujua ni jinsi gani TANESCO wanaweza kutu-compensate.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wengi sana wamezungumzia suala la Nyamongo na mimi nasikitishwa kwamba, nilikuwemo suala la Nyamongo lilikuwepo, nimetoka sasa sijui karibu miaka mingapi suala la Nyamongo bado linaendelea. Mheshimiwa Waziri, hii Nyamongo ina shida gani, kwa nini hii issue haiishi? Maana yake imekuwa ya muda mrefu sana na miaka mingi, pengine labda kuna kitu Waheshimiwa Wabunge hatujui, labda kuna tatizo fulani, tunaomba Mheshimiwa Waziri anapomaliza hoja yake, atueleze kuna shida gani na hili suala la Nyamongo ambalo tumelizungumza miaka nenda miaka rudi!
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ambayo nimepewa kuweza kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niunge mkono hotuba ya Kambi ya Upinzani ambayo ilitolewa kabla. Katika mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano ni Tanzania ya viwanda, nimepitia katika Mpango huo ambao umewasilishwa na nasikitika kusema kwamba, katika Mpango wote ambao umewasilishwa pamoja na umuhimu wa kukuza viwanda, sijaona ni kwa namna gani rasilimali watu imepangwa kusudi kusaidia kuendesha viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu mwaka jana katika ule Mpango kulikuwa na suala la kupeleka wanafunzi 159 wa petroleum and gas kwenda kusoma, lakini sioni katika mpango wa mwaka huu ni kwa jinsi gani tumefikia wapi na wale 159 kwamba wanatosha au tunahitaji ku-train watumishi wengine kwa ajili ya petroleum and gas.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mwaka jana Serikali iliahidi kwamba itajenga vyuo vinne vya ufundi katika mikoa mbalimbali lakini katika mpango wa mwaka huu Serikali haijaainisha kama bado tunaendelea na hivyo vyuo vinne vya ufundi, imekuja na mawazo mapya ya kutengeneza karakana, sijui miundombinu. Je, vile vyuo vinne ambavyo Serikali iliahidi itavijenga, imefikia wapi? Ingependeza zaidi kama tungeweza tukapata status ya yale ambayo yalisemwa mwaka jana tuweze kufuatilia kama kweli yanatekelezwa au la! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mikopo ya elimu ya juu. Kama nilivyosema juzi, hii taasisi ya mikopo ilianzishwa ili kupanua udahili si kupanua udahili tu na kusaidia wanafunzi ambao ni wahitaji, lakini tumeona mwaka jana, kwa bajeti ya juzi hakuna pesa iliyotolewa ya kutosha na kwa mpango huu ambao umewasilishwa inasemekana kwamba udahili utaongezwa na tuta-train watu wengi, kama ikiwa mpaka sasa hivi bajeti inayotoka hata haikidhi wale wanafunzi waliokuwepo, je, ni kweli Serikali itakuwa na hiyo pesa ya kuingiza kwenye mzunguko mwaka kesho?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ningependa Waziri anisaidie kujibu, kuna hii hoja ambayo imeshajitokeza kwamba kuna wanafunzi ambao wanaendelea wananyimwa mikopo, mimi nauliza busara ya kawaida tu inasema kwamba hawa wameshaingia kwenye mkataba na Loans Board na wamesaini mikataba ya jinsi ya kurudisha hiyo hela na leo Serikali inasitisha kuwapa mikopo hawa wanafunzi wanaoendelea, ni kwamba Serikali imekiuka utaratibu wake wenyewe wa kuwapa wanafunzi hawa mikopo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, busara ya kawaida ingekuwa kuendelea kuwapa hawa wanaoendelea, halafu mipango mipya au uhuishaji au utaratibu mpya ungeanza na hawa ambao ni wapya, ndiyo utaratibu tunaofuata. Ningependa kupata ufafanuzi kuhusu hawa wanafunzi wanaoendelea ambao walikuwa wanapewa mikopo na sasa inasitishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu, ni suala la Watumishi wa Umma. Naomba ku-declare kwanza interest kwamba nilikuwa Katibu Mkuu Utumishi. Nasikitishwa kwa jinsi ambavyo watumishi wamekuwa wanatumbuliwa left and right. Utakuta Mawaziri wanatumbua japokuwa tangu majuzi kidogo wametulia, Ma-RC wanatumbua, DC anatumua, DED anatumbua, wakati tunajua kabisa Mamlaka ya nidhamu ni watu gani ambao Rais amewakasimu. Hii inapelekea watumishi kukosa imani, kukosa amani na kukosa ubunifu na matokeo yake Utumishi wa Umma ambao ndiyo injini ya maendeleo utashindwa kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Makada wengi ambao hawakuwepo katika Utumishi wa Umma kabisa wamewekwa kwenye maeneo ya utendaji ambayo inakwenda ku-compromise uadilifu na uimara wa Utumishi wa Umma. Utumishi wa Umma duniani kote unaishi zaidi ya Wanasiasa. Wanasiasa malengo yao ni miaka mitano tu. Utumishi wa umma ambao ni legelege hautaweza kutekeleza huu Mpango ambao unaletwa. Kwa hiyo, hili jambo ni lazima liangaliwe kwa ukaribu sana ili kusudi Watumishi wa Umma wapate imani na waweze kufanya kazi zao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Local Government Reforms, Serikali Kuu imekasimu madaraka kwa Local Government na kati ya maeneo ambayo ilikuwa imekasimu ni property tax au kodi ya majengo, tumeona Awamu hii ya Tano imeanza tena kurudisha collection ya property tax kwa TRA. TRA walishashindwa siku nyingi na ndiyo maana ilihamishiwa Local Government.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kigezo gani ambacho Serikali imetumia kuhamisha tena property tax kutoka Serikali za Mitaa kuja TRA wakati walikwishashindwa na tunajua kwamba Serikali Kuu imekasimu madaraka kwa Local Government. Inawezekanaje umpe mtu madaraka, umpe na rasilimali watu, lakini ukamnyima rasilimali fedha ya kuifanyia kazi, wakati Local Government ndiyo ina mashule, Local Government ndiyo ina hospitali, Local Government ndiyo ina barabara, watafanyaje hizi kazi ikiwa resources Serikali Kuu imewanyang’anya? Hili ni janga la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mikubwa ambayo imezungumziwa. Makaa ya mawe - Liganga, Mchuchuma, reli ya kati, general tyre, hizi story za siku nyingi tangu nikiwa Katibu Mkuu, nimestaafu miaka mitano sasa bado hadithi ni ile ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Bado hadithi ni ile ile. Tunataka Mheshimiwa Mpango aje atueleze ni namna gani hili jambo litatekelezwa. Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia hoja ambayo ipo hapo mezani na na-declare kwamba mimi pia ni Mjumbe mmojawapo wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa. Naona Mheshimiwa Suzan Kiwanga hajaja mimi nitaendelea tu na dakika zangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo langu kubwa ambalo nalikazia ni eneo la Utawala Bora ambalo Kamati imezungumza na kuainisha maeneo mbalimbali ambayo hayazingatii utawala bora katika Awamu hii ya Tano. Tukiangalia katika ile taarifa ya Kamati tumeona jinsi watu wanavyoswekwa jela kwa kutokuhudhuria tu vikao, ambayo ni kinyume za kanuni na taratibu za uendeshaji Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hata kule Singida, Daktari ameswekwa rumande, kwa sababu kuna mgonjwa alikufa. Mimi sitetei uzembe lakini kuna factors nyingi ambazo zinaweza kufanya mgonjwa kufariki dunia. Kwa vile huyu Daktari amewekwa rumande, nasikia ame-resign na sioni ni jinsi gani huyu Daktari angerudi tena akaweza kufanya kazi vizuri katika ile hospitali. Hata wale watumishi wengine ambao wanafanya kazi na yule Daktari watapoteza morali kabisa ya kufanya kazi. Sidhani kama wale wagonjwa watapata tiba stahiki na huduma stahiki kwa jinsi ambavyo mwenzao ametupwa rumande. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hao ndio wanyonge tunaowazungumzia, maana yake hakuna Mbunge atakwenda kutibiwa huko Singida tunakozungumza. Kwa hiyo ni muhimu Serikali ikazingatia kanuni na taratibu za kuchukulia watumishi hatua za kinidhamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona jinsi gani Mtwara kule, Walimu Wakuu wameteremshwa vyeo kwa sababu tu ya matokeo ya form four. Hiyo siyo sahihi, kwa sababu tunamtafuta mchawi. Mchawi ni Serikali yenyewe, haijawekeza kwenye elimu. Kama Mwalimu ana wanafunzi 100 darasani, hana vitendea kazi, marupurupu yake hayajalipwa, utamtegemeaje huyu Mwalimu afanye kazi kwa ufanisi? Kwa hiyo Serikali, ijikite katika kuangalia factors ambazo zinateremsha elimu yetu na inafanya wanafunzi wetu wasiweze kufaulu vizuri madarasani. Hivyo kwa kweli hiyo haipendezi hata kidogo, Serikali isitafute mchawi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nikaangalia pia hii Mihimili miwili ya Bunge na Mahakama. Nakumbuka juzi Spika alisema kwamba Bunge tuko huru kabisa, sikubaliani kama sisi Bunge tuko huru! Juzi hapa tumenyimwa Bunge live na sisi ni Bunge, hakuna mtu amesimama kulisemea mbali ya Wapinzani, halafu tunasema Bunge tuko huru, tuna uhuru gani? Tukitaka kusafiri nje, mpaka tupate kibali Ikulu, tuna uhuru gani? Wakati iko namna ya kudhibiti matumizi ya Serikali, unaifanya katika bajeti tool. Inasema Bunge ninyi kwa mwaka huu mtapata milioni kadhaa kwa ajili ya safari zenu, lakini siyo tuombe ruhusa kwa Executive. Ina maana Bunge limekuwa compromised na hakuna mtu anayelisemea. Kwa hiyo, sisi hapa ni Bunge butu, hatuna meno na huu ndiyo ukweli na lazima tuukubali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia upande wa Mahakama, Mahakama tumenyimwa kufanya mikutano ya kisiasa na hiyo ni kinyume cha Katiba. Mahakama iko kimya, wala haijasema kitu. Jana Mheshimiwa Rais amesema kwamba wale Mawakili wanaowatetea watu ambao wamekosa wawekwe ndani, itakuwaje wawekwe ndani na juzi tumepitisha sheria ya Paralegals ya kutetea wanyonge. Sasa huyo Wakili unamweka ndani atamtetea nani?
watatetewa wale wenye pesa, kwa hiyo wale wanyonge watashindwa kutetewa. Hiyo haiendi sawa na lazima turudi katika misingi ya mihimili mitatu kila mmoja iwe inamwangalia mwenzake lakini kwa sasa hivi ilivyo Mahakama na Bunge tumekuwa compromised na huo ni ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja suala la decentralization kwa upande wa kimitaa. Ilipitishwa sera miaka kadhaa ya decentralization by devolution lakini kwa jinsi ambavyo Serikali inafanya sasa hivi, inapoka mamlaka ya Serikali za Mitaa. Tanzania ina kilomita za mraba karibu 945,000. Lazima Serikali za Mitaa iwe very strong na kwa mtindo huu, wamenyanganywa property tax na je, huu utawala bora tunaousema ni upi, wakati mkono wa Serikali wa Local Government unanyimwa pesa ambazo zingewasaidia kupeleka huduma kwa wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili haliko sawa na ili neno la good governance tunalizungumza tu lakini kwa kweli hatulizingatii. Nashukuru sana Suzan Kiwanga amerudi sijui kama bado ana dakika. Ahsante.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ilikuwa ni hili la TASAF. TASAF tumekwenda kutembelea maeneo mbalimbali na wanafanya vizuri. Mimi naungana na wengine wote waliozungumza, napendekeza kwamba TASAF iendelee na TASAF sasa iwekewe mfumo mzuri kuweza kuwatambua. Kwa sababu inaelekea siyo kila mara Serikali ikishindwa kitu inafikiri kwamba itafanya kitu tofauti badala ya kuangalia imeshindwa wapi na kurekebisha. Kwa hiyo Serikali iangalie kwa nini huu mfumo haufanyi kazi vizuri na ni jinsi gani watu hewa wanaingizwa kuchukua hizo pesa za TASAF ifanyie kazi na siyo kumtafuta mchawi mwingine tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu kunipa uhai na kuweza kuchangia hoja iliyoko mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro kati ya hifadhi na wananchi imekuwa sugu na ya muda mrefu. Nilipokuwa Mjumbe wa Bodi ya TANAPA ulitayarishwa mpango mkakati wa kutatua migogoro hiyo, watendaji wa TANAPA waliainisha maeneo yote yenye migogoro na wananchi, yaliwasilishwa kwenye Bodi ya Wadhamini na maamuzi yalifikiwa kama ifuatavyo:-

(a) Maeneo yenye migogoro na ambayo hayana madhara yoyote kwa hifadhi au ekolojia ya eneo la hifadhi waachiwe wananchi na mipaka irekebishwe.

(b) Maeneo yale yenye migogoro na uwepo wa human activities kuhatarisha bionuai na ekolojia ya hifadhi, wananchi washawishiwe kuachia maeneo hayo na Serikali iwape ardhi nyingine na kuwalipa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi haya hayakutekelezwa kwa sababu muda mfupi baadae aliyekuwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Pinda aliunda Tume ya kuchunguza migogoro yote ya ardhi na kutoa mapendekezo, baadae tena Waziri wa Ardhi naye aliunda Tume kwa jambo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kwa Serikali kushindwa kutoa uamuzi kwa jambo nyeti linalogusa hisia za jamii. Serikali ichukue maamuzi magumu ya kutatua kero hii badala ya kujificha nyuma ya Tume na Kamati zinazoundwa kila mara ili tu isifanye maamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro hii sasa na zaidi ya miaka kumi tangu nimeanza kuisikia, ni matumaini yangu kwamba kabla Awamu ya Tano haijamaliza muda wake wa miaka mitano itaacha alama ya kudumu ya kutatua kero hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nichukue pia nafasi hii kuwapa pole watu wa Arusha kwa ajili ya vifo vya Watoto wetu wa shule ya Lucky Vincent na Walimu pamoja na wafanyakazi Mungu awarehemu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya elimu ina changamoto nyingi sana na mengi yameshazungumzwa. Mimi nitajikita kwenye maeneo kama matatu tu.

Kwanza ni suala la lugha ya kufundishia. Kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala mkubwa sana kama tutumie kiswahili au tutumie kiingereza nafikiri baadae, kwa sababu tulishakubali kwamba kiswahili ndiyo lugha ya Taifa nafikiri huo ndiyo msimamo kwamba kiswahili ni lugha ya Taifa bila shaka na lugha ya kufundishia iwe kiswahili. Mpaka sasa hivi hatujachukua hatua. Tunakuwa na wanafunzi wanasoma kiswahili kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la saba, halafu unamtegemea mwanafunzi huyu aende form one akajifunze masomo kwa kiingereza! Kwa kweli huo ni mtihani mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa tumeamua kwamba kiswahili ndiyo tuwe nacho basi kazi ifanyike kubadilisha mitaala yote ya Sekondari mpaka Chuo Kikuu tujue tuna lugha moja kwa sababu ufanisi wa lugha inamjengea hata mtu confidence unakuwa na confidence kwamba unaweza ukaizungumza lugha yako vizuri na ukaeleweka na ndiyo maana kila mara tunasema Watanzania hatupati kazi Kenya ni kwa sababu ya confidence ya lugha. Tunafundisha watoto kiswahili na tunategemea wafanye mambo mengine kwa kiiingereza, kama tumeamua kiswahili basi tuende nacho moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya Serikali ya Awamu Tano ni Serikali ya Viwanda, nauliza hatujajua viwanda ni vipi kama ni textile, kama ni agri, kama ni nini sujui, lakini nilitegemea kwamba Wizara ya Elimu nayo itajipanga kuona kwamba sera ya viwanda ni hii na viwanda gani tunataka kuvianzisha basi Mheshimiwa Waziri aje atuambie katika kutekeleza hii sera ya viwanda ni skills zipi ambazo zinakuwa imparted kwa ajili ya baadae kutumika kama wataalam katika viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea na hiyo ya viwanda, labs (maabara) ni muhimu sana na shule nyingi hazina maabara, tutakuaje sasa na Serikali ya viwanda wakati maabara zetu haziko sawa sawa? Nchi za wengine wanakuwa hata na mobile maabara, mobile kits za lab ambazo zinahamishika kutoka mahali pengine kwenda mahali pengine. Pengine hilo ni jambo muhimu pia la kuweza kujifunza kusudi tuwe na mobile lab kits ambazo tunaweza tukatembea nazo katika shule zetu na watoto waweze kafundishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi na kwenye kiswahili, kiswahili ni fursa pia Wizara imejipangaje ku-train wakalimani kwa sababu tayari African Union kiswahili kimekubalika, East Africa kiswahili kimekubalika, Wizara imejipangaje kutayarisha wakalimani wa kiswahili kwa sababu ni ajira pia kwa ajili ya Watanzania, vinginevyo tutakuta wakalimani watakuwa ni Wakenya wamejaa kule sisi wenyewe, wenye kiswahili chetu tutabaki nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge lako Tukufu lililopita, lilipitisha bill hapa kwamba wanafunzi wote wanaochukua loans wakatwe asilimia 15, wengine wameshalizungumzia na mimi nakazia hapo pamoja na hotuba ya Upinzani kwamba pamoja na kwamba hili Bunge lilipitisha 15 percent, lakini haikuwa inatarajiwa kwamba ingerudi nyuma kuhusisha wale wanafunzi wengine wote ambao walikuwa wamesaini mkataba wa asilimia nane.

Kwa hiyo, ni maoni ya Kambi kwamba siyo sahihi kwa sababu unakuwa ume-change position in the mid of the stream. Mimi nimesaini nitatoa eight percent, tumepitisha bill hapa 15 percent, hiyo isingemu-affect mtu ambae ameshasaini mkataba wa eight percent, ingehusisha wale ambao ni wapya... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mungu kunipa afya na nguvu kuwatumikia wananchi Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania imejaliwa kuwa na maji mengi sana kutoka vyanzo mbalimbali kama maji juu ya ardhi, maji chini ya ardhi na maji ya mvua yanayosababisha mafuriko mara kwa mara. Hata hivyo, kila mara Tanzania imekuwa inakabiliwa na uhaba wa maji safi na salama katika maeneo mengi mjini na vijijini. Uhaba wa mvua unaosababisha ukame na kusababisha njaa na adha kubwa ya kiuchumi. Mfano, wanyama kufa na kukosekana kwa mazao, vilevile nchi imekuwa mhanga mkubwa wa mvua kubwa inayosababisha maafa ya mafuriko, uharibifu wa mazao na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka 53 ya uhuru pamoja na wataalam waliobobea katika taaluma ya maji na mipango, Serikali imeshindwaje ku-manage suala la maji ili kupunguza kero na umaskini?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini Serikali haisimamii kwa Sheria ya Uvunaji wa Maji ya Mvua na Sheria ya Ujenzi irekebishwe kujumuisha miundombinu ya kuvuna maji kwenye majengo mbalimbali. Kwa nini mabwawa makubwa ya kukinga na kutunza maji kwenye maeneo ambayo kila mara kuna mafuriko na ya katumika kwa ajili ya kilimo, mazao na mboga mboga za muda mfupi ili kuinua uchumi wa wananchi na kupunguza umaskini?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini maeneo yenye maji chini ya ardhi wananchi wasichimbiwe visima ili kuwanusuru na kero ya maji? Katika hotuba, maeneo yenye maji chini ya ardhi yameainishwa, lakini hakuna popote fedha imetengwa kwa ajili ya kuchimba visima vichache kwa vipaumbele?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni rai yangu kwamba Wizara ijipange kukusanya/kuvuna maji mengi yanayopotea na kwenda baharini. Nchi ya Israel ni mahali pazuri pa kujifunza, maji ni almasi, hakuna tone linalopotea. Hapa kwetu tuna maji mengi lakini tunafanya mzaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia hoja iliyopo hapa mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyozungumza Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba kila mwananchi na kila mtu ana haki ya kupata taarifa. Hii ni haki ya msingi ambayo tumepewa na Mwenyezi Mungu na Serikali pia inatupa hiyo nafasi ya kupata taarifa wakati wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hii sheria ambayo ipo mezani na nina mawazo ambayo napenda kuleta mbele ya meza yako. Kwanza, namshukuru mwenzangu wa Kambi ya Upinzani kwa hotuba nzuri sana ambayo ameitoa na ninamuunga mkono kwa ile article 6 ambayo imeainisha information ambayo inakuwa exempt. Sasa najiuliza, kama hii information yote ni exempt, hiyo haki ya sisi kupata taarifa iko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukingalia hapo kipengele (e) ambayo inakataza private individual information, mimi nasema kwamba private information iko ndani ya kuta zako nne nyumbani, lakini inapokuja kwenye public, we have no private life in public. Kwa sababu kama kiongozi au kama mtu mwingine yeyote, unapotoka nje, wewe ni barua, ni mtu unayesomwa na jumuiya au na wananchi au na watu wa Jimbo lako. Kwa hiyo, hakuna private life kwenye public. Private life tunazo nyumbani kwetu wenyewe. Kwa hiyo, sioni kama hiki kifungu kinahitajika kuwepo hapa kwa sababu kinachochea kukosekana kwa maadili kati yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikaangalia pia pale ambapo kuna informations ambazo hazitolewi mpaka baada ya miaka 30. Utakubaliana na mimi kwamba hata duniani kote, information zinakuwa categorized. Kuna information ambao unapata immediately, kuna information unaweza ukapata baada ya mwezi, kuna information miaka mitano, kuna information miaka 15 na kuna information miaka 30. Kwa hiyo, kama ni hivyo basi, tuainishe tujue information zipi zinapatikana immediately na information zipi ambazo haziwezi kupatikana mpaka baada ya miaka 30. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja pia kwenye suala la National Security. Nakubaliana kwamba National Security ni jambo muhimu, lakini kwa kweli ingependeza kama hii National Security tunge-interpret maana yake sijaiona. Nimeangalia kwenye interpretation haipo kwa sababu tunataka tujue kusudi isiwe ni kichaka cha kuzuia information zisitafutwe na kuibuliwa. Tukubaliane kwamba information inapoibuliwa ndiyo inaleta maendeleo, ndiyo inaongeza speed ya maendeleo katika Taifa lolote kwa sababu kama hakuna information na inatokea, watu wanashindwa kuibua hata ideas, wanashindwa kuibua vitu vya maendeleo. Kwa hiyo, National Security naomba ifanyiwe interpretation tujue what we mean by national security.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna issue nyingine ambazo tunajua ni security, kwa mfano, mambo ya vita, mambo ya intelligence ni national security. Kwa sababu tumeona hata juzi unaambiwa uchochezi ni national security. Uchochezi wenyewe hata haueleweki ni uchochezi gani. Kwa hiyo, tui-define hiyo national security. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye access of information, nimeangalia kwenye sheria inasema siku 30; siku 30 ni nyingi sana. Wakati mwingine unahitaji information immediately kwa sababu unaitumia; kwa sababu information delayed is no longer information na haifai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, siku 30 ni nyingi sana, tunaomba itazamwe upya. Maana yake nikiangalia siku hizi tuna ICT, tuna IT unless kama bado tunaendelea na utaratibu wa kizamani ule wa kuweka ma-record na kuyafunga kwenye box. Siku hizi tuna mambo ya ICT, kwa hiyo, hakuna sababu yoyote ya mtu anataka information aipate mpaka baada ya siku 30; maana naona nyingine ukitaka tena zaidi siku 14. Tunataka information immeadiately, kama mtu anaitaka information aipate aweze kuitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taifa letu hili tunahitaji sheria ambayo ina-facilitate watu kutafuta taarifa na kuzifanyia kazi na kuleta maendeleo chanya katika Taifa letu. Kama tutaendelea na utaratibu wa kuzibwa midomo na kuzuiliwa kuzungumza, hatuwezi kufika popote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo mchango wangu kwa ufupi sana. Ahsante.

Whoops, looks like something went wrong.

1/1 ErrorException in Filesystem.php line 75: file_put_contents(): Only 0 of 292 bytes written, possibly out of free disk space

  1. in Filesystem.php line 75
  2. at HandleExceptions->handleError('2', 'file_put_contents(): Only 0 of 292 bytes written, possibly out of free disk space', '/data/gov_websites/clients/client2/web9/private/polis/vendor/laravel/framework/src/Illuminate/Filesystem/Filesystem.php', '75', array('path' => '/data/gov_websites/clients/client2/web9/private/polis/storage/framework/sessions/652ab5afb23abb9b3e2b1b9fec13ef15b8f4b34a', 'contents' => 'a:4:{s:6:"_token";s:40:"LcYWNaTa2hFfLgY3x6rkroprRt0Gm8CTddddgdVn";s:9:"_previous";a:1:{s:3:"url";s:55:"http://parliament.go.tz/polis/members/385/contributions";}s:9:"_sf2_meta";a:3:{s:1:"u";i:1516304729;s:1:"c";i:1516304729;s:1:"l";s:1:"0";}s:5:"flash";a:2:{s:3:"old";a:0:{}s:3:"new";a:0:{}}}', 'lock' => true))
  3. at file_put_contents('/data/gov_websites/clients/client2/web9/private/polis/storage/framework/sessions/652ab5afb23abb9b3e2b1b9fec13ef15b8f4b34a', 'a:4:{s:6:"_token";s:40:"LcYWNaTa2hFfLgY3x6rkroprRt0Gm8CTddddgdVn";s:9:"_previous";a:1:{s:3:"url";s:55:"http://parliament.go.tz/polis/members/385/contributions";}s:9:"_sf2_meta";a:3:{s:1:"u";i:1516304729;s:1:"c";i:1516304729;s:1:"l";s:1:"0";}s:5:"flash";a:2:{s:3:"old";a:0:{}s:3:"new";a:0:{}}}', '2') in Filesystem.php line 75
  4. at Filesystem->put('/data/gov_websites/clients/client2/web9/private/polis/storage/framework/sessions/652ab5afb23abb9b3e2b1b9fec13ef15b8f4b34a', 'a:4:{s:6:"_token";s:40:"LcYWNaTa2hFfLgY3x6rkroprRt0Gm8CTddddgdVn";s:9:"_previous";a:1:{s:3:"url";s:55:"http://parliament.go.tz/polis/members/385/contributions";}s:9:"_sf2_meta";a:3:{s:1:"u";i:1516304729;s:1:"c";i:1516304729;s:1:"l";s:1:"0";}s:5:"flash";a:2:{s:3:"old";a:0:{}s:3:"new";a:0:{}}}', true) in FileSessionHandler.php line 70
  5. at FileSessionHandler->write('652ab5afb23abb9b3e2b1b9fec13ef15b8f4b34a', 'a:4:{s:6:"_token";s:40:"LcYWNaTa2hFfLgY3x6rkroprRt0Gm8CTddddgdVn";s:9:"_previous";a:1:{s:3:"url";s:55:"http://parliament.go.tz/polis/members/385/contributions";}s:9:"_sf2_meta";a:3:{s:1:"u";i:1516304729;s:1:"c";i:1516304729;s:1:"l";s:1:"0";}s:5:"flash";a:2:{s:3:"old";a:0:{}s:3:"new";a:0:{}}}') in Store.php line 255
  6. at Store->save() in StartSession.php line 89
  7. at StartSession->terminate(object(Request), object(Response)) in Kernel.php line 135
  8. at Kernel->terminate(object(Request), object(Response)) in index.php line 63