Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Leonidas Tutubert Gama (1 total)

MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali juu ya ujenzi wa daraja la Kilombero lakini ahadi ya Serikali ya kukamilisha ujenzi wa barabara kupitia daraja la Kilombero kwenda Songea kupitia Namtumbo ni ya muda mrefu sana na hivi sasa wananchi wa Songea ukitaka kusafiri kwa kawaida ni masaa 15 kutoka Dar es Salaam mpaka Songea. Hii barabara kutoka Kilombero kukatiza Namtumbo kwenda Songea ingerahisisha sana na usafiri ungekuwa mwepesi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni vizuri Serikali itupe majibu ni lini tunatazamia tuanze ujenzi wa barabara hii ya kuelekea Songea kupitia Kilombero? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hoja ya kujenga barabara hii ilianza toka mwaka 1996, tunafahamu. Tatizo lililokuwepo katika kipindi kirefu sana tulikosa fedha lakini hatimaye katika kipindi hiki na Serikali hii ya Awamu ya Tano naomba nimhakikishie kwamba kazi hii itafanyika muda si mrefu na kwa vyovyote ni ndani ya kipindi cha miaka mitano ambayo ahadi imetolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu, akiangalia kitabu chetu cha Ilani atakuta hii barabara imeandikwa itajengwa kwa kiwango cha lami na hatua za mwanzo ndio hivyo tunazikamilisha mwezi Mei na baada ya hapo tunaanza utaratibu wa kutafuta fedha za kujenga hiyo barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine vile vile mimi mwenyewe natoka Namtumbo na nimetoa ahadi kwamba barabara hii mwaka huu lazima itoboke, isipotoboka TANROADS watatoboka! Kwa hiyo, nimhakikishie suala la kutoboa barabara hii, itatoboka mwaka huu, lakini kuanza ujenzi ni baada ya miaka ijayo ya fedha.