Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Elias John Kwandikwa (329 total)

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, barabara hii ambayo inaunganisha Mkoa wa Mara na Mkoa wa Arusha imetengewa fedha mwaka 2016/2017, shilingi bilioni 12. Tender ikatangazwa kuanzia mwezi wa Disemba, 2016, hivi ninavyoongea ni mwaka mwingine wa fedha bado mkandarasi hajapatikana. Wananchi wa Jimbo la Serengeti, wananchi wa Mkoa wa Mara na Arusha wanataka kusikia, ni lini compensation na ujenzi wa barabara hii utaanza?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa sasa kipande cha Barabara Nata – Mugumu hakipitiki, kimesababisha mfuko wa cement sasa hivi ni shilingi 22,000. Mna mpango gani wa kutengeneza kipande hiki kwa kiwango cha changarawe kwa wakati huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana na mimi kuwa Serikali inafanya juhudi ya kufanya barabara hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja ambayo inatoka maunganiko ya barabara kwenda Sanzate - Mugumu - Nata mpaka Arusha kama alivyotaja ina urefu wa kilometa 472.
Kwa hiyo, kwenye Awamu ya Kwanza barabara hiyo ya maunganisho imeshakamilika lakini sasa kwa eneo hili ambalo Mheshimiwa Mbunge anataja ni kweli kuna fedha zilitengwa katika mwaka 2016/2017, shilingi bilioni 20, hii ilikuwa ni sehemu ya barabara nzima, lakini kwa mwaka huu wa fedha pia kuna shilingi bilioni 17.397 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
Mheshimiwa Spika, hatua za ujenzi ni process, ni hatua ya tathmini na kulipa fidia ni hatua ya ujenzi wa barabara hii. Kwahiyo, baada ya tathmini ambayo imeshapelekwa, kiasi cha kama shilingi bilioni 4.1 ambazo zinahakikiwa kwa sababu zoezi la kuhakiki ni kujihakikishia kwamba malipo yanafanyika kwa uhalali, kumekuwa na matatizo kwenye utathmini, saa nyingine kumekuwa na rekodi ambazo sio sahihi, kwahiyo baada ya kukamilisha zoezi hili, process ya manunuzi itakuwa inakamilishwa na ujenzi utakuwa unaendelea kwenye awamu hii ya pili.
Mheshimiwa Spika, nitoe tu agizo kwa upande wa TANROADS, kama eneo hili halipitiki basi TANROADS Mkoa wa Mara waende waliangalie eno hili ili warekebishe maeneo wananchi waendelee kupita wakati hatua za ujenzi zinaendelea. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Niulize maswali mawili ya nyongeza, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, lakini kabla sijauliza niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuteuliwa kwake, vile vile kutokana na majibu mazuri ambayo yamelenga utekelezaji wa Ilani ya CCM kutatua kero za wananchi, kwa majibu haya nimefarijika sana, ni imani yangu kwamba tunakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa sababu eneo hili bomba la mafuta linapita nyuma ya Hospitali yetu ya Mji wa Makambako na linapita eneo la polisi pale na linapita kwenye maeneo ya wananchi kama ambavyo swali la msingi limesema.
Je, sasa kutokana na kwamba amesema atawatuma watu wa TANROADS ili waweze kwenda kuona na kushughulikia. Ni lini sasa hao watu wa TANROADS waende mapema ili kusudi kabla ya mvua za Disemba hazijaanza kunyesha ili kutatua kero ambayo ipo kwa sababu wananchi wanashindwa kupita na magari katika maeneo haya ambayo nimeyataja?
Mheshimiwa Mweyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuambatana na mimi baada ya kumalizika Bunge hili, ili akaone maeneo ambayo yametajwa katika maeneo hayo? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza pongezi zake nazipokea, lakini pia eneo hili linalopita bomba lina changamoto ipo. Pamoja na kuleta shida kwa wananchi kupita katika eneo hili, lakini pia ni hatari ndio maana niseme tu kwamba, nimeagiza mara moja sehemu hii iangaliwe, ili pia tuweze kuepusha hatari kwa sababu kama bomba linapita maeneo ya makazi na huu Mji wa Makambako ni mji ambao unakua kwa haraka, shughuli za kibinadamu nazo zimeongezeka, ili waangalie pamoja na kuona kama kuna hatari yoyote inaweza ikatokea, kitaalam tuweze kulisimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge. Nitatembelea Makambako ili pia nione hizi hatua za haraka zimechukuliwa na kwamba tatizo hili linaweza kumalizika. Ahsante.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishukuru sana Serikali kwa juhudi kubwa ya kujenga barabara nyingi za lami hapa nchini, lakini naomba nioneshe masikitiko yangu kuhusu uwiano wa barabara za lami hapa nchini, kwa sababu, tunajua baadhi ya wilaya zina barabara za lami vichochorini hadi katika vijiji mbalimbali. Katika mkoa wetu wa Manyara, hususan Wilaya za Kiteto, Simanjiro na Mbulu, hakuna barabara ya lami inayounganisha Makao Makuu ya Wilaya na Makao Makuu ya Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, labda tukiacha Wilaya ya Hanang ambayo kwa bahati imepitiwa na Barabara ya kutoka Singida, Babati, Arusha, tunaomba kwa kuwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kuna barabara ambazo Serikali imedhamiria kujenga; kwa nini Serikali isiweke kipaumbele kuhakikisha kwamba, barabara zilizoko kwenye Ilani ya Uchaguzi kwa kulenga zile Wilaya ambazo hakuna barabara za lami zinazounganisha makao makuu ya mkoa na Makao Makuu ya Wilaya? Kwa nini isitoe kipaumbele ikajenga barabara za lami, hususan lami kutoka Wilaya ya Kiteto – Kibaya hadi Makao Makuu Babati? Lami kutoka Mbulu hadi Babati na lami kutoka Simanjiro – Orkesmet hadi Babati? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nilipokee hili suala la kuangalia uwiano kama ushauri, lakini yako mambo ambayo lazima tuyatazame wakati tunakamilisha ujenzi wa barabara, kwa sababu eneo hili analolizungumza Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba kuna uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na mifugo. Mimi nilipata brief ya mkoa juu ya network ya barabara za Manyara na niseme baada ya Bunge hili pia nitakwenda kwa ajili kuangalia miradi inayoendelea, lakini pia kuweza kuona siku za usoni tuweze kukimbizia hii barabara iweze kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikiri tu kwamba, Serikali ya Awamu hii ya Tano imefanya kazi kubwa, kwa sababu barabara za lami zilizotengenezwa katika kipindi cha miaka miwili zenye urefu wa kilometa 1,500 si haba, kiasi cha shilingi trilioni 1.8 kimetumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yangu kukamilika kwa barabara hizi ni fursa pia, ya kwenda kushughulikia barabara nyingine ambazo tayari shughuli za upembuzi yakinifu zinaendelea, zitakapokamilika tuweze kwenda kujenga barabara hizi. Ahsante.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa hii niulize maswali mawili ya nyongeza na ninampongeza Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwamba kuanzia mwaka ule mlipatambua kwamba pana umuhimu wa kuwa na soko la kimataifa na ni ukweli ulio wazi kwamba sisi tuko mpakani na tumepakana kwa ukaribu na tunafanya biashara ya pamoja. Lakini huu mpango mliokuwanao wa masoko ya mpakani bado ni muhimu sana kutekelezwa katika maeneo haya ya Mnanila.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu niseme eneo tulilokuwa tumelitoa halikuwa na fidia yoyote. Sasa nataka kujua Wizara sasa itafanyaje kwa sababu umetuomba Halmashauri tuweze kuliweka kwenye mpango, lakini fedha zinazohitajika kujenga soko hili ni kubwa.
Je, Wizara itafanya nini sasa kuhakikisha kwamba, soko hili linajengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tumejenga soko lingine la mpakani ambalo liko maeneo ya Kijiji cha Nyamugali; tulikuwa na mpango vilevile Kibande na Kilelema, lakini tuna changamoto ya daraja sasa hivi kwenye Soko la Nyamugali ambalo Wizara yako ilijenga, ili watu wa Burundi waweze kuingia nchini. Je, Wizara iko tayari kutujengea daraja Nyamugali pale, ili wafanyabiashara waweze kupita kirahisi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Obama, kwamba suala la masoko ya mipakani ni suala muhimu na linaongeza tija katika uzalishaji na ukuzaji wa mazao ya viwanda ambayo Serikali yetu ndicho inachokisisitiza. Sasa kama ambavyo nimemueleza awali, ni kwamba nimuombe aweke uhitaji wa soko hilo katika bajeti ya halmashauri, na wakati huo kama tulivyoahidi tutaendelea kuwatafuta wahisani mbalimbali ili kuweza kusaidia ujenzi wa soko hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Daraja la Mto Kigale, kama sikosei ulivyotamka, ni kwamba kama ambavyo tunazidi kusisitiza kwamba biashara za mipakani kati ya nchi na nchi mbali tu ya kufanya shughuli za kibiashara zinajenga pia mahusiano na kuziwezesha nchi hizi mbili kuishi vizuri na kuondoa umaskini kwa pamoja. Kwa hiyo, mimi suala hilo nalichukua na litaendelea kufanyiwa kazi.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri hapa kwamba kutokana na jiografia yake kisiwa cha Mafia, kiwanja cha ndege ni muhimu sana katika kukuza uchumi. Lakini mimi nataka nimuongezee, kuna ziada pia masuala ya jamii. Hivi ukiwa Mafia ikifika saa kumi na mbili na ukapata dharura ya ugonjwa huna namna ya kutoka kwenda katika Hospitali ya Rufaa kwa sababu kiwanja hakina taa.
Sasa kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri kwamba usanifu na upembuzi ulishafanyika toka mwaka 2009 na leo ni miaka minane kwa hesabu za haraka bado unakuja kutuambia kwamba pesa hazija patikana?
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini hizi pesa zitapatikana ili ujenzi wa kuweka taa katika uwanja wa Mafia na jengo la abiria ufanyike?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara ya kurukia na kutua yani runway ya kiwanja cha Mafia ina mita kama 800 hivi, hivyo ndege kubwa haziwezi kutua na unasema kuna fursa za kitalii pale.
Je, ni lini sasa Serikali itaongeza urefu wa uwanja ule kwenda mpaka kilometa mbili ili kuruhusu ndege kubwa zitue moja kwa moja kutoka Ulaya na kuleta watalii Mafia? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ninapenda nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dau mjukuu wangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada anazozifanya ili kuhakikisha kwamba kisiwa cha Mafia kinachangia pia katika ukuaji wa uchumi Taifa, kwa maana ya kuleta maendeleo katika kisiwa cha Mafia.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi kwamba upembuzi yakinifu na kazi ya ukarabati wa uwanja baada ya usanifu ilishaanza, kwa sababu kazi iliyofanyika ya kupanua kiwanja na kukarabati ilikuwa ni awamu ya kwanza. Kwa hiyo, kuna awamu ya pili ambayo itafanyika kwa ajili ya kuhakikisha kwamba uwanja huu sasa unafanana na kwamba unatoa pia huduma. Kwa sababu Serikali tunapanua viwanja vikubwa kwa mfano Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa KIA, kwa maana hiyo na viwanja vingine vya Mikoani tunavyovifanyia upanuzi sasa vitakuwa na tija kwa kutoa huduma katika viwanja hivi vikubwa.
Mheshimiwa Spika, ni nia ya Serikali kufanya upanuzi, na mimi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Mafia kwamba kwenye awamu ya pili tutazingatia ushauri wake kwamba tuone namna ya kuvipanua vile viungio ili huduma ziweze kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, mimi nitahakikisha kwamba kwenye bajeti zinazokuja awamu hii ya pili tutaiwekea fedha ili huu uwanja wa Mafia uweze kufanana na hali ilivyo na kwamba tuweze kukuza utalii, lakini pia uweze pia kuweza ku-feed viwanja vikubwa ambavyo tunavipanua.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Dau mjukuu wangu usiwe na wasiwasi tutakuja Mafia na mimi nitahakikisha kwamba jambo linakwenda vizuri. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika majibu yake imesema kwamba upana huo wa mita 120 ni kwa mujibu wa Sheria ya Barabara ya mwaka 1932; sheria ambayo kwa sasa haipo, kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya Barabara ya mwaka 2007, kifungu cha 62.41 sheria hiyo ya mwaka 1932 ilifutwa. Kwa hiyo, tafsiri yake nini? Serikali ilifanya bomoa bomoa haramu, ambayo ni kinyume cha sheria. Sasa kwa kuwa Rais Magufuli akiwa Mwanza alitoa kauli ya kibaguzi yenye kueleza kwamba…
…nauliza swali sasa.
Nauliza swali, kwa kuwa Rais magufuli alitoa kauli ya kibaguzi yenye kuonesha kwamba wananchi wale wa Mwanza hawatabomolewa…
Swali ninalotaka kuuliza Serikali; kama Mheshimiwa Rais Magufuli si mbaguzi, Serikali itoe kauli hapa ya kuwalipa fidia wananchi wa Jimbo la Kibamba waliobomolewa kwenye barabara ya Morogoro.
Swali la pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu serikali imesingizia Sheria, mimi nilichukua hatua kama Mbunge Rais alipopiga Mbezi akasema kwamba kama Wabunge wanataka upana wa barabara urekebishwe wapeleke Muswada wa Sheria Bungeni nilileta muswada wa sheria wa marekebisho ili barabara yote iwe mita 60 lakini Serikali ikaa njama na Katibu wa Bunge aliyekuwepo Dkt. Kashililah kuzuia muswada huu. Ni lini sasa Serikali itaachana na hizi njama na itakubaliana na kauli ya Mheshimiwa Rais na muswada utaletwa hapa Bungeni ili barabara hii iwe na upana wa mita 60 kama zile barabara nyingine nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la barabara limeainishwa vizuri katika sheria kuanzia sheria niliyoitaja katika jibu la msingi, sheria ya mwaka 1932. Vilevile nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba iko pia Sheria Namba 27 ya mwaka 1959, ipo Sheria Namba 40 ya mwaka 1969, pia iko Sheria Namba 13 ya mwaka 2007.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hizi zilivyokuwa zikitungwa zilikuwa zinatazama maendeleo ya barabara siku za usoni na wala siyo siku za nyuma na ukizisoma sheria hizi zilikuwa zinaainisha barabara. Kwa mfano hii sheria ya mwaka 1932 ilitaja kabisa barabara kutoka Dar es Salaam kwenda mpaka Ruvu na maeneo gani yawe na ukubwa gani, eneo lipi liwe na ukubwa upi kwa ajili ya kuzingatia maendeleo na ukuaji wa shughuli za kibinadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimshauri Mheshimiwa Mnyika, ziko taratibu za kuhakikisha kwamba kama kuna barabara inatakiwa itajwe na kufanyiwa maboresho ziko taratibu zinaanzia katika Halmashauri na Mamlaka ambazo zinasimamia barabara. Atumie fursa hiyo kuwasiliana na mamlaka yake upande wa Serikali ya Manispaa ya Kibamba ili kweza kuleta maombi. Na kwa hii Sheria Namba 13 inampa nafasi Mheshimiwa Waziri kupitia maombi kutoka kwenye mamlaka zinazosimamia barabara kuona kama kuna eneo linaweza likafanyiwa jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hakuna njama yoyote na suala la fidia itakwenda kwa mujibu wa sheria.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana ambayo ameyatoa hivi punde. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninayo majibu machache tu ya nyongeza. Kwa mujibu wa kanuni zinazoendesha Bunge sehemu ya Nne ya kanuni zetu zinaonesha mpangilio wa shughuli katika Bunge letu. Sehemu ya Tano ya kanuni zetu inaonesha mpangilio wa namna majadiliano yatakavyofanywa ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa faida ya Watanzania, si kweli, si kweli, si kweli kwamba Serikali ilikula njama na Ofisi ya Bunge ili kuzuia muswada wowote ambao uliletwa katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo, ili kuweka majibu ya Serikali vizuri katika swali la nyongeza la Mheshimiwa Mnyika tunaomba tulieleze Bunge lako Tukufu kwamba swali la nyongeza lililoulizwa na Mheshimiwa Mnyika si swali ambalo lina tafsiri ya ukweli wa hali halisi iliyojitokeza katika muswada wake, na Bunge hili linaongozwa kwa kuzingatia kanuni na taratibu na sisi Serikali hatuna utaratibu wowote wa kula njama na Bunge hili.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali na kuipongeza kwa kuanza ujenzi wa barabara ya Mbande – Kongwa – Mpwapwa kwa kiwango cha lami. Naamini mwaka ujao wa fedha barabara hii itakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali; kwa kuwa mji wa Dodoma na viunga vyake unakua kwa kasi sana kutokana na Serikali kuhamia Dodoma, na kwa kuwa tusingependa mji wa Dodoma ukawa na msongamano kama Dar es Salaam; je, Serikali iko tayari na ina mkakati gani madhubuti wa kuhakikisha kwamba barabara za mzunguko katika mji huu zinaanza kujengwa kupunguza Msongamano unaoweza kuwepo mji utakapokua?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, ni lini Serikali itajenga barabara nyingine baada ya barabara iliyokuwa inatoka Shabiby Petrol Station na Area D kufungwa kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege na sasa wananchi wa Area D, Mlimwa, Majengo Mapya na maeneo mengine wanazunguka mpaka Swaswa ndipo waje mjini, je, ni lini barabara hiyo itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba Dodoma ndiyo makao Makuu na mpango mzima wa kuhamia Dodoma unaendelea. Pia Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha barabara zake ili kuondoa usumbufu ambao unaweza kujitokeza kutokana na ukuaji wa mji wa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeshaweka mkandarasi kwa ajili ya usanifu wa barabara za mzunguko za Dodoma ambazo zitakuwa na ukubwa wa kilometa 96. Tulitenga fedha kiasi cha shilingi 959,812,000 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba usanifu unakamilika; na usanifu wa barabara za Dodoma utakamilika mwezi wa tano mwaka 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua iliyofikiwa sasa hivi tuko zaidi ya asilimia 25 ya zoezi la usanifu na mimi ni wito wangu tu kwa maana kwamba hii kazi isimamiwe vizuri na upande wa TANROADS iliusanifu ukamilike ikiwezekana mapema kabla ya muda huu ili harakati za kutafuta fedha na kujenga barabara za mzunguko wa Dodoma ziweze kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, tunatambua usumbufu ambao unajitokeza na sasa hivi pia tunaona kuna foleni zimeanza kuonekana. Hii barabara anayoitaja Mheshimiwa Mbunge ambayo inaleta usumbufu kwa wakazi la eneo la Area D, Mlimwa na Majengo Mapya kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema ninatambua urefu wa kilometa kama mbili; barabara hii mawanzoni ilikuwa inasimamiwa na CDA kabla haijavunjwa. Kwa hiyo, upande wa Serikali tumechukua jukumu la kuhakikisha sasa kipande hiki cha barabara kinatengenezwa haraka ili Waheshimiwa Wabunge wakiwa Dodoma pamoja na wananchi wa Dodoma kwa ujumla wasipate shida kutokana na shida ambayo imejitokeza baada ya ujenzi wa uwanja ule wa ndege kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo zoezi la kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha kipande hicho pamoja na kusimamia maeneo ambayo yametengewa fedha kwa tija tutapokuwa na balance kidogo imebakia tutaanza kupeleka eneo lile ili barabara iweze kujengwa, Ahsante.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwanza nianze kuwapongeza Mawaziri na Manaibu Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya, Mheshimwa Rais amewaona ninyi na sisi Wabunge wenzenu tuna imani na ninyi katika kutatua kero za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize swali la nyongeza. Wakati wa Kampeni za Uchaguzi Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliahidi ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, barabara inyoanzia Wilayani Namtumbo katika vijiji vya Mtorapachani, Ligusenguse na kuelekea Mchoteka na Lasi hadi Tunduru. Naomba nijue ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa ufupi kabisa tunaratibu ahadi zote za Mheshimiwa Rais, ahadi zote za Makamu wa Rais kwa maeneo ambayo yanahusu ujenzi wa barabara. Nimuahidi tu kwamba katika kipindi cha miaka mitano hivi zoezi hili litakuwa linaendelea kukamilisha barabara zote zilizoko kwenye ahadi, ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa wananchi hawa walifanyiwa tathmini ya muda mrefu mpaka sasa hawajalipwa, nataka kujua, je, ni lini Serikali sasa itawalipa wananchi hawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa wananchi hawa walifanyiwa tathmini muda mrefu ya nyumba zao na wameshindwa kuziendeleza na kufanya maendeleo. Je, Serikali iko tayari kuwaongezea tathmini ya fidia ili walipwe kiasi kikubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia maendeleo mbalimbali kwa wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kwamba hivi karibuni Mheshimiwa Waziri alitembelea eneo hili walizungumza na alipata pia taarifa kwamba muda siyo mrefu, wakati wowote wananchi watalipwa hizi fidia. Kwa hiyo, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge avute subira wakati wa hatua za kukamilisha ili tuweze kuwalipa wananchi wale na ujenzi uweze kuanza basi avute tu subira na wananchi wa Sumbawanga nawashukuru kwa uvumilivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kulipa kwa ziada inategemea na sheria yenyewe na utaratibu wenyewe. Kwa hiyo, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge labda kama kuna suala la ulazima basi tuzungumze tuone kwamba je, wanastahili kulipwa ziada kutokana na kuchelewa au iko katika hali gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. KEMIREMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhimu wa daraja hili na kuagiza lijengwe haraka iwezekanavyo. Pamoja na hayo, kumekuwa na tatizo kubwa sana ambalo linatengeneza usumbufu mkubwa sana kwa wananchi kutokana na ubovu wa meli zilizopo. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kurekebisha vyombo hivi wakati tunasubiri ujenzi huo wa daraja? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu mara nyingi tumezungumza juu ya changamoto mbalimbali ambazo zinawapata wananchi ambao wanavuka kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu tunafuatilia sana matatizo ambayo yapo hapa kutokana na hivi vivuko vipo, najua vipo vivuko vikubwa vitatu lakini iko changamoto ambayo vikiharibika vinasababisha usumbufu mkubwa sana kwa wananchi wa pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme tu matatizo haya pia yanachangiwa na wananchi wenyewe. Nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge tushirikiane kuwaomba sana wananchi katika maeneo haya hasa wavuvi, wanavua katika maeneo haya ya kivuko, matokeo yake zile nyavu zinanaswa na vivuko hivi na mara nyingi inasababisha uharibifu wa vivuko hivi ambavyo vinafanya kazi pale. Kwa hiyo, niombe tu wananchi tushirikiane na tusimamie jambo hili ili wananchi wasije wakaendelea kuvua maeneo haya ya karibu ili vyombo hivi vifanye kazi kwa efficiency. Kwa hiyo, nasisitiza tu kwa upande wa wenzetu wa TEMESA, wasimamie vizuri wakati harakati za ujenzi wa kivuko zinaendelea. Baada ya ujenzi naamini kwamba usumbufu utakuwa umeisha lakini pia itachangia sana katika ukuaji wa uchumi wa maeneo hayo na Tanzania kwa ujumla.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashindwa kuelewa wananchi wa Mkoa wa Singida tumeikosea nini Serikali hii. Toka miaka ya 1970 uwanja huu ulipojengwa, haujawahi kufanyiwa maintenance ya aina yoyote, uwanja ni pori, hauna fence, imefikia hatua wananchi wameanza kupima viwanja na kujenga nyumba zao. Nataka commitment ya Serikali very seriously, ni lini mnakwenda kujenga uwanja wa ndege Mkoa wa Singida? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa umeme wa upepo Singida umewashinda, treni inayokwenda Singida kwa sasa hivi imeshakufa, ujenzi wa vyuo vikuu Singida umeshawashinda, aiport Singida imeshawashinda. Je, hii ndiyo fadhila mnayowalipa wananchi wa Mkoa wa Singida pamoja na wao kuwa champions kutoa kura kwa Chama cha Mapinduzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, utakubaliana na mimi kwamba kwa commitment hii Serikali iliyoifanya kwa ajili ya ujenzi wa viwanja mbalimbali kama nilivyojibu katika swali la msingi ni kuonesha namna Serikali hii ilivyo serious kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa viwanja mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii tu kuwaonya wananchi ambao wanakwenda kujichukulia maeneo hayo na kujipimia viwanja, kwa sababu sio sahihi, wanavunja sheria na sheria itachukua nafasi yake. Kwa hiyo, waache uwanja huu wazi ili taratibu zikamilike tujenge uwanja huu, wananchi wa Singida na Watanzania kwa ujumla waweze kupata huduma kupitia uwanja huu.
Swali lake la pili, Serikali haijashindwa, kwa fedha ambazo ziko committed kwa viwanja vyote ambavyo tunaendelea kufanya matengenezo ni kuonesha Serikali ya Awamu ya Tano iko serious. Kuna fedha karibu shilingi trilioni moja imetumika kwa ajili ya marekebisho ya viwanja vikubwa na niwaalike Waheshimiwa Wabunge wanavyopita maeneo kama ya KIA waone matengenezo yanayoendelea, wanavyopita Dar es Salaam waone namna tunavyouboresha uwanja ule na maeneo mengine, wakienda Shinyanga waone shughuli zinavyoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba Serikali iko serious, hatujashindwa, tunaenda kutengeneza viwanja, tunakwenda kuwahudumia wananchi na Mheshimiwa Kishoa asiwe na wasiwasi.
Suala hili nimuombe tu awe mvumilivu kwa sababu wapo Mheshimiwa Mlata, Mheshimiwa Kingu, wamekuwa wakija kuulizia juu ya uwanja huu kuonesha namna Serikali ya Chama cha Mapinduzi imejipanga kisawasawa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na hatua kubwa inayochukuliwa na Serikali yetu.
Je, kutokana na gharama kubwa inayotumika ya matengenezo ya kawaida katika barabara hii inayounganisha mikoa minne kwa kiwango cha changarawe na kwa kuwa katika majibu ya msingi Mheshimiwa Waziri hakueleza mkataba huu unaisha lini, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuharakisha kazi hii ya usanifu ili barabara hii ipate kutengenezwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Mheshimiwa Rais aliahidi ahadi nyingi wakati wa kampeni kama sehemu ya utatuzi wa changamoto za wananchi. Katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu aliahidi kilometa tano kwa barabara ambazo zinamilikiwa na Serikali za Mitaa wakati ule. Kwa kuwa sasa barabara zile zimehamia kwa TARURA, je, ni nani atakayetekeleza ile ahadi ya kilometa tano katika barabara zile kwa kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa sasa haziko tena kwenye utaratibu wa kuzihudumia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia sana hii barabara muhimu ambayo inaunga mikoa mingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba kwanza barabara hii pia inafuatiliwa na Waheshimiwa wa mikoa hii. Mheshimiwa Flatei Massay naye anaifuatilia sana barabara hii tumezungumza, lakini wako Wabunge wa Mkoa wa Singida, wako Wabunge wa Simiyu wanafuatilia hii barabara muhimu sana. Na sisi upande wa Serikali, ili kuharakisha ujenzi wa barabara hii, tumeanza ujenzi katika Mto Sibiti, sehemu ambayo ilikuwa ni mbaya sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba kwa sasa kwanza wananchi wanapita. Wakipita katika barabara hii kwa mtu ambaye anaenda Karatu tuna-save zaidi ya kilometa 400, kwa mtu anayekuja Singida tuna-save zaidi ya kilometa 200; tuna-save muda, lakini pia tuna-save gharama mbalimbali.
Mheshimiwa NAibu Spika, ili kuharakisha ujenzi wa barabara hii, Serikali imechukua hatua kuhakikisha kwamba ujenzi wa daraja utakapokamilika mwishoni mwa mwaka huu, tutakuja kwenda haraka katika ujenzi wa barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ahadi za kilometa tano, ninajua kwamba nchi nzima ziko ahadi ambazo sisi kama Serikali tunaendelea kuzitekeleza, ikiwepo ahadi ambayo imetolewa huko Mbulu.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira, tumejipanga tunaendelea kuratibu kuona kwa kiasi sasa tunapoenda nusu ya kipindi cha miaka mitano tumetekeleza ahadi ngapi ili tuweze kukamilisha ahadi hizi ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira. (Makofi)
MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii na nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Natambua juhudi za Serikali zinazofanyika kwa kuunganisha Mkoa wa Simiyu na Mikoa jirani ya Singida na Arusha. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ningependa kufahamu kama huo mpango mkakati wa miaka mitano alioutaja Mheshimiwa Waziri, unashabihiana vipi na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 na 2020?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019 kuingiza sehemu ya barabara hiyo ya Moboko – Mwandoya – Kisesa - Bariadi kwa upande wa Mkoa wa Simiyu; na mto Sibiti – Mkalama – Nguguti - Iguguno na Singida ili sehemu hizi mbili za barabara hii muhimu ziweze kufanyiwa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Chenge kwa namna ambavyo anapigania hii barabara iweze kujengwa, lakini kwa maendeleo kwa ujumla katika Mkoa huu wa Simiyu.
Vilevile niseme kwamba barabara hii ambayo anaizungumza Mheshimiwa Chenge ni muhimu sana kwa mikoa mingi ikiwemo Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara kwa sababu barabara hii itakapojengwa itawezesha watu wote katika mikoa hii ninayoitaja kupita na kupunguza umbali katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kama alivyosema katika swali lake la kwanza, kwamba katika mpango wa miaka mitano, tunashughulikia hii kwa sababu imetajwa pia katika ilani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Mheshimiwa Andrew Chenge mwenyewe anafahamu kwamba tumeshaanza ujenzi katika Mto Sibiti na kazi hii itakamilika mwishoni mwa mwaka huu na ule utaratibu wa uratibu wa usanifu wa barabara hii, fedha nyingi sana zimetengwa. Zimetengwa Euro milioni 2.8 ili kuweza kukamilisha kazi hii. Niseme tu kwamba ili kazi ikamilike kuendana na kipindi hiki cha miaka mitano na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, ziko consultancy nne ambazo zimeungana pamoja ili kuhakikisha kazi inakamilika kwa haraka. Kwa hiyo, utekelezaji wa Ilani utakwenda sambamba na kazi kubwa sana ambayo inaendelea kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu kuingiza hii sehemu kwenye usanifu katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha, ushauri wako huu muhimu nauchukua ili wakati wa process ya bajeti hii inaendelea, tulifanyie kazi itakapowezekana, tutaweka fedha ili kuanza usanifu wa vipande hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande hiki cha barabara kutoka Mkalama kwenda Singida, iko barabara nyingine ambayo inatoka upande wa Sibiti, inapita Msingi kwenda Ulemo hii pia itawezesha watu wa maeneo yale waweze kupita kiurahisi wakitokea Mkoa wa Simiyu.
Mhesimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa wananchi wa Meatu, Simiyu watakuwa na access nzuri kwenda kutibiwa Haydom. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tunatambua umuhimu wa barabara hii na ndiyo maana tumeiweka katika ilani na tutaitekeleza ili wananchi waweze kupata manufaa makubwa zaidi. Ahsante.
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina tatizo kuhusu barabara hii kupitia kwenye milima, tatizo langu ni uwepo wa sheria kwamba kama nilivyozungumza kwenye swali langu la msingi, mji huu wa Newala upo tangu mwaka 1800; kama wakati ule ilikuwa inaitwa Dutch East Africa. Hii sheria ya mwaka 2007 imekuta wananchi wale wakiwa na taasisi zile katika uwepo halali. Kuna polisi, mabenki na wananchi, maana yake walikuwepo kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake wanachopinga wao ni kwamba hii sheria imewakuta wao wakiwepo kisheria. Kwa hiyo, swali langu la msingi, je, ni lini TANROADS watafanya mazungumzo na wananchi hawa wa Newala ili tukaondoe kesi ile Mahakamani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kutokana na ufinyu wa Mji wa Newala, je, sasa TANROADS wako tayari badala ya kupitisha ile barabara Newala Mjini, wapitishe Kiduni hadi Nambunga kwa Mheshimiwa Mkuchika ili kuepuka mrundikano wa barabara katika ya mji?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, anafuatilia sana maendeleo ya Newala na anajua eneo hili ambalo analizungumza pia ni maarufu sana kwa uzalishaji wa korosho.
Kwa hiyo, namuahidi kwamba sisi Serikali tuko tayari kwenda kufanya mazungumzo na ninampongeza sana kwa nia yake thabiti ya kuhakikisha kwamba kama shauri hii tunalimaliza, itaharakisha pia ujenzi wa barabara. Kwa hiyo, tuko tayari kuzungumza ili tulimalize ili wananchi hawa waweze kupata haki zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa ule utaratibu ambao wanafikiria, na mimi eneo lile nilitembelea, ni kwamba tukiweza kupitisha bypass kwenye eneo hilo, tutaweza pia kuufanya mji upendeze lakini pia kupanua huduma, kwa hiyo, tutakuwa tuko tayari kuhakikisha kwamba tunarekebisha michoro na saa nyingine wananchi waweze kupata haki zao. Ahsante. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli huyu mshauri yuko site na kazi hii inaendelea, lakini nina swali moja la nyongeza. Kwa sababu barabara hii ilivyo sasa katika Miji ya Bukene na Itobo inapita katikati ya miji na kwa mfano Bukene ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami tutalazimika kuvunja Kituo cha Afya, jengo la Polisi, tanki kubwa la maji, ma-godown makubwa na kuvunja nyumba nyingi tu cha wananchi.
Je, Serikali itakuwa tayari kutoa kauli itakayoondoa hofu na itakayofanya kuepusha fidia kubwa kwamba usanifu huu ujumuishe kuichepusha barabara hii katika miji ya Bukene na Itobo ili isipite katikati ya Miji ya Bukene na Itobo ili kuondoa kwanza fidia kubwa ambayo itatokea baada ya kuvunja taasisi nyingi hizi na nyumba nyingi za wananchi?
Je, Serikali iko tayari kutoa kauli ili wananchi wa Bukene na Itobo wawe hawana hofu kwamba barabara hii itachepushwa pembeni ya miji hii na kuondoa gharama zote hizi ambazo zitajitokeza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifuatilia sana hii barabara ambayo inatoka Tabora - Mambali kuja Itobo. Niseme tu kwamba upo utaratibu kwa upande wa Serikali wa kuangalia hizi gharama wakati tukisanifu hizi barabara. Kwa hiyo, niseme kwamba tutazingatia ushauri wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo jambo geni kwa sababu zoezi hili tumelifanya katika Mji wa Nzega, kuna mchepuo; tumefanya katika Mji wa Urambo, kuna mchepuo; lakini pia tumezingatia tulivyosanifu barabara ya kule Kasulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikutoe wasiwasi na niwatoe wasiwasi wananchi wa Bukene kwamba tutazingatia wakati tunakamilisha zoezi la usanifu wa barabara.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Changamoto za Jimbo la Bukene zinafanana na changamoto za Jimbo la Karagwe. Kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kuweka mpango wa kuweka lami barabara ya kuanzia Karagwe kwenda Benako - Ngara na barabara ya kuanzia Karagwe kwenda Murongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mipango hii mizuri ya Serikali wananchi wanaoishi katika barabara hizi wamesubiri fidia kwa muda mrefu, je, ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi wa Karagwe wanaopakana na barabara ya Karagwe - Benako na Mugakorongo - Murongo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amefuatilia sana barabara za Karagwe na anafahamu kwamba ziko barabara nyingi ambazo zinaunganisha nchi yetu na nchi ya jirani ambazo ziko kwenye mpango wa ujenzi wa lami. Hii ni pamoja na juhudi zake Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampongeza sana na na sisi kama Serikali tunaendelea kushirikiana naye kuhakikisha kwamba wananchi wa Karagwe wanapata huduma hii ya barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili suala la fidia, tunategemea tutakapopata fedha tutaweza kulipa mara moja. Kwa hiyo, namuomba tu Mheshimiwa Mbunge labda baada ya kikao hiki tuwasiliane ili tuzungumze ofisini tuweze kuona hatua gani tumefikia ili aweze pia kuwapa taarifa wananchi wa Karagwe juhudi ambazo tumefikia upande wa Serikali. Kwa hiyo, tuonane tutalizungumza suala hili.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuuliza swali ndogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wilaya ya Kilolo ni Wilaya ambayo ina matatizo makubwa sana ya miundombinu na kupelekea usafiri wa magari usiwepo, kwa hiyo, mawasiliano pekee tuliyokuwa tunategemea, ni simu.
Sasa kuna vijiji ambavyo havina kabisa mawasiliano na hivyo kupelekea watu kupata shida na hata kupoteza maisha. Kwa mfano, Masisiwe, Ilambo, Magana, Mdaila, Kising’a, Masege na Uruti, hakuna kabisa. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri, hebu unawaambiaje watu wa Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Serikali ilitambua kata zenye uhitaji wa mawasiliano 443.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya kata hizo, tayari tumeshapeleka huduma za mawasiliano kupitia mkataba wa Serikali ya Viatel, ambao ndiyo wanatoa huduma za Halotel.
Pia mtambue kwamba Kata 75 ambazo zina vijiji 154 zinatakiwa ziongezwe kwa ajili ya kufikishia mawasiliano itakapofika Juni, 2018 .
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba moja kati ya kata hizo na vijiji alivyovitaja, vitakuwemo kwenye mpango wa kupelekewa huduma za simu itakapofika Juni, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Venance Mwamoto, kama ana mashaka niko tayari kwenda naye Jimboni kwake kwa ajili ya kuendelea kuhakikisha kwamba wananchi wa Kilolo ambako bahati nzuri nimeshafika, tena zaidi nilifika kwenye kijiji chake cha Masege, wanapata huduma ya mawasiliano. (Makofi)
MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ziara yake Wilayani Ngorongoro mwaka jana aliahidi nyongeza ya kilometa 50 kwenye ujenzi wa barabara unaoendelea. Je, ahadi hii itatekelezwa lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 – 2020 imeainisha ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 65 kutoka Sanya Juu hadi Longido; ni lini ujenzi wa barabara hii utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze sana Wabunge wa Chama cha Mapinduzi waliopo Mkoa wa Arusha, ninatambua juhudi nyingi wanazozifanya ili kuhakikisha miundombinu ya barabara katika mkoa inaimarika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza sana Mheshimiwa Olenasha kwa sababu amefuatilia barabara hii ya Loliondo – Mto wa Mbu, na mimi niseme tu kwamba tutaendelea kuhakikisha kwamba barabara zinajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri Mkuu alitembelea Loliondo na aliahidi ujenzi wa barabara ya nyongeza kwa kilometa 50, kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili tunalishughulikia na tunaangalia kadri itakavyowezekana katika bajeti hii inayokuja nyongeza ya hii barabara tutaendelea kujenga. Kwa sababu barabara hii inayo urefu wa kilometa 218 kwa hiyo karibu asilimia 25 sasa barabara hii inajengwa, sasa tukiendelea kuongeza tutapata asilimia 50 na hatimaye barabara hii itakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, barabara hii ya Sanya Juu hadi Longido imetamkwa katika Ilai ya Uchaguzi, na niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako Tukufu kwamba tunaendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na tuna kipindi cha miaka mitano nah ii barabara tutaitazama katika bajeti zinzaokuja ili tuhakikishe ahadi za Chama cha Mapinduzi na tuna kipindi cha miaka mitano nah ii barabara tutaitazama katika bajeti zinazokuja ili tuhakikishe ahadi za Chama cha Mapinduzi zinatekelezwa kikamilifu. Ahsante. (Makofi)
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi yetu ya Tanzania kuna baadhi ya barabara za lami zimejengwa chini ya kiwango, kwa mfano barabara ya Chalinze hadi Mlandizi.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kuzikarabati barabara hizi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J.KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu barabara hii imekuwa ni barabara ya siku nyingi, barabara hii ilijengwa kwa kiwango kizuri, lakini kwa sababu haikudumu kwa muda mrefu na matumizi ya barabara yameongezeka kwa maana ya kupitisha magari mengi na mizigo, kwa hiyo barabara imechakaa. Serikali inao mpango wa kuifanyia matengenezo makubwa barabara hii ili iweze kuwa imara zaidi.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kibena – Lupembe – Madeke, kilometa 126 ni barabara pekee ambayo inaunganisha Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Morogoro kupitia Mlimba. Barabara hii mwaka wa fedha 2016/2017 ilitengewa fedha, mwaka 2017/2018 ilitengewa fedha lakini mpaka leo hii haijaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.
Nataka kupata kauli ya Serikali, ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuweza kuokoa uchumi unaopotea kule Lupembe na Mkoa mzima wa Njombe kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J.KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Hongoli kwa sababu amekuwa akiifuatilia sana hii barabara, na hii barabara ni muhimu sana inapita sehemu ambazo zina uzalishaji mkubwa lakini pia ni kiungo kikubwa cha wananchi wa Njombe na wananchi wa Morogoro, na tumezungumza juu ya ujenzi wa hiyo barabara, barabara hii imeshasanifiwa. Kwa hiyo niseme ujenzi wa kiwango cha lami umeshaanza kwa sababu baada ya usanifu wa barabara hizo ndiyo harakati za kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge, kwa vile barabara hii ilikuwa imetengewa fedha na Serikali ilikuwa inaendelea kupata fedha mara tu fedha zikipatikana ujenzi wa barabara hii utaanza mara moja. Naomba tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Njombe wawe na matumaini, wawe na imani na Serikali, inatafuta fedha na itaendelea kujenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na niliambie tu Bunge lako Tukufu kwamba kila mwezi tunatumia fedah nyingi sana kulipa certificates zinazotoka, takribani bilioni 80 zinalipwa kila mwezi, kwa hiyo hii ni ushuhuda kwamba Serikali inafanya kazi kubwa kuhakikisha kila wakati, kila siku barabara tunaendelea kuziboresha na kuzijenga. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Lushoto kwenda Mlalo, lakini pia kutoka Mlalo kwenda Bombo Mtoni hadi Maramba ni ya muda mrefu sana na inakuwa inajengwa kwa kiwango cha kilometa mbili mbili kila mwaka. Je, ni lini sasa Serikali itaweka nguvu ili barabara hii ya kutoka Lushoto - Mlalo na kutoka Mlalo kwenda mpaka Maramba ijengwe kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J.KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Shangazi amekuwa akifuatilia sana barabara pamoja na maendeleo mbalimbali katika Jimbo la Lushoto. Ninatambua mahitaji ya barabara katika maeneo haya ambayo ameyataja maeneo ya kiunganishi cha Lushoto - Mlalo na ile barabara ya Mlalo kupita Maramba kwenda Mkinga na Mheshimiwa Kitandula amekuwa akifuatilia hii.
Kwa hiyo, kama nilivyojibu pale awali kwamba tunaendelea kutafuta fedha kama Serikali inavyokusanya fedha vizuri tutaendelea kujenga barabara mbalimbali. Kwa hiyo, niwaombe tu wananchi wa Mlalo, Maramba Mkinga na wananchi wa Lushoto kwa ujumla na watanzania wote kwamba waendelee kuvuta subira tu kadri fedha zinavyopatikana tutaendelea kuboresha barabara zote nchini ili ziweze kutoa mchango mkubwa katika ujenzi wa uchumi wa nchi yetu.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Mbozi ambayo ni Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe inapakana na Wilaya ya Songwe lakini Wilaya hizi mbili hazijaunganishwa kwa barabara na hivyo wananchi wa Wilaya ya Songwe hulazimika kupita Mkoa mwingine wa Mbeya kupitia njia ya Mbalizi kwenda Makao Makuu ya Mkoa ambayo yako Mbozi.
Naomba sasa kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini Wilaya ya bozi na Wilaya ya Songwe zitaunganishwa kwa barabara ili kuwasaidia wananchi wa maeneo haya yote mawili kuweza kurahisisha mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J.KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mbunge nikupongeze tu kwa kufuatilia na unajua umuhimu wa barabara ina mchango mkubwa sana kwenye maendeleo. Kwa vile sijapata fursa ya kutembelea wa Mbeya mimi napenda tu nilichukue hili ni jambo la kufanyia kazi na mimi nitatembelea Mbeya ili niweze kufika maeneo haya ili tuweze kushauriana vizuri na Mheshimiwa Mbunge wakati Serikali inafanya harakati za kufanya makusanyo na kuboresha barabara nchini. (Makofi)
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza niipongeze Serikali kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Mto wa Mbu lina linalingana kabisa na tatizo la Mji wa Mombo. Mji wa Mombo toka Awamu ya Nne ulihaidiwa na Serikali kwamba utajengwa kiwango cha lami kilometa moja na nusu, na wataalam walienda pale wakapima na wakachukua sample ya udongo, lakini cha kushangaza mpaka leo hii barabara hile ya Mji Mdogo wa Mombo haijafanyiwa utafiti wala haijafanyiwa chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini tamko la Serikali kuhusiana na Mji Mdogo wa Mombo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J.KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana na mimi kwamba amekuwa akilifuatilia suala hili na tumezungumza naye. Nitumie tu nafasi hii nimuelekeze Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga ili aweze kuharakisha zoezi la kusanifu eneo hili ili sasa tuweze kujenga na kuboresha kama ilivyo kwenye ahadi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwanza kabisa nianze kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa mapokezi makubwa kabisa ya ndege ya Bombadier ambayo jana ilitua na Mheshimiwa Rais akiwa anaongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili pia niipongeze Serikali kwa kuanza sasa kujenga kiwanja chetu cha Nduli kwa sababu nina imani kabisa sasa hata utalii utafunguka katika Mkoa wetu wa Iringa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ndege ya Bombadier ina uwezo wa kutua katika kiwanja chenye urefu wa kilometa 1.2 na kiwanja chetu cha Nduli kina urefu wa kilometa 1.6, tatizo ni kipande tu kidogo cha mita kama 100 ambacho ni kibovu sana ambacho hakiwezi ndege kubwa kutua na hata zile ndege ndogo ambazo zinatua, zinatua kwa matatizo makubwa sana na mpaka sasa hivi kiwanja chetu kina abiria karibu 20,886,000. Je, Serikali sasa haioni umuhimu sasa wa kujenga hicho kipande kidogo cha mita 100 ili tuweze kupata ndege kubwa na hizo ndogo zipate kutua vizuri wakati tunasubiri huo ujenzi wa kiwanja hicho, kwa ufadhili wa Benki ya Dunia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; nimesikia tayari zoezi la uthamini wa mali limeshaanza katika kiwanja chetu cha Nduli. Hofu yangu kubwa ni kwamba zoezi hili huwa linafanyika mapema kabisa lakini huwa linachukua muda mrefu sana kwa wananchi kulipwa mali zao, nina mfano halisi kabisa wa kiwanja cha ndege cha Songea ambacho toka mwaka 2010 karibu miaka nane bado hawajalipwa na vilevile hata barabara yetu ile ya mchepuo ilichukua karibu miaka sita mpaka wananchi kuanza kulipwa. Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kuwa wananchi hawa ambao wanapisha hiki kiwanja wanalipwa mapema zaidi? Mheshimiwa Naibu Sika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nizipokee pongezi nyingi ambazo amezitoa kwa kupokea ndege ambayo jana Mheshimiwa Rais ameipokea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia uboreshaji wa kiwanja hiki, amekuwa akifuatilia na mimi binafsi nilifika kuona hali ya uwanja. Suala la kwanza ambalo amelizungumzia juu ya kuongeza urefu wa kiwanja. Ilikuwa imetengwa shilingi bilioni 47 kwa ajili ya upanuzi wa kiwanja hiki lakini kwa bahati nzuri tumepata fedha kwa udhamini wa Benki ya Dunia tutakwenda kujenga kwa thamani ya shilingi bilioni 94.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inaonesha kwamba huduma nyingi katika uwanja huu zitakuwa zimeongezeka. Hii ni pamoja na kuweka taa za kuongozea ndege, kuongeza urefu wa uwanja na sasa huu uwanja pamoja na taa zitakapowekwa utakuwa na urefu wa mita 2,500 kwa maana utaweza kumudu kiwango hiki ambacho Mheshimiwa Mbunge anaomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge, wananchi wa Iringa na Watanzania kwa ujumla tuvute subira, tunaenda kuboresha huu uwanja utakwenda kuwa wa kisasa pamoja na kuweka majengo, jengo la abiria pamoja na jengo la wafanyakazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni ushahidi tosha kwamba sasa hivi compensation hazichelewi kulipwa. Viko viwanja ambavyo vinaendelea kujengwa kule Shinyanga, compensation imelipwa lakini uthamini umeshakamilika, tunaendelea kuhakiki wenzetu wa Wizara ya Fedha wanahakiki umethaminishwa kama Sh.3,043,626,000 kwa ajili ya kulipa compensation. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge uvute subira, uhakiki unafanyika na mara uhakiki ukikamilika fedha hizi zitalipwa kwa wananchi. Kwa hiyo, wananchi wasubiri kulipwa compensation yao. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na kutambua na kupongeza kazi nzuri ambayo inafanywa katika kuboresha viwanja mbalimbali vya ndege hapa nchini, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa nilizonazo ni kwamba uwanja wa ndege wa Lindi umeshafanyiwa upembuzi na usanifu. Sasa, Serikali iko tayari kuanza kutenga fedha za ndani badala ya kutegemea fedha za nje kwa ajili ya kuanza ukarabati wa uwanja huu wa ndege ikizingatiwa uwanja ulivyokaa kimkakati, lakini historia ya uwanja huu na mahitaji ya uwanja huu kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, nimjulishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba avute subira wakati wa bajeti ataona kwamba tumeweka fedha za kutosha kupitia mapato ya ndani. Ile asilimia ya fedha ambazo tumetenga kupitia mapato ya ndani ni kubwa. Kwa hiyo, ilikuwa sio vema nizungumze hapa lakini labda kama baadaye tunaweza tukaonana nimwoneshe, lakini wakati wa bajeti tutaonesha namna ambavyo Serikali imedhamiria kuboresha viwanja vyake kupitia mapato ya ndani. (Makofi)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja wa ndege wa Kanda ya Kusini ni uwanja ambao upo Mtwara Mjini na ule uwanja wa Mtwara Mjini nimekuwa nazungumza sana kwenye Bunge hili kwamba ni uwanja ambao hauruhusu ndege kuweza kutua wakati wa usiku, miaka ya nyuma huko taa zilikuwepo zikaondolewa. Je, mpango wa Serikali wa ahadi inazotoa kila mwaka wa kukarabati na kuweka taa za kuongozea ndege Mtwara Mjini kiwanja hiki cha Kanda ya Kusini utaanza lini.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Maftaha kwa kuendelea kufuatilia ujenzi huu wa uwanja wa ndege wa Mtwara. Kikubwa tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni kwamba katika Bajeti ya fedha ya mwaka uliopita kulikuwa kumetengwa fedha, pia katika mwaka huu unaokuja kwa ajili ya kuongeza zile huduma ambazo zilikuwa zimepungua katika uwanja huu tumeweka fedha za kutosha. Kwa hiyo, avute tu subira, nimefika uwanja wa ndege wa Mtwara nimeuona kwanza sasa hivi huduma zinaendelea vizuri, hili zoezi la taa litakamilika tu Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba niiulize Serikali, je, ni lini uwanja wa ndege wa Njombe utawekwa lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja wa ndege wa Njombe ni kati ya viwanja 11 ambavyo viko kwenye utaratibu wa kuboreshwa. Kulikuwa kuna changamoto kidogo pale ya wale majirani kwenye uwanja Mheshimiwa Mbunge anatambua, kuna watu wameendelea kuweka majengo marefu kandokando ya uwanja huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na mawazo ya kuuhamisha ule uwanja ili uwe nje ya sehemu hiyo uliopo. Kwa hiyo, zoezi hilo tuliwaachia wataalam waendelee kuliangalia itakapokuwa imekamilika au itakapokuwa imeonesha tofauti basi tutaendelea na hatua ya kuujenga huu uwanja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu changamoto zilizokuwepo na Mheshimiwa Mbunge tumekuwa tukizungumza nae, lakini nasi tumelichukulia hatua tumewaagiza wataalam wa upande wa TAA na Mkoa waweze kukaa na kuona kama tutauhamisha huu uwanja basi tusichelewe kuchukua hizo hatua ili tuweze kufanya ujenzi wa uwanja huu.
MHE. HAROON M. PIRMOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu lake Mheshimiwa Waziri amesema kazi ya usanifu pamoja na utayarishaji wa tender documents umefanyika tangu mwezi Agosti, 2012 sasa ni zaidi ya miaka mitano. Sasa nimuombe kwamba airuhusu Wizara yake itenge fedha kwa mwaka 2018/2019 kwa ajili ya kukamilisha barabara ya Rujewa – Madibira ili ujenzi wa lami ukamilike? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia, anafuatilia sana barabara hii. Nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti inayokuja tumetenga fedha za kutosha na kwamba ujenzi wa barabara hii utaanza.
Pia nikufahamishe Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Mbarali, pamoja na barabara hii pia iko barabara hii ya Igawa – Mbarali ambayo umekuwa ukiifuatilia; sehemu ya Mbarali – Ubaruku kilometa 8.9 nayo iko kwenye mpango katika mwaka unaofuata tutaijenga barabara hii. Ahsante sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza naipongeza Serikali kwa hatua kubwa inayochukua ya kutekeleza miradi ya barabara nchini.
Swali langu dogo, katika utaratibu wa awali nilijibiwa hapa Bungeni kwamba barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom mpaka Shinyanga iko katika hatua ya mwisho a kupatiwa fedha za usanifu kina.
Je, Serikali kwa mwaka huu wa fedha imetenga kiasi gani kwa ajili ya kufanya usanifu wa Barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom mpaka Shinyanga kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, anaifuatilia sana hii barabara na anajua umuhimu wake. Barabara hii itakuwa kwa kweli ni dawa kwa ajili ya kusaidia uzalishaji katika eneo hili. Nafahamu hatua ile ya awali ya usanifu imekuwa ikiendelea, lakini katika mwaka huu wa fedha unaokuja tutaendelea na kuhakikisha kwamba utaratibu wa kukamilisha michoro na ujenzi wa barabara hii unaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ila nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wanaotoka maeneo ya Simiyu, Shinyanga na maeneo ya Arusha na Singida kwamba ule ukamilishaji wa ujenzi wa lile daraja pale Sibiti unaendelea. Vile vyuma vilivyokuwa vinasubiriwa kwa muda mrefu vilishafika, kwa hiyo sasa kipande kile tutaweza kupita wakati tunakamilisha hii hatua ya michoro na kuanza huu ujenzi. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, ile kasi ya kukamilisha kazi hii inaendelea vizuri, na kwamba hii barabara sasa iko kwenye hatua nzuri ya kuanza ujenzi.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa barabara nyingi za mikoa sasa zimeshajengwa na kuna tatizo kubwa sana la barabara Wilayani na vijijini; na TARURA wamepewa jukumu la kujenga barabara hizi, lakini pesa wanazozipata bado hazitoshi. Serikali sasa haioni sababu za msingi za kubadili formula ya ugawaji wa pesa kati ya TANROADS na TARURA ili kuongeza percentage ya pesa zinazoenda TARURA? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kati ya Lugezi na Kisorya kuna kivuko ambacho ni mbadala wa daraja, lakini katika kivuko kile kuna tatizo kubwa la utozaji wa nauli, hususan mizigo ambayo inaleta kero sana kwa wananchi kwa mizigo iliyo chini ya kilo 20. Inategemea busara ya mtozaji kama kilo moja atatoza kiasi gani? Kilo mbili kiasi gani?
Sasa Serikali haioni sababu kuweka kiwango maalum, kwa mfano, chini ya kilo 20 wananchi wasitozwe tozo zozote za nauli ya mizigo ili kuondoa migogoro ambayo imekuwa inajitokeza mara kwa mara kati ya vivuko vya Kisorya na Lugenzi na Bugorora na Ukara? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tunaendelea na ujenzi wa barabara na kipaumbele kilikuwa kwenye barabara kuu. Barabara kuu zina urefu wa zaidi ya kilometa 8,000 na kwa sasa hivi tumeshavuka nusu ya urefu huo. Kwa maana hiyo, sasa ni fursa ambayo itawezesha Serikali kuelekeza fedha nyingi kwa ajili ya kutengeneza barabara ambazo zinaunganisha mikoa na hatimaye pia kwenda kuunganisha barabara ambazo ziko chini ya Wilaya.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba utambue hivyo, pamoja na wapiga kura wa Ukerewe kwamba tumejipanga vizuri. Mara baada ya kukamilisha sehemu kubwa ya barabara kuu, nguvu kubwa ya Serikali itaelekezwa katika eneo la barabara ambazo ziko kwenye Mikoa na Wilaya.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kwamba tunachukua hatua gani kwa ajili ya gharama ya kivuko hiki cha MV Ujenzi?
Mheshimiwa Spika, ninatambua, nasi upande wa Serikali tumelichukua hili, lakini tumeshaanza kufanya utafiti wa kuhakikisha kwamba suala la bei hii ya vivuko tunaliangalia kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Spika, iko hoja kwamba gharama ya ubebaji wa mizigo iko chini kwenye baadhi ya maeneo, lakini yako maeneo yanaonesha kwamba gharama ni kubwa. Kwa maana hiyo sasa, tunafanya utafiti ili tuweze kuja na bei ambayo itakuwa rafiki kwa watumiaji wa vivuko hivi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Ukerewe tuvute subira. Nawaomba na wenzetu wa upande wa TEMESA waharakishe hili zoezi la kufanya utafiti ili tuweze kuchukua hatua ambayo itafanya usafiri huu uwe rafiki kwa watumiaji wa vivuko. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Kwanza nafurahi kukuona ukiwa mzima wa afya na tunakupongeza sana kwamba Bunge hili lilikuwa limeku-miss, sasa tunafurahi kukuona kwenye kiti chako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na makofi hayo na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, muuliza swali Mheshimiwa Mkundi amezungumzia suala la Ukerewe. Ukerewe inaunganishwa na barabara inayotoka Nyanguge kupita Busega mpaka pale Ndabaga. Barabara kuu ni mbovu kabisa, hata daraja la Mto Simiyu pale Magu halikidhi mahitaji ya usafirishaji katika mikoa hiyo. Je, Serikali inatoa commitment gani ya kuweza kukarabati barabara hii kutoka Nyanguge - Magu - Busega mpaka pale Ndabaga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze na kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa sababu barabara hii tumekuwa tukizungumza kwa maana ya kuifanyia maboresho.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba kabla commitment haijatolewa, lakini niseme tuko committed kwa sababu ule usanifu umefanyika na kwa maana hiyo, hata katika bajeti inayokuja, Mheshimiwa Mbunge tumetenga fedha kwa ajili ya kuboresha eneo hili.
Mheshimiwa Spika, niahidi tu kwamba baada ya Bunge nitatembelea eneo hili. Sijapata fursa ya kutembelea maeneo haya ili Mheshimiwa Mbunge tuweze kushauriana vizuri, na mimi nijionee mwenyewe namna gani tunaweza kusukuma kwa haraka ili barabara hii iweze kupitika.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri, tunafahamu kwamba swali hili limekaa muda mrefu kwa sababu hizi barabara zinafahamika kwamba zimekamilika kwa kiasi fulani kwa sasa hivi. Kuna barabara za muhimu ili kuweza kukamlisha matumizi na kupunguza foleni kwa wakazi wa Dar es Salaam na hasa Jimbo la Kibamba inayoanzia Mbezi Mwisho - Mbezi Sekondari inayokwenda kuunganisha Bunju pamoja na Kibaha. Barabara hii mnategemea kuikamilisha lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hizo barabara nilizozitaja, kuna wananchi wa maeneo hayo walibomolewa nyumba zao, wengine wamewekewa ‘X’ nyekundu wanakaa pale bila kuwa na amani kwa sababu hawajui lini wataondolewa; je, ni lini Serikali imepanga kulipa fidia ili kuweza kupisha wananchi wale, waendelee na kazi nyingine za maisha? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza napenda nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba upande wa Serikali tumejipanga vizuri kupunguza au kupambana na suala la msongamano wa magari. Kwa ujumla wake, zipo barabara zenye urefu wa zaidi ya kilometa 124 ambazo tunaendelea kuzishughulikia ili kuhakikisha kwamba msongamano unapungua na hatimaye unaweza kwisha kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la nyongeza, anataka kujua, lini hii barabara ya Mbezi – Kibamba itakamilika? Kubwa alilotaka kujua ni kama kuna compensation. Niseme tu kwamba kwa wale ambao wanastahili kulipwa fidia watalipwa baada ya fedha kuwa zimepatikana. Kwa hiyo, utaratibu unaendelea kwa wale wanaostahili. Niseme tu kwamba kwa upande wa Kibamba zipo barabara nyingi ambazo tunaendelea kuhakikisha kwamba tunasaidia kupunguza msongamano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, iko barabara ambayo inatoka Kibamba kwenda Kisopwa kilometa 12. Kilometa nne kutoka Kibamba kwenda Mloganzila imeshakamilika kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Kibamba, Serikali imejipanga vizuri kwa ajili ya kufanya marekebisho ya hizi barabara ili ziweze kupitika kiurahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama Mheshimiwa Mbunge atapenda kujua maelezo ya ziada, ipo mipango mingi na barabara zipo nyingi, naomba tu tuonane ili wakati mwingine aweze kupata kwa undani kwamba ni barabara kiasi gani ambacho kinakwenda kutengenezwa upande wa Kibamba?
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba kwa barabara hizi za kupunguza msongamano upande wa Kibamba tunazo barabara nyingi sana ukilinganisha na maeneo mengine kutokana na umuhimu wake.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nashukuru Serikali kutambua umuhimu wa barabara hiyo kiuchumi. Barabara hiyo ipo toka enzi ya mkoloni na kutokana na milima na miinuko iliyopo katika barabara hiyo, kipindi cha masika husababisha ajali nyingi sana, jambo ambalo huwatia hasara wananchi, pia Serikali kwa matengenezo ya mara kwa mara. Kwa nini Serikali isikubali kutengeneza hiyo barabara kwa kiwango cha lami?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, maeneo ya mlimani ni kilometa nane, barabara hiyo ni finyu sana, ikitokea lori limekwama, hakuna gari yoyote inayopita na husababisha adha kubwa kwa wananchi, kwa nini eneo hilo lisipanuliwe na kuwekewa kingo mlimani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu hili eneo la barabara hii ambalo linapita kwenye milima mikali amekuwa akilifuatilia sana mara nyingi, na mimi binafsi tumezungumza naye sana juu ya eneo hili na nilimwahidi pia kwamba baada ya Bunge hili nitatembelea eneo hili ili tuone namna bora zaidi ya kuweza kuboresha eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatambua hii sehemu ambayo ina milima ndiyo maana kwa upande wa Serikali tunajenga barabara hii kwa kutumia zege na ninaamini kabisa tutakapokuja kufanya uamuzi wa kuweka lami katika barabara hii hatutarudia kufanya matengenezo kwenye sehemu hii ambayo tumeweka zege kwa sababu barabara iliyotengenezwa kwa zege ya cement inadumu kwa muda mrefu na inakuwa imara. Kwa maana hiyo ni kwamba matengenezo yanayoendelea ni sehemu ya mkakati wa kupunguza na kukamilisha matengenezo ya barabara katika sehemu hii korofi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, pamoja na wananchi wa Kwela kwamba tutalitazama vizuri eneo hili na ninatambua kwamba eneo hili la milima mikali na kule chini kuna utelezi mkali ambapo tunaweka changarawe. Kwa hiyo, tutaliangalia kwa macho mawili ili tuone namna bora ya kuboresha eneo hili. Barabara hii kama ulivyosema ni muhimu, tutajipanga kama Serikali tuweze kuiangalia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge na wananchi wavute subira, wakati tunaendelea na michakato mbalimbali ya kukamilisha barabara katika maeneo mbalimbali, eneo hili tutalitazama kwa makini. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ni lini Serikali itakamilisha kutengeneza Barabara ya Bigwa – Kisaki kwa kiwango cha lami ikiwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKA): Mheshimiwa Naibu Spika, nimelitembelea eneo hili la barabara kutoka Bigwa – Kisaki kwenda mpaka Dutumi, nimeona upo umuhimu wa kufanya maboresho mbalimbali pamoja na kupanua madaraja. Ukienda upande wa Dutumi lipo daraja jembamba sana. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la barabara hii ni muhimu kwa sababu tunategemea pia barabara hii kupitisha mitambo na vifaa vingine wakati wa ujenzi wa umeme kule Stiegler’s Gorge kilometa 189 kutoka Ngerengere.
Kwa hiyo, tutaitazama barabara hii na ni muhimu. Kwa sasa kuna fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya kuboresha ili huduma ziendelee kufanyika wakati tunaendelea kujipanga kutengeneza hii barabara kwa kiwango cha lami.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa mwaka huu tumebarikiwa mvua lakini mvua hizi zimeleta madhara sehemu mbalimbali na kuharibu miundombinu ya barabara.
Ningependa kujua, je, Serikali imejipanga vipi kukabiliana na majanga haya ya barabara hususani zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA)? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Serikali tumejipanga na kama ilivyo kawaida kila mwaka tunatenga fedha kwa ajili ya kutibu dharura kwa maana ya emergency, kwa sasa hivi maeneo mengi ambayo barabara hazipitiki tumewaagiza Meneja wa TANROADS washirikiane na TARURA ili kuweza kuokoa sehemu hizi ambazo hazipitiki na Wizara tunaendelea kuratibu na kufuatilia ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma wanapita kwenda kwenye shughuli zao za maendeleo. Ahsante.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Igunga kwenda Mwanzugi hadi Itumba ilikuwa na mkandarasi wa TARURA aliyewekwa na TARURA anaijenga, lakini uharibifu ulikuwa mdogo sana. Sasa hivi kutokana na mvua kama ulivyosema barabara hiyo imeharibika sana, naiomba Serikali itakuwa tayari kweli kuongezea bajeti kwa ajili ya kuijenga hiyo barabara ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa Igunga? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu kwa ujumla ni kweli hali ya mvua zimekuwa excessive kwa maana ya kwamba kuna maeneo mengi yameharibika. Tunazo taarifa kule Koga hapapitiki, lakini tunazo taarifa kule Solwa hapapitiki na maeneo mbalimbali. Kama nilivyosema wakati nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Catherine kwamba tumejipanga kuhakikisha kwamba maeneo yanapitika.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dalaly Kafumu sana muda mwingi tumezungumza juu ya barabara hii na kwa kweli swali lako nazungumza juu ya kuongeza bajeti. Tumejipanga kuitazama hii barabara, najua pia una hamu ya kwenda kuunganika na wenzetu kule upande wa Nyahua. Kwa hiyo, tunaitazama kwa umakini na tutakapopata fursa tutaendelea kuongeza bajeti ili hatimaye hii barabara iweze kutengenezwa vizuri na ipitike muda wote na pia ni huduma kwa wananchi wetu wa Igunga na maeneo ambayo yanazunguka Igunga. (Makofi)
MHE. DANIEL N. NSWANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri barabara ya Kidawe - Kasulu kilometa 63 tumezungumza na wewe na nikakujulisha kwamba mkandarasi hafanyi kazi sasa, anafanya kazi ndogon dogo tu kwa sababu hajalipwa fedha zake, barabara hiyo sasa ni miaka 12 inajengwa, ni kwa nini mkandarasi hapewi fedha zake akamaliza barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge najua tumeongea mara nyingi sana kuhusu barabara za Kigoma, lakini niseme tu kwa wananchi wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla, Serikali imejipanga vizuri sana kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara kwa sababu kipaumbele chetu ni kuunganisha Mikoa yetu ya jirani na nchi za jirani. Kwa hiyo Mheshimiwa Nswanzugwanko unafahamu Kidahwe kwenda Kasulu kilometa 63 yuko mkandarasi pale, lakini kwa sasa kutokana na hali ya hewa kuna kazi ambazo zinafanyika wakati wa kipindi cha mvua, pamoja na kuwa tuna deni na mkandarasi yule upande wa Wizara tunafanya kila juhudi tuweze kuhakikisha kwamba tutapeleka fedha ili mvua zitakapopungua speed iwe kubwa.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwa barabara zote ukianzia Nyakanazi kuja Kakonko; kutoka Kankonko kuja Kibondo na kuja kuunganika Kigoma kuna juhudi nzuri na hatua nzuri tumefikia kwa ajili ya kutengeneza mikataba kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii ili pamoja na viungo vyake kutoka Kasulu kwenda Manyovu pale border ziko kilometa 58 hivi lakini zipo tena kutoka Kakonko kwenda Mabamba na wewe unafahamu.
Kwa mkoa huu ambao ulikuwa umechelewa kufanya matengenezo ya barabara kiwango cha lami kwamba sasa ziko fedha ambazo harakati zinaendelea, kwa hiyo, Kigoma itafunguka na itaungana na mikoa mingine. Mheshimiwa Nswanzugwanko na wananchi wa Kigoma naomba wavute subira na tutaendelea kukupa feedback kujua hatua nzuri zinazoendelea kule Kigoma. Ahsante.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa maijibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuzingatia majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba GNT inatarajia kukamilisha majadiliano hivi karibuni. Sasa wananchi hawa watatakiwa bila shaka kuhama baada ya majadiliano kukamilika na ujenzi unaanza mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wananchi 687 ambao walithibitika kuwa na mapunjo katika fidia zao na wakahakikiwa na Mthamini Mkuu wa Serikali. Je, wananchi hawa lini watalipwa fidia zao ambazo tayari zimeshahakikiwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa fidia ya wananchi haijakamilika katika eneo hilo la Bandari, moja katika bilioni 57.7 imelipwa mpaka sasa bilioni 45 peke yake, lakini pia kuna hawana wananchi ambao walikuwa wana mapunjo katika fidia zao na wao hawajalipwa. Je, nini kauli ya Serikali kuhusu miundombinu ya Shule ya Msingi Pande, Shule ya Msingi Mlingotini na Zahanati Pande ambazo wananchi wanaendelea kuzitumia. Kwa vile watatakiwa kuondoka, nini kauli ya Serikali kuhusu kuihamisha miundombinu hiyo kuwapelekea mahali ambapo watakuja kuitumia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kawambwa kwamba anafuatilia sana upatikanaji au ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na anafahamu kabisa kwamba Bandari hii itakapojengwa ni fursa kwa wakazi wa Bagamoyo. Kwa hiyo nimpongeze sana Mheshimiwa kwa kutetea wananchi wake lakini pia amekuwa akifuatilia sana juu ya fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza, kwamba Serikali inawajali wananchi ndiyo maana jumla ya shilingi bilioni 48 imelipwa kama fidia kati ya kiasi cha fedha cha bilioni 57 ambayo ilikuwa imetengwa kwa ajili ya kulipa fidia wananchi hawa. Eneo hili ni kubwa, lina ukubwa wa hekta 800 ni eneo kubwa sana, kwa hiyo changamoto zilikuwa nyingi, lakini Serikali imekamilisha kuwalipa wananchi. Wako wananchi wachache ambao walikuwa hawajalipwa pamoja na taasisi ikiwemo Taasisi hii ya Uvuvi Mbegani pamoja na hizi shule ambazo Mheshimiwa amezitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu kwamba, kwa sababu Serikali iko committed; ni kwamba wananchi ambao walipunjwa uhakiki umekamilika, kwa hiyo wakati wowote kama ilivyofanya kwenye malipo yao ya awali watalipwa hawa wananchi. Kwa hiyo niwahakikishie wananchi wa Bagamoyo kwamba utaratibu unakamilishwa ili sasa hizi fedha ambazo zimekuwa ni za nyongeza; ni kiasi kidogo tu kama, Serikali imelipa bilioni arobaini na nane na bilioni zingine nane zipo; ni kwamba tupo committed kulipa hizi fidia. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi wananchi hawa watalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, anauliza juu ya hatima ya shule hii ya Pande. Ni dhahiri kwamba kati ya zile fedha bilioni nane zilizobaki ni hizi taasisi ambazo ziko chini ya Serikali ambazo ni pamoja na Shule ya Msingi ya Pande, Shule ya Msingi ya Mbegani, Zahanti ya Pande pamoja na Mbegani. Kwa hiyo hizi ndizo shilingi bilioni nane zilizobaki kwa ajili ya kulipa na kuhamisha hizi taasisi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi tumejipanga vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa kuna uhakiki wa kuhamisha makaburi lakini pia tuliweza kupata thamani ya shilingi zaidi ya milioni mia tano ili kuweza kuhamisha makaburi pamoja na kuhamisha hizi shule. Kwa hiyo fedha zimeshapatikana na kibali kimeshatolewa. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Bagamoyo wasiwe na wasiwasi, fedha hizi zilizobaki bilioni nane pamoja na hii milioni mia tano zipo, tutahamisha hizo shule ili wananchi wapate huduma na ujenzi uweze kuanza mara moja.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Tatizo la kutoanza ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo linafanana sana na tatizo la kutokuanza ujenzi wa Bandari ya Nyamisati katika Wilaya ya Kibiti. Bandari ya Nyamisati ni Bandari ambayo ni kiungo baina ya wananchi wa Mafia wanapokuja Dar es salaam. Mkandarasi ameshapatikana toka mwaka jana mpaka leo hajafika site, ni nini kauli ya Serikali kuhusu Mkandarasi huyu? Nakushuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua na Mheshimiwa Dau hapa amekuwa akipiga kelele kweli, uko ule utaratibu wa kujenga Bandari ya Nyamisati unaendelea. Nimwombe tu asiwahishe shughuli hata wakati wa bajeti ataona tumependekeza fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa Bandari hii ya Nyamisati. Kwa hiyo kama atataka taarifa za ziada basi naomba tuonane ili angalau nimwoneshe mpango madhubuti uliopo kwa ajili ya kuokoa wananchi wa Mafia na Watanzania wengine ambao watakuwa wakisafiri kwenda Mafia.
MHE. ZITTO R. Z. KABWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la changamoto za Bandari ya Bagamoyo, Bandari ya Nyamisati ni changamoto zinazofanana kabisa na miradi minne ya Bandari ya Kigoma. Uboreshaji wa Bandari ya Kigoma, Bandari kavu ya Katosho, Bandari ya Ujiji na Bandari ya Kibirizi; lakini tu ni kwamba fedha zimetengwa toka mwaka 2016/2017 na tayari Mamlaka ya Bandari imekwishaweka utaratibu wa manunuzi. Wizara imezuia Mamlaka ya Bandari kutangaza zabuni hizo za Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ilieleze Bunge hapa, ni kwa nini haijaidhinisha zabuni hizo kutangazwa ili wananchi wa Mkoa wa Kigoma waweze kupata faida ya uchumi wa jiografia kwa kuboresha Bandari ya Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza si kweli kwamba Serikali imezuia; unajua ujenzi una hatua zake, Mheshimiwa Zitto anafahamu. Ziko hatua, ndiyo maana tunaanza kwenye usanifu, tunaanza kuweka fedha na mijadala iko mingi kama kunajitokeza jambo ambalo linahitaji labda wakati mwingine kupata muda kuli-clear kwamba kama kuna risk inajitokeza lazima Serikali ichukue hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe wasiwasi na asubiri. Mheshimiwa Waziri wakati akijibu katika hotuba ya Waziri Mkuu alisema hapa Bungeni na alijaribu kusema kwa ufupi na akasema tusubiri wakati wa bajeti Mheshimiwa Zitto ataona namna tulivyojipanga ili kuhakikisha Bandari zote kwa upande wa Kigoma, kwa upande wa Ziwa Victoria, kwa upande wa Ziwa Nyasa na maeneo mengine. Kwa hiyo, niseme tu kwamba maeneo yote ambayo Mheshimiwa Zitto anataja kwa maana ya Katosho na Kibirizi tumeonesha vizuri katika mapendekezo ya bajeti ambayo ni Jumatatu tu tutaanza kuizungumza bajeti ya Wizara hii.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa vile kipande cha barabara hiki cha Mambali – Bukumbi – Shitage - Mhulidede mpaka Kahama kupitia Tulole ni muhimu sana kiuchumi kwa sababu ya biashara ya mikoa miwili hiyo; Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
Swali la pili, ni lini uchambuzi yakinifu na usanifu utaanza kwa ajili ya barabara hiyo? Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia hii barabara, barabara hii ambayo anaizungumza kutoka Mambali – Bukumbi- inakwenda mpaka Mhulidede ni barabara ambayo inapakana na Jimbo la kwangu kule Ushetu. Kwa vile amekuwa akifuatilia barabara hii imewezesha hata kile kipande cha kilometa 21 nilichokitaja kwenda Tulole hadi Kahama Mjini ili kuleta ulinganifu na kuleta maana kimeanza kuhudumiwa.
Mheshimiwa Spika, namwomba tu Mheshimiwa Mbunge kwamba avute subira, Serikali imefanya juhudi kubwa sana kuunganisha mikoa na mikoa na kuunganisha mikoa na nchi jirani. Kwa vile kazi inaendelea vizuri nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa maeneo ya Bukumbi, Mhulidede, Mambali na majirani zake kule upande wa Bukene kwamba baada ya kazi nzuri ya kuunganisha mikoa sasa nguvu kubwa itaelekezwa kuunganisha barabara hizi ambazo zinaunganisha wilaya na mikoa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge avute subira baada ya kuwa kazi nzuri ya kuunganisha mikoa na nchi za jirani ikikamilika basi zoezi la usanifu kwa kipande hiki cha barabara kutoka Mambali ambacho kimsingi kitapunguza umbali wa mtu anayetoka Tabora kwenda Kahama kwa takribani kilometa 50.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuvute subira tutakuja kufanya usanifu na kuweza kujenga barabara hii. Usanifu utaanza baada ya kuwa tumejipanga vizuri na kuhakikisha kwamba, sasa tunafanya muunganiko wa sehemu hii ya barabara.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, pamoja na shukrani kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu hayo ambayo amenipa.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, eneo lile la Kitongoji cha Sanzale ni Bagamoyo Mjini na wananchi hawa wamewekewa alama za “X” miaka nane imepita, hawawezi kukarabati nyumba zao, hawawezi kujenga upya, hawawezi kufanya chochote na majibu ni kwamba watafidiwa pale maeneo yatakapohitajika. Je, ni lini maeneo hayo yatahitajika kwa sababu wananchi hawa psychologically wameendelea kupata matatizo makubwa sana? Wafanye nini maana wanaishi na watoto wao katika nyumba ambazo zimewekewa “X” lakini hawajui lini watalipwa fidia.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika barabara ya Makofia - Mlandizi ambayo imo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010 pia katika Ilani ya mwaka 2015 kujengwa kwa kiwango cha lami. Wananchi hawa wanapenda kujua fidia zao zitalipwa lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASLIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kawambwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Kawambwa kwa kufuatilia sana maendeleo ya Bagamoyo kwa ujumla wake. Natambua kwamba kutakuwa na ujenzi wa bandari ya Bagamoyo na hivyo hizi barabara ambazo Mheshimiwa Mbunge anazitaja ni muhimu kweli. Yeye mwenyewe anatambua kwamba zipo harakati za awali ambazo zimefanyika ili kuhakikisha kwamba fidia kwa wananchi wake zinalipwa mapema.
Mheshimiwa Spika, swali lake anasema ni lini sasa tutalipa fidia hiyo. Niseme kwamba harakati za ujenzi wa barabara ya lami kwa barabara ambazo zinaingia Bagamoyo zinaendelea na hatua za tathmini zimeshafanyika na kwa vile zina hatua mbalimbali, kwa upande wa TANROADS tumeshafanya jukumu letu na tunaendelea kuwasiliana ili kuweza kupata fedha ili wakati wowote tuweze kuwalipa wananchi hawa.
Mheshimiwa Spika, najua kwa eneo hili amelitaja mahsusi Mheshimiwa Mbunge, wapo wakazi wasiozidi 20 ambao wanahitaji kufanyiwa malipo ya compensation. Kwa hiyo, nikuombe tu Mheshimiwa Mbunge na Ndugu zangu wananchi wa Bagamoyo eneo hili wavute subira wakati wowote tutafanya zoezi la kuweza kuwalipa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, anauliza juu ya compesation kwenye barabara hii inayotoka maeneo ya Mlandizi kuja Bagamoyo. Kama nilivyosema barabara hii ni muhimu sana kwa ajili ya kuja kutoa huduma katika Bandari ya Bagamoyo itakapojengwa hii ikiwa ni pamoja na eneo lingine kuja Bagamoyo ukitokea Kibaha, maeneo ya Vikawe kuja Mapinga na kwenyewe harakati zinaendelea vizuri.
Mheshimiwa Spika, natambua Ilani ya mwaka 2010 ya Chama cha Mapinduzi na Ilani ya mwaka 2015 imetaja kupanua barabara hii. Kwa hatua ambazo tumefikia wananchi wameshapata valuation form wazijaze, wazirudishe halafu Serikali tutasimamia kwa haraka ili wananchi hawa pia waweze kulipwa kulingana na sheria inavyotaka.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, majanga mengi sasa hivi yanasababishwa na binadamu zaidi ya asilimia 96 ikiwepo kwenda kinyume na uumbaji wa dunia ya Mwenyezi Mungu. Sheria hii ya tangu mwaka 1932 mpaka 2007 kwa kiasi kikubwa ni uharibifu mkubwa wa mazingira na hasa barabara za vijijini. International Standard na vigezo vyake vya ujenzi wa barabara huwezi uka-upgrade barabara kutoka stage moja kwenda stage nyingine za vijijini ukafanya mita 60.
Mheshimiwa Spika, barabara hizi zinazoenda vijijini, kwa mfano barabara ya Kawawa - Pakula, Jimbo la Vunjo na barabara ya Himo na Himo - Mwika, kwa nini mnaamua kuchukua mashamba bila fidia na siyo standard? Barabara zinajengwa kwenda juu na siyo kupanua tu kwa horizontally?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ELIAS KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbatia, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, nitumie nafasi hii kulipongeza Bunge kwa kutunga Sheria hii Na.13 ya mwaka 2007 ambayo kwa kweli ilizingatia sana mabadiliko, ukiisoma Sheria ya mwaka 1932 utaona namna ilivyokuwa. Kwanza ilikuwa ni ndogo sana, ilikuwa na kama section saba tu na ilikuwa inatoa mamlaka makubwa sana kwa wale watekelezaji wa ujenzi wa barabara wanaweza wakafanya maamuzi, sheria iliyowaruhusu. Mabadiliko haya yaliyokuja mwaka 1969 na baadaye kuja hii Sheria Na.13 imetoa nafasi kwa Mamlaka zetu za Barabara kuweza kuzingatia maeneo maalum na kuweza kufanya declaration ya ujenzi wa barabara. Hivyo, sheria ipo vizuri ni vema tu tuendelee kuitekeleza.
Mheshimiwa Spika, nimueleze Mheshimiwa Mbatia niseme kwamba Serikali inalipa fidia kulingana na sheria zilizopo pia lazima tuangalie na mamlaka zetu katika halmashauri. Mamlaka za Barabara zipo kwenye Halmashauri zetu, kwa mfano, sasa hivi tunayo TARURA na TANROADS kwa upande wa Serikali Kuu.
Mheshimiwa Spika, ni muhimu tu tukatazama sheria zote, Sheria za Barabara pamoja na sheria za kusimamia mamlaka zetu ili wananchi waweze kupata haki. Kama jambo hili linaweza kuwa mahsusi Mheshimiwa Mbunge alilete tulizungumze tuone namna nzuri ya kulishughulikia lakini Serikali ina nia thabiti ya kuwalipa wananchi fidia kulingana na sheria zilizopo.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mbunge wa Segerea, Mheshimiwa Bonnah Kaluwa kwa kazi nzuri za miundombinu anazofanya kwenye jimbo lake. Hivi karibuni alikuwa na ziara na Waziri wa Ujenzi kutazama miundombinu kwenye jimbo lake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Segerea na Mkoa wa Dar es Salaam, naomba kujua ni lini sasa Serikali itaweka mkazo kwenye barabara za Jimbo la Ilala ambalo ndilo linabeba magari yote kutoka maeneo yote ya Mkoa wa Dar es Salaam? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Naibu Waziri, TAMISEMI kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Zungu kwa kufuatilia kwa pamoja na maeneo mengine. Kama alivyosema nimekuwa na ziara Segerea Jumamosi, nimezitembelea barabara ambazo pia ziko chini ya TARURA ili kuweza kuona changamoto zilizopo ili kwa upande wa Serikali tuweze kuona namna sahihi ya kuweza kuzitatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme tu kwa maana ya kupunguza msongongamano katika Jiji la Dar es Salaam hususani Ilala, kama tulivyopitisha bajeti tunaendelea na ule mkakati wa kupunguza msongamano. Tutakuwa na BRT III na IV lakini pia ipo mbioni BRT V na VI ili hatimaye msongamano katika Jiji la Dar es Salaam uweze kuondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira na wakati mwingine tunaweza kupeana mrejesho ili aone namna tulivyojipanga. Kwa kweli BRT I na II imefanya vizuri na imekuwa na rekodi nzuri kitaifa na watu na mashirika mengi yapo tayari kuja ku-support tutakwenda mpaka BRT V na VI.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, nina imani wahanga wengi akiwemo ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa atakuwa amefurahishwa sana na majibu haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari yetu ya Dar es Salaam ina ushindani mkubwa sana kutoka Bandari za Angola, South Africa pamoja na Msumbiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itajenga Bandari ya Inyara ikiwa ni pamoja na reli ya kutoka Mbeya kwenda Ziwa Nyasa ili kukabiliana na ushindani huu wa kibiashara ambao ni karibu asilimia 70 ya biashara ya nje kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwa mizigo inayokwenda nchi za nje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mbalizi - Shigamba - Isongole na barabara ya Mbalizi - Makongorosi ambazo ni barabara za kimkakati na ilikuwa ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne na Rais wetu wa Awamu ya Tano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niruhusu nimpe pongezi nyingi Mheshimiwa Mbunge Oran kwa kufuatilia mambo mbalimbali kwa sababu nafahamu anafuatilia masuala ya barabara, Uwanja wa Ndege wa Songwe, bandari kavu kama alivyouliza, lakini mambo muhimu kama ya kilimo na wachimbaji wake wadogo wadogo na mara nyingi tunapokea ushauri wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujibu swali lake la kwanza kuhusu ujenzi wa bandari kavu hususan eneo la Inyara, niseme tu kwamba Serikali inafanya maandalizi muhimu kwa ajili ya ujenzi wa hii bandari kavu ikiwa ni pamoja na kutenga eneo la heka 108 kwa ajili ya ujenzi huo. Eneo hili tumelitazama kimkakati kwa kweli kwa maana ya kuangalia ile chain supply yaani kuwa na mnyororo wa muunganiko kwa maana kwamba eneo hili linapakana na barabara inayotoka Mbeya au Kyela kwenda Malawi pia iko kandokando ya reli ya TAZARA.
Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga kwa ajili ya kuboresha bandari hii na hatua ambayo tuko nayo ni kufanya tathmini ya maeneo ya wakazi wanaopitiwa na mradi huu ili tuweze kuwalipa fidia na harakati zingine zitakazofuata kwa ajili ya ujenzi wa bandari hii kavu ziwezi kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu barabara ya Mbalizi - Shigamba na barabara ya Mbalizi - Makongorosi ni barabara ambazo tumezizingatia pia katika bajeti yetu hii kwa maana ya kuziboresha. Mheshimiwa Mbunge anatambua kwamba tumetenga fedha nyingi kuboresha barabara hizi ili ziendelee kupitika wakati wote, wakati tunazitazama kwa ajili ya kuziboresha kwa kiwango cha lami.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kwamba barabara ya kutoka Magu (Ilungu) – Nkalalo – Ngudu - Hungumalwa ni barabara muhimu sana katika kuleta uchumi kwa maeneo yale na imeshafanyiwa usanifu wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Je, ni lini sasa barabara hiyo itajengwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwani amekuwepo katika Bunge hili muda mrefu na naamini kabisa hata hii hatua ya barabara hii kusanifiwa na kupata michoro ni pamoja na juhudi zake mwenyewe. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Ndassa tuendelee kuwasiliana kuifuatilia barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme kwamba Serikali ilikuwa inafanya juhudi kubwa sana za kuunganisha mikoa. Baada ya kuwa sasa tumekuwa na hatua nzuri, naamini tutaendelea kutafuta fedha na muda siyo mrefu barabara hii ya Ilungu – Ngudu – Hungumalwa tutaweza kuitafutia fedha ili tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimuombe tu uvute subira yeye na wananchi wake muda siyo mrefu tutaipatia ufumbuzi barabara hii.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Swali la msingi linasema pia vyanzo sababishi ni ajali na ajali nyingi zimekuwa zikitokea kwa uzembe. Sasa niulize Serikali, Kitengo cha Kupambana na Majanga yaani Risk Management katika Wizara ambapo kuna known risk, known-unknown risk and unknown–unknown risk lakini ajali nyingi zinasababishwa na known-known risk ambazo tunajitakia sisi binadamu. Sasa Serikali ni kwa kiasi gani inaimarisha Kitengo cha Risk Management kitaalamu na kibajeti ili kiweze kupunguza vyanzo vya ajali hizi ambapo maisha ya binadamu hayana thamani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tunatambua kwamba kumekuwa na ajali nyingi na hizi tumezizungumza sana kwenye Baraza la Usalama Barabarani. Ziko hatua kabambe nyingi ambazo zinachukuliwa na Serikali ili kuhakikisha kwamba ajali hizi zinapungua. Kwa kipindi hiki kifupi ajali zimepungua lakini tunapenda tuendelee kuzipunguza zaidi na zaidi. Nafikiria tunajaribu kutazama muundo wa Baraza hili sasa ili kuwa na mechanism nzuri ya kuhakikisha kwamba tunazitambua vizuri hizi risk ambazo zipo ili tuweze kuzishughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu suala la kupunguza ajali ni letu sisi wote. Kwa hiyo, nitoe tu ombi kwa Waheshimiwa Wabunge tuendelee kushauri wanaotumia vyombo, madereva wetu, madereva wa bodaboda ili wakati Serikali inachukua hatua ni vyema wote tuwe pamoja ili kuhakikisha kwamba tunatoa hamasa, tunatoa elimu na kuwafanya watumiaji wote wa vyombo waweze kutumia barabara vizuri. Pamoja na watumiaji wa miguu, hatari ziko nyingi tunaziona katika majiji na maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tushirikiane ili tuhakikishe kwamba ajali zinapungua na kama ikiwezekana tuziondoe kabisa.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa mujibu wa sheria, uthamini ukishafanyika, ndani ya miezi sita waathirika wote wanapaswa wawe wameshalipwa fiidia zao. Wako wananchi wa Arusha na wananchi wa Rombo, Lotima na Holili, ambao bado wana malalamiko ya kutolipwa fidia zao. Je, Serikali iko tayari kupokea majina ya wananchi hawa wanaolalamika na kuwalipa fidia zao?
Swali la pili, barabara kutoka Mamsera Jimboni Rombo mpaka Mahida KNCU na kwa Abiola ilichukuliwa na TANROADS mwaka 2014/2015 lakini TANROADS wameitelekeza hadi sasa, Halmashauri, TARURA na TANROADS hawaiangalii.
Naomba kauli ya Serikali, barabara ile imerudishwa TARURA ili waitengeneze au TANROADS wako tayari kuendelea kuihudumia hiyo barabara? Kwa sababu, imekuwa kero kubwa kwa wananchi wa Mahida, Chana na maeneo mengine ambayo hiyo barabara inapita? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Selasini kwa kufuatilia na anajua kwamba ziko harakati na juhudi kubwa ambazo zinafanyika kuhakikisha tunaboresha miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza niseme tu kwamba suala hili la kulipa fidia ni kwa mujibu wa sheria. Mheshimiwa Mbunge anatambua kwamba sheria hii namba 13 ya 2007 inatoa mamlaka ya kufanya fidia kwa wananchi pale ambapo mradi wa barabara unapita na hususan ukiangalia section 16 inasema pamoja na mambo mengine, Sheria ya Kutwaa Ardhi (Land Acquisition Act), pia iko Land Act na Village Land Act ambapo zinatumika sambamba na sheria hii ya barabara ili kufanya wananchi waweze kupata haki zao. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi kama wapo wachache kama nilivyosema, wengi wamelipwa, basi tutatazama, lakini sambamba na sheria, haki zao watazipata kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili amezungumza juu ya hii barabara ambayo anasema inatoka Mamsera, kulikuwa na sintofahamu labda kuhamishwa kwenda TARURA. Cha muhimu ni kuhakikisha barabara inaboreshwa. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hizi zinavyojengwa, ziko kwenye mpango, kwa maana ya kwamba sisi upande wa TANROADS iko strategic plan ambayo ina-monitor ujenzi. Tutazama tu kuona kama inakwenda TANROADS au TARURA lakini lengo itaweza kutengenezwa kwa mujibu wa taratibu zilizokuwepo.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nitumie nafasi hii kwa ruhusa yako niwape pole sana wananchi wa Jimbo la Nyamagana kwa mafuriko makubwa sana kwa siku ya jana ambayo yalisababisha shughuli za kijamii kusimama takribani masaa saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu dogo, Jiji la Mwanza ni moja kati ya majiji yanayokuwa kwa kasi sana Barani Afrika ikiwemo Nyamagana. Sasa nataka kujua barabara kubwa ya Kenyatta ambayo inatoka Mwanza Zero kupita Kata za Mkuyuni, Butimba, Nyegezi kwenda mpaka Buhongwa ikiwemo na Mkolani ni barabara finyu sana kwa sasa. Serikali inao mkakati gani kuhakikisha barabara hii inapanuliwa angalau kwa njia nne ili ionekane taswira halisi ya Jiji la Mwanza na ukuaji wake kwa kasi? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa ujumla kwamba Jiji la Mwanza linakua kwa kasi lakini shughuli za maendeleo ziko nyingi, nasi kama Serikali tunatazama ili kwamba miundombinu hii tunayoweza kurekebisha iende sambamba na kasi ya ukuaji wa shughuli za maendeleo na ongezeko la watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mabula na tumeshazungumza kwamba nitakwenda kutembelea Mwanza, tutaitazama kwa sababu hii anayoizungumza ya Kenyatta kwenda Buhongwa ikipitia maeneo ya Makuyuni - Mkolani kwenda Nyegezi kama alivyozungumza, ni muhimu. Ni nia yetu kuhakikisha kwamba tunaboresha miundombinu ili iende sambamba na ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Moja ya changamoto inayokabili sana Mji mkongwe wa Mbulu ni pamoja na barabara ya Magara - Mbulu kupita katikati ya Mji Mkongwe wa Mbulu. Kwa kuwa jambo hili linaathiri uchumi wa wananchi, je, Serikali ina utaratibu gani sasa ikiwemo Mji wa Mbulu na miji mingine nchini namna ya kupata barabara ya mchepuo katika miji yetu ikiwa ni pamoja na athari za kiuchumi lakini pia na jiografia ya miji hiyo inavyokua kwa kasi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anatambua kwamba tunatazama sana maeneo haya kadri yanavyokua na anatambua ziko barabara ambazo zitakuja kuunganisha Mbulu Mjini. Nampongeza sana kwa kufuatilia, anajua tutatoka Mbulu Mjini kwenda Karatu, tutakwenda kutoka Mbulu kupitia Magara kama alivyosema na kuja Mbuyu wa Mjerumani. Vilevile ipo barabara kubwa ambayo itakuwa inakwenda Katesh – Dongobesh. Sasa barabara hizi zinavyokuja kuunga Mbulu, tunazitazama pia ukuaji wake na kuweka barabara za mchepuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo mbalimbali katika miji kama alivyosema, tunayatazama yakiwemo maeneo ya Songea. Najua ndugu yangu alikuwa anafuatilia kilometa 11 zile, lakini maeneo mbalimbali ukienda Mwanza, tunayatazama ili kupunguza msongamano katikati ya mji. Zipo barabara ambazo zimekamilika kwa ajili ya mchepuo. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili la by-pass la Mji wa Arusha linafanana kabisa na tatizo la by-pass Mji wa Babati ambako kuna by-pass ya Arusha – Singida na Arusha - Dodoma. Wananchi takribani miaka saba wanasubiri fidia hawajawahi kulipwa na hawajui ni lini watalipwa juu ya by-pass hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumwuliza Mheshimiwa Waziri, Babati ni karibu, yuko tayari kuambatana nami ili akawajibu wananchi hao ni lini wanalipwa fidia zao za by-pass hizi mbili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi kabisa niko tayari.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nilitaka nimuulize Mheshimiwa Waziri, kutokana na mvua ambazo zinaendelea kunyesha Dar es Salaam na Mheshimiwa Waziri alishafanya ziara Jimbo la Segerea na kuona barabara nyingi ambazo zimekatika na nyingine zimekata kabisa mawasiliano.
Sasa Serikali ina mpango gani wa haraka kuhakikisha kwamba hizo barabara zinarudi kwenye matumizi ya kawaida hasa katika Jimbo la Segerea, Kata ya Kimanga, Segerea pamoja na Kinyerezi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kwamba tumekuwa na mvua nyingi na maeneo mengi nchini yameharibika. Kwa Jiji la Dar es Salaam kuna hali mbaya sana naye mwenyewe kwa sababu anatokea Jijini Dar es Salaam kwa kweli miundombinu ya barabara imeharibika sana na kwa sababu mvua ni nyingi na zimeendelea kunyesha na ile mito mikubwa inaendelea kumomonyoka na kufuata makazi ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi tu ni kwamba tunatazama kwa macho mawili Jiji la Dar es Salaam kwa maana kwamba mvua zitakapopungua tuweze kwenda kufanya marekebisho makubwa. Niseme tu na niendelee kurejea kwamba upande wa TANROADS na upande wa TARURA wamekuwa wakifanya uratibu wa kuangalia uharibifu mkubwa uliofanyika. Kwa sababu uharibifu unaendelea kutokea, nawaomba tu kila kukicha waendelee kuona kama kuna ongezeko la uharibifu, tufanye makadirio kuona namna gani tutafanya ili kurejesha miundombinu iliyoharibika kwa sababu bado mvua zinaendelea kunyesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Bonnah Kaluwa, aendelee kufuatilia na tuendelee kupeana taarifa, Serikali iko macho kuangalia na kufanya marekebisho.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ametoa majibu yake kuhusiana na swali la msingi, je, ahadi hizi zinazotolewa kuhusu barabara hizi hasa ya Mbulu by-pass ambayo inakwenda mpaka Maswa, ni lini sasa Serikali itakuja na mpango wa kuzijenga kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti tumeonesha na Mheshimiwa Mbunge anajua na namshukuru kwa kufuatilia kwa sababu anajua ziko barabara mbili, hii by-pass ya kupita Eyasi na hiyo inayopita kwenye Jimbo lako Katesh, Haydom kwenda Mbulu Mjini na unafahamu tuko kwenye hatua nzuri tunaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutaendelea kupeana taarifa na Mheshimiwa Mbunge ili kuona hatua nzuri zinavyokwenda ili naye aendelee kuwapa taarifa wananchi katika Jimbo lake la Mbulu. Ahsante sana.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Chifu Kwandikwa, Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo amerasimisha hapa kwa sababu tunayaongea sana haya hata jana tulikuwa tunaongea ofisini kwake. Lakini nilipenda tu angalau anisaidie kurasimisha pia mengine ambayo tuliyaongea lakini hayako kwenye jibu hili la msingi yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, barabara ya kutoka Kahama kwenda Mwanza kupitia Bulige imekatika kabisa kile kipande cha kutoka Bulige kwenda Mwakitolyo kwa sababu ya hizi mvua zinazoendelea, lakini vilevile hata ile ya kupita Busangi - Kharumwa hadi Busisi na yenyewe imeharibika kwa kiasi kwamba magari madogo hayawezi kabisa kupita. Wakati mipango hiyo ya kujenga kwa kiwango cha lami ikiendelea ni hatua gani Serikali inafanya kwa dharura ili kuzitengeneza barabara hizi ziweze kupitika.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali ilishaahidi kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Kahama kupitia Segese – Mgodi wa Bulyanhulu hadi Geita kwa kiwango cha lami. Kwa miaka miwili mfululizo mwaka wa fedha uliopita na huu mwaka tulionao sasa hivi, Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha lami. Nilitaka tu Mheshimiwa Naibu Waziri kama ulivyonithibitishia mimi tulivyokuwa wenyewe, wathibitishie wananchi na watanzania ni lini hasa sasa ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Kahama - Geita utaanza. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza pongezi alizozitoa nazipokea. Lakini nitakuwa mchoyo kama sitakushukuru wewe binafsi wakati wa mjadala wa Bajeti ya Maji ulilisemea sana Jimbo la Ushetu, kwa hiyo nakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, nimjibu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nakupongeza sana kwa kufuatilia barabara hizi ambazo zinaunganisha Mji wa Kahama ikiwepo hii barabara muhimu uliyoisema inayotoka Mji wa Kahama ikipitia maeneo ya Ntobo, maeneo ya Segese ikipitia pia katika Jimbo la Mheshimiwa Bukwimba ikielekea kule Geita na wewe mwenyewe unafahamu kwamba tumeanza ujenzi wa barabara hii kiwango cha lami.
Kwa hiyo, niwathibitishie tu wananchi wote maeneo hayo kwamba ujenzi umeanza ila juhudi zitaendelea kufanyika kuweka fedha za kutosha ili barabara muhimu hii iweze kukamilika.
Mheshimiwa Spika, niwape pole wananchi kote nchini kwamba tumepata mvua nyingi na Mheshimiwa Ezekiel unajua kwamba barabara hii unayoitaja inayopita maeneo haya ya Mwakitolyo kwenda Mwanangwa kumekuwa na shida kubwa kwamba barabara zimekatika lakini bado pia kuna wananchi ambao nyumba zao zilidondoshwa kutokana na kuwa na mvua nyingi.
Mheshimiwa Spika, sisi upande wa Serikali tumejipanga kwa hatua ya kwanza kwamba kwanza tunayo bajeti kwa ajili ya kutibu emergency kama hizi. Tutatumia fursa hiyo, lakini pia tunafanya uratibu maeneo yote nchini lakini pia ninazo taarifa kuwa Mkoa wa Shinyanga kwamba Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza amefanya survey kwenye barabara hii na kutambua mahitaji muhimu ya maboresho katika barabara hii. Kwa hiyo, nikuombe tu uvute subira na niwatoe hofu wananchi kwamba barabara hii tunaenda kuifanyia marekebisho na niwapongeze kwa kweli Mameneja wa TANROADS mikoa yote kwa kazi nzuri ya uratibu wanayoendelea kuifanya muda huu ambao tuko kwenye shida. (Makofi)
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika Kesi Na. 9 iliyofunguliwa na Jebra Kambone katika Mahakama Kuu ya Tanzania iliyokuwa ina-challenge baadhi ya vifungu vya sheria hii, Mahakama Kuu ilisema kifungu Na. 50 kinachozungumzia nguvu ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali kuunganisha makosa na kumpa mtu haki ya kukiri mbele yake inakiuka Katiba na hadi sasa sheria hiyo haijafanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kesi iliyofunguliwa na Jamii Forum, pia Mahakama ilisema sheria hii inatafsiriwa vibaya na Jeshi la Polisi. Swali la kwanza, je, kwa maelezo hayo ya Mahakama, Serikali haioni kwamba kuendelea na sheria hii ni kukiuka Katiba ambayo yenyewe imeapa kuulinda na kuitetea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sheria hii imeleta mgogoro mkubwa na malalamiko mengi ndani na nje ya nchi wakiwemo nchi wahisani. Kwa nini Serikali inatafuta ugomvi mwingine na makundi mengine ambayo inaweza kuepukana nayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Kubenea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mbunge akubaliane nami kwamba sheria hii imesaidia sana na imetatua matatizo mengi. Kama zilivyo sheria nyingine, upo utaratibu wa kufanya marekebisho. Lazima Serikali ipitie hatua kadhaa kabla haijaleta marekebisho Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kujibu swali lake, niseme tu kwamba hizi kesi ambazo amezitaja ni mahsusi na yumkini inaweza ikasaidia pia kufanya marekebisho. Kwa hiyo, tunaichukua tu kama ni kitu ambacho lazima tupitie kama Serikali kwa maana ya kutazama mbele ya safari. Ni kawaida sheria ambazo zipo kufanyiwa marekebisho mbalimbali. Kama ilivyozoeleka, zipo sheria nyingi kila wakati inapohitajika, kwa sababu sheria siyo static, inavyotazamwa na marekebisho yataweza kuja kwenye Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili aliposema ni kwamba yapo malalamiko ambayo yanaweza yakaleta ugomvi. Niseme kwamba siyo kweli kwa sababu sisi ni kama Taifa na kama nchi, lazima tuangalie taratibu zetu. Ni lazima tuhakikishe kwamba sheria tulizonazo wa kwanza kunufaika nazo ni wananchi wenyewe na Taifa. Kwa hiyo, hili ni suala la kulitazama tu kwa upana wake, lakini hatuwezi kwenda kutunga sheria kwa kufuata shiniko la mtu, tutatunga sheria ili kuleta haki kwa wananchi na Tanzania kwa ujumla.
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Niwatakie mfungo mwema ndugu zangu Waislam ndani ya Bunge na nchi nzima. Kwa wale ambao ni viongozi watumie Mwezi huu Mtukufu kujitathmini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii pamoja na sheria nyingine mbovu za habari, siyo tu zinabana wananchi kupata habari, bali zinatumika pia kufunga watu jela ovyo kisiasa. Mfano, mimi nilifungwa kwa kujadiliana na wananchi wangu taarifa za watu kupigwa risasi, watu kutekwa, maiti kuokotwa kwenye viroba, watu kutokuwa na uhuru wa kuongea na kadhalika…
Kitu ambacho siyo mimi tu niliyejadili, kwa sababu kilishajadiliwa ndani ya Bunge hili na pia Maaskofu wa Katoliki pamoja…
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, ni lini sheria hizi zitafutwa ili kulinda Katiba ya nchi hususani Ibara ya 18? (Makofi). Maslahi mapana ya demokrasia nchini. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sugu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie nafasi hii nimkaribishe Mheshimiwa Sugu hapa kwenye Jumba, karibu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake linasema kwamba zipo sheria ambazo wakati mwingine zinatakiwa kutazamwa. Kama nilivyojibu kwenye swali la nyongeza lililotangulia ni kwamba sheria zote, siyo hiyo sheria moja, Serikali inayo mechanism ya kuzitazama wakati wowote. Kama kuna maeneo ambayo yanahitaji marekebisho au kuunganisha sheria au kuiondoa, ni Bunge hili linapata nafasi hiyo ya kufanya hivyo. Kwa hiyo, labda kama kuna eneo mahsusi Mheshimiwa Sugu kwa sababu umekuja, tuonane ili nami nipate kwa upana unachokizungumza, halafu baadaye sisi kama Serikali tutatazama kwa nia nzuri ya kuweza kufanya sheria iwe bora zaidi.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza, pamoja na majibu yasiyoridhisha ya Mheshimiwa Naibu Waziri, atakubaliana nami kwamba imekuwa ni kawaida kwa Serikali kutokuwalipa waathirika wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwepo Wilaya hii ya Kyela? Barabara hii toka imejengwa hakuna aliyelipwa mpaka sasa na ndiyo maana wananchi wamefungua kesi Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, imekuwa ni kawaida ya Serikali kutokulipa wananchi wengi katika Taifa hili wanapowabomolea kwa kigezo cha ujenzi wa barabara, wakati huohuo mmewawekea umeme na maji. Kama mlijua wameingia kwenye hifadhi ya barabara kwa nini mlitoa huduma hizo za kijamii? Nataka majibu ya Serikali ni kwa nini wanafanya hivyo, wananchi hawapati haki zao wakati wamekaa kwa muda mrefu, zaidi ya miaka 50 katika eneo husika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza, namuomba sana Mheshimiwa Mbunge aridhike tu kwa hatua ambayo Serikali inachukua. Kwa sababu hivi navyozungumza shilingi bilioni 1.008 zililipwa kwa wananchi ambao walikuwa wanaathirika na ujenzi wa barabara. Hao wachache waliobakia kwa sababu wamepeleka kesi Mahakamani, ni haki yao wasikilizwe na Mahakama ili waweze kupata haki zao.
Mheshimiwa Spika, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba sisi kama viongozi tunalo jukumu kubwa sana la ku-influence wananchi wetu. Kwa hiyo, labda nikuombe tu kwa sababu hii kesi iko Mahakamani tuonane ili angalau nikupe mbinu za kushawishi wananchi hawa ili waweze kuondoa kesi yao na ikiwezekana huduma ya barabara iweze kupita kwa sababu ni muhimu sana katika ujenzi wa uchumi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kwamba zimekwenda huduma kwa wananchi sehemu ambazo tunatekeleza miradi, inaweza kuwa kweli kwamba pale ambapo wakati mwingine ujenzi wa barabara haujaanza au hata kabla ya kuwa na mradi wa barabara, yaweza kuwa kulikuwa na huduma, lakini wakati sasa mradi wa ujenzi wa barabara unakuja ndipo sasa pale tunalazimika kufanya zoezi hili la kuweza kuwaondoa wananchi lakini na kuwapa haki zao kwa mujibu wa sheria.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nafikiri ukiliangalia kwa ukaribu unaweza ukagundua kwamba ni wakati gani huduma ilikwenda na wakati gani mradi huu wa barabara umekuja. Ahsante sana.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Changamoto iliyopo Wilaya ya Kyela inafanana kabisa na Wilaya ya Mpanda katika barabara ya Stalike – Misunkumilo, bado wananchi wanadai fidia na ni miaka mitano sasa. Je, ni lini Serikali itawalpa fidia wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbogo anafuatilia sana juu ya wananchi hawa ambao wanastahili kulipwa au wana madai yao na amenipa barua ambayo inahusiana na madai haya.
Mheshimiwa Spika, lakini niseme tu kwamba sheria inaangalia pande zote; inaangalia upande wa wale wahusika ambao wana madai yao lakini pia inatazama kwa sisi Serikali wakati tunafanya malipo ya madai ya wananchi. Kwa maana hiyo, malipo yote yanafanyika kwa kufuata sheria.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia Sheria ya Barabara Namba 13 ya 2007, hasa section 16 inaonesha utaratibu unaotakiwa utumike kulipa fidia. Hii ni pamoja na kuitazama Sheria hii ya Utwaaji wa Ardhi (Land Acquisition Act), Sheria ya Ardhi yenyewe na Sheria ya Ardhi ya Vijiji pamoja na sheria nyingine.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo napenda kumwambia Mheshimiwa Mbunge avute subira wakati tunaendelea kutazama uhalali wa fidia hizo baada ya hapo wananchi hawa wataweza kupata haki zao. Kwa hiyo, nimtoe hofu lakini niwatoe hofu wananchi wa Nsimbo kwamba suala lao liko mikononi mwetu na tunaendelea kulishughulikia, haki za watazipata.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa maeneo ambayo barabara hii inapita sasa hivi ni miaka mitatu walishawekewa alama za X na hawajaambiwa nini kinaendelea kwa sababu wameshindwa kuendeleza hata maeneo yao. Naomba kauli ya Serikali, Mheshimiwa Waziri anaposema hapa mbele ya Bunge kwamba imetengwa shilingi bilioni moja sina uhakika kama amesoma vizuri hapo au amekosea? Nini kauli ya Serikali kuhusu wananchi hawa wa maeneo haya ambao wamewekewa alama za X?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu alama hizi za barabarani ni muhimu sana zinavyowekwa kwa sababu alama hizi zinaleta mawasiliano, zinawajulisha wananchi kwa ujumla kwamba eneo hili litakuwa na mradi wa barabara. Kwa hiyo, tahadhari hii inasaidia kwenye mipango yetu ya wananchi na upande wa Serikali kwa ujumla ili wananchi hawa wasije wakaweka vitu vya thamani kama sheria inavyotaka. Kwa hiyo, niseme tu kwamba alama ni muhimu zinavyokuwepo zinatuweka kwenye alert ili tuweze kujua kwamba kuna mradi mkubwa wa maendeleo unakuja.
Mheshimiwa Spika, nini kauli ya Serikali, niseme kwamba ujenzi wa barabara hii umeshaanza. Nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Chemba na Watanzania kwa ujumla, barabara hii tumeiainisha kati ya barabara ambazo zipo kwenye integration ya East Africa (mtandao wa barabara za Afrika Mashariki). Kwa hiyo, kuiweka katika mtandao wa barabara za Afrika Mashariki kunaonesha namna gani barabara hii tumeipa kipaumbele cha hali ya juu katika kuitafutia fedha.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaambie tu wananchi kwamba alama hizi zimewekwa kwa ajili ya kuwatahadharisha wasiweke vitu vya thamani kubwa wakati tunafanya maandalizi ya kulipa compensation (fidia). Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, ni mpango wa Serikali. Mimi niseme tu ukweli kwamba ujenzi wa barabara hii umeshaanza kwa sababu ujenzi tunaanza katika hatua tofauti; unaanza kwanza usanifu, michoro halafu sasa tunatafuta fedha na tumeuza mradi huu kwa wafadhili wanaofadhili Afrika Mashariki. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge uvute subira, mambo mazuri yanakuja. (Makofi)
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwanza mimi niishukuru Serikali kwa kujenga na kukamilisha barabara ya Dodoma hadi Babati kwa ufanisi na sasa inatumika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, cha kusikitisha ni kwamba vyombo vya usafiri kutoka Dodoma, Singida, Babati wanatoza nauli kiasi cha shilingi 17,000 hadi shilingi 20,000 na wanatoza kiasi hichohicho kutoka Dodoma kupita Kondoa kwenda Babati, umbali ambao ni sawa na Dodoma kwenda Iringa kwa gharama ya shilingi 8,000 hadi shilingi 10,000 tu.
Je, Serikali iko tayari kurekebisha hitilafu hiyo ili wajasiriamali wetu sasa watoke Babati asubuhi kuja kufanya ujasiriamali katika Jiji la Dodoma kwa ufanisi na kwa nauli nafuu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia suala la nauli kwa wananchi kwa ujumla lakini pia kwa kufanya mchanganuo ambao nimemsikiliza hapa.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba pale nauli zinapopanda zinawiana na ubora au ubovu wa barabara. Kwa hiyo, yaweza kuwa labda watumiaji wa barabara hiyo walikuwa wamekariri nauli kubwa wakati barabara haikuwa nzuri.
Kwa hiyo, nizichukue pongezi zake lakini hili suala tutalifanyia kazi, ziko mamlaka zinazoshughulika na masuala ya nauli ili waweze kuona stahili kamili ya nauli katika barabara hii Mheshimiwa Mbunge aliyoitaja ili tuweze kuchukua hatua zinazostahili. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Sera ya Ujenzi inaelekeza kuunganisha mikoa na mikoa kwa kiwango cha lami na kumekuwa na kilio cha muda mrefu na ahadi ya muda mrefu ya ujenzi wa kiwango cha lami ya barabara ya kutoka Njiapanda – Karatu – Mang’ola - Lalago. Je, ni lini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli ni sera ya Serikali kuunganisha mikoa na mikoa. Kwa hiyo, tunaanza kuunganisha mikoa na mikoa, tunaungamisha mikoa pamoja na nchi za jirani na hizi harakati zinaendelea, zipo barabara chache sana ambazo zimebakia kuunganishwa kwa maana ya mikoa kwa mikoa.
Mheshimiwa Spika, kwa barabara kubwa ambazo zimebakia ni chache ikiwemo barabara hii ambayo Mheshimiwa Mbunge anaitaja ikiwa inatokea kule Simiyu – Lalago – Sibiti – Mbulu – Karatu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba ukitoka Sibiti yako matawi mawili ya barabara, iko barabara ambayo inapita kandokando ya Mto Eyasi kwenda Karatu na hii barabara ambayo inapita Haydom – Dongobesh - Mbulu Mjini lakini itaunganika na barabara inayotoka Mbuyu wa Mjerumani - Mbulu Mjini - Karatu.
Kwa hiyo, hizi barabara zote ziko katika hatua mbalimbali. Barabara inayopita Eyasi tayari michoro yake imeshakamilika tunatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi na katika bajeti hii iliyopitishwa na Bunge lako tumetenga fedha za kuanza ujenzi katika maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, lakini kizuri pia nimjulishe tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa maeneo ya Lalago kuja upande huu wa Manyara na Arusha kwamba pale Sibiti tulikuwa na tatizo kubwa sasa ujenzi wa lile daraja unakamilika, vile vyuma ambavyo tulivisubiri kwa muda mrefu vilishafika na baada ya mvua kupungua tutapandisha vile vyuma hata kabla ya harakati za kukamilisha lami basi wananchi wataweza kupita kutoka Lalago kuja katika mikoa hii pamoja na kuja Singida. Tutapunguza kilometa karibu 400 kwa mtu anayetoka Mwanza na Simiyu kwenda Karatu kama atapita pale Sibiti akipitia Eyasi kwenda Karatu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge vuta subira, sisi tumejipanga vizuri na Serikali inaendelea kutoa huduma na kuunganisha mikoa.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Spika, ahsante na ubarikiwe kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, tunaposubiri ujenzi wa barabara kutoka Handeni - Singida na Waziri amezungumzia ubora wa barabara ile tukitambua kuna milima na mabonde. Nini kauli ya Serikali kuhusu ubora wa barabara ya kutoka Sekenke - Shelui ambayo imekuwa ikiua watu takribani kila mwezi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nikupongeze sana Mheshimiwa Martha Mlata kwa kufuatilia barabara za Singida na kila wakati tumezungumza ndani na nje ya Bunge, unafuatilia sana hizi barabara.
Mheshimiwa Spika, nimuahidi tu Mheshimiwa Martha na watumiaji wa barabara hii wakiwemo wananchi wa Singida kwamba tumeiona barabara hii. Barabara hii hatutaitazama upande wa Sekenke tu, tutaitazama kutoka Singida Mjini tunakwenda mpaka Misigiri tunashuka Sekenke. Tumetenga fedha ya kuweza kufanya usanifu wa barabara hii kwa sababu imekuwa ni ya muda mrefu na imechakaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Singida na Watanzania kwa ujumla kwamba sasa hivi tunakwenda na teknolojia mpya kwa barabara hiyo kama unavyoona kwa ile miteremko ile lami inakimbia. Kwa hiyo, tutaiangalia ili tuitengeneze kiasi kwamba ubora wake uwe mkubwa zaidi na watumiaji wa barabara watumie vizuri na pia kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Mheshimiwa Kalanga na Mheshimiwa John Mnyika, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; moja kati ya barabara muhimu za ring road ama barabara za pete ambazo zimeainishwa hapa ni barabara ya Goba kwenda Makongo – Chuo cha Ardhi, barabara hii kama ambavyo mnafahamu kwa siku yanapita magari zaidi ya laki moja (100,000) lakini vilevile ni barabara yenye umuhimu mkubwa sana pale ambapo tutakuwa tunajenga interchange ya pale Ubungo kwa sababu magari mengi yatahitaji barabara za kuweza kuchopoka kwenda Mbezi na hatimaye Morogoro Road.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nipate majibu ya Serikali, kwa sasa zimejengwa kilometa nne tu halafu zinaonekana zime-stuck hakuna kitu kinachoendelea. Naomba majibu ya Serikali ni lini uendelezaji wa barabara kwa kilometa tano zilizobaki utafanyika kwa kiwango cha lami? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, maelezo ama majibu ya Mheshimiwa Waziri yanaainisha kama vile barabara ya Goba – Madale – Tegeta Kibaoni imekamilika, lakini ukweli ni kwamba barabara iliyokamilika ni kipande cha Goba, kipande cha Goba – Madale ndiyo kinajengwa sasa hivi kwa kilometa tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri ambayo inaanza sasa kufanywa, swali langu ni dogo, kiwanda cha Twiga kimekuwa kinafanya matumizi mabovu ya hii barabara kwa kupaki magari yake barabarani, hali ambayo inahatarisha uhai wa barabara, lakini inahatarisha uhai wa wananchi wetu. Kama Serikali ya mtaa imejaribu kuingilia kati, Serikali ya Kata imeingilia kati, Mbunge nimeingilia kati, lakini kiwanda kinaonekana ni kiburi. Nataka commitment ya Serikali kwamba itafuatilia kiwandani ili matumizi ya barabara yaachwe kwa ajili ya barabara na isihatarishe uhai wa wananchi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nashukuru kuona kuwa, Mheshimiwa Halima Mdee anatambua juhudi kubwa ambazo Serikali hii inazifanya katika kujenga barabara na kuweza kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyopitisha kwenye bajeti barabara zinazohusiana na kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam ziko kama kilometa 156, baadhi ya barabara zimekamilika lakini baadhi ya barabara juhudi zinaendelea kuweza kukamilisha. Kwa hiyo, niseme tu kwamba Mheshimiwa Halima, hii barabara ambayo unaizungumzia barabara ambayo inapita Madale kwamba kuna kipande cha kilometa tano kinaendelea kukamilishwa, ni mpango wetu na hata ukiangalia kwenye bajeti ni kuweza kuikamilisha barabara hii nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe tu avute subira na wananchi wavute subira, tunafahamu umuhimu na uharaka wa kutengeneza barabara katika Jiji la Dar es Salaam kupunguza msongamano.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko awamu nyingi zitakuja, kila awamu ikikamilika ni fursa ya kuanza awamu nyingine ili hatimaye tumalize kabisa msongamano katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumza juu ya barabara kipande ambacho unasema kilometa tano kutoka Makongo Juu kwenda Chuo cha Ardhi, najua tunafanya juhudi ya kumaliza tatizo la compensation eneo lile ili wananchi waweze kupisha barabara ikamilike. Niseme tu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na watumiaji wa barabara kwamba, ni mkakati wa Serikali kwamba wakati wa ujenzi wa interchange ya Ubungo barabara hiyo anayoitaja Mheshimiwa Mbunge ni muhimu sana. Ni muhimu sana kuhakikisha kwamba tunapunguza msongamano kipindi chote cha ujenzi wa barabara pale Ubungo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo Serikali tunaona uko umuhimu na kwa haraka sana kukamilisha barabara hii. Kwa hiyo avute tu subira, barabara hii tutaitengeneza pamoja na barabara zingine. Iko mipango mingi tu mizuri katika kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe tu Mheshimiwa Halima, akisoma pia kwenye hotuba ya bajeti ambayo Mheshimiwa Waziri aliwasilisha hapa ukurasa wa 17 hadi wa 18 na ukurasa wa 25 ataona mambo mazuri yaliyoko huku. Angepitia tu ili aone namna tulivyojipanga kuhakikisha kwamba Dar es Salaam inabakia vizuri barabara zinakuwa zinawasaidia wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kiwanda cha Twiga Cement kupaki magari, naomba nilichukue hilo, lakini niseme tu kwamba tunao mpango kabambe wa kuwashughulikia wanaotumia barabara vibaya katika Jiji la Dar es Salaam, pia tunafanya patrol na kwenda na mizani ile ya kuhama.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe tu watumiaji wa magari, siyo hao wa barabara hii lakini na maeneo mbalimbali ambao na wengine wanatumia wakati wa usiku. Tumeshaliona hilo tunalifanyia kazi ili kuhakikisha kwanza magari yanaegeshwa vizuri kwa ajili ya usalama, lakini pia kwa ajili ya kufanya barabara zetu zisiweze kuharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili nimelichukua nakushukuru tutaendelea kulifanyia kazi ili tuweze kuondosha hili tatizo. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Hali ya ahadi kwa barabara za Dar es Salaam inafanana sana na ahadi ya barabara ya Tanga - Mabokweni - Maramba - Bombo Mtoni - Kitivo hadi Same ambapo barabara hii ilikuwa kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami kupitia fedha za MCC II, lakini mradi ule ukashindikana. Sasa ni lini Serikali itaanza usanifu wa barabara hii ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, najua suala la barabara hii ya Tanga - Maramba Mawili- Bombo Mtoni kupanda mpaka kwenda upande mwingine tunakwenda Same na upande mwingine tunapita Lushoto, barabara hii nimeipita nimeiona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ilikuwa kwenye mpango hauku-mature nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge na mara nyingi nampa feedback kwamba tunaitazama sasa ili tuone namna bora ya kuweza kuitengeneza barabara hii muhimu. Wananchi wa Maramba kwa kweli barabara hii nilipita niliiona wana shauku kubwa sana ya barabara hii. Mheshimiwa Mbunge naomba avute subira na nitaendelea kumpa mrejesho namna tunavyoweza kujipanga kuitengeneza barabara hii.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Kwandikwa, ni mchapa kazi na msikivu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, barabara hii ya Nyakahanga – Nyabionza – Chamchuzi kwenda Nyakakika imekuwa korofi miaka yote na ndiyo maana wakati wa kampeni Mheshimiwa Rais aliona ipo haja ya kuweka lami kilometa 5 kipande cha Kajura - Nkeito. Mvua iliyonyesha imefanya mawasiliano ya hii barabara yawe magumu sana na maeneo mengine ya Karagwe, Mheshimiwa Naibu Waziri anawaambia nini wananchi wa Karagwe kuhusu kukatika kwa mawasiliano ya barabara hii na maeneo mengine ya Wilaya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi wanaoishi katika barabara za Bugene, Kasulo na Mgakorongo Mlongo wamesubiri kwa miaka mingi sana kupata fidia ili kuweza kujengwa lami barabara hizi. Je, ni lini wananchi hawa watalipwa fidia zao? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bashungwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza pongezi nazipokea lakini kwa ruhusa yako nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Bashungwa kwa sababu anazifuatilia sana barabara hizi za Jimbo lake. Nimwambie tu eneo lake hili ni kati ya maeneo ambayo yanaunganika na nchi za jirani, ndiyo maana kuna vipaumbele vingi tunavifanya kuhakikisha kwamba tunatekeleza sera ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi ya kuungana na wenzetu, kwa maana ya Intergration ya East Africa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza, ninawaambia nini wananchi, upande wa Serikali tunao mkakati ule wa kuhakikisha kwamba barabara hizi zote zinapitika wakati wote. Kwa hiyo, kama ilivyo kawaida tumetenga fedha mwaka 2017/2018, lakini mwaka 2018/2019 pia tunazo fedha za kuhakikisha kwamba tunaboresha. Kwa sababu, tumekuwa na mvua nyingi kama tulivyoshuhudia, labda niweke msisitizo tu, tumeelekeza TANROADS Mikoa yote na TARURA kwenye maeneo yote kuhakikisha wanayatambua maeneo ambayo yameharibiwa na mvua na kuleta gharama zake. Upo utaratibu wa kupata gharama za pamoja ili tuweze kurejesha hiyo miundombinu iliyoharibika. Kwa hiyo, niwatoe tu hofu wananchi wa Karagwe na Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaenda kurejesha maeneo haya ambayo yameharibiwa na mvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia ya muda mrefu, niseme tu kwamba kama ilivyo utaratibu suala la fidia ni la kisheria, sisi Serikali tutaendelea kulipa fidia kulingana na taratibu na sheria zilizopo, kwa hiyo, wananchi hawa wa Karagwe watalipwa fidia. Hata hivyo, Mheshimiwa Bashungwa azingitie kwamba katika bajeti tuliyopitisha, barabara aliyoitaja ya Bugene – Kasulo – Mlongo tunategemea kuipandisha hadhi kwenda kwenye kiwango cha lami (double surface dressing), kwa maana hiyo, uko umuhimu wa kuzingatia tunalipa fidia haraka ili wakati wa kuipandisha hadhi tuweze kwenda bila mkwamo wowote.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa daraja la Sanjo katika Mto Simiyu na kilometa 4 za lami Mjini Mwanhuzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Komanya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi za Viongozi Wakuu zipo nyingi na kuna baadhi ya maeneo ambapo ahadi zinaendelea kutekelezwa na maeneo mengine tunaendelea na utaratibu wa kuhakikisha kwamba tunatekeleza. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika kipindi hiki cha miaka mitano tutahakikisha sehemu kubwa ambazo viongozi wameahidi tunaendelea kutekeleza. Kikubwa tu ni kwamba kila wakati tunaendelea kufanya uratibu ili kuhakikisha hizi ahadi zinatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira. Maeneo haya nina interest ya kuyatembelea, nitatembea pia niweze kuona hili daraja alilolitaja pamoja na mipango mizima ya kuhakikisha kwamba ahadi zinatekelezwa, lakini kikubwa tunaboresha miundombinu ya barabara maeneo yote.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Miongoni mwa hizo ahadi napenda kusikia katika barabara ya kutoka Redio Habari…
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Redio Habari Maalum Arusha kwenda katika Hospitali ya Wilaya ya Oltrumet katika Halmashauri ya Arusha DC. Tungependa kusikia ni lini sasa mtatimiza ujenzi wa barabara hiyo kama ilivyokuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amina Molle, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema tunaendelea na uratibu wa kuona kwamba ahadi hizi zote zinatekelezwa, tumejipanga vizuri. Nimpongeze sana Mheshimiwa Amina Mollel kwa concern yake ya kuboresha barabara hii inayokwenda katika Hospitali ya Arusha DC maana tumeizungumza mara nyingi. Nami kwa uzito aliouweka Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge hili nilikuwa nimepanga kwamba nitatembelea Arusha, nilipotembelea safari iliyopita niliangalia barabara zingine hii sikuiona, ili tuweze kushauriana na kuweka msukumo kuhakikisha watu wanaoenda kupata huduma katika hospitali hii wanapita bila usumbufu wowote, kwa hiyo, tutaifanya namna hiyo.
MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo ya Karagwe yanafanana sana matatizo ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala kuhusiana na barabara kutoka Newala kupitia Kitangali hadi Mtama. Je, ni lini sasa Serikali itatimiza ahadi yake ya kujenga kilometa 5 - 10, kuanzia pale Kitangali ambapo wameanza kujenga kilometa 3, kama Serikali ilivyokuwa imeahidi hasa ukizingatia ni sehemu korofi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Akbar, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa ujumla kwamba tunatambua mahitaji ya uboreshaji wa barabara hasa upande wa Kusini. Hii barabara anayoizungumzia Mheshimiwa Mbunge niliipita wakati nikiangalia barabara ile ya Kutoka Mtwara kwenda Mnivata tunavyoendelea kujenga kwa kiwango cha lami. Nimeona barabara hii ya Newala – Mtama lakini pia hicho kipande kingine cha kutoka Tandahimba kwenda Mtama ni muhimu sana kwa vile maeneo haya kwa kweli yanazalisha sana korosho na mazao mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Newala kwa ujumla kwamba barabara hizi tunazitazama. Nami nimeziona barabara hizi na hata ile barabara ya ulinzi ina umuhimu wake. Kwa hiyo, nimwambie tu kwamba Serikali tunalitazama kwa macho mawili eneo hili ili tuweze kuendelea kuboresha. Tumeshaanza na hizi kilometa 3 lakini tutaendelea ili kuhakikisha barabara hii inapitika wakati wote na kuiboresha zaidi.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Meneja wa TARURA wa Lindi DC, hii barabara sasa hivi iko kwenye matengenezo, kipande cha kutoka Nangalu kwenda mpaka Moka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii inahusisha Halmashauri mbili, Manispaa ya Lindi kwa eneo la Mtange, Chikonji na maeneo ya Kineng’ene pamoja na Lindi DC. Sasa nilitaka kujua, ili barabara hii yote ikamilike ni Meneja gani wa TARURA anahusika kwa sababu barabara hii ni zaidi ya kilometa 50 na inahusisha Manispaa pamoja na Lindi DC?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kama nilivyosema kwenye swali la msingi kwamba Mheshimiwa Rais alikwenda Nangalu wakati wa kampeni, akaahidi barabara hii ataipandisha hadhi na kuna vitu aliviangalia ndiyo maana akaahidi hivi. Sasa Mheshimiwa Waziri naomba mtufikishie salamu hizi kwamba ile ahadi ya Mheshimiwa Rais kuna haja ikatekelezwa kwa sababu ya umuhimu na urefu wa barabara hii. Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Bobali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza zile pongezi ambazo amezielekeza TARURA nazipokea na tutazifikisha TARURA. Niseme tu ni azma ya Serikali kwa kweli kuja na TARURA ili kuhakikisha kwamba barabara zetu sasa tunazisimamia na tunazitengeneza kwa kufuata weledi (Professionalism).
Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA ni mwaka tu toka waanze na wameanza kwa kupokea bajeti iliyokuwa kwenye Halmashauri na wameanza vizuri na uratibu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wameratibu barabara zote, kwa maana kwamba sasa hata allocation ya mafungu itakwenda kwa kulingana na kuwiana na mahitaji ya barabara zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la barabara hii aliyoitaja kuhusisha Lindi Manispaa na Lindi DC, uko utaratibu wa usimamizi wa barabara. Kama hii barabara aliyoitaja imetajwa kwa maana ya kwamba ina jina moja project namba fulani, kama itaunganisha barabara zote utaratibu wetu kama Serikali ni kwamba mafungu yanaweza kutengwa kupitia TARURA upande mmoja lakini upo utaratibu wa hawa Mameneja kuwasiliana kuhakikisha kwamba barabara inakwenda kwa standard zilezile. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi lengo ni kuhakikisha barabara aliyoitaja itapata huduma bila kujali Meneja yupi amesimamia. Cha msingi ni kupeana mrejesho kama kuna sehemu ambayo tunatakiwa kuitazama kwa umakini zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ahadi za Mheshimiwa Rais kama alivyosema, hizo salamu kwa kweli Mheshimiwa Rais amezisikia, tunakushukuru sana kwa pongezi zako. Kwa kweli ni hulka nzuri kutoa kutoa shukrani pale ambapo jambo jema limetokea. Kwa hiyo, nasi tukupongeze sana Mheshimiwa Mbunge na tutaendelea kushirikiana, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kutokana na umuhimu wa barabara hii ambao unatupeleka kwenye Stiegler’s Gorge na kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Pwani katika maeneo ya Kibiti, je, ni lini barabara hiyo itakamilika kwa kiwango cha lami ili masuala ya kiuchumi ya Stiegler’s Gorge, kilimo na utalii yaweze kunufaika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa tatizo hilo linafanana na tatizo lililopo la kuunganisha kati ya Wilaya ya Malinyi Mkoa wa Morogoro na Namtumbo Mkoa wa Ruvuma. Je, ni lini barabara hiyo inayounganisha Malinyi, Kilosa Mpepo, Londo mpaka Lumecha itaweza kujengwa angalau ipitike kwa kiwango cha changarawe kwa sababu sasa hivi haipitiki kabisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaona umuhimu wa kutengeneza barabara hizi ambazo zinaelekea eneo hili la Stiegler’s Gorge kwa kutokea Kibiti hali kadhalika ile barabara inayotokea upande wa Morogoro kama nilivyojibu katika swali la msingi. Mheshimiwa Mbunge atakumbuka pia katika mwaka wa fedha kuna kiasi cha shilingi bilioni 5 zilitengwa na kupitishwa na Bunge kwa ajili ya kuboresha barabara hii kutoka Kibiti kuelekea sehemu ya Stiegler’s Gorge.
Mheshimiwa Spika, jambo kubwa niseme kama Serikali tumejipanga kwanza kuhakikisha barabara hii inapitika ili iweze kutoa huduma kwa shughuli ambazo zitakuwa zinaendelea kufanyika katika eneo hili. Ule utaratibu wa kujenga katika kiwango cha lami utafanyika katika siku za usoni.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, barabara inayotoka upande wa Malinyi, Kilosa kwa Mpepo kwenda Lumecha kule Namtumbo ukitokea Ifakara (km 499) usanifu ulishakamilika, Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kujenga barabara hii. Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge avute subira pindi fedha zitakapopatikana barabara hii muhimu itaanza kujengwa. Hata hivyo, kuhusu kuboresha barabara hii ipitike Mheshimiwa Mbunge anafahamu yako maeneo ambayo ni hatari, yana milima mikali, tunajipanga ili kuhakikisha kwamba tunafungua barabara hii ili iweze kupitika muda wote kabla hatujaijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, kwanza niruhusu niipongeze Serikali kwa siku za karibuni imeongeza kiwango cha usimamizi wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Nyakanazi kuelekea mpaka Kabingo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa barabara hiyo inajengwa na inaishia katika kijiji cha Kabingo; na kwa kuwa kipande cha kutoka Kabingo kwenda mpaka Kibondo, Kasulu hadi Kidahwe bado ni vumbi. Je, kwa muendelezo huohuo ambao Serikali imetuonyesha, ina mpango gani sasa kipande cha kutoka Kabingo kwenda Kibondo, Kasulu mpaka Kidahwe kiweze kutekelezwa ili Mkoa wa Kigoma uweze kufunguka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Chiza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Chiza kwa kuchaguliwa na wananchi wa Buyungu kuwa Mbunge na Mwakilishi wao na namkaribisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utaratibu wa kujenga barabara katika Mkoa wa Kigoma. Nafahamu na Mheshimiwa Chiza anafahamu pia kwamba barabara ya kutoka Nyakanazi kuja eneo lake ujenzi unaendelea, lakini utaratibu ule wa manunuzi unafanyika na hivi karibuni kilomita karibu 87 hivi zitaanza kujengwa zikipita katika eneo hili la Kabingo kama alivyolitaja. Pia kilomita zote 300, Serikali iko katika hatua nzuri ya kujenga kwa maana ya kutoka sasa upande wa Kakonko, Kibondo kwenda Kasulu na viunga vyake vinavyoenda kuunganisha nchi ya Burundi kwa maana ya Manyovu na kipande kile cha Mabamba.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatua iliyofikiwa ni nzuri na kwa vile Mheshimiwa Mbunge yupo nafikiri itakuwa ni vizuri sasa tuzungumze ili angalau nikupe picha ili uweze kuona na kutimiza wajibu wako kama Mbunge wakati ukiwawakilisha wananchi wako kwamba Serikali imejipanga vizuri kujenga barabara hizi.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na vilevile nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ajali nyingi zinazotokea katika Wilaya ya Mbeya na hasa katika Milima ya Uyole na Mbalizi. Je, ni lini Serikali itafanya upanuzi wa barabara zinazoelekea kwenye nchi za jirani za Zambia na Malawi?
Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itajenga by pass ya Inyala – Simambwe na Inyala – Songwe? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza niseme kwamba study zilizofanyika zinaonyesha kuwa ajali nyingi zinazotokea asilimia 78 zinatokana na makosa ya kibinadamu (human behavior) na asilimia 12 iliyobaki ndiyo inasababishwa na mambo mengine ikiwepo miundombinu. Kwa ajali ambazo zinatokea katika Mkoa wa Mbeya niseme tu ajali iliyotokea juzi kwa mfano nimepata fursa ya kuwepo Mbeya juzi, eneo ajali ilipotokea ni eneo ambalo barabara ni nzuri na alama za barabarani zipo, inawezekana lilikuwa tatizo la kiufundi lakini tu kwa ujumla wake Serikali imechukua hatua ya kuendelea kuboresha barabara za Mbeya kwa sababu nature ya eneo la Mbeya ni milima na miteremko mirefu ili kuweza kupunguza ajali kwa maana kwamba ile barabara sasa anayoitaja Mheshimiwa Mbunge Inyala – Simambwe ni kati ya barabara ambazo tunaendelea kufanya usanifu ili tuweze kupunguza ule msongamano mkubwa wa magari.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa ujumla wake tu ninapende kutoa wito kwa watumiaji wa barabara kwamba maeneo haya ambayo yanakuwa na milima mikali na alama za barabarani zipo, watumiaji wa magari tuzingatie hizo kanuni za barabarani ili tupunguze ajali wakati Serikali inafanya juhudi za kuboresha barabara zake. Kwa hiyo, tatizo la Mbeya niseme kwa ujumla Serikali inalitambua na tunafanya haraka kuhakikisha kwamba tunaboresha miundombinu na kupunguza ajali katika eneo hili.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mwaka wangu wa nane nikiuliza swali la ahadi ya viongozi wetu ambao wamefika katika Jimbo la Nyang’hwale.
Mwaka 2010, Rais wa Awamu ya Nne alikuja akaahidi katika kampeni zake barabara ya lami kutoka Kahama – Nyang’olongo – Busolwa – Karumwa hadi Busisi, Sengerema kujengwa kwa kiwango cha lami. Mwaka 2015 pia Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli alikuja akaahidi vilevile.
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hii ya ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kahama – Nyang’hwale mpaka Busisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kuratibu ahadi za viongozi wakuu, kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema. Tayari tunaendelea kufanya uchambuzi ili kuendelea sasa kujenga katika kiwango cha lami. Hata hivyo, kwa barabara hii Mheshimiwa Mbunge anayoitaja kuja Kahama ni barabara ambayo kwenye mpango mkakati tumeiweka. Tuwasiliane tu uone namna tulivyojipanga kwa sababu tunaendelea kupata fedha kidogo kidogo ili uweze kuona na wakati mwingine uweze kuwapa taarifa wananchi wa Nyang’hwale kwamba ni lini sasa ujenzi utakuwa umeanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zile hatua za awali tumeshaanza, tunatambua umuhimu wa barabara hii kuiunganisha kutoka Sengerema kuja Kahama. Pia wananchi wajue kwamba eneo la jirani kabisa kutoka Kahama Mjini kwenda Geita, Bunge limepitisha fedha za kutosha, tutaanza ujenzi wa barabara hii ya lami. Kwa maana hiyo tunatambua umuhimu wa kutekeleza ahadi za viongozi pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge niwahakikishie tu kwamba tunaendelea kuhakikisha kwamba ujenzi wa barabara unafanyika.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Kilolo kuna barabara ambayo inaunganisha na Mkoa wa Morogoro, swali hili nimeshaliuliza zaidi ya mara tatu na ahadi ya Serikali ilikuwepo. Hivi leo ninavyozungumza wananchi wa Kimala, Itonya, Muhanga, Idete na Idunda wanafanya kazi kwa mikono, na mimi kama Mbunge nimechangia na wananchi wengine wamechangia.
Je, sasa Serikali itakuwa tayari na yenyewe kuchangia ili wale wananchi wa Kilolo kwa nguvu zao waweze kupasua barabara kuelekea Morogoro ambako naunganishwa na Jimbo la Mheshimiwa Susan Kiwanga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZU NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua umuhimu wa kuunganisha Mikoa. Kwa Mkoa wa Iringa tunao mpango wa kuunganisha eneo hili la Kilolo kuja Mkoa wa Morogoro kupitia Mlimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nimpongeze tu Mheshimiwa Mwamoto kwa sababu amekuwa mfuatiliaji mzuri na mwenyewe anafahamu hii barabara kutoka Iringa kuja Kilolo na sehemu ambayo ilikuwa inasumbua kwa maana ule mpango wa Halmashauri kufanya marekebisho ya maana alignment ya ile barabara; tumetoa maelekezo ili waweze kurekebisha ili wananchi ambao walikuwa wamepata usumbufu tatizo lao litakuwa limeondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge hii eneo hili tunalolizungumza ni kilomita chache sana, lakini kwa sababu ya nature ya eneo tunalifanyia kazi ili tuweze kukuunganisha na eneo la Mlimba.
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tatizo la uwanja ambalo limeongelewa na Mheshimiwa Matiko ni sawa sawa kabisa na tatizo la Uwanja wa Ndege wa Songea, uwanja ambao unahudumia Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Njombe. Tangu mwezi wa tatu mwaka huu uwanja huo umefungwa na hautumiki tena. Jitihada za Serikali kuleta ndege hazisaidii kwa sababu ndege haziwezi kutua katika uwanja huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni, je, ni lini uwanja huo utafanyiwa ukarabati na kuanza kutumika ili kuwanufaisha wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Njombe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua umuhimu wa huduma hii ya usafiri wa ndege katika Mkoa wa Ruvuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliarifu tu Bunge kwamba tulishapata mkandarasi wa kufanya ukarabati wa uwanja huu; taratibu za manunuzi zilikuwa zinakamilishwa ili ujenzi kwa haraka ufanyike. Sambamba na ukarabati wa uwanja huu wa Songea tutafanya pia uwanja wa ndege wa Iringa ili lengo sasa la kuweza kufanya haya mashirika ya ndege yaweze kujiendesha kwa faida kwa maana ya viwanja vyote vitatu cha Mtwara, Ruvuma pamoja na Iringa kwa pamoja tukikarabati tutafanya na wao waweze kufanya kazi kwa tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa vuta subira, tuko tayari kufanya matengezo kwenye uwanja huo. (Makofi)
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Njombe una uwanja wa ndege lakini wa nyasi; lakini katika ule uwanja kuna wananchi wana nyumba pembezoni mwa ule uwanja. Hakuna mipaka ya uwanja na hawaruhusiwi kuendeleza maeneo yao. Je ni lini Serikali itaenda kufanya utambuzi na kuwalipa fidia wale wananchi ili wapishe ule uwanja?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwalongo jirani yangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua changamoto zilizokuwepo kwenye Uwanja wa Ndege wa Njombe na hata hivi karibuni Mheshimiwa wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano amefika Njombe kwa ajili ya kuona namna bora ya kuweza kukamilisha na kuweka mipaka katika eneo hili. Kilichokuwa kimetuchelewesha ilikuwa pia ni wazo la Mkoa kuweza kuomba kuhamisha uwanja katika eneo hili. Hata hivyo baada ya mazungumzo nafikiri sasa tuko tayari kuweka mipaka hiyo ili na ukarabati wa uwanja huu kati ya viwanja 11 uweze kufanyika.
MHE. MARTIN A. M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri yenye kutia moyo wananchi wa Mbinga na Nyasa nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kujenga kwa kiwango cha lami barabara inayotoka Mbinga kwenda Litembo hospitali kupitia Kijiji cha Muyangayanga, Kindimba na Mahenge, je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali kupitia swali namba 438 lilojibiwa hapa Bungeni tarehe 27 Juni, 2016 ilisema kwamba taratibu za kumpata mwandisi mshauri kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa barabara inatoka Kitai hadi Lituhi ulikwishakamilika, je, barabara hii ya kutoka Kitai hadi Lituhi itajengwa lini kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali tunaendelea kuratibu ahadi za viongozi ili kuhakikisha kwamba ahadi hizi zinatekelezwa. Yako maeneo ambayo kwa kiasi kikubwa ahadi zimeshatekelezwa na yako maeneo ambayo pia tunaanza kufanya utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge na kwa vile amekuwa mfuatiliaji mzuri labda saa nyingine tuonane kwa sababu ninalo kabrasha ambalo linaonesha hatua mbalimbali ya hizi barabara ambazo zimeahidiwa na viongozi ili tuweze kuona lakini aweze kuwa na uhakika na hatimaye awaeleze wananchi wa eneo la Mbinga Vijijini juu ya hatua ambayo tumeshaifikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kwamba amewahi kujibiwa hapo awali kwa ujenzi wa barabara hii ya Kitahi – Lituhi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ziko barabara nyingi ambazo usanifu wake umekamilika, Serikali inajipanga kutafuta fedha ili kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo barabara hii ya Kitahi - Lituhi nimeipita kwa sababu najua pia tunajenga daraja kubwa katika Mto Luhuhu, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mbinga ni kwamba kwanza barabara hii tumeiboresha sana kuhakikisha inapitika na kwa umuhimu wa ujenzi wa hili daraja kubwa tunapitisha material mbalimbali katika eneo hili kuliko kuzunguka kupitia kule Madaba. Kwa hiyo, tunaendelea kuiangalia kwa makini barabara hii lakini wakati huo tunatafuta fedha ili kiweza kujenga barabara katika kiwango cha lami.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba, barabara ya kutoka Isandula, Magu inayopita Bukwimba kuja Ngudu mpaka Gungumalwa ni ahadi ya siku nyingi kwamba itatengenezwa kwa kiwango cha lami. Tungependa kujua sasa kwa sababu mwanzo tuliambiwa kwamba upembuzi yakinifu umeshakamilika, upembuzi wa kina umeshakamilika, wananchi wa Magu, Kwimba wanataka kujua sasa barabara hiyo itaanza kujengwa lini kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu mara nyingi sana amekuwa akifuatilia barabara hii. Niseme tu kwa ufupi kabisa upembuzi wa kina unaendelea kukamilishwa, ni hivi tu jana Meneja wa TANROAD, Mkoa wa Mwanza amepokea report ya awali ya usanifu wa kina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo tunafanya mapitio ili sasa tuweze kukamilisha zoezi hili. Zoezi hili likikamilika litatuwezesha kujua gharama za mradi ili sasa tuiweke kwenye bajeti na hatimaye tutafute fedha kwa ajili ya kuijenga barabara hii kutoka Isandula Magu kupitia Bukwimba kuja Hungumwalo.
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa Serikali imeanza kujenga barabara ya Bariadi na barabara ya Magu Ndagalu tumejenga vipande viwili, hapa katikakati barabara ya Magu – Ndagalu - Bariadi ni lini itakamilishwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili la Bariadi, Magu tuna miradi mingi ambayo inaendelea kujengwa na Mheshimiwa Mbunge anatambua pia tunajenga daraja la Sukuma kwa nia ya kuboresha eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu network ya barabara katika eneo hili ni kubwa, tuonane ili angalau nimpe hatua ambayo tumefikia, lakini ni dhamira ya Serikali kuhakikisha maeneo haya yanaunganishwa vizuri ili wananchi waweze kujiimarisha kuchumi.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali moja. Kwa kuwa tayari Serikali imeshakubali kujenga barabara ya lami kutoka Mpwapwa kwenda Kongwa, ninachotaka Mheshimiwa Naibu Waziri awathibitishie wana Mpwapwa ni lini barabara hiyo itaanza kujengwa na kiasi gani kimetengwa kwa sababu ni muda mrefu, sasa ni mwezi wa Tisa?(Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO – (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi barabara hii ya kutoka Mpwapwa kuja Kongwa ni sehemu hii ya barabara ambayo inakuja mpaka eneo la Mbande na kwa kiasi kikubwa barabara hii inaendelea na ujenzi. Najua concern ya Mheshimiwa Mbunge ni ule ujenzi wa barabara hii sasa kuwa na kasi kubwa kutokea Mpwapwa kuja Kongwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kiasi cha fedha ambacho kimetengwa, najua tumetenga fedha, tuwasiliane tu na Mheshimiwa Mbunge ili angalau basi tuone kwa undani kwamba ni kiasi gani kimetengwa. Nimhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mpwapwa eneo la Mpwapwa nimelitembelea tumejipanga ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Mpwapwa wanaunganika vizuri na Makao Makuu ya Nchi hapa Dodoma.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka nimkumbushe tu kwamba jambo hili lipo ndani ya Ilani na kwa kuwa ni msikivu na Mheshimiwa Eng. Kamwelwe ni msikivu zaidi, naomba jambo hili walisimamie ili liweze kukamilisha ndoto ya Watanzania ambao wamekuwa wanalala pale, hasa panapotokea matatizo ya ajali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali dogo, pamoja na matatizo yaliyopo katika Daraja la Wami, lakini pia iko ahadi ya Serikali ya kutengeneza barabara inayotoka Mbwewe - Mziha - Kibindu, je, hili jambo nalo Mheshimiwa Waziri mmefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nizipokee pongezi nyingi ambazo amezitoa kwa Serikali, lakini pia nimpongeze yeye binafsi kwa namna anavyofuatilia masuala mbalimbali katika jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii ya Mbwewe – Mziha – Kibindu inafanyiwa matengenezo makubwa. Kuhusu kuiboresha barabara hii, nimuombe tu Mheshimiwa Ridhiwani, kwa sababu ni mfuatiliaji mzuri, baadaye tuonane ili tuangalie kwenye bajeti na mipango yetu ili niweze kumpa taarifa sahihi ili aweze pia kuzitumia kuwajulisha wananchi wa Jimbo la Chalinze. (Makofi)
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile Serikali imetenga pesa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Bagamoyo – Pangani - Tanga. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri kama yuko tayari ujenzi huo kutumia wakandarasi wawili ili mmoja aanze Tanga mwingine aanze Bagamoyo kwa madhumuni ya kuharakisha ujenzi lakini kuwapa faraja pia wananchi wa pande hizo mbili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu anatambua kabisa hatua nzuri za ujenzi wa barabara hii upande wa Serikali tulipofikia kwa vile anaendelea kufuatilia vizuri. Nichukue tu wazo lake kama ushauri ili wakati sasa wa kuanza ujenzi tutaona namna nzuri ya kufanya lot ili tuone kama hilo analolisema tunaweza tukalifanya tutaweza kulitekeleza.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nishukuru kwa kilio chetu watu wa Kanda ya Kaskazini…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa sisi watu wa Kanda ya Kaskazini kwa maana ya Mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimajaro, Manyara na Pwani, kilio chetu kusikilizwa na Serikali kwa ujenzi wa Daraja Jipya la Wami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na ujenzi wa daraja jipya, tatizo kubwa limekuwa ni magari aina ya semi kushindwa kupanda milima sababu ya mlima mkali uliopo pale. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuweka magari maalum ya kusaidia kuvuta haya magari ya semi pale ambapo yanashindwa kupanda milima kama ilivyo kwa njia ya Kasumulu Boarder karibu na Malawi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbarouk, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la magari kushindwa kupanda katika milima ni suala ambalo kwa upande wa Serikali tunaendelea kulitazama kwa sababu ya ukuaji wa teknolojia na magari yanayokuja sasa yamekuwa ya kisasa zaidi. Tunaliangalia kwa upana wake kwa sababu kwa records za ajali ambazo zimetokea hivi karibuni tunayo pia mashaka ya kuona namna gani magari haya yanakuja ya kisasa lakini pia madereva ambao wanaendesha magari haya waweze kupata elimu ili waweze kumudu kuyaendesha. Kwa hiyo, mara nyingi unaona technical faults zinazotokea inawezekana kuwa uko uwiano kati ya teknolojia mpya na elimu ambayo wanaipata madereva wetu. Kwa hiyo, tutaendelea kulifuatilia ili tuweze kutatua tatizo hili.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipa nafasi.
Katika Bunge lililopita niliweza kuorodhesha vijiji vya kata tatu ambavyo havina mawasiliano mazuri Kata ya Kala vijiji vyote; Kata ya Sintari kijiji kimoja na Kata ya Ninde vijiji viwili, nataka kujua, Serikali ina mpango gani wa haraka kuhakikisha kwamba mawasiliano yanapatikana katika vijiji hivyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni nayo orodha ya vijiji vingi hapa. Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tuwasiliane ili tuweze kuona hivi vijiji katika hizi Kata tatu alizozijata pamoja na hii Kata ya Kala na Minde ili tuweze kuona kwa sababu tunaendelea kupeleka hii huduma ya minara. Kwa hiyo, nakuomba tu tuwasiliane ili uwe na uhakikika kwamba vijiji vyako na kata hizi zote ziko katika hiyo orodha. (Makofi)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kumekuwa na ahadi nyingi sana na za muda mrefu kwenye mitaa ya pembezoni mwa Manispaa ya Mtwara Mikindani ambayo hakuna mawasiliano maeneo hayo na nimekuwa nikichangia ndani ya Bunge hili na kuyataja maeneo hayo kwa muda mrefu kwamba maeneo ya Namayanga, maeneo ya Naulongo, Mkunjanguo, Mbawala Chini na Mkangara, mawasiliano hayapo kabisa ya simu. Je, ni nlini Serikali hii itapeleka mawasiliano kwenye mitaa hii ambayo ni muhimu ndani ya Manispaa ya Mtwara Mikindani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mahitaji ni mengi ni kweli ahadi ni nyingi, lakini ni ukweli pia kwamba ahadi nyingi tunaendelea kuzitekeleza kadri tunavyokwenda.
Nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla, kadri tunavyoweka minara katika maeneo mbalimbali na baada ya minara kuwashwa bado tunahitaji kuona changamoto ambazo zitakuwa zimejitokeza baada ya hii minara kuwashwa kwa sababu suala la mawasiliano ni suala ambalo baada ya kuwasha minara inaweza ikajitokeza baadhi ya maeneo yakawa na uhafifu wa mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwaomba tu tuendelee kuwasiliana pamoja tunavyoendelea kutekeleza ahadi hizi. Lakini pia tuendelee kupata feedback baada ya minara kuwashwa ili tuhakikishe kwamba maeneo yote yanafikiwa na mawasiliano haya kupitia minara yetu.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika Wilaya ya Kakonko takribani kata sita zimepakana na nchi ya Burundi na Kata ya Lugenge na Kasuga nazo pia zimepakana na maeneo hayo ambayo hayana mawasiliano kwa njia ya simu. Mawasiliano ni hafifu na ni shida kabisa, nataka kujua, ni lini Serikali itapeleka minara katika maeneo hayo kiusalama kwa sababu maeneo hayo yamekaribiana na nchi ya Burundi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi nikupongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu kuna mambo mengi kweli unafuatilia katika maeneo haya. Ni kweli maeneo haya yaliyo mpakani yana usumbufu mkubwa hii ni pamoja na mwingiliano kwa sababu niwahi kutembelea maeneo haya utaona kabisa kwamba tunapata mawasiliano kutoka nchi za jirani. Tutahakikisha tu Mheshimiwa Mbunge tunajenga minara ili pia iweze kupunguza ule mwingiliano wa mawasiliano ambayo yanatokea nchi za jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe pia tuwasiliane nina orodha ndefu hapa ili tuje tuone maeneo haya kama hatujaya-cover basi tuendelee kupeleka minara mingine.
MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kwenye jibu lake la msingi amekiri kwamba tathmini ilifanyika 2012/2013; swali sasa watu hawa wamekatazwa wasiendeleze na nyumba zao zimebomoka na tathmini hairudiwi na anasema kwamba mkandarasi anaanza ujenzi; je, anaanzaje ujenzi wakati wananchi hawa hawajalipwa fidia yao?
Swali la pili, kwa kuwa tathmini ilifanyika 2012/2013 na sasa hivi ni miaka mitano imepita, je, Serikali ina jibu gani kuhusu kurudiwa kwa tathmini au malipo yao itakuwa vipi kwa sababu nyumba nyingine zimebomoka na nyingine zimeanguka. Ni mkakati gani ambao wataufanya ili wananchi wale waweze kupata malipo yao kwa tathmini mpya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, eneo hili la barabara ya kutoka TAMCO kwenda Mapinga ni barabara muhimu sana, hivi ninavyoongea tunaendelea na utaratibu wa kuhakikisha ujenzi unafanyika ili kuweza kukamilisha kilometa tano za eneo hili. Eneo hili ni muhimu sana kwa sababu barabara hii sehemu ambayo tunayoanza kujenga ndiyo maeneo ambayo ndiyo kitovu cha Mji wa Kibaha kwa maana ya kwamba maendeleo yanafanyika katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa eneo hili ujenzi unaanza, lakini kuhusu fidia ni kwamba kumbukumbu muhimu za fidia katika eneo hili zimeshachukuliwa na kumbukumbu muhimu zimekubaliwa na wananchi ambao wamepisha eneo la ujenzi, kwa sababu hiyo haitaathiri malipo yao wakati ujenzi unaendelea.
Kwa hiyo, kikubwa tu niwapongeze na kuwashukuru wananchi wa eneo hili kwa uzalendo na kwa kweli nao wanahitaji hii barabara iweze kuwepo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge usiwe na wasiwasi tumeweka kumbukumbu vizuri na wananchi wameshasaini kukubali malipo ya kwao na pia upo utaratibu kama tukichelewa kulipa kuna viwango huwa vinabadilika kutokana na utaratibu uliopo.
Mheshimiwa Spika, pia kwa eneo hili ambalo ujenzi utaanza, utaratibu wa kuwalipa wananchi fidia upo mbioni, kwa hiyo niwatoe hofu wananchi kwamba wakati ujenzi unaendelea kufanyika na malipo yao yatafanyika hususani kwa kilometa hizo tano ambazo tumetathmini kwa sababu eneo lote hili la barabara wanastahili kulipwa kama shilingi bilioni 8.9 hivi. Kwa hawa wa kilomita tano, kama shilingi bilioni moja hivi itatumika kulipa fidia. Niwatoe wananchi wa maeneo haya watalipwa fedha zao kulingana na taratibu ili kupisha barabara hii muhimu kwa ajili ya maendeleo yao wao wenyewe.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana naomba niulize swali langu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa upatikanaji wa kivuko baina ya Kata ya Msinjahili na Kitumbikwera ulikuwa uende sambamba na ujenzi wa sehemu za kusubiria abiria; na kwa kuwa takribani mwaka mmoja umeshapita tangu kivuko kipatikane.
Je, lini Serikali itajenga sehemu za kusubiria abiria baina ya Kitumbikwera na Msinjahili ili kuwaondolea adha wananchi hawa?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa, kwa sababu suala hili amekuwa akilifuatilia sana ni muda mrefu na mimi nilifika eneo hili la kivuko na hali niliyoikuta pia nilitoa maelekezo ili tuweze kupata kibanda cha abiria na pia ujenzi wa huduma zingine.
Mheshimiwa Spika, ni furaha yangu tu kumueleza Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Lindi kwamba tumeshapata mkandarasi, ameshasaini Mkataba kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya abiria ya kusubiria usafiri, maeneo yote ya pande mbili za vivuko tutaweka pia huduma zingine kama vyoo vya kisasa na tumetoa maelekezo kwamba ujenzi uanze haraka kabla ya msimu wa mvua.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikupe tu taarifa kwamba tutasimamia kuhakikisha huduma muhimu katika maeneo haya yanapatikana haraka kabla ya mvua. (Makofi)
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa barabara ya Ngara Mjini - Nyamiaga - Murukulazo - Lusumo yenye urefu ya kilomita 24 ni barabara muhimu ambayo ipo chini ya Wakala wa Barabara (TANROADS) lakini ni barabaara inayounganisha Makao Makuu ya Wilaya na nchi jirani ya Rwanda na kuna mradi mkubwa wa umeme unaoshirikisha nchi tatu, je, Serikali iko tayari kupandisha barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami ikiwa ni pamoja na kujenga daraja kwenye Mto Ruvubu ambapo kwa sasa tunatumia ferry? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara ya Kumwendo - Kigarama - Mururama - Bukiriro ni barabara inayounganisha kata tatu, Kata ya Kabanga (kijiji cha Juligwa); Kata ya Mbuba na Kata ya Bukiriro. Kipo kipande cha Mkajagali ambacho kiko karibu na mto lakini barabara hii wakati wa mvua haipitiki inatakiwa kujengwa daraja na tayari Meneja wa TARURA alishapeleka maombi maalum ili kujenga box culvert mbili zenye kipenyo cha mita 2.5 kwa ajili ya kuunganisha kata hizi…
Mheshimiwa Spika, nauliza, Serikali iko tayari kutoa fedha kwa ajili ya kujenga daraja hili ili kurahisisha mawasiliano kwa kata hizi tatu, fedha zisizozidi shilingi milioni 300? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Gashaza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu barabara hizi naweza kuzifahamu kwa sababu tumezungumza naye mara nyingi sana. Nimpongeze wakati akizungumza imenipa nafasi ya kuzifahamu vema barabara hizi lakini pia kuona changamoto zilizokuwepo tuweze kuzishughulikia.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la kwanza, hii barabara ambayo inatoka Rusumo inapita ng’ambo kwenda Ngara ina urefu kama kilometa 24 hivi, najua kuna kivuko pale lakini barabara hii ni muhimu kwa sababu ujenzi wa barabara hii utatufanya sisi tutekeleze sera ambayo inataka mikoa yetu tuweze kuiunga na nchi za jirani na maeneo haya yanaunga upande ule wa Rwanda. Kwa hiyo, hiyo hii barabara itafupisha safari kwa wasafiri wanaotoa Rusumo kwenda Ngara. Ziko kata mbili hizi, niseme tu kwa maeneo hayo ya Murukuruzo na Nyamiyaga ni muhimu na pia tutaweka kivuko kwenye upande mwingine ambapo tunahamisha kile kivuko baada ya kujenga daraja.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo hili ili kutoa hiki kivuko ambacho tutakiweka tutakifanyia kazi. Nimuombe tu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera atazame eneo hili tuone uwezekano wa kuweka daraja. Kadri tunavyofanya improvement kubwa katika maeneo mbalimbali kwetu sisi ni fursa ili kuja na hatua zingine za kuendelea kutibu maeneo ambayo ni korofi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, eneo hili la Rulenge ni kweli yapo madaraja ya chini na ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo haya yanapitika. Kuna wakati mwingine tunapata mvua nyingi inalazimika wananchi wa maeneo haya kutopita kwa muda kupisha maji yapite na hivyo kuwa na usumbufu kidogo wakati wa mvua nyingi. Kwa hiyo, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba wamewasilisha maombi maalum, tutayazungumza ili tuone hili ombi maalum linashughulikiwaje ili hiki kiasi cha takriban shilingi milioni 300 kiweze kutumika kuboresha eneo hili.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, maeneo mengi nchini kunapokuwa na drift hizi ni kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapita maeneo haya wakati wowote. Kila wakati tunaendelea kufanya maboresho ya barabara zetu lakini tunaanza kutengeneza madaraja ili wananchi waweze kupita. Kwa hiyo, nimtoe hofu yeye pamoja na wananchi wa Ngara na hususan wa maeneo haya ya Rulenge kwamba eneo hili tutalitazama ili Kata hii ya Kabanga pamoja na kata mbili jirani zake ziweze kuunganika vizuri.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa ni suala la kisera kutengeneza kwa kiwango cha lami barabara zinazounganisha mikoa lakini pia ukizingatia ahadi ya Rais wa Awamu ya Tatu Mheshimiwa Mkapa na ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Kikwete na ahadi ya Waziri Mkuu wa sasa Mheshimiwa Majaliwa kuhusu kutengeneza barabara hii ya kutoka Mlowo Mkoa wa Songwe kupitia Kamsamba kwenda Kwera Mkoa wa Rukwa, ni kwa nini barabara hii imecheleweshwa? Je, hatuoni kama vile tunawadhalilisha viongozi wetu walioahidi ujenzi wa barabara hii? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali inasema mwaka wa fedha 2017/2018 zimetengwa shilingi milioni 1,439.021 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hii. Kama fedha hizi zilitengwa mwaka 2017/2018 zaidi ya shilingi bilioni 1.4 yako maeneo mbalimbali ambayo wakati wa mvua yalikuwa hayapitiki, mfano Vijiji vya Sasenga, Itaka, Nambizo, Utambalila na maeneo mengine...
Mheshimiwa Spika, naomba niuliza swali. Je, fedha hizi zilifanya kazi gani ikiwa maeneo mbalimbali yalikuwa hayapitiki msimu wa mvua? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Haonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nakubaliana naye kwamba ni sera ya Serikali kuunganisha mikoa na mikoa na kuunga mikoa na nchi za nje na utekelezaji wake unaendelea katika maeneo mbalimbali. Nafurahi kusikia Mheshimiwa Haonga anakumbushia ahadi za Waheshimiwa Marais na Waheshimiwa viongozi wetu. Kwa kweli akubaliane na mimi tu kwamba zile ahadi zilizotolewa kipindi cha nyuma ndiyo zimesababisha hata ujenzi wa hili daraja kuanza na pia usanifu na hatua mbalimbali za manunuzi zinaendelea. Kwa hiyo, nimtoe tu wasiwasi kwamba ule utekelezaji wa ujenzi wa barabara kama ahadi zilivyokuwa unaendelea kutekelezwa na tutaendelea kutekeleza na nimhakikishie tutaendelea kutekeleza kwa kasi zaidi.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki ambacho tumepita, Serikali imefanya juhudi kubwa sana kuhakikisha madeni mengi sana ya wakandarasi maeneo mbalimbali ya nchi yanalipwa. Kwetu sisi ni fursa sasa ya kuongeza kasi kwa ajili ya kuendeleza kukamilisha huu ujenzi. Kwa hiyo, tutaenda kuungana na wenzetu wa kule Rukwa kupitia barabara hii. Nimhakikishie Mheshimiwa Haonga baada ya Bunge hili nitaipita barabara hii ili niweze kuona pia hali ilivyo tuweze kushauriana vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili anasema kwamba katika kipindi kilichopita tulikuwa tumetenga fedha lakini wakati huu wa mvua kumekuwa na uharibifu na haoni sababu kwa nini sasa maeneo hayapitiki. Mheshimiwa Haonga ajue mwaka huu ulikuwa wa neema kwa upande mwingine lakini kwenye miundombinu kumekuwa na uharibifu. Ilikuwa siyo rahisi wakati mvua zinaendelea kunyesha twende kufanya matengenezo. Baada ya mvua kupungua, nimhakikishie Mheshimiwa Haonga, tunarudi sasa kurejeshea sehemu ambazo zilikuwa korofi wakati hatua ya kuimarisha barabara na kujenga katika kiwango cha lami inaendelea, maeneo yote ambayo yalikuwa yameharibika tunaenda kuyafanyia marekebisho.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, zile fedha ambazo zilikuwepo kwa ajili ya emergency zitatumika kwa ajili ya kuhakikisha barabara hii inatengenezwa. Kama nilivyosema, nitapita maeneo ambayo yatakuwa maalum zaidi tutaendelea kuzungumza kuona namna nzuri ya kushirikiana. (Makofi)
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuniona. Barabara aliyoulizia Mheshimiwa Haonga ina umuhimu wa kipekee kwani inaunganisha mikoa mitatu, Mkoa wa Songwe, Rukwa na Katavi na ni barabara yenye umuhimu wa kiuchumi kwa mikoa ile mitatu hata kwa Taifa zima kwa ujumla. Katika Ilani ya CCM mwaka 2010, ukurasa wa 62, barabara hiyo iliingizwa kufanyiwa upembuzi yakinifu. Sasa hivi tumebakiza miaka miwili na nusu sioni dalili ya kuanza kazi ya upembuzi yakinifu, ni lini Serikali itaanza kazi katika barabara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Malocha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Mbunge tumezungumza sana kuhusu maeneo yake na maeneo haya ambayo anazungumza ya Kwera yana structure special. Nimhakikishie yeye na wananchi kwamba eneo hili tunaendelea kulitazama vizuri.
Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii inaunga Mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi. Barabara hii ukiifuatilia kutoka Kamsamba inaenda kuungana kule Kibaoni. Kama nilivyosema nitapita kuangalia lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa kwamba zile ahadi zinaendelea kutekelezwa. Bado miaka miwili lakini naamini hapa mwishoni speed yetu itakuwa kubwa.
Mheshimiwa Spika, hatua za awali za ujenzi zimeshaanza. Kwetu sisi kutambua mahitaji, kufanya usanifu na michoro ni hatua za ujenzi. Kwa hiyo, tutakwenda kwenye hatua nyingine ya mwisho kwa ajili ya ujenzi. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi na nimwombe tuendelee kushirikiana na kupeana mrejesho ili hatimaye hii barabara tuweze kuiunga na mikoa hii mitatu iweze kuwa katika muunganiko mzuri.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na mahitaji makubwa ya barabara nchini, bado gharama za ujenzi wa barabara Tanzania ni kubwa mno ukilinganisha na mataifa mengine. Utakuta hata mjini barabara moja ina-cost mpaka shilingi bilioni 1.4, hakuna madaraja hakuna ma-culvert. Ni lini sasa Serikali ita-revisit gharama zake za ujenzi wa barabara ili iweze ku-save pesa na zitumike kwenye maeneo mengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zungu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli ujenzi wa barabara unaonekana gharama ni kubwa. Sisi kama Serikali tunachukua hatua kufanya mapitio ili kuona kwa kiasi kikubwa tunapunguza hizi gharama.
Mheshimiwa Spika, gharama kubwa zinaweza kusababishwa na interest, bei ya vifaa, teknolojia na usimamizi. Kwa upande wa Serikali tumejipanga ili kuhakikisha kwamba kwanza taasisi zetu ambazo zitakuwa zinasimamia ubora na gharama, kwa mfano tunafanya mapitio ili tuone Baraza la Ujenzi (NCC) tunalifanyia mabadiliko makubwa ili sasa lije na utaratibu wa kutazama hizi gharama za miradi ili uwiano wa ujenzi wa barabara uwe mzuri. Kwa sababu pia Serikali sasa inalipa kwa haraka wakandarasi hili eneo la interest litapungua lakini pia kwa sababu teknolojia inabadilika, sasa hivi tumekuja na teknolojia mpya na wataalam wetu katika Wizara tunaendelea kuwapeleka kujifunza teknolojia hii, teknolojia hii pia itakuwa muarobaini.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwa ujumla wake kwamba sisi kama Serikali tunaona kuna variance kubwa kati ya barabara na barabara pia kati ya maeneo na maeneo lakini pia ule utaratibu wa manunuzi tunaendelea kuutazama ili mwisho wa safari tuje na muarobaini wa kupunguza gharama za barabara. Kwa hiyo, nimtoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Serikali tumeona kwamba iko haja ya kufanya juhudi za makusudi kuhakikisha kwamba ujenzi wa barabara nchini unakuwa na gharama ya chini lakini itatupa fursa ya kuweza kutengeneza barabara nyingi zaidi kama control ya cost itakuwepo. (Makofi)
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Kibaoni – Majimoto - Mamba – Kasansa – Mfinga – Muze – Kilyamatundu - Mbozi imekuwa ikiandikwa sana katika vitabu vya bajeti kwa takriban miaka 10 sasa. Ni lini barabara hii ya kutoka Kibaoni - Kilyamatundu - Mbozi itafanyiwa upembuzi yakinifu na kujengwa kwa kiwango cha lami kwa sababu pia iko ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa miaka 15 mfululizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Kikwembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Kikwembe kwa sababu kuna wakati nimeahidi hapa kwamba baada ya Bunge hili nitakwenda eneo hili la Kavuu tuweze kuona eneo hili. Kwenye mpango mkakati wa ujenzi wa barabara, barabara hii imetajwa lakini tunajua umuhimu wa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi. Baada ya dhiki ni faraja, kweli ni miaka mingi tumesubiri barabara hii na pia kwenye bajeti yetu tumetenga fedha kwa ajili ya kuendelea sasa kufanya usanifu wa barabara hii na itakuwa ndiyo mwanzo wa kutengeneza barabara hii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba Mkoa wa Katavi ulikuwa ni mkoa ambao ulikuwa unahitaji kuunganishwa sana. Utaona kwenye barabara ukitoka Tabora tunakuja Mpanda, ukitoka Mpanda pia tunakwenda katika Mkoa wa Kigoma, wakandarasi katika hatua mbalimbali wanaendelea ili kuonesha msisitizo kwamba Serikali imetambua umuhimu wa maeneo haya kuweza kuyaunganisha na mikoa mingine.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimueleze tu Mheshimiwa Dkt. Kikwembe kwamba tumejipanga vizuri, kati ya mikoa ambayo ilikuwa bado ina shida ya kuunganishwa, huu ni mkoa mmojawapo. Nimshukuru kwa juhudi hizo, tutaendelea kuhakikisha kwamba barabara hii inapata tiba, inakuwa ni huduma kwa ajili ya kusaidia maeneo haya ambayo pia ni muhimu sana kwa uzalishaji wa mazao na shughuli zingine za kuongeza uchumi wa wananchi wetu. (Makofi)
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya Vigwaza - Kwala - Kimaramasale inayounganisha Majimbo matatu ya Mkoa wa Pwani, Jimbo la Bagamoyo, Kibaha Vijiji na Kisarawe, ni lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ikizingatiwa kule kuna bandari kavu? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na nimshukuru Mheshimiwa Hawa Mchafu kwa swali lake.
Mheshimiwa Spika, niseme tu barabara hii inahudumiwa na TANROADS na katika ule mpango mkakati wetu tunao utaratibu wa kuitengeneza. Kwa sasa tunajitahidi kuhakikisha barabara hii inapitika wakati wote na kwa umuhimu wa kipekee kwa sababu ya kuwa na hii bandari kavu tutaipeleka kwenye kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge avumilie kidogo utaratibu upo wa kuifanya hii barabara iwe nzuri zaidi. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nami nina swali dogo la nyongeza. Tatizo lililopo katika Jimbo la Igalula lipo vilevile katika Jimbo la Momba hususan katika barabara ya kutoka Kakozi-Kapele - Ilonga ambako ni Jimbo la Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Kandege, Jimbo la Kalambo.
Mheshimiwa Spika, wakati tunasubiri ahadi ya TANROADS ya kutengeneza barabara hiyo na yeye sasa hivi ndiye Waziri, haoni sasa ni wakati muafaka kutengeneza barabara hiyo ambayo inaunganisha mikoa miwili ya Songwe pamoja na Mkoa wa Rukwa, lakini vilevile Jimbo la Momba na Jimbo lake la Kalambo? (Makofi). Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nataka nimwombe Mheshimiwa Silinde tu avumilie kwa sababu sijatembelea Mkoa wa Songwe, lakini utaratibu wa Serikali kisera ni kwamba umuhimu wa kwanza ni kuhakikisha tunaunganisha mikoa. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi na katika bajeti yetu tuna provision na nikienda kule tutazungumza kwa upana zaidi ili aone namna ambavyo tumejipanga kuijenga barabara hii Mheshimiwa. Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri yanayotoa faraja kwa wananchi wa Tunduma pamoja na Ileje, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, wananchi wa Kata ya Bupigu, Kata ya Malangali, Kata ya Isoko na Kata ya Ikinga katika Wilaya ya Ileje wamekuwa na adha kubwa sana ya kuamka Saa nane ya usiku na kusubiri usafiri kuja makao makuu ya Mkoa wa Songwe. Ni lini Serikali itajenga barabara hii ya kutoka Isongole mpaka Ikinga, ili kuondoa adha hii ya Wananchi wa Ileje?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna kipande cha barabara kilometa 1.6 kimejengwa katika Mji wa Tunduma na kimejengwa kwa sababu, wananchi wa Mji wa Tunduma wakati Mheshimiwa Rais akiwa Waziri wa Ujenzi, wakati anapita anakwenda Rukwa, walimsimamisha pale na wakamwomba barabara ile ijengwe haraka iwezekanavyo na sasa Serikali imejenga kipande kile cha kilometa 1.6, lakini kipande kile kimejengwa chini ya kiwango. Je, ni lini Serikali itakuja kuhakiki kipande kile cha barabara ili wananchi wa Tunduma waweze kufurahia mpango wa ujenzi wa barabara kwenye Mji wa Tunduma?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kama anavyouliza, anapenda kujua katika swali lake la kwanza, katika hizi Kata za Lupingu, Malangali na Ikinga, kuna sehemu ambayo ina uharibifu mkubwa, kwamba, kwa kweli, maeneo mengi tumekuwa na uharibifu kutokana na mvua zimekuwa nyingi, lakini kama tulivyopitishiwa bajeti na Bunge lako, tumetenga fedha kwa ajili ya kufanya matengenezo, ili kuhakikisha kwamba, maeneo haya yanapitika.
Mheshimiwa Spika, kabla hatujapata kipande cha lami katika eneo hili nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Tunduma kwa ujumla kwamba wakati hizi mvua zinapungua tumejipanga kwa ajili ya kufanya marekebisho makubwa ili maeneo haya yapitike. Kwa hiyo, nimtoe tu wasiwasi kwamba tutafanya marekebisho ili wananchi waendelee kupata huduma ili waondokane na hii adha ambayo wanaipata.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kuhusu kile kipande cha kilomita 1.6 ambacho Mheshimiwa Mbunge anaona kwamba hakikujengwa katika standard inayotakiwa; niseme tu kwa sababu nitakuwa na ziara ya maeneo yale kwamba tutayaona kwa pamoja ili tuone kwamba hii kilomita 1.6 ina shida gani ili tuone kama kweli ni kiwango hakikuwa kimefikiwa au labda saa nyingine ndiyo ilikuwa kuna shida tofauti ya hapo kwa sababu kuna wakati mwingine barabara zinajengwa lakini mazingira ambayo hayakutegemewa yanaweza yakatokea barabara ikaharibika.
Mheshimiwa Spika, tutaiona kwa pamoja na Mheshimiwa Mbunge halafu tuone tutachukua hatua kama kutakuwa na shida yoyote kuhusu kipande hiki ambacho umekitaja.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ninalo. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu hayo ya Serikali lakini mpaka Mheshimiwa Mbunge anaandika swali hili ni kwamba katika Kata hiyo ya Mateves bado kuna wananchi ambao wanadai fidia ya malipo hayo kwamba bado hawajatimiziwa. Je, Waziri yuko tayari kufuatilia na kuhakikisha kwamba wananchi hawa wote wanapata malipo yao kama ilivyokubalika awali? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ningependa tu kupata commitment ya Serikali amesema kwamba atakapopokea fedha hizo. Je, katika msimu huu wa mwaka 2017/2018 au ni mpaka katika bajeti nyingine na pengine tu kwamba Waziri wenyewe yupo tayari kwenda sasa na Mheshimiwa Mbunge ili kwenda kusikiliza hizo kero na malalamiko ya wananchi na kuweza kuwakamilishia fidia yao. Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Mollel na Mheshimiwa Mbunge Catherine Magige kwa ushirikiano wao namna ambavyo wanafuatilia ili kuhakikisha kwamba wananchi wao katika maeneo haya ya Arusha wanapata haki zao.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya juhudi kubwa sana kulipa fidia hizi. Ukiangalia kwa ujumla wake kwamba kulikuwa na jumla ya madai ya shilingi bilioni 2.5, lakini mpaka sasa tunavyozungumza bilioni 2.291 zimekwishalipwa ina maana kwamba asilimia 92 ya madai yote imeshalipwa. Hii inaonesha kwa jinsi gani Serikali iko committed kuhakikisha kwamba hawa wananchi wanaodai wanapata haki zao na kwa haraka.
Mheshimiwa Spika, nimtoe tu wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba hiki kiasi cha shilingi milioni kama 214 kilichobaki ni kiasi ambacho ni kidogo, lakini ni muhimu kilipwe mapema. Kwa hiyo, tunafuatia na niseme tu kwamba ni wakati wowote na niko tayari kuhakikisha kwamba fedha zikipatikana kutoka Hazina hawa wananchi wanalipwa mara moja. Kwa hiyo, wasiwe na wasiwasi, kama tulivyowalipa hawa wengine na wao watalipwa mara moja.
Mheshimiwa Spika, kuhusu commitment ya Serikali , nisema wakati niko committed kama nilivyoahidi hata wiki iliyopita wakati nikijibu swali lako Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafika maeneo haya ili sasa tuweze kuona pia kwamba ni nini kinachotakiwa kufanyika ili mambo yaende sawia. (Makofi) Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu, japokuwa niseme tu kwamba barabara hii imekuwa kwenye mpango kwa muda mrefu sana. Kulingana na majibu yake ni kwamba upembuzi yakinifu umekamilika tangu 2014/2015, ni muda mrefu sasa inakaribia miaka minne. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Geita na Mkoa wa Shinyanga na ni muhimu kiuchumi. Mimi na wananchi tungependa kujua ni lini fedha itapatikana ili utekelezaji uanze mara moja? Hilo ni swali langu la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015, Mheshimiwa Rais akiwa pale Katoro aliweza kuahidi kilomita 10 za lami; kilometa 5 Katoro na kilometa 5 Buseresere lakini mpaka sasa hakuna chochote kinachoendelea. Je, ni lini sasa utekelekezaji huu utaweza kuanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lolesia Bukwimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba uniruhusu nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Lolesia Bukwimba kwa sababu amekuwa akifuatilia sana juu ya maendeleo katika Jimbo lake. Niseme tu kwamba barabara hii tumezungumza naye sana nje ya Bunge lakini naona pia anavyoshirikiana na pia na Wabunge wengine kwa sababu barabara hii inagusa maeneo mengi na kama alivyosema inaunganisha Mkoa wa Shinyanga na Mkoa wa Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mpango wa kuitengeneza barabara hii na niseme kweli imekuwa ni muda mrefu tangu usanifu ukamilike na kwa kuwa Serikali inaendelea kutafuta fedha, nimjulishe tu Mheshimiwa Lolesia Bukwimba juhudi zake zimesababisha angalau kwa kuanza katika mwaka wa fedha 2018/2019, Bunge lako limetenga shilingi bilioni 13 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii. Wakati tunatafuta fedha za kutosha lakini juhudi zimeshaanza kwa kuweza kupata hizi fedha ambazo Bunge limepitisha ili kuanza kuitengeneza hii barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Lolesia Bukwimba pamoja na wananchi wa Jimbo la Kahama Mjini, Jimbo la jirani yangu pale Mheshimiwa Maige kule Msalala pamoja na Jimbo lake la Busanda pamoja na Geita na wananchi wote wa Nyarugusu, Bukoli, Bulyankulu, Itobo, Busoka na Kahama Mjini kwamba ujenzi sasa unaanza na tunaendelea kusukuma ili tuweze kupata fedha za kutosha kujenga barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ahadi ambayo ilitolewa na Mheshimiwa Rais katika Mji wa Katoro na Buseresere, Serikali inatambua kilometa kumi ziko kwenye ahadi, kilomita 5 ziko Katoro na kilomita nyingine 5 ziko Buseresere. Niseme tu kwamba tumefanya uratibu ili kuweza kuzitambua barabara zote ambazo zimeahidiwa na Mheshimiwa Rais nchi nzima. Tumeendelea kuzipanga zile zinashughulikiwa na TARURA na TANROADS na tunaendelea kuhakikisha kwamba kwenye ule mpango mkakati wa Wizara basi barabara zote ambazo Waheshimiwa viongozi wametoa ahadi zinatekelezwa. Kwa hiyo, nimtoe hofu, tunazisimamia kwa nguvu kuhakikisha kwamba ahadi hizi za Mheshimiwa Rais na zilizopita katika awamu nyingine tunaendelea kuzishughulikia ili tuweze kutengeneza barabara hizi. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kabla ya kuuliza swali, naomba kuipongeza Wizara ya Kilimo, Bodi ya Wakurugenzi wa Pamba kwa kuwapa nafuu wakulima wa pamba kwa kuwapa utaratibu mzuri wa ununuzi wa pamba na kuwaondolea kero ambayo ilikuwa inawapa usumbufu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, barabara ya Mgeta – Mihingo – Nikomalile na Sirolisimba imekuwa na ahadi ya muda mrefu na imeharibika sana na ina umuhimu mkubwa wa kuleta wateja katika Mnada mkubwa wa Mgeta ambao unafanyika mara mbili. Je, ni lini barabara hii itakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Getere kwa sababu mimi kila nikikutana naye namuita mzee wa Silolisimba kwa sababu yah ii barabara ya Mgeta – Silolisimba, anaifuatilia kweli. Kwa kweli kama nilivyokuwa nimemuahidi ilikuwa ni kuhakikisha kwamba barabara hii tunaipa kipaumbele kwa sababu ina matatizo makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Bunda kwa ujumla kwamba baada ya mvua kuwa zimepungua mkandarasi yuko site na nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge mazungumzo ambayo tumeyafanya na kuhakikisha kwamba barabara inatengenezwa majibu yake yanapatikana kwa sababu fedha za kupeleka kwa ajili ya barabara hii zimeshapatikana, kati ya wiki hii na wiki ijayo fedha zitakwenda. Nimuombe na kumuagiza tu mkandarasi aliyeko site afanye kazi kwa nguvu na mimi baada ya Bunge hili ntafika kuona kwamba kazi inaendelea ili kuweza kuondoa hii shida ambayo ipo katika eneo hilo. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Getere, tuendelee kushirikiana na kubadilishana mawazo lakini nia yetu ni moja ni kuhakikisha kwamba tunaboresha miundombinu hii ya barabara. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda Mheshimiwa Naibu Waziri pia atueleze, kwa sababu wakati alipokuja Mtwara alipita pia kukagua barabara ya Umoja, hii inayoanzia Mtwara – Newala mpaka Masasi lakini pia inayokwenda mpaka Nachingwea. Wakati wa kampeni Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba barabara ile itajengwa kwa mara moja na wataweka pale wakandarasi wanne ili kuweza kufanya barabara hiyo ijengwe kwa haraka zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kufahamu, ni lini hasa barabara inayotokea Masasi - Nachingwea - Lukuledi - Chikunja - Ndomoni - Nachingwea, itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kama ambavyo iliahidiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nimetembelea Mtwara na Lindi na nimeona harakati za ujenzi. Kwanza kwa ufupi tu ni kwamba maeneo yote yaliyokuwa na shida kubwa ujenzi unaendelea. Ukiangalia kwenye bajeti hii pia tuliyopitisha tumeweka fedha za kutosha kukamilisha daraja katika Mto Lukuledi kwa sababu eneo hili lilikuwa ni hatari, wananchi walikuwa wanapita kwenye maji na walikuwa na hatari ya kuliwa na mamba. Kwa hiyo, tumeweka fedha za ujenzi pale na tunaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kifupi kwa barabara hii ambayo ameitaja ili kuwa na Lot 4 kama alivyosema kuharakisha ujenzi ule, utaratibu unaendelea vizuri kwa sababu tunatafuta fedha. Wakati tunafanya juhudi za kupata fedha za kutosha ziko fedha ambazo zimetengwa wakati wowote tutaweza kutangaza ili kuweza kuanza ujenzi huu. Kwa hiyo, nimpongeze sana, tuendelee kuwasiliana, nami nitapita pia wakati mwingine nione harakati hizi zikiendelea. Nimeona barabara hii ni muhimu sana inawaacha watu wengi walioko kule Liwale kwani tukikamilisha eneo hili tunaweza kwenda tena kilometa 129 kutoka Nachingwea kwenda Liwale ambayo sasa tumeiweka kwenye hatua ya usanifu ili wananchi wa maeneo yale waweze kunufaika na barabara hii itakapokuwa imejengwa.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama lilivyo swali la msingi, barabara inayotoka Mgakorongo – Kigalama – Bugomola - Mlongo ni barabara muhimu na inaunganisha nchi jirani pamoja na Wilaya jirani ya Karagwe. Barabara hii ni ahadi ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne, lakini na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi itajengwa kwa kiwango cha lami. Ni lini barabara hii itajengwa na wananchi wakalipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Innocent Bilakwate, maarufu kama Mchungaji, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ya Mgakorongo – Kigalama – Mlongo ni barabara ambayo inaunganisha nchi yetu na Uganda na inahudumiwa na Wakala wetu wa Barabara TANROADS. Katika sera ni kati ya barabara ambazo zina kipaumbele katika kutengenezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo tumeongelea hizi barabara, sijafika Kagera kwa ziara lakini nazitambua kwa sababu tumekuwa tukibadilishana mawazo. Niwapongeze sana wananchi wa Kyerwa kwa kweli hawakukosea kumchagua Mheshimiwa Bilakwate kwa sababu kazi nzuri anaifanya. Jukumu ambalo wamempa analifanya kisawasawa na sisi kama Serikali tunaendelea kushirikiana naye kuhakikisha kwamba hatuwaangushi wananchi wa Kyerwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu barabara hii urefu wake ni takribani kilometa 79 hivi, ambapo itakwenda kuungana na barabara kubwa ambayo inakwenda kuunganisha nchi yetu pia na upande ule wa Mtukula. Kwa hiyo, tunatambua umuhimu wa barabara hii, inapita maeneo yenye uzalishaji mkubwa na itakuwa na mchango mkubwa sana kwenye uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ipo kwenye mpango kwa kweli, labda Mheshimiwa Bilakwate baada ya hapa tukae tuzungumze ili tuangalie kwa upana kwenye strategic plan tumepanga namna gani hatua kwa hatua kuikamilisha barabara hii. Pia tumetenga fedha kuhakikisha kwamba barabara hii inaimarishwa ili dhana nzima ya kuhakikisha tunatekeleza sera yetu ya kuunganisha mikoa yetu na nchi za jirani inakamilika na wananchi wanapata huduma na kwa kweli inachangia pia katika uchumi wa nchi yetu.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anafahamu barabara ya Muheza – Amani, kilometa 36 ambayo aliipita, imepangiwa fedha mwaka uliopita shilingi bilioni 3 kujengwa kwa kiwango cha lami na bajeti hii pia imepangiwa shilingi bilioni 5 ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Ni lini barabara hii itaanza kutengenezwa kwa sababu inazidi kuharibika? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nilitembelea Muheza na nilipita barabara hii Mheshimiwa Mbunge anayoizungumzia na nilizungumza na wananchi kule Amani, hata kiu ya wananchi wa maeneo yale kuunganishwa na majirani zao wa Maramba na Korogwe ni kubwa. Kuna kitu ambacho kinaendelea kuhakikisha kwamba fedha hizi sasa zinakwenda ili barabara itengenezwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli maeneo haya ni hatari kwa sababu hata barabara zake tutengeneza kwa kutumia zege la saruji kwa sababu ina miteremko mikali sana. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Balozi Adadi, kama tulivyokubaliana nitaendelea kuhakikisha wakati wowote fedha hizi zitolewe hii barabara itengenezwe kwa wakati kwa sababu sehemu ambazo zina maporomoko makubwa ni hatari sana na wakati mwingine inakuwa kikwazo wananchi kupita kabisa katika maeneo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali inatambua hivyo, sisi kama Wizara tutahakikisha kwamba fedha ambazo zilikuwa zimetengwa mwaka wa fedha unaoisha na mwaka unaokuja zinakwenda kutibu na kuhakikisha barabara hii inatengenezwa. Kwa hiyo, nitampa mrejesho kuona hatua gani kama Wizara tunachukua kwa kadiri tunavyopata fedha kutoka Hazina tuweze kuipelekea barabara hii ili iweze kutengenezwa na ipitike kwa urahisi.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la barabara ya Bukoli - Kahama linafanana kabisa na barabara ya Davis Corner – Jeti Lumo ambayo ipo kwenye ule mpango wa barabara pete za Dar es Salaam kwa ajili ya kupunguza foleni. Mkandarasi Nyanza Construction alipewa pesa ya kujenga kipande kidogo tu cha kutoka Tandika - Yombo Dovya – Makangarawe – Buza - Mwisho wa Lami, kipande kilichobaki cha kutoka Mwisho wa Lami - Jeti Lumo bado hakijafanyiwa kazi na kina mashimo makubwa. Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha ili mkandarasi amalize kujenga barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna mradi huu wa Davis Corner - Jeti Lumo na natambua pia kuna kiasi ambacho kimeshatengenezwa. Matumaini yangu baada ya kukamilisha kipande hiki sasa ile safari ndefu ya kuitengeneza barabara hii imeshaanza. Tulikuwa na shida kidogo ya kuendelea kulipa wakandarasi lakini mpaka hivi navyozungumza karibu wakandarasi wote nchi nzima wamelipwa. Kwa hiyo, kwetu sisi ni fursa ya kuendelea kufanya matengenezo ya barabara. kwa hiyo, nafikiri hata baada ya kikao tuzungumze ili tuone kwamba hiki kipande kinachobakia tuweze kuona kwamba kinaweza kukamilishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba hizi barabara za Dar es Salaam na mzunguko wake zinaweza kutengenezwa. Pia kuna fedha ambazo zimeendelea kutolewa ili kuhakikisha kwamba kazi hazisimami na hasa baada ya mvua hizi kupungua tunarejeshea maeneo ambayo yalikuwa yameharibika ili waanchi wasipate adha. Kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wa Dar es Salaam na maeneo yote kwamba tumejipanga vizuri kuhakikisha shughuli za ujenzi zinaendelea.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kazi kubwa sana ya kutujengea barabara ya kutoka Ndono - Urambo na sasa hivi inaendelea kutoka Urambo - Kaliua. Je, Serikali haioni kwamba kazi nzuri inaharibiwa na kipande ambacho mpaka sasa hivi hakijajengwa kutoka Posta - Seed Farm? Mheshimiwa Naibu Spika, halafu pili, je, Serikali…
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la mama yangu, Mheshimiwa Margaret Sitta, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, najua Mheshimiwa Mbunge anatambua kwamba hii barabara kutoka Urambo - Kaliua kipande kilichobakia kilometa 48 mkandarasi yuko site. Tutakuwa tumefanikiwa kuunganisha sasa kutoka Tabora Mjini mpaka Urambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua pia kiu ya Mheshimiwa mama hapa hiki kipande cha barabara kutoka Posta – Seed Farm kiunganishwe lakini kwetu tuliona kwamba muunganiko wa barabara kubwa ulikuwa na kipaumbele lakini baada ya hapo tutaendelea mama yangu kukiangalia hiki kipande. Najua pia ana kiu ya kupata round about ambayo tutaiita Mama Round About. Kwa hiyo, tunaendelea kuiangalia uwezekano wa kupata round about ili tuweze kuunganisha vizuri na kuhakikisha kwamba ajali katika makutano ya hii barabara tunaziondoa.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote kwanza napenda sana nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo ynanaleta matumaini kwetu na kwa wapiga kura wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015 kulitolewa ahadi na Mheshimiwa Makamu wa Rais ya kujenga barabara inayoanzia Wilaya ya Namtumbo - Lusewa – Mchoteka - Nalasi kwa kiwango cha lami. Ni nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha tunatekeleza ahadi hii kabla ya mwaka 2020 wakati wa uchaguzi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sikudhani Yassini Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitembelea maeneo haya nikitokea Nakapanya kuja Tunduru. Natambua pia ile kiu ya wananchi wa Tunduru ili kuweza kupita kwenye barabara hii kutoka Namtumbo - Lusewa - Nalasi lakini nia yao twende kuunganisha na wananchi wa Msumbiji. Najua katika Mto Ruvuma maeneo haya ya kutoka Nalasi tunahitaji kuwe na kivuko.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie tu kwa ujumla wake kwamba barabara hii iko kwenye mpango na hata kwenye bajeti kuna kiasi cha fedha kimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara hii. Vilevile nimhakikishie pia tutakapokamilisha Daraja la Ruhuhu kile kivuko ambacho muda mwingi tumezungumza tutakipeleka eneo hili ili wananchi wa Nalasi na majirani zao waweze kuvuka kwenda Msumbiji. Ahsante sana.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona, nilikuwa nimetoka kidogo nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara kule Manyara inafanana na barabara iliyoulizwa na muuliza swali la msingi, inaitwa Mogitu – Basotu - Hyadom na Hyadom ni hospitali kubwa ya rufaa kule ambayo inahudumia watu wengi wa Mkoa wa Manyara. Barabara hiyo ni ahadi ya Rais akiomba kura; je, process au mchakato wa kujenga barabara hiyo utaanza lini ili watu wanufaike na ile Hospitali ya Hyadom ambayo kwa kweli imekuwepo kwa miaka mingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la shemeji yangu, Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ambayo anaizungumzia Mheshimiwa Mbunge ni barabara ambayo kwa kweli imekuwa ikisemewa na Waheshimiwa Wabunge wengi. Kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa Mbulu wana ushirikiano mkubwa maana wanaizungumzia sana barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba wakati wowote wadau wote ikiwemo Waheshimiwa Wabunge tutakuwa na kikao cha kuzungumzia barabara hii ambapo sasa itakuwa inatoka Mbulu Mjini - Katesh - Hyadom - Sibiti tunaungana pia na mikoa ile ya upande wa Kanda ya Ziwa. Barabara hii usanifu wake na michoro imeshakamilika, hatua iliyopo sasa ni kuzungumza na wadau ili tuendelee na hatua nyingine kwa sababu zipo indication za kupata fedha kutoka Serikali ya Ujerumani kama sikosei kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii. Kwa hiyo, natambua umuhimu wa muunganiko wa barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Bunge linaendelea kama wiki mbili zilizopita nimetembelea kipande ambacho kinakwenda kuunganisha barabara hii kikitokea Singida. Kutokana na umuhimu wa eneo hili la Hyadom kwa sababu ile hospitali ni kubwa na huduma nyingi sana kwa wananchi wengi kutakuwa na kipande cha kilometa 93 kutoka Singida kwenda Hyadom. Wakati naikagua ile barabara kwa sababu ilikuwa haipitiki, nimeenda mpaka Hyadom lakini nimeona pia logistics za barabara hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge anaizungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu na wananchi wote wa maeneo yake kwamba hii barabara sasa ujenzi wake uko karibu. Imechukua muda mrefu lakini wasiwe na wasiwasi, upo mpango mzuri wa kujenga barabara hii inayounganisha Mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Simiyu, Shinyanga pamoja na Mwanza. Hii ni barabara muhimu sana kwa sababu eneo hilo linazalisha sana mazao mengi na huduma ya afya kama nilivyosema ni muhimu sana kwa wananchi wa maeneo haya.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wa Kigamboni shida waliyokuwa wanaipata kabla ya kujengwa daraja lile la Nyerere ilikuwa ni kubwa sana. Pia wananchi wangu wa Kata ya Ilagala na kata zingine za Ukanda wa Lake Tanganyika wanapata shida kubwa sana kwa Kivuko kilichopo pale, kila siku ajali za magari yanaingia kwenye Mto Malagarasi. Je, kwa nini Serikali sasa isiwajengee Daraja la Ilagala na wanajua kabisa waliahidi kujenga daraja hili tangu 2008?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Serikali inaendelea kuboresha mawasiliano ya usafiri katika maeneo ya Mheshimiwa Mbunge ambayo anatoka na natambua kwamba uko usanifu wa kuunganisha barabara kupita kwenye daraja ambalo analizungumza kwa hiyo Mheshimiwa Mwilima nafikiri baadaye tunaweza tukazungumza ili aone mpango mahususi tuliokuwa nao kuhakikisha daraja hili linaweza kutengenezwa ili tuweze kuunganisha maeneo haya na maeneo mengine ya Kanyani kule tukiwa tuaelekea kule Kasulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tulizungumze ili aone namna tulivyojipanga kwa ajili ya kutoa hii adha na najua na suala la kivuko kulikuwa na shida pia ya kuvuka usiku katika eneo hili, yote haya tunayashughulikia ili wananchi hawa wasipate adha ambayo ilikuwepo katika eneo hili.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa mchakato unaoendelea kuibadilisha barabara hii kuwa kiwango cha lami. Barabara hii kuanzia Ifakara – Lupiro – Malinyi mpaka Kilosa kwa Mpepo kutokana na mvua za mwaka huu, barabara hii kwa kiasi kikubwa sana imeharibika sana na bajeti ambayo tumeipitisha hapa ya Wazara ya Ujenzi haitoshelezi kabisa kipande kile ambacho wamewekea bajeti. Swali langu hapa, Je, Waziri yupo tayari kutumia hela ya dharura kuongezea bajeti kipande hicho cha barabara kuanzia Ifakara mpaka Malinyi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sera ya barabara inaelekeza Makao Makuu ya Wilaya zote zijengewe barabara kwa kiwango cha lami. Wilaya yetu ya Malinyi haina hata chembe ya lami; je, Serikali ni lini watatekeleza sera hiyo ya ujenzi wa barabara ya lami katika Makao Makuu ya Malinyi?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nizipokee pongezi ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitoa kwa sababu nafahamu kwamba sasa ujenzi wa barabara hii muhimu kama unavyosema umekwishaanza na unakwenda kwa hatua na tupo hatua nzuri. Pia nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia barabara hii muhimu na katika kufuatilia kwake nilipita barabara hii ili kujionea mwenyewe namna changamoto ilivyokuwa, lakini tunaendelea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kuhusu swali lake lwa kwanza ni kweli fedha hazitoshelezi kwa mujibu wa bajeti na kwa hali ya mvua iliyokuwa imetokea katika kipindi hiki na niseme tu kwamba tulikuwa tumetoa maagizo kwa Mameneja wa TANROADS mikoa yote ili kuweza kutumia hiyo fursa ya bajeti tuliyokuwa nayo kwenye dharura kuweza kutengeneza maeneo korofi nchini kote ili kuhakikisha kwamba barabara zinapitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niendelee kusisitiza kumwomba Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Morogoro kwa namna tunavyoendelea kwamba aendelee kutazama kwa macho mawili barabara hii na kwa sababu tumeshatoa maelekezo naamini kwamba utaratibu wa kukurejeshea hali ilivyoharibika unaendelea. Kwa hiyo, niwatoe wasiwasi Mheshimiwa Mponda na wananchi wa Malinyi na nitahakikisha kwamba maeneo ambayo yamekuwa korofi tunaendelea kuyashughulikia wakati utaratibu wa kujenga kwa kiwango cha lami unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kweli Serikali ina mpango wa kuunganisha Makao Makuu ya Wilaya na Makao Makuu ya Mikoa na niseme tu eneo hili la Malinyi na mwenyewe nilipita kama ninavyosema nimeona hiki kipande kidogo sana kwenda kuunganisha na Makao Makuu ya Wilaya hii ambapo pale njia panda ya kwenda Londo, Kilosa kwa Mpepo kuna kipande hiki cha barabara ambacho ni korofi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nielekeze tu kwamba kwenye mipango yetu upande wa TANROADS Mkoa wa Morgoro, tutaendelea kuitazama ili tuweze kutibu eneo hili tuweze kuunganisha ili wakati tukipata barabara hii inayokwenda Lumecha kule Namtumbo basi itukute tayari kipande hiki cha barabara kuunganisha na hii barabara kubwa kinaunganika ili Wilaya hii ya Malinyi iweze kuunganika kama ilivyokuwa kwenye sera yetu ya Serikali. (Makofi)
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza swali. Kwa kuwa barabara ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala – Masasi imeshaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kilometa 50, je, ni lini wananchi wa maeneo ya Nagaga, Mbuyuni, Chiungutwa pamoja na Mpeta watalipwa fidia zao ili barabara hii iweze kuendelea kufanyiwa kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inafanya juhudi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba tunaboresha barabara hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameizungumza. Sasa yupo mkandarasi anatengeneza barabara kutoka Mtwara kuja Mnivata, lakini tutatoka Mnivata – Tandahimba – Newala mpaka Masasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili ambalo Mheshimiwa Mbunge anauliza, ni muhimu ili utaratibu wetu uweze kuendelea wa kutengeneza hii barabara kuiunganisha na Mtwara, tuhakikishe tunalipa fidia. Nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu suala hili la fidia tumelizungumza na nilimwambia kwamba muda sio mrefu nitampa majibu kwa sababu nilikuwa naweka msukumo ili wananchi waweze kulipwa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli fidia hii ikilipwa pia inatupa sasa fursa ya kuendelea kuboresha barabara hii ili tuweze kuiunganisha kutoka Mtwara kuja Masasi iweze kukamilika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Bwanausi naomba avute subira na kweli najua kwamba kasi iko kubwa ya Serikali kulipa fidia na katika maeneo mbalimbali tunaendelea kulipa fidia lakini na wananchi wa eneo hili la kwako tutaweza kuwalipa mara moja. Ahsante. (Makofi)
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Mkoa wa Mbeya ni mkoa wa pili kwa wananchi wake kuwa na pato la Taifa ukitanguliwa na Mkoa wa Dar es Salaam, lakini miundombinu yake si rafiki kwa wananchi wake. Je, ni lini Serikali itatengeneza barabara iliyoahidi kutoka mchepuo wa Uyole kwenda Mbalizi pamoja na barabara kutoka Katumba, Ruangwa, Masoko mpaka Mbambo na Tukuyu yenye kilometa 83? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu barabara hii amekuwa akiizungumza kweli. Tumezungumza naye hapa ndani ya Bunge, tumezungumza naye nje ya Bunge na hata wakati akitoa mchango wake wakati wa Wizara hii tulivyowasilisha bajeti aliizungumza barabara hii, hata akasema kama hatutengenezi basi yuko tayari kutupeleka shambani tukashirikiane naye kulima, nami nilikuwa tayari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, niwapongeze pia wananchi wa Busokelo kwamba wamepata mwakilishi mzuri kwa sababu anashughulikia sana mipango na mambo mbalimbali kuhakikisha wananchi wake wananufaika na rasilimali za nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu barabara hii ya Katumba – Suma – Ruangwa – Mbambo kuja Tukuyu ni kati ya barabara ambazo pia tumezitengea fedha. Natambua kwamba mwaka 2017/2018 pia tulitenga fedha na mwaka huu tumetenga fedha. Niseme tu kwamba ukiangalia kwenye kitabu cha bajeti huu mradi namba 4150, tumetenga bilioni 17 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mwakibete na kwamba barabara hii tunakwenda kuijenga, muda sio mrefu harakati za ujenzi zitakuwa zimeanza, fedha zipo na nalishukuru Bunge kwa kutenga fedha hizi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa barabara ya kutoka Puge – Ndala – Nkinga – Ziba inapita kwenye hospitali kubwa sana za Mission, je, ni lini sasa hizo barabara zitajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, hii barabara tumeizungumza mara nyingi sana ili tuweze kuiweka kwenye usanifu. Nami nitumie nafasi hii kumkumbusha tu kwa sababu niliongea na Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Tabora kwamba kipande hiki cha barabara ni muhimu na anawatambua kwamba wananchi wengi wanakwenda Nkinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni muhimu sana kwa barabara kuja Ziba kwa sababu wananchi pia wanatoka maeneo ya Tabora wengine wanakuja Nkinga kutokea Ziba. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge tutaiweka kwenye mpango ili barabara iweze kutengenezwa na pia iweze kuongeza huduma muhimu katika maeneo haya.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ninayo barabara ya Kitunda – Kivule – Msongola, mkandarasi yupo site kwa zaidi ya miezi 10 sasa na barabara hii inahudumia kata tano na magari yanakwama hata wakati wa jua kali. Ningeomba nipate kauli ya Waziri kwa nini mkandarasi asilipwe fedha ili aendelee na kazi kuondoa kero kwa wananchi wa Jimbo la Ukonga? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waitara anatambua barabara hii tumezungumza mara nyingi na hata tulikuwa na utaratibu wa kutembelea maeneo haya na wakati wa mvua kwa kweli eneo hili limeharibika sana na nilikuwa nimeelekeza kwamba sasa mkandarasi alipwe pamoja na juhudi kubwa za kulipa wakandarasi sehemu zote nchini lakini alipwe ili barabara hii iendelee kutengenezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitaendelea kufuatilia kuhakikisha kwamba mkandarasi anapata fedha na binafsi nimeongea na mkandarasi ili ajiandae kwamba atakapolipwa tu mara moja aingie kazini ili sehemu hii korofi iweze kurekebishwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika mkakati wa Serikali kuhakikisha mikoa yote inaungana inakuwa na mtandao wa barabara; kuna barabara inayoanzia Mahenge – Mbuga kupitia Mbuga ya Selous mpaka Liwale. Rais aliahidi wakati wa kipindi cha kampeni, lakini sijaona mahali popote katika Wizara kama kuna mchakato wa kutoboa barabara hii kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Lindi. Je, Serikali inatoa kauli gani kutokana na hili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inafanya utaratibu na ni sera kwa kweli kuunganisha mikoa yote. Mheshimiwa Mlinga tumezungumza kwamba barabara hii niliyojibu swali la msingi pia urefu wa kilometa alizozitaja unaunganisha pia sehemu ya Mahenge kuja pale Lupiro. Pia iko haja ya kuunganisha Mahenge na wenzetu wa kule Liwale, lakini kunahitaji logistics nyingi sana kwa sababu inapita katika hifadhi ya mbuga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Mlinga avute subira, tutaendelea kuzungumza wakati tunaangalia logistics nzuri ili tuweze kuwaunganisha wananchi wa Mahenge na eneo la Liwale kwa maana ya Mkoa wa Lindi.
MHE. DEVOTA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Serikali iliwazuia wananchi wa Kata ya Bigwa, Kilakala na Kola wasifanye maendeleo yoyote kwenye maeneo yao ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo. Nataka kujua, kwa kuwa tathmini imekwishafanyika, ni kwa nini Serikali isiwalipe fidia wananchi hawa badala ya kuwaacha kwa zaidi ya miaka 14 mpaka sasa wanashindwa kuendeleza maeneo yao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali ina mpango wa kujenga barabara hii muhimu sana kutoka Biggwa kwenda mpaka Kisaki. Barabara hii niliipita kutoka Biggwa nimeenda mpaka Dutumi kuangalia miundombinu iliyopo katika maeneo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimfahamishe tu Mheshimiwa Devota kwamba pia tutaitumia hii barabara kwa ajili ya kupitisha vifaa na huduma mbalimbali kwa ajili ya access ya kwenda kwenye ujenzi wa Stiegler’s Gorge kule tunapokwenda kutengeneza umeme. Kwa hiyo, tunaona umuhimu wa barabara hii pamoja na barabara inayotokea Ngerengere kuja Mvuha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru wananchi kwa kweli kwa kuacha maeneo wazi kwa sababu itatuwia urahisi wa sisi kuanza taratibu kwa sababu ujenzi wa barabara unaanza katika hatua ya usanifu, kufanya michoro na hatua ambayo ilikuwa inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Devotha avute subira na nitalifuatilia suala hili kuona wananchi wanalipwa haki zao, lakini pia ni fursa kwetu kuweza kushughulikia barabara hii kwa sababu barabara ni huduma. Tutakapowapa barabara wananchi wake pia watanufaika na barabara hii.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza moja la nyongeza. Mkandarasi aliyepewa barabara ya Urambo – Kaliua kilometa 28 tu ameonesha udhaifu mkubwa kuanzia mwanzoni sasa hivi ni karibu miezi 10 kazi iliyofanyika ni ndogo sana. Wakati wa ziara ya Mheshimiwa Waziri anaweka vyombo kwenye site, Waziri akiondoka anaondoa vyombo. Serikali haioni sasa sababu ya kubadilisha mkandarasi huyu ili wananchi wa Kaliua na Urambo waweze kupata barabara ambayo ni kubwa sana kwa ajili ya uchumi wa Kaliua na Urambo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hizi taarifa nizipokee kama ni taarifa mpya kwangu kwa maana kwamba tutafanyia kazi ili tuone kama kuna huu mchezo unafanyika wa kuweka vifaa site wakati wa ukaguzi halafu baadaye vinaondolewa ili tuweze kuangalia na tuchukue hatua. Kwa sababu ujenzi wa barabara hii na mkandarasi kuwepo site ni kwa mujibu wa taratibu na pia iko mikataba na kama kuna mchezo huu tutaona rooms zilizoko kwenye mkataba wetu ili tuweze kuchukua hatua stahiki na mwenyewe nitahakikisha nalifuatilia hili mguu kwa mguu. (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa barabara kutoka Mpwapwa – Lupeta kwenda Matomondo – Mlali mpaka Pandambili ni barabara ya mkoa. Namshukuru sana Meneja wa Mkoa anajitahidi lakini kwa kuwa kuna daraja la Matomondo la Tambi linashindikana kujengwa kwa sababu ya gharama kubwa. Je, Waziri anasemaje kuhusu daraja hilo na yuko tayari kutembelea hiyo barabara? Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli mara kwa mara nimetembelea eneo hili la Mpwapwa ili kuweza kujionea hali ya uharibifu kwa sababu tuko karibu hapa na nimeweza kuona kwamba ziko changamoto. Ni kweli daraja ambalo Mheshimiwa Mbunge anazungumza ni daraja kubwa, iko nafasi ya kuweza kuhamisha ili daraja liwekwe sehemu ambapo gharama za ujenzi zitakuwa ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nia ya Serikali tuweze kujenga kwa tija lakini pia kupunguza gharama, gharama zikipunguza zitatuwezesha kutoa huduma maeneo mengine. Kwa hiyo, namwambia Mheshimiwa Mbunge, nitakuwa tayari kutembelea eneo hili ili wakati mwingine mimi na yeye tukiwa na wataalam tuweze kuona kwamba ni wapi tunaweza tukahamishia daraja hili ili tusaidiane pale itakapohitajika saa nyingine wananchi kuachia maeneo haya. Lengo tuweze kupata daraja ambalo linawapa huduma wananchi hawa wa maeneo haya. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ina kata 29. Kati ya hizo, kata 20 zinahudumiwa na barabara niliyoitaja. Kata hizo ni Katerero, Kemondo, Ibwera, Nakibimbiri, Kasharu, Kisogo, Kaibanja, Katoro, Kyamuraire, Ruhunga, Mugajalwe, Izimbya, Kibirizi, Kaitoke, Kikomero, Rukoma, Rubare, Buterakuzi, Mikoni na Bujugo. Aidha, Bukoba kuna mvua nyingi sana barabara ya udongo inaharibika, mara nyingi inakuwa haipitiki na huko ndiyo kuna mazao mengi kama kahawa na ndiyo uchumi mzima uko kule. Kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kujenga lami barabara hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rweikiza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua maeneo haya ni muhimu sana katika uzalishaji na pia tunatambua kwamba ziko mvua nyingi na kumekuwa na uharibifu wa mara kwa mara. Nampongeza tu Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu mara nyingi tumezungumza juu ya kuhakikisha kwamba barabara hizi tunazitengeneza na kwa kweli kama alivyosema, hizi ni kata nyingi sana, kata 20 kati ya kata 29.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge ikiwa ni pamoja na wananchi wa maeneo ya Kata hizi ikiwemo Kata za Katerero, Kemondo, Ibwera na kata nyingine kwamba baada ya kukamilisha kuunganisha mkoa na mikoa mingine nguvu kubwa tutailekeza katika maeneo haya ya barabara ambazo zinapita kwenye wilaya zetu ikiwemo maeneo haya aliyoyataja ili sasa tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Bukoba Vijijini kwamba maeneo haya tutayatazama na tutayaweka katika mpango ili siku za usoni tuweze kuitengeneza barabara kwa kiwango cha lami.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri kuhusu swali lililopita, naomba kuiuliza Serikali, barabara ya Kyaka 2 kutoka Katoro - Ishembulilo - Kashamba - Kyaka; eneo lile ni bovu sana kila mwezi Aprili barabara haipitiki. Pamoja na kwamba amesema inahudumiwa na TANROADS, naomba commitment ya Serikali ya kuweka madaraja kwenye maeneo yale ili mwezi wa Aprili kuwe kunapitika kama sehemu nyingine. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bulembo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu nimhakikishie Mheshimiwa Bulembo kwamba nimemsikia, nami nimwelekeze tu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera aende kuangalia eneo hili na kushauri tufanye nini juu ya kutengeneza daraja eneo hili korofi. Kama ilivyo kawaida, maeneo yote korofi nchi nzima tunaendelea kuyashughulikia wakati tukiendelea na harakati za kuboresha barabara kuhakikisha wananchi wetu wanapita muda wote katika maeneo yao.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Rais mwezi Mei alifika Iringa katika Wilaya ya Kilolo na akatoa ahadi kwamba barabara ile ya kutoka Ipogolo - Kilolo ambayo inaitwa sasa barabara ya Mfugale ianze kujengwa mara moja. Je, ni lini barabara hiyo itaanza kujengwa ili ahadi ile ya Rais aliyotoa kwa wananchi iweze kutimia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwamoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana kwa sababu tumezungumza sana juu ya barabara hii hata kabla ya ahadi ya Mheshimiwa Rais. Kwa vile Mheshimiwa Rais ametoa ahadi kuitengeneza barabara hii, tulikubaliana kwamba baada ya Bunge hili nitatembelea huko ili tuweze kuweka msisitizo kuhakikisha kwamba barabara hii inajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi natambua kwamba barabara hii ilishasanifiwa. Kwa hiyo, harakati za ujenzi wa barabara hii, napenda wananchi wa Kilolo wajue ujenzi ulishaanza kwa sababu hatua za awali tumeshaanza, sasa ni zoezi la kupata fedha ili barabara ijengwe. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwamoto asiwe na wasiwasi barabara hii itajengwa na kwa msisitizo wa Mheshimiwa Rais tutakwenda kuijenga barabara hii. (Makofi)
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ujenzi wa barabara ya Oldian Junction – Mang’ola – Matala - Kolandoto umeshakamilika miaka miwili iliyopita na barabara hiyo ni muhimu sana kwa sababu inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu. Je, ni lini sasa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hiyo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Qambalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ukiotokea upande wa Lalago ukivuka Sibiti kwa kushoto kule iko barabara hii ambayo itakuwa inakwenda Karatu ambayo michoro na usanifu wake umeshakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii ina interest kubwa sana kwa sababu kuna uzalishaji mkubwa, historia muhimu na pia kuna utalii mkubwa katika maeneo haya. Kwa hiyo, kwa sababu hatua hii imeshakamilika, tuko kwenye hatua ya kutafuta fedha, wakati wowote tukipata fedha ujenzi utaendelea. Ahsante sana.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Makofia - Mlandizi ni muhimu sana ambayo inaunganisha wananchi wa Halmashauri ya Bagamoyo na Kibaha Vijijini. Barabara hiyo sasa hivi ina matatizo sana ya kupitika hasa baada ya mvua hizi nyingi zilizopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara ni ahadi ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2005, 2010 na 2015 kujengwa kwa kiwango cha lami. Ni lini fidia italipwa kwa ajili ya barabara hiyo na lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kawambwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Kawambwa ni shahidi kwamba tumezungumza muda mwingi sana juu ya barabara hii. Barabara itakuwa na urefu wa kilometa zaidi ya 30 kuja Mlandizi. Kuhusu fidia tulishafanya tathmini tayari, tutaendelea kuwasiliana na wenzetu Wizara ya Fedha hizi fedha zipatikane ili wananchi hawa walipwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi watalipwa kwa sababu tulikuwa na fidia nyingi nchi nzima katika maeneo mbalimbali, lakini tumefika hatua nzuri, maeneo mengi tumeshalipa fidia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Kawambwa asiwe na wasiwasi. Nafikiri baadaye tuzungumze na tuongee na wataalam tuone hatua hii imefika wapi ili tuweze kulipa mara moja hii fidia ya wananchi wake.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali la kwanza, kwa sababu ni Sera ya Serikali kuunganisha mikoa kwa barabara ambazo ndizo tunazitegemea kwa ajili ya maendeleo yetu. Ni lini tutegemee Serikali itaunganisha barabara inayotokea Liwale Mkoa wa Lindi kuweza kufika Morogoro?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa muda mrefu sana Serikali imekuwa ikijificha kwa kusema kwamba kumekuwa na upembuzi yakinifu ukiwa unafanyika na mara nyingi upembuzi huu umekuwa ukichukua muda mrefu na wakati mwingine inaweza kufika hata miaka 10 tunakuwa kwenye upembuzi yakinifu. Ni lini tutegemee Serikali itaweza kuweka limitation au taratibu ambapo kutakuwa na muda maalum wa upembuzi yakinifu kufanyika ili ujenzi wa barabara uwe unaanza kufanyika mapema? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lathifah, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba ni Sera ya Serikali kuunganisha mikoa. Kama nilivyojibu wiki iliyopita wakati nikijibu swali la Mheshimiwa Mlinga, nilisema kwamba tutakwenda kutazama kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Lindi kwa maana ya Liwale na Mahenge, lakini hii ni siku za usoni, kwa sababu ziko logistics nyingi lazima zifanyike kwa sababu barabara hiyo itapita katika Hifadhi ya Selous lakini pia structures zake zinahitaji fedha nyingi. Kwa hiyo, tutaendelea kuitazama na Serikali inajua umuhimu wa kipande hiki cha barabara kuunganisha kuja Mahenge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwamba Serikali inajificha kwa kusema inasanifu na kutengeneza michoro; hili siyo kweli. Niseme kwamba mpaka sasa hivi barabara za lami zinazounganisha mikoa karibu mikoa yote tunakamilisha. Barabara zaidi ya kilometa 13,000 tumeshatengeneza kwa lami kwa maana ya kuunganisha mikoa na nchi za jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata katika bajeti hii ya mwaka 2018/2019, tumependekeza kufanya usanifu wa barabara kilometa 3,856. Hizi ni kilometa nyingi sana na hii ni kuonesha jinsi namna gani Serikali ya Chama cha Mapinduzi iko committed kuhakikisha kwamba kila tunapokamilisha barabara fulani ni mwanzo wa kuendelea kusanifu barabara nyingine. Kwa hiyo, Mheshimiwa Lathifah ataendelea kusikia tukisanifu na kutengeneza michoro ya barabara kila wakati kwa sababu kila wakati tunavyokamilisha ujenzi wa barabara, kwetu sisi kama Serikali ni fursa ya kutengeneza barabara nyingine. Ahsante sana.
MHE. AYSHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, barabara inayotokea Singida Mjini – Ilongero – Mtinko – Mudida – Kidarafa – Ikungi - Haydom yenye urefu wa kilometa 93.4 ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekuwa ukisuasua. Kukamilika kwa barabara hii kutaharakisha sana shughuli za maendeleo kwa Singida Vijijini. Barabara hii ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne…
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia iko katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015. Je, ni lini sasa barabara hii itakamilika kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuharakisha shughuli za maendeleo kwa wananchi wa Singida Vijijini? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aisharose Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara hii imekuwa ikitengenezwa kidogo kidogo lakini nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba matengenezo yale aliyoyaona yalitokana na usimamizi mzuri wa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida. Kila alivyobakiza fedha ameendelea kutengeneza kilometa moja, kilometa mbili na takriban sasa tuna kilometa 10 zimetengenezwa kwa mtindo huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu, mwaka huu wa fedha 2018/2019, tumetenga shilingi milioni 200 kuanza usanifu wa kilometa hizi 93 kwenda Haydom. Nami wiki zilizopita nimepita kwenye barabara hii kuweka msisitizo kwamba usanifu uanze mara moja mara baada ya kupata fedha ili sasa barabara hii iungane na barabara itakayokuwa inatoka Haydom kuja Sibiti, barabara kubwa hii ambayo itajengwa kwa kiwango cha lami ili wananchi wa Singida na maeneo mengine ya jirani waweze kwenda kirahisi kupata huduma katika Hospitali ya Haydom.
MHE. CECIL M. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kufahamu kutoka Serikalini kwamba barabara ya Masasi inayopitia Vijiji vya Nangaya – Chikunja – Lukuledi – Naipanga – Mkotokuyana mpaka Nanganga inaelekea kujengwa kwa lami hivi karibuni. Hata hivyo, uthamini wa mali na rasilimali za watu katika maeneo hayo yote niliyoyataja umefanyika zaidi ya miaka mitano iliyopita. Je, Serikali itakwenda kurudia kufanya uthamini au itawalipa watu wale fidia zao kutokana na uthamini uliofanyika miaka mitano iliyopita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mwambe pamoja na wananchi kwamba uthamini uliofanyika kama hakuna matatizo makubwa ya kurudia, ndiyo utakaotumika kulipa wananchi hawa. Niwafahamishe tu wananchi kwa ujumla kwamba utaratibu uliopo kuna namna ya kuangalia thamani ya fedha kwa sasa, lakini base itakayotumika ni ule uthamini uliofanyika kipindi ambacho Mheshimiwa Mbunge amekitaja. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, uko utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba fedha zile zitalipwa kulingana na hali ya sasa.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa sababu swali hili lilikuwa la mwezi wa Pili mwaka huu. Hivi sasa ni kweli, barabara hizo nilizozitaja zimefanyiwa matengenezo, lakini kwa kuwa, sasa fedha zinazotengwa kwa wenzetu wa TARURA kutengeneza hizi barabara za vijijini ni kidogo sana je, Serikali haioni umuhimu mkubwa wa kutafuta vyanzo vingine na kuhakikisha kuwa, barabara zote zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini, anaweza kupatiwa fedha za kutosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sisi wote Wabunge humu ndani ni mashahidi, maeneo mengi yanayopata makorongo makubwa katika halmashauri zetu na majimbo yetu yanahitaji mdaraja makubwa. Fedha zinazotolewa kwa wenzetu wa TARURA ni kidogo sana kiasi kwamba, hata kama wangepewa fedha makorongo hayo hayapo katika jiografia au mtandao wa barabara wanazohudumia wenzetu wa TARURA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa je, Serikali haioni ni wakati wa kuja na mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayohitaji madaraja makubwa ambayo ni kikwazo kwa huduma za kijamii zikiwemo kliniki za akinamama, huduma za afya na elimu zinapatiwa mpango mkakati wa kujengewa madaraja hata ya chuma? Kwa kuwa, eneo hilo ni tete na…
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni kweli, fedha ambazo tunazipata kwa ajili ya matengenezo ya barabara nchi nzima, ikiwemo pesa za TANROADS na TARURA ni kidogo. Sasa hivi uwezo wa fedha tunazopata ni asilimia 57 ya mahitaji. Hata hivyo niseme tu kwamba, kati ya fedha tunazozipata asilimia 90 zinakwenda kufanya matengenezo ya barabara, kwa hiyo, utaona kwamba ni asilimia 10 tu ndiyo inayokwenda kujenga barabara mpya. Kwa hiyo iko haja ya kuongeza fedha kwenye matengenezo ya barabara zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, lile zoezi la kutambua network ya barabara kwa upande wa wenzetu wa TARURA, limefanyika, lakini kulikuwa na changamoto ya data ambazo zilipatikana; ikalazimika TARURA waende maeneo husika ili tuweze kuzitambua barabara zote ili sasa mgawo wa fedha na mahitaji ya fedha tuweze kuyaona kwa uhakika zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo ambavyo vinatumika ni pamoja na urefu wa mtandao wa barabara, tunatumia vigezo pia vya aina ya barabara, kama ni barabara ya lami, barabara ya changarawe, barabara ya udongo na hali ya barabara ilivyo na idadi ya magari yanayopita katika maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga na TARURA wanafanya kazi nzuri na ni kesho tu tunategemea taarifa itawasilishwa TAMISEMI, itawasilishwa kwenye Mfuko wa Barabara na upande wa kwetu kwenye Wizara, ili tuangalie mahitaji yetu halisi na tuweze kuomba fedha zaidi kukamilisha maeneo ambayo ni korofi. Kwa hiyo, kazi inaendelea ya kuhakikisha barabara zetu tunaziboresha.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa barabara hii imechukua muda mrefu sana kukamilika kwa kiwango cha lami, na kwa kuwa tunayo Sheria ya PPP, ili kuacha kuendelea kutegemea zaidi bajeti, kwa nini Serikali imeshindwa kuweka msisitizo kwenye PPP ili kuhakikisha kwamba miradi hii pamoja na miradi ya ujenzi wa barabara inatekelezeka kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jesca Kishoa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifahamishe tu Bunge lako Tukufu kwamba harakati za ujenzi wa barabara hii zimeshaanza, kwa sababu ujenzi wa barabara unaanza kwenye hatua ya usanifu, kupata michoro na tuko kwenye hatua ya kutafuta fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu katika bajeti hii tutakayoanza mwezi wa Julai ya 2018/2019 tumetenga shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kuanza ujenzi. Vilevile yapo mazungumzo ambayo yanaendelea ili kuweza kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua umuhimu wa hii barabara kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, Serikali imetupia macho na kwa kweli imeonyesha commitment ya hali ya juu kuhakikisha kwamba barabara hii inakamilishwa. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Jesca Kishoa pamoja na hii concept ya PPP, tunakaribisha wadau wa PPP kama watajitokeza na kama mradi wao hautakuwa mzigo kwa wananchi Serikali iko tayari kuchukua mawazo yake hayo.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuweza kunipatia nafasi hii. Umuhimu wa barabara ambayo imeulizwa katika swali hili inafanana kabisa na umuhimu wa barabara ya kutoka Haydom - Kidarafa - Mwanga - Nkhungi - Nduguti mpaka kwenye Daraja la Sibiti kwenda Simiyu. Ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiula, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu Mheshimiwa Kiula anafahamu kwa sababu muda si mrefu tulitembelea barabara hii kutoka Iguguno kupitia Gumanga, tukaenda mpaka Sibiti kuona maendeleo ya ujenzi wa daraja ambalo muda si mrefu litakamilika. Cha msingi niseme tu kwamba barabari hii ya Haydom – Kidarafa hatua zake za kuanza ujenzi ni nzuri na kama nilivyojibu siku chache zilizopita sasa tutakwenda kufanya mkutano wa wadau ikiwemo Waheshimiwa Wabunge na viongozi mbalimbali wa mikoa ambayo barabara hii itapita kwa sababu itaunganisha Mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Simiyu na mikoa mingine ile ya Kanda ya Ziwa. Kwa upande wa Serikali tuko katika hatua nzuri na wakati wowote tutaweza kuanza kujenga barabara hii muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Kiula asiwe na wasiwasi. Najua tu barabara hii ikikamilika hiki kiungo cha hii barabara tena kutoka Singida kwenda Sibiti nayo ni muhimu ili kufupisha gharama za usafiri kutoka Singida kwenda kwenye Mikoa ya Kanda ya Ziwa.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wakati tunapitisha bajeti hapa nilizungumza juu ya barabara muhimu sana Kanda ya Kusini inayopita mikoa yote ya Kusini, kwa maana ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, barabara ya Ulinzi. Kwa kuwa bajeti haijasema chochote juu ya barabara hii kwamba imetengewa kiasi gani, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara hii ili huu mpaka wa Kusini unaoanzia Mtwara Mjini maeneo ya Mahurunga, Kitaya, Tangazo, Tandahimba, Newala mpaka kule Ruvuma uweze kulindwa sawasawa pale ambapo maadui wa nchi hii wanaweza wakatokea? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maftaha, Mbunge wa Mtwara Mjini maarufu kama Gas City, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua umuhimu wa barabara hii ya ulinzi. Sisi kama Serikali ambacho tunakifanya kabla hatujaja kuboresha barabara iwe kiwango cha lami, tunahakikisha inapitika muda wote. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mtwara kwa ujumla tunahakikisha kwanza barabara hii inapitika lakini kwenye strategic plan zetu za Wizara tumeitazama. Labda tu akipata nafasi tuzungumze ili tuangalie tumeipanga lini tutakuwa kwenye hatua ya lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi msukumo mkubwa ilikuwa ni kuhakikisha hii barabara inayotoka Mtwara Mjini - Mnivata - Tandahimba - Newala - Masasi inakamilika kwa kiwango cha lami. Ukiwa Tandahimba iko barabara inakwenda kuungana na barabara hii ya msingi, lakini kama alivyosema ukiwa Newala kiko kipande kinakwenda kuungana na barabara hii, kwa hiyo, barabara hii kubwa ikikamilika basi tutaweza kuzingatia na hii barabara ya msingi kuhakikisha inajengwa kwa kiwango cha lami. Tuonane tuangalie kwenye mipango ya Wizara ni lini tutakwenda kwenye hatua ya lami.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, hayo marekebisho anayoyasema Mheshimiwa Waziri yalishafanyika tangu mwaka jana na sasa hivi tuko kwenye hatua ya kusubiri fedha kama anavyosema. Kwa kuwa barabara hii umuhimu wake umeongezeka kitaifa kwa sababu mradi wa kufua umeme wa Stiegler’s unaojengwa utatumia barabara hii lakini pia mpango wa Serikali wa kufufua utalii katika Ukanda wa Kusini hasa katika Mbuga ya Selous barabara hii itahitajika. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuharakisha ujenzi wa barabara hii ili kufungua utalii katika ukanda wa Kusini katika Mbuga ya Selous ukizingatia zaidi ya 70% ya mbuga hii iko Mkoa wa Morogoro? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa, Sheria Tathmini inasema kwamba mtu akishafanyiwa tathmini alipwe ndani ya miezi sita na Serikali sasa inasema kwamba itajenga barabara hii kwa kutegemea upatikanaji wa fedha. Kwa kuwa malipo ya fidia yanalipwa baada ya fedha kupatikana, je, Serikali inatoa kauli gani kwa watu watakaoathirika na mradi huu ambao hawafanyi maendelezo ya nyumba zao zaidi ya miaka nane sasa ili waweze kuendelea na ujenzi wao mpaka hapo hizo hela zitakapopatikana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mgumba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Mgumba kwa sababu amefuatilia sana barabara hii. Tangu niingie kwenye Bunge hili kila wakati nimemsikia akizungumza juu ya barabara ya Bigwa – Kisaki. Hata Waswahili wanasema baada ya dhiki ni faraja, ni faraja kwamba sasa tunaenda kutengeneza hii barabara na hatua iliyofikia siyo haba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza, amezungumza juu ya umuhimu wa barabara hii kujengwa kwa haraka. Kweli maeneo haya ni muhimu sana kwa sababu barabara ya Bigwa – Kisaki ita-facilitate upitishaji wa mizigo na vitu muhimu kwenda kwenye ujenzi sehemu tunayoenda kufua umeme kule Stiegler’s Gorge, lakini pia nayafahamu maeneo haya yana utalii kama alivyosema na eneo hili pia ni muhimu sana kwa kilimo cha mazao ya chakula na biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeitazama barabara hii tumeitazama na hatua iliyofikiwa siyo hatua mbaya, kipande cha kilometa 78 tutakwenda kuungana na barabara inayotoka Ngerengere ambayo ndiyo tumeipa kipaumbele zaidi ili mizigo ianze kupita Ngerengere kwenda Mvuha mpaka Stiegler’s Gorge. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi barabara zote hizi mbili zitaunganika tu, tukianza na ile ya Ngerengere pamoja na hii aliyozungumza. Barabara zote ziko katika maeneo yake nasi tumejipanga kuhakikisha tunaendelea kujenga kwa kiwango cha lami. Hatua iliyofikiwa ni nzuri ya kutafuta fedha ili tuanze ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa eneo hili la Morogoro kwa ujumla wawe na subira wakati tunaendelea na harakati hizi. Hata kwa mwaka huu tumetenga shilingi bilioni 5 kuanza kujenga barabaa hii ya Ngerengere - Mvuha, kwa hiyo, kuja kuunganisha na barabara hii itakuwa rahisi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia utaratibu na kanuni zipo kwamba tutalipa fedha kulingana na thamani ya fedha kwa wakati huo. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mgumba na wananchi wake ambao wamepisha maeneo kwa muda mrefu, niwapongeze sana, wamevumilia miaka nane, tunaendelea kutafuta fedha ili tulipe fidia hii. Tutalipa fidia hii kulingana na kanuni na sheria zinavyosema ili tuweze kuwa-compensate wananchi hawa kwa sababu wamesubiria fidia yao kwa muda mrefu.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri anaifahamu vizuri sana Mpwapwa na barabara ya kutoka Kongwa - Mpwapwa anaifahamu vizuri sana; na kwa kuwa Serikali imekubali kujenga barabara ya lami kutoka Kongwa - Mpwapwa, je, barabara hii kama nilivyoomba itaanzia Mpwapwa - Kongwa? Naomba Waziri awathibitishie hilo wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa au yeye anasemaje?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwei Mheshimiwa Lubeleje amekuwa akifuatilia sana barabara hii. Wiki kama nne zimepita baada ya mvua kupungua nilitembelea eneo la Mpwapwa nimeenda kuona hata eneo la Godegode ambalo amekuwa akipigia kelele sana ili tuje na utaratibu wa kuhakikisha turekebisha barabara iweze kupitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu barabara hii ya lami inayotokea barabara kuu kwenda Kongwa ujenzi unaendelea vizuri, hii ndiyo sehemu ya barabara ambayo Mheshimiwa Mbunge anazungumza. Nafahamu concern yake ni kuhakikisha tunajenga ile barabara ya kutoka Mpwapwa Mjini ili ije ikutane na hii barabara inayotoka Kongwa na tumetenga fedha. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Lubeleje juhudi zake zinazaa matunda na anafanya kazi nzuri na wananchi wa Mpwapwa watambue hivyo kwamba tutaendelea kujenga barabara hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata jana tulipiga hesabu kidogo kuona kwamba kwa kiasi cha fedha ambacho tumetenga tunaweza sasa tukawa na utaratibu wa mkataba wa kilometa karibu 7 hivi tukaanza kujenga kutoka Mpwapwa Mjini. Kwa hiyo, tutakwenda hatua kwa hatua kadiri fedha zinavyopatikana kuhakikisha eneo lake lote hili linapata barabara ya lami. Kwa hiyo, Mheshimiwa Lubeleje asiwe na wasiwasi.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mzumbe – Mgeta ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne kujengwa kwa kiwango cha lami. Je, ni lini itajengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uko utaratibu wa kuratibu ahadi zote za viongozi wetu wakuu kuhusu ujenzi wa miundombinu hii ya barabara. Kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia barabara hii ya Mgeta, tutaitazama kadiri itakavyowezekana tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami. Nilikuwa nimepata kabrasha kwa maana ya kuziangalia ahadi zote za viongozi kuanzia Awamu zilizopita mpaka sasa hivi, labda hata baadaye tunaweza tukazungumza ili tuone tumejipanga vipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini fursa zimekuwa nzuri kwa kuwa zile harakati za kuunganisha mikoa hatua iliyofikiwa ni nzuri sasa tutakwenda kuunganisha wilaya na mikoa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira lakini tutazungumza ili tuione sasa kwenye strategic plan yetu kwamba barabara hii tumeipangia nini. Muhimu zaidi ni kuhakikisha kwamba ahadi zote ambazo viongozi wakuu wamezitoa na sisi kama Wizara tunazitekeleza ili kutekeleza ahadi za viongozi.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mji wa Tunduma ni wa kibiashara na kuna mpaka ambao unatumiwa na nchi karibu nane za Kusini na Kati mwa Afrika. Kumekuwa na msongamano mkubwa sana wa malori yanayovuka mpaka ule na kusababisha wananchi wa Tunduma kuchelewa kufanya shughuli zao kwa sababu ya msongamano ule. Kuna barabara ya kilometa 12 kutoka eneo la Mpemba kuja Tunduma Transfoma ambapo viongozi wengi wameahidi kuijenga kwa kiwango cha lami ili kupunguza msongamano kwa magari yanayotoka Sumbawanga kwenda Mbeya na yanayotoka Mbeya kwenda Sumbawanga lakini pia kuwarahisishia usafiri wananchi wa Mji wa Tunduma. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kama ahadi za viongozi zilivyotolewa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakajoka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua ziko challenge kubwa za msongamano wa magari kwa sababu Mji wa Tunduma unakua kwa kasi na huduma za kijamii zimeongezeka sana. Nimhakikishie Mheshimiwa Mwakajoka na wananchi wa Tunduma kwamba tumejipanga vizuri kuhakikisha maeneo yote ambayo yana changamoto za msongamano tunayashughulikia, kwa hiyo, nimtoe hofu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijafanya ziara Mkoa wa Songwe, baada ya Bunge hili nitatembelea huko, nafikiri itatupa nafasi zaidi tuweze kuzungumza na niweze kuona. Pia niione mipango iliyoko TANROADS Mkoa kuhusu maboresho ya eneo hili la Tunduma ili tuweze kuondoa shida ambazo zinawapata wananchi na kuondoa tatizo la kupoteza muda kwa ajili ya kwenda kuzalisha katika maeneo mbalimbali.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza, ukiangalia majibu ya Mheshimiwa Waziri anasema kwamba baada ya kukamilika barabara ya Kinyerezi - Mbezi ndipo wanapotegemea kuanza ujenzi wa barabara hii inayoongelewa hapa na Mheshimiwa Kubenea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba hizi ni barabara mbili tofauti na mahitaji ya wananchi wale ni tofauti. Tunataka kufahamu ni lini Serikali specifically itaanza ujenzi wa barabara inayotajwa iliyoahidiwa miaka mitano iliyopita? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, suala lililopo Jimbo la Ubungo linafanana moja kwa moja na masuala yaliyopo katika Jimbo la Ndanda, Mkoa wa Mtwara kwamba Serikali iliahidi kujenga kwa kiwango cha lami barabara inayoanzia Mtwara Mjini – Nanyamba – Tandahimba – Newala - Masasi mpaka Nachingwea kuja kutokea Nanganga. Sasa tunataka kufahamu pamoja na mkandarasi kuwepo pale ambaye anasuasua kwenye kazi hii, ni lini Serikali specifically itaanza ujenzi wa barabara inayotokea Masasi kwenda Nachingwea kuja kutokea Nanganga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika barabara ambazo nimezitaja awali ndiyo zilikuwa na matatizo makubwa na ndiyo zilikuwa kipaumbele. Niseme tu kwamba nafahamu maeneo haya ambayo Mheshimiwa Mbunge anayazungumzia ni korofi na kama nilivyosema tutaendelea kuyashughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo matatu ambayo tulikuwa tunaendelea nayo kuhakikisha kwamba barabara hii inatoa huduma iliyokusudiwa wakati sasa tukikamilisha hii barabara ni fursa tosha kuja kuijenga barabara hii. Yako maeneo pale Kwa Bichwa, Kwa Mahita na eneo la Makange Sekondari ndiyo zilikuwa sehemu korofi. Alikuwepo mkandarasi anaendelea kurekebisha maeneo yale lakini kutokana na mvua nyingi zilizonyesha amesimama kidogo ili hali ya hewa ikiwa nzuri hii barabara tuiimarishe halafu baadaye sasa wakati barabara hizi zinakamilika ni fursa tosha kuja kuijenga hii barabara kama ahadi ilivyokuwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Ndanda kuja Nachingwea kupitia Nanganga kama tulivyoizungumza katika bajeti tumetenga fedha kwa ajili ya kutengeneza kipande hiki kutoka Nachingwea - Nanganga na Nachingwea – Ruangwa – Nanganga. Mheshimiwa Mbunge anafahamu pia liko daraja katika Mto Lukuledi tunaendelea kulijenga na hii ni sehemu ya kukamilisha barabara hii anayoitaja ili sasa tuweze kuunganisha kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimsihi tu Mheshimiwa Mbunge avute subira na wananchi wa Ndanda wategemee kwamba barabara hii tunaenda kuikamilisha ili waendelee kupata huduma kama wananchi wengine katika maeneo ya Tanzania.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Pamoja na juhudi za Serikali za kuweka barabara nyingi za kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam hatua ambayo naipongeza, lakini ninalo swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Nzasa - Kilungule kuungana na Buza ni muhimu sana kwa wakazi wa Mbagala katika kuondoa msongamano. Je, Serikali lini itaanza ujenzi wa barabara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa amekuwa akifuatilia barabara nyingi lakini nimhakikishie kwamba katika harakati za kukwamua msongamano katika Jiji la Dar es Salaam barabara 12 zimekamilika. Ziko barabara 10 ambazo mpaka kufikia mwezi Aprili tunaendelea nazo lakini ziko barabara nyingine ambazo tutazishughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Serikali iko committed kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linafunguka. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge hii barabara anayoizungumza kutoka Nzasa – Kilungule - Jeti Kona itashughulikiwa na mradi wa DMDP. Nitajaribu kufuatilia baada ya mkutano wa leo ili nione hatua ilivyo na nitampa mrejesho lakini niombe tu tuendelee kushirikiana na kupeana taarifa kwa sababu lengo la Serikali ni kurekebisha maeneo mbalimbali ili yaweze kupitika vizuri.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba nimuulize Naibu Waziri swali ndogo la nyongeza. Kwa kuwa hizi barabara zimekuwa zikijengwa kwa gharama kubwa sana, halafu zinaharibika kwa muda mfupi, je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha wakandarasi wote wanaojenga barabara hizi wanachukuliwa hatua na kurudia ujenzi ili kuepusha kutumika tena gharama nyingine ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli kuna baadhi ya maeneo baada ya barabara kutengenezwa zinaharibika, lakini ni hali ya kawaida kwa sababu ziko sababu nyingi ambazo zinaweza kusababisha miundombinu hii kuharibika. Ndiyo maana baada ya ujenzi wa barabara katika kipindi cha maisha ya barabara tunatenga fedha kwa ajili ya kufanya rehabilitation na baada ya miaka 20 tunafanya matengenezo makubwa kwa maana kwamba ule muda wa maisha ya barabara unakuwa umekwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Serikali…
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alikuja jimboni na akaahidi ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kahama – Nyang’olongo – Bukwimba - Kalumwa - Busolwa hadi Busisi Sengerema na Rais wa Awamu ya Tano pia aliahidi hivyo hivyo. Je, Serikali ni lini itatenga fedha ya upembuzi yakinifu ili kuanza kuijenga barabara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua hii barabara Mheshimiwa Mbunge tumezungumza mara nyingi, ni barabara ambayo inaenda kuunganisha pia katika Jimbo la Msalala kuja Kahama Mjini. Kwa hiyo, kama tulivyozungumza tutaangalia sasa namna nzuri tuweze kuiingiza kwenye usanifu, kwa sababu zile barabara ambazo zinakwenda kuunganishwa na barabara hii Mheshimiwa Mbunge, unajua ile barabara inayokwenda Geita ni muhimu sana kwamba tutaweza kuwa na kipande cha kwenda Sengerema. Ni kipande kifupi Mheshimiwa Mbunge kinahitaji commitment ya fedha siyo nyingi sana. Kwa hiyo, azidi kuvuta subira tutaendelea kutazama kwenye bajeti zinazokuja.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana. Naomba nimuulize swali dogo Mheshimiwa Naibu Waziri. Barabara ya Kitunda – Kivule - Msongora mkandarasi yupo site kwa zaidi ya mwaka mzima sasa, lakini hajatekeleza kazi ile hata zaidi ya asilimia 20, amechimbachimba na kuiharibu. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kwenda Kivule ili akaangalie usumbufu ambao wananchi wanapata na kulazimisha ujenzi ufanyike haraka ili watu wapate barabara ya kupita?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niko tayari na inawezekana kesho pia…
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kutokana na usanifu ambao unafanyika sasa na timu ya wataalam wa bandari ili eneo hili liweze kupatiwa vituo vya kushusha na kupakia abiria, je, timu hii ni lini itamaliza kazi hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tayari kuna tengo la mwaka 2017/2018 kwa ajili ya kujenga gati katika Bandari za Lupingu na Manda. Je, wananchi hawa ambao walipisha maeneo haya watalipwa lini fidia yao ili waendelee na shughuli nyingine? (Makofi)
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA - NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifuatilia sana huduma ya usafiri wa majini lakini huduma ya usafiri wa nchi kavu. Niseme tu kwamba zoezi hili litakamilika kwa muda mfupi kwa sababu hivi ninavyozungumza wataalam wanaelekea maeneo haya na najua adha wanayoipata wananchi kule ziwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, litakapokuwa limekamilika, siyo lazima vijiji vyote alivyovitaja tuweze kuweka vituo vya kushusha na kupakia lakini wataweza kutambua maeneo gani ambayo yatawafanya wananchi hawa wasisafiri sehemu ndefu sana kwa ajili ya kupata huduma. Kwa hiyo, avute subira na sisi tutampa mrejesho. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa maeneo haya watoe ushirikiano ili tupate information za kutosha tuweze kukamilisha zoezi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wale wananchi ambao wanapisha maeneo yao kwa ajili ya maendeleo na sisi kama Serikali tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba fedha zikipatikana tunawalipa mara moja. Kwa sababu tunajua kwamba fidia kama itachelewa kulipwa pia huduma itachelewa kwenda kwa wananchi hawa.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, swali langu kubwa hapa lilikuwa ni barabara zinazoelekea Mamba Miamba Kiwandani, basi naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali moja kubwa kidogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, barabara zinazoelekea Mamba Miamba Kiwandani zipo za aina mbili, ya kwanza ni barabara inayounganisha Kiwanda cha Tangawizi na masoko ya ndani na nje ya nchi na barabara hii inatokea Mkomazi Kisiwani kwenda Same na barabara ya pili ni barabara zinazounganisha walima tangawizi (wakulima) na kiwanda chao.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Rais wa Awamu ya Nne mwaka 2009 alikuja Mamba Miamba yeye mwenyewe akaona jitihada za wananchi, akatoa bilioni 2 za kujenga barabara za kuwaunganisha wakulima na kiwanda chao. Je, Mheshimiwa Waziri huoni kwamba ili uelewe tatizo kubwa la miundombinu ya kiwanda kile ni vyema wewe mwenyewe ukawaahidi wananchi wa Mamba Miamba utakwenda lini kule ili uweze kujibu haya maswali vizuri, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nipo tayari kwenda, lakini uniruhusu nimpongeze tu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu najua kupatikana kwa kiwanda hiki ni pamoja na juhudi zake, lakini niwashukuru na kuwapongeza Mkuu wa Wilaya kwa sababu Mkuu wa Wilaya pia amekuja akiwa na ombi la kutembelea maeneo haya. Natambua kwamba lazima tuboreshe barabara ambazo zinawahudumia wananchi kupeleka malighafi kwenye kiwanda hiki, lakini pia kutoa mazao yanayotokana na kiwanda hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia barabara hii ambayo nimeizungumza ni muhimu sana kwa sababu inapokwenda kuunganisha Mkomazi pia inatoa huduma kwa ajili ya utalii. kwa hiyo, nipo tayari Mheshimiwa Mbunge nitakuja Same tutembelee maeneo hayo. (Makofi)
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa barabara ya Likuyufusi – Mkenda mpaka Msumbiji ambayo inaunganisha Jimbo la Mheshimiwa Jenista Mhagama na nchi ya Msumbiji ambayo katikati hapa kuna wawekezaji wengi sana wamefungua na viwanda lakini barabara hiyo bado ni ya vumbi.
Je, ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kunufaisha Jimbo la Songea Mjini, Jimbo la Peramiho pamoja na wawekezaji waliopo ikiwa kuleta masoko nchini Msumbiji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Ndumbaro kwa sababu ukikutana naye yaani ni barabara ya mchepuo, barabara ya Likuyufusi – Mkenda, kwa hiyo, nimpongeze pia Mheshimiwa Jenista kwa sababu mara nyingi sana amefuatilia barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme tu tumetenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii ya Likuyufusi – Mkenda lakini pia tumetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja kule Mkenda, najua hii ndio changamoto ilikuwa kubwa sana ya eneo hili kwa maana hiyo kwamba tumetenga fedha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nitaendelea tu kukupa mrejesho na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo Mheshimiwa Jenista usiwe na wasiwasi eneo hili tumelitengea fedha.
Mheshimiwa Spika, pia daraja hili la Mkenda ni muhimu sana pia kwa wananchi ambao wanakwenda Mbamba Bay kwa sababu ukitoka Mkenda kwenda kule Tingi hii ni muhimu sana wanaitegemea barabara hii ili waweze pia kutembea na kuvuka kuja upande huu wa Peramiho. Kwa hiyo, tumejipanga vizuri. (Makofi)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, asante. Nashukuru kwa majibu mafupi na precise ya Mheshimiwa Naibu Waziri, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa utaratibu wa manunuzi ni mchakato na majibu yake hayajaeleza kwamba exactly timeframe ni lini Serikali imempa huyu mkandarasi kukamilisha mchakato wake ili ujenzi na ukarabati uanze mara moja.
Sasa nilikuwa naomba kupata majibu kwamba ni lini hasa, ni baada ya miezi mingapi huyu mkandarasi atakuwa amemaliza?
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na utaratibu huko miaka ya nyuma kwamba baadhi ya vitu vinahamishwa mikoa ya Kusini na baada ya uhuru tu mapema ilihamishwa reli lakini pia na taa za Uwanja wa Ndege wa Mtwara. Sasa nilikuwa naomba kujua kwamba ukarabati ambao unatarajiwa kufanyika katika uwanja huu utahusisha pamoja na uwekaji wa taa za kuongozea ndege ambazo zilizoondolewa miaka ya nyuma? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza niseme ujenzi umeshaanza kwa sababu ujenzi una hatua mbalimbali, kwenye hatua hii mpaka mkataba umesainiwa na tumepata fedha nyingi. Kwa taarifa tu Mheshimiwa Nachuma awali tulikuwa tunakadiria tufanye matengenezo kwa shilingi zipatazo bilioni 39 lakini kwa kuzingatia maboresho na kufanya uwanja uwe na uwezo wa kupokea hata ndege Airbus aina ya A340-200 kwa hiyo, tumezingatia, huwezi kupokea ndege hii bila kuwa na taa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kutakuwa na barabara na kutua na kurukia zenye urefu wa mita 3,000, kutakuwa na maegesho ya ndege, kutakuwa na barabara za kuingilia katika uwanja na jengo la abiria lakini kuweza kutua ndege kubwa kama nilivyosema lakini pia taa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Nachuma usiwe na wasiwasi kwamba ule uwanja nafikiri miezi 20 ijayo utaona huduma zimeongezeka na utaendelea ku-enjoy huduma za ndege.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nichukue fursa hii kuipongeza Serikali yetu chini ya Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ya ujenzi wa barabara inayofanya. Pamoja na pongezi hizo nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri inayofanywa kero kubwa kwa wananchi wetu ni fidia. Barabara hii ya kilomita 23 ina jumla ya fidia ya bilioni 8.9; je, kwa nini Serikali sasa isilipe wananchi hawa fidia wakaweza kufanya shughuli zao za kiuchumi na ikaendelea na ujenzi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna barabara ya Kwa Mathias mpaka Msangani ambako ndiyo Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi la Ardhini (Land Force). Barabara hii ina ahadi ya lami muda mrefu. Je, Serikali imefikia wapi kukamilisha au kujenga lami hii katika barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kulipa hizi fidia kwa wananchi. Nimpongeze tu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu mara nyingi nimemsikia hapa ndani ya Bunge na hata tukizungumza kule nje amezungumza juu ya fidia hii ya wananchi wa maeneo haya. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba suala hili linaendelea kushughulikiwa na kwa mujibu wa taratibu na sheria wananchi watalipwa mapema sana fidia yao hii ambayo Mheshimiwa Mbunge anaitaja. Kwa hiyo, nimwondoe hofu pamoja na wananchi kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, kuhusu barabara ya Kwa Mathias – Msangani ni ahadi ya Serikali. Katika mwaka huu wa fedha 2018/2019, Mheshimiwa Mbunge anatambua tumetenga fedha kwa ajili ya kuendelea kuboresha barabara hii ili hatimaye iweze kutengenezwa katika kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatoe hofu wananchi wote wa maeneo ya Kwa Mathias na maeneo ya Msangani na maeneo yote ya Kibaha kwa ujumla tu kwamba, Serikali imeitazama barabara hii na kuangalia umuhimu wa maeneo yenyewe tutaendelea kuiboresha ili barabara hii iweze kupitika vizuri zaidi na kutoa huduma kwa vikosi vyetu ya Jeshi vlivyopo katika maeneo haya.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali dogo. Barabara ya Msangani –Kwa Mathias ni sawasawa na barabara ya Ifakara – Mlimba kwa umuhimu wake kwa uzalishaji wa mpunga. Je, ni lini barabara hii ya Ifakara – Mlimba itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha maeneo haya, kwa sababu maeneo haya ambayo Mheshimiwa Mbunge anayazungumza ni korido ambalo lina uzalishaji mkubwa wa mazao ya mahindi na mazao ya mpunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kuanzia Kidatu sasa ujenzi wa kilomita 66 unaendelea kwenda Ifakara na ili tuweze kuwa na muunganiko mzuri, hii barabara ya kutoka Ifakara kwenda Mlimba na kutoka Mlimba kwenda Madeke itaenda kuungana na wenzetu kule upande wa Njombe. Barabara hii tayari iko kwenye utaratibu, mchakato wa kuitengeneza barabara hii na kuiboresha kwa kiwango cha lami unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, huduma zitakuwa nzuri pia kwa wananchi ambao wako maeneo haya ya Mlimba tutaweza kuwaunganisha na wenzao wa upande wa Malinyi, kwa maana tutakuwa na kivuko ambacho tutakiweka ili kuboresha huduma ya mawasiliano ya huko.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika swali la msingi la Korogwe Vijijini na hali ya pale inafanana kabisa na Mbulu Vijijini. Barabara ya kutoka Sibiti-Hyadom-Mbulu kuelekea Karatu imeahidiwa kwenye Ilani. Je, ni lini sasa barabara ile itawekewa fedha hasa ukizingatia kwamba huu mwaka unaelekea kuwa wa mwisho?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Flatei kwa sababu ameifuatilia sana barabara hii lakini anafahamu pia kwamba barabara hii muhimu ziko hatua muhimu sana ambazo zinaendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na kuanza kukamilika kwa ujenzi wa daraja katika Mto Sibiti. Ziko hatua nzuri zinaendelea ili kuweza kujenga kwa kiwango cha lami sehemu ambayo ilikuwa korofi katika eneo hili. Mheshimiwa Mbunge anafahamu pia harakati za usanifu kutambua gharama za barabara hii ambayo anaizungumzia kwamba tunaendelea kukamilisha zoezi la usanifu ili tuweze kujua gharama za ujenzi wa barabara hii. Baada ya kupatikana kwa gharama za ujenzi wa barabara hii, Serikali itaendelea kutenga fedha kuweza kuiboresha.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na naishukuru Serikali kwa kazi waliyoifanya. Pamoja na majibu hayo nina maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa barabara hii kwa mara ya kwanza kabisa iliwekwa kwenye Ilani mwaka 2010 na mwaka 2015 na kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii Serikali haioni iko haja sasa ya kutenga fedha zaidi na kuongeza kasi ya utekelezaji ili tujenge barabara hii isivukwe na muda wa Ilani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wananchi wa Korogwe Vijijini wamekuwa wakisubiri utengenezaji wa barabara hii kwa hamu na kwa muda mrefu, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili kuongozana nami kwenda Korogwe akaone hali ya barabara hii na kutoa neno la matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Korogwe Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Timotheo, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Timotheo kwa sababu amekuwa anafuatilia sana mambo mbalimbali kuhusu eneo lake, nampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maswali yake, kwa ufupi nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kama ilivyo kawaida kwamba Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kufanya maboresho ya barabara katika eneo lake. Kwa hiyo, nimuahidi tu tutaendelea kutenga fedha kadri tunavyopata bajeti ili tuendelee kuboresha barabara katika eneo hili. Niliwahi kutembelea katika eneo hili lakini nakubalia nitakuja kwa sababu zipo changamoto nyingi ili nije kuona pia na maeneo mengine. Ahsante sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Nataka nipate majibu kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kahama – Nyangolongo - Bukwimba, Kalumwa - Busolwa – Busisi, ni lini ujenzi huo utaanza kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein, Mbunge wa Nyang’wale, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ziko barabara nyingi nchini ambazo ziliahidiwa na Mheshimiwa Rais na viongozi wengine wakuu. Ni kweli pia katika eneo hili la Nyang’wale kuna ahadi hii ya barabara kutoka Kahama kwenda hadi Busisi. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge labda baadaye tuonane ili angalau tuzungumze kwa upana ili apate details.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni juzi tu hapa tuliona kwamba barabara ya Dodoma-Morogoro ilipata tatizo pale Dumila na watu walipata tabu sana na kuzunguka kule Kilosa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa na barabara mbadala na kutengeneza barabara ya lami ya kutoka Dumila-Kilosa mpaka Mikumi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbilinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu upo na barabara hii iko kwenye mpango wa kuboreshwa.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze sana Serikali kwa usimamizi makini wa barabara ambao ndiyo ulibaini kwamba barabara hii ilijengwa chini kiwango na kumtaka mkandarasi airudie kwa gharama zake hata hivyo nina maswali mawili madogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, baadhi ya mitaro iliyojengwa katika barabara hii inapeleka maji kwenye majumba ya watu hasa maeneo ya Mtoni kwa Azizi Ally na Mtoni Mtongani. Je, Serikali itakuwa tayari sasa kuwapeleka wataalam kwenda kuiangalia upya mifereji hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini sasa Serikali itamalizia kipande cha kutoka Mbagala Rangi Tatu mpaka Kongowe kwa ujenzi wa barabara mbili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza pongezi alizozitoa nazipokea. Pili, kuhusu mitaro kupeleka maji majumbani, sisi kama Serikali tutashirikiana na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kuhakikisha kwamba tunayatazama vizuri maeneo ambayo yana matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuendelea na ujenzi wa barabara kutoka Mbagala Rangi Tatu kwenda Kongowe, niseme tu kwamba Serikali inayo mipango ya muda mrefu kuboresha barabara hii.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi za Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika kufanya maboresho ya barabara mbalimbali katika Jiji la Dar es Salaam jambo ambalo tunaipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi, kwa kuwa barabara ya Kilwa maeneo ya Mbagala Rangi Tatu - Kokoto kuelekea Kongowe Mwisho kumekuwa na ufinyu wa barabara na kusababisha foleni kubwa ya magari muda wa asubuhi na jioni. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza upana wa barabara na kuweka vituo vya mabasi maeneo ya Mzinga na Kongowe mwisho ili kuondoa kero kwa wananchi wanaokwenda Kongowe, Tuwangoma, Kigamboni na wale waendao Mkuranga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam Kisangi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza pongezi nyingi alizozitoa nazipokea lakini niseme tu kwamba nampongeza kwa kufuatilia barabara hii na barabara zingine katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu mwanzo kwamba tunao mpango wa kuitazama kwa upana barabara hii na mmeshuhudia tunaendelea kuweka maboresho mbalimbali ili kuweza kumudu foleni katika Jiji la Dar es Salaam, kwa hiyo, uvute subira tunalifanyia kazi.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwa nini ujenzi wa barabara ya Ifakara-Kidatu unasuasua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia naomba nifahamu ni lini yupo tayari twende wote kwenye hii barabara tukakague tuone shida?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kama ulivyoelekeza tutaongea na Mheshimiwa Mbunge ili baada ya Bunge tutembelee eneo hili.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, nashukuru pia kwa majibu ya Serikali hasa kwa kutambua kuwa hizi ni barabara muhimu za kimkakati na kwa umuhimu huo huo ilikuwa ni ahadi ya kujengwa kwa kiwango cha lami, ambayo ilitolewa na Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete na pia ilikuwa ni ahadi ya Rais wetu wa sasa Mheshimiwa Dkt. John Magufuli kuwa hizi barabara zijengwe kwa lami. Kwa umuhimu huo huo katika Ziara ya Waziri pamoja na Naibu Waziri nao kwa wakati tofauti walitembelea hizi barabara na kuona umuhimu wake na sasa labda ningependa kama ilivyo kwenye swali langu la msingi, ni lini barabara ya Mbalizi – Shigamba – Isongole itajengwa kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa umuhimu huo huo ni lini barabara ya Itewe - Mlima Nyoka - Songwe ambayo ni by pass itajengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Njeza kwa kufuatilia maendeleo ya Jimbo lake hususan mambo ya miundombinu. Maana yake hii naiona ni style ya Mpwapwa hii ni Lubeleje style, maana kila ukikutana nae anazungumzia juu ya barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niseme tu kwamba barabara hii natambua kwamba ni ahadi ya Viongozi, lakini nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Mbeya Vijijini kwamba barabara hii ya Mbalizi – Shigamba – Isongole iko kwenye mpango mkakati wa Wizara kwa ajili ya kuiboresha. Kwa hiyo pindi tukipata bajeti tutafanya usanifu wa barabara hii na kuanza kuijenga katika kiwango cha lami. Vilevile kuhusu barabara hii ya Uyole – Mlima Nyoka hadi Songwe ambayo ni by pass Mheshimiwa Mbunge anatambua kwamba usanifu ulifanyika na kupitia Jiji la Mbeya na anafahamu kwamba eneo hili ni la uzalishaji mkubwa, kuna pareto inazalishwa kwa wingi lakini kuna viazi vinazalishwa kwa wingi, kuna mazao ya mbao, hii ni barabara muhimu pia kuna mahindi yanazalishwa kwa mwaka mzima katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi leo mtaalam mwelekezi anakwenda kufanya mapitio ya barabara hii kwa sababu uko uelekeo sasa wa kupata fedha ya kuijenga barabara hii by pass muhimu ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nitaendelea kuku- update, kukupa taarifa zaidi tuone namna tunavyokwenda, lakini niseme tu kwa wananchi wa Mbeya Vijijini kwamba tumejipanga vizuri sasa kuanza kuijenga hii by pass kwa ajili ya huduma muhimu katika eneo hili.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Pamoja na majibu yaliyotolewa na Serikali, nina maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali sasa hivi ina ndege zaidi ya sita; na kwa kuwa ndege hizo zina uwezo wa kubeba abiria wengi; na kwa kuwa Mafia ni kisiwa ambacho kiko katika ramani ya Tanzania kutokana na shughuli zake za utalii, utalii wa samaki aina ya potwe ambapo kila mwaka watalii wengi wanakwenda, je, ni lini sasa Serikali itaona umuhimu wa kuongeza ukubwa wa kiwanja na kuhakikisha Shirika la Ndege la Tanzania linapeleka ndege zake kwa ajili ya abiria wanaosafiri na wanaokwenda kuangalia utalii huko wanakokwenda?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa bado hakuna utaratibu wa Serikali kupeleka ndege kubwa; na kwa kuwa wananchi wa Mafia wana adha kubwa ya usafiri wa baharini na ndege. Je, huoni sasa kuna haja ya kuongeza speed ya kupata meli au boti ambayo itasaidia na kurahisisha usafiri kwa wananchi wa Mafia?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli Mafia ni eneo muhimu na kuna vivutio vingi sana vya utalii katika eneo hili, lakini nimuhakikishie tu Mheshimiwa Vulu, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba hatua madhubuti Serikali inazichukua ili kuhakikisha kwamba tunaboresha usafiri wa Mafia ikiwemo usafiri huu wa ndege na usafiri wa vyombo vya majini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Vullu usiwe na wasiwasi kwa sababu kama nilivyosema tunakwenda kuufanya uwanja huu uwe katika kiwango cha daraja C. Lakini kikubwa ambacho kama Serikali tutafanya kwa sababu tumeendelea kuongeza kununua ndege pia tutaongeza idadi ya miruko katika kisiwa hiki. Tukiongeza idadi ya miruko katika kisiwa hiki tutaweza sasa kuweka uwiano wa abiria na huduma ambayo inahitajika Mafia kwa hiyo sisi kama Serikali tuko makini kuhakikisha kwamba tutakwenda kuhuduamia kisiwa cha Mafia kulingana na mahitaji ya wakati ili tuweze kusaidia pia kuchangia uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu wa kuwa na usafiri wa majini kama Mheshimiwa Vullu alivyosema Serikali inayo Mpango wa kutengeneza boti maalum ambayo itakuwa inatoka Nyamisati kwenda Kilindoni Mafia. Kwa hiyo, utaratibu wa manunuzi Mheshimiwa Vulu zinaendelea , kwa hiyo baada ya muda ambao siyo mrefu wananchi wa Mafia wataweza kuunganika vizuri na upande huu wa bara. Kwa maana hiyo kwamba Mheshimiwa Vulu na wananchi wa Mafia wasiwe na wasiwasi tunatambua umuhimu wa kuhudumia kisiwa cha Mafia kwa umaridadi wa hali ya juu.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, kuna ujenzi wa kiwango cha lami unaendelea kutoka Kisolya, Jimbo la Mwibara inapita Bunda Mjini na kuishia Nyamswa, Jimbo la Bunda Vijijini; na kwa kuwa, katika Jimbo la Bunda Mjini barabara hiyo imeingia kwenye makazi ya wananchi na wananchi hao wamewekewa alama ya X, maana yake wanapaswa kulipwa fidia. Je, ni lini na kwa uhakika Serikali itawalipa Wananchi hao fidia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali ya Awamu ya Nne ilitoa ahadi ya ujenzi wa kilometa nane katika Mji wa Bunda zijengwe kwa kiwango cha lami lakini mpaka leo ahadi hiyo haijatekelezwa na barabara hizo hazijaanza kujengwa. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Paresso, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, mradi wa ujenzi wa barabara ya lami unaoendelea sasa ni kati ya Bulamba na Kisolya, lakini nimfahamishe pia Mheshimiwa Mbunge kwamba, tuko kwenye hatua ya manunuzi ya kujenga barabara kutoka Bulamba kupita Bunda kwenda Nyamswa, kilometa 56 na wakati wowote mkandarasi atapatikana barabara hii itaanza kujengwa, lakini Mheshimiwa Mbunge afahamu pia kwamba, harakati za ujenzi wa barabara zitaanza pindi ambapo wananchi watalipwa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti,Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge na wananchi wawe na subira kwamba, sasa mkakati wa kujenga barabara hii kilometa 56 utaanza na hii itakuwa kwa kweli, ni neema kwa wananchi wa Bunda na Musoma kwa ujumla kwa sababu, itaungana na barabara inatoka Makutano kwenda hadi Mugumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu swali lake la pili kuhusu ahadi za kilometa nane, ahadi za viongozi wakuu; nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, sisi kama Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi tumejipanga kuhakikisha kwamba, tunatekeleza ahadi zote za viongozi. Kwa hiyo, wananchi wavute subira, kama wanavyoona sasa tunajenga barabara hii kubwa kupita katika mji wa Bunda, kwa hiyo, sina mashaka pia kilometa nane hizi zitajengwa na wananchi wataendelea kunufaika na barabara.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa ujenzi wa reli ya Mtwara ambao ulipangwa kupita kwenye baadhi ya maeneo ya Jimbo la Mtama, Kata ya Nyangao, Mtama, Kiwalala, Mnolela kuelekea Mtwara maeneo ambayo reli imepangwa kupita wananchi walizuiwa kufanya uendelezaji mpaka pale watakapofidiwa; na kwa kuwa, sasa huu ni mwaka karibu wa nne na hatuoni dalili za ujenzi wa reli hiyo, kwa nini wananchi hawa sasa wasiruhusiwe kuendeleza maeneo yao mpaka pale Serikali itakapokuwa tayari kuyachukua kwa ajili ya ujenzi wa reli na ikafanya tathmini upya na kufidia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Nape, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Nape atakubaliana nami kwamba, ujenzi wa reli hii ni kitu muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya nchi na ni muhimu kwa ajili ya wananchi wenyewe. Kwa hiyo, nataka nimwombe tu avute subira kwa sababu, tunavyotambua kwamba, kuna mradi utapita hapa, ni vema sasa kwamba, wananchi wakaona wasije wakaweka vitu ambavyo vitakuwa na gharama kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuchumi kama tutawaruhusu wafanye vitu vya maendeleo halafu baadaye tukabomoa kwa ajili ya kuweka miundombinu muhimu kama hii ya reli, tutakuwa tunabomoa ile dhana nzima ya ukuaji wa uchumi. Kwa hiyo, niwaombe tu wananchi wasiweke vitu vya thamani kubwa, reli ni kwa ajili yao, reli ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Kwa hiyo, tushirikiane tu, lakini Serikali inaendelea kusukuma jambo hili ili tuweze kupata hii reli ambayo itatupa manufaa makubwa katika nchi yetu.
MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Taarifa zinaeleza wazi na takwimu zinaonesha kwamba, takribani asilimia 45 ya bajeti ya Serikali iko upande wa miundombinu, lakini kati ya hizo asilimia 45 za bajeti nzima ya Serikali karibu asilimia 40 inakwenda kwenye maintenance. Maintenance ambayo ni matengenezo ya barabara baada ya kuwa zimekamilika na kuanza kutumia ni eneo ambalo kama Taifa tunatakiwa kuliangalia vizuri zaidi ili tuweze kuokoa fedha zinazokwenda huko kutumika kwa maintenance ziweze kutumika katika miradi mingine ya sekta mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya jamii. Nikisema bajeti ya maendeleo kwa upande wa miundombinu, nazungumza ile bajeti ambayo iko Wizara ya Miundombinu pekee, lakini miundombinu pia, iko kwenye miradi mingine kama ya umeme, maji, mifugo, kilimo, elimu, afya, kote kuna miradi ya miundombinu ambayo tafsiri yake ni…

MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa muda unakwenda.

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, sasa nataka kuuliza swali, nilikuwa najenga mazingira ya kuuliza swali. Sasa kutoka na ukweli huo wa kwamba, fedha nyingi zinakwenda kwenye maintenance. Je, Serikali inajipanga namna gani licha ya hizi njia walizozieleza kwenye swali za kimaabara, upande wa watalaam Serikali inajipangaje kuhakikisha kwamba, wataalam wanaoshiriki katika kufanya kazi hizo wakati wa matengenezo ya barabara wanazingatia misingi ya kuwa na miundombinu bora ili isije ikasababisha kuwa na gharama kubwa upande wa maintenance?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Jimbo la Tunduru Kaskazini iko miradi ambayo nasisitiza kwamba, katika mipango yake Serikali inapokwenda kutekeleza iitekeleze miradi hiyo kwa kuzingatia viwango. Miradi hiyo ni pamoja na Barabara ya Mji Mwema kupitia Ngapa kwenda Nachingwea kwa kiwango cha lami, Barabara ya Mironde kwenda Kalulu mpaka Selous kwenye Hifadhi ya Taifa kule kwa kiwango cha changarawe, Barabara ya Nandembwe – Nampungu mpaka Mbatamira kwa kiwango cha changarawe na Barabara ya Kangomba kupitia Kidodoma mpaka Machemba na kule Chiwana kwa kiwango cha changarawe na pia mwisho kabisa Daraja la Fundi Mbanga. Je, Serikali itatekeleza lini mipango hii ya kutengeneza miradi hii kwa viwango?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Makani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba uniruhusu nitoe shukrani sana kwa Mheshimiwa Rais wetu kwa kuendelea kusukuma tuweze kupata fedha nyingi kwa ajili ya kuendeleza hii miundombinu muhimu. Pia nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa sababu mara nyingi tumezungumza na ushauri wake tunaendelea kuuchukua, lakini nilishukuru Bunge kwa sababu limeendelea kututengea fedha za kutosha. Katika mwaka tu wa Fedha huu ambao tunaendelea nao Wizara yetu imetengewa trilioni 4.2, sasa hii ni fedha nyingi sana kuonesha concern ya Bunge nalo lipo pamoja na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kujibu swali lake la kwanza niseme kwamba, yako mambo mengi kama Serikali kupitia Wizara hii ya Ujenzi tunafanya ili kuhakikisha kwamba, tunafanya kazi vizuri na kuboresha miundombinu. Kama unavyoshuhudia Mheshimiwa Makani sheria zimekuwa zikifanyiwa mabadiliko mbalimbali, kumekuwa na miongozo mingi inatolewa, lakini ziko programu nyingi sana ambazo hapa siwezi kuzitaja kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, kazi inafanyika kwa weledi. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, kupitia Bodi ya Wahandisi (ERB) tunaendelea kusimamia maadili ya wataalam wetu, tunaendelea kukuza namba ya wataalam katika nchi hii ili kuweza kusimamia miradi hii. Pia tutaendelea kuchukua hatua kwa wataalam hawa ambao watakwenda kinyume na utaratibu ambao tunautaka, lengo tu ni kuhakikisha kwamba, utaalam unatumika vizuri na miundombinu yetu inajengwa vizuri, lakini pia, tunaisimamia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwango vya ujenzi wa barabara, amezungumza barabara hizi alizozitaja Mheshimiwa Mbunge. Natambua kwamba, barabara hizi karibu zote ziko kwenye upande wa TAMISEMI, lakini sisi kama Serikali, tunashirikiana na TAMISEMI kuhakikisha kwamba, barabara hizi zinaenda kuwahudumia wananchi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge usiwe na wasiwasi, natambua kwamba, liko Daraja hili la Fundi Mbangai, hili daraja tayari upande wa Serikali za Mitaa kwa maana ya kupitia Halmashauri ya kwake waliomba utaalam kutoka kwenye Serikali na daraja hili limetengenezwa, isipokuwa zile approach road ndio zinahitajika kufanyiwa matengenezo. Naamini kutokana na concern ya Halmashauri yake hizi barabara zitatengenezwa, lakini Barabara hii ya Mji Mwema – Ngapa kwenda Nachingwea itaenda kutuunga na Mkoa wa Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Ruvuma, upande huu wa Tunduru, hii Barabara kutoka Mji Mwema kwenda Ngapa tumeshaichukua na eneo la Ngapa pale tutahitaji kujenga daraja. Kwa hiyo, wananchi wa Tunduru wawe na imani kwamba, tutakwenda kujenga daraja hili ambalo litatuunga na Mkoa wa Lindi. Ahsante.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali ya chama changu kwa kuunganisha jimbo letu na miradi barabara ya lami. Tumeunganishwa na Arusha Dodoma na Singida lakini tuna kilomita 10 za lami ambazo zinaendelea na taa za barabarani zinawekwa. Kwa hiyo, nashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, huu mchakato wa kumpata Mhandishi Mshauri umechukua zaidi ya miaka mine. Naomba nifahamu Wizara yako ipo tayari kuwasiliana na African Development Bank ili huu mchakato ufike mwisho na wale wananchi wapate fidia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa hizi barabara za lami zilivyopita mita 7.5 ziliongezeka tangu 2007 kwa mujibu wa Sheria ya Barabara lakini wananchi hao hawajafidiwa na wameshindwa kujenga nyumba zao. Naomba nifahamu kwa nini Serikali isipitie kanuni hii ya fidia muone wananchi hawa ambao wapo kwenye road reserve walipwe at least wale ambao wamejenga nyumba zao kwa sababu sasa wanashindwa hata kuzikarabati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gekul, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda uniruhusu nitumie muda mfupi huu nimkaribishe sana Mheshimiwa Gekul upande huu. Nimpongeze sana kwa sababu anapigania kweli maendeleo ya Mji wa Babati. Nami namuahidi kwamba tutaendelea kushirikiana kama tunavyoshirikiana na Waheshimiwa Wabunge wote ili kuhakikisha kwamba maendeleo yanawafikia wananchi wetu kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza ametoa ushauri, kwa hiyo, nikubali kuwa ushauri wake tutauchukua na tutaufanyia kazi. Kikubwa ni kwamba tunaendelea kushirikiana na wafadhili kwa sababu wamekuwa na imani na Serikali yetu na nimuahidi kwamba AfDB tutaendelea kuwasiliana nao ili kuhakikisha kwamba yale yote yanayohitajika kuweza kutekeleza mradi huu tunaweza kutekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu fidia ya wananchi ambao walipisha eneo la mradi, nakubaliana naye kwamba tutaendelea kulitazama. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo yote tunaendelea kulipa kwa kasi na maeneo yote ambayo miradi inapita tutaendelea kufanya malipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme kwamba jambo hili nimelichukuwa, nitaendelea kuzungumza na wenzetu ili tuweze kuhakikisha kwamba wale wanaostahili fidia wanalipwa kulingana na taratibu ambazo zipo. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Babati kwamba tutaliangalia suala lao kwamba wamepisha eneo la mradi na wanastahili kulipwa kama sheria inavyotaka.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itaandaa jedwali la kuonyesha miradi mikubwa ya barabara zinazounganisha miji mikuu ya mikoa ili kuonyesha hali ilivyo na hivyo kuweza kuwaanika wakandarasi wanaochelewesha kazi hiyo kwa makusudi na kuwapa wananchi dhiki mfano barabara ya Nyakanazi – Kabingo - Kidahwe - Kasulu ambazo kwa muda mrefu hazikamiliki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko miradi mingi sana ya ujenzi wa barabara inatekelezwa kote nchini. Nawaona Waheshimiwa wa Kigoma wanatabasamu kwa sababu wanafahamu fika kwamba miradi hii ambayo ilikuwa inatekelezwa katika Mkoa wa Kigoma ukianzia Nyakanazi – Kibondo - Kidahwe – Kasulu inaendelea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie wananchi wa Kigoma kwa ujumla kwamba ipo miradi mingi sana ambayo kwa hapa siwezi kuitaja inaendelea vizuri. Mheshimiwa Nsanzugwanko na Mheshimiwa Zitto wanafahamu kwamba sasa appetite ya matengenezo ya barabara kwenye Mkoa wa Kigoma ipo juu sana na barabara karibu zote zina fedha kwa ajili ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Asha asiwe na wasiwasi. Hata eneo hili lililokuwa linasuasua kutoka Nyakanazi - Kakonko tumeendelea kulisimamia. Mimi mwenyewe nimekwenda mara kadhaa na tumezungumza na mkandarasi na zile changamoto zilizokuwa zinamkabili kama Serikali tumezitatua. Tunaendelea kusukuma na nitahakikisha barabara hii inakamilika ili wananchi wa Kigoma nao wapate faraja ya kuwa na miundombinu kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya mkoa wao.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba kiwanja hicho kilijengwa kabla ya uhuru; na kwa kuwa kiwanja hicho kilijengwa kabla ya makazi ya watu hayajasogea maeneo yale na sasa hivi maeneo yale yamejaa makazi ya watu; na kwa kuwa Liganga na Mchuchuma ndiyo mradi ambao unakaribia sasa kuingia katika Mji wetu wa Njombe. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kukihamisha kiwanja hicho na kupeleka sehemu za Tanwati au Mgodeti, ama Ilembula? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS JOHN KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mlowe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Serikali tunatambua umuhimu wa kujenga kiwanja hiki. Pia nafahamu Njombe ina fursa nyingi za kiuchumi, mojawapo Mheshimiwa Mbunge ametaja, tunafahamu pia uhitaji wa huduma hii ya usafiri, hususan wa ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu, suala la ujenzi wa uwanja huu pia mimi mwenyewe nimetembea Njombe, nimefanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa, lakini mara nyingi nimefanya mazungumzo na Mbunge wa Jimbo Mheshimiwa Mwalongo. Kwa hiyo, tulijaribu kuona namna bora ya kuweza kuendeleza uwanja huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mahitaji ya kuendeleza uwanja huu bado yapo, kwa sababu kwenye taarifa ile ya usanifu kama ingeonesha kutokuwa na mahitaji ya kuendeleza kiwanja hiki katika eneo hili, basi ningeshauri namna tofauti. Hata hivyo, jambo hili kama wana Njombe mtaona kwa kushirikiana na Uongozi wa Mkoa mnaweza, mkalizungumze mlilete.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakutahadharisha tu kwamba kwa sababu kulikuwa kuna hatua ambayo imefikiwa na kuna gharama ambazo kama Serikali tumetumia kwamba kuhamisha uwanja huu kupeleka maeneo mengine kunaweza kupoteza fursa ambayo ilikuwa iko tayari imeshapatika kwa sababu inaweza ikatahitaji muda mrefu kufanya usanifu mpya na wananchi hawa wanahitaji huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri tu kwamba uwanja huu tuujenge na kama mtahitaji kuwa uwanja mkubwa, mzungumze katika level ya Mkoa halafu ushauri wenu muulete, sisi kama Serikali tutauzingatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi nami niulize swali moja dogo la nyongeza. Dodoma sasa ni Makao Makuu ya nchi, kiwanja cha ndege kilichopo hakikidhi haja ya kutua kwa ndege kubwa. Je, ule mkakati wa Serikali kukamilisha uwanja wa ndege wa Msalato umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS JOHN KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nkamia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme tu kwamba ni kweli Serikali imefanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi na niseme tu kwamba uhimu wa kuwa na kiwanja kikubwa cha Kimataifa upo. Hatua ambazo zimefikia Mheshimiwa Nkamia anafahamu, liko eneo la kutosha kabisa kuweza kujenga huo uwanja.

Mheshimiwa Naibu Spika, anafahamu na kwa kauli ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa kwamba ule ufadhili kwa ajili ya kujenga uwanja huu kulikuwa kuna hatua nzuri kwamba tutapata fedha za kutosha kujenga uwanja huu. Ili huduma iweze kuanza, Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo kwamba badala ya kuanza na kujenga majengo makubwa ili huduma ianze, tutaanza kutengeneza runway ili ndege zianze kushuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Nkamia juhudi za kuujenga uwanja huo ziko katika kasi ambayo siyo ya kawaida. Kwa hiyo, nimtoe hofu yeye na Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote ambao wanakuja kupata huduma katika Makao Makuu kwamba tumejipanga vizuri kuweza kujenga huu uwanja. Kwa hiyo asiwe na wasiwasi. Avute subira, muda siyo mrefu ataona mambo yanavyoendelea. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Changamoto iliyopo Njombe inafanana kabisa na changamoto iliyopo uwanja wa ndege wa Bukoba kwamba ni mfupi na kupelekea ndege kutua kwa shida au kuruka kwa shida mfano kama Bombadier. Je, ni lini Serikali itaongeza urefu wa uwanja huo?
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS JOHN KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, nianzie uwanja wa ndege wa Bukoba, yako maboresho muhimu yamefanyika na huduma inaendelea vizuri na ndege zinashuka vizuri na miruko imeongezeka. Pia ule mpango wa kuuboresha uwanja huu tunaendelea na hatua ya kutathmini maeneo ambayo tutahamisha wananchi, Mheshimiwa Mbunge anafahamu ili sasa ule urefu wa sehemu ya kurukia na kutoa ndege iweze kuongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba zile hatua za kufanya maboresho ya viwanja mbalimbali nchini ziko kwenye mpango na Waheshimiwa Wabunge wanafahamu, mara kadhaa tumezungumza namna ya viwanja, hata leo nimerejea kuzungumza viwanja vingi ambavyo tunaendelea kujenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutaendelea kuimarisha ili kuhakikisha kwamba tuna viwanja wa ndege ambavyo vitamudu kutoa huduma katika maeneo ya Mikoa yote. Tutaendelea kutoa maeneo mengine ambayo ni maalumu kama ilivyoonekana kwamba uwanja wa ndege wa Mafia, kama nilivyozungumza jana, tunaupeleka katika hatua uwe na hadhi ya kimkoa ili huduma ziongezeke.

Mheshimiwa Naibu Spika, viko viwanja vingine ambavyo tunaendelea kuvipanua. Kwa mfano, tunaendela kupanua uwanja wa ndege wa Kigoma, Tabora, Shinyanga na Bariadi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge waamini tumejipanga kuhakikisha kwamba pamoja na Serikali kuendelea kuliboresha shirika letu kwa kununua ndege, italeta maana pale ambapo Serikali inanunua ndege na ndege zinaenda kuwahudumia Watanzania kwa ujumla. (Makofi)
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake yenye matumaini kwa sababu barabara ya kutoka majimoto Inyonga zabuni imeshatangazwa. Swali langu ni kwamba kwa kuwa barabara hii iko chini ya TANROADS na TANROADS wamesema kwamba wanatangaza zabuni ya kumpata mpembuzi na msanifu ili waweze kuianza barabara hiyo na kwa kuwa zoezi la kutangaza zabuni na mpaka kumpata mkandarasi ni la muda mrefu. Je, ni lini sasa katika maombi yangu maalum ya kilomita 2.0 katika Mji wa Usevya yatapatiwa majibu na barabara hiyo ianze kutengenezwa kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa mkandarasi alipatikana ambaye ameweza kujenga kilomita
1.7 katika Mji wa Inyonga, lakini katika mwaka wa fedha 2018/2019 mkandarasi wa kujenga kilomita 2.5 amepatikana na yupo katika eneo la mradi. Je, ni eneo gani la mradi ambapo mkandarasi huyo yupo?
NAIBU WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nazipokea shukurani alizozitoa, nazipokea kwa dhati, lakini pia kwa furaha nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi ya usanifu kama nilivyojibu katika jibu la msingi tarehe 11 ambayo ni Jumatatu ijayo zabuni itafunguliwa na hii hakuna namna kwa sababu, harakati za ujenzi zinazingatia pia Kanuni na Sheria za Manunuzi. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge tupo kwenye hatua nzuri, mzabuni atakapokuwa amepatikana na sisi tutasimamia kwa umahiri ili hii kazi hii iweze kukamilika kwa wakati. Kwa hiyo, nimtoe hofu pamoja na wananchi wa Kavuu kwa ujumla kwamba sasa ujenzi wa barabara hii utakuwa umeanza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu eneo la kilomita 2.0; eneo hili ni mwendelezo katika Mji wa Inyonga, lakini Mheshimiwa Mbunge nafahamu kwamba iko haja ya kuweka msukumo wa kujenga kipande cha barabara kutoka Kibaoni kuja kwenye Mji wa Usevya ambao ni Makao Makuu ya Halmashauri. Kwa hiyo nimtoe hofu tu kwamba, usanifu utakapokamilika na sisi tutaweka kipaumbele ili wananchi hawa wanaokwenda makao makuu waweze kuunganika vizuri na barabara ambayo sasa ukitoka Kizi kuja Kibaoni, hatimaye tuunganishe kipande hiki cha kuja Makao Makuu ya Wilaya, lakini pia sehemu ya Majimoto ambayo ina wafanyabiashara wengi na kuna sehemu kubwa ya uchumi. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi, tutazingatia haya maeneo ambayo ni muhimu kuhakikisha wananchi wanaunganishwa vizuri.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Mwaka 2015, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli aliwaahidi wananchi wa Makamboko kulipa fidia kwa ajili ya eneo hili linalojengwa Kituo cha One Stop Centre yalikuwa maeneo mawili, tunaishukuru Serikali imelipa fidia kwa ajili ya kujenga soko la kimataifa na sasa bado hili la Idofi ambalo linajengwa kituo hiki. Nashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alipotoka Njombe alifika eneo la Makambako na tukampeleka pale Idofi ambapo alikutana na wananchi na Mheshimiwa Diwani mhusika na wananchi wana imani kubwa na Serikali juu ya kulipa fidia zao. Je, ni lini sasa Serikali itawalipa fidia wananchi wa Idofi ili waweze kuendelea na shughuli mahali pengine watakapohamia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa mwaka huu wa fedha wa 2019/2020, hivi sasa tutaanza kuandaa bajeti, naiomba Serikali, ni kwa nini kwenye bajeti hii ya 2019/2020 usiingizwe mpango huu ambao umeingizwa hapa? Nakushukuru.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Deo Sanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais aliahidi, lakini aliahidi kujenga mradi wa Kituo cha Ukaguzi wa Pamoja sasa katika ujenzi wa kituo hicho kuna process kama ambavyo jibu la msingi limesema; kuna usanifu wa awali usanifu wa kina na hatuwezi kujenga mradi bila kulipa fidia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Deo pamoja na wananchi wa Jimbo lake Makambako ni kwamba mradi ni ujenzi wa kituo cha pamoja lakini katika mradi ndio kuna hizo hatua zingine, kwa hiyo nimhakikishie kwamba…

MWENYEKITI: Waheshimiwa tunaomba utulivu ndani ya Bunge.

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Kwa hiyo nimwahidi Mbunge na wananchi wa Makambako kwamba mradi utatekelezwa hatua zote pamoja na ulipaji wa fidia utafanyika.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza, niwashukuru sana Wizara ya Ujenzi kwa kunipa fedha za kutengeneza barabara ya Mugeta Siloli Simba. Na kwa kuwa ile barabara ilikuwa na km 21 na zimetengenezwa kilomita fulani na zimebaki kilomita tisa. Naomba kujua kutoka kwa Waziri ni lini sasa watapeleka fedha ili kumalizia kilomita tisa zilizobaki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Getere kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumefanya ujenzi wa kuboresha sehemu ya barabara ya Mugeta kwenda Siloli Simba, lakini Mheshimiwa Mbunge atakubaliana name kwamba sehemu ya kilomita 11 iliyojengwa, barabara haikuwepo kabisa, lakini kile kiwango cha barabara kimewavutia Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa eneo hili ili sehemu ambayo ilikuwa na barabara awali na yenyewe ifanyiwe maboresho. Kadri tunavyopata fedha kilomita hizi chache zilizobaki tunafanya maboresho.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Madai ya wananchi ya kudai fidia kutokana na miradi ya ujenzi nchini yapo kila siku, ni mengi na ni makubwa. Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wanawalipa wananchi hawa kwa uhakika na kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Paresso kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu tumeendelea kufanya malipo ya fidia miradi inapotekeleza nchi kote katika maeneo mbalimbali. Pia niseme tu shughuli za miundombinu zinaendelea, kwa hiyo tutaendelea kuwalipa wananchi fidia na kadri miradi itakavyoendelea tutaendelea kufanya malipo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge tusiwe na wasiwasi tumejipanga vizuri, kwa mwaka wa fedha mmetupitishia fedha zakufanya usanifu kilomita 3,856. Sasa tuone kwamba hitaji la kufanya maboresho ya miundombinu litaendelea na kulipa fidia kwa wananchi tutaendelea kulipa kulingana na sheria na taratibu.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa Majibu mazuri. Pamoja na majibu yake, lakini naomba niulize swali la nyongeza. Katika kutekeleza mradi wa barabara kwa kiwango cha lami barabara ya Namtumbo - Tunduru – Tunduru – Mjini Nakapanya wananchi wale wamekuwa wakusubiri kulipwa fidia zao kwa muda mrefu. Je, Serikali ina mkakati gani katika kuhakikisha wanalipwa na kuwaondolea adha hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chikambo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, mradi huu ulikopita wananchi walipwa fidia isipokuwa natambua tumezungumza na Mheshimiwa Chikambo, wapo wananchi wachache sana ambao walikuwa wana malalamiko yao, suala hili tunaendelea kulifuatialia, tukitatua tutawalipa hawa wachache kulingana na stahili zao.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi shapu wa Jimbo la Kishapu, naomba nitoe pongezi kwa Wizara kwa kazi nzuri manayoifanya, lakini nina swali la nyongeza kwakuwa bararaba ya Kolandoto kwenda Kishapu ni muhimu kwa kuwekwa lami kwa sababu za kiuchumi na mambo mengine. Je ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hiyo ya lami kutoka angalau Kolandoto kwenda Kishapu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nchambi, Mbunge shapu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba eneo hili kutoka Kolandoto kwenda Mwangongo na bararaba hii inaenda kuunganisha kupita Sibiti na maeneo ya mikoa mingine. Kwa hiyo, tutakapopata fedha tutaanza kujenga barabara hii muhimu.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, ni lini sasa watamalizia barabara ya Kimanga ambayo inajengwa sasa kwa muda wa miaka miwili, mpaka sasa imeleta usumbufu mkubwa katika Kata ya Kimanga na mpaka sasa haijamalizika imesimama na mkandarasi hayupo, ni lini Serikali itamalizia hiyo barabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kaluwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba, baada ya Bunge hili nitatembelea mradi huu niangalie pamoja na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kuona changamoto zilizopo ili tujue hatua za kuchukua kwa haraka ili barabara iweze kuboreshwa.

MWENYEKITI: Kwa hiyo unakwenda jimboni kwake?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la mradi.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya barabara ambayo nimeizungumza sana na Mheshimiwa Waziri pamoja na TAMISEMI wanajua, ni Barabara ya Chuo cha Ardhi – Makongo - Goba. Imekwama kutengenezwa kwa sababu ya fidia, sasa nataka Waziri aniambie, ni lini kipande hicho kitalipwa fidia ili wananchi wa Makongo waweze kujengewa barabara ya lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali na nyongeza la Mheshimiwa Halima Mdee kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa sana imefanyika kuboresha miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam na Mheshimiwa Mbunge anafahamu. Changamoto ambazo zimebaki ni kulipa fidia kwa hizi kilometa nne zilizobaki. Barabara hii ni muhimu kwa sababu tunavyojenga barabara ya juu pale Ubungo, barabara hii itatumika pia kupunguza msongamano ili kufanya ujenzi uende kwa haraka. Tunatambua umuhimu huo, kwa hiyo nimwombe tu Mheshimiwa Mdee avute subira, suala hili tunalifuatilia kwa umakini kuhakikisha kwamba kipande hiki kinatengenezwa.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Eneo hilo la kilometa 86 ni eneo korofi na liko katikati ya mbuga ya wanyama, wakati mwingine kama gari zinasafiri inafika gari inakwama katikati ya mbuga, jambo ambalo ni hatari kwa raia ambao watakuwa wamepanda basi hilo. Je, Serikali ituambie imetilia umuhimu gani kuliko kusema kwamba itakapopata fedha kwa sababu jambo hili ni muhimu mno kuliko, naomba majibu ya Serikali katika suala hilo, ni lini?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, nashukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja la Mto Momba ambalo linaunganisha mikoa mitatu. Nataka kuuliza baada ya ujenzi wa daraja hilo ni lini sasa Serikali itatenga pesa kwa ajili ya upembuzi yakinifu, kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, barabara inayounganisha mikoa mitatu, Mkoa wa Songwe, Rukwa na Katavi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Malocha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii ambayo nimetoka kujibu swali lake kwa sababu utagundua kwamba asilimia 65 ya barabara hii baada ya usanifu tulifanya ujenzi na ujenzi ulizingatia maeneo korofi zaidi. Nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba sehemu hii iliyobaki bado ina maeneo changamoto wakati fulani. Sisi kama Serikali tumeendelea kutenga fedha ili kushungulikia maeneo haya korofi. Hata katika mwaka huu wa fedha unaoendelea tumekuwa na fedha za kutosha kuhakikisha maeneo korofi wakati wowote tunayapa umuhimu wa kuyafanyia matengenezo.

Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa eneo hili watakuwa mashuhuda wa kuona kwamba wakati wote tunahakikisha kwamba barabara hii inapitika wakati tunajiandaa kwa ajili ya kuitengeneza katika kiwango cha lami. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira kwa vile sehemu kubwa ya barabara tumeitengeneza hii sehemu ndogo iliyobaki tutakwenda kuitengeneza kwa kiwango cha lami. Tumeweka mapendekezo katika bajeti hii inayokuja kama Bunge lako litatupitishia na Serikali ikapata fedha tutakwenda na hatua ya mwisho kuikamilisha barabara hii.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu barabara hii inayopita katika Daraja la Mto Momba, Mheshimiwa Mbunge anafahamu na nimetembelea eneo hili, ujenzi wa daraja umekamilika kwa sehemu kubwa na sasa tunaweza kupita mto huu. Mheshimiwa Mbunge anafahamu barabara hii ni ndefu sana ukitoka Momba mpaka uje Majimoto na mimi nimeliipita. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeiweka kwenye mpango wetu mkakati kwa maana ya sasa kufanya usanifu baada ya kukamilisha sehemu ya Mto Momba ambayo ni korofi ili sasa tuweze kuitazama kwa ajili ya kuitengeneza katika kiwango cha lami. Kwa hiyo, tuvute subira Serikali ikipata fedha tutakamilisha barabara hii.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nimepokea majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa upembuzi yakinifu umeshafanyika kuanzia Ifakara mpaka Kihansi; na kwa kuwa barabara hiyo hakuna kabisa sehemu ambayo unaweza ukapata changarawe kwa sababu upande wa kulia ni bonde oevu na upande wa kushoto ni Udzungwa. Je, Waziri husika yupo tayari kuongea na Waziri mwenzake wa Maliasili ili wakandarasi hao wanaotengeneza hiyo barabara ingawaje kwa kiwango cha changarawe waweze kupata kifusi au moramu katika eneo ambalo watalitenga kwenye eneo la Udzungwa? Nasema hivyo kwa sababu ni udongo tupu na hii barabara inabomoka kwa muda mfupi sana na wananchi wanapata tabu.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa pale Mlimba Mjini, TARURA kwa bajeti zao wanasema wataweka angalau kilometa 1 kiwango cha lami lakini kuna mita 500 za TANROADS zinazopita kwenda pale mjini. Je, TANROADS sasa wako tayari kwenye ile barabara yao pale Mlimba Mjini hizo mita 500 kuunganisha na ile lami ya Kihansi, Mlimba Mjini ili TARURA wanapofanya kazi yao kusiwepo na kipande kingine cha vumbi pale Mlimba Mjini, kwenye mji wa Mlimba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Susan Kiwanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu tulipata nafasi ya kutembelea barabara hii na changamoto ya kupata changarawe ili kuifanya barabara iwe bora zaidi tuliizungumza na tulikuwa tumefanya mazungumzo na wenzetu upande wa Maliasili. Hata hivyo, kwa vile amelisema tena hapa nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafanya mazungumzo ili tuweze kupata kibali cha kifusi ambacho kitafanya barabara hii matengenezo yake yawe imara.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili la kipande cha mita 500, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nalichukua ili niweze kulielekeza upande wa wenzetu wa TANROADS, Mkoa wa Morogoro ili kilometa 1 itakayotengenezwa na TARURA iwe na muunganiko mzuri na hizi mita 500, hii nimelichukuwa.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na maelezo mazuri sana ya Serikali, barabara hii imekuwa na maelezo ya muda mrefu kwa maana ya kwamba kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Rais wa Awamu ya Tano kwamba barabara hiyo itatengenezwa kwa kiwango cha lami. Kwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri anasema kwamba usanifu wa kina utakamilika Mei, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Mwanza. Usanifu wa kina umeshakamilika na baada ya usanifu wa kina kukamilika nilienda kwa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, ofisini kwake, akaniahidi kwamba ataiingiza kwenye bajeti ya mwaka huu kwa maana ya 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka kuuliza, kwa maelezo haya, Barabara ya Isandula – Hungumalwa itaingizwa kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha 2019/2020?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kama ahadi inatolewa na Mheshimiwa Rais na Serikali imekiri kwamba barabara hii ni muhimu na ni kiungo kikubwa kwa Sirari, Mwanza na Shinyanga: Je, Serikali sasa kwa umuhimu huo, iko tayari barabara hii ambayo ni muhimu kuiingiza kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza unipe ruhusa nimpongeze sana Mheshimiwa Richard Ndassa, Senator huyu, amekuwa akiifuatilia sana barabara hii na ni kweli barabara hii imeahidiwa muda mrefu na ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge amekuwa akiifuatilia sana barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa umuhimu huo, tumesimamia vizuri kuhakikisha kwamba usanifu unakamilika. Tulipokea rasimu ya kwanza ya usanifu wa barabara hii ambayo angalau ime-indicate kwamba barabara hii inaweza ikawa na gharama gani. Kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa Ndassa avute subira na kwa sababu jambo hili tumelishika na tumedhamiria kujenga barabara hii na sisi tunaitazama barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili amezungumza juu ya bajeti, niseme tu kwamba asiwahishe shughuli, tunaitazama vizuri barabara hii, na Mungu akijaalia tunaweza tukaja na mapendekezo ya kuijenga barabara hii. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Ndassa pamoja na wananchi wa Isandula, Bukwimba, Nyambiti, Ngudu, Nyamilama, Hungumalwa (Magu), Sumve na Ngudu kwa ujumla kwamba tunaona umuhimu wa kuijenga barabara hii. Tukipata fedha na bajeti ikiruhusu tutaijenga barabara hii kwa kiwango cha lami.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mara kuna tatizo kubwa sana la barabara hasa barabara ya Wanyele – Kitario. Barabara hii imekatika, hakuna mawasiliano. Barabara ile inahitaji kujengewa daraja na barabara hiyo pia ilishaua watoto zaidi ya 20:-

Je, ni lini Serikali itaweka mkakati wa kipaumbele kuhakikisha inajenga daraja na tukichukulia kwamba kipindi cha masika kinakaribia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inao utaratibu wa kutenga fedha kushughulikia maeneo korofi kama hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge anayataja. Namwomba tu Mheshimiwa Mbunge, labda tuwasiliane baadaye kwa sababu ni eneo limekuwa mahsusi na kwa wakati huu tuone kama lipo tatizo kwa kupitia utaratibu ambao tupo nao wa kushughulikia maeneo korofi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya barabara wakati wote, tuweze kushughulikia eneo hili. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ili niipate sawasawa tuweze kushughulikia eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. OLIVER D. SEMGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, wananchi wamesubiria fidia kwa muda mrefu sana na kabla ya ujenzi wa lami, fidia huwa inatangulia. Sasa Serikali inawaambiaje wananchi wangu wanaoishi kwenye hii barabara kuanzia Nyakahanga, Nyaishozi, Nyakasindi hadi Benako Ngara?

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Bugene kupitia Nkwenda – Kaisho - Mlongo ni barabara muhimu sana kwa wananchi wa Karagwe, Kyerwa na Misenyi. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii muhimu kwa uchumi wa Wilaya hizi na Taifa kwa ujumla.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) : Mheshimiwa Naibu Spika, ni utaratibu wa Serikali kulipa fidia kwanza kabla ya kuanza ujenzi. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wa maeneo haya ambapo mradi utapita watalipwa fidia zao kabla ujenzi haujaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia mambo mbalimbali ya maendeleo katika eneo lake lakini pia niwapongeze wananchi kwa kupisha mradi; kwa maana hiyo kwamba kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa ajili ya maendeleo yetu kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, amezungumza juu ya barabara hii ambayo inakwenda Mrushaka – Mlongo kilometa 125. Mimi nimetembelea eneo hili, ni eneo muhimu sana sasa kuunganishwa kwa sababu ni sera ya Serikali kuunganisha nchi yetu na nchi za jirani. Barabara hii Mheshimiwa Mbunge anaitaja inatuunganisha sisi Tanzania na Uganda. Kwa hiyo, tunayo mipango ya kuijenga kwa kiwango cha lami lakini namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, asiwahishe shughuli na ikiwezekana tunaweza kuteta ili ajue mpango wa Serikali juu ya kuijenga barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tunaendelea kuihudumia hii barabara na maeneo ambayo ni korofi. Kwa mfano, ile milima, maeneo ya Rwabunuka kuna mipangilio ya milima ambayo ni mikali sana. Tumetenga fedha kwa ajili ya kuanza kushughulikia maeneo korofi wakati tunajiandaa kuiboresha hii barabara katika kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa maeneo haya wavute subira, tumejipanga vizuri na tunafahamu maeneo haya ni muhimu sana kwa uchumi. Tutashughulikia barabara hii muhimu.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu linahusu barabara ya Kidatu – Ifakara; barabara yenye urefu wa kilometa 69.9. Mradi wake wenye thamani ya shilingi bilioni 109 ambao unafadhiliwa na DFID na European Union.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ilifunguliwa tarehe 5 Mei, 2018. Wakati inafunguliwa vifaa viliwekwa vingi na Mheshimiwa Rais lakini Mheshimiwa Rais alipoondoka na Mkandarasi akaondoa vifaa vyake. (Kicheko)

Je, Serikali inatuambia nini kuhusu barabara hii? Ina maana ndiyo tumepigwa changa la macho sisi pamoja na Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) : Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mlinga kwa sababu mara zote amekuwa ukifuatilia sana ujenzi wa barabara hii. Niseme tu kwamba tunawaambia nini wananchi na Watanzania kwa ujumla kuhusu barabara hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tulivyoanza ujenzi wa barabara hii kulikuwa na changamoto kuhusu vifaa na material kwenye ujenzi wa barabara hii. Hii ilitokana na mabadiliko ya Sheria ya VAT, kwa hiyo, tulichelewa kidogo. Niwaambie wananchi na Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya changamoto hizi kutatuliwa, sasa Mkandarasi atakwenda kwa kasi kubwa na wananchi wategemee kupata barabara ya lami, bora na itakayowahudumia wananchi wa maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ambapo imekiri uwepo wa matuta hayo ambayo siyo rafiki barabarani na wameanza kuchukua jitihada, nilitaka kujua ni lini sasa Serikali itakuwa imemaliza kuyapitia na kuyarekebisha matuta yaliyopo kwenye barabara ya Msata – Bagamoyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; hivi karibuni Jeshi la Polisi kwa kupitia Kitengo chake cha Usalama Barabarani, wamekuwa wakifanya kazi nzuri ya kuwadhibiti madereva wakorofi. Je, pamoja na kazi nzuri hii ya Jeshi la Polisi bado tunaona kuna tija ya kuendelea kuweka matuta kwenye barabara kuu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, tunaendelea kuyatoa matuta yote ambayo yameonekana kwamba hayafai kulingana na mwongozo ambao tumeutoa. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mtolea kwamba muda siyo mrefu tutakamilisha kazi hii kwa sababu mpaka hivi ninavyoongea, tuko karibu asilimia 90 ya matuta yote ambayo tuliyatambua kwamba ni hatarishi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge uvute subira kwa sababu kuyatoa matuta haya pia ni gharama; tutaendelea kuyatoa matuta yote sehemu hiyo uliyosema kutoka Msata kwenda Bagamoyo na maeneo mengine nchini. Kwa hiyo, vuta subira kasi yetu ni nzuri, tutayatoa matuta yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mtolea kwa kutambua na kuona udhibiti wa madereva tunaoufanya Serikali kupitia Mambo ya Ndani na sisi upande wa ujenzi. Mimi kama Makamu wa Mwenyekiti wa Baraza la Usalama Barabarani, tunahakikisha kwamba kwanza wananchi wanabaki salama, watumiaji wengine wa barabara wanabaki salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa tutaendelea kufanya udhibiti ili kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa salama kwanza, halafu tuendelee na hatua nyingine. Kwa hiyo, ni muhimu sana kuhakikisha watu wetu wanakuwa salama. Kwa hiyo, tutaendela kudhibiti na kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa salama.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Maswali yangu mawili ya nyongeza.

(a) Pamoja na wataalam kuangalia athari ya fidia lakini wataalam hawa kwa nini hawakuangalia upande wa pili wa Mkoa wa Kagera? Uwanja wa Mkoa wa Kagera unaweza ukapakia Airbus kutoka Bukoba, ikajaa bila kwenda popote, kwa sababu watu wa Uganda, Burundi, Congo, wote wanapandia pale.

Je, upanuzi huu kwenda Daraja C mnategemea ufanyike lini? Naomba wataalam waangalie faida wasiangalie hasara peke yake.

(b) Kwa sababu kuna uwanja wa ambao ulikuwepo miaka yote, awamu zote kuanzia Mwalimu Nyerere zaidi ya miaka 41, Omukajunguti, leo hii Bukoba haiwezi kupanuliwa, kwa nini uwanja huu usiendelee kubaki ndani ya mamlaka ya viwanja vya ndege ili miaka ijayo mkitaka kupanua labda pesa zipo tusihangaike kutafuta mahali pa kwenda?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia maendeleo siyo ya Bukoba peke yake, lakini ya nchi nzima. Nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumeliona hilo kwamba Uwanja wa Ndege wa Bukoba ni muhimu sana. Ndiyo maana katika mipango yetu na wakati mwingine Mheshimiwa Mbunge avute subira, ataona namna tulivyojipanga, kama nilivyosema kuuboresha uwanja huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejipanga ili uwanja huu tuweze kuuwekea pia VIP Lounge, tumejipanga pia kwa ajili ya kufanya maboresho kama nilivyosema ili tuweze kutoa huduma ya ndege nyingi. Kwa maana hiyo, ili kuweza kukidhi mahitaji ya matumizi ya uwanja huu, tutakapofanya maboresho, ikiwa ni pamoja na kuweka taa za kuongoza marubani, ina maana tutaongeza idadi ya miruko. Kwa sababu siyo suala la kuongeza ndege kubwa peke yake linaweza kukidhi mahitaji ya Bukoba, lakini ni pamoja na kuongeza idadi ya miruko katika uwanja huu. Kwa hiyo, tukifanya maboresho, idadi ya miruko tutaiongeza wakati tunatazama siku za usoni tufanye nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, matumizi ya uwanja wa Omukajunguti, niseme tu uwanja huu bado unamilikiwa na Serikali na bado utaendelea kumilikiwa na Serikali kwa sababu maendeleo ya nchi hii yanakwenda kwa kasi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, nasi wakati tunasonga mbele tunaendelea kutazama matumizi mazuri na maboresho ya uwanja huo wa Omukajunguti.

Nimhakikishie tu Mheshimiwa kwamba tunautazama vizuri na nitoe tu maelekezo kwa wenzetu upande wa TAA tuutazame uwanja huu kama kutahitaji kuweka uzio, tuweke kwa maana ya kuulinda. Pia niwasihi tu wananchi wa Bukoba na watu wanaozunguka eneo hili tusivamie eneo hili, eneo hili litakuja kutupa manufaa sisi na Watanzania wote kwa ujumla. Ahsante.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi ya kutafutwa pesa kwa ajili ya barabara hii ni ahadi ya muda mrefu sana, lakini pia naomba niweke kumbukumbu vizuri kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, zoezi la kufanyia upembuzi yakinifu barabara hii lilikamilika mwaka 2015 wakati mimi naingia kuwa Mbunge na siyo 2008. Sasa naomba kujua, nini dhamira ya Serikali juu ya kutekeleza ahadi yake ya muda mrefu kuhakikisha fedha ndani ya mwaka huu wa bajeti inapatikana ili barabara hii iweze kufanyiwa kazi kwa kiwango cha lami? Hilo ni swali la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ambalo naomba nipate majibu, barabara hii kwa mujibu wa nyaraka nilizonazo, mwanzo kabisa wakati inafanyiwa upembuzi yakinifu ilikuwa inasomeka Masasi – Nachingwea – Nanganga, lakini baadaye ikaja kuanza kufanyiwa kazi barabara ya kutoka Nanganga – Ruangwa – Nachingwea. Sasa hivi majibu yanayotoka, kuna kipande cha kilometa 45 cha kutoka Nachingwea kwenda Nanganga hakisemwi na hakionekani katika maelezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua msimamo wa Wizara juu ya kioande hili cha Nachingwea kwenda Nanganga ambacho ni kilometa 44.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa umakini na ufuatiliaji wa maendeleo ya Nachingwea lakini siyo Nachingwea peke yake, bali pia maeneo ambayo kimsingi yanaunganika na Wilaya hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kweli usanifu ulikamilika kipindi cha nyuma, lakini kwa jibu ambalo nimelitoa sasa hivi, kwa yale maandalizi ya kuanza ujenzi huwa kuna kitu ambacho tunaita mapitio. Tunafanya review ili tuweze kutangaza ujenzi wa barabara. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Masala kwamba records ambazo nimeziweka hapa kwa maana ya review ilikuwa ni maandalizi sasa ya kuanza ujenzi. Hivi tulikuwa tunafanya mawasiliano na wenzetu wa upande wa Wizara ya Fedha, fedha zikipatikana tunaanza kujenga barabara hii. Kwa hiyo, nimtoe hofu yeye pamoja na wananchi wa Nachingwea na majirani zake, ni kwamba harakati za kufanya ujenzi wa barabara hii tumezifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la (b); kutokana na review ambayo nimeisema hapa imefanyika ili tuanze ujenzi, haimaanishi kipande hiki cha Nachingwea - Nanganga kwamba tunakiacha. Hiki ni vipambele tu kutokana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Masala kipande cha Nachingwea - Nanganga na chenyewe kiko kwenye mpango na vile vile tuwasiliane baadaye, atakuja kuona kwenye mpango mkakati wetu baada ya review kwamba tumejipanga vipi kuanza kujenga kwa kiwango cha lami. Kwa maana hiyo ni kwamba tukipata fedha tunaanza ujenzi wa barabara hizi muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Masala ajue kwamba wakati huo tunajiandaa, tunaendelea kushughulikia maeneo ambayo ni korofi, tunaendelea kushughulikia maeneo ambayo ni maalum, tunaendelea kujenga madaraja. Labda kwa manufaa ya wananchi wa Nachingwea niseme kwamba tumeendelea kukamilisha daraja la Lukuledi ambapo barabara niliyoijibia itapita ili tuwaungenishe vizuri wananchi hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tunaendelea kujenga maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Lindi, madaraja ya kule Chumo, kuna daraja Mlowoka, Mtakuja na Nanjilinji. Hii ina maana kwamba maeneo ambayo tumeyatengea fedha za kutosha na maeneo ambayo wananchi walikuwa wanapata usumbufu kupita katika maeneo haya tumeyazingatia. Kwa hiyo, wananchi wa Ruangwa, Nachingwea na maeneo yote ya Lindi, ni kwamba tumejipanga ili tuwahudumie vizuri.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niipongeze sana Serikali kwa kuunganisha barabara nyingi za nchi yetu kutoka Wilayani na Makao Makuu ya Mikoa yetu. Sambamba na hilo napenda niulize swali langu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Bungu - Nyamisati inaunganisha Wilaya ya Mafia na Kibiti. Sasa barabara hii iko chini ya kilometa 50 na kama mnavyojua historia, Mafia ni Kisiwa, wanatumia usafiri mmoja tu ambao ni ndege. Je, ni lini barabara hii itaunganishwa kwa kiwango cha lami ili kuwasaidia wananchi wa Mafia?
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kikwete kwa namna anavyofuatilia maendeleo ya sehemu mbalimbali. Kwa hiyo mara nyingi nimemsikia akizungumza juu ya Lindi, leo anazungumza juu ya Pwani, kwa hiyo nampongeza sana. Hata maeneo mengine, nimemsikia pia akiwasemea walimu kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la Nyamisati ni eneo muhimu sana. Nifahamishe tu Bunge lako pamoja na wananchi kwa ujumla, ni kwamba tunatengeneza gati katika eneo hili la Nyamisati kwa lengo la kuhudumia kivuko ambacho pia tumeanza hatua za manunuzi, kivuko ambacho kitatuvusha kutoka Nyamisati kwenda Kilindoni kule Mafia. Tunaendelea vizuri. Kwa hiyo, niwahakikishie tu wananchi hawa wa Nyamisati na wananchi wa Pwani na Watanzania kwa ujumla kwamba tutakuwa na kivuko ambacho kitatusaidia kupunguza usumbufu uliokuwepo kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapotengeneza kivuko pamoja na gati hii lazima ule mnyororo wa usafiri tuuweke vizuri. Ndiyo maana nami nimetembelea eneo hili kilometa kama 48 hivi kutoka Bungu kwenda Nyamisati ili kuhakikisha kwanza barabara tunaiweka katika ubora unaohitajika, lakini pia mipango yetu ipo ili tuje kuweka lami barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii muhimu itatusaidia pia kusafirisha mizigo mingi kutoka Nyamisati kwenda hata sehemu hii ambayo tunajenga umeme (Stiegler’s Gorge) kwa sababu barabara hii kutoka Kibiti kwenda Stiegler’s Gorge tumeiboresha na tunaamini kwamba gati hii ikiboreshwa kutakuwa na vyombo ambavyo vitabeba mizigo mizito kuja Nyamisati ambavyo vinaweza vikahitajika kwenda kwenye maeneo ya mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatumaini kwamba barabara hii kuiboresha pamoja na kuiweka kiwango cha lami itatusaidia sana kubeba mizigo na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsnate sana.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba hadi sasa amefikia asilimia 25.2 barabara inayokwenda Njombe - Makete na asilimia 20 barabara ya Itone – Ludewa: Je, kama sasa hivi ni asilimia 25 na mwakani mwezi wa kwanza iwe imekamilika, ni muujiza gani utatendeka hapo kuikamilisha kwa miezi nane tu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Hali ya barabara za Njombe Mjini na Vijijini ni mbaya sana kwa kuwa mvua sasa hivi zinaendelea kunyesha. Kuna hali mbaya sana kwenye zile barabara na watu sasa hivi wamesimamisha shughuli, hawawezi tena kusafirisha bidhaa au mazao: Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha inakarabati barabara hizi kwa haraka iwezekanavyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba tuko asilimia hizo 25.2 na asilimia 20 kwa eneo la Itone – Ludewa, lakini labda nilifahamishe tu Bunge lako kwamba Mkoa wa Njombe hali ya jiografia yake ni maalum sana, ni special. Udongo wa Njombe siyo mchezo, kwa hiyo, hata kufikia asilimia hizi ilitakiwa Mheshimiwa Mbunge aipongeze Serikali. Ndiyo unaona kwamba barabara hii ambayo tunaijenga Lusitu - Mawengu ni barabara chache sana tumeweza kujenga kwa kiwango cha zege.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kutokana hata na udongo wake tuliotumia kwa ujenzi, ulikuwa unatoka zaidi ya kilometa 200, kwa sababu udongo wa Njombe uko maalum kidogo. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango kazi ambao sisi kama Serikali tunausimamia, tutahakikisha kwamba kila wakati tunakwenda nao ili kama kutatokea zile natural calamity kama mvua kuwa nyingi, kama maporomoko katika maeneo haya, hata juzi tu barabara hii ilijifunga kwa sababu udongo wake unaporomoka sana. Kwa hiyo, nasi tunachukua hatua kila wakati ili kuhakikisha kwamba tunafanya marekebisho, ujenzi unaendelea, tukamilishe mradi huu kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ule mpango kazi yaani action plan tutaendelea kuisimamia ili kuona kama kutakuwa na matatizo makubwa ya hali ya hewa tuangalie alternative ya kufanya barabara hii ikamilike na barabara hii wananchi wa Njombe na Watanzania wanaitumia. Kwa hiyo, miujiza ni ile ya Mungu kwamba tunasimamia vizuri na mvua ziwe nzuri, tuombe Mungu pamoja ili tukamilishe barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu (b), amesema barabara za vijijini hali ni mbaya. Ni kweli kama nilivyosema, hali ya jiografia ni mbaya, lakini sisi tumejipanga vizuri ndiyo mana utaoa kwamba tunao mpango kama tukipata fedha tutaanza kutengeneza hii barabara ya kipande cha kutoka Kibena kwenda Lupembe kwenye mpango wa manunuzi tunaoendelea nao, kilometa 50, tuanze kupunguza na kuwafanya wananchi wa maeneo ya Njombe waweze kwenda Morogoro kupitia Madeke na Mlimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, yale maeneo ambayo yako korofi sana, tunaendelea kujenga barabara za zege kwa hiyo, zipo kilometa 126, ukitoka Lupembe pale ziko kilometa ambazo tunaendelea kuziunganisha na wananchi sasa wana-enjoy magari yanatoka Mlimba yanakuja Njombe. Kwa hiyo, ni hatua za Serikali kuwajali wananchi wa Njombe kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge, hata hii barabara tunayozungumza ya kutoka Mawengi – Lusitu, sehemu ya Itoni kwenda Lusitu na yenyewe tunaitazama kwa sababu ni muhimu tuwaunganishe vizuri. Pia tunatengeneza daraja kule Mto Ruhuhu ili wananchi hawa wa Njombe tuwaunganishe vizuri na wenzao wa Manda kule Ruvuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwa ufupi kwamba tumejipanga vizuri, Njombe iko so special lakini nasi kama Serikali tuko special kwa ajili ya Njombe ili wananchi wapate huduma vizuri.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza pia Mbunge wa Jimbo la Peramiho, dada yangu, Mheshimiwa Jenista Mhagama, kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia ujenzi wa barabara hii na hata alipokuja Mheshimiwa Rais, alijaribu kusema pale ili barabara hii iweze kujengwa.

(a) Swali langu la kwanza; ni kwa nini Serikali inachukua muda mrefu sana kufanya upembuzi yakinifu lakini pia na usanifu wa kina? Barabara hii imechukua karibu miaka kumi kupitia maneno hayo ya upembuzi na usanifu. Ni lini Serikali itamaliza upembuzi huu na usanifu huu ili barabara hii ianze kujengwa?

(b) Swali la pili; licha ya Serikali kuonesha kwamba imetenga shilingi bilioni 5.86, lakini fedha hizi hazikuweza kwenda kwa mwaka 2018/2019: Je, Serikali haioni kwamba kutokupeleka fedha hizi inaendelea kuchelewesha maendeleo kupitia barabara hii kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, hususan Jimbo la Peramiho?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, uniruhusu tu nimpongeze Mheshimiwa Jacqueline, lakini nimpongeze Mbunge wa Peramiho kwa kufuatilia kwa sababu amekuwa akifuatilia sana jambo hili. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge mwuliza swali kwamba inachukua muda mrefu kwa sababu kwanza mtandao wa barabara ni mkubwa, mahitaji ya ujenzi ni makubwa na tunaendelea kutafuta fedha na kutenga fedha. Hata mwaka unaokuja tutaliomba Bunge lako liweke fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Fedha. Tukipata fedha tu mara moja tutatangaza na kuanza kujenga barabara hii. Kwa hiyo, kwa majibu hayo, Mheshimiwa Jacqueline avute subira kidogo, tumejipanga vizuri, mahitaji ni makubwa, tunakuja Peramiho kuhakikisha kwamba tumewaunga wananchi wa…

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Kemi.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya Nyakato Steel – Igombe, kilometa 18 na Barabara ya Mwaloni – Kirumba, kilometa 1.2 zimekuwa zikisuasua na ujenzi wake kwa muda mrefu sana. Mheshimiwa Angeline Mabula, amekuwa akifuatilia barabara hizi kwa muda mrefu lakini bado hatujapata majibu sahihi ya Serikali. Ni lini sasa barabara hizi zitakamilika na wananchi wa Mkoa wa Mwanza, hususan Wilaya ya Ilemela waweze kupata barabara safi na salama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua changamoto za barabara za Ilemela, nami nimekwenda, nimeona. Nitoe tu maelekezo na wito kwa Mameneja wetu kule kwenye Mkoa wa Mwanza kwamba wasimamie kwa ukaribu nami nitakwenda kuhakikisha kwamba maeneo haya; na yapo maeneo siyo haya tu aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge, yapo maeneo mengi kwenye Jimbo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Angeline Mabula kwa sababu amekuwa akifuatilia sana, ilinichukua siku nzima, mtandao ni mkubwa sana kwenye Jimbo lake, mjini lakini…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, majibu mazuri na muhimu, fanya ziara naye.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, nitakwenda.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya kutoka Tabora kwenda Kigoma ambayo inatuunganisha na Tabora bado haijakamilika; na kipande cha kutoka Malagarasi mpaka Uvinza ambacho kilikuwa na Mkandarasi wa Abu Dhabi Fund tumesikia kuna matatizo ya kiufundi: Je, Mheshimiwa Waziri unasema nini juu ya jambo hilo? Vinginevyo barabara hii haitakamilika mpaka tufike mwaka 2020.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nsanzugwanko anafahamu, tumezungumza mara nyingi sana juu ya barabara hizi. Niseme tu kwa ufupi, Chagu – Kazilambwa pamoja na barabara ya Malagarasi – Uvinza zitakamilisha mtandao wa barabara kutoka Tabora kwenda Kigoma tukikamilisha vipande hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutazungumza tu na Mheshimiwa Mbunge tuone kama kuna changamoto, basi tujue nini kinachoendelea. Kwa kifupi tunakwenda kujenga barabara hii.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Barabara za lami hugharimu pesa nyingi za Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mara tu barabara hizo zinapojengwa, hubomolewa na kupitishwa miundombinu mingine, hatimaye hazirejeshwi katika ubora wake:-

Je, Serikali inatuambia nini juu ya jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ujenzi wa barabara unachukua fedha nyingi, lakini niseme tu shughuli zozote zitakazohusisha kukata barabara lazima zifanyike kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, kama kuna mtu anakata barabara na kuacha uharibifu ni makosa. Nami nielekeze viongozi wote, Mameneja wote wa Mikoa; mtu ambaye atafanya shughuli za kibinadamu na kuharibu barabara bila kurejesha kwa ubora wake na bila kupata kibali kwa mujibu wa sheria ni makosa, wachukue hatua kwa mujibu wa sheria.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza nisikitike kwa niaba ya wananchi wa Busokelo kwa sababu barabara hii aliitembelea aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi kipindi hicho, Mheshimiwa Eng. Ngonyani tangu tarehe 21 Novemba, 2016 na aliahidi kwamba ingetengenezwa kwa kiwango cha changarawe kilometa 7.5. Hili swali nimeliuliza Bungeni zaidi ya mara tatu na kila jibu linalokuja linakuwa tofauti na jibu lililotangulia. Wananchi wa Busokelo wanataka kujua ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za wananchi wa Jimbo la Busekelo, Kata ya Luteba ambao wameanza kutengeneza barabara hii kwa kilometa 4 wao wenyewe kwa jembe la mkono pamoja na Mbunge wao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa barabara hii imeanzishwa na nguvu za wananchi na kwa maana hiyo Serikali haitambui kama iko TARURA, TANROADS ama kwenye vijiji. Ni lini sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuunganisha nguvu za pamoja za TANROADS na TARURA ili tujue ni nani atakayehusika na barabara hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tumezungumza sana juu ya barabara hii na mimi kipande hiki cha barabara nilikitembelea eneo hili kweli lina changamoto kubwa. Barabara hii kimsingi inasimamiwa na wenzetu upande wa TARURA na sisi kwa maelekezo ya aliyekuwa Naibu Waziri wakati ule ni kwamba TANROADS twende tusaidie kutambua mahitaji na namna nzuri ya kuiboresha barabara hii, kazi ilifanyika na mawasiliano yalikuwa yanaendelea ya kupata fedha. Nitumie nafasi hii kuwaelekeza wenzetu wa Mfuko wa Barabara wafanye haraka kwa maana ya kuitoboa barabara hii ili ianze kutumiwa na wananchi na mimi nitaifuatilia ili kuhakikisha tunaitoboa barabara hii.

Mheshimiwa Spika, lakini tunasanifu barabara hii ambayo nimeitaja kutoka Isyonje – Kikondo - Makete na hiki kipande cha kilometa 7.5 kinatoka eneo la Busokelo kinaunga kwenye barabara hii ambayo itasanifiwa. Labda nielekeze pia wakati wa usanifu tuiangalie barabara hii kwa sababu kwenye milima hii ni hatari sana, kama itawezekana tuifanye kuwa spur ya barabara hii ambayo tutakuwa tukiisanifu. Kwa hiyo, wakati wa usanifu wa kilometa 7.5 tuiweke ili siku za usoni barabara hii iwe bora na iendelee kuwasaidia wananchi wa maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza naishukuru sana Serikali yetu kwa kujenga barabara ya Ndono - Urambo ambayo imekuwa msaada kwetu sana. Tatizo tulilonalo katika barabara hiyo ni kona inayoingia Urambo kwa kuanzia Ndorobo. Kona hiyo ni hatari kwa magari na pia kwa watembeaji wa miguu. Je, Serikali ni lini itaturekebishia barabara hiyo inayoingia Urambo Mjini kwa usalama wa watembea kwa miguu na magari kwa kutuwekea round about?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mama yangu Mheshimiwa Sitta, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli eneo analolitaja Mheshimiwa Mbunge hata mimi mwenyewe nimeliona, ni eneo ambalo linaunganisha barabara tatu lakini wataalam wa TANROADS, Mkoa wa Tabora wanapatazama hapa ili tuone kama tutaweza kuwa na design ya kuweka mzunguko hapo tutaweka lakini kama italazimika kuweka eneo lingine ili kuweza kudhibiti usalama wa watumiaji wa barabara maeneo hayo tutafanya hivyo. Tunalitazama kwa upana mkubwa ili tukitengeneza kitu tuweke kitu ambacho kitaweza kusaidia lakini kuleta maana na mahitaji ambayo Mheshimiwa Mbunge anayataja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira wanapatazama kwa sababu kwa namna inavyounganisha barabara tatu pale kidogo kulikuwa kuna changamoto fulani ambazo wataalam wanazifanyia kazi ili tuje tupate mchoro mzuri ambao pia hata gharama zake kuweza kurekebisha zitakuwa nzuri. Tunalifanyia kazi, vuta subira na wananchi wa Urambo wanasikia kwamba tupo pamoja nao.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Naomba kuuliza swali moja tu la nyongeza kwamba barabara ya Handeni – Kiberashi – Kiteto – Chemba - Kwamtoro - Singida ilishafanyiwa upembuzi yakinifu muda mrefu na wananchi walishawekewa alama za X. Naomba Mheshimiwa Waziri anihakikishie katika bajeti ya mwaka huu wataanza kulipwa fidia na kuanza ujenzi wa barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nkamia, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli usanifu wa barabara hii ya Handeni – Kiberashi - Chemba - Singida kilometa 461 usanifu wake ulishakamilika na Serikali inatafuta fedha. Hata hivyo, kabla ya kuanza ujenzi utaratibu ni kwamba lazima wananchi wote wanaopitiwa na eneo hili la barabara waweze kulipwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Nkamia tunaendelea kuwasiliana na wenzetu wa Wizara ya Fedha ili wananchi hao walipwe haki zao ili tukipata fedha ya kuanza kujenga barabara isiwe kikwazo kwa sababu wananchi hawajalipwa fidia. Kwa hiyo, vuta subira na nitaendelea kukupa update ili basi ile appetite ya wananchi kupokea fedha za compensation waweze kujiandaa kwa maendeleo yao mengine.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spoika, kwa kuwa barabara ya kutoka Gulwe – Berege – Mima - Sazima - Seruka na barabara hiyo Spika unaifahamu kwa sababu umeishi Mima. Barabara hii TARURA hawawezi kuitengeneza kwa sababu hawana fedha za kutosha na Serikali ilikubali kuichukua barabara hii ili ifanyiwe matengenezo makubwa. Je, Mheshimiwa Waziri unasemaje kuhusu suala hili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lubeleje, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli eneo alilotaja Mheshimiwa Mbunge la Gulwe – Berege – Mima - Seruka ni eneo ambalo lina changamoto zake kwa sababu linapitiwa na maji mengi wakati wa mvua na kumekuwa na uharibifu mara kwa mara. Kikubwa tu Mheshimiwa Lubeleje nikuondoe hofu usubirie ni wiki ijayo tu Jumanne utaona namna tulivyojipanga kurekebisha barabara hii ikiwa ni pamoja na eneo la Godegode.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Bunge lako likitupitishia fedha tunakwenda kufanya usanifu na kufanya ujenzi kwenye eneo hili ambalo Mheshimiwa Mbunge amelitaja. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi eneo hili na mimi nililitembelea na yako maeneo mengine pia Mheshimiwa Lubeleje atayaona kwa maana ya Mpwapwa kwa ujumla wake tumeitazama kwa macho mawili kwa sababu tunajua changamoto za barabara katika maeneo yake.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona na kunipa fursa niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa moja ya changamoto za maendeleo vijijini ni ukosefu wa barabara zinazopitika na kwa kuwa TARURA imeundwa ili ku-address changamoto hiyo. Kwa kuwa katika Wilaya nyingi nchini, TARURA haina mitambo ya kutengeneza au hata kufungua hizo barabara vijijini ikiwemo Wilaya ya Longido. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba Wilaya zote ambazo TARURA haina mitambo ya kufanyia kazi wanapata mitambo hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, niseme kweli tumekuwa na chombo hiki TARURA na imeanza kufanya kazi vizuri na Waheshimiwa Wabunge watakuwa mashahidi. Yako maeneo ambayo yalikuwa na changamoto kipindi cha nyuma sasa yanafayiwa kazi vizuri. TARURA watasimamia shughuli za ujenzi wa barabara za vijijini kama wanavyosimamia TANROADS, kwa maana hiyo wakipata fedha uko utaratibu wa kutangaza, tunapata wazabuni, wakandarasi mbalimbali wanakwenda kufanya matengenezo ya barabara kwa utaratibu ule ule kulingana na Sheria za Manunuzi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi na TARURA wamefanya kazi nzuri na kwa muda mfupi wameshazitambua barabara zote na kuziingiza kwenye mfumo kwa sababu kulikuwa na changamoto ya barabara zingine ambazo zilikuwa hazitambuliki. Hivi karibuni wamepita karibu maeneo yote nchini kufanya sasa uhakiki kuona kama kuna sehemu barabara ilisahaulika iweze kuingia katika mtandao wa barabara.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo la Longido ni sehemu ambayo pia TARURA wamefanya kazi ya kutambua barabara. Kama nilivyosema ni kazi yetu sisi Bunge tukiwapa fedha za kutosha ninaamini barabara zote zitaboreshwa kulingana na changamoto zilizoko katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Ahsante sana.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu haya mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kutambua kwamba hii ni ahadi ya chama chetu ya muda mrefu tangu Ilani ya mwaka 2010, huu ni mwaka wa tisa na sasa usanifu umekamilika, je, Mheshimiwa Naibu Waziri haoni kwamba ni muafaka sasa kwa kipande kile cha Makofia hadi Mlandizi ambacho usanifu wake umekamilika kuanza taratibu za ujenzi mapema iwezekanavyo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu hivi sasa usanifu umekamilika na wananchi hawa walikuwa wanasubiri fidia ya maeneo yao tangu kipindi ambapo barabara hii ilitangazwa kujengwa kwa maana ya takribani imefika miaka tisa. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuwalipa fidia wananchi hawa kutoka Makofia hadi Mlandizi mpaka Vikumburu ili waweze kupisha ujenzi wa muundombinu huu muhimu kwa furaha?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shukuru Jumanne Kawambwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Kawambwa kwa sababu nafahamu amekuwa akifuatilia sana barabara nyingi za Mji wa Bagamoyo, ikiwemo barabara hii ya Makofia-Mlandizi lakini pamoja na barabara nyingine ambazo zinaunganisha Mji wa Bagamoyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la kwanza, ni kweli kwamba barabara hizi alizozitaja, ukiichukua kutoka Bagamoyo - Mlandizi - Kisarawe ziko kilometa 100, lakini kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi kwamba kazi kubwa imeshafanyika na sasa tunakamilisha kufanya mapitio ya compensation (fidia) kwa wananchi ambao watapisha mradi huu. Kama ilivyo kanuni, tukishawalipa wananchi hawa sasa tutakuwa na haki ya kuanza kuenga kipande hiki cha barabara.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimtoe hofu tu Mheshimiwa Dkt. Kawambwa kwamba kipande cha barabara hiyo kutoka Makofia mpaka Mlandizi kilometa 36.7 sasa tunakamilisha. Tathmini ya awali ilionyesha kama fidia ya shilingi bilioni 11 au 12, hivi sasa Mtathmini anafanya review ili tuweze kuwa na uhakika wa kiasi gani wananchi hawa wanastahili ili tuwalipe tuanze kujenga kipande hiki.

Mheshimiwa Spika, lakini niseme tu kwamba kwa sababu barabara hii inaunganisha vipande viwili, kile cha kutoka Kisarawe - Mlandizi, kile kipande cha kutoka Kisarawe - Maneromango kama kilometa 10, hivi sasa ujenzi unaendelea. Kwa hiyo, niseme tu kwa ujumla wake kwa wananchi wa Bagamoyo na Pwani kwa ujumla kwamba barabara hii yote kwa ujumla wake ujenzi tumeshaanza na tukilipa fidia pia kipande cha kutoka Mlandizi - Bagamoyo tutaanza kukijenga ili wananchi waweze kunufaika na matokeo makubwa ya kazi nzuri ya Serikali yao.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Nangurukuru-Liwale ni muhimu sana kwa wakazi wa Liwale, lakini siyo hivyo tu ni barabara iliyoahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2015-2020. Je, Serikali inawaambia nini wana Liwale juu ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kuchauka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimpongeze tu Mheshimiwa Kuchauka kwa sababu namfahamu amekuwa akiifuatilia sana barabara hii, ni kilometa 230 kutoka Nagurukuru - Liwale. Niwahakikishie tu wananchi wa Liwale kwa ujumla wake, maana walikuwa wanajiona kama wako Kisiwani. Mheshimiwa Kuchauka anafahamu tunatoka Nachingwea, kilometa 129 kuja Liwale na tuko kwenye hatua ya usanifu. Namwomba Mheshimiwa Mbunge asiharakishe tu shughuli, tutakuja na pendekezo kwenye bajeti yetu inayokuja kwa ajili ya kusanifu barabara hii ya kutoka Nangurukuru - Liwale.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niliombe tu Bunge lako tutakapokuja na pendekezo hilo watupitishie ili twende kusanifu barabara hii ya Mheshimiwa Mbunge Kuchauka na hatimaye tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza kabisa napenda kuishukuru Serikali kwa kusikia kilio cha Wanahandeni cha muda mrefu kwa kuitengea hela hiii barabara. Barabara ya Mziha - Handeni matatizo yake ni sawasawa na barabara inayotoka Handeni kwenda Kilindi. Barabara hii inaunganisha mikoa karibu minne ambayo ni Tanga, Manyara, Dodoma mpaka Singida. Barabara hii asilimia kubwa wanayoitumia ni wakulima na huwa wanapata tabu sana…

MWENYEKITI: Mheshimiwa uliza swali sasa.

MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni lini barabara hii inayotoka Handeni kwenda Kilindi itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Omar Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inayo mpango wa kujenga barabara hiii kutoka Handeni kilometa 461 inapita katika maeneo ya Handeni, Kivirashi, Kijungu, Kibaya, Njoro, Mrijo chini inakwenda Chemba hadi Singida. Tunao mpango wa kujenga barabara hii na tayari imeshasanifiwa. Niseme tu kwamba katika mwaka huu wa fedha unaokuja tutapendekeza kwenye Bunge lako ili tuanze kujenga kwa kiwango cha lami barabara hii muhimu kwa sababu barabara hii itakwenda sambamba na bomba la mafuta ambalo litajengwa. Kwa hiyo ni barabra muhimu sana, kwa hiyo nimwombe tu Mbunge avute subira kwamba tutakuja kujenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwenye maeneo ambayo ni korofi ambayo yanapita eneo la Kilindi, kwa mfano, eneo la kutoka kwa Luguru kwenda Kibirashi ni eneo ambalo kidogo lina ukorofi, tumepanga katika mwaka unaokuja kwamba wakati tuna harakati za kujenga kiwango cha lami tutaiimarisha eneo hili kwa kujenga daraja katika eneo la Kigwangulo. Mheshimiwa Kigua naona anapiga makofi pale anafahamu eneo hili lina changamoto, kwa hiyo tutakuja kuimarisha wakati huo Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kujenga kiwango cha lami.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda tu kumkumbusha kwamba Mheshimiwa Rais aliahidi barabara ya kutoka Dutwa Jimboni kwa Mheshimiwa Mwenyekiti kuja Ngasamo kuja mpaka Nyashimo iwekwe kwa kiwango cha lami na maandalizi yameshaanza kidogo kidogo. Nataka tu nipate comfort ya Serikali, ni lini sasa utekelezaji halisi wa barabara hii utaanza kwa ajili ya kuweka lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chegeni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Chegeni nafahamu barabara hii tumeizungumza sana, ni barabara muhimu na hatua kama alivyosema mwenyewe kwamba ziko hatua kwenye ujenzi wa barabara hii tumeshazifikia. Kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Chegeni kwamba tunaendelea kuhakikisha kwamba kila tukipata fedha barabara hii tunaijenga ili tuweze kuikamilisha barabara hii muhimu. Kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Chegeni na wananchi wa maeneo yote ya Dutwa na Simiyu kwa ujumla kwamba tunawaunganisha vizuri katika maeneo yao.
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya Singida- Ilongero –Ngamu ambayo pia inaunganisha Mkoa wa Manyara ni barabara muhimu sana kwa wananchi wa Mkoa wa Singida. Barabara hii ilitangazwa kipande cha kilometa 12.6 kutoka Njuki kwenda Ilongero kujengwa kwa kiwango cha lami tangu mwezi Novemba mwaka jana.

MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua ni lini ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hiyo kutoka Njuki kwenda Ilongero utaanza? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Monko kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumejipanga kujenga barabara hii muhimu kutoka Singida- Ilongero- Ngamu tunakwenda mpaka Hydom na tumetenga fedha katika mwaka huu wa fedha unaoendelea, zoezi la usanifu ili
kujenga barabara hii yote inaendelea. Hata hivyo, kipande hiki cha barabara anachokizungumza kutoka eneo la Njuki kwenda Ilongero ni sehemu muhimu sana kwa kuwahudumia wanachi wa Singida Vijijini. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea na utaratibu wa harakati za manunuzi, zikikamilika tu tutaanza ujenzi wa barabara hii muhimu, kwa hiyo Mheshimiwa Monko avute subira tunakwenda Ilongero kujenga barabara hii.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kuniona. Matatizo yaliyopo Handeni-Mziha- Kibindu mpaka Mbwewe yanalingana kabisa na hii barabara ya kutoka Handeni kwenda Mziha. Je, ni lini Serikali inakuja kutujengea barabara ile kwa kiwango cha lami kama ambavyo sasa hivi nyumba zote zimepigwa X kupisha ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Mbunge anauliza juu ya barabara ya kutoka Mbweni inakwenda Kibindu ikipita kwa Luhombo itaungana na barabara hii niliyoijibia swali la msingi kwa maana ya kwamba kuwaunganisha wananchi wa maeneo haya na barabara hiyo itakuwa inakwenda Tanga na sehemu hii kweli ina uzalishaji mkubwa. Niombe tu Mheshimiwa Ridhiwani kwamba avute subira kwa sababu najua barabara karibu zote zipo kwenye mpango mkakati wetu wa Wizara na ikimpendeza tuonanane baadaye tuitazame hii barabara
kwamba kwenye mpango wetu wa kipindi cha miaka mitano tumekipangia nini kipande hiki cha barabara kwa maana ya kwamba inajengwa kwenye kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa sasa tunaiboresha barabara hii na mimi nimeipita mara kadhaa kwamba iko katika kiwango kizuri kwamba inaendelea kuwapa huduma nzuri zinazohitajika wananchi wa maeneo haya.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, alipokuwa kwenye ziara yake Wilaya ya Mufindi alisema ahadi ni deni na hii barabara ni ya muda mrefu. Akaahidi kwamba hii barabara itajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Wilaya ya Mufindi na Rujewa na ni short-cut kwa wasafiri wanaotoka Mbeya. Nini commitment ya Serikali, lini wataanza kujenga barabara hii hata kwa kilometa mbili-mbili?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri uko tayari kuja Wilaya ya Mufindi kukutana na wananchi wote waliopo kandokando ya barabara hii kusudi uweze kuwaambia hatma ya tathmini na malipo yao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mgimwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mgimwa kwa sababu anafuatilia kweli siyo barabara hii tu peke yake lakini pia barabara inayoenda kumuunga kule Kihansi na kila wakati yuko Wizarani kufuatilia barabara hii. Kwa hiyo, nampongeza sana naamini kwamba wananchi wa Mafinga hawakukosea kumpa nafasi ya Ubunge.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba ahadi ni deni ni kweli na ndiyo maana tumeendelea kuiwekea kipaumbele barabara hii ili tuweze kujenga kwa lami. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mgimwa nakubaliana na wewe lakini tatizo ni fedha, tukipata fedha tutaendelea kupunguza kwa maana ya kujenga kwa awamu kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba kadiri tunavyopata fedha tutaendelea kujenga barabara hii muhimu kwa sababu inapita maeneo ya uzalishaji mkubwa wa mpunga kule Mbarali.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kutembelea eneo hili, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili nitatembelea eneo hili ili kuweza pia kuwahakikishia wananchi wa Tarafa hii ya Sadani na maeneo mengine kwamba tumejipanga kuwaletea barabara ya lami lakini pia kuwalipa fidia ili kupisha mradi huu muhimu. Ahsante.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami napenda niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikisimama mara kwa mara nikimuomba Waziri atujibu ni lini wataleta pesa na kujenga barabara ya kilometa 142 kutoka Dumila – Kilosa mpaka Mikumi ambayo kwa sasa imejengwa kuanzia Dumila mpaka Ludewa na bado kilometa 21 Ludewa – Kilosa? Kila siku nimekuwa nikijibiwa kwamba tuko kwenye upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na vitu kama hivyo. Wananchi wa Kilosa wanataka kujua ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hii muhimu kwa uchumi wao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Haule, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara hii muhimu inayotoka Dumila - Kilosa, inapita maeneo ya Ulaya mpaka Mikumi, niseme tu kimsingi barabara hii imeanza kujengwa lakini tunaenda kwa awamu. Mheshimiwa Mbunge unafahamu eneo hili la Ludewa – Kilosa ambalo sasa tuna mpango wa kujenga kwa kiwango cha lami na katika bajeti inayokuja kipande hiki tutaanza kujenga ili tupunguze uelekeo wa kwenda Mikumi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikuombe tu Mheshimiwa uvute subira, tumejipanga na tunaendelea kujenga kama unavyofahamu ili kuweza kuwaunganisha wananchi hawa wa Mikumi. Hii njia kwa kweli ni fupi, itapunguza gharama na muda lakini pia inapita maeneo muhimu ya uzalishaji na utalii kwenye maeneo yetu ya Mikumi. Ahsante.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri tuliambatana naye mpaka Kipiri Port. Sasa namuuliza lini usanifu wa barabara ya Namanyere – Kipiri Port utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Keissy, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli nimetembelea eneo la Kipili, Mheshimiwa Mbunge anafahamu yapo mambo mengi, nimpongeze tu kwa kweli kwa ufuatiliaji wake kwa sababu hata hii Bandari ya Kipili kule iko vizuri, tumeona maendeleo mazuri lakini uko umuhimu sasa wa kuunganisha kwamba tunakuwa na bandari nzuri lakini tunahitaji pia tuwe na barabara nzuri ya kuwapeleka wananchi katika maeneo hayo. Tumeona pia kuna uchumi mzuri, kuna samaki wanavuliwa maeneo yale wananchi hawa wanahitaji hii barabara.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Keissy, kama tulivyojipanga katika mwaka huu wa fedha tuliitengea fedha kwa ajili ya usanifu, harakati za awali zinaendelea, lakini katika mwaka unaokuja pia tutaweka mapendekezo ya fedha,ili tukamilishe usanifu na tuweze kuanza kujenga kipande hiki cha barabara kilometa kama 72 hivi kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kama ilivyo kwa wananchi wa Ludewa ni lini Serikali itaweka na kuharakisha utekelezaji wa kuwalipa fidia wale wananchi wa Wilaya ya Kyela waliopisha mradi wa Boarder Post? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakagenda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. Magufuli alipokuwa ziara Kyela ametoa maelekezo ili tuweze kuwalipa mara moja wananchi katika eneo hili, nimwarifu tu Mheshimiwa Mbunge, nami nimeongea na wananchi hawa baada ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais na tunalifanyia kazi suala hili ili tuweze kuwalipa wananchi hawa. Kwa hiyo Mheshimiwa Mwakagenda avute subira, sisi tumejipanga kama Serikali na kwa sababu Mheshimiwa Rais pia amekuwa na concern hiyo, wananchi watapata haki zao mara moja.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; ili haya makampuni ya kihandisi yapate usajili, inasemekana na wahandisi wenyewe kwamba kumewekwa tozo kubwa sana na hii Bodi. Je, Serikali iko tayari hivi sasa kupunguza tozo hizo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ili uweze kujenga nyumba, angalau ghorofa moja Tanzania ni lazima upate vibali vya makampuni ya kihandisi na vibali hivyo ni lazima uwe na kibali cha architect, structure, quantity QS, Contractor na pia ulipe malipo ya halmashauri na TRA. Sasa, je Serikali haioni kwa sababu ili upate vibali hivi, fedha ya tozo ya vibali vya wahandisi inaizidi fedha uliyokuwa nayo ya ujenzi. Je, haioni kwamba Serikali kwa kuruhusu suala hili wananchi wengi wanashindwa kujenga nyumba bora nzuri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nachuma almaarufu kama Mashine ya Kusini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze tu Mheshimiwa Nachuma kwa kuwa mfuatiliaji mzuri, lakini kwa sababu huyu Mheshimiwa ni Mwalimu niombe tu hata baada ya majibu yangu, baadaye pia nikusheheni documents za kutosha ili kwanza aone kazi nzuri ambayo bodi inafanya, lakini pia aweze kuona umuhimu wa kutumia taaluma hii. Taalum hii ni muhimu sana kwa sababu katika ujenzi lazima weledi uzingatiwe ili kuhakikisha kwamba hizi rasilimali zinazojengwa, majengo na huduma zingine kwa sababu bodi hii inasimamia wahandisi wa aina tofauti; wako wahandisi wa umeme, majengo, wako ma-technician na makundi mbalimbali. Kwa hiyo aone kazi hii kubwa inafanyika na kazi inafanyika vizuri. Pia Bodi hii inafanya kazi ya kusimamia zoezi zima la uadilifu katika sekta hii, lakini vile vile inasimamia kuhakikisha kwamba hata usalama unakuwa wa hali ya juu katika ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kujibu swali lake, anaona kwamba tozo ni kubwa. Ziko bodi m balimbali, kwa ulinganifu naona kwamba tozo ambayo inatozwa na bodi hii ukiwianisha na bodi zingine tofauti, sio ukubwa. Labda Mheshimiwa Mbunge tutaweza kuzungumza tuone ushauri wake unalenga nini ili tuone kama kutakuwa na jambo la kufanya kazi tutafanyia kazi, lakini kimsingi ukilinganisha tozo inayotozwa na huduma inayotolewa na gharama za rasilimali ambazo zinafanyika, kwangu naona kwamba bado ilikuwa ni reasonable na kwa muda mrefu hatujapata malalamiko mbalimbali kutoka kwa wateja ambao wanahudumiwa na bodi hii, lakini nalichukua pia kwa ajili ya kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vibali mbalimbali, kila tozo zinazotozwa kwenye vibali hivi, vingi amevitaja Mheshimiwa Mbunge inakuwa na sababu zake, lakini nijikite tu kwenye eneo hili kama nilivyosema, tutajaribu kuangalia lakini kwa sababu ziko taasisi mbalimbali zinatoza, tunaweza tukaangalia tuone kama kutakuwa na tozo ambayo itakuwa inaleta meaning moja basi hizo tutazifanyia kazi tukishirikiana na wenzetu ili tuhakikishe kwamba kusiwepo na tozo ambayo inafanana na madhumuni ya tozo nyingine ili tuwe na tozo ambazo kimsingi zitakuwa zinalenga kutoa huduma ambayo tumelenga tukusanye ili tuweze kufanya kazi nzuri kuhakikisha kwamba taaluma hii inawatendea haki Watanzania na kuimarisha uchumi na asset ambazo zinajengwa.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, uzembe na uchovu wa madereva, ubovu wa barabara, hii ni kampeni ya kila siku ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuzuia ajali lakini katika eneo hili bado ajali zinaendelea kutokea. Nilidhani labda Wizara ya Ujenzi itoe jibu la kiufundi zaidi kwa maana ya kurekebisha eneo hilo. Je, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi iko tayari kufanya usanifu upya katika eneo hilo na kufanya marekebisho ili kupunguza ajali?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa ajali zimekuwa nyingi sana katika eneo hilo, kwa mfano magari ya mafuta yamekuwa yakidondoka pale na moto unalipuka, majeruhi ni wengi lakini tumekuwa na tatizo la magari ya zimamoto pamoja na ambulance.

Je, Serikali iko tayari kutuletea magari ya zimamoto pamoja ambulance katika Wilaya ya Manyoni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kujibu swali la nyongeza kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba kabla ya ujenzi wa barabara katika eneo ambalo analitaja, ajali zilikuwa nyingi sana kuliko ilivyo sasa. Pamoja na ajali kuendelea kutokea, sisi Wizara ya Ujenzi baada ya ujenzi mara zote huwa tunaendelea kufanya tafiti ili kuona changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge eneo ambalo analitaja tutaweka msukumo mkubwa tuone kwa nini hizi ajali zinaendelea kutokea kutokana na hali ilivyo pale ili tuweze kuchukua hatua muafaka. Ni muhimu tu niendelee kusisitiza kama ilivyo kwenye jibu la msingi watumiaji wa barabara maeneo yote wazingatie alama za barabarani zinazowekwa kwa sababu maeneo ambayo ni hatari, sisi Wizara ya Ujenzi tumejitahidi kuweka alama kutoa tahadhali kwa watumiaji wa barabara ili muda wote tuwe salama tukiwa barabani.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumwambia Mheshimiwa Mtuka kwamba eneo hilo tutaliangalia kwa macho mawili ili tuone nini la kufanya. Hata hivyo, jambo hili lazima tushirikiane na watumiaji wengine wa barabara. Ahsante sana.
MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amasema barabara hizo zitapewa kipaumbele, je, ni vipi atazipa kipaumbele huku tayari bajeti imeshasomwa na pesa hazijatengwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari sasa kwenda kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo ili kuwaambia juu ya barabara hizo kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIAN (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali, Mbunge wa Manonga, kama ifuatavyo:-


Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Seif Gulamali kwa kufuatilia mipango ya ujenzi wa barabara lakini pia maendeleo mbalimbali. Mheshimiwa Gulamali nakumbuka wakati wa ziara ya Makamu wa Rais pia amefuatilia na kuzungumza juu ya barabara hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi sasa hivi tunaendelea na kukamilisha kuunganisha mikoa yetu kwa barabara za lami. Pia kama nilivyosema kwamba tutakapokuwa tumefika hatua nzuri tutaingiza kwenye mpango ujenzi wa barabara hizi muhimu ambazo umezungumza kwa sababu zinahudumia watu wanaokwenda kupata huduma ya matibabu pale Nkinga. Kwa umuhimu huo ndiyo maana katika mwaka 2018/2019 kama nilivyojibu tulitenge fedha nyingi karibu bilioni nzima, zaidi ya shilingi milioni mia nane themanini zilitengwa kwa ajili ya kuboresha maeneo korofi ili wananchi waweze kupita katika maeneo hayo bila shaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna ujenzi wa madaraja Mheshimiwa Gulamali anafahamu kule Mto Manonga, daraja kubwa tunaendelea kujenga lakini pia tunaendelea kuwaunganisha wananchi kutoka Ziba - Choma kwenda Kanawa kule upande wa Shinyanga kwa maana ya Wilaya ya Kishapu. Pia iko miradi mingine kutoka upande mwingine wa Shinyanga tunajenga ili kuweza kuwafanya hawa wananchi wawe kwenye mtandao mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, nitakuwa tayari kwenda kuzungumza na wananchi lakini Mheshimiwa Gulamali kumbuka wakati nikiwa na ziara na Makamu wa Rais pia nilipata nafasi ya kutoa ufafanuzi juu ya mpango kabambe wa kuiboresha barabara hii. Hata hivyo, kwa sababu unahitaji twende nitakwenda nizungumze na wananchi ili waone mipango mizuri ya Serikali tuliyojipangia kwa ajili ya kuboresha barabara hizi muhimu.
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Barabara ya Same - Kisiwani - Mkomazi ilishafanyiwa usanifu na umekamilika na Mheshimiwa Rais alitoa ahadi barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami. Je, ni lini barabara hii itaanza kujengwa ili kuondoa kero ya muda mrefu kwa wananchi wa Jimbo la Same na majimbo mengine yanayoweza kutumia barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Grace Kiwelu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba Serikali inayo mpango wa kujenga barabara hii kutoka Same
- Kisiwani - Mkomazi lakini pia tutakwenda mpaka kule Mkinga ili iweze kwenda mpaka Tanga. Ni kweli usanifu ulishafanyika, sasa hivi Serikali inafanya mapitio ili tuweze kwenda kwenye hatua ya manunuzi, sasa hivi Mkandarasi Mshauri anaendelea na kazi katika mwaka huu wa fedha ili kufanya review ya barabara hii ili tuweze kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute subira tukamilishe zoezi hili. Pamoja na hayo tumeweka mpango katika mwaka wa fedha unaokuja kwa maana ya kwamba kidogo kidogo kuna sehemu ambayo tutaanza kujenga kwa kiwango cha lami. Ahsante sana.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa ambayo Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeipa miradi mikubwa ya barabara ya kutoka Kisolya mpaka Bunda na barabara ya kutoka Makutano Butiama mpaka Mugumu. Barabara hizi zimekuwa zikijengwa kwa kusuasua, napenda kujua ni lini ujenzi wa barabara hizi utakamilika maana sasa ni miaka sita (6) tangu ujenzi uanze?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Makilagi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna ujenzi wa barabara unaendelea katika Mkoa wa Mara na Mheshimiwa Mbunge anafahamu na mara nimpongeze tu amekuwa akifuatilia sana hizi barabara. Mradi unaoendelea sasa hivi ni barabara kutoka Bulamba kwenda Kisolya.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mbunge anafahamu kwamba Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli alipofanya ziara katika Mkoa wa Mara alitoa maelekezo ili tuweze kujenga barabara hii kutoka Bulamba – Bunda -Nyamuswa kilometa 56. Utaratibu wa hatua ya manunuzi unaendelea na wakati wowote tutapata mkandarasi ili barabara hii ijengwe. Mheshimiwa Mbunge pia anafahamu tunajenga barabara kutoka Makutano – Sanzate, ni kweli kuwa barabara hii na mimi nimeitembelea ilikuwa inasuasua kidogo lakini tumechukua hatua ili kwa haraka hii iweze kukamilishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara nyingine ambayo itakuwa inashughulikiwa kwa maana ya kutangaza kupata mzabuni kutoka Sanzate - Nata. Kwenye mpango huu wa bajeti ambao tumepitishiwa na Waheshimiwa Wabunge juzi tutatoka tena kutoka Nata - Mugumu lakini tutatazama pia kujenga barabara kutoka maeneo ya Mugumu - Tabora B ili tuunganishe kwenda mpaka Loliondo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, iko mipango mizuri tu, nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute subira lakini kwa Mkoa wa Mara tumejipanga vizuri yale maeneo ambayo wananachi walikuwa na shida sasa neema inakuja. Ahsante sana.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Sisi wananchi wa Mkoa wa Njombe tunaishukuru Serikali kwa hatua za awali ilizofanya katika barabara ya Kibena – Lupembe – Madeke, usanifu yakinifu umeshafanyika na vilevile barabara hii imewekwa kwenye bajeti ya mwaka huu. Nilitaka kujua lini Serikali itaanza kujenga barabara hii ya Kibena – Lupembe - Madeke?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mgaya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu siyo hapa tu Bungeni ameendelea kufuatilia sana barabara za Mkoa wa Njombe.

Naiseme kwamba katika mwaka wa fedha 2018/2019 tunayo bajeti, harakati za kuanza kujenga kilometa 50 kutoka Kibena kwenda Lupembe zinaendelea. Kama hiyo haitoshi tukifika Lupembe, katika mwaka wa fedha unaokuja iko bajeti ambayo tumepitishiwa tutatoka eneo la Lupembe kuelekea Madeke mpakani na Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kuna maboresho makubwa maeneo ambayo yana uzalishaji mkubwa wa matunda, miti, na kadhalika yale maeneo ambayo ni korofi tunaendelea kujenga kwa kiwango cha zege, yale maeneo ambayo yalikuwa na vilima. Harakati hizi zimetusaidia sana kwani sasa hivi wananchi wanaotoka Mlimba wanaweza sasa kuja Lupembe wanakwenda mpaka Makambako kupitia hiyo barabara ambapo awali ilikuwa haipitiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, tumejipanga vizuri kwa sababu tunaitazama barabara hii kutoka Kibena ili tuweze kuwaunganisha wananchi wa Mikoa ya Njombe na Morogoro.

Ndugu yangu Mheshimiwa Mbunge wa Mlimba alitoa machozi hapa katika eneo lake lakini upo mpango unaoendelea wa kujenga kutoka Ifakara - Kihansi kwa maana ya kujenga kwa kiwango cha lami ili tuunganishe na kile kipande cha kilometa 28 kutoka Kihansi - Mlimba.

Vilevile ile sehemu ya kutoka Mlimba - Madeke nayo tumeiweka kwenye mpango ili mnyororo mzima usafiri ukitoka katika eneo hili la Ifakara tunaunganisha mpaka kwenda Njombe, tumejiwekea mipango mizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira na wakati nyingine tuonane ili aone mipango yote kwa maana ya barabara nzima ukitoka Njombe kwenda kwa wenzetu wa Morogoro na utusaidie pia kuzungumza na wananchi waone kwamba Serikali hii imejipanga kuwasaidia wananchi wa maeneo haya.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili. Kwa kuwa daraja lililosombwa na maji lilijengwa kwa gharama ya shilingi milioni 500 na limesombwa na maji, leo mnajenga daraja la shilingi milioni 325 hilo si ndiyo litachukuliwa mapema. Kwanini msiongeze fedha Mheshimiwa Naibu Waziri?

Swali la pili kwa kuwa barabara ya kutoka Mpwapwa, Lupeta, Mbori, Makutupa, Chamkoroma, Mlali mpaka Pandambili ni barabara muhimu sana kwa Majimbo mawili. Jimbo la Mheshimiwa Spika Mheshimiwa Ndugai Kongwa na Mpwapwa. Na kwa kuwa barabara hili huwa linatengewa fedha kidogo sana kwa ajili ya ukarabati.

Je, ni lini mtatenga fedha za kutosha ili barabara hii iweze kutengenezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Lubeleje, kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Lubeleje, mimi siku hizi namuita mzee wa Godegode, anafuatilia sana ujenzi wa daraja hili na Godegode na maeneo mengine. Nikiri kwamba ni kweli, kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema, kwamba daraja hili lililokuwepo lilijengwa muda mrefu na lilijengwa kwa gharama alizozitaja Mheshimiwa Mbunge, kwa milioni 500. Katika jibu langu la msingi nimezungumza juu ya kutenga milioni 325 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuhakikishie kwanza Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hii itafanyika vizuri tunafanya shughuli ya ujenzi kwa kutumia utaratibu wa design and construction. Kwa maana hiyo niseme tu kwamba tumetenga milioni 325 kwa ajili ya ule usanifu ambao utachukua muda mfupi sana kwasababu tutafanyakazi wenyewe kupitia wakala halafu baadaye tutaanza kujenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nikuhakikishie Mheshimiwa Lubeleje ukiangali kwenye kitabu chetu cha bajeti ukurasa 323 utaona kwamba pamoja na fedha hizi nilizozitaja kwamba baada ya design tutaanza kujenga na tumetenga milioni 180 ili sasa approach ya Kilomita 6 kwenye daraja la Godegode ili ujenzi uende sambamba kwa hiyo kuna fedha zingine milioni 180 tumezitenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalenga kwamba katika ujenzi wetu maeneo haya Godegode na maeneo mengine kusimamia vizuri ili gharama za ujenzi ziende chini huu ni mkakati wetu kama Wizara sio kama kujenga kwa fedha nyingi tumejipanga ili kusimamia vizuri gharama za ujezi ziweze kupungua. Mheshimiwa Lubereje utakubaliana na mimi kwamba sehemu ambapo daraja hili lipo ni sehemu ambayo imejengwa muda mrefu na mmomonyoko ni mkubwa na urefu wa daraja lile ni kubwa sana. Sasa tumejipanga kwamba kwenye daraja na godegode upande wa kulia kwake kama unaelekea kibakwe kwa maana kwamba tutalijenga upande kulia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalenga kwamba span ya daraja lile itakuwa fupi, sasa span ikiwa fupi gharama ya ujenzi zitapungua, span ikiwa fupi pia tutatumia muda ili wananchi haya waweze kupata huduma za kupita katika maeneo haya. Na kwa maana hiyo pia tumejipanga ndio maana nikasema tutakuwa na approach tutaboresha ili ku- control mmomonyoko ili daraja hili liwe bora. Kwa hiyo, Mheshimiwa Lubereje nikutoe wasiwasi kwamba tumajipanga vizuri kwamba tumejipanga vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu B Mheshimiwa Lubereje anasema kumekuwa bajeti ndogo katika eneo la mpwapwa, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Mpwapwa ni kati ya Wilaya zilizokuwa katika Mkoa wa Dodoma ambayo ni Makao Makuu na Mpwapwa ndio wilaya pekee ambayo haijaunganishwa vizuri na mkoa wa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumejipanga kama Serikali kufanya Mpwapwa iwe na barabara nzuri ili sasa iweze ku-support kazi nyingi ambazo zinafanyika katika Makao Makuu. Na kwa ushahidi tu Mheshimiwa Mbunge anafahamu tutaanza ujenzi wa lami kuanzia Mpwapwa kilometa kadhaa kuja kongwa. Lakini Mheshimiwa Lubereje nikuhakikishie kwamba kutoka Mpwapwa kwenda Gulwe kwenda Rudi, Chipogolo na penyewe tunasanifu kwa ajili ya ujenzi wa lami. Na barabara uliyo itaja barabara ya pandambili, Mlali Nghambi yapo kama maeneo manne matano ambayo tumeyatengea fedha za kutosha eeh…

MWENYEKITI: Ahsante

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): …sehemu korofi tumetengea milioni 120 kuna daraja pia milioni 150, tatu kuna zaidi ya milioni 600 ambazo tumezipanga katika mwaka huu wa fedha unaokuja ili kuifanya mpwapwa nao iweze kupata huduma za barabara.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kabla ya maswali kuna marekebisho kidogo katika maandishi aliyoandika hapa Mheshimiwa Naibu Waziri, inasomeka barabara ya Busisi - Busolwa, Nyijundu – Kharumwa - Bukwimbwa – Nyang’holongo siyo Nyang’hongo.

Mheshimiwa Spika, baada ya marekebisho hayo, napenda kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Kwa kuwa Serikali inakiri kutekeleza ahadi hizo za viongozi kwa kujengwa barabara ya lami kutoka Kahama hadi Busisi kupitia Kharumwa pindi pesa zitakapopatikana. Swali la kwanza, kwa nini wakati Serikali ikitafuta fedha za kutengeneza hizo kilomita nyingi tusitengewe fedha za kujenga kilomita 3 Makao Makuu ya Wilaya Kharumwa ili kupunguza vumbi kutokana na msongamano mkubwa wa magari uliopo pale?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Naibu Waziri amesema wanaendelea na kupeleka mawasiliano katika kata alizozitaja lakini Kata ya Nyijundu kuna matatizo ya usikivu. Je, Vodacom wako tayari kwenda kufunga mnara huo ili wananchi wa maeneo yale waweze kutuma na kupokea fedha kupitia Mpesa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza uniruhusu nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tumezungumza mambo mengi sana kuhusu uboreshaji wa miundombinu katika Wilaya hii ya Nyang’hwale. Tulifanya discussion na Mheshimiwa Mbunge na anakumbuka nilitoa maelekezo upande wa wenzetu wa TANROADS Mkoa wa Geita kwamba tutazame Makao Makuu ya Mji ya Nyang’hwale. Kama tulivyokubaliana tutaanza na kilometa 2 pamoja na kuboresha mitaro iliyowekwa katika Mji wa Kharumwa, Makao Makuu ya Nyang’hwale. Kwa hiyo, nimtoe hofu tumejipanga kufanya Makao Makuu ya Nyang’hwale kukaa vizuri.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mawasiliano, tunaendelea na hatua ya kuboresha mawasiliano nchi nzima. Nimsihi tu Mheshimiwa Mbunge baadaye tuonane ili tuangalie kwenye orodha maana kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tutapeleka mawasiliano katika vijiji 521 ambavyo viko kwenye kwenye hatua ya manunuzi inawezekana vijiji vyake vikawepo. Kwa hiyo, tuonane tu, ninayo orodha hapa, nawakaribisha na Waheshimiwa Wabunge wengine ili tuone tumejipangaje kupeleka mawasiliano maeneo ambayo tumejipangia katika awamu hii ya nne. Ahsante sana.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona. Tatizo la miundombinu lipo pia katika Jimbo la Ikungi Mashariki katika barabara yetu ya Makiyungu - Misughaa. Changamoto hiyo imekuwa kubwa sana wakati wa masika. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kuunganisha Mikoa ya Singida na Dodoma na kuharakisha shughuli za maendeleo katika maeneo hayo? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aisharose Matembe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Aisharose Matembe amekuwa mahiri sana kufuatilia barabara mbalimbali. Barabara hii anayoitaja Mheshimiwa Mbunge ni sehemu ya kilomita 461 ya barabara inayotoka Handeni – Kibirashi – Kijungu - Chemba - Singida. Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge avute subira kwani katika bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha kuanza ujenzi wa barabara hii muhimu. Tukipata fedha eneo hili litapitiwa na mradi wa barabara ya lami inayotoka Handeni – Singida.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba pia nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, ndugu yangu Chifu Kwandikwa kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Pamoja na majibu hayo mazuri nilikuwa naomba niulize swali moja dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara kubwa tatu zinazopita Jimbo la Msalala kwa maana ya barabara hii ya Solwa - Kahama kupitia Bulige; Busisi, Nyang’hwale - Kahama na Kahama – Geita, zote upembuzi yakinifu ulishakamilika. Bajeti ya mwaka huu mwezi Juni, tulipitisha fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kahama - Geita. Barabara hii imekuwa ni kero kubwa, nilitaka kujua na wananchi wafahamu ni hatua gani sasa imefikiwa ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Kahama - Geita kuanzia pale Manzese – Segese - Bukoli - Geita?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maige, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa Mbunge alivyozungumza ukiangalia kwenye ukanda ule barabara hizi zote zinahusiana. Sisi kama Serikali tumejipanga kufanya barabara hizi ziwe kwenye mnyororo mzuri. Mheshimiwa Maige anafahamu hatua nzuri tuliyofikia ya ujenzi wa barabara hii kutoka Kahama kupitia maeneo aliyoyataja ya Bulige, Jimbo la Mheshimiwa Bukwimba kwenda mpaka Geita Mjini. Tumejipanga na tupo kwenye hatua za mwisho kuanza ujenzi wa barabara hii muhimu. Hatua hii sasa itapunguza urefu wa barabara hii ambayo Mheshimiwa Nassor naye ameuliza hapa na nimejibu muda uliopita kwa maana itaunganisha barabara hiyo kwa maana ya kupita kwenye mji wa Nyang’hwale.

Mheshimiwa Spika, hata barabara hiyo niliyojibu kwenye swali la msingi inapita kwenye maeneo mengi, alijaribu kutaja maeneo machache. Kimsingi inagusa Jimbo la Misungwi, inapita kwenye eneo la Kwimba na inaunganisha pia Jimbo la Solwa, Msalala na Mji wa Kahama.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwa wananchi wa Kahama kwa ujumla na wananchi wa Mkoa wa Geita na Mwanza kwamba tumejipanga vizuri, tutaenda kwa awamu hivyo hivyo. Barabara hii kubwa itaanza lakini pia barabara hizi zingine tuko kwenye mpango wa kuzishughulikia. Tukionana baadaye ataangalia pia kwenye mpango mkakati wetu kama Wizara tumejipangaje hatua kwa hatua kukamilisha barabara zote hizi. Nampongeza sana kwa umahiri mkubwa katika kuwahudumia wananchi wa Msalala.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona, barabara ya kutoka Iringa Mjini kwenda Wilaya ya Kilolo kilometa 133 ambayo kuna kipande cha Jimbo la Kalenga napo kuna changamoto ya barabara mvua zimenyesha barabara nyingi zinakuwa hazipitiki vizuri wananchi wanapata adha na mazao yao yanashindwa na ni ahadi ya Rais ambayo alitoa kwamba kufikia 2020 itakuwa imetengenezwa.

Ni lini sasa Serikali itahakikisha barabara hii inatengenezwa na wananchi wanapita bila matatizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge watakubaliana na mimi kwamba kipindi hiki tumepata mvua myingi sana na uharibifu wa miundombinu umekuwa ni mkubwa sana, sisi
kama Seriikali tumejipanga kuhakikisha kwamba tunakwenda kufanya urejeshaji wa miundombinu hii. Niseme tu kilometa 4217 hadi Desemba zimekuwa na hali mbaya hizi ndiyo barabara katika nchi tunaendelea na uratibu nimuombe Mheshimiwa Mbunge avute subira tumeshatambua maeneo yote yenye shida na tunahitaji fedha za ziada kwenda kufanya marejesho ya miundombinu ya barabara.

Kwa hiyo, wananchi wavute subira sisi kama Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na wenzetu upande wa Serikali za Mitaa kwa maana TARURA tunafanya uratibu wa pamoja ili tuhakikishe kwamba tunaenda kufanya uridhishaji maeneo mbalimbali ya nchi maeneo ambayo yameharibiwa na mvua, ahsante sana. (Makofi)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ni miongoni mwa halmashauri ambazo zilielekezwa kuhamisha Makao yake Makuu ya halmashauri kutoka Mjini kwenda kwenye maeneo yake ya utawala, lakini kuna changamoto kubwa sana ya barabara haswa kwa wananchi wa Tarafa ya Bungu barabara ya kutoka Makuyuni Kwemshai na barabara ya Makuyuni, Zege Mpakayi.

Je, Serikali iko tayari sasa kuwa na mkakati maalum wa kusaidia uboreshaji wa miundimbinu ili wananchi hawa waweze kufika kiurahisi kwenye maeneo ya Makao ya halmashauri mpya zilizoanzishwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa kwanza nimpongeze kwa namna anavyohangaika na barabara za eneo lake na nimshukuru alinipa ushirikiano wa hali ya juu nilivyotembelea maeneo haya na maeneo mengine ambayo hakuyataja.

Mheshimiwa Naibu Spika, na niseme tu labda ni kwa kutoa kumbukumbu sahihi kwa mvua ambazo ambazo ziliathiri Mkoa wa Tanga zilikuwa ni kubwa sana kiasi kwamba urejeshaji wa maeneo ambao tumeyafanya hadi sasa tumetumia bilioni 7.8 kurejesha eneo la Tanga peke yake kwa mvua za mwezi Octoba peke yake na nikubaliane na yeye kwamba sasa tumefanya tena kwenye uratibu huu wa mvua zilizonyesha kuanzia Octoba kuja Januari kwa upande wa Tanga pia kumbukumbu kwamba kuna mahitaji makubwa ikiwepo maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge umeyataja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumetambua maeneo yote yenye shida hizi ikiwepo maeneo uliyoyataja na tunafanya utaratibu wa kuwa na fedha tena kama tulivyofanya Awamu ya I ya mvua za mwezi Octoba tutakwenda kufanya kazi kubwa kufanya marejesho ya maeneo haya ambayo nayataja kwa sababu nafahamu eneo la kwako pia ndiyo limekumbwa na maporomoko ya udongo wananchi wamepata athari kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunatambua hivyo na tutakuja kufanya uharaka wa kurejesha maeneo hayo uliyoyataja,ahsante sana.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona, kufuatia mvua kubwa ambazo zinaendelea kunyesha nchini kumekuwa na uharibifu mkubwa sana wa miundombinu jambo ambalo limesababisha vifo kwa baadhi ya wananchi na kudhorota kwa shughuli za kiuchumi na za kijamii.

Je, Serikali ina mkakati gani maalum wa kuhakikisha kwamba baraka hii ya mvua inakuwa fursa na chachu ya maendeleo na siyo majanga kama ilivyo sasa hivi kwenye nchi yetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunao utaratibu kawaida kama sehemu ya mkakati wa kushughulikia hali mvua zinavyokuwa nyingi, ndiyo maana katika bajeti ya mwaka huu unayoendelea kupitia Bunge lako Serikali ilitenga bilioni 8 zaidi ya bilioni 8 kwa ajili ya kumudu dharura zinavyojitokeza, kwa hiyo mkakati tuko nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mvua zimekuwa nyingi ndiyo maana tumeendelea kufanya utambuzi wa mahitaji hasa mvua zinavyoendelea, na hapa ninavyozungumza mpaka kufikia Januari tuna mahitaji ya shilingi bilioni 13.6 kwa ajili ya maeneo ya Mikoa 14 ambayo tumeitambua imekuwa na shida. Kwa hiyo, tunaendelea kupitia utaratibu wa kibajeti Serikali itafanya utaratibu wa kuona namna nzuri ya kutatua maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo mengine yatahitaji mvua ikipungua ndiyo tuende tufanye marekebisho makumbwa, sasa hivi TARURA kushirikiana na TANROAD tunafanya utaratibu wa ku-harmonize yaani kufanya kazi kwa pamoja ili kutengeneza barabara mbadala kwenye maeneo ambayo yana shida ili wananchi waendelee kupata huduma ya barabara mvua zikipungua tutarudi kufanya marejesho makubwa kwenye maeneo ambayo yamepata athari kubwa. Kwa hiyo, utaratibu upo wa kibajeti tutaendelea kuufuata kwa kuzingatia taratibu na sheria ili tuone tunafanya vizuri katika maeneo na kuwanusuru wananchi na hali hii ya mvua kubwa zilizoendelea kunyesha. Ahsante sana.
MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kule kwenye Jimbo langu kuna ujenzi wa barabara ya Ifakara – Kidatu. Barabara hii ilizinduliwa na Mheshimiwa Rais mwaka 2018 na akatoa ahadi kwamba mpaka mwaka huu mwezi wa Nne itakuwa imeshakamilika. Barabara hii mpaka hivi sasa imekamilika kwa asilimia takribani tano tu na bado mwezi mmoja mradi uweze kufungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kauli ya Serikali, ni kwa nini barabara hii imechukua muda mrefu hivi na ni lini itakamilika ili adha ya watu wa Kilombero iweze kwisha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara ya Kidatu - Ifakara ilianza kujengwa kwa kiwango cha lami na katika hatua za awali kumekuwa na kusuasua. Nami nimetembelea eneo hili, hata juzi RAS alitembelea eneo hili na kutoa maagizo makali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunafahamu changamoto zilizopo lakini hapo awali kulikuwa na changamoto ya masuala ya vifaa kwa maana ya zile excemptions. Tatizo hili lilishaisha na tumetoa maelekezo mkandarasi afanye kazi usiku na mchana ili kuweza kufidia muda ambao ulipotea wakati ule wa malumbano wa masuala ya VAT Excemption.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge wewe vuta subira, sisi tunaendelea kuisimamia kwa nguvu na utaona kwamba sasa kutakuwa na uhai mkubwa wa kuhakikisha barabara hii inajengwa na inakamilika na wananchi wanapata manufaa ya kuitumia barabara hii ikiwa katika kiwango cha lami. (Makofi)
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niulize, Serikali ina mpango gani kuhusiana na barabara za Mkoa wa Dar es Salaam hususan barabara ya Vingunguti - Liwiti ambapo kuna mradi mkubwa wa machinjio lakini barabara yake ni mbovu sana, ina mahandaki makubwa? Sasa Serikali ina mpango gani kuhusiana na hizo barabara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kama jana nilivyozungumza ni kwamba kati ya maeneo ambayo yamepata athari kubwa hasa kwa mvua za mwezi Oktoba na Novemba ni Mkoa wa Dar es Salaam. Nilisema kwamba katika hatua zile za awali, kama mkakati wa kunusuru hali ya uharibifu wa barabara katika Jiji ni pamoja na kupeleka fedha za dharura. Kwa hiyo, tulitumia takribani shilingi milioni 500 kurejesha maeneo ambayo yalikuwa yameharibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mvua zinaendelea kunyesha, bado uharibifu unaendelea kutokea. Nasi kama Serikali tunajipanga na kila wakati tumetoa maelekezo kwa Mameneja wa Mikoa, waendelee kutuletea hizo taarifa za uharibifu unaotokea ili tuendelee kufanya uratibu kwa sababu suala la kurejesha miundombinu hasa kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha ni endelevu. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana, watupe taarifa za maeneo ambayo yanaendelea kupata uharibifu na sisi tulivyojipanga tutaendelea kuwahudumia wananchi katika maeneo haya ili kwanza waweze kupita, lakini mvua zikipungua tutakuja na mkakati wa kuona tunafanya maboresho makubwa.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri alikuwa Mlalo mwezi wa 12 baada ya zile mvua kubwa ambazo zimesababisha mafuriko na maporomoko makubwa sana kule na ameona barabara ile na hali ilivyo. Je, anatupa majibu gani ya haraka kuhakikisha kwamba fedha zinapatikana na pia waongeze ujenzi angalau kwa kilometa 10 kila mwaka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; barabara ya kutoka Maramba kwenda Mnaro – Lunguza hadi Mnazi na yenyewe pia ni ni ya Wakala wa Barabara wa Mkoa. Halikadhalika, barabara ya kutoka Lukozi kwenda Mtae kupitia Manoro lakini pia kupitia Makose zote hizi ni barabara ambazo zinahudumiwa na Wakala wa Barabara wa Mkoa. Mpaka sasa hivi ninavyozungumza barabara hizi hazipitiki kwa maana kwamba wananchi wanapata, shida inabidi watumie usafiri wa bodaboda na kutembea kwa miguu. Serikali inatuhakikishia msaada gani wa haraka wa kuhakikisha kwamba barabara hizi zinapitika haraka inavyowezekana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza uniruhusu nitoe pole kwa Mheshimiwa Shangazi na wananchi wa Mlalo kwa sababu wakati ule wa mvua nyingi za mwezi wa kumi na mwezi wa kumi na moja tulipata maporomoko ya udongo ambayo pia yalisababisha vifo vya watu kama watano hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uniruhusu nimpongeze pia Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Shangazi kwa kweli ni mahiri kwa kushughulikia mambo na nafikiri wananchi wa Mlalo hawakufanya makosa kumchagua kwa sababu Mheshimiwa Shangazi utamuona anazungumzia juu ya barabara lakini sio barabara yake, amezungumza juu ya barabara ambazo zinaunganisha na maeneo mengine. Pia tumeona kwa umahiri wake hapa akishughulika na masuala ya michezo, wote tunafahamu. Mheshimiwa Shangazi pia ni coordinator mzuri kwenye upande wa chama, kwa hiyo, Mheshimiwa Shangazi nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lako la barabara ya Mlalo, nafahamu kwamba kwenye mafuriko yaliyotokea hata eneo kubwa la uchumi kwenye eneo lako la umwagiliaji kule Mlalo ulipata shida na barabara haipitiki na ndio maana nilitembelea maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Shangazi kwamba kwa jinsi nature ilivyo, tulikubaliana na tumetoa maelekezo kwamba angalau tuongeze kidogo kwenye bajeti zetu ndio mkakati wetu ili angalau maeneo yale yote yaliyo makorofi kama kilometa 10 hivi tuweze kuya-cover ili wananchi wasiendelee kupata shida tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuhakikishie tunajitahidi kadri tutakavyoweza kupata nafasi kwenye bajeti yetu tupatazame eneo hili ili wananchi wa eneo hili la Mlalo waweze kupata huduma vizuri na hasa ukianzia kule Mlalo kuelekea Lushoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kama nilivyosema Mheshimiwa Shangazi anafuatilia kuona wananchi wa Mlalo wanaweza kusafiri kwa vizuri kabisa kuja huku Lushoto lakini wanaweza wakasafiri vizuri kabisa kwenda kule Malamba na Same kupitia kule Bondeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Shangazi nikuhakikishie kwa wananchi wako wa Malamba, Lunguza, Mnazi, Lukozi, Manolo na hadi kule Mtai kwa jinsi tulivyoona hali ilivyo na tumetoa maelekezo kwa Meneja wa TANROAD Mkoa wa Tanga kwamba tuweze kuweka fungu la kutosha kwa sababu hizi barabara angalau tuziboreshe ili madaraja yaweze kukaa vizuri, tuweke changarawe katika maeneo haya ili barabara ikae vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Shangazi vuta subira tu kwa sababu maeneo haya yote nimeyatembelea, nitakuwa na umakini mkubwa kuhakikisha kwamba wakati tunaangalia bajeti yetu basi wananchi wa maeneo haya wanapitika vizuri. Kwa sababu kisera lazima tuhakikishe wananchi kwanza wanapita halafu tuendelee ku-deal na uboreshaji wa makalavati na madaraja ili wananchi hawa waweze kuwa supported kwenye hali ya uchumi katika eneo hili, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALHAJI ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana,kutokana na swali la msingi, barabara ya Korogwe – Magoma- Mashewa – Mtoni Mombo – Kibaoni – Kalahani – Maramba kwenda Tanga Mjini ina tatizo kama la Mlalo lakini barabara ile tatizo kubwa kuna makalavati madogo madogo ambayo mngeyafanyia haraka ili wananchi waweze kupita. Je, Wizara inatuamnia nini wale wananchi watoke kwenye kisiwa kilichopo sasa hivi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli maeneo haya Mheshimiwa Mbunge aliyoyataja yana changamoto, Mheshimiwa Bulembo nikuhakikishie kwamba nilivyofanya ziara maalum kuangalia maeneo ambayo yameathirika na mvua katika maeneo ya Mkoa wa Tanga nikianza kule Kilindi, nimekwenda Handeni lakini kwenye maeneo hayo umeyataja tumefanya ziara na Waheshimiwa Wabunge kwa hiyo nimeona. Na yale maeneo ambayo kimsingi yameharibiwa na yana nafasi ya kufanyiwa matengenezo kwa sababu yapo maeneo mengine ambayo bado maji yanapita kwa wingi sio rahisi kwa muda huu kufanya matengenezo makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa maeneo hayo tulitoa maelekezo kwa maana kwamba TANROADS na TARURA washirikiane maeneo ambayo tuliyaona kwamba kwa haraka waweze kuweka makalavati na maeneo hayo mengi mengine ujenzi umekwishafanyika. Lakini kwa maeneo ambayo changamoto zake zinahitaji utatuzi wake kufanyika baada ya mvua kukoma, haya nayo tunayaweka kwenye utaratibu kama nilivyozungumza tumeshayatambua, tunayatengea fedha. Tunawahakikishia wananchi kwamba wanapita kwenye maeneo yale.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge uvute subira tumetambua maeneo yote, tutaendelea kuyashughulikia kulingana na changamoto na hali ilivyo kutokana na sehemu mahsusi.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Tabora – Ipole – Koga – Inyonga kuelekea mpaka Mkoa wa Katavi kwa kipindi hiki cha mvua, barabara hii ni mbaya na haipitiki. Na wiki moja iliyopita daraja la Koga lilifungwa kwa hiyo ikasababisha wananchi wa Mkoa wa Katavi wakaanza kuzunguka kutoka Mpanda kuelekea Kigoma na kwenda mikoa mingine.

Je, Serikali hii ya Awamu ya Tano inajipangaje kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa barabara hii wenye kilometa 359 ili wananchi hawa wa Mkoa wa Katavi waepukane na usumbufu na gharama ambazo wanazipata. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba ni muda mrefu fursa ya kutengeneza barabara ya lami kutokea Tabora kwenda Mpanda haikuwepo. Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba zipo kandarasi kubwa pale zinaendelea, mradi wa kilometa 103,
kilometa 105 na kilometa 108 unafahamu na kwamba makandarasi waliopo hapo wana uwezo mkubwa hata kasi ya utengenezaji wa barabara upo mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu ushoroba ule kwa maana ya ukanda ule tunautazama kwa macho mawili ndio maana tumeweza kuweka fedha nyingi. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa msukumo mkubwa, ujenzi unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za mvua hatuwezi kuzikwepa, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana na mimi kwamba kwenye Mto Koga, ule mto ni mkubwa sana na tunapopata mvua nyingi, miaka mingi iliyopita tumekuwa na shida hiyo na hata hivyo tulikuwa tumetoa maelekezo kwa makandarasi kwamba wanavyoanza kufanya ujenzi waanze kushughulikia sehemu ambazo zina changamoto, ni kitu ambacho kinaendelea kufanyika lakini kwa sababu ya nature ya mvua kuwa nyingi, tulilazimika kuifunga ile barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge mkakati mkubwa wa kuunganisha Mkoa wa Katavi na mikoa mingine unafanyika kwa Serikali ya Awamu ya Tano unafahamu kwamba ipo barabara ile ukitoka Mpanda kwenda kule Malagarasi ujenzi unaendelea na unafahamu tumeshaunganisha vizuri na Rukwa na unafahamu upo mpango wa kujenga barabara kutoka maeneo ya Stalike kwenda Kizi kule unafahamu.

Kwa hiyo, niseme katika Mkoa wa Katavi miradi mikubwa sana ipo kuhakikisha kwamba mkoa huu unaunganishwa na mikoa mingine kama ilivyofanyika kwenye mikoa mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge wakati huu wa mvua tuvumiliane na tuendelee kumuomba Mungu atupe mvua zenye heri ili adha kubwa ambayo wananchi wanaipata tuweze kuondokana nayo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza Mji wa Korogwe upo bondeni, mvua zote ambazo zinanyesha kuanzia vuli hadi sasa masika zimeendelea kuathiri sana miundombinu iliyopo kwenye mji ule. Na mara nyingi nikiiomba Serikali kwamba kama inawezekana ni vizuri tukatengewa fedha za kutosha ili tuweze kujenga mifereji ambayo itasaidia kupunguza kasi ya uharibifu wa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, sasa mtakuwa tayari angalau kuweza kuwa mnatutengea fedha ziweze kujenga mifereji wakati tukiendelea kusubiri barabara za lami ambazo Serikali imeendelea kutupa angalau kwa kidogo kidogo ili kupunguza hata hiyo gharama ambayo kila mwaka mnatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za changarawe, nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Chatanda kwa kufuatilia mambo ya Mji wa Korogwe. Na ninafahamu Mheshimiwa Chatanda utakubaliana na mimi, zipo barabara za lami ambazo zimejengwa pale mjini ni matokeo ya ufuatiliaji wako, kwa hiyo nakupongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kudhibiti maji ya mvua kwenye barabara zetu, tunafahamu pia kwamba maji yasipodhibitiwa ni adui mkubwa wa barabara; kwa hiyo, maji yasipodhibitiwa unakuta barabara zetu hizi zinazojengwa zinaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge tumeshatoa maelekezo kwamba wenzetu upande wa TARURA, TANROADS lakini na wenzetu upande wa halmashauri zetu watu wa mipango miji na afya tushirikiane kuona kwamba tunakuja kuwa na mipango mizuri ya kuhakikisha kwamba maji ya mvua tunaya-control vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu muda mwingi nimekuwepo Tanga na niseme kwamba kati ya mikoa ambayo mwaka huu imeshambuliwa sana na maji ya mvua, kati ya mikoa hiyo Mkoa wa Tanga. Na tumetoa maelekezo pia kwa wenzetu upande wa TANROADS kwamba katika katika bajeti hii inayokuja, mikoa ambayo tunaiona imekuwa na nature ya uharibifu mkubwa wakati wa mvua tuitazame kwa macho mawili ikiwemo Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Chatanda uvute subira, mimi na wewe tutakuwa bega kwa bega kuhakikisha mipango inakuwa mizuri ya kuwa na ubora wa miundombinu katika Mji wa Korogwe. Lakini pia kuhakikisha kwamba angalau tunapata allocation nzuri kwa sababu kibajeti hali sio nzuri lakini tutahakikisha tunaweka vipaumbele kwenye maeneo ambayo tumeona yamekuwa na shida. Kwa hiyo, vuta subira, ahsante sana. (Makofi)
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi lilikuwa linazungumzia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami. Mheshimiwa Waziri ningependa kujua sasa kwa sababu tunayo barabara yetu ya kutoka Isandula inayopita Mkalama na kwenda Ngudu mpaka Hungumalo. Ningependa kujua sasa ni lini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami ili kuchachua maendeleo na uchumi katika Mji wa Ngudu.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara yangu imeshakamilisha usanifu wa awali na upembuzi yakinifu wa barabara hii muhimu ambayo Mheshimiwa Mbunge anaitaja. Barabara hii inapita kwenye Majimbo matatu kama alivyozungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie Mheshimiwa Ndassa baada ya kukamilisha zoezi hili ambalo barabara hii ina urefu wa kama kilometa 60 hivi na kidogo ambayo inaanzia kule Isandula, inakuja Ngudu, Nyaminama inapita Mabuki hadi kule Hungumalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa vile tumeshamaliza zoezi la usanifu na kutambua gharama za barabara hii, tunajipanga tukipata fedha nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa eneo lako hili kwamba tutaanza ujenzi wa barabara ya lami. Tunajua inapita katika maeneo ambayo ina uchumi mkubwa, ahsante sana.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona, mvua zinazoendelea kunyesha nchini kote zimeleta madhara makubwa Mkoani kwangu Singida na kusababisha barabara inayoanzia Mjini Singida – Ninyuhe hadi Iyumbu yenye urefu wa kilomita 115 madaraja kukatika na kusitisha shughuli zote za kiuchumi kwa wananchi wa Jimbo la Singida Magharibi. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami na kurekebisha miundombinu ya barabara hii, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara hii ambayo inapita maeneo ya Ngungila inakwenda kule Iyumbu ni barabara ambayo imepita kwenye bonde kubwa ambalo wananchi wa maeneo haya wanategemea sana uzalishaji wa mpunga. Kwa hiyo, tunafahamu kama Serikali lakini niseme hatua kubwa ambazo tumezichukua kazi iliyokuwa inaendelea ni pamoja na kujenga madaraja na makalavati katika eneo hili la Ngungila ili wananchi waweze kupita pamoja na kujaza vifusi kufanya barabara iwe juu katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatambua umuhimu wa barabara hii na tumeona uharibifu uliotokea kutokana na mvua. Lakini namuomba anikubalie kwamba hatua ya kwanza ni ya kuboresha barabara hii ili wananchi waweze kupita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile hatua ya kujenga kwa barabara hii kwa kiwango cha lami itafanyika baadaye lakini Mheshimiwa Mbunge unafahamu barabara hii itaunganishwa na barabara ile ya kutoka Sabasaba inapita Sepuka – Ndago inaenda kutoka Kizaga. Kwa maana hiyo tutakuwa tumeipunguza sana barabara hii kwa kiu yako ya kuijenga barabara kiwango cha lami tutaizingatia baada ya barabara hii niliyoitaja kuwa imekamilishwa. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kama alivyosema kwenye jibu lake la msingi kuna kiasi cha fedha kimetengwa katika bajeti ya 2019/2020; na kwa kuwa, barabara iliyojengwa kwa sasa imeishia Mnivata na kutoka Mnivata hadi Nanyamba ni kilometa 20; na kwa kuwa, kuna mkandarasi yuko pale.

Je, ni kwa nini sasa, bila kuathiri taratibu za manunuzi, kipande hicho asingepewa mkandarasi ili ajenge kwa kiwango cha lami hadi Nanyamba Mjini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Barabara ya Mtwara – Nanyamba – Masasi kuna barabara pacha tunaita Barabara ya Ulinzi ambayo inakwenda mpaka Mahurunga, Kitaya, Mnongodi na Michenjele. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami, ukizingatia sasa hivi kuna changamoto ya kiulinzi kati ya Tanzania na Msumbiji?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chikota, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza uniruhusu nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Chikota kwa ushirikiano. Kwa kweli, mara zote nimefanya ziara mara nyingi sana kukagua barabara hii Mtwara – Mnivata, lakini muda wote Mheshimiwa Chikota alikuwepo na tumefanya kazi kwa pamoja. Kwa hiyo, Mheshimiwa Chikota namshukuru sana.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kama ambavyo nimetoa jibu langu la msingi kwamba, harakati za ujenzi kwa maana ya shughuli za manunuzi zinaendelea ili kujenga kilometa 160 ambazo zimebakia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Chikota anafikiria kwamba, ili twende haraka ni kumruhusu mkandarasi aendelee kwa vile tulivyotenga fedha kidogo, lakini nimwombe Mheshimiwa Chikota avute subira na sisi mpango wetu ni kuhakikisha kwamba, tunafanya ujenzi wa haraka, ili wananchi wake kwenye Vijiji vya Malanje, Mnivata, Nanyamba, Mtimbwilimbwi, Mbambakofi, Mtopwa na majirani wa Tandahimba, Newala na kule Lulindi na Masasi waweze kupata huduma hii nzuri ya barabara.

Kwa hiyo, avute subira kwa sababu ziko taratibu za manunuzi zinafuatwa, sasa mkandarasi huyu kama ataomba na atakuwa na sifa basi anaweza akapewa, ili aanze kukamilisha upande ambao ameutaja.

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara pacha, hii barabara ya ulinzi kilometa 310; nimeitembelea baadhi ya maeneo katika sehemu hii ili kuona kwamba, tunafanya maboresho makubwa katika maeneo ambayo ni korofi, maeneo ambayo yanahitaji madaraja na makalavati. Kwa hiyo, cha kwanza ni kuhakikisha kwamba, tunaifanyia maboresho makubwa barabara hii kuhakikisha inapitika, kwa sababu ni muhimu sana katika shughuli za uchumi, lakini na za ulinzi.

Mheshimiwa Spika, sasa tutakwenda kwa kufuata vipaumbele. Tukimaliza barabara hii ambayo nimeitaja tutakwenda kuitazama sasa Barabara ya Ulinzi, ili iweze kuwasaidia wananchi wanaoishi maeneo haya. Ahsante sana.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika, naishukuru tena Wizara kwa kazi kubwa inayofanyika hasa kwa kukamilisha Daraja la Sibiti. Napenda kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, Wizara ipo tayari kujenga kilometa 40 kutoka Iguguno mpaka Nduguti kabla ya barabara yoyote ile kukamilika kwa sababu shughuli nyingi zinafanyika sasa pale makao makuu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu barabara hiyo sasa ni barabara ya kiuchumi na magari mengi yanapita huko. Je, Naibu Waziri yuko tayari kufuatana na mimi baada ya Bunge hili ili akaone umuhimu wa uwekaji wa lami katika barabara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika jibu la msingi kwamba juhudi kubwa zinafanyika kuunganisha mikoa. Hata hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Kiula tumefanya juhudi za makusudi kuhakikisha kwamba barabara hii aliyoitaja kutoka Iguguno – Nduguti - Igumanga kwenda mpaka Sibiti imekuwa bora na hata kufanya ujenzi wa madaraja makubwa.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Kiula kwa sababu tumejenga daraja kubwa pale Mnolo ni kwa sababu ya juhudi zake pia na ushirikiano anaoutoa. Kwa hiyo, tutaendelea kufanya hivyo kuhakikisha maeneo mengi yamekuwa bora na yanapitika halafu kidogokidogo mbele ya safari tutakuwa na harakati ya kujenga barabara kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu kuambatana na Mheshimiwa Kiula, Mheshimiwa Kiula anafahamu ipo miradi mingi inayofanyika katika eneo lake ikiwepo kwenye Daraja la Msingi kuna ujenzi mkubwa unaendelea vizuri na miradi mingine mingi ipo na ipo sababu pia ya kutembelea Mkalama. Nitatembelea huko ili tuweze kuona pia miradi mingine inakamilishwa kwa ubora mkubwa. Ahsante sana.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, sambamba na ujenzi wa barabara za lami, Mkoa wa Tabora sasa hivi tuna matatizo makubwa ya mafuriko. Mafuriko ni makubwa, naomba Serikali itambue kwamba Tabora nayo ni miongoni mwa mikoa yenye mafuriko.

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Tabora Manispaa, Kata ya Ipuli ambayo tunaitwa Freemason au Chuo cha Utalii pamoja na Malolo wananchi mpaka sasa wako nje, wanateseka kutokana na kutokuwa na miundombinu ya mifereji inayopitisha maji mengi. Mifereji iliyopo ni midogo mno, nimeomba univumilie kwa sababu hali tuliyonayo sasa wananchi wote wa Mkoa wa Tabora hususan Manispaa wana matatizo makubwa.

Mheshimiwa Spika, nimuombe sasa Mheshimiwa Naibu Waziri aende Tabora akutane na Wahandisi wa TANROADS pamoja na TARURA ili watafute njia gani mbadala ya kuwasaidia wakazi wa maeneo hayo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwanne Mchemba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimwa Mbunge maeneo mengi tumepata adha ya hizi mvua kubwa ambazo zinaendelea kunyesha. Nitumie nafasi hii nimpe pole Mheshimiwa Mbunge lakini pia niwape pole wananchi wa Tabora Mjini. Natambua maeneo haya uliyoyazungumza ya Ipuli na Malolo kuna shida na nakubaliana na ushauri wako.

Tunaendelea kufanya uratibu wa maeneo yote nchini kuhakikisha kwamba tunafanya maboresho.

Mheshimiwa Spika, nitoe wito kama nilivyozungumza hivi karibuni wakati nikijibu swali la Korogwe Mjini tuwe na ushirikiano kama Mbunge unavyosema wenzetu wa TARURA na TANROADS na upande wa Mipango Miji tushirikiane ili miji yetu hii inayokua kwa kasi lazima tuje na mipango mizuri ya kudhibiti maji ya mvua hususan tunapopata mvua nyingi namna hiyo. Kwa hiyo, nakubaliana na ushauri wako nitakwenda Tabora kufanya hivyo kama ulivyoshauri.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuishukuru Serikali kwa niaba ya wananchi wa Kata za Kalela, Kwaga, Lusesa, Kasangezi, Muzi pamoja na Bugaga kwa kweli barabara ya kutoka Kidahwe - Kasulu sasa ni lami. Wananchi hawa tangu uhuru sasa wamepata barabara ya lami na wana furaha kubwa sana wanaishukuru Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, nini kauli ya Serikali kuhusu barabara ya kutoka Kasulu - Uvinza ukizingatia wananchi wa Kata za Lungwe Mpya na Asante Nyerere na maeneo mengine wanapata tabu sana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nini mipango ya Serikali kuhusu barabara ya kutoka Kitanga - Kibondo ukizingatia wananchi wa Kata za Kitanga, Kigabye na maeneo ya jirani wanapata tabu sana wanapoenda Kibondo? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vuma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Vuma kwa umahiri wake, najua anawapigania sana wananchi wake.

Mheshimiwa Spika, kuhusu maswali yake niseme kwamba tunazitazama hizi barabara alizozitaja lakini kwa sababu tumekuwa na changamoto ya ujenzi wa barabara za lami hususan kuunganisha Mkoa wa Kigoma, naomba wananchi hawa watuvumilie. Hata hivyo, niseme tu hii barabara ya kutoka Kasulu kwenda Uvinza kwa maana inaanzia pale Kanyani kwenda Kibaoni kilometa 53 tunajitahidi kuiweka barabara hiyo katika hali nzuri. Niwahakikishie wananchi wa maeneo haya ikiwemo wananchi wa Nguruka wataweza kupita vizuri.

Mheshimiwa Spika, tukikamilisha ujenzi wa barabara hii kubwa ambayo nimeitaja kwenye jibu la msingi, tutatazama namna nzuri ya kufanya ili tuone tunafanya maboresho makubwa kwenye barabara hii. Hii ni pamoja na kuiangalia kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara yake ya pili hii aliyoitaja kutoka Kitanga kwenda Kibondo ni barabara ambayo inasimamiwa na TANROADS, Mkoa wa Kigoma na ipo katika hali nzuri. Niseme tu kuna changamoto katika Daraja hili la Mto Malagarasi, eneo hili ndiyo wananchi wanapata shida kuvuka kwenda Kibondo. Nimhakikishie Mheshimiwa Vuma na wananchi wa maeneo haya kwamba mara baada ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami, lipo daraja la chuma katika Mto Malagarasi, tutaangalia uwezekano wa daraja hili kulihamishia kwenye maeneo haya ili wananchi wa Kitanga waweze kupita kwenda Kibondo bila matatizo yoyote. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika kusema kwamba silizishwi na majibu ya Mheshimiwa Waziri. Toka nimekuja katika Bunge hili nimeshazungumzia hili suala la uwanja wa ndege wa Mkoa wa Mara, mara kwa mara. Majibu ya Waziri ukizingatia Mkoa wa Mara una vivutio vingi sana vya utalii. Kwanza tuna mbuga, ya wanyama ya Serengeti, pia tuna kivutio cha Kumbukumbu ya Baba wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni umuhimu wa kujenga uwanja ule au kuupanua uwanja ule ukawa uwanja ambao utaleta watalii wengi katika Mkoa wa Mara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba comentiment ya Serikali, Je ni lini uwanja ule utakamilishwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na malipo ya wananchi wale wananchi wanazunguka eneo lile na uwanja wa ndege zile nyumba zilishawekewa X muda mrefu sana. Takribani sasa hivi ni mwaka mmoja na nusu au miaka miwili. Wale wananchi wanaishi kwa wasiwasi hawajawahi kulipwa hata senti tano, mpaka imeshasababishia baadhi ya wananchi wameshakufa.

Je, serikali itawalipa lini wananchi wale ili waendelee kuwa na maisha yao bila wasiwasi kusema kwamba ni lini watalipwa. Kwa sababu wale wananchi hawakopesheki. Ahsante nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, ni kweli zoezi la kufanya ujezi wa uwanja huu tumekuwa tukiendelea nao kwa muda. Lakini Mheshimiwa Mbunge nikufahamishe kwamba hatua nzuri zimefanyika, kwa sababu pale awali wananchi ambao walikuwa imeonyesha watalipwa fidia walikuwa wapo wengi gharama zilikuwa kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuishukuru uongozi wa mkoa na mwandisi mkoa wa Mara. Kwamba kazi kubwa iliyofanyika kuendelea kutambua upya wananchi watakaohitajika kulipwa fidia na zoezi hili lilikamilishwa Mheshimiwa. Tumeokoa kama bilioni 10 hivi, hii ni kazi kubwa imefanyika.

Kwa hiyo, ninawapongeza sana lakini nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge wananchi 135 watalipwa fidia kwa sababu tumeshawatambua baada ya kufanya mapitio wananchi hawa wanatoka katika Kata Nyasho, niwahakikishie wananchi 97 watalipwa, wananchi wa Kata ya Kamnyonge wananchi 38 watalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ime-indicate kwamba bilioni 4.319 zitalipwa kwa wananchi hawa. Kwa hiyo, wavute subra kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi kwamba ni lazima kwanza wananchi tuwalipe ili tuweze kupeleka huduma katika eneo hili.

Kama alivyosema mwenyewe anatambua record zinaonesha 95% ya matumizi ya uwanja ni wale watu wanaokuja kwa ajili ya utalii. Serikali inatambua hivyo na watalii wengi kutoka Kenya, kutoka Uganda wanatumia uwanja huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua ndio maana Serikali imefanya juhudi kubwa kuhakikisha kwamba uwanja huu tunaupanua tunauweka ukae vizuri ili huduma iwe kubwa zaidi katika eneo hili. Kwa hiyo, tunakuomba uvute subra kazi nzuri Serikali ya Awamu ya Tano inafanya na uwanja huu tutakwenda kuujenga na utatumika kwa wananchi na watalii pia.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja dogo la nyongeza lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii katika suala la usanifu na upembuzi wakina sasa hivi limechukua miaka nane. Sasa swali langu ni kwa nini Serikali inachukua muda mrefu kiasi hiki kwa ajili ya kufanya tu usanifu na upembuzi wa kina?

(b) Barabara hii imebeba uzito mkubwa sana katika kuharakisha shughuli za kiuchumi ili tuweze kufikia uchumi wa kati itakapofika mwaka 2025. Lakini kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri kwamba upembuzi yakinifu unaendelea na usanifu mpaka inakapofika Juni, 2020 ninapata mashaka kwamba huenda hii barabara ikaendelea kuchelewa ziadi.

Je, Serikali haioni kwamba kutoleta maendeleo au kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami ambayo inapita katika kata zifuatazo zinazoendelea kujishughulikisha katika shughuli za uchumi ikiwa pamoja na makaa ya mawe yanayochimbwa huko? Lakini pia shamba kubwa la miwa linaloenda kuanzishwa huko. Na kata hizo ningependa nizitaje, ni kata ya Likuyufusi, Litapwasi, Ndogosi, Muhukulu lilayi na Muhukulu barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa serikali itakwenda kuanza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza uniruhusu nitumie nafasi hii nishukuru kwa swali nzuri lakini niseme tu, eneo hili la Likuyufusi barabara hii ya Likuyufusi Mkenda ni barabara ambayo inagusa majimbo mawili; Jimbo la Peramiho kwa Mheshimiwa Jenista Mhagama, lakini pia inawahudumia kwa kiasi kikubwa wananchi wa jimbo la Nyasa. Ambapo kuna kazi kubwa imefanyika kwa sababu barabara hii ina wapunguzia adha wananchi wa kata hii ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwa juhudi ambazo zinafanyika na kwa ushirikiano mkubwa kwa Mheshimiwa Jacqueline na Wabunge wa majimbo inayofanyika, barabara hii ipo katika ubora kwa kuzingatia mahitaji ambayo nimeyata. Tunatambua kwamba ili tuweze kujenga uchumi ni lazima miundombinu iwe bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetembelea na nimejionea namna ambavyo Waheshimiwa Wabunge hawa akinamama, na niseme Wabunge wakinamama kazi nzuri wanafanya. Nimekwenda kule nimeona kule Mitomoni kuna MV Stella inasaidia wananchi wale kuvuka ili watumie barabara hii ambayo kwa kiasi kikubwa tumeiboresha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga vizuri. Wakati harakati za kujenga barabara ya lami zinafanyika, tunazingatia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha barabara hii inakuwa bora. Yako maeneo ambayo tumeweka madaraja ya chuma, yako maeneo tumeelekeza ili wakati huu tunafanya harakati za kuhuisha kujua gharama halisi za ujenzi wa barabara za lami, barabara hii inakuwa bora na makaa ya mawe yanabebwa, hata mwekezaji anaendelea na harakati zake za uwekezaji wa kiwanda cha sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga vizuri, tutawa-support wananchi wa maeneo haya ya Peramiho, wananchi wa Kata alizozitaja ili nao waende katika harakati; hatupendi tukifika uchumi wa kati wawe chini ya mstari ule wa wastani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, tumejipanga vizuri kwenda kuiboresha barabara hii. Waheshimiwa Wabunge wa maeneo hayo; Mheshimiwa Mhagama na Mheshimiwa Manyanya, tumejipanga vizuri, vuteni subira, muwe comfortable, tutaenda kuijenga barabara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekwenda Mkenda nimeona pia kuna soko zuri, nimeona wananchi wa kule Msumbiji wana mahitaji makubwa ya mahindi ambayo yanazalishwa upande wa Peramiho. Kwa hiyo, tunatambua umuhimu huo wa kufanya maboresho ili wananchi hawa waweze kupata manufaa makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake lakini nimfahamishe tu kwamba miaka mitatu iliyopita wananchi wa maeneo ya Mruki, Hangoni, Sinai pamoja na Kwere walizuiwa na Halmashauri kuendelea kuendeleza maeneo yao yaliyohisiwa kwamba ndiko barabara itakapopita wakiwa wamefanyiwa tathimini nakuhadiwa fidia. Je, kwa kauli ya Serikali sasa wananchi hawa wanaruhusiwa kuendelea na majukumu yao ya kuendeleza maeneo yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa majibu ya Serikali pia hayajatoa time frame yaaani lini sasa upembuzi huo wa kina utakamilika. Je, Serikali iko tayari kusema ni lini upembuzi utaanza na kukamilika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze tu Mheshimiwa Mbunge Mahawe kwa sababu amekuwa akifuatilia sana juu ya maendeleo ya Babati na Manyara kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Halmashauri kuwazuia wananchi au kuwaelekeza wananchi kwa vyovyote vile haikuwa sahihi sana kwa sababu ilitakiwa Mamlaka inayohusika na ujenzi wa barabara ifanye hivyo. Kwa hiyo, niwaombe mahali popote kutakapokuwa na miradi ya barabara tusubiri kupata kauli ya Mamlaka halisi ili tusiweze kuwachanganya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya usanifu inaendelea sasa hivi kuanzia tarehe 01 Julai, 2019 kazi hiyo imeanza na wakati wowote tutapata inspection report, kwa maana ya report ya awali itakapokuwa imepatikana tutaweza kufanya sasa maamuzi, kwa sababu tutakuja na altenative kama tatu, halafu Serikali iamue tuende hatua ya mwisho sasa ya kukamilisha michoro pamoja na kuona kwamba tunapata gharama halisi za kuwafidia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo uvute subira kazi inaendelea na ninalishukuru sana Bunge lako limetupitishia fedha kwa ajili ya kazi hii ya usanifu wa hii barabara na kwamba kazi itaisha haraka sana, katika mwaka huu wa fedha kwa sababu fedha tunazo na kazi inaendelea itakamilika, gharama zitajulikana na wananchi tutawajulisha wale watakaopitiwa na mradi na Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tuko pamoja hapa taarifa hizi za kuhusu wananchi ni wepi watapitiwa na mradi ili tuweze kuwalipa fidia tutaweza kuwasiliana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika kuboresha miundombinu ya barabara, lakini kipo kipande cha barabara kutoka eneo la Rusaunga kuelekea Rusumo mpakani barabara inayoelekea Rwanda kimeharibika kuna mashimo utafikiri ni mahandaki, hii inapelekea magari kuharibika na kusababisha ajali zisizo za lazima. Magari sasa yanachepuka kupitia barabara ya Rusaunga, Rurenge, Mrugarama ambayo ni ya vumbi na hivyo kuendelea kusababisha uharibifu kwenye barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini commitment ya Serikali katika kuhakikisha kwamba barabara hii inatengenezwa kwa kiwango kinachostahili ukizingatia kwamba ni barabara ya kiuchumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara hii kutoka Rusaunga kwenda Rusumo kilomita 92 ni barabara ambayo imechoka imechakaa ina mashimo, ina mahandaki na imekuwepo kwa miaka mingi sana ni zaidi ya miaka 34 na Serikali imekuwa ikifanya juhudi ya kuiboresha barabara hii kwa sababu imejengwa muda mrefu kutoka Isaka kwenda Rusumo, kwa sehemu kubwa ya barabara hii matengenezo yamekuwa yakifanyika tumebakiza hizo kilomita 92.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote katika Mkoa huu wa Kagera kwamba tumetenga fedha kwenye Bunge hili la kuifanyia matengenezo upya barabara hii, lakini kwa hatua za awali kuboresha haya mahandaki ambayo Mheshimiwa Mbunge anayaita kuna fedha tayari Serikali imeshatoa na tulikuwa tunakamilisha hatua za manunuzi, mkandarasi ameshapatikana tutaanza kwanza kuboresha ili kuyapunguza haya mashimo Mheshimiwa Mbunge, tutayapunguza wakati harakati zile za kuanza mradi mkubwa wa kuboresha barabara hii haya mashimo tutakuwa tumeyaondoa.(Makofi)
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu baada ya kupiga kelele hatimae kuna kila dalili za kujengwa barabara ya Pangani. Nataka kujua sasa je, wale wananchi ambao walielezwa kwamba wasiendeleze mashamba na majengo waliyoko pembezoni mwa barabara, ni lini wataanza kulipwa fidia zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejipanga vizuri kujenga barabara hii ya Tanga - Pangani kama Mheshimiwa Mbunge ulivyosema, lakini ni utaratibu wa Serikali ni kulipa fidia kwanza kabla ya ujenzi kuanza, kwa vile Mkandarasi ameshapatikana niwahakikishie tu wakazi wa maeneo haya ambao mradi utapita watalipwa fidia yao mara moja. (Makofi)
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali kwa kutupa barabara nzuri ya kutoka Ndono mpaka Urambo na inakatisha mpaka katikati ya Mji, naishukuru sana Serikali kwa niaba ya wananchi wa Urambo. Swali ni kwamba ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja kuangalia round about ambayo wameiweka pale inasababisha ajali kwa jinsi ambavyo kona iliyopo ni kali sana, magari yanapata ajali, watu wanapata ajali. Kwa heshima na taadhima naomba kujua ni lini Serikali itakuja kutusaidia round about ya Urambo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisha kwenda Urambo lakini nitakwenda tena kwa sababu nafikiri kuliwa na zoezi hili la kuangalia sehemu bora zaidi ya kufanya marekebisho kuweka round about katika Mji ule. Kwa hiyo, Mama yangu nikuhakikishe kwamba tutakwenda lakini wataalam wanaendelea kukamilisha ili kuona ni wapi patafaa vizuri ili tuweze kuweka huo mzunguko. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Swali la kwanza napenda niipongeze Serikali kwa kusikia kilio chetu Wabunge na kilio cha wananchi sasa wameanza kufanya tathmini ya barabara ya Kirwa Road kutoka eneo la Mbagala Kokoto kwenda Kongowe, eneo ambalo lilikuwa na msongamano mkubwa wa magari naiopongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kusikia kilio chetu Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wa eneo la Mbagala Kokoto mpaka Kongowe wameanza sasa kufanyiwa tathmini ya maeneo yao na kuwekewa alama ya X. Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kwamba wananchi hawa watalipwa kwa wakati ili kupisha zoezi hilo la upanuzi wa barabara ya Kirwa Road. Ahsante sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mbunge najua tumezungumza miradi mingi sana na anafahamu juhudi ambazo zinafanyika ndiyo maana anatoa pongezi, kwa niaba ya Serikali nazipokea pongezi hizo.

Mhehimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga kuboresha barabara hii ili kuweza kupunguza pia msongamano ambao unajitokeza na usumbufu ambao unajitokeza, nami eneo hili nimelitembelea. Vile vile niwahakikishie tu wananchi hawa kwamba tumejipanga vizuri kwa sababu hata kwenye bajeti tuna fedha kwa ajili ya kuendeleza maendeleo ya maeneo haya na kulipa fidia, tutawalipa mara moja wakati tukiendelea kuboresha mradi huu. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuwa barabara ya Karatu - Mang’ola katika Mkoa wa Arusha imekuwa ikitengenezwa mara kwa mara na kuisababishia Serikali gharama kubwa. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami kwa sababu eneo la Mang’ola ndilo linalotegemewa kwa uchumi wa Karatu kwa sababu lina ulimaji Mkubwa wa zao la vitunguu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejipanga vizuri kuijenga barabara hii. Barabara hii ni muhimu inaunganisha Mkoa wa Arusha pamoja na Mikoa mingine Ukanda wa Ziwa, kwa hiyo, tuko katika hatua za mwisho kwa sababu kazi ya kufanya usanifu katika barabara hii ilishafanyika tunafanya review na mara tu tutakapopata fedha barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa changamoto iliyopo katika Bypass ya Babati inafanana kabisa na katika Jimbo letu la Iringa Mjini ambako Serikali imeshabomoa makazi ya watu lakini ujenzi haujaanza. Je, Serikali itaanza lini ujenzi huo ili kupunguza adha kubwa kabisa wanayopata wananchi kwenda katika stendi mpya ya Igumbilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejipanga kuijenga barabara hiyo ni kilomita Saba na katika bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha kuanza ujenzi wa barabara hiyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Ritta Kabati ninakupongeza tu unafuatilia sana barabara hii lakini nikuhakikishie pia kwamba tumejipanga vizuri tunajua usumbufu wananchi wa Iringa Mjini wanaopata wa magari makubwa yanayopita katika ya Mji, kwa hiyo ujenzi wa barabara hii utaanza tu mara moja kwa sababu tumeshajipanga vizuri na tutaendelea kutoa feedback. (Makofi)
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante pamoja na changamoto za kulipa fidia wananchi katika Taifa hili lakini Mkoa wa Katavi katika barabara ya kutoka Sumbawanga kuelekea Kigoma wakazi wa Kata ya Mpanda hoteli Misukumilo pamoja na Ilembo pamoja na Milala walirukwa katika masuala ya fidia mpaka sasa ni mwaka wa nne hawajalipwa pesa hizo. Je, ni kwanini Serikali mnawazungusha kuwalipa watu hawa ambao walitumia gharama kubwa kujenga nyumba zao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa ujumla hii Serikali hii inawajali sana wananchi wake na hakuna sababu ya kutokumlipa mwananchi haki yake. Kwa hiyo, naomba tu nilichukuwe hili kama ni suala mahususi ili nilifuatilie nione nini kilitokea kwa sababu ni nia ya Serikali kuwahudumia vema wananchi na kuwalipa haki zao kwa hiyo, tutalifuatilia suala hili.
MHE. BONAH KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Mheshimiwa Waziri Serikali ina mpango gani kuhusiana na Barabara ya Kimanga, kwa sababu last time Naibu Waziri alienda kufanya ziara lakini ile barabara mpaka sasa hivi imeachwa kutengenezwa. Pia nauliza kuhusiana na daraja la Segerea Seminari ambalo limechukuliwa na maji tangu mwaka 2012 lakini pia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais mpaka leo halijatengenezwa ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu anapigania sana barabara za eneo la jimbo lake. Lakini niseme tu ile barabara ya Kimanga kulikuwa na mradi unaendelea nitafuata tu ufuatiliaji nione nini kimetokea kama ule mradi unasua sua na tutawasiliana na Mheshimiwa Mbunge tukatembelee mradi tuone changamoto iliyokuwepo ili tuweze kuitatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu lile daraja la upande ule wa Seminari, nilitembelea eneo hili tunahitaji kuweka daraja kubwa pale, Serikali bado inajipanga kutafuta fedha za kutosha hili tuweze kuboresha katika eneo hili. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba uvute Subira tutajipanga vizuri tutaporesha eneo hili kwa sababu linahitaji fedha nyingi ili kuweza kuboresha mahali hapa ambapo ni sehemu korofi ahsante sana.
MHE. MWIGULU L. NCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujenzi wa barabara ya Singida, Sepuka, Ndago, Kizaga kwa kiwango cha lami ni ahadi ya Mheshimiwa Rais na ipo kwenye ilani ya uchaguzi ukurasa wa 56. Kwa kuwa upembuzi yakinifu katika barabara hii ulishafanyika na Mheshimiwa Naibu Waziri alishafanya ziara kukagua masuala yote katika barabara hiyo ni lini sasa ujenzi kwa kiwango cha lami utaanza katika barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mbunge nakupongeza sana kwa sababu nimefuatilia kweli barabara hii muhimu na niseme tu ni mwaka wa fedha uliopita ndiyo tulikuwa tunaendelea kufanya kazi ya usanifu wa kina kwa ajili ya Ujenzi wa lami wa barabara hii. Mheshimiwa Mbunge vuta subira kwa sababu tunakwenda kwa hatua baada ya kukamilisha hili zoezi ambalo tulikuwa tunalifanya sasa tunatafuta fedha ili tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami barabara hii muhimu.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kata hizi alizozitaja Mheshimiwa Dkt. David Mathayo ni Kata ambazo ziko kwenye milima mirefu. Naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba alikuja Same Mheshimiwa Dkt. Mathayo akaingia kwenye gari yake na mimi nikaingia kwenye gari yake tukazizungukia kata hizi zote ambazo zimetajwa hapa na Kata ya Vuje, kata ya Bombo, Kata ya Mtina kata ya Lugulu.

Mheshimiwa Waziri uliona hali halisi ya kata hizi kwamba ni korofi mno hazina mawasiliano ya uhakika pamoja na mawasiliano ya Barabara, Mheshimiwa Waziri unakuja na mikakati gani sasa ya kuhakikisha hizi kata ambazo ziko milimani zinaondoka na matatizo haya ahsante Mheshimiwa.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza uniruhusu tu nitoe shukrani kwamba nilivyofanya ziara katika maeneo haya nilipata ushirikiano wa hali ya juu sana kwa Mheshimiwa Mbunge lakini pia kwa viongozi wa wilaya, kwa hiyo nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na niseme tu yapo maeneo mbalimbali ambayo yanakuwa na changamoto kutokana na hali ya jiografia, eneo la Same hili linamilima lakini yapo maeneo mengine ambayo yana misitu ambayo hii ni vikwazo kwa mawasiliano kwa hiyo utaona changamoto ya mawasiliano imekuwa kubwa katika eneo hili kwa sababu ya hali ya jiografia kwa maana hiyo milima na misitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumejipanga kama Serikali ndiyo maana utaona katika awamu ya nne tuko kwenye hatua ya manunuzi, tutaendelea kuweka hiyo minara ambayo imetajwa na katika eneo hili tutakuwa na kata tano vijiji kumi na tatu na baada kusimika hiyo minara tutafanya tadhimini kuona maeneo yapi kutokana na geografia ambayo yatakuwa hayajapata tena mawasiliano kwahiyo hizi changamoto tunaendelea kuziondoa tunavyokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge mkakati mkumbwa uliokuwepo ni kuhakikisha kwamba tunaweka maeneo haya katika mipango yetu kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote. Lakini pia tunaweka bajeti ya kutosha tunavyokwenda ili sasa tuhakikishe kwamba baadaye tunamaliza changamoto ya mawasiliano katika eneo hili lakini unafahamu pia tunaendelea kufanya usanifu mkubwa katika barabara kutoka Same kwenda Mkomazi lakini tutakwenda mkinga kule tumejipanga ili tuondolee shida wananchi wa maeneo haya ambayo hali ya geografia inawaathiri sana kwa maana ya usafiri wa barabara hali ni mbaya lakini pia upande wa mawasiliano ahsante sana.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza, Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikiuliza mara nyingi katika Bunge hili vijiji vya Imbilili, Imiti na Chemchem kwamba havina mawasiliano na nimekuwa nikipatiwa majibu ya Serikali kwamba dawa ya tatizo hili ni kuongezea nguvu minara ya Voda na Airtel, lakini kazi hii haifanyiki naomba nifahamu ni lini sasa kazi hii itafanyika ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata mawasiliano.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, nampongeza sana Mbunge kwa sababu tumeongea mara nyingi sana kuhusu changamoto za jimbo lake Mheshimiwa Mbunge na sisi tumejipanga. Kama nilivyozungumza juzi kwamba katika mradi huu wa Awamu ya IV ya kupunguza changamoto ya mawasiliano tunazo kata mia tano 21 na vijiji 1222 ambavyo viko kwenye mpango. Nimuombe tu Mheshimiwa Gekul kwa sababu kile kijitabu ninacho hapo baadaye tuwasiliane ili tupitie kwa pamoja uweze kuona namna tulivyojipanga kutatua changamoto za mawasiliano katika eneo la kwako na tutaendelea kufanya hivyo mpaka wananchi waweze kuwasiliana vizuri katika maeneo yao ahsante.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana mwaka 2016 Serikali ilituambia sisi Wabunge tuweze kuorodhesha maeneo yote ambayo hayana mawasiliano Wabunge tulifanya hivyo na tena mwaka huu Serikali ikatuambia tuweze kufanya hivyo tena, na mimi baadhi ya maeneo yangu kwa mfano kata ya Halungu, Kata Nambizo, Bara Magamba, Itaka na maeneo mengine hayana mawasiliano ya simu. Je, ni lini Serikali sasa itapeleka mawasiliano ya simu katika maeneo hayo ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa Jimbo la Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, niseme tu kama nilivyozungumza, tumekuwa tukiwasiliana na Waheshimiwa Wabunge vizuri ili kutatua tatizo la changamoto ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali. Na kupitia huu utaratibu ambao tunaufanya kupata maoni na ushauri wa Wabunge ndiyo maana katika Awamu ya IV tumekuja na orodha kubwa sana ambayo tunaendelea kutatua matatizo yaliyokuwa maeneo yetu, vijiji 1222, ni vijiji vingi sana lakini kupitia kwenye awamu zilizopita tumeendelea kufanya hivi ninavyozungumza iko miradi mingine ambayo inaendelea wakati tutakuja na awamu nyingine ya nne. Kwa hiyo, Mheshimiwa Haonga nikutoe hofu tu kwamba ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba suala la mawasiliano litakuwa kwa wote kama tulivyoanzisha mfuko na nishukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru Bunge lako kuanzisha Mfuko wa mawasiliano kwa wote umekuwepo kwa miaka kumi na kazi kubwa sana imefanyika ili kuhakikisha mawasiliano yanakuwa bora katika maeneo ya nchi yetu.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi napongeza sana Serikali kwa hatua zake za kusambaza na kusimamia mawasiliano pamoja na kujenga minara sehemu zote. Pamoja na hayo nataka niulize Serikali ina mikakati gani na ya haraka kwa kiasi gani katika kudhibiti au kuimarisha kikosi kazi cha kupambana na hawa wahuni kila siku wanaosumbua wananchi katika kuwaibia pesa zao kupitia mtandaoni kwa kuwaambia tuma hela hii kwa namba hi, tuma hela hii kwa namba hii, Serikali inafanya nini kuwadhibiti wahuni hawa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, ipo mikakati mingi ya kupambana na hali hii ambayo inajitokeza kwa sababu ya ukuwaji wa teknolojia pia changamoto nazo zinakuwa zipo nyingi, tunao mkakati kwanza wa kuelimisha wananchi ili kuwaokoa na hii hali ambayo inajitokeza lakini pia mara kwa mara mnaona tunaendelea kuboresha Sheria na Kanuni hata hili zoezi la uandikishaji wananchi kwa kupitia alama za vidole kufanya usajili wa simu ni hatua hizo madhubuti za kuhakikisha tutaendelea kumbambana nah ii changamoto ambayo ipo. Kwa hiyo, ni kuahakikishie tu kwamba kila wakati changamoto inapojitokeza kama sisi Serikali tunachukuwa hatua hii kuwafanya wananchi wetu kuwa salama.
MHE. AYSHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, changamoto ya mawasiliano iliyopo Same Magharibi inafanana kabisa na changamoto iliyopo Singida Magharibi. Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano katika maeneo ya Iyumbu, Ingombwe, Mtunduru, Sepuka, Mwaru, Ingriasoni, na Irisia ili kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo hayo hawaachwi nyuma na mawasiliano ya simu za mkononi? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kama nilivyozungumza kwamba maeneo nchi nzima tunafanya juhudi za kuhakikisha kwamba tunaboresha mawasiliano na iko orodha ndefu tu katika Mkoa wa Singida. Nimsihi tu Mheshimiwa Aysharose Matembe na nimpongeze sana kwa kweli hata nilivyofanya ziara Singida nilipokea orodha ndefu sana kwa ajili ya kuboresha mawasiliano katika mkoa huu. Kwa hiyo, nikuombe tuonane tu ili tuweze kupitia hii orodha ili ufanye kazi ya kuwaelimisha wananchi kwamba Serikali inajipanga mwaka huu wa fedha kuna kazi kubwa itafanyika kwa ajili ya kuendeleza kuboresha…

MWENYEKITI: Ahsante
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza Kijiji cha Misiaje kilichopo katika Kata ya Malumba na Kijiji cha Imani na Kaza moyo kilichopo Kata ya Lukumbule havina mawasiliano. Je, ni lini Serikali itajenga minara katika vijiji hivyo ili kuwapa mawasiliano wananchi hao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naompongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu nilivyofanya ziara Mkoani Ruvuma tulikuwa na mawasiliano mazuri sana kulikuwa na changamoto nyingi sana na hasa hasa maeneo haya ambayo yapo mpakani. Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge avute subira kama nilivyosema tunaorodha ndefu sana, aje tu tupitie kwa pamoja halafu tutakapoweka minara hii katika maeneo ambayo yameainishwa tutaangalia tena tuone kama kuna maeneo bado yanachangamoto Serikali itakuwa ipo tayari kuendelea kupunguza tatizo ambalo lipo katika maeneo yetu.

MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nimekuwa nayataja maeneo kadhaa ambayo yapo jimbo la Mtwara mjini kwa muda mrefu ndani ya Bunge hili na maeneo hayo, Naulongo, Mkunjanguo, Namayanga, na Mbawala Chini ambapo hakuna mawasiliano ya simu kabisa. Nilikuwa naomba commitment ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba ni lini atafanya ziara ya Mtwara Mjini kuja kukagua mguu kwa mguu maeneo haya ili aweze kudhibitisha kwamba maeneo haya yanahitaji mawasiliano kwa simu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anaomba nifanye ziara katika Mkoa wa Mtwara na sisi unafahamu Mheshimiwa Mbunge tuna miradi mingi sana ambayo Wizara yangu inasimamia, nitafanya ziara mapema baada ya Bunge hili katika Mkoa huu wa Mtwara.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza Kijiji cha Yaeda Chini, Masieda, Endamilay na Mbullu Vijijini wamesaini mikataba ya kujenga minara TTCL na Holotel wameondoka. Je, ni lini Mheshimiwa Waziri watarudi hawa TTCL kujenga minara Mbullu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu TTCL wamepewa kandarasi ya kujenga minara maeneo mbalimbali. Tatizo au changamoto ambayo ilikuwepo kidogo ni kwamba TTCL wanavyopewa kazi sambamba na wakandarasi wengine kwa maana hawa Tigo, Airtel, Vodacom kidogo tumekwenda kusuasua, siyo kusuasua kwa sababu wenyewe sasa kama taasisi ya Serikali lazima wafuate Sheria ya Manunuzi ambayo imetuchelewesha kwenda kusimika minara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hatua za manunuzi ziko vizuri kwa maana TTCL watakuja katika eneo lake na kusimika ile minara ambayo wamepewa fedha na Mfuko wa Mawasiliano. Kwa hiyo, avute tu subira wanakuja na tutaweka hiyo minara kuongeza mawasiliano katika eneo lake.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona niulize swali dogo la nyongeza. Matatizo ya usikivu wa simu yaliyopo Same Magharibi ni sawa na matatizo yaliyopo katika Wilaya ya Ngara, Kata za Keza, Mganza, Mrusagamba, Mgoma, Kabanga na Rusumo, ambapo yanaingiliana na nchi jirani za Rwanda na Burundi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha usikivu wa mawasiliano katika kata hizi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia maendeleo katika eneo lake. Niseme tu maeneo ya mipakani yanazo changamoto za kuingiliana kwa mawasiliano. Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote jambo hili tumeshalitambua na tuna mkakati wa kuwasiliana na wenzetu nchi za jirani kwa sababu upo utaratibu ambao tunajiwekea kwamba ile minara iwekwe umbali fulani ili ipunguze changamoto hii ya kuingiliana kwenye mawasiliano. Pia, tunaendelea kusimika minara katika maeneo haya ya mipakani ili kuhakikisha wananchi wetu wa maeneo hayo hawapati changamoto hii ya kuingiliana kwa mawasiliano.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Yapo mawasiliano hafifu katika Kijiji cha Kamnyazia, Kata ya Lusaka, Vitongiji vya Mpande. Halotel walishajenga foundation toka mwaka jana mwezi Agosti hawajaonekana. Ni lini sasa watakwenda kumalizia kazi ile ili wananchi waweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Malocha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wameuliza maswali mengi sana kuonesha kwamba tunazo changamoto kubwa za minara katika maeneo yetu. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge swali hili alilouliza kuhusu mnara wa Halotel nilichukue tu kama suala mahsusi ili tuweze kujua nini kilichotokea ili tuweze kuliondoa tatizo hilo na hatimaye mnara huu uweze kukamilishwa. Ahsante sana.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Katika Jimbo langu la Nkasi Kusini kuna Vijiji sita vya Kisambala, Ng’undwe, Mlalambo, Kasapa na Izinga, mara nyingi nimepeleka orodha Wizarani ili vipatiwe mawasiliano. Je, ni lini Serikali itavipatia mawasiliano vijiji hivi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu changamoto zilizoko katika maeneo haya sababu ya jiografia yake, naona ndiyo maana amekaa na jirani yake pale Mheshimiwa Malocha. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo hili ambalo analizungumzia tutaweka msukumo wa kipekee ili tuone changamoto hizi zinakaa vizuri kwa sababu nafahamu kwamba kuna changamoto nyingi sana kwenye eneo lake, kwa hiyo, avute subira. Pia, naomba tuonane na Mheshimiwa Mbunge ili aweze kuona kwenye orodha namna ambavyo tumejipanga ili aweze kwenda kusema kwa wananchi kwamba Serikali hii imejipanga kuhakikisha kweli mawasiliano yanakuwa mawasiliano kwa wote.
MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwanza kwa barabara hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne mwaka 2015 ahadi hiyo iliendelea kuwekwa kwenye ilani kutokana na uzalishaji wa mazao ya kutosha ya mahindi, Alizeti, Mbaazi, ufuta na mazao mengine. Tunayo minada mingi mikubwa ya mifugo minada ya Dosidosi, minada ya Kibaya, minada ya Raiseli, na kwa umuhimu wa barabara hii, nilitaka kuomba kwamba Jitihada za Serikali ni lini sasa zitafanyika ili hii barabara iweze kutumika na mazao ya wakulima kutoka Wilaya ya Kilindi, Simanjiro, Kiteto, Kongwa, haya mazao yaweze kuhama kwenda Dar es Salaam kwengineko ili wakulima wetu waweze kupata faida kwenye maeneo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifanya juhudi nyingi sana kuhakikisha kwamba eneo hili la Kiteto linaunganishwa vizuri na juhudi kwa kutokana na umuhimu kama alivyotajwa Mheshimiwa Mbunge tunafahamu sote kwamba eneo hili na uzalishaji mkumbwa na mazao, eneo hili lina mifugo, eneo hili pia lina changamoto na wananchi wengi sana wapo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, juhudi zimeshaanza, kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi kwamba tuko harakati ya kufanya ujenzi na tunaenda vizuri na hatua hiyo ya usanifu kwa hiyo Mheshimiwa uvute subira tu na eneo hili kwakweli tumeliangalia vizuri kwa sababu hata ile barabara kubwa kutoka Handeni litapita kwenye eneo hili lakini pia kwenye mwaka huu wa fedha tutasanifu barabara kutoka babati kuja katika eneo hili kwa hiyo vuta subira tumejipanga vizuri tunakuja kutengeneza barabara ahsante sana.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa niaba ya Wananchi wa Serengeti naomba kuuliza ni lini barabara ya Makutano Sanzate, Mugumu, Tabora B, Kilensi, Loliondo Mto wa Mbu itakamilika na nilini watapata fidia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze tu Mbunge kwa sababu anafuatilia hii barabara na anafahamu hatua nzuri ambayo barabara hii muhimu imefikiwa kwa sababu tunao mradi wa kutoka makutano sanzate ambapo tupo karibu asilimia 85 ya Ujenzi wa barabara hiyo na muda mrefu tunaendelea kuijenga lakini tunatoka Sanzate tunakwenda Nata tunafahamu kwamba tupo kwenye hatua ya kumpata mkandarasi ili ujenzi uendelee lakini kutoka Sanzate kwenda Mugumu na sehemu ya barabara pia upande ule wa kutoka Loliondo kwenda Salensi Junction kuna mradi unaendelea. Barabara hii ni muhimu sana kwa sababu harakati za kuijenga barabara hii kutoka makutano kwenda hadi Mto wa Mbu ahsante.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii nimweze kuuliza swali la nyongeza, tulipata Kilolo Kata ya Dabaga, Nangage, na Boma la Ng’ombe tulipata mradi kupitia mradi kupitia EU ya kilometa 18 wa lami na moja ya sharti ilikuwa ni lazima wananchi wakubali kutengenezewa barabara bila fidia, wananchi waliitikia na kubomoa wenyewe nyumba zao na baadhi ya miundombinu. Sasa tulikuwa tunaomba kwakuwa mradi huo ulikuwa haujaanza Serikali itakuwa tayari sasa kuwaondoa wasiwasi wale wananchi wale ambao wamekosa kabisa amani itakuwa tayari kusema lini au mradi huo ukoje?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza niseme tu barabara hii inasimamiwa na wenzetu upande wa TARURA lakini nafahamu pia hatua nzuri ambayo imefikiwa. Labda kubwa tu nimpongeze tu Mheshimiwa Mwamoto kwa kuwaamasisha wananchi kwa ridhaa yao wenyewe najua na wewe umewaamasisha sana na niwapongeze kwa kweli kwa kukubali kwamba wanaona faida ya hii barabara ya ambayo itapita maeneo pamoja na kwamba barabara ni ya kwao na maendeleo ya wananchi wenyewe. Kwa hiyo, nakupongeza sana Mheshimiwa Mwamoto kwa kazi nzuri uliyoifanya nafikiri ni jambo la kuingwa na maeneo mengine tukipata wananchi kwa ridhaa yao kupisha mradi inatuarakishia kwenda kufanya maendele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwahakikishie wananchi hawa ambao wamepisha barabara hii muhimu tu kwamba ipo tu kwenye hatua ya ujenzi na mkandarasi ameshapatikana kwa taarifa nilizokuwa nazo na inafadhiliwa na hii barabara na wenzetu wa EU kwa hiyo wavute subira kwamba barabara hii kwa vile mkandarasi amepatikana itaenda kujengwa kwa haraka na huduma itakuwepo katika maeneo haya ya kilolo.
MHE. ESTHER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naomba niulize swali dogo la nyongeza, najuwa kuna ujenzi wa barabara kutoka Mbezi Mwisho ile ya Kimara, Goba, mpaka Makongo mpaka kutokea Survey. Sasa kwa upande wa Goba tayari huu mradi umekamilika kwa upande wa Jimbo la Kawe kumejengwa kilometa moja na ninajua Mheshimiwa Naibu Waziri kuna bilioni nne za TARURA kwa ajili ya fidia sasa hivi ule mradi kwa upande wa Jimbo la Kawe umesismama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kujuwa ni lini sasa kwa upande wa Kawe kuanzia kwenye mpaka wa Goba mpaka Survey utakamilika kwa sababu wananchi tayari wako tayari kutoa maeneo yao kwa sababu hii barabara kwa kweli haipitiki na inawasaidia sana wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kupunguza foleni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana na mimi kwamba kazi kubwa sana kazi nzuri sana imefanyika kupunguza msongamano katika jiji la Dar es Salaam na ninafahamu pia kwamba Mheshimiwa Mbunge unafahamu kumekuwepo na changamoto baadhi ya watu kunapokuwa na harakati za kulipa fidia wanakuwa na mahitaji labda kuna mambo kadhaa wa kadha kwa sababu hiyo saa nyingine inatuchelewesha kwamba kukamilisha ili tuendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo Serikali ilikuwa inafanya juhudi za kuhakikisha kwamba kwanza eneo la fidia linakaa vizuri kwamba watu wote wanaridhika watu wote wanakuwa wamelipwa ili mradi uweze kuendelea kwahiyo nikusihi Mheshimiwa Mbunge uvute subira lakini pia endelea kuamasisha wananchi hawa ambao saa nyingine wanaweka pingamizi kidogo kwenye maeneo yao wanatuchelewesha kwenye mradi. Kwa hiyo, tukimalizana na wananchi tutaenda kumalizia eneo hilo kufanya ujenzi wa lami uweze kukamilika maeneo yote ambayo tayari tumeshakuwa na mkataba. Ahsante sana.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, barabara hii ya Mlalo, Ngwelo, Mlola, Makanya, Milingano mpaka Mashewa ambazo ni kilomita 53. 7 inapita kwenye halmashauri tatu na majibo manne. Na barabara ya kutoka dochi Ngulu hadi Mombo ambayo yenye kilometa 16.3 inapita kwenye halmashauri mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na isitoshe tumeandika barua ya kupandisha hadhi barabara hizi kabla ya kuanzishwa kwa TARURA lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea zaidi ya wananchi kuendelea tabu ya usafiri pamoja na mazao yao. Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka barabara hizi ziweze kushughulikiwa kwa haraka ili tukiendelea kusubiri upandishwaji wa hadhi wa barabara hizi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwakuwa mheshimiwa Waziri wewe mwenyewe ni shahidi kwa kuona barabara hii ya dochi Nguli Mombo na kuongea na wananchi wa kijiji cha Nguli na ukawahidi kwamba changamoto hii utaimaliza. Je, upo tayari sasa kutuma wataalam wako kwenda kuona hali halisi ya barabara hiyo ili kuondoa kadhia wanayoendelea kuipata wananchi wa Nguli?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizi anazotaja Mheshimiwa Mbunge ni kweli kwamba inapita katika maeneo mengi kwa maana jimbo lake la Lushoto, Jimbo la Mlalo, Jimbo la Bumbuli, na Korogwe vijijini na eneo hili ni muhimu sana kwa sababu inapitisha watali wengi kwenda kwenye hifadhi yetu ya Mkomazi lakini pia kuna uzalishaji mkubwa wa mazao na nilitembelea eneo hili nilishuhudia changamoto ambazo ziko kwenye barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kujibu swali lake niseme tu mkakati wa kwanza mkubwa ni uanzishwaji wa TARURA na TARURA wamefanya kazi kubwa wa kuzitambua barabara zote nchini kwa lengo la kuhakikisha kwamba barabara zinapata bajeti au zinapata fedha kulingana na changamoto na hali ya barabara ilivyo kwa hiyo hii zoezi ilikuwa inafanyika na kazi ya TARURA ilipokamilika imepelekwa taarifa zimepelekwa kamati maalum ambayo inashirikisha wenzetu wa TAMISEMI wenzetu wa Wizara inayoshughulikia mambo ya utalii wenzetu wa Wizara ya ardhi kwa hiyo kamati muhimu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu Mheshimiwa Mbunge anahitaji wataalam waende nimuelekeze tu Meneja wa TANROAD wa Mkoa wa Tanga na coordinator wa TARURA wa Mkoa wa Tanga watembelee barabara hizi mbili muhimu ili waweze kushauri kamati maalum tuone namna gani ya kuzifanyia matengenezo makubwa barabara hizi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba uvute subira nitafuatilia kuona wataalam wanatembelea eneo lako ili kuweza kuwezi hizi juhudi ambazo unazifanya Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba wananchi wako wanapata huduma nzuri ya barabara katika maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitaifuatilia na niwaombe hao kwa sababu ni wajumbe wa bodi ya barabara kwenye mkoa mapendekezo yatakayokuwa nayo pia wayazungumze katika bodi ya mkoa ili tuweze kuzitendea haki barabara hizi.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza naomba nishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuweza kukamilisha daraja la Sibiti na hiyo ni kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Singida pamoja na Simiyu kwa thamani ya daraja lile nilikuwa naomba nimuulize mheshimiwa Naibu Waziri, ili tuweze kuwa na dhamani ya daraja lile ni ujenzi wa Barabara ya lami unaotoka Iguguno, Nduguti, kupita Sibiti, Meatu na kuendelea mpaka Bunda ili wananchi wale waweze kufanya shughuli za maendeleo. Je, ni lini Serikali itaanza Ujenzi huo kama ilivyoahidi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mlata kwa sababu umekuwa umefuatilia barabara zote za Mkoa wa Singida na ninafahamu hata sasa tuna ujenzi mkubwa mwingine unaendelea katika daraja la Msingi ili tuweze kuwaunganisha wananchi wa Wilaya ile ya Kiomboi na waweze kupita nao Sibiti. Kwa hiyo, tunaendelea na ujenzi na ujenzi unaendelea vizuri, lakini niseme tu kwamba mkakati mkubwa wa kuiboresha barabara hii ambayo ni muhimu sana itapunguza pia wasafiri wanaokwenda Arusha, wanaokwenda Manyara, wanaokuja Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilika daraja lile tunajenga kiwango cha lami kilometa 25 ili eneo lote la bonde hili ambalo lilikuwa na changamoto kubwa wananchi waweze kupita vizuri ujenzi ule unaendelea kilomita 25.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunakamilisha usanifu wa barabara hii muhimu ambayo inaunganisha mikoa ya Kanda ya Ziwa tukipita Sibiti tunakwenda Haydom tutakwenda Ndogobeshi, itakwenda hadi Mbulu itoke Karatu. Kwa hiyo, juhudi kubwa zinafanyika kuiboresha barabara hii muhimu na itawafanya wakazi wote wa Manyara wakazi wote wa Arusha waweze kupita barabara hii kwa sababu itapunguza zaidi kilomita mia mbili kwa mtu anayekwenda Mwanza, Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaendelea na kazi nzuri kubwa inafanyika, vuta subira na kwakweli ninashukuru sana kwa ushirikiano unaotoa Mheshimiwa Mbunge kwa kutupa information nyingi ili tuweze kuwaudumia wananchi wa Singida.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naipongezs Serikali kwa kazi kubwa inayoendelea ya ukarabati na ujenzi wa barabara mbalimbali pale Wilayani Temeke. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipande cha barabara kutoka Keko Furniture mpaka kwenye geti la Chuo Kikuu cha DUCE imekuwa na mashimo makubwa na imekuwa ni usumbufu kwa wanaotumia barabara hiyo ikiwa ni sambamba na kipande cha barabara ya Devis Corner, Jet corner hasa kipande cha kutoka Lumo mwisho mpaka Jet corner, vimekuwa na mashimo mengi sana na barabara hizi ziko chini ya TANROADS: Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuiagiza TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam kwenda kuziba mashimo katika barabara hizi haraka? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha, barabara nyingi zilizo chini ya TANROADS na TARURA hasa barabara ya kutoka Temeke Veterinary kupitia Mwembe Yanga mpaka Tandika na barabara zote zinazoingia Tandika barabara zote katika Kata ya Temeke 14, Kata ya Sandali na Kata ya Buza hazipitiki kabisa; na uwezo wa Halmashauri ya Temeke kuzikarabati barabara hizi zote kwa kipindi hiki umekuwa ni mgumu: Je, Wizara yako kama mdau mkubwa wa miundombinu, ina mpango gani wa dharura wa kuisaidia TARURA kukarabati barabara hizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli baada ya mvua nyingi hizi kunyesha barabara zetu nyingi zimeharibika kwa kiasi kikubwa. Nianze tu kumshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo anafanya kazi kwa ushirikiano. Na mimi nimetembelea barabara hizi ikiwemo hii barabara ya Keko Furniture - DUCE nimeipita tena ni wiki ya juzi tu kuona hali ilivyo mbaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwahidi Mheshimiwa Mbunge na kwa maelekezo yangu kama tulivyojipanga ni kwamba tutarejeshea miundombinu ya barabara hii mvua zitakapopungua. Inakuwa siyo rahisi wakati huu mvua nyingi zinaendelea kunyesha kufanya ujenzi wa kiwango cha lami kwa maana ya kurudishia sehemu zilizoharibika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira, tumejipanga vizuri, ndiyo maana tumeendelea kuyatambua maeneo yote ambayo yanahitaji kufanyiwa matengenezo na tutarudi kufanya matengenezo mvua zitakapopungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu pia barabara hii ambayo ameitaja ya Tandika na kimsingi barabara ambazo ziko TARURA, niseme tu kwa ujumla kwamba tunao utaratibu wa kushirikiana kama Serikali kwa upande wa TARURA na TANROAD. Inapokuwa tumepata dharura (emergency) au shida kama wakati huu, tunafanya kazi kama timu moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakubaliana na ushauri wa Mheshimiwa Mbunge, tutashirikiana na wenzetu wa TARURA kuhakikisha kwamba mvua zikipungua tutafanya urejeshaji wa miundombinu muhimu katika maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyofanya, nami namwahidi kumpa ushirikiano mkubwa; tutashirikiana naye kuhakikisha kwamba tunawahudumia vizuri wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Dodoma – Kondoa – Babati ilifunguliwa mwaka 2018 na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini katika baadhi ya maeneo ya barabara hii kumeshaonekana uharibifu wa kuwa na mashimo na hivyo kuhatarisha usalama wa raia pamoja na magari: Je, Serikali inatoa tamko gani kwenye hii barabara mpya ambayo imeshaanza kupata uharibifu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yako maeneo ambayo yamekuwa dhaifu baada ya ujenzi wa barabara. Hata hivyo, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba barabara hii ya kutoka Dodoma - Kondoa – Babati ni kati ya barabara ambazo zipo kwenye kiwango kizuri na imejengwa kwa teknolojia mpya, hii ni super pave ukiilinganisha na barabara nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni kweli kwamba yako maeneo ambayo yamekuwa na upungufu. Vile vile uko utaratibu wa kimkataba kwamba kipindi cha matazamio barabara inafanyiwa urejeshaji. Kwa hiyo, tutaendelea kusimamia taratibu zilizokuwepo ili kuona maeneo ambayo yana upungufu yanafanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia mara baada ya miaka mitano ni utaratibu wetu wa kawaida kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya mara kwa mara. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na ubora wa barabara hii, maeneo yote ambayo yana upungufu tutaendelea kuyasimamia ili kuhakikisha kwamba barabara inakuwa kwenye kiwango cha hali ya juu na wananchi wanapata huduma nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. DKT SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Barabara ya Makurunge - Saadani - Pangani mpaka Tanga ni barabara ambayo inaunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga kwa njia ya mkato.

Pia barabara hii ni kichocheo kikubwa sana cha utalii hasa kwa hifadhi yetu maalum ya Saadani ambayo kwa sasa haipati watalii wa kutosha kwa sababu barabara hiyo ipo katika hali mbaya. Barabara hii pia imeahidiwa; au iko katika mipango ya Serikali kwa ujenzi wa kiwango cha lami kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali: Ni nini mkakati wa Serikali kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge ikitokea Tanga – Pangani – Makurunge – Sadani, inakuja mpaka Bagamoyo, ni barabara ambayo iko kwenye mpango wa ujenzi wa lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi tumeshaanza ujenzi, tumeshapata mkandarasi ambaye anajenga barabara hii kutoka Tanga kwenda Pangani. Pia tuko kwenye mpango wa kujenga daraja katika Mto Pangani. Tunaamini kwamba baada ya ujenzi wa daraja hili katika Mto Pangani, italeta sasa mantiki ya kumalizia ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kuja Bagamoyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Bagamoyo na Watanzania kwa ujumla kwamba ni mpango wa Serikali kuikamilisha barabara hii kwenye kiwango cha lami na ujenzi umeshaanza, tuvute subira, tutakuja kumalizia kipande hiki kinachobaki kwa maana ya kutoka Bagamoyo kwenda Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuko kwenye mpango na itafupisha barabara hii ukitokea Tanga kwa sababu itakuwa na kama kilomitaa 240 hivi tu kutoka Tanga kuja bagamoyo. Kwa maana hiyo, pia itatusaidia sana kufanya watalii waende maeneo ya Sadani kwa maana ya kutuingizia fedha za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumza na Naibu Waziri wa Maliasili kwamba tutaitembelea barabara hii kwa maeneo ambayo ni korofi kwa kipindi hiki baada ya mvua kupungua, tuhakikishe kwanza inapitika, inatupa huduma lakini wakati ule ule tutaendelea na utaratibu wa kuijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. OLIVER D. SEMUGULUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kivuko hiki cha Kyanyabasa wanafunga kazi saa 12.00 jioni ambapo inaleta adha kubwa kwa wananchi. Kwa mfano, imetokea umeuguliwa usiku, inakulazimu kuzunguka Kishogo – Nyakibimbili – Ibwela – Katelero kuja kwenye Hospitali ya Wilaya inayojengwa Kanazi eneo la Bujunangoma:-

Je, ni lini Serikali itatuondolea adha hiyo ya kufunga kivuko mapema? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Tatizo lililopo katika kivuko cha Kyanyabasa ni sawa na kivuko kilichopo Kata ya Kashalu maarufu kwa jina Kansinda kinachounganisha Wilaya ya Bukoba na Misenyi:-

Sasa ni lini Serikali itaweka kivuko cha Uhakikika kuliko kuvuka na mitumbwi ambapo inahatarisha maisha ya wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza uniruhusu nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayofanya, kwa sababu mara nyingi kwa kweli amekuwa akitusumbua kwa nia ya kuhakikisha wananchi wa eneo hili la Kagera wanapata huduma nzuri. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nakupongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maswali yake mawili, niseme, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, ni kwamba tumedhamiria kufanya maboresho makubwa ya kivuko hiki. Nimesema kwamba pia tutaweka taa pale. Tukiweka taa za usalama pale na tutahakikisha kwamba tunatoa huduma vizuri usiku na mchana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimtoe hofu Mheshmiwa Oliver kwamba tumejipanga kuona tunatoa huduma usiku na mchana. Hata hivyo kwa sasa eneo lile tunavusha kwa kutumia dakika tano tu, tunafanya mivuko pale mara 35 hadi 40 ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri. Kwa hiyo tuendelee kuwasiliana tu na pale ambapo kuna dharura, kwa mfano tuna wagonjwa au misiba na hata wakati wa sherehe kama harusi, tuwasiliane. Tuko tayari kuwahudumia usiku na mchana wakati harakati za kufanya maboresho makubwa yanaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu eneo eneo alilotaja la Kata ya kasharu umeita mwenyewe Kasinda, nielekeze tu wenzetu upande wa TAMESA waende wakaangalie kwa makini eneo hili tuone namna nzuri ya kuleta huduma hii ili tuwaokoe wananchi na hatari ambayo inaweza ikasababishwa na kuvuka kwa kutumia mitumbwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge, suala hili nitalisimamia ili tuone kwamba tunafanyaje wananchi hawa nao waendelee kunufaika na huduma nzuri ya vivuko kuliko kutumia mitumbwi?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali moja la nyongeza. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa miradi mbalimbali: Ni lini ahadi za Mheshimiwa Rais zitatekelezwa kwa kujengwa kwa kiwango cha lami katika Mji wa Makambako?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, amekuwa jirani yangu, tumezungumza mambo mengi ya Makambako. Niseme tu, ahadi za Viongozi Wakuu zikiwemo ahadi za Mheshimiwa Rais tunaendelea kuzitekeleza. Ziko ahadi ambazo tumemaliza kuzitekeleza, ziko ambazo ziko na asilimia kadhaa na zipo nyingine ambazo bado. Naahidi tu Bunge lako kwamba ahadi zote ambazo zimetolewa na viongozi, tutaendelea kuzitekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ahadi ambazo zilitolewa Makambako, ziko ahadi nyingi; iko ahadi ya ujenzi wa barabara kiwango cha lami, tunaendelea na ujenzi, Mheshimiwa Mbunge anafahamu, tumeshaanza kidogo kidogo, tutajitahidi tuweze kuweka kiasi kikubwa ili tuendelee kwa Mji wa Makambako uweze kukaa vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu pia kwamba pale barabara kubwa tumeitengeneza vizuri, kulikuwa na foleni nyingi pale kwenye mizani, tumeziondoa kabisa; Mji wa Makambako unawaka taa vizuri kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla, waende wajifunze waone namna nzuri tu kuweka taa katika Mji wa Makambako. Ukienda Makambako, hali ni nzuri kabisa. Tunajua tena tuna ujenzi wa One Stop Station pale Idofi; nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na yenyewe ni sehemu ya ahadi, tuko kwenye mpango wa kufanya ujenzi pale. Kwa hiyo, tunaendelea na hatua nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu ahadi zote za viongozi tutaendelea kuzitekeleza na kwa ufundi mkubwa, Serikali imejipanga vizuri kuona ahadi hizi za viongozi wetu tunaweza kuzitekeleza.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Bajeti ya mwaka jana nilipata fedha kwa ajili ya kujenga barabara ya kutoka Igunga kwenda Itumba na barabara ya kutoka Mbutu kwenda Kininginila lakini niliuliza swali Bunge lililopita kwamba kwa nini barabara hizi hazijajengwa na Waziri aliniahidi kwamba wataanza kujenga mara moja lakini hadi sasa barabara hizi hazijaanza kujengwa. Nini kinachojiri huku?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Kafumu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Kafumu, nafahamu kwamba tumeongea mara nyingi juu ya mtandao wa barabara katika Jimbo lake la Igunga na kwa kweli eneo lake hili ni bonde, kuna mabonde makubwa sana. Nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Kafumu kwamba tumejipanga na nimwombe tu baada ya Bunge hili tukutane ili angalau tuweze kupitia kwa upana kabisa juu ya barabara zake na kuona namna ambavyo tumejipanga kuzishughulikia. Ipo mipango mizuri tu, namwomba sana tuonane ili aweze kupata ufahamu wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kweli nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Kibaha kumpongeza sana Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake kwa kazi nzuri ya ujenzi wa daraja lile la Ubungo, lakini vilevile barabara hii kubwa ambayo kwa sasa itaishia Kibaha na itaokoa gharama kubwa za msongamano wa magari kutoka Mjini Dar es Salaam kuja Pwani. Pamoja na pongezi hizo kubwa, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ambayo ni kilometa 19.2 inaishia kidogo tu baada ya mizani ya zamani pale Kibaha. Maana yake ni kwamba ile trafic ya magari yote ambayo yatakuwa yanakwenda mikoani yatakuja kwa kasi na yataishia pale ambapo ni almost katikati ya mji wetu mdogo wa Kibaha. Kwa maana hiyo ni kwamba Mji wetu wa Kibaha magari yatakuwa mengi na hakika utakuwa umesimama wananchi wa Kibaha hawataweza kufanya shughuli zao za kiuchumi katika mji ule kwa sababu ni mdogo na magari yatakuwa mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kikao chetu cha Regional Road Board tuliomba barabara hii angalau iongezewe mpaka pale Kwa Mathias ili sasa iweze kuhudumia Mji ule wa Kibaha na kuleta maana njema zaidi ya maendeleo katika mji wetu. Vilevile kama tutamwongezea mkandarasi huyu aliyepo kazini gharama zitapungua kwa maana hakutakuwa na mobilization hata process za tenda. Je, Serikali ina mpango gani sasa kukubaliana na ombi letu ili barabara hii iweze kuleta manufaa zaidi katika mji wetu wa Kibaha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili barabara Kwa Mathias hadi Msangani ambayo inakwenda mpaka Makao Makuu ya Land Force tumejenga mita 400 za lami na barabara ya TAMCO kwenda Mapinga inaendelea kujengwa kilometa 4 na wananchi hawajapata fidia. Je, Serikali ina mpango gani kukamilisha barabara hizi na kuhakikisha wananchi wanapata fidia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nizipokee pongezi nyingi alizotoa Mheshimiwa Koka lakini pia nimpongeze sana kwa juhudi anazofanya kwa kushirikiana na Mkoa wa Pwani kuhusu maendeleo mbalimbali ya Jimbo lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anazungumzia juu ya kuendelea na ujenzi wa barabara hii kutoka eneo ambalo tunaishia kwa maana ya Maili Moja kwenda mpaka Kwa Mathias. Kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi ni kwamba ujenzi wa kilomita 19.2 ni awamu ya kwanza. Kwa hiyo, tutaendelea na awamu zingine kadri tunapopata pesa kwa maana ya kuendelea na ujenzi kwenye eneo hili kupita Picha ya Ndege - Kwa Mathias - Mlandizi – Chalinze. Kwa hiyo, nimtoe hofu tu tumejipanga vizuri na Serikali tunafahamu kwamba baada ya upanuzi huo wa barabara kwa kweli tutaleta magari mengi sana kwa upande wa Kibaha na maeneo haya Mlandizi kwa maana hiyo tutakuwa tumehamishia foleni kwenye maeneo haya. Kwa hiyo, tumejipanga vizuri kwamba tutakuja na awamu zingine ili tuweze kutatua na kuendelea kufanya maboresho makubwa ya ujenzi wa barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia amezungumzia barabara ile ya Kwa Mathias kwenda Msangani na barabara ya kutoka TAMCO kwenda Mapinga ambayo ni kilometa 24 na tumeshapata wakandarasi kuanza ujenzi katika maeneo haya. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la fidia tunalishughulikia kwa sababu ni utaratibu na kanuni kwamba kabla mkandarasi hajaanza kazi fidia zitakuwa zimelipwa. Tunafanya jitihada za kuwasiliana na wenzetu Wizara ya Fedha ili tuweze kulipa fidia. Pia niwahakikishie tu wananchi wa maeneo haya waondoe hofu tumejipanga kuwafanyia maboresho ya barabara zao lakini pia tutawalipa stahili zao za fidia kama ilivyo kulingana na taratibu zetu.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Waziri nikushukuru pia kwa majibu ya Serikali ambayo ni mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza Mheshimiwa Waziri, Serikali haioni kwamba sasa badala ya barabara hii inayotoka Babati mjini hizi kilomita 20 kuendelea kuwekewa fedha za maintenance, ni vizuri wakatenga fedha za kuweka lami hizo kilomita 20 hadi lango la Tarangire ili watalii wanapofika Babati wasafiri vizuri mpaka hapo Hifadhini kuliko ambavyo sasa ni rough road.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Swali la pili miongoni mwa vitu ambavyo vinachochea utalii wetu ni pamoja na miundombinu mizuri barabara pamoja na viwanja vya ndege uwanja wetu wa Mkoa wa Manyara ambao uko pale Magugu sasa haujawahi kutengewa fedha na watalii wamekuwa wakilazimika sasa watue Arusha na watembee umbali mrefu.

Je, Serikali iko tayari kututengea fedha haraka iwezekanavyo kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mkoa wa Manyara ili watalii waweze kufika mapema hifadhini Tarangire?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI MAWASILIANO NA UCHUKUZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuhusu barabara hii ya Babati kwenda Tarangire kwenye lango niseme iko kwenye mipango na sasa kama kinachofanyika ni kuhakikisha kwamba inakuwa vizuri ndiyo maana Bunge lako imetutengea fedha kwa ajili ya kufanya maboresho makubwa ili kuondoa usumbufu kabisa ili wananchi wakati tunafanya harakati za ujenzi watalii waweze kupita bila shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu ujenzi wa uwanja wa ndege kwanza niipongeze Serikali ya mkoa, kupata eneo hili la Mbuyu wa Mjerumani kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha ndege na nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla ni kwamba Wizara yangu kupitia TIA inaendelea na usanifu ili sasa tuweze kujua namna uwanja utakavyokuwa na gharama zake na hatimaye tuweze kujenga uwanja huu wa ndege. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais Jimboni Ukerewe mwaka jana tarehe 5 Septemba, 2018, alitoa maelekezo ya ujenzi wa km 14 za lami kutoka Lugeze - Nansio mjini. Nataka kujua ni hatua ipi imefikiwa ili ujenzi huo uweze kuanza? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu barabara hii ameifuatilia muda mrefu na matokeo yake niseme kwamba usanifu wa barabara hii umeshaanza ukikamilika tutajenga barabara hii kwa kiwango cha lami.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Serikali ina mpango gani wa kutenga pesa kwa ajili ya upembuzi yakinifu kwa barabara ya kutoka Njia Nne - Kipatimu (km 50)? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la rafiki yangu Mheshimiwa Ngombale ,kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza mara nyingi juu ya barabara hii. Niombe tu tuwasiliane ili tuone kwa sababu kwenye Mipango Mikakati yetu katika Wizara tumeiweka katika Mpango ili tuweze kuendelea na hatua ya ujenzi wa lami. Kwa hiyo, tuonane na Mheshimiwa Mbunge ili nimpe taarifa za kukutosha ili aweze kutoa maelezo mengi kwa wananchi wake. Ahsante.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi lakini pia niishukuru Serikali kwa majibu mazuri kwa sababu barabara hii imekuwa ni ya muhimu sana lakini sasa tumeenda kupata hizi bilioni 4 kwa hiyo tunaishukuru sana Serikali kwa jitihada hizi.

Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza, swali la kwanza ningependa kujua je, katika utaratibu ambao unaendelea sasa hivi wa upembuzi yakinifu, Serikali imejipaga vipi kuhakikisha kumba fidia kwa wananchi wale katika barabara ile inapatikana kwa wakati na yenye tija?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nilitaka nifahamu, kuna barabara ambayo inatoka Wasa kuelekea Kiponzelo mpaka Kalenga ambapo unaenda kuunganisha katika na hiyo barabara ya Ruaha Msembe. Ningependa kufahamu, kwa kuwa barabara hii nayo ni ya muhimu sana kiuchumi. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inaitengeneza au kuiboresha barabara hii katika kiwango cha lami ili wananchi wa maeneo haya waweze kuungana na wale wanaoenda Ruaha National Park? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mgimwa kwa sababu amekuwa akifuatilia sana barabara hii na barabara nyingine hii ya Wasa – Kiponzelo – Kalenga aliyoitaja. Serikali imekamilisha uthamini, wa wananchi watakuwa na stahili ya kupata fidia katika maeneo haya na takribani shilingi bilioni 2 imekadiriwa kwamba itatumika kuwalipa fidia wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie tu kabla ujenzi haujaanza kama ilivyo taratibu wananchi hawa wa maeneo haya watalipwa fidia kama wanavyostahili kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara yako ile uliyoitaja Wasa – Kipanzelo – Kalenga takribani kilomita 70 hivi, ni barabara ambayo inasimamiwa na wenzetu upande wa TARURA na sisi mkazo mkubwa kupitia Mfuko wa Barabara ni kuhakikisha kwamba wanapata fedha za kutosha barabara iweze kupitika.

Kwa hiyo, utaratibu wa sasa wa Serikali ni kuunganisha maeneo ya mikoa na mikoa, na maeneo muhimu ya uzalishaji. Kwa hiyo, siku za mbeleni pia barabara hii tutaitazama baada ya kuwa muunganiko umekuwa mzuri kwa barabara za lami.
MHE. OMARY A. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Handeni - Mziha na barabara ya Handeni- Kibirashi kutokana na mvua hazipitiki sasa hivi. Je, ni nini uamuzi wa Serikali kuhakikisha kwamba wanaokoa zile barabara ziweze kupitika wakati tunasubiri ziwekwe lami ili wananchi waweze kusafirisha mali zao na wao waweze kusafiri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Omary Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza uniruhusu niwape pole sana wananchi pamoja na Mheshimiwa Mbunge Kigoda kwa sababu maeneo yale nilitembelea walipata shida kubwa sana wakati wa mvua ilipokuwa kubwa na maji yalikuwa mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake tumechukua hatua za dharura kurejesha miundombinu katika maeneo haya. Kulikuwa na uharibifu mkubwa daraja lilikatika pale Nderemi pamoja na bwawa kubwa ambalo lilisababisha pia kukatika kwa daraja hili, tumerejesha kwa kushirikiana na Jeshi na sasa panapitika na maeneo mengine pia tumeweza kutengeneza barabara ya kilometa 24 kuunganisha Mji wa Handeni pamoja na Mziha na sasa panapitika.

Pia tumeiunga barabara ya Handeni pamoja na Korogwe, niseme kwa ujumla tumejipanga kuimarisha maeneo yote yaliyoathirika na mvua na Bunge lako limetenga fedha kwa ajili ya kumudu dharura zinazojitokeza, tutaendelea kutumia fedha za dharura katika maeneo yote nchini ambapo tutakuwa tunapata uharibifu wa mvua, kurejesha miundombinu ili wananchi waendelee kupita wakati wote.
MHE. OMARY M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Handeni- Kibirashi hadi Kiteto imekwisha na hatua zote za mwisho zimeshakamilika; na kwa kuwa barabara hii ni barabara ya kimkakati inaunganisha mikoa minne kwa maana ya Mkoa wa Tanga, Manyara, Singida na Dodoma. Je, Serikali sasa haioni umuhimu kuanza kutengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami ili kuondokana na kero hii ya mara kwa mara? Hivi ninavyosema muda huu barabara hii haipitiki kwa wiki sasa.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kigua, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali inafahamu umuhimu wa barabara hii ndio maana usanifu wa kujenga barabara hii kilometa 461 kutoka Handeni kwenda hadi Singida umeshakamilika. Kwenye bajeti yetu tumetenga fedha kuanza ujenzi wa lami wa barabara hii kilometa 50, kwa hiyo Mheshimiwa Kigua naomba avute subira na kwamba tukipata fedha tutaanza ujenzi. Hata hivyo, kuna maeneo yalikuwa yameathirika na mvua kama nilivyojibu swali langu la msingi, ni kwamba tumejipanga kurejesha maeneo yote ambayo ni korofi na kama mvua zitaendelea kunyesha maeneo yoyote yatakayoonekana kuwa ni korofi tutakwenda maeneo hayo kufanya marejesho ya barabara.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni lini Serikali itajenga barabara ya baypass ya kutoka Mpemba kwenda Tunduma kwa sababu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati anafanya kampeni zake kipindi cha mwaka 2015?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakajoka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua umuhimu wa baypass na usanifu unafanyika, tutajenga mara moja tukipata fedha kwa ajili ya barabara hii.
MHE. SHABAN O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Barabara ya kuanzia Dochi- Nguli – Mombo ambayo ni kilometa 16 mara nyingi nishauliza swali hili lakini sipati majibu na sasa hivi hali ya barabara ile sio nzuri. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuhakikisha kwamba barabara ile inatoboka ili wananchi wangu waweze kupata huduma ya haraka?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shekilindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mvua zilizonyesha hivi karibuni ziliathiri karibu maeneo yote ya Mkoa wa Tanga na sisi kama Serikali tumejipanga kurejesha maeneo hayo yaliyoharibiwa ikiwemo maeneo ya Dochi kwenda Mombo na eneo la kule Mchinga na maeneo mengine ya kule Pangani tumejipanga vizuri, wenzetu wa TANROADS wako kazini, Mheshimiwa Kilindi aondoe hofu tunafanya marejesho makubwa na kazi zinaendelea.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ya kukamilisha Daraja la Sibiti. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la pili, kwa sababu sasa Daraja hilo Sibiti limekamika na magari makubwa yanapita juu yakiwemo ma-semi trailer na makampuni mbalimbali ya mabasi yanayoonesha nia ya kupita huko ikiwemo Simiyu, Turu basi. Je, Serikali ipo tayari kuimarisha madaraja madogo madogo yanayokadiriwa kufikia nane ambayo yapo hatarini kuvunjika kutokana na uzito wa magari yanayopita kwenye daraja hilo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; barabara hiyo kwa sababu tumeelezwa kwamba itajengwa, Serikali ina kauli ipi kwa wananchi ambao wamewekewa alama ya X kwenye Vijiji vya Chemchem, Ibaga, Gumanga, Kisuluiga, Nduguti, Ishenga, Kinyangiri na Iguguno? Wangependa kupata kauli kuhusu hatima yao ya maeneo ambayo walikuwa wanayamiliki.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiula, kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kiula namna anavyopigania maeneo ya Mkalama na Mkalama inafanya uzalishaji mkubwa sana wa mazao ikiwemo vitunguu na mahindi. Mheshimiwa Kiula mwenyewe ni mkulima kwa hiyo anafahamu mahitaji muhimu ya barabara katika maeneo yake. Niseme tu kweli barabara hii kutoka Iguguno Shamba kwenda Sibiti kilomita 103, iko kwenye utaratibu mzuri wa kuiboresha sana na Mheshimiwa Kiula atakubalina nami kwamba yale madaraja makubwa tumeshaanza kuyafanyia ujenzi na kuna miradi ya ujenzi inaendelea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Kiula kwamba, yale makalavati madogo madogo ambayo sehemu nyingi yanaonesha kuwa yana usumbufu tunaendelea kuyashughulikia ili yakae vizuri ikiwa ni pamoja na kuondoa zile kona, kwa sababu sasa hivi baada ya kukamilika Daraja la Sibiti magari makubwa nafahamu kwamba yanapita katika barabara hii kwenda kwenye mikoa hiyo ya Simiyu pamoja na Mwanza. Kwa hiyo tunaendelea kufanya marekebisho makubwa ili kusiwe na usumbufu, lakini pia kuepusha ajali ambazo zinaweza kutokana na barabara jinsi ilivyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu wananchi waliowekewa alama ya X niwahahakikishie wananchi hawa, kwanza niwapongeze na kuwashukuru kwa kutoa ushirikiano kwa kuwa na utayari wa kupisha eneo la mradi wa barabara hii muhimu na wananchi hawa wanafahamu kwamba barabara ni kwa ajili ya maendeleo yao. Kwa hiyo, niwahakikishie tu kwamba tumeweka alama za X ili kuwatahadharisha wananchi wasifanye maendelezo makubwa katika maeneo haya. Baada ya kumaliza usanifu wa awali na upembuzi yakinifu, tutajua gharama za kuwafidia wananchi hawa. Niwahakikishie wananchi hawa kwamba tutawafidia ili kupisha mradi ili tuweze kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.

Matatizo ambayo ameyaeleza Mheshimiwa Kiula yamefanana na Wilaya ya Ikungi ambayo ndiyo Jimbo la Singida Mashariki lilipo. Wakati nauliza swali hili naomba niwahakikishie wananchi wa Jimbo la Singida Mashariki, niko imara kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitaka niseme tu, kwa kuwa barabara au miundombinu ya barabra ndiyo inayosaidia kukuza uchumi wa wananchi; na kwa kuwa barabara ya Njiapanda – Makiungu – Kwamtoro mpaka kule Handeni ni barabara ambayo imekuwa ikifanyiwa upembuzi muda mrefu: Ni lini sasa Serikali itaanza kuijenga na kuweza kusaidia kukuza uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Ikungi na Mkoa wa Singida? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mtaturu na nimhakikishie tu kwamba tutampa ushirikiano wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yake ya kibunge katika eneo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba, barabara anayoitaja Mheshimiwa Mbunge kutoka Njiapanda kupitia Makiungu kwenda kwa Mtoro, itatoka Chemba kwenda mpaka Handeni, kilometa 461; ni kweli kwamba usanifu umeshakamilika na kwa kadri tutakavyopata fedha tutaanza kujenga barabara hii. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi kwamba mradi huu mkubwa wa Kilometa 461 utawanufaisha sana wananchi wa eneo lake na kwa kweli tumejipanga kama Serikali kuona kwamba tunawahudumia vizuri wananchi katika eneo lake.nnAhsante. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Barabara ya Mitema Upinde kwenda Msinji iliyopo upande wa Tunduru ni sehemu ya barabara hiyo ya ulinzi katika upande wa mto Ruvuma. Barabara hiyo ilitolewa madaraja yake wakati wa vita vya Nduli Iddi Amin, na tangu yametolewa madaraja yale mpaka leo bado hayajaweza kurudishwa. Ni lini Serikali itarudisha madaraja yale ili barabara hiyo iweze kupitika kwa urahisi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Barabara ya Tunduru na Masakata Liwanga mpaka Misechela ni barabara ya ulinzi ambayo inaunganisha Msumbiji na Tanzania kupitia katika Kijiji cha Misechela. Je, Serikali haioni haja ya kukichukua kipande hicho kiwe Barabara ya Mkoa kwa sababu mchakato wote wa kufanya barabara hiyo ichukuliwe na TANROADS ulishafanyika kwa ngazi ya Mkoa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, anafuatilia sana hususani mtandao wa barabara katika maeneo yake. Niseme tu kwamba hii barabara ya Itema Msinji ilitolea madaraja. Utaratibu wa kwetu kawaida ni kwamba madaraja yaliyowekwa kwa wakati wa dharura huwa tunayatoa na kuyahifadhi kama asset; pale ambapo itahitajika sasa kuyaweka madaraja haya sehemu zingine tutaenda kuyaweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge nielekeze tu wataalamu waangalie maeneo haya kama yanastahili kurudishia madaraja haya yaliyotolewa tutafanya utaratibu huo, lakini kama tutakuwa na mahitaji ya kujenga upya maeneo hayo ili kutoa huduma nzuri kwa wananchi pia tutafanya hivyo. Kwa hiyo nielekeze tu TANROADS Mkoa wa Ruvuma waangalie sehemu hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme tu kwamba tunafanya upembuzi yakinifu wa barabara hii kutoka Mtwara – Pachani – Lusewa – Ligusenguse kwenda Nalasi (km 211), na tumetenga fedha za kutosha. Kwa hiyo wakati wa zoezi hili la kutambua changamoto zilizoko katika maeneo haya pia tutatazama kwa macho mawili maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu barabara hii ya Misechela kuwa Barabara ya Mkoa tumeanzisha chombo hiki cha TARURA. Sisi juhudi zetu ni kuhakikisha TARURA inapata fedha za kutosha, lakini kama kutakuwa na mahitaji mahsusi ya kupandisha Barabara hii tutaiangalia kwa nia hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge umeomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza, pamoja na majibu hayo, si ya kuridhisha kwa sababu Mheshimiwa Naibu Waziri Bunge lililopita Abdallah Mabodi alishasema kuwa pesa zimeshatengwa kwa bandari hiyo lakini mpaka sasa hivi bado yaliyofanywa ni madogo tu. Je, ni lini itajengwa bandari hiyo kwa sababu ina umuhimu sana Bandari ya Wete?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Bandari iliyoko Zanzibar ni bandari kuu, ambayo huwa wafanyabiashara wote wanaitegema bandari hiyo na bandari hiyo ni ndogo inabeba meli moja tu kuteremsha mizigo na meli hiyo inapoteremsha mizigo inachukua kati ya wiki tatu mpaka nne na kusababisha meli kuondoka na kuteremsha mizigo Bandari ya Mombasa, nchi jirani na kuikosesha mapato Serikali ya Tanzania. Je, ni lini utafanyika upanuzi wa bandari hiyo ili tuondokane na matatizo. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba Serikali ilitazama mahitaji kwa maana yale mahitaji ambayo nimejibu katika jibu la msingi yamefanyika, huu upanuzi ambao nimeutaja hapa lengo ni kuhakikisha kwamba wakati hizi juhudi kubwa zinafanyika za kufanya maboresho makubwa, zile huduma muhimu zinaendelea kufanyika katika bandari hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimtoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nilikuwa najaribu kufanya rejea kwenye commitment nzima ya upanuzi wa bandari upande wa Zanzibar. Kiasi ambacho kilipitishwa na wakuu wa nchi kama level funding kwa ajili ya bandari za Zanzibar peke yake ni dola milioni 2.131. hii ni kuonesha kuwa wakuu wako committed kuonesha kwamba tunafanya maboresho makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati huo sasa utaratibu ule wa kutafuta fedha unaendelea kufanya upanuzi mkubwa ndiyo maana unaona juhudi zimefanyika na juhudi zinaendelea ili kuhakikisha tunafanya maboresho makubwa. Kwa hiyo, nikutoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba upanuzi utafanyika, hii ni commitment ya hali ya juu ambayo inasimamiwa na wakuu wa nchi, tutakwenda kufanya upanuzi wa bandari hii.
MHE. MATTAR ALI SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Bandari ya Zanzibar kiukweli kwa sasa imekuwa ndogo sana na haiwezi kufanya kazi lakini Serikali zetu zimefanya mazungumzo na Benki ya Exim ya China, mpaka leo ni kimya hakuna kinachoendelea mpaka sasa. Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha hii bandari ya Mpigaduri inajengwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mattar kwa sababu mara nyingi nimemsikia akizungumzia sana juu ya Bandari ya Mpigaduri. Mheshimiwa Matar nikuhakikishie kwamba kweli Serikali imefanya kazi kubwa, kumekuwa na hatua mbalimbali, jitihada nyingi zimefanyika kupanua bandari na wewe unafahamu kwamba juhudi za kupanua bandari zimeanza muda mrefu tangu mwaka 2011 lakini hatua ambayo imefikia sasa hivi baada ya hiyo Benki ya Exim kuchukua hatua za kufanya funding kwa ajili ya upanuzi wa bandari hii sasa hivi draft financial agreement ilishasainiwa kwa hiyo wanafanya mapitio ya mwisho ili sasa kwenda kwenye hatua ya kwenda kwenye financing na kuanza kufanya maboresho Bandari hii ya Mpigaduri au Maruhubi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri ni mara kadhaa Serikali imekuwa ikichukua ahadi ikisema kwamba itaweza kujenga Bandari ya Wete, hayo ni masuala ya mdomoni lakini ukija kwenye vitabu halisi, kwenye Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Vote 34 fedha hizo haziko, mmekuwa mkidanganya mara nyingi watu wa Pemba. Mmekuwa mkisema uongo mchana kweupe bila giza. Kwenye Vote 34 ndiyo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, fedha hizo huwa haziko, hamtengi lakini mmekuwa mkisema mdomoni tu. Mtuambie hasa mna mkakati gani wa ziada muone kama fedha hizi mara hii mtazipeleka na bandari hii ya Wete mtaenda kujenga. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimualike tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tuonane uone ile document ya retreat nzima. Ninapozungumza juu ya miradi 17 ambayo kwa Afrika Mashariki ambayo inasimamiwa na wakuu wa nchi, kuna commitment ya jumla ya dola 61,000,212, ni fedha nyingi sana na ukiangalia kwa undani utaona miradi ilivyochambuliwa na hatua zinazokuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukiiangalia hii document na hii commitment ambazo tunzisema hapa ni commitment ambazo zinachukua muda mrefu na kuna action plan. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, nikuombe tu tuonane ili kwa pamoja tuzungumze ili upate picha, na uweze pia kuisema kazi nzuri Serikali inayofanya kuhusu maendelezo ya bandari hii muhimu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa kuwa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Jiji la Mwanza unahusisha makazi ya watu katika Kata za Shibula na Kahama, na kwa kuwa Mwezi Januari mwaka huu timu ya Mawaziri wanane ilifika katika kata hizo na kuwaahidi kwamba watalipwa fidia zao. Sasa nataka kujua; Serikali inawaambia nini wananchi wa kata hizo kuhusu fidia hizo?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kumekuwa na kusuasua katika ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Mtwara, na taarifa zilizopo ni kwamba kwa sababu hakuna fedha za uhakika. Swali langu; je, ni lini Serikali itapeleka fedha hizo ili uwanja ule uweze kukarabatiwa kwa kiwango kinachokubalika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kwenye eneo hili la Uwanja wa Ndege wa Mwanza wapo wananchi ambao wanadai fidia. Na ni kweli kuna timu ya Mawaziri ambao wanahusika na ulipaji wa fidia hii walikuwa na jukumu la kushughulikia ili wananchi waweze kulipwa mapema. Ninawaambia nini wananchi wa maeneo haya; ninawaambia ule utaratibu unakamilishwa na ni mapema kadri itakavyowezekana watalipwa hizi fidia, kwa hiyo wasubiri tu mambo yanaendelea kukamilishwa.

Mheshimiwa Spika, na niseme na pia Mheshimiwa Mbunge Mabula yuko hapa, anafahamu kwa sababu karibu kila siku anafuatilia juu ya ulipaji wa fidia ya wananchi ambao wengi wako pia kwenye eneo lake. Kwa hiyo wananchi hawa wasiwe na wasiwasi, tunalifuatilia na kulishughulikia suala hili ili waweze kulipwa mapema iwezekanavyo. Lakini pia wakilipwa kuna kazi ambayo nimeitaja itafanyika ili iweze kufanyika, na utaratibu ulivyo ni wananchi walipwe kwanza fidia ili maboresho kadhaa yaweze kuendelea katika uwanja huu.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu Uwanja wa Ndege wa Mtwara, labda nimkumbushie tu Mheshimiwa Mbunge, atakuwa amesahau, ni hivi karibuni tu Mheshimiwa Rais alivyofanya ziara Mtwara alitoa maelekezo na sisi kama Wizara maelekezo yale kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, kuna fedha zilitolewa na kazi inaendelea vizuri katika ujenzi huu wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara.

Mheshimiwa Spika, na nikwambie Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu tumejipanga kuhakikisha kila wakati tunaboresha uwanja huu na mwaka wa fedha huu unaokuja Bunge hili, Bunge lako limetupitishia fedha ambazo ni takribani bilioni 4.5, mmetuidhinishia ili sasa hii kazi isilale, kwamba kwa maana ya fedha zilizokuepo katika mwaka huu wa fedha na mwaka ujao tuna fedha za kutosha, hatutasinzia kwenye ujenzi wa uwanja, maboresho yatafanyika tuweze kukamilisha na wananchi waweze kupata huduma ya Uwanja wa Ndege huu wa Mtwara.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, utakubaliana na mimi kwa sababu na wewe pia ni mdau wa Zanzibar, unalea chama chako kwa upande wa Kaskazini na upande wa Kusini na mara nyingi unatumia usafiri wa bandari, hutumii usafiri wa ndege na unakutana na wapigakura.

Mheshimiwa Spika, changamoto iliyopo bandarini ni kuwa hata kilokumi zinakuwa charged na imekuwa ni malalamiko sana kwa wananchi. Ni vigezo gani ambavyo vinatumika kwa mizigo ya biashara na mizigo binafsi kwa hawa wasafiri? Naomba Serikali ifafanue kwa sababu mtu anapita na kilo 20 za mchele anakuwa charged. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukilalamika mara kwa mara abiria wanaokwenda Zanzibar. Kuna hizi boti za Bakhresa wana nauli zao kwenye mizigo, lakini sasa pale kwenye bandari imekuwa mara kwa mara inarudiana. Naomba kauli ya Serikali, hizi kauli zinazotolewa humu Bungeni ni lini zitafanyiwa kazi kwa vitendo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, vigezo vinavyotumika nimevitaja na vinapatikana kwenye tariff book. Labda hata baadae Mheshimiwa Mbunge naweza pia nikamuelekeza kwa sababu pia tariff book iko kwenye website ya Mamlaka ya Bandari ili kuweza kuongeza ufahamu na atusaidie kupunguza pia usumbufu.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hapa inaonekana kwamba ni uelewa na mimi nitumie tu nafasi hii kutoa maelekezo kwa Mamlaka ya Bandari ili kwamba tuweze kuweka ufafanuzi wa kutosha kwa abiria wanaotumia bandari hii kwenda Zanzibar ili waweze kuweka mabango yanayoonekana kuonesha vigezo vinavyotakiwa huu uzito wa kilo 21 na kwenda mbele ndiyo wanatakiwa kutozwa. Lakini pia waweze kutoa ufafanuzi na kutoa maelekezo na mimi ntalifuatilia hili ili kuona kwamba hili tunalitekeleza kupunguza usumbufu kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo nia ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuona wananchi wake wanateseka.

Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hiyo ndiyo maana nasema nitafuatilia ili kuona kwamba usumbufu unaondoka, uelewa unaongezeka kwa wananchi wanaotumia bandari. Wakati mwingine wanaingia kwenye kutozwa kutokana na kutokuelewa.

Mheshimiwa Spika, lakini msisitizo mkubwa niseme tu kwamba wale wanaofanya biashara wapitie kwenye eneo maalum kama nilivyosema, ambalo ni kwa ajili ya biashara, wakijichanganya na abiria wengine inaongeza usumbufu ambao Mheshimiwa Mbunge ameutaja.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, amezungumza kwamba kuna usumbufu kwenye usafiri wa boti ya Bakhresa, na wiki iliyopita tu kulikuwa na swali lilijibiwa hapa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Serikali tutaendelea kuchukua hatua na tutafuatilia vizuri ili menejimenti ya mamlaka iweke usimamizi madhubuti ili wananchi hawa wasiendelee kupata shida na sisi kama viongozi upande wa Wizara tutalisimamia hili ili usumbufu tuweze kuupunguza na hatimaye tuumalize kabisa.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Mindombinu ya Bunge ilitoa maelekezo kwa Serikali kwamba iangalie sasa barabara zinazounganisha Wilaya na Wilaya, Mkoa na Mkoa zipewe kipaumbele za kupandishwa hadhi kuwa barabara za TANROADS. Barabara hii mchakato wa kupandishwa hadhi ulianza mwaka 2013, lakini mpaka leo hii kumekuwa kuna maneno haya kwamba tumesimamisha. Nataka nipate tu kauli ya Serikali, sababu zipi zilizopelekea kusimamisha barabara ambayo tayari mchakato wake ulishaanza mwaka 2013?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mpaka sasa hivi barabara haipitiki kabisa na nimeuliza katika swali langu la msingi, ni hatua gani za dhararu Serikali inaweza kuzichukua ili kuhakikisha barabara hii inapitika.

Sasa maelezo yaliyozungumzwa na Mheshimiwa Naibu Waziri ni mipango ya muda mrefu. Sasa hivi watu hawapati nafasi ya kupita, watu wanakufa katika maeneo yao, mazao yanaharibika, ni hatua zipi za dharura zitakazosaidia barabara ipitike?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Mgimwa kwa sababu barabara hii ameizungumza sana hata wakati akichangia kwenye bajeti ya Wizara, ameizungumza barabara hii. Pia niseme tu kwamba tumekuwa na chombo hiki cha TARURA na niseme kwamba TARURA imeanza vizuri kwa sababu imefanya kazi kubwa sana kwa muda mfupi. Hivi ninavyozungumza TARURA wamemaliza zoezi la kuzitambua barabara zetu ili sasa kuona urefu wa barabara zote kwenye Halmashauri za Wilaya zetu, kuangalia hali za barabara na idadi.

Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi linafanyika kuangalia idadi ya magari yanayopita katika maeneo, lengo kubwa ni kuweza kufanya uchambuzi na hivi ninavyozungumza iko kamati maalum ambayo inakaa kule Morogoro itamaliza kazi yake mwezi huu wa Juni, ikiwa na wajumbe kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara, Wizara ya Ujenzi, TAMISEMI, Maliasili na Utalii, TANROADS, TARURA wenyewe, Wizara ya Ardhi na Ofisi ya AG ili sasa kuweza kuzipanga upya barabara zetu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mgimwa naomba uvute subira tu kwamba pamoja na status ya barabara pia itatazamwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumza juu ya maboresho ya haraka kwenye maeneo haya kama hapapitiki. Nafahamu kwamba kipindi kilichopita tumekuwa na mvua nyingi sana na maeneo mengi yamekuwa hayapitiki kwa sababu pia kumekuwa na changamoto hii ya wakati wa mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuelekeze tu Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Iringa ashirikiane na wenzetu upande wa TARURA tuone maeneo ambayo wananchi hawapiti tuweze kukwamua waweze kupita.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi hili nitalifutilia ili wananchi wapite wakati hizi hatua nzuri ambazo nimezitaja za kuiboresha hii barabara ili kuiunganisha kutoka eneo hili la Mufindi kwenda Morogoro kupitia Mlimba liweze kwenda vizuri.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mgimwa naomba uvute subira, natambua pamoja na Kamati kutoa maelekezo lakini hatua za haraka tumezichukua, tutazipanga barabara zetu na hii barabara yako Mheshimiwa Mgimwa tutaitendea haki.
MHE. WILLIAM D. NKURUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme kwamba TARURA naikubali na nafahamu uwezo wake lakini ni kwamba kuna maeneo TARURA inakuwa na uwezo mdogo ndiyo maana tunakuja na haya maswali.

Sasa nilitaka nimuulize Mheshimiwa Waziri kwamba ni lini barabara kutoka Mangaka hadi Matekwe Wilaya ya Nachingwea mpaka Liwale Wilaya ya Liwale itaweza kupandishwa hadhi kwa sababu tayari Wilaya zote tatu zimeshaombea kupanda hadhi? Naomba majibu ya Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme kama nilivyozungumza muda mfupi kwamba kulikuwa na changamoto ya mgao wa fedha kwa kuzingatia mahitaji ya maeneo husika na hali ya jiografia ndiyo maana baada ya TARURA kuwepo tumelazimika kufanya uratibu na kuzitambua barabara zote ili sasa ziweze kupata huduma kadri inavyostahili kutokana na uwiano wa namna pia tunavyopata fedha. Kwa hiyo, hilo zoezi limeenda vizuri na ninaamini kabisa kati ya maeneo ambayo labda wakati mwingine hayakupata allocation nzuri, baada ya zoezi hili yatapata mgao kulingana na uwezo wa kifedha, lakini pia kulingana na mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara ya Mangaka - Nachingwea kwenda Liwale zipo hatua kadhaa zinaendelea, kutoka Nachingwea kwenda Liwale kilometa 129 tumeanza usanifu kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami, lakini nafahamu kutoka Nachingwea kuja Mangaka kwamba liko zoezi wakati wote tumetenga fedha tutaanza ujenzi wa lami. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dua na kwa vile pia ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu tukutane tu hata baadae pia uweze kuona mpango mzima wa maeneo tulivyojipanga kwa ajili ya kuboresha barabara zetu katika mkoa huu wa Mtwara pamoja na barabara zetu upande wa Lindi.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa kweli ukizungumza suala la barabara, ukiangalia Mheshimiwa Mgimwa, Mheshimiwa Mwamoto na Mheshimiwa Hongoli wote hawa wanatobozana kwenye Jimbo langu. Hiyo inakuza uchumi ndani ya Mkoa wa Morogoro Wilaya ya Kilombero hususan Jimbo la Mlimba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ulivyosema siku ile nipewe maji hivi sasa hali ya barabara ya Ifakara – Mlimba inapitika kwa magari tu ya mizigo midogo midogo, magari ya abiria hayapiti kwa hiyo kupata taabu sana kina mama ambapo wanakwenda kufuata huduma ndani ya Wilaya ya Kilombero - Ifakara.

Je, Serikali ina mpango gani wa dharura kurekebisha ile barabara ya kutoka Mlimba hadi Ifakara ili kina mama na watoto na abiria wengine na mizigo sasa hivi tunavuna ili ipate kupita kwenda sokoni na kupata huduma za jamii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mlimba pamekuwa special kidogo kwa sababu yako mahitaji ya kuunganika na Njombe kwa maana ya kutoka kule Lupembe, Madeke kuja Mlimba, lakini iko kiu ya kuunganishwa na Mufindi kama Mheshimiwa Mgimwa alivyozungumza, lakini pia kutoka Kilolo kuja Mlimba. Kwa hiyo, utaona wananchi wa maeneo haya na kihistoria walikuwa sehemu moja na bado shughuli zao za kiuchumi zinafuatana. Niseme tu kuhusu mpango wa dharura wa kutengeneza maeneo haya na Mheshimiwa Susan amerusha picha nyingi sana kuonesha wananchi walivyopata adha nyingi sana wakati wa mvua zikiwa nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, atakubaliana na mimi kwamba wakati wa mvua zikiwa nyingi na maji yakiwa mengi kufanya matengenezo kwenye barabara zetu inakuwa ni ngumu, lakini kwa vile mvua zimepungua na tunazo fedha za emergency kwa ajili ya matengenezo. Tumetoa maelekezo kwamba mvua zikipungua mara moja cha kwanza ni kuhakikisha kwamba maeneo ambayo yameharibiwa na mvua yanarekebishwa ili wananchi waendelee kupata huduma hii ya barabara, huduma muhimu.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Susan vuta subira tumea maelekezo na ninarudia kuelekeza wenzetu TANROADS Mkoa wa Morogoro baada ya mvua kupungua sasa nguvu kubwa ielekezwe kwenye maeneo ambayo wananchi wamepata shida wakati wa mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni. Ahsante sana.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya kuanzia Mlalo – Ngwelo – Mlola – Makanya – Milingano hadi Mashewa iliombewa kupandishwa hadhi toka mwaka 2009 sambamba na barabara ya Dochi hadi Mombo.

Je, ni lini barabara hizi zote mbili zitapandishwa hadhi ili wananchi wangu waweze kuondokana na adha wanayoendelea kuipata sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shekilindi al-maarufu kama Bosnia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara alizotaja Mheshimwa Mbunge yaani kwa maana ya ile barabara ya kutoka Mlalo kwenda Makanya na hii barabara ya Dochi, kama nilivyozungumza kwamba kamati maalum inaendelea na kikao kufanya mapitio ya kuweza kurekebisha na kuweka hadhi za barabara zetu zote nchini. Kwa hiyo, Mheshimiwa Shekilindi naomba avute subira, baada ya zoezi hili tutamfahamisha kwamba barabara zake hizi zime-meet vigezo ili tuone kama zinaweza kupandishwa hadhi, lakini lazima shughuli za kitaalum zifanyike kabla ya hatua ya kupandisha hadhi barabara hii, kwa hiyo, vuta subira muda siyo mrefu utapata majibu yake.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba tu kupata ufafanuzi wa Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na majibu yake mazuri. Tatizo la barabara la Dutwa – Imalamate – Ngasamo kwenda mpaka Nyashimo lilikuwa kwenye ahadi ya Mheshimiwa Rais na huu ni mwaka wa nne kwamba iwe kwa kiwango cha lami.

Nilitaka tu kujua, ni lini sasa barabara hii itawekewa lami kulingana na ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amefuatilia sana hii barabara, kwa hiyo hata nikikutana naye nje huwa namwita Mzee wa Nyashimo kwa maana ya umuhimu wa barabara hii. Nafahamu pia Mheshimiwa Chenge anaizungumza sana barabara hii, lakini nafahamu pia kwamba iko ahadi ya Mheshimiwa Rais. Niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Chegeni kwamba ahadi zote za viongozi tunaendelea kuzitekeleza, kadri tunavyopata fedha tutatekeleza ahadi za viongozi.

Kwa hiyo, ahadi ni deni na usiwe na wasiwasi na mimi naifuatilia sana barabara hii kwa umuhimu wake ili tuweze sasa kwenda kwenye kujenga katika kiwango cha lami, tukipata fedha tutakwenda kujenga barabara hii.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, pia naipongeza Serikali kwa kutenga shilingi milioni 100 kwa kuanza matengenezo haya ya barabara ya Iyogwe – Chakwale – Ngilori. Barabara hii ni muhimu sana na hasa kwa upande wangu naona ni muhimu sana kwa upande wa jamii pamoja na uchumi. Nikisema jamii ni kwa sababu wakati wa kipindi cha mvua inakuwa matatizo kupitika hii barabara. Mto huu wa Chakwale, Nguyani na Matale mpaka sasa hivi zina drift culverts, lakini inakuwa muhimu sana na inakuwa matatizo kwa sababu maporomoko ya maji yanakuwa mengi sana wakati wa mvua kiasi wanafunzi wanashindwa kupita na magari.

Je, nauliza Serikali kwa sababu mpaka sasa hivi kuna drift culverts ambazo bado matatizo, kwa nini haikufikiria kuwa iweke box culverts kwa mito hii mikubwa yote mitatu ya Chakwele, Nguyani pamoja na Matale? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, barabara ya Gairo – Enongwe pamoja na barabara ya Mzumbe – Mgeta ni barabara muhimu sana kwa mazao ya mboga mboga. Barabara hizi zina ahadi za Mheshimiwa Rais kwa kutengeneza kwa kiwango cha lami; Je, ni lini barabara hizi zitaweza kutengenezwa kwa kiwango cha lami? ahsate. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwenye barabara hii ni barabara ambayo ina changamoto. Mimi nimeitembelea barabara hii, nimeona maeneo haya anayataja Mheshimiwa Mbunge, lakini pia Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano hivi karibuni alitembelea eneo hili akajionea changamoto ambazo zipo. Kuna maeneo korofi kwa mfano eneo la Nguyani ambalo tunasema tutaweka drift daraja ili iweze kutusaidia wakati ule mpango mkubwa wa kufanya box culvert kubwa inatengenezwa pale.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tatizo la eneo hili tunalitambua, wapo watu ambao wamepoteza maisha katika eneo hili, ukienda eneo hili la Nguyani wanapaita ni mto kaburi kwa sababu ya historia kwa muda mrefu kumekuwa na changamoto. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tunalitambua hili na niseme katika bajeti yetu ya mwaka huo unaokuja ziko fedha ambazo tumezitenga kwa ajili ya kushughulikia maeneo korofi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sambamba na kuweka hii culvert, lakini pia tunaitazama kwa mapana kwa sababu Mheshimiwa Mbunge wa eneo la Gairo tumekubaliana tutafuatana naye pamoja na Katibu Mkuu kwa sababu ya kuona namna ya kwenda kwa haraka kuwarekebishia wananchi hawa.

Kwa hiyo, nikutoe hofu kwamba eneo hili tunalifahamu na tunachukua hatua, na kupitia fedha ambazo Bunge hili limetupitishia yapo maeneo pia ambayo tuna allocation ya fedha kwa maana ya kushughulikia maeneo korofi. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na kiasi cha fedha tulizotenga, lakini jicho la pili linatazama eneo hili tuweze kuliboresha ili wananchi tuwaokoe kwenye hatari waliokuwa wanaipata, lakini waweze kupita kwenda kwenye shughuli za kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ahadi za Mheshimiwa Rais barabara unayoitaja ya Mzumbe – Mgeta kama nilivyozungumza, ahadi zote za viongozi wakuu ikiwemo Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu tutaendelea kuzitekeleza. Katika Mkoa wa Morogoro yako maeneo ambayo utekelezaji wake wa ahadi hizi uko karibu asilimia 100. Kwa hiyo, uone kwamba tunakwenda hatua kwa hatua, kwamba baada ya kufanya utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais kwenye baadhi ya meneo kwenye Mkoa wa Morogoro, itafika zamu ya eneo hili tutakwenda kufanya matengenezo kulingana na ahadi ya kiongozi mkuu Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

Mheshimiwa NaibU Spika, barabara mbili katika Jimbo la Nkasi Kusini zinazounganisha Makao Makuu ya Kata, Kata ya Kizumbi barabara ya Wampembe Junction - Kizumbi na barabara ya kwenda Makao Makuu ya Kata ya Ninde zote zimevunjika, madaraja yamevunjika na sasa hazipitiki kabisa na barabara ya Kizumbi tuliweza kumpeleka Mheshimiwa Waziri Jaffo alipotutembelea lakini bado mpaka sasa tunafuatilia sana hatujapata hizo pesa.

Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba barabara hizi zinafunguka na wananchi wa Kata hizi wanafikiwa kwa huduma mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu utaratibu wa matengenezo wa barabara zetu kupitia fedha ambazo zinatoka kwenye mfuko wa barabara ambao unapeleka fedha TANROADS na kupeleka fedha pia upande ule wa TARURA, utaratibu ni kwamba asilimia 90 ya fedha zote zinakwenda kwa ajili ya kurejeshea miundombinu hii kwa maana ya matengenezo na asilimia 10 ndiyo inakwenda kwa ajili ya ujenzi wa barabara mpya.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mipata sijafahamu sawasawa labda baadae tuzungumze tuone kama hii barabara iko chini ya TARURA kwa sababu mmemtembeza Mheshimiwa Jaffo, lakini sisi kama Wizara ya Ujenzi tunashughulikia sera hii ya barabara, tunao wajibu wa kushirikiana na wenzetu upande wa TAMISEMI, kwa hiyo tuione, lakini kikubwa ni kwamba nimuombe tu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa aweze kuwasiliana na wenzake upande wa TARURA tuone kwamba eneo hili nani analishughulikia, lakini ni muhimu kwamba eneo hili lishughulikiwe mapema. Naelekeza kwamba lishughulikiwe mapema haya madaraja yatazamwe yarekebishwe ili wananchi wapate huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nitatazama kwa makini eneo hili na saa nyingine utanipa details za kutosha ili tushughulikie eneo hili wananchi wako wasipate shida na najua wanayo hamu ya kupita katika maeneo haya kwa sababu maeneo haya yana uzalishaji mkubwa sana hasa mazao ya kilimo.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na matengenezo ya mara kwa mara ambayo hayakidhi haja ya barabara kubwa inayotoka Mtwara Mjini mpaka pale Mnazi Mmoja, Manispaa ya Lindi kwa sababu barabara hii imekuwa inaharibika sana kwa magari yanayosafirisha saruji kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam na Serikali inaahidi kutengeneza kwa kiwango kikubwa lakini mpaka leo barabara hii ina mashimo, wanaweka viraka vidogo vidogo lakini hairekebishwi vile ambavyo inatakiwa kujengwa.

Je, ni lini Serikali inatekeleza ahadi yake ya kutekeleza na kutanua barabara hii kwa kiwango cha lami kutoka Mtwara Mjini mpaka Mnazi Mmoja na kule Nanganga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hii ya kutoka Mtwara kuja Mnazi Mmoja - Mingoyo inatumika sana na magari makubwa ambayo yanabeba mzigo mkubwa hususan saruji, na ni kweli barabara hii nimeipita ina mashimo na tunaendelea kuyaziba hayo mashimo ili huduma iweze kurejea, lakini Mheshimiwa Mbunge utakubaliana na mimi kwamba barabara hii imedumu kwa muda mrefu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zina umri wake na barabara ndiyo maana zinaendelea kuhudumiwa lakini barabara ukiikuta imekaa zaidi ya miaka 30 inastahili sasa hiyo barabara tuibadilishe kabisa kwa sababu ndiyo maana unaona ukiziba hapa sehemu nyingine inafumuka kwa sababu ule muda wa kuishi wa barabara hii umetimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba uko mpango kabambe ambao tutakuwa na mradi wa World Bank ambao taratibu zinaendelea vizuri kwamba tutaifanyia matengenezo na kuijenga upya barabara hii kutoka Mtwara kuja Mnazi Mmoja kwa maana hiyo na kutoka pia Mnazi Mmoja kwenda mpaka Masasi kwa hiyo upo mradi unaendelea vizuri. Kwa hiyo wewe uwe comfortable hatua zinaenda vizuri. Wakati ukifika utaona tunaenda kufanya maboresho makubwa ya barabara hii muhimu na mahitaji ya matumizi ya barabara hii sasa hivi yameongezeka sana, hali ya Mtwara sio kama zamani, utakubaliana na mimi kwamba tunaitazama kwa macho mawili.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la msingi namba 358 limetaja barabara hii ambayo inaunganisha Wilaya ya Gairo na Kilindi, swali langu la nyongeza ni kama ifuatavyo; mwaka 2010 Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga barabara hii kw akiwnago cha lami. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kigua kwa sababu tumezungumza sana juu ya barabara hizi ambazo zinaunganisha Wilaya ya Kilindi na hii barabara ambayo nilikuwa nimeijibia swali kutoka Gairo kwenda Kilindi kama Mheshimiwa Kigua anavyosema ni barabara ambayo tunaitegemea siku za usoni na kutokana na ahadi ya Mheshimiwa Rais tutaiunganisha na barabara hii muhimu ambayo kwa hatua za ujenzi zimeshaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu tukishaanza kufanya usanifu hata barabara hii kubwa ukitoka Handeni unapita eneo la Kibirashi ambapo ndiyo barabara hii anaitaja Mheshimiwa Mbunge, itaungana na hii barabara tukiendelea kwenda kule Chemba hadi Singida. Kwa hiyo unafahamu kabisa tuko kwenye hatua ya ujenzi wa barabara ile. Niombe uvute subira, mahitaji ya ujenzi wa barabara ni mengi, tutaenda kidogo kidogo kadri fedha zinavyoruhusu ili tuweze kuendelea kufanya ujenzi huu na ahadi itakuwa inaendelea kutekelezwa hivyo. Kwa hiyo, vuta subira barabara ile kubwa itakwenda na hii ambayo itatuunga kutoka barabara kubwa ya kutoka Dar es salaam – Morogoro kuja Dodoma kwa maana ya Gairo kwenda Kilindi itaungana na hii barabara. Tunafahamu hivyo, kwa hiyo naomba uvute subira tu, usiwahishe shughuli, siku za usoni tutakwenda kujenga barabara hii.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, mwezi uliopita tarehe 15 Mei ilitokea ajali mbaya ikaua watu wanne papo kwa papo na wengine watano wakafa baadae na majeruhi katika Kivuko cha Daraja la Mto Una njiapanda ya kwenda KINAPA ambapo barabara hii ina madaraja manne na madaraja haya ni single deck na sio double deck ambayo yanasababisha ajali na hali sio nzuri.

Je, Serikali kwa udharura huu ambao barabara hii inapitisha watalii pia inayatengenezaje madaraja haya yawe na double deck badala ya single deck ili kuweza kuondoa ajali hizi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbatia amezungumza juu ya ajali, lakini akubaliane na mimi kwamba kunapotokea ajali yako mambo mengi, mengine ni yale makosa ambayo sisi kama binadamu tunayafanya na mengine yapo yanahusisha miundombinu, lakini engineer utakubaliana na mimi tafiti zinaonesha asilimia 80 ya ajali inatokana na human behavior (tabia za kibinadamu).

Kwa hiyo, kwanza nianze kutoa wito tu kwa watumiaji wa barabara wawe makini kwa sababu ninaamini kwamba sehemu ambayo tuna barabara hii kama unavyosema iko na single deck ziko alama ambazo zimeoneshwa kuchukua tahadhari, lakini wako watumiaji wachache wa barabara hawazingatii maelekezo yanayokuwa katika barabara zetu. Kwa hiyo nisisitize hilo tu watumiaji wote wa barabara wazingatie matumizi ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala lako la kuitengenza barabara hii katika madaraja hayo manne uliyoyataka kuwa double deck naomba nilichukue kama ushauri tuifanyie kazi tuone kwamba tunaweza kurekebisha kadri itakavyokuwa imewezekana.
MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ni dhahiri Mheshimiwa Waziri anafahamu wakazi hawa wananchi hawa wa maeneo ya Kata ya Genge, Kata ya Tanganyika, Kata ya Tingeni na Kata ya Bwembwera wamekuwepo katika maeneo haya zaidi ya miaka 50.

Naomba nifahamu kwa kuwa Serikali ilikuwa inaendelea kupeleka huduma na Serikali imesajili mpaka baadhi ya vijiji ambavyo vina maeneo yaliyopitiwa na reli ambayo sasa hivi imeekewa ‘X’. Je, Serikali iko tayari kuwalipa fidia wananchi wale kwa kuwa wao ndio walibariki wananchi kuendelea kuishi pale zaidi ya miaka 50? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Wilaya ya Muheza kunaendelea urasimishaji wa makazi na katika maeneo na nyumba za watu ambao wana ‘X’ wamewekewa ‘X’ wanaambiwa na wao walipe kwa ajili ya urasimishaji. Nilitaka kufahamu Mheshimiwa Waziri yuko tayari kusitisha zoezi hili ili mpaka wananchi wale wenye nyumba za ‘X’ wapatiwe ufumbuzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme kwamba wananchi wanastahili kupewa ile huduma muhimu ambazo Serikali inapaswa kuwapa wananchi inastahili wazipate kwamba hakuna sababu ya kuwaadhibu wananchi kutokana na makosa labda ambayo yalitokana na watendaji. Kwa hiyo kupata huduma wananchi ni haki yao, lakini niseme tu kwamba kuhusu fidia, zoezi la kulipa fidia linafanyika kwa mujibu wa sheria, tutaangalia Sheria ya Ardhi, Sheria ya Ardhi ya Vijiji ndio inatumika kulipa fidia kwa wananchi, kwa maana hiyo Mheshimiwa Mbunge ukubaliane na mimi kwamba fidia inalipwa kutokana na sheria na taratibu ambazo zipo, kwa wale wanastahili kulipwa fidia Serikali inaendelea kufanya hivyo kwa sababu ni haki yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu urasimishaji wa maeneo ambao zoezi linaendelea niseme tu kwamba sio vyema kurasimisha maeneo ambayo sio halali na mimi nafahamu wataalam waliopo kwenye maeneo haya watarasimisha maeneo tu ambayo ni halali kurasimisha na niseme tu kwamba Serikali itawachukulia hatua watumishi ambao watarasimisha maeneo ambayo hayastahili kurasmishwa kwa sababu ni kuvunja sheria, kwa maana hiyo wale watu waliowekewa ‘X’ kwa maana ya kupisha niwasihi tu wapishe maeneo haya kwa sababu ni maeneo ya reli na sio vyema kuendelea kuendeleza maeneo haya, kwa sababu tutaendelea kupata hasara bila sababu.

Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Mbunge tusaidiane tu kwamba wananchi wa maeneo haya ya Muheza uwashauri kwa maeneo ambayo unaona kabisa kiuhalali yako maeneo ya reli wapishe maeneo haya na kama kuna tatizo lilijitokeza kutokana na utendaji basi Serikali itachukua hatua kutokana na namna ya hali ilivyokuwa. Ahsante.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa. Nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, nilipenda kutoa nyongeza tu kwenye swali la pili la Mheshimiwa Yosepher.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba lengo na dhamira ya Serikali ni kuwawezesha Wananchi. Sasa unapokuta kwamba yuko kwenye eneo ambalo halitakiwi lifanyiwe urasimishaji maana yake ameingia kwenye eneo ambalo haliko kwenye mpango. Sasa na unaposema kwamba kuzuia watu wengine mpaka ufumbuzi upatikane, wale watu tayari wako ndani ya maeneo ambayo hayaruhusiwi kujengwa kwa sababu ni kwa kazi nyingine ambayo imewekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niombe tu Halmashauri zetu wawe makini katika kuangalia namna ambavyo vipimo vya barabara na reli ambavyo vimekaa kiasi kwamba watu wasiingie kwenye yale maeneo. Na sasa hivi Wizara imeanza kuweka mpango wa upimaji katika maeneo yanayopitiwa na reli. Kwa hiyo, ni vizuri wakazingatia yale masharti ambayo tunayatoa ili baadae wasije wakajikuta wameingia kwenye eneo ambalo haliruhusiwi. Ahsante.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara ya kutoka Masasi hadi Newala Serikali imekwishadhamiria kuijenga kwa kiwango cha lami na kwamba inatarajia kutangazwa zabuni mwezi wa saba.

Je, wananchi wa Kijiji cha Mpeta, Chiungutwa, Nagaga, Mkangaula pamoja na Msanga ambao walipaswa kulipwa fidia ni lini Serikali itawalipa fidia ili kupisha ujnzi huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni utaratibu wa Serikali kulipa fidia kabla ya kuanza ujenzi na kwa kuwa utaratibu wa kuanza ujenzi wa barabara hii muhimu, barabara ya uchumi hii kutoka Mtwara – Masasi – Newala utaanza hivi karibuni, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi hawa wa maeneo ya Mpeta, Chiungutwa, Kangaula na Lulindi kwa ujumla kwamba watalipwa fedha zao mapema, ili kupisha ujenzi kuanza kwa maana hiyo kwa sababu, tutaanza hivi karibuni ina maana kwamba ni hivi karibuni watalipwa kabla ujenzi haujaanza.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Shirika la Reli la Taifa linamiliki hayo maeneo kihalali, lakini kwa kuwa Wizara ya Ardhi na Halmashauri za Wilaya mbalimbali zimetoa hati za umiliki wa ardhi katika maeneo hayo hayo ambayo ni maeneo ya reli; kwa mfano kule Moshi Kiwanda cha Serengeti kiko chini ya eneo ambalo linamilikiwa na reli.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuondoa msuguano uliopo kati ya hati halali zilizotolewa na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na zile hati ambazo ziko chini ya Shirika la Reli la Taifa ili wananchi hawa na maeneo haya yaweze kuendelezwa kwa haraka iwezekanavyo? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Kubenea kwa kutambua kwamba maeneo haya yanamilikiwa kihalali na Shirika la Reli na ndio maana niendelee kumsihi Mheshimiwa Mbunge Kubenea na Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuwasaidia wananchi wetu kwa sababu maeneo ambayo unatambua ni halali na kama inatokea makosa ambayo ni ya kiuadilifu, wananchi wanapewa maeneo ambayo ni halali kwa ajili ya miundombinu ya reli kwamba sio vema. Kwa hiyo, tuwasaidie wananchi wetu na tuchukue hatua mnapema, ili Wananchi wasidumbukie kwenye shida ambayo inajitokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, na niseme tu hakuna msuguano, hakuna msuguano kwa sababu kama maeneo haya ni halali kwa ajili ya shirika la reli msuguano haupo, isipokuwa ni ile hali tu ya utovu wa nidhamu uliotokea kusababisha baadhi ya wananchi wachache labda wakamilikishwa maeneo sio kihalali. Kwa maana hiyo niendelee kutoa wito tu kwa watumishi wote wa umma kwamba tunapotekeleza majukumu yetu tutekeleze kwa kuzingatia sheria, ili tusiendelee kuwasumbua wananchi wetu kama tutakuwa tumevunja sheria.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo Muheza linafanana kabisa na tatizo lililoko pale Kurasini ambapo nyumba zilizokuwa za TRC zilikabidhiwa kwa TBA na TBA iliwauzia wapangaji waliokuwa katika nyumba hizo, lakini sasa hivi baada ya TRC kuwa vizuri imeenda tena kuzidai nyumba zile na kuwavunjia vibanda wale watu ambao wamenunua nyumba hizo.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inakwenda kutatua tatizo hili kwa kuwataka TBA kuwapa hati wale wote walionunua nyumba hizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, uko utaratibu wa kuwalipa fidia wananchi pale ambapo wanapopisha maeneo kwa ajili ya maendeleo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mtolea nikuhakikishie tu kama wananchi hawa walipewa hizi nyumba kihalali na wanastahili kulipwa, ni kwamba utaratibu uleule wa kupisha maeneo kwa ajili ya maendeleo utatumika kwa ajili ya kuwatazama hapo, lakini kwa sababu suala hili umelileta hapa naomba nilichukue kama mahususi ili tuangalie nini kilitokea na ili haki iweze kutendeka kwa wananchi hawa. Ahsante sana.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa kufanya ukarabati wa reli Tanga - Korogwe - Mombo na Mazinde na kuendelea. Nilikuwa nataka kujua kwenye maeneo yale ya reli kuna nyumba za Serikali ambazo zilikuwa zimejengwa kwa ajili ya watumishi ambao walikuwa wanaishi katika maeneo yale. Sasa katika ukarabati huu wa reli, je, mko tayari sasa kuzikarabati nyumba zile ili kusudi wale wafanyakazi waendelee kukaa kwenye zile nyumba kwa kusaidia kulinda mataruma yale yasiendelee kuibiwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza pongezi za Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya Serikali nazipokea, lakini na nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali imedhamiria kufanya maboresho makubwa katika mtandao wa reli ikiwepo maeneo haya ambayo umeyataja na kwa sababu hiyo, hivi karibuni tu Bunge lako limetupitishia fedha kwa ajili ya kufanya pia maendeleo ya mtandao mzima wa reli.

Nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, hizi nyumba ambazo zilikuwa za watumishi unazizitaja tutazifanyia ukarabati na kwa sababu, tumedhamiria kufanya maboresho tutaboresha mtandao wa reli pamoja na huduma nyingine ambazo zinahusiana na huduma hii ya reli. Ahsante sana.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kama ambavyo ameeleza kwamba maeneo yenye makazi wamepanua barabara kwa ajili ya kuangalia usalama wa raia na sasa hivi tunaweka zebra na matuta, lakini kumejitokeza matumizi mabaya ya zebra kwa sababu wakati mwingine unakuta waenda kwa migu ndio wanapewa muda mrefu sana kuliko hata magari na hivyo kusababisha msongamano.

Je, kwa nini Serikali isiweke taa za kuruhusu waenda kwa miguu, ili wao wawe wanapita pale kwa zamu badala ya kuwa wanapita wakati wote?

Mheshimiwa Spika, pili, matuta nayo imethibitika kwamba, kwa kuweka matuta mengi barabarani na matumizi ya madereva wetu imesababisha matatizo ya mgongo, hasa kwa wanaotumia magari.

Je, hakuna utaratibu mwingine wa kuweka usalama kwa waenda kwa miguu zaidi ya kuweka matuta barabarani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge na kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Hawa Ghasia kwa namna anavyofuatilia mambo mbalimbali ya maendeleo. Na niseme kuhusu matumizi ya zebra na matuta ni kwamba ni kweli kumekuwepo na changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini utakubaliana na mimi kwamba tunaweka zebra na matuta ni kwa ajili ya kuhakikiha wananchi wetu wanakuwa salama kutokana na baadhi ya watumiaji wa barabara kuwa wanatumia barabara zetu bila kuzingatia utaratibu na masharti yaliyowekwa ili kuwafanya wananchi wetu waweko salama. Kwa hiyo, nilikuwa napenda Bunge lako litambue kwamba uwekaji wa zebra na matuta haya ambayo saa nyingine yameonekana kuwa ni usumbufu, lakini ni nia njema ya Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wake wanabaki kuwa salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata hivyo Mheshimiwa Mbunge atakubaliana na mimi kwa siku za hivi karibuni tumejipanga vizuri maeneo mengi nchini tunaendelea kuweka taa. Kwa hiyo, iko mipango ambayo imefanyika na Halmashauri zetu, kuna taa nyingine wanaweka kupitia halmashuri zetu za wilaya na miji tunaendela kuweka taa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge hilo nimelichukua kwa maana ya kuweka msukumo mkubwa zaidi ili maeneo mengi tuweke taa kutoa usumbufu ambao unajitokeza, ili matumizi ya barabara yaweze kwenda sawasawa na watumiaji wa magari pia waweze kwenda vema.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme kuhusu matuta, kipindi sio kirefu sana nilijibu hapa swali kuhusu matuta kwamba, sisi Serikali tumeendelea kuyapunguza matuta maeneo mengi. Tuliweka matuta kwa sababu ya usalama wa wananchi, lakini tumegundua baada ya kuweka matuta elimu imeendelea kuwa kubwa kwa wananchi wetu wanaotumia barabara pale tunapothibitisha kwamba sasa eneo fulani hali ya hatari ya wananchi imepungua matuta hayo tumeyaondoa. Tumeondoa matuta mengi sana kwa hiyo, Mheshimiwa Hawa Ghasia kubaliana na mimi hilo, lakini kama kuna maeneo ambayo ni mahususi tutaona kuna matuta yanaleta shida mtufahamishe na sisi Serikali tutakuwa tayari kwenda kufanya marekebisho, ili kutoa usumbufu wa watumiaji wa barabara hususan wanaotumia magari.
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya maeneo tunaona kwamba kuna upanuzi wa barabara nikitolea mfano barabara ya Dodoma mpaka Morogoro, maeneo ya Gairo na maeneo ya Dumila. Je, ni hatua zipi zinazochukuliwa sasa kwa wale wakandarasi ambao kazi zao hazikukidhi viwango?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunaendelea kupanua barabara maeneo mbalimbali. Kama nilivyozungumza jana hapa ni kwamba asilimia 90 ya fedha zinazokwenda kwenye ujenzi wa barabara ni kwa ajili ya matengenezo, kwa hiyo, zoezi linaloendelea nchi nzima kufanya maboresho ya barabara ni la kawaida kwa sababu barabara zinavyotumika zinachakaa na saa nyingine kutokana na umri, kutokana na hali ya hewa na mambo mbalimbali, kwa hiyo, matengenezo hayo ni muhimu yanaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme tu kwamba upanuzi huu wa barabara au kazi zinazoendelea barabarani ni kwa mujibu wa mikataba ambayo ipo na mikataba imezingatia specifications za kitaalam na mikataba pia imeweka masharti ya pande zote mbili, upande wa sisi Serikali, lakini upande wa mkandarasi na ziko hatua ambazo zinachukuliwa, tunacho chombo ambacho kinawasimamia wakandarasi, tuna Contractors Registration Board na lakini pia kuna ERB yaani Engineers Registration Board ambayo hawa wanafuatilia miradi mbalimbali kukagua kuona kama shughuli hizi zinaenda vizuri, lakini kwa kuzingatia pia mikataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo idadi ya makandarasi ambao wamechukuliwa hatua, wapo ambao amesimamishwa kwa muda, wapo ambao wamefutiwa usajili wao na tutaendelea kuchukua hatua kwa mtu ambaye anakiuka taratibu za ujenzi.

Kwa hiyo, nikuhakikishie tu na Bunge lako kwamba, sisi Serikali tuko makini kuhakikisha kwamba kazi zinafanyika kufuatana na mikataba iliyokuwepo, kufuatana na taratibu zilizokuwepo, ili kuhakikisha kwamba kazi ambazo tumeziweka kwa ajili ya ukarabati au ujenzi zinakamilika, lengo ni wananchi waweze kupata huduma nzuri na kwa haraka inavyowezekana.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, umepita Barabara ya Mbulu kwa upande wa Mashariki na Mheshimiwa Naibu Waziri amepita barabara hiyo ya Mbulu kwa upande wa Magharibi. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri utuambie sasa na uwaambie wananchi wa Mbulu, barabara ile ya Mbulu – Haydom – Mbulu inajengwa lini kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ziko changamoto katika huu ushoroba kwa maana ya hii barabara kuu ambayo anaizungumza Mheshimiwa Mbunge kwa maana itatuunganisha kutoka Karatu, tutakuja Mbulu, tunakwenda Dongobesh, tunakwenda Haydom, tunapita kule Sibiti ambako daraja kubwa limekamilika halafu tutakwenda kwenye Mikoa ile ya Shinyanga, Mkoa wa Simiyu, Mwanza, hii barabara muhimu na niseme tu na kuwahakikshia wananchi wa Mbulu na majirani zao ni kwamba, tunaanza sasa ujenzi kwa sababu ule usanifu ulishakamilika na katika bajeti hi mliyotupitishia tumetenga kuanza ujenzi wa kiwango cha lami wa kilometa 50 kutoka Mbulu kuja Dongobesh na tutaendelea hivyo hivyo kadri tutapopata fedha mpaka barabara hii muhimu iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante sana.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika Tunduma ni mpakani na kuna msongamano mkubwa sana wa malori yanayovuka mpaka wa Tunduma kuelekea Zambia, lakini pia wananchi wamekuwa wakipata shida sana ya kuweza kutumia barabara moja ambayo iko kwenye mji wetu wa Tunduma, lakini kuna bypass ya barabara inayotokea Mpemba kuelekea Tunduma Mjini kilometa 12 na Mheshimiwa Naibu Waziri alipita kuja kuingalia barabara ile na akatuahidi kwamba barabara ile ingeweza kujengwa katika mwaka huu wa fedha.

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ile ili kupunguza msongamano na kuwapa unafuu Wananchi wa kuendelea kutumia barabara yetu ya Mji wa Tunduma? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mji wa Tunduma unakua kwa kasi na ni ukweli inahitajika maboresho mbalimbali ya miundombinu katika eneo hili na Serikali inachukua hatua nyingi kupaboresha sehemu hii ya Tunduma kwa sababu hata ukifika pale utaona magari ni mengi sana na sisi tumejipanga pia kuboresha kwenye kituo chetu hiko cha Mpemba pale, tukatakuwa na ujenzi wa kituo kile ambacho kitashughulikia mambo mengi, Mheshimiwa Mwakajoka anafahamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Mwakajoka hapo amechomekea kidogo kusema nilitoa ahadi ya kujenga kiwango cha lami katika mwaka huu wa fedha, siyo kweli. Nilichokisema ni kwamba Serikali inayo mpango wa kufanya maboresho maeneo haya ikiwepo kuangalia zoezi zima la ujenzi wa bypass ili kukwepesha adha ambayo watumiaji wa barabara wanaipata wakipita katika Mji wa Tunduma hususan wanaokwenda maeneo ya Rukwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa kweli tulifanya mazungumzo na mimi pia niliwatahadharisha uongozi uliopo pale ili tuanze kuangalia mipango kwa mapana, kwa sababu mji ule unakua sana. Utaona ile hifadhi ya magari (parking) muda siyo mrefu zitafika mpaka kwenye Mji wa Mbozi, kwa hiyo, ukuaji ni mkubwa sana. Kwa hiyo, kwa upande wa Serikali sisi tunaona kwamba mipango yetu lazima tuiweke vizuri ili siku za usoni kulingana na ule ukuaji wa mji huu kwamba huduma zile muhimu zinapatikana.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwakajoka nakuomba uvute subira tu, wewe unafahamu umejaribu kuchomeka hapa lakini unafahamu kwamba umuhimu wa hii bypass lakini na sisi tumeichukua hiyo tunaendelea kuiweka kwenye mipango yetu ili kwa haraka tuje tuweke huduma hii ya barabara kwa maana ya bypass. Wewe vuta subira tu na ikikupendeza ukipata muda uje tuzungumze tuone kwenye strategic plan yetu tumeiweka namna gani ili hata ukipeleka information kwa wananchi wetu usiwaambie kwamba tutaanza kujenga mara moja, lakini uwaambie kutokana na hali ambayo ipo, kwenye utaratibu wetu ambao tumejiwekea ambao ni mzuri tu, kwa kweli tumewajali sana wananchi wa Tunduma.
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza, Mheshimiwa Naibu Waziri huyu mkandarasi kama ameomba muda wa nyongeza na atapewa na Serikali, je, ikifikia muda huo ikiwa barabara hiyo haijamalizika nini kitafanyika? Je, atapewa muda tena aendelee au atapewa muda mkandarasi mwingine ili aimalizie hii barabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Agness amekuwa akifuatilia sana juu ya maendeleo ya Mkoa wa Mara juu ya barabara nyingi ambazo kimsingi Serikali imepeleka miradi mingi sana katika Mkoa huu na hivi karibuni Mheshimiwa Marwa unakumbuka Mheshimiwa Rais ameongeza miradi kadhaa ya ujenzi wa barabara ya lami katika Mkoa wa Mara, kwa hiyo nakupongeza sana.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu swali lake anasema kwamba endapo tutamuongezea mkandarasi huyu kwamba muda na asipokamilisha itakuwaje; kimsingi niseme kwamba zoezi la kumuongezea muda linazingatiwa kitaalam ili kuona nini kazi iliyo mbele ya safari ili kukamilisha mradi huu. Kwa hiyo, ninaamini muda ambao utaongezwa utakuwa ni muda ambao utawezesha kutekeleza mradi huu kwa wakati kulingana na utaalam kulingana na taratibu. Kwa vile suala hili ni la kimkataba nikuhakikishie Mheshimiwa Marwa kwamba sisi tunatasimamia vizuri mkataba huu ili kazi ikamilike na zipo hatua za kuchukua kulingana na utaratibu wa kimkataba kama wakandarasi hawa watakiuka mkataba basi sheria itachukua nafasi yake.

Mheshimiwa Spika, lakini niseme kwamba mradi huu unajengwa kwa kutumia joint venture na nia ya Serikali kuwasadia wakandarasi wazawa ili waweze kujenga uwezo, ili waweze kujenga mitaji, lakini ili waweze kusababisha ajira nyingi kwa vijana wetu lakini hili pia ile faida inayopatikana iweze kubaki hapa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni nia ya Serikali kuwawezesha hapa, sasa watumie fursa hiyo ambayo Serikali niwaombe sana wakandarasi hawa wakiingia kwenye joint venture watumiea fursa hii nzuri ili kuhakikisha kwamba tunawasidia kama Serikali na kama watashindwa basi Serikali itaendelea na taratibu ambazo zipo. Kwa maana hiyo kwamba kulikuwa kuna changamoto za kiuendeshaji na za kiutawala katika JV hizi ambapo tumeelekeza wenzetu au pande wa CRB na wenzetu wa ERB kwamba ndio walezi wa hizi taasisi wawasimamie vizuri na wahakikishe ubora, wahakikishe nidhamu ili tuwajenge vizuri waweze kusaidia nchi yetu, ahsante sana.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi tatizo la kusuasua kwa miradi ya barabara Mkoa wa Mara halijaanza kwenye Bunge hili tu, tangu Bunge lililopita na Wabunge wa Mkoa wa Mara kujali itikadi zetu katika vikao vyetu tumekuwa tukionesha uhitaji wa miradi hii kukamilika mapema. Issue ya mradi wa Natta - Mgumu - Serengeti ni wa muda mrefu na unafanana kabisa na mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Kisolya - Bunda - Nyamuswa na wenyewe umekuwa ukisuasua mbali na tatizo la wakandarasi, lakini tatizo kubwa ni Serikali kutopeleka pesa ili miradi hii ikamilike haraka.

Sasa ni lini Serikali itapeleka pesa za kutosha barabara hizi za muda mrefu takribani miaka 10 ziweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimuombe Mheshimiwa dada yangu Ester Bulaya kwamba hata hiki kinachofanyika na kwa sasa na kwa kasi hii angalau aone shukrani, aweze kushukuru kwa sababu niseme kazi kubwa inafanyika barabara hii ya Bulamba - Kisolya ni muda mrefu imekuwepo na kumekuwa na changamoto nyingi. Zipo changamoto ambazo zimekuwa kwa upande wa mkandarasi na zipo changamoto ambazo zimekuwepo kwa upande wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, lakini nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali sasa ipo kazini, Serikali sasa inafanya kazi nzuri na wiki iliyopita mkandarasi huyu kwa miradi ambayo anaendelea amelipwa zaidi ya bilioni tano. Nitumie nafasi hii niishukuru sana Wizara ya Fedha. Sasa kazi yetu kubwa ni kusimamia yale ambao yalikuwa saa nyingine tunaona kwamba tumekuwa na madeni mengi, lakini wakandarasi wote nchini wamelipwa sasa tupo current tunaenda vizuri.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Ester nenda Bunda uone kazi inavyoendelea na tumepokea wiki mbili tu zilizopoita zaidi ya shilingi bilioni 184 kwa ajili ya kulipa wakandarasi nchi nzima. Kwa hiyo kwa upande wa Serikali tupo vizuri, Wizara ya Fedha inafanya vizuri na sisi kwenye usimamizi tuko vizuri.

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kweli kwa sababu unaona tunaanza mradi wa kutoka Bulamba kuja Bunda kwenda Nyamuswa kilometa 56 na Bunge lako limetenga fedha kuhakikisha kwamba mradi huu nao unaenda.

Mheshimiwa Spika, niseme kama nilivyosema mwanzoni kwamba ipo mradi mingi, ipo mradi mzuri iko hatua katika Mkoa wa Mara, miradi mingi inaendelea kutekelezwa, ahsante.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza niwapongeze wenzetu wa TARURA kwa kazi nzuri wanazofanya pale Korogwe ajili ya ujenzi wa zile barabara kwa kiwango cha lami na kiwango cha changarawe. Nina swali la nyongeza.

Kwa kuwa mnawapa fedha kwa ajili ya ujenzi wa zile barabara za changarawe na Mji wa Korogwe umekaa bondeni, mvua zikinyesha kama hivi sasa barabara zile zote zinasombwa na maji.

Je, Serikali itakuwa tayari sasa mnapotupa fedha hizo kutuwekea na fedha za kujenga mifereji ili kusudi ziweze kuhimili hizo barabara kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa na chombo hiki cha TARURA ambacho wenzetu upande wa TAMISEMI wanakisimamia, hata jana nilizungumza hapa kwamba TARURA wameanza vizuri kwa sababu kazi iliyokuwa inafanyika ilikuwa ni kuzitambua barabara zetu, kuzichambua barabara zetu na hivi ninavyozungumza lipo zoezi linaloendelea kule Morogoro kwa ajili ya kuzipanga barabara zetu pamoja na kuainisha changamoto ambazo zimejitokea katika maeneo yetu. Kwa hiyo Mheshimiwa Chatanda uvute subra najua tumezungumza sana mara nyingi, sasa uchambuzi unaendelea.

Mheshimiwa Spika, lakini niseme tu kwamba pamoja na hayo zoezi hili la kuangalia juu ya mifereji sio kwa Korogwe peke yake lakini nchi zima tunaingalia, kwa sababu barabara zetu zikijengwa kwa namna yoyote ile kama hatutazingatia kuweka vizuri mifereji hii, maji ya mvua ni chanzo cha uharibifu wa barabara zetu. Kwa hiyo, hii tunalizingatia na nilipokee tu pia kama ushauri na tulingalia kwa macho mawili ili kuhakikisha kwamba wakati tunaboresha barabara zetu vizuri lakini suala la ku-control maji hasa maji ya mvua tunalifanya ili barabara zetu ziweze kudumu, ili pia katika makazi ya watu wananchi wetu waweze kuwa salama.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali.

Kwa kuwa barabara ya kutoka Mwitika kwenda Maparawe na kutoka Chiungutwa - Mipande hadi Mtengula haipitiki kutokana na madaraja hayo kung’olewa na mafuriko miaka mitano iliyopita na Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba madaraja hayo yatajengwa.

Je, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli zipo ahadi za Mheshimiwa Rais zipo ahadi nyingi na niseme tu kwamba ni ukweli baadhi ya ahadi zimetekelezwa 100%. Zipo baadhi ya maeneo ambazo tumetekeleza kwa kiasi fulani na tunaendelea kutekeleza na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge ahadi zote za Mheshimwa Rais na viongozi wakuu tunaendelea kuzitekeleza.

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Bwanausi umezungumza juu ya haya madaraja na utakuwa shaidi kati haya madaraja ambao yalikuwa ni sehemu ya ahadi madaraja manne kama zikosei matatu tayari yamekwisha tekelezwa, tumebakiza lile daraja moja naomba uvute subira kwa sababu tunawenda hatua kwa hatua kwa dhamira ile ile kuhakikisha kwamba tunafanya maboresho makubwa katika kutekeleza ahadi ya kiongozi wetu mkuu Mheshimiwa Rais wetu, ahsante sana.
MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunamshukuru Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kutupa barabara ya Makutano - Sanzate na kuna kipande cha Sanzate cha kwenda Nata - Mugumu na barabara ya Nyamswa - Bunda, Bunda - Buramba, Buramba - Kisorya.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Makutano - Sanzate kama ni mkandarasi amepewa nafasi ya kumaliza barabara hi ni zaidi ya mara saba na tarehe 06.09.2018 Mheshimiwa Rais ameenda pale na akaagiza barabara hii imalizike haraka iwezekanavyo.

Sasa ni nini kifanyike sasa ili barabara hii ikamilike kwa sababu kama mkandarasi ambae tunamuita wazawa amepewa fedha, ana vifaa, ana wataalam lakini barabara haiishi. Nini kifanyike barabara hii ikamilike?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kuna barabara ya Mgeta - Sirorisimba ambayo TANROADS waliitengeneza ikabaki kilometa tisa. Nilikuwa namuomba Waziri sasa atamke kwamba hiki kipande cha kilometa tisa kitaisha lini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze tu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifuatilia sana hii barabara lakini pia hiyo barabara aliyoitaja ya kutoka Mgeta - Sirorisimba. Ninampongeza sana na niwashukuru tu Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Mara kwa sababu siku ya Jumatano nilijibu swali kama hili hili, swali namba 377 la Mheshimiwa Agness Marwa kuonesha namna wanavyoshirikiana, lakini kuonyesha barabara hii ni kipaumbele kwenye Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nini kifanyike; kweli kumekuwepo na changamoto muda mrefu wa ukamilishaji wa barabara hii lakini labda nipende tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna sehemu ya kilometa 18 ilikuwa ina shida mpaka tulilazimika kubadilisha design kwa maana ile barabara ya kutoka Makutano kuja Butiama kilometa 18. Ni sehemu ambayo ilikuwa ni korofi, ni sehemu ya mlima ilikuwa na mawe mengi, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi sasa ninavyozungumza changamoto ile mkandarasi ameiondoa kwa maana yale mawe ameshayatoa na kilometa 13 sasa ameshaweka tabaka la sub-base kwa maana ya kwamba cement na mchanga wameweka kilometa 13 na kilometa sita wameshaweka base.

Nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi ni kwamba sasa kufikia Januari kama makubaliano ambayo watayakamilisha kesho, kesho kutakuwa na kikao kati ya mkandarasi na uongozi wa TANROADS Makao Makuu kwa maana ya kuijadili barabara hii muhimu. Vuta subira Mhehsimiwa Mbunge nitakupa feedback kwamba hayo makubaliano yatakuwa ya mwisho kuhakikisha kwamba tunakubaliana na barabara hii inakwenda kukamilika, kwa hiyo, usiwe na wasiwasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu barabara ya Mgeta - Sirorisimba; zipo kilometa 22 katika barabara hii. Kimsingi barabara hii inasimamiwa na TARURA, lakini kulikuwa kuna ombi maalum la Mheshimiwa Mbunge ndiyo maana nilianza kwa kumpongeza ili sasa upande wa TANROADS kuweza kusaidia barabara hii muhimu na barabara hii kilometa 22 ulifanyika ujenzi wa kuweka kokoto kilometa zote 22; lakini kuna maeneo ambayo barabara ilipanuliwa na kuweka makalavati makubwa kama sita hivi kilometa zile 13 na ikabakia kilometa tisa ambazo Mheshimiwa Mbunge unaulizia hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, na niseme tu kwamba tumekubaliana na nielekeze pia zaidi watu wa TANROADS Mkoa wa Mara hizi kilometa tisa maeneo ambayo yalikuwa yamebakia kama ni korofi waweze kumalizia na natumaini pia upande wa TARURA kuna fedha wametenga kwa ajili ya kufanya maboresho. Na niwahakikishie wananchi wa Mgeta na Sirorisimba kwamba barabara hii tunaijali na mimi mwenyewe binafsi nimefika maeneo haya na nimeongea pia na Wananchi wa Sirorisimba na Mgeta wameridhika kwa kiwango kikubwa kazi iliyofanyika kwa hiyo Mheshimiwa Getere nafahamu na unafahamu kwmaba tunafanyakazi nzuri katika maeneo yako.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa barabara ya Puge - Ziba - Manonga hufanyiwa matengenezo mara kwa mara na kutoa gharama kubwa sana ya matengenezo hayo, je, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kujenga barabara hii kwa awamu kama ifuatavyo; kujenga kutoka Puge - Ziba - Manonga kwa kiwango cha lami angalau ianzie Ndala mpaka Ziba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Mwanne Mchemba kwa sababu barabara hii ameifuatilia sana na imezaa matunda kwa kweli kwa sababu maeneo yote korofi tunafanya matengenezo makubwa ikiwepo ujenzi wa daraja kubwa kabisa katika Mto Manonga. Nia ya Serikali ni kuboresha maeneo haya. Kwa sasa Serikali ilikuwa inaendelea kuunganisha mikoa na Mkoa wa Tabora umeunganishwa na mikoa mingine kwa maana ya Tabora kwenda Shinyanga kuja Singida. Uvute subira tu kidogo tumeiweka kwneye mpango barabara hii na sasa eneo hili unalolisema la kutoka Ndala kwenda Ziba ni eneo muhimu ambao linapita kwenye Hospitali ya Nkinga, tutaliangalia ili tukipata fedha tuanze na eneo hili ambalo pia lina shughuli nyingi za kiuchumi. Ahsante sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante wka kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Sera ya Wizara hii ni kuunganisha mikoa na mikoa kwa kiwango cha lami na kumekuwa na ahadi ya muda mrefu ya ujenzi wa barabara ya kutoka NJiapanda - Mang’ola - Karatu mpaka Lalago ambayo inaunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu na kumekuwa kuna ukarabati mdogo mdogo unafanyika mara kwa mara ambao unagharimu fedha nyingi.

Sasa kwa nini Wizara isifikirie angalau kuanza kilometa chache chache kwa kiwango cha lami mpaka itakapokamilika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naona Mheshimiwa Mbunge anatabasamu anafahamu kwamba Serikali inayo nia thabiti ya kufanya maboresho ya barabara katika maeneo haya na ndiyo maana kuna usanifu umefanyika wa barabara hii, hii bypass hii kutoka Karatu kupita eneo la Mang’ola kwenda Sibiti halafu kuunganisha katika Mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mwanza. Unafahamu kinachoendelea na nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge hivi wiki iliyopita Mameneja wa TANROADS pamoja na wenzetu ambao pia walikuwa wanasanifu eneo hili wamekuwa na kikao madhubuti kwa maana ya kuliangalia eneo hili kwasababu usanifu ulishakamilika kwa barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini barabara hii tunaitazama sambamba na barabara ya kutoka Karatu- KIlimapunda kuja Mbulu Mjini, kuja Dongobeshi kwenda Haidom, kwenda Sibiti tunakwenda kuungana na hiyo barabara uliyoitaja Mheshimiwa Mbunge. Zote hizi barabara tunaziangalia kwasababu eneo la Mang’ola ni eneo muhimu na lina historia, Wahadzabe wako maeneo haya, lakini pia kuna kilimo cha vitunguu kikubwa katika maeneo haya kwahiyo Serikali imeliona eneo hili kwa maana ya kuwasaidia wananchi maeneo haya ili uchumi uweze kupanda kwa maana hiyo vuta tu subira tumejipanga vizuri, tunazitazama hizi barabara zote ili sasa eneo hili tuweze kulifungua na tuweze kutoa huduma muhimu hii ya barabara. Ahsante sana.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, barabara ya kutoka Uvinza kuelekea kwenye Daraja la Kikwete - Malagarasi, barabara hii iliahidiwa kujengwa kwa pesa za kutoka Abu Dhabi. Nataka Serikali iniambie ni lini sasa kipande hiki cha kilometa 48 kitakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwanza nikupongeze Mheshimiwa Genzabuke kwa sababu unafahamu na unafuatilia sana juu ya barabara hii na ni faraja kwa wakazi wa Kigoma na Tabora na wananchi wengine kwa ujumla kwamba hii barabara muhimu kutoka Tabora kwenda Kigoma sasa maeneo yote pamoja na hili eneo yameshapata mkandarasi kwa maana ya ujenzi, kwa maana hiyo zile taratibu za kimanunuzi zilikuwa zimekamilishwa na kweli tumepata fedha kutoka Abu Dhabi na pia tumeonyesha kwenye bajeti Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba tumeonesha kwamba ujenzi unakwenda kuanza.

Kwa hiyo vuta tu subira zile taratibu za kimanunuzi zinaendelea vizuri na nikuhakikishie muda siyo mrefu utaona mkandarasi yuko site anaendelea na ujenzi katika eneo hili la Uvinza-Malagarasi kilometa 48 ambazo Mheshimiwa Mbunge unafahamu na umeizungumza hapa.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Kiwanda cha Dangote, lakini yale magari makubwa ya Dangote yanapita barabara ya kutoka Mtwara kuja Mnazi Mmoja kwenda Mtama - Masasi. Ile barabara hali yake haikutengenezwa kubeba magari makubwa ya kiasi kile kwa hiyo hali yake imekuwa mbovu sana. Kila mara unafanyika ukarabati na barabara inaendelea kuwa mbovu. Sasa Serikali inachukua hatua gani kumaliza tatizo hili la ubovu wa hii barabara kwa kila mara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hii imekuwa ikifanyiwa matengenezo lakini Mheshimiwa Nape atakubali kabisa kwamba hii barabara ni ya zamani, hii barabara ina zaidi ya miaka 30 na imekuwa ya muda mrefu na hata ukisoma kibao pale imeandikwa T2 (T Namba 2) na uone hata kwenye usajili wake ni kati ya barabara ambazo ni za zamani sana kwa maana hiyo iko haja sasa ya kufanyia rehabilitation kwa maana ya matengenezo makubwa na wiki iliyopita nilijibu hapa kwamba Serikali tumejipanga kwa ajili ya kuijenga upya barabara hii kutoka Mtwara kuja Mnazi Mmoja na kutoka Mnazi Mmoja kwenda Masasi kwa ufadhili wa World Bank.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Nape vuta subira ule utaratibu wa kawaida wa kifedha na kimanunuzi unaendelea. Tutakwenda kuifumua barabara hii na kuitengeneza kabisa ili iwe mpya kwa hiyo niwahakikishie wananchi wa Mtama, wananchi wa Mtwara, wananchi wa Lindi na Watanzania kwa ujumla kwamba tunakuja kufanya maboresho makubwa ya barabara hii.
MHE. MWIGULU L. NCHEMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kibaya, Urughu - Mtekente - Mtowa na Sheluwi ni moja ya barabara inayobeba uchumi wa Iramba na katikati ya Mtekente na Mtowa pana daraja la kisasa sana limejengwa.

Je, kwa nini Wizara ya Ujenzi isiipandishe barabara hii kufuatana na umuhimu wake ili iwe chini ya TANROADS iweze kujengwa kwa kisasa na iweze kusaidia wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli Waheshimiwa Wabunge watakubaliana na mimi kwamba tumekuwa na chombo hiki TARURA na dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba TARURA inafanya kazi nzuri na kweli nitumie nafasi hii niwapongeze TARURA kwa sababu wameanza vizuri maeneo mengi, wanafanya vizuri na kumekuwa na mchakato wa kuzitambua barabara zetu kwa nia dhabiti ya kuweza kuziboresha.

Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu wa kupandisha barabara uko kisheria na kama saa nyingine itapendeza watumie nafasi hiyo kwa vikao walivyonavyo ili waweze kuleta mapendekezo na sisi kama Serikali tutazama kwa namna hiyo kwa mujibu wa taratibu zilizokuwepo ili kama itakidhi kupandishwa basi Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana atafanya hivyo. Lakini kimsingi ni kwamba TARURA ipo kwa ajili ya kuboresha barabara zetu na nifahamishe tu kwamba itaenda kujenga barabara zetu mpaka kiwango cha lami.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Spika, tatizo lililoko Iramba halina tofauti na tatizo lililoko katika Mkoa wa Mara hasa barabara ya Musoma - Busekela ambayo ilitengewa kilometa 42 lakini cha ajabu barabara hii iliyojengwa ni kilometa tano tu. Ninachotaka kujua hizi kilometa 37 zitajengwa lini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kwa kutambua umuhimu wa barabara hii anayozungumza Mheshimiwa Mbunge tumeanza kufanya ujenzi wa kilometa tano na hii tunazingatia kwamba yale maeneo ambayo ni korofi tunaanza kuyawekea lami na hivyo hivyo maeneo yote nchi nzima kwamba tunapokuwa na utaratibu wa kujenga barabara zetu yale maeneo ambayo tunaona kwamba ni muhimu tuyaboreshe tunaanza kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwanza nimuombe Mheshimiwa Mbunge aridhike kwamba tumeanza kuchukua hatua nzuri ili kufanya ujenzi kwenye maeneo ambayo tunaona kwamba ilikuwa ni muhimu tuyaboeshe na tutaendelea kufanya hivyo. Tukipata fedha za kutosha tutakwenda kujenga barabara hii yote, kwa hiyo, uvute subira hatua ndio hivyo tumeanza kidogo lakini kadri tunavyopata fedha tutakwenda kuiboresha barabara hii na tutaendelea kuboresha maeneo yote ambayo yanaleta usumbufu kwa wananchi wakati wanasubiri barabara ya lami yote ijengwe basi waweze kupita na kufanya shughuli zao za maendeleo, ahsante sana.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nampongaza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri kwamba TARURA sasa inashughulikia barabara hii. Kwa kuwa barabara hii ni muhimu sana kiuchumi kwenye Wilaya ya Geita na Wilaya ya Nyanghwale, kwa sababu ni kiunganishi kikubwa kati ya Wilaya ya Nyang’hwale na Geita. Je, Serikali iko tayari kuongeza fedha TARURA ili waweze kuikamilisha hiyo barabara kwa kiwango cha changarawe ili wananchi wafanye shughuli zao vizuri?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ziko ahadi mbalimbali za Mheshimiwa Rais za muda mrefu sana ikiwemo kilomita 10 za lami Katoro – Guselesele, barabara ya kutoka Katoro kwenda Ushirombo na barabara ya kutoka Geita kupitia Bukori kwenda mpaka Kahama.

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuanza kutekeleza barabara hizi kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyofuatilia maendeleo ya Busanda na Geita kwa ujumla, hapa tu ametaja barabara nyingi kweli kwa pamoja na kwa ufundi mkubwa, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nakupongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu barabara hii ya Busanda ambayo inaelekea Nyang’hwale kuiongezea fedha, kama nilivyojibu siku zilizopita hivi karibuni niseme tu sasa kazi ambayo ilikuwa inafanyika na TARURA ipo Kamati maalum inaitwa National Road Classification Committee, nilisema hapa kwamba baada ya TARURA kufanya kazi nzuri ya kuzitambua barabara zetu na kufanya uchambuzi wa kina ili sasa tuweze kuzipanga upya hizi barabara kulingana na mahitaji yake. Kwa hiyo nitumie nafasi hii tu kwa sababu Kamati hii inamalizia kazi yake iweke kipaumbele na msisitizo mkubwa kuingalia barabara hii tuweze kuitendea haki ili tuweze kuijenga katika kiwango cha changarawe kama Mheshimiwa Mbunge unavyoshauri, mimi hili nitalisimamia ili nione kwamba barabara hii tunaifanyia maboresho makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla kwamba kuwa na chombo hiki TARURA, Serikali imedhamiria ili kuhakikisha kwamba barabara zote zinajengwa katika standard ambayo inafanana. Siyo kwamba barabara zitakazosimamiwa na TARURA zitakuwa tofauti na barabara zinazosimamiwa na TANROADS, naomba tuamini hilo, kwamba tutazingatia ubora, tutazingatia weledi, tutazingatia pia kwamba gharama ambazo zinatatumika ziwe reasonable kiasi kwamba tuweze kuhudumia barabara kwenye mtandao mkubwa, kwa hiyo niwatoe wasiwasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ahadi za Mheshimiwa Rais katika ujenzi wa barabara ya eneo hili la Katoro na Buselesele kwa Mheshimiwa Kalemani. kwa sababu Mji wa Buselesele na Katoro umeumana, ziko ahadi za kilomita 10, tulizungumza wa wenzetu upande wa TAMISEMI kwamba tutaanza ujenzi pale. Kwa hiyo, tukipata fedha tutaanza ujenzi ili angalau wananchi hawa wa eneo hili ambalo linakuwa kwa kasi waweze kupata huduma vizuri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Lolesia usiwe na wasiwasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ipo barabara hii uliyoitaja kutoka Ushirombo kuja Mji wa Katoro kwenda Geita kilomita kama 53 hivi tumeitengea fedha na hivi ninavyozungumza tuko kwenye harakati ya kuanza kujenga katika kiwango lami. Nikuhakikishie tu kwamba tutakavyoanza kujenga barabara hii tutaweka msisitizo mkubwa ili Mji huu wa Katoro tuweze kuanza katika maeneo haya ili wananchi wawahi kupata huduma muhimu maeneo ambayo pia yana changamoto kubwa, Kwa hiyo nikuhakikishie tutaanza nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, umezungumzia pia barabara hii ambayo inatoka Kahama inapita Bulyanhulu, Bukori inakwenda mpaka Geita kilomita 120, Kilomita 51 ziko katika eneo lako Mheshimiwa Mbunge. Nikuhakikishie tu kwamba Mheshimiwa Waziri alikuwa anashughulikia ili tuanze ujenzi wa barabara hii, na Bunge hili limetupitishia fedha ili tuanze kuijenga hii barabara muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Lolesia nikuhakikishie tu kwamba wakati wowote tunaweza tukaanza ujenzi wa barabara hii muhimu na kwa vile tutakuwa na lot mbili, lot moja itakuwa katika eneo lako.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Nichukue nafasi hii kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Wizara ya Ujenzi kupitia TANROAD wamekuwa wakifanya kazi ya kuweka alama za X kwenye maeneo ambayo wanakusudia kufanya upanuzi wa barabara, lakini kazi hiyo ambayo wamekuwa wakiifanya hawawahusishi wananchi wa maeneo husika kwa kuwaarifu kwamba wanakusudia kufanya hivyo, watu wanawaona tu wanaweka alama za X. Je, kwa nini wanafanya kazi hiyo bila kuwahusisha wananchi ili waweze kuwafahamu na kuondoa taharuki ambazo zinajitokeza katika kuwekewa alama za X? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Chatanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza pongezi alizozitoa nazipokea kwa moyo mnyoofu, lakini pili niseme kwamba zoezi la kuweka alama za X kwamba inawezekana labda kuna baadhi ya maeneo wananchi hawakujulishwa labda hili litakuwa ni tatizo, lakini kimsingi tunavyoweka alama za X barabarani inaenda sambamba na kutoa elimu na kuwafahamisha wananchi juu ya alama hizo kwa sababu yako maeneo ambayo ni uvamizi, wananchi wamevamia lakini yako maeneo ambayo labda saa nyingine mradi unawafata wananchi na wanastahili kulipwa fidia, kwa hiyo suala la elimu linatakiwa.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii tu nielekeze maeneo yote nchini pale ambapo tuna miradi ya barabara na miradi yoyote inayosimamiwa na Wizara na taasisi zingine kwa maana ya TANROADS, TARURA na maeneo mengine kwamba kwamba wananchi lazima wahusishwe kikamilifu na viongozi walioko maeneo hayo. Sambamba na hilo elimu itolewe ili wananchi wafahamu nini wanatakiwa kufanya na pia wafahamu haki zao. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba niulize swali la nyongeza kutokana na swali la msingi. Kwanza tunaishukuru Serikali kwa kutupatia fedha kwa kukarabati barabara tajwa ya Kilwa eneo la Rangi Tatu – Kongowe - Mikwabe na kadhalika. Barabara hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya mkoa wa Dar es Salaam na maeneo yake ya jirani, barabara hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya Mkoa wa Lindi, Mkoa wa Mtwara na kuelekea maeneo mengine. Sasa kwa kuwa barabara hii inajengwa nyakati za mchana na sasa hivi mkandarasi yuko kazini na imekuwa ni kero kubwa juzi wakati tukiwa Misri dunia sasa hivi ni kiganja tukiwa Misri tumepata taarifa na tumeona jinsi watu wa maeneo ya Dar es Salaam wale wanaokwenda Lindi na Mtwara wamekaa zaidi ya masaa manne wakisubiri kwa kuwa mkandarasi yuko barabarani. Sasa kwa nini kusiwe na utaratibu badala ya kujenga barabara hii mchana ijengwe jioni au usiku ili watu mchana waendelee na kazi zao kwa ajili ya kujipatia maendeleo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete, mama yangu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru pia kwa maelekezo yako kwa sababu na wewe nafikiri jambo hili umeliona, niseme tu kwamba, kwanza nilipokee kama ushauri kwamba tutafanyia kazi ili wananchi wasipate adha wakati wa matengenezo yanavyoendelea. Hata hivyo, niseme tu kwamba, matengenezo yanayoendelea nia yake kubwa ni kuhakikisha kwamba tunapunguza ule muda wananchi wanakaa barabarani tutapunguza msongamano, lakini pia tunapunguza ajali. Niseme tu kwamba tutalisimamia jambo hili kwa sababu suala la kujenga usiku na mchana tutaliangalia, lengo kwanza mradi huu ukamilike haraka ili wananchi waweze kupata hii huduma muhimu.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa na mjadala mrefu kidogo na Mheshimiwa Mbunge wa Mkuranga na tulikuwa tumezungumza juu ya suala hili, kuna baadhi ya mambo ambayo tayari tumeyatolea maelekezo. Hii ni pamoja na kuangalia kwamba tunapokuwa na matengenezo hasa hasa katika Jiji la Dar es Salaam tuone pia alternative route zingine ambazo zinaweza zikapunguza watumiaji wa barabara ili msongamano usiwe shida.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tutaliangalia kwa umakini na nitalifuatilia ili sasa tuone kwamba kwanza mradi unafanyika kwa haraka, zoezi linakamilika kwa haraka, lakini ile adha wanayoipata wananchi iweze kuondoka. Kwa hiyo, nashukuru tutalichukua hili kwa umakini mkubwa na tutalisimamia kama Serikali ili shida hii iweze kuondoka kabisa.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika sana kiukweli majibu haya hayaridhishi hata kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulienda Serengeti na Naibu Waziri pamoja na Kamati ya Miundombinu, Naibu Waziri gari lake lilipata pancha mara nne, matairi manne. Tukampa spare zikaisha mpaka raia wananchi wakampa spare, hali ni mbaya kwa wananchi wa Serengeti. Ukiangalia barabara imeanza kujengwa tangu 2013, miaka sita (6) imepita kilomita 50 hazijakwisha; Je, itachukua miaka mingapi kumaliza kilomita 80 kutoka Sanzate mpaka Mugumu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wananchi wa Mugumu kwenye hiyo kandokando ya barabara walishafanyiwa tathmini na kila mtu anajua analipwa shilingi ngapi, ni lini watalipwa fidia zao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ryoba Chacha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, pamoja na masikitiko yake lakini niruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Ryoba kwa namna anavyofuatilia hasa miradi hii ya barabara. Ni kweli niseme tu kwamba barabara hii kwa historia ni barabara muhimu, hizi kilomita 452 mimi nimeipita hii barabara ina changamoto zake. Kwa historia Marehemu Baba wa Taifa alikuwa akipita barabara hii akitokea Arusha miaka ile, kwa hiyo ni muhimu na sisi kama Serikali tunaiangalia kwa macho mawili. Niseme tu pamoja na kuwa ujenzi huu umekwenda kwa hatua hiyo ya kusuasua lakini kama nilivyosema na kwa kweli kwa ushirikiano wa Wabunge wa Mkoa wa Mara nimejibu wiki juzi swali la Mheshimiwa Agness Marwa na wiki iliyopita nimejibu swali la Mheshimiwa Getere kuonesha umuhimu wa barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Ryoba avute subira, lakini niseme tu kwamba kama commitment nilivyosema hapa na namna tunavyosimamia vizuri sasa pamoja na kuchelewa lakini barabara hii itakamilika na kama nilivyokuwa nikizungumza hapa, kwa hiyo tunaisimamia vizuri itakamilika vuta subira.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kilomita 452 tuko asilimia 41 ya commitment ya barabara, kwa Mradi huo wa Makutano Juu – Sanzate kilomita 50. Kama nilivyosema kutoka Sanzate – Natta kilomita 40 tuko hatua ya manunuzi, lakini pia kwenye bajeti Natta – Mugumu kilomita 45 tumeitengea bajeti na ujenzi wa eneo la Wasso – Sale kilomita 49. Utaona asilimia 41 tunaendelea kuisogelea kuweza kuikamilisha barabara hii, kwa hiyo avute tu subira Mheshimiwa Ryoba tutaisimamia vizuri barabara hii ili iweze kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili ya swali lake kuhusu tathmini ya wale wananchi; kama nilivyosema, kiutaratibu tunatakiwa tulipe kabla ya ujenzi kuanza. Kwa hiyo tutazingatia sheria, kanuni na taratibu zilizokuwepo, Sheria ya Ardhi, Sheria ya Utwaaji wa Ardhi, wananchi watalipwa haki yao kulingana na sheria, kwa hiyo avute tu subira kabla ya kuanza ujenzi wananchi hao watalipwa mara moja.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba niulize swali la nyongeza, naamini kwamba kwa watu wale ambao wanategemea usafiri wao wa maji kivuko ni barabara. Sasa kwa kuwa kivuko ni barabara nataka kuzungumzia kivuko cha Lindi ambacho kinatoka Msinjaili kuelekea Kitumbikwera. Kivuko hiki ni muhimu sana kwa usafiri wa watu wa eneo lile. Sasa kivuko kile kimeshawahi kuharibika na kikapotea kikaelekea maeneo ya mbali. Kutokana na kupotea huko tunamshukuru Mungu hakikuweza kusababisha ajali ya kuua watu. Kwa kuwa kivuko hiki kinaharibika mara kwa mara; Je, Serikali ina mpango gani wa kututengenezea kwa uhakika ili kivuko hiki kiendelee kutumika katika eneo husika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mama yangu amekuwa akifuatilia sana mambo mbalimbali hasa kwenye Mkoa wa Lindi, kwa hiyo nitumie nafasi hii kumpongeze. Niseme tu kwa ufupi kabisa tunafahamu umuhimu wa kivuko hiki na tunafahamu namna kivuko hiki kinavyowahudumia wananchi wa Lindi. Tumefanya kwa kweli maboresho makubwa sana katika eneo hili, tumetengeza eneo la maegesho ya kivuko, tumetengeneza nyumba kwa ajili ya abiria wanaovuka kwenda ng’ambo kule. Niseme tu kwa tatizo la kivuko hiki kweli kimekuwa na matatizo kidogo na tumefanya ukarabati mkubwa lakini nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga kwa sababu Bunge hili limetupitishia fedha za kutosha kwa ajili ya kuongeza vivuko katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapatazama pale, itakapokuwa imewezekana tutabadilisha injini ya kivuko hiki, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge avute subira, tumejipanga ili tuone kwamba changamoto ambazo zilikuwa zinajitokeza na zinaendelea kujitokeza tutaendelea kuzitatua na kuziondoa kabisa. Kwa hiyo wananchi wa Lindi wawe na subira lakini niwape comfort tu kwamba, tumejipanga vizuri tutafanya maboresho makubwa pamoja na ile barabara ya kule ng’ambo tutaifanyia matengenezo ili wananchi baada ya kuvuka waweze kwenda na shughuli zao bila kikwazo chochote. Ahsante sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Swali langu, barabara hii iliyojibiwa na Serikali muda huu ina miaka miwili kwenye bajeti ya Serikali na barabara hii tumeiombea kura kwa maeneo yote ya Majimbo matano ambamo barabara hii inapita.

Mheshimiwa Spika, ni masikitiko yangu kwa majibu ya Wizara kwa kuwa tumebakiza miezi minne ya bajeti ya mwaka huu wa fedha unaoisha. Je, Serikali haioni kuwa kitendo cha kuombea barabara hii kura kutoka Karatu, Mbulu Mji, Mbulu Vijijini mpaka Maswa inawapa changamoto na imani ndogo wananchi wanaotuchagua na kutufikisha hapa tulipo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika barabara hii ninayoizungumza sisi Mbulu Mheshimiwa Waziri Mkuu ni shahidi na viongozi wengine wakuu, walipokuja kwenye kuomba kura walitegemea sana kauli ya Serikali juu ya utekelezaji wa barabara hii kuanzia Jimbo la Karatu, Jimbo la Mbulu Mji na Jimbo la Mbulu Vijijini hadi huko Maswa. Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka sasa kujibu kiu na imani ya wananchi wa Majimbo yote matano kwa barabara hii ambayo ni muhimu iliyoko juu ya bonde la ufa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kujibu swali la nyongeza, lakini nimshukuru Mungu sana na nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa imani kunipa nafasi ya kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, napenda nimjibu ndugu yangu wa Mbulu kwamba anafahamu na wananchi wa Mbulu na Manyara kwa ujumla wanafahamu juhudi za Serikali kuweza kuwakwamua wananchi kwa kujenga na kuimarisha barabara za maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge atakuwa shahidi kwamba katika juhudi za kuwasaidia wananchi wa Mbulu tumejenga daraja la maghala kwa gharama kubwa na wananchi sasa wanapita.

Mheshimiwa Spika, lakini siyo hivyo tu tumejenga daraja la Sibiti kwa nia ya kuwanusuru wananchi katika maeneo hayo, nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wanafahamu na wanaona na maboresho ya barabara katika barabara hizi ukitoka Karatu kuja Mbulu kupita Kilimapunda barabara zimeimarishwa ili kuwasaidia wananchi katika uzalishaji kwa ajili ya utalii, kwaajili ya kilimo na nataka kusema hivyo kwa ajili ya vipaumbele na upatikanaji wa fedha Serikali inafanya juhudi kubwa kuwasaidia wananchi wa Mbulu.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge hata hizo kilomita 50 ambazo zimewekewa mpango kazi wa kujengwa, kilomita 50 ilikuwa ni kipaumbele kwa kuwasaidia wananchi ambao kuna sehemu kubwa wanazalisha mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Spika,kwahiyo Mheshimiwa Mbunge na wananchi niwatoe tu hofu, mpango ambao upo, majibu mazuri ya Naibu Waziri aliyoyajibu hapa ikitekelezwa kwa kweli wananchi tunaenda kuwasaidia sana. Ahsante sana.
MHE. FLATEI G. MASSAY:Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali hili muhimu sana la nyongeza. Kwa kuwa amesema katika majibu yake ya msingi kwamba ametenga milioni 401 na ni wazi haiwezi kujenga barabara na Rais ameahidi mara mbili kwenye vipindi vyake viwili, je, haoni sasa aje na mpango mzuri wa kujenga barabara hii kwa kuitengea fedha?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naomba nimalize tu mwenyewe kwa vile nimeanza. Nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na anafahamu na niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge kama walivyosimama, nilipokuwa Naibu Waziriwa Ujenzi nilitembelea sana maeneo haya kwa sababu ya upendo mkubwa sana wa Waheshimiwa Wabunge, lakini pia kwa shida ambazo niliziona katika maeneo haya. Jiografia ya maeneo haya siyo nzuri Mheshimiwa Spika ndiyo maana kama nilivyosema awali kwamba Serikali imetenga fedha kuweza kuwakwamua wananchi wa maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu hata ile barabara kuja Babati imeendelea kutengenezwa naamekuwa na mradi wa kilomita mbili za lami pale kwake ni kwasababu Serikali ina upendo mkubwa.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana na kumshukuru Mheshimiwa Rais sana kwasababu katika juhudi za kutengeneza barabara za nchi hii tumeshuhudia kipindi kilichopita madeni ya wazabuni kiasi kikubwa sana yamelipwa na hii inaashiria kwamba tutaenda kutengeneza barabara kwa kasi kubwa zaidi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ucheleweshwaji wa ukamilishaji wa miradi ya barabara limekuwa tatizo sugu, ninapozungumza ujenzi wa barabara wa kutoka Kisolya, Bunda, Nyamswa, ahadi na uanzaji umechukua takribani miaka 15. Sasa nataka kujua ni lini barabara hiyo itakamilika kwasababu ikishakamilika kuanzia Kisolya inakuja Bunda Mjini kwenda Nyamswa inaunganika na barabara ya Serengeti na ni kilio cha muda mrefu cha Wilaya ya Bunda na wananchi wa Mkoa wa Mara, lini itakamilika baada ya ahadi na uanzaji takriban imechukua miaka 15? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, bado nanukia nukia ujenzi. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Bulaya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tujifunze tu kushukuru kwa sababu najaribu kuangalia miradi ambayo inaendelea sasa hivi kwenye Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Ester dada yangu anacheka pale, kuna miradi kemkem.

Mheshimiwa Spika, labda nimkumbushe tu Mheshimiwa, kweli barabara ya Bulamba-Kisorya, ilichelewa lakini imekamilishwa. Kuna mradi wa kutoka Kisorya kwenda Nyamuswa tayari mkandarasi ameshapatika, barabara inajengwa. Iko barabara ya kutoka Makutano – Nata - Sanzate imejengwa na kuna mradi kutoka Sanzate kwenda kule Serengeti na harakati za kujenga barabara kwenda kule Arusha zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafikiri Mheshimiwa Bulaya nimkaribishe tu Bungeni na anafahamu kwamba Serikali inafanya kazi kubwa sana katika Mkoa wa Mara. Kimsingi niseme Mheshimiwa Rais ameyapendelea sana maeneo hayo na kuyapa kipaumbele ili wananchi wa Mara waweze kupata barabara nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ningeanza kutaja miradi iliyoko Mara nadhani Mheshimiwa Ester anafahamu, nafikiri niishie tu hapo. (Makofi/Kicheko)
MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Waziri, naomba kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa inafahamika wazi kwamba baada ya Kambi ya Wakimbizi kuondoka, Serikali ilifanya expansion, yaani iliongeza mipaka ya Kambi ile ikamega Vijiji vya Katonga, Mgombe, Nyamusanzu na Buhoro bila kufuata taratibu. Bahati mbaya wakawa wamekabidhiwa Jeshi; na kumekuwepo na jitihada za Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wakishirikiana na Jeshi kutaka kuwarudishia wananchi maeneo. Sema walitaka kuwarudishia kipande kidogo, wananchi wakawa wamegoma.

Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kufanya jambo hili kwa haraka ili wananchi wale waweze kupata haki yao ya mashamba hayo ambayo yamechukuliwa kwa muda mrefu, aidha kwa fidia ya maeneo au fidia ya fedha? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vuma kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza uniruhusu nimpongeze tu Mheshimiwa Vuma, kwa juhudi zake anazozifanya kuhakikisha kwamba mgogoro ambao ulijitokeza tunaweza kuumaliza. Nampongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wafahamu kwamba Jeshi ni la kwao. Hili ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Watambue kwamba uwepo wa Jeshi ni kwa manufaa yetu sote. Kwa hiyo, tumekuwa na maeneo makubwa katika maeneo yetu, lakini lengo lake ni kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanatumika kwa ajili ya shughuli za Jeshi na vifaa vya Jeshi. Kwa hiyo, wananchi wakitambua hivyo, nawaomba tu wawe na ushirikiano. Nafahamu ipo migogoro kadhaa lakini nafahamu pia juhudi imefanyika kuhakikisha migogoro mingi tumeweza kuimaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namhakikisha Mheshimiwa Vuma kwamba suala la kumaliza mgogoro tunamaliza kwa kuwa kuna hatua nzuri tumezifikia. Vikao vya awali kama nilivyosema, vimeshafanyika, lakini sasa vikao ambavyo vitakuja kuendelezwa ni kuhakikisha kwamba tunamaliza mgogoro huu. Zipo Sheria za Ardhi na Sheria za Vijiji zitatumika ili kuhakikisha wananchi hawa wanapata haki zao.

Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, lakini naomba tuendelee kushirikiana; na wananchi wavute subira, tuko kwenye hatua nzuri ya kumaliza mgogoro huu. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Matatizo yaliyoko Kasulu Vijijini yanafanana na matatizo yaliyoko kwenye Jimbo langu la Mbozi katika Kijiji cha Sasenga na Itewe, kuna mgogoro kati ya wananchi na Kambi ya Jeshi. Napenda kumuuliza Waziri wa Ulinzi. Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua huo mgogoro ambao umekuwa ni wa muda mrefu kati ya hivyo vijiji na Kambi ya Jeshi 845KJ. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kwamba katika Kambi ya Itaka kuna shida hiyo ya mgogoro. Niseme kwamba migogoro hii imesababishwa na mambo mengi ikiwemo lile suala tu la uzalendo, majeshi yetu, pale ambapo tulikuwa tunawaruhusu wananchi kufanya shughuli zao; na walipozoea kufanya shughuli zao wakaamua kuhamia katika maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, kwamba tunafanya utaratibu maeneo yote na tumeshatambua maeneo yote yenye mgogoro na kwa hiyo, tumejipanga kwa ajili ya kuitatua. Tumeanzisha kitengo maalum cha miliki kuhakikisha kwamba migogoro yote tunaimaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mwenisongole kwamba tunafahamu shida ya Itaka na kuna hatua zinachukuliwa, tunakwenda kutatua shida ambayo iko kwa wananchi. Vilevile nawasihi sana wanasiasa na viongozi mbalimbali, kwamba kuna wakati mwingine tumetafuta kura Waheshimiwa Wabunge tukiahidi kwamba tutawasaidia wananchi kupata maeneo ambayo ni ya Jeshi. Niwahakikishie tu kwamba tutafuata taratibu kuhakikisha kwamba haki inatendeka, wananchi wanapata haki zao na Jeshi linaendelea kufanya shughuli zake bila kikwazo chochote. (Makofi)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Matatizo yaliyojitokeza huko Kigoma, ndiyo hali ilivyo katika eneo la Kampuni Mpanda Mjini.

Je, ni lini Serikali itakuja kutatua mgogoro wa wananchi na Jeshi katika eneo la Kampuni?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu la nyongeza la Mheshimiwa Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua mgogoro uliopo na nikipongeze Chama Cha Mapinduzi kwa sababu mlezi wa Chama katika Mkoa ameliwasilisha suala hili mezani kwangu na mimi nimeshachukua hatua. Nimetoa maelekezo ili uchambuzi wa kina juu ya mgogoro huu niupate.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Kapufu asiwe na wasiwasi na tutakwenda kwa kasi kubwa kuhakikisha kwamba wananchi katika Jimbo hili la Mpanda wanakaa vizuri, waendelee na shughuli zao na Jeshi nalo liendelee na shughuli zake. Kwa hiyo, taratibu zinaenda vizuri Mheshimiwa Kapufu naomba avute Subira tu kidogo.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Wananchi wa Mtaa wa Kenyambi na Bugosi katika Mji wa Tarime wana mgogoro wa muda mrefu na Jeshi la Wananchi na Serikali imeshafikia hatua nzuri tu ya kufanya tathmini na ikarudia tena kufanya tathmini bado imebakiza malipo. Napenda kujua ni lini wananchi wale wataenda kulipwa fidia yao ili waweze kuondoka maeneo yale na kuwaachia Jeshi la Wananchi wa Tanzania? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Matiko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru kwa kutambua kwamba tunaendelea kuwajali wananchi wetu wa Tanzania na niseme tu kwamba migogoro hii ilikuwepo kadhaa lakini niseme kwamba kati ya migogoro hiyo, zaidi ya asilimia 50 ya migogoro tumeshaitatua. Yako maeneo ambayo tumeyatambua kwa ajili ya fidia na wananchi wameshalipwa, yapo maeneo mengi ambayo tayari tumeshalipa. Hii inaonesha tunao mwendelezo mzuri wa kuendelea kulipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wananchi hawa wa Tarime wavute subira kwa sababu tunatafuta fedha. Tukipata fedha kwa maeneo yote ambayo tumeyatambua yanahitaji fidia kwa wananchi wetu tutakwenda kuwafanyia malipo. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Mbunge kuvuta Subira na wakati mwingine tunaweza tukaonana ili nimueleze kwa kinagaubaga namna tunavyokwenda kutatua matatizo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Kicheko)
MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamona na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini je, kwa vile tunafahamu kwamba, vijana hawa wanaokwenda JKT takribani wengi wao ni kutoka katika familia maskini na wanatumia gharama kubwa mpaka kufikia kwenye makambi. Je, Serikali iko tayari kuweka utaratibu pindi inapotokea dosari kama hii kuwarejeshea gharama ambazo wanatumia kwa ajili ya safari hizo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Omar Issa Kombo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyosema kwamba, lengo la kuwarudisha vijana ilikuwa ni kuhakikisha kwamba, tunaweka utaratibu mzuri. Nafikiri Mheshimiwa Mbunge akubaliane na mimi kwamba na kwa haraka utaratibu ukikamilika tutawahitaji tena vijana kwa sababu, yako manufaa makubwa sana kwa mafunzo ambayo yanatolewa kwa vijana kwa sababu, hawa vijana tunawaandaa, kuna mafunzo ambayo yanawasaidia pia kwenda kujitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kwamba, tutoe ushirikiano kwa Serikali, tutoe ushirikiano kwa Wizara kama wazazi. Kama anavyosema hata tulivyowarudisha tulizingatia kuona kwamba, vijana hawa wanarudi kwa kufuata utaratibu ambao tumeuweka. Tutaendelea kuona namna nzuri ya kuwasaidia vijana kupitia utaratibu ambao nilikuwa nimeutoa katika jibu langu la msingi.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Jeshi ni mali ya wananchi na wananchi ni sehemu yao. Sehemu ya Idofi Kihanga, eneo la pale Makambako kuna tatizo kati ya jeshi na wananchi na wananchi hawa wana eneo ambalo wanalima, wamepanda ulanzi, wanagema ulanzi kwenye eneo hilo. Sasa wana zaidi ya takribani miaka saba au nane wamekosa kupata kipato chao kupitia ulanzi. Je, Waziri atakuwa tayari kuongozana na mimi ili akaone mgogoro huu namna ambavyo tunaweza kuutatua, ili wananchi hawa waendelee kugema ulanzi wao?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sanga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Sanga sababu hata kipindi nilipokuwa kule Ujenzi, niliwahi kutembelea eneo la Idofi kwa sababu ni sehemu ambapo kuna mradi wa Serikali pale. Niseme tu kwa ujumla wake iko migogoro kadhaa kwenye maeneo mbalimbali ambayo yanamilikiwa na majeshi yetu. Kama alivyosema Mheshimiwa Sanga ni kweli kwamba Jeshi ni la wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niendelee kuwaomba tu Waheshimiwa Wabunge ikiwemo Mheshimiwa Sanga tuendelee kushirikiana na ameshauri nitembelee sehemu husika ili kutatatua mgogoro uliokuwepo. Nimhakikishie Mheshimiwa Sanga kwamba maeneo yote ambayo yana migogoro iko kamati maalum tuliiunda imetembelea maeneo yote. Kwa hiyo, Mheshimiwa Sanga tunafahamu changamoto iliyokuwepo pale Idofi nimhakikishie tu tutaenda kuimaliza kwa sababu uko mkakati Wizara tumeutengeneza ili kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yanamilikiwa na Jeshi ambayo yana changamoto tutaenda kuzimaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Najikita katika jibu la msingi la Mheshimiwa Waziri, amesema walisitisha mafunzo ya vijana kwa sababu kuna mambo wanataka kuyaweka sawa. Tunajua moja ya mafunzo wanayopewa vijana wa JKT ni pamoja na matumizi ya silaha na mbinu mbalimbali za kivita na ulinzi wa nchi yetu. Naamini Serikali inajua ni idadi gani ya jeshi la akiba wanaowahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha wanajipanga vizuri kwa nini wasihakikishe mafunzo fulani fulani ya silaha wanapewa watu kadhaa ambao wanajua wataajiriwa katika vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na wale wengine ambao hawaajiriwi wapewe mafunzo ya ujasiriamali ili waende kujiajiri wenyewe? Nasema hivyo kwa sababu siyo wote watakaopewa mafunzo ya kutumia silaha za kivita wakayatumia vizuri wanapokosa ajira. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bulaya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunatoa mafunzo kwa vijana na ziko sababu na uko utaratibu mzuri wa mafunzo hayo. Hatutoi mafunzo tu kiholela bali ni kulingana na mahitaji na matumizi ya nguvu kazi ya vijana tuliyokuwa nayo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mafunzo haya tunayoyatoa yana dhamira ya kulifanya taifa letu likae katika hali nzuri. Ahsante sana.
MHE. EDWARD K. OLELEKAITA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri, nini kauli ya Serikali kwa vijana waliomaliza mafunzo ya JKT na wameshiriki katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa nchi yetu lakini sasa wamerudi nyumbani bila ajira?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ni mara kadhaa amekuja tumezungumza juu ya hatma ya vijana na inaonyesha namna anavyowajali vijana wake. Kwa hiyo, nampongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema nafasi hizi za mafunzo ya vijana wetu zina nia nzuri, kwanza ya kuwafanya vijana ambao tunawafundisha kuwaunda ili kuwa na umoja wa kitaifa. Hiyo haipingiki kwa sababu tunavyokuwa tunawafundisha kule hatuna siasa, hatuna maneno mengi, tunawaunda wakae vizuri. Pia tunawaunda kuwa viongozi, wanaweza kuwa viongozi kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uongozi katika biashara na mambo mbalimbali ya ujasiriamali. Pia tunawafundisha kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na ubunifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba kwa vijana ambao wamepata nafasi ya kupata mafunzo haya pamoja na kupata stadi za kazi, tunawaandaa hawa vijana kwenda kujitegemea. Pia upande wa Serikali ziko fursa kadhaa ambazo Waheshimiwa Wabunge tunazifahamu ni za kuwafanya vijana hawa waweze kuchangamkia fursa ambazo zipo kwa maana ya kupata mitaji na kadhalika. Mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge tukiwaunganisha hawa vijana kwa skill ambazo wamezipata katika mafunzo yetu tutawafanya waweze kujitegemea na kutoa mchango mkubwa sana kwenye taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe Wabunge pale ambapo vijana wetu hawana taarifa hizi za fursa ambazo Wabunge tunazifahamu, tutumie nafasi hiyo kuwaunganisha vijana hawa, wawe kwenye makundi au binafsi ili Serikali iweze kuwasaidia vijana hawa na lengo ambalo limewekwa kwa ajili ya kuwasaidia vijana wetu liweze kutimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumejipanga vizuri na Waheshimiwa Wabunge niwakaribishe pale ambapo labda wanaweza wasiwe na uelewa wa kutosha niko tayari kuwaweka vizuri ili tuweze kuwasaidia vijana wetu kadri tutakavyokuwa tumejipanga. Ahsante sana.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini ningependa kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Mtaa wa Kinyambi na Bugosi hawafanyi shughuli zozote katika maeneo yale, na wengi wao walikuwa wanafanya shughuli ndogo ndogo za kujikimu kama kilimo na shughuli zingine na ukizingatia kwamba ni muda mrefu sasa tangu uthamini ufanyike, mwaka 2013 hadi sasa.

Je, wale wananchi wanaweza kuruhusiwa kuendelea na shughuli zile ili waendelee kujikimu badala ya kutaabika na kuendelea kukaa pale bila kufanya shughuli ambazo zinawaongezea kipato? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwita kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu kwamba maeneo yote ambayo yanamilikiwa na Jeshi letu ni muhimu na kwa manufaa ya nchi yetu na kwa wananchi kwa ujumla. Lakini niseme tu kwamba uwepo wa maeneo haya umepangwa kistratejia (strategically), tumejipanga kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kazi za jeshi zinafanyika vizuri. Niwaombe tu wananchi waweze kuvuta subira; kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, tunafanyia kazi ili tuweze kuwatendea haki wananchi hawa; hii ni pamoja na kuwalipa fidia zao ambazo zitawawezesha kwenda kufanya shughuli zao zingine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge kwanza nikupongeze kwa namna ambavyo mara kadhaa tumeweza kuzungumza na Mbunge ili tuone namna nzuri. Kikubwa nachoweza kusema hapa ni kwamba sisi tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba zoezi hili linakamilika mapema na wanachi wanapata haki zao. Tunaogopa kwamba tukiwaruhusu wananchi wakiendelea kutumia maeneo haya wanaweza wakafanya vitu ambavyo vina gharama kubwa na baadaye vikawatia hasara ndugu zetu hawa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo wavute subira tu, nafikiri tutaendelea kushughulikia suala hili kwa kuwasiliana Serikali zetu za Wilaya na Mkoa ili tuone namna nzuri ya kuwafanya wananachi wasikwame, waendelee kufanya uzalishaji na shughuli zao zingine. Ahsante sana.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru ni dhahiri kwamba maeneo ya Bugosi na Kinyambi ni tatizo la takriban miaka 17. Mara ya mwisho Serikali kupitia aliyekuwa Waziri wa Ulinzi ambaye ni Rais wa Zanzibar kwa sasa walifanya tathimini kwa mara ya pili hapo mwaka jana na wakawa wameshajiridhisha kwamba ile ya kwanza ilikuwa inawapunja Watanzania wale wa Tarime, na wakasema tayari wameshapitisha wanasubiri HAZINA kulipa hela na aliyekuwa Waziri wa Fedha ambaye ni Makamu wa Rais alidhihirisha hili kwamba tayari Fedha za Tarime zipo tayari kulipwa.

Mheshimiwa Spika, sasa hayo wanayokuja kusema leo inaonyesha ni jinsi gani Serikali haitoi umakini na uzito pale ambapo wananchi wamekuwa wametwaliwa ardhi. Sasa, ningeomba Mheshimiwa Waziri alete zile fedha ambazo zilishapitishwa tayari walikuwa wanasubiria Hazina kutoa ziende kuwalipa wale wananchi wa Tarime ili waende maeneo mengine wapishe jeshi lifanye shughuli zao. Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Matiko kama ifuatavyo:-

Mheshimwa Spika, niseme tu kwamba ule umakini wa kuhakikisha kwamba wananachi wanapata haki yao ndio huo ambao kwa namna nyingine umesababisha tumechelewa. Pia tumechelewa kwa sababu yapo matatizo kadhaa, Mheshimiwa Matiko anafahamu. Kwamba wakati wa zoezi hili likifanyika kwenye uthamini, na kwa uzoefu umeonyesha maeneo mengi, kumekuwa na changamoto hizi, na hasa Serikali inapoona kwamba kuna wananchi watakosa haki zao.

Mheshimiwa Spika, ni muhimu sana tukazingatia kwamba wananchi wapate haki zao. ndiyo maana unaona hata uthamini uliochelewa kwa utaratibu wa sheria na kanuni zilizokuwepo kwa nia hiyo hiyo ya kuwa-compensate wananchi kile ambacho wamechelewa kukipata ndiyo maana tunafanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge, vuta Subira; na sisi tumejipanga na sasa tunacho kitengo cha milki kwa nia ya kuhakikisha kwamba kinafanya kazi yake vizuri kwa matatizo hayo. Yako matatizo mengi maeneo mbalimbali; kwamba tumeweka kitengo hiki ili kiweze ku-coordinate ili tuone zile changamoto ambazo zilikuwa zinatokea zinaondoka. Tukienda kwenye hatua ya uhakiki wenzetu upande wa Hazina na kadhalika; changamoto nyingi zimekuwa zikionekana lakini tumedhamiria kuona kwamba maeneo haya,maeneo ya Tarime na maeneo mengine nchini yako mengi tunafanya hivyo kuhakikisha kwamba ile migogoro iliyokuwepo tunaenda kuimaliza. Kwa hiyo Mheshimiwa Matiko naomba uvute subira na ninaamini kwamba tutaenda kulimaliza mapema, tumejipanga vizuri. Ahsante sana.
MHE. AHMED YAHYA ABULWAKIL: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri na yenye tija, naipongeza Serikali kwamba hivi karibuni itapata kituo kile na kuondokana na gharika ya majambazi waliovamia miaka ya nyuma. Kwa sababu hiyo, nashawishika kumwuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kituo cha Polisi cha Kwahani Eneo la Ng’ambo Jimbo la Kwahani ni Kituo cha Polisi cha muda mrefu tangu ukoloni; na kwa sasa hakikidhi mahitaji kuhudumia wananchi wakati huu: Je, Serikali ina mpango gani wa kukitanua ili maofisa wetu waweze kufanya kazi kwa utulivu na ufasaha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kwamba, hivi karibuni Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amezindua soko jipya la kisasa eneo la Kibanda Maiti au tunaweza kusema Kibanda cha Demokrasia; linahudumia zaidi ya watu 10,000 usiku na mchana: Je, Wizara yako ina mpango gani kulinda usalama wa raia na mali zao? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwanza uniruhusu nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge anafanya kazi kubwa na wananchi wake hawakukosea kumchagua. Ninafahamu Mheshimiwa Mbunge amekuwa mstari wa mbele kwenye kuchangia maendeleo iwe kwenye elimu au vituo hivi vya Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kujibu swali lake, ninafahamu pia kwamba hii miji inapanuka na ongezeko la watu linakuwa kubwa. Ongezeko hili linaendana na changamoto mbalimbali zikiwemo za ulinzi. Kwa hiyo, niendelee tu kumsihi Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla tuendelee kuhamasisha wananchi kwamba jukumu la ulinzi ni letu wote ili tuweze kushirikiana kwanza kuhakikisha kwamba tunafanya maboresho makubwa katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, kazi kubwa ya Serikali imefanyika; yako maeneo mbalimbali ambayo ujenzi umeendelea kukamilishwa na kama nilivyosema katika jibu la msingi ni kwamba Mfuko huu wa Tuzo na Tozo umefanya kazi kubwa. Katika mwaka 2020/2021 peke yake zaidi ya nyumba 431 zimekamilishwa ili kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira mazuri ya askari wetu kufanya kazi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tuendelee kuhamasisha wananchi na Serikali kupitia mfuko huu tutaendelea kufanya maboresho makubwa.

Mheshimiwa Spika, mkakati tunaoufanya katika eneo hili la Kibanda Mauti, ni kweli kwamba kuna doria zinafanyika, wale wanaojihusisha na uhalifu wanaendelea kukamatwa na kufikishwa kwenye taratibu zetu za kisheria, lakini pia tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi, tunaendelea kuwashirikisha wananchi ili waweze kusaidia katika ulinzi na tunaendelea pia kushirikiana na vyombo vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe maelekezo kwa Jeshi la Polisi kule Zanzibar, washirikiane na Uongozi wa Soko katika eneo Mheshimiwa Mbunge amelitaja ili tupate eneo ambalo sasa tutaanza mkakati wa kujenga kituo katika eneo hili kwa sababu changamoto zimeongezeka na idadi kubwa ya watu katika maeneo haya na kuwepo kwa soko kunahitaji ulinzi madhubuti. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza; kwa kuwa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alitoa maagizo, taasisi na kampuni za Serikali kutumia Kampuni ya Ulinzi ya SUMA JKT. Je, hadi sasa ni makampuni mangapi au Taasisi ngapi za umma au Serikali zinazotumia Ulinzi wa SUMA JKT? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; je ni fedha kiasi gani hadi sasa Kampuni ya SUMA JKT inadai kwa wateja wake? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza la Mheshimiwa Angelina Malembeka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Malembeka kwa namna ambavyo anafuatilia maelekezo ya viongozi wakuu, lakini pia kufuatilia maendeleo hususan ya SUMA JKT. Kwa kujibu maswali yake niseme tu baada ya maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kuyatoa juhudi zimefanyika mpaka sasa idadi ya malindo 443 tunayo, ikiwemo malindo 259 ya Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma na malindo 184 ya watu binafsi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, ni kweli kwamba baada ya maelekezo yale tumefanya ufuatiliaji kama Wizara kulikuwa na rekodi ya madeni ya shilingi bilioni kama kumi na mbili na milioni mia tano (12,500,000,000) hivi, lakini baada ya uhakiki, deni hilo lilikuwa kwenye bilioni kumi na mbili na milioni tisini na sita (12,096,000,000), lakini kwa juhudi zilizofanyika asilimia 70 ya madeni yale ya kama bilioni nane na milioni mia tano (8,500,000,000) hivi zimeshalipwa. Bado tunalo deni kama la bilioni tatu nukta tano (3,500,000,000). Kwa hiyo, niendelee kuwashukuru wateja wetu kwa kutupa kazi, lakini niwashukuru pia kwa kuendelea kufanya malipo.

Mheshimiwa Spika, pia niwaombe wateja wetu waendelee kufanya malipo ya madeni haya kwani yapo manufaa makubwa kwamba tunapokusanya fedha hizi tunaendelea kuongeza ajira mbalimbali kwa vijana wetu lakini pia kadri tunavyoongeza huduma hizi za ulinzi, usalama kwenye mitaa unaongezeka kwa sababu pale ambapo tuna walinzi wetu wa SUMA JKT, ni msaada mkubwa kwa maeneo pia ya jirani na malindo yao. Kwa hiyo tunaendelea kupata manufaa makubwa, lakini kubwa zaidi pia tunaongeza uchumi katika nchi yetu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya Serikali nadhani haielewi Swali langu la Msingi. Chikongo tunaposema upande wa pili wa Msumbiji, wenzetu tayari wanacho kituo cha uhamiaji, upande wa Tanzania ndio hatuna kituo cha uhamiaji: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali languni kwamba, ni lini Serikali itapeleka kituo cha uhamiaji upande huu wa Tanzania? Si suala la mashauriano na Msumbiji kwa sababu, Msumbiji wao tayari wanacho kituo cha uhamiaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili. Je, wenzetu wa Msumbiji tunapopeleka bidhaa kule wana custom pale, wana shughuli zote pale. Upande wa Tanzania wananchi wetu wakileta bidhaa wanapata shida kwa sababu hawana custom hapo, TRA hawapo pale. Tupe kauli ya Serikali, ni lini mtajenga kituo cha uhamiaji pale na kupeleka huduma nyingine zote za msingi ili Watanzania wapate huduma kwa urahisi pale?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Katani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Katani kwa kazi nzuri anayoifanya; na ndiyo maana wananchi wa Tandahimba walimuamini na kumpa nafasi ya kuwawakilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme kwa ujumla wake kwamba lengo la Serikali ni kudhibiti maeneo yote ya mipaka yetu, ikiwemo uingiaji wa wageni na utokaji pia wa wananchi wetu. Pia kudhibiti mapato kupitia TRA, yako pia masuala ya afya pamoja na masuala ya usalama kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kuhusu maswali yake yote mawili kwa ujumla. Ni kwamba niwatoe hofu tu wananchi wa Tandahimba, tunaona uko umuhimu. Kituo cha uhamiaji ambacho tunacho kiko makao makuu ya wilaya, ni mbali kidogo na sehemu ambapo wananchi wanavuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Katani, kwamba suala hili tumelichukua. Nitumie nafasi hii tu kumuelekeza Kamishna wa Uhamiaji atume wataalam pale. Kwa sababu wananchi kama wanagonga passport zao ng’ambo wanapoingia; ni muhimu wananchi pia wa Tanzania waweze kupata huduma vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala hili nalielekeza tu lifanyiwe kazi mara moja na sisi tutaendelea kusimamia kama Serikali kuona wananchi hawapati shida na tunapata manufaa makubwa sana kutoka kwa nchi za majirani kupitia biashara na mambo mengine ambayo yanahusiana na mambo ya mipakani. Ahsante sana.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mimi ninauliza swali moja ambalo ni, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi kwenye Soko la Kimataifa la Mwika ambalo liko mbali sana kutoka Himo ambako ndiko kwenye kituo cha polisi?

Mheshimiwa Mwneyekiti, ahsante sana.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, nimjibu Mheshimiwa Kimei, swali lake la nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kimei, kama ulivyosema, na niseme tu kwamba uko umuhimu wa kuwa na kituo cha polisi. Si maeneo tu haya ya Mwika, lakini maeneo mengi ambayo yanaweza yakawa yanajihusisha na biashara kama ilivyo eneo la Mwika. Nilichukue suala hili ili tuone upande wa Serikali kulifanyia kazi haraka ili tuweze kuleta manufaa makubwa. Ili biashara iweze kushamiri vizuri tunahitaji kwa kweli kuwa na ulinzi wa kutosha katika maeneo haya. Ahsante sana.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kata ya Mwakijembe tuna changamoto kubwa sana ya ukame. Kwa hiyo, eneo hili lililotwaliwa ndilo eneo pekee linalofaa kwa kilimo; na kwa sababu, wananchi hawa wameondolewa kwenye eneo lile.Je, Serikali iko tayari kufanya mchakato wa haraka wa kuwafidia watu hawa ili waondokane na madhila wanayoyapata sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili. Kwa kuwa imebainika wazi kwamba eneo hili ni hatarishi; kwa miaka miwili mfululizo yametokea mafuriko makubwa na tumewahatarisha Askari wetu kwenye eneo lile: Je, Serikali ipo tayari kuwahamisha Askari hawa kwenda kwenye eneo la awali ambalo Kamati ya Bunge ililiona ili Askari hawa wakae kwenye eneo ambalo ni salama? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kitandula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, ni dhamira ya Serikali kupitia Wizara yangu kuwalipa fidia wananchi wa maeneo yote ambayo yametwaliwa kwa ajili ya matumizi ya shughuli za kiulinzi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Kitandula kama tulivyowahi pia kuzungumza, ni kwamba tunashirikiana na wenzetu Wizara ya Ardhi na Wizara ya Fedha, na yako maeneo mengi ambayo tayari tumeshalipa fidia; pia uko mpango wa Serikali kupitia Wizara ya Fedha kutupatia fedha na taratibu zikikamilika wananchi hawa nawahakikishia kwamba watalipwa mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kuona umuhimu wa eneo hili kutumika tena kwa wananchi, niseme tu kwamba, labda kutokana na changamoto za mvua nyingi tulizozipata hivi karibuni, umevutiwa pia kuona uko umuhimu wa wananchi kuendelea kufanya umwagiliaji katika eneo hili; niseme tu kwamba zile sababu za kupewa eneo hili bado zipo. Hata hivyo tunaweza tukalitazama kutokana na maoni ya Mheshimiwa Mbunge kwa sababu, iko kamati maalum ambayo inaendelea kuyapitia maeneo yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbune kwamba, naelekeza wafanye pia marejeo katika eneo hili kwa kushirikiana na Kamati yetu ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na pia kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge ili tuone kama pia tunaweza tuka-reallocate, tukapata eneo lingine bila kuondoa sababu muhimu za kufanya vijana wetu waendelee kufanya shughuli zao muhimu katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba tutaendelea kushirikiana ili kuona tunaweza kutenda vema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kuona umuhimu wa eneo hili kutumiwa tena na wananchi, labda kutokana na changamoto ya mvua nyingi tulizozipata hivi karibuni, Mbunge amevutiwa kuona kwamba upo umuhimu wa wananchi kuendelea kufanya umwagiliaji katika eneo hili. Niseme tu kwamba, zile sababu za kupewa eneo hili bado zipo, lakini tunaweza tukalitazama kutokana na maoni ya Mbunge kwa sababu ipo Kamati Maalum ambayo inaendelea kuyapitia maeneo yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nimhakikishie tu Mbunge kwamba naelekeza wafanye pia marejeo katika eneo hili kwa kushirikiana na Kamati yetu ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya lakini kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge ili tuone kama tunaweza tuka-reallocate, tukapata eneo lingine bila kuondosha sababu muhimu za kufanya vijana wetu waendelee kufanya shughuli zao muhimu katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba tutaendelea kushirikiana ili kuona tunaweza kutenda vema.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niunge katika swali alilouliza ndugu yangu Mheshimiwa Dunstan Kitandula, kwamba kumekuwa na utaratibu au zoezi ambalo linaendelea kule Msata katika maeneo ya Kihangaiko na Pongwe Msungura wakipima maeneo ya wananchi katika maana ya kulipa fidia, lakini kwa taarifa nilizozipata za juzi ni kwamba zoezi lile limesimama kwa sababu ya Mkataba ambao walikuwa wamepeana baina ya Wizara na yule mpima kuhusiana na eneo lile. (Makofi)

Mheshimimiwa Mwenyekiti, sasa katika spirit ya kuondoa migogoro iliyoko baina ya Jeshi na wananchi…

MWENYEKITI: Sasa uliza swali.

MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inasemaje? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, maarufu kama Baba Aziza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira yetu kupima maeneo yote yanayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Kwa hiyo huo ni utaratibu unaoendelea na nimhakikishie tu Mheshimiwa Ridhiwani, sio kwamba zoezi limesitishwa, zoezi la upimaji maeneo yote linaendelea lina hatua zake. Kwa hiyo niwatoe wasiwasi tu wananchi wa eneo la Msata Kihangaiko, wanavyoona wale wapimaji hawapo wanafikiri labda shughuli imesita, hapana.

Nimtoe wasiwasi pia Mheshimiwa Ridhiwani zoezi linaendelea, tutahakikisha maeneo yote tunamaliza kufanya upimaji na wananchi wanapata haki zao. (Makofi)