Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Edwin Mgante Sannda (5 total)

MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza Sera ya Elimu Bure kwa kidato cha tano na sita ambalo ndilo kundi pekee lililobaki kugharamiwa na Serikali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekonolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Mgante Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka kipuambele cha kuhakikisha fursa sawa ya kupata elimu kwa ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari, kidato cha kwanza hadi cha nne kwa sababu hii ndiyo ngazo ya elimu ambayo humpatia mhusika study za msingi za kuweza kukabiliana na mazingira yake. Dhana ya elimu bila malipo inazingatia uendeshaji wa shule bila ada wala michango ya aina yoyote ya lazima kutoka kwa wazazi au walezi wa wanafunzi na hivyo kuondoa vikwazo vya uandikishaji na mahudhurio ya watoto shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, chini ya mpango huu, Serikali inafidia gharama za uendeshaji wa shule ambapo hupeleka fedha moja kwa moja shuleni kama fidia ya ada, chakula cha wanafunzi na fedha za ruzuku ya uendeshaji wa shule (capitation grants). Jumla ya fedha ya kugharamia elimu bila malipo inayotolewa na Serikali kila mwezi kwa ajili ya shule za msingi na sekondari ni shilingi 20,805,414,286.14. Katika hizo, shilingi 5,459,265,929 ni kwa ajili ya shule za msingi na shilingi 10,054,298,857 ni kwa ajili ya shule za sekondari; na shilingi 5,091,850,000 ni posho ya madaraka ya Maafisa Elimu Kata, Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule. Serikali pia hupeleka fedha kiasi cha shilingi 6,005,374,781 kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wa bweni wa shule za sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Elimu Bila Malipo umeonesha mafanikio makubwa tangu ulipoanza mwaka 2016. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na uandikishaji na uimarishaji wa mahudhurio ya wanafunzi darasani, kwa mfano, watoto wa darasa la awali walioandikishwa wameongezeka kutoka wanafunzi 1,015,030 mwaka mwaka 2015 hadi wananfunzi 1,320,574 mwaka 2017 sawa na ongezeko la watoto 300,544, yaani ongezeko la asilimia 30.
Mheshimiwa Naibu Spika, idadi ya wanafunzi wa darasa la kwanza walioandikishwa imeongezeka kutoa wanafunzi 1,028,021 mwaka 2015 hadi wanafunzi 1,896,584 mwaka 2017 sawa na ongezeko la wanafunzi 868,563 ambalo ni ongezeko la asilimia 84.48.
Aidha, udahili wa wanafunzi wa kidato cha kwanza umeongezeka kutoka wanafunzi 451,392 mwaka 2015 hadi wanafunzi 554,400 mwaka 2017. Hili ni ongezeko la wanafunzi 103,000 ambalo ni sawa na asilimia 22.82. Hali hii imetokana na mwitikio chanya wa wazazi na jamii kuhusu elimu bila malipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mafanikio ya Mpango wa Elimu Bila Malipo, Serikali inafanya jitihada za kukabiliana na changamoto zilizojitokeza kama vile mahitaji makubwa ya vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, maabara, madawati, walimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na TEHAMA. Aidha, Serikali inaendelea kufanya ukarabati wa majengo ya shule yaliyochakaa. Lengo ni kuhakikisha kuwa elimu inatolewa kwa ubora unaotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba kwa sasa Serikali haijaandaa Mpango wa Elimu Bila Malipo kwa ngazi ya elimu ya kidato cha tano na sita bali inaelekeza jitihada zake za kuboresha miundombinu na ubora wa elimu kwa ngazi zote za elimu ikiwemo elimu ya kidato cha tano na sita.
MHE. FELISTER A. BURA (K.n.y. MHE. EDWIN M. SANNDA) aliuliza:-
Mtandao wa miundombinu ya usambazaji wa maji toka chanzo kikuu cha maji ya chemchem katika Jimbo la Kondoa Mjini ni ya zamani na chakavu. Katika ziara yake mwaka jana, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliahidi kutupatia fedha za ukarabati wa miundombinu hiyo:- Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Sannda, Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uchakavu wa miundombinu ya usambazaji maji katika chanzo kikuu cha maji ya chemchem katika Jimbo la Kondoa Mjini. Serikali imekwishafanya tathmini ya awali ya ukarabati wa chanzo hicho unaokadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.1. Ukarabati wa chanzo hicho unatarajiwa kufanyika katika mwaka wa fedha 2019/2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wa Jimbo la Kondoa Mjini, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Kondoa ilikamilisha uchimbaji wa visima vinne vyenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 2.6 kwa siku. Ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa maji kutoka kwenye visima hivyo unaendelea. Kazi zinazotekelezwa ni pamoja na ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa kilomita 9.912, ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji yenye urefu wa kilomita 30.172 na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 33. Kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha wakazi wapatao 13,191 wa maeneo ya mitaa ya Kwapakacha, Bicha, Kilimani, Kichangani na Tura.
MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:-
Wananchi wa Vijiji vya Hurumbi, Dumi na Chandimo Kata ya Serya, Ausia, Mulua na Guluma (Suruke) pamoja na Hachwi, Kutumo na Chora (Kolo) katika Jimbo la Kondoa Mjini, kijiografia wana changamoto kubwa ya huduma muhimu za afya ambapo wanalazimika kufuata huduma hizo katika zahanati za jirani au hospitali ya mjini:-
Je, ni lini Serikali itatupatia Mobile Clinic kutatua changamoto hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Mgante Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa wanahitaji huduma za Hospitali Tembezi (Mobile Clinic) katika kuhakikisha wanapata huduma mbalimbali za kinga na tiba kwa urahisi. Hata hivyo, Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma imekuwa ikitoa huduma za Hospitali Tembezi katika Halmashauri zote za Mkoa kwa awamu.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa kuanzia tarehe 10 – 19 Agosti, 2017 Halmashauri ya Mji wa Kondoa, Chemba na Kondoa Vijijini kwa Kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa ziliendesha huduma ya kibingwa kwa Hospitali Tembezi katika Hospitali ya Kondoa. Katika zoezi hili, jumla ya Madaktari Bingwa 31 walitoa huduma mbalimbali za kibingwa kwa wagonjwa 6,873 kwa mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri kupitia Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mji imeanzisha huduma za Hospitali Tembezi kwa watu wanaoishi na VVU kila mwezi katika Zahanati za Kingale na Kolo ili kuwapunguzia wagonjwa adha ya kufuata huduma hii katika Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa itaendelea kutoa huduma hizi mara kwa mara kwa lengo la kuwasaidia wagonjwa kupata huduma za kibingwa na huduma nyingine katika maeneo yao na kuepusha kuingia gharama kufuata huduma za kiafya.
MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:-
Pamoja na kuhudumia wagonjwa wengi wakiwemo watokao Wilaya ya Kondoa, Chemba, Kiteto, Babati na wakati mwingine hata Hanang’, lakini Hospitali ya Mji wa Kondoa haina gari la wagonjwa (Ambulance) na uhitaji wa huduma za dharura na rufaa umeongezeka sana baada ya kukamilika kwa barabra kuu itokayo Dodoma – Babati:-
Je, ni lini Serikali itaipatia gari la wagonjwa hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Mgante Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa kwa muda mrefu hospitali ya Mji wa Kondoa imekuwa na ukosefu wa gari la wagonjwa hali ambayo imechangiwa na uchakavu wa gari lililokuwepo. Hata hiyo, Halmashauri ya Mji wa Kondoa imepata gari la wagonjwa (Ambulance) iliyotolewa tarehe 16 Machi, 2018 katika mgao wa magari yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
MHE. EDWIN M. SANNDA aliuliza:-

Halmashauri ya Mji wa Kondoa imepata eneo la iliyokuwa kambi ya ujenzi wa barabara ya Mela – Bonga pale Kolo kwa ajili ya uanzishwaji wa Chuo cha VETA:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza azma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Mgante Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kwa ajili ya kuandaa rasilimali watu itakayotumika katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha uchumi wa viwanda. Hivyo, ujenzi na uboreshaji wa vituo vya mafunzo ya ufundi stadi unaendelea kupewa kipaumbele katika mipango ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya mikoa na wilaya kutegemeana na upatikanaji wa fedha. Lengo ni kila mkoa na wilaya kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi. Aidha, Serikali kupitia Mradi wa Kukuza Stadi za Kazi (Education and Skills for Productive Jobs – ESPJ) inaendelea na ukarabati wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) ikiwemo Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Munguri kilichopo Wilaya ya Kondoa ili kuongeza fursa na ubora wa mafunzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ombi la Mheshimiwa Mbunge, mwezi Aprili, 2018, Serikali ilipeleka wataalam wake katika Kambi ya Ujenzi wa Barabara ya Mela – Bonga iliyopo Kolo Wilayani Kondoa kwa lengo la kukutana na Halmashauri na kufanya ukaguzi wa awali wa eneo ili kuona kama miundombinu iliyopo inakidhi kuanzisha Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA). Kufuatia tathmini hiyo, ushauri ulitolewa kuwa majengo yaliyopo yanahitaji maboresho na ukarabati mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili majengo haya yaweze kukarabatiwa na kuanzisha Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), ni jukumu la Halmashauri husika kupitia vikao vyake kuandika barua ya kuomba Wizara kutumia majengo hayo. Hivyo, tunasubiri barua ya Halmashauri husika kuruhusu VETA kutumia miundombinu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na jitihada hizi, nashauri wananchi wa Wilaya ya Kondoa kuendelea kutumia Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Munguri.