Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Edwin Mgante Sannda (7 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa jina naitwa Edwin Sannda, wengi huwa wakisikia hili jina wanashtuka kidogo; lakini msishtuke, Sannda hii ni nzuri tu, siyo kama ile ya kuzikia. Ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nachukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwepo hapa, lakini pia nikishukuru chama changu kwa kupitisha jina hatimaye likaenda kupigiwa kura. Nawashukuru wadau wangu wote, familia, ndugu jamaa na marafiki na hatimaye wapiga kura wa Jimbo la Kondoa Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja napenda kuchangia kwenye hotuba ya Rais. Kwanza kabisa naipongeza; imekaa vizuri, imegusa nyanja zote, lakini pia nawapongeza kwa wale waliotupa Mpango wa miaka mitano wa Maendeleo, wameakisi moja kwa moja hotuba ya Rais, wamegusa kila nyanja, nawapongeza sana. Pia yule aliyewasilisha ule mpango ni pacha wangu, kwa hiyo naye nampongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichangie pale kwa maana ya vitu vikubwa vinne. Mpango mzuri, lakini huwa tatizo letu linakwenda kwenye utekelezaji (execution). Nawaomba hasa wale Wizara ya Fedha na Mipango na Serikali nzima kwa ujumla, suala la utekelezaji ndiyo liwe msingi mkubwa wa kuangalia (execution). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, yameongelewa mengi sana kuhusiana na government efficiency na effectiveness (ufanisi wa Serikali), lakini kila tunapoongelea ufanisi wa Serikali, tunazungumzia kupunguza gharama na kubana matumizi. Napenda pale kwenye suala la efficiency ya Serikali tuongezee suala la delivery time, kukamilisha miradi, kufikisha huduma na yenyewe mwisho wa siku inaingia kwenye gharama. Tukiweza kufanikisha eneo hili napo tutakuwa tumefanya vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mbali na delivery pia suala la ubora. Tunatengeneza vitu, tunakamilisha miradi chini ya viwango, hatimaye tunahitaji kufanya marekebisho muda siyo mrefu, ambayo pia ni gharama tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwenye government efficiency, labda tungeangalia sehemu tatu, gharama inavyozungumziwa ya kwanza, delivery time, pamoja na quality ya huduma zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha tatu ningependa kuzungumzia suala la ubunifu kidogo. Kila mmoja aliyesimama kati yetu hapa anavutia kwake, tatizo liko hili, huduma zinahitajika hizi lakini mwisho wa siku ni lazima tujue ni namna gani tutatoka nje ya box tuwe wabunifu kuongeza kipato chetu. Tukiwa na kipato kikubwa kabisa kama nchi, ina maana hizi huduma zote zitafika, siyo tunagombea zile rasilimali chache. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nafikiri, tujaribu kuangalia kama inawezekana, maana na sisi wenyewe ndio tunaotunga sheria, tukawekeza kwenye baadhi ya sekta. Hawa wawekezaji wakubwa wanaokuja au sekta ambazo tutaziona ni nzuri kabisa zitatuletea tija, mbali na kodi tunayopata, vyanzo vya kawaida vya mapato ya Serikali, lakini tuwe na hisa tuwekeze ili tuwe tunapata magawio yaongeze katika Pato zima la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri Wizara ya Fedha pamoja na nyingine, hebu tuangalie eneo hili, kama litahitaji sheria ya kubadilishwa au kutungwa, siyo kwamba tunaenda kufanya biashara per se lakini angalau tuwe na uwekezaji na sisi tuongeze vyanzo vya mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ninalotaka kuongea ni suala la…
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza kabisa naanza na itifaki ya pongezi kwa Rais wetu, Waziri Mkuu kwa mpango mzuri na timu yake nzima ya Mawaziri na Manaibu Waziri.
Kwa ujumla mpango huu ni mzuri sana, nami nimeupitia, nimeuangalia kwa kina, kwa upana wake na kwa ujumla wake ni mpango mzuri kweli kweli; wanastahili pongezi sana. However, kuna marekebisho kadhaa yanahitajika katika maeneo mbalimbali ili mwisho tuweze kuunga mkono hoja kikamilifu. Marekebisho hayo ndiyo yataukamilisha mpango huu uwe bora zaidi ya ulivyo sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie maeneo mawili tu kwa leo; la kwanza ni lile la uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Tukienda ukurasa wa 15, wanasema Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kuwadhamini wajasiriamali wenye miradi inayokidhi vigezo kwenye taasisi za fedha ili wapate mikopo yenye masharti nafuu.
Haya mafunzo pamoja na mpango ule ambao upo ukurasa wa 16 wa shilingi milioni 50 kila kijiji, nafikiri mpango ni mzuri, utekelezaji wake ndiyo huwa tatizo.
Sasa ili tuweze kusaidia, nasi Wabunge kwanza tushirikishwe katika mpango wa utekelezaji mapema, tuwe nao. Tutakachofanya, kikubwa zaidi tunaenda kuandaa watu wetu, kwa sababu mpaka sasa hivi, wana matumaini makubwa kweli kweli, wanasubiri, wana kiu na kadri wanavyosubiri, tunatoa fursa ya maneno ambayo huenda siyo sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge tukiupata mapema kama Wawakilishi wa wale wananchi, tukaenda kule, tukauangalia, tukaanza kuujaribu, tukaanza kuustadi kwa kina, tutaweza kubaini upungufu na kuufanyia marekebisho. Kwa hiyo, kabla ya utekelezaji, tutakuwa tumeweka kila kitu kimekaa sawasawa na hatimaye muda wa utekelezaji unapofika, bajeti inakuwa imekaa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine napenda kushauri na hili lipo kwenye Wizara ya Fedha nafikiri kuna umuhimu sana katika maeneo ya kuboresha, ni kutengeneza mechanism ya monitoring na control, watu watakuwa wameshapata zile fursa, fedha zimetolewa lakini unawezaje kuhakikisha na kutengeneza mfumo wa kwamba tunawakagua hawa watu kadri wanavyokwenda? Vinginevyo hizi fedha zitatoka, mikopo itatolewa, lakini lile lengo tunalotaka lifikiwe mwisho, watu wafanikiwe, wapunguze umaskini, wainue uchumi, tutakuwa tumekwama kama hatutatengeneza mfumo na muundo imara wa monitoring na control.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale wanapokosea, kweli watu wetu sio wote wana ujuzi wa ujasiriamali, wanafundishwa leo, halafu unamkabidhi hela mtu ambaye huenda hajashika kiwango hicho cha hela kwa muda mrefu au labda toka azaliwe, halafu ukategemea atafanikisha kadri tunavyotegemea, inaweza ikawa mtihani mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali, tutengeneze mechanism nzuri sana ya kuweza kuwachunguza na kuwasimamia hawa mpaka mwisho tuone matokeo yake. Hapo kweli tutakuwa tumefanikisha zoezi na azma yetu ya kuwawezesha wananchi wetu kiuchumi ili tuweze kupunguza umaskini. Hili ndilo eneo ambalo tukiwawezesha hawa wananchi wa kawaida tunaosema ni maskini, ile macro-economy itakuwa supported vizuri sana na wananchi wa kawaida kwa sababu kila mmoja sasa atakuwa kidogo ana nguvu yake na anaweza kuendesha maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo moja la uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, naomba niachie hapo, nafikiri Waziri wetu wa Fedha na Mipango amelipata na Naibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia suala zima la elimu. Mpango wa elimu ni mzuri, maeneo yote yameelezewa. Hili lipo kwenye ukurasa wa 49, naomba nisome kidogo mwone jinsi ambavyo inatakiwa iwe. Anasema:
“Hatua zinazochukuliwa zinalenga kuhakikisha kwamba elimu ya Tanzania ni ya viwango vya ubora wa hali ya juu ili kuwawezesha vijana wetu kukabiliana na changamoto za maisha ya kujiajiri wenyewe na kumudu ushindani katika soko la ajira la ndani kikanda na Kimataifa.” Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kauli ni nzuri sana na imewasilishwa vizuri kweli kweli, lakini lazima tuangalie kwa ujumla wake, ule mfumo, muundo na taratibu za utoaji wetu wa elimu kuanzia awali zinamjenga mtu kwa namna gani. Tunataka practically ziweze kutoa matunda au matokeo ya wanafunzi ambao ni competent, kwenye soko la ajira tukienda huko, tunaona namna tunavyo-perform.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukilinganishwa tu na wenzetu wengine wa nchi za jirani na hapa tumezungumzia kikanda na tumezungumzia Kimataifa, competence yetu kwa kweli inahitaji kuboreshwa sana. Hili ndilo eneo ambalo kwenye hotuba hii ya Waziri Mkuu, kuna umuhimu sana wa kuliboresha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ubora tuuteremshe chini practically, tuhakikishe mifumo, muundo na utaratibu wetu wa kutoa elimu kuanzia chini, unamjenga kijana awe na uwezo, ajiamini, ajitambue kwenye suala zima la nidhamu ya mafanikio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumze jambo moja ambalo kwa kweli linanisikitisha na Naibu Waziri wa Elimu nafikiri yupo hapa. Watu wanaopata Division IV wanachukuliwa kwenda kuwa Walimu.
Sasa kipindi chote hiki ambacho tulikuwa na Walimu waliopata Division IV ndio wanakwenda kufundisha watu, halafu tunataka kujenga matunda ya watu ambao wana kiwango bora cha elimu, hapa kidogo pana mtihani, lazima tubadilishe hili, haiwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatumia neno failure, kwamba Division IV ni failure ingawa kwa sasa kiwango cha Division IV inaonekana ni ufaulu. Sitaki kuamini kama ni ufaulu na ipo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza pia tubadilishe, ufaulu uishie Division III. Unapozungumzia Division one, two, three, ndiyo ufaulu. Sasa tunapiga mahesabu mpaka Division IV mtu anaaminika kwamba amefaulu halafu ndio hao wanaenda kufundisha, halafu tunategemea watoe product ambazo ni nzuri! Siyo rahisi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tujenge uwezo, tujenge wanafunzi wanaotoka wanajiamini huko nje; akienda anajieleza, anajiamini. Akiambiwa afanye kazi, ana competence ya kutosha.
Kwa hiyo, napenda nitumie fursa hii kuwasilisha marekebisho kwenye hii hotuba kwamba, suala zima la elimu, dhana ni nzuri sana, lakini ni lazima tuboreshe mfumo na muundo, utujengee na kutoa competence katika elimu yetu kuanzia elementary mpaka Chuo Kikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kubwa nataka niwasilishe hili la Division III kuendelea kuwa ufaulu, nashauri libadilishwe. Sasa tukishafanya maboresho hayo yote, kimsingi nitakuwa sina shida ya kuunga mkono hoja hii. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, kwanza kabisa pamoja na kazi kubwa, kazi nzuri inayofanywa na Waziri pamoja na timu yake yote, lakini napenda kusema kwamba, naona bajeti hii haija-reflect ile safari tunayotaka kwenda, haija-reflect mapinduzi ya elimu ambayo tunataka kwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumzia tunakwenda kwenye uchumi wa kati, uchumi wa kati tukasema tunahitaji mapinduzi ya viwanda, lakini kunahitajika mapinduzi mengi tu, mojawapo ni mapinduzi ya elimu, tuweze kweli kweli kupata transformational change. Sasa kama safari ni hatua, tuone kabisa hatua inayokwenda, kama nakwenda tuseme Kondoa, basi naona nimetokea Dodoma naona nimefika Aneti, nione nimefika Chemba, mwisho wa siku nifike Kelema na hatimaye nifike Kondoa. lakini kwa bajeti hii na malengo yetu ya muda mrefu ambayo tunataka kuyafikia, kwa kweli Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yako, nafikiri kuna kazi kubwa sana ya kufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri inabidi tuamue sasa kuwekeza kwenye elimu kwa kiwango kikubwa kweli kweli. Huu uwekezaji tulioufanya sasa hivi katika bajeti, naona hautatufikisha pale tunapotaka kwenda, hiyo nilipenda nianze kuzungumzia kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye hoja mahususi katika bajeti nzima ya elimu. Kwanza napenda kuongelea wanafunzi. Suala la mfumo, muundo na kanuni za ufundishaji na kwa maana ya kutoa mitaala naona haimjengi mwanafunzi wa Kitanzania katika kwenda kuingia umahiri katika soko la ushindani kwa maana ya competence. Sisi hatuko wenyewe, dunia siku hizi ni kijiji na inatakiwa wanafunzi wetu wanapotoka huko nje waweze kushindana katika soko duniani, waweze kujiamini, wajenge uelewa badala ya kujenga kukariri na kufaulu mitihani, wajenge uwezo wa kujieleza, matokeo yake wanapofika huko mbele wana uwezo mkubwa wa kupambana na ku-survive, wanasema survival for the fittest. Sasa kama elimu yetu haitujengi kwenda kuwa fit duniani itatukwamisha sana, tutakuta tu tunaendelea ku-import knowledge kutoka kwa wenzetu, lakini wa kwetu sisi hawatoki kwenda nje nao wakafanye vitu vyao huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri ni wakati muafaka kabisa Wizara ikae na kujiuliza, hivi tatizo liko wapi? Tujiulize sana na tufanye tafiti za kutosha sana, tunao Wataalam, tujiulize tatizo liko wapi? Kwa nini output, kwa nini products za wanafunzi wetu siyo mahiri? Kwa nini hatuko competent sana on average? Wapo watu wazuri, wanatokea wazuri, lakini on average elimu yetu hairidhishi. Kwa hiyo katika hili, ningesisitiza sana uwekezaji investment ifanywe kubwa sana kwenye RND kuweza kuhakikisha tunainua ubora wa elimu yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nataka nizungumzie kwa upande wa Walimu. Hapa hasa ndiyo kwenye kasheshe. Ifike mahali sasa ile dhana iliyopo kwamba Ualimu ni kazi ambayo ni dhaifu, mtu huwezi kujivunia, hatuwezi kuikimbilia, tubadilike kabisa. Ifike mahali Ualimu uheshimike, mtu unapoamua kwenda kusomea Ualimu una-proud kwamba mimi ni Mwalimu. Mwalimu awe na uhakika wa ajira, lakini awe na uhakika wanasema maslahi mazuri, very well paid, waweze kuwa motivated vizuri sana, waweze kuwa na incentives kubwa, lakini mazingira pia ya kazi lazima yawe tofauti sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaowachukua hawa kuwa Walimu, siyo ile ya sasa hivi labda tunakwenda mpaka division tofauti tofauti, Walimu wanatakiwa kuwa top scores, top performance ndiyo wawe Walimu na mwisho wa siku na kama maslahi yako mazuri na wanalipwa vizuri, kila mtu atakuwa ana pride kusema akawe Mwalimu na watu wengi watakimbilia kwenda kufundisha. Ualimu uwe ni kazi ya bright students. Tukifanya hivyo kweli tutakuwa tumefanya transformational change, mwisho wa siku Walimu wetu kama ni wazuri, obviously products zao zitakuwa ni nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, napenda kuchangia kwenye suala zima la polytechnic, Vyuo vya Ufundi. Hapo zamani tulikuwa na Vyuo vya Ufundi Dar Tech, chuo ambacho nilisoma mimi, Chuo cha Ardhi kilikuwa kinatoa Wataalam, Mafundi, lakini sasa hivi vile vyuo vyote tumevigeuza vinapanda hadhi vinakuwa Vyuo Vikuu. Sasa kama kila mtu atavaa tai, kila mtu anataka kuwa meneja, kila mtu anataka kuwa na degree, nani atakwenda site kusimamia kazi? Nani ataingia maabara kuhakikisha kazi za kitaalam zinafanywa vizuri?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kuwa na Vyuo Vikuu vingi, ni sawa tuwe na Vyuo Vikuu vingi, lakini polytechnic ni muhimu sana kuhakikisha kazi za kitaalam zinafanywa. Rai yangu kwa Serikali, hebu tuache hili suala la degree na tai, lakini tuwe na FTC‟s za kutosha. Arusha tech ziimarishwe, ziwe bora zaidi, ziwe equipped, ziwe resourced ili watu wetu wanaotoka kule wakienda kazini, wawe na uwezo hasa wa kusimamia details za kitaalam. Turudishe polytechniques zetu. Kwa hiyo, pamoja na jitihada kubwa ya kuongeza idadi ya Vyuo Vikuu na kutoa degree, hebu na suala la polytechnique tuliangalie sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tano na la mwisho, napenda kuongelea kuhusiana na wataalam, watu wanao-qualify, wamekwishasoma degree zao au kama ni FTC, wametoka wameingia kwenye soko la ajira, tutengeneze utaratibu mmoja wa kuwekeza kwa hawa watu ili wakapate exposure programs, wajifunze, waige utaalam, waige experience. Nchi za wenzetu ambazo kwa baadhi ya taaluma zinafanya vizuri. Nitatolea mfano suala la Madaktari, hata Walimu au Wahandisi, lakini nitatolea mfano suala la Madaktari; watu wawe wanatoka tunawapa Mikataba specific wameshamaliza shule, lakini anapelekwa mtu zaidi ya miaka mitano mpaka hata kumi, si tunawekeza kwa ajili ya generation zijazo? Tunawekeza kwa ajili ya kupata transformation ya elimu yetu kwa ujumla wake, watu waje hapa wana uwezo mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi tu tumeshuhudia Tanzania zimefanyika operations za kwanza kubwa za moyo. Watu wanafunua moyo ule ndani wanazibua mirija iliyoziba, lakini waliokuja kufanya ile operation wanatoka India. Kawaida kuna ushirikiano na Australia, Saudi Arabia na Marekani, basi tuwapeleke Madaktari wetu nao wakasome, tuweke mikataba mahususi, watu wakasome, tukishamaliza kuwekeza kwenye elimu hapa, wakimaliza wanakwenda nje, wakirudi they bring back wealth of experience ambayo itatusaidia sana kubadilisha mfumo mzima wa uwezo na knowledge hapa nchini. Kwa hiyo, nasisitiza sana, katika jambo kubwa tunalotakiwa kulifanya kama Serikali ni kuwekeza kwenye elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumerudia na tunaendelea kuimba kwamba tunakwenda kwenye uchumi wa kati, lakini huu uchumi wa kati bila mapinduzi na transformation ya sekta nyingine hizi kama elimu, pia ni mtihani mkubwa tunaweza tusifike. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Elimu kama pioneer katika Serikali kwenye suala zima la elimu, hebu tuangalie maeneo yote haya, kuanzia mitaala, kuufanya Ualimu uwe ni kazi ya kujivunia, shule zetu za polytechnique pamoja na hawa wataalam tuweze…
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa niweze kuchangia kwenye hotuba ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nawapongeza Mawaziri wote wawili kwa hotuba zao nzuri sana, zimesheheni mambo mengi, hata hivyo, pamoja na hotuba nzuri napenda kutoa maboresho kwenye maeneo machache yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ni suala zima la utawala bora na uwajibikaji. Taarifa na hotuba inaeleza vizuri baadhi ya watumishi ambao wamekuwa wakifanya makosa na wakivuruga wanawajibishwa kwa kufuata taratibu za kinidhamu na hatimaye pia za kijinai. Wapo ambao pia wamepelekwa Mahakamani, wapo ambao wamefukuzwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na taarifa hii inaonesha tuko vizuri sana katika utaratibu huu, lakini kiuhalisia nikitoa mfano wa Halmashauri kama ya kwangu ya Kondoa Mjini wamekuwepo watu wengi sana ambao wamekuwa wakivuruga hasa Maafisa Ardhi, hata Mkurugenzi aliyekuwepo. Kinachotokea badala ya kuwajibishwa kutokana na makosa yaliyofanyika, wanahamishwa. Sasa unapomhamisha huyu mtu unahamisha tatizo siyo? Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Mawaziri, badala ya kufanya suala la kuwa-reshuffle hawa watumishi wanaovurunda, taratibu za kuwawajibisha kinidhamu na hatimaye kijinai zifanyike kwa wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na Maafisa Ardhi wengi sana wamekuwa wakituvuruga, anatoka Kondoa anapelekwa Rombo, anatoka Rombo anapelekwa sijui eneo lingine, wanaenda kuhamisha matatizo tu hayo. Pia wapo ambao kesi zimepelekwa Mahakamani, lakini wanatoka pale wanakwenda Makao Makuu TAMISEMI, wanasema sijui wamekaa benchi au vipi, sasa utaratibu huu haujengi nidhamu ya kuwafanya hawa watumishi wengine wawe waadilifu na wafanye kazi zao kadri ya miongozo na taratibu zinavyowataka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri huu utaratibu wa kutumbua majipu, huku kwenye Halmashauri zetu uende vizuri kabisa, watu kweli watumbuliwe maeneo yote, siyo mtu anavuruga halafu anahamishwa, hii haitatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, ipo hali ya baadhi ya watumishi kutokuwajibika, mfano, sasa hivi Halmashauri yangu ni zao la Halmashauri iliyokuwepo, wale wote ambao walionekana kwamba they are non- performance, wanahamishwa wanapelekwa kwenye Halmashauri mpya, kweli hakuna utaratibu tunaoweza kujiwekea kupima performance ili hawa ambao mwisho wa siku hawa-perform wawajibishwe? Nafikiri hilo ni suala muhimu sana la kuliangalia Waheshimiwa Mawaziri, ili watumishi wetu wanaokuwa Serikalini na kwenye hizi Halmashauri waweze kuwa wawajibikaji wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala zima la elimu, kwenye elimu naongelea suala la Walimu, nikianza na upungufu wa Walimu. Upungufu wa Walimu ni tatizo kubwa, najua utaratibu unafanywa ili Walimu wengine watoke vyuoni waweze kuingia kwenye mashule kufundisha, lakini wanapotoka upungufu ni mkubwa sana hapa katikati, shule zinateseka, wanafunzi wanaumia, wanashindwa kupata masomo yao kadri inavyostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale kwangu kwenye elimu ya Sekondari tuna upungufu wa Walimu zaidi ya 80. Jibu dogo tu la Kondoa Mjini upungufu zaidi ya Walimu 80, kwenye shule ya msingi kuna upungufu wa Walimu zaidi ya 60. Mpaka waje kutimia na mahitaji najua ni ya nchi nzima, utakuwa mtihani mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nishauri kitu kimoja, wapo wale Walimu ambao in the interim kama mpango wa muda mfupi tu wakati tunasubiri uzalishaji wa wale Walimu wengine wapya. Wapo Walimu ambao walistaafu, haiwezekani tukawapa mikataba ya muda mfupi, wa- fill hii gap in the interim wakati tunasubiri hao wengine wanakuja, itusaidie kidogo kupunguza makali ya upungufu wa Walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niliweke hilo kama changamoto na mapendekezo ya kuboresha hawa Walimu ambao tunazungumzia wanadai mafao, wanadai malimbikizo ya mishahara, hebu tuwatumie wale wanaweza wakatusaidia kwa muda mfupi.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa hapo, katika suala la Walimu, najua hili litamgusa zaidi Waziri wa Elimu Profesa Ndalichako, pia nataka niliweke hapa kwenu, Walimu na nilizungumza kwamba mkazo wangu upo sana kwenye elimu. Walimu watokane na best performance, siyo Walimu watokane na yale madaraja ya mwisho ndiyo wanaenda kuwa Walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kufanya ni kuboresha maslahi yao pia kuwa-remunerate vizuri, kuwa- compensate vizuri na kwa kuwa ajira yao itakuwa inaonekana ina uhakika zaidi na iko vizuri wanafunzi wengi watataka kwenda kufanya hii kazi ya Ualimu. Tutakuwa tumewa-motivate, tumewa-inspire, matokeo yake kazi ya Ualimu itaonekana ni kazi yenye heshima, siyo kazi tu ya wale wanaofeli. Wanalipwa vizuri, wanatengenezewa mazingira mazuri ya kazi, matokeo yake inawa-motivate na kuwa-inspire watoto wetu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Profesa Ndalichako katika marekebisho yetu tunayoyafanya, moja ya vitu vya kuhakikisha vinarekebishwa ni kuona kwamba Walimu wanatokana na best performance.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa hapo elimu, naomba sana hili najua linaenda zaidi kwa Profesa Ndalichako Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi tena, tubadilishe huu utaratibu wa madaraja, tunasema ufaulu ni asilimia kubwa, tunaamini kwamba mpaka division IV ni ufaulu!
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tusijidanganye, tunajipa picha kwamba watu wetu wanafaulu, kumbe tunakwenda kupeleka katika soko la ajira watu ambao hawako competent. Turudishe ufaulu division one mpaka three, ndiyo iwe maximum ya ufaulu na watu watajitahidi, watu watapambana, na Walimu watapambana kuhakikisha kwamba vijana wetu wanafaulu katika madaraja hayo.
Mheshimiwa Nabu Spika, tunajiridhisha tu kwamba ufaulu mwaka huu asilimia 69 kumbe kuna division four kule ndani, division four ni ufaulu? Haiwezekani tunataka tutoe Taifa la watu ambao wanajiweza. Taifa la watu ambao wako competent, tukitoka hapa tunashindanishwa na watu wa Mataifa mengine, tuweze ku-survive. Naomba sana hilo tulizingatie na kama inawezekana , tuanze kulibadilisha sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu nataka kuliongelea kidogo ni maji. Katika Jimbo langu la Kondoa kuna upungufu mkubwa sana na tatizo kubwa sana la maji Mjini pamoja na Vijijini. Pamoja na upungufu wa maji huu na miradi inayokwenda michache, bado usimamiaji wa miradi ambayo ilikwenda kule mwanzo siyo mzuri kiasi kwamba miradi inakufa, visima vinashindwa kuendeshwa vizuri, wale watu hawapati elimu ya kutosha, Kamati za Maji hazijielewi, matokeo yake hata ile miradi michache iliyokwenda inakufa na tatizo linazidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba Waziri wa TAMISEMI suala hili tuliangalie, tuhakikishe maelekezo mazuri yanakwenda kwenye Halmashauri zetu, watu wasimamiwe wapate maelekezo mazuri, Kamati ziundwe, ziwe zinakuwa monitored, matokeo yake miradi iweze ku-survive. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najua bajeti yenyewe ni ndogo, hiyo miradi michache itakayokwenda kule lazima tuilee na iwe endelevu, bila usimamizi mzuri, tunawaelewa watu wetu vijijini, itakuwa changamoto kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimependa nizungumze hayo matatu tu katika hotuba hizi mbili. Nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Kwanza kabisa nipende kuchukua fursa hii kuzipongeza Kamati zote mbili kwa taarifa na mapendekezo yao na pia nianze kwa kusema naunga maoni na mapendekezo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi nichukue fursa kuzungumzia machache. Kwa upande wa Kamati ya Maliasili napenda kwanza kushauri kutolewe na zitengwe fedha kwa ajili ya kutoa elimu ili watu wafahamu umuhimu na faida za uhifadhi kati ya mipaka ya mapori ya akiba, mapori tengefu na maeneo ya makazi. Watu wamekuwa hawaelewi umuhimu wa hili jambo; ndiyo maana unakuta watu wanavamia, mifugo mara nyingine inakwenda inaingia ndani ya hifadhi, kunakuwa na vurumai sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufuatilia hakuna fedha hata kidogo zinazotengwa za kutoa elimu kupitia Wizara na hizi Mamlaka za Uhifadhi; sasa wanawezaje kuendesha hiyo kampeni ya kuelimisha wananchi? Matokeo yake wanakwenda na nguvu tu, wakati mwingi wanatumia nguvu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kwenye Jimbo langu Kondoa kufanya zoezi hili na likafanikiwa kwa kiwango kikubwa, watu wameanza kuelewa kutii sheria bila shuruti, kwa maana ya kutokuingia kule ndani, lakini pia taasisi hizi zinazohusika na uhifadhi ni lazima ziwe na fungu la kufanya zoezi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwetu kuna pori la akiba la Swagaswaga na lipo Mkungunero na watu lazima waelewe namna ya ku-co-exist, tusipo co-exist na wananchi wakajua kuna faida gani ya haya mapori, wakaziona na wakanufaika nayo ina maana itakuwa vurumai inaendelea tu. Kwa hiyo, nataka kusisitiza Wizara lazima kutengwe fungu hawa watu waweze kuelimishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika hiyo hiyo namba mbili, askari wa wanyamapori; kweli wana jukumu la uhifadhi, lakini ndugu zetu hawa kwa kuwa wamekuwa wanahifadhi wanyamapori wamekuwa na wenyewe kama wanyama, wanaua hovyo. Wakati mwingine hata hakuna sababu ya kutumia nguvu kubwa hiyo, lakini wanakutana na mtu labda tena wakati mwingine; mimi nina kesi mwezi wa 12 hapa, alikuwa ameonekana kijana ana pikipiki amebeba kifurushi cha sukari guru, kinavuja vuja hivi wao wakadhani ni nyama ya pori labda ni swala. Walimfuatilia wao wana gari lao land cruiser yule kijana ana pikipiki wamekwenda kumuua kwenye kijiji wala si kwenye hifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijana mmoja, hana silaha hana lolote, anaendesha pikipiki yake of course na yeye alikimbia maana wale askari wa hifadhi wakionekana watu wanapata hofu; akawa anakimbia na pikipiki yake wale jamaa wamemkimbiza wamefika hatua kijana asiye na silaha anapigwa risasi sita. Sasa hata kama angekuwa ni Thomson Gazelle ameuwawa pale si furushi la sukari guru kweli hukumu yake ilistahili kupigwa risasi zote zile? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara na mamlaka, hizi taasisi hebu tuwafundishe hawa askari wetu wawe na ubinadamu kidogo. Halafu baada ya kumuua wamemchukua wakamkimbizia porini ili waje kudai kwamba mtu huyu ameuwawa ndani ya hifadhi; mtu kauwawa kijijini. Wakachukua na furushi lake la sukari guru na pikipiki wakaingia nayo ndani kwenda kupotosha ushahidi. Kumekuwa na taratibu hiyo mara nyingi sana kwa sababu askari kwa askari taarifa ikiripotiwa wanalindana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuona dalili zile, bahati nzuri nilifika kwenye tukio mapema sana, nimshukuru sana Mheshimiwa Mwigulu nilizungumza naye nikamwambia nina wasiwasi hapa kuna dalili za kupotosha ushahidi, watu wameingiza maiti ndani. Wewe umeua mtu si unamuacha kwenye crime scene? Tena ni askari una ujuzi, unaondoa kwenye crime scene unapeleka porini ili ukamsingizie. Basi akaweka jitihada ule utaratibu ukafuatwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, walikuwa ni askari saba mpaka sasa hivi wamekamatwa askari watatu tu wako ndani including wawili waliopiga risasi; mmoja ali-shoot risasi mbili na mwingine risasi nne. Imeenda kupasua mapafu na moyo mpaka kijana wa watu akapoteza maisha namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuwafundishe askari wetu; Mheshimiwa Waziri na viongozi wote huko; hawa jamaa wawe na ubinadamu. Kuwa wahifadhi wa wanyampori haina maana nao ni wanyama. Nataka kupendekeza, tukio lile lilitangazwa na likawa kubwa sana kwenye vyombo vya habari, basi hata hawa maaskari watakapohukumiwa nalo lijulikane ili wananchi wapate imani na Serikali yao kwa sababu wanaona watu wanawekwa ndani kwa muda tu halafu wanapotea. Mtu aliyeua namna hii stahili yake ni hukumu ya kunyongwa mpaka kufa, umeua makusudi, si bahati mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nisisitize sana Wizara iliangalie hili kwa kina sana na limetokea, Mkungunero; miaka ya nyuma wakati wa tokomeza tuliona haya yamekuwa kwa wingi sana. Kwa hiyo, nisisitize Wizara ilitilie mkazo na kuwafunda wale askari, si wanyama wale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka kuzungumzia uimarishwaji wa ile mipaka kati ya mapori tengefu, mapori ya akiba, hifadhi na maeneo ya wananchi. Ndugu zangu siku vile vikosi kazi vinapokwenda kuweka ile mipaka ishirikishe wananchi. Kwa sababu unaweza ukasema usishirikishe wananchi baadaye migogoro inaendelea miaka nenda rudi. Wawe sehemu ya uwekaji wa mipaka ile. Idara za ardhi katika Halmashauri zetu zishiriki, wanakwenda na GPS wanaona mipaka na wanajiridhisha hii ndio iliyoandikwa na ndio tunayoijua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu vinginevyo malalamiko yanaendelea, aaa, mpaka ulikuwa hapa, sasa wameusogeza mbele. Sasa tutaendekeza malalamiko ya namna hii kwa muda gani? Kuna ugumu gani Wizara na hizi mamlaka za hifadhi kuwashirikisha wananchi na idara za Halmashauri zikaenda na vifaa; na document zao wanazo basi utaratibu unakuwa clear. Hilo nalisisitiza sana ili tuweze kupunguza hii migogoro isyokwisha kati ya hifadhi na maeneo ya makazi na kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo kwa ufupi sana kuhusu kilimo; jamani tutazungumza sana kilimo na uchumi wa viwanda. Hiki kilimo kama hatutakiwekea bajeti kubwa kabisa ya kutosha kwenye upande wa umwagiliaji tutakuwa tunapiga story tu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia kwenye hotuba ya bajeti ya TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora. Kwanza kabisa nawapongeza kwa kuwasilisha hotuba nzuri na kuwasilisha mpango wa bajeti mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia siyo vibaya na ni muhimu tukaweza kutoa maboresho pale ambapo panaonekana panahitaji kuboreshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na eneo la kujenga uwezo kwa maana ya mafunzo. Nimemsikia kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene namna alivyoliweka; tunaelewa mlipotoka, tunaelewa maana yake, lakini nataka niseme, mafunzo ya kujenga uwezo ni jambo muhimu sana. Hata ukiwa umesoma namna gani, una Ph.D, umetoka umewiva, una experience nzuri kabisa kwenye eneo lako la kazi, lakini kujifunza ni dhana endelevu. Utajifunza mpaka siku ya kwenda kaburini.
Sasa tunaposema kwenye baadhi ya maeneo kwamba tumechagua watu au tumeteua watu ambao wamekwishawiva, nafikiri pale kidogo tunahitaji tulitafakari upya. Nashauri, jambo hili la wenzetu Wazungu, wanasema “learning is a continuous process.” Mpaka siku ya mwisho
utaendelea kujifunza tu, hautafika mahali ukasema wewe umekamilisha, unajua kila kitu, haiwezekani. Ni lazima tuendelee kujifunza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napendekeza kwamba Wizara, kwa maana ya Serikali, bajeti ya kujenga uwezo iendelee kuwepo na izingatiwe sana. Taifa ambalo halijifunzi, hili litakuwa ni Taifa la namna gani? Kweli mtu anasema nimeshamaliza kujua! Haiwezekani. Ndiyo maana wakati mwingine tunakutana na changamoto za makosa madogo madogo ambayo yangeweza kuepukika kupitia capacity building.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisisitize sana, nimeona kuna bajeti kidogo kwa wale ambao wengine wanawaita maarufu kama wateule kwa maana DED, DC, DAS na Wakuu wa Idara wengine, lakini nataka niseme pia hii capacity building isiishie kwa hawa wateule peke yake,
hata sisi Wabunge, lakini wale Madiwani, Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji ambao toka wameingia, sehemu kubwa mfano kwa Wenyeviti hakuna chochote walichojifunza. Matokeo yake unajikuta wako tu kule hawajui hata wanakwenda vipi pamoja na kwamba waliomba zile nafasi
wakiamini wana uwezo na zile nafasi lakini kwa kweli wanahitaji kufanyiwa mafunzo ya kujenga uwezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nisisitize kwamba katika bajeti, hili ni jambo la msingi sana na kama tunakwenda na falsafa ya kwamba hakuna tena; kulikuwa na ile dhana ya Semina Elekezi. Naishauri tu Serikali yetu, naamini Serikali yetu ni sikivu, jambo hili tutakuwa tunakwenda kidogo kwa kimakosa. Tujaribu kulitazama upya, tutenge bajeti kwa ajili ya shughuli hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nitapenda nichangie, kumejitokeza kule kwenye Halmashauri zetu ukinzani kati ya maelekezo kutoka Serikali Kuu na vipaumbele kutoka kwa wananchi. Sisi tunaokwenda kwa wananchi tunakutana na changamoto. Tunataka kuzitatua
changamoto kutokana na vipaumbele ambavyo tumefikuta kwa wananchi, lakini mkikaa kwenye vikao vile pale Halmashauri wakati mwingine tayari kuna maelekezo, safari hii kipaumbele ni moja, mbili, tatu, huku kwingine hapana.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua hata hii Serikali tumeiweka kwa ajili ya kuhudumia wale wananchi. Tunapoweka one size fits all kwamba katika ngazi ya Serikali, sawa. Kulikuwa na jambo ambalo limeonekana safari hii tufanye operesheni hii twende namna hiyo, lakini vile vipaumbele ambavyo tunakwenda kuviibua kwa wananchi, tusiviache. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, hebu labda kuwe na maelekezo kwamba panapotokea mambo ya vipaumbele na maelekezo kabisa ya labda miongozo, maana yake hii miongozo ndiyo Watendaji wengi wanafanya nayo kazi hiyo, ili kusiwe na migongano sana katika hilo. Mwenyekiti, Mbunge na Madiwani wengine wanapambana na vipaumbele vilivyoibuliwa huko na wananchi; lakini Watendaji wa Halmashauri, wanapambana na melekezo. Mwisho wa siku hatutafika. Naomba sana Mheshimiwa Waziri hilo tuliangalie vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, napenda kuongelea kuhusiana na suala zima la huduma kwa wazee kwa maana ya kule hospitali. Niko sasa kwenye mpango wa afya kwa maana ya hospitali. Sera ipo vizuri na mipango ni mizuri. Nataka niwaambie, utekelezaji wake kule hospitali hebu tengenezeni mkakati au mechanisms za kuhakikisha unatekelezwa kadri mnavyopanga, kwa sababu utekelezaji kule haupo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaambie kama kwangu kule Hospitali ya Mji wa Kondoa, ukiuliza habari ya Dirisha la Wazee, halipo. Ukiwauliza, sera hii ipo vipi? Wengine hawaelewi. Kwa hiyo, hebu tuhakikishe kuna mikakati mahususi ya kuona hii mipango tunayoiweka katika ngazi ya kitaifa inatekelezwa mpaka kule chini. Tuwe na mechanisms za kusimamia utekelezaji ambao utakuwa makini.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la vitambulisho; hao wazee wa kuanzia miaka 60 wapate vitambulisho ili waweze kuhudumiwa. Siyo tena kila wakati wakija wapite kwa Mtendaji wa Kata waandikiwe barua. Hiyo haijakaa sawa! Ni usumbufu ambao unapunguza ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa hapo hapo kwenye suala la afya, napenda niongelee suala la dawa. Malalamiko juu ya dawa ni mengi kweli kweli. Hapa tunasikia kwamba hela zimepelekwa nyingi kwa ajili ya dawa, lakini kule unakuta hakuna dawa. Tatizo liko wapi hapa? Nataka
nishauri Serikali tufanye utaratibu wa kuweka procurement experts kule kwenye Hospitali zetu ili waweze kujua supply chain ya dawa inakwenda vipi? Inapofika wakati mtu anasema matumizi yake ya dawa ni shilingi milioni 15 kwa wiki, huku analetewa hela tofauti, au ana-order kila baada ya quarter moja wakati dawa zinakatika katikati hapo ina maana hatuna mpango mzuri wa dawa. Tuweke taratibu
ambao kutakuwa na minimum reorder level, ikifika kiasi fulani wana order tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, bila kuwa na experts wa procurement kule kwenye hospitali zetu, tutaendelea kusumbuka na haya malalamiko yatakuwepo na hela zipo, zimepelekwa. Ukiangalia kwenye upande hela, zipo dawa hakuna. Naomba na hilo nalo liangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwenye upande huo huo wa afya, kuna baadhi ya hospitali zinakutana na changamoto kubwa sana kama ile hospitali ya Mji, Kondoa. Inahudumia Halmashauri tatu Kondoa Mji, Kondoa Wilaya, Chemba, lakini pia na sasa hivi barabara kubwa ya lami
imepita na dharura zinaongezeka, lakini fungu kubwa la bajeti linakwenda kwa ajili ya Hospitali ya Mji; haitatosha. Hebu tuangalie kama pale tunaweza kuboresha kufikiria mpaka hao wengine watakapojenga hospitali zao za wilaya, lakini kwa sasa hivi wote wanahudumiwa kupitia Hospitali ya Mji, Kondoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, niguse kidogo tu kwenye upande wa TASAF. Napongeza mpango huu, ni mzuri na malengo yake yana tija sana, lakini nataka niwaambie, utelezaji wake unahitaji mkakati wa kuusimamia ili ukidhi malengo. Kwa sasa hivi kuna upungufu mkubwa na kunatokea malalamiko mengi…(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa, kwanza kabisa niipongeze Waziri, Wizara na timu yake nzima kwa uwasilishaji mzuri. Napenda kusema machache kwa maana ya kuboresha na kurekebisha pale ambapo panahitaji marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nataka niongelee kuhusiana na hospitali yetu ya Kondoa ambayo kabla ya kugawanywa Halmashauri kidogo tulikuwa tunakwenda vizuri, lakini sasa hivi kutokana na utaratibu bajeti yake imebaki kuwa kutokana na idadi ya watu wanaotokana na Halmashauri ya Mji Kondoa ni kidogo sana. Inapigiwa bajeti kwa ajili ya watu 68,000 wakati inahudumia watu 250,000 wa Kondoa Vijijini, inahudumia watu wa Chemba karibu 250,000, kwa hiyo jumla inahudumia watu karibu 600,000 ingawa inatengewa bajeti kwa ajili ya watu 68,000. Kwa hiyo uwezekano wa kutoa huduma kwa ufanisi haupo kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana jambo hili pamoja na kwamba tunaangalia kigezo cha population, hebu tuende mbele zaidi, hospitali hii inahudumia na akina nani wengine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, babaraba ya kutoka Dodoma - Kondoa kwenda Babati inaeelekea mwisho kumalizika kwa kiwango cha lami. Sasa hivi tena ndiyo tatizo linaongezeka kutakuwa na wasafiri pale watakaohitaji huduma, wako hata jirani zetu wa Wilaya zingine za pembezoni nao wanapata huduma pale. Ninakuomba suala hili la kuangalia kigezo hiki cha idadi ya watu peke yake kwa hospitali kama ya Kondoa najua na wengine wapo wanakumbana na matatizo kama haya, hebu tuliangalie tuweze kutoa huduma hii vizuri kuliko ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa hapo hapo niongelee kidogo kuhusiana na upungufu wa Miundombinu na vifaa muhimu. Kwanza kabisa ni ambulance, pongezi kwa kazi ambayo tayari imeshafanywa kwa Halmashauri nyingine kupata ambulance, ninakuomba Shemeji yangu Mheshimiwa Waziri Dada Ummy kwamba itakapofika awamu ya pili basi na mimi niwepo katika Halmashauri ambazo zitafuata awamu ya pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunachangamoto kubwa sana ya mortuary, mortuary ina uwezo wa kuchukua miili minne tu, kwa hospitali kubwa namna ile miili minne ni kitu kidogo sana. Tunahitaji kufanya utaratibu kuongeza facility hii. Hata maabara nayo ni changamoto. Upande wa madaktari pia tuna upungufu, ninakuomba katika utaratibu wako basi na kwenyewe utufanyie mpango.

Pia niongelee suala la dawa, tunazungumza hapa bajeti ipo vizuri fedha zimepelekwa, lakini Mheshimiwa Waziri hoja isiishie tu kwenye fedha zimepelekwa. Fedha zipo lakini ukitafuta mrejesho kwa wananchi huku dawa hazipatikani. Wananchi siyo kwamba wanaangalia fedha zimeingia au wanataka maelezo, wanataka dawa ziwepo, kuna tatizo pale. Kuna tatizo ambalo nahisi kwenye utaratibu wa manunuzi lakini pia na madaktari wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri vitu viwili, namba moja tupate wataalamu ma-expert wa manunuzi ili supply chain ya madawa iweze kwenda vizuri isije ikafika wakati dawa zinakatika hela ziko kwenye hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili labda tutengeneze muundo wa ki-digital ambapo madaktari watakuwa wanajua stock gani ipo ndani kiasi kwamba hata anapo- prescribe dawa zile anajua dawa zilizopo, siyo daktari anatoa dawa kumbe kwenye stock hakuna. Sasa tutengeneze mfumo ambapo kila zinapotumika, zinapopungua anajua kiasi cha dawa zilizopo na ni dawa za aina gani. Hiyo itatusaidia sana kupunguza hii changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule site watu hawaangalii hela, wanaangalia dawa zipatikane. Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri jambo hili na mtuambie tu sasa hivi kuna mechanism gani ya kwenu kuhakikisha kweli dawa zinafika na mnapata mrejesho na mfumo gani unawekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu nataka kuzungumza kidogo kuhusiana na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Sannda.