Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Andrew John Chenge (9 total)

MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali napenda tu nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba katika vile vijiji 73 ambavyo vimeshaandaa Mpango Shirikishi wa Matumizi Bora ya Ardhi, ni vijiji vingapi vipo katika Wilaya ya Bariadi. Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtemi Andrew Chenge, kama ifuatavyo:-
Kwanza kabisa vijiji vilivyoulizwa kwenye swali la msingi baadhi yake mimi nilishafika akiwa amenipeleka Mheshimiwa Njalu enzi zile nimeenda na helicopter wakati wa kampeni na nikapokea kile kilio cha wananchi wake, nilipanga kwamba nitafika katika eneo hilo baada ya bajeti kwa ajili ya kujionea hali hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukirudi kwenye swali hili alilolisemea Mheshimiwa Mtemi Andrew Chenge linalohitaji idadi ya vijiji, suala hili la migogoro limekuwa endelevu kutokana na kupanuka kwa idadi ya mifugo pamoja na ongezeko la wanadamu na mahitaji ya matumizi ya ardhi, kwa hiyo, kila wakati panapokuwa pamepimwa, panakuwa pana uhitaji zaidi.
Mheshimiwa Spika, hivi tunavyoongea tayari zaidi ya vijiji 23 vilishafanya upimaji huo lakini mahitaji ni makubwa kuliko idadi hiyo ya vijiji na nitawaomba Wabunge wanaotoka maeneo ya wafugaji waungane na viongozi wa wafugaji ambao tumewaomba watuorodheshee mapendekezo ya maeneo yanayoweza kutatua matatizo haya, lakini pia na maeneo ambayo yana migogoro ili Serikali tuweze kupitia mgogoro mmoja baada ya mwingine ili tuweze kupata majibu ya kudumu kwa ajili ya watu wetu wanaogombana katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, jambo hili tumelipanga kati ya Ijumaa na Jumatatu tutakuwa tumeshapata taarifa hiyo na Waheshimiwa Wabunge wote mnaotoka maeneo ya aina hiyo mtatangaziwa ili tuweze kukaa pamoja. Jambo hili linahitaji ushirikiano wa pamoja na uamuzi wa pamoja katika kupata majawabu ya kudumu na kuondokana na tatizo hili.
MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii, lakini pia niishukuru sana majibu ya Serikali kwa swali hilo, swali langu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mgao wa mwisho wa fedha hizi za kuchochea maendeleo ya jimbo, baadhi ya majimbo nchini hapa likiwemo na Jimbo la Bariadi mgao wake wa kisheria ambao umetajwa na Mheshimiwa Waziri katika majibu yake, mgao wake haukuzingatiwa. Majimbo hayo likiwepo na la Bariadi walipewa fedha pungufu kinyume na vigezo hivyo. (Makofi)
Je, Serikali iko tayari kusahihisha dosari hiyo? Ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wangu mwenye dhamana alitoa maelezo hapa katika nyakati mbalimbali suala zima baadhi ya majimbo fedha kuwa pungufu zaidi na hasa katika Mkoa wa Mwanza. Ninafahamu kwamba Mkoa wa Mwanza ulikuwa umeathirika kwa kiwango kikubwa sana lakini mgao ule kipindi kile ulitokea kwa sababu bajeti yetu ilikuwa inalenga bajeti ya majimbo ya mwanzo, kwa hiyo, majimbo mengine yalivyoongezeka kutoka Majimbo 189 mpaka 220 ikasababisha zile fedha zikawa na mgao mdogo, hata hivyo kulikuwa na makosa ya kimahesabu ambayo ofisi yetu ilitoa maelekezo kwa ma-RAS kwamba zile fedha ambazo baaadhi ya majimbo yaliongezewa zirudi kwa ma-RAS wa mikoa, lengo kubwa ni kufanya usahihisho kwa bajeti ile ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti yetu ambayo tumeipitisha juzi hapa mwaka 2017/2018 ninaamini tumeshafanya marekebisho makubwa na Majimbo yote tarajieni katika bajeti ya mwaka huu unaokuja, imefanya mazingatio ya ongezeko la Majimbo mapya haya ambayo mimi nina imani hatutakuwa na shida tena huko tunakokwenda.
MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii na nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Natambua juhudi za Serikali zinazofanyika kwa kuunganisha Mkoa wa Simiyu na Mikoa jirani ya Singida na Arusha. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ningependa kufahamu kama huo mpango mkakati wa miaka mitano alioutaja Mheshimiwa Waziri, unashabihiana vipi na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 na 2020?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019 kuingiza sehemu ya barabara hiyo ya Moboko – Mwandoya – Kisesa - Bariadi kwa upande wa Mkoa wa Simiyu; na mto Sibiti – Mkalama – Nguguti - Iguguno na Singida ili sehemu hizi mbili za barabara hii muhimu ziweze kufanyiwa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Chenge kwa namna ambavyo anapigania hii barabara iweze kujengwa, lakini kwa maendeleo kwa ujumla katika Mkoa huu wa Simiyu.
Vilevile niseme kwamba barabara hii ambayo anaizungumza Mheshimiwa Chenge ni muhimu sana kwa mikoa mingi ikiwemo Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara kwa sababu barabara hii itakapojengwa itawezesha watu wote katika mikoa hii ninayoitaja kupita na kupunguza umbali katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kama alivyosema katika swali lake la kwanza, kwamba katika mpango wa miaka mitano, tunashughulikia hii kwa sababu imetajwa pia katika ilani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Mheshimiwa Andrew Chenge mwenyewe anafahamu kwamba tumeshaanza ujenzi katika Mto Sibiti na kazi hii itakamilika mwishoni mwa mwaka huu na ule utaratibu wa uratibu wa usanifu wa barabara hii, fedha nyingi sana zimetengwa. Zimetengwa Euro milioni 2.8 ili kuweza kukamilisha kazi hii. Niseme tu kwamba ili kazi ikamilike kuendana na kipindi hiki cha miaka mitano na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, ziko consultancy nne ambazo zimeungana pamoja ili kuhakikisha kazi inakamilika kwa haraka. Kwa hiyo, utekelezaji wa Ilani utakwenda sambamba na kazi kubwa sana ambayo inaendelea kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu kuingiza hii sehemu kwenye usanifu katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha, ushauri wako huu muhimu nauchukua ili wakati wa process ya bajeti hii inaendelea, tulifanyie kazi itakapowezekana, tutaweka fedha ili kuanza usanifu wa vipande hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande hiki cha barabara kutoka Mkalama kwenda Singida, iko barabara nyingine ambayo inatoka upande wa Sibiti, inapita Msingi kwenda Ulemo hii pia itawezesha watu wa maeneo yale waweze kupita kiurahisi wakitokea Mkoa wa Simiyu.
Mhesimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa wananchi wa Meatu, Simiyu watakuwa na access nzuri kwenda kutibiwa Haydom. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tunatambua umuhimu wa barabara hii na ndiyo maana tumeiweka katika ilani na tutaitekeleza ili wananchi waweze kupata manufaa makubwa zaidi. Ahsante.
MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Napenda niiulize Serikali, kwa sababu tatizo hili ni kubwa katika maeneo mengi nchini na nichukue tu kwa upande wa Jimbo langu la Bariadi na Jimbo la jirani la Itilima, malambo kama la Sakwe, Igegu, Sapiwi, Matongo, Mwamapalala na Mwamoto yote haya yameshambuliwa na magugu maji na maeneo mengi nchini najua hali ni hii.
MHE. ANDREW J. CHENGE: Na Malya. Je, Serikali haiwezi ikaja na mpango kabambe kama ilivyofanya kwa Ziwa Victoria miaka ya 1990 wakati limeshambuliwa na magugu maji ili kunusuru malambo haya hasa katika maeneo ambayo tuna pressure kubwa sana ya population kuliko kuziachia Halmashauri kwa mtindo huu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Chenge amezungumzia suala la mpango kabambe wa kushughulikia tatizo la magugu maji lakini kuhakikisha kwamba huduma ya maji inapatikana kwa wananchi. Nadhani Waziri wa Maji katika bajeti yake alizungumzia suala la kukamilika kwa mpango wa maji wa awamu ya kwanza sasa tunaendelea katika mpango wa maji wa awamu ya pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa maji wa awamu ya pili maelekezo yake ni nini? Maelekezo yake ni kwamba tutabainisha fursa mbalimbali, kwa mfano, ukiacha watu wa Kanda ya Ziwa wanaopata fursa ya maji kutoka Ziwa Victoria lakini na maeneo mbalimbali kuona ni jinsi gani wataweza kupata maji. Ndiyo maana nikimkumbuka au nikim-quote Waziri wa Maji alisema tutaangalia fursa zote zilizokuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo mengine yamechimbwa visima virefu (bore holes) lakini vimekosa maji. Ndiyo maana ya maelekezo haya kwamba kila Halmashauri angalau kwa mwaka mmoja itenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa lambo moja. Huo ni mpango mdogo wakati mpango mkubwa ni kwamba katika miaka hii mitano inayokuja ya ya programu ya maji ya kuhakikisha tunamtua ndoo mama kichwani tutahakikisha tunatumia fursa mbalimbali ikiwemo mito mikubwa, malambo na hata maziwa ya jirani ili mradi wananchi wa maeneo husika wapate maji. Kwa hiyo, napenda kumjulisha Mheshimiwa Chenge kamba jambo lake Serikali imelisikia na ndiyo mkakati mpana wa Serikali katika kuhakikisha tunamtua ndoo mama kichwani kama tulivyoahidi katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi.
MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Gereza la Matongo ni miongoni mwa Magereza yaliyoanzishwa na Serikali katikati ya miaka 1970 kwa lengo hilo hilo ambalo Waziri amesema katika jibu lake, lakini zaidi ya miaka 40 ukifika pale Matongo hakuna cha maana kinachoendelea. Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake anasema Gereza hili limo kwenye mpango wa kuboresha kilimo, ni lini mpango huu mahsusi kwa Gereza la Matongo utaanza kutekelezwa na Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake ametambua mazao yanayolimwa katika eneo hilo likiwepo eneo lenyewe la Matongo. Je, yuko tayari na ikiwezekana kushirikiana na Mbunge wa eneo hilo kutafuta mwekezaji ili kuanzisha kiwanda ili kuongeza thamani ya mazao yatakayolimwa na Magereza lakini pia kusaidia soko kwa wananchi ambao wanazunguka eneo hilo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza nimeshamjibu katika majibu yangu ya msingi, naomba tu nichukue fursa hii kufafanua. Nimesema kwamba tuna mkakati wa kuhakikisha kwamba Jeshi la Magereza linajitosheleza kwa chakula. Kwa sasa hivi Jeshi la Magereza linajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 30, malengo yetu ni kuhakikisha kwamba tunafikia asilimia 70.
Mheshimiwa Spika, mkakati huu utatekelezwa baada ya kuhakikisha kwamba tumepata fedha za kutosha kuwekeza. Katika bajeti ya maendeleo ya mwaka huu tunatarajia kupata takribani shilingi bilioni 3 ambazo zitatumika katika moja ya mikakati ya kuimarisha kilimo pamoja na kujitosheleza katika Magereza yetu. Pia tuna mpango vilevile kupitia jitihada za Mheshimiwa Waziri Mkuu kupata matrekta 50 kwa kuanzia ambayo tutayapeleka katika Magereza ikiwemo Gereza hili la Matongo ili kuweza kusaidia kuimarisha kilimo katika maeneo hayo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kuvuta subira lakini ni jambo ambalo tayari liko katika hatua nzuri za utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili kwamba kama Serikali iko tayari kushirikiana na mwekezaji kuwekeza. Ndiyo mikakati ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kwamba nchi yetu inafikia uchumi wa kati kupitia viwanda. Kwa hiyo, nina uhakika kabisa Mheshimiwa Mbunge akiweza kuwasiliana na mamlaka husika kwa maana ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji atapata mwongozo na msaada mzuri wa kuweza kusaidia jitihada za Serikali za kuimarisha viwanda katika nchi yetu. Sisi kama Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pale ambapo tunaweza kutoa mchango wetu kwa namna yoyote ile tutakuwa tayari kushirikiana naye.
MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Serikali kwa majibu yake. Nina maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza, muuliza swali alilenga hasa katika Sheria ya Usalama Barabarani. Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya marekebisho katika sheria hiyo?
Swali la pili; natambua kazi nzuri inayofanywa na Tume ya Kurekebisha Sheria; je, Serikali inaweza kwa wakati muafaka ikatoa report za kazi ambazo zimefanywa na Tume hiyo kama mapendekezo kwa Bunge lako tukufu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Spika, nikianza na swali la kwanza, ni kweli kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Tume ya Kurekebisha Sheria Sura Na. 171 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002, moja kati ya kazi ya Tume ni kuandaa report ambayo hupelekea mabadiliko ya sheria au kutungwa kwa sheria mpya.
Mheshimiwa Spika, katika Sheria za Usalama Barabarani tayari Tume imeshafanya kazi yake na tunayo report ya Tume ya mwaka 2004 ambayo imeshawasilishwa kwa Mheshimiwa Waziri. Pindi pale itakapoonekana kuna mahitaji ya kufanya marekebisho katika sheria husika, sharia hii itawasilishwa hapa Bungeni kwa ajili ya kuweza kufanyiwa marekebisho kama ambavyo Mheshimiwa muuliza swali amesema.
Mheshimiwa Spika, la pili, kuhusiana na report za Tume kuwasilishwa katika Bunge; kwa mujibu wa sheria Tume hii inapaswa kutoa taarifa yake ya kila mwaka ya namna ambavyo imezipitia sheria. Tunao mpango mkakati wa kuanzia mwaka 2013 mpaka mwaka 2018 wa marekebisho hayo ya sheria.
Mheshimiwa Spika, suala la uwasilishwaji wa taarifa hii, itakuwa ni kati ya Serikali na Bunge kuona namna bora ya kuwasilisha, lakini kwa hivi sasa taarifa zetu zinapatikana katika mitandao yetu mbalimbali na utaratibu mwingine wa Kiserikali kuhakikisha kwamba wananchi wengi wanazipata.
Mheshimiwa Spika, kwa maombi ya Mheshimiwa Mbunge, kama Serikali tumesikia na tutaona namna bora ya kuweza kulifanyia kazi jambo hilo.
MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa majibu yake mazuri. Napenda nithibitishe kabisa kwamba jibu lake ni sahihi na nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, alikuja Bariadi na kuzindua barabara hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo nina swali moja tula nyongeza.

Mheshimiwa Spika, chini ya mradi huu halmashauri ya Mji wa Bariadi imenunua vifaa mbalimbali kwa kuendeleza maboresho hayo ikiwemo magari ya maji taka, grader na vifaa vingine. Vifaa hivi viko bandarini kwa muda mrefu sana; na hili siyo kwa Bariadi tu lakini kwa vifaa kama hivyo kwa miji mingine ambayo iko chini ya mradi huu ambao unafadhiliwa na World Bank.

Mheshimiwa Spika, napenda nifahamu suala la VAT kwa miradi inayotekelezwa na Serikali ambayo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alishalitolea maelekezo, ni lini sintofahamu hii kati ya TAMISEMI na Wizara ya Fedha itamalizika ili vifaa hivi vitoke bandarini viende vikafanye kazi iliyokusudiwa chini ya mradi huu? Naomba majibu.
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii, na nimshukuru Mheshimiwa Andrew Chenge Mtemi kwa swali hili muhimu. Pia nimshukuru yeye kwa sababu ni mmoja wa wajumbe wa Kamati yetu ya Bajeti, Kamati inayofanya kazi kubwa katika kuishauri Serikali na kutoa maelekezo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo ni sahihi na tayari tulishaanza kuyafanyia kazi kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018, Sheria ya Fedha ya mwaka 2019 na sasa tunaanza mchakato wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2020 ambapo nina uhakika tulikofika sasa tutaweza kushughulikia tatizo hili la miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia tutaweza kuikamilisha katika mwaka huu wa fedha. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wilaya Bariadi kama ilivyo wilaya ya Busega, Bunda na Serengeti ni miongoni mwa Wilaya au maeneo yanayopakana na Hifadhi ya Serengeti. Lakini kikosi dhidi ya ujangili ofisi zake zipo Bunda na ofisi hiyo ndio inahusika na malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi. Imekuwa ni shida sana kwa wananchi wanaotoka nje ya eneo la Bunda kama Baridi na baya zaidi wanapokuja kufanya malipo haya wanakuja kulipia malipo haya kwenye guest house.

Je, ni lini Serikali itafungua ofisi ya KDU mjini Bariadi ili kuondokana na adha hii hasa kwa akina mama ambao hawapendi kwenda guest house kwenda kupokea malipo yao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba ofisi yetu ya KDU kwa sasa kikosi cha ujangili ipo Bunda na ni kwa sababu tuliamini kwamba Bunda ni katikati na eneo la Serengeti. Lakini nimhakikishie kwamba eneo hili analo lizungumzia yeye la Bariadi linapakana na Maswa, tunao maafisa wetu wa wanyamapori na tunaye afisa wa wanyamapori katika Maswa Game Reserve na wengine.

Mheshimiwa Spika, tutakachofanya ni kuwaelekeza hawa watu wa KDU wahakikishe kwamba wanakuwa na mawasiliano ya haraka na watu wetu wa halmashauri ambao kwa utaratibu ni watu wa kwanza wanafika maeneo ambayo mazao yameharibiwa kabla ya maafisa wa KDU kufika ili kutupa taarifa na kuweza kurahisisha mfumo wa malipo. Kwa hiyo, tumechukua ushauri wake wa kuwa na ofisi Bariadi, na tutakapo liangalia suala hili kulingana na uwezo wetu tutalizingatia.
MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru sana kwa majibu ya Serikali, hata hivyo nina maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, Ofisi ya Rais, TAMISEMI haiwezi ikatoa waraka kwa halmashauri zetu zote nchini ikiainisha kodi zote za kero ambazo zilifutwa na Bunge hili? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa vitambulisho vya wajasiriamali pamoja na nia njema iliyo nyuma yake, utekelezaji wake bado ni kero kubwa nchini. Je, Serikali pia haiwezi ikatoa maelekezo ya jinsi ya kutekeleza zoezi hilo ili tuwe na usare nchi nzima kuliko hali ilivyo sasa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, anauliza kama Serikali inaweza ikatoa waraka ambao unaainisha kodi za kero ambazo zilifutwa na Bunge hili Tukufu.

Naomba tupokee ushauri huo na naomba niahidi kwamba waraka huu utatengenezwa na utasambazwa nchi nzima na Waheshimiwa Wabunge watapata nakala wa kuonesha kodi ambazo ni kero zilizofutwa na Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameuliza habari ya vitambulisho vya wajasiliamali. Ni kweli kama ambavyo wewe mwenyewe umeongezea, nilitoa tamko la Serikali katika Bunge hili Tukufu ulinipa fursa hiyo, lakini vilevile pamoja na waraka wetu ambao umetolewa nchi nzima na maelezo uliyotoa mara kadhaa katika Bunge hili, bado inaonesha kuna changamoto katika utekelezaji wa jambo hili.

Mheshimiwa Spika, tulisema tunapoanza 1st July, mwaka wa fedha mpya wa 2019/2020, tutatoa waraka mahsusi na Waheshimiwa Wabunge watapata nakala ukianisha nani anapaswa kutozwa kodi ya wajasiriamali na nani anapaswa kupewa kitambulisho. Kwa kweli baada ya kutoa waraka huo, wale wote ambao watakiuka wakaienda kinyume na maelekezo haya ambayo kimsingi siyo matamanio ya Serikali na siyo matakwa ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais alimaanisha kuwasaidia wajasiriamali wadogowadogo wasipate usumbufu mtaani kwao wanapofanya biashara ndogondogo ya kujikimu kutozwa kodi kubwa na watu wa TRA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania waendelee kuvuta subira, jambo hili tunalifanyia kazi na kwa kweli baada ya hapo itakuwa ni utekelezaji, hakutakuwa na msalia Mtume. Watu wote wafanye shughuli zao bila kuvunja sheria lakini wasipate bughudha ambazo kwa kweli ni kero. Ahsante. (Makofi)