Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon Faida Mohammed Bakar (31 total)

MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri Kigwangalla, kwa niaba ya wananchi na wanawake wa Zanzibar, tunapenda kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia kufungua Benki ya Wanawake, Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kumshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kukubali kutoa ofisi yake. Ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa baadhi ya Wabunge wanawake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tulikuwa ni miongoni mwa waanzilishi wa benki hii kwa kutoa hela zetu kuweka hisa, lakini mpaka hii leo hatujui chochote kinachoendelea na hatujapatiwa gawio la hisa kutokana na Benki hii ya Wanawake.
Je, Serikali itaanza lini au inasema nini kuhusu gawio letu la hisa la wananchi wote, sio lazima Wabunge tu na wananchi wote? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kabla sijajibu swali lake, nitumie nafasi hii kwa namna ya kipekee kumpongeza sana aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mheshimiwa Sophia Mnyambi Simba, kwa chachu ya kuanzisha benki hii. Pia nimpongeze aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo ambaye sasa ni bosi wangu, Mheshimiwa Ummy Ally Mwalimu, kwa kutia chachu ya kukua kwa kasi ya benki hii. Zaidi nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kujitolea kufanya uamuzi makini wa kuchangia mtaji kwenye benki hii wa shilingi bilioni mbili kila mwaka. Naamini Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ataendelea kuipa uwezo benki hii kwa kuendelea kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze Wabunge wote wa Viti Maalum ambao nao kwa dhati kabisa waliamua kujitolea michango kwa kununua hisa kwenye benki hii. Kilichokwamisha wao kupata hisa hizi rasmi kwa maana ya utaratibu wa kisheria ni kwamba wakati benki inaanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni ya mwaka 2002, Cap. 212, ilikuwa imesajiliwa kama Private Limited Company. Kwa maana hiyo ilikuwa na benki binafsi ya wanahisa binafsi ambao walikuwa wameteuliwa kuianzisha benki hiyo na Mheshimiwa Rais wa wakati huo na kwa maana hiyo Wabunge walipochangia michango ile kwa maana ya kununua hisa kwa ajili ya kujiunga kwenye benki hii haikuweza kurasimishwa kwa haraka kwa sababu ya utaratibu wa kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumbukumbu za Wabunge wote walionunua hisa pale awali wakati benki inaanzishwa zipo. Machi, 2012 baada ya kutambua michango hii ya Waheshimiwa Wabunge wote wa Viti Maalumu bila kujali itikadi zao, ilionekana kwamba usajili wa benki kwa mujibu wa sheria ubadilike, badala ya kuwa private sasa iwe public kwa maana ya kuwa Public Limited Campany ambapo kwa mujibu wa sheria sasa inaruhusiwa kuongeza wanahisa wengi zaidi. Lakini benki imeenda mbele, sasa hivi itakuwa benki ya wananchi wote kwa maana ya kwamba tuna mkakati wa ku-issue IPO, kufanya Initial Public Offering kwenye Soko la Hisa ili wananchi wengi zaidi wanunue hisa na iweze kuwa na mtaji mkubwa na kufika kwa wananchi wengi zaidi. Kwa maana hiyo, wale Wabunge walionunua hisa wakati huo, watapewa hati rasmi za hisa zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kupewa hati rasmi za hisa na wananchi wengine watakaonunua hisa nao pia watapewa hati za hisa hizo. Sasa benki kwa kuwa imeanza kupata faida kuanzia mwaka jana na mwaka huu, itaweza kutoa gawio. Huo ulikuwa ni utaratibu wa kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakusukuru kwa kunipa nafasi hii.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuuliza kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kauli chafu za baadhi ya wahudumu zinatuumiza sana mioyo yetu sisi wanawake hasa pale tunapokwenda kujifungua. Nikisema mfano hapa utalia, sitaki niseme mfano maana yake mambo mengine aibu. Je, Serikali inawachukulia hatua gani wahudumu kama hao na wako wengi tu? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa, katika Tanzania kuna wale Wakunga wa jadi ambao hasa hasa vijijini wanatusaidia sana sisi wanawake wakati tunapojifungua. Naomba kujua kwamba, je, Serikali inawathamini vipi Wakunga hawa wa jadi ili kuwaweka katika mazingira mazuri au mazingira rafiki? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba tu Mheshimiwa Dada yangu Mheshimiwa Faida Mohammed Bakar asitoe machozi na naomba nimjibu kama ifuatavyo; kwamba Serikali inawachukulia hatua gani wahudumu ambao wanatoa lugha chafu kwa wateja. Kwanza Serikali imeweka utaratibu mzuri sana wa kukusanya maoni na malalamiko ya wateja kwenye mahospitali yote. Pia Mheshimiwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Ally Mwalimu ambaye ni champion wa haki za uzazi na watoto hata kabla hajawa Mbunge amefika tu Wizarani na ameanzisha utaratibu wa kuwa na namba maalum ambapo maoni ya wateja kutoka popote pale, kona yoyote ya nchi yetu wanaweza wakayawasilisha kwenye namba hiyo na sisi moja kwa moja tukayashughulikia.
Mheshimiwa Spika, sambamba na jitihada hizo Mabaraza ya Weledi kwa maana ya Mabaraza ya Wauguzi, Mabaraza ya Madaktari, Mabaraza ya Wafamasia yana utaratibu wa kimaadili wa kuchukua hatua dhidi ya wataalam ambao wamesajiliwa na Mabaraza hayo pindi ushahidi utakapopelekwa kwenye mabaraza hayo na wana nguvu ya kimahamaka wakikaa kwenye Baraza la Kimaadili pale wanakuwa na nguvu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi na kwa maana hiyo wanaweza kuchukua hatua za kisheria ikiwemo kuwaadhibu wataalam hawa kwa kuwapeleka jela.
Swali la pili, kwamba Serikali ina mikakati gani ya kuboresha huduma hizi? Tumejipanga vizuri Wizarani kuboresha huduma za akinamama wajawazito na watoto na hasa kuanzia ngazi ya kwenye jamii, kwa maana ya kuwatumia vizuri wakunga wa jadi. Serikali inawawezesha vipi jibu ni kwamba Serikali yetu ina utaratibu wa kuwapa mafunzo wakunga hawa wa jadi kwa maana ya traditional birth attendant kule kule kwenye maeneo yao, lakini pia kuwapa vifaa.
Mheshimiwa Spika, wanapewa vifaa kama gloves, pia kama wakigundua kuna tatizo kwa mama mjamzito mapema kabla hata siku ya kujifungua haijafika, wamepewa maelekezo ya namna ya kuwapa rufaa kuingia kwenye mfumo rasmi ya kutoa huduma za afya ya uzazi kwa akinamama. Kwa maana hiyo, wanapewa mafunzo wanathaminiwa, wanapewa vifaa na wanapewa maelekezo ya kuwa absorbed kwenye mfumo rasmi wa huduma ili akinamama hawa waondokane na hatari za kutibiwa katika hali ya complications na watu ambao hawana special skills za kuweza kutoa huduma hizo.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka tu kumthibitishia Mheshimiwa Faida na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania tumeshatoa maelekezo kwa watumishi wetu wote katika sekta ya afya kuvaa vitambulisho. Kwa hiyo, pindi unapohudumiwa kitu cha kwanza ni vizuri uangalie anayekuhudumia ni nani, ni Ummy Ally Mwalimu na pale unapopata matatizo, tuletee jina la huyo mhudumu na tumesema hatutavumilia lugha chafu kwa wahudumu wetu kwa hiyo, tuletee jina na tutawapeleka katika Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania na nimeshalielekeza baraza liongeze jitihada katika kuhakikisha tunarudisha nidhamu na maadili katika utumishi wa sekta ya afya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Faida naomba usilie suala lako tunalifanyia kazi. (Makofi)
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba Serikali imebaki katika kuweka mazingira mazuri, lakini naona kwamba mazingira mazuri hayo si kweli sana kwa sababu hayaonekani maana wananchi wanalalamika sana. Kwa sababu ukienda Bureau de Change hii ina rate hii, ukienda Bureau de Change nyingine ina rate tofauti na zimetapakaa sehemu zote kama sisimizi. Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha rates hizo zinalingana? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kuwa Serikali imejitoa katika biashara hii ya kumiliki Bureau de Change lakini huo ulikuwa ni uamuzi wa zamani na tujue kwamba sasa hivi dunia imebadilika, ni dunia ya sasa. Je, atakubaliana nami kwamba sasa umefika wakati wa Serikali kumiliki huduma hii ili kuwaondolea wananchi wake matatizo ambayo wanakabaliana nayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru kwa kuuliza maswali mazuri ya nyongeza ambayo yanakidhi haja na yanaakisi kinachoendelea katika maduka yetu ya kubadilisha fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, jibu la swali lake la kwanza kwamba rates ni tofauti sana kutoka duka moja kwenda duka lingine, nakubaliana naye na hii yote ni kuonesha kwamba tuko ndani ya soko huria na kila mtu anatakiwa ku-charge anavyoona inafaa. Pia kiuchumi, sisi wachumi tunafahamu kwamba bei ya bidhaa yoyote ile hutegemea na demand na supply. Kwa hiyo, kama demand ya bidhaa hiyo ni kubwa bei zitakuwa tofauti kutoka kwa muuzaji mmoja kwenda kwa muuzaji mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, Serikali iweze kurudi kwenye kuendesha biashara kama hizi na kwamba huo ulikuwa ni uamuzi wa zamani, naamini uamuzi ule ulikuwa ni sahihi na bora. Kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba tangu mwaka 1991 Serikali ilishajitoa kuendesha mabenki haya. Tunaendelea kusisitiza, sisi kama Serikali tutaendelea kutunga sera na sheria mbalimbali za kusimamia maduka haya ili yaweze kutoa huduma zilizo bora kwa wananchi wetu.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitendo hivi vya kuwaua wazee wetu ama tunavyoita vikongwe lakini hao mimi kwa lugha hii ya vikongwe hata siipendi, wazee wetu! Wazee ni dhamana yetu sisi vijana ama wananchi wote, lakini kuna watu katika mikoa mingine wanawaua wazee wetu, wengine wakiwa hai wanawafukia. Hiyo tunaoneshwa kabisa katika vyombo mbalimbali vya habari. Wengine wanawaua watu kwa kuwafukia kwa sababu wazee wetu wana macho mekundu na watu hawajui kwamba kuwa na macho mekundu ni kupikia kuni kwa wingi, sasa...
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Na mavi ya ng‟ombe, wengine wanasema kinyesi cha ng‟ombe, wanapikia kinyesi cha ng‟ombe wengine macho yanakuwa mekundu.
Je tutawasaidiaje wazee hawa kuwaondoshea kuwa na macho mekundu kwa kuwapelekea gesi kwa wingi kule vijijini ili waweze kuwa na macho mazuri, wasipate kuuliwa kwa itikadi za kishirikina? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amejibu hapa kama kunatolewa elimu.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Faida hilo ni swali la nyongeza au la pili?
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: La pili la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amesema kwamba hapa Serikali inatoa elimu, hata sisi Wabunge tunapaswa kutoa elimu katika maeneo yetu, lakini sasa athari hii ya kuwaua wazee wetu itakwenda vizazi na vizazi vijavyo huko mbele. Watoto wetu wanajifunza nini kuhusiana na jambo hili hapo mbele?
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inawachukulia hatua gani kuwaondosha hawa watu wanaowaua wazee wetu? Inawachukulia hatua gani kali kukomesha hasa katika mikoa hiyo ya Mwanza, Shinyanga, Tabora na kwingineko, wazee wetu wanauliwa sana? Naomba jibu maridhawa.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna mikakati mbalimbali ambayo tayari imeshaanza kuchukuliwa na Serikali kuhakikisha kwamba matumizi ya kuni ama hayo mavi ya ng‟ombe kwa ajili ya kupikia yanapungua, ikiwemo kuanzisha kwa nishati mbadala, matumizi ya majiko bunifu na kadhalika, lakini pia harakati za Serikali kusambaza umeme vijijini zinasaidia sana kuhakikisha wananchi wanatumia nishati iliyokuwa bora zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lake la pili anazungumzia kwamba hatua gani ambazo Serikali imechukua ili kudhibiti matukio kama haya. Nataka tu nimhakikishie kwamba takwimu ambazo tunazo kuanzia mwezi Julai, 2015 mpaka Machi, 2016 tayari kuna watuhumiwa 135 ambao wameshakamatwa na kesi kama 222 ambazo zinaendelea mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Jeshi la Polisi ama Serikali kupitia Jeshi la Polisi, linafanya kazi kubwa sana kuhakikisha kwamba linawadhibiti wale wananchi wote ambao wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza:-
Kwa kuwa, Naibu Waziri amekiri kwamba wameshaanza kujenga uzio katika kituo cha Ziwani pale Zanzibar, tunashukuru sana Serikali. Naomba kumuuliza sasa, Zanzibar ina vituo vingi sana ikiwemo na vituo vya Pemba, je, ni lini Seriali itajenga uzio katika vituo vya kule Pemba?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amejibu kwamba itajenga uzio katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, ninavyoelewa kwamba bila ya bajeti uzio hizo hazitoweza kujengwa na hatujaona katika bajeti yake kukiwemo ni makisio hayo. Je, Serikali itakubaliana na mimi kwamba katika mwaka ujao wa 2017/18 iweze kuweka bajeti ya kuwajengea uzio katika vituo mbalimbali na makambi ya Polisi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza kwamba ni lini vituo vitajengewa uzio. Kama ambavyo nimekuwa nikizungumza kila siku kwamba ujenzi wa uzio, ukarabati wa vituo na kadhalika inategemeana na uwezo wa kifedha. Hata hivyo, kwa kuwa malengo ya kujenga vituo ambavyo kwa mujibu wa PGO namba 287 inaonesha kwamba maeneo ambayo vituo vinavyohitaji kujengewa uzio ni vituo class (a) na (b), lakini kwa mujibu wa PGO namba 314 vilevile inaonesha dhamira ya ujenzi wa uzio ni kuhakikisha usalama unaimaridhwa katika maeneo husika.
Hata hivyo kwa kukidhi ile PGO 314 ni kwamba unaimarisha ulinzi katika maeneo hayo katika kipindi hiki ambako bado bajeti haijaweza kukidhi kujenga vituo vyote. Kwa hiyo, kimsingi ni kwamba tunaweza kutekeleza hili jambo la kuimarisha usalama katika vituo vyetu kwa kuimarisha ulinzi. Kwa kuanzia wakati huo huo tunatafuta fedha za kuweza kujenga uzio.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kwamba anajaribu kupendekeza bajeti ya mwaka ujao wa fedha tuweze kuwa na bajeti ya kutosha kwa ajili ya kujenga uzio. Mimi naamini kabisa chini ya utaratibu ambao Serikali hii ya Awamu ya Tano tunakwenda nao ya kuhakikisha kwamba tunaongeza kukusanya mapato katika nchi hii, basi imani yangu ni kwamba kadri ya miaka inavyokwenda mbele tunaweza kupata bajeti ya kutosha na Wizara ya Mambo ya Ndani kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ujenzi wa uzio katika vituo vyetu vya Polisi.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wastaafu wa Afrika Mashariki hakuna tena na Serikali haidaiwi tena lakini mimi nasema Serikali inadaiwa, wako wengi. Mimi mwenyewe nina ushahidi, kuna mzee mmoja kule Pemba alikuwa anafanya kazi Custom, anaitwa Mzee Mohamed Kombo Maalim, alikuwa Askari wa Custom, mpaka kafariki hajalipwa mafao yake, ni mzee wetu kabisa. Sasa naomba kusema kwamba Mheshimiwa Waziri asitudanganye, aseme ukweli na sisi atujibu hapa, hawa waliobakia watalipwa lini? Wapo, hawajalipwa, nina ushahidi kamili!
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, hawa ambao hawakuridhika walienda tena Mahakamani wakafungua kesi, Shauri la Rufaa Na. 73 la 2013. Mahakama ya Rufaa imeamua tarehe 29 Januari, 2016, mwaka huu, kwamba madai hayo waliyokuwa wanadai kwamba wamepunjwa hayakuwa halali na hayapo tena. Kwa hiyo, ile ndiyo mwisho wa safari…
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Sasa hii ni Mahakama ya Rufaa, ndiyo mwisho wake pale.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa benki nyingi hapa Tanzania zinatoa mikopo kwa riba kubwa sana na zinafanya wafanyabiashara ama wananchi wa Tanzania kukopa lakini kutokurudisha mikopo hiyo kwa wakati kutokana na riba kubwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha benki hizo zinapunguza riba hizo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa hivi sasa kumejitokeza taasisi nyingi ambazo zinatoa mikopo, lakini hazifuati taratibu za kitaalamu je, Serikali inalijua hilo na kama inalijua hilo inazichukulia hatua gani taasisi kama hizo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Faida Bakar kwa umakini wake wa kufuatilia masuala ya kifedha hapa nchini. Hili ni swali lake la pili katika Bunge hili nalijibu akiulizia masuala haya, hongera sana Mheshimiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kumekuwa na riba kubwa, lakini naomba tufahamu kuwa kufuatia mabadiliko ya mfumo wa kifedha hapa nchini kuanzia mwaka 1991, Serikali ilijitoa katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za kifedha hapa nchini, ili kuruhusu ushindani huru na kuboresha huduma katika sekta yetu ya fedha. Hivyo, viwango vya riba na mikopo zinazotozwa na benki zetu na taasisi nyingine za kifedha zinapangwa kutokana na nguvu ya soko huria ambalo tuliamua wenyewe kuingia katika soko hilo.
Mheshimiwa Spika, pia napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba katika upangaji wa viwango hivyo vya tozo mbalimbali na riba benki pia na taasisi zetu za kifedha huzingatia gharama za upatikanaji wa fedha, pia gharama za uendeshaji na sifa alizonazo mkopaji katika kuliendea hilo. Hivyo Serikali pia tunaendelea kuwasisitiza mabenki yetu pamoja na taasisi zetu za kifedha kutumia takwimu za credit reference bureau ili kuweza kujua taarifa halisi na historia za wakopaji na pia ushindani uliopo ili tuweze kushusha riba hizi, lakini kama Serikali hatuwezi kuingilia tena katika soko hili.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili Mheshimiwa Faida Bakar, amependa kujua kwamba kumekuwepo na taasisi nyingi za kifedha na je, zile ambazo hazifuati utaratibu je, Serikali ina mpango gani wa kuzitambua na kuzirasimisha?
Napenda kumjibu Mheshimiwa Faida Bakar kwamba Serikali inafahamu tatizo hili la Taasisi zilizopo za binafsi ambazo zipo na zinasumbua sana wananchi wetu. Katika kulitambua hilo Serikali kwa sasa iko katika mpango wa kuandaa Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2016 ambapo sasa hivi ipo katika hatua nzuri, itapelekwa kwenye Baraza la Mawaziri na hatimaye tutaweza kuwa na Microfinance Act itakayoweza kudili na tatizo hili moja kwa moja. Nashukuru.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mbali na suala hili kwamba Serikali inachukua muda mrefu kusema kwamba haijapatikana ushahidi, lakini ushahidi anaweza akautoa mtoto kwamba ni fulani ndiyo kanifanyia kitendo hiki, lakini Serikali inasema bado ushahidi.
Pia kuna baadhi ya wazazi huwa wanaficha makosa haya, ama sijui kwa kuona aibu ama kwa kuoneana sijui vipi, labda huwa wanapewa hela na wale watuhumiwa. Je, Serikali inawachukulia hatua gani wazazi kama hawa wanaoficha ukatili huu dhidi ya watoto wao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, endapo mtoto ameathirika kiafya, yaani yule ni mtoto mdogo ujue, lakini kaathirika kiafya, maumbile yake yameathirika, Serikali inamsaidiaje mtoto kama huyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Utaratibu wa kesi ni utaratibu wa kisheria na haijalishi sana jambo lenyewe lina maumivu kiasi gani kwa watu wanaohusika kwenye kesi hiyo. Hivyo, utaratibu wa kisheria unataka ushahidi ufikishwe Mahakamani na Mahakama ishawishike bila kuwa na shaka kwamba kosa kweli limetendeka. Kwa sababu raia wote wana haki ya kutendewa sawa mbele ya macho ya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, haiwezekani Serikali hata kama ina uchungu kiasi gani na watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili, basi ikalazimisha tu hatua zichukuliwe dhidi yao bila utaratibu wa Kimahakama kufuatwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo nitoe wito, wazazi watoe taarifa kwenye vyombo vya sheria kuhusiana na vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa watoto pindi vinapotokea. Kwa sababu pia jambo lingine ambalo linajitokeza kutokana na utafiti uliofanywa kwa kushirikiana na Wizara yetu pamoja na Chuo kikuu cha Muhimbili, ni kwamba maeneo hatarishi ya vitendo vya ukatili kwa zaidi ya asilimia 60 ni nyumbani ambapo watoto wanaishi, ikifuatiwa na shule kwa zaidi ya takriban asilimia 56.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama hayo ndiyo mazingira ambayo watoto wanafanyiwa vitendo hivi, basi wazazi wakishirikiana na Walimu watoe taarifa kwenye mamlaka za kisheria na watoe ushahidi na wawe tayari kwenda kutokea Mahakamani ili kutoa maelezo yatakayowezesha watuhumiwa kuwekwa hatiani.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Nataka tu kuongezea na kutoa rai kwa wazazi na kutoa onyo kwamba pale ambapo mtoto atatoa ushahidi na ikidhihirika kwamba amefanyiwa vitendo vya kikatili, tukigundua mzazi ama jamaa analegalega kwenye kutoa ushahidi, tutamuunganisha na wahalifu na hatua zitachukuliwa bila kujali kwamba yeye ni mzazi wake.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza baada ya majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi juzi tu, gazeti moja la Mwananchi lilitoa habari kuwa, huduma za dawa zitatolewa yaani kwa kununuliwa katika hospitali kuu ya Muhimbili. Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na habari hizo?
Swali la pili, kwa kuwa ajali ni jambo baya sana, na ajali huweza kutokea kwa mtu yeyote na wakati wowote ule, na kwa kuwa watu wanaopata ajali huwa wanalipishwa dawa hata kama ni kwa baadae. Je, Serikali itakubaliana nami kwamba sasa ni wakati muafaka wa kuingiza katika mfumo kwa hao watu wanaopata ajali, kutolipa malipo ya huduma na dawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NAWATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya MheshimiwaFaida Mohammed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kuhusu taarifa za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imetoa tamko kwamba itaanza ku-charge dawa zote; naomba nirejee maelezo niliyoyatoa hapa juzi, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Mrisho Kikwete, Mbunge wa Chalinze. Kuhusu jambo hilo hilo ambalo leo tena Mheshimiwa Faida Mohammed Bakar analiuliza,kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haijafanya mabadiliko yake kwenye Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007; na nimeeleza kwenye majibu yangu ya msingi kwamba kuna magonjwa ambayo yanapewa msamaha kwa mujibu wa sera hiyo, kwenye ile Ibara ya 5.4.8.3 cha sera hiyo ambapo tunaelezea makundi ambayo yanapaswa kupata huduma za afya kwa msamaha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitarudia tena kuyataja kwa faida ya Wabunge lakini pia kwa faida ya watanzania wote. Kwamba wagonjwa wote wanaoumwa magonjwa ya muda mrefu, yaani chronic illnesses, wanapewa msamaha na Sera ya Taifa ya Afya; na kwa kutaja machache tu nitasema kuna magonjwa ya moyo, magonjwa yote ya akili, magonjwa ya saratani, kifua kikuu, ukoma, UKIMWI, pumu, sickle cell, magonjwa yote haya yanapewa msamaha kwa mujibu wa Sera ya Afya. Lakini pia kuna makundi maalum machache nayo yanapewa msamaha na Sera ya Afya na makundi hayo ni makundi ya wazee wenye umri wa miaka zaidi ya 60, watoto wenye umri chini ya miaka mitano, akina mama wajawazito na watu wenye uwezo mdogo wa kifedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama kuna gazeti liliandika taarifa hizo, basi gazeti hilo linapotosha na taarifa hizo haziwezi kuwa sahihi, na mimi kama Naibu Waziri mwenye dhamana ya kusimamia utekelezaji wa sera ya afya hapa nchini, ninarejea tena kutoa msimamo wa Serikali kwamba sera yetu haijabadilika na kwa maana hiyo makundi haya ambayo yanapewa msamaha na Serikali kwa mujibu wa sera yataendelea kupata msamaha huo kwa mujibu wa sera yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, kuhusu ajali. Matibabu yote ya dharula kwa mujibu wa Sera ya Afya hapa nchini ni bure, mtu akiugua ghafla achilia mbali kupata ajali; akiugua tu ghafla, akaanguka, jambo la kwanza akifika hospitalini atapewa tiba hiyo bure bila kuulizwa gharama yoyote ile. Huo ndio utaratibu na ikitokewa mahala mtu akawa-charged naomba azifikishe taarifa hizo kwangu na mimi nitachukua hatua hapo hapo.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR:Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mbali na tatizo la upatikanaji wa mbolea kwa wakati kwa wakulima, lakini kuna tatizo kubwa la elimu juu ya utumiaji wa mbolea hizo kwa hao wakulima.
Je, Serikali imejipangaje juu ya kutoa elimu endelevu,kwa utumiaji wa mbolea hizo, hususani kwa wakulima wanawake ili kupatikane mazao ambayo yana tija?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama alivyosema kwamba kuna changamoto kubwa ya elimu na ufahamu miongoni mwa wakulima wetu, kuhusu utumiaji wa pembejeo. Nikiri kabisa kwamba moja kati ya matatizo ya matumizi ya pembejeo kuweza kuongezeka nchini kwetu, ni kwa sababu ya hamasa ndogo ambayo wananchi wanayo. Kwa hiyo, sisi tunaamini kwamba zoezi la kutoa elimu na uhamasishaji lazima liende sambamba na utoaji wenyewe wa ruzuku ili hatimaye wananchi waweze wenyewe kujinunulia kwa sababu utaratibu wa kutoa ruzuku kwenye pembejeo sio endelevu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Ofisi zetu za Kilimo na Maafisa wetu wa Kilimo walioko kwenye Halmashauri, wanaendelea kutoa elimu na kuamasisha wananchi, kuhusu umuhimu wa kutumia pembejeo na hii ni bila kuchagua jinsia, wakulima wote wanapatiwa elimu hii na tunaendelea kuhamasisha wananchi wetu waweze kutumia pembejeo.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya ngongeza. Kwa kuwa mbali na matatizo ya Madaktari hatari feki ambao wameenea katika baadhi ya hospitali zetu, lakini pia kuna tatizo sugu la dawa feki ambazo zinateketeza ama zinaleta athari kwa watumiaji wa dawa hizo. Je, Serikali inalishughulikiaje tatizo hilo la dawa feki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Waganga wa Tiba Asilia wameenea katika maeneo mengi ya nchi yetu ya Tanzania na kwa kuwa baadhi yao hutumia dawa feki ambazo hazijathibitishwa.
Je, kwa nini Serikali inawaruhusu Waganga hao wa Tiba za Asili kufanya kazi zao na baadhi yao kutoa dawa feki kwa watumiaji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kuhusu dawa feki, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Waheshimiwa Wabunge wote na wananchi kwa ujumla kwamba uwezekano wa kuwa na dawa feki kwenye vituo vya kutolea tiba hapa nchini ni mdogo sana, almost hakuna kwa sababu tuna utaratibu mzuri wa kuhakiki viwango vya ubora wa dawa ambazo zinatolewa kwa ajili ya matumizi ya binadamu na hata zile za mifugo hapa nchini kwetu, utaratibu huu ni mgumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kusajili dawa ambayo itaingia kwenye soko inachukua muda mrefu, inachukua Mamlaka mbalimbali za uchunguzi kuichunguza dawa hiyo na hatimaye kuiruhusu iweze kutumika katika vituo vyetu. Kama ikijitokeza kukawa kuna walau fununu tu za uwepo wa dawa feki basi, Serikali kutumia mamlaka zake za uchunguzi hutuma kikosi cha ukaguzi kwenye eneo hilo ili kuweza kuthibitisha kama kweli maneno hayo yanayosemwa kuhusu uwepo wa dawa feki ni ya kweli ama laa. Mara nyingi hatua kali huchukuliwa dhidi ya mtu yoyote yule ambaye atakutwa na dawa feki.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu waganga wa tiba asili, waganga wa tiba asili wapo kisheria, wanatambuliwa kwa mujibu wa sheria na wanasajiliwa kwa mujibu wa sheria ya waganga wa tiba asili na tiba mbadala ya mwaka 2002.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa ni kweli baadhi yao wanatoa dawa ambazo ni feki na siku zote tumekuwa tukiwabaini na tukichukua hatua za kuwadhibiti. Napenda kutumia Bunge lako Tukufu kuwaeleza waganga wote feki ambao hawajasajiliwa kuchukua hatua za kufika kwenye Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala mara moja, kwa ajili ya kusajiliwa pia kutumia utaratibu mpya ambao tumeuanzisha baada ya lile tukio la Dkt. Mwaka nilipoamua kumtembelea kwa ghafla. Tumeanzisha utaratibu mpya sasa wa kusajili dawa zote ambazo zinatolewa na waganga wa tiba asili na tiba mbadala hususani zile ambazo zinafanyiwa packaging kisasa. Utaratibu huo na wenyewe utakuwa mgumu kama ulivyo huu wa dawa hizi za tiba ya kisasa ili kuweza kudhibiti uwezekano wa uwepo wa waganga wa tiba asili ambao wanaweza wakawa wanatoa dawa ambazo zina sumu ndani yake.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na matatizo ya mishahara kwa wafanyakazi wengi wa viwandani, lakini pia kuna tatizo moja sugu la ukatiwaji wa bima, yaani wafanyakati wa viwandani kupatiwa bima. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvilazimisha viwanda viwakatie bima za maisha wafanyakazi wao?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA, NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Serikali imegundua kwamba yapo matatizo ya namna mbalimbali ambayo wafanyakazi wanatakiwa wahifadhiwe kwa kufuata mifumo inayotakiwa katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua tatizo hilo, Serikali imeanzisha ule Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na baada ya kuanzisha mfuko huo na kuwalazimisha waajiri watii takwa la kisheria la luchangia mfuko huo, sasa tunauhakika na ninaomba niwahakikishie wafanyakazi watulie kwa sababu sasa Serikali itakuwa ikiwafidia kupitia kwenye mfuko huo ambao umeanzishwa na Serikali na sisi tutaendelea kuusimamia kuhakikisha wafanyakazi wanafidiwa katika viwango vinavyostahiki kulingana na sheria ilivyo na namna mbalimbali ambazo zitakuwa zimetokea katika sekta zao za kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Serikali imelisimamia hilo na tutaendelea kulifanyia kazi vizuri.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa simu fake mpaka sasa hivi zinaingizwa hapa nchini na wananchi wengi huwa wanazinunua kwa kuona kana kwamba sio simu fake, maana hazina utambulisho rasmi kuonekana hii ni fake ama hii si fake, unaweza ukaiona simu kubwa, ukaipenda kumbe hiyo ndiyo fake yenyewe. Sasa baada ya wananchi kuzinunua simu hizo hapo, TCRA wanazifungia kwa kuona kwamba ndiyo simu fake, mimi naomba kuuliza hivi; kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kuwafungia wale wanaozileta badala ya kuwanyanyasa wananchi? Ahsante sana.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ni kweli bado zinaingia simu fake lakini mara ukienda kununua simu, ukiiwasha pale kama simu fake haiwezi kuwaka. Sasa kabla ya kulipia simu unaponunua hakikisha kwamba unamwambia yule muuzaji akutilie line pale na ujaribu, kama ni simu fake simu hiyo haiwezi kuwaka kwa sababu simu zote fake sasa hivi zinazoingia nchini haziwezi kufanya kazi.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa kuna baadhi ya maeneo ambayo wananchi wamelipia katika eneo la Kigamboni - Kibada na wamepewa hatimiliki na nina ushahidi kamili kwa sababu mimi ni mmojawapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ile ya Kigamboni - Kibada kuna eneo ambalo watu wamepewa hatimiliki na mpaka hivi sasa watu wameshindwa kujenga kutokana na wananchi fulani fulani wanasema ni maeneo yao na ukitaka kwenda kujenga wanaandamana. Je, Serikali inalijua hilo? Kama inalijua, italichukulia hatua gani suala kama hilo ili watu waliopewa hatimiliki waweze kujenga nyumba?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Faida Bakar kuhusiana na mgogoro ambao uko katika eneo la Kigamboni hasa katika eneo la Kibada kama alivyolitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kwanza nimhakikishie kwanza, migogoro ya Kigamboni ambayo imekuwepo kwa sasa ni kama imepungua na Mheshimiwa Mbunge wa eneo lile amekuwa akifuatilia mara kwa mara kuweza kujua watu wake hatima yake inakuwaje. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba, pamoja na kwamba kuna ule mradi ambao unasimamiwa na Wizara ambao umechukua karibu hekta 6,000 katika lile eneo lakini bado kuna maeneo mengine ambayo yana migogoro kama alivyoitaja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Wizara imetoa maeneo katika eneo la Kigamboni ambapo kuna wapimaji ambao wamepima maeneo yao. Ni kweli kuna watu ambao wana hati zao na wameshindwa kuendeleza kutokana na migogoro hiyo. Kwa sababu mgogoro huu ni mkubwa, Wizara yangu itakuwa tayari kwenda kuhakiki katika maeneo yale yote ambayo watu wana hati zao lakini kila wakitaka kuendeleza kuna watu wanaandamana ili tuweze kuondoa mgogoro huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kigamboni imekuwa kama ni jicho la Wizara katika kuona kwamba ule mpangilio unaokwenda kufanyika pale unafanyika kwa taratibu ambazo ni za kisheria na ambazo zitakuwa hazikuvunja haki za wamiliki wa awali katika upande huo. Kwa hiyo, namhakikishia tu kwamba suala hili tutalifanyia kazi na tutachunguza yale yote ambayo yanalalamikiwa katika utaratibu mzima wa umilikishaji wa ardhi.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri Masauni huwa ana kawaida ya kutembelea mikoa mbalimbali ili kuona matatizo ama changamoto za askari na hata Pemba alifika na yeye mwenyewe alijionea tatizo sugu lililopo katika Mkoa wa Kusini Pemba, Wilaya ya Mkoani kituo cha Mkoani na kituo cha Kengeja, zile ofisi zinavuja. Je, Serikali itakubaliana nami kwamba hela hizi zilizopangwa na nyumba hizo zitakazojengwa zianzie katika ofisi za kule Mkoa wa Kusini Pemba Wilaya ya Mkoani na kule Kengeja ili kuwaondoshea askari hao usumbufu mkubwa wanaopata? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa kutokana na tatizo kubwa la ukosefu wa nyumba za askari hasa kule Pemba; askari wengi wanakaa katika nyumba za kupanga ambazo zipo mbali sana na vituo vyao vya kazi. Je, Serikali ipo tayari kuwaondoshea tatizo hili askari hao kwa kuwakopesha vifaa vya usafiri lakini vifaa hivyo viwe na riba nafuu ili kuwaondoshea tatizo hilo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama alivyosema kwamba Kusini Pemba kuna changamoto kubwa kama nilivyosema kwamba nchi nzima kuna changamoto ya nyumba za polisi kiasi kwamba kuna upungufu mkubwa. Katika kutimiza azma ile ya Serikali ya kuhakikisha kwamba askari wetu wanapata nyumba nchi nzima tutaanzia kwenye maeneo yale ambayo tunafikiri kuna tatizo zaidi na Kusini Pemba ni moja kati ya maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na kujenga nyumba mpya kama nilivyosema katika majibu ya swali la awali ni kwamba Serikali vilevile iko kwenye utaratibu wa kukarabati nyumba kwa kuanzia na yale maeneo ambayo yana shida zaidi. Kwa hiyo, nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Kusini Pemba ni moja kati ya maeneo ambayo yameonekana yana changamoto kubwa na mpango huo wa kufanya ukarabati pamoja na ujenzi vilevile utahusisha kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kutoa mikopo ya riba nafuu kwa ajili ya kununulia vifaa naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni moja kati ya masuala ambayo yanafanyiwa kazi ili askari wetu hasa wale ambao hawana nyumba waweze kufika kazini bila matatizo yoyote.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa askari wengi wa wanyamapori huwa wanapata athari ama wanafanya kazi katika mazingira magumu ya wanyama wakali. Je Serikali inawafidia nini wale askari wa wanyamapori ambao wanaathiriwa na wanyamapori wakali?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Faida Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze kwa kuwa imekuwa ni jambo la kawaida na linalojitokeza mara nyingi sana tunapowazungumzia askari wa wanyamapori tunazungumzia juu ya yale ambayo si ya maslahi zaidi kwao na mara nyingi ni lawama tu juu ya utendaji wao wa kazi. Kwa hiyo, kutokana na mwelekeo huu mpya wa Mheshimiwa Faida Bakar wa kuona kwamba na askari wa wanyamapori na wenyewe wana haki zao na maslahi yao yanapaswa kuboreshwa kutokana na kazi ngumu wanayoifanya natoa pongezi juu ya hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kujibu swali lake ni kwamba kwa mujibu wa kanuni na taratibu za ajira zilizopo na kwa mujibu wa sheria maslahi au haki za wafanyakazi hawa ambao ni askari wa wanyamapori zinazotokana na mazingira yao ya kazi zimezingatiwa. Ili kuongeza tija kwenye eneo hili huko tuendako na mkakati wa Kitaifa wa kuboresha zaidi ulinzi wa rasilimali zetu, Serikali inao mpango wa kuboresha hali na mazingira ya kazi hii ikiwa ni pamoja na ulipaji wa fidia, vifuta jasho pamoja na vifuta machozi kwa namna ambavyo itaonekana inafaa. Tutapitia utaratibu huo ili kuboresha mazingira na kuongeza ari zaidi kwa wafanyakazi wetu ikiwa ni pamoja na askari wa wanyamapori.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE WALEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini naomba nilipe taarifa Bunge lako Tukufu kwamba Serikali kupitia Bunge hili limeshapitisha Mfuko wa Fidia kwa wafanya kazi wote wanaoumia katika nchi yetu ya Tanzania wakiwa kazini. Mfuko huu ni kwa wafanyakazi ambao wapo kwenye private sector na wafanyakazi ambao wanafanya kazi ndani ya Serikali yetu. Katika Mfuko huo utaratibu umewekwa ambapo waajiri sasa wameanza kuchangia na pale ambapo mfanyakazi anapoumia kazini akiwa sekta binafsi ama Serikalini Mfuko huo sasa una jukumu la kulipa fidia kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niwahakikishie Wabunge, Ofisi ya Waziri Mkuu imeanza kusimamia utaratibu huo. Mfuko huo utaanza kazi hiyo mwaka huu ili kuweza kutatua tatizo la wafanyakazi wengi wanaoumia kazini wakiwemo hao askari wa wanyamapori pia.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa wavamizi ama majambazi hao, baadhi yao inasemekana wanatoka nje ya nchi yetu ambao wanaingia kwa njia za panya ama njia nyingine zozote na hawa wanakuja kufanya uhalifu na hata kuwaua askari wetu. Je, Serikali ina mkakati gani mahususi wa kulinda mipaka yetu?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru na nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa hoja aliyoitoa. Tunatambua kweli katika matukio ya uhalifu ambayo yamejitokeza tumebaini wahalifu wakiwa wanatoka nje ya nchi, kwa mfano, silaha zile tulizokamata pale Mbezi na watuhumiwa kati ya wale watu sita baadhi yao walikuwa sio Watanzania. Pia kati ya silaha zilizokamatwa Tabora, Mkoa wa Kigoma kwenye operesheni mbalimbali tulipoziangalia hazikuwa na usajili wa hapa ndani, ni silaha za kutoka nje ya nchi, kwa hiyo tumeendelea kuimarisha operesheni za aina hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunatoa rai kwa wananchi pale wanapotambua kwamba, katika nyumba ya jirani ama katika mtaa wao kuna watu wasiofahamika ama watu wasiotambulika au watu wasioeleweka kama ni Watanzania na kazi zao hazieleweki watoe taarifa katika vituo vya jirani ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaimarisha taratibu zote za mipakani, lakini wengi wanaoingia hawaingii katika njia rasmi, wanatumia njia za panya. Kwa hiyo, ni muhimu sana kila Mtanzania aweze kutambua kwamba ana wajibu wa usalama wake pamoja na mali zake kwa ujumla wake.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa, kumekuwa na ubadilishanaji wa fedha kiholela sana hasa katika sehemu za mipaka yetu na nchi jirani. Mfano, kama kule Tunduma ambapo ubadilishanaji huu huwa kama vile tunagawiana njugu yaani holela. (Makofi)
Je, Serikali ina mkakati gani wa kurasimisha kazi hii inayofanywa na watu wa kawaida na kuweza kuchukuliwa na Serikali ili kuwaondoshea hata wale watu wanaofanya kazi hiyo, inawezekana hata wakapoteza maisha yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali haioni kwamba inapata hasara na haipati mapato mengi ikiachia biashara hii iendeshwe isivyo halali?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar kwa umakini wake katika ufuatiliaji wa masuala ya kifedha na uchumi wa Taifa letu. Serikali inakiri uwepo wa watu wanaojihusisha na biashara hii kiholela hasa katika mipaka mbalimbali ya nchi yetu na nchi jirani, kwa mfano, kule Tunduma kama alivyosema, Namanga, hata pia katika Miji yetu mikubwa kama Arusha na Mwanza, lakini Serikali yetu haipo kimya katika kulishughulikia tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kupitia Sheria yetu ya Fedha za Kigeni ya Mwaka 1992 na Kanuni tulizozipitisha mwaka 2015, Serikali inaendelea kushughulikia tatizo hili. Pia, tunakiri kwamba, mapato ya Serikali yanapotea ndiyo maana Benki Kuu pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wamekuwa wakiendesha operation na warsha mbalimbali katika sehemu hizi nilizozitaja ili sasa kuwasaidia wananchi wetu hawa kuwa na uelewa wa hatari ya biashara wanayofanya, pia na kuonesha kwamba, ni kwa jinsi gani Taifa letu linapoteza mapato katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba, tunatambua hili na tumeendelea kutoa warsha katika maeneo haya na kwa watu hawa tunafanya jitihada za hali ya juu kuhakikisha sasa watu hawa wanarasimishiwa biashara zao hizi wanazozifanya, ili kwanza kama alivyosema Mheshimiwa Faida, kupunguza hatari ya maisha yao na pia kuhakikisha Serikali yetu inapata mapato ambayo tumekuwa tunapoteza.
MHE FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mbali na kujitokeza watu ambao wanawanyanyasa binadamu wenzao kwa kuwapiga lakini kuna baadhi ya watu hususani kule Pemba wanachoma mashamba ya mikarafuu, wanawapiga watu na kuwachomea nyumba. Je, Serikali imechukua hatua gani ya kuwalipa fidia watu waliodhalilishwa kwa matukio kama hayo? Vilevile imewachukulia hatua gani wahalifu hao?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwepo na matatizo ya wananchi kujichukulia sheria mkononi na hili si tu kwenye mikarafuu lakini tumeshuhudia hata kwenye upande wa wakulima na wafugaji. Tamko letu kama Wizara na kama Serikali tunasema hakuna sababu yoyote ile inayotosha kuhalalisha mwananchi kuchukua sheria mkononi dhidi ya mwenzake iwe kwa kudhuru maisha yake ama kwa kudhuru mali zake. Yeyote atakayefanya hivyo tumesema atafika kwenye mkono wa sheria na wale ambao walishafanya hivyo tumesema wachukuliwe hatua ili iwe mfano na kwa wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeelekeza na Waheshimiwa Wabunge nawaomba kwenye hili tukubaliane, ili Serikali ionekane ipo na inatetea wale wanaoonewa tutachukua hatua kali kwa wale wanaofanya vitendo hivi vya kihalifu dhidi ya wenzao. Hii ndiyo itakuwa njia pekee ya kuweza kuhakikisha kwamba wananchi hawajichukulii sheria mkononi kwa sababu duniani kote sheria isipochukua mkondo wake ndipo wananchi huchukua sheria mkononi.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.kwa kuwa ni miaka mingi sasa kila tunapoulizia kuhusiana na suala hili la Benki ya Wanawake kuanzishwa Zanzibar, mimi mwenyewe nimeulizia mara nne mpaka leo tawi hili halijafunguliwa kule Zanzibar. Na kuna mara moja niliulizia Mheshimiwa Waziri Ummy alinijibu kwamba ilitakiwa Serikali ya Zanzibar ichangie shilingi milioni 10. Nataka niulize ile shilingi milioni 10 ishalipwa ili hii benki ianzishwe au kama haitolipa hiyo shilingi milioni 10 ndio basi wanawake wa Zanzibar hatutopata benki hii? Mchakato wake ukoje?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante! Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Faida kwa kuuliza swali hili mara nyingi sana. Nina uhakika ndio maana wanawake wa Zanzibar wameendelea kumchagua kuja kuwawakilisha hapa Bungeni kwa sababu amekuwa balozi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu letu ni kwamba shilingi milioni 10 bado haijapatikana lakini azma yetu ya kufungua tawi Zanzibar iko pale pale na Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan amejitolea kutupa eneo kwa ajili kufungulia tawi hilo la benki yetu pale Zanzibar; tutaendelea kufuatilia kwa ukaribu. Na nitakapofanya ziara kwa ajili ya kufuatilia tumekwama wapi kwa ajili ya tawi hili la Zanzibar nitamshirikisha Mheshimiwa Faida.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Naibu Waziri amenijibu majibu mazuri sana na ndiyo kawaida yake. Pamoja na majibu mazuri, naomba kuuliza swali moja na nikipata baadaye hata la pili naweza kuongezea. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba Wizara ya Afya ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itashauriana na Wizara ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kuona uwezekano wa kuwapatia posho wataalam hawa wanaotoka Chuo Kikuu cha SUZA ambao wanafanya kazi za vitendo katika maeneo mbalimbali ya hapa Tanzania Bara, nakubali atashauriana, lakini anaweza akasema kwamba atashauriana, lakini tukasubiri mwaka mzima umeisha; naomba kujua, ni lini hasa ushauri huu utaanza, natamani uanze hata leo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri huyu ameonesha nia safi ya kusaidia suala hili na kwamba amesema atashauriana na Waziri mwenzake wa Zanzibar, naomba kushauri, akishauriana naye aweze kumweleza sheria kama hii ya huku iwekwe au mwongozo ili kuwaondoshea madhila wataalam wetu ambao wanafanya kazi kiuzalendo.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Faida Mohammed Bakar kwa kunipiga fagio zito kama alilonipa hapa siku ya leo.
Mheshimiwa Spika, kwamba ni lini tutashauriana na wenzetu wa upande wa Zanzibar, utaratibu tulionao kila baada ya miezi mitatu Wizara hizi mbili huwa zinakutana, kikao cha kwanza cha mwaka huu kimefanyika mwezi Januari na cha pili kitafanyika mwezi wa tatu kwa ajili ya mashauriano ya mambo mbalimbali na hili sasa litakuwa ajenda ya kikao cha Mawaziri kitakachofanyika mwezi wa Tatu.
Mheshimiwa Spika, ili kumtoa wasiwasi, na kuwatoa wasiwasi wahitimu wote wa kozi ya Environmental Health Sciences wanaotokea Zanzibar ambao wanapenda kufanya internship huku Tanzania Bara, ni kwamba kuna utaratibu ambao sio rasmi sana umewekwa ambao umekuwa ukiwasaidia kwa muda mrefu wahitimu wote ambao wanahitaji kufanya internship Tanzania Bara ambao wanaotokea upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu utaratibu huo umekuwepo na haukuwa rasmi ndiyo maana leo hii ninavyoongea hapa Wizara ya Kazi ya Jamhuri ya Muungano imeita wadau kwa ajili ya kutengeneza kitu kinachoitwa National Framework on Internship Programme ambapo ndani yake utawekwa utaratibu wa namna ya kuwahudumia wanafunzi wanaotoka Zanzibar ambao wanataka kufanya internship huku Tanzania Bara.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Nataka kujibu sehemu ya pili ya swali la Mheshimiwa Faida kwamba ni kwa nini sasa na yeye anatushauri na sisi tukashauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walifanyie kazi suala hili. Tunao Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ndani ya Bunge hili, kwa hiyo, napenda kuwashauri walibebe suala hili walieleze pia katika Baraza la Wawakilishi ili liweze kupata nguvu, kwa hiyo litatoka katika Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Muungano lakini pia litoke kwenye Baraza la Wawakilishi la Zanzibar mwisho wa siku watoto wetu wataweza kufanya internship bila shida.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kumrekebisha Mheshimiwa Naibu Waziri kidogo, mimi siyo Mbunge wa Viti Maalum Chakechake. Ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba ikiwemo Chakechake na Mkoani. Ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kama kawaida yake, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania yanaleta uharibifu wa mazingira katika nchi yetu; na kwa kuwa gesi ipo lakini haifikishwi hasa kule vijijini ambako hiyo miti ndiyo inakatwa na kufanywa mikaa: Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasambazia wananchi gesi hasa za majumbani kwa ajili ya matumizi na waachane na tabia ya kukata miti na kutengeneza mkaa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa watu wengi wana hamu kubwa sana ya kutumia hii gesi hasa ya majumbani lakini wanaogopa, wanasikia kwamba gesi inaua; hawana elimu hiyo: Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kutoa elimu ya kuwaelimisha wananchi hasa vijijini na mijini ili kuweza kutumia gesi hiyo kwa manufaa ya wananchi wote hasa vijijini na mijini kwa ajili ya matumizi ya kupikia majumbani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Faida kwa jinsi anavyohangaika na kushughulika na kupambana na uharibifu wa mazingira hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ambayo Serikali imechukua katika kuhakikisha kwamba uharibifu wa mazingira unapungua kwa kiasi kikubwa ni kuongezeka kwa matumizi ya gesi asilia hapa nchini. La kwanza, nimshukuru Mheshimiwa Mbunge, na hatua ya kwanza ambayo Serikali imeanza, TPDC imeanza sasa mradi wa kusambaza gesi majumbani na katika matumizi ya magari kwa ajili ya Dar es Salaam. Hatua ya kwanza imekamilisha usanifu ambao hivi karibuni utaanza utekelezaji wake na maeneo yatakayoanziwa ni pamoja na maeneo ya Mikocheni, Tabata na Sinza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, waharibifu wa kwanza kabisa wa mazingira hapa nchini ni wakazi wa Dar es Salaam. Dar es Salaam na wananchi kwa ujumla ni jumla ya magunia 45,000 yanaingia kwa siku kwa Jiji la Dar es Salaam. Sasa ili kupunguza athari hiyo, hatua ya kwanza ni kupunguza matumizi ya mkaa kwa wananchi wa Dar es Salaam kwa kutekeleza mradi huu.
Awamu ya pili itaenda katika maeneo ya Tabata, maeneo ya Ukonga kwa Mheshimiwa Waitara, lakini maeneo ya Kigamboni na maeneo mengine. Utaratibu huu utaenda sambamba na maeneo ya Lindi na Mtwara ambapo mradi huu pia utaanza mwezi Juni mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo utekelezaji huu wa kutumia gesi utaendelea katika Mikoa ya Morogoro na Dodoma ambayo inakuja kuwa Makao Makuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi kwamba matumizi ya gesi yatapunguza kwa kiasi kikubwa sana uharibifu wa mazingira. Huo ni mkakati wa kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa pili, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali imetenga pesa, jumla ya shilingi bilioni 6.5 kwenye bajeti ya mwaka huu ili gesi iweze kusambazwa katika maeneo mengi hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu; ni kweli TPDC wameanza kutoa elimu japo siyo kwa kiwango kikubwa. Elimu ya kwanza ambayo imefanyika ni katika maeneo ya minada pamoja na maeneo ya maonyesho, lakini katika Mikoa ya Lindi na Mtwara TPDC imetoa elimu mashuleni, wameanza kutoa makongamano katika maeneo ya Mikoa ya Lindi na Mtwara, Mwanza, Arusha pamoja na Mkoa wa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, harakati za kutoa elimu ili matumizi sahihi yaende sambamba na mahitaji, yanaendelea.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu hayo ambayo hayajaniridhisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba sheria hii haina ubaguzi lakini mimi nasema ina ubaguzi. Kwa sababu iweje sheria ipingane na Katiba? Katiba imetutambua Wabunge wa Viti Maalum na Wabunge wa Majimbo sote ni sawa, tuna haki sawa, tunafanya kazi sawa za kuiletea maendeleo nchi yetu hii iweje leo useme haina ubaguzi?
Je, ni lini sheria hii italetwa hapa Bungeni ili tuirekebishe tupate haki sawa sote, Wabunge wa Majimbo na Wabunge wa Viti Maalum, kwa sababu sote tunafanya kazi sawa?
Pili, kwa kuwa Wabunge wa Viti Maalum tunafanya
kazi zaidi kwa sababu sisi tuna-handle mikoa, lakini Wabunge wa majimbo wanakuwa na majimbo. Jimbo liko ndani ya mkoa, Wabunge wa Viti Maalum tuko kwenye mkoa mzima tunafanya kazi za maendeleo, lakini tunatumia hela zetu za mfukoni tukipata posho, tukipata mshahara, ndiyo tunatumia Serikali haituhurumii?
Je, ni kitu gani chenye kigezo muafaka ambacho amekisema Naibu Waziri kati ya Jimbo na Mkoa upi wenye kigezo ambacho kinakubalika watu wengi, sijui Mkoa ni mkubwa kama alivyosema kuliko Jimbo...
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anipe kigezo, bado hajaniambia kigezo.(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nimesema kwa sababu sijasema mimi kama Jafo, nimesema kwa mujibu wa sheria. Bahati nzuri mnafahamu ndugu zangu kwamba sheria hii ilitungwa humu Bungeni na sheria hii ilipata msuguano mkubwa sana, ndiyo maana ukija kuangalia ni kwamba sheria hii hata suala la vile vigezo vilivyotengwa ndiyo maana inaitwa Sheria ya Mfuko wa Jimbo. Kwa hiyo, kama itaonekana kwamba nini kifanyike hayo sasa ni mawazo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu lazima tufahamu kuna Wabunge wa Majimbo, kuna Wabunge wa Viti Maalum kutoka Mikoa, kuna Wabunge wengine wanateuliwa na Rais maana yake wanazungumza karibu Tanzania nzima. Kwa hiyo, kama tukitaka tufanye tafakari hiyo na kutakuwa na Wabunge wengine ambao wao wanahudumu Tanzania nzima ndiyo maana nimesema Bunge hili ndiyo lenye dhamana ya kutunga sheria ikionekana jambo hilo linahitajika lifanyike, Bunge litafanya maamuzi sahihi. Tufahamu vilevile hata mkoa hauwakilishwi na Mbunge mmoja. Inawezekana mikoa mingine ina Wabunge wa Viti Maalum saba. Ndiyo maana nimesema jambo hili linatakiwa ifanyike needs assessment kwa ujumla wake kupata maamuzi kama Taifa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS,TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Dada yangu Faida Bakar kuna sehemu ya pili alisema Wabunge wanatumia fedha zao. Naomba niwaambie hasa na Wabunge wa Majimbo, fedha za Mfuko wa Jimbo siyo fedha za kwenda kugawa kama zawadi. Fedha za Mfuko wa Jimbo zinapita katika akaunti maalum na zina Wajumbe maalum akiwepo Afisa Mipango ni Katibu wa Mfuko wa Jimbo, fedha ile inaingia mara moja kwa mwaka na Kamati inafanya maamuzi kutekeleza miradi, fedha ile siyo fedha ya kuingia mfukoni kwa mtu kwenda kutoa sadaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, niwatahadharishe Wabunge wa Majimbo kwamba mfahamu fedha hii inakwenda kujibu matatizo ya wananchi. Mlivyopita kuna mahitaji mbalimbali wananchi wameibua sasa katika vikao vyenu mnafanya maamuzi kwenda kujibu matatizo.(Makofi)
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Kwanza napenda kuishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kusikia kilio cha askari wetu wa Tanzania, wakiwemo askari wa kule Pemba kwa kuwatengea bajeti kwa mwaka 2018/2019 ya kuwajengea nyumba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imekiri na kukubali na kuweka ahadi kwamba itatenga bajeti hiyo ya kuwajengea askari wa Zanzibar nyumba. Je, Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba bajeti hiyo ikitengwa na nyumba hizo zitakapoanza kujengwa kipaumbele kipewe kwa askari wetu wa Mkoa wa Kusini Pemba? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Faida Bakar, kwa kweli ni balozi wa askari wote hapa nchini kwa kuwasemea vizuri sana kuhusu mahitaji yanayowahusu kwenye mahitaji yao na Waheshimiwa wengine wanaokuwepo kwenye Kamati inayosimamia mambo ya ndani akiwemo Mheshimiwa Masoud.
Mheshimiwa Spika, nakubaliana tutaweka kipaumbele hicho cha askari walioko Pemba na mimi nilishafika kwa kweli mazingira yao ni magumu ya kufanyia kazi kwa kukosa nyumba. (Makofi)
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, napenda kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kuwajengea wanajeshi kituo kizuri cha afya pale Ali Khamis Camp Jimbo la Wawi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa vitu vingi vya afya vinavyomilikiwa na Jeshi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hakuna majokofu ya kuhifadhia maiti, hata kwa Askari wenyewe pale wanapofariki kwa sababu wengine wanakaa mbali sana na maeneo ya mikoa yao. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka majokofu katika vituo tofauti vya Afya vya Jeshi ili Askari wenyewe wanapofariki waweze kuhifadhiwa vizuri?Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba kuna umuhimu wa kuwa na majokofu ya kuhifadhia maiti katika vituo vyetu vya Jeshi, kwa sababu vingi sasa hivi vinatoa huduma ya rufaa na bila shaka ni muhimu kuwa na majokofu hayo endapo itatokea vifo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi, ni kwamba lazima twende kwa awamu. Tunaanza kwenye vituo vikubwa na kazi hii tumeshaifanya pale Lugalo ni matarajio yetu kwamba kila fedha zitakapokuwa zinapatikana, basi huduma hii tutaiendeleza katika vituo vya chini. Kwa hiyo, nataka nimtoe hofu, jambo hili tunalijua na tutalifanyia kazi ili hatimaye vituo hivyo vipate majokofu ya kuhifadhia maiti.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali inafanya kazi kama timu moja, kwa nini marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 isibadilishwe ili itambue Mahakama ya Kadhi kama chombo cha kuamua hatima ya ndoa za kiislamu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa hili la Mahakama ya Kadhi nitaomba Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali anisaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sehemu ya kwanza ya swali lake, ufafanuzi ni kwamba Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kile kifungu cha 13 na 14 kwa kiasi kikubwa vinahusu mambo ya nodal, hususan vinaruhusu mtoto mwenye miaka 14 kuolewa kwa sababu mbalimbali ambazo nitazitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi sheria ile ilitungwa katika zama ambapo mila na desturi za baadhi ya makabila yaliyopo katika nchi yetu zikizingatiwa. Pia sheria ile ilitungwa kwa kuzingatia pia misingi ya dini mbalimbali ikiwemo dini ya kiislamu ambapo katika imani hiyo inaruhusiwa mtoto kuolewa ama kuoa tu pindi anapobalehe ama anapovunja ungo. Kwa hiyo, haya ni mambo ambayo kama Serikali tunahitaji kuyachukua kwa utaratibu sana kwa sababu yanahusu imani, yanahusu mila na desturi za watu wetu na hivyo lazima ipatikane consensus ya kitaifa kabla hatujafanya uamuzi wowote wa mabadiliko ya suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Serikali ipo wazi na taratibu kadri tunavyojifunza kwa wenzetu kama nchi ya Kiislam ya Bangladesh, nasi tutaona ni njia ipi muafaka tuweze kupitia. (Makofi)
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini kuna kitu amekiongelea, amesema kutibu. Mimi ninavyoona kinga ni bora kuliko tiba; na kwa kuwa Serikali inawatibu vijana hawa baada ya kuathirika lakini ni bora ingewakinga wasiathirike. Je, Serikali itachukua hatua gani za haraka au madhubuti za kuwakinga vijana wake wasitumie madawa ya kulevya badala ya kuwapeleka kwenye sober house wakati wameshaathirika na kuwatibu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa scanning machine katika maeneo mbalimbali ni muhimu sana katika maeneo kama airport, bandarini na sehemu nyingine zozote. Hata hivyo, kuna maeneo mengine kama kule kwetu Pemba, juzi nimesafiri kuja huku scanning machine yake haifanyi kazi na sehemu hizi ndizo wanazopitisha vitu vyao watu hawa wabaya.
Je, Serikali itachukua hatua gani kuwanunulia mashine nyingine pale airport ya Pemba ama kuwatengenezea ile mashine ili kuepukana na matatizo haya ya kusafirisha madawa haya ya kulevya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge ni kweli, kinga ni bora zaidi. Katika utaratibu wa kushughulikia masuala ya dawa za kulevya, hatua ambazo Serikali imezichukua zipo katika mgawanyo wa sehemu tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya kwanza tunaiita ni supply reduction, ni punguzaji wa upatikanaji wa dawa za kulevya ikiwa ndiyo sehemu ya kwanza kusaidia kumfanya
kijana huyu au mtu yeyote asipate madawa ya kulevya. Ni dhahiri kabisa kwamba baada ya Mamlaka ya Dawa za Kulevya kuanza kazi yake, kuanzia Januari mpaka Desemba, 2017 ninavyozungumza hivi sasa tayari wamefanyakazi kubwa ya kuzuia upatikanaji wa madawa ya kulevya.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa takribani kilo 196 za heroin zilikamatwa lakini takribani tani 47 za bangi zilikamatwa, tani 7 za Mirungi zilikamatwa na mashamba ya bangi hekari 542 yaliteketezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ukiyafanya haya sasa, yanasaidia kupunguza upatikanaji wa dawa za kulevya huko mtaani. Kwa hiyo, kazi ya kwanza Serikali inayofanya ni hiyo ya kusaidia hiyo kitu inaitwa supply reduction.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha pili tunachokifanya ni demand reduction, tunapunguza pia uhitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ya tatu ni harm reduction. Harm reduction sasa huyu ameshatumia dawa za kulevya hatuwezi kumuacha hivyo hivyo ndiyo maana sasa tunakuja na tiba lakini vilevile kumsaidia mtu huyu aweze kurudi katika hali yake ya kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa ninavyozungumza mamlaka imefanya kazi yake vizuri sana, hata katika uagizaji wa methadone hapa nchini tumetoka katika kiwango cha kawaida cha kilo 120 mpaka kilo 300, maana yake nini? Maana yake ni kwamba dawa za kulevya sasa hivi mtaani hazipatikani, kwa hiyo, hawa waathirika wanapata tabu kubwa ndiyo maana wanakwenda kutibiwa katika vituo vyetu ambavyo tumeviweka kwa ajili ya kuwatibu waraibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali inalitambua hilo na ndiyo maana tumekuja na hiyo mikakati tofauti tofauti kuhakikisha kwamba dawa za kulevya hazipatikani na tunawalinda vijana wetu.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napenda kuongezea kwenye swali la pili la Mheshimiwa Faida Bakar kwamba kwa mujibu wa taarifa tulizonazo kutoka Zanzibar Airport Authority (ZAA), scanner ya Pemba inafanya kazi vizuri kabisa na inafuatiliwa kila siku na kila wakati. Scanners zote za viwanja vyetu vya ndege tunazifuatilia mara kwa mara, ahsante sana.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu yote yaliyotolewa na Naibu Mawaziri kuhusu suala hili, tunatambua umuhimu mkubwa wa kuhakikisha viwanja vyetu vyote vya ndege scanner zinafanya kazi na hizo ndizo zinazoweza kutusaidia kudhibiti tatizo la uingizaji wa dawa za kulevya.
Kwa hiyo, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge kama kuna tatizo kwenye scanner ya Zanzibar basi tutafanya utafiti wa kina ili ndani ya Serikali tuzungumze ili scanner hiyo iweze kufanya kazi na tuweze kuendelea kudhibiti tatizo hilo la dawa za kulevya. (Makofi)
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa katika uanzishwaji wa Benki hii ya Wanawake wa Tanzania, Wabunge wengi hususan Wanawake wakati ule walichangia mtaji ama fedha katika benki hii. Hata hivyo, Wabunge hao na wengine sasa hivi siyo Wabunge tena, hawajapewa hata shukrani hata ya kutambulika tu, hata shukurani hawajapewa. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, Wabunge hao wa wakati ule watapatiwa lini barua hiyo ya utambulisho na hata kupatiwa hisa zao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa katika majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kuwa uadilifu hapa hapana na kwamba wanataka kuteua tena Watendaji ama Maafisa mbalimbali ambao watakuwa waadilifu, ndiyo sasa imedhihirika kwamba, watendaji wa hii benki hawana uadilifu watendaji wake ndiyo maana ikafikia hapa ilipofikia. Je, uongozi na watumishi hao ambao si waadilifu wamechukuliwa hatua gani za kisheria? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Dada yangu Mheshimiwa Faida Bakar kwa kazi nzuri sana ya kufuatilia masuala ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, sio tu Zanzibar lakini pia Tanzania Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na swali lake la pili, hawa watumishi ambao wamekosa uadilifu wamechuliwa hatua gani. Kuanzia mwezi wa Agosti mwaka 2017 tumewapeleka katika vyombo vya usalama ikiwemo TAKUKURU na Polisi, Watumishi zaidi ya 20 akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji Magreth Chacha, kwa kukosa uaminifu na hivyo kusababisha benki kukosa hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni benki kupata hasara, Kiswahili kidogo kimepiga chenga. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo yamefanyika ya hovyo unakuta kuna SACCOS inakopeshwa shilingi bilioni moja, tunaifuatilia hiyo SACCOS haionekani hizo fedha zimeenda kwa nani. Kwa hiyo, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Faida kwamba tunaamini PCCB na Polisi watakamilisha uchunguzi haraka na lengo letu watumishi hawa ambao hawakuwa waaminifu waweze kwenye mbele ya vyombo vya dola na kuchukuliwa hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa nataka kumthibitishia Mheshimiwa Faida kwamba, Serikali imedhamiria kuhakikisha tunapata fedha ya kukuza mtaji wa benki, tumepewa miezi sita na BOT na nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge kwamba, Mkurugenzi mpya ambaye tumemwajiri amefanya kazi kubwa, niseme ingawa ni Benki ya Wanawake lakini tumeajiri Mkurugenzi mwanaume ambaye ndani ya miezi mitano amefanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba angalau hesabu za benki zinakaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, lilikuwa ni suala la hisa, tunatambua mchango mkuwa sana wa Wabunge wa Bunge la Tisa ambao waliweza kununua hisa kwa ajili ya kuhakikisha mtaji wa benki unakua na moja ya jambo ambalo limekwama ni lile la BOT kwamba lazima tuweke vizuri suala la shareholders, halafu ndiyo tutawapa certificate zao za hisa. Kwa hiyo, suala hili pia tutalikamilisha ndani ya siku chache. Nakushukuru sana.
MHE. FAIDA MOHAMED. BAKAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuuliza maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu hapa kwamba maji yanatosheleza kulingana na ujazo uliopo, lakini cha kushangaza ni kwamba maji hayo hasa vijijini hayapatikani kwa ukamilifu.
Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuyasambaza hayo maji anayosema yapo, maana kuwepo tu ardhini na juu ya ardhi si sababu ya kuyasambaza maji hayo ili yawafikie wananchi na kuwapunguzia matatizo hususani wanawake? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa maji ya baharini tunayaona, hasa mvua ikinyesha maji ya mvua yanaelekea baharini, mwisho wake ni baharini. Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga mabwawa yaliyo mengi katika nchi yetu kila eneo ili kuyahifadhi maji hayo kwa matumizi ya wananchi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ni kwamba kweli kuna kiwango kikubwa cha maji hapa nchini, lakini yapo maeneo hapa nchini ambayo hayana maji. Hilo ni kweli kabisa kwamba yapo maeneo na ndiyo maana Serikali kuanzia bajeti ya mwaka 2006/2007 ilianzisha Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Malengo yake ni kuhakikisha kwamba tumeyachukua haya maji na kuyafikisha maeneo ambayo yana ukame. Programu hiyo imeenda mpaka Juni mwaka 2015, na sasa hivi tumeingia kwenye awamu ya pili.
Mheshimiwa Spika, lakini matokeo ya programu hiyo ni nini? Tayari tumesaini mikataba ya kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka Shinyanga na sasa hivi tumesaini mkataba mwingine tunatoa Shinyanga kupeleka Nzega, Tabora hadi Igunga. Hiyo ndiyo tunaendelea utekelezaji wa kuichukua sasa hiyo hazina ya maji iliyopo ili tuweze kuyasambaza kwa wananchi, na tunapoyapeleka tunapita kwenye vijiji mbalimbali vingi kuhakikisha wananchi wanapata maji.
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kweli mvua zinanyesha ni nyingi katika nchi yetu na maji haya yanapotea yanakwenda baharini, tunafanyeje? Tayari tumeshatengeneza utaratibu, tumeagiza kila Halmashauri kila mwaka kwenye bajeti zao watenge fedha ili kuhakikisha wanavuna maji. Si hilo tu, ni kwamba kwenye maeneo ambayo Halmashauri wanahitaji hayo maji kwa ajili ya wananchi kupata maji safi na salama, Wizara ya Maji na Umwagiliaji pia tunatoa fedha kwa ajili ya kujenga hayo mabwawa madogo na ya kati. Pia tunaendelea sasa kujenga mabwawa makubwa ya kimkakati ambayo yatazalisha umeme wakati huo huo tutapata maji kwa ajili ya umwagiliaji na tutapata maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu. (Makofi)
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hili tatizo la udhalilishaji wa watoto sasa hivi limekuwa ni sugu ama ni donda ndugu yaani ni zaidi ya kila kitu na sisi wazazi inatuuma sana. Unaweza ukamuona mtoto anatoka mafunza mwanamume anamdhalilisha mtoto mchanga, hii iko sana kule kwetu Zanzibar, inauma sana maana hata wazazi wenyewe wengine wanawaingilia watoto wao. Je, Serikali inatoa kauli gani kwa watu kama hao wanaofanya udhalilishaji wa watoto wetu hasa ikizingatiwa kwamba wakifanyiwa tatizo hilo wanaficha na wanamalizana wenyewe kule nyumbani hawapeleki taarifa kunakohusika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Faida Bakar ambalo amelielezea kwa hisia kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria na Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008, mtoto ana haki zake tano na naomba nizinukuu kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge. Mtoto ana haki ya kuishi; kulindwa; kuendelezwa; kushirikishwa na kutobaguliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambasamba na hilo, Serikali inakemea sana udhalilishaji wowote wa kijinsia dhidi ya mtoto. Ndiyo maana tumesema kwamba tumeweka mkakati wa kiserikali wa mwaka 2017/2018 ambao utaisha 2020/2021 na lengo na kusudio ni kuhakikisha kwamba tunatokomeza kabisa ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimetoka kusema kwamba udhalilishaji mwingi unafanyika katika ngazi ya familia. Naomba nitoe rai kwetu sisi Wabunge wote na jamii yote ambayo inaendelea kutusikiliza, tusiyafumbie macho matukio na udhalilishaji wowote dhidi ya wanawake na watoto na sisi kama Serikali tutaendelea kushirikiana na jamii kuchukua hatua za haraka kwa wote wanaofanya matukio kama haya.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri niko na maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa hizi sheria naona kama zitakuwa zimepitwa na wakati; na kwa kuwa Mheshimiwa Rais wetu amekuwa mfano mzuri wa kuhamasisha utumiaji wa lugha ya Kiswahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni je, Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami kwamba sasa umefika wakati muafaka wa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa matumizi ya Kiswahili katika Mahakama, katika kuandika maamuzi yake kwa lugha hii ya Kiswahili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa hata hapa Bungeni unaletewa hii Miswada hii unaiona hii kwa lugha ya Kiingereza, hii ni Tanzania tunaletewa Miswada kwa lugha ya Kiingereza na humu Bungeni kuna watu tofauti na elimu zetu tofauti, watu wanaweza wakajadili wakawa hawapati muafaka mzuri kwa sababu hawaelewi hii lugha iliyomo katika Miswaada mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana nami sasa kwamba ni wakati muafaka katika nchi yetu ya Tanzania tutumie lugha yetu ya Kiswahili, Lugha ya Taifa katika Mahakama na katika Mabunge na katika sehemu zote? Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika majibu ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameshayatoa. Kuhusiana na lile suala la kwanza la kuendesha mashitaka kwa Kiswahili halafu hukumu zinatolewa kwa lugha ya Kiingereza ametoa maelezo ya kutosha na nafasi ipo kwamba kama mashtaka yanaendeshwa Hakimu au Jaji anaweza kuruhusu yaendelee kwa Kiswahili au kwa Kiingereza; na sababu nadhani amezitoa za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuhusu Miswada na pengine sheria kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili hilo lipo katika mpango wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanza na kutafsiri karibu sheria zote ziwe na zisomeke kwa lugha ya Kiswahili kwa sababu ndiyo lugha inayozungumzwa na kueleweka na watu wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, suala hili linahitaji rasilimali na tuna changamoto kidogo za rasilimali lakini pia hata utaalam wa kutosha kwa sababu kuna hatari, sheria ina lugha yake unapoitafsiri tu moja kwa moja kwenda Kiswahili kuna hatari kubwa pia ya kupoteza mantiki iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuna changamoto pia ya kuwa na wataalam wanaoweza kutufanyia kazi hii kwa usahihi. Hata hivyo, hilo ni kati ya mambo ambayo tumeyawekea mipango tuanze kuyafanyia kazi sheria zote ziandikwe kwa Kiswahili. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.