Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Elias John Kwandikwa (15 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti,naipongeza Serikali kuja na Mpango wa Pili mzuri wa Maendeleo, ambao utagusa maeneo mengi, ikiwemo Ilani ya uchaguzi tulioinadi mwaka jana 2015. Pia napongeza Hotuba ya Waziri Mkuu ambayo inaonesha commitment ya Serikali kwa wananchi wake. Hatua hii na hatua nyingine mbalimbali ambazo Serikali imeendelea kuchukua, imesaidia kuwapa Watanzania mtazamo mpya wa kufanya mabadiliko kuanzia kwenye ngazi ya familia.
Mheshimiwa Mwenyekiti,rasilimali watu, naomba na kuishauri Serikali iangalie kuboresha maslahi ya watumishi ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuchangia ukuaji wa uchumi. Na-declare interest mimi ni mhasibu, mkulima na mfanyabiashara pia.
Naishauri Serikali iwatazame kwa jicho kuu watumishi wa Idara ya Takwimu, kwani ikiboreshewa vifaa na huduma wataisaidia Serikali kupata taarifa muhimu zinazohusu hali ya uchumi, changamoto, pamoja na namna ya ufafanuzi wa changamoto kwa wakati. Pia kada ya uhasibu itazamwe, itumike kuisaidia Serikali, kada hii inatumika zaidi kwa sasa kuandaa taarifa tu na hawatumiki kwenye maamuzi, kwani hawaonekani kama viongozi kwenye idara na agency za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti,huduma za jamii katika Jimbo la Ushetu; maeneo ya Majimbo, Halmashauri za Wilaya zilizopo nje ya Makao Makuu ya Wilaya zimesahaulika na Serikali kuendelea kuamini huduma zikifika Makao Makuu ya Wilaya mwonekano unakuwa huduma imewafikia wananchi wengi, hivyo naomba yafuatayo Ofisi ya Waziri Mkuu iyazingatie:-
(a) Kwanza, afya, tunahitaji tupatiwe hospitali ya Wilaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, katika Kituo cha Afya cha Mbika, Kata ya Ushetu. Kituo hiki hivi sasa kinahudumia Jimbo la Ushetu na Majimbo jirani ya Ulyankulu na Urambo. Hospitali ya Wilaya ya Kahama pekee imezidiwa kwani inahudumia Wilaya za Mbogwe, Bukombe, yaani wagonjwa wa nje na ndani ni 600 kwa siku.
(b) Huduma ya utawala; tunaomba kupewa Wilaya ya Ushetu ili usimamizi na uratibu wa shughuli za huduma na maendeleo zisimamiwe vizuri. Tuliahidiwa kupewa Wilaya baada ya kupewa Halmashauri ya Wilaya na Jimbo, jambo ambalo limekamilika (rejea hotuba wa Waziri Mkuu ya 2010/2011).
(c) Ujenzi wa barabara kutoka Mpanda- Ulyankulu- Ushetu - Kahama kwa kiwango cha lami; kama ilivyo kwenye Mpango wa Maendeleo na Ilani ya Uchaguzi, barabara hii itajengwa. Hata hivyo, inaonesha usimamizi wa barabara hii itakayohusu mikoa mitatu, yaani Katavi, Tabora na Shinyanga, inaonesha usimamizi unasimamiwa na Meneja TANROAD Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti,nashauri ifuatavyo:-
(i) Usimamizi ufanywe na mameneja wote, kila mmoja eneo la mkoa wake na kuwe na project tatu ili usimamizi na uwajibikaji upimwe kimkoa.
(ii) Ujenzi uanze kwenye kila Mkoa husika ili huduma kwa wananchi iende kwa uwiano.
(d) Ushirika; suala la ushirika litazamwe, tuwe na ushirika kwenye sekta zote, wafugaji hawana ushirika madhubuti, hivyo wasaidiwe kikamilifu.
(e) Maji; maji yaliyotoka Ziwa Victoria yamefikishwa Wilayani Kahama, kwa nini yasisambazwe kwa wananchi wa Jimbo la Ushetu.
Mwisho, naunga mkono hoja. Taarifa yangu iingizwe kwenye Kumbukumbu Rasmi za Bunge.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shida kubwa sana ya malisho ya mifugo yetu Jimbo la Ushetu kwenye Kata za Ulowa, Ubagwe, Ulewe, Nyankende na Idahina na Mheshimiwa Waziri atakumbuka tumepewa muda wa ukomo 15 Juni, 2016 tuwe na eneo mahsusi la malisho kutokana na kauli ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili ya tarehe 2 Aprili, 2016. Nimesoma hotuba na jedwali Na.12 sijaona kuwa tumetengewa maeneo ya malisho. Naomba ufafanuzi hali ni mbaya na tuna eneo la misitu ya Usumbwa na pori la Ushetu – Ubagwe ambalo linaweza kutuondolea adha na mgogoro wa wafugaji na wakulima wa Jimbo la Ushetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya yana ukubwa ufuatao, Usumbwa kilomita 360 na Ushetu – Ubagwe kilomita 310. Idadi ya ng‟ombe peke yake Jimbo la Ushetu inakadiriwa kuwa zaidi ya 300,000. Hivyo, naomba ulitolee commitment jambo hili na itapendeza pia ukitoa kauli juu ya maeneo yote yanayozunguka hifadhi ya Kigosi – Muyowosi. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara hii kupigania ongezeko la bajeti, pia irekebishe sura yake ya bajeti. Haya ni maoni yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti yetu bado ni ndogo sana, shilingi trilioni 1.4; ni vema tufuate azimio la Abuja (E.F.A Goals). Bajeti ya Elimu ifike ifike 6% ya Tanzania GDP. Mfano, bajeti ya mwaka 2014, GDP ilikuwa inakadiriwa kuwa trilioni 100+, hivyo bajeti ya elimu ingekuwa shilingi trilioni 6.055.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Bajeti ya Elimu kwa matumizi ya kawaida, kujumuisha mikopo ya wanafunzi, nashauri siyo vema bajeti ya maendeleo kujumuisha mikopo ya wanafunzi; hii ina-mislead budget structure ya Wizara. Mbona ununuzi wa magari inawekwa kwenye matumizi ya kawaida?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Idara Ukaguzi wa Elimu itengewe bajeti ya kutosha na iongezewe rasilimali za kutosha ikiwemo rasilimali watu. Kwa sasa mawanda ya ukaguzi ni madogo, yaani asilimia 20 tu. Ni vema ukaguzi uweze kufikia angalau asilimia 30, itasaidia kugundua mapungufu na kufanya marekebisho mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara hii ifanyie kazi tafiti zilizofanyika pamoja na ripoti za CAG hususan maeneo ya value for money, audit (VFM Audit). Mfano, wanafunzi kutofanya vizuri masomo ya hisabati, viwango vya ufaulu kwa watoto wa kike na kadhalika, Wizara ifuatilie maoni hayo ili tufanye vizuri na kuinua viwango vya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie kuanzisha Shule za High School katika Jimbo la Ushetu hususan Shule za Bulungwa Secondary School (Kata ya Bulungwa) na Mweli Secondary School (Kata ya Ushetu). Mimi Mbunge na wananchi tutahamasishana kuongeza madarasa na mabweni, naomba Wizara mtuunge mkono. Naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuunga mkono hoja. Naomba Serikali itengeneze mnyororo wa huduma na kuhudumiana (chain supply) ili uzalishaji wa viwanda vyetu ulenge kwanza kuhudumia mahitaji ya ndani (soko la ndani). Yapo mahusiano kati ya viwanda, masoko na ubora wa miundombinu ya umeme, maji, barabara, mawasiliano na uzalishaji wenye tija. Hivyo namwomba Mheshimiwa Waziri awasiliane kwa karibu na Wizara nyingine ili kuwe na matokeo chanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri elimu itolewe ili wananchi na wataalamu, viongozi waliopo vijijini waelewe viwanda vinaanza na viwanda vyenye kuajiri watu 1, 2, 3, 4 - 9 hadi viwanda vikubwa. Wananchi hawaelewi kama shughuli wanazofanya kama usindikaji wa vyakula ni viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utunzaji wa data, naishauri Wizara iwe na utaratibu wa kuweka kumbukumbu (data) ili kuweza kuchambua maendeleo ya uendeshaji viwanda na matokeo yake kama vile idadi ya walioajiriwa Kiwilaya hadi Kivijiji. Hii itasaidia kufanya maboresho ya mara kwa mara. We need to have proper and useful information.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nashauri utafiti ufanyike mara kwa mara ili Wizara iweze kutoa ushauri, maagizo na maelezo ya namna Sera ya Uchumi wa Viwanda uweze kutekelezeka. Utafiti ufanyike pia ili tujue changamoto za uendeshaji wa viwanda na utatuzi wa changamoto kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la ufafanuzi kwa Waziri: Je, Mheshimiwa Waziri, Wizara ina mpango gani wa kuhimiza ushirika na wenye viwanda hususan viwanda vidogo vidogo ili iwe rahisi kuwafundisha kupima maendeleo yao na kuona kwa kiasi gani viwanda vimepunguza hali ya umasikini na kuongeza ajira?
Je, Mheshimiwa Waziri ana mpango gani kuhimiza mafunzo ya uendeshaji viwanda kwa ufanisi hususan Jimboni Ushetu?
Je, tutawatumiaje vijana waliohitimu mafunzo ambao hawana ajira kushiriki na kutumika katika ukuzaji wa viwanda?
Je, Sekta ya Viwanda inapunguza kwa kiasi gani mfumuko wa bei kwa kusogeza huduma ya masoko karibu na wananchi?
Je, hadi sasa kuna changamoto zipi za kiteknolojia kifedha, kisera na kiutawala ambazo bado hazijatatuliwa na zinazokwamisha maendeleo ya haraka katika viwanda vyetu na kwa namna gani changamoto hizi zitatatuliwa?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia makadirio ya Ofisi ya TAMISEMI na Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu, nitumie nafasi hii nimshukuru sana Mungu ameniwezesha kuingia kwenye nyumba hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nikupongeze sana wewe mwenyewe kuchaguliwa kuwa kiongozi wetu. Niseme najivunia kuwa Mbunge wa Jimbo la Ushetu na najivunia pia kuwa na Madiwani wote wa Chama cha Mapinduzi. Nilikuwa napata shida kidogo na maswali, watu wengine hawajui Jimbo la Ushetu liko wapi, Jimbo la Ushetu limetokana na lile Jimbo la Kahama. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya. Mheshimiwa Rais ametupa Baraza zuri la Mawaziri, Mawaziri ambao wanatusikiliza na naamini kwamba watafanya kazi vizuri kwa maendeleo ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Chama cha Mapinduzi kimetupa ilani nzuri sana. Niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge ambao labda hawajaipitia vizuri waisome, ni msingi mzuri wa kwenda kwenye maendeleo na kasi ambayo tunaihitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sikupata nafasi ya kuchangia kwenye Mpango wa Pili wa Maendeleo lakini nitumie nafasi hii niseme kwa ufupi kabisa kwamba nilisoma Mpango wa Maendeleo umezingatia sana Ilani ya Chama cha Mapinduzi lakini pia umeangalia sana kwenye ule MKUKUTA. Kwa hiyo, niipongeze sana Serikali kwa kutazama kwa umakini na uhakika Mpango huu kwa madhumuni ya kuwaletea maendeleo wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze kwa ujumla juu ya Halmashauri zetu. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri Simbachawene kwa kazi ambayo anaifanya. Nina uhakika kwenye mpango huu aliouleta utakapokwenda kufanyika kuna mambo mengi ambayo tutakwenda kufaidika nayo sisi wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kwanza suala la kuzisaidia Halmashauri zetu kuhusu watumishi. Rasilimali watu ni muhimu sana kwa sababu ndio rasilimali ambayo itakwenda kusimamia rasilimali zingine, itakwenda kusimamia rasilimali fedha na mambo mengine ya kiutekelezaji. Kwa sababu ukija kuangalia, TAMISEMI ndiyo Wizara ambayo inakwenda kusimamia mambo mengi ambayo pia yatakuwa yameonekana kwenye Wizara zingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka nishauri tu kwamba, Serikali itazame eneo hili la watumishi pamoja na namna ambavyo inachukua hatua mbalimbali za kuweza kuhakikisha kwamba watumishi wa umma wanakuwa na nidhamu lakini lazima tupeleke msukumo mkubwa kuhakikisha kwamba tunawapa weledi wa kutosha watumishi wetu, tunakuwa na idadi ya kutosha lakini pia tuangalie kama tunaweza kuwapa motisha ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi ili kuendana na kasi hii ya Rais wetu ya kuchapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nizungumzie juu ya mapato, uko umuhimu wa kutazama sana katika hizi Halmashauri zetu. Nilikuwa nikiangalia kwenye majedwali ya namna ambavyo fedha zimekuwa zikienda kwenye Halmashauri zetu lakini pia nimeangalia na ongezeko la makusanyo, ningependa nimshauri Mheshimiwa Waziri tuweze kuongeza ruzuku kwenye Halmashauri zetu. Kwa sababu ukisoma kwenye mtiririko wa fedha inaonekana kwamba ruzuku zimekuwa zikishuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwa hesabu kuanzia za mwaka 2013/2014, Halmashauri zimekuwa zimetengewa shilingi bilioni 704, mwaka uliofuata 2014/2015 zilitengewa shilingi bilioni 563 na mwaka wa fedha uliofuata Mkuu ya mwaka wa fedha 2011/2012, kati ya wilaya ambazo zilikuwa zimekuwa proposed kuanzishwa ni Wilaya ya Ushetu lakini haikuanzishwa kwa sababu hatukuwa na halmashauri. Sasa tunayo halmashauri ambayo ilianzishwa mwaka 2012 na sasa tunalo jimbo na ili tuendane na maendeleo ambayo tunahitaji, tunahitaji kwa kweli tupate wilaya. Yako mambo mengi ambayo yanatupita kutokana na ile dhana tunapokuwa tunayapeleka maendeleo tunayapeleka kwenye Makao Makuu ya Wilaya tunasahau kwenda kwenye halmashauri ambazo haziko kwenye Makao Makuu ya Wilaya ambako ndipo watu wengi walipo. kwa hiyo, nafikiri hili linaweza kuwa ni changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mtizamo uwe kuangalia huduma zinaenda kwa wananchi walio wengi ambao wako nje ya makao Makuu ya Wilaya. Kwa hiyo, napenda niombe sana Mheshimiwa Waziri aliangalie hili kwa sababu ni muda mrefu tumechelewa kupewa Wilaya kwa sababu ya kutokuwa na Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengine ya huduma ambayo kwa sehemu kubwa kama nilivyozungumza Serikali zetu za Mitaa ndiyo zinasimamia pamoja na kuwa yanasimamiwa na Wizara zinahusika lakini ile manpower kubwa iko katika halmashauri zetu. Nikianza na eneo la afya tupate fedha za kujenga Hospitali ya Wilaya ya Ushetu.
Mheshimiwa Naibu, ahsante, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Ushetu halikubahatika kujengewa miundombinu ya umeme. Tumepata vijiji viwili tu. Tunao uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na misitu na tunahitaji kuchakata mazao yetu ili tuinue uchumi wa wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumehamia Makao Mapya ya Halmashari ya Ushetu ambayo yako katika Kata ya Nyamilangano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu Mheshimiwa Waziri, tupelekewe umeme kwa haraka Makao Makuu ya Halmashauri yetu ya Ushetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tujengewe miundombinu ya umeme kwenye vijiji vyote REA II ili tuweze kuchangia katika kukuza viwanda na uchumi wa nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, Mheshimiwa Waziri nakushukuru kwa ushirikiano wako na nia yako thabiti kutusaidia wana Ushetu. Naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Spika, kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia Hotuba ya Waziri wa Fedha. Hotuba ambayo ni muhimu sana; na nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuipongeza Wizara na Watendaji wote, na wote waliohusika kutuandalia kwanza Mpango ule wa Maendeleo kama tulivyousikia; lakini pia hotuba hii nzuri. Niipongeze kwa dhati kwa sababu ukiangalia bajeti hii utaona imezingatia mambo muhimu sana, imezingatia pia mwelekeo ambao tunautarajia. Ukiisoma bajeti hii utaona yako maeneo muhimu sana. Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, imezingatia maboresho ya mfumo wa kodi na tozo na mabadiliko makubwa sana na sura ya bajeti na mambo mengi ambayo tumeyaona. Kwa hiyo, nipongeze kwa dhati juu ya kuwa na bajeti nzuri namna hii, inatupa matumaini kwamba kweli tunaelekea kwenye uchumi wa kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba mwaka huu ni mwaka wa kizio (it‟s base year) kwa hiyo upo umuhimu wa kuangalia data na kumbukumbu zetu za mwaka huu kwa ajili ya kuweza kuzitumia siku za usoni; ili kuona mwelekeo wa ukuaji wa uchumi unavyokuwa kuanzia mwaka huu. Ni mwaka ambao tumekuwa na Rais mpya, mchapakazi na ambaye anadhamira ya dhati kutupeleka sehemu nzuri, lakini ni mwaka ambao pia tuna Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano mpya na yamkini pia tuna Waziri wa Fedha ambaye kama anavyoonesha kwamba atatusaidia sana ili tuweze kuona hali ya uchumi inakwenda kule tunakostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwa na mimi nichangie tu upande huu wa data zetu nikizingatia kwamba Ofisi ya Takwimu inafanya kazi nzuri. Nilikuwa nafikiri ni muhimu niseme kidogo hapa, kwamba hii Idara inafanya vyema. Lakini nilikuwa nafikiria nishauri idara hii sasa iwezeshwe kwa haraka ili tuweze kupata data ambazo zitatusaidia kufanya analysis zaidi tunapo kwenda mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu utaona kwenye kitabu hiki cha hali ya uchumi ile price index iliyotumika ni ya mwaka 2007, inaonesha pale nyuma ilikuwa ina shida kidogo ya uwezeshaji, lakini nilikuwa nafikiria kwa sababu tumeanza mwaka na mambo mapya ni vizuri sasa; hao wenzetu wa takwimu wawezeshwe mwaka huu ili basi tupate price index mpya ambayo itatufanya tuweze ku-determine ukuaji wa uchumi unavyokwenda kwenye hii miaka kumi inayofuata na tuweze kuwa na indicator mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu katika hali ya kawaida, tutazungumza kwamba hali ya uchumi inakuwa lakini utaona bado tunaweza kuwa na maswali mengi ambayo tunaweza kujiuliza. Kwa sababu kutakuwa kuna gape kati ya nominal income na real income hasa kwenye maisha yale ya kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba wakati tukizungumza juu ya kukua kwa hali ya uchumi lakini ukienda kule chini utaona kabisa kwamba bado kuna hali isiyo nzuri. Kwa hiyo Idara hii ya Takwimu iwezeshwe ili basi takwimu zinavyokuja hapa tuweze kuona zinaenda na hali halisi. Utaona kabisa kwamba kama ni mishahara itaonekana haitoshi kulingana na hali ya maisha, utaona kama ni bei ya mazao haitoshi kulingana na maisha. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiria kwamba Idara ya Takwimu iwezeshwe ili iweze kuleta uhalisia.
Mheshimiwa Naibu Spika, utakuja kuona kwamba bado tuna income gape kwenye society, kwa hiyo, tuone hili gape likizibwa ili lisitupe nafasi ya kuburuza wale wanaoishi maisha ya hali ya uduni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuangalia kwenye kitabu cha hali ya uchumi, kumbukumbu nyingi zinaonesha zimechukuliwa hasa katika maeneo ya mjini, na sehemu kubwa utaona majedwali yanaonesha hali hii imechukuliwa katika masoko ya Dar es Salaam na yameacha kuchukua maeneo ambayo pia yametajwa kwamba ni maeneo ambayo yana umasikikini mkubwa, wananchi wanaishi chini ya mstari ule wa umaskini. Kwa Mikoa kama Kigoma, Geita, Kagera, Singida, Mwanza utaona kwamba upo umuhimu sasa hizi data zichukuliwe kwenye maeneo haya zikichanganywa na maeneo mengine, ili tukipata wastani uwe wastani ambao utakuwa unagusa wananchi walio wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nizungumze juu ya hii dhana ya ukuaji wa uchumi kwa ujumla hii; kwamba tunataka twende kwenye uchumi wa viwanda, tuwe na uchumi wa kati. Sasa nilikuwa najaribu kujiuliza, kwa sababu kama Mheshimiwa Waziri wakati anamalizia kusoma hotuba yake alizungumza juu ya umuhimu wa wananchi wote kutakiwa kushiriki katika kuhakikisha kwamba uchumi unakua. Lakini walio wengi tunaweza tusielewe tunavyozungumza juu ya tunahitaji kwenda kwenye uchumi wa kati. Je, wastani wa pato kwa mtu unatakiwa uwe wapi, iwe ni dola 1,500 kwa mtu au 3,000 kwa mtu?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo yako mambo ambayo tunahitaji pia ili wananchi wetu kwa ujumla, ambao pia kila mmoja ana mchango wake katika ukuaji wa uchumi, aweze kuelewa kwamba tunataka twende kwenye uchumi unaotegemea viwanda na biashara. Tunahitaji pia wastani wetu wa kipato kupanda kwenda dola 3,000 kwa mtu kufika mwaka 2025; kila mwananchi aweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, na hii pia itawezesha wananchi wetu wengi ambao bado hawajapata ajira, wapate ajira ili waweze kushiriki vizuri katika ujenzi wa uchumi. Lakini pia bidhaa zetu tutakazozizalisha katika viwanda ziwe na ubora kiasi cha kumudu ushindani katika masoko ya dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni muhimu sana jambo hili litafsiriwe vizuri, wakati mwingine Wizara ifanye utaratibu wa kutoa vipeperushi virahisi ili wananchi mpaka aliyeko huko chini aweze kujua kwamba kwa pamoja tunaelekea wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipenda nishauri kwamba ni vyema tutafsiri vizuri ili wananchi waelewe, na hasa watumishi walioko kwenye Halmashauri na watumishi wengine, waweze kuijua hii dhana nzima ya kwenda kwenye uchumi wa kati na wa viwanda, na hivyo tuweze kuielewa vyema na kushiriki ujenzi wa uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka niseme kwamba Serikali imechukua hatua nzuri kwa sababu hapo nyuma tulikuwa na matatizo makubwa ya kutokukusanya kodi kiasi cha kutosha. Sasa inaonesha kabisa kwamba Serikali inafanya juhudi kubwa ya kufanya makusanyo. Ukiingalia hii bajeti ambayo imekuja leo utaona kabisa kwamba ipo dhamira ya Serikali ya kufanya tutegemee mapato yetu ya ndani; hili ni jambo la kupongeza sana Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kulikuwa na tatizo la kutokutolewa kwa mafungu, kwamba mtiririko wake haukuwa mzuri. Naamini kama juhudi za makusanyo zitaongoezeka kile ambacho tumekipitisha hapa kikiweza kufika na kwa wakati tutayaona maendeleo kwa haraka. Pia ninaona Serikali ina dhamira ya dhati kwa kusimamia nidhamu ya makusanyo na matumizi. Mwanzo ilikuwa ni shida lakini kwa hali iliyoko sasa hivi inatutia matumaini kwamba tunakwenda kwenye mwelekeo mzuri. Kwa hiyo, nishauri tu, tuweke hamasa kubwa kwenye makusanyo ya mapato ya ndani ili tuweze kujitegemea, lakini pia tusimamie nidhamu katika ukusanyaji na matumizi ya rasilimali zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nizungumze kidogo juu ya sura ya bajeti. Kuna mambo ambayo nilikuwa nafikiri niweze kushauri. Kwanza napongeza ukuaji wa bajeti hii, kutoka trilioni 22 kwenda trilioni 29, si jambo dogo, ongezeko la zaidi ya asilimia 23, ni jambo la kuipongeza Serikali. Pia uwiano wa matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo umeongezeka. Nilikuwa nafikiria kwamba tuiangalie vizuri kwa baadhi ya maeneo, kwa mfano kwenye Halmashauri zetu au Serikali za Mitaa bajeti ya maendeleo iongezwe. Kwa sasa hivi tuna kama trilioni 1.3 ambayo tunaipeleka kwenye Serikali zetu za Mitaa. Hali itakapokuwa nzuri tusukume hizi pesa za maendeleo ziende zaidi kwenye Serikali zetu za Mitaa ili isaidie kuondoa baadhi ya matatizo yaliyo mengi huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahishwa pia na juhudi za Serikali kuangalia suala zima la usimamizi wa kodi. Kwa hiyo, ni…
NAIBU SPIKA: Muda wako umeisha Mheshimiwa Kwandikwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia kwenye hoja hii ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nianze kwa kuunga mkono hoja. Pia nimshukuru Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa namna ambavyo ameanza kwa kuonesha juhudi ya kuweza kuhakikisha kwamba rasilimali hii muhimu inakuwa katika hali ambayo inalineemesha Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana wananchi wa Jimbo langu la Ushetu kwa sababu tumekuwa na matatizo makubwa sana, lakini wamekuwa wavumilivu lakini pia wamekuwa sehemu ya kutoa ushirikiano ili kuweza kutatua matatizo ya migogoro ambayo ipo kwenye mipaka. Sisi katika Jimbo letu la Ushetu tumepakana na Hifadhi ya Kigosi Moyowosi lakini pia tuna hifadhi za misitu nyingi kwenye Kata za Ulowa, Ubagwe, Ulewe, Nyankende, Idahina na Igomanoni. Kote huko tunapakana na misitu lakini wananchi hawa wamekuwa na utayari wa kushirikiana ili tuhakikishe kwamba uhifadhi unaendelea lakini pia mifugo yetu inapata sehemu ya malisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakubaliana kwamba sekta hii ya maliasili na utalii imetoa mchango mkubwa sana kwenye Taifa letu. Utashuhudia kwamba kuna ajira imepatikana maeneo mbalimbali ya moja kwa moja na ile ambayo ni indirect. Pia imechangia kama wachangiaji wengine walivyosema katika pato la Taifa, fedha za kigeni tumezipata lakini mchango mkubwa umekwenda katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Jambo lingine pia uhifadhi wetu umeipa heshima nchi yetu, niipongeze sana Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini utaona katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumza pia kwamba uko mchango mkubwa kwenye nishati. Asilimia 90 ya nishati imetokana na rasilimali zetu hasa hasa za kwenye misitu. Pia kumekuwa na 75% kwa mujibu wa taarifa ya Mheshimiwa Waziri imetupa faida ya kupata vifaa vya ujenzi. Kwa hiyo, utaona kabisa sekta hii ni muhimu lakini ni lazima kuhakikisha kwamba kunakuwa na uhifadhi lakini pia kutokuwa na migogoro ambayo inatusumbua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alivyoanza kutoa hotuba yake aliturejesha kwenye Ibara ya 27 ya Katiba lakini napenda nimshauri Mheshimiwa Waziri ajaribu kuiangalia Ibara ya 24 kwa madhumuni ya kuziangalia sheria zetu. Hizi sheria zetu ambazo zinatoa fursa ya uhifadhi wa misitu yetu zinahitajika ziletwe katika Bunge lako kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho. Kwa sababu ukiiangalia Ibara ya 24, naomba kwa ruksa yako niisome kwa haraka, inazungumza juu ya haki ya kumiliki mali, inasema kwamba:-
“(1) Kila mtu anayo haki ya kumiliki mali, na haki ya hifadhi ya mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria.
(2) Bila kuathiri masharti ya Ibara ndogo ya (1), ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang’anywa mali yake kwa madhumuni ya kuitaifisha au madhumuni mengineyo bila idhini ya sheria ambayo inaweka masharti ya kutoa fidia inayostahili”. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo yetu tumekuwa na utaifishaji wa mifugo, sasa nashauri sheria hizi zije hapa tuzitazame. Sheria hizi zimepitwa na muda kwa sababu ukiangalia hata zile sheria ambazo zinatoa uhifadhi katika maeneo kama ya TANAPA ziko faini ndogo sana. Nilikuwa nafikiria kwamba tufanye marekebisho lakini pia itupe nafasi sisi wananchi, kama Mheshimiwa Waziri alivyozungumza katika hii Ibara ya pili, anapozungumza juu ya uhifadhi, nani ahifadhi na hizi rasilimali ni za nani, ni zetu sisi sote. Kwa hiyo, lazima tushiriki pia kuhifadhi na kulinda hizi rasilimali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri afanye mapitio ili tu tupate sheria ambazo na sisi wananchi kwa kupitia vikundi vyetu kama wakati mwingine nilivyoshauri hapa tuweze kutoa nafasi kwa wananchi kupitia vikundi vyetu na uongozi wa mila kuweza kupeana faini kidogo kidogo za kila siku ili kuhakikisha kwamba uhifadhi unakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kuangalia katika migogoro hii ambayo imekuwepo, chanzo chake ni nini? Ni ukweli Mheshimiwa Waziri akubaliane na mimi kwamba siku za nyuma tumekuwa na utaratibu kwamba wale wahifadhi walikuwa kwanza hawatoshi lakini pia wamekuwa wakitumika katika kuhifadhi watu ambao walikuwa wanawachukua kwa muda ambao sasa kutokana na kutokuwa na nidhamu tulichochea sana wananchi wetu kuingiza mifugo katika hifadhi. Matokeo yake ilizoeleka kama ni jambo la kawaida kwa mwananchi kupeleka mifugo yake katika hizi hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo kadhaa napenda kushauri. La kwanza Mheshimiwa Waziri lazima tuwe na dhamira ya kweli kwa upande wa Serikali na kwa upande wa wananchi na Waheshimiwa Wabunge ya kutatua hii migogoro, lazima tudhamirie kuliondoa hili suala. Tukidhamiria tutapata nafasi ya kurejesha yale mahusiano ambayo yalianza kupotea ili tushirikiane kwa pamoja kuona kwamba uelewa wa uhifashi unapanuka lakini pia tunashiriki kuweza kuhifadhi maeneo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko pengo la uelewa ambalo nimwombe Mheshimiwa Waziri na timu yake wajipange vizuri ili tuendelee kuwaelimisha wananchi kwa kuweka vile vikundi ambavyo vimetajwa na sheria kwa ajili ya kushiriki katika uhifadhi, kwa pamoja tatizo hili tutaweza kuliondoa. Pia bajeti ya Mheshimiwa Waziri haitoshi ili kuhakikisha mafunzo yanatolewa na vikundi vinasaidiwa ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la wafanyakazi hawa kwa ajili ya doria hawatoshi. Mheshimiwa Waziri litazame suala hili ili tupate watu wenye weledi ili tuweze kwenda vizuri. Pia liko jambo ambalo nafikiria kwamba lazima tuwe na sheria ndondogo kwa upande wetu wa uhifadhi ili tuweze kusaidia kama walivyofanya wenzetu upande wa TANAPA na maeneo ya kwetu iwe hivyo ili tuweze kupiga hatua vyema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kuangalia taarifa hizi za bajeti katika kipindi hiki cha miaka miwili, mitatu, utaona uharibifu kwa mwaka ni hekta 372,000 lakini kwa mwaka tunapanda miti 95,000 na tunasema ikifikia 2030 tutakuwa angalau tumeweza kuwa na misitu ya kutosha, haiwezekani kwa sababu uharibifu huu ni mkubwa kuliko namna ambavyo tunaweza kufanya hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kuangalia gharama za kupanda miti, miche ya miti ina bei kubwa sana Mheshimiwa Waziri aangalie eneo hili kwani wananchi wetu wakipata miche ya miti watasaidia kupanda miti mingi ili tuweze kurejesha huu uharibifu. Kwa hiyo, ukiangalia uwiano wa uharibifu na namna ambavyo tunarejeshea misitu utaona kabisa haiwezekani kuhakikisha kwamba kweli hii maliasili inabaki vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi tumeyazungumza kwenye mifugo, lakini tumesahau kuna eneo lingine ambalo pia linaharibu misitu yetu. Utaona kabisa kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba mkaa tani milioni 1.7 inaingia mjini, asilimia 50 inaingia Dar es Salaam, inatoka maeneo ya pembezoni kuja mjini. Eneo hii ni muhimu sana tuliangalie vinginevyo tutaona kwamba labda mifugo ndiyo inaharibu misitu hii, lakini bado nishati ni sehemu kubwa ya uharibu wa misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri aje na mkakati mzuri wa kuhakikisha kwamba tunaweza kushikiriana na upande mwingine wa nishati mbadala ili kuhakikisha kwamba hii retention ya misitu inakwenda vizuri. Suala la uhifadhi shirikishi ni muhimu sana, lazima tushirikiane na wananchi ili kuhakikisha kwamba misitu yetu inakaa vizuri. Twende sambamba na Wizara zingine kuhakikisha wananchi wetu tunawajengea kipato cha kutosha ili ule ushawishi wa kuharibu na kutumia rasilimali zetu uweze kupungua ili misitu yetu iweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze juu ya utafiti na sensa ya wanyamapori. Nimejaribu kuangalia ripoti mbalimbali naona kwamba kulikuwa kuna sample tu ya sensa kwa kuangalia namna ambavyo wanyama wamepungua, kama tembo wamepungua sana...
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la malisho katika Jimbo la Ushetu, napenda kushauri na kuomba Wizara iturejeshee msitu wa Usumbwa uliochukuliwa na Serikali mwaka 2002 ili wananchi wapate sehemu ya malisho na kushiriki kikamilifu kuhifadhi Mbuga ya Kigosi-Moyowosi. Ushetu tumeanza kutoa hamasa ya wananchi kushiriki katika hifadhi kwa kutozana faini za kimila ili kuzuia uharibifu, shida yetu ni eneo la malisho.
Pili niombe na kushauri tupewe eneo la msitu wa akiba wa Ushetu/Ubagwe ili tupate eneo la malisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikiano; naomba sana Wizara itoe ushirikiano kwa wananchi na Wabunge wanaopakana na hifadhi, mashirika mbalimbali ikiwemo ya dini, vikundi na uongozi wa kimila ili tuzungumze namna bora ya kutatua migogoro katika maeneo yetu baina ya wahifadhi na wananchi ama wafugaji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi na ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ameniwezesha kusimama kwenye Bunge lako hili. Pia nishukuru kwa dhati Wizara hii ni Wizara ambayo mimi nimefanya kazi nikitumika katika Ofisi ya Taifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kwa hiyo, kufika kwangu hapa kwa moyo wa dhati naamini uko mchango mkubwa wa Wizara hii.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwamba Wizara hii inasimamia mafungu mengi na kama tulivyoona kwenye report hii kuna mambo mengi ambayo ameyaonyesha Mheshimiwa Waziri niwashukuru kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka niende moja kwa moja kwenye kuchangia hoja hii. La kwanza nilitaka nijue tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Rais hapa aliahidi kwamba Sheria ya Manunuzi italetwa katika Bunge hili. Nilikuwa nikipitia report, sijaona kwamba tumejiandaa namna gani ili sheria hii ambayo ni mwiba inakuja kwenye Bunge hili ili tuweze kuipitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nilitaka nizungumze juu ya hizi idara chache tu ambazo ziko chini ya Wizara hii nikianza na hii ya Ofisi ya Msajili wa Hazina. Utaona kabisa kwamba inalo jukumu kubwa sana la kusimamia taasisi nyingi ambazo ziko chini yake na hizi taasisi tunategemea zikisimamiwa vizuri ili ziweze kutoa mchango mkubwa wa mapato katika Serikali. Niko kwenye Kamati ya Uwekezaji ya Mitaji ya Umma, utaona kabisa kwamba mashirika yaliyoko huko na taasisi ziko 215 lakini tunahitaji tuwe na watumishi wengi sasa utaona kabisa hata bajeti ta TR iko ndogo sana na bado tumeona hapa, tumesikia kutoka kwenye taarifa ya Kamati wamepata asilimia nane ya kilichokuwa kimebajetiwa kipindi kilichopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji kuangalia mambo mengi sana katika taasisi hizi ili ziweze kutoa mchango mkubwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali. Capital structure ya mashirika haya haiko vizuri, lakini utaona mashirika yaliyo mengi hata investment plan hayana, kwa hiyo, utaona tunahitaji watu wenye weledi tofauti katika ofisi ya TR ili iweze kuweka msukumo mzuri na mwisho wa safari tuone mchango mkubwa unakwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ukiangalia kwenye kiasi ambacho kitachangiwa na non-tax revenue bado kiasi hiki ni kidogo lakini ukienda kuangalia kwa undani kabisa nafasi ipo kama tutasimamia vizuri Mashirika haya naamini kwamba mchango mkubwa utakuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nilitaka nichangie tu kwenye hii Wizara, kwamba nilikuwa nafikiria Mheshimiwa Waziri atasema hii kada ya wahasibu. Kada ya wahasibu bado inatoa tu taarifa, msukumo haujawekwa vizuri nilikuwa nafikiria labda tungeweza kuzipandisha hadhi angalau ziwe katika hadhi ya Ukurugenzi ili waweze kutoa mchango mkubwa wa uchambuzi lakini pia kushiriki katika maamuzi kwenye Wizara. Kwa hiyo, utaona tumeendelea kuwa na unit, lakini umeona kabisa katika Wizara kuna fedha nyingi sana ambazo Wahasibu wanasimamia nilikuwa nafikiri Mheshimiwa Waziri alitazame. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine nilitaka nizungumze juu ya uandaaji wa hesabu. Serikali imefanya uamuzi mzuri utayarishaji wa hesabu kwa viwango hivi vya Kimataifa kwenye Accrual Basis, utaona sasa karibu kile kipindi cha mpito karibu kinakwisha, hatutakuja kuwa na hesabu nzuri. Tunahitaji tupate hesabu ambazo zitaonyesha ile National Wealth tuone majengo yanaonekana kwenye hesabu, jumuifu tuone madaraja gharama zake, tuone ardhi, tuone madeni na mali mbalimbali, utaona sasa tangu tulivyoingia kwenye mfumo huu ikifika mwaka 2017 itakuwa kile kipindi cha mpito kinaisha, tutategemea kuwa na hesabu ambazo zinaweza zisipate hati safi kama ilivyokuwa kwenye Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa liko jambo la kufanya Mheshimiwa Waziri, uliangalie hili, kikubwa zaidi kwenye kufanya uthamini wa mali utaona kwamba hata Kwenye Halmashauri za kwetu tunao ma-valuer lakini hawafanyi kazi ya kutathmini mali hizi za Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nafikiri nimshauri Mheshimiwa Waziri kwamba hili suala la kuthamini mali lichukuliwe kama ni National issue ili tuwe na frame work nzuri ya kuhakikisha kwamba tuna muda wa haraka kukamilisha uthamini wa mali ili hesabu zetu siku za usoni ziweze kuwa nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliombe kupitia Wizara yako Mheshimiwa Waziri, mafunzo ya IPSAS kwa sababu update zipo kila wakati, tuweke msukumo ili tuweze kuwa na hesabu nzuri ambazo zitatusaidia kufanya maamuzi mbalimbali tunahitaji kuwa na kuhasibu oil and gas, tunahitaji kuhasibu shares na investment, kwa hiyo kila wakati kuna update zinakuja nilikuwa najaribu kuangalia kwenye bajeti ninaona kwamba saa nyingine upande wa mafunzo bado kidogo tunahitaji tuweze kusukuma tuweze kuweka mafungu ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nilitaka nizungumze juu ya accountability (uwajibikaji). Nilikuwa najaribu kuzitazama hizi ofisi za Internal Auditor General lakini naangalia pia na ofisi ya CAG. Nilivyokuwa nikiangalia kule naona kwamba tutakuwa na shida kubwa kwa sababu pamoja na kuwa kulikuwa na utaratibu ule wa kupunguza matumizi kwenye OC lakini utakuja kuona kabisa kuna kazi hazitafanyika. Mheshimiwa Waziri alitazame hili, Internal Auditor General ofisi yake ikiwezeshwa, itamuwezesha CAG iwe nyepesi na saa nyingine hata gharama za ukaguzi zinaweza zikapungua lakini bado naona hapa msukumo upo mdogo, hivi kwa nini Mheshimiwa Waziri ofisi ya Internal Auditor General isipewe full vote ili uwajibikaji uweze kuongezeka? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia bajeti ya CAG imepungua sana na ukija kuiangalia kwa undani nilikuwa naangalia kitabu Volume II, utaona kabisa kwamba hizi kaguzi kwenye Serikali za Mitaa hazitafanyika Mheshimiwa Waziri hebu litazame kwa sababu utaona kwamba imetengewa kwenye ule upande tu wa kwenda kutembelea Halmashauri, kwa mfano, ziko shilingi milioni 332 kwenye kile kifungu ukiangalia. Sasa hii ni wastani tu labda wa mtu mmoja siku 20 kila Halmashauri ataenda kufanya kazi haitawezekana, kwa hiyo utaona kabisa kwamba hii funding iliyokuwepo kwenye ofisi hii Mheshimiwa Waziri itazame vizuri lakini vinginevyo hatutategemea kuwa na report nyingi kama ulivyozionyesha kwenye report hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna report nyingi sana mwaka huu tumezipokea, kwa hiyo tutegemee siku za usoni hatutakuwa na report za ukaguzi nyingi kama ilivyokuwa kwa sababu hali iliyopo hapa siyo nzuri. Utaona kabisa sehemu ambayo ilikuwa imetengewa kwa mwaka uliotangulia shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya ukaguzi wa Wizara, ziko shilingi milioni 280, sasa hii inatuonyesha nini? Inaonyesha kwamba hii kazi ya ukaguzi haijapewa msukumo wa kutosha ili kuhakikisha kwamba tunapata report lakini mwisho wa safari tunaweza kufanya maamuzi mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka pia nimalizie kwa kutoa ushauri tu kwamba kama tulivyosikia kwenye report ya Kamati pia kwamba kiasi ambacho kilikuwa kimetengewa kwenye bajeti ni kiasi kidogo, kwa hiyo, wakati msukumo mkubwa unakwenda kufanya makusanyo ya kutosha basi tuhakikishe kwamba kiasi ambacho kinatengwa kwenye Bunge lako hili Tukufu kinapelekwa na kwa wakati ili kama kiasi chote kitatolewa basi itakuwa ni wakati mzuri wa miradi mbalimbali ya maendeleo kuweza kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakati huo huo tuendelee kuangalia maeneo mengine ambayo yataweza kuongeza mapato ya Serikali na hasa hasa hii non-tax revenue yako maeneo mengi ambayo tukiweza kuweka msukumo mkubwa tutaweza kuona kwamba tunapata fedha za kutosha na mwisho wa safari utaona kwamba angalau hata ule mtiririko wa fedha kwenda kwenye Halmashauri utakuwa unakwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusisitiza tena suala la asset valuation ni suala muhimu sana ili national accounts ziweze kuficha vizuri ili mali zetu kwenye Halmashauri zetu ziweze kuonekana vizuri, lakini pia hati safi ziweze kuongezeka. Utakuja kuona kwamba kwenye Halmashauri zetu kwa mwaka huu uliokwisha saa nyingine tunaweza tusiwe tumefanya vizuri sana lakini kutokana na hili tatizo kubwa la asset evaluation imekuwa ni tatizo kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimia Naibu Spika nashukuru sana kwa nafasi hii naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia huu Mpango wa Maendeleo. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa sababu ukiuangalia kwa ujumla mpango huu, nimeusoma vizuri na pia niseme kwamba nimechangia kwa maandishi kwa sababu ya muda. Mpango huu ni mzuri kwa sababu mpango huu ni muendelezo wa ule mpango wa miaka mitano. Kwa hiyo ukiusoma vizuri utaona kabisa kwamba uko mwendelezo mzuri, sasa kuna mambo kadhaa ya kufanya, ambayo nilikuwa napenda kushauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu umezingatia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, lakini pia umezingatia mpango wa maendeleo endelevu. Kwa hiyo, nilikuwa nataka ni- appreciate kwa kuona kwamba kwa kweli ukiangalia hali ya uchumi kwa ujumla kwa taarifa ilitolewa na BOT mwezi Agasti, utaona kabisa kwa performance ya bajeti ya Julai, maendeleo ni mazuri, kwa hiyo, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende tu moja kwa moja kwenye ushauri, nilikuwa napenda nishauri mambo kadhaa, ambayo tumeyaona kama changamono na Waheshimiwa wengi wamechangia hapa. Ipo changamoto ya ukusanyaji kodi kwamba yako maeneo kama mpango unavyosema kwamba unakwenda kutazama sekta binafsi, lakini pia tumezungumza juu ya kuendeleza viwanda, lakini uko uhusiano mkubwa kati ya sekta binafsi na ukuaji wa viwanda na suala la ukuaji wa uchumi kwa ujumla. Kwa hiyo kuna mambo ya kuyaangalia hapa ili sasa tuweze kusaidia sekta, Mheshimiwa Waziri ajaribu kuangalia maeneo haya ya kodi, kwa sababu ukweli lazima wafanyabiasha na sekta binafsi walipe kodi. Lakini kuna maeneo ambayo ni ya kuyatazama ili kuweza kufanya ile tax compliance iwe ya hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kuangalia kwa mfano, upenda wa VAT kwenye viwanda vyetu ambavyo vipo kwa mfano, viwanda ambavyo vinasindika mafuta, mashudu yale yamewekea VAT, utakuja kuona kwamba VAT register ni kama agent wa TRA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapokuwa na hii VAT kwenye uzalishaji wa kwanza utaona inavutia kuongeza bei na kwamba ule ushindani sasa wa bei unakuwa ni mgumu kwa product inayofanana na wenzetu nje ya nchi na hata kwa watumiaji wa bidhaa hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tulitazame hili suala la namna ambayo kodi itahamasisha ili ule ulipaji wa kodi, compliance iwe kubwa kwamba mtu alipe bila kushurutishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo lipo nilitaka nishauri, kumekuwa na tatizo hili la mzunguko wa fedha. Sasa nilikuwa najaribu kufikiria kwamba tulikuja na sheria ya bajeti ili mwezi ule wa saba kuwe na kiasi cha kutosha cha fedha kuweza kuendesha bajeti zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kunahitajika kutazama hili suala la cash flow management, Wizara ilitazame ili tunapokuja kupitisha bajeti mwanzoni mwa mwezi wa saba kuwe na flow nzuri ya fedha kulingana na uhitaji katika maeneo mbalimbali, katika Halmashauri zetu. Kwa hiyo, sikuona tatizo sana kwa sababu kama bajeti ipo na fedha inayotolewa iko within the budget, hapa hakuna shida, ila lipo suala la kuangalia ile flow ya pesa inayokwenda kwa ajili ya matumizi, kwa hiyo, Wizara hapa iangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mzunguko wa fedha, hili linaonyesha kwenye sekta ya fedha, Wizara ilitazame kwa sababu kunapokuwa na mabadiliko ya hizi sheria za kodi zilivyokuja, lakini pia mabadiliko katika taasisi zetu za kifedha, watu wanapata hofu ya kupeleka fedha katika hizi taasisi za fedha. Kwa hiyo, utaona kabisa kwamba zile deposit kwenda kwenye mabenki zimepungua kiasi kwamba ule mzunguko umepungua. Kwa hiyo, sasa BOT iangalie namna yaku-regulate ule mzunguko wa fedha ili tuione inaleta impact kwenye mzunguko na ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uko uhusiano mzuri sana kati ya sekta binafsi na ukuaji wa viwanda, sasa uko umuhimu pia wa kuliangalia suala la kilimo. Kilimo chetu hakijapewa msukumo wa nguvu ili kuhakikisha kwamba sasa tunapata raw material za kutosha kuendesha viwanda vyetu. Ukija kuangalia kwenye zao la pamba, uzalishaji wa pamba umeshuka, katika msimu huu ununuzi wa pamba umefanyika kwa wiki mbili tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utakuta sekta binafsi watu wana viwanda vyao vya kuchambua pamba vimesimama mtu ambaye alitakiwa kununua tani 60,000 katika msimu huu amenunua tani 14,000 utaona kabisa kwamba tuna dead asset, ziko asset za wafanyabiashara hazisaidii mchango katika uzalishaji. Kwa hiyo, Wizara itazame namna gani ya kuweza kusaidia haya maeneo ili tuwe na uwiano mzuri kati ya uzalishaji katika kilimo, uzalishaji katika viwanda vyetu ili tuweze kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata fedha za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Serikali ijaribu kuangalia kusaidia tuje tupate kiwanda ambacho kita-support hivi viwanda vidogo ambavyo vipo vinachambua pamba, tupate kiwanda kikubwa kwa ajli ya kutengeneza nguo ili pia sasa tuweze kuzalisha nguo za kutosha ili wananchi wa Tanzania waweze kupata nguo kwa bei ambayo inakuwa ni nafuu na kufanya kwamba hali ya uchumi iweze kuwa nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitaka pia nimalizie kutoa ushauri kwamba tulipokuwa tumeanzisha mfumo wa usimamizi wa fedha tumekuja na hii concept ya accrual basis, sasa…
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono, ninashukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye taarifa za Kamati ya PAC na LAAC. Nianze kwanza kuishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali ambayo imekuwa ikizichukua ili kuweza kupunguza yale mapungufu mengi ambayo yalikuwepo kipindi cha nyuma. Tumeshuhudia kumekuwa na reforms mbalimbali hususani financial management reforms zenye lengo la kuleta udhibiti wa matumizi ya Serikali, lakini pia kuondoa mapungufu mengi ambayo yamekuwa yakijitokeza siku za nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine kumpongeza CAG na wafanyakazi walioko chini yaOfisi ya CAG kwa sababu taarifa hizi ambazo tumeletewa ni matokeo ya kazi nzuri ya CAG ambayo ameifanya. Wachangiaji wengi wamekuwa wakizungumza juu ya mapungufu yaliyokuwepo, kikubwa yanasababishwa na ule udhibiti wa ndani, lakini kama nilivyosema kwamba Serikali imeanzisha pia Ofisi ya Internal Auditor General kwa nia hiyo ya kuleta udhibiti madhubuti kwenye taasisi zetu na mashirika yetu na hasa hata kwenye Serikali zetu za Mitaa. Kwa hiyo, naona Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa na naamini kwamba kadri tutakavyokwenda mambo yataendelea kuwa mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa ya ukaguzi ni kututhibitishia kwamba rasilimali za umma, zile asset za umma ziko katika hali nzuri, lakini pia tunapata ushauri kutokana na ukaguzi na matokeo yake ndiyo kama hivi kwamba Kamati zetu zimepata input ya kuweza sasa kuliletea mapendekezo Bunge ninaunga mkono mapendekezo yote ambayo yapo kwenye Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite zaidi kwenye mashirika ya umma. Niko kwenye Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma. Nilitaka nizungumze machache kuhusu ufanisi ambao utatekeleza saa nyingine haya mashirika ya umma kuweza kupunguza matatizo yaliyokuwepo lakini pia kuweza kuongeza mapato, non-tax revenue katika Serikali. Kwa sababu ukiangalia bado ule mchango ambao unakwenda kwenye Serikali kwenye mapato bado uko mdogo, ukiangalia kwenye bajeti ya 2016/2017, mchango huu ambao ni non-tax revenue ukijumlisha pamoja na Halmashuri uko asilimia 11.3; lakini ukiona kwenye mwaka huu ambao tunakwenda kuzungumzia kipindi kijacho projection iko asilimia 12.35. Kwa hiyo, bado mchango uko mdogo kwa hiyo, ninaamini kwamba kuna mambo mengi yakishughulikiwa hasa hasa kuboresha mashirika yetu, mchango utakuwa mkubwa katika Pato lile la Taifa.
Mhesimiwa Naibu Spika, nizungumze mambo mawili, jambo la kwanza nilitaka niseme kuhusu kuwezesha Ofisi ya Msajili wa Hazina. Utakuja kuona kwamba Msajili wa Hazina amekuwa akifanyakazi kubwa kwa upande wa Mashirika ya Umma lakini pia kwenye upande wa PAC naamini kwamba amekuwa kitoa mchango wao kuwezeha kazi za Kamati kufanyika vizuri. Lakini bado liko jambo la kumwezesha huyu Msajili ili aweze kupata uwezo mkubwa wa kufanyakazi na kuweza kusimamia mashirika haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaona kwamba kazi ya kwake ya kushauri mashirika juu ya uanzishwaji na hata saa nyingine kufutwa baadhi ya mashirika ambayo hayana ufanisi lakini liko jambo pia la kuangalia ule utendaji wenye tija katika mashirika. Kupitia mipango na bajeti za mashirika na hata jana umeshudia tumepitisha mabadiliko ya sheria kwa nia ya maana kusaidia katika mashirika haya ili kuwa na uwiano ule wa matumizi na mapato yanayotoka kwenye mashirika haya hii itaiwezesha Serikali kuweza kupata gawiwo au fedha kutoka kwenye mashirika yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini anayo majukumu mengi, hii ni pamoja na kuweka viwango vya mashirika yetu kuweza kufanya makusanyo, lakini pia kuweza kuzisimamia hizi Bodi za Mashirika, kusimamia management na Kamati zake. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiria nipendekeze tu kwamba Serikali iitazame hii ofisi ya Msajili wa Hazina ili iweze kusaidia kuleta tija na kupunguza mambo ambayo yamejitokeza katika mashirika yetu ambayo yana changamoto nyingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika mashirika yetu ukiingalia sura ya mitaji iliyoko kwenye mashirika yaliyo mengi sura yake siyo nzuri inahitajika ifanyike uchambuzi wa makusudi wa nguvu na kushauri ili tuweze kuona zile capital structure kwenye mashirika yetu zinakuwa ni nzuri lakini kunahitaji pia kuweza kuona kwamba kuna mambo ambayo yameonekana kwenye report hii kwamba kuna madeni mengi kwa mashirika ambayo yanakusanya mapato yameshindwa kukusanya mapato vizuri, ipia utakuja kuona kwenye mizania kuna matatizo kwamba kuna rasilimali au asset za mashirika haya hazijafanyiwa evaluation muda mrefu, utaona matatizo yako mengi, iko ile mikakati ya kuweza kudhibiti vihatarishi (risk management) katika haya mashirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa nafikiria niliseme hili kwamba Serikali iangalie sana hii ofisi. Ofisi inayo majukumu mengi na kama itawezeshwa kwa maana ya kuweza kuhakikisha kwamba wamekuwa na rasilimali za kutosha ili kuweza kushughulikia mashirika haya, tutaona kwamba tutaweza kuongeza ufanisi katika haya mashirika ambayo yapo kwa sababu ukija kuangalia mashirika yaliyo mengi hawana investment plan, mashirika yaliyo mengi utaona hakuna risk strategy za kuweza kuondosha hatari ambazo zinafanya mashirika haya yasiwe na ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, haya yote haya Msajili wa Hazina anatakiwa kuyatazama na kwa kasi kubwa ili tuweze kuondokana na hayo matatizo ambayo yapo. Utakuja kuona hata kuna taasisi zingine za kifedha ziko chini ya Msajili wa Hazina na zenyewe zimekumbwa na matatizo haya ya kutokupata faida. Kuna mikopo chechefu, lakini pia ule uwekezaji lazima usimamiwe vizuri ili tuone kwamba mashirika haya yanaweza kufanya vizuri. Kumekuwana pia kutokuwa na record nzuri kwenye hesabu, kuna over statement za asset au under statement kwa hiyo haya mambo hayo ni muhimu sana yaweze kutazamwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la internal control, udhibiti wa ndani ni muhimu sana kutazama katika maeneo yote ili tuweze kupunguza hizi hoja lakini kikubwa tuweze kuwa na ufanisi mzuri katika kusimamia hizi rasilimali. Kwa hiyo, nilitaka nishauri tu kwamba jambo la kwanza Serikali isisitize sana kuhakikisha kwamba kunakuwa na Kamati za Ukaguzi ambazo zinatakiwa ziimarishwe, ziwe na watu wenye weledi lakini kama itawezekana pia kwenye mabadiliko ya sheria zetu tuzitazame ili Wajumbe wa Kamati hizi za Ukaguzi waweze kutoka nje ya taasisi husika ili ule ushauri uweze kusaidia kuboresha mashirika yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la lingine; wakaguzi wa ndani utakuja kuangalia hata katika Halmashauri zetu wakaguzi wa ndani ni wachache. Unakuta wakati mwingine wakipata fursa ya kwenda kwenye mafunzo ofisi zinafungwa zina wakaguzi wawili, zina wakaguzi watatu na hawa wakaguzi wa ndani ni jicho kwenye management iweze kusaidia kurekebisha mambo mapema kabla mambo hayajaharibika.
Kwa hiyo, ni muhimu Serikali itazame, imuwezeshe Mkaguzi mkuu wa ndani lakini pia wakaguzi wa ndani walioko kwenye taasisi zetu waweze kupata mafunzo lakini pia waweze kuongezwa ili waweze kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kuangalia pia kuwezesha mashirika yetu yana upungufu wa fedha, Serikali kama inaweza kwa sababu imekuwa ikiongeza makusanyo tuanzishe huu mfuko wa uwekezaji ili uweze kusaidia mashirika na taasisi ambazo ziko chini ya TR ili ziweze kuweza kupata fedha kutoka kwenye mfuko huu. Tuyaimarishe haya mashirika ili mwisho wa siku yaweze kuongeza gawiwo upande wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kukushukuru kwa kunipa nafasi hii kilio changu kikubwa ilikuwa ni kuhakikisha kwamba Ofisi ya TR inawezeshwa ili ikiungana na taasisi nyingine zinazoshughulikia masuala ya uadilifu, masuala haya ya tija, ziweze kufanya vizuri ili mwisho wa siku hoja zipungue lakini kikubwa ziweze kuchangia kwenye maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu nzima ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuja na mpango ambao unatekeleza ule mpango wa miaka mitano, Mpango wa Maendeleo endelevu na ilani ya CCM. Nipongeze mambo yafuatayo ambayo ni makusanyo yameongezeka na udhibiti wa matumizi umeongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara iangalie kwa makini changamoto zifuatazo:-
Ukusanyaji wa kodi wenye ufanisi na matatizo ya ukusanyaji kwa maofisa na walipa kodi. Uwekezaji sekta binafsi kumudu ushindani wa bidhaa nje unaotokana na “application ya VAT; cash flow management, mzunguko wa fedha (money supply), ukuaji wa uchumi na hali halisi ya maisha, kupeleka fedha za bajeti zilizotengwa na kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri, Serikali iendelee kupanua wigo wa ukusanyaji, mkazo uwe pia kwenye makato yasiyo na kodi (non-tax revenue) hususan taasisi zilizo chini ya TRA. Tuangalie namna kodi (VAT) itakavyowalinda sekta binafsi, tuangalie mnyororo wa huduma, mfano tuwezeshe kilimo chenye tija, kilimo kitoe malighafi za viwanda tujenge viwanda ambavyo ni soko la viwanda vyetu. Kilimo na viwanda vitainua uchumi na kuleta ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie vizuri utekelezaji accounting framework ya “accrual basis of accounting ili tuweze kuwa na cash ya kutosha mwanzoni mwa mwaka miradi isisimame mwanzoni mwa mwaka. Uwepo uhakiki wa data “data integrity” ili consumer price index” ijengwe kwa kuzingatia mtawanyiko wa masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii itawasaidia menejimenti ya real economy na Nominal economy ili kuondoa dhana ya ukuaji uchumi na hali halisi. Program based on budgeting inayolenga kuanza na Wizara nane itayarishwe kwa makini kwani inahitaji taarifa nyingi, inataja kuwa na “activity” nyingi, ngumu sana kuainisha shughuli (activity) na matokeo lengwa/malengo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono mpango huu.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana kwa kunipa nafasi ili
niweze kuchangia kwenye taarifa za Kamati ya Nishati na Madini na ile ya Miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii nipongeze sana kamati zote hizi mbili
kwa kuja na ripoti nzuri; ripoti ambazo ukizisoma zimesheheni mapendekezo mazuri sana na
maazimio mazuri kwenye ripoti hizi na imani yangu kwamba Serikali itafanyia kazi na
kuyatekeleza vema mapendekezo ambayo yapo kwenye ripoti ya Kamati hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya ya miundombinu pamoja na nishati na madini
ni muhimu sana katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Stadi zinaonesha asilimia 80
ya uwezeshaji wa uwekezaji inatokana na nishati hizi pamoja na miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mkazo mkubwa ukiwekwa kwenye sekta hizi
utachochea kiasi kikubwa sana cha maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimboni kwangu Ushetu hatuna umeme, tumebahatika kuwa
na vijiji vitatu tu ambavyo vimepata umeme, imekuwa ni vigumu sana kushawishi wawekezaji
kuja kuweka uwekezaji wa aina mbalimbali. Kwa hiyo, ninaamini kabisa katika hii REA III kwa vile
vijiji vyangu vimeonekana kwenye ule mpango basi nafikiri Mheshimiwa Waziri hapa
atanihakikishia kwamba tutapata umeme ili ile kasi ya kuvutia wawekezaji katika maeneo ya
kwetu tuweze na sisi kuweza kusukuma katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii ninasema ni muhimu katika ukuaji wa uchumi; hivi
majuzi tulikuwa tunazungumza juu parameter mbalimbali za ukuaji wa uchumi ikiwemo
mfumuko wa bei; nilitaka nijikite hapa kidogo nizungumze na namna ambavyo hata wakati
mwingine bei hii ya nishati ya umeme na mafuta inavyoweza kuathiri; kuna muda wa kutafsiri hili
suala la mfumuko wa bei.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu utakuja kuona mfumuko wa bei umekuwa
mkubwa sana katika hizi nishati za petroli, mafuta ya taa pamoja na vitu vinavyoambatana na
petroli. Kwa mfano kwa ripoti za BOT zinaonyesha kwamba kwa mwezi ule wa Oktoba na
Novemba mfumuko wa bei umepanda sana kwenye nishati hii ya mafuta na umeme kutoka
asilimia 6.2 kwenye asilimia 11.7. Sasa utakuja kuona kwamba hii ndio maana wakati mwingine inaleteleza tukitafsiri mfumuko wa bei inakuwa haieleweki kwa watumiaji hasa kule vijijini kwa
sababu utaona kwamba maeneo mengine kumekuwa na mfumuko katika rate ndogo, lakini hii
ukija kuchanganya kwa ujumla wake utakuja kuona unapata wastani wa nne nukta tano
mpaka nne nukta nane katika mwezi ule tu wa kutoka mwezi wa kumi kwenda mwezi wa kumi
na moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukizungumza juu ya hali ilivyo vijijini saa nyingine inaweza
isieleweke sasa nataka niseme kwamba upo umuhimu sasa wa Serikali kutazama eneo hili la
nishati ili kuweza kuudhibiti huu mfumuko katika maeneo haya ya nishati ili ule uwiano wa ujumla
ulete maana halisi. Kwa hiyo, nilikuwa naona hii ni sehemu muhimu sana kwamba Serikali iweze
kuiangalia. Kwa sababu ukiona upandaji wa gharama hizi za nishati za mafuta na umeme
zinasababisha ukuaji ambao uko shaghala bagala katika maeneo mbalimbali ya utumiaji kama
kwenye chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu nilikuwa najaribu kuangalia ripoti hii utaona
kabisa kwamba wakati mfumuko wa bei unapanda kwenye nishati hii, bei ya chakula inakuwa
ni shida. Nilikuwa najaribu kuona katika kipindi kirefu kwa mfano, nimeangalia kipindi cha mwezi
Mei mpaka Oktoba, 2016 hii ilikuwa imeshuka inflation katika eneo hili. Lakini kipindi kilichofuata
baada ya Oktoba kume-shoot sana katika nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali naishauri ijaribu kuangalia kwa sababu nishati
hii inavyopanda, bei ya chakula inapanda ukizingatia kwamba wananchi wetu sasa
kwasababu ya miundombinu iliyopo mjini sehemu ambayo kuna umeme kumekuwa na
uzalishaji wa vyakula na bidhaa nyingine zimekuwa bora zaidi. Kwa hiyo, wananchi wanauza
mazao yao yanakuja mjini halafu baadae yanarudi kwa ajili ya utumiaji kule; kwa hiyo
kunakuwa kuna athari kubwa ndio maana tunaona kwamba bei ya chakula inakuwa ni shida.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nizungumze eneo lingine kwa sababu natoka maeneo
ya uzalishaji wa chakula, umuhimu wa matumizi ya nishati yetu katika kutengeneza mbolea,
niishauri tu Serikali kwamba ilitazame eneo hili ili uzalishaji wa mbolea uwe kwa wingi ndani ya
nchi lakini pia wananchi tuweze kupata mbolea kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka pia nijue kwamba ule mradi wa kutengeneza
mbolea ya Urea ambao kulikuwa kuna majadiliano kati ya TPDC na wale Wajerumani umefikia
wapi kwa sababu sisi ndiyo matumaini yetu. Katika msimu huu hatukupata kabisa mbolea,
tulipata mbolea kwa ajili ya kilimo cha tumbaku, wakulima wa mahindi hawajapata mbolea
sasa na wananchi wameitika vizuri sana kutumia hizi pembejeo. Na kwa kweli inatia matumaini
kwa sababu sasa wananchi wanaweza kuzalisha hadi gunia 30 kwa eka kama watawezeshwa.
Kwa hiyo, nilitaka niisemee Serikali itazame uzalishaji wa mbolea kwa kutumia hizi nishati zetu za
gesi asili ili mbolea ipatikane kwa wingi wananchi waweze kupata mbolea na kuweza kufanya
uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kusaidia wachimbaji wadogo, maeneo
ninayotoka tuna maeneo ambayo wachimbaji wadogo wanachimba. Sasa ni ombi langu tu
kwa Serikali kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni isaidie kuweka mazingira
mazuri kwa wachimbaji wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu kwa kusema naunga mkono hoja hizi, Serikali iweze
kutusaidia tuweze kusonga mbele. Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye Muswada huu wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa mwaka 2016. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kutujalia afya, nimepata fursa hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Wizara, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam kwa kuja na muswada huu. Kwa kweli huu muswada umekuja ukiwa umechelewa, ulitakiwa uje wakati ule tunaanza kufanya reforms mbalimbali, kwa sababu unakuja sasa kutuondolea matatizo mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu unajaribu kutoa kielelezo cha utawala bora kwa sababu tutakapokuwa na Sheria hii ya Uthamini kuna mambo mengi yatakuwa kwa uwazi na itaongeza pia uwajibikaji katika usimamiaji wa hizi rasilimali ikiwemo ardhi, nyumba na assets nyingine ambazo zimetajwa kwenye sheria hii. Pia inaongeza dhana nzima ile ya ushirikishaji, kwamba inatoa fursa ya kushirikisha makundi mbalimbali. Kwa hiyo, nilifikiria nianze kwa kuipongeza sana Serikali kuja na muswada huu na nina uhakika kuna mambo mengi yatakaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niseme tu faida chache kwa sababu yapo mambo mengi sana, kutokana na muda niseme tu faida chache ambazo ninaona zitaenda kuondolewa na kuwa na muswada huu. Kwanza utaona kabisa kwamba ili kuweza kutoa ile risk iliyokuwepo kwenye assets zetu kwamba wakati mwingine kulikuwa kuna over valuation wakati labda rasilimali au mali za Serikali zikinunuliwa na labda wakati mwingine kulikuwa na undervaluation wakati mali za Serikali zikiuzwa. Kwa hiyo, hii itaenda kutibu na utaona kabisa kwamba kwenye ile section ya 49 inaonesha kabisa kwamba kutakuwa na vigezo vya ukadiriaji kwenye hizi rasilimali. Kwa hiyo, itatoa zike double standards ambazo zilikuwa zinajitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri wakati akiwasilisha hapa, inaenda tena pia kutupa faida kubwa ya kuweka vizuri ule uthamini wa mali na kupatikana kwa haki za wananchi hasa wanavyopata fidia. Utakuja kuona pia kwamba inatoa fursa sasa ya kuwa na assessment nzuri za kodi na ninaamini Wizara na maeneo mbalimbali yataenda kupata kodi iliyostahiki huku ikiwaacha pia wananchi waweze kulipa kile ambacho wanastahili kulingana na sheria hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo ambayo yalikuwa yanasumbua sana. Wananchi walio wengi wakati mwingine wamekuwa wakichelewa kupata mirathi kutokana na tatizo lililokuwepo. Sasa sheria hii inaenda kuondoa na kufanya urahisi wa kuweza kupata thamani hasa kwenye zoezi la usimamizi wa mirathi huko kwa wananchi wetu; lakini pia ku-facilitate zoezi la mauzo na manunuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa kilichokuwa kinanitia moyo, utaona lilikuwepo tatizo kubwa sana kwenye reporting framework ya hesabu zetu za upande wa Serikali. Utaona sasa hii inaenda kutibu, kwa sababu ukija kuangalia, siyo Tanzania tu, lakini nchi nyingi kuna tatizo la uthamini wa ardhi na nyumba, kuweza kuingia kwenye zile hesabu. Kwa hiyo, utaona kabisa kwamba huu ni mwanzo mzuri wa kuweza kufanya tuweze kuja kuwa na taarifa nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nimsahihishe kidogo msemaji aliyenitangulia kwamba tatizo la uthamini halijafika katika hatua hiyo katika Halmashauri zetu. Zoezi ambalo lilikuwa linafanyika kule alivyokuwa anzungumza hapa, hii ni stock taking, stock count ambayo ndiyo walikuwa wanafanya mara kwa mara, lakini walikuwa waniacha nje, zoezi la kuthamini mali kama vile ardhi pamoja na nyumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unaona kabisa kwamba kupitia sheria hii, tunaenda ku-improve ile reporting framework kuanzia kwenye Halmashauri zetu na pia kwenye Serikali Kuu, vilevile kwenye ile consolidation ya national wealth.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, muswada huu ni muhimu sana, utarahisisha. Kwa sababu ukiuangalia kwa upana, unatoa nafasi sasa wale ma-valuer ambao tulikuwanao kuanzia kwenye ngazi ya Halmashauri, sasa wanaenda kuwa authorized valuers, kwa sababu walikuwa hawajapata ile nguvu ya kuweza kufanya kazi yao. Kwa hiyo, ninaamini kwamba tutaenda kuwa na improvement kubwa sana kwenye hesabu zetu. Yapo mambo mengi yanaonekana hapa na zoezi zima ata kuhusu watu kupata haki kupitia Bima, lakini pia kikubwa itaenda kusaidia kwenye soko letu la hisa, soko la mitaji. Kwa maana hiyo, kwamba tunapokuwa tumefanya uthamini kwa maana ya kwamba zile kampuni zitakapokuwa zinakwenda ku-deal na hii biashara kwenye soko la mitaji au soko la hisa, kwa hiyo sheria hii inaenda kuweka ubora zaidi katika ku-facilitate ili soko liweze kuwa effective. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka tu nichangie kwenye suala zimala muundo wa huyu Chief Valuer. Nafikiri la muhimu hapa ni upande wa Serikali kuangalia ni namna gani sasa huyu Chief Valuer kumwezesha aweze kufanya kazi vizuri. Kwa sababu utakuja kuona kwamba nilitaka nitofautiane na msemaji aliyetangulia kwamba, kumfanya Chief Valuer awe kama CAG. Ni kwa sababu Chief Valuer ana Bodi. Kwa hiyo, la muhimu ni kuifanya hii Bodi iweze kufanya kazi vizuri. Bodi hii ikiwezeshwa itamwezesha huyu Chief Valuer afanye kazi vizuri. Muhimu ni hicho kwamba tumwone sasa huyu Chief Valuer anaweza kufanya kazi yake kwa nguvu tuweze kuwa na mali yetu iweze kujulikana kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nikubaliane kwamba Chief Valuer huyu ni mtu ambaye atasimama kwenye nafasi yake, ataweza kusimamia sekta mbalimbali, ni cross-cutting. Kwa hiyo, ipo umuhimu tu wa Serikali kuitazama ofisi hii ili itakapoanza kufanya kazi zake aweze kufanya kazi kwa uzuri na kwa haraka zaidi ili tuweze kuondoa yale mambo ambayo tuliyaona kama ni shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilitaka niseme kidogo kwamba nimevutiwa na kuwa na hii Bodi, kwa sababu utakuja kuona katika sehemu hii ya uthamini tunapokuwa na bodi; hii bodi ikifanya kazi kama tunavyoziona bodi nyingine kama NBAA, tumeona bodi inayoshughulikia hawa Maafisa wa Ununuzi, lakini tumeona pia hata kwenye upande wa sheria kwamba kabla watu hawajaenda ku-practice kipo chombo ambacho kinawa-regulate. Nimeona kwamba itakwenda vizuri kwa sababu inatoa fursa ya kwamba hawa wathamini kila wakati kuweza kufanya mitihani lakini pia ku-practice ili tuone kwamba wanaenda kufanya kazi nzuri. Utaona kabisa imeweka mamlaka ya bodi ili kuwa na labda na code of ethics, kuondoa ile hali ya uzembe. Kwa hiyo, yale yote ambayo yalikuwa yanaonekana kwamba kuna over valuation na under valuation yametajwa kwenye sheria hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona kabisa bodi hii inapewa fursa ya kusimamia miongozo mbalimbali ya ndani lakini pia miongozo ya Kimataifa. Kwa hiyo, utaona kabisa kwamba tumekuja sasa kuwa na chombo ambacho kitatufanya twende vizuri zaidi. Kwa hiyo, nataka niipongeze sana Serikali kwa kuja na sheria hii, lakini mimi ninaamini kabisa kuna mambo mengi yataenda kukaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho tu nilitaka nizungumzie pale kwenye usajili. Kwenye kile kifungu cha 26, ukikiangalia pamoja na kifungu cha 27, ili usajili wa hizi firm uzingatie kwamba mtu ambaye anaweza kwenda kusajili firm awe full registered, iwalazimishe hawa temporary registered na provisional ili waweze ku-team up na huyu ambaye yupo full registered ili firm ziweze kufanya vizuri. Nakushukuru kwa nafasi hii.