Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon Faida Mohammed Bakar (13 total)

MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Je, ni lini Benki ya Wanawake itaanza kutoa huduma zake Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Faida kwa kufuatilia na kuuliza swali hili kwa mara ya tatu sasa. Hii inaonesha dhamira ya dhati aliyonayo kwa wanawake na wananchi wa Zanzibar. Mheshimiwa Faida aliuliza swali hili mara mbili katika Bunge la Kumi na aliendelea kuuliza swali hilo kwenye vikao mbalimbali vya iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii katika kipindi kilichopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya Wanawake ilianzishwa kwa mtaji wa shilingi bilioni 2.8 ambao ni kiasi kidogo sana. Ili Benki iweze kutimiza kigezo cha kuwa Benki ya Biashara kamili na kuweza kupata kibali cha Benki Kuu cha kufungua Matawi nchi nzima, inahitaji mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni 15. Hivi sasa benki hiyo ina mtaji wa shilingi bilioni 8.5.
Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi za kuanzisha shughuli za kibenki Zanzibar zilianza tangu mwaka 2013, kwa Menejimenti kutembelea Zanzibar katika lengo lake la kupata jengo zuri kwa shughuli za kibenki. Hata hivyo, juhudi hizi hazikuzaa matunda na ndipo Makamu wa Rais wa sasa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, aliporidhia kutoa Ofisi yake ndogo iliyokuwa katika Hoteli ya Bwawani ili kuanzisha huduma hiyo na kuwanufaisha wananchi wa Zanzibar, hususan wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa, benki ipo katika hatua za mwisho za kupata kibali cha Benki Kuu ili kuanzisha rasmi Kituo cha Mafunzo na Mikopo kwa Wajasiriamali wa Zanzibar na tunategemea kitaanza shughuli zake kabla ya mwezi Juni mwaka huu yaani mwaka 2016 na kama nilivyoeleza awali mtaji wa benki hii ukiimarika benki itafungua tawi kamili Zanzibar.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR aliuliza:-
Kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa huduma za afya na haki za uzazi katika baadhi ya sehemu jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha ya wanawake:-
Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali namba 54 la Mheshimiwa Faida Mohammed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nasikitika kuwa bado kuna ukiukwaji wa huduma za afya, haki za afya na haki za uzazi katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Tafiti zinaonyesha kuwa suala hili linadumaza matumizi ya huduma na kuhatarisha maisha ya wanawake. Serikali inajukumu la kutoa na kusimamia na kutoa utoaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto na jukumu hili linatekelezwa kwa kutumia vituo vya kutolea huduma za afya ya uzazi na mtoto vya umma na binafsi kote nchini. Huduma hizi hutolewa kwa kuzingatia haki za wateja kama ilivyoainishwa kwenye miongozo ya utoaji wa huduma hizi. Haki hizi ni pamoja na upatikanaji wa taarifa sahihi, ubora na usalama wa huduma, usiri na ufaragha katika utoaji wa huduma, haki ya kusikilizwa, haki ya kuheshimiwa na haki ya kutumia huduma kwa hiari pasipo shuruti.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa haki hizi zinapatikana, Serikali kwa kupitia mifumo yake ikiwa ni pamoja na Mabaraza ya weledi kwa maana ya Mabaraza ya Wauguzi, Madaktari, Wafamasia, Wataalam wa Radiolojia na kadhalika, Kurugenzi ya Uhakiki na Ubora wa Huduma za Afya na idara mbalimbali zilizo chini ya Wizara zinatoa mafunzo kwa watoa huduma za afya kuhusiana na haki za wateja na mahitaji muhimu ya mtoa huduma ili waweze kutekeleza haki hizo. Aidha, wateja wanaotumia huduma mbalimbali za afya uzazi na mtoto hupewa elimu kuhusu haki zao ili kuzifahamu na kuchukua hatua pindi wanapoona haki zao zinakiukwa.
Katika kutekeleza hili, vituo vyetu vya kutolea huduma za afya vina masanduku ya maoni na ofisi za malalamiko ambazo ni sehemu muhimu ambapo wateja wanaweza kupeleka malalamiko yao ili hatua zaidi zichukuliwe kukomesha na kutokomeza ukiukwaji wowote wa haki za mteja.
Mheshimiwa Spika, Serikali hufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa kushtukiza katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma na binafsi kwa lengo la kutambua malalamiko yaliyofumbiwa macho na kujiridhisha na ubora wa huduma zinazotolewa. Ukaguzi huu wa kushtukiza hufanywa na Kiongozi yeyote wa Serikali mwenye dhamana ya kusimamia huduma za jamii. Ukaguzi huu wa kushtukiza huleta matunda katika uboreshaji wa huduma na haki kwa wateja. Kwa mikakati hii, nina imani kuwa tatizo hili litapungua kama siyo kumalizika kabisa.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha na kumiliki Bureau de Change zake yenyewe badala ya kuacha huduma hiyo kuendelea kutolewa na watu au taasisi binafsi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Mbuge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haina mkakati wa kufungua au kuanzisha Bureau de Change zake kwa sababu imejitoa kuhusika moja kwa moja na biashara ya fedha kama vile benki na Bureau de Change kutokana na mabadiliko ya mfumo katika sekta ya fedha nchini unaotekelezwa kuanzia mwaka 1991. Sekta binafsi imeachiwa jukumu la kuanzisha na kuendesha biashara ya fedha nchini chini ya usimamizi wa Benki Kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imebaki na jukumu la kuweka mazingira mazuri na salama ya uwekezaji katika sekta zote, ikiwemo sekta ya fedha ili kuiwezesha sekta binafsi kuanzisha, kuendesha na kutoa huduma bora za kifedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka sheria na taratibu za kusaidia nguvu na juhudi za wananchi katika kuanzisha benki au taasisi za fedha katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni.
Kwa hiyo, Serikali inategemea kuwa wananchi watatumia fursa hii ya mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo nchini na kuanzisha huduma za kubadilisha fedha za kigeni katika maeneo yenye uhitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kusimamia kwa ukaribu zaidi maduka ya kubadilisha fedha za kigeni nchini ili yaweze kutoa huduma bora na inayokidhi matakwa ya sheria na kanuni za biashara ya fedha. Hivi karibuni Benki Kuu imetoa kanuni mpya kwa lengo la kuimarisha usimamiaji wa maduka hayo. Maduka yote ya kubadilisha fedha za kigeni yanatakiwa kufunga mashine za EFDs ili kuiwezesha TRA na BoT kupata taarifa za moja kwa moja juu ya miamala inayofanywa kwenye maduka hayo.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha Benki ya Wafanyabiashara Wakubwa na Wadogo ili kuwawezesha wafanyabiashara hao (wajasiriamali) kupata huduma iliyo bora kupitia benki yao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu na Mchango wa wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali haina mpango wa kufungua benki mpya za wafanyabiashara wakubwa na wadogo, isipokuwa inafanya jitihada za kuimarisha benki zake zilizopo ikiwemo Benki ya Kilimo na Benki ya Wajasiriamali.
Mheshimiwa Spika, ni vema tukaimarisha benki za Serikali zilizopo kwa sasa kuliko kuanzisha benki zingine. Tukianzisha benki mpya tutaipunguzia Serikali uwezo wa kifedha wa kuziimarisha benki zilizopo. Mfano, Benki ya Posta ni benki ya Serikali na imeenea nchi nzima kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wetu, hususani wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati. Kama Serikali, tutaimarisha benki hizi zilizopo na pia kuipa sekta binafsi fursa ya kuanzisha benki zaidi kwa kadri soko litakavyoruhusu, ni imani yetu kubwa kwamba wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo watapata huduma husika.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Askari wa Wilaya ya Mkoani katika Mkoa wa Kusini Pemba wanakabiliwa na tatizo la uchache wa nyumba za kuishi na ubovu wa ofisi zao:-
Je, ni lini Serikali itawajengea Askari nyumba za kuishi na ofisi za kisasa katika kituo cha Mkoani na Kengeja – Pemba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali inatambua tatizo la uchache wa nyumba za kuishi askari na ubovu wa ofisi zao; kwa sasa Jeshi la Polisi lina mpango wa kujenga nyumba za polisi nchi nzima ambapo kwa awamu ya kwanza zitajengwa nyumba 4,136 katika mikoa 17 ikihusisha Mikoa ya Tanzania Bara pamoja Mikoa ya Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuboresha makazi ya askari na ofisi za polisi kwa awamu kwa kadri hali ya kiuchumi itakavyoruhusu.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Matumizi ya dola katika maeneo mengi nchini ndiyo sababu kubwa ya kushuka kwa thamani ya fedha yetu:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhamasisha matumizi ya fedha yetu kwa wananchi wake pamoja na wageni nchini ili kukuza thamani ya fedha yetu na maendeleo ya nchi kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakari, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sarafu ya shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali kwa malipo hapa nchini na hakuna sarafu nyingine yoyote iliyowahi kuidhinishwa kisheria kutumika kwa malipo hapa nchini badala ya shilingi. Hakuna sababu ya kuhamasisha matumizi ya shilingi kwa sababu Watanzania wote wanajua fedha halali kwa malipo ni shilingi na si vinginevyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti uliofanyika mwaka 2013 ulionesha kuwa, malipo ambayo hufanyika kwa dola ya Marekani hapa Tanzania ni asilimia 0.1 tu ya malipo yote na haya hufanyika zaidi katika maeneo yanayohusisha wageni kama vile mahoteli ya kitalii, mashirika ya ndege, shule za kimataifa na nyumba za kupanga kwenye baadhi ya maeneo mijini. Sababu mojawapo ya maeneo haya kuwa na bei kwa dola ya Kimarekani ni kurahisisha uelewa wa bei hizo kwa wageni na kuwarahisishia malipo. Pamoja na mambo mengine malipo kwa fedha za kigeni yanachangia upatikanaji wa fedha za kigeni hususani pale wazawa wanapouza bidhaa na huduma kwa wageni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya dola nchini Tanzania siyo sababu kuu ya kushuka kwa thamani ya shilingi yetu. Mfano, wakati Tanzania haijafanya mabadiliko yoyote katika kanuni ya fedha za kigeni tangu mwaka 1992 thamani ya shilingi ilikuwa ikishuka na kupanda kama zilivyo thamani za sarafu nyingine duniani. Aidha, kutokea mwezi Desemba, 2011 hadi Desemba, 2014 thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani ilikuwa imara zaidi ya sarafu nyingine za washirika wetu kibiashara kama vile Rand ya Afrika ya Kusini, Yen ya Japan, Euro ya Jumuiya ya Ulaya na Paundi ya Uingereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu kuu zinazopelekea kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya fedha za kigeni ni tofauti ya mfumuko wa bei kati ya Tanzania na nchi tunazofanya nazo biashara. Nakisi ya biashara ya nje ya bidhaa na huduma ambayo imekuwepo kwa muda mrefu na mabadiliko ya mara kwa mara ya kiuchumi duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kanuni zilizotokana na sheria ya Fedha za Kigeni ya mwaka 1992 na tamko la Serikali kuhusu matumizi ya fedha za kigeni la mwaka 2007, sarafu ya shilingi ya Tanzania ndiyo fedha halali kwa malipo. Aidha, Benki Kuu ikishirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania imeongeza usimamizi katika maduka ya fedha za kigeni ambapo miamala yote ya fedha za kigeni inatakiwa kuoneshwa. Pia, Benki Kuu imechukua hatua za kuhakikisha kuwa miamala ya fedha za kigeni inayofanywa na mabenki ni kwa ajili ya shughuli za kiuchumi, kidiplomasia na kijamii pekee.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha SUZA wa Sayansi ya Afya na Mazingira (Bachelor of Science in Environmental Health) ambao wanafanya internship ya mwaka mmoja Tanzania Bara sambamba na wale wanaomaliza Vyuo vya Tanzania Bara, hawalipwi posho yoyote ya internship wakati wenzao wanaomaliza Tanzania Bara wanalipwa posho hizo:-
Je, ni kwa nini wanafunzi hao hawalipwi posho hizo kama ambavyo wenzao wa Tanzania Bara wanalipwa ili kuwaondolea maisha magumu waliyonayo wakati wa internship ambayo yanaweza kusababisha kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Baraza la Kusajili Wataalam wa Afya ya Mazingira, huratibu zoezi la internship na hutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Sheria ya Kusajili Wataalam wa Afya ya Mazingira ya mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika, Sheria hii, inawataka wataalam wa Afya ya Mazingira wote wanaomaliza Shahada ya Afya ya Mazingira Tanzania Bara, washiriki mafunzo ya kazi kwa vitendo (internship) kwa kipindi cha miezi 12 kabla ya kuajiriwa. Hivyo basi, Serikali hulazimika kuwalipa posho ya kujikimu wakati wa mafunzo kwa vitendo ili kukidhi matakwa ya sheria hii.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itashauriana na Wizara ya Afya Zanzibar ili nao waangalie uwezekano wa kuwalipa wahitimu kutoka Chuo Cha SUZA, waweze kutekeleza vyema mafunzo ya kazi kwa vitendo (internship) kwa kipindi cha miezi 12 kabla hawajasajiliwa ili kuwaondolea maisha magumu waliyonayo wakati wa mafunzo haya, ambayo yanaweza kusababisha kushindwa kutekeleza wajibu yao kwa ufanisi.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR aliuliza:-
Majukumu ya Mbunge kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 63(3) yameainisha kwa ujumla wake bila kubagua aina ya Ubunge; lakini Sheria Namba 16 ya mwaka 2009 iliyounda Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF) imeonesha ubaguzi mkubwa kwa kumtambua Mbunge wa Jimbo pekee ambaye ndiye aliyetajwa na sheria hiyo kama Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Mfuko huo na kuwatenga Wabunge wa Viti Maalum licha ya kwamba Wabunge wote wanatekeleza majukumu sawa ya kuwatumikia wananchi.
Je, ni lini Serikali itarekebisha sheria hii ili ijumuishe Wabunge wote ikiwemo Wabunge wa Viti Maalum?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohammed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo ulianzishwa mwaka 2009 kwa Sheria Namba 16 ya mwaka 2009 iliyotungwa na Bunge. Fedha za Mfuko wa Jimbo hutolewa katika Majimbo yote ya uchaguzi Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kwa kuzingatia vigezo maalum vilivyopitishwa kisheria. Vigezo vinavyotumika kugawa fedha za Mfuko wa Jimbo ni idadi ya watu asilimia 45, mgao sawa (pro-rata) kila Jimbo asilimia 25, kiwango cha umaskini asilimia 20 na ukubwa wa eneo asilimia 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za Mfuko wa Jimbo huingizwa moja kwa moja katika account ya Halmashauri na zinasimamiwa kwa taratibu za Sheria ya Fedha isipokuwa Mbunge wa Jimbo ni Mwenyekiti wa Mfuko huo. Kimsingi sheria haina ubaguzi kwa Waheshimiwa Wabunge wa Viti Maalum kwa sababu fedha hizo za Serikali zinatumika kutekeleza miradi ya kipaumbele iliyoibuliwa na wananchi wenyewe kwenye Jimbo husika kwa kuzingatia mahitaji ya Jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na malengo yaliyounda Sheria ya Mfuko wa Jimbo na vigezo vinavyotumika katika kupeleka fedha za Mfuko wa Jimbo, Serikali inaona sheria hiyo inajitosheleza kwa sasa kwa kuzingatia misingi ya uundwaji wake, labda Bunge ambalo ndilo lenye mamlaka ya kutunga sheria litakavyoamua vinginevyo.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatenga bajeti kwa ajili ya kuwajengea nyumba askari polisi wa Pemba ili kuwaondolea adha ya makazi askari hao?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI aliuliza:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohammed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa nyumba za kuishi askari Pemba hazitoshi kama ilivyo katika maeneo mengine nchini na hivyo kusababisha adha kwa askari wetu. Serikali itatenga bajeti katika mwaka ujao wa fedha ili kujenga nyumba za askari wa Zanzibar husasan Pemba ambako Mheshimiwa Mbunge ameuliza ili kuwaondolea adha wanazozipata kutokana na kutokuwa na nyumba za kutosha. (Makofi)
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Sheria nyingi nchini hususan zile zinazohusu haki na stahili za wanawake zimepitwa na wakati na hivyo kuwanyima haki wanazostahili makundi hayo.
Je, ni sheria zipi zinazowanyima haki wanawake na watoto nchini?
Je, ni lini Serikali italeta miswada ili kuboresha au kubadilisha sheria hizo ili ziendane na wakati na kuwapatia haki zao wanawake na watoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohammed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
– Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria za Mirathi za Kimila (Customary Declaration Orders, GN. No. 279 na 436 za mwaka 1963 zimekuwa zikiwanyima haki za urithi na umiliki wa ardhi wanawake na watoto.
Vilevile Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 katika Kifungu cha 13 na 17 vinaruhusu mtoto wa kike kuolewa katika umri mdogo wa miaka 14 au 15 kwa ridhaa ya wazazi au uamuzi wa mahakama. Vifungu hivi humnyima mtoto haki zake za msingi.
– Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya maboresho ya Sheria ya Ndoa na Sheria ya Mirathi tayari yamewasilishwa Wizara ya Sheria na Katiba pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi. Taratibu zote zitakapokamilika muswada utawasilishwa Bungeni.
Aidha, katika jitihada za kukomesha ndoa za utotoni, mwaka 2016 Serikali ilifanyia marekebisho Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 ili kuzuia watoto wa shule wasiolewe. Kwa mujibu wa Sheria hii Na. 4 ya mwaka 2016 Kifungu cha 60A hairuhusiwi mtu yeyote kuoa au kumpa ujauzito mwanafunzi wa Shule ya Msingi au Sekondari. Kwa kuwa sheria hii inalenga zaidi ulinzi kwa watoto walio mashuleni, bado ipo haja ya kuviondoa kabisa vifungu vinavyoruhusu ndoa za utotoni kwenye Sheria ya Ndoa kama ilivyofanyika kwa nchi nyingine kama vile Bangladesh, Yemen, Kenya na Malawi ili kuondoa mkanganyiko wowote unaoweza kujitokeza.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR aliuliza:-
Je, ni lini Benki ya Wanawake Tanzania itaanzisha tawi lake Zanzibar kwa madhumuni ya kuwapatia huduma za kibenki na mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kuwainua kiuchumi wajasiriamali wanawake wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Wanawake Tanzania ilianzishwa mwaka 2009 kwa lengo la kuwawezesha wanawake kupata huduma za kibenki, ikiwemo mikopo yenye masharti nafuu ili kujikwamua kiuchumi. Mpaka sasa, Benki imefungua matawi mawili yaliyopo jiji Da es Salaam na vituo vya kutolea mikopo na mafunzo 305 katika Mikoa Saba ya Dar es Salaam, Mbeya, Njombe, Iringa, Mwanza, Ruvuma na Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa benki ni kuhakikisha kwamba huduma zake zinawafikia wanawake waliopo katika mikoa yote ya Tanzania ikiwemo Zanzibar. Hata hivyo, utekelezaji wa mpango huo unakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa mtaji wa benki hivyo, benki imekuwa ikipanua huduma zake katika mikoa mbalimbali ya Tanzania kwa awamu kwa kufungua vituo vya kutolea mikopo na mafunzo kwa wajasiriamali. Aidha, hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha benki zinajiendesha kwa ufanisi na kukuza mtaji ikiwemo kufanya mabadiliko katika Benki kwa kuweka uongozi na watumishi waadilifu wenye uwezo pamoja kutafuta fedha kwa ajili ya mitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Benki ya Wanawake Tanzania itaendelea kufungua vituo vya kutolea mikopo na mafunzo katika Mikoa yote ya Tanzania, ikiwemo Zanzibar kulingana na upatikanaji wa mitaji.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-
Kumekuwa na upungufu mkubwa wa maji safi na salama kutokana na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu nchini na mpaka sasa nchi yetu bado inategemea maji kutoka vyanzo vichache kama mabwawa, mito, maji ya mvua na kadhalika.
Je, Serikali ina mkakati gani maalum wa kubadilisha matumizi ya maji ya bahari kwa ajili ya matumizi ya kawaida ili kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la upatikanaji wa maji nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nchi yetu kwa sasa kulingana na takwimu zilizopo ina maji juu ya ardhi na chini ya ardhi yanayofaa kwa matumizi mbalimbali kiasi cha kilomita za ujazo elfu 96.27, ambapo kila mwananchi ana uwezo wa kupata maji wastani wa mita za ujazo 1,800 kila mwaka hadi mwaka 2035 iwapo hatua madhubuti zitachukuliwa za kusimamia rasilimali za maji. Kiwango hicho cha maji kwa kila mtu kwa mwaka ni kikubwa ukilinganisha na kiwango cha chini cha mahitaji ya maji kwa kila mtu kinachokubalika kimataifa cha mita za ujazo 1,700 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kukabiliana na changamoto ya kupungua kwa rasilimali za maji ikiwa ni pamoja na uhamasishaji wa uvunaji maji ya mvua ili nchi yetu isifike kiwango kikubwa cha uhaba wa maji na kusababisha athari kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa maji yaliyopo yanatosha, na gharama za uwekezaji katika maji ya bahari kwa matumizi ya kawaida ni kubwa Serikali itaendelea kutumia vyanzo vingine vilivyopo, na endapo itabainika vyanzo hivyo vimepungua maji Serikali itajielekeza kuwekeza katika maji ya bahari kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKARI aliuliza:-
Kiswahili ndiyo lugha ya Taifa letu na kinapaswa kutumika katika nyanja zote ili kukipa hadhi yake:-
Je, kwa nini baadhi ya Mahakama nchini zinatumia lugha ya Kiingereza wakati zinapoendesha mijadala yake na katika kutoa hukumu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Faida Bakari, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya lugha katika Mahakama zetu yamewekwa kwa mujibu wa sheria. Kwa mujibu wa kifungu cha 13(1) na (2) cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu, Sura ya 11 (The Magistrates Courts Act, Cap 11) lugha inayotumika kuendesha kesi katika mahakama za mwanzo ni Kiswahili. Vile vile lugha itakayotumika katika mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya ni Kiswahili au Kiingereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, shauri linaweza kuendeshwa kwa lugha yoyote kwa maelekezo ya Hakimu anayeendesha kesi katika Mahakama hizo, japokuwa kumbukumbu za shauri na maamuzi zinapaswa kuandikwa katika lugha ya kiingereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika kwa mujibu wa Kanuni ya Pili ya Kanuni za Lugha za Mahakama na Kanuni ya Tano ya Kanuni za Mahakama ya Rufani ya Mwaka 2009, lugha itakayotumika kuendesha mashauri katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani ni Kiswahli au Kiingereza kutegemea na maelekezo ya Jaji au Mwenyekiti wa Jopo la Majaji japokuwa kumbukumbu na maamuzi ya shauri vinapaswa kuandikwa katika lugha ya Kiingereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuendelea kutumika kwa Kiswahili katika Mahakama zetu na hukumu kuandikwa kwa Kiingereza kunatokana na kwamba Tanzania ni Mwanachama wa Jumuiya ya Madola na inafuata mfumo wa Common Law. Kwa kuandika hukumu kwa lugha ya Kiingereza imewezesha Mahakama za nchi nyingine za Jumuiya ya Madola kutumia hukumu zetu kama rejea na vivyo hivyo Tanzania kutumia hukumu za nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa mashauri katika Mahakama zetu unaruhusu kutumia lugha zote mbili, Kiswahili au Kiingereza na Mahakama zetu zimekuwa zikizingatia hilo.