Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng. Ramo Matala Makani (1 total)

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza majibu mazuri ya Serikali kwa swali hili. Lakini pamoja na pongezi zangu hizo naomba kuwasilisha maswali yangu mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwanza takwimu zilizosomwa kwa ufupi zinaonesha kwamba kwa wastani uchangiaji wa mazao katika sekta ndogo hizo za kilimo, misitu na uvuvi ni 26.1%. Lakini pia wastani wa fedha za kigeni katika miaka hiyo mitano ni dola za Kimarekani milioni 864.68.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Taifa letu limepanda treni ya mwendo kasi inaitwa viwanda kwa ajili ya kukamilisha safari yake kuelekea uchumi wa kati inaonekana wazi kabisa, ushahidi upo unaoonesha kabisa juu ya umuhimu wa sekta hii ya kilimo, lakini mahususi kabisa mazao yale matano yaliyotajwa yaani tumbaku, korosho, kahawa, pamba na chai.
Mheshimiwa Mwenyeki, sasa maswali yangu ya nyongeza yatajikita zaidi kwa korosho kwa leo na nikisema kwamba swali la kwanza, kwa kuwa sasa tunataka mazao haya yachangie zaidi uchumi na kuongeza kasi hiyo yakufikia malengo ya Taifa ya kiuchumi. Je, Serikali inajipanga namna gani kuondoa vikwazo, kuondoa hali yoyote ile ambayo inawafanya wakulima washindwe kuzalisha zaidi? Kwa mfano kwa sasa hivi kule Tunduru wananchi wanapata matatizo ya upatikanaji…
Ndiyo, Serikali itaboresha namna gani utaratibu wa kibenki, unaowafanya Wananchi wa Wilaya ya Tunduru wapate shida katika kupata fedha zao baada ya kuuza mazao ya korosho miezi kadhaa iliyopita waondokane na misururu mirefu lakini pia na kusafiri kilometa nyingi zinafikia 120 na kukaa Makao Makuu ya Wilaya kwa siku mbili mpaka tatu? Hilo ni swali la kwanza.
Swali la pili linausiana na suala la pembejeo, upande wa pembejeo ningependa kuzungumzia ubora wa pembejeo zenyewe, lakini pia ningependa kuzungumzia upatikanaji kwa wakati wa pembejeo zenyewe, lakini pia bei ya pembejeo zenyewe. Kwa ujumla Serikali inajipanga namna gani katika kuhakikisha kwamba wananchi hawa wa Tunduru hasa wa zao la korosho, ni wa mazao yote lakini hususani wa zao la korosho kwa leo ili waweze kupata pembejeo hasa mbolea na madawa ya kuweza kuboresha, kilimo na hasa mazao ya ya korosho upande wa sulphur?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaifahamu changamoto hiyo ya wananchi wetu na hasa wakulima wetu wa kule Tunduru kwenda kupanga foleni katika mabenki yetu na hili hata Mheshimiwa Naibu Waziri wa Viwanda tarehe 10 Januari aliwasiliana na mimi akiwa Masasi, akiwa kwenye foleni na wananchi hao kwa ajili ya kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kwamba kama ambavyo nimekuwa nikiliambia Bunge lako Tukufu kuanzia mwaka 1991 tuliingia katika soko uria kuhusu sekta ya kifedha na mabenki nchini. Lakini pia, mabenki yetu kwenda kufungua matawi maeneo mbalimbali huwa inahitaji kuangalia nguvu ya soko (demand and supply) katika hilo, maana na wao ni wafanyabiashara wanahitaji kupata faida wanapofungua matawi yao.
Ninafahamu kuhusu wakulima wetu wa korosho kule Tunduru na Mtwara kwa ujumla na Wilaya zake na zao hili ni la msimu kwa hiyo kunakuwa na wateja wa msimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokifanya kama Wizara ya Fedha kwa sasa ni kuongea na mabenki yetu kuona jinsi gani watafikisha huduma za mawakala (Agent Banking) au waweze kutumia Mobile Banking katika kuwahudumia Wananchi wetu wa maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili Serikali inatambua umuhimu wa mazao yote kwa ujumla na particular mazao haya matano niliyoyasema na ndiyo maana Serikali mwaka 2013 ilikuja na Regulatory Authority ambayo ni TFRA inayoshughulika na pembejeo za wakulima wetu. Tunaendelea kuimarisha wakala huu ili uweze kufanya kazi nzuri kuhakikisha wananchi wetu wanapata pembejeo wanazozihitaji hasa katika ubora na bei ambayo wanaweza kuihimili kuinunua.