Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Felister Aloyce Bura (21 total)

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mgogoro uliopo kati ya Wananchi wa Buger na Hifadhi ya Taifa ya Manyara ni sawasawa na mgogoro uliopo kati ya Hifadhi ya Mkungunero na wananchi wa vijiji 11 vya Wilaya ya Kondoa. Katika mgogoro huo wananchi wameuawa, Askari wa Hifadhi ya Mkungunero wamekufa na mgogoro huu ni wa muda mrefu na tumeiomba Serikali washughulikie mgogoro huo na wananchi wanaomba kilometa 50 tu ili mgogoro umalizike.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mawaziri waliopita wametembelea na wamefanya mikutano na wananchi wa vijiji 11 wa Wilaya ya Kondoa pamoja na Chemba. Je, Mheshimiwa Waziri ni lini mgogoro wa wananchi wa Wilaya ya Kondoa, vijiji 11 utaisha kati ya Hifadhi ya Mkungunero na wananchi hao?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la nyongeza kuhusu Mbuga ya Mkungunero. Wizara yangu pamoja na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, imeandaa mpango wa kupima maeneo yote ambayo yana mgogoro kati ya wananchi na Hifadhi za Taifa ili kufanya juhudi za kutatua matatizo haya moja kwa moja.
Mh
MHE. FELISTER A BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Dodoma ilijengwa mwaka 1923 na ilipojengwa ilikuwa na wakazi wasiozidi elfu hamsini lakini kwa sasa Dodoma ina wakazi takribani laki sita na majengo yako vilevile wala hayajaongezeka. Bima ya Afya waliamua kujenga jengo kwa ajili ya kupunguza wingi wa watu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambalo lina miaka mingi halijakamilika, limekabidhiwa lakini hakuna samani ndani yake.
MWENYEKITI: Uliza swali sasa.
MHE. FELISTER A. BURA: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuishawishi Bima ya Afya ambayo ipo chini ya Wizara yake kuleta samani na kukamilisha jengo lile ili lianze kutumika kwa wagonjwa wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Bura kwa swali lake la nyongeza. Sisi hatuna shida na kuishawishi taasisi ya NHIF kuwakopesha Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, lakini ukweli utabaki palepale, narudia tena ukweli utabaki palepale kwamba hospitali hizi za mikoa zipo chini ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Naomba Waheshimiwa Wabunge tunapohudhuria vikao vya RCC tuikumbuke sekta ya afya kwa kushawishi bajeti maalum za mikoa na hata bajeti za kawaida za mikoa kwa kiasi kikubwa zielekezwe kwenye kuboresha hospitali zetu ikiwa ni pamoja na utanuzi wa majengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia suala la mikopo NHIF ni suala la kibiashara zaidi. Kama hospitali husika ina makusanyo na vigezo vinavyotosha kuwezesha kupata pesa kwa mkopo kutoka NHIF basi uongozi wa hospitali husika utafanya mazungumzo ya kibiashara ambayo yana faida kwa pande zote mbili baina ya wao wenyewe. Hili wala siyo suala la sisi kama Wizara kwenda kuishawishi NHIF kwa sababu mambo haya yanahusu fedha na fedha zinataratibu zake.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwa kuwa barabara hii ni sehemu ya Great North Road iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu na Watanzania; na kwa kuwa ni sehemu ya Tanzania tu ambayo haijakamilika mpaka sasa; na kwa kuwa baadhi ya Wakandarasi wanasuasua; kazi zimesimama kwa baadhi ya maeneo; je, Serikali inatuhakikishiaje Watanzania kwamba barabara hii itakamilika kwa wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Mheshimiwa Rais wakati akiwa Waziri wa Ujenzi katika Mkutano wa Wadau uliofanyika Saint Gaspar aliwaahidi Wanadodoma kwamba atajenga ring roads ili magari yanayotoka mikoa mbalimbali yaishie nje ya Mji kupunguza msongamano wa magari; je, ni lini upembuzi yakinifu utaanza kwa ajili ya kujenga barabara hizo za ring roads?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kuhusiana na kipande kilichobakia cha Msalato na vipande vichache vilivyobaki vya kukamilisha hii barabara ya North Great Road, kwa vyovyote vile muda si mrefu barabara hii itakuwa imekamilika na naomba kumhakikishia hilo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la ring roads, aliyeahidi ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Ujenzi, hivi sasa ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, labda tu nimjulishe; hapa nina ramani nitamwonesha, labda kwa niaba ya wengine, hasa Waandishi wa Habari... (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, tayari tuna mpango mkubwa kabambe wa kujenga za ring roads ndani na nje ya Manispaa ya Dodoma katika kipindi cha miaka mia moja ijayo. Mpango huu utatekelezwa kwa kadiri mahitaji yanavyokuja. Barabara ambazo tunazo hapa za miaka mia moja ijayo, ziko barabara nane kubwa na jumla yake ni Kilometa 147.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali
la nyongeza.
Pamoja na njaa iliyowakumba wananchi wa Mpwapwa, Kongwa, Bahi, Chemba,
Kondoa na maeneo mengine ya ukame katika Mkoa wa Dodoma, lakini mvua iliyonyesha na
inayoendelea kunyesha imeleta mafuriko makubwa kwa baadhi ya vijiji na vyakula ambavyo
wananchi walikuwa navyo vimesombwa na maji, mahitaji ya ndani, magodoro, vitanda,
vyombo vimesombwa na maji.
Je, Serikali iko tayari kuwasaidia wananchi hao kwa kushirikiana na Wabunge?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, VIJANA, AJIRA NA WALEMAVU:
Mheshimiwa Spika, nchi yetu imekumbwa na mabadiliko ya tabianchi na kusababisha majanga
ya mafuriko katika maeneo tofauti katika nchi yetu ya Tanzania. Sisi wenyewe kama Serikali
tumekuwa tukitembelea maeneo hayo nakuona madhara yaliyopatikana.
Mheshimiwa Spika, inawezekana tukaweza kufanyakazi ya kuwasaidia Watanzania kwa
namna ile ambayo Serikali ina uwezo kwa sasa. Kwa hivyo, naomba niwahakikishie
Waheshimiwa Wabunge, tutajitahidi kuendelea kufanya tathmini na kuona tunafanya nini
kutoka eneo moja hadi jingine, lakini ninaziomba kamati za maafa kwenye ngazi ya Kata, ngazi
ya Wilaya, ngazi ya Mkoa kuona yale yanayoweza kufanyika ndani ya uwezo wao, na
yanayoshindikana wayalete Serikalini ili tuweze kushirikiana kwa pamoja.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini pamoja na majibu hayo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa vijana ndio nguvu kazi ya Taifa hili na kwa kuwa vyuo vikuu vinazalisha vijana asubuhi na jioni wenye elimu nzuri ya kufanya ujasiriamali, lakini tatizo ni wapi watapata mikopo kwa njia rahisi zaidi na kwa riba nafuu zaidi? Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia hawa vijana kupata mikopo kwa urahisi na kwa riba nafuu zaidi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa ajira ambayo ni rahisi kwa vijana na hasa kwa wanawake pia ni kilimo; lakini kilimo kinacholimwa kwa sasa hakina tija; kwanza, masoko hayapo kwa urahisi, mazao mengine yanaoza mashambani; lakini la pili, maeneo ya kulima. Vijiji vingi havijatenga maeneo kwa ajili ya kilimo kwa vijana na hata kwa wanawake ambao wameshajiunga kwenye vikundi mbalimbali. Je, Serikali iko tayari kutenga maeneo na kuzihimiza Halmashauri zetu kutenga maeneo kwa ajili ya vijana na hata kwa wanawake ambao wako tayari kuwa wajasiriamali kupitia kilimo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na la kwanza la mikopo na mitaji kwa wahitimu wa elimu ya vyuo vikuu na elimu ya juu, ni kweli natambua kwamba vijana wengi sasa hivi wanapenda kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali hasa kilimo, lakini changamoto kubwa wanayokutana nayo ni ukosefu wa mitaji na mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeliangalia hili kwa macho mawili na katika mtazamo wa mbali kuhakikisha kwamba vijana hawa wanapata fursa ya mikopo na mitaji kwanza kabisa kupitia Mfuko wetu wa Maendeleo ya Vijana ambao umekuwa ukikopesha makundi mengi ya vijana kupitia SACCOS ambazo ziko katika Halmashauri zetu. Vilevile tumeendelea kuwa na msisitizo kwa kuwataka vijana hawa wajiunge katika makampuni na vikundi mbalimbali ili waweze kupata fursa ambazo zinatokana na mikopo na mitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunayo program maalum sasa hivi kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi, ambapo tuna program ya Kijana Jiajiri inahusisha young graduates, wanaandika proposals zao wanazi-submit katika baraza na baadaye wanapatiwa mikopo na mitaji. Pia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi imezungumza kuhusu kuwawezesha vijana wakae katika vikundi na makampuni kutumia fani zao na taaluma zao mbalimbali ili waweze kukopesheka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu rai kwa vijana wote wale wa vyuo vikuu na wahitimu wa elimu ya juu kutumia fursa hii ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na mikopo inayopita katika Halmashauri zetu kwa kukaa katika vikundi na makampuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, limeulizwa swali kwamba Serikali ina nia gani ya kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za kilimo? Mwaka 2014, Wizara yetu ilikutana na Wakuu wa Mikoa wote nchi nzima hapa Dodoma na likatengenezwa azimio, ambapo moja kati ya kilichoamuliwa ni kutengeneza kitu kinaitwa Youth Special Economic Zone, ni ukanda maalum ambao utakuwa unasaidia utengaji wa maeneo kwa ajili ya shughuli za vijana. Mpaka sasa tayari ekari 8000 zimeshatengwa nchi nzima kwa ajili ya maeneo haya ili vijana waweze kufanya shughuli za kilimo na biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumezungumza na Waziri wa Kilimo, yako mashamba makubwa ya Serikali ambayo wanayafanyia utaratibu sasa hivi nayo tuweze kuyatenga kwa ajili ya kuwagawia vijana waweze kufanya shughuli za uzalishaji mali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya yetu ya Kondoa haina ultra sound na kuna Kata zaidi ya 30, lakini wanawake wanapopata shida, wanaletwa Dodoma Mjini. Kituo cha Afya cha Chamwino lkulu, kiko katika geti la Ikulu pale Chamwino hakina ultra sound, na wanawake wanatoka kilometa 50, 80, 90 wakija Dodoma Mjini,kwa ajili ya matibabu.
Je, Serikali iko tayari sasa kuongea na Bima ya Afya ili tupate mkopo huo wa shilingi milioni 72 kwa haraka?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali iko tayari kuisaidia Hospitali ya Kondoa, ambayo pia haina kifaa tiba hicho; na wanawake wengi wa Kondoa, wanabebwa kilometa 150 kuja Dodoma Mjini kwa ajili ya ultra sound. Je, wako tayari kuisaidia hospitali hii ya Kondoa wakapata kifaa hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tarehe 24 Februari katika ziara yangu katika Wilaya ya Chamwino niliweza kufika Chamwino soko la Bwigiri na kuangalia ujenzi wa Halmashauri ya Chamwino. Nilipofika pale kweli nilitembelea majengo yote na kuangalia kituo cha afya kile kikoje, na kwakweli na mimi sikuridhika, ndiyo maana nikatoa maelekezo siku ile ile, kwamba kinachotakiwa sasa tuangalie jinsi gani kituo kile kitapata ultra sound. Na bahati mbaya wakati ule bajeti ilikuwa haijaanza, na niliwaelekeza kwamba ikiwezekana waangalie kupitia mfuko wa Bima ya Afya, hali kadhalika katika mpango wao wa bajeti. Lakini kwa bahati mbaya kutokana na ukomo wa bajeti walishindwa kungiza katika bajeti yao.
Mheshimia Naibu Spika, lakini hata hivyo katika maagizo yangu niliyoyatoa nimshukuru sana DMO wa Chamwino na timu yake ya Mkurugenzi kwamba waliweza kufanya utaratibu wa kuwahusisha wenzetu wa NHIF. Na mchakato huu upo mbioni na mimi nina imani kwamba ombi lako Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko tayari, ni kwamba tulishakuwa tayari ndiyo maana nikaagiza. Kwa hiyo, jukumu letu kubwa ni kuendelea kupambana ili wenzetu wa NHIF waweze kusaidia Kituo cha Afya Chamwino.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala zima la Kondoa; ni kweli kutoka Kondoa mpaka hapa ni mbali; na pale ultra sound hakuna, kama Serikali tumeliona hili. Lakini vilevile naomba nisisitize jambo hili jamani; kwamba mambo haya wakati mwingine yote lazima yaanze katika mchakato wetu wa bajeti. Kama bajeti katika vipaumbele inawezekana hatukuweka ultra sound inaonekana kwamba sisi wenyewe tumedhulumu vityo hivyo. Kwa hiyo, jukumu langu kubwa mimi ni kuwasisitiza ndugu zangu Wabunge, tunapoweka katika mchkato wa bajeti tuangalie kipi kipaumbele cha zaidi? Tupunguze yale mambo mengine ambayo hayana maana tuweke katika sehemu ambayo moja kwa moja tunaenda kumsaidia mama na mtoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama Serikali tumelisikia hili na kwamba tutawahusisha wenzetu wa NHIF ili kama itawezekana waangalie ni jinsi gani waipe kipaumbele Hospitali ya Kondoa. Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kuwa Mheshimiwa Mbunge yuko makini katika hili, najua tutashirikiana na wenzetu wa NHIF. Na siku ile alizungumza pale katika Hospitali yetu ya General, wenzetu watalisikia hili watatupa kipaumbele pale Kondoa.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wangu wa Shabiby round about, Arusha Road walifanyiwa tathmini mwaka 2006 na waliambiwa wakati wowote Serikali itabomoa nyumba zao na kujenga barabara pale lakini mpaka leo wananchi hawa hawajalipwa na huu ni mwaka wa 10 hata choo kikibomoka hawajengi. Naomba Waziri aniambie, ni lini wale watu watalipwa fidia zao halali kwa maana zinazostahili kwa leo ili waondoke?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILANO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba umenizuia kusema yale yaliyopo ndani ya roho yangu lakini naomba uniruhusu, unafahamu fika Mheshimiwa Felister Bura…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, ni kwa sababu muda wetu ni mfupi ndiyo maana nimekusaidia kuwatangazia wote kwamba sifa zile zinamwendea kila Mbunge hapa ndani ili wewe uendelee tu kujibu maswali. (Kicheko/Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa juhudi za Mheshimiwa Felister Bura, hivi sasa tunaendelea kukamilisha kilomita nane za lami eneo la Msalato na kwa juhudi zake hizo hizo namhakikishia tutaendelea kuhakikisha tunawalipa fidia hawa watu ambao wanahusika katika hilo eneo. Kama ambavyo nilijibu awali, hakuna sababu ya kufanya tathmini upya badala yake ile formula ya kuongeza riba ndiyo inayotumika na hawa watu watalipwa haki yao bila matatizo yoyote mara fedha zitakapopatikana.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, sisi suala la Pori la Mukungunero ni tofauti na maeneo mengine kwa sababu mauaji yamekwishatokea, maaskari watatu walikwishauawa pale, wananchi walishaandika barua mpaka kwa Waziri Mkuu na Waziri Mkuu akapeleka suala hili Wizara ya Maliasili lakini tangu mwaka 2013 suala la Mukungunero halijashughulikiwa. Naomba suala la Mkungunero sasa litazamwe kwa jicho lingine la haraka. Je, ni lini sasa Wizara ya Maliasili itaishughulikia barua iliyoandikwa kwao na Waziri Mkuu aliyepita?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, jibu fupi kabisa, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge swali lake la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa maelezo aliyoyatoa ni wazi kwamba suala hili la Mkungunero, kwa jinsi swali lilivyoulizwa na uhalisia ulivyo lina upekee kama ambavyo na yeye ameweza kubainisha. Kwa hiyo, ushughulikiaji wa suala hili ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii unavuka mipaka, unahusisha masuala yanayohusiana na Wizara ya Mambo ya Ndani. Hapo unahusisha polisi na mambo mengine ya utendaji wa Kiserikali lakini nje ya mipaka ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Hata hivyo, kwa sababu ni suala linalohusiana na Wizara ya Maliasili na Utalii basi tutakwenda kuona namna ambavyo tunashirikiana na vyombo vingine ambavyo vinahusika katika kuweka msukumo kukamilisha ushughulikiaji wa changamoto hii.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa lengo la Serikali la kuanzisha benki hii ni kuwasaidia wanawake wanyonge waliopo vijijini; na kwa kuwa masharti ya Benki ya Wanawake haina tofauti na masharti ya mabenki mengine; na kwa kuwa riba inayotozwa na benki hii pia haina tofauti na riba inayotozwa na mabenki mengine. Je, lengo la Serikali la kuanzisha benki hii kuwasaidia wanawake wanyonge limefikiwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa wanawake wengi wao wapo vijijini na benki hii haijaweza kuwafikia wanawake hao wa Tanzania waliopo vijijini. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wanawake wengi wanyonge waliopo vijijini wanafikiwa na huduma ya benki hii?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, (a) swali lake linahusu riba ya benki hii kuwa sawa na riba inayotolewa na mabenki mengine. Majibu yetu ni kwamba mwezi Machi mwaka huu wakati tukisherehekea sherehe ya Siku ya Wanawake Duniani, Waziri wa Afya alitoa agizo tena kwenye mkutano wa hadhara kwa Mkurugenzi wa Benki hii kwasababu kipindi hicho hakukuwa na bodi, waweze kulishughulikia suala hilo, ili kutengeneza dirisha maalum ambalo litawafikia wanawake wa nchi hii na mikopo yenye riba nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa msimamo wetu ni kwamba bodi ambayo tayari Mheshimiwa Waziri ameiunda inalishughulikia suala hilo na tutatoa majibu baada ya kupata mwongozo kutoka kwa bodi husika ni namna gani wametekeleza agizo la Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wanawake wa vijijini watafikiwa na benki hii lakini pia pamoja na benki nyingine lakini pia pamoja na schemes nyingine za kuwawezesha wanawake kujiendeleza katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Na ndiyo maana kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 Serikali imeanzisha mpango wa kupeleka shilingi milioni 50 kwenye kila kijiji kwa ajili ya kuwafikia makundi mbalimbali ya kujijenga kiuchumi. Benki yetu itaendelea kushirikiana na benki nyingineza kijamii kama hizi community banks na benki nyingine kubwa ili kuweza kutoa mikopo kwa wanawake.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo lililoko Mara la ambulance ya kuwachukua wagonjwa, ni sawasawa na tatizo lililopo Wilaya ya Kondoa ambako Kituo cha Afya cha Wilaya ya Kondoa hakina ambulance kwa muda mrefu sasa; iliyopo ni mbovu ya mwaka 2008 na inahitaji matengenezo makubwa sana kiasi kwamba Halmashauri haiwezi kumudu. Je, Serikali iko tayari kutuletea ambulance Wilaya ya Kondoa ili wagonjwa ambao wanatakiwa kupata Rufaa ya kuja Dodoma Mjini wapate usafiri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, tumelisikia suala zima la request katika Wilaya ya Kondoa. Niseme wazi, ukiangalia hata katika database ya mwaka huu, katika Halmashauri ambazo ziliomba kupata ambulance zilikuwa 18, katika kumbukumbu yangu ya karibuni. Hili sina hakika hapa kama tuliweza kuliainisha katika mpango wetu wa bajeti wa Halmashauri ya Kondoa kwa mwaka huu wa fedha, lakini tutaenda kuliangalia. Kama Kondoa haipo, itabidi tujipange kwa pamoja, tuone ni jinsi gani tutafanya katika mchakato wa bajeti ambao utaanza siyo muda mrefu; na mpango wake tumeujadili hapa siyo muda mrefu, tujadili kwa pamoja kwa sababu hii needs assessment inaanzia kutoka katika vikao vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakapolifanya hivi na kwa sababu jambo hili ni pana na ninavyojua, mgonjwa kutoka Kondoa mpaka aletwe Hospital ya General hapa Dodoma ambapo ni mbali sana, tuna kila sababu kuwezesha eneo hilo lipate vifaa vizuri hasa ambulance kuwafikisha wagonjwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Felister Bura kwamba, hili tutaliangalia kwa upana wake, tuone ni jinsi gani tutafanya ili eneo lile lipate huduma bora.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Serikali kwa kupanua uwanja wa ndege wa Dodoma, lakini upanuzi huo umeathiri sana barabara ya Area D round about ya Shabiby, na wananchi wanaotoka Area D na Majengo Mapya
hurudi mpaka Kisasa kuja mjini kilometa nyingi.
Je, Serikali iko tayari kujenga barabara nyingine ya
lami kuwapunguzia safari ndefu wananchi wanaokaa maeneo ya Area D na Majengo Mapya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tunahitaji kuangalia upya namna Area C na Area D inavyoweza kufikika ukitokea Dar es Salaam bila mzunguko huo mkubwa kwa kuhakikisha tutapata barabara nyingine badala ya ile ambayo sasa hivi imefungwa kwa ajili ya kiwanja cha ndege. Kwa hiyo, namhakikishia Serikali nayo inalifikiria na tutalifanyia kazi kwa haraka hilo.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali kwa uamuzi wa kufungua Benki ya Maendeleo ya Kilimo Mkoani Dodoma na kukubali kutoa mafunzo kwa wakulima wadogo wadogo Mkoani Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo imeanzishwa kwa malengo ya kuwawezesha wakulima kupata mikopo kwa masharti nafuu na kwa haraka zaidi. Je, Serikali iko tayari kupunguza sasa riba ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili wakulima wengi wapate kufaidika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ni mkombozi kwa wakulima. Je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha kwamba mikoa yote wanapata matawi ya benki hii ili wakulima wasihangaike kwenda Dar es Salaam na Dodoma kufuatilia mikopo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Felister kwa kuwa mbele katika kufuatilia miradi ya maendeleo ndani ya Mkoa wetu wa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ameuliza kuhusu kupunguza riba. Kwanza nimkumbushe kwamba Benki hii ya Maendeleo ya Kilimo ilianzishwa kwa malengo makuu mawili. Moja ni kuchangia utoshelezi na usalama endelevu wa chakula nchini na pia kusaidia mapinduzi ya kilimo kutoka katika kilimo cha kujikimu na kwenda kilimo cha kibiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutimiza malengo haya, Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili iweze kufanya kazi hizi ni lazima iwe na mtaji wa kutosha na pia imekuwa iki-lobby katika taasisi nyingine za kifedha ili ziweze kutoa mikopo katika sekta ya kilimo. Benki hii ili iweze kupata mtaji wa kutosha sasa hivi Serikali imeshairuhusu Benki ya Maendeleo ya Kilimo iweze kupata mkopo wa bei nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika na iko mbioni kuupata na nina uhakika itaweza kutoa mikopo hii kwa bei nafuu kwa wakulima wetu wadogo wadogo na wa kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ili kutimiza pia malengo haya Benki yetu ya Kilimo iliandaa mpango wa biashara wa miaka mitano ambao umeanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2017 - 2021. Katika kutekeleza mpango huu wa biashara wa Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo imedhamiria kufungua ofisi sita za kikanda ndani ya Tanzania, ambazo ni Kanda ya Kusini, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Ziwa Viktoria pamoja na Zanzibar. Baada ya kufunguliwa ofisi hizi za kanda nchi nzima ni imani yetu sasa tutaweza kuwafikia wakulima wetu kule walipo.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Kibaigwa unakua
kwa kasi sana na kwa sasa mji ule ni Mji Mdogo. Hata hivyo, kwa kuwa hatuna watumishi wa kutosha na mji ule haujafanywa kuwa mamlaka, naiomba Serikali sasa ituambie ni lini Mji wa Kibaigwa utapewa mamlaka ili waweze kupanga shughuli za mji wao na kupewa watumishi wa kutosha kuendeleza Mji ule Mdogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, toka asubuhi nimesema leo kuna utaratibu wa kuhamisha goli katika uwanja. Naomba nikuambie Mheshimiwa Felister Bura kwamba hoja yako imesikika na lengo letu ni kupanga miji hii yetu yote vizuri, kuna Kibaigwa, Kibakwe na maeneo mengine katika Mkoa wako wa Dodoma najua inakua kwa kasi sana. Hata hivyo, wakati tunajielekeza katika mipango ya Mamlaka ya Miji Midogo tutajielekeza jinsi gani tupate watumishi kuweza kuziba nafasi hizo ili wananchi wetu wapate huduma vizuri. Nakushukuru sana.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama tena kwa sababu jambo hili limekuwa likiwagusa Waheshimiwa Wabunge wengi na katika maeneo mengi na hasa pale inapoanzishwa Mamlaka za Miji Midogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiutaratibu mwenye dhamana ya kuendeleza miji hii kuweza kuanza kufanya shughuli zake inapokuwa imeanzishwa Miji hii Midogo ni Halmashauri Mama. Kwa hiyo, inapokuwa Serikali tumekubali kwamba mji huo uanze mipango yote na utaratibu wa uanzishwaji unaanzia kwenye Halmashauri Mama kuijengea uwezo Halmashauri hiyo ya Mji Mdogo ili iweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwasihi Waheshimiwa Wabunge kwamba mipango yote itapaswa iingie kwenye mipango ya Halmashauri Mama na ndipo sasa kwa yale maeneo ya upungufu wa watumishi Serikali inaweza kuwaleta. Hata hivyo, kama hakuna bajeti au mpango kutoka kwenye Halmashauri Mama sio rahisi kwa Halmashauri hizo za Miji Midogo kuweza kuanza.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi, kwanza naipongeza Serikali kurudisha Ardhi ya Dodoma mikononi mwa wananchi yaani Baraza la Madiwani. (Makofi)
Kwa kuwa CDA imevunjwa na ndio mamlaka iliyokuwa na madaraka juu ya ardhi ya Dodoma na wakati inavunjwa wapo wananchi ambao walishapata barua za kumiliki ardhi, lakini walikuwa hawajaonyeshwa maeneo yao na wapo wananchi ambao wanalipa kidogo kidogo pale CDA, je, Serikali imeweka utaratibu gani wa dharura wa kuhakikishwa kwamba wananchi wa Manispaa ya Dodoma wanahudumiwa wakati taratibu zingine zinaendelea?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunashukuru kwa Mheshimiwa Mbunge ku- recognize kwamba kilio cha wananchi wa Dodoma katika hilo, lakini jambo la pili government works on papers, hakuna haki mtu itayopotea. Kwa hiyo, Serikali itaandaa utaratibu wowote ambao unawezekana na kikosi kazi kwa mujibu Serikali itakavyokuwa imejipanga naomba muondoe hofu kwamba Ofisi ya Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo jambo hili inaisimamia vizuri tutakuja kutoa taarifa hapa iliyokuwa rasmi juu ya jinsi gani jambo hili linatekelezeka na wananchi wote wa Dodoma wasiwe na hofu kila jambo litakuwa limewekwa vizuri kwa utaratibu wa Kiserikali.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa majibu ya nyogeza kwa niaba Waziri wa Ofisi ya Rais -TAMISEMI kuhusiana na swali lililoulizwa na Mheshimiwa Bura kama ifuatavyo:-
Naomba niwahakikishie wananchi wa Dodoma kwamba mbali na kuvunjwa na CDA huduma zote za ardhi zinaendelea chini ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma na watumishi waliokuwa wakifanya kazi sekta ile wapo ambao wataendelea na kazi hiyo na wale ambao walikuwa wamelipia nusu ya maeneo yao wataendelea na utaratibu huo mpaka pale watakapokamilisha kulingana na makubaliano waliopeana awali.
Aidha, wale wote ambao wana zile hati ambao si
hati miliki ambazo tunazitambua kutakuwa na utaratibu wa kubadilishiwa na kupewa zile hati ambazo watapewa muda wa miaka 99 kuanzia pale alipopewa awali. Kwa hiyo, wasiwe na hofu Wizara imejipanga vizuri na kila mmoja atapata haki yake kadri utaratibu wa ofisi ilivyopanga.(Makofi)
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Chemba ni kati ya Wilaya mpya katika Mkoa wetu wa Dodoma. Ukitoka Kondoa kwenda Chemba ni zaidi ya kilomita 50 na ukitoka Dodoma Mjini kwenda Chemba ni zaidi ya kilomita 100 lakini Kituo cha Afya kilichopo pale hakikidhi mahitaji na Kituo cha Bahi ambacho kinahesabika kama Hospitali ya Wilaya bado kina upungufu makubwa. Je, lini Serikali itaungana na wananchi wa Chemba kuhakikisha kwamba Makao Makuu ya Wilaya inapata hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini ni kwamba mpango wa Serikali wa mwaka huu imetengwa shilingi milioni 23 ambayo ni kwa ajili ya kuhakikisha tunafanya maandalizi ya awali lakini tumeshaingiza katika mpango mwingine na vilevile wenzetu wa Chemba wako katika mchakato wa kushirikisha National Health Insurance Fund katika jambo hilo. Kwa hiyo, naomba tuseme kwamba mipango hii yote itaenda kwa pamoja kusaidia Chemba iweze kupata kituo cha afya. Hata hivyo, ndiyo maana tunaamua kufanya ukarabati mkubwa katika Kituo kimoja cha Afya cha Chemba na Bahi tupunguze referral system ili kusaidia wananchi kupata huduma za upasuaji wakiwa katika maeneo yao.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali na kuipongeza kwa kuanza ujenzi wa barabara ya Mbande – Kongwa – Mpwapwa kwa kiwango cha lami. Naamini mwaka ujao wa fedha barabara hii itakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali; kwa kuwa mji wa Dodoma na viunga vyake unakua kwa kasi sana kutokana na Serikali kuhamia Dodoma, na kwa kuwa tusingependa mji wa Dodoma ukawa na msongamano kama Dar es Salaam; je, Serikali iko tayari na ina mkakati gani madhubuti wa kuhakikisha kwamba barabara za mzunguko katika mji huu zinaanza kujengwa kupunguza Msongamano unaoweza kuwepo mji utakapokua?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, ni lini Serikali itajenga barabara nyingine baada ya barabara iliyokuwa inatoka Shabiby Petrol Station na Area D kufungwa kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege na sasa wananchi wa Area D, Mlimwa, Majengo Mapya na maeneo mengine wanazunguka mpaka Swaswa ndipo waje mjini, je, ni lini barabara hiyo itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba Dodoma ndiyo makao Makuu na mpango mzima wa kuhamia Dodoma unaendelea. Pia Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha barabara zake ili kuondoa usumbufu ambao unaweza kujitokeza kutokana na ukuaji wa mji wa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeshaweka mkandarasi kwa ajili ya usanifu wa barabara za mzunguko za Dodoma ambazo zitakuwa na ukubwa wa kilometa 96. Tulitenga fedha kiasi cha shilingi 959,812,000 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba usanifu unakamilika; na usanifu wa barabara za Dodoma utakamilika mwezi wa tano mwaka 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua iliyofikiwa sasa hivi tuko zaidi ya asilimia 25 ya zoezi la usanifu na mimi ni wito wangu tu kwa maana kwamba hii kazi isimamiwe vizuri na upande wa TANROADS iliusanifu ukamilike ikiwezekana mapema kabla ya muda huu ili harakati za kutafuta fedha na kujenga barabara za mzunguko wa Dodoma ziweze kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, tunatambua usumbufu ambao unajitokeza na sasa hivi pia tunaona kuna foleni zimeanza kuonekana. Hii barabara anayoitaja Mheshimiwa Mbunge ambayo inaleta usumbufu kwa wakazi la eneo la Area D, Mlimwa na Majengo Mapya kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema ninatambua urefu wa kilometa kama mbili; barabara hii mawanzoni ilikuwa inasimamiwa na CDA kabla haijavunjwa. Kwa hiyo, upande wa Serikali tumechukua jukumu la kuhakikisha sasa kipande hiki cha barabara kinatengenezwa haraka ili Waheshimiwa Wabunge wakiwa Dodoma pamoja na wananchi wa Dodoma kwa ujumla wasipate shida kutokana na shida ambayo imejitokeza baada ya ujenzi wa uwanja ule wa ndege kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo zoezi la kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha kipande hicho pamoja na kusimamia maeneo ambayo yametengewa fedha kwa tija tutapokuwa na balance kidogo imebakia tutaanza kupeleka eneo lile ili barabara iweze kujengwa, Ahsante.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, takribani zaidi ya vijiji 12 vinavyozunguka Pori la Akiba la Mkungunero hawafanyi kazi ya kilimo kwa sababu ya mgogoro mkubwa ambao umedumu zaidi ya miaka 10, kati ya wafanyakazi wa pori la Akiba la Mkungunero na wakulima wanaozunguka pori lile. Suala hili limeshafika Serikalini, lakini hakuna hatua zinazochuliwa. Wabunge wa Majimbo Mheshimiwa Juma Nkamia na Mheshimiwa Dkt. Ashatu wanapata shida sana wakati wa kampeni na hata wakati wa kuwatembelea wananchi wao.
Je, ni lini sasa matatizo haya yatakwisha mpaka halisi wa pori la Mkungunero litabainishwa ili wakulima wale wafanye kazi yao kwa uhuru na kwa amani?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na tatizo la muda mrefu la vijiji hivi 12 katika pori la Akiba la Mkungunero ambapo wananchi walikuwa wanagombania mipaka, hili ni mojawapo ya eneo ambalo Kamati ya Kitaifa imeyapitia na wenyewe tumeipitia tumeona kweli kuna mgogoro ambao unatakiwa kutatuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii kumuomba Mheshimiwa Felister Bura kwamba katika hili eneo Serikali iliagiza kwamba maeneo yote yenye migogoro yawekewe mipaka na muda wa mwisho ulikuwa ni tarehe 31 Desemba, 2017. Hivi sasa tunafanya tathmini kupitia maeneo yote sio tu katika eneo hili la Mkungunero, katika mapori yote ya akiba na mengine yote kuangalia baada ya kuweka mipaka na vigingi katika haya maeneo ni maeneo yapi ambayo yana migogoro, ni maeneo kiasi gani tunatakiwa tuyaachie ama tuendelee kuyahifadhi na wananchi watafutiwe maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya haya yote kukamilika basi Waheshimiwa Wabunge watajulishwa na hatimae tutajua kabisa kwamba wananchi sasa watatatuliwa haya matatizo na hili tatizo la Mkungunero na vijiji hivi 12 vyote vitakuwa vimepata ufumbuzi wa kudumu.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kero ya maji iliyopo Nyang’hwale inawasumbua sana wanawake wa Wilaya ya Kongwa na Mheshimiwa Naibu Waziri nimekuuliza mara nyingi ukipita hapa jirani yangu kuhusu Wilaya ya Kongwa na ukaniambia umetoa fedha kwa ajili ya maji Wilayani Kongwa. Visima vinavyotoa maji Wilayani Kongwa havizidi vitatu, visima vingine vilivyobaki vilivyochimbwa na World Bank havitoi maji. Ni jana tu nimeongea na Mkurugenzi wa Kongwa akaniambia shida ya maji ya Kongwa ipo palepale, maji yanayotoka ni kwa maeneo machache sana.
Naomba leo Naibu Waziri aniambie maji yatatoka lini Kongwa ya kuwatosha wanawake wa Kongwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, nina umakini mkubwa sana na Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa nimeifanyia kazi sana tangu nakuwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji. Ni juzi tu nilipeleka mtambo wa kuchimba visima Kongwa na kwamba tayari kuna visima vya kutosha ambavyo vimechimbwa lakini siyo kwamba tumekamilisha Jimbo zima au Halmashauri nzima ya Kongwa, kwa hiyo, tunaendelea. Kama bado kuna maeneo yanahitaji kupata visima tupo tayari kuendelea kuchimba na hasa kwa kuzingatia kwamba katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 tumeweka fedha tena kwa ajili ya kuendelea kuwapatia akina mama maji.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie mama yangu Mheshimiwa Bura kwamba sisi tumedhamiria kuhakikisha kwamba kweli tunamtua mama ndoo kichwani. Yule ambaye hatatuliwa ndoo kichwani ni kwamba atakwenda kuchota maji umbali usiozidi mita 400 kutokana na sera yetu. Kwa bahati nzuri na mimi mwenyewe naishi Dodoma Mama Bura, kwa hiyo, tutakuwa pamoja na kwa vyovyote vile tuambatane tukaangalie maeneo mengine ambayo hayana ili tuweze kuyapatia maji. (Makofi)

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, ili kulinda Kiti cha Spika kwa sababu wewe huwezi kuuliza swali la nyongeza, naomba nikiri kwamba Mji wa Kongwa tumepata kisima ambacho kinatoa maji mengi. Sasa hivi kinachotakiwa ni kupeleka fedha ili tuweze kujenga miundombinu. Naomba nikuahidi kwamba tutapeleka fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu ili wananchi wa Kongwa waweze kupata maji ya kutosha. (Makofi)
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ilianzishwa zaidi ya miaka Kumi iliyopita na Halmashauri hii Makao yake Makuu yako karibu sana na Chamwino Ikulu. Kwa hiyo, nilitegemea Serikali ingeliangalia hili suala kwa jicho la kipekee kabisa. Idara za Halmashauri hii zimetawanyika, ukitoka Ofisi ya Mkurugenzi hadi Ofisi ya Ardhi ni kilometa tano.

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka Ofisi ya Mkurugenzi hadi Idara nyingine ambazo nyingine ziko kwenye shule za msingi, nyingine ziko kwenye nyumba za watu binafsi kwa hiyo, ufanyaji kazi na huduma kwa wananchi uko katika hali ngumu kabisa kutokana na jengo lile kutokamilika. Halmashauri waliwafuata TBA wakafanya tathmini wakaona kwamba, zinahitajika shilingi…

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa shilingi bilioni 2.3 na Serikali imetenga shilingi milioni 600 tu kukamilisha lile jengo.
Je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha za kutosha kwa ajili ya lile jengo la Halmashauri na likamilike kwa wakati, japo floor ya chini, ili watumishi wahamie wakafanye kazi pale?
Swali la pili, Halmashauri ya Chemba iliomba shilingi milioni 950 kwa mwaka huu wa fedha na wamepata shilingi milioni 450 tu. Je, shilingi milioni 500 zilizobaki watapata lini ili waendelee na ujenzi wa jengo la Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, watumishi wa Halmashauri ya Chamwino wanapata shida kubwa sana na hili tunalijua wazi. Ninajua kwamba mkataba wa kwanza wa mkandarasi wa kwanza umevunjwa lakini commitment ya Serikali iko pale pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali mpaka hivi asubuhi na-cross check pale tumeshapeleka shilingi milioni 750 hivi sasa. Kama ulivyosema tathmini iliyofanywa na TBA imeonekana kumaliza lile eneo la ground floor peke yake karibu ni shilingi bilioni mbili. Hata hivyo, nimeongea nimeongea na Kaimu Mkurugenzi pamoja na Engineer leo wafike ofisini kwangu kuangalia way forward tunafanyaje kwa sababu tathmini iliyofanywa gharama yake ni kubwa, lakini Engineer na timu yake wanasema kwa kutumia wao utaalamu wao pale ile shilingi milioni 750 wataweza kumaliza ile ground floor na hivi sasa tunajielekeza kuangalia jinsi gani fedha zitumike vizuri.
Kwa hiyo, nimemuagiza Kaimu Mkurugenzi na Engineer leo hii wanakuja kukutana na wataalam katika ofisi yetu tuangalie tufanye nini ili tumalize ile ground floor.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la ujenzi pale Chemba, ni kweli tumepeleka shilingi milioni 500 mpaka hivi sasa, tunachotaka kufanya ni kuhakikisha kwamba, fedha tunazipeleka maeneo haya na maeneo mengine tofauti, lengo kubwa ofisi hizi ziweze kukamilika na watumishi wetu wapate maeneo mazuri ya kufanya kazi. (Makofi)
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kutupa fedha kwa ajili ya upanuzi wa Kituo cha Afya cha Bahi. Kituo hiki kinawahudumia wananchi wengi sana kwa sababu mji ule unaendelea kupanuka kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo tulilonalo, upanuzi unafanyika lakini hatuna vitendea kazi, watumishi walioko pale ni Manesi wanne tu na yuko Daktari mmoja na Matabibu wachache sana ambao hawakidhi mahitaji ya wagonjwa wanaokwenda katika kituo kile cha afya. Ni lini sasa Serikali italeta watumishi na vitendea kazi vya kutosha kwa ajili ya huduma za Kituo cha Afya cha Bahi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba nimshukuru Mheshimiwa Bura kwa sababu yeye amekuwa Msemaji wa Mkoa wa Dodoma kwa nafasi yake ya Viti Maalum na anautendea haki sana mkoa huu. Naomba ku-declare interest, jengo ambalo tumemaliza hivi sasa katika Hospitali ya General, amefanya kazi kubwa sana kuhakikisha tumepeleka pesa na hivi sasa tumepeleka karibuni shilingi bilioni mbili hospitali ile inapata huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, eneo la Bahi kweli tumeboresha kituo kile cha afya lakini siyo hivyo tu kwa kelele zake na za Mbunge wa Bahi mwaka huu tunakwenda kuanza ujenzi wa hospitali mpya za Wilaya za Bahi, Chemba pamoja na Chamwino. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hilo, wenzetu kupitia Utumishi kabla ya Juni, kuna mpango mkakati kupata watumishi wapya katika sekta ya elimu na sekta ya afya. Pia kwa vile tunajua Bahi ni pumulio la makao makuu yetu ya nchi kwa maana ya hapa Dodoma tutajitahidi kuhakikisha tunawapeleka watumishi wa kutosha ikiwa lengo kubwa ni wananchi wa eneo lile waweze kupata huduma vizuri. (Makofi)
MHE. FELISTER A BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maporomoko ya Ntomoko ni janga kwa wananchi wanaoishi kandokando ya maporomoko haya. Wananchi wa Wilaya ya Chemba vijiji kumi na vijiji vitatu vya Wilaya ya Kondoa wamesubiri mradi huu kwa muda mrefu sana na fedha zilishatolewa zaidi ya bilioni mbili kwa ajili ya kukarabati mradi ule, watumishi ambao walizembea mradi ule hawajachukuliwa hatua yoyote. Wananchi wanateseka na hakuna jibu lolote linaloonesha kwamba hivi vijiji vitapata maji hivi karibuni.
Je, watumishi waozembea na wakapoteza zaidi ya shilingi bilioni mbili na kufanya mradi huu ukasimama wamechukuliwa hatua gani?
Swali la pili, mradi huu umekwishatembelewa na viongozi wengi na tumekwishachangia mara nyingi na Wabunge wa maeneo yale mimi na Mheshimiwa Juma Nkamia na Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji sasa hivi hatueleweki kwa wananchi.
Je, kuna mkakati gani wa haraka wa kuwapatia wananchi wa vijiji vile maji ili wasiendelee kuhangaika kwa sababu hata DUWASA wenyewe hawajapata fedha kwa ajili ya ule mradi? (Makofi)
NAIBU WA WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimpongeze Mama yangu Felister Bura kwa namna ya kipekee anavyowapigania wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa ambalo nashukuru sana ni taarifa ambayo amenipa kama Naibu Waziri wa Maji, nataka nimhakikishie fedha za Serikali haziliwi bure. Kama kutakuwa na watumishi ambao kwa kuzembea au kwa maksudi fedha zile zimepotea, tutafanya mawasiliano ya haraka na watu wa Kondoa katika kuhakikisha hatua za haraka zitachukuliwa kwa watumishi wale ambao wamefanya uzembe wananchi waweze kupata taabu.
Swali lake la pili, amesema huu ni mradi wa muda mrefu sana nataka nimuhakikishie sisi ni Wizara ya Maji na jukumu letu ni kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama yenye kuwatosheleza na ndiyo maana tumeahidi kwamba katika bajeti hii ya mwaka 2018/2019 tumeshatenga fedha ili katika kuhakikisha mradi ule uweze kukarabatiwa kwa haraka ili wananchi wake waweze kupata majisafi salama na ya kuwatosheleza. Ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kumfahamisha Mheshimiwa Felister Bura kwamba kuna hatua za dharura ambazo tunaendelea nazo, tunachimba visima katika vijiji vyote eneo la Kondoa na tumeshaanza na visima 15 ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)