Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Leonidas Tutubert Gama (10 total)

MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii nishukuru kwa majibu ya Wizara, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wananchi wa Songea Mjini na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla wanapata shida sana ya kupata mbolea kwa wakati, mbolea huchelewa sana kufika. Lakini vilevile wanakopwa mahindi yao, pamoja na kununua mbolea kwa bei kubwa, lakini wamekuwa wakikopwa mahindi yao na NFRA matokeo yake wakulima hawa wanaendelea kuwa maskini, wanateseka sana.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa wakulima hawa wanapata haki yao kwa muda unaostahili?
Swali la pili, mwezi Disemba mwaka jana Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, alifanya ziara Songea Mjini; na alipata bahati ya kutembelea ghala la hifadhi ya mahindi la NFRA. Alikutana na matatizo mengi ya wananchi pale NFRA; na akatoa maagizo na agizo moja alitoa la kwamba NFRA hivi sasa inunue mahindi moja kwa moja kwa wakulima badala ya walanguzi. Lakini la pili alitoa maagizo kwamba bei elekezi ya Serikali ihakikishe inamfikia mkulima wa kawaida kule anakolima; na ya tatu aliagiza kwamba magunia ambayo yamekuwa yakitolewa kwa walanguzi, na kwa hiyo kuwalangua wakulima wa kawaida. Alipiga marufuku akataka magunia yote wapelekewe wakulima wa kawaida wa mahindi.
Sasa nataka niulize je, Wizara imejipangaje kuhakikisha inasimamia maagizo haya ya Waziri Mkuu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema kwamba, mbolea mara nyingi hazifiki kwa wakati, na imekuwa ikiuzwa kwa bei ya juu; na ndio maana nimeeleza katika jibu langu la msingi kuwa tupo katika mkakati wa kuhakikisha kwamba ruzuku zinapatikana kwa bei nafuu, kwa kujaribu kuhuisha utaratibu mzima unaotumika kwa sasa wa kupeleka pembejeo kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika msimu utakaokuja, maana yake tukianza kutekeleza Bajeti yetu ya mwaka unaokuja wa fedha, hatutasikia tena kitu kinachoitwa utaratibu wa vocha wa kupeleka pembejeo kwa wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakuwa na utaratibu mpya kabisa, na tunaamini kwamba kwa kiasi kikubwa itaondoa shida iliyopo. Lakini vilevile nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tatizo lingine ambalo linatokea Ruvuma kama ilivyo katika maeneo mengine nchini; ni kwa sababu malipo ya mahindi kwa wakulima yanachelewa kwa sababu kunakuwa na walanguzi wa kati. Nimfahamishe tu kwamba kwa sasa utaratibu huo utaondolewa, wakulima wanakuwa wanalipwa moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile nipende kujibu swali lake la pili la nyongeza, kuhusu ziara ya Waziri Mkuu aliyofanya ya tarehe 6 Januari mwaka huu Ruvuma; ambapo pamoja na mambo mengine alitoa maagizo matatu kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge.
Moja ni kuhusu kuwaondoa watu wa kati nimueleze Mheshimiwa Mbunge kwamba maagizo ya Waziri Mkuu sisi tunayafanyia kazi, na nimhakikishie kwamba kuanzia sasa mahindi yatanunuliwa moja kwa moja kutoka kwa wananchi na sio kupitia kwa watu wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile kuhusu bei elekezi, nimueleze kwamba kuanzia sasa bei ile ya dira bei elekezi ambayo inatolewa na NFRA bei hiyo ndio inatumika kununua mahindi ya wananchi; na hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kwenda kupunguza bei hiyo, kwa hiyo watu wa kati hawataweza tena kufanya biashara kama hiyo.
Lakini vilevile kuhusu magunia na vifaa vingine, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, agizo la Waziri Mkuu kuhusu hili linatekelezwa; na kwamba sasa magunia yanapelekwa moja kwa moja kwa wananchi, na sio kupitia kwa watu wa kati.
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri aliyonipatia, lakini naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni kwamba amesema Mji wa Songea una uwezo wa kupata megawatt 4.7 na hivi sasa wana uwezo wakuzalisha megawatt 9.5. Lakini naomba niseme kwa masikitiko kwamba bado katika mji wa Songea kuna maeneo ambayo hayajafikishiwa kabisa umeme, maeneo kama Ndilima Litembo, Mletele, Lilambo B, Mwanamonga, Sinai, Mwenge Mshindo, Chandarua, Luhilaseko, Kuchile, Lizaboni katika eneo la London, Mang‟ua, Subira, Mtendewawa, Mkesho na kadhalika hayajafikishiwa umeme. Sasa naomba Mheshimiwa Naibu Waziri anithibitishie, je, maeneo haya ambayo umeme haujafikishwa ni lini Serikali itayafikishia umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, lipo tatizo kubwa sana kwa Songea Mjini, la umeme kukatika mara kwa mara, na umeme unapokatika mara kwa mara unasababisha kuunguzwa kwa vifaa vya wananchi katika nyumba zao. Lakini la pili, inazuia kukua kwa shughuli za kiuchumi katika mji wa Songea. Je, Serikali ina mpango gani wa kukomesha tatizo la kukatika katika kwa umeme na lini litakuwa na utaratibu wa kuwalipa fidia wale wote wanaounguza vifaa vyao kwa sababu ya kukatika kwa umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri anijibu maswali yangu.
NAIBU WAZIRI NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Gama na Waheshimiwa Wabunge, kama tulivyoeleza kwenye bajeti yetu na kama ambavyo kila mara ninaeleza, kwamba wananchi wa Songea, Ludewa, Njombe Mjini na Vijijini, utaratibu wa kuwapelekea umeme wa uhakika kutokana na usafirishaji wa umeme wa kilovoti 220 kwa umbali wa kilometa 250 ambao utaanza Januari mwaka huu unakuja, na kazi yake itakamilika mwezi Juni, 2018. Kwa hiyo, Mheshimiwa Gama nimhakikishie kwamba vijiji vya Mlima Litembo pamoja na Mwengemshindo na vingine vitapatiwa umeme kuanzia mwezi Juni 2018 na utakuwa ni umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili la Mheshimiwa Gama, juu ya kukatika katika kwa umeme. Ni kweli kabisa na Waheshimiwa Wabunge kama mnavyojua, sasa hivi tunafanya kazi kubwa tatu. Kazi ya kwanza ni kuongeza nguvu ya umeme kutoka kilovoti 132 hadi kufikisha kilovoti 400. Lakini kwa Makambako – Songea tunaongeza umeme wa kilovoti 33 hadi kilovoti 220 ambao sasa utamaliza tatizo la kukatikakatika katika miji ya Songea, Njombe, Ludewa pamoja na maeneo ya jirani.
Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Gama, mara baada ya kuweka kilovoti 220 maeneo yote ya Jimbo la Songea Mjini, Ludewa, Njombe Mjini na Njombe Vijijini kukatikakatika kwa umeme kutakoma mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Gama kuhusiana na suala la fidia. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge, lakini pia nichukue nafasi hii kuwatangazia wananchi wote, kukatikakatika kwa umeme inawezekana kukachangia sana kuharibika kwa miundombinu ya nyumbani lakini pamoja na vifaa vinavyotumia umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hata hivyo matumizi sahihi ya umeme ni muhimu sana. Niwaombe sana wananchi na Waheshimiwa Wabunge, mara TANESCO na mashirika yanapokuwa yanakata umeme kwa ajili ya kufanya marekebisho tuwe tunapunguza au kuzima vyombo vyote vinavyotumia umeme ili umeme ukija sasa usisababishe uharibifu.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Gama kwamba kusababaishwa kwa uharibifu wa umeme kwenye vyombo vya ndani inawezekana kabisa ama uzembe wa matumizi, ama uzembe wa TANESCO. Mahala ambapo TANESCO itasababisha tutafanya utafiti, na tukiona kwamba kuungua kwa vyombo hivi kumesababisha na TANESCO tutafanya fidia kulingana na uharibifu uliotokea.
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kule Songea kuna uchimbaji wa makaa ya mawe katika eneo Ngaka na uchimbaji wa makaa yale ya mawe unapita katika Mji wangu wa Songea. Kwa hiyo, pale Songea kuna uharibifu mkubwa sana wa mazingira kwa sababu yale magari yanayopita ni magari ya open body sio box body, matokeo yake ni kwamba mji unaharibika kimazingira lakini vilevile barabara zinaharibika. Nataka nijue Serikali ina mpango gani wa kuulipa fidia Mji wa Songea ili kukabiliana na majanga yanayotokana na usafirishaji wa makaa hayo ya mawe?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama mnavyotambua, shughuli za uchimbaji wa madini zinaathiri mazingira kwa vyovyote vile hasa katika kusafirisha mitambo, kusafirisha madini lakini hata wakati wa uchimbaji. Nikubaliane na Mheshimiwa Gama kwamba kama kuna uharibifu wa mazingira kama ambavyo Sheria ya Madini inataja kwenye kifungu cha 65(1) (b) kwamba kama kutakuwa na uharibifu wa mazingira, Halmashauri inayohusika watakaa na mgodi kujadili uharibifu uliotokea kwa ajili ya kulipa fidia. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge akae na Halmashauri yake, kama itadhihirika kwamba kuna uharibifu wa barabara unaosababishwa na kampuni hii basi wakubaliane suala la fidia kwa mujibu wa Sheria ya Madini pamoja na Sheria ya Ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo, yapo majukumu mengine ya mgodi pamoja na Halmashauri. Nawashauri wakae wakubaliane juu ya tozo zinazoweza kutozwa kutokana na uharibifu wa mazingira. Hata hivyo, kabla ya mgodi kufungwa kwa kawaida kuna jambo linaitwa mine closure plan, hawa wamiliki wa leseni wana mine closure plan inayoonesha kwamba kama kuna uharibifu wa mazingira basi utafidiwa kulingana na uharibifu ulivyotokea.
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali juu ya ujenzi wa daraja la Kilombero lakini ahadi ya Serikali ya kukamilisha ujenzi wa barabara kupitia daraja la Kilombero kwenda Songea kupitia Namtumbo ni ya muda mrefu sana na hivi sasa wananchi wa Songea ukitaka kusafiri kwa kawaida ni masaa 15 kutoka Dar es Salaam mpaka Songea. Hii barabara kutoka Kilombero kukatiza Namtumbo kwenda Songea ingerahisisha sana na usafiri ungekuwa mwepesi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni vizuri Serikali itupe majibu ni lini tunatazamia tuanze ujenzi wa barabara hii ya kuelekea Songea kupitia Kilombero? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hoja ya kujenga barabara hii ilianza toka mwaka 1996, tunafahamu. Tatizo lililokuwepo katika kipindi kirefu sana tulikosa fedha lakini hatimaye katika kipindi hiki na Serikali hii ya Awamu ya Tano naomba nimhakikishie kwamba kazi hii itafanyika muda si mrefu na kwa vyovyote ni ndani ya kipindi cha miaka mitano ambayo ahadi imetolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu, akiangalia kitabu chetu cha Ilani atakuta hii barabara imeandikwa itajengwa kwa kiwango cha lami na hatua za mwanzo ndio hivyo tunazikamilisha mwezi Mei na baada ya hapo tunaanza utaratibu wa kutafuta fedha za kujenga hiyo barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine vile vile mimi mwenyewe natoka Namtumbo na nimetoa ahadi kwamba barabara hii mwaka huu lazima itoboke, isipotoboka TANROADS watatoboka! Kwa hiyo, nimhakikishie suala la kutoboa barabara hii, itatoboka mwaka huu, lakini kuanza ujenzi ni baada ya miaka ijayo ya fedha.
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kwa mheshimiwa Waziri kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi sote tunajua kwamba tutakuwa wazee, hawa wazee hivi sasa wanateseka sana, hali zao za maisha ni ngumu, uwezo wao wa kupata huduma za dawa ni mdogo. Sasa nilitaka nijue katika mpango wetu tumepanga mpango wa kuhakikisha wazee hawa wanatibiwa bure. Je, ni lini Serikali itatoa uamuzi wa kuwatibu bure wazee ili angalau waondokane na matatizo waliyonayo? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, tulizungumza sana juu ya suala la wazee kupata pensheni ili ziwawezeshe kupata huduma muhimu. Mpango huu tumeuzungumza lakini hatujapata mwelekeo wa nini tunafanya kwa wazee ili waweze kupata pensheni zao. Sasa naomba nipate uhakika Serikali ina mpango gani na imejipangaje, lini tutaanza utaratibu wa kuwapa pensheni wazee ili waweze kujipatia huduma muhimu kama za matibabu, elimu na kadhalika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la kwanza, kwamba ni lini Serikali itaanza kutoa huduma bure za afya kwa wazee, jibu letu ni rahisi tu kwamba tayari Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007 inatoa msamaha wa matibabu kwa wazee wote wenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea wasiojiweza; napigia mstari neno wasiojiweza. Kwa hivyo, taratibu za kuwahudumia wazee wasiojiweza zipo na zimewekwa wazi na Sera ya Afya ya Taifa lakini pia na miongozo mbalimbali ya kutoa huduma za afya nchini. Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakoelekea mkakati wetu kama Serikali ni kutafuta namna bora zaidi ya kuzihamasisha na kuziwezesha Halmashauri zetu nchini kuwakatia kadi za CHF wazee wote ambao wanakidhi vigezo hivyo. Tayari Waziri wa Afya mwezi wa 12 alitoa agizo hilo kwenye Halmashauri zote nchini na kuna baadhi ya Halmashauri zimeanza utekelezaji wa agizo hilo na ninaamini wazee wanafaidika na mpango huo. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la pensheni kwa wazee; Serikali inatambua mchango mkubwa uliotolewa na wazee wetu kwenye ujenzi wa Taifa hili, na ndiyo maana tunaweka mikakati mbalimbali ya kuwahudumia wazee wetu hususani katika kipindi ambapo wame-retire na hawawezi kuendelea kufanya kazi za nguvu za kuzalisha na kukuza kipato chao. Na kwa msingi huo ndiyo maana tumeanza mchakato wa kutengeneza mkakati ambao utatuwezesha kuwahudumia wazee. Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya kwanza tuliyoifanya ni kutazama takwimu za sensa na kuona kama tutakuwa na uwezo wa kuwa hudumia na kwamba tutakuwa tunabeba mzigo kiasi gani wa wazee ili tuweze kufikiria kama ni kitu tunachoweza kukitekeleza na pengine kukiingiza kwenye bajeti. Kwa sasa kamati ambayo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge inaendelea kutekeleza utaratibu mbalimbali wa kupitia takwimu hizo na kufanya tathmini na baadaye mchakato wa ndani ya Serikali utakapokamilika tutafanya utekelezaji wa mpango huo. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nitumie nafasi hii kuwahamasisha Waheshimiwa Wabunge wote tuliopo hapa na wananchi wote wakazi wa Dodoma kushiriki kwenye mazoezi ambayo yataongozwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kesho asubuhi saa 12 kuanzia kwenye viwanja vya Bunge tutatembea kilometa 5.2 tukiongozwa na Waziri Mkuu wetu mpaka kwenye viwanja vya Jamhuri. Hii itatusaidia kuondokana na changamoto za kutumia sana dawa za shinikizo la damu, lakini pia dawa za kisukari kwa sababu tutakuwa na afya bora. Nakushukuru.
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini nataka nimjulishe kwamba Hospitali ya Rufaa hiyo ya Mkoa wa Ruvuma ina msongamano mkubwa sana wagonjwa na hasa akinamama wajawazito na watoto. Kwa mfano, hivi sasa Hospitali ya Mkoa ina vitanda 13 tu kwa ajili ya akinamama wajawazito na watoto. Akinamama hawa kwa wastani wa siku ni wagonjwa 25 mpaka 35 wakitumia vitanda 13.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile lipo tatizo la msingi kweli kweli; pale katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa akinamama wajawazito wananunua dawa, damu, mipira ya kujifungulia na vifaa vingine vyote vya kujifungulia, wananunua wenyewe. Sasa nauliza: Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba huduma zinazotolewa za akinamama wajawazito na watoto zinatolewa katika kiwango kinachotakiwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa vile hivi sasa tunategemea sana Kituo cha Afya cha Mji Mwema ambacho Mheshimiwa Naibu Waziri amesema bado hakijafika mahali kikapandishwa hadhi ya kuwa hospitali kamili. Je, Serikali ni lini italeta gari ya wagonjwa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wanaofika katika Kituo cha Afya cha Mji Mwema hasa akinamama wajawazito na watoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nipokee malalamiko ya Mheshimiwa Mbunge kwamba pale akinamama wananunua dawa, vifaa tiba na mambo mengine; hili Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ameshali-cite pale, ina maana jambo hilo lipo. Katika ziara zangu kwa maeneo mbalimbali nilikuwa nikitoa maelekezo kwamba Serikali inapeleka fedha katika Vituo vya Afya hasa katika Halmashauri zetu; lengo kubwa watu wapate dawa na vifaa tiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza hapa mara kadhaa kwamba kwa kipindi cha sasa suala la uzembe kwamba Serikali inatoa fedha lakini watu hawazitumii kama inavyokusudiwa (kununua dawa na vifaa tiba), niliwaeleza DMOs wote na Waganga Wakuu wa Mikoa sehemu nilizopita kwamba wahakikishe fedha zinazokwenda lazima ziweze kutumika kama inavyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nichukue concern hii, lakini hata hivyo, nafahamu kwamba Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alitoa fedha kwa ajili ya kununua vitanda katika Halmashauri zetu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na hivi vitu vimeshakuwa tayari, naomba na yeye avipokee aende akakabidhi mwenyewe pale. Lengo kubwa ni kupunguza changamoto katika maeneo yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kwamba hakuna ambulance; mara kadhaa nimekuwa nikitoa ufafanuzi hapa ikiwezekana mchakato uanze katika Halmashauri zetu. Naomba niseme kwamba kilio hiki cha Mheshimiwa Mbunge tumekisikia, japokuwa suala la ambulance lazima lianzishwe katika Halmashauri kuonesha yale mahitaji, lakini tutaangalia nini kifanyike sasa kushirikiana pamoja Serikali Kuu na Halmashauri ya Songea ili tupate ambulance. Wapi itakapotoka, hiyo haijalishi, lakini cha msingi tupate ambulance kwa ajili ya wakazi wengi sana nikijua wazi kwamba hata watu kutoka eneo la Namtumbo wanakuja pale Songea kwa ajili ya kupata huduma ya afya.(Makofi)
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa wananchi wa Mkuranga na Kisiju pale Songea Mjini na sisi tuna tatizo hilo hilo la ‘X’. Barabara ya Mtwara Corridor ambayo inapita Songea Mjini inafanya mchepuko katika eneo la Ruhilaseko kuelekea Masigira, Msamala, Mkuzo na Luhuwiko. Eneo hili wananchi wamewekewa ‘X’ kwa muda mrefu lakini hawajalipwa fidia yao na wala barabara haijaanza kujengwa. Sasa naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, je wananchi hawa ambao wana alama za ‘X’ za muda mrefu ni lini watalipwa fidia zao ili barabara ianze kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jibu la haraka kwa swali lake ni kwamba tutalipa fidia mara pale barabara hiyo au barabara ile ya mchepuko tutakapoanza kuijenga. Katika fedha tutakazozitenga kwa ajili ya kujenga barabara ile ya mchepuko zitahusisha vilevile na fedha za fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda tu niongeze kidogo kuhusu eneo analoliongelea, kwa bahati nzuri ule mchepuko ni lazima ujengwe haraka kutokana na mazingira ya mji wa Songea yalivyo, na hivyo nimhakikishie tu kwamba malipo haya hayatachelewa sana kwa sababu ujenzi wa barabara ile ya mchepuko hautachelewa sana kushughulikiwa.
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Songea Mjini katika maeneo hayo niliyoyataja niishukuru sana Serikali kwa kutupa matumaini kwamba fidia hiyo italipwa kipindi cha bajeti ya fedha mwaka 2018/2019. Sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, la kwanza, katika eneo hilo wapo wananchi 157 ambao wanadai kwa namna moja ama nyingine majina yao yaliondolea kwenye eno la fidia. Sasa naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, Serikali iko tayari kufuatilia ukweli juu ya wananchi hawa 157 ili ukweli ukijulikana walipwe fidia zao?
Mheshimiwa Spika, la pili, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, kwa sababu wananchi wa aneo hilo pamoja na kupata maji kutoka hilo bwawa lililotengenezwa lakini bado kuna migogoro mingi kati yao na SOUWASA. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kwenda Songea ili kukutana na wananchi wa eneo hilo ili kuwasikiliza matatizo yao na kutatua? Naomba kuwasilisha.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali inaipokea hiyo shukurani aliyoitoa, lakini kuhusu wananchi 157 ambao inaonekana wako nje ya wale 872 tutakwenda kufuatilia na ninamuomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge hili nitakwenda Songea, nitakwenda kuona hali halisi na tuweze kuchukua hatua kwa Wananchi wale ambao bado wanadai hiyo fidia.
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali moja la nyongeza kwa vile barabara inayounganisha Tanzania na Msumbiji iliyopo Mkoani Ruvuma, inatokea katika Jimbo la Songea Mjini katika Kijiji cha Likofusi kuelekea Mkenda katika Jimbo la Peramiho, barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Mkoa wa Ruvuma na kwa uchumi wa nchi kwa ujumla. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, ni lini Serikali itafanya utaratibu wa upembuzi yakinifu wa barabara ile na kuijenga kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Likofusi hadi Mkenda ambayo inatuunganisha na wenzetu wa Msumbiji tumeishaifanyia kazi kuanzia siku nyingi. Kwanza tumeishajenga daraja ambalo tayari limekamilika, lakini vilevile wenzetu wa viwanda na biashara wamejenga soko, nalo limekamilika, halafu na sisi vilevile tumefanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii na umekamilika; hivi tunavyoongea tupo katika hatua ya kutafuta fedha kuhakikisha barabara hii inajengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa umuhimu wa barabara hii na hasa tukifahamu kwamba barabara hii inaunganisha Jimbo la Songea Mjini na Jimbo la Peramiho ambalo Mheshimiwa Jenista Mhagama ndiye anayeliongoza, na tunaona jinsi Mheshimiwa Jenista Mhagama anavyotuhangaikia humu ndani kitaifa, Mheshimiwa Waziri wangu alitoa ahadi kwamba atahakikisha barabara hii inatekelezwa kwa maana ya hatua hii ya ujenzi mapema iwezekanavyo, na si zaidi ya miaka miwili kuanzia sasa tutakuwa tumeanza kujenga.
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Songea kwanza naomba nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla pamoja na Serikali kwa kuanza ukarabati katika vituo 89, hivyo, katika vituo 187 tunabakiwa na vituo 98 vya maji ya mtiririko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengi ambayo yana matatizo ya maji, maeneo hayo ni pamoja na Mlete, Lilambo, Chandarua, Mahilo, Ndilima Litembo, Lizaboni, Tanga na Mletele, Subira na Mwenge Mshindo na Making’inda. Nataka nipate uhakika wa Serikali. Je, Serikali inaweza kuwahakikishia wananchi wa Songea ni lini tatizo la maji litakuwa limekwisha kabisa katika Mji wa Songea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili naomba nimuulize Waziri liko tatizo kubwa sana la mamlaka za maji hasa SOWASA, kuwabambikizia wananchi bili za maji za uwongo. Mtu anaweza asitumie maji mwezi mzima lakini akakuta anabambikiziwa bili isiyo na sababu. Je, ni lini Serikali itahakikisha inasimamia kidete kuhakikisha bili zinazokwenda kwa wananchi ni zile zinazotokana na matumizi ya maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Gama kwa jinsi ambavyo anawahangaikia wananchi wake. Wakati tuko Dar es Salaam amekuja zaidi ya mara saba ofisini na ndiye aliyefanya tukafanikisha ukarabati wa hivi visima vifupi 89, nampongeza sana. Hata hivyo, hata wakati anaondoka kwenda kutibiwa aliniachia maagizo kwa ajili ya kushughulikia Mji wake wa Songea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumemaliza awamu ya kwanza ya maendeleo ya sekta ya maji sasa tumeingia awamu ya pili. Tutahakikisha kwamba maeneo yote aliyoyataja vijiji vinavyozunguka Mji wa Songea katika awamu ya pili na katika hii miaka miwili inayofuata ya bajeti tutahakikisha kwamba maeneo yote tumeyapatia maji. Hilo ndiyo lengo la Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba tutakapofika mwaka 2020 basi tuwe tumefikia asilimia kubwa ya wananchi wa vijiji kuwapatia maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la bili, nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na nilizungumze kwa niaba ya Wabunge wote sasa. Ni kweli Mamlaka zetu za Maji Mijini kuna hiyo hali ya kwamba unaletewa bili hata kama maji yalikuwa hayatoki hata Mheshimiwa Rais juzi ameizungumzia hii, lakini hili tumeshaliona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo mawili ambayo tumeyagundua; moja kuna kitu wanaita service charge inakuwa kwamba wewe umekodi ile mita, kwa hiyo kwa maana ya kuikodi walikuwa wameweka utaratibu kwamba hata kama maji hayajatoka kwa sababu umekodi wanakuchaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji juzi baada ya bajeti Wakurugenzi wote walikuwa hapa amewaagiza wakaiangalie hii kwa maana ya kuitoa. Kwa sababu siwezi nikakodi kifaa sipati huduma lakini naendelea kukilipia kwa kuwa nyumbani kwangu. Kwa hiyo, suala hili Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tayari tumeanza kulifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini liko tatizo la pili ambalo nimelifanyia study kupitia Mamlaka ya Maji DAWASCO. Hawa wahudumu wetu system yetu ya kusoma mita unasoma halafu unakwenda kupachi kwenye computer. Unaweza ukakuta unit 15 ukapanchi ukaona 15 baadaye ukarudia tena ile inaji-double ndio maana bili zinakuwa kubwa. Kwa hiyo, hilo nalo tunaliangalia kitaalam ili hiyo double isitokeze, kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge niwahakikishieni kwamba hili suala tumeshaliona, tunalishughulikia na tutalimaliza.