Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Eng. Edwin Amandus Ngonyani (39 total)

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa hii ya kuingia katika jengo hili kwa mara ya kwanza. Kupitia fursa hiyo naomba niwashukuru wapiga kura wote wa Jimbo la Namtumbo kwa kazi waliyoifanya pamoja na mateso yote ya kupiga kura mara tatu na mwisho nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kunipa nafasi hii ya kuwatumikia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Pili ni mwendelezo wa Mpango wa Kwanza pamoja na nyongeza inayozingatia dhima ya Serikali ya Awamu ya Tano kuijenga Tanzania ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la miundombinu iliyopangwa katika Mpango wa Kwanza na hii iliyoongezeka katika Mpango wa Pili yote inahitajika na tutaihitaji katika mpango wa tatu. Kwa hiyo, hoja kwamba tulitekeleza asilimia 53 tu katika awamu ya kwanza ni kutokana na uwezo wetu, sasa tunaingia katika Mpango wa Pili tutamalizia asimilia 47 pamoja na nyongeza nyingi ambazo zipo katika Mpango huu wa Pili, ambao Mheshimiwa Dokta Mpango ameuleta na kwa kweli naomba nichukuwe fursa hii nimshukuru sana alikuwa amechelewa kuja nafasikatika hiyo!
Mheshimiwa Naibu Spika, wengi wameongelea umuhimu wa miundombinu, nashukuru sana Bunge zima limeungana katika kukubali Mpango, tunatofautiana katika utekelezaji, wapo wanaodhani utekelezaji hautafanyika na wapo wanaoomba tupate nguvu tutekeleze. Kwa maana nyingine Mpango wote tunaukubali, labda katika eneo moja tu ambalo Mheshimiwa Bashe ametoa maoni tofauti kwamba suala la kufufua Shirika letu la ATCL liangaliwe kwa namna tofauti kwa kuzingatia hasara zinazopatikana katika mashirika ya ndege duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Bashe na wengine wenye dhana kama yake, usafiri wa anga ni necessary evil kwa nchi yoyote, hatuwezi kuukwepa. Inawezekana from micro point of view kampuni ikapata hasara, lakini kama nchi usafiri huo unachangia katika sekta mbalimbali na overall sekta hiyo ya usafiri wa anga inatuletea faida kubwa, hatuwezi tukaiacha ikashikiliwa na wafanyabiashara peke yao, muda wowote wanaweza wakaondoka kwa sababu wao wanaangalia faida na wanaangalia faida katika kampuni yao peke yake, wakati sisi tunaangalia faida kwa mapana yake ni pamoja na mchango wake katika sekta ya utalii na masuala mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumedhamiria, kujenga reli ya standard gauge ya Kati na matawi yake yote, ya Mtwara Corridor na ya Kaskazini. Dhamira hiyo kama ambavyo mtaiona katika bajeti inayokuja na mmeona katika kitabu cha Mheshimiwa Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango, tumeshaonyesha kwa kutenga trilioni moja haijawahi tokea! Kwa hiyo, naomba mtuamini. Ninalo jembe linaloniongoza, linaloongoza Wizara hii, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa. Kwa wale wanaomfahamu yale aliyoyafanya katika Wizara ya Mawasiliano, aliyafanya kimya kimya wanamfahamu ni mtu wa aina gani na mimi nashukuru kufanya kazi chini yake, kwa sababu naamini nitaweza kukidhi haja yangu ya kuwatumikia Watanzania kwa namna ambayo tutafika huku tunakokwenda, uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tutatoka kwenye kusherehekea flyover na interchanges moja tutakuwa na flyovers na ma-interchanges nyingi sana.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri Ngonyani muda wako umekwisha!
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Aah, ni kengele ya kwanza hiyo!
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kuunga mkono kwa nguvu sana na kwa kutupendelea sisi watu wa miundombinu na hatutawaangusha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Namtumbo tunashukuru sana kwa kupewa heshima kwa mwakilishi wao kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Imani hiyo ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hakika itazaa imani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa MIVARAF unaihusu sana Wilaya ya Namtumbo ambayo wakazi wake ni wakulima kwa zaidi ya asilimia tisini. Ujenzi wa miundombinu ya barabara za kuwezesha mazao ya wakulima kuyafikia masoko pamoja na ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mazao ni muhimu. Shughuli zinazofanyika katika mradi wa MIVARAF ni muhimu sana kwa wakulima wa Namtumbo. Nitashukuru kujulishwa mradi huo unaanza kutekelezwa lini Wilayani Namtumbo na una bajeti ya kiasi gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti,naunga mkono hoja ya bajeti iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu hapa Bungeni kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti,naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Waziri, wewe ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama ilivyo kuwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la Wananamtumbo, mtujengee Chuo cha VETA. Aidha, mtusaidie Chuo cha Ualimu kilichoanzishwa Namtumbo katika Kijiji cha Nahoro, chini ya mwavuli wa Ushirika wa SONAMCU na Mkufunzi Mstaafu Bwana Awadh Nchimbi kiendelezwe na changamoto zililoko zitatuliwe. Nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunipa uhai, nguvu, afya njema na akili timamu ili niweze kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kujibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge.
Naomba nichukue fursa hii kwa heshima kubwa, kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa na Watanzania kuongoza nchi yetu katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba, 2015. Kwa kipindi kifupi alichokaa madarakani Watanzania kwa ujumla wetu tumefarijika na uongozi wake mahiri ambao unaonesha nia ya dhati ya kuiwezesha nchi yetu kupiga hatua kubwa kimaendeleo na kufikia kiwango cha uchumi wa kati. Na mimi naungana na Watanzania wenzangu kuendelea kumuombea afya njema ili aweze kuendelea kututumikia kwa mapenzi makubwa kama alivyoanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kwa kishindo kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ninampongeza pia Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa kuteuliwa kwake kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile napenda kukupongeza wewe, Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wengine wa Bunge kwa kuchaguliwa kuliongoza Bunge letu Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchaguliwa kwao kuwawakilisha wananchi katika Bunge hili. Nina imani kwamba sote tutatekeleza kazi zetu za kuwatumikia wananchi kufuatana na kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu ili tufikie malengo yetu ya kujikwamua kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwashukuru kwa namna ya pekee wapigakura wangu wa Wilaya ya Namtumbo kwa namna walivyojituma katika kuhakikisha ninaipata fursa hii ya kuwatumikia katika nafasi ya Ubunge, pamoja na kwamba muda mwingi sipo nao kutokana na majukumu ya Kitaifa, wanajua ninawawakilisha kwa kiwango kikubwa katika kutatua changamoto zao. Ninawaahidi, mambo yote niliyoyaahidi na yaliyoahidiwa ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi nitayasimamia yatekelezwe kwa kadri Mwenyezi Mungu atakavyonijalia. Changamoto zote za kilimo, hususan kilimo cha tumbaku na mazao mchanganyiko pamoja na masoko ya uhakika, maji, umeme, mitandao ya simu, barabara, maeneo ya kilimo na mipaka ya kiutawala, zinazowakabili wakazi wa Wilaya ya Namtumbo nitazishughulikia kikamilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati kabisa ninapenda kumshukuru Mheshimwa Rais kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kumsaidia Mheshimiwa Profesa Makame Mnyaa Mbarawa katika nafasi yake. Napenda kuwaahidi Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Watanzania wote kuwa sitawaangusha.
Aidha, ninaomba niishukuru familia yangu, mke na watoto wangu kwa kuniunga mkono, kunivumilia na kunitia nguvu katika kutekeleza dhamira yangu ya kuwatumikia Wana Namtumbo na Watanzania wote katika nafasi hii ya Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusema kwamba, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa ndugu zangu Wabunge wote tuunge mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, pamoja na kwamba inawezekana barabara ama ahadi yako nyingine haipo katika mpango wa utekelezaji kwa mwaka huu. Ni wazi ahadi zipo nyingi na sisi tutajitahidi kuzitekeleza kikamilifu kwa awamu, kwani tunaye jemedari, Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kazi anayoifanya mnaiona na dhamira yake ya kututumikia Watanzania, hususan wananchi wa vipato vya chini haina mashaka kwa yeyote mwenye mapenzi mema na Taifa letu. Hivyo, kwa heshima na taadhima nawaomba mtuunge mkono na kwa kweli, tupeni moyo wa kuwatumikia. Nawashukuru Wabunge wote kwa namna mlivyochangia, mawazo na mapendekezo yenu yote kwetu ni maelekezo.
Tutayafanyia kazi kwa kuanzia na kusimamia kutekeleza miradi ambayo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano amewasilisha kwa mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze katika kujibu hoja na nitajibu baadhi tu ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamechangia. Hoja ni nyingi, kwa hoja ambazo tutashindwa kuzitolea majibu leo kutokana na muda tutazijibu kwa maandishi. Kama nilivyosema, hoja ni nyingi na, nitaanza na hawa ambao hatujazijibu rasmi kwenye vitabu ambavyo baadaye tutawagawia. Nitaanza na wale waliochangia mwishoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa Bandari ya Nyamisati naomba nikuhakikishie, zimetengwa shilingi bilioni 1.5 kushughulikia bandari hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa barabara ya Bumbuli - Korogwe, Soni - Bumbuli, fedha zimewekwa sifuri kwa sababu study imekamilika. Sasa tunatafuta fedha ndani na nje ili mwaka ujao wa fedha, 2017/2018 tuanze kujenga, lakini Waziri wangu atalifafanua zaidi hilo na kama kutakuwa na mabadiliko atayaeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetenga jumla ya shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya malipo ya fidia katika eneo la Muhalala, pale ambapo panajengwa One Stop Inspection Station. Naomba tukubaliane, hiyo hela imetengwa na tutawalipa fidia ili kile kituo kianze kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara nyingi ambazo zimeongelewa hapa, ziko ambazo kwa sasa tumezitengea bajeti ya matengenezo peke yake. Naomba kuwahakikishia, huu ni mwaka wa kwanza, ahadi iliyoko katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi na ahadi ambazo viongozi wetu wamezitoa kuanzia Serikali ya Awamu ya Tatu, ya Nne na ya Tano, ninawahakikishia zote tutazikusanya na tutatafuta namna tuziwekee priority tuanze ipi na hatimaye tutamalizia na ipi kwa sababu nadhani sio rahisi kwa mwaka huu wa kwanza kuingiza barabara zote zilizoahidiwa na viongozi wetu wakuu na tulizoahidi katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Naomba mtuamini, tutahakikisha ahadi zote ambazo zilitolewa na viongozi wetu wakuu pamoja na chama kupitia, kitabu cha Ilani tutazitekeleza; ndiyo kazi tuliyopewa katika Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kibondo - Kasulu - Manyovu imeongelewa kwa kirefu sana na Wabunge wengi sana wa upande wa Magharabi. Labda kitu ambacho wengi wamekihoji ni kwamba, fedha zilizooneshwa na AfDB hazijaonekana katika kitabu cha bajeti. Hizo fedha zinazotumika kwa sasa kwa ajili ya feasibility study na detailed design zimeshatolewa, ziko dola 1,286,685 ambazo ziko katika bajeti ya East African Community na Sekretarieti ya East African Community ndiyo inayosimamia ujenzi wa barabara hiyo. Ninawahakikishia barabara hiyo kipande kilichobaki ni kirefu, ndiyo, lakini tutahakikisha kinajengwa kwa kadiri ambavyo wahisani na wengine wametusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende Kusini. Barabara ya Mtwara - Masasi - Nachingwea - Ruangwa hadi Nanganga. Mimi naomba mtuamini, tumepanga bajeti, ni kweli ni kidogo, lakini tuanzie na hicho ambacho tumekipanga. Na kwa upande wa Nachingwea - Ruangwa hadi Nanganga tutaanzia na feasibility study na detailed design. Ile nyingine ambayo feasibility study na detailed design imekamilika, ile inayoanzia Masasi - Nachingwea - Nanganga, tutaanza kuijenga, lakini kwa kiwango hicho ambacho tumekitenga. Ni kidogo lakini mimi naomba tukubaliane kwamba mwaka huu wa kwanza tuanze na tuone tutaendeleaje; na mimi nina uhakika tutaendelea vizuri kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudi kwenye barabara ya Soni - Bumbuli; pamoja na kwamba imewekwa sifuri na tumeweka hela hizi za matengenezo, nawahakikishia mwaka ule mwingine 2017/2018 tutaiangalia kwa macho zaidi kama mlivyosema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijibu machache. Kimsingi vitabu hivi tutawapa kwa hiyo, majibu kwa wote walioongea humu ndani Bungeni ambao wamefikia zaidi ya 84 na waliotuletea kwa maandishi wamefika 105. Wote majibu yenu tutayaingiza katika kitabu hiki na tutawagawia kabla wiki ijayo haijaisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wachache ambao nitafungua tu popote pale, kwa sababu ni mengi sana, sitaweza kumaliza, kwa mfano Mheshimiwa Shaban Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, pamoja na Mheshimiwa Rashid Shangazi Mbunge wa Mlalo; hoja yao walitaka Serikali ianze kujenga Bandari ya Tanga sambamba na ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali kupitia TPA imetenga jumla ya shilingi bilioni 14.461 kwa ajili ya kuboresha Bandari ya Tanga na katika mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya Shilingi bilioni 19.798 zimetengwa. Aidha, Bandari ya Tanga ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi TPA kwa kushirikiana na wataalam waelekezi inarejea upembuzi yakinifu uliofanywa mwaka 2012 kwa kuzingatia shehena iliyobainishwa kupitia katika bandari hiyo. Mtakumbuka huko nyuma tulisema ile bandari ilionekana haina faida na wengi walikataa kuwekeza, lakini baadaye tulipoingiza reli ya kutoka Musoma hadi Tanga bandari ile sasa inaonekana ina faida na hivyo uwekezaji ni wa dhahiri.
MWENYEKITI: Ahsante!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunipa uhai, nguvu, afya njema na akili timamu na kuniwezesha leo kuchangia hoja ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kujibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kwa heshima kubwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Viongozi wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wao mahiri. Hakika Watanzania kwa ujumla wetu tumefarijika na uongozi wao mahiri ambao unaonesha nia ya dhati ya kuiwezesha nchi yetu kupiga hatua kubwa kimaendeleo na kufikia kiwango cha uchumi wa kati. Nami naungana na Watanzania wenzangu kuendelea kuwaombea afya njema ili waweze kuendelea kututumikia kwa mapenzi makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kukupongeza wewe binafsi, Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wengine wote wa Bunge kwa kuliongoza vyema Bunge letu Tukufu. Napenda pia kuwapongeza Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete, Mheshimiwa Dkt. Gertrude Pangalile Rwakatare, Mheshimiwa Anne Kilango Malecela na Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Katiba na Sheria walioteuliwa na Mheshimiwa Rais kuungana nasi katika Bunge hili. Nina imani kwamba sasa sote tutatekeleza kazi zetu za kuwatumikia wananchi kufuatana na kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ‘Hapa Kazi Tu’ ili tufikie malengo yetu ya kujikwamua kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwashukuru kwa namna ya pekee wapiga kura wangu wa Wilaya ya Namtumbo, kwa namna wanavyojituma katika kuhakikisha kwamba kwa pamoja tunatatua changamoto zinazowakabili. Pamoja na kwamba muda mwingi sipo nao kutokana na majukumu ya Kitaifa, wanajua nawawakilisha kwa kiwango kikubwa katika kutatua changamoto zao. Nawaahidi tena kwamba mambo yote niliyoyaahidi na yaliyoahidiwa ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi nitaendelea kuyasimamia yatekelezwe kadri Mwenyezi Mungu atakavyonijalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zote za kilimo hususan kilimo cha tumbaku na mazao mchanganyiko pamoja na masoko ya uhakika, maji, umeme, mitandao ya simu, barabara, maeneo ya kilimo na mipaka ya kiutawala zinazowakabili wakazi wa Wilaya ya Namtumbo naendelea kuzishughulikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nishukuru familia yangu, mke wangu na watoto kwa kuniunga mkono, kunivumilia na kunitia nguvu katika kutekeleza dhamira yangu ya kuwatumikia wananchi wa Namtumbo na Watanzania wote katika nafasi hizi za Ubunge na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwashukuru Wabunge wote kwa namna mlivyochangia, maoni na mapendekezo yenu kwetu ni maelekezo. Naomba sasa ndugu zangu, Waheshimiwa Wabunge wote, tuunge mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na naomba sasa nijielekeze katika kujibu hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamechangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia, Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu ameongelea kuhusu kutotolewa kwa fedha za ujenzi wa viwanja vya ndege vya Kigoma, Mpanda, Tabora, Songwe, Mtwara, Sumbawanga na Shinyanga na vilevile Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani naye ameongelea kutotolewa kwa fedha za ujenzi wa jengo la tatu la abiria JNIA Dar es Salaam na uwanja wa Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa viwanja vya ndege vya Kigoma, Tabora, Shinyanga, Mtwara na Sumbawanga, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba hadi kufikia Machi 2017, ujenzi wa viwanja vya ndege tajwa ulikuwa katika hatua ya manunuzi kwa hiyo hakuna fedha iliyotolewa kwa sababu bado hatujawapata wakandarasi wa kufanya kazi zinazotakiwa kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Mpanda kwa kiwango cha lami ulikamilika mwaka 2012 na katika mwaka 2016/ 2017, Serikali ilitenga jumla ya shilingi milioni 700 kwa ajili ya kulipa deni la Mkandarasi. Serikali itahakikisha kuwa deni hilo la Mkandarasi linalipwa mapema. Kazi zinazoendelea katika Kiwanja cha Ndege cha Songwe ni ujenzi wa jengo kubwa la abiria na mradi unaoendelea ambapo Mkandarasi amekwishalipwa shilingi bilioni 3.3 na hadi sasa hana deni lolote analoidai Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiwanja cha ndege cha Mtwara, zabuni ya upanuzi na ukarabati wa kiwanja hicho imeshatangazwa na inatarajiwa kufunguliwa mwezi Mei, 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya 2017/2018, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kulipa fidia kwa viwanja vya Kigoma, Shinyanga, Sumbawanga, Iringa, Musoma, Msalato, Bukoba, Umkajunguti na JNIA. Kwa viwanja vilivyobaki Serikali itaendelea kulipa fidia kadri ya upatikanaji wa fedha. Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imeweka mkakati wa kupima na kupatiwa hati miliki kwa viwanja vya ndege 15 Mwanza, Songwe, Msalato, Dodoma, Iringa, Kilwa Masoko, Mtwara, Lindi, Lake Manyara, Songea, Tabora na Shinyanga na kwa mwaka wa fedha 2017 hicho ndicho tutakachokifanya. Maombi ya kupimiwa na kupatiwa hati miliki yameshawasilishwa kwa mamlaka husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze katika hoja mbalimbali za barabara. Wabunge wengi sana wameongelea barabara na muda ulivyo siyo rahisi sana kuzieleza zote, nitachukua moja moja kadri muda utakavyoniruhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na barabara ya Tabora – Sikonge – Koga – Mpanda vilevile inaunganika na barabara ya Mbinga hadi Mbamba bay, barabara hizo zote ni lot moja, ni project moja inayofadhiliwa na Benki ya AFDB na fedha za ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami tayari zimeshapatikana kutoka Benki ya Maendeleo ya AFDB. Zabuni za ujenzi wa barabara hii zimetangazwa na taratibu za kukamilisha manunuzi ya Mkandarasi zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kibondo – Kasulu – Mnanila, tunatarajia kupata rasimu ya usanifu wa kina na utayarishaji wa nyaraka za zabuni mwezi Juni, 2017 kwa ajili ya kutoa maoni kabla zabuni za ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kibondo – Kasulu – Manyovu hazijatangazwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Masasi – Nachingwea – Nanganga umepangwa kuanza mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, kulingana na Ilani ya CCM ya mwaka 2015 ambayo ndiyo tunayoitekeleza, barabara za Nachingwea hadi Liwale na barabara ya Nangurukuru hadi Liwale zinatakiwa zifanyiwe upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge walioongelea hili ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Lathifah Hassan Chande kwamba barabara hii tutaifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika kipindi hiki cha miaka mitano kabla hakijakwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Butengulumasa - Iparamasa – Mbogwe – Masumbwe, Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kufanyia matengenezo na kukarabati barabara hii ili iweze kupitika katika kipindi chote cha mwaka. Ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara hii utafanyika kadri bajeti itakavyoruhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kahama hadi Geita, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 12,403 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Barabara ya Mafia – Kilindoni – Rasimkumbi; upembuzi yakinifu na usanifu wa kina utafanyika ili barabara hii ambayo pia ipo katika ahadi za Viongozi Wakuu iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Wakati fedha za ujenzi zinatafutwa, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.0422 katika bajeti ya 2017/2018 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara ya Kilindoni – Rasimkumbi ili iendelee kupitika wakati wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa barabara ya Makutano – Mugumu hadi Mto wa Mbu na hasa kipande cha Makutano hadi Sanzate kinachoendelea kujengwa, ujenzi wa barabara ya Makutano – Nata – Mugumu, sehemu ya Makutano hadi Sanzate umefikia hatua ifuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tabaka la udongo (G 15) ni kilometa 38 ambayo ni sawa na asilimia 76; tabaka la chini la tuta (sub base) kilometa 8.5; na tabaka la juu la barabara (base course) ni kilometa mbili, lami nyepesi (prime course) ni kilometa 1.2, madaraja ya makalavati makubwa na madogo asilimia 98 yamekamilika. Maendeleo ya jumla ya mradi ni asilimia 43, mradi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Septemba, 2017. Aidha, Serikali inasimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huu ili kuhakikisha kuwa mkandarasi anapata ujuzi uliokusudiwa na barabara inajengwa kwa kuzingatia viwango kulingana na mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya barabara kati ya Mugumu hadi Tabora B ambayo ni kilometa 18, mpango wa Serikali ni kuijenga barabara hii mpaka Mugumu. Aidha, ujenzi kwa sehemu nyingine ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Mugumu – Tabora B – Clensi Gate– Loliondo itajengwa kwa kiwango cha changarawe ili kutunza mazingira ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambapo sehemu ya Mugumu hadi Tabora B Clensi Gate na sehemu ya Clensi Gate hadi Longido zitatumika kama buffer zone.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipande cha Mugumu - Natta, zabuni zilitangazwa tarehe 07/09/2016 na ufunguzi wa zabuni ilikuwa tarehe 25/10/2016 lakini ulisogezwa hadi tarehe 27/02/2017. Zabuni iliyopokelewa haikukidhi vigezo na hivyo mradi huu utatangazwa tena tarehe 03/05/2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara Tanga - Pangani - Bagamoyo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2017/2018. Serikali tayari imetenga shilingi bilioni 4.435 katika bajeti ya mwaka 2017/2018 na inaendelea kukamilisha taratibu za kupata fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja jipya la Wami kwenye barabara ya Chalinze - Segera liko katika hatua ya kumpata mkandarasi wa kuanza ujenzi. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 daraja hili limetengewa shilingi bilioni 4.351 kwa ajili ya kuanza ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara ya Lindi – Morogoro, kupitia Mpango Mkakati wa Wakala wa Barabara (TANROADS) wa mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021, Mkoa wa Lindi umepangwa kuunganishwa na Mkoa wa Morogoro kwa kuanzia na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Nachingwea – Liwale – Ilonga - Mwaya - Mahenge kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Naibu Waziri wa TAMISEMI ameongelea barabara zote za miji mbalimbali ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi na nimshukuru kwamba majibu yake yako sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara ya Kiboroloni – Kiharara - Suduni – Kidia katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilikamilisha usanifu wa kina. Katika mwaka wa 2017/2018 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 811 ili kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarabati wa barabara ya Kibosho – Shine - Mto Sere ambayo ina kilometa 27.5. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 61 ili kuanza ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeulizwa ni hatua gani zimefikiwa katika kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Kitai – Lituhi na Lituhi -Mbamba Bay. Nimuombe Mheshimiwa Jacqueline Msongozi aondoe tishio lake la kushika shilingi kwa sababu akishika shilingi hapa mimi nitakwenda kushika shilingi Ruvuma. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Kitai - Lituhi umefikia asilimia 50. Mhandisi Mshauri amekwishawasilisha rasimu ya taarifa ya upembuzi yakinifu. Kwa barabara ya Mbamba Bay - Lituhi upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umefikia asilimia 60. Mhandisi Mshauri (M/s H.P Gauff Ingenieure) anaendelea kumalizia kazi ya usanifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa barabara inayounganisha Maramba na Makao Makuu ya Wilaya ya Mkinga yenye urefu wa kilometa 49 utatekelezwa na kukamilika kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 zimetengwa shilingi milioni 87.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kizi - Sitalike – Lyamba Lya Mfipa, Mji wa Mpanda kupitia Sitalike unaungwa na barabara mbili za Kizi - Lyamba Lya Mfipa - Sitalike ambayo ni kilometa 86.24 na Kibaoni - Sitalike ambayo ni kilometa
71.6 ambazo zote bado kujengwa kwa kiwango cha lami. Mpango uliopo kwa sasa ni kujengwa kwa kiwango cha lami barabara ya Kibaoni - Sitalike ambayo imetengewa kiasi cha shilingi milioni 480 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami. Aidha, barabara ya Kizi - Liamba Lya Mfipa - Sitalike itaendelea kupatiwa matengenezo ili kuhakikisha kuwa inapitika wakati wote. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, kiasi cha shilingi milioni 1,950 kimetengwa kwa barabara ya Lyamba Lya Mfipa - Mpanda - Uvinza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kibondo – Kasulu – Mnanila, nashukuru nimeieleza. Nachoomba tu Waheshimiwa wa Kanda ya Magharibi watuamini, siyo kweli kwamba hilo eneo tumelitelekeza, mnafahamu sasa hivi nguvu zote zinaelekezwa huko na mtuamini tunachokisema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Tarime - Mugumu inaendelea na usanifu. Limeulizwa swali ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii unaendelea na utakamilika mwezi Machi, 2018. Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hiyo baada ya kukamilisha usanifu wa kina na kujua gharama halisi za mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Handeni – Kiberashi - Kibaya – Singida; katika mwaka wa fedha 2017/2018 barabara hii imetengewa jumla ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Ni maandalizi siyo ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa barabara ya Amani - Muheza, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais.

Hata hivyo, kutokana na uhaba wa fedha, ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami utafanyika hatua kwa hatua kutegemeana na fedha zitakavyopatikana. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, barabara hii imetengewa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niingie kwenye barabara ya Bwanga - Kalebezo. Tumepokea shukrani na nimhakikishie Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania itaendelea kumsimamia mkandarasi ili ajenge…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. TANROADS watamsimamia mkandarasi ili ajenge barabara ya Bwanga - Kalebezo kulingana na mkataba na hivyo kukamilisha mradi kama ilivyopangwa. Aidha, Wizara itafuatilia ili kuhakikisha mkandarasi anaweka alama za barabarani na kuhakikisha usalama kwa watumiaji wa barabara na wafanyakazi wanaojenga wakati wote wa ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu minara ya simu, niwahakikishie tuna dhamira ya dhati kuhakikisha vijiji vyote Tanzania tunapeleka mawasiliano kupitia Mfuko wetu wa Mawasiliano kwa Wote, lakini vilevile kupitia Kampuni ya Halotel kwa mujibu wa mkataba tulioingia nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nami napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujaalia kufanya shughuli zetu tukiwa na afya njema.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishukuru sana Kamati yangu ya Miundombinu kwa taarifa nzuri na kwa mwongozo mzuri. Nachukua fursa hii kuunga mkono taarifa ya Kamati ya Miundombinu. Naomba niwahakikishie tu Kamati yetu kwamba maelekezo yote waliyotoa tutayatekeleza kwa maslahi ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika mwaka wa fedha 2017/2018, tulitengewa shilingi trilioni 4.5. Fedha hizi tumezitumia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Sekta ya Uchukuzi kwa upande wa Bandari; Bandari yetu ya Dar es Salaam imeanza kuimarika vizuri kwa sababu sasa hivi tumeongeza uadilifu mkubwa na tumejipanga katika kuboresha miundombinu. Kwa taarifa tu, katika mwaka wa fedha 2016/2017, tani milioni 14.7 zilipita kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Katika kipindi cha miezi minne kutoka Julai mpaka Septemba, miezi mitatu, quarter ya mwanzo, mizigo ya nchi za jirani imeongezeka kutoka tani milioni 1.16 mpaka tani milioni 1.479. Hii imetokana na kujipanga vizuri na wafanyakazi wetu kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mapato, mwaka 2016/2017, Bandari ya Dar es Salaam au Bandari zote zilitengeneza karibu shilingi bilioni 734.9 wakati matumizi yalikuwa shilingi bilioni 446. Salio lilikuwa ni shilingi bilioni 288. Kwa quarter ya kwanza kuanzia mwezi Julai mpaka Septemba mwaka 2017/2018, Bandari ya Dar es Salaam imekusanya mapato ya shilingi bilioni 207.5 wakati matumizi ni shilingi bilioni 67. Inaonesha sasa Bandari ya Dar es Salaam imejipanga kuhakikisha kwamba hata matumizi yenyewe wanapunguza kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake ni kwamba pato halisi ni shilingi bilioni 139.6. Hii ina maana, kama tutaendelea namna hii, itakapofika mwisho wa mwaka wa fedha huu, bandari itaweza kuwa na mapato halisi takriban shilingi bilioni 450. Haijawahi kutokea katika historia ya bandari zetu za Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo haya yote hayakuja bure, yamekuja kutokana na miundombinu ambayo sasa hivi inaendelea hapo Bandari ya Dar es Salaam. Tukianzia Bandari ya Dar es Salaam sasa hivi, tuna mradi mkubwa wa uboreshaji wa gati ya kwanza mpaka gati namba saba ambayo tutatumia takriban shilingi bilioni 336. Kazi kubwa inayofanyika ni kuongeza kina cha maji kwenye bandari hiyo, pia na kuboresha bandari yenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara baada ya ukarabati huo, tutahakikisha sasa meli kubwa zenye uwezo wa kuchukua kontena 19,000 za tani 20 zinaingia Bandari ya Dar es Salaam bila matatizo yoyote. Tunaamini tukifanya hivyo, tutaweza kushindana na bandari zote zilizopo katika maeneo ya jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatukusimama hapo tu, lakini hata Bandari ya Mtwara tuna mradi ambao sasa tunajenga gati jipya lenye urefu wa mita 350 ambalo lenyewe litagharimu shilingi za Kitanzania bilioni 149 na Mkandarasi yuko kwenye site na kazi inaendelea. Hatukusimamia hapo, lakini tumeendelea na ujenzi wa matishari ambayo tuyatumia kwa ajili ya kupeleka mizigo katika bandari zetu za kule Kyela na maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna mradi wa ununuzi wa scanner ambapo tayari sasa scanner nane zimefika Dar es Salaam. Kwa mara ya kwanza katika Bandari ya Dar es Salaam mwaka huu tumeingiza scanner maalum kwa ajili ya reli. Pia tumeingiza scanner nyingine nne (mobile scanners) pamoja na scanner nyingine tatu ambazo gharama yake ni shilingi bilioni 52.2. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu flow meter, kazi tunaendelea nayo ya utaratibu wa ununuzi wa flow meter na hivi karibuni manunuzi hayo yatakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuwa na Bandari imara kama huna usafiri wa barabara imara. Kwa kulijua hilo, Serikali ya Awamu ya Tano tumeanza ujenzi wa reli ya kiwango cha standard gauge. Awamu ya kwanza imeanza Dar es Salaam mpaka Morogoro yenye urefu wa kilometa 300. Treni hii ni ya kipekee katika nchi za Afrika ya Mashariki na Kati. Treni hii itatumia umeme na itakuwa inakwenda mwendokasi wa kilometa 160 kwa saa. Itakuwa na uwezo wa kubeba tani milioni 17 kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu utagharimu takribani shilingi za Kitanzania trilioni 2.7. Jumatano hii Mungu akipenda, Wajumbe wa Kamati ya Bajeti na Kamati ya Miundombinu watatembelea eneo la ujenzi; na nawataka Wajumbe hawa watembelee usiku, ndiyo unaona raha ya ujenzi, siyo mchana. Pale watu wanafanya kazi saa 24 kwa wiki, siku saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitafurahi kama ninavyosema; na nimemwalika hapa Mheshimiwa atembelee lakini atembelee usiku, siyo mchana, kwa sababu usiku ndiyo utaona ile raha ya ujenzi wenyewe. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeanza awamu ya pili. Awamu ya pili inaanzia Morogoro mpaka Makutupora yenye urefu wa kilometa 442. Wiki iliyopita Serikali ililipa advance payment, yaani malipo ya awali dola za Kimarekani milioni 215 sawa na shilingi bilioni 483. Wakati wowote mwezi huu tutaweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa kutoka Morogoro mpaka Makutupora ili kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2020 ifikapo mwezi Juni, Watanzania wataanza kufurahia treni ya kisasa kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma ambapo sasa watatumia masaa mawili na nusu mpaka masaa matatu kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi haikuishia hapo tu, tunaendelea na mpango wa kuanzia Makutupora mpaka Tabora, Tabora - Isaka, Isaka – Mwanza. Tunatoka Tabora – Kigoma – Uvinza - Msongati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wiki mbili zilizopita, wenzetu wa Rwanda walikuja hapa na tuliweka makubaliano sasa ya kujenga reli ya kisasa kutoka Isaka mpaka Kigali yenye urefu wa kilometa 521 na tunategemea jiwe la msingi litawekwa mwezi Oktoba mwaka huu, kwa vile tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba Bandari ya Dar es Salaam tunaiboresha kwa miundombinu ya aina yoyote ili kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa usafiri wa anga; ili anga zetu ziwe salama tunajipanga tunanunua radar nne za kisasa ambapo radar moja itafungwa Dar es Salaam, moja itafungwa Mwanza, moja itafungwa Mbeya na nyingine itafungwa Kilimanjaro. Hiyo imegharimu takriban shilingi za Kitanzania bilioni 63. Tunafanya hivyo kwa sababu tunapoteza mapato mengi kwenye sehemu ya madini, watu wanaingia na ndege ndogo hatuwezi kuona.

Tunaamini sasa, tukiweka radar hizo za kisasa ndege yoyote itakayoingia Tanzania hasa ndege hizi za kiraia, tutaweza kuiona na tutakusanya mapato yanayostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa viwanja vya ndege; tunaendelea na ujenzi wa jengo la abiria pale Dar es Salaam ambalo litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria milioni sita ikilinganishwa na jengo la abiria terminal II lenye uwezo wa kuchukua abiria milioni mbili na nusu. Jengo hili litagharimu shilingi takriban bilioni 560 litakapomalizika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wakati mmoja kwenye jengo lile zitaweza kukaa ndege 22 kwa wakati mmoja. Kwa kweli ni jengo la kisasa ambapo kazi inaendelea na ujenzi umefika asilimia 70. Kwa upande wa Mwanza, tumetenga takriban shilingi bilioni 110 ambapo tunajenga runway na maegesho mengine kuhakikisha kwamba uwanja wa Mwanza sasa unakuwa uwanja wa Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa uwanja wa Shinyanga tumetenga shilingi bilioni 49.18 na Mkandarasi tumeshampata kwa ajili ya ujenzi. Kwa upande wa uwanja wa Sumbawanga tumetenga shilingi bilioni 55 na Mkandarasi tumempata. Kwa upande wa uwanja wa Songwe vile vile tumetenga bilioni 17 na kazi inaendelea. Uwanja wa Musoma, Songea na Iringa tayari tunahangaika kuwatafuta Wakandarasi kuhakikisha kwamba nako mambo yanakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali hii imejipanga kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwa kiwango cha lami. Sasa hivi kuna mradi unaendelea kutoka Katavi mpaka Tabora ambapo Serikali itatumia shilingi bilioni 770. Huu ni mradi mkubwa na tutajenga barabara ya kisasa. Pia kuna mradi unaendelea baina ya Katavi na Kigoma, Kigoma - Kagera, Kigoma - Tabora na mengineyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja ya Kamati yangu ya Miundombinu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono kwa asilima mia moja hoja ya Mheshimiwa Waziri ya Bajeti ya mwaka 2016/2017. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa namna unavyomsaidia Mheshimiwa Rais kuikuza nchi hii kupitia utatuzi wa migogoro ya ardhi kati ya wakulima, wafugaji, wawekezaji na maeneo ya hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri anisaidie katika Jimbo langu la Namtumbo katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezindua mji mdogo wa Lusewa tarehe 4/4/2016 kwa kumteua TEO na Maafisa Ardhi wapime. Tunahitaji mji huo mdogo upimwe na kuainisha maeneo ya matumizi mbalimbali. Mchango wenu unahitajika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jedwali namba 138 la hotuba ya Mheshimiwa Waziri katika ukurasa 144 inayosema Shirika la Nyumba limenunua ekari zao katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo si sahihi, NHC ilitengewa viwanja 40 katika eneo linalopakana na TANESCO, viwanja vya low density, lakini NHC hawajatoa fedha za fidia na kwa sababu NHC hawatoi ushirikiano wowote kuhusu fidia na mpango wao wa kujenga nyumba hizo, Halmashauri inakusudia kugawa viwanja hivyo kwa wahitaji wengine watakaokuwa tayari kutoa fedha za fidia. Masharti ya kuitaka Halmashauri izinunue nyumba zitakazojengwa na NHC na kulipa fidia hayajakubalika na kwa kweli hayatekelezeki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipaka ya hifadhi ya Sebu inapanuliwa bila ya taarifa kwa vijiji husika vinavyoguswa na upanuzi. Vijiji vinavyohusika ni vya Kitanda, Mpuka, Luhangano, Mhangazi, Nangero, Nambecha, Likuyu mandela na kadhalika. Vijiji hivyo vitatenga sehemu ya ardhi yao kama Hifadhi ya Jamii (WMA) chini ya umoja wao wa Mbarang‟andu. Hivi sasa wanavijiji husika wanataka kurekebisha mpaka wa WMA waliojiwekea mwaka 1992 ili kupata eneo zaidi la kilimo kufuatia kuongezeka kwa wakazi wa upande mmoja na upanuaji wa mipaka ya hifadhi za kitaifa za Selous Game Reserve na Undendeule Forest Reserve; upanuzi huo unaochukua maeneo ya WMA kwa upande wa pili. Mazingira haya yanaleta mgogoro unaoanza kukiathiri CCM kwa kupoteza kata ya Mputa na vurugu za wakulima kuchomewa nyumba zao na kufyekwa mazao yao mashambani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafadhali Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, Mbunge wa Isimani na Waziri mahiri tusaidie kuituliza Namtumbo na Halmashauri yake kwa kurekebisha kasoro hizo hapo juu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nawapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, hongereni sana kwa kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu. Niwaombe mnisaidie kutatua migogoro ya maeneo yaliyohifadhiwa na jamii (WMA) ya Kimbanda, Kisungura na Mbarangandu dhidi ya wananchi walioyatoa maeneo hayo. Wananchi hao walitegemea mipaka ya WMA hizo ingepitiwa upya baada ya miaka kumi, kama walivyoahidiwa lakini inaonekana hakuna mpango wowote wa kupitia upya mipaka hiyo. Wananchi wameongezeka na wanahitaji maeneo zaidi kwa shughuli za kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naomba mridhie kuachia eneo linalogombaniwa kati ya Chuo chenu cha Likuyu Sekamaganga (Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi), hususan eneo ambalo halitumiwi na chuo hicho na limevamiwa na wakulima wakazi wa kijiji cha Kikuyu Sekamaganga. Eneo husika lilikuwa ni sehemu ya eneo la kijiji hicho na lilichukuliwa bila ya kulipiwa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri aliyetembelea kijiji cha Likuyu Mandela kilichokumbwa na uharibifu wa mashamba uliofanywa na tembo ambapo baadhi ya wanakijiji hao kupoteza maisha kwa kuvamiwa na tembo hao. Naomba ahadi ya kulipa kifuta machozi na kipangusa jasho kwa waliouawa na tembo na walioliwa mazao yao na tembo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono kwa asilimia mia moja na nawataka utekelezaji mwema.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu hongera kwa kazi nzuri unayoifanya wewe na Naibu wako na watendaji wako. Ni kazi iliyotukuka hadi mmewezesha Namtumbo tutarajie kuwa na huduma za upasuaji kupitia Kituo cha Afya cha Namkumbo kinachotarajiwa kukamilika kujengwa tarehe 31 Mei, 2018. Ahsante ninyi ndio mlitafuta fedha za ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Namtumbo ni Wilaya kubwa nawaomba mtutafutie fedha zaidi kwa ajili ya kuendeleza nguvu za wananchi kupitia Halmashauri yao ya Namtumbo kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya vingine viwili vya Lusewa na Mtakanini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Lusewa kiliahidiwa kukamilishwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne pamoja na Makamu wa Rais wa Awamu ya Tano. Ni vyema ahadi hiyo ikatekelezwa ili wananchi wa Lusewa na Tarafa nzima ya Sasawala waache kuwabeba akina mama wajawazito wanaoshindwa kuzalishwa na waganga wa kienyeji kupakiwa kwenye baiskeli ndani ya matenga au machakacha kupelekwa Kiuma (Tunduru); Mbesa (Tunduru) au Songea umbali wa kilometa 72, 95 na 150; Mtawalia na ni wazi huwa hawafikishwi katika maeneo hayo yenye huduma ya upasuaji na huishia kugeuza safari, mama akibadilishwa jina kwa kuanzia na marehemu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kituo cha Mtakanini kiliombwa na Marehemu Mheshimiwa Rashid Mfaume Kawawa kwa Rais wa Awamu ya Tatu na Rais huyo Mheshimiwa Benjamin William Mkapa kukubali ombi hilo mbele ya familia na wanakijiji wote wa Mtakanini na ikakubaliwa kuwa ndio kiwe Kituo cha Afya cha Kata ya Msindo. Aidha, kituo hicho kitahudumia kata tatu, Kata za Msindo, Hanga na Namabengo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Rais kuikabidhi Wizara hii kwa Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, Mbunge ambaye ni mbobevu wa hifadhi za wanyamapori na misitu. Naamini tembo wa Selous Game Reserve sasa wamepata mlinzi na naahidi kwa eneo la Namtumbo nitamsaidia kwa uwezo wangu wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba atusaidie wakazi wa Wilaya ya Namtumbo katika masuala yafuatayo:-
(i) Vijiji saba vya Jumuiya ya Mbarang‟andu na vijiji vingine vinavyounda jumuiya mbili, nyingine za Kimbanda na Kusangura vinahitaji kuhuisha mipaka yao ya WMA ili kutoa fursa ya ardhi ya kilimo. Wananchi wameongezeka, wanahitaji maeneo zaidi ya kilimo kwa ajili ya kujikimu kimaisha. Muda wa kupitia upya mipaka hiyo ilikubalika miaka kumi na hadi sasa miaka imezidi bila kufanyika kwa makubaliano hayo ya kupitia upya mipaka hiyo ya WMA.
(ii) Watumishi wa Selous Game Reserve wameonekana wakiweka beacons ndani ya maeneo ya vijji vya Mputa, Luhimbalilo, Luhangano, Mhangazi, Kitanda, Nangero, Mtumbatimaji na Nambecha na hivyo kutishia ama kuenea uvumi wa maeneo yao kuchukuliwa, yaani kupanua mipaka ya hifadhi na kuingilia WMA na mashamba ya wanavijiji bila taarifa yoyote kwao. Nitashukuru kama wananchi hao watahakikishiwa usalama wa maeneo yao.
(iii) Vijiji vinavyoizunguka Selous Game Reserve, Undendeule Forest Reserve na Lukwika Forest Reserve wala Halmashauri yetu ya Wilaya Namtumbo hainufaiki na uwepo wa hifadhi hizo. Namuomba Mheshimiwa Waziri atufikirie kama ilivyo kwa wenzetu wanaozunguka hifadhi za Kaskazini.
(iv)Operesheni Tokomeza imewaacha baadhi ya wakazi wa Namtumbo bila silaha zao walizokuwa wakizimiliki kihalali kwa mujibu wa sheria na walielekezwa wakazikabidhi kwa uchunguzi na hadi leo hawajarudishiwa bila maelezo yoyote. Naomba Mheshimiwa Waziri silaha hizo warudishiwe waliokuwa wakizimiliki ili waendelee kuzitumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Waziri kwa kutusikiliza na kutujali. Tafadhali Waziri chapa kazi ukimshirikisha Naibu wako Mheshimiwa Engineer Ramo Makani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilichangia kwa maandishi masuala manne yaliyojitokeza kwa nguvu kipindi cha Kampeni ya Uchaguzi Mkuu. Leo asubuhi Mkuu wa Wilaya ameniomba nikueleze yafuatayo ambayo kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama yanasumbua sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana hiyo alitembea Kijiji cha Likuyu Mandela ambacho asili yake ni waliokuwa wakimbizi kutoka Msumbiji na wamepata uraia wa Tanzania. Tembo wanaingia majumbani wanaipua hata mahindi yaliyoko jikoni. Mazao yao yamekuwa yakiliwa kila mwaka na maombi yao ya kulipwa fidia au kifuta jasho hayajashughulikiwa toka mwaka 2011. Wiki iliyopita mkazi mmoja ameuawa na tembo. Hiyo ni moja kati ya matukio ya karibuni ya madhara ya tembo ambao idadi yao imeongezeka sana baada ya ujangili kudhibitiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba hoja za wakazi hao wa kijiji cha Likuyu Mandela zipatiwe ufumbuzi. Aidha, kijiji hicho kisaidiwe chakula na itafutwe njia nzuri ya kuwazuia wanyamapori kutovuka mipaka ya hifadhi hata kwa kutumia uzio wa umeme kama inavyofanyika katika nchi za wenzetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hoja hii iunganishwe na hoja zangu nyingine nne za jana nilizochangia vilevile kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Namtumbo na mimi mwakilishi wao tunaiunga mkono hii hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kwa niaba ya wananchi wa Namtumbo kukuomba radhi kwa kauli ya kiongozi wetu wa Wilaya aliyedai eti Mheshimiwa Waziri wa Kilimo pamoja na sisi viongozi wa Wilaya ya Namtumbo wa Chama na Serikali tunawadhulumu wakulima wa tumbaku kwa kuwakopesha mbolea kwa bei ya juu tofauti na iliyotangazwa na Serikali na kwa kuwacheleweshea mbolea hiyo. Tumempuuza kwa sababu najua kabisa na wala hataki kujua utaratibu wa msimu wa kilimo cha Tumbaku ulivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri ili aelewe vizuri tatizo tulilonalo kiongozi wetu huyo wa Wilaya alitembelea mashamba ya mpunga yanayolimwa na wakazi wa Kata ya Mchomono na alipoona mpunga ulivyostawi akadhani ni magugu na akatoa amri magugu hayo yateketezwe kwa kutumia kemikali ya kuunguza magugu iliyotolewa na NGO ya PAMS Foundation ya Wajerumani na Wajerumani hao walitoa dawa husika na ikanyunyiziwa kwenye mashamba ya wakulima hao wa mpunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hao hawajui wataishije kufuatia tendo hilo la kiongozi wetu Luckiness Adrian Amlina, DC wa Namtumbo. Nikuombe utumie nafasi yako kumjulisha Mheshimiwa Rais atuondolee adha hii ili wananchi wa Namtumbo waendelee kuishi kwa kutegemea mavuno ya mashamba yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Mheshimiwa Dkt. Charles Tizeba, Waziri wa Kilimo tunashukuru kwa kutuwezesha kumpata mnunuzi wa tumbaku ya Moshi, Kampuni ya Premier Leaf Tanzania Limited. Ulitoa kibali kwa kampuni hiyo kusafirisha green leaf nje ya nchi kwa miaka miwili kwa masharti kuwa katika kipindi hicho wajiandae kuchakata tumbaku nchini na maandalizi wameanza kwa kushirikiana na SONAMCU kufufua kiwanda cha kusindika tumbaku cha Songea. Ungekosa kutoa kibali kile kampuni hiyo haingeingia mkataba wa kununua tumbaku Namtumbo na Songea na hivyo kutuwezesha kulima tumbaku mwaka huu na miaka itakayofuata na hivyo kufufua zao hilo la kibiashara na la muda mrefu huko nyuma. Mwezi ujao tu pesa zitaingia Namtumbo kupitia kufufuliwa kwa zao hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri udumu kuhudumu katika Wizara hii. Amina!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii. Kwa kweli kazi uliyoifanya umeliletea heshima Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nieleze tu eneo moja dogo. Kwa kawaida wenzetu wa upande wa pili wanapochangia, hata wakisema maneno mabaya kiasi gani upande huu wanakaa kimya. Tunapochangia sisi wanaanza kutuzomea hata michango yetu haisikiki. Naomba na hili nalo tulidhibiti. Tukilidhibiti hilo Bunge hili litakuwa zuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Dkt. Philip Mpango kwa mipango yake kabambe na hasa katika miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujibu maswali machache ambayo Waheshimiwa Wabunge wamechangia. Moja, kuhusiana na bandari bubu. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Serikali imejipanga kudhibiti bandari bubu. Kama mtakumbuka hivi karibuni nilijibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge wa Mtwara; kwamba tuna vikao vinavyoshirikisha Serikali za Mwambao pamoja na Zanzibar kuhakikisha tunazitambua bandari zote bubu na hatimaye kudhibiti mapato yanayopotea kupitia hizo bandari bubu. Tutaendeleza na katika Maziwa Makuu. Kazi hiyo tutaifanya kwa kasi, mwaka huu ujao wa fedha hiyo kazi lazima ikamilike.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee TTCL. TTCL naomba niwaote wasiwasi. Tulivyojipanga Wizarani na ndani ya Serikali TTCL mnayoiona sasa, TTCL mliyoizoea kuanzia mwezi wa Tisa itakuwa ni TTCL tofauti kabisa. TTCL hii itaingia kwenye kusambaza teknolojia za simu na mitandao ya 2G, 3G na 4G kuanzia Dar es Salaam na mikoa mingine tisa mpaka mwezi Desemba mwaka huu na miaka inayofuata tutasambaza Tanzania nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hilo, na kwa sababu Mkongo wa Taifa uko chini yetu hatutakuwa na mshindani. Tutashindana kibiashara na sisi tutaingia katika mashindano ya kutoa vifurushi, kwa sasa hatujaanza kutoa. Nawahakikishia TTCL hii itakuwa tofauti kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha alivyoniahidi, madeni yote ya TTCL yatalipwa na baada ya hapo tunaiwezesha TTCL si kwa mtaji, kwa namna tulivyojipanga sasa wala hawahitaji mtaji tena, wanaingia kwenye biashara za ushindani na tuna makamanda pale. Baadhi tutawaondoa ili tuhakikishe kile tunachokikusudia katika TTCL kinapatikana katika muda mfupi na hatimaye Serikali nzima itatumia huduma za TTCL.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee TEMESA nayo. Nayo tuna mipango kabambe ya kuibadilisha. Zile tabia za ajabu ajabu za kudhani TEMESA haina mwenyewe zitakwisha. Masuala ya kuvuruga vuruga, mtu analeta gari zima linatoka bovu mwisho wao ni mwaka huu, baada ya mwaka huu hali itabadilika na Serikali itapunguza matumizi kwa kutumia huduma za TEMESA.
Mheshimiwa Naibu Spika, TRL na RAHCO. Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea kuhusu kuunganisha TRL na RAHCO. Wametoa maelezo marefu, Serikali imeyachukua. Lakini, upande wa pili hawauongelei sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tuna mpango wa kujenga reli kutoka Tanga hadi Musoma, tuna mpango wa kujenga reli kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay, tuna reli ya TAZARA, tuna reli ya Kati na matawi yake yote. Hapa ni wajibu wa Serikali na ushauri wenu tutauchukua, kuamua je miundombinu hiyo ya reli zote isimamiwe na TRL peke yake? Kuna faida lakini vile vile kuna hasara zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia upande wa hasara, ujenzi wa miundombinu unahitaji fedha nyingi sana na fedha hizo sehemu kubwa tutazipata kupitia mikopo. Mikopo hii ikikaa TRL kazi yao ya kutoa huduma inaweza ikakwamishwa kutokana na ukubwa wa madeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunadhani TRL ifanye kazi ya kutoa huduma halafu RAHCO kiwe ndicho chombo cha Serikali cha kuwekeza na tutakopa mikopo yote itaingia RAHCO ili TRL iweze ku-operate kibiashara. Kama nilivyosema, kupanga ni kuchagua, tumesikia maoni yenu, tutayajadili ndani ya Serikali na hatimaye uamuzi utatoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ATCL. Kuna baadhi walichangia kuhusu ATCL. Tutafanya kazi ya kuirekebisha ATCL, tutafanya kazi ya kuibadilisha ATCL. Tatizo kubwa la ATCL liko kwenye mindset. Tutafanya kazi ya kuondoa matatizo ya kwenye mindset ili tuwapate watu ambao wana fikra za kibiashara waweze kutusaidia tuweze kuinua na kuisimamisha ATCL iweze kutoa huduma za usafiri. Kwa kweli, ndege nyingi zinatumia sana fedha za Serikali na fedha za Serikali zinakwenda nje na tunalazimisha kulipa hela nyingi sana kwa gharama za usafiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiweza kuimarisha ATCL kwanza tutatoa ushindani kwa nchi, lakini vile vile tuta-save fedha nyingi sana zinazopotea sasa kutokana na gharama ambazo hawa wenzetu wachache wanajipangia kwa namna wanavyotaka wao. Naomba tushirikiane tuifanye kazi ya kuibadilisha ATCL iweze kutusaidia kwa namna ambavyo tunataka.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nirudi tena kwenye TTCL. TTCL mnafahamu kwamba tulikuwa na partnership na Bharti Airtel. Hivi sasa tunaongelea tutaanza mwezi wa Tisa kwa sababu kwanza tunalitatua hili tatizo la Bharti Airtel na tuna uhakika itakapofika mwezi wa Saba tatizo hili litakuwa limekwisha, TTCL itamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, ndipo tutakapoanza kuingiza hiyo mitaji na mitaji haitoki Serikalini, inatoka kama mkopo, TIB anafanya Syndication na makampuni yanayotoa Service kama vile Alcatel, ZT ya Japani pamoja na Huawei. Watu wa TIB wanatusaidia kufanya Syndication na ndiyo mtaji tutakauotumia kuibadilisha TTCL.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na hayo machache na nakuomba sana tena sana utusaidie kulirekebisha Bunge hili. Uwezo unao, umeanza vizuri na naamini hili eneo dogo lililobakia tukilikamilisha kulirekebisha, Bunge hili litakuwa na heshima inayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja na ahsante sana kwa kunipa fursa.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika,
nakushukuru kwa kunipa nafasi, na niseme mapema kabla sijagongewa kengele,
nimefurahishwa sana na Taarifa ya Kamati ya Miundombinu na yote mliyoyaandika
tutayazingatia kwa umakini kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge
wote kwamba mambo yote ambayo mmetuambia iwe kuhusu barabara, mawasiliano,
tutayafatilia kama ambavyo mmetuelekeza. Najua hii ni taarifa ya Kamati, lakini mmetupa fursa
na sisi tusikie yale ambayo mnahitaji kuyasikia. Na tumeyasikia, tutayachukua na tutayafanyia
kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda tu niende kwa haraka sana katika maeneo machache.
Kwanza naomba sana Waheshimiwa Wabunge wale wa upande wa Mtwara, walioongelea
barabara ya Mtwara hadi Mnivata, naomba nitoe taarifa rasmi kwamba ni kweli mkataba
umesainiwa tarehe 19 Januari. Taarifa ambayo tulikuwa tumetoa mwanzo ilikuwa inazingatia
taarifa mpaka tarehe 31 Disemba, 2016, ambacho ndicho kipindi tulichokuwa tunakitolea
taarifa. Naomba nitoe taarifa rasmi kwamba huo mkataba umesainiwa. Na ninamshukuru sana
AG personally kwa namna alivyofuatilia kuhakikisha kazi ya kukamilisha kile kipengele kidogo
ambacho kilikuwa kinaleta matatizo amekishughulikia kwa haraka sana. Nakushukuru sana AG.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, ningependa vilevile kuongelea suala
la ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Mtwara nikianzia na cha Mtwara, kazi ya
usanifu imeshakamilika hivi sasa taarifa ya mwisho inafanyiwa kazi na wataalam na mara
watakapoikamilisha tutaenda kwenye hatua inayofuata ya kutafuta fedha kuanza ukarabati.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwa viwanja vya Tabora, Sumbawanga, Shinyanga na
Kigoma, fedha tunazo kwa sababu tuna hela kutoka European Investiment Bank na suala la
mikataba hivi sasa tunavyoongeelea ndio tupo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha
uchambuzi, umeshafanyika, muda sio mrefu watatoa taarifa ya akina nani watakuwa
wameshinda katika maeneo hayo na kazi ya ukarabati wa viwanja hivyo vinne ianze. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu kwa viwanja vya Musoma, Iringa na Songea,
usanifu na ukarabati pamoja na usanifu kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa viwanja hivyo nao
upo katika hatua ya mwisho. Taarifa itakapokamilika zabuni zitatangazwa kwa ajili ya ukarabati
na upanuzi wa viwanja hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye kiwanja cha Mwanza, walisimama muda mrefu.
Nimshukuru Mheshimiwa Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango, ametuwezesha tumelipa
shilingi bilioni 7.6 na kazi ya ujenzi wa kiwanja kile cha Mwanza sasa imeanza kuchangamka
zaidi. Tunashukuru sana kwa hilo na tunaomba wenzetu wa Fedha waendelee kutupa hela zaidi
tuondoe maeneo yale yote ambayo tunadaiwa, ili kazi hii ya kujenga miundombinu kwa ajili ya
Watanzania tuweze kuikamilisha kwa haraka kwa sababu tunataka tufanye hivyo, lakini wenzetu wa Hazina ndio wanaotuwezesha. Nishukuru kwa kiwango hicho mlichotuwezesha
hadi sasa na ninaamini mtaendelea kutuwezesha zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, na vivyo hivyo kwa Kiwanja cha Songwe tulichokamilisha,
kwanza ni usimikaji wa Taa za kuongozea ndege, hiyo tumekamilisha. Kilichobakia ni ujenzi wa
jengo la abiria na ambalo tulikuwa na ubishani kidogo au kuna mgogoro kidogo wa malipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nashukuru suala la mgogoro huo limekaribia kukamilika,
tupo katika hatua ya mwisho ya kusainiana kwamba, ni kiasi gani tuliwalipa zaidi na hivyo
waanze sasa kujenga kwa kiasi kile tulichowalipa zaidi, na bahati nzuri sasa tumeanza
kuelewana. Mwanzo tulikuwa hatuelewani na ndio maana tumechelewa kidogo katika kuanza
kujenga kiwanja hicho cha Songwe, sasa tumefikia mahali pazuri, naamini tutafika mahali sasa
kiwanja hiki nacho kitakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kidogo kuhusu TCAA; labda kitu kimoja tu, kuhusu
radar. Najua kuna wachangiaji wa maandishi wanatuletea, naomba tu nao niwathibitishie
kuwa ujenzi wa radar au usimikaji wa radar katika sehemu kuu nne za Tanzania, kwa maana ya
Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mwanza na Songwe, mkataba wake tunatarajia muda si mrefu, sasa
hivi zipo katika process za procurement, nina uhakika katika kipindi kisichozidi wiki mbili tutakuwa
tumefika hatua nzuri na mwezi Machi mjenzi wa hizo radar itapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu ni kuhakikisha Tanzania yetu inakuwa covered na
radar. Si sahihi nchi yetu iwe inaangaliwa na Kenya, iwe inaangaliwa na Rwanda na sisi
wenyewe tupo kwenye giza. Hatutakubali hilo, na tunahakikisha katika miaka miwili ijayo
Tanzania yote tutakuwa tumei-cover kwa radar na tutakuwa tume-recover yale maeneo
ambayo wenzetu walikuwa wajanja, waliwahi kuwekeza katika radar na wakaanza kupata
mapato ambayo kwa kweli, yalistahili kuja katika nchi yetu; tutahakikisha mapato hayo
tunayarudisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu kwa upande wa mawasiliano; ninawashukuruni
sana kwa mambo mengi mnayotusaidia. Kulikuwa na tatizo kubwa sana kwenye Kampuni ya
Halotel, tumewapa mikataba ya kuweka mawasiliano katika vijiji mbalimbali karibu 4,000 lakini
mmekuwa mkitupa taarifa (mrejesho) kwamba hapa wanasema wameweka na wakati
mwingine ninyi Wabunge mnatuambia kwamba mawasiliano hayapo. Sasa nashukuru
kuwaambia kwamba tuna mitambo imeagizwa na taasisi yetu ya TCRA sasa ina uwezo wa
kupita kuhakiki katika kila maeneo ambayo wenzetu makampuni ya simu yamepewa kazi ya
kuweka mitandao hiyo, hawawezi kutudanganya tena kwa kuwa tutakuwa na uwezo wa
kuhakiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa hilo na
tunawahakikishia hivi vijiji 4,000 lazima tukamilishe itakapofika mwezi Novemba, kama mkataba
ambavyo tulikubaliana na watu wa Halotel. Vilevile niwambie tu kwamba hata Vodacom, Airtel
na TiGo, mwanzo waliokuwa wanadai kwamba, vijijini hakuna fedha kwa hiyo, hawataki
kwenda, sasa hivi wanavyoona jinsi Halotel wanavyochangamkia maeneo ya vijijini na jinsi
anavyo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kweli, naunga mkono sana na sasa naelewa
kwa nini nina Maprofesa upande wa Kamati na upande wa Wizara. Nawashukuruni sana kwa
kazi kubwa mnayoifanya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai, hatimaye nimepata fursa hii kupitia wewe ya kuchangia hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Niombe kuchukua fursa hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano, Rais wa hapa kazi tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Profesa Makame Mnyaa Mbarawa kwa kazi kubwa anayoifanya ikiwa ni pamoja na kunifundisha mimi siasa. Nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie baadhi ya michango ambayo ni kuongezea au kukazia ambayo wamechangia wenzangu. Moja, ni kuhusu barabara inayounganisha Mikoa ya Morogoro na Ruvuma kupitia Wilaya yangu ya Namtumbo. Barabara hii tulitoa matumaini mwaka jana mwezi Julai kwamba imetoboka na kwa matumaini yale kuna watu wamepoteza maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri nimemwandikia kilichotokea, naomba atusaidie kuikata zaidi ile barabara ili iweze kupitika, tuanze kupita kwa magari na pikipiki kabla hiyo lami haijaanza. Najua lami ni Ilani ya Uchaguzi ya Serikali ya Awamu ya Tano lakini vilevile ilikuwa Awamu ya Nne na tulianza usanifu Awamu ya Tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, katika kipindi kifupi ameiwezesha barabara hii kukamilika kwa maana ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, umekamilika. Najua hii ni hatua kubwa sana katika ujenzi wa lami wa barabara hii. Nimwombe sana anisaidie kukikata kile kipande cha kuanzia Kilosa Kwampepo mpaka Londo ili tuweze kupita kutoka pande zote mbili; tukitoka Namtumbo kwa maana ya Kitanda, lakini vilevile tukitokea Kilosa, Kwampepo ambako sisi kule ndiyo nyumbani kwetu, kule ndiyo kuna mizimu yetu. Naomba sana atusaidie ili tuweze kufika katika maeneo ambayo ndiyo tunayaabudu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Profesa Makame Mnyaa Mbarawa kwa jinsi alivyonisaidia kukubali kuanza kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa kampeni. Ni kiongozi pekee aliyepita Barabara ya Mtwara - Pachani – Ligera – Lusewa – Magazini – Likusanguse hadi Nalasi wakati wa kampeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana kwa kutoa fursa hii ya kuanza kutekeleza ahadi hii kwa kumpata mkandarasi wa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Namshukuru sana hii kazi inaendelea na naomba waendelee kutenga fedha ili Mhandisi Mshauri huyo aweze kuikamilisha hiyo kazi kwa wakati kwa maana ya mwakani, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Profesa Makame Mnyaa Mbarawa kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ameuwezesha kwa namna ya ajabu kabisa kukamilisha mawasiliano kwa sehemu kubwa sana ya Wilaya ya Namtumbo. Nimwombe tu Mheshimiwa Waziri, akamilishe kipande hiki kidogo kilichobakia, tumebakiwa na kata kama tatu hivi ambazo hazina mawasiliano, mpaka leo bado wanalazimika kupanda kwenye miti au kusafiri umbali wa kilometa tatu, nne ili waweze kupata mawasiliano. Nimwombe Mheshimiwa Waziri anisaidie kupitia Mfuko huu wa Mawasiliano kwa Wote tukamilishe mawasiliano kwa Wilaya nzima ya Namtumbo kama ambavyo alianza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri; kuna ahadi imetolewa na Taasisi yake ya TEMESA kutujengea kivuko. Sisi tunapakana na Msumbiji kwa maana ya Wilaya ya Namtumbo na tuna kivuko cha zamani sana, enzi na enzi, kinachotumika kufanya biashara kati ya Wilaya ya Mavago ya upande wa Msumbiji na Wilaya yetu ya Namtumbo. Nimwombe sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa hii na nikushukuru kwa fursa uliyonipa. Kwanza kabisa, naunga mkono hoja hii asilimia miamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze na suala la upigaji chapa kwa sababu muda wenyewe ni mfupi. Kule kwangu Namtumbo nimepata malalamiko mengi sana ya waliopigiwa chapa. Chapa imepigwa na kuna data/taarifa fulani katika kile chuma wanachopigia chapa, lakini kila chapa iliyopigwa ng’ombe wale wameendelea kutibiwa na hakuna takwimu yoyote inayoonekana katika ile chapa zaidi ya kidonda. Kwa hiyo, hata utambuzi kwamba huyu ng’ombe ni wa Wilaya fulani haupo kutokana na namna chapa ya moto ilivyokuwa inapigwa zaidi ni kidonda tu.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea kwamba njia inayotumika katika kupiga chapa siyo sahihi. Naomba kabisa jambo hilo lirekebishwe, itafutwe njia nyingine ya kuwatambulisha ng’ombe lakini siyo kuwachoma moto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, kwetu sisi Namtumbo eneo letu ni dogo sana, zaidi ya asilimia 67 ni hifadhi, tumeletewa ng’ombe kupita kipimo. Ng’ombe wamekuja wengi sana na matokeo yake wameleta ugomvi mkubwa sana kwa wale wakulima ambao sehemu kubwa ya Wana Namtumbo ni wakulima zaidi ya asilimia 90, inaleta ugomvi mkubwa sana. (Makofi)

Mimi sielewi, sijui kwa nini wafugaji hawatofautishi kati ya mpunga na magugu. Wanasema haya ni magugu, hizi ni nyasi, wakati ule ni mpunga. Wanasema hizi ni nyasi wakati yale ni mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe sana Namtumbo hatuna eneo, wale ng’ombe ambao wameingizwa naambiwa kwamba walijazwa kwenye hifadhi, kwa hiyo walikuwa wanakula kwenye hifadhi hakukuwa na ugomvi. Kwa maana nyingine ng’ombe wengi walikuwa wanakula ndani ya hifadhi na wakulima walikuwa wanalima eneo lao. Sasa wale ng’ombe wameondolewa kwenye hifadhi wanakwenda wanavamia eneo la wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe sana tena sana mtusaidie kutatua tatizo hili. Njia pekee ya kutatua tatizo hili ni kuwaondoa wale ng’ombe au turuhusu wale ng’ombe waendelee kukaa ndani ya hifadhi kwa sababu sisi wakulima hatuingii kwenye hifadhi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, Profesa Makame Mbarawa, hongera sana kwa kazi kubwa na ya kutukuka unayoifanya wewe na timu yako ya Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi zote. Hakika mnatubeba wananchi, CCM wote chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Mwenyezi Mungu aendelee kuwabariki, Amen.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, naomba tu nikumbushie masuala yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara ya Lumecha – Kitanda – Londo – Kilosa kwa Mpepo hadi Lupiro kwa kiwango cha lami, barabara hiyo inaunganisha Mikoa ya Ruvuma na Morogoro kupitia Wilaya za Malinyi na Namtumbo ambao ni majirani wa asili wanaounganishwa kwa njia ya miguu tangu enzi za Wajerumani na Waingereza waliokuwa wakiitumia kusafirisha manamba kwa ajili ya kilimo cha mkonge katika Mikoa ya Pwani na Tanga. Tunaomba ujenzi uanze Lumecha kuelekea Londona - Lupiro ambapo kuna daraja linalotenganisha Wilaya na Mikoa hiyo miwili na hivyo kutekeleza Ilani ya CCM ya 2015/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tukisubiri lami iliyoahidiwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, tunaomba juhudi za kutoboa na kuchonga kipande cha barabara kuanzia Londo hadi Kilosa kwa Mpepo zingeharakishwa ili barabara hiyo inayounganisha Wilaya ya Namtumbo (Ruvuma) na Wilaya ya Malinyi (Morogoro) ianze kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanadhani barabara hiyo imetoboka na hivyo inapitika, kumbe bado haijachongwa na kusababisha wanaotamani kuitumia na kuanza kupita kwa gari ama pikipiki kudhurika kama ilivyotokea kwa Padri wa Hanga Monaskeri aliyetumia pikipiki ambayo ilikwama na hatimaye kutembea kwa miguu hadi kifo kilipomfika kwa sababu ya uchovu na njaa ya siku zaidi ya tatu. Nikuombe Waziri mpendwa, Mheshimiwa Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, ushirikiane na Katibu Mkuu wako, Engineer Nyamhanga mtusaidie fedha za kukamilisha uchongaji wa kipande hicho cha barabara ili ianze kupitika. Mameneja wa TANROADS Mikoa ya Ruvuma na Morogoro wana dhamira ya dhati ya kuifanya kazi hiyo lakini wanakwamishwa na ukosefu wa fedha za kutosheleza ukamilifu wa kazi hiyo ya kuchonga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, nashukuru kwa kumlipa advance payment Mhandisi Mshauri wa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Mtwarapachani – Likusanguse – Nalasi hadi Tunduru ili ijengwe kwa kiwango cha lami kama ilivyoahidiwa na Waheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Serikali hii ya Awamu ya Tano waliofanikiwa kupita katika barabara hiyo na kujionea wingi wa wakazi wanaotegemea barabara hiyo na fursa kubwa zilizopo katika maeneo hayo. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri uendelee kuwalipa certificates zao za kazi ili kazi hiyo ikamilike mwakani kama ilivyokubalika katika mkataba na ujenzi kuanza kwa wakati. Hivyo, naomba fedha za kutosha zitengwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, naomba ahadi ya kukipeleka Kivuko cha Ruhuhu kihamishiwe eneo la custom katika Kijiji cha Magazini, Wilaya ya Namtumbo ili safari za wakazi wa Namtumbo, Tarafa ya Sasawala na wakazi wa Tunduru Kusini, Nalasina Mbesa wapate kivuko salama cha kuwapeleka katika vijiji vya Wilaya ya Mabhagho nchini Msumbiji kwa shughuli za kijamii na kibiashara. Vilevile kwa wananchi wa Mabhagho kuja Mkoani Ruvuma kwa shughuli za kibiashara na kijamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, nikuombe uiwezeshe TANROADS Mkoa wa Ruvuma kifedha, watekeleze miradi ya barabara zao ikiwa ni pamoja na barabara za Wilaya ya Namtumbo kama vile Namtumbo – Likuyu – Mkuju kunakojengwa Mgodi wa Madini ya Urani, Utwango – Namabengo – Mbimbi – Luegu, Mkonya – Mgombasi – Nangero – Naikesi na Mkongo Nakawale – Matimila – Mleke. Barabara hizo zipo maeneo ya kiuchumi ya Wilaya ya Namtumbo na zinahudumia wakazi wengi wa Wilaya hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, UCSAF na TCRA wanatekeleza majukumu yao vizuri katika eneo langu na ninawaomba tu watekeleze ahadi zao kwa wananchi wa Namtumbo kupitia mimi Mbunge wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kijiji cha Lumecha wanaleta tena changamoto ya ardhi yao ya shamba la Likenangena waliyoikabidhi kwa Kampuni ya Tumbaku waliyoiazima kwa ajili ya kuandaa mbegu za tumbaku. Baada ya kusitisha kuendelea na uzalishaji wa mbegu za tumbaku Kampuni hiyo ya TLTC ambayo kwa sasa wamehamia Morogoro hawajairudisha ardhi hiyo ya Likenangena kwa wenyewe, yaani Kijiji cha Lumecha, Kata ya Msindo, Wilaya ya Namtumbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hao hawana uwezo wa kuwafuatilia Kampuni ya TLTC huko Morogoro, wanamwomba Mheshimiwa Waziri awasaidie wananchi hao warudishiwe ardhi yao waweze kuitumia kwa kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, historia ya shamba hilo ni ndefu na Mheshimiwa Waziri anao uwezo wa kuipata kupitia watalaam wako wa ardhi wa kuanzia Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Mkoani Ruvuma hadi hapo Wizarani. Wananchi hao kila wakitoa changamoto yao kwa wataalam wako, wataalam hao wanasikiliza lakini hawafanyi chochote cha kuwasaidia wananchi hao wakidhi haja zao. Ardhi hiyo ilitolewa bila malipo yoyote na hivyo dhana ya kuwa ardhi hiyo ni mali ya TLTC haikubaliki na haipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri William Vangimembe Lukuvi, Mbunge wa Isimani mwenye dhamana ya Ardhi, anisaidie wananchi wa Kijiji hicho cha Lumecha wapate haki yao, warudishiwe ardhi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ninalo tatizo la pili, katika Jimbo langu ambalo ni Wilaya yote ya Namtumbo tatizo lenyewe limesababishwa na Wizara yako kutoa Hatimiliki kwa Chuo cha Wanyamapori cha Likuyu- Sekamaganga kwa eneo kubwa lililochukuliwa na eneo la Kijiji cha Likuyu-Sekamaganga linalotumiwa na wanakijiji hao kwa shughuli za kilimo cha mazao mchanganyiko bila ya kuwahusisha wanakijiji hao wenye ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipaka ya ardhi ya Chuo hicho ilipanuliwa na kuchukua ardhi ya kilimo cha wakazi wa Kijiji cha Likuyu-Sekamaganga bila ya ridhaa yao, matokeo yake baada ya hatimiliki kutolewa na Kamishna wa Ardhi, Uongozi wa Chuo hicho umekuwa ukiwatumia Askari Wanyamapori kuwanyanyasa wakulima wa Kijiji cha Likuyu-Sekamaganga huku wakiwafukuza katika ardhi yao na kupelekwa mahabusu kwa makosa ya kutungwa. Hatimiliki ya ardhi iliyotolewa katika ardhi yao wanakijiji kwa chuo ndiyo kinga ya kuwapiga na kuwanyanyasa wanakijiji hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ninakuomba kero hii uichunguze kwa umakini na hatimaye utoe haki kwa kurekebisha mipaka ya eneo lililotolewa hatimiliki kwa chuo kwa kuondoa eneo ambalo siyo sehemu ya chuo bali ni eneo la kilimo kwa wakazi wa Kijiji cha Likuyu- Sekamaganga ndani ya mipaka ya kijiji hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha ili alifanyie kazi Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, Mbunge wa Isimani mwenye dhamana ya ardhi nchi hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa taarifa ya awali kabisa kuwa naunga mkono hoja hii ya Mhesahimiwa Profesa Joyce Lazaro Ndalichako (Mb) Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa asilimia mia moja. Aidha, nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa William Ole Nasha (Mb) Naibu Waziri wake kwa kazi nzuri anayoifanya ya kumsaidia Waziri wake kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika Profesa Ndalichako amethubutu kutembelea Wilaya ya Namtumbo na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha VETA kinachojengwa katika eneo la Suluti, Wilaya ya Namtumbo. Niombe radhi kwa niaba ya wananchi wa Namtumbo waliojipanga kumpokea lakini walichelewa kuja au tuseme kwa fikra za wananchi hao Mheshimwa Waziri aliwahi sana kuingia Wilayani humo, akizingatia kauli mbiu ya kipenzi cha wana Namtumbo Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wetu ya “Hapa Kazi Tuu!

Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako (Mb) wananchi wangu watafurahi sana kama utawapa fursa ya kukukaribisha kama mkombozi wao kwa kuwazawadia mambo makubwa yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni ujenzi wa Chuo cha VETA katika Wilaya na hivyo mafunzo yatakapoanza kutolewa tutapata fursa ya kushiriki katika uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili utoaji wa fedha (milioni 180) zilizowezesha kujenga majengo ya kisasa ya shule ya msingi mpya katika Kitongoji cha Miembeni/Chatisa na Kijiji cha Likuyu Mandela na hivyo kuondoa jengo hafifu lililoezekwa kwa nyasi lililokuwa likitumika kwa watoto wa darasa la kwanza hadi tatu na kama sehemu ya shule ya Likuyu Mandela walitenganishwa na Mto Usio na daraja la uhakika na lisilopitika kipindi cha masika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kukipokea Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Mputa na kuwawezesha wanafunzi kufanya mitihani yao chini ya mitaala ya VETA. Mheshimiwa Waziri , chuo hiki kina changamoto lukuki ambazo zinahitaji kushughulikiwa na Wizara yako.

Mhesimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri licha ya kuzikabili changamoto za Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Mputa, utusaidie kuweka msukumo wa hali ya juu kwa majengo ya Chuo cha VETA cha Namtumbo yakamilike kujengwa kwa wakati kwa awamu zote mbili ikiwa ni pamoja na kujengwa mabweni ya wanachuo na kantini ili mafunzo yaanze kabla ya mwaka 2020.

Mheshimiwa Waziri, tunacho Chuo cha Ualimu cha Nahoro kinachomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Songea na Namtumbo (SONAMCU). Nimehakikisha mfuko wa jimbo (CDCF) unachanga katika kutekeleza masharti ya kukiwezesha kiendelee kutoa mafunzo ya ualimu ngazi ya astashahada.

Aidha, mmetufungulia shule nne za kata kati ya 23 tulizonazo kutoa elimu ya kidato cha tano na sita. Nguvu za wananchi zimechangia katika kujenga majengo mapya yaliyohitajika katika kuziwezesha shule hizo za sekondari za Kata za Nanungu, Luegu pamoja na Namabengo kuweza kutoa elimu ya kidato cha kwanza hadi cha sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri atusaidie kuboresha utoaji wa elimu katika shule hizo hususan majengo, walimu na vitabu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI:Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa George Huruma Mkuchika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) pamoja na Naibu Waziri na Katibu Mkuu kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naombawaangalie suala la watumishi wa afya walioajiriwa kihalali na Serikali baada ya kuwalegezea masharti ya ajira na ambao waliondolewa kwenye utumishi wa umma kwa kukosa sifa ya kumaliza kidato cha nne. Ni vyema watumishi hao wakarudishwa kazini ama kustaafishwa na kulipwa mafao yao. Baadhi ya watumishi hao wapo wa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo ambao wameleta malalamiko yao ya kutotendewa haki kwa Katibu Mkuu Dkt. Laurean Ndumbaro na nakala ya malalamiko hayo nilimkabidhi Mheshimiwa Dkt. Mary M. Mwanjelwa, Naibu Waziri.Watumishi hao wamekuwa wakipoteza nauli mara kwa mara kuja Dodoma kufuatilia majibu ya malalamiko yao na hivyo kujiongezea machungu na umaskini. Naomba suala lao lishughulikiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikipokea vilio vya baadhi ya watumishi wa Serikali hususan wa TAMISEMI (Makao Makuu) wanaolalamikia maslahi duni. Wanasema wenzao wa kada moja walioajiriwa kwenye Taasisi za Serikali wanapata mishahara minono wakati wao walioajiriwa TAMISEMI mishahara wanayoipata haikidhi kabisa mahitaji ya msingi na hivyo kujikuta na madeni lukuki na kuendelea kuishi kwa kuombaomba. Wameniomba nifikishe kilio chao kwa Mheshimiwa Rais kupitia Wizara hii yenye dhamana na mishahara ya watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia 100 na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii, ingawa nikiangalia saa pale inanipa shida kidogo, lakini nitajitahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza moja kwa moja na suala la Jimbo langu la Namtumbo. Miradi iliyokuwa inaitwa ya World Bank ambayo ilianza mwaka 2005/2006 na kwa maana hiyo ni wakati ambapo Serikali ya Awamu ya Nne ilipokuwa inaingia madarakani, kwangu kwa kweli imepata msukumo mkubwa sana na Mheshimiwa Engineer Kamwelwe kama Waziri wa Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji. Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri, umelipa certificates mbili za Mradi wa Mkongo - Gulioni na Nahimba na nimeambiwa kwamba kutokana na ile certificate uliyoilipa katika wiki zijazo maji yatakuwa yametolewa kutoka kwenye chanzo na kuingizwa kwenye matenki na baada ya hapo, hatua ya pili ya kuyatoa kwenye matenki na kusambaza kwa wananchi itafuatia, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nikuombe mradi mwingine katika hii miradi ya World Bank wa Likuyu - Sekamaganga ambayo advanced payment au certificate ya awali inahitaji nayo ilipwe ili na huo mradi nao upate msukumo mkubwa kama ambavyo umeipa msukumo mkubwa huu Mradi wa Mkongo - Gulioni na Nahimba. Naomba na huu Mradi wa Likuyu - Sekamaganga nao upate msukumo mkubwa kama huu mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile Mradi wa Luhimbalilo na Naikesi ni kati ya miradi hiyohiyo ya World Bank. Nikuombe nayo uipe msukumo mkubwa, kulikuwa na tatizo la ubadilishaji wa chanjo kwa sababu chanjo cha mwanzo ilionekana maji sasa yalikuwa hayatoshi kutokana na miaka hii kumi yote iliyopita na sasa chanzo kipya kimepatikana, kina maji mengi sana. Nikuombe na huo mradi tupate fursa ya kuutangaza ili nao utekelezwe. Pamoja na kwamba ulitakiwa utekelezwe miaka kumi iliyopita lakini kwa namna wewe Mhandisi ninavyokuona utanisaidia na huo mradi uanze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mradi mwingine mkubwa unao-cover vijiji karibu vitano, unajulikana kama Mradi wa Hanga – Mawa – Msindo. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, kwa kasi kubwa uliyoianza ya kutusaidia miradi hiyo miwili ya mwanzo na huu nao uupe msukumo mkubwa ili hatimaye Wananamtumbo, ambao zaidi ya asilimia 95 ni watu wa vijijini waweze nao kunufaika na sera au na kaulimbiu ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwafikia wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie katika miradi hii ambayo umeanza kuipa msukumo, hakika unatekeleza kauli mbiu hii ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano ya kuwafikia wanyonge, watu wa chini na kwa kweli kwa upande wa Wilaya nzima ya Namtumbo tunaongelea zaidi ya asilimia 95. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna certificate ya pili kwa Mradi wa Kumbara – Litola ambao naamini Mheshimiwa Rais atakapofika kutembelea Wilaya ya Namtumbo pengine tutapata fursa ya ama kuwekea jiwe la msingi au pengine ukiwahisha kulipa fedha hizo atafika tayari maji nayo yatakuwa yametoka kwenye chanzo na kufika kwenye matenki kwa sababu ujenzi wa matenki tayari umeshakamilika. Nikuombe sana hii certificate ya pili ya kazi nayo ilipwe ili miradi hii ipate msukumo, imechelewa kwa muda wa miaka kumi lakini tunataka kuitekeleza katika miaka miwili, mitatu ya Serikali ya Awamu hii ya Tano. Nikuombe kwenye hilo unisaidie sana iweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna miradi hii iliyokuwa imetwa ya quick win, ni kwa ajili ya vijiji vya Namabengo na Mchomoro. Tuliiweka katika Programu ya Miradi ya Quick Win, ilitengewa shilingi milioni 300 kwa mwaka huu unaokaribia kuisha, nadhani unafahamu kwamba tumeomba toka mwezi wa saba na baadae kukawa na mawasiliano ya kubadilisha makadirio na namna ya ku-design tukabadilisha, mwezi wa tisa tukawaletea. Tunaomba tupate kibali cha kutangaza kwa sababu huo ndiyo utaratibu, pamoja na kwamba fedha zimetengwa hizo milioni shilingi 300 katika hiyo miradi miwili na lengo lilikuwa ni quick win lakini mpaka sasa hatujapata kibali cha kutangaza. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, hebu ongeza msukumo kwa watendaji wako, miradi hii miwili ya quick win ipate ruhusa ya kutangazwa ili hatimaye tuitangaze na tuwahi kabla ya tarehe 30 Juni tuweze kutumia hizo shilingi milioni 300 tulizotengewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu fedha hizi za shilingi milioni 300 kwa miradi hii miwili ya quick win kama hatutaweza kutangaza ina maana tutashindwa kuzitumia. Sasa mmetutengea shilingi milioni 80 kwa kila mradi, toka shilingi milioni 300 tunashuka kwenye shilingi milioni 80, tusipoitumia ile shilingi milioni 300 hiyo shilingi milioni 80 haitafanya kazi kubwa na kwa kweli maana halisi ile ya quick win haitakamilika. Nikuombe sana utusaidie, tupe ruhusa ya kutangaza ili tuweze kutangaza na tuweze kuzitumia hizi shilingi milioni 300 ili hizi shilingi milioni 80 zinazofuata kwa mwaka 2018/2019 tuweze sasa kukamilisha kabisa na wananchi wale wa Mchomoro pamoja na Namabengo waweze kupata maji kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano ilikusudia kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana liangalie hilo. Kibali cha kutangaza ni barua tu na kwa maana ya kuutathmini huo mradi mlishafanya hiyo kazi kuanzia mwezi Julai mwaka jana. Nikuombe sana, hebu tupe hicho kibali ili hii miradi iweze kuanza kutekelezwa na maana ya quick win ikamilike.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana unisaidie katika maeneo mengine sugu sana ya Mgombasi, Matepwende ya Msisima, Matempwende ya Ligera au Matepwende ya Milonji, Lometa pamoja na Mtakanini, ni vijiji ambavyo vina matatizo makubwa sana ya maji. Labda tu nikwambie pale Mtakanini hilo ombi lilitolewa na Marehemu Mzee Kawawa na likakubalika na wakati huo Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Mkapa lakini mpaka sasa hatujapaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe sana na hapo napo tupaweke vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii, ingawa nikiangalia saa pale inanipa shida kidogo, lakini nitajitahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza moja kwa moja na suala la Jimbo langu la Namtumbo. Miradi iliyokuwa inaitwa ya World Bank ambayo ilianza mwaka 2005/2006 na kwa maana hiyo ni wakati ambapo Serikali ya Awamu ya Nne ilipokuwa inaingia madarakani, kwangu kwa kweli imepata msukumo mkubwa sana na Mheshimiwa Engineer Kamwelwe kama Waziri wa Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji. Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri, umelipa certificates mbili za Mradi wa Mkongo - Gulioni na Nahimba na nimeambiwa kwamba kutokana na ile certificate uliyoilipa katika wiki zijazo maji yatakuwa yametolewa kutoka kwenye chanzo na kuingizwa kwenye matenki na baada ya hapo, hatua ya pili ya kuyatoa kwenye matenki na kusambaza kwa wananchi itafuatia, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nikuombe mradi mwingine katika hii miradi ya World Bank wa Likuyu - Sekamaganga ambayo advanced payment au certificate ya awali inahitaji nayo ilipwe ili na huo mradi nao upate msukumo mkubwa kama ambavyo umeipa msukumo mkubwa huu Mradi wa Mkongo - Gulioni na Nahimba. Naomba na huu Mradi wa Likuyu - Sekamaganga nao upate msukumo mkubwa kama huu mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile Mradi wa Luhimbalilo na Naikesi ni kati ya miradi hiyohiyo ya World Bank. Nikuombe nayo uipe msukumo mkubwa, kulikuwa na tatizo la ubadilishaji wa chanjo kwa sababu chanjo cha mwanzo ilionekana maji sasa yalikuwa hayatoshi kutokana na miaka hii kumi yote iliyopita na sasa chanzo kipya kimepatikana, kina maji mengi sana. Nikuombe na huo mradi tupate fursa ya kuutangaza ili nao utekelezwe. Pamoja na kwamba ulitakiwa utekelezwe miaka kumi iliyopita lakini kwa namna wewe Mhandisi ninavyokuona utanisaidia na huo mradi uanze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mradi mwingine mkubwa unao-cover vijiji karibu vitano, unajulikana kama Mradi wa Hanga – Mawa – Msindo. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, kwa kasi kubwa uliyoianza ya kutusaidia miradi hiyo miwili ya mwanzo na huu nao uupe msukumo mkubwa ili hatimaye Wananamtumbo, ambao zaidi ya asilimia 95 ni watu wa vijijini waweze nao kunufaika na sera au na kaulimbiu ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwafikia wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie katika miradi hii ambayo umeanza kuipa msukumo, hakika unatekeleza kauli mbiu hii ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano ya kuwafikia wanyonge, watu wa chini na kwa kweli kwa upande wa Wilaya nzima ya Namtumbo tunaongelea zaidi ya asilimia 95. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna certificate ya pili kwa Mradi wa Kumbara – Litola ambao naamini Mheshimiwa Rais atakapofika kutembelea Wilaya ya Namtumbo pengine tutapata fursa ya ama kuwekea jiwe la msingi au pengine ukiwahisha kulipa fedha hizo atafika tayari maji nayo yatakuwa yametoka kwenye chanzo na kufika kwenye matenki kwa sababu ujenzi wa matenki tayari umeshakamilika. Nikuombe sana hii certificate ya pili ya kazi nayo ilipwe ili miradi hii ipate msukumo, imechelewa kwa muda wa miaka kumi lakini tunataka kuitekeleza katika miaka miwili, mitatu ya Serikali ya Awamu hii ya Tano. Nikuombe kwenye hilo unisaidie sana iweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna miradi hii iliyokuwa imetwa ya quick win, ni kwa ajili ya vijiji vya Namabengo na Mchomoro. Tuliiweka katika Programu ya Miradi ya Quick Win, ilitengewa shilingi milioni 300 kwa mwaka huu unaokaribia kuisha, nadhani unafahamu kwamba tumeomba toka mwezi wa saba na baadae kukawa na mawasiliano ya kubadilisha makadirio na namna ya ku-design tukabadilisha, mwezi wa tisa tukawaletea. Tunaomba tupate kibali cha kutangaza kwa sababu huo ndiyo utaratibu, pamoja na kwamba fedha zimetengwa hizo milioni shilingi 300 katika hiyo miradi miwili na lengo lilikuwa ni quick win lakini mpaka sasa hatujapata kibali cha kutangaza. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, hebu ongeza msukumo kwa watendaji wako, miradi hii miwili ya quick win ipate ruhusa ya kutangazwa ili hatimaye tuitangaze na tuwahi kabla ya tarehe 30 Juni tuweze kutumia hizo shilingi milioni 300 tulizotengewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu fedha hizi za shilingi milioni 300 kwa miradi hii miwili ya quick win kama hatutaweza kutangaza ina maana tutashindwa kuzitumia. Sasa mmetutengea shilingi milioni 80 kwa kila mradi, toka shilingi milioni 300 tunashuka kwenye shilingi milioni 80, tusipoitumia ile shilingi milioni 300 hiyo shilingi milioni 80 haitafanya kazi kubwa na kwa kweli maana halisi ile ya quick win haitakamilika. Nikuombe sana utusaidie, tupe ruhusa ya kutangaza ili tuweze kutangaza na tuweze kuzitumia hizi shilingi milioni 300 ili hizi shilingi milioni 80 zinazofuata kwa mwaka 2018/2019 tuweze sasa kukamilisha kabisa na wananchi wale wa Mchomoro pamoja na Namabengo waweze kupata maji kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano ilikusudia kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana liangalie hilo. Kibali cha kutangaza ni barua tu na kwa maana ya kuutathmini huo mradi mlishafanya hiyo kazi kuanzia mwezi Julai mwaka jana. Nikuombe sana, hebu tupe hicho kibali ili hii miradi iweze kuanza kutekelezwa na maana ya quick win ikamilike.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana unisaidie katika maeneo mengine sugu sana ya Mgombasi, Matepwende ya Msisima, Matempwende ya Ligera au Matepwende ya Milonji, Lometa pamoja na Mtakanini, ni vijiji ambavyo vina matatizo makubwa sana ya maji. Labda tu nikwambie pale Mtakanini hilo ombi lilitolewa na Marehemu Mzee Kawawa na likakubalika na wakati huo Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Mkapa lakini mpaka sasa hatujapaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe sana na hapo napo tupaweke vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa hii ya kusema mbele ya Bunge lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo manne mahsusi yanayohusu Jimbo la Namtumbo. La kwanza, ni ardhi ya Kijiji cha Likuyu Sekamaganga ambayo imechukuliwa na Chuo cha Wanyamapori cha Likuyu Sekamaganga bila kuwashirikisha wanakijiji wa Likuyu Sekamaganga. Sasa hivi pana ugomvi pale na ugomvi huu unakuzwa na kiongozi wa chuo, ambaye inaonekana ametumia ujanja amepata hati miliki katika eneo ambalo ni la Kijiji cha Likuyu Sekamaganga bila kuwashirikisha wenye ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri aliangalie suala hili na atatue ugomwi ule. Ile ardhi ni kubwa, chuo kinahitaji ardhi lakini ardhi iliyochukuliwa na chuo ni kubwa sana sehemu ambayo hawaitumii wairudishe kwa wanakijiji, wanakijiji wanaihitaji ardhi hiyo. Tuache kugombana, tuache kupelekana mahakamani, tuache nguvu za dola kuwaweka lock-up watu ambao hawana makosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu yaliyotokea wakati wa Operesheni Tokomeza. Wananchi wetu wa Wilaya ya Namtumbo kuna baadhi walichukuliwa silaha zao kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki. Tunaongelea Operesheni Tokomeza iliyoendeshwa mwaka 2012/2013, leo ni zaidi ya miaka mitano, uhakiki haujakamilika. Wale watu wakidai silaha zao ambazo walizinunua kihalali, wamezisajili kwenye vyombo vya dola kwa mujibu wa sheria na wakaambiwa wazilete wakazipeleka kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki sasa ni zaidi ya miaka mitano hawajarudishiwa silaha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila wakiulizia wanasema sijui kiongozi wa ile Operesheni Tokomeza kwa upande ule wa Kusini yuko Mtwara. Ukienda Mtwara wanasema kule kule Songea na Polisi ndiyo wanashughulikia, ukienda Polisi hakuna majibu kamili yanayopatikana. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, hii operesheni ilikuwa ni ya kwako utusaidie, wale wananchi warudishiwe silaha zao, wanazihitaji kwa ajili ya kujilinda na wanyama wakali lakini vilevile kujilinda, kwa wale walichukuliwa pistol maana silaha zilizochukuliwa ni magobore, shortgun na pistol. Pistol zilikuwa zinatumiwa na watu waliokuwa na maduka kujilinda wao na mali zao mbalimbali sasa hawana ulinzi huo na wanaibiwa kila wakati. Nimwombe Mheshimiwa Waziri anisaidie silaha hizo zirudi kwa wenyewe ili wawe na utulivu na hasa kujilinda na wanyama ambao wanaharibu mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ni hoja ya mipaka ya WMA (Hifadhi za Jamii). Kule kwetu tuna Hifadhi za Jamii tatu, tuna Hifadhi ya Jamii inaitwa Kimbanda pamoja na Kisungule ambazo ziko katika Tarafa ya Sasawala. Maeneo haya ya WMA yalikusudiwa zaidi kulinda ushoroba. Wananchi waliyatoa maeneo makubwa zaidi kuliko yale yanayohitajika kwa ajili ya shughuli za ushoroba kwa makubaliano kwamba wataendelea kulima lakini hawatajenga. Kwa hiyo, wale wananchi ndani ya maeneo yale wamekuwa wakiendelea kulima miaka hadi miaka na ni wakulima hodari wa mpunga unaitwa mpunga wa Lusewa ambao ni maarufu sana una harufu nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tokea mwaka 2015 wamezuiwa kulima wakidai kwamba haya maeneo ni ya Hifadhi za Jamii wakati makubaliano ilikuwa ukulima uendelee ila wasijenge makazi. Kwa sababu kilimo na njia za wanyama wale tembo wanaovuka kwenda Nyasa haviingiliani na nyakati ni tofauti. Nyakati ambazo wale tembo wana-cross ni kipindi ambacho wale watu wanakuwa wameshavuna zamani lakini sasa wamezuiwa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, WMA ni zetu, ni mali ya hifadhi za jamii lakini sasa inaonekana udhibiti mkubwa uko Wizarani na hivi sasa hata viongozi wetu wanakubali kuruhusu ng’ombe wafugiwe mle ndani lakini siyo kilimo cha mpunga ambacho kimekuwa kikifanyika miaka nenda miaka rudi. Wananchi wa Tarafa ya Sasawala na hasa hasa wa maeneo ya Mtanga, Msangesi, Semeni, Msukunya na mengineyo ya Kata ya Lusewa, Kata ya Msisima na Kata ya Magazine hawaelewi nini kinachoendelea. Maisha yao muda wote wamezoea kulima mpunga katika maeneo hayo na wamekuwa wakiyalinda maeneo hayo na wakiwalinda wanyama lakini sasa wanakuwa ni maadui, wanataka kuwageuza sasa wale watu wawe maadui hata kwa wale wanyama kitu ambacho siyo kizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mtusaidie, hizi WMA zilitolewa kwa muda wa miaka 10 na baada ya miaka 10 tulitakiwa tupitie upya mipaka na muda wa miaka 10 ulishapita zamani. Naomba sana mtusaidie tupitie upya mipaka ile ya WMA ili wale wananchi waweze kutofautisha na waendelee kulima katika maeneo ambayo wamezoea kulima, yale maeneo tembo hawapiti. Maeneo yanayopitiwa na tembo yanajulikana toka enzi hizo za mababu. Wanayajua na wanayaheshimu. Niombe hizo WMA zipitiwe upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, WMA ya tatu inaitwa Mbarang’andu, hiyo ipo nje ya Nyasa Corridor. Tatizo la eneo hili la WMA la Mbarang’andu ni wananchi kunyanyaswa. Kuna maeneo ambayo wananchi wa Kata ya Mchomoro wamelima mpunga na wamekuwa wakilima mpunga miaka nenda miaka rudi. Miaka ya hivi karibuni imetokea NGO moja kutoka nje ya nchi na uongozi wa Wilaya umeiruhusu kunyunyizia dawa ya kuuwa magugu kwenye mipunga ambayo wananchi wamelima. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri tumeliongea hili na najua ameanza kuchukua hatua naomba azikamilishe hizo hatua alizoanza kuzichukua. Niombe sana viongozi hawa wakuu wa maeneo yetu wazuiwe kuendelea kuwanyanyasa wananchi, wazuiwe kuendelea kuwafanya wananchi waichukie Serikali yao. Serikali hii inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wanaipenda sana lakini chokochoko hii ya kutaka kuwagombanisha wananchi wale na Serikali yao naomba Mheshimiwa Waziri aikomeshe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya WMA ni wananchi na yale maeneo ambayo yanalimwa mpunga mengine yapo nje ya maeneo hayo lakini bado watu wanawafuata huku wanakolima mpunga na kuwamwagia madawa ambayo yanakausha mipunga yao. Mwaka huu tunavyoongea sina uhakika wale watu waliozoea kujipatia kipato chao kupitia mpunga itakuwaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, baba yangu na kwa kweli nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa wanazozifanya. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuridhia kuanzisha zile taasisi mbili zinazojitegemea, moja Kurugenzi ya Mashtaka na Ofisi ya Solicitor General. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa sababu sasa tunaamini mambo ya haki yatafanyika vizuri zaidi kuliko ilivyokuwa katika mfumo wa zamani. Nimeona bajeti imeongezeka kwa sababu tumeanzisha taasisi tofauti na bajeti yake sasa hivi imekuwa kubwa na mnakumbuka kipindi cha nyuma aliyekuwa Mwanasheria Mkuu alikuwa analalamika sana kuhusu bajeti, lakini nina uhakika sasa huyu Mwanasheria Mkuu wa sasa amepata bahati kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni dakika tano tu, naomba niongelee kitu kimoja tu kidogo cha kuhusiana na matumizi ya Mfuko wa Mahakama. Nimwombe sana Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria atusaidie sisi Wananamtumbo, tuna idara ya mahakama pale ngazi ya wilaya inafanya kazi vizuri sana, lakini mazingira waliyonayo sio mazuri. Wamekaa katika majengo ambayo ni ya kuazima na kwa bahati mbaya sasa hivi wamezungukwa na Kituo cha Afya cha Namtumbo. Nimwombe aingize katika bajeti ya mwaka huu Wilaya ya Namtumbo kujengewa Mahakama ya Wilaya ili pale walipo sasa waweze kupisha shughuli za Kituo cha Afya kipya kabisa cha Namtumbo kiweze kufanya kazi vizuri zaidi kuliko kuchanganya haya mambo mawili katika eneo moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa fursa, nilitaka niliongelee hilo jambo moja, dakika tano sio muda mrefu, ni kwa sababu tu unapoanza kuongea moja kwa moja unaanza kwenye hoja, lakini ukianza kuogelea maeneo mengine unajikuta muda umeisha, hoja uliyotaka kuongea unaikosa na ni kitu ambacho wenzetu inabidi wajifunze ili tuweze kwenda vizuri katika kuwatumikia wananchi wetu majimboni kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kauli hiyo, naomba nisisitize Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo ipate fursa ya kujengwa... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Engineer Ngonyani.

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti nampongeza Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria kwa kupata fursa ya kuiongoza Wizara hii ya learned friends. Aidha, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri ahakikishe Mfuko wa Mahakama kwa Mwaka 2019/ 2020 unatumika vilevile kujenga Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo pamoja na Mahakama za Mwanzo ambazo wamechukua viwanja vya kujenga kwa muda mrefu na hawajaanza kujenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Namtumbo wa maeneo waliyochukua na kuweka vibao vya kuonyesha kama maeneo ya Mahakama wanashangaa hakuna kinachoendelea. Maeneo hayo ni pamoja na Kijiji cha Mawa. Naomba sana Wizara itenge fedha za Mfuko wa Mahakama tunazozipitisha kuanza kujenga Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo na ikiwezekana na ujenzi wa Mahakama za Mwanzo walizozipanga kuanza kujenga katika Wilaya ya Namtumbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, nawapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake pamoja na Katibu Mkuu kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya. Wana Namtumbo wanafurahia utendaji wao na wanaomba yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, wanachi wa Namtumbo wanaomba wapewe Vitambulisho vya Taifa, maana taarifa zao na picha vimechukuliwa muda mrefu sana lakini hawaoni matokeo.

Mheshimiwa Spika, lingine, baadhi ya Askari Polisi wasio waaminifu wanaodai hawajalipwa haki zao wanawanyanyasa wakazi wa Namtumbo kwa kuwabambikizia kesi na kwa waendesha bodaboda kushikwa mara kwa mara na kutakiwa walipe faini bila kosa lolote. Mtusaidie tuishi kwa amani bila bugudha ya baadhi ya Maaskari wasio waaminifu.

Mheshimiwa Spika, Polisi wanatumika vibaya na WMA ya Mbarang’andu na Kimbanda kwa kuwanyanyasa wakazi wa Namtumbo wanaoishi karibu na maeneo ya Hifadhi za Jamii (WMA) kwa kuwapa adhabu za kuwatweza utu wao na kutakiwa kulipa faini ama tozo za malaki na mamilioni ya shilingi eti kwa sababu wamekutwa majumbani mwao wamepika samaki au uyoga wakidai lazima watakuwa wameingia kwenye maeneo ya Hifadhi za Jamii kinyume na Sheria.

Mheshimiwa Spika, nashauri Polisi wasitumike kwa operesheni za aina hii, badala yake hizo WMA zijisimamie zenyewe. Polisi walipwe stahiki zao kwa wakati ili wasirubuniwe na viongozi wa WMA wanaowalipa posho zinazotoka kwa NGO za Kimataifa ambazo zina dhamira mbaya za kuwagombanisha wananchi na Serikali yao inayoongozwa na mpendwa wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa hii ya kuongea leo, pili nikushukuru wewe kwa kunipa hii fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii, inayoongozwa na Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako, kwa kweli sina maneno ya kusema, na wana Namtumbo wote hawana maneno ya kusema, ni furaha tu kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa mara ya kwanza, Tanzania inajenga vituo vya VETA katika ngazi ya wilaya na wameanzia Namtumbo, nawashukuruni sana. Nashukuru sana Mheshimiwa Rais amekuja na kukipa heshima kubwa zaidi kile kituo cha VETA cha Namtumbo kwa kukifungua, nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, hakikisha kwamba yale yaliyobaki madogo madogo tuyamalize, ili mafunzo yaanze kutolewa katika kile chuo. Kile chuo kimejengwa pembeni kidogo na maeneo wanayokaa watu, kwa hiyo, wanafunzi wanahitaji mabweni, lakini vilevile walimu wanahitaji nyumba. Niombe sana tusaidiane hayo nayo yakamilike ili wana Namtumbo na watanzania wote kwa ujumla waweze kuanza kukitumia kile chuo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, katika sera ya kila kata kuwa na Sekondari, lengo la Serikali ilikuwa kwamba kila Sekondari, iwe ni ya day, iwe ni ya kutwa, na kisera tuko sahihi kabisa. Lakini tunapokuja kwenye utekelezaji, kuna baadhi ya kata zinaunganisha vijiji ambavyo viko mbalimbali sana. Nikitolea mfano, Kata yangu ya Magazine, kijiji hadi kijiji ni kilomita zisizopungua 20 na viko vijiji vitatu. Siyo hiyo tu, kuna Kitongoji ambacho kipo kilomita 26 kutoka kwenye makao makuu ya kijiji, cha mwisho kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika mazingira haya, hatutarajii sekondari hiyo isikose mabweni. Tunakubaliana kwamba sekondari zote za kata ni za kutwa, sisi hatuna tatizo na hilo, tatizo tulilonalo ni kwa idara hii ya udhibiti elimu kutuzuia kujenga mabweni, ni sisi wenyewe tunaamua kujenga mabweni, na tunayahudumia wenyewe kwa sababu tunataka watoto wetu wale waliokusudiwa kuitumia hiyo shule ya sekondari, waweze kupata masomo, isitokee ni kile kijiji kimoja tu ambacho sekondari imejengwa na vijiji vingine vikakosa hiyo fursa kwa sababu ya umbali, umbali ni mkubwa sana na haiwezekani wakasoma kwa kutwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe, ni kata nyingi ambazo katika wilaya yangu zina mazingira hayo na kata zote zenye mazingira hayo zimeamua kujenga mabweni, wenyewe, na wenyewe wanahudumia! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna walaka umetolewa, na hii idara ya kudhibiti elimu inayokataza mabweni hayo yasifanye kazi na yasiendelee kujengwa. Niombe sana hilo liangaliwe. Shule hizo ziendelee kuchukuliwa kama shule za kutwa, lakini sisi wenyewe tulioamua kuhudumia wanafunzi wetu wanaosoma katika shule hizo kwa kujenga mabweni na kujenga eneo la kulia chakula na shuguli zote zile tunahudumia wenyewe, turuhusiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani siyo sahihi kutuzuia kwa sababu ukituzuia, maana yake unatuzuia fursa ya kutumia hizo shule za kutwa kupata elimu kwa watoto wetu. Niombe sana hilo liangaliwe kwa makini sana. Lakini ni utekelezaji mzuri sana wa hiyo sera kwa sasa kwa kweli ni kwa mara ya kwanza sisi Namtumbo napo tunapata wanafunzi wengi wanaomaliza kidato cha nne na wengine sasa wanaingia kidato cha tano kwa sababu kiwango kile cha ufaulu kimeanza kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niombe, kama ambavyo wengine wamesema, naomba hasa walimu wa sayansi, tunaomba sana muendelee kutusaidia. Najua mnaendelea kuajiri, lakini kasi ya kuajiri ni ndogo sana, hata kama tatizo ni ukubwa wa bajeti ya mishahara ya Serikali kwa ujumla, naomba sana Serikali itoe kipaumbele kwa masuala ya elimu pamoja na afya kwa maana ya zahanati na vituo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hizi sekondari pamoja na shule za msingi, tutoe kipaumbele, tusijali sana ukubwa wa bajeti ya mishahara katika kuzuia kuajiri. Nikuombe sana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) utusaidie kwenye hilo. Tunaomba walimu ili tuweze kupata ile elimu iliyokusudiwa kupitia hizi shule za sekondari za kata lakini vilevile shule za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vyuo vya walimu, hapa nilitaka tu kusema, kule kwetu Namtumbo, kilianzishwa chuo cha Walimu, kipo katika Kijiji cha Nahoro, kinamilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Songea na Namtubo, (SONAM). Chuo hiki kilianzishwa ili kujaribu kutatua changamoto za watoto wetu wengi wanaomaliza kidato cha nne lakini hawapati fursa ya kwenda kwenye vyuo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kilipoanza, kimedahili mara mbili kwa kutumia kile kibali cha muda, (provisional registration). Sasa baada ya miaka miwili, mmetuzuia tusiendelee kudahili, ni sawa, ni suala la udhibiti, lakini kinachoshangaza ni kwamba, katika miaka ile miwili ya udahili, kile chuo kilikuwa ni kati ya vyuo bora Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ile miaka miwili, mitihani waliyofanya miaka ile miwili, hicho chuo kilikuwa bora kabisa na kikaanza kuvuta wanafunzi wengi kutoka maeneo, nje ya Namtumbo, nje ya Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hatuelewi, kimezuiwa kweli ni kwa sababu hakijakidhi viwango kwa maana hawana jengo la kompyuta na mengine, au pengine ni kuzuia tu watu wasiende Namtumbo au na watu wa Namtumbo wasipate fursa ya kudahiliwa katika chuo hicho! Maana yake inawezekana tatizo tunaofanya kazi kwenye idara mbalimbali, unaweza ukafanya kitu sahihi kabisa, lakini motive yako ikawa tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu kwa mfano, nilifikiria, badala ya kukizuia, mngeweza kukisaidia kimalize zile changamoto kilizonazo ili wanafunzi waendelee kudahiliwa. Kwa sababu, tatizo halikuwepo katika ubora wa elimu inayotolewa, ubora wa elimu unaotolewa katika kile chuo ni the best na ndiyo maana katika ile miaka miwili kilikuwa kati vya vyuo bora Tanzania, kwa hiyo, hakukuwa na tatizo la ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kukizuia, inawezekana kweli ni kwa sababu ya hizo sababu ambazo Idara ya Udhibiti wa Ubora wa Elimu imezitoa kwa kuzuia lakini sisi kule tunaona kama ni kutunyima fursa ya kukitumia kile chuo. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, changamoto hizo, kama ni kweli ndiyo, is it core or subsidiary. Mimi nadhani, kama siyo core reasons, kile chuo kiendelee kudahili, kwa sababu kinatoa mafunzo mazuri na kwa kweli, kinatoa walimu the best kati ya the best vyuo katika Tanzania. Nikuombe sana uliangalie hilo kwa makini na utusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, nichukue fursa hii kuipongeza tena Wizara kwa kukiorodhesha Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Mputa, kati ya vyuo vitakavyofanyiwa ukarabati katika Awamu ya II, nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri, Umeendelea kutembea katika kivuli cha Mheshimiwa Rais, cha kuiona Namtumbo ambayo iko nyuma sana, ni kati ya wilaya ambazo ziko nyuma sana katika wilaya zile ambazo ziko Tanzania nyuma sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, na wewe unaanza kutembea katika kivuli cha Mheshimiwa Rais, cha kutuona sisi wana Namtumbo na kutusaidia. Nimefurahi sana na wana Namtumbo watafurahi sana kusikia chuo chao cha Mputa cha Maendeleo ya Jamii kinakwenda kukarabaitiwa… (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimwa.

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Kimekuwa kikiishi kama chuo yatima…

MBUNGE FULANI: Muda umeisha, unga mkono hoja.

MHE. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia 100 na kwa kweli nashukuru sana, kama nilivyosema hatuna maneno juu ya Wizara hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja ikiwa ni pamoja na zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsanteni sana na kwa kumwalika Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuja kukifungua Chuo cha VETA cha Namtumbo na hivyo kukipandisha hadhi. Nawaomba mkamilishe nyumba za walimu na mabweni ya wanafunzi ili chuo kianze kutoa mafunzo bila kusahau vifaa vya kufundishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha mlizotoa kuunga mkono ujenzi wa Shule ya Msingi ya Miembeni katika Kijiji cha Likuyu Mandela ni shilingi milioni 180 na shule ya kisasa kabisa imekamilika kujengwa na imeanza kutumika. Ahsanteni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu usimamizi thabiti wa Sera ya kila Kata kuwa na Sekondari moja ya kutwa, sera hii imewezesha Wilaya ya Namtumbo kuwa na Sekondari 23 katika Kata 20. Ni Kata moja tu haina Sekondari kutokana na kuanzishwa hivi karibuni (Kata ya Msisima). Tuombe tu, shule hizi za kutwa zinahudumia Vijiji na Vitongoji vilivyosambaa kwa zaidi ya kilometa 5 - 26 na hivyo kulazimika wanafunzi kupanga ama kuwa na mabweni katika shule hizo kinyume na madhumuni ya kuanzishwa kwa shule hizo za kutwa. Mazingira hayo tuomba yavumiliwe badala ya kupigwa vita na Idara ya udhibiti ubora wa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Mikopo imeundwa na inafanya kazi vizuri. Hongereni sana, maana Bodi hii imefanikiwa kuwahudumia baadhi ya wanachuo wenye uhitaji. Katika eneo hili nampongeza sana Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Tate Olenasha, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kufuatilia wanachuo wenye uhitaji mkubwa wa mikopo katika Wilaya ya Namtumbo na nchi nzima kwa ujumla ambao kwa namna moja ama nyingine vigezo vilivyowekwa na Bodi na njia inayotumika, uthibitishaji wa vigezo hivyo vinaifanya Bodi kuwakosa wenye uhitaji na kuwapa wasio nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri anatusikia Wabunge na ni mwepesi wa kufuatilia taarifa tunazompa na pale inapothibitika kuwa haki haikutendeka, huirejesha haki kwa mhusika. Hakika unaye msaidizi mwenye hekima ya Mfalme Suleiman anayetajwa katika Biblia na anaitendea haki taaluma yake ya Sheria. Hongera sana Profesa Joyce Lazaro Ndalichako na kupitia kwako tumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukuibua wewe na Naibu wako na kuwakabidhi uongozi wa Wizara hii nyeti ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kipindi hiki muhimu cha mustakabali wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko sababu nyingi, itoshe kuishia hapa, naomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie katika haya yetu wana-Namtumbo:-

(a) Tukamilishiwe ujenzi wa Chuo cha VETA cha Wilaya ya Namtumbo;

(b) Tuondolewe waraka unaozuia ujenzi wa mabweni katika shule zetu za Sekondari za kutwa;

(c) Turekebishiwe mfumo unaotumika katika kuwapa wahitaji wa mikopo kutoka HESLB ili wahitaji halisi wasiachwe solemba na kukatisha ndoto zao za kutaka kujiendeleza kielimu;

(d) Naomba Chuo cha Ualimu kinachomilikiwa na SONAMCU kilichoko katika Kijiji cha Nahoro kiwezeshwe kuendelea kutoa huduma; na

(e) Naomba ukarabati wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Mputa ufanyike kwa wakati uliopangwa ili u- yatima wa chuo kile ufutike mioyoni mwa wanafunzi na Walimu wa chuo hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha. Naunga mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri, Prof. Joyce Lazaro Ndalichako, Mbunge kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Medard Matogolo Chananja Kalemani, imetutendea makuu. Miradi ya REA III na Makambako – Songea 220kv grid imetutoa matongotongo sisi Wana- Namtumbo. Katika mwaka huu wa fedha wa 2018/2019 Namtumbo imenufaika kwa baadhi ya vijiji vyake kuwashiwa umeme. Nikuombe Mheshimiwa Waziri tufikishie shukrani zetu sisi Wana-Namtumbo kwa Kiongozi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha zilizowezesha mtukune sisi Wana-Namtumbo katika sekta hii ndogo ya umeme. Hakika tumepata kiongozi anayetujali hata sisi wakazi wa Wilaya ya Namtumbo.

Mheshimiwa Spika, naamini Mheshimiwa Waziri atatekeleza kauli yake aliyoitoa Namtumbo tarehe 05/04/ 2019 mbele ya Mheshimiwa Rais kuwa vijiji vyote na vitongoji vyote vya Wilaya ya Namtumbo vitafikishiwa umeme. Katika kulitekeleza hili, nikuombe uwakumbushe REA kusaini addendum inayompa ridhaa na nguvu mkandarasi wa REA III wa Namtumbo kusambaza umeme kwenye vijiji vyote vilivyobaki, hususan vijiji vya Kata za Limamu, Ligera, Lisimonji, Lusewa, Msisima na Magazini. Maeneo hayo ndiyo yanayotarajiwa kuunda Wilaya ya Sasawala ambapo Lusewa ndiyo makao makuu. Lusewa kwa sasa ni mamlaka ya mji mdogo na hivyo ni muhimu sana kutufikishia umeme wa uhakika kutokana na uchumi wa eneo hilo. Hongera sana wewe, Naibu wako na watendaji wote wanaokusaidia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia 100 kwa sababu Mheshimiwa Waziri Ummy Ally Mwalimu na Naibu Waziri, Dkt. Faustine Ndugulile wametufanyia mambo makubwa ikiwa ni pamoja na yafuatayo:-

(i) Wamehamasisha upatikanaji wa shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Namtumbo na ujenzi umekamilika.

(ii) Wamehamasisha upatikanaji wa shilingi milioni 1,500 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Namtumbo na ujenzi unaendelea.

(iii) Wamenihamasisha mimi Mbunge wa Namtumbo kutumia Mfuko wa Jimbo pamoja na mchango wangu binafsi kukamilisha ujenzi wa zahanati saba za Njoomlole, Mwangaza, Namanguli, Mageuzi, Ruvuma, Kitanda na Songambele, pamoja na zahanati zinazoendelea kujengwa kwa nguvu za wananchi na mchango kidogo wa mimi Mbunge za Nahimbo, Ulamboni, Mwinuko, Ukiwayuyu, Msufini, Mhangazi na Luhangano. Hatua hii ikikamilika tutakuwa tumeongeza vijiji 15 vitakavyokuwa na zahanati.

(iv) Wamehamasisha nguvu za wananchi zitumike kuunga mkono Mbunge wao katika kujenga Kituo cha Afya cha Mchomoro na kukamilisha ujenzi wa baadhi ya majengo ya Kituo cha Afya cha Lusewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna alivyotuchekecha sisi Wabunge na kugundua kipaji kikubwa cha uongozi na unyenyekevu alionao Waziri na kumteua kuwa Waziri mwenye dhamana ya afya ya Watanzania. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais na Waziri hongera kwa kazi iliyotukuka unayoifanya. Naamini chini ya ushawishi wa Waziri akiungwa mkono na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, wana Namtumbo wanatarajia yafuatayo:-

(i) Vituo vya afya kwa umuhimu na au mpangilio huu wa Lusewa, Mchomoro, Mkongo Gulioni na Mtakanini vitaimarishwa kwa kujenga majengo mapya.

(ii) Vituo vya afya nane vilivyopo na vitakavyojengwa katika Wilaya ya Namtumbo viimarishwe kwa kupatiwa wahudumu wa afya, vifaa tiba, vitendanishi na madawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Namtumbo ina changamoto kubwa za upatikanaji wa huduma za upasuaji. Kutokana na umbali uliopo kwenda Kituo cha Afya cha Lusewa na Hospitali ya Mkoa kunakopatikana huduma hiyo ya upasuaji, naomba tusaidie kwa uharaka utakaowezekana tupatiwe fedha za kujenga Kituo hicho cha Lusewa pamoja na vituo vingine vitatu vya Mchomoro (ambako Mheshimiwa Rais ameahidi kuchangia shilingi milioni 100), Mkongo Gulioni (kinahudumia Kata sita za Mkongo Gulioni, Mkongo, Luchili, Limamu, Ligera na Lisimonji na mwisho Kituo cha Mtakanini kilichoahidiwa na Mheshimiwa Benjamini William Mkapa, Rais wa Awamu ya Tatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli huduma za afya bure kwa watoto wa chini ya miaka mitano, wajawazito na wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 ni changamoto kubwa lakini kabla ya miundombinu ya afya kukamilika kujengwa ni kazi bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie kukupongeza na kukushukuru kwa namna unavyoakisi dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kuwagusa na kuwainua wanyonge katika sekta zako hususan sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Kwa kweli nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa hii ya kuwa hai na kuchangia leo hii. Kwa sababu muda ni mfupi, naomba sana nianze na suala moja la taasisi mbili za TARURA na TANROADS. Kwa hivi sasa kwa mfumo tulionao, TARURA iko chini ya TAMISEMI na TANROADS iko chini ya Wizara hii tunayoiongelea leo.

Mheshimiwa Spika, hawa wote wanapata fedha kutoka Mfuko wa Barabara unaosimamiwa na Bodi ambapo mgawanyo wake TANROADS wanapata asilimia 62.46, TARURA wanapata asilimia 26.77, Ujenzi wanapata asilimia 6.94, TAMISEMI wanapata asilimia 2.97 na mfuko wenyewe wa barabara kwa maana ya taasisi inayosimamia inapata asilimia 0.86.

Mheshimiwa Spika, wajibu wa road fundboard ni pamoja na kusimamia au kufuatilia utekelezaji au matumizi ya fedha zinazokwenda katika taasisi ya TARURA, Ujenzi na TANROADS. Wakati huo huo TAMISEMI wanapata hiyo asilimia 2.97 kwa ajili ya ufuatiliaji wa miradi hiyo hiyo na Ujenzi wanapata asilimia 6.94 kwa ajili ya ufuatiliaji wa ujenzi wa barabara hizo hizo.

Mheshimiwa Spika, kwa maana nyingine Ujenzi, TAMISEMI na mfuko wa barabara wote wanasimamia barabara zinazoshughulikiwa na TANROADS na TARURA. Naomba, ni mawazo yangu kwamba TANROADS na TARURA wawe chini ya Wizara moja na kwa sababu Wizara inayohusika na barabara ni Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, basi ningependa TARURA maadam imeshaundwa chombo kinachojitegemea, basi sasa isimamiwe na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano badala ya TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii haina maana kwamba D by D itakuwa imekufa, hapana. Bado watu wa TAMISEMI suala la eyes on, hands off litabakia pale pale, linaendelea. Ni kama ilivyo katika barabara za TANROADS, nazo zinasimamiwa na TAMISEMI hata kama hawapati fedha na wala hawawajibiki, kuisimamia lakini wana eyes on katika shughuli zote zinazofanywa na TANROADS. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba vilevile eyes on iendelee na watu wa TAMISEMI kwa maana ya Wizarani pamoja na mkoani katika barabara za TANROADS wanavyofanya sasa na wafanye sasa na TARURA, lakini suala la usimamizi lirudishwe liwe chini ya Wizara moja, chini ya Waziri mmoja ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Hii itasaidia mambo mengi. Kwanza hizi hela zote za usimamizi asilimia 6.94, 2.97 na 0.86 zote zitaungana zitafanya kazi kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halafu na mgawanyo wa bajeti hiyo suala la asilimia 70 kwa 30 halitakuwa na mvutano tena na wala hatutakuwa na mvutano tena wa kusema kupandisha barabara hadhi lakini sababu tu ni kutaka hizo barabara zishughulikiwe na TANROADS. Mvutano huo hautakuwa tena kama taasisi zote hizo mbili zitasimamiwa na Wizara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuliongea hilo, naomba tena upande wa mawasiliano TTCL, Mkongo wa Taifa, Tume ya TEHAMA, pamoja na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. Taasisi hizi nimeangalia kwenye vitabu vya Mheshimiwa Waziri, sijaona kama amezipa mtaji wowote. Tatizo la taasisi hizo ni mtaji. mimi nina uhakika taasisi hizi zina wataalam wa kutosha, lakini hawafanyi kazi yoyote kwa sababu hawana mtaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri, ni vizuri kutoa zile trilioni kwa upande wa uchukuzi pamoja na ujenzi lakini upande wa mawasiliano hajapewa fedha ya kutosha au hajaomba fedha ya kutosha. Ni fedha ndogo sana na kwa hiyo, haiwezi kufanya kazi kubwa inayotakiwa katika kutuimarishia mawasiliano na tunashida kubwa katika uimarishaji wa mawasiliano pande zote; mawasiliano ya simu pamoja na data. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana taasisi hizo zipate fedha za kutosha, zipate mtaji ili ziweze kujiendesha na kushindana na taasisi nyingine.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hii kwa asilimia 100 na niombe yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, mkongo wa Taifa. TTCL na Tume ya TEHAMA iimarishe kwa kuwekeza mtaji wa kutosha ili sekta ya mawasiliano ichangie zaidi katika uchumi wa Taifa na ukuaji wa sekta ya viwanda.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya yangu ya Namtumbo kuna maeneo yenye wakazi wengi lakini hayana mitandao ya mawasiliano ya simu. Ni maeneo yote ya Kata za Msindo, Mgombasi na Lisimonji. Aidha, vijiji vya Mtewamwachi, Likusanguse, Limamu na Mtakuja navyo havina usikivu wa mawasiliano ya simu. Naomba Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote utusaidie kukamilisha na kufungua mawasiliano ya simu na data katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuisemea barabara ya kuunganisha Mikoa ya Ruvuma na Morogoro ya Lumecha - Kitanda-Londo - Kilosa Kwa Mpepo – Lupiro - Ifakara - Mikumi. Mheshimiwa Rais ameliisemea barabara hii wakati akifungua Daraja la Kilombero na Kituo cha Mabasi cha VETA cha Namtumbo au tuseme alipokuwa kwenye ziara Mkoani Ruvuma kuanzia tarehe 4 hadi 09 Aprili, 2019 lakini katika kitabu naona shilingi milioni 80 tu ambazo haziwezi kujenga barabara kati ya Lupilo- Kilosa Kwa Mpepo-Londo - Lumecha kupitia Kitanda. Hii ni sawa kweli? Namwomba Mheshimiwa Waziri aliangalie suala hili.

Mheshimiwa Spika, kwa wana Ruvuma barabara ya kuunganisha Mikoa hii inaanzia Kilosa Kwa Mpepo - Londo - Kitanda. Kipande hiki cha kilometa 121.5 hivi ndiyo inaweza kuitwa kiungo cha mikoa hiyo miwili. Naomba fedha zilizotengwa zishughulikie kipande hiki cha barabara vinginevyo tafsiri ya bajeti hii ni kujenga barabara ya Mikumi - Ifakara - Mlimba na kuelekea Njombe badala ya barabara yetu wana Namtumbo.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kutufikiria wana Namtumbo kwa barabara zetu za kutoka Naikesi - Mkonga na Namtumbo – Likuyu –Namabengo – Mbimbi - Libango - Namtumbo na nyinginezo kwa kuzitengea fedha za matengenezo hususani lami nyepesi ya mita 100 katika barabara ya Naikesi - Mtonya.

Mheshimiwa Spika, aidha, kupitia Waziri, nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wetu mpendwa kwa kuitengea fedha ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara ya Mtwarapachani - Likusanguse - Nalasi jumla ya shilingi milioni 450 na hivyo kumfanya Mhandisi Mshauri aendeleze na kukamilisha kazi iliyoanza.

Mheshimiwa Spika, TARURA na TANROADS, taasisi hizi mbili zinapata fedha kutoka Hazina na Road Fund Board (RFB) kwa kuwa taasisi hizi ni za kushughulikia barabara. Naomba taasisi zote za TANROADS, RFB na TARURA ziwe chini ya usimamizi wa mamlaka moja ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Kuziweka taasisi hizo katika Wizara mbili tofauti inaongeza gharama za utawala na uendeshaji na kugawana wataalam hususani Wahandisi wa sekta ya barabara wachache tulionao nchini. Hoja za kupandisha hadhi barabara pamoja na kuiongeza TARURA mgao wa fedha za Mfuko wa Barabara zitaondoka ikiwa taasisi hizi za TARURA na TANROADS zitawekwa chini ya Wizara moja yenye wajibu wa kujenga na kukarabati barabara.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunipa pumzi. Aidha, nimpongeze Waziri na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiwezesha mihimili ya utawala na Bunge kufanyakazi kwa umakini na kwa umoja kwa kiwango cha kutuwezesha wana Namtumbo kuanza kuona maendeleo katika sekta mbalimbali hususani barabara, mawasiliano ya simu, umeme na kadhalika. Ahsanteni sana.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia 100 na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, niombe kutamka kuwa naunga mkono hoja hii kwa asilimia 100. Napenda Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Joseph Kakunda (Mbunge) anipe ufafanuzi katika maeneo yafuatayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala imeleta waraka wa kununua mazao ya ufuta, soya, alizeti na choroko kwa mfumo wa stakabadhi ghalani katika kipindi cha uvunaji wa mazao hayo hususan zao la ufuta katika Wilaya ya Namtumbo bila maandalizi yoyote. Hakuna maghala yaliyoandaliwa wala Vyama vya Msingi vya Ushirika havina maandalizi yoyote. Kwani suala hili ni la dharura au ni njama za Bodi hiyo kuwagombanisha wananchi na Serikali yao?

Mheshimiwa Naibu Spika, Vyama vya Msingi vilivyopo Namtumbo vinajihusisha na zao la kimkakati la tumbaku na wananchi wana uzoefu mbaya wa kuibiwa mauzo ya tumbaku yao na hivyo wana uoga ulio dhahiri wa kupeleka ufuta wao kwa Vyama hivyo vya Msingi bila kulipwa fedha zao kutokana na walivyodhulumiwa siku za nyuma. Tunalazimisha na matokeo yake sisi viongozi wao wa kuchaguliwa tunachukiwa. Naomba Waziri mwenye dhamana na biashara usitumie nguvu ya sheria kijeshi, badala yake wasiliana mapema na Waziri mwenzako mwenye dhamana ya ushirika na kilimo mpange na kufanya maandalizi ya utekelezaji wa sheria yoyote ile ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wakulima kabla ya msimu wa mavuno kuwadia.

Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya korosho kwa msimu huu unaomalizika haijaisha vizuri pamoja na uamuzi wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wa Serikali kununua korosho kwa bei nzuri ya Sh.3,300 kwa kilo moja. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais lakini Mawaziri mnaohusika na biashara hiyo mmetuangusha. Mpaka leo hii wananchi 76 wa Tarafa ya Sasawala, Wilaya ya Namtumbo hawajalipwa jumla ya Sh. 344,800,500/=. Wananchi hao ni wakulima waliozalisha na kuuza zaidi ya kilogramu 1,500 kwa kila mkulima. Dhana ya “kakumba” iliyotumika kuchelewesha malipo kwa wakulima hao imesababisha mateso makali kwa wakulima hao na kwa msimu huu wamenyimwa fursa ya kupalilia na kupuliza viualitifu katika mikorosho yao kwa kukosa uwezo. Tafadhali wakulima hao walipwe ili wajikimu na kuendeleza kilimo cha korosho.

Mheshimiwa Naibu Spika, wana Namtumbo kupitia Chama Kikuu cha Ushirika (SONAMCU) tumefanikiwa kumpata mnunuzi wa tumbaku, lakini kuna changamoto mbili kubwa Serikali isaidie kutatua. Moja, soko la tumbaku yetu ya Moshi (DFC) liko zaidi nchi za kiarabu kupitia mlango wa nchi ya Misri. Kwa kutokuwa wanachama wa COMESA, tumbaku yetu inaingia Misri kwa bei kubwa kutokana na ushuru unaotozwa na hivyo kushindana na washindani wetu ambao ni wakulima wa tumbaku hiyo na ni wanachama wa COMESA, ambao huingiza tumbaku yao bila kutozwa ushuru. Pendekezo, Serikali iingie “bilateral agreement” na Misri ili tumbaku yetu iingizwe nchini Misri bila ushuru kama ilivyo kwa nchi za COMESA vinginevyo turudi kuwa wanachama wa COMESA.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbili, mnunuzi wetu kampuni ya Premier Active Tanzania Ltd. wanaidai Serikali shilingi bilioni 12 zilizohakikiwa kama marejesho ya VAT. Hawarudishiwi, hivyo uwezo wa kampuni wa kuendelea kununua tumbaku ya wakulima wetu unapungua na nia yake ya kufufua kiwanda cha kuchakata tumbaku cha Mjini Songea haitekelezeki na hivyo kutunyima fursa za ajira na soko la uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni biashara, hivyo Waziri shirikiana na Waziri wa Kilimo na Waziri wa Fedha na Mipango haki ya kampuni ya kulipwa marejesho ya VAT yaliyohakikiwa ipatikane ili nasi wakulima wa tumbaku tuendelee kunufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na za kutukuka anazozifanya. Namtumbo tumeshuhudia maendeleo makubwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo na upatikanaji wa soko la tumbaku na soya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana. Naunga mkono hoja kwa asilimia 100. Nawasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu, kunipa afya leo naongea mbele ya Bunge lako Tukufu. Pili, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa kazi kubwa aliyoifanya na ninajua kazi hiyo inaakisi kazi kubwa inayofanywa na Serikali nzima ya Awamu ya Tano, ikiongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, nawapongezeni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, katika vipaumbele ambavyo umetuletea, kama rasimu, nimevisoma sana, umesheheni vyote, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, niombe mambo machache, mengi yamesemwa na wenzangu, lakini ninayo machache, kama utapata nafasi uyaongeze katika vipaumbele vya rasimu hii ambayo umetuletea. Nianze na eneo la sekta ya kilimo, wengi wameongea, kwamba kilimo ndiyo kinachoibua na kuimarisha sekta ya viwanda. Nikuombe, sekta ya kilimo ikiunganisha maeneo yote matatu, kilimo cha mazao, ufugaji mifugo na uvuvi, vipewe kipaumbele zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ilivyowekwa kwenye mpango, nina wasiwasi haijakaa vizuri. Katika eneo hili la kilimo cha mazao, ningeomba sana uliangalie sana eneo la pembejeo, hususani mbolea, lakini vilevile mbegu na viuatilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mbolea, ni kweli, tumeondoa ruzuku, nikuombe hilo uliangalie upya. Kilimo, ndiyo kinachukua watu wengi zaidi na wengi wanaojihusisha na kilimo hawana uwezo wa kumudu bei ya mbolea ambayo sasa tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali ya Awamu ya Tano, kama ambavyo imeweka kipaumbele kikubwa katika miundombinu, niombe muweke kipaumbele katika mbolea, mbegu,viuatilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza tu, kwamba katika mbolea, tuna uwezo kabisa wa kuweka ruzuku kwa asilimia 100, kwa maana ya kwamba, wakulima wapate bure. Kama hilo haliwezekani, walau ukaweka bei kama shilingi elfu 10, kama ambavyo mkulima wangu, Kuhoa amependekeza katika meseji aliyoniletea leo, kwamba walau ukiweka hata shilingi elfu 10 kwa mfuko katika kilimo, utakuwa umewasaidia sana wakulima wengi sana ambao kwa kweli hawana uwezo wa kununua mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa mbegu, hata Wizara ya Kilimo inafahamu, kwamba matumizi ya mbegu bora, ni kwa kiwango kidogo sana kwa sababu bei yake ni kubwa. Bei iliyopo katika mbegu wakulima hawaiwezi. Tunaishia kutumia mbegu zetu za asili ambazo hazina ufanisi katika uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ama tuimarishe taasisi zetu zinazozalisha mbegu nchini, tuingize fedha nyingi upande huo, badala ya kutegemea mbegu zinazotoka nje ama zinazozalishwa ndani, lakini zinazofadhiliwa na makampuni ya nje, bei muda wote itakuwa kubwa. Hebu tuliangalie lile eneo, kama tunaweza tukaingiza ruzuku ya kutosha, nina uhakika mazao yatakayozalishwa katika kilimo, tukiondoa ruzuku, yatarudisha hasara ambayo unadhania utaipata ukiweka ruzuku katika eneo hilo, nikuombe uliangalie hilo kwa makini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni maji, kipaumbele katika ulivyovyiorodhesha, hata katika eneo hili la maji nalo halijakaa vizuri sana. Nikuombe, jaribu kuliangalia kwa macho manne, matano, sita, hapo peke yenu mlipokaa una macho manne hapo, ya Waziri pamoja na Naibu, hebu ongezeni macho mengine katika eneo hili la maji. Najua mna sababu za msingi kukataa kuongeza shilingi elfu 50 kwenye mafuta, kwa ajili ya kuuongeza ule mfuko wa maji, ili utoke kutoka shilingi 50 uende shilingi 100, najua mna sababu za msingi, lakini hebu liangalieni hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumelipigania sana hilo la kuongeza shilingi elfu 50 zaidi, siyo kwa sababu tunataka kuongeza bei ya mafuta, lakini tunataka maji. Kwa hiyo, kama kuna namna ya kutuwezesha kupata maji, angalia katika vipaumbele vyako na eneo hilo nalo liguswe kwa namna ambayo kwa kweli watanzania watafurahia maisha, hasa watanzania wa kijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la miundombinu, umeelezea kwa kirefu sana maeneo ya reli yanayoshughulikiwa, lakini hii reli ya kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay kupitia Namtumbo, umeiweka chini sana ni kama umeificha hivi na kwa kweli ukiangalia kazi inayotakiwa kufanywa katika reli hii, inaonekana kabisa umeiweka pembeni. Yaani pamoja na kwamba umeandika sehemu ya kipaumbele, lakini in reality, nadhani bado haijaingia kwenye matrix yako kichwani mwako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe, tumeamua reli hii ijengwe kwa PPP, wenzangu waliotangulia wameeleza, kwamba fursa za wawekezaji binafsi wanaotaka kushughulika na hiyo reli wako wengi, lakini tatizo lipo katika masharti, liko katika masharti yanatakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu mliangalie hili kwa makini. Kwanza linapunguza matumizi ya fedha za Serikali. Tunatumia fedha kutoka sekta binafsi, hebu tujaribu kuangalia kama tunaweza tukapunguza masharti ili reli hii iweze kujengwa. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mpango, reli hii ukiikamilisha ukaipitisha pale Namtumbo ikafika mpaka Mbamba Bay na hatimaye ikafika Liganga na Mchuchuma, itajiendesha yenyewe na gharama zake zitarudi haraka zaidi. Kwa sababu mzigo ulioko katika hiyo corridor mwingi sana; ukiacha ile chuma ya Liganga na Makaa ya mawe ya Mchuchuma kuna madini mengine mengi sana ikiwa ni pamoja na Uranium ya Namtumbo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi madini ya Uranium yanashindikana kuchimba kwa sababu bei ya Uranium iko chini sana. Kwa sababu ya gharama zilizopo za usafirishaji, tukipunguza gharama za…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Engineer Ngonyani.

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa pumzi na kuniwezesha leo kuongea mbele ya Bunge lako Tukufu. Pili nikushukuru sana kwa kunipa furs hii na kwa kweli nitajitahidi kwenda haraka nikiwa kama mmoja kati ya wajumbe wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji.

Mheshimiwa Spika, kwanza ningeanza na taarifa ya jumla kwanza nimpongeze sana Mwenyekiti wa Kamati kwa kutuletea mapendekezo saba tu na kwa kweli sekta nzima ya maji ameleta pendekezo moja sekta nzima ya mifugo ameleta pendekezo moja, kilimo pendekezo moja, umwagiliaji pendekezo moja na uvuvi mapendekezo matatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuombe sana na Bunge lako Tukufu mapendekezo hayo tuyapitishe yawe maazimio ya Bunge letu Tukufu ili Serikali iyafanyie kazi. Nafahamu kuna pendekezo moja halijawekwa wazi ni pendekezo la kuhakikisha kwamba maazimio yaliyopitishwa mwaka jana tunaomba Serikali iendelee kuyatekeleza kama tulivyoyapitisha mwaka jana. Mapendekezo hayo ndio yanagusa watu wengi wameyachangia hapa wanadhani kwamba hayapo katika taarifa hii ya Kilimo, Mifugo na Maji lakini kwa sababu tayari yalishafanyiwa maazimio mwaka jana ikiwa ni pamoja na pendekezo ambalo Mheshimiwa Kiruso ameongelea suala la uendelezaji wa malisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono sana hoja ya kuanza viwanda vinavyotumia mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kama malighafi, hili pendekezo tukilipitisha na Serikali ikilichukulia kwa ukina wake litatusaidia sana katika kuendeleza sekta yetu ya viwanda lakini wakati huo huo kutoa fursa kwa wakulima kupata masoko ya mazao yanayozalishwa na vilevile kuongeza thamani mazao hayo na kwa maana hiyo kuongeza ajira kupitia sekta hizo za viwanda.

Mheshimiwa Spika, vilevile katika suala la umwagiliaji ni muhimu sana na tunaomba sana Serikali itilie mkazo katika kuhakikisha kwamba eneo hili la umwagiliaji linawekewa bajeti ya kutosha ili researchers wetu wanaoshughulikia na masuala ya mbegu ambazo zinagunduliwa na wataalamu wetu katika vituo mbalimbali vya utafiti viweze kuendelezwa na hivyo kupunguza kiwango kikubwa cha mbegu kinachoagizwa kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spia, nafahamu kwa sasa tunaagiza zaidi ya asilimia 60 na kwa kweli sio sahihi kabisa kutegemea kiwango kikubwa cha mbegu kutoka nje. Ningeomba sana Serikali itilie mkazo suala hili la umwagiliaji kwa sababu ni kweli changamoto kubwa kwa sasa haiwezekani kuandaa mbegu kwa kutumia mvua na wakati huo kipindi hicho hicho ndio uzalishaji wa mazao unatakiwa ufanyike.

Mheshimiwa Spika, ni kwa vyovyote vile utakuta mbegu zinazalishwa kwa wakati mmoja na kilimo chenyewe na njia pekee ya kuondokana na hili ni kuboresha umwagiliaji ili mbegu ziweze kuzalishwa kipindi cha kiangazi kisha wakulima wazipate kipindi cha masika tuweze kupanua kilimo chetu na wakulima wetu wapate mbegu bora na waongeze tija katika uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningeomba kuongelea vilevile suala la force account, wapo walioongelea, mimi nina mtizamo tofauti kidogo kwa maana naungana na Kamati lakini wakati huo kuna eneo nataka niliongezee. Kitu cha kwanza niipongeze sana Wizara ya Maji na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kweli suala hili la kutumia force account limetusaidia sana limebadilisha uwezekano wa kutekeleza miradi mingi sana ya maji kwa muda mfupi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miradi mingi ya maji kwa maana ya kwa utaratibu ule wa zamani wa kutumia wakandarasi ilikuwa unatumia fedha nyingi sana, mradi mmoja unatumia fedha nyingi sana lakini kwa namna ambavyo sasa hivi unafanyika fedha zile zinaweza zikafanya miradi mitano hadi sita badala ya mradi mmoja na mfano huo upo katika eneo ambalo natoka Wilaya ya Namtumbo. Nashukuru sana Waziri wa Maji amesitisha mikataba miwili na mingine miwili nayo amerekebisha ili kuhakikisha force account inatumika katika kununua vifaa na wale wakandarasi wanatoa tu labor force peke lakini vifaa vinanunuliwa na Serikali kupitia force account na matokeo yake gharama za mradi zimeshuka sana kwa zaidi ya asilimia 40 na hivyo kuwezesha miradi mingine mingi kuweza kutekelezeka.

Mheshimiwa Spika, napongeza sana hilo vilevile naungana na pendekezo la Kamati na mimi nimeshiriki kutoa hilo pendekezo kwamba tuangalie suala la ajira kwa makandarasi wetu na hasa wale wanaomaliza mafunzo katika vyuo vyetu vya VETA waweze kupata kazi kwa hiyo watumike na hivyo licha ya kutumia hiyo force account ni nzuri itumike lakini wakati huo tuangalie kuingiza na uwezekano wa kuzalisha ajira kwa private sector. Kwa hiyo, nilikuwa naomba na hilo liangaliwe kama ambavyo Kamati imependekeza. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja zote mbili asante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa pumzi. Aidha, nimshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa iliyofanyika katika kufufua zao la tumbaku Wilayani Namtumbo, pamoja na kutuletea soko la Stakabadhi Ghalani kwa mazao ya ufuta, soya, alizeti na dengu. Nimpongeze pia Mheshimiwa Rais kwa kumwona mchapa kazi, Waziri Mheshimiwa Japhet Hasunga na kumkabidhi Wizara hii ngumu ya Kilimo na Umwagiliaji. Yeye ni msikivu bila kujali aina ya hoja anazoletewa, anatusikiliza kwa unyenyekevu, ahsante sana.

Hata hivyo, kama mwakilishi wa wananchi wa Wilaya ya Namtumbo ambayo wakazi wake ni wakulima wadogo wasio na kipato cha uhakika, naomba aendelee kupokea hoja zifuatazo na kuzifanyia kazi:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, Benki ya Kilimo iwahudumie wakulima. Itoe mikopo kwa wakulima wadogo kupitia Vyama vyao vya Ushirika kama vile AMCOs zinazounda Chama Kikuu cha SONAMCU. SONAMCU inalazimika kukopa kwenye benki za kibiashara kwa ajili ya pembejeo na hivyo kutozwa riba kubwa inayomwongezea mkulima mdogo umaskini.

Mheshimiwa Spika, pili, Mfuko wa Pembejeo nao uwahudumie wakulima wadogo. Changamoto kubwa ya wakulima wadogo ni upatikanaji wa mbegu bora na mbolea. Pembejeo sio matrekta tu, tukopeshwe vile vile kwenye upatikanaji wa mbegu na mbolea.

Mheshimiwa Spika, tatu, tunampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa maamuzi ya kijasiri ya kununua korosho baada ya soko la zao hilo kuvurugwa na kutaka kumuumiza mkulima. Kwa Namtumbo, tunayo Tarafa moja ya Sasawala ambayo wakazi wake hutegemea zaidi zao la korosho. Wapo walioanza na kulipwa lakini wapo wakulima 76 waliouza jumla ya tani 104.485 za korosho hawajalipwa kabisa hadi hivi leo. Nimwombe Mheshimiwa Waziri ahakikishe wakulima hao wanalipwa haraka ili wapate nguvu ya kuendelea na kilimo cha korosho cha msimu mpya ambao umeshaanza na palizi na upuliziaji wa sulphur.

Mheshimiwa Spika, nne, kuna vikwazo vingi vinavyoathiri soko na uzalishaji wa zao la tumbaku na mazao wengine ya kimkakati. Tozo ni nyingi mno na utekelezaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) hauko sawa. Marejesho ya kodi hiyo hayafanyiki kwa wakati na hivyo kuathiri mtaji wa kufanyia kazi working capital kwa wanunuzi na wachakataji wa mazao hayo hususan zao la tumbaku. Hebu Mheshimiwa Waziri amshawishi Waziri wa Fedha na Mipango na Wajumbe wa Baraza la Mawaziri waelewe madhara ya kutolipa VAT return kwa wakulima wetu. Soko la mazao hayo litakufa na watakaoathirika ni wakulima wetu maskini.

Mheshimiwa Spika, tano, taasisi za udhibiti katiba sekta ya kilimo ni nyingi mno na zinafanya kazi zinazofanana. Ukienda kwenye tumbaku, sukari, korosho, chai ama pamba hali ya utitiri wa tozo inafanana. Viwango vya tozo za taasisi za udhibiti ni vikubwa mno, vinaongeza gharama za uzalishaji na kuzifanya bidhaa zetu zishindwe kushindana kwenye soko huria.

Mheshimiwa Spika, naiunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kwa asilimia mia moja na naomba majibu chanya ya maeneo matano ya hapo juu.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na naomba niendelee pale nilipokatishwa katika mchango wangu Bungeni. Kwa maoni yangu binafsi TMX iongoze soko na WRS iishie kumsimamia mtunza ghala/mwendesha ghala, na Sheria ya Ushirika ihusike na ukusanyaji wa mazao na kuyawasilisha kwa mwendesha ghala na kusimamia malipo kwa wakulima kupitia AMCOS.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ya mifuko inayotengenezwa na viwanda vitatu nchini kwa sasa ya kuhifadhi mazao, hasa ya nafaka, ili yasiharibike. Mifuko hiyo inapunguza Post harvest loss ambayo kwa sasa ni zaidi ya asilimia 40 hadi chini ya asilimia 10. Mifuko hiyo inakosa soko kwa sababu mbili kubwa. Kwanza VAT ya asilimia 18 inayosababisha bei yake kufikia sh. 5,000/= kwa mfuko mmoja na hivyo wakulima kushindwa kuinunua. Pili wakulima bado hawajaelimishwa faida na umuhimu wa kutumia mifuko hiyo na hivyo kuona bei ya 5,000/= kwa kila mfuko mmoja unaoweza kuhifadhi kilogramu 100 kuwa kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ifanye mambo mawili. Kwanza iondoe VAT kwenye vihifadhi nafaka ama vifungashio hivyo ili bei ishuke hadi 4,000/= na pili Serikali itoe elimu kwa wakulima juu ya umuhimu wa kutumia mifuko hii maalum ya kuhifadhi mazao ili yatumike kwa mwaka mzima bila ya kuharibika na wapate fursa ya kuyauza wakati bei ikiwa nzuri bdala ya kulazimika kuyauza wakati wa mavuno kipindi ambacho bei inakuwa ya chini sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeze Serikali chini ya Uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miradi mikubwa ya kielelezo inayotekelezwa; ya SGR, Umeme, upanuzi wa magati ya Bandari za Dar es Salaam Mtwara na Tanga; vile vile ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi, bwawa la kuzalisha umeme katika Mto Rufiji pamoja na bwawa la kuzalisha umeme kwenye Mto Rusumo. Hakika miradi hii ni ya kihistoria na itatuaondoa kwenye umaskini wa kipato na usio wa kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, historia nyingine ni pamoja na kuhamishia Makao Makuu ya Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kutoka Dareslaam na kuja hapa Dodoma. Dodoma ni katikati ya nchi yetu na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni historia ya kitaifa inayoandikwa na Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano (5). Kuna historia nyingi zimeandikwa na Serikali hii ya CCM ya awamu ya Tano katika Wilaya zetu zote nchini. Kwa mfano Namtumbo kwa mara ya kwanza Serikali hii iliyoundwa na Mheshimiwa Rais na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu Wilaya yetu tumejengewa kituo cha afya kimoja cha Kisasa kabisa, hospitali ya Wilaya, VETA; miradi mikubwa ya maji minne; umeme vijiji 43 kwa mpigo; minara ya mawasiliano katika kata 18 kati ya 21 tulizonazo; zahanati 11 kwa mpigo na kadhalika. Aidha, imetuleletea soko la mazao ya ufuta, tumbaku, soya na korosho pamoja na historia nyingine nyingi. Serikali hii idumu milele na milele, na tusiruhusu awamu nyingine ya utawala iingie.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba vituo vya afya, barabara, minara ya mawasiliano, miradi ya maji, zahanati na masoko ya mazao zaidi ili wata wa Namtumbo tuneemeke.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia kwa maandishi na nitachangia hotuba hii ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika maeneo mawili ya afya na maji.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza na maeneo hayo mawili, naomba kuipongeza Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na wasaidizi wake wakuu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu kwa makubwa wanayowatendea Watanzania hususan wakulima, wafugaji na wavuvi wadogo wadogo pamoja na wafanyabiashara-wamachinga nchini. Ahsanteni sana kwa kuwatetea na kuwasitiri utu wao kwa namna iliyotukuka, ni Mwenyezi Mungu pekee ndiye atakayewalipa.

Mheshimiwa Spika, Job Yustino Ndugai pamoja na msaidizi wako Mkuu Dkt. Tulia Ackson, Naibu Spika hongereni sana kwa kulisimamia na kuliendesha Bunge hili la Kumi na Moja kwa ustadi wa hali ya juu. Mmetupitisha salama katika majaribu mengi na sasa mmeendelea kutudhihirishia uwezo wenu mkubwa katika kipindi hiki kigumu cha janga la dunia la maambukizi ya Covid-19. Kwa kweli mlistahili nafasi hizo na mnastahili kuendelea kuliongoza Bunge la Kumi na Mbili ili nchi hii ya Tanzania iendelee kuwa tulivu na yenye amani.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri anayehusika na afya kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya ya kusimamia kudhibiti maambukizi ya virusi vipya vya Corona nchini kwa ustadi mkubwa. Kwa kweli ni muhimu kufuata miongozo ya WHO katika vita hii ya dunia nzima. Nilitaka kuiomba Serikali ijiandae na kukabiliana na mlipuko utakapoingia kwenye jamii mapema ikiwa tutafikia hatua hiyo itakayolazimu kuwa na wahudumu wa afya wengi na vifaa tiba na vitendanishi kwa wingi sana. Ni bora kujiandaa hata kama Mwenyezi Mungu atatuepusha na janga hilo na kwa kweli tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu atuepushe na janga hili.

Aidha, naomba tusilisahau tatizo la UKIMWI, na naomba Serikali izingatie mapendekezo ya Kamati ya UKIMWI hususan kuutunisha Mfuko pamoja na kutenga fedha zetu za ndani za kutosha kuwezesha kazi za kudhibiti maambukizi mapya na kuwahudumia wanaoishi na VVU zifanyike kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niongelee eneo moja la sekta ya maji ambalo ni matumizi ya force account katika kutekeleza na kusimamia miradi ya maji nchini. Uamuzi huu uliofanywa na Serikali ya awamu ya tano na kusimamiwa na Mheshimiwa Makame Mnyaa Mbarawa, Waziri wa Maji pamoja na timu yake yote ya Wizara ya Maji ni uamuzi wa kihistoria unaotuondolea dhulma waliyokuwa wanaipata wananchi hasa wa vijijini ya kutopata huduma stahiki ya maji na kwa wakati. Nikitolea mfano miradi ya maji ya Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, tulikuwa na wakandarasi wanne, (Ockra, Elegance, Vibe na Kipera) pamoja na mhandisi mshauri, Norplan. Baada ya Waziri wa Maji kuachana nao kwa sababu za mikataba, miradi hiyo sasa inatekelezwa kwa force account na gharama za miradi yote kwa ujumla imeshuka kwa zaidi ya asilimia 45! Hiyo ni faida kubwa sana, imeokoa rasilimali fedha.

Mheshimiwa Spika, wasiwasi wangu ambao ningependa Serikali iniondolee ni rasilimali watu kwa upande mmoja wa TARURA na kupotea kwa kazi na ajira kwa upande wa wakandarasi. Ushauri wangu ni kuwa wakandarasi wajirekebishe kwa kushirikiana na wahandisi wa Wizara wanaoandaa BOQs, waache kuifilisi Serikali na kuwadhulumu wananchi wanaokosa huduma ya maji wanayostahili na kwa wakati na TARURA waongezewe uwezo wa kuwasimamia wakandarasi kwa miradi mikubwa na uwezo wa kutekeleza miradi wao wenyewe kwa miradi midogo na ya kati.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba kutamka kuwa naunga mkono hoja kwa asilimia 100 na naomba kuwasilisha.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2018
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nachukua fursa hii kuwapongeza sana mwenzetu walioko Serikalini na hasa Waziri wa Sheria na Katiba pamoja na Mwanasheria wake Mkuu na timu yote iliyoko katika Wizara ile. Hiki walichotuletea kimekuja kwa wakati muafaka.

Mheshimiwa Spika, nawashukuruni sana katika kuleta marekebisho haya kwenye Sheria ya Michezo. Sasa tunaamini kwamba hakutakuwa tena na vurugu katika michezo na hasa kuchanganya kati ya michezo ya ridhaa na michezo ya biashara, kwa mfano, ngumi za kulipwa. Nashukuru sana, mmeileta kwa wakati na ni siku nzuri sana mmeleta huu Muswada siku ambayo tumeamkia na furaha iliyoletwa na Bondia wetu aliyeshinda kwa kishindo huko London, usiku wa kuamkia jana, nawashukuruni sana. Tunaomba mwendelee kurekebisha hili eneo, lakini tuzingatie vilevile masharti ambayo baadhi ya michezo yanatawaliwa na sheria za Kimataifa. Tusizipuuze, tuziangalie zikae vizuri, tuziingize katika mfumo wetu wa utoaji haki katika maeneo ya michezo.

Mheshimiwa Spika, vile vile ningeusemea huu Muswada wa Marekebisho unaohusu Mtakwimu Mkuu wa nchi yetu. Ni kweli kumekuwa na vurugu nyingi sana katika utoaji wa taarifa kiasi ambacho watu wengi sana tumekuwa tukishindwa kuamini taarifa ipi ni ya kweli. Serikali inatoa taarifa yake kupitia National Bureau of Statistics lakini tunapata taarifa nyingine kutoka vyanzo mbalimbali vinavyopingana na statistics hizo, tukimtaka mtu wa NBS ajaribu kuangalia au kuhakiki taarifa zinazotoka, kwamba pengine kutokana na kupitwa kwa muda taarifa zake hazikuwa sahihi lakini kumbe tunao watu wengi tu wanaotengeneza taarifa mbalimbali kwa madhumuni mbalimbali na mara nyingi sana wanaishia kuyumbisha watafiti ambao wanapenda sana kutumia taarifa mbalimbali kama reference ya kufanya utafiti ambao utaweza kusaidia nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nampongeza sana Mwanasheria Mkuu na Mwandishi Mkuu wa Sheria, lakini najua hawa wote wanaongozwa na Mheshimiwa Waziri Prof. Palamagamba Kabudi, hongera sana kwa kazi kubwa unayoifanya. Najua kuna changamoto nyingi, watu wamezoea kujitolea takwimu wanavyopenda, tumeona mara nyingi sana taarifa zinatoka zinazopingana, zote zimefanywa kwa wakati mmoja na ukubwa wa sampuli ni ule ule, lakini matokeo yanakuwa tofauti kabisa. Ni kwa sababu tu kila anayefanya utafiti kwa kawaida wengine wanaanza kwanza na majibu halafu wanakwenda kufanya utafiti ku-justify majibu wanayotaka kuyatoa. Kwa hiyo, tunashukuru sana kwa sasa Muswada huu kuletwa kuhakikisha kwamba takwimu yoyote kabla haijaenda kwa walaji, lazima kwanza ihakikiwe na ikubaliwe na National Bureau of Statistics. Tunakushukuru sana kwa kazi hiyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa na wasiwasi na mobile courts lakini pengine siyo vizuri kuiongelea tena kwa sababu mmekubali ushauri wa Kamati yetu ya Katiba na Sheria, tunashukuru. Hizi mobile courts zina uzuri wake, lakini kuna changamoto zake na kwa sababu ni masuala ya haki hata kama changamoto ni kidogo, mimi nashukuru sana kwa Serikali kukubali kuondoa vifungu hivyo ili tukaliangalie upya kwa undani zaidi kabla hatujarudi tena au tukaliweka vizuri zaidi kwa namna ambayo mtaona inafaa.

Mheshimiwa Spika, nawashukuruni sana kwa kazi hiyo kubwa mliyoifanya na kwa kweli sikupenda sana nichangie baada ya mabadiliko haya yaliyoletwa na Serikali kwa sababu mengi yaliyoletwa yameniondoa katika maeneo yale ambayo nilikuwa na dukuduku nayo na kwa kweli sikujua kama Serikali hii ni sikivu kiasi hiki. Nawashukuruni sana, mwendelee kuwa sikivu katika maeneo mengi ili hatimaye nchi hii iende kwa namna ambayo hakuna ambaye atasikia amenyimwa haki, hakuna ambaye atafika mahali atakata tamaa ya maisha kwa sababu upatikanaji wa haki unakuwa mgumu.

Mheshimiwa Spika, tunashukuru sana kwa namna walivyorahisisha na hasa lile eneo walilogusa la matajiri ambao kila wakati tumekuwa tukipata nao shida kwa kutumia wanasheria waliobobea na badala ya kuzungumzia changamoto au dhuluma iliyopo wanaanza kubishana kwenye utaalamu wa uandishi, hapa koma ilikosewa, mara suala hili halikuanza kwa muda ambao ulitakiwa, siku zimezidi, technicalities. Nawashukuru sana kwa kuliondoa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini wataondoa hili katika maeneo mengi zaidi, siyo haya machache tu ambayo kwa hapa naona zaidi wameyaingiza kwenye masuala ya ardhi na makosa mengine machache yaliyoyaingizwa katika Muswada huu. Naomba sheria nzima ile ya Mwenendo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018
MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu wka kunipa fursa hii ya kusimama mbele yako na kutoa mchango wangu.

Pili, niishukuru Kamati yangu ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa kunipa fursa ya kueleza taharuki zangu na hatimae kufanyiwa kazi, nashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, naomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuiangalie kwa makini Ibara ya 62 ya Muswada wa Maji (The Water Supply and Sanitation Act of 2018). Ibara hii inakusudia kuharamisha matumizi ya maji kutoka katika kila aina ya chanzo. Kidogo wakati tunaijadili wengine ilitupa taharuki kidogo kwa sababu kule tunakotoka tuna vyanzo vingi vya maji ambavyo wananchi wetu wanavitumia. Kwa hiyo, kuharamisha matumizi mpaka mtu apate kibali kwa kweli ilikuwa ni jambo la hatari sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali kwa kuwa imeliangalia hilo pamoja na kwamba haijaliweka kwa namna ambavyo tulitaka, lakini angalau kuna unafuu na sasa tunaacha matumizi ya maji yaendelee kusimamiwa na Sheria ya Matumizi ya Rasilimali Maji Namba 9 ya mwaka 2009 badala ya kuyaingiza katika muswada huu. Muswada huu ubakie kushughulikia huduma na watoa huduma wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tulipoliona hilo tukaangalia Sheria ya Matumizi ya Rasilimali Maji kifungu cha 11, 12, 52 na 54 ni kweli kinaondoa yale maji ambayo yanatumiwa na watu mbalimbali kimila watu waendelee kuyatumia maji hayo kwa namna walivyozoea na kufuata desturi za maeneo hayo. Hata hivyo bado kuna mapungufu yapo, na tunaiomba Serikali, na bahari nzuri Mwenyekiti wangu amelieleza kwa upana kwamba Sheria hiyo tuipitie upya ili tuweze kuboresha pale ambapo tunadhani ni muhimu tukapaweka sawa ili umuhimu wa maji ni uhai tusiuvuruge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye Ibara ya 63 ya muswada huo huo wa maji. Kuna dhana ya kuharamisha matumizi mabaya ya maji. Kwa namna ilivyowekwa katika Ibara hiyo ya 63 imetupa wasi wasi mkubwa kwamba tunaweza tukawa tunaandaa eneo ambalo watendaji wasio waaminifu wenye nia ya kuigombanisha Serikali na wananchi wake wakaitumia vibaya. Kwa hiyo, tunaomba kama ambavyo imesisitizwa na Taarifa ya Kamati neno hili la misuse of water au matumizi mabaya ya maji lifafanuliwe ndani ya sheria ili wote tuwe na uhakika kwamba tunaposema matumizi mabaya ya maji tunamaanisha nini. Isitokee wajanja wakatumia nafasi hiyo kutuvuruga ndani ya nchi, maji ni uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuangalie jedwali la tatu, fasili ya 1(a), lakini vilevile tulinganishe na jedwali la nne, fasili ya tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa tafsiri yangu, maeneo haya yanaondoa watumishi wa umma katika usimamizi au katika uendeshaji wa bodi mbalimbali za maji. Ni kweli tuna wataalam wengi kwenye sekta binafsi wanaoweza kuongoza hizo bodi na wakawa Wajumbe na Mwenyekiti, ni kweli, lakini inaweza ikatokea kwamba tuna wataalam waliobobea zaidi ndani ya public service, ndani ya utumishi wa umma ambao wanaweza wakatupa huduma kubwa zaidi katika uendeshaji au usimamizi wa bodi hizi. Niombe sana, sina uhakika dhamira ilikuwa nini ya eneo hilo la kutaka Mheshimiwa Rais azuiwe kuteua Mwenyekiti wa Bodi kutoka kwenye sekta ya umma na kwamba ni lazima aende kwenye sekta binafsi, sina uhakika dhamira yake hasa ni nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tunajua dhamira ya sekta binafsi ni kutengeneza faida, dhamira ya sekta binafsi muda wote na faida nyingi itatokana na kuongeza kodi, kuongeza ushuru na kukwepa ulipaji wa kodi na ushuru; huko ndiko kunakopatikana faida nyingi. Sasa tukifanya bodi zetu za maji zote ziongozwe na dhamira hiyo ya utengenezaji faida wakati maji ni huduma nadhani si sahihi sana kwa maoni yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana, hebu angalieni upya hilo eneo. Turuhusu watu ambao ni competent iwe kutoka kwenye public au private sector nao waweze kufikiriwa katika uongozi wa bodi hizo, hicho kizuizi cha public sector kiondolewe. Kwa bahati mbaya sina schedule of amendments na wala Kamati haikuliongelea hilo kwa undani, kwa hiyo, natoa tu kama ushauri kwa Serikali waliangalie hilo kwa makini ili kama wataridhika wafanye amendments ili turuhusu public sector nayo ifikiriwe na Mheshimiwa Rais katika kuteua Wenyeviti wa taasisi hizi za maji RUWA au RUWASA vile vile na ile National Water Fund.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba twende kwenye jedwali la kwanza, fasili ya tano inayoongelea kwamba angalau theluthi moja ya Wajumbe wa Bodi wawe wanawake.

Mheshikmiwa Mwenyekiti, maji kwa maeneo mengi sana ni shughuli ya akina mama. Wanaojua uchungu wa ukosefu wa maji ni akina mama. Niiombe sana Serikali, tumevutana sana hili na tunajua msimamo wa Serikali, lakini tunawaomba sana hapa kabla hatujamalizia hebu lifikirieni hilo. Mimi binafsi ningependa asilimia 100 ya Wajumbe wa kuteuliwa wawe akina mama; lakini nadhani kwa kufuata…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Engineer Ngonyani kwa mchango wako.

MHE. ENG. EDWIN A. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia 100, ahsante sana.