Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Andrew John Chenge (6 total)

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii niweze kuchangia kidogo tu katika hoja hizi mbili zilizo mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa taarifa zake nzuri alizoziwasilisha siku ya Jumatano, tarehe 8 Juni humu Bungeni, kwa maana ya kwamba ile taarifa ya uchumi (the state of the economy) pamoja na taarifa kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2015/2016 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha. Aliziwasilisha kwa ufasaha, na nimshukuru sana na timu yake, sio kazi rahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, hii ni bajeti ya kwanza kwa uongozi wa awamu ya tano ya nchi yetu. Lakini kama ilivyo bajeti yoyote, lazima uangalie kwa mwaka uliopita, kwa maana hiyo ni mwendelezo wa hayo mazuri ambayo yamefanyika huko nyuma, na tunaendelea kuyaboresha zaidi. Na unaiona sura ya bajeti hii, imebeba mambo mengi mazuri, ukianzia kwenye mpango, na bahati nzuri mwaka huu tunaanza kutekeleza mpango huu wa pili wa maendeleo, na mwaka wa kwanza katika Mpango huo wa Pili wa Maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 30, ameeleza maeneo ya vipaumbele katika mwaka ujao wa fedha; yapo katika makundi manne, kwa sababu ya muda sitaweza kuyasema, lakini ndiyo naona mwelekeo mzuri wa kule ambako Serikali inataka kuipeleka nchi yetu, lakini hasa katika kukuza uchumi na hivyo kuleta ustawi mzuri wa wananchi wetu, mimi naipongeza sana Serikali kwa hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, niwapongeze sana, unafahamu ukiangalia mapato, ongezeko la makusanyo ya mapato, Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuipongeze Serikali, tuipongeze TRA na wote hao walioifanikisha kwa sababu kwa mara ya kwanza tumeweza kwenda zaidi ya shilingi trilioni moja kwa mwezi, sio kitu kidogo, ukilinganisha na mwaka jana ambapo tuliweza kwenda mpaka shilingi bilioni 900 na kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tuna changamoto kubwa ambayo Waziri wa Fedha ameielezea kwenye hotuba hii, kwamba tukiweza kuyasimamia maeneo ambayo tunajua ni oevu kwa mapato ya Serikali, tutaweza kufanya vizuri zaidi. Ameelezea matumizi ya mfumo wa zile mashine elektroniki. Tupende tusipende Waheshimiwa, najua bado utamaduni wetu wa kutodai risiti na kutotaka kufanya nini, bado, lakini huu ni mwanzo mzuri. Tukiweza kuyasimamia hayo sasa hii dhana nzima mimi naiona ya kuingiza mapato yasiyo ya kodi kwamba TRA iyakusanye, mimi naamini tutafanya vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la misitu na mazao yanayotokana na misitu, mimi naelewa there is a lot to be collected na ninarudia msemo wa Kiingereza; taxes are never paid, taxes are collected. Na tukiangalia maeneo ambayo tunajua yapo mapato halali ya Serikali tutayakusanya, na hilo nimpongeze sana Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kuanza na kasi hiyo ya kuziba mianya ambayo ilikuwa inapoteza mapato ya Serikali. Kwa hiyo natoa pongezi hizo kwa nia njema kabisa na kuwataka wote tukaze buti, twende mbele kwa faida ya Taifa hili. (Makofi)
Kwa Watanzania, na sisi kama viongozi, mimi nasema kama tunataka Tanzania uchumi ukue, lazima tukubali wote sasa leo tutoe jasho kidogo kwa faida ya kesho. Unaumia leo, lakini unajua unajenga msingi imara wa uchumi wa nchi yako kwa faida ya watoto wako, kwa faida ya wajukuu zako, kwa faida ya Tanzania hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo moja, wataalam wa uchumi watasema, lakini mimi niliyefundishwa, unaiona kabisa bajeti ya Serikali, nia ni nzuri kabisa lakini nakisi ya bajeti tuliyonayo ni shilingi trilioni 7.48. Sasa imepanda kidogo ukilinganisha na huu mwaka tunaomaliza na ukiipima dhidi ya Pato la Taifa unaona imepanda kutoka asilimia 4.2 kwenda asilimia 4.5, sasa hii ina implications nyingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nasema wataalam wetu waliangalie hili, kwa sababu standard norm ni asilimia tatu, sasa tukiruhusu iende kwa speed hiyo, hii nakisi ya bajeti itatusumbua. Ukiangalia kwa sasa Waziri anapendekeza shilingi trilioni 5.37 zipatikane kutoka ndani, maana yake ni nini kwa benki zetu? Kwa benki zetu hizi, shilingi trilioni 5.37 ni pesa nyingi, na maana yake uwezo wa sekta binafsi kwenda kufika tena kwenye benki hizi tunaanza kuiminya; tulione hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi nasema lazima tukope na nilisema juzi, tunakopa pesa hizi kwa masharti yapi na tunazielekeza wapi? Naona haziendi kwenye matumizi ya kawaida, hongereni sana Serikali kwa hilo, zinakwenda kwenye maendeleo, zinakwenda kulipa hati fungani na dhamana za Serikali ambazo zimeiva, huo ni utaratibu wa kawaida. Lakini sehemu kubwa inakwenda kwenye maendeleo na ndiko tunakotaka tuone. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema juzi wakati tunajadili Fungu 50 (Vote 50), basi Serikali itueleze zoezi la nchi yetu kupata sovereign rating limeishia wapi? Kwa sababu tukiweza kupata sovereign rating na inakuwa inahuishwa kila wakati tutaweza ku-access mikopo hii kwa gharama nafuu lakini pia na Private Sector itaweza na yenyewe hivyohivyo ikapata access kwenye masoko ya Kimataifa kupata fedha ambazo tunazihitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niunganishe hapo hapo miradi ya maendeleo kwa upande wa PPP. Kweli twende mbali zaidi, maana sasa hivi kila siku unaambiwa ni mradi wa Dar es Salaam, mabasi ya kasi yale; sawa ni PPP ile au kutengeneza dawa inasemwa inakuja, sawa, barabara ya Chalinze - Dar es Salaam, sawa, Kinyerezi umeme sawa. Lakini yapo maeneo mengi, kwa nini Serikali inakuwa nzito sana katika eneo hilo la ubia kati ya sekta binafsi? Kwa sababu hiyo ndiyo itaiwezesha Serikali kuachana, maeneo fulani yaende kwa sekta binafsi kwa ubia na Serikali, tufanye hivyo kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho, unaona ukurasa wa sita wa taarifa ya uchumi, kilimo...
Ohoooo! Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, naunga mkono hoja hizi mbili.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa Mwaka 2016
MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii jioni ya leo. Nianze kwa kusema naunga mkono hoja hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kabla sijaanza kuchangia, napenda nichukue nafasi hii na mimi kuwapongeza Wabunge wenzetu hawa wanne; Mbunge wa Jimbo la Dimani Mheshimiwa Juma Ali Juma, na walioteuliwa na Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, rafiki yangu Profesa Palamagamba Kabudi na rafiki yangu Abdallah Bulembo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na niseme tu mimi na ninaamini kwa Wabunge wote tunawahakikishia ushirikiano wa karibu na niwatakie kila lililo jema katika shughuli zenu za Ubunge, karibuni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili niishukuru sana Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa muswada huu, amewasilisha vizuri shabaha ya muswada huu, marekebisho yote ambayo yamebebwa na muswada huu katika sehemu mbalimbali. Ni muswada mzuri na huwa nasema mimi mara nyingi humu Bungeni, uzuri wa sheria yeyote ni pale unapoanza kuitumia ndipo utaona. Mojawapo kazi kubwa ya Bunge hili ni kutunga sheria, hatuwezi kuogopa kutunga sheria kwa kusema kwamba kitu hiki kimeletwa haraka sana, lakini tunapaswa sasa tuwe watulivu na tujenge hoja ambazo zinaweza zikaboresha muswada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi namheshimu sana rafiki, msomi mwenzangu Tundu Lissu, kayasema mazuri tu mengine. Lakini mimi ningesaidia kama angeenda step further kutusaidia hapa kifanyike nini? Ame-fall shot ya hiyo, because hata mimi hapa naweza nikalalamika tu hapa, lakini nikishamaliza kulalamika hatujalisaidia Bunge, hatujasaidia nchi, lakini bado tuna muda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu mimi nitajielekeza kwenye eneo moja tu hili la mikopo, dhamana na misaada ya Serikali. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mikopo ya nje na dhamana inayotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mikopo hiyo, suala la Muungano, hasa utatungaje au utaletaje sheria ambayo inakinzana na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana inayoweza kwenda kukopa nje, ni ile sovereign inayotambulika Kimataifa, ambayo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sasa kupitia muswada huu inapendekezwa angalau tufanye utaratibu ambao utawezesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenda kupata mikopo hii, lakini kupitia mgongo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna njia nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 12 kilichoandikwa, tena kimeandikwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yaweza (may), mahali ambapo yule mkopeshaji anataka aone kwamba kuna mkataba wa kuhamisha zile pesa kwenda kwenye Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni matakwa ya lender yule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali halisi uendeshaji wa Serikali na kutafuta mikopo duniani hauendi katika hili mnalotuambia hapa. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaweza ikaenda mahali pa source ambayo haihitaji kupitia mlango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kama lender yule hahitaji masharti hayo, hakuna tatizo kabisa! Hakuna tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiwadanganye Watanzania kwamba eti mlango umefungwa, ni pale tu ambapo mkopeshaji yule anasema, hapana mimi nadhani wewe unapaswa upitie mlango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni masharti ya mkopaji kwa sababu yeye anasema wewe nataka uje na kofia ya sovereign state. Sasa mimi hata tungeliongea mpaka asubuhi misingi ya sheria za kimataifa ndiyo hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapo on-lend (kufaulisha) lazima yale masharti ya mkopo, ule mkopo mama, lazima uyazingatie unaweza ukayapeleka yakawa juu zaidi, tumefanya kwa mashirika mengi ya umma hapa. Kile ambacho Serikali ya Jamhuri ya Muungano inakopa kutoka Benki ya Dunia, Benki ya Afrika au kokote kule, kwa sababu kuna gharama ya kutoa ule mkopo kwenda kwa yule. Lakini pia kama una uwezo unaweza ukatoa kwa masharti nafuu, maana yule wa nje yeye hajali, mkopo unapoiva lazima ulipwe in full.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 27 cha Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada kiko wazi. Lender yeyote wala hahitaji kujua kama ukopaji wenu umezingatia matakwa ya sheria ya Tanzania, na ndio uzuri wa sheria hii kwamba inawalinda wale waiamini Tanzania kwamba ukiikopesha Tanzania hata yule aliyetoa zile pesa uka-on-lend aki-default lakini bado unaikamata Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huo ndio utaratibu. Kwahiyo, nadhani Mheshimiwa Tundu Lissu unanielewa ninachokisema iki-default ni nini anaye-default katika hali hiyo ime-default Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yetu ya ndani tuyaache ya ndani, katika hali hiyo inakuwaje, itakuwa ni mara ya kwanza hii? Mbona tunadaiana tu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa inatudai nafahamu mimi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano inaidai Zanzabar na mashirika mengine, wanadaiana ni masuala ya biashara mengine mengi hayo. Sasa ukiongelea TANESCO tunadaiana, TANESCO wanaidai bilioni 60 lakini yote haya Tanzania itaendelea kuwepo tu leo na kesho na kesho kutwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la msingi ni kuweka utaratibu ambao mhusika ataambiwa kwamba tulikubaliana haya na haya, wataketi kitako. Suala la misaada nakubaliana na Mheshimiwa Lissu lilikuwa na maneno neno sawa, lakini mimi siamini kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina wasemaji wake. Msemaji wake mkuu ni Rais wa Zanzibar na washauri wake. Lakini mimi ushauri wangu kama mnasumbuka kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewekwa kwenye sehemu ya parastal local government unaweza ukaiondoa tu ukaipatia kifungu cha peke yake. Lakini lengo likawa ni ku-on lend, misingi ni ile ile, tatizo liko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nisaidie kwenye maeneo machache ya kiuandishi. Ili tuende pamoja na Waheshimiwa Wabunge nitumie muswada kama ilivyokuwa published na Serikali tarehe 21 Oktoba, 2016. La kwanza nimemsikia AG wakitoa definition mpya ya mikopo inayotoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wametoa definition ambayo katika schedule of amendment mnaiona resident sources lakini nonresident sources haipewi definition. Pamoja na kwamba hii ni definition ya IMF lakini mimi napata shida kidogo kwa sababu mikopo, tunayoiongelea ni mikopo ya sovereign state, sovereigh borrowing. Sasa unaposema non-residents tutakapoenda kwenye ukurasa unaofuata maana yake ni nini? Mnatuchanganya kweli kweli. Mimi ningelipenda ile non-residents source na yenyewe ipewe definition, ili tukae vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafanya marekebisho kwa sheria iliyopo, na lazima tutumie terminology ambazo zimo na zimepewa definition au zimetumika throughout kwenye sheria ya sasa, sheria mama. Ukichukua schedule of amendment primary loan wanasema means any loan secured by the government.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa secured hatujawahi kulitumia katika sheria hii, tunatumia neno raise, you raise a loan. Nimeona maneno mengine utayaona contracted haya maneno hatujawahi kuyatumia katika sheria hii. Ni vyema tukawa na mtiririko ulio sahihi katika maeneo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine, nimemsikiliza sana Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu alipokuwa anasoma hotuba yake nzuri, anasema neno stock or stocks vifutwe lakini maelezo sikuyapata vizuri, labda naweza nikasaidiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa wanasheria na wafanyabiashara, kwa ngazi za kimataifa, na kule tulikotoa sheria hii neno bonds ukienda kwa Waingereza traditionally maana yake ni stocks na ndiyo maana sheria hii ilikuwa inatumia yote na kwa vile sasa tunataka kwenda kukopa kwenye Soko la Fedha la Kimataifa mimi ninaomba sheria hii ichukue sura pia za nchi nyingine ambao tutaenda kwenye masoko yao ya fedha, nashauri tusiiondoe definition ya stock or stocks. Lakini kama mnaiondoa, sasa msiiondoe kwa utaratibu mliotumia wa short hand maana tutapata matatizo, ningependa wanasheria wa ofisi yako wakusaidie AG.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukienda ukurasa wa 7, 8 na 15 unapokuta maneno hayo yalivyotumika ukifuta tu neno stock yanayobaki hayana maana. Kwa hiyo, kama mnataka kwenda kwa namna hiyo lazima muifuatilie sheria kila kifungu muone ilivyokaa na muionyooshe ikae vizuri, ndio ushauri wangu katika eneo hilo. Lakini ningekuwa mimi ningeomba sana tusi-disturb environment ya mikopo na hasa tu kule tunakoelekea sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja ukurasa wa tano wa muswada. Nimeyaeleza yaliyoko kwenye tano pale, kama tungependa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar isionekane, or tuandike ka-paragraph kanakosimama peke yake; lakini inaongeza nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashuka kidogo ya stocks nimeiongelea, nashuka tena kidogo foreign loan means any loan contracted; nimesema tutumie maneno raised throughout ambayo ndio maneno ambayo yako kwenye sheria ya mikopo. Tunashuka kidogo, kwenye 6(b), mimi hapa nakubaliana sana na Serikali kwa sababu concession loan zimepungua sana, mikopo ya masharti nafuu, na Mheshimiwa Waziri wa Fedha huwa anatukumbusha mara nyingi hapa Bungeni.
Sasa hivi dunia hii inaenda kwenye mikopo ya kibiashara zaidi, lazima tuyakubali haya; mimi nayakubali hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaposhuka chini kwenye kile kifungu kipya cha 2 kinachopendekezwa hapo ndio sasa nimepata shida sana, pamoja na marekebisho ya Serikali yaliyoletwa. Kinasema foreign loan ambapo walipashwa waanze a foreign loan may be raised.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nina matatizo na hapo hayajakaa vizuri yatatuchanganya. Maana tunapaswa tuseme, moja, a foreign loan by direct borrowing, pili, non-resident, sasa na hapo nimeshtuka kidogo, non-residents tuna maana gani hapa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini unasema futa neno issue or issue ingiza maneno ambayo mnayaona katika ile schedule of amendments, inapoteza meaning mpaka uje tena uhangaike kuingiza issuance of bonds halafu ndipo uendelee. Ndiyo maana ikiandikwa vizuri inaweza ikatusaidia labda AG atatusaidia anapo-windup kumalizia kuhitimisha hoja yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeni-warn kuhusu muda wangu. Nimalizie la mwisho ni la msingi sana, ukurasa wa 6 clause ya 8(b) kwenye provisory wanasema uingize neno not naombeni sana mkisome kifungu hicho, is mirror image ya kifungu cha 3 cha sheria hii. Ukisoma vizuri ule mtiririko ningekuwa na muda wote mngeona, lakini AG na team yako mimi naona mtaliona hilo hakuna haja ya kuongeza neno not yanajitosheleza yalivyo sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi. Nimalizie kwa kusema naunga mkono hoja hii mia kwa mia, lakini ninawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, kazi yetu mojawapo ya kufanya ni kutunga sheria za nchi yetu, tuziboreshe pale tunapoona panahitaji maboresho na tunafanya vizuri, lakini tusiwe tunaendelea kulalamika katika Bunge lako haitasaidia Watanzania na Bunge lenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge katika kuchangia hoja iliyo mbele yetu. Nianze kwa kusema naiunga mkono hoja hii asilimia mia moja lakini mniwie radhi kwa sauti yangu kidogo leo haijakaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili na mimi niseme, haya yanayoendelea pamoja na kwamba ni michezo ya kisiasa lakini isitukwaze. Sisi kwa mujibu wa Katiba, Sheria na Kanuni za Bunge, akidi ya maamuzi tunayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kama kuna kitu Mbunge amekereka kanuni zina utaratibu. Mimi nawasihi wenzangu hawa tutumie Kanuni zetu, huo ndiyo utaratibu wa Kibunge na siyo kwenda kufanya vikao kantini na maeneo mengine. Mimi siko nyuma yako, bali niko bega kwa bega na wewe. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Deni la Taifa, nimesikiasikia hata kwenye hotuba ya wenzetu wanalisemea hili, ndiyo linakua lakini Tanzania ya leo siyo ile ya mwaka 1960, 1970, 1980. Taifa hili linakua na mahitaji yake yanazidi kuwa makubwa na lazima Serikali kupitia bajeti yake iweze kuwahudumia wananchi katika sura hii. Hoja siyo deni la nchi hii kukua, hoja ni kwamba tunapochukua mikopo hii iwe ni mkopo wa muda wa kati au muda mrefu tunazielekeza wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika,tukizielekeza kwenye consumption ndiyo inakuwa tatizo, lakini tukizielekeza katika maeneo ya uzalishaji yanayotujengea uwezo ya uchumi wetu kukua kwa haraka deni letu litaendelea kuwa himilivu. Tulielewe hilo lakini kusema kwamba tunagawanya deni hilo kwa population haiendi hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa mkakati wetu wa kusimamia Deni la Taifa na Sheria yetu ya Mikopo, Dhamana na Misaada labda Waziri angeweza kutusaidia tu tukajua huwa tunafanya tathmini ya Deni la Taifa baada ya muda gani maana ni vizuri tukajua deni la kipindi cha muda wa kati au muda mrefu. Pia vile viashiria ambavyo vinatumika, maana ukichukua kwa mfano thamani ya sasa ya deni la Taifa uwiano wake na Pato la Taifa ni asilimia ngapi. Maana nadhani haya ndiyo yanapaswa sisi kama Wabunge Serikali iwe wazi ili kupunguza haya maneno. Unapolinganisha ukomo, ule ukomo ukisema ni asilimia 50 msingi wake ni nini au unaposema deni letu la Taifa kwa sasa thamani ni hii lakini ukilipima kwa mauzo yetu ya nje ya bidhaa zetu na huduma ni asilimia ngapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ndiyo masuala ya msingi. Nadhani Waziri wa Fedha anapokuja kuhitimisha atusaidie katika kuyasema haya ili nchi na Wabunge tuweze kulipata hili suala vizuri. Naamini deni hili linahimilika na tutaendelea kuwa nalo na tutaendelea kukopa lakini tukope kwa misingi ambayo inajenga Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili amelisema kwa sura tofauti Mheshimiwa Janet Mbene, nataka niulize tu tumekuwa na hili zoezi la nchi yetu kufanyiwa tathmini ili iweze kukopesheka nje, ile sovereign rating imesemwa sana humu. Mara ya mwisho nakumbuka katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/2014 Serikali ilisema wako advanced sana lakini sasa hivi hatusikii tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna faida zake kwenda route hiyo kwa sababu ndiyo unapata access kwa mikopo from masoko ya kimataifa ya masharti nafuu lakini pia na makampuni ya Kitanzania yanaweza pia na yenyewe kupata mitaji kutoka kwenye masoko ya Kimataifa. Sasa tungependa tuelezwe ni nini kimetukwamisha tena tunarudi nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni hili la Public Private Partnership. Kusema kweli visingizio vimekuwa vingi. Naiomba Serikali ile miradi 125, maana mwanzoni tuliambiwa sheria haijakaa vizuri, ni kweli maana mtu anakuja hapa na pesa zake umuambie afuate Sheria ya Manunuzi kulikuwa na mgongano, tukasema tuunyooshe na Bunge likafanya kazi yake. Wakasema kuna centers nyingi sana za maamuzi na kadhalika tukanyoosha sheria. Wakasema sasa imeleta miradi 125 inafanyiwa uchambuzi ili kuona kama inakidhi kuingia katika mfumo huo mpaka leo hatuoni kinachoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu unachochea uwekezaji lakini pia unapunguza mzigo wa Serikali kwenye bajeti ili tuelekeze nguvu katika maeneo ya afya na maji lakini barabara, miundombinu ya reli, bandari na kadhalika tunashirikiana na private sector kwa misingi tuliyojiwekea na hili mimi nasema linawezekana na linafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la nne limesemwa ni Benki ya Kilimo, inatia huruma sana kwa ahadi ya Serikali ya muda mrefu kutotekelezeka na mimi nasema there is more than one way of skinning a cat. Benki ya Rasilimali ya Tanzania Serikali ilipoianzisha miaka 1970 na ile iliyokuwa Tanzania Rural Development Bank kabla ya kuwa CRDB, Serikali ilichukua line of credit kutoka AIDA, European Investment Bank na Nordic Investment Bank kuweza ku-capitalize hizi benki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuwe wabunifu tukienda na lugha hii, kwanza Benki ya Maendeleo kwa Sheria ya Mabenki na Financial Institution unahitaji upate leseni minimum fifty billion, ten billion ndiyo fedha za kwenda kukopesha halafu tunasema ikopeshe kwa masharti nafuu maana yake ifanye hasara tangu day one haiwezekani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kweli kwa hili tu-capitalize the bank na tuone namna ya kufanya. Hizi hati fungani za mtaji zinawezekana zikatumika kwa sababu ukinitolea ni kama I owe you money, interest utakuwa unanilipa ndani ya miezi sita na principal mwisho wa mwezi, angalau una-clean up balance sheet yangu na wengine wanaoniangalia kama benki niweze kukopesheka, ndiyo tunaiomba Serikali ilione kwa mtazamo huo.
I owe you money, interest utakuwa unanilipa ndani ya miezi sita na principle mwisho wa mwezi ili kama benki niweze kukopesheka, ndiyo maana tunaiomba Serikali ilione kwa namna hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho. Hii Mifuko ya Hifadhi kwa principle hiyo hiyo, najua Serikali ime-underwrite Mifuko hii hasa PSPF; lakini kwa vile tumechukua pesa na tumezitumia kwa maendeleo yetu, nadhani tuwe wakweli tu, tunapowasema tutatoa a non cash bond kweli tuitoe. Tukisema tutatoa bilioni 80 mwaka huu kwenye bajeti zionekane kuliko kuzidi kuididimiza Mifuko hii halafu wafanyakazi waliostaafu kama mimi unakuta hawalipwi kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mimi nilikaa kwa kipindi cha miezi saba silipwi pensheni na, ni kweli eeh, lakini ndiyo haya mambo tunayosema, Serikali wasikasirike maana tumezitumia pesa hizi kwa nia njema, lakini tuje sasa na utaratibu utakaotusaidia kuyajibu hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa, Waheshimiwa Wabunge Kanuni za Bunge zinawaruhusu wala tusionekane kuwa ni wanyonge; hii Sheria ya Manunuzi kama Serikali hawataileta sisi wenyewe; hata mimi mmoja wao kwa sababu najua kuandika hizi sheria, tutaleta amendment ya sheria humu! Eee! Hilo tusiogope maana fursa hizi zipo tunaweza kuyafanya haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, amelisema vizuri sana Mheshimiwa Ritha, kwenye Sheria ya Micro-finance. Mimi nilikuwa consulted kufanya kazi hiyo na tulifanya kazi kubwa na akina Dunstan Kitandula. Sasa kwa kuiheshimu Serikali tukasema kwa sababu wanalifanya tukasema hebu waanze tutakuja ku-takeover baadaye, lakini naona sasa again halisemwi tena. Sasa tutayafanya hayo Waheshimiwa Wabunge tukitaka na ndio moja ya kazi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja hii mia kwa mia.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ANDREW J. CHENGE – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA SHERIA NDOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii niweze kuhitimisha hoja yangu, hoja ya Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo. Niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu. Niwashukuru sana waliochangia kwa kuongea humu Bungeni, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, Mheshimiwa Mlinga na Mheshimiwa Aida Khenani. Pia kuna Waheshimiwa Wabunge wamechangia hoja hii kwa maandishi ambao ni Mheshimiwa Lucia Mlowe, Mheshimiwa Zuberi Kuchauka na Mheshimiwa Juma Othman Hija. Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongea kwa kifupi sana. Ukimuona nyani mzee porini ufahamu kwamba amekwepa mishale mingi sana. Kwa hiyo, ndugu zangu hii ndiyo hali ya maisha. (Makofi/Kicheko) Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewasilisha hoja hii, Waheshimiwa Wabunge mtakapopata fursa isomeni, hoja ya msingi hapa ni kwamba Sheria Ndogo ni sheria halali za nchi hii na zinawagusa wananchi wetu katika maisha yao ya siku hadi siku. Mimi nashukuru sana uamuzi wa Mheshimiwa Spika kwamba Kamati hii iwe inapewa fursa ya kuwasilisha taarifa yake mapema kabla ya taarifa zote. Kwa sababu tusipofanya hivyo kama mnavyoona sasa hivi wananchi wataendelea kuumizwa tu kwa sheria ambazo zina dosari na ambazo zingeweza kurekebishwa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu amesema ziko kodi, ada na tozo nyingi sana kwenye mazao hasa ya biashara, hilo ni agizo, tunategemea kwamba Wizara zenye sekta hizo watafanya haraka ndani ya uwezo wao kuzipitia zile sheria na kanuni, kama msingi wake uko kwenye sheria mama basi wafanye marekebisho kupitia sheria mama kuleta Muswada wa Marekebisho hapa Bungeni. Kama ni kwenye Sheria Ndogo ndiyo unachukua nafasi ya Kamati hii kuyaleta mapema ili tuweze kuyapitia tuyanyooshe twende mbele. Hivyohivyo kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, maelekezo mazuri sana ameyatoa alipokuwa katika ziara Mikoa ya Kusini. Maana tukiacha hizi zitaendelea kutumika, ni sheria. Kwa hiyo, nimeona hilo niliseme kwa sababu linatuhusu sote. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Hija ameshauri tu kwamba labda Kamati ya Sheria Ndogo itusaidie hii migogoro ya wafugaji na wakulima, mtoe mchango wenu kwa hilo. Napenda sana hiyo lakini hali halisi sio hivyo. Kamati hii inafanya uchambuzi wa Sheria Ndogo ambazo zimewasilishwa hapa Bungeni na Serikali. Ombi langu kwenu kama viongozi, kwa sababu tatizo hili ni kubwa, tukianzia chini kwenye maeneo yetu katika kutunga au kupendekeza maoni yetu ya kutunga Sheria Ndogo ambazo zitasimamia matumizi bora ya ardhi, Sheria Ndogo hizo ndiyo zitaweza sasa kufanikisha hilo ambalo Mheshimiwa Juma Othman Hija anapendekeza lakini sisi hatuwezi kwenda tukafanya kazi ambayo siyo sehemu ya majukumu ya Kamati hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la elimu, kuwawezesha wanasheria, kwanza wanasheria kwenye Serikali za Mitaa au Halmashauri zetu tumelisema kwenye taarifa, hiyo ndiyo inachangia dosari nyingi ambazo zinaonekana katika Sheria Ndogo hizi. Hata hivyo, mimi najua uandishi wa sheria ni taaluma ya kipekee na ndiyo maana hata kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ni wachache na wale wazuri, hii siyo feature ya Tanzania tu, nenda kokote ndani ya Nchi za Jumuiya ya Madola tatizo hili lipo, kwa sababu hawa is a special breed, wanafunzwa namna ya kuandika. Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili uweze kufika ile grade tunayoitaka lazima uwe una uzoefu mpana sana wa sheria lakini pia na masuala ya kijamii sasa kuwapata hao itatuchukua muda. Hata hivyo, tukasema tunapendekeza angalau kwa wanasheria waliopo katika Halmashauri zetu wakinolewa kila baada ya muda kama walivyofanya juzi hapa Dodoma, wamefanya semina ya wanasheria wote hawa waliletwa hapa, ya siku tatu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imetoa inputs zake, wanasheria wa TAMISEMI wametoa inputs, ndivyo inavyotakiwa, labda itatusaidia sana katika kuimarisha uandishi wa sheria. Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema vizuri, jamani Ofisi ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali, ofisi kwanza yenyewe ni hatari. Serikali imetoa ahadi na sisi tunaamini kabisa kwamba ahadi ni deni tunategemea tuone ndani ya muda mfupi ofisi hiyo inaboreshwa kiutendaji lakini kwa vifaa vya kisasa. Maana haya tunayoyasema ya kuwasilisha Sheria Ndogo kwa mujibu wa Kanuni ya 37(2) na kwa mujibu wa kifungu cha 38 cha Sheria ya Tafsiri yanategemea ofisi ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali. Kama hajafanya utakuwa unaonea Serikali kwamba kwa nini hamjaleta mawasilisho yenu Bungeni, lakini acha tuone. Kuna mchango mzuri tu wa Mheshimiwa Kuchauka, yeye anasema hawa wananchi wanaokaa karibu na hifadhi ndiyo wanasaidia kutunza hifadhi hizi lakini tunapata mapato kiduchu asilimia 25. Sasa yeye anapendekeza waongezewe, hayo ni ya kwenu huko, sisi tunasimamia Sheria Ndogo kama itakuja na mapendekezo hayo na yamekubalika kule itakuwa ni uamuzi wenu. Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme moja, Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290, kupitia Bunge la bajeti mwaka wa fedha 2011/2012 wote mliokuwa Bungeni mnakumbuka, yaliletwa marekebisho ya kuongeza cess ya mazao ili watoze kwa kuangalia hali halisi ya Halmashauri yako, kati ya asilimia tatu mpaka asilimia tano. Hata hivyo, ukweli wa mambo, hakuna Halmashauri nchini ambayo imetoza chini ya asilimia tano, zote zimepiga ile ceiling. Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa Kamati, ingawa siyo la kwetu lakini tunayaona, tumemwambia na Waziri wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwamba kama malalamiko ni haya hebu tujitahidi basi tukaweka ifahamike. Maana sasa hivi mmewapa ile leeway wanapiga mpaka kwenye ceiling, ni afadhali ikafahamika kama ni asilimia tano iwe asilimia tano, kama ni mbili au tatu iwe tatu, tutakuwa tumeiweka sheria katika msingi mzuri. Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa nipigiwe kengele ya pili, kazi hii tumeianza, tunaomba Kamati hii iendelee kuungwa mkono kwa kuwezeshwa. Hawa wajumbe wa Kamati hii kazi yao ni kusoma documents. Wenyewe pia ili waweze kuifanya kazi hii vizuri lazima wawezeshwe vizuri. Tofauti na baadhi ya wajumbe ambao ni wanasheria kama akina Mheshimiwa Ridhiwani, Mheshimiwa Ngeleja na wanasheria wengine lakini wengine hawa siyo wanasheria na siyo lazima uwe mwanasheria kuweza kuzifanya kazi hizi lakini ukisaidiwa ukawasikia wale ambao wamebobea katika masuala haya mtakuwa mmeisaidia sana Kamati hii. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, nisichukue muda wako mwingi, tuna mambo mengi sana leo, lakini niwashukuru Waheshimiwa Wabunge waliotuunga mkono. Nami nimalizie kwa kusema maoni na mapendekezo yote ambayo yamo kwenye taarifa ya Kamati sasa Bunge lako iyakubali kama Maazimio yaliyopitishwa na Bunge. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii asubuhi hii ya leo ili nichangie hoja iliyoko mbele ya Bunge lako Tukufu. Nianze kwa kusema naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa wasilisho lake zuri. Naelewa nyuma ya wasilisho hilo ni kazi nzuri iliyofanywa na viongozi wa Wizara hiyo pamoja na taasisi ambazo zipo chini ya Wizara hiyo. Hongereni sana kwa kazi nzuri, tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, niungane tu na Waheshimiwa Wabunge waliotangulia kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa uamuzi wa hekima na busara lakini wa kijasiri sana kuhusiana na reli ya Kati. Uamuzi huu ni wa msingi sana katika kufungua fursa mbalimbali za maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika,Naendelea kuiomba Serikali iendelee kuweka kipaumbele cha juu katika upatikanaji wa fedha za ujenzi wa reli hii kwa sababu wenzetu wa Northern Corridor wako mbali sana na shughuli hii. Kwa hiyo, nami naiomba sana Serikali twende nalo lakini naipongeza sana Serikali kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye mambo ya nyumbani, politics is always local. Nianze kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 11- 12 Januari, alitembelea Mkoa wa Simiyu hususan Bariadi Makao Makuu ya Mkoa na Maswa. Akiwa Bariadi alifanya mambo makubwa sana na ndiyo maana wananchi wa Mkoa wa Simiyu tunaendelea kumshukuru sana. Moja, Mheshimiwa Rais alizindua barabara iliyokamilika ya kutoka Lamadi mpaka Bariadi yenye kilometa 71.8.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, akiwa pale pale alitoa tamko kuhusiana na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Simiyu. Tatu, alimaliza ngebe kuhusiana na mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Viktoria, matenki makubwa yakae wapi. Nne, alitoa maelekezo kuhusu gharama za ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwamba waziangalie kwa lengo za kuzipunguza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kwenda Maswa Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwamba ujenzi wa barabara ya kutoka Bariadi kwenda Maswa kilometa 49.7 utangazwe; na kweli naona kwenye Bajeti hii Wizara imezingatia hilo. Tukiwa Maswa aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara inayoendelea sasa hivi kutoka Mwigumbi kuja Maswa. Haya ni mambo makubwa sana katika kufungua Ukanda huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Simiyu ni Mkoa mpya, Makao Makuu yake yako Bariadi. Tunahitaji tuunganishwe sisi na Mikoa jirani ya Singida na Arusha. Ndiyo maana Ilani ya Uchaguzi ya CCM inatamka, tufanye Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya kutoka Bariadi kwenda Kisesa - Mwandoya - Mwanhuzi mpaka Sibiti. Njia tunayoona sisi ni kupitia Mkalama kuja Iguguno. Kwa hiyo, tungependa sana hili lionekane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, mimi nimekuwa Mwanasheria Mkuu nikiwa Mbunge. Hii barabara ya kutoka Odeani - Mang’ola - Matala, Sibiti kwenda Mwanhuzi – Lalago – Mhunze – Kolandoto, imekuwa inaongelewa story, story, story. Kwa mwaka huu nakubaliana na Serikali kwa hayo waliyosema kwamba wamekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Mwaka kesho kama ikiendelea hivi mimi nitasema, maneno waache sasa waweke muziki. Hii barabara tunataka ijengwe. Kusema kweli ukishakamilisha usanifu huo, inakuwa sehemu ya kutoka Bariadi mpaka Mwanhuzi kwa sababu sehemu nyingine umeshamaliza. Kwa hiyo, waache maneno, waweke muziki. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukishafungua ukanda huo na kwa mapendekezo mengine ambayo tumeweka, barabara za kufunguliwa Ukanda wa Mkoa wa Simiyu, tutafungua maeneo hayo kiuchumi na kijamii. Sasa nilihangaikia sana hii Sheria ya Barabara kuweka vigezo vya namna ya kupandisha madaraja barabara hizi, basi tupate angalau maamuzi kwa nchi mzima. Vigezo vipo kwenye sheria hiyo. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri waliangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema ya nyumbani hayo, lakini nami kama Kiongozi wa Kitaifa niseme. Nchi hii ya Tanzania inafunguka kwa barabara. Angalia hizi barabara za kikanda, maeneo yote kuunganisha Tanzania na nchi jirani tumefanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi jirani sehemu ambayo naiona ni muhimu kwetu sana na nimeiona kwa mbali kwenye hotuba hii ni Kasulu – Kibondo – Manyovu na Burundi. Pia naiona kwa mbali Sumbawanga – Matai – Kisesya – Sanga Port ni muhimu sana. Naiona kwa mbali pia, Bagamoyo – Saadani – Tanga – Horohoro – Lungalunga – Mombasa – Nairobi – Isiyolo – Moyale – South Ethiopia. Haya ndiyo mawazo tumekuwa nayo, maana upande wa Uganda - Sudan ya Kusini Arua - kuja mpaka Kyaka tayari tunaendelea. Tukikamilisha kazi inayoendelea ya kutoka Nyakanazi – Kakonko – Kasulu mpaka Kigoma na tukashuka sasa kutoka Uvinza tukaelekea Mpanda - Stalike twende mpaka Kithi – Sumbawanga – Laela – Kikana – Tunduma unaiona nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nimesafiri, namwelewa rafiki yangu Mheshimiwa Zuberi aliyoyasema, lakini nimeona humu, kutoka Masasi tukijenga barabara Masasi pale Nachingwea unaenda Nanganga, halafu Nanganga unaweza kushuka hivi kwenda Ruangwa. Haya ndiyo tunataka kuyaona humu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesafiri juzi pia, sikuamini, nimetoka Masasi nikaelekea Mtambaswala, Mangaka kule nikatoka pale nikarudi kutoka Mangaka nikaelekea Tunduru, barabara safi. Tukatoka pale tumekwenda mpaka Tunduru mpaka Namtumbo, Songea. Safi! Songea unakwenda mpaka Mbinga, sasa tunabaki sehemu ya Mbinga kwenda Mbamba Bay. Jamani, mambo yanafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambayo naitaka sana na nimeona kwa mbali, tukifungua Ukanda wa Kusini kwa chakula, angalieni ukitoka Kidatu uje Ifakara, piga hilo Lupilo uende mpaka Malinyi - Londo unakuja Lumecha, Songea, unafungua yote. Ni ukanda tajiri sana. Tukiyafanya hayo tutakuwa tumeisaidia sana nchi hii. Naiona Tanzania ikifunguka. Kwa sababu ya muda, siwezi kuyasemea yanayoendelea Ukanda wa juu wa kwetu kule, lakini yamo kwenye taarifa hii. Naishukuru sana Serikali kwa kazi hii wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa reli ya kati, kwa sababu tunatafuta mzigo utakaoweza kulipa reli hii, nadhani tuje tuiangalie kutoka Isaka kwenda Keza – Kigali - Msongoti. Pia Kaliua – Mpanda – Karema, maana mzigo wa DRC kwa Ziwa Tanganyika tungependa sana tuubebe huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sipendi kupigiwa kengele, Mheshimiwa Waziri akinisaidia; aah, nimalizie, sehemu moja ambayo nataka tuangalie pia, kutoka Mpemba pale kwenda Isongole upande wa Malawi tutakuwa tumekamilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa hayo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kuchangia kwenye hoja hii. Nitamke naunga mkono hoja hii mia kwa mia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Naibu wake na timu yake kwa kuandaa hotuba nzuri, ina taarifa nyingi za manufaa kwa maendeleo ya nchi yetu. Mnyonge mnyongeni lakini haki tuwape. Hii Wizara inajitahidi sana Waheshimiwa, kwa nchi nzima tunaona sura hiyo lakini ni kwa saabu ya rasilimali fedha ambalo ndilo linalotusumbua wengi hapa, lakini tunawapongeza wanafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mkoa wa Simiyu, naendelea kuishukuru Serikali kupitia hotuba hii kwa mradi mkubwa ambao ni wa kihistoria kwa Mkoa wa Simiyu kutoka Ziwa Victoria ambao utahusisha Wilaya zote tano za mkoa huo. Lakini nitakuwa mchoyo sana wa fadhila nisipotambua kazi kubwa iliyofanywa na Rais mstaafu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete, maana yeye tangu mwaka 2005 alipoingia madarakani ndio amehangaika sana na mradi huu kwa kutambua hali halisi ya ukame katika Mkoa wa Simiyu. Mimi naamini mbele ya safari mradi huu utakapokamilika hata katika awamu ya kwanza wamkumbuke angalau awepo katika uzinduzi wa mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nirudie tena kumshukuru sana Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, juzi alipokuwa Bariadi aliusemea mradi huu kwa nguvu na akamaliza kabisa akakata mzizi wa fitna kuhusiana na mradi huu ambao ulikuwa umeanza kuoneshwa kuhusu wapi matenki ya maji yakae na alisema bila kumung’unya maneno mradi huu utatekelezwa na matenki ya maji yatakaa palepale kwenye Mlima wa Ngasamo, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utekelezaji, mimi ningependa tu Waziri labda kesho anapohitimisha anithibitishie, kwa sababu mradi huu umesanifiwa kwa kutambua hali halisi ya mkoa huo, kwamba yatakuwepo mabomba makubwa mawili, bomba moja la maji ambayo hayakutiwa dawa (raw water) na bomba lingine ndiyo la maji safi ambayo ndiyo yatatumika kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lile la maji ambayo hayakusafishwa, hayakutiwa dawa ni kusaidia kurejesha hali ya uoto wa asili katika maeneo hayo lakini pia kwa mifugo; na ndiyo maana hoja kubwa ya mradi huu ilikuwa ni kuangalia hali nzima ya mkoa huo ili mifugo hii isiende maeneo mengine kwenda kuharibu mazingira. Kwa hiyo ningependa hiyo confirmation tuipate, kwamba bado dhana ni ile ile katika usanifu wa mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali, nimeona pesa ambazo zimetengwa kwa Mji wa Bariadi ambao ni makao makuu ya Mkoa wa Simiyu. Mahitaji ya maji ni makubwa, idadi ya watu inazidi kuongezeka Bariadi na viunga vyake, tunahitaji hizo pampu tano kwa sababu visima vile vitano vimechimbwa mwaka juzi na viko pale. Sasa tungependa tupate umeme, ziunganishwe, tuongeze uzalishaji wa maji na tusambaze kwa matumizi ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye Jedwali Namba 5A, pesa ambayo imetengwa kwa kutekeleza miradi ya maji vijijini. Nina vijiji vitatu ambavyo tumepata maji tangu mwaka 2012; vijiji hivyo ni Igegu, Masewa na Sengerema katika kata ya Dutwa, kata ya Sapiwi na kata ya Masewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wananchi hawa wanajua kuna maji, wanafahamu, waliyaona wakati wanachimba visima hivi, ningependa sasa zile pesa ambazo nimeziona angalau zikatumika katika kusambaza mabomba ili maji yatoke chini yawafikie wananchi hawa kwa matumizi ya maendeleo yao. Naendelea kushukuru Serikali, nimepata maji ya msaada wa Serikali ya Misri, kisima kirefu pale Kololo lakini nazidi kuomba tena kwa Ngulyati, Mhango na Kasoli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu skimu ya umwagiliaji, nimeona ya Mwasubuya, lakini tuna eneo kubwa ambalo tunaamini Kasoli tukiweza kujenga bwawa kubwa tukafanya shughuli ya umwagiliaji sehemu kubwa ya eneo la Simiyu tutaweza kujitosheleza kabisa kwa mahitaji yetu ya chakula, kwa hiyo, naiomba Serikali ione hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije sasa mwisho, kwamba niliposema mnyonge mnyongeni. Waheshimiwa Wabunge na mimi nakubaliana na walionitangulia kwa kusema kwamba tutafute njia nzuri ya kuishauri Serikali ituongezee pesa katika Wizara hii na njia nzuri ni hii ambayo kesho Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha hoja hii, tujaribu kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naona nia njema ya Serikali, lakini tukifuata Kanuni zetu suala hili likarejeshwa kwenye Kamati ya Bajeti tuweze kufanya uchambuzi wa kina, njia ambayo naiona ya haraka ambayo hata kwenye ukurasa wa 13 wa hotuba hii mnaona, iliyonyanyua bajeti hii ni tozo ya shilingi 50. Asilimia 52.7 ya pesa ambazo zimefika zimetokana na tozo hii. Sasa hivi kwa wastani tunaingiza lita bilioni 1.8 za dizeli na lita bilioni 1.2 za petroli. Tukiangalia kwa suara hiyo uwezekano wa kupata fedha tukaongeza kwa asilimia 100 tena yaani shilingi 50 na tukipiga mahesabu tunaweza tukaongeza shilingi 100. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unafahamu maendeleo lazima tuyatolee jasho na ninawaomba sana Waheshimiwa Wabunge safari hii hii lugha ya kusema kwamba tutaongeza mfumuko wa bei, tulikatae kwa sababu sio hoja ya msingi. Hii inawezekana tukayafanya haya, mahitaji ya maji kwa watu wetu ni makubwa na tunaona, sasa tukiendelea namna hii hatutafika kokote, mimi ndiyo ushauri wangu na inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii.