Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Stephen Julius Masele (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. STEPHEN J. MASELE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ya Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ambayo anafanya ya kujenga nidhamu ya nchi yetu na kurejesha nidhamu ya Utumishi wa Umma na nidhamu ya wananchi kutii sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kumpongeza sana Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nimpongeze Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo kwa kazi nzuri ambayo anaifanya ya kusukuma mbele Sekta ya Nishati na Madini nchini.
Mheshimiwa Spika, wote sisi ni mashahidi, Wizara hii ina changamoto nyingi sana kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamezieleza, lakini wizara hii haihitaji malaika wa kwenda kufanya kazi pale. Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo ameonesha ubora na anastahili kupewa support, anastahili kuungwa mkono na Waheshimiwa Wabunge na tutakuwa tumelitendea haki Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimefanya kazi na Mheshimiwa Muhongo, namwelewa, tunapozungumzia moja ya Mawaziri makini nchi hii ni mmojawapo. Waswahili wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Leo Mheshimiwa Rais ameeleza wazi anataka Tanzania iwe nchi ya viwanda, Mheshimiwa Rais ameeleza wazi, anataka asilimia 30 ya ajira za vijana zitokane na viwanda. Sasa Wizara hii na Hotuba ya Mheshimiwa Muhongo ndiyo ambayo itatupeleka kwenye kuwa na Tanzania ya viwanda.
Mheshimiwa Spika, leo Waziri wa Viwanda na Biashara hata aseme ataleta viwanda elfu ngapi, kama hakuna nishati ya umeme ni sawa na kazi bure na Waziri ameonyesha kwa vitendo kwa kutenga asilimia 94 ya bajeti yake kwenye maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na niseme tu kwamba kwenye REA kila mtu anafahamu kazi inayofanywa ni nzuri, lakini changamoto zipo, najua ataendelea kuzitatua. Nimpongeze pia kwa kuteremsha gharama za umeme, Watanzania wengi wanalia gharama za umeme ziko juu na nakumbuka aliahidi kwamba atalifanyia kazi atapunguza gharama za umeme leo ametekeleza.
Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwenye viwanda nchini moja ya changamoto kubwa ambayo wanahangaika nayo ni bill zisizoeleweka ambazo wanapelekewa na TANESCO kwenye maeneo husika. Ziko charge nyingi ambazo viwanda vinapelekewa ambazo zinakatisha tamaa uwekezaji wa viwanda vilivyopo na hata hivyo vinavyokuja. Nina hakika kama bili hizi zitaendelea kuwa hivyo, basi kutakuwa na changamoto kubwa ya bidhaa zinazozalishwa nchini kushindana na bidhaa za masoko za kutoka nchi za jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aliahidi kwa Watanzania kwamba atafanya mahesabu na atahakikisha hata nguzo za umeme itafika mahali atatutangazia atazigawa bure, tunasubiri ahadi hiyo na nina uhakika anaweza.
Mheshimiwa Spika, leo Tanzania, Mheshimiwa ameeleza kwenye hotuba yake, inazalisha megawati 1,400. Ili tuweze kuwa nchi kweli ya kipato cha kati, ili tuweze kuwa Taifa la Viwanda ni lazima tuongeze speed ya uzalishaji wa umeme. Speed ya uzalishaji wa umeme ni kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji hasa kupitia gesi asilia. Leo Tanzania tunazalisha gesi yetu wenyewe na Mungu ametusaidia, tusingekuwa na hii gesi na tusingekuwa na uimara wa Mheshimiwa Profesa Muhongo kusimamia bomba la gesi likamilike kwa kutegemea mvua haya malengo yote tusingeweza kuyafikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie, Taifa la Uturuki leo linaongoza kwa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kwenye soko la Ulaya, ni kwa sababu wana umeme wa kutosha na hata hiyo gesi yenyewe hawana, wanaagiza kutoka kwenye Mataifa yenye gesi. Uturuki peke yake inazalisha megawatt 60,000 za umeme. Afrika Kusini inazalisha megawati 80,000 za umeme. Unapokwenda kule kama Waziri unamwambia mwekezaji kama Toyota njoo uwekeze kiwanda cha ku-assemble magari Tanzania atakuomba megawati 5,000 peke yake, huna, safari yako haina maana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Bunge hili litatenda haki kwa Watanzania endapo tutafikiri kimkakati namna gani Tanzania itazalisha umeme wa kutosha ili kuweza kukidhi mahitaji ya majumbani lakini pia tuweze kukidhi maendeleo ya viwanda tunayoyazungumza.
Mheshimiwa Spika, umeme tulionao huu vikiunganishwa migodi mitano tu Tanzania tutaingia kwenye mgao. Leo iko migodi hapa inazalisha yenyewe umeme. Tukiunganisha viwanda vikubwa tutaingia kwenye mgao. Kwa hiyo, bado tuna kazi ya kufanya, bado tuna kazi ya kumpa ushirikiano Waziri kwa jitihada ambazo amezionyesha kwenye bajeti hii ili tuweze kufikia hayo malengo tunayoyataka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa leo Tanzania tunazalisha kupitia TANESCO, malengo yetu kama nilivyosikia kwenye hotuba tunatakiwa tuwe na megawatt 2,500, tunatakiwa tuwe na megawatt 10,000 ifikapo 2025. Tutafikishaje megawatt 10,000 kama hatuvutii uwekezaji binafsi kuja kuwekeza katika Sekta ya Umeme? Serikali peke yake kuzalisha megawatt 100 za umeme ni zaidi ya Dola za Marekani milioni mia moja na! Tukitaka megawatt 10,000 leo tunahitaji zaidi ya dola bilioni 10 za Marekani labda ni bajeti yetu hii ya miaka 10 ijayo tusifanye jambo lingine lolote. Kwa hiyo, lazima Serikali tuwe na mikakati ya kuhakikisha kwamba tunawekeza katika umeme sawa, lakini tuvutie pia sekta binafsi kuwekeza katika miradi hii.
Mheshimiwa Spika, nizungumzie kwenye Sekta ya Madini, zipo jitihada kubwa Wizara inafanya, niwapongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuendeleza jitihada za kuwainua wachimbaji wadogo Tanzania, nimpongeze Naibu Waziri kwa kazi kubwa ya kusuluhisha migogoro ya Nyamongo, lakini bado ziko changamoto ambazo tunatakiwa kuzishughulikia na bado katika uwekezaji mkubwa pia tunahitaji kuwa na migodi mipya.
Mheshimiwa Spika, tulipitisha miaka miwili iliyopita hapa sheria inayotoza kodi kwenye vifaa vya utafiti. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri ni mjiolojia bingwa duniani, tunapoweka sheria hizi za fedha za kutoza kodi kwenye vifaa vya utafiti ni sawasawa unasema tunataka kilimo cha kisasa halafu tunakwenda kuweka kodi kwenye matrekta, tunakwenda kuweka kodi kwenye mbegu.
Mheshimiwa Spika, kwenye uzalishaji wa migodi mipya haiwezi kutokea migodi mipya Tanzania endapo utafiti utakufa, endapo makampuni yanayofanya utafiti yatapunguza bajeti ya kufanya utafiti. Mheshimiwa Waziri naomba hili alifanyie kazi tupitie upya hizi sheria hasa kwenye eneo hili la utafiti ili kuweka unafuu wa utafiti na hatimaye nchi yetu iweze kupata viwanda vipya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuiwezesha Tanzania kupata mradi mkubwa wa kujenga bomba la mafuta kutoka Uganda. Nafahamu jitihada zako, nafahamu jitihada za Serikali. Miradi hii itasaidia sana kukuza uchumi wa Taifa letu. Nimwombe aendelee na jitihada, natambua Uganda imetuomba Tanzania tupeleke bomba la gesi, natambua Kenya tume-sign makubaliano nao ya kuwauzia megawatt 1,000. Leo wapo Watanzania wanajiuliza kwa nini shilingi haina nguvu? Wachumi wanasema unapoingiza zaidi kuliko kupeleka nje zaidi maana yake unadhoofisha shilingi yetu. Tukiweza kuuza megawatt 1,000 za umeme Kenya tutaingiza mapato ya kigeni mengi ambayo yatasaidia hata kuimarisha shilingi yetu.
Mheshimiwa Spika, miaka mingi tangu uhuru tumetegemea mazao ya mashambani; pamba, tumbaku, madini kidogo bei imeshuka, uzalishaji umeshuka; lakini tuna bidhaa, tuna zao jipya la gesi ambayo tunaweza tukazalisha megawati 1,000 ambazo Kenya wanazihitaji na tuka- export megawatt 1,000 tukapata mapato mengi ya kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. STEPHEN J. MASELE: Mheshimwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja hii ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri ambayo imetoa dira ya nchi yetu inakoelekea hasa kwenye siasa za Kimataifa na diplomasia ya uchumi. Nitumie nafasi hii kumpongeza Naibu Waiziri Mheshimiwa Dkt. Susan Kolimba, Katibu Mkuu Dkt. Aziz na watumishi wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya ya kuitangaza nchi yetu na kuvutia uwekezaji katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ina historia na ina historia kubwa hasa kwenye siasa za kimataifa. Tangu tupate uhuru chini ya uongozi wa Baba wa Taifa alijenga misingi imara ya kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa na sauti kwenye ukanda wa Kusini mwa Afrika na hasa kwenye masuala ya ukombozi wa Bara letu la Afirika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, misingi ile ilijengwa na msingi imara na unatakiwa kuendelezwa kwa kukifanya Tanzania kuwa nchi yenye sauti kubwa na ushawishi wa kisiasa na kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na Kusini mwa Bara la Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kupongeza uongozi mzima wa Wizara pamoja na Serikali kwa kushiriki kikamilifu kusuluhisha mgogoro wa Kongo (DRC). Wote hapa tunafahamu umuhimu wa Kongo (DRC), mahusiano yetu ya kindugu, ya kijamii na kiuchumi. Kwa hiyo, uhusiano na ushiriki wa Tanzania kuhakikisha kwamba nchi ya Kongo inapata amani ya kudumu ni jambo la kipaumbele kwa Tanzania na kwa Serikali yetu. Lakini hivyo hivyo niipongeze Serikali kwa kuhakisha kwamba Burundi inaendelea kuwa salama na Baba wa Taifa alieleza kabisa kwamba huwezi kuwa salama kama majirani zako wote hawako salama, na wote tunatambua umuhimu wa kiuchumi wa nchi hizi zinazotuzunguka kwa maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitajikita zaidi kwenye diplomasia ya uchumi ambayo mwelekeo wa Wizara na Serikali kwa sasa imeweka mkazo mkubwa kwenye diplomasia ya kiuchumi.
Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba zako zinazofuata ni vyema ukaja na takwimu uoneshe Watanzania mipango na safari na mikutano ya nje ambayo nchi yetu inashiriki imeleta faida gani kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa taarifa na Ripoti ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa Tanzania kwa mwaka 2014 imeongoza kwa kuwa ni Taifa la kwanza kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuingiza mapato mengi ya uwekezaji wa fedha za kigeni kwa maana ya Foreign Direct Investments. Leo kwa ripoti ile Tanzania iliingiza zaidi ya dola za Marekani bilioni 2.14 ukilinganisha na Taifa ambalo lina uchumi mkubwa kwenye ukanda wetu la Kenya ambalo liliingiza dola milioni 900. Uganda ilifuatiwa ya pili nyuma ya Tanzania kwa kuingiza zaidi ya dola bilioni 1.1. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mafanikio Mheshimiwa Waziri, kwa sababu haya ndio majukumu ya Wizara yako kwa shughuli zote zinazohusiana na uchumi wa Taifa hili na hasa uwekezaji kutoka nje na ukitazama katika uwekezaji huu unaona kabisa ni Sekta ya Gesi, Sekta ya Madini kwa Tanzania ndio imeongeza kwa kuingiza mapato mengi ya uwekezaji baada ya kugundua gesi asilia, Taifa letu limeingiza mapato mengi ya kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ni vyema sasa kuangalia ushiriki wetu kwenye majukwaa mbalimbali ya kiuchumi kwa mfano tunaposhiriki kwenye Jukwaa la Kiuchumi la TICAD kwa mahusiano ya Japani na Afrika ama India na Afrika, ama Marekani na Afrika, na block zingine za kiuchumi kwa mfano block ya BRICS lazima tuoneshe kwa takwimu tunapata faida gani. Taifa linapata mapato kiasi gani kutoka nje kwa maana ya uwekezaji unaotoka nje. Hiyo itaweza kuonesha uhalali wa safari ambazo tunakuombeeni fedha mnazokwenda nje na huwezi kuwa mwana diplomasia ambaye unaishia kwenda Shinyanga badala ya kwenda nje kutafuta uwekezaji kwa faida ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima niseme kwamba ukitazama kama nilivyoeleza awali, Sekta ya Nishati kwa maana ya utafiti na gunduzi za gesi na madini ndio zimeongeza mapato mengi ya kigeni hasa katika uwekezaji. Je, Wizara inajipangaje sasa kuhakikisha kwamba sekta zingine kama Sekta ya Kilimo na Viwanda inafanya vizuri kuwekeza, kuingiza fedha nyingi za kigeni.
Ukitazama kama Ethiopia imefanikwa sana kwenye viwanda hasa kwenye maeneo ya kilimo, imefanikiwa sana kuvutia uwekezaji kwenye kilimo na viwanda ambayo imechangia mapato makubwa ya Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kama Afrika Kusini ambayo ndio inaongoza kwa Afrika kwa zaidi ya dola bilioni 145 za uwekezaji ambazo imepokea, imewekeza zaidi kwenye Sekta ya Viwanda, Biashara pamoja na Madini. Sasa Sekta zingine zinasubiri nini! Je, wizara yako inawezaje kusaidia kutafuta wawekezaji zaidi wa kuongeza mapato na uwekezaji katika sekata za Kilimo, biashara pamoja na viwanda katika nchi yetu.
Mheshimiwa Rais amesema anataka Tanzania iwekeze zaidi kwenye viwanda. Je, Wizara yako inafanya nini na hawa wawekezaji wanaokuja kuwekeza hapa baada ya kuwekeza je, Wizara yako inafuatilia kuona wanaendeleaje? Maana wawekezaji wengine wanakuja kwenye sekta hizi mbalimbali lakini wanaishia kuchanganyikiwa, wanaishia kuwa frustrated na mazingira mengine ya uwekezaji. Je, Wizara hii inafuatilia kujua wanaendeleaje? Na kama kuna changamoto ambazo zinawakabili mnafanya nini kuhakikisha kwamba mnashirikiana na sekta zingine kuhakikisha changamoto hizi mnazitatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa kwamba Taifa lolote duniani haliwezi kuendelea bila uwekezaji, hasa uwekezaji wa fedha zinazotoka nje. Marekani yenyewe inashika nafasi ya tatu kwa kupokea fedha nyingi za uwekezaji kutoka mataifa mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, China imeendelea kwa sababu imepokea fedha nyingi za uwekezaji kutoka mataifa mengine, na kutoka ndani ya China wenyewe. Lakini Tanzania tunapovutia wawekezaji lakini tunatumia muda mwingine kuwa-frustrate wawekezaji na kuona kama ni maadui ama wezi wa mali za asili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wetu kuwa na sheria nzuri, ni wajibu wetu kusimamia vizuri rasilimali zetu, lakini taifa hili linahitaji kuendelea, Taifa hili linahitaji kuwa Taifa la uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Hatuwezi kuwa na uchumi wa kati mwaka 2025 kama dira ya Taifa ya uchumi ya maendeleo inavyoelekeza kama hatutoweza kuvutia uwekezaji kutoka nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri, badala ya kufanya siasa, badala ya maelezo mengi, next time uje na data, uje na figures uoneshe faida, ya kushiriki kwenye mikutano hii yote, Taifa linapata nini. Uoneshe fedha tunazozipokea kutoka Asia, Marekani, Uingereza katika uwekezaji, wala sio fedha za misaada, nazungumzia fedha za uwekezaji ambazo zinaongeza mzunguko wa uchumi katika Taifa letu. Leo katika mradi wa bombo la gesi tu, tulipokea zaidi ya dola bilioni 1.2, dola bilioni 1.2 imetumika hapa Tanzania, na makampuni ya kitanzania yamepata fedha, na mzunguko wa fedha umemfikia kila mwananchi wa Tanzania.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja, na nampongeza Waziri na Wizara yake. Yeye ni mzoefu nina uhakika kwamba atalisaidia Taifa hili, kuhakikisha heshima ya Tanzania, kwenye nyanja za kimataifa inaendelea kuwepo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. STEPHEN J. MASELE: Mheshimiwa Spika, ahsante
kwa kunipa nafasi pia ya kuchangia bajeti hii ya Mheshimiwa
Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, nami nianze kwa kumpongeza
sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake ambayo
inatoa dira ya mipango ya maendeleo ya Serikali. Nitumie
nafasi hii pia kuwapongeza Mawaziri, Mheshimiwa Jenista
Mhagama, kwa kazi nzuri na anaonesha kweli akinamama
wanaweza. Nimpongeze pia Naibu Waziri kijana, Mheshimiwa
Anthony Mavunde kwanza kwa kazi kubwa ambayo
anaifanya ya kuwaunganisha vijana wa Tanzania lakini pia
kwa programu ile ya mafunzo ya vijana ambayo anaifanya.
Nimwombe tu programu hiyo pia ifike Shinyanga kwa sababu
kuna vijana wengi wanahitaji programu kama hiyo na
kusema kweli kama vijana wenzako hujatuangusha.
Mheshimiwa Spika, kipekee sana kwa niaba ya
wananchi wa Shinyanga nataka nimshukuru sana
Mheshimiwa Rais. Alipofanya ziara Shinyanga alitoa
maelekezo kwa Mamlaka na Wizara ya Maji kushughulikia
tatizo la bei ya maji Shinyanga. Kama Mheshimiwa Shabiby
alivyosema, leo nazungumzia kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu
kwa sababu bado hatujaona jitihada za Waziri wa Maji
kushughulikia tatizo la uendeshaji wa Mamlaka ya Maji
Shinyanga.
Mheshimiwa Spika, maji ni huduma ya msingi, maji
sio anasa. Shinyanga na mikoa ya Kanda ya Ziwa ni mikoa
michache ambayo ina chanzo cha maji cha uhakika cha
Ziwa Victoria. Serikali imetumia shilingi bilioni 250 kujenga
Mradi wa Maji wa Ihelele, kodi za Watanzania, leo Wizara
haiweki msisitizo wa kutunza mitambo ile. Shilingi bilioni 250
hazijamaliza hata miaka 10, Serikali haipeleki pesa za kutunza
mitambo ile. Ni asilimia 25 tu ya mitambo ile ndiyo inafanya
kazi, asilimia 75 haifanyi kazi. Ipo mikoa mingine kama Arusha
wanahangaika vyanzo vya maji, Gairo huku amezungumza
Mheshimiwa Shabiby wanahangaika na vyanzo vya maji,
lakini sisi tuna chanzo cha maji cha uhakika lakini hatukitunzi,
tumeweka shilingi bilioni 250 hatutunzi.
Mheshimiwa Spika, wiki iliyopita Shinyanga, Kahama,
Ngudu, Igunga ambayo yote yapo kwenye Mradi huu wa
Ihelele yanatakiwa yapelekewe maji lakini hayajapelekwa.
Mradi ule umekatiwa umeme, siku nne wakazi wa Shinyanga
hawana maji kwa sababu Serikali haijapeleka mchango
wake wa asilimia 60 wa kuendesha mradi ule. Sasa wananchi
wanapata adhabu ambapo wamelipia bili zao za maji
wanastahili wapate huduma wanaikosa huduma kwa
uzembe wa watu wengine, hii inasikitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mradi ule hauwezi kuharibika
kwa uzembe wa watu wachache. Nimwombe Waziri,
namheshimu, ni rafiki yangu, akae na Wabunge wa Kanda
ya Ziwa ambao wanahusika na ule mradi wa maji tushauri
namna bora ya uendeshaji wa mradi ule. Mradi ule ukiweza
kuwafikia watumiaji wengi, kwa mfano wa Ngudu, Kwimba, Igunga, Nzega, Tabora, Sikonge na kwa capacity ya mradi
ule unaweza kuleta maji mpaka Mkoa wa Dodoma. Pampu
zile nane zikifunguliwa zote Dodoma inaweza kupata maji
ya Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, andiko la mradi ule linaweza
kuhudumia watu milioni 10. Leo ni wakazi wa Manispaa ya
Shinyanga ambao hawafiki 200,000 na wakazi wa Mji Mdogo
wa Kahama ambao hawafiki 200,000 ndiyo wanahudumia
gharama za uendeshaji za mradi wa shilingi bilioni 250.
Naomba Serikali iangalie kwa upana mradi huu. Naomba
pia Serikali iongeze bidii za kusambaza haya maji kwenye
vijiji vile vinavyohusika, zile kilometa tano vijiji vile vipate maji.
Mheshimiwa Spika, lakini yapo mambo ambayo
tunaweza kumshauri Waziri, kwa mfano, mamlaka hizo zote
mfano SHUWASA na mamlaka nyingine, kwenye vifaa vya
mabomba kwa mfano vya kuunganisha maji, vimewekewa
kodi, kuna SDL iko pale, kuna VAT iko pale. Vitu kama hivi
vikiondolewa kwa sababu maji ni huduma, gharama za
uendeshaji wa mamlaka hizi zitakuwa chini na hatimaye
wananchi watapata huduma ya maji kwa gharama nafuu.
(Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia madeni hayalipwi. Sasa
taasisi muhimu kama Mamlaka za Maji zinakatiwa huduma,
nilikuwa naangalia television, Kigoma pale wananchi
wanagombania maji kwa sababu mamlaka imekatiwa maji.
Shinyanga pale tumekatiwa maji siku nne, tuna viwanda pale
vya maji, kuna viwanda vya soda, wananchi wanakosa maji
eti kwa sababu bili ya KASHUWASA haijalipwa na huyo
KASHUWASA hiyo pesa anayotakiwa atoe inatakiwa itolewe
upande wa Serikali. Sasa sisi wananchi tumelipa bili tunataka
huduma tu. Tunapata adhabu kwa sababu ya watu wengine.
Hospitali haina maji, imagine hospitali ya mkoa inayopokea
wagonjwa zaidi ya 200 inakatiwa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimezungumza hili kwenye
hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu kule
nyumbani wananchi wamenituma wamesema tunataka nizungumzie suala la maji. Naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu
suala hili ulisimamie kwa karibu kwa sababu pale tumeweka
pesa nyingi za walipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Shinyanga
imejengewa mtandao wa maji safi lakini hakuna mtandao
wa majitaka, majitaka yote yanayonyonywa hakuna pa
kuyapeleka. Naomba Serikali itenge fedha kwenye bajeti
hasa ya Waziri wa Maji, tujenge mtandao wa maji taka kwa
sababu ulikuwepo kwenye andiko la mradi huu kwamba
lazima na mitandao ya majitaka pia ijengwe. Leo majitaka
pale Shinyanga hakuna pa kuyapeleka, mbaya zaidi hata
vifaa vinavyokuja vyote ikiwemo na mita zinakuja mita feki,
bili za wananchi zinachakachuliwa, wananchi wanapigwa
bili kubwa kwa mita feki zinazokuja.
Mheshimiwa Spika, naomba Waziri asimamie hizi
mamlaka kwa karibu, aangalie hata hizo mita zinazoagizwa,
huyo mtu aliyepewa tenda ya kuagiza mita ziwe zina ubora
unaostahili sio kuwaibia wananchi kwa kuleta mita ambazo
ni feki, zinaongeza gharama za uendeshaji, zinaongeza bili
ya maji kwa wananchi. Wananchi wangu bado hawana
uwezo mkubwa wa kubeba mzigo wa gharama za
kuhudumia maji ambayo kimsingi Serikali ilitakiwa isaidie
ruzuku ili kuweza kuhakikisha mradi huu unawafikia watumiaji
wengi.
Mheshimiwa Spika, tukiongeza foot print ya mradi huu
gharama zile tutagawana wote, maji yale yafike mpaka
Tabora, Sikonge, Ngudu, Sumve, Igunga, Singida na Malya,
wote wapate yale maji ili tuweze kugawana gharama za
uendeshaji. Tusipofanya hivyo tutaendelea kubeba msalaba
huu sisi peke yetu na mradi ule utakufa kwa sababu hatuna
uwezo wa kuuhudumia.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.